Contributions by Hon. Maimuna Ahmad Pathan (13 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku ya leo kwa kunipia pumzi ya uhai na pia kupata nafasi hii ya Ubunge. Pia nawashukuru akina mama wa Mkoa wa Lindi kwa kuniamini na kunipa nafasi hii ya Ubunge ili niweze kuwatumikia miaka hii mitano. Vilevile nakishukuru chama change, Chama cha Mapinduzi na shukrani za pekee pia ziende kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa alitekeleza vizuri Ilani ya chama chetu kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 jambo lililotopelekea kutubeba Wabunge wengi wa CCM kuingia humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia sana kwenye suala la maji. Ukurasa wa 34 Mheshimiwa Rais alisema kwamba atalipa kipaumbele sana suala la maji na pia alisema sehemu nyingi alipokuwa anazunguka kwenye kampeni wananchi wengi sana walikuwa wanalalamika kuhusu maji hasa maeneo ya vijijini. Kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, amejitahidi sana kutekeleza suala la maji katika maeneo mengi. Kwa Mkoa wangu wa Lindi tunamshukuru sana ametusaidia akina mama kututua ndoo kwa asilimia kubwa sana. Sehemu zilizobakia na changamoto ya maji ni chache sana. Tunaomba Waziri wa Maji na viongozi wengine mnaohusika na suala hilo la maji mjitahidi sehemu zile chache ambazo zimebakia ili nao wanachi wa vijijini waweze kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kuchangia ni huduma ya afya. Tunashukuru sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi sana kuboresha huduma ya mama na motto. Kwa kweli imejitahidi sana ukiangalia kwenye Wilaya ya Nachingwea wamefanya maboresho kwenye jengo la akina mama na watoto, wodi ya wazazi imekuwa nzuri na inahuduma nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambao napenda kuchangia ni kilimo, ukurasa wa 19. Pia nako kwenye suala la kilimo Rais wetu mpendwa amejitahidi sana kutekeleza Ilani hiyo ila kuna changamoto chache tu ambazo tunaomba na zenyewe zitiliwe mkazo ili wananchi wafaidike na Serilikali yao ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Lindi wanalima sana mbaazi, lakini bahati mbaya kidogo mwaka huu na mwaka jana bei ya mbaazi imeshuka sana na Akinamama wengi wameanzisha vikundi, wameungana na biashara yao kubwa ni kulima mbaazi kwa ajili ya biashara.
Tukifuata kwenye ukurasa wa 19, Mheshimiwa Rais amesema tufanye kilimo kiwe biashara, na akinamama wale walijitahidi sana kulima mbaazi lakini bahati mbaya soko kidogo limeshuka. Ninachoomba, Mawaziri husika wajitahidi kutafutia akinamama wa Mkoa wa Lindi masoko ya mbaazi ili na sisi tuinuke katika maisha yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi hii ya kuchangia hoja. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wake na leo hii tunaweza kuhudhuria Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Rais wetu kipenzi, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake kubwa anayoifanya kwa awamu hii. Mama huyu ametoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali katika Halmashauri zetu. Ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya, ametoa fedha nyingi kwa ajili ya umaliziaji wa maboma mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa shule, madarasa na mambo mengineyo. Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali kwa Halmashauri. Tumebaini udhaifu mwingi sana kwenye ripoti ya CAG kwenye halmashauri zetu. Kwanza kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa maeneo ya ununuzi na mikataba. Kama tunavyofahamu kwamba eneo la manunuzi linatumia fedha nyingi sana za Serikali, ni zaidi ya asilimia 70 ya pesa zote za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo basi, ndiyo maana Serikali ikaona ni vyema Bunge litunge sheria kwa ajili ya matumizi ya fedha hizi za manunuzi. Kuna Public Procurement Act ya 2011 pamoja na Regulation yake ya mwaka 2013. Lengo kubwa ilikuwa ni kudhibiti fedha hizi za Serikali ili zitumike vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kitu cha kusikitisha na kushangaza sana kwenye halmashauri zetu hili eneo limekuwa ni bovu kweli kweli. Kuna fedha nyingi za Serikali zimetumika isivyo. Inaonekana kuna halmashauri 42 zilitumia fedha zenye thamani ya Shilingi bilioni 7.93 bila idhini ya Bodi ya Zabuni. Kwa kweli hapa nashindwa kuelewa. Hivi unafanyaje manunuzi bila kupitisha kwenye Bodi ya Zabuni? Hapa kuna question mark, huu unawezekana ukawa ni mpango wa makusudi wa kutaka kutumia vibaya na kutumia tofauti fedha ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri 24 zilifanya ununuzi wa Shilingi bilioni 3.84 bila kuzingatia Mpango wa Manunuzi ya Mwaka. Kwenye Taasisi zote za Serikali ikiwemo halmashauri, huwa tunakaa, tunaandaa procurement plan ya mwaka husika. Unapoona kuna matumizi ya dharura yamekuja, labda kuna fedha zimekuja, mnatakiwa mwombe kibali maalum kwa matumizi hayo, na pia mnatakiwa muweke kwenye nyongeza ya mpango wenu wa manunuzi. Unapoona haya hayafanyiki, tunaanza pia kuwa na question mark kwamba fedha hizi hazikutumika kihalali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna Halmashauri 39 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Shilingi bilioni 5.37 bila kuitisha nukuu za bei (competitive tendering/competitive quotation). Ni kitu cha kushangaza kama hujaitisha nukuu za bei, umempataje huyo mzabuni kwenda kuleta bidhaa katika halmashauri? Hapo panaonesha kuna upendeleo, rushwa na ubadhilifu wa fedha za Umma. Haiwezekani mimi kama procurement officer nimekaa ofisini kwangu nikaamua kampuni ‘X’ ije ifanye kazi ya Ujenzi, au Kampuni ‘Y’ ije ifanye kazi ya kuleta bidhaa fulani, hiyo siyo sahihi na haikubaliki. Moja kwa moja inaonesha kwamba kuna rushwa ndani yake, kuna upendeleo na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna baadhi ya halmashauri 21 zilinunua bidhaa ya Shilingi bilioni mbili, lakini cha ajabu ziliingizwa kwenye ledger bila Kamati ya Mapokezi kuzikagua bidhaa hizo. Pia hapa kuna ukakasi ndani yake. Sheria inatutaka tunaponunua bidhaa zozote au huduma yoyote accounting officer aunde Kamati Maalum kwa ajili ya Ukaguzi na mapokezi ya bidhaa hizo. Ni ajabu, inaonekana baadhi ya halmashauri wanapokea kinyemela hivyo vitu, mtu wa procurement ameagiza yeye na anapokea yeye na anaingiza kwenye ledger yeye na ana-issue yeye. Hii haikubaliki. kwanza tuna wasiwasi, inawezekana hizo bidhaa hazikufika ipasavyo au hazikufika kabisa au hizo huduma hazikufanyika na ndiyo maana Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi haikufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri wanafanya ununzi wa bidhaa mbalimbali au huduma mbalimbali kwa kuwatumiua wazabuni ambao hawajasajiliwa GPSA. Hili ni kosa kubwa kwa Sheria za Manunuzi. Ina maana mtu anaamka tu nyumbani kwake asubuhi anaenda kupanga, leo nitachukua Kampuni ‘Z’ ilete bidhaa fulani. Hiyo siyo sahihi, kwa sababu manunuzi haya ni ya Serikali, yana sheria na taratibu zake, siyo kama manunuzi ambayo tunayafanya majumbani kwetu.
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache tu kwanza Kamati ilibaini kwamba kuna upendeleo, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inashangaza pia kuna halmashauri nyingine ilionekana imenunua vitu lakini haijaingiza kwenye ledger na wala hawaja mu-issue local fundi. Kuna mizania ambayo iko tofauti kwenye hizi force account, watu wanataka kuzitumia vibaya hizi force account. Haiwezekani mimi nimenunua labda mchanga au nimenunua matofali halafu fundi anayajengea bila mimi kumkabidhi. Sidhani kama hiyo ni sahihi. Hapa pia kuna ukakasi, inaonekana kuna mambo yanaenda ndivyo sivyo kwa dhamira ya makusudi, kwa nia potofu na nia ovu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunachoomba Wabunge, ushauri wetu, watu wanaofanya haya mambo, wachukuliwe hatua kali kwa haraka. Tatizo linaonekana kwamba, kama mtu amefanya kosa mwaka 2022, inafika mwaka 2023, 2024, 2025 issue ni ile ile moja haijachukuliwa hatua, kwa kweli hii haikubaliki na ndiyo maana watu wengi wanaendelea kufanya mambo haya wanaona kwamba zile sheria za kinidhamu hazichukuliwi kwa haraka. Vilevile tunapendekeza kwamba ifanyike hivyo, haya mambo yatapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna uteketezaji wa dawa za binadamu katika vituo vinavyotoa huduma ya afya. Hii inasikitisha sana. Kuna vituo vya afya, zahanati na hospitali hazina dawa. Hivi inakuwaje mpaka dawa zinafikia wakati wa kuteketezwa? Kuna sheria inaruhusu, kama mimi kituo ‘X’ nina dawa za ziada/za nyongeza, nimeona labda baada ya miezi mitatu zinaweza ku- expire au miezi minne, ninaruhusiwa kuwapa zahanati ‘Y’ hizo dawa. Kwa nini wasipeane hivyo? Kwa nini kama unajua kwenye eneo fulani hayo magonjwa siyo mengi, upeleke dawa ziwe nyingi?
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kwa sababu inaonekana kuna fedha nyingi zimetumika kununulia dawa hizo ambazo wananchi wetu wanazihitaji, lakini baadaye zinakwenda kuteketeza. Hiki nacho ni kichaka kingine, tunatakiwa tukiangalie sana, haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna maeneo manne ambayo Kamati imeyabaini ambayo ni mianya ya upotevu wa mapato ya halmashauri. Vilevile kuna ushuru wa huduma (service levy), inakusanywa bila uthibitisho wa mapato halisi ya kampuni ya mwaka (turnover). Hiki kitu siyo halali, inabidi kifuatiliwe. Kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kukata kodi la zuio (withholding tax five percent).
Mheshimiwa Spika, hii ni fedha ya Serikali ambayo inatakiwa itumike kwa ajili ya Serikali, lakini cha kushangaza, mzabuni analipwa fedha yake kama kawaida, inakuwaje halmashauri usikate hii kodi ya zuio ukairudisha TRA ili iweze kutumika na Taifa letu? Huu ni mwanya mwingine wa matumizi mabaya ya fedha ya Serikali. Pia tumebaini kuwa kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kutumia risiti ya electronic. Hiyo ni kosa kisheria.
Mheshimiwa Spika, pia inaonekana kuna halmashauri nyingine zinaendelea kutoa leseni mbalimbali za biashara nje ya mfumo. Pia hicho ni kichaka kingine. Vile vile kuna baadhi ya stahiki za watumishi kutolipwa ipasavyo. Rasilimali watu ndiyo msingi wa utendaji wa mafanikio ya taasisi yoyote, lakini rasilimali watu usipoitendea haki kuna matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inaonekana kuna watumishi wengi wa halmashauri wanadai stahiki zao; wengine wanadai malimbikizo ya mshahara baada ya kupanda cheo, lakini hawapati kwa muda mrefu. Hiyo ipo sana, na mimi mwenyewe ni mfano halisi nikiwa mtumishi wa Serikali, nilipokuwa Serikalini, nilifanya kazi, nikapanda cheo, lakini nilikaa zaidi ya miaka sita bila kulipwa arrears. Hiyo inashusha morali na ari ya kufanya kazi. Kwa sababu hiyo ni haki yao, tunaomba TAMISEMI na Serikaki kiujumla iangalie eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kuna wafanyakazi wengine wanahamishwa; kwa mfano, anahamishwa kutoka Wilaya ya Buchosha unampelewa Wilaya nyingine. Mtumishi huyu ana familia na mizigo yake, anatakiwa alipwe stahiki yake, lakini unamwambia aripoti ndani ya siku saba au siku 14 aende pale lakini fedha yake haumlipi, anaendaje kule? Hii nayo inashusha morali ya kufanya kazi vizuri. Tunaomba wafanyakazi hawa walipwe stahiki zao vizuri ili waweze kufanya kazi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kunipa pumzi ya uhai, pia nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi zake anazozifanya kwa kasi Sana kwa kipindi kifupi, aidha nikupongeze wewe kwa kuendesha Bunge letu kwa weledi mkubwa pasipo kupindapinda.
Mheshimiwa Spika, naomba kupongeza pia juhudi za Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Jenerali Jacob John Mkunda, pia nampongeza Luteni Jenerali Salum Haji Othman kwa kupandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi letu.
Mheshimiwa Spika, nina ombi kwa Serikali yetu Sikivu, kuna maeneo katika Wilaya ya Nachingwea ambayo baada ya ku- review mipaka ya Kikosi cha Jeshi Majimaji yalichukua maeneo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na wananchi wa Nampemba kwa miaka yote tangu enzi za mababu na mababu.
Mheshimiwa Spika, maeneo yale wazee wetu wengi wameweka mashamba ya mikorosho ambayo yanawapatia riziki kwa miaka yote. Ombi langu kwa Serikali kwa kuwa wameyachukua yale maeneo na watu wameyahudumia na kuwa tegemeo la maisha yao, naomba sana wale watu wafikiriwe wapewe hata kifuta jasho kwa kuwa maeneo hayo yalikuwa ni tegemeo kwa maisha yao.
Mheshimiwa Spika, ombi lingine ni kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya JKT Nachingwea; maeneo kama ya Mapochelo, Mkukwe na mengineyo nao pia wameathirika sana baada ya kupanua na ku-review maeneo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Nachingwea niombe sana Serikali yetu ijitahidi kuwapa kifuta jasho wananchi wale.
Mheshimiwa Spika, wananchi wale yale maeneo yalikuwa ni tegemeo lao katika kuendesha maisha yao, niombe sana wananchi hawa wa maeneo haya ambayo nimeyataja wapewe kifuta jasho ili waweze kwenda kutafuta maeneo mengine ya mashamba kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
Mheshimiwa Spika, najua Serikali yetu ni sikivu ijitahidi kuwasaidia wananchi wale wako kwenye hali mbaya sana.
Mheshimiwa Spika, ombi langu lingine ninaomba Kikosi cha Jeshi Farm Seventeen kilitunza viongozi wengi sana waliokuwa wanapigania uhuru nchi za Kusini mwa Bara la Afrika, niombe Serikali yetu ikumbuke maeneo yale kufanya matengenezo na marekebisho kwa kuwa yamekuwa machakavu sana.
Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi ya kuchangia hoja ya mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, na wote tuliopo humu ndani tumepewa uhai na Mwenyezi Mungu, tunatakiwa tumshukuru wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuendeleza miradi mbalimbali ya zamani na kuanzisha miradi mipya. Kwanza kuna miradi ya kuchochea uchumi; pili, kuna miradi ya huduma za jamii. Mama huyu amefanya kazi kubwa na kazi zote zinaonekana, mama huyu tumpe maua yake kwa kweli. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha, kwa kazi zao nzuri ambazo wamezifanya kwa kutuletea bajeti yenye mashiko. Bajeti hii ni bajeti nzuri ambayo inakidhi kwa mwananchi wa kawaida, kwa kweli ni bajeti nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi tunampongeza na kumshukru sana mama Dkt. Samia kwa mradi wa EPC+F wa barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale. Barabara hii kwa kweli kila siku nilikuwa nikiinuka, nikisimama hapa nalia na hii barabara. Maswali yangu ya msingi kila siku ilikuwa ni hii barabara. Lakini tunamshukuru sana mama huyu kwa kutukubalia sisi watu wa Mkoa wa Lindi, tumesaini mkataba tarehe 16 Juni; kwa kweli tunashukuru sana, mama ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunamshukuru mama Dkt. Samia kwa kutuletea Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko. Tunashukuru sana, kazi zimeanza kufanywa pale, hatua za mwanzo za ujenzi zinaendelea; tunamshukuru sana mama Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kwenye maeneo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna wastaafu kwenda kuhakikiwa mkoani. Sisi wote hapa, asilimia kubwa sisi ni wastaafu, tuko hapa ndani wastaafu wa Serikali. Tunajua kuna wastaafu wengine walistaafu miaka mingi, hali zao za uchumi ni mbaya. Fedha wanayopata ni ndogo sana. inakuaje hili suala la kuhakikiwa kila mwaka watoke kule vijijini wapite wilaya, waende mkoani? Kitu gani kinashindikana Wizara ya Fedha kufanya utaratibu wakafuatwa kwenye wilaya zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hela walizokuwa nazo za mafao yao ni ndogo sana jamani. Niombe sana, kwa mfano umtoe mtu wa Kilima Rondo afike Nachingwea, aende Lindi, aisee, ni mbali sana. Umtoe mtu wa Kilwa huko ndani ndani, afike mjini, aende Lindi, nafikiri hii siyo sawa. Hebu tufanye marekebisho watumishi waende kila wilaya kuwasaidia hawa watu kuhakiki taarifa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kulizungumzia ni ajira ya maafisa ustawi wa jamii, siyo maendeleo ya jamii, maafisa ustawi wa jamii. Sasa hivi kuna matatizo sana ya afya ya akili, watu wengi kutokana na msongo wa mawazo wamekuwa na matatizo ya afya ya akili. Lakini cha kushangaza kwenye nchi yetu hawa maafisa ustawi wa jamii wako wachache sana. Mbaya zaidi hao wachache waliokuwepo wanapewa kazi za maendeleo ya jamii kuzifanya badala ya kazi za ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ndiyo consultants ambao wanatakiwa kuwasaidia watu wenye msongo, watu wenye matatizo ya afya ya akili. Sasa inakuaje badala ya kufanya kazi zao au watu wengine waongezeke, wale wanakwenda kufanya kazi za maendeleo ya jamii? Nafikiri hii siyo sawa. Kwanza tujitahidi maafisa ustawi wa jamii waajiriwe wa kutosha, waongezeke, wako wachache sana. Wale ni watu hot cake, wanatakiwa sana kwa matatizo tuliyokuwa nayo kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine kwa Serikali ni kwa ajili ya tembo. Huyu tembo huyu, kwa jina lingine ndovu, anatuchanganya sana akili. Naona maeneo mengi ya Tanzania wanalalamika kuhusu ndovu. Sasa huko kwetu Mkoa wa Lindi ndiyo kichekesho, maana yake sasa imekuwa ni too much, mpaka saa 12 asubuhi wako nyumbani kwa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekula mazao yote mashambani yamekwisha, wanachofanya sasa hivi wanabomoa nyumba za watu. Juzi kuamkia jana kuna Kijiji kinaitwa Nambalapala huko Wilaya ya Nachingwea, wameingia ndovu wametafuta mashambani mtama, wameshamaliza kila kitu, kilichofuatia wamekwenda kubomoa nyumba kutafuta vyakula ndani. Hivi sasa tutakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, nitoe ushauri wangu mdogo kama wataweza kuusikiliza ili tunusuru wananchi wa Tanzania. Naomba tuweke solar electric fences. Kuna nchi mbalimbali ambazo wamefanya hiki kitu kama India, South Africa, hata hapo Kenya kidogo wameanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoijua Serikali yetu inaweza hiki kitu. Kama tumeweza kuweka umeme sasa hivi tunategemea kila kijiji kutakuwa na umeme, sidhani kama tutashindwa kuweka hiki kitu. Kwa sabbu hizi solar electric fences siyo kila sehemu, ni sehemu zile ambazo zinazungukwa na mbuga za wanyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi solar electric fences zikifungwa vizuri, mnyama yeyote hawezi kuvuka. Wanavyotengeneza pale yule mnyama akisogelea tu karibu na ile fensi kuna kashoti fulani kanatokea, mnyama anaogopa, anarudi ndani. Niombe sana Serikali yangu, najua hii Serikali ni sikivu – iweke hizi solar electric fences kwenye mbuga za wanyama ili kunusuru wananchi hawa ambao tunasumbuliwa na tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yaliyochukuliwa na vikosi vya jeshi 41KJ Nachingwea na kikosi cha JKT hapohapo Nachingwea. Kulikuwa na mashamba ya muda mefu ambayo yanahudumiwa na wananchi pale tangu mababu na mabibi zetu wanahudumia yale mashamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali yetu sikivu iwalipe kiinua mgongo angalau wale watu wapate pesa za kwenda kuanzia sehemu nyingine kununua mashamba. Hali ni mbaya, watu hawana uwezo wa kununua mashamba, hela imekuwa ngumu, ndovu ndiyo kama hao, vyakula mashambani hakuna, hali ni mbaya. Tunaomba wasaidiwe watu hawa walipwe ili waweze kusaidiwa kupata hela kwenda kununua maeneo mengine. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Chinguile, karibu.
TAARIFA
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza sasa kwamba haya maeneo ambayo wananchi wana mgogoro na Jeshi letu la Wananchi, siyo tu kwamba wanapaswa kulipwa, maeneo haya kumekuja na taarifa mbili tofauti. Taarifa za awali ni kwamba walielekezwa watapata malipo, lakini taarifa nyingine walivyokuja maafisa wengine wa Jeshi wakaeleza kwamba eneo hili hawatalipwa. Kwa hiyo kwa sasa wananchi wamebaki bila kujua hatma yao ni nini. Naomba kumpa taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, taarifa unaipokea?
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matengenezo ya viwanja vya ndege; Kiwanja cha Ndege cha Lindi Mjini na Nachingwea. Tunaomba viwanja vile vitengenezwe. Nimeangalia kwenye bajeti sijaona, sijui labda kama macho yangu yamekuwa yana matatizo. Tunaomba viwanja hivi vitengenezwe kwa sababu sasa hivi tunategemea mradi mkubwa sana wa gesi pale Lindi tusije tukatia aibu viwanja vikiwa vibaya jamani. Tunaomba tuangaliwe kwa macho mawili, tutengenezewe viwanja hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia pia suala la ofisi za CAG. Kila mwaka na kila siku tunazungumza masuala haya, tukiangalia kwenye ripoti za CAG makosa mara nyingi ni yaleyale yanajirudia kila mwaka. Leo utaona kosa hili, ikija ripoti ya mwakani kosa ni hilohilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipendekeze kitu kimoja; hawa ma-internal auditors walioko kule nafikiri wanashindwa kufanya vizuri kazi zao. Ombi langu kwa Serikali, hawa maafisa wa CAG sasa wapelekwe kila Wizara ili waende kushauri kule na kupunguza haya matatizo. Tupunguze hoja nyingi zinazojirudia kila siku kuja Bungeni. Tunaona makosa yanayotokea kwenye ripoti zile za CAG kila siku yanarudi yaleyale. Mnashauri vizuri, Bunge tunakaa tunashauri lakini inapokuja ripoti ya mwaka mwingine yaleyale tena. Sasa inakuaje?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi kuchangia hoja katika Serikali za Mitaa, sehemu ya kwanza napenda kuchangia ni uhamisho wa watumishi wa Serikali za Mitaa kumekuwa na matatizo sana la watumishi wa Serikali za Mitaa kuhama kwa suala kubwa hili la kubadilishana hilo suala limekuwa kizungumkuti.
Mheshimiwa Spika, kuna mtu ambaye nilikuwa namshughulikia kabisa mwenyewe aliniomba document zake nizishughulikie nimeangaika nazo muda mrefu karibu miaka miwili bila mafanikio na huyo mtu alishapata mtu wa kubadilishana naye na kulikuwa na nyaraka zote ambazo zilikuwa zinatakiwa kwa ajili yakubadilishana.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa kila siku naenda Mtumba kila baada ya siku mbili tatu lakini nikifika kule naambiwa document hazipo natoa kopi zingine naacha, nikika siku mbili nikienda tena naambiwa hizo document hazipo natoa copy nyingine naziacha pale, nimefuatilia hiyo issue karibu miaka miwili mpaka ilipofika kipindi cha kwenda kwenye kampeni nikaacha nikamwambia yule binti aje mwenyewe kibaya zaidi alivyokuja mwenyewe ndio yalitokea mambo ya ajabu sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia pale aliandikiwa barua feki ya uhamisho yule binti yangu alitaka kufukuzwa kazi alipokwenda kuripoti sehemu ambayo anatakiwa kwenda kuripoti walipofuatilia ile barua ilionekana ni feki. Kwa kweli matatizo yalikuwa makubwa sana, ikabidi niingilie kati yale mambo yakaisha akarudi kwenye kituo chake kilekile cha kwanza. Kwa hiyo, tunaomba TAMISEMI iangalie kitengo hicho cha uhamisho mambo yanayofanyika ni mabaya naya aibu sana tunaomba kuwaomba mjitahidi kurekebisha hapo Serikali yetu Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni eneo la watumishi wa afya na walimu kuna maeneo mengi katika mkoa wetu ya Lindi ni sehemu ambazo sio rafiki sana kwa kuishi, ni sehemu zenye mazingira magumu. Watumishi wanakwenda pale kwenda kuchukuwa cheki namba baada ya muda wanatafuta uhamisho kuhama kwenda sehemu nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba kuna watumishi vijana ambao wamemaliza chuo wako kwenye maeneo yale wameomba nafasi za kazi naomba wapewe kipaumbele wale vijana kuliko mkiwachukuwa watu ambao wanatoka maeneo ya mbali wanafika pale kuchukuwa cheki namba wanaondoka mfano halisi ni Wilaya ya Liwale, Nachingwea huko Kilimarondo kuna shida sana za watumishi na sehemu nyingi.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya tunacho kikubwa kizuri cha Kilimarondo lakini inakatisha tamaa watumishi wako 12 pale wanafanya operation zote wana huduma nyingi zote afya lakini hali ni ngumu. Kwanza hata jokofu lile la theatre hawana, hawana vifaa tiba, watumishi ni wachache. Na pia kuna hospitali zetu za wilaya kuna Hospitali ya Wilaya Nachingwea, ina hali mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hospitali ile ya Nachingwea haina vifaa tiba muhimu kwa mfano kuna wodi ya wazazi iliyopo pale haina kifaa hata kimoja ni jengo tu lipo pale mapambo lakini hakuna kifaa tiba kwenye ile theatre na theatre kubwa iliyopo katika Wilaya ile ya Nachingwea haina hata zile taa hakuna hata washing machine vitanda ni vya kizamani vimechakaa sana, tunaomba Waziri husika atupie macho hospitali za Mkoa wa Lindi zaidi zile zilizopo pembezoni na Vituo vya Afya ili waweze kusaidia wananchi wa kule wapate huduma stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo tunaliomba kwako kwa hawa watumishi ambao wanakwenda kwenye sehemu mazingira magumu tunaomba iweke posho kwa watu wale ahsante naomba kuchangia hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi kwanza napenda Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na sisi wote kuwa hai kwa siku hii ya leo. (Makofi)
Napenda pia kumpaongeza Rais wetu mpenzi Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na timu yake yote. Pia napongeza Waziri wa Ulinzi kwa hotuba yake nzuri ambayo ametusomea leo asubuhi, kwa kweli imeshiba, inapendeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa Lindi, kule kwetu Lindi na Mtwara tupo mpakani kabisa, mwaka jana kuanzia mwezi wa sita/wa saba mpaka kumi kidogo tuliishi kwa mashaka. Watu walikuwa hawawzi kufanya kazi zao, kazi kubwa ambayo inafanywa na wakazi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni uvuvi na kilimo. Kipindi kile watu walikuwa wanashindwa kwenda mashambani kwao kwa sababu kuna watu waliingia ambao sio watu wazuri kutoka kwenye nchi za wenzetu japokuwa siwezi nikasema ni nchi gani, lakini inaonekana kuna watu waliingia wakawa wanafanya matendo ambayo hayafurahishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nashukuru sana nilipongeze Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania walichukua jitihada za haraka wakatuma vikosi vya Jeshi kwenye mipaka ile na ulinzi uliimarishwa, hatimaye hali ikarejea vizuri sana kwa kweli tunawapongeza sana tunasema ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Lindi na Mtwara kwa sasa wanaamani wanaendelea na kufanya kazi zao na tunaona bajeti iliyowekwa hapa tunaomba ipitishwe tu kwakweli tusishike shilingi ipitishwe vizuri kwa sababu wanaonesha wanania ya kulinda mipaka na walilinda mipaka ipasavyo, tunaomba bajeti yao iende vizuri ili kazi iendelee kusiwe na mkwamo wowote wa ulinzi na usalama wa mipaka yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni suala la nyumba za wanajeshi, katika Wilaya ya Nachingwea kuna kikosi cha Jeshi kinaitwa Majimaji na Old Camp, nyumba zilizopo pale ukiziona kwa kweli zinakatisha tamaa na ukiambiwa wanaishi watu/wanajeshi kwa kweli inatisha. Ombi langu kwa Serikali kwa Wizara ya Ulinzi mfanye marekebisho ya zile nyumba ili watu wanaoishi mle wajisikie ni watu kama watu wengine wanaishi vizuri, zile nyumba zimechoka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine nililonalo kwa Wizara ya Ulinzi ni ofisi zao, nimeshaingia kwenye ofisi zao mara nyingi hata pale Kikosi cha Mgulani ofisi zao kwa kweli haziko vizuri. Tunaomba Waziri wa Ulinzi ulichukuwe hilo ujaribu kuangalia kuboresha ofisi za jeshi kwa sababu zile ni ofisi kama zilivyo ofisi nyingine, tunaomba uboreshe ziwe vizuri ili na wao wafanye kazi vizuri, wajisikie wanapotimiza majukumu yao ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine napenda kuliongelea ni kuhusu barabara za mipakani. Wabunge wengi wameongelea hizo barabara, tunashukuru Serikali yetu kupitia Wizara ya Ujenzi wamejitahidi kutengeneza barabara hizo. Ila tunaomba tunatia msisistizo kwamba barabara zile ziendelee kuimarishwa ili ziwe vizuri hata kama kukitokea suala lolote kusiwe na tatizo jinsi ya kupita kwenye zile barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sina mengi ya kuongea kwenye Wizara hii ila ombi langu naomba tusishike shilingi tuwaache Wizara hii wapewe pesa zao vizuri ili waweze kufanya majukumu yao vizuri, kwa kweli wanajitahidi, wanafanya kazi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii nyeti sana ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kutoa shukrani zangu za dhati na pongezi nyingi sana kwa Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi yao nzuri ambayo wameifanya kupitia kwa Mwenyekiti wake na wajumbe wote kwa kuishauri vizuri Wizara hii ya Nishati na mpaka inaendelea kufanya vizuri kwa sasa. Pia napenda kumpa pongezi nyingi sana Mheshimiwa Kalemani, Msaidizi wake na Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kalemani kwa kweli ni mtu ambaye ni msikivu, anajitahidi sana kutusikiliza. Mimi nimemsumbua mara nyingi sana lakini namshukuru Mungu kila napomuendea kwa suala linalohusu TANESCO na mambo mengine ya Wizara yake, huwa ananijali na huwa tunampigia simu Meneja wa TANESCO na matatizo yote tunayaongelea vizuri. Kwa kweli, Mungu akubariki Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati kwenye eneo la umeme ni Wizara nyeti sana. Umeme ni kitu cha msingi sana kwenye maendeleo kwenye nchi yoyote. Tunashukuru mmeweka umeme wa REA sehemu nyingi sana kwenye vijiji vyetu. Ombi langu ambalo bado liko kwenu umeme wa Mkoa wa Lindi haueleweki au hauaminiki kwani unakatika sana mara kwa mara. Ndani ya dakika 20 au 10 umeme lazima ukatike, hauwezi ukanunua vitu ukaweka kwenye friji vikakaa salama, itakuwa ni uongo vile vitu vinaharibika. Kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa mmesema kukuza ushiriki wa sekta binafsi kwenye maendeleo ya kiuchumi kwa kweli tunatakiwa tujitahidi kwa sababu kuna watu wengi wamejiajiri kupitia kazi hizi za umeme lakini wanashindwa kufanya kazi zao vizuri kwa kuwa umeme huu hauko stable. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru Mheshimiwa Kalemani amesaidia sana kwenye Mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa. Inaonekana kweli kuna mafanikio lakini naomba uongeze nguvu kwa sababu ile kasi ya kuzimika sana imepungua lakini bado unaendelea kuzimikazimika. Naomba Waziri atusaidie ili wananchi wale waweze kufaidi huduma hii ya umeme na wao wajisikie vizuri waone kama vile walivyo watu wa Dodoma wanavyofaidi umeme wao. Sisi wananchi wa Lindi tungefurahi sana tupate umeme kama huu wa Dodoma ili tuweze kujisikia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia kwenye Wizara ya Nishati ni kuhusu gesi asilia. Gesi asilia ni muhimu sana kwa sisi wananchi wa Tanzania hasa wenye kipato cha chini ili iweze kutusaidia. Tunaomba sana hii gesi asilia ingeanza kutumika vizuri na pia isambazwe sehemu zote vizuri sana ili iweze kusaidia. Matumizi ya gesi asilia ukiangalia gharama zake ni nafuu sana kuliko vitu vingine.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna magari yanayotumia gesi asilia sasa hivi, matumizi ya yale magari nimejaribu kuongea na wale wataalam yako chini sana karibu nusu ya gharama ya mafuta ya petroli tunayotumia sasa hivi. Kilo moja ya gesi asilia ni Sh.1500 ambayo inaweza kutumika kwa zaidi ya kilomita, samahani kidogo nimesahau lakini gharama yake ni chini zaidi ukilinganisha na petroli lita moja. Tunaomba Wizara hii ya Nishati ijitahidi sana kusambaza hizo gesi asilia na pia iweze kutoa elimu kuhusu matumizi ya gesi asilia ili Watanzania tuweze kufaidika na gesi yetu ambayo iko katika nchi yetu ya Tanzania zaidi Mikoa ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa karibuni kulitokea tatizo la LUKU kwenye ununuzi wa umeme. Tunashukuru Waziri wetu alifanya jitihada na tuliona juhudi alizokuwa amefanya hali ikarejea. Hata hivyo, siku mbili, tatu za juzi mpaka jana ile hali imerudi tena kwa Mkoa wa Dodoma. Watu wengi wamejaribu kununua umeme wameshindwa lakini sasa hivi kuna watu nimewasiliana nao wanasema sasa hivi ile hali imeanza kurudi umeme umeanza kupatikana lakini kulikuwa na kama siku mbili tatizo lilirudia tena. Tunaomba Waziri wetu ambaye anajituma sana Mheshimiwa Kalemani ajaribu kuliangalia tena tatizo hili ili wananchi wako tuweze kuwa vizuri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kuweza kuchangia siku hii ya leo. Pia, namshukuru sana Rais wetu kipenzi mama Samia Hassan Suluhu kwa kazi yake nzuri aliyoifanya. Amemwaga fedha nyingi sana kwenye sehemu zetu za kazi kwa ajili ya afya na elimu. Tunamshukuru sana Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali zetu za Mkoa wa Lindi zimechakaa sana na zinakatisha tamaa. Kuna hospitali za wilaya ukifika pale huwezi ukaamini kama ni hospitali ya wilaya, hospitali zile ni kongwe na zimechakaa sana. Hospitali hizo zina matatizo mengi, kwanza hazina vifaa tiba, zina matatizo ya watumishi, wataalam mbalimbali hakuna. Kuna tatizo lingine la kukosekana kwa umeme, unazimika mara kwa mara. Tunaomba wapatiwe hata solar kwenye zile sehemu muhimu katika Hospitali hizo. Zaidi kwa mfano kuna Hospitali ya Nachingwea tunahitaji kupatiwa solar kwenye jengo la mama na mtoto, pia kuna tatizo la taa ile kubwa ya theatre hakuna kabisa kwenye hospitali ile. Ni Hospitali ya Wilaya lakini haina hicho kitu, taa ile kubwa ya theatre hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la ambulance, Wilaya nzima kuna ambulance moja ambayo iko kwenye Kituo cha Afya Kilimalondo, ni mbali sana kutoka pale Wilayani Nachingwea. Tunaomba sana sana tupate ambulance kwa sababu, kuna Ambulance ambayo ni mbovu zaidi ya miezi sita na haitengenezeki. Tunaomba sana watuangalie kwa jicho la pili tupate ambulance kwenye hospitali hiyo. Hakuna ukumbi wa mikutano, asubuhi kunakuwa na ile morning report, hakuna ukumbi wa kufanyia kile kitu, wanasimama tu wanapeana ripoti. Tunaomba watusaidie tupate ule ukumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wodi ya wanaume imechakaa sana, inakatisha tamaa. Hakuna kichomea taka kulingana na uwezo wa hospitali ile. Incinerator iliyopo ni ndogo sana tunaomba watusaidie tupate hiyo incinerator. Uzio wa Hospitali ya Nachingwea ule unakatisha tamaa, ni mbovu mbovu, mbovu mno. Tunaomba watusaidie tupate matengenezo ya hospitali hiyo. Pia, hakuna dental chair kwenye hospitali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Hospitali ya Liwale, katika hospitali hiyo tunashukuru wametuletea X-Ray, lakini X-Ray hiyo kuna mtaalam mmoja tu, akiumwa au akiwa na dharura yoyote au akienda likizo, hakuna huduma inayoendelea pale. Tunaomba tuongezewe wataalam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kuna hizi barabara. Barabara zinakatisha tamaa sana, kuna barabara ya kutoka Lupota kwenda Chingunduli, huwezi kupita imekufa ile barabara, inakatisha tamaa. Tunaomba watusaidie tutengenezewe hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi niliuliza swali kuhusu barabara ya Nanganga – Nachingwea – Masasi – Liwale, lakini bahati mbaya nimejibiwa jibu la Mkoa wa Mtwara barabara tofauti kabisa. Naomba sana tupate jibu la msingi baadaye kabla hawaja-wind up Wizara husika, hizo barabara tupate majibu ya msingi ili tujijue na sisi tuko katika sehemu gani. Wananchi wa kule tangu tumezaliwa na wengine mpaka wamekufa, hatuijui lami jamani, hatuijui lami, inasikitisha na barabara hizo ni za mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana watuangalie kwa jicho lingine, kwa jicho la huruma, barabara zinakatisha tamaa. Akinamama wajawazito wanajifungua njiani kwa kukosa barabara. Barabara na madaraja hakuna, tunaomba sana watusaidie, tunaomba sana TAMISEMI waangalie hilo suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la watumishi naomba niongee kidogo nieleweke. Watumishi wengi wanaoajiriwa wanaopelekwa Mkoa wa Lindi, wanakwenda kuchukua check number, then wanaomba uhamisho wanageuza. Matokeo yake kule kwetu kunakaa hakuna watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa hivi, kuna vijana wengi wanajitolea, kuna wanaojitolea nafasi za ualimu na nafasi zingine. Tunaomba sana wapewe kipaumbele wazawa wa kule kwa sababu wamezoea mazingira ya kule. Wakiajiriwa watu wa kule watakaa. Inasikitisha sana wanapoajiriwa watu wengi tunasema tuna watumishi, lakini baada ya muda mfupi watumishi wote wanakuwa wameshaondoka. Sijui ni kwa nini, sijui kunaonekana vipi kule kwetu. Tunaomba sana hili suala lipewe kipaumbele. Watumishi wakiajiriwa waanze kuajiriwa wazawa wa kule. Kwanza wana uchungu na kwao; pili wamezoea mazingira magumu watakaa. Naomba sana, haya masuala yaangaliwe sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nalirudia ni barabara, jamani barabara, barabara jamani, barabara za kwetu zinasikitisha. Tunaomba jamani watufikirie kwa barabara za kwetu na sisi wenzao ni binadamu pia, tunaomba. Barabara za kwetu ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini nasisitiza kuhusu suala la barabara. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja kwenye Wizara ya Elimu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi yake ya uhai na kufikia siku hii ya leo. Pia naomba nitoe sifa nyingi sana kwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa sana anazozionesha kwa upande wa elimu. Ameweka majengo mengi sana, madarasa ya kutosha, kwa kweli anastahili sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri wa Elimu, ndugu yangu Profesa Mkenda na Msaidizi wake na Katibu Mkuu, Dada Carolyne na wasaidizi wake, kwa kweli wanajitahidi wanafanya kazi kubwa sana. Tumeona mitaala hii iliyotoka, kwa kweli kazi yao inaonekana, tunaendelea kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu mambo yawe mazuri ili nasi tufaidi, na nchi yetu Tanzania iwe vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuunga mkono hoja zilizopo mbele yetu mezani. Pili, nawaunga mkono Wabunge wengi waliotoka kuongea, akiwepo dada Latifa sasa hivi. Mitaala hii mipya inayokuja, tujitahidi sana tuwekeze kwa walimu. Tusipowekeza kwa walimu tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Walimu wapewe semina, wapewe mafunzo mbalimbali, tuache tabia ya kuanza kubagua. Najua Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wake huko Wizarani hawana nia mbaya, lakini huku chini ukishuka, kuna mambo yanaendelea siyo mazuri. Kuna shule nyingine utakuta kuna mwalimu fulani na mwalimu fulani wanajua kila kizuri kitakachotokea wao wanakuwepo, kila semina itakayotokea watakuwepo, kwenye kusimamia mitihani, watakuwepo, lakini kuna baadhi ya walimu masikini wa Mungu wananyanyasika kama wao ajira yao walikuwa wameenda kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kutumia wafanyakazi wake walioko Wizarani, afuatilie vizuri haki itendeke kwa walimu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wakipata mafunzo vizuri na pia haki zao za msingi, naomba zikumbukwe. Wakati mwingine unaweza ukaenda kwenye shule za sekondari na za msingi, ukasikitika juu ya viti walimu wanavyokalia na meza. Kwa kweli wanakaa kwenye ofisi mbaya, viti vya ajabu, vimevunjika vunjika, meza ziko ovyo ovyo. Wakati huo tunawapa watoto wetu wawafundishe, unategemea watafanya kazi vizuri kweli! Basi tujitahidi. Kama mama yetu Rais alivyoleta majengo mazuri, na yale ya zamani tuyaboreshe na ofisi zao tuziboreshe. Tujitahidi. Tuweke agent ambaye atakwenda kurekebisha...
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa anayechangia kwamba ni kweli, walimu wanatakiwa waboreshewe mazingira, kwa sababu kuna shule nyingine, ofisi za walimu ziko chini ya mti. Yaani mvua ikinyesha, kila kitu kilichoko pale kinapeperuka. Kwa hiyo, waboreshewe mazingira, yaani wawe na ofisi ambazo zina furniture. Unakuta wakati mwingine walimu wengine wanabeba viti kutoka nyumbani wanaenda navyo mashuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuunga mkono mchangiaji kwamba Serikali iwajali walimu, maana yake ndio wanatengeneza wataalam mbalimbali, hivyo iwaboreshee maofisi na ikiwezekana wawekewe na AC kabisa ili wawe na fikra nzuri wanapofanya kazi hizi za ualimu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili taarifa hiyo, ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala moja, kuhusu Chuo Kikuu cha Iringa, ambacho zamani kiliitwa Tumaini University. Naomba Serikali yetu kwa kupitia Waziri wetu mpendwa, itupie macho mawili iangalie sana kile chuo, kina matatizo makubwa sana. Chuo hicho system yao ya kulipa ada na administration kwa ujumla iko weak so weak, haiko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo wa wahanga wa Chuo kile cha Tumaini cha zamani, sasa hivi kinaitwa Chuo Kikuu cha Iringa. Kuna watoto ambao walikuwa wanasoma pale walikuwa wamefanya malipo. Wanapofanya malipo, namba wanazopewa za kulipia, wanapewa na Wahasibu na watu wa IT, kumbe wanapewa namba fake za malipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazazi wengi tunajua hali zao kiuchumi. Watoto wamefanya malipo yale, kumbe malipo yale kulikuwa na makundi mawili; wengine hawakujua, walijua ndiyo namba halisi za kulipia, zaidi ni wale wa mwanzo mwanzo, lakini kuna wengine walikuwa wamekaa na hao baadhi ya wahasibu, wakaamua ku-fake yale malipo yakalipwa. Ilipofika kipindi cha kufanya mitihani, watoto wengi wakaanza kudaiwa. Wale ambao walikuwa wahawajui, wakasema tumelipa, wakapeleka risiti zao, lakini ikaonekana zile akaunti walizolipia ni fake. Baada ya kufuatilia mpaka wazazi, wakaamua wawaruhusu wafanye mitihani lakini wakaambiwa matokeo yenu yatazuiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli matokeo yalizuiliwa, baadaye uongozi wa chuo ukaanza kufuatilia tatizo ni nini kwa kuwaambia wanafunzi waliopata changamoto hiyo ambao ni zaidi ya 40, (na orodha ninayo Mheshimiwa Waziri nitakupatia), kwamba waandike barua za maelezo za kujieleza. Wanafunzi wale waliandika barua za kujieleza. Kweli kuna wengine walikuwa hawajui kinachoendelea, walioamua ku-tamper ni baadhi ya wafanyakazi ambao sio waaminifu. Kuna wengine baada ya kufungiwa matokeo yao, wakaambiwa tu wewe ume-sup somo fulani na somo fulani unatakiwa uje urudie mtihani, lakini kwenye mtihani unatakiwa ulipie tena ada kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri, mtu kama mimi, angalau namshukuru Mungu nina uwezo wa kulipia ile ada mara ya pili: Je, yule mkulima au yule mama aliyeko kule ndani na baba aliyeko kule ndani wenye uwezo wa chini, wana uwezo wa kulipia kweli mara ya pili jamani? Hiyo ni haki kweli kwa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, walipofanya vile, watu wengine wakalipia, mmojawapo ni mimi nikalipia mara ya pili. Baada ya kulipia mara ya pili, tena niliwafuatilia sana kutaka wanipe hiyo akaunti hiyo ya uhakika. Nilisumbuana nao kwa muda mrefu sana, mpaka nikaamua kumshirikisha rafiki yangu Mheshimiwa Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini anisaidie. Baada ya kulipia mara ya pili, hawakutaka kufungua matokeo ya Watoto. Ilivyoanza semester nyingine, tukaanza kuwasiliana nao kusumbua, kwamba mlisema tulipie mara ya pili, tumeshalipia, mbona hatuelewi kinachoendelea? Majibu yao ni kwenye simu, “mtoto wako amefaulu aje.” Matokeo yako wapi? Tutajuaje kama amefau? “Aje baada ya kufanya marudio ya mitihani anafaulu tu, aje tutakupa matokeo baadae.” Sasa unajua ukifuatilia muda mrefu kila siku unaona kama utakuwa ni kero unaamua umruhusu mwanafunzi nenda chuo ukasome. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunafanya ufuatiliaji pale chuoni kwa Mkuu wa chuo, unapewa namba ya Mhasibu, unapewa namba ya Mwanasheria yaani tuna namba kibao za pale Chuo Kikuu cha Iringa. Tukiwasiliana nao wanapiga dana dana “sasa hivi lipeni hela tu ya hostel msilipe ada lakini mtoto atasoma”. Anasoma vipi? Basi tukaona tuwasikilize wao walichosema. Wazazi wakalipia hostel wanawapa na watoto hela za chakula lakini coursework zao hazirekodiwi wala hawajasajiliwa. Tukawa tunafuatilia kila siku muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni walipoona tunafuatilia sana wakasema “senate haijakaa kutoa majibu japokuwa walishafaulu subirini msiwe na wasiwasi majibu yatatoka”. Ni lini? Baada ya kuona nimemshirikisha Mbunge wa Iringa, wakaanza kushtuka sasa, wakaanza ku-forge barua ku-backdate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina barua hapa na baadae nitaomba nimpatie Waziri wa Elimu. Wakiwa wanaandika barua hii ambayo imeandikwa tarehe 5 Desemba, 2022 wakati nimeulizia mpaka Machi wakawa wanasema bado senate haijakaa, wamejisahau wamenijibu hivyo. Pia, wakasema kwamba kikao kilichokaa tarehe 14 Octoba, 2022 kimeamua Kumfukuza huyo mwanafunzi. Naomba ninukuu hivi “This is to inform you that based on your abscondment from studies, The university Senate sitting on 14th October 2022. Wakati waliniambia hizo tarehe mpaka Machi mwaka huu nawasiliana nao wakasema bado senate haijakaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakasema kwamba unaweza ku – appeal before 10th January 2023. Wakati huo wanasema unaweza ku – appeal before hiyo ni Machi nimewasiliana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barua ni halali, forgery au ni nini? Ina maana kwenye ofisi nyingine bado mpaka sasa hivi kuna forgery za ajabu namna hii kweli? (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha?
MWENYEKITI: Ndio, kengele imelia mara ya pili.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nitaonana na Mheshimiwa Waziri wa Elimu kumpatia documents zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuongelea Bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai wake na pia tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu kwa miradi ambayo ametuletea pesa nyingi katika nchi yetu na miradi hiyo inaendelea. Tunampongeza sana na tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Waziri Mkuu, tumeiona iko vizuri sana. Tunashukuru imekwenda vizuri na waliofanya kazi, kwa kweli wamechakata wamefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina nyongeza ya mambo ya msingi sana yanayoendelea, lakini hayana matokeo mazuri. Naongea kwa masikitiko makubwa sana na maumivu makubwa sana kutoka moyoni mwangu. Wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Nachingwea wanavyouawa na wanyama tembo. Ukienda kwenye mashamba ya wananchi wale utatoa machozi, utalia njaa itakayotokea sasa hivi ni kubwa mno. Tuna vijiji vingi ukienda maeneo yanaitwa Nditi, Namapwiya, Ngumichile, Mbute, Nyambi, Mwandila, Matekwe, Majonanga na ukienda Liwale; Kibutuka, Mkutano, Lilombe na Kilangala inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya wamepelekwa Askari Wanyamapori wachache. Hivi kwa hali ya kawaida kwenye shamba wakiingia tembo hamsini kwa mara moja hawa askari wetu wawili, watatu wataweza kufanya ile kazi kweli? Wataweza kweli? Hali ni mbaya. Mwisho juzi kuamkia jana kuna kijana amefariki ameuawa na tembo mchana kweupe katika maeneo ya Mwinyichile saa tisa mchana, amejitoa nyumbani akasema akaangalie shamba lake kama limebakia mahindi kidogo au alizeti, amefika kule yeye ndiye wamemfanya chakula inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea ingetokea hali ya dharura, ya tahadhari ya haraka ya kupeleka helikopta, lakini tumelizungumzia sana. Haijapelekwa helikopta kufukuza wanyama wale mpaka leo lakini angeuawa ndovu mmoja ingeenda helikopta na maaskari pale kwenda kuwaletea vurugu wananchi, inasikitisha sana hii hali, inasikitisha mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza na wananchi wa kule wanajiuliza ndovu na binadamu nani ni muhimu? Inafikia wakati wanasema mtapigiwa kura na ndovu, siyo kwamba wanaongea vile kwa kutulaghai ni hatua na uchungu waliokuwa nao. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya Mhata, taarifa.
TAARIFA
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la tembo kwa kweli ni la hatari sana. Hata Jimboni kwangu tembo ni tatizo, kwa hiyo namuunga mkono kabisa mzungumzaji. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Maimuna taarifa unaipokea?
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Hali ni mbaya. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, nimeona kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Pallangyo.
TAARIFA
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji pia kwamba kule kwetu Arumeru Mashariki, Kijiji cha Kilinga, tembo wamehamia kwenye nyumba za wananchi. Hali ni mbaya sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi hali ya dharura ingetokea, kwa sababu ndovu wanaoingia kwenye shamba moja ni zaidi ya Hamsini, wanapelekwa askari wawili, watatu wanashindwa wanakimbia na wao wanaondoka. Wabunge wenzangu na viongozi mbalimbali wameripoti hicho kitu mara chungu nzima, tulitegemea wangeleta helikopta kufukuza wale wanyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali iko tofauti. Tunajiuliza wangeuawa ndovu wawili pale pangetulia vile, wananchi wetu wangepona kweli? Inasikitisha sana. Tunaomba…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, kuna wahanga wananchi wetu wa Wilaya ya Kilwa Masoko na wa Nachingwea kulikuwa na upanuzi wa viwanja vya ndege, walitwaliwa maeneo yao, ni siku nyingi, lakini mpaka sasa hivi hawajawapa pesa zao. Hiyo hali inakatisha tamaa na inarudisha maendeleo. Pia kuna barabara hii ya Masasi – Nachingwea – Liwale. Hii Barabara tangu 2015 kila siku tunaambiwa ipo kwenye upembuzi yakinifu, kila siku tuaambiwa inajengwa, kwani hii keki ya Taifa na sisi pia hatuitaki? Tugawane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba na sisi barabara ile ni ya muhimu ni ya kimkakati ile barabara itengenezwe. Jamani ikinyesha mvua dakika kumi tu, huwezi kupita ile barabara.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, endelea na mchango wako.
MHE MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtuangalie kwa jicho la huruma. Kuna akinamama, kuna vitu vingi, kilimo kikubwa kule kinaendelea, lakini hatuna barabara, lami hatuijui kule kwetu. Watu wanazaliwa mpaka wanakufa. Tunaomba watusaidie tuwekewe lami barabara ile, kila siku tunapigwa danadana na maelekezo, lakini ilani haitekelezeki, ni kwa nini hii huku tu? Tunaomba watusaidie barabara itengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna migogoro ya wafugaji na wakulima. Hali ni mbaya, kuna watu wanauawa, tuna uhakika na tuna uthibitisho watu wameuawa na wafugaji. Tunaomba watusaidie, hali ni mbaya ni mbaya sana, kwa hiyo hakuna amani, hakujatulia watusaidie wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba malambo kwa ajili ya mifugo, Mheshimiwa Dkt. Samia, aliahidi yafufuliwe yatengenezwe tunaomba tusaidiwe kwa Mkoa wa Lindi, hakuna kabisa malambo hali ni mbaya. Pia tunaomba na scheme za umwagiliaji kwa sababu kilimo cha sasa hivi mvua haziaminiki. Mabadiliko ya hali ya hewa ni kila siku, tunaomba tusaidiwe tupate na scheme za umwagiliaji ili vijana wetu waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mikoa ya Kusini karanga na alizeti zinastawi sana lakini wananchi wa kule wanashindwa kulima vizuri kwa sababu hawana mbegu nzuri. Tunaomba Serikali sikivu ilete mbegu na wataalam kule wa kuweza kuwaelewesha wale ndugu zetu kilimo cha karanga na alizeti. Pale Nachingwea kuna maeneo yalikuwa yanaitwa farm one mpaka farm 17, yale maeneo yalikuwa maeneo mazuri sana kwa ukulima wa karanga. Zilikuwa zinatoka karanga nzuri sana lakini sasa hivi watu wakilima hakuna, tunaomba Serikali yetu sikivu itusaidie tupate mbegu nzuri na tupate na Wagani waweze kuwaelimisha watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kuwa na afya njema kuweza kuhudhuria Bunge lako Tukufu. Pia nashukuwa nafasi hii kumpongeza Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Mawaziri wa Wizara ya Ujenzi na Manaibu na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya, hakika wanajitahidi na kazi wanazichapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Wizara ya Ujenzi jambo la kwanza linazungumzia mambo ya viwanja vya ndege. Kwa Mkoa wangu wa Lindi kuna viwanja viwili vya ndege kiwanja cha Lindi Mjini na Kiwanja cha Nachingwea. Viwanja hivi ni muhimu sana kwa kuwa Mkoa wa Lindi uko mpakani mwa Tanzania. Mikoa hii ya pembezoni ni muhimu sana barabara na viwanja vya ndege viwe vizuri kwa ajili ya usalama wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Kiwanja cha Ndege cha Lindi kiwekewa lami na Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea kifanyiwe matengenezo kwa haraka. Pia kuna wananchi wengi wa Nachingwea walitoa viwanja vyao na maeneo yao Mei, 2018, wananchi hao walikuwa 107, kupisha mwendelezo wa viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kwamba imepita miaka minne na huu unaingia mwaka wa tano wananchi wale hawajapewa haki yao, wananchi wale walikuwa wanalima pale, wanafanya mambo yao mengi ya maendeleo yao na haki zao za msingi zipo kwenye maeneo yale. Serikali wanaposhikilia maeneo yale mpaka leo miaka mitano haijawa-compensate wale wananchi kwa kweli hatuwatendei haki. Naiomba Serikali, najua Waziri wa Ujenzi na Naibu Waziri ni wachapa kazi, naomba walichukue hili wawalipe wananchi wale kwa maeneo yao waliyoyatoa kwa ajili ya kupisha viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie masuala ya barabara. Ninapoongelea suala la barabara Mkoa wa Lindi naanza nachanganyikiwa sana. Mikoa mingi ya pembezoni tulisahaulika sana zaidi Mikoa ya Kusini, hilo nitaliongea wazi kama walivyokuwa wamechangia Wabunge wengine wa Mkoa wa Mtwara na wengine, Mkoa wa Lindi tulisahaulika katika barabara nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani kwa Wizara ya Ujenzi, kuna baadhi ya barabara tumeziona zimewekwa kwenye na bajeti, lakini kuna barabara zingine hatujaziona. Kuna barabara ya Njia Nne - Tingi kwenda Kipatimu, hii barabara ni kilomita 50. Hii barabara ni ya muhimu sana, inapita kwenye Milima ya Matumbi kwenye Pori la Akiba la Selous na ni ya kimkakati na barabara ile iko kwenye milima, barabara ni mbaya sana, kwa uchumi wa nchi yetu hii barabara ni muhimu kwa ajili ya utalii. Tunaomba barabara hii itengenezwa, imetegenezwa kilomita 1.4, sawa tunaishukuru Serikali, lakini bado kilomita 48.6. Tunaomba Wizara iiweke kwenye bajeti ili itengenezwe barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani kwa Wizara ya Ujenzi, kuna baadhi ya barabara tumeziona zimewekwa kwenye na bajeti lakini kuna barabara zingine hatujaziona. Barabara ya njia Nne Tingi kwenda Kipatimo hii barabara ni Km 50, barabara ni ya muhimu sana inapita kwenye milima ya Matumbi kwenye pori la akiba la Selous hii barabara ni ya kimkakati na iko kwenye milima ni mbaya sana, kwa uchumi wa nchi yetu hii barabara ni muhimu kwa ajili ya utalii tunaomba hii barabara itengenezwa, imetegenezwa kilomita 1.4 sawa tunaishukuru Serikali lakini bado kilomita 48.6 tunaomba muiweke kwenye bajeti itengenezwe barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni muhimu sana kwa kumbukumbu na Vita ya Maji Maji tunaomba muikumbuke. Pia kuna barabara nyingine ya Nachingwea - Nanganga kilomita 40, barabara hii ni muhimu lakini nimesikitika sana kwenye bajeti hii sijaona kutengewa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru barabara ya Nanganga kwenda Ruangwa - Nachingwea, Nachingwea - Masasi tayari imewekewa bajeti, kwa kweli niwashukuru sana Wizara ya Ujenzi. Barabara ya Nanganga - Nachingwea ni muhimu sana naomba muifikirie. Pia kuna barabara ya Nachingwea kwenda Liwale nikianza kuongelea hii barabara nachanganyikiwa, barabara hii ni kilomita 130 ni barabara mbovu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara hata ikinyesha mvua ya dakika tano tu ile barabara uwezi kupita, barabara ile ni mbaya, barabara ile inakatisha tamaa, tunaomba mtukumbuke barabara ya Nachingwea - Liwale itengenezwe, barabara ile ni ya mkakati, kule Liwale kuna Kilimo kinaendelea, kuna Mbuga tunapita pale katikati, jamani tunaomba barabara hii ifikiriwe, barabara hii tunapiga kelele kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nachingwea alishaiombea barabara hiyo sana siyo mara moja, Mheshimiwa Chinguile, Mheshimiwa Kuchauka amesema mara chungu nzima kuhusu hiyo barabara, jamani tunaomba barabara ile tutengenezewe, barabara ile ni muhimu na ni ya mkakati sana. Barabara hiyo wananchi wa kule kwanza hawaijuwi lami, tangia wamezaliwa na wengine mpaka wanakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara zingine zilishatengenezwa lakini baadaye zimekuja kufanyiwa matengenezo mara ya pili, yaani zina lami lakini wanakwangua wanaweka lami ya pili, jamani Tanzania hii moja tufikiriane, jamani na sisi tuomba lami na sisi tunasikitika wananchi wetu kule hatujui lami, kama mnakwangua barabara zingine manarudia kuweka lami ya pili, kwa nini sisi hata ile barabara ya kwanza hamtuwekei lami jamani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Lindi, naomba mtufikirie sisi tulioko pembezoni, kwanza kuna Kambi za Jeshi kubwa za muhimu sana kwa ajili ya usalama zile kambi kubwa za Nachingwea Lindi kunatakiwa kuwe na barabara nzuri kwa kweli na viwanja vya ndege vizuri, suala lolote linaweza likatokea, kule ni mpakani bila kuwa na barabara nzuri ni changamoto jamani, kuna akina Mama wanafia njiani, watoto wanafia njiani kwa ajili ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siyo mruka sarakasi wala mimi sifanya kitu, lakini najua Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan ni msikivu naomba watufikirie watu wa Mikoa ya Kusini zaidi pembezoni huku Mikoa ya Lindi na Mtwara, barabara zetu hazipitiki jamani tunaomba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nachingwea kuna Kambi ya Jeshi na ile Kambi ya Jeshi imetunza Viongozi wengi wa Afrika.
NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini naomba mtufikirie barabara watu wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii leo ya kuchangia kwenye Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya uzima na wenzangu wote tulioko humu ndani tunatakiwa tumshukuru Mungu kwa sababu ametupatia uzima kwa siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumshukuru Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu. Miradi mingi ambayo anaifanya inaonekana, kazi kubwa anazozifanya zinaonekana. Tunatakiwa tumpongeze sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Waziri wa Utumishi, Naibu Waziri na jopo lake lote la Utumishi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa kutuletea bajeti nzuri inayoonesha mwanga endapo itatekelezwa vizuri kwa watumishi wetu wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina masuala machache kidogo. Suala langu la kwanza ni malipo ya wastaafu. Naongelea hili suala kwa huzuni kubwa na kwa uchungu mkubwa sana, kwa sababu kuna watumishi wengi wameitumikia Serikali yetu tukufu kwa weledi mkubwa, wamefanya kazi vizuri sana, lakini wamestaafu wametupwa na mpaka leo hawajapata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana, nina baadhi ya watu na nina evidence za kutosha. Nina mtu wa kwanza hapa alikuwa ni dereva wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, anaitwa Hamis Mnali. Huyu baba amefanya kazi yake vizuri, amestaafu mwaka 2009. Jamani, mtu amestaafu mwaka 2009 mpaka leo hajapata mafao yake. Hebu tuangalie hapo utu upo kweli? Ukitaka hii hali iume, hebu jaribu kurudisha vidole mikononi mwako wewe. Ufanye kazi, utumikie, halafu umalize utumishi wako mwaka 2009 mpaka leo hujapata mafao yako. Jamani tunakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yetu Samia Suluhu anafanya kazi kubwa sana na inaonekana. Pia, viongozi wetu wakubwa wanafanya kazi kubwa sana, lakini huku chini kuna watu wanamwangusha. Nina mifano mingi na hata Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, tukimaliza hapa tutaonana. Huyu baba amestaafu 2009, amezungushwa na nina evidence ya barua zake zote hapa alizoandika utumishi, akaambiwa sijui leta nini, akapeleka. Mpaka baadaye akaamua kuandika barua ya kulalamika. Barua nyingine ikarudi kwenye kile Chuo cha Ualimu Nachingwea, huyo mtu afuatiliwe kisha majibu yarudishwe imefikia wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo aliyoyafanya huyu baba mpaka leo hii ninavyongea na hili Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 19 Aprili, 2024 huyu baba hajapata mafao yake. Hii ni haki kweli? Tunakwama wapi Serikali yetu ya Tanzania? Tunawafanyia nini wananchi wetu? Huyu baba mshahara wake ulikuwa ni mdogo tu, ni dereva wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, lakini mpaka leo hajapata haki yake. Amefuatilia amemaliza, amekopa hela kwa watu, amehangaika, aliwatumia mpaka Wabunge na barua ziko humu ndani. Kitu cha kushangaza hajapata haki yake. Apate wapi na huyu ni Mtanzania halali? Documents ninazo, Waziri na Naibu Waziri, nikitoka naomba hapa tuonane ili tufuatilie suala la huyu baba, apate haki yake. Pia, wapo wengine wengi nitampa Waziri evidence zao. Inasikitisha sana na inaumiza sana. Nitapeleka hizi barua, vithibitisho na mambo mengine kwa Waheshimiwa Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kuhakiki watumishi mkoani. Hili suala nilishaliongelea kwenye Bunge na nikauliza swali. Unapostaafu uchumi unakuwa umerudi chini, umri unakuwa umesogea na hauna nguvu. Kwa nini tusiwafuate hawa watu kwenda kuwahakiki kule kila mwaka? Nilijibiwa kwamba, wanakwenda kuwafuata wilayani, hawajaanza hicho kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaamini sana viongozi, Waziri na Naibu Mawaziri waliopo kwenye Wizara hii. Naomba walishughulikie hilo ili watu waende wakahakikiwe huko, hawana uwezo wa kutoka. Hivi umtoe mtu Kilimarondo au Liwale aende akahakikiwe Lindi, hivi jamani mnajua kilometa zilizopo? Mnajua nauli ni kiasi gani? Kwa kweli hatuwatendei haki ndugu zetu kwa sababu na sisi pia ni wastaafu wajao hapo mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine tulikuwa watumishi wa umma, hii hali tunaijua. Tunaomba kuhakikiwa kusiwe mikoani, tuwafuate hawa watu. Ni bora ukamlipa mtendaji wako akaenda kuwafuata hawa watu kwenye kila wilaya akahakiki ili kuwasaidia hawa watu. Watu wazima maradhi yako mengi, uwezo wa kifedha hamna, leo wakahakikiwe mkoani? Hatuwatendei haki na naomba hii ibadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la ajira, hili suala la ajira ndiyo kizungumkuti kabisa kusema ukweli. Wabunge wenzangu wameshaongelea hapa, unawaita watu wanatoka Liwale, wanatoka huko, wanatoka wapi, wanakuja kufanya interview Dodoma. Anakuja hapa mzazi wake hali yenyewe ya maisha ni ngumu. Wanakopa hela huko wanakuja hapa wanakaa hata wiki kwenye hoteli. Hebu tuifikirie hii kwa kweli, inaleta msingi kweli? Naomba tubadilishe hili suala la ajira sasa hivi liwe linafanyika kiwilaya. Tena ikiwezekana tunaomba na mgawanyo wa kiwilaya, kwa sababu ajira zinafanyika kwenye system, tunaomba tugawane kiwilaya ili na wilaya nyingine zisikose. Inaonekana kuna wilaya nyingine wanapata watumishi wengi na wilaya nyingine hazipati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la lingine linaniumiza sana kichwa na evidence pia ninazo. Kuna baadhi ya askari polisi walifukuzwa kazi kwa uonevu. Nina evidence popote nitakaposimama na nitawaita na wenyewe. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, naomba walifuatilie hili suala. Mmoja alikuwa ni polisi anafanya kazi Kigamboni katika Kitengo cha Anti-Robbery, mmoja alikuwa anafanya kazi central pale kwenye Kitengo cha Rider (wale waendesha pikipiki). Siku moja wakiwa kazini usiku walikamata dawa za kulevya (ni siku nyingi kidogo mwaka 2013). Walipokamata dawa ya kulevya na gari wakaamua kuongea kwenye zile simu zao kutoa taarifa makao makuu kwamba kuna gari tumelikamata na lina madawa ya kulevya, kwa uhakika kabisa na kwa uaminifu kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamejipalia makaa. Siwezi kuthibitisha kwamba zile dawa zilikuwa ni za wakubwa, ila naomba wani-quote, “Inawezekana zilikuwa dawa za wakubwa au dawa ya watu wenye pesa sana”. Hali ilikuwa mbaya kwao, kilichofuatia waligeuziwa kesi na wakabambikiwa kesi za ajabu. Baada ya siku mbili, tatu walikwenda kukamatwa wakawekewa kesi ya kwanza kwamba, wameiba kwa Wachina, kesi ya pili wameiba bar. Mtu amekamata dawa za kulevya ameokoa vijana wetu ambao wanaharibika na madawa ya kulevya, leo wanakuja kubambikiwa kesi kubwa kama hizo? Inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichofuatia ni kwamba kesi ilikwenda mpaka 2016 ikaonekana hawana hatia na wenye hatia walikamatwa wakafungwa. Kibaya zaidi, baada ya kesi kwisha wale walianza kuandika barua ili waweze kupata stahiki zao za miaka yote ambayo walikuwa wamewekwa ndani na kurudishwa kazini, inasikitisha. Wamepigwa danadana na kibaya zaidi kuna baadhi ya watu wakaanza kuwafanya mtaji wao kwa kuwachukulia hela ya kuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha, watu wamejitolea kutetea Taifa letu, leo hii ndiyo wanaambiwa ndiyo wametenda yale madhambi…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maimuna Pathan, muda wako umekwisha kaa chini…
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba hizi kesi ambazo nawapa, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, niwaone ili hawa watu wasaidiwe, warudishwe kazini, walipwe haki zao za msingi. Hii ni Tanzania, wako kwenye nchi zao, wana… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pathan utaratibu ni kwamba kama una mengine ya ziada unaandika kwa Waziri.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nimekusikia.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/2025. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya uhai na pia nampongeza Rais wetu kipenzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi zake kubwa ambazo anaziendeleza na tunaziona na pia nimpongeza Waziri wetu Mwigulu na Waziri wa Mpango, mmeandaa kitu kizuri tumekiona, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu ni mdogo sana. Mchango wangu wa kwanza nataka nizungumzie Kada ya Ununuzi na Ugavi, sana sana Serikalini. Kada hii ya ununuzi na ugavi tunaona imeongezewa kazi, kuna kazi ambayo ilikuwa inafanyika kwenye kada ya uhasibu na ilikuwa inapatikana kwenye Finance Act, kuna masuala ya vifaa (assets) kazi hii ikiwa inafanywa na uhasibu lakini sasa hivi kuna mabadiliko ya sheria kazi hii imerudi inatakiwa ifanyike kwenye kada ya ununuzi na ugavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali. Kwanza naomba tuiandae kada hii kwa kazi rasmi ambayo inaingia kwenye kada yao. Tutaiandaaje kada hii? Kwenye Serikali yetu ninaona kada mbalimbali ambazo zipo, kwa mfano, kada ya uhasibu. Kuna Mhasibu Mkuu wa Serikali, kuna Mganga Mkuu wa Serikali, kuna Mfamasia Mkuu na kada nyingi zina Mkuu, mkuu mkuu wa Serikali lakini hii kada ya ununuzi ni kama vile imetengwa fulani kama vile siyo kada rasmi au siyo kada ambayo inafanya mambo ya muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke ndugu zangu, pesa kubwa ya Serikali, hela nyingi zaidi ya 80% inaingia kwenye ununuzi. Sasa kwa kuwa pesa nyingi ya Serikali inatumika kwenye ununuzi hii kada ninaomba tuiboreshe apatikane Afisa Ununuzi Mkuu wa Serikali. Kada inapokuwa haina mkuu kule juu inakuwa inalega lega, kwa sababu kuna mambo mengi yanashindwa kwenda sawa, kada hii inatumia pesa nyingi sana za nchi hii. Ninaomba sana kada hii iandaliwe, iwekewe Mnunuzi Mkuu wa Serikali, waweke malengo vizuri na kuwawekea kupokea kwenye kazi hii ya vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia kunapokuwa na Mkurugenzi wa Ununuzi awe na wasaidizi wake wawili. Mmoja awe anaenda kwenye ununuzi, mmoja awe anaenda kwenye vifaa kwa sababu, kada hii imeongezewa vitu ambavyo vilikuwa vipo kwenye uhasibu. Kada hii ya ununuzi naomba ku-declare interest, mimi mwenyewe ni mnunuzi, ninaifahamu. Kada hii huwa inapigwa vita na kupewa mizigo ambayo wakati mwingine siyo ya kwake. Mara nyingi malalamiko yakitokea kwenye ununuzi wa Serikali kwenye miradi mbalimbali ya Serikali wanatupiwa mizigo kada ya ununuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie leo, mara nyingi kesi mbalimbali zinazotokea, barabara mbovu, majengo mabovu, ununuzi wakati mwingine labda vitu vimefanyika visivyo, wakati mwingine siyo wanunuzi wanaofanya hayo mambo. Mnunuzi anafanya sehemu yake anayotakiwa afanye lakini yeye ni mtaalam wa ununuzi. Tukumbuke kwamba kwenye barabara kuna wataalam ma-engineer, kwenye majengo kuna wataalamu ma-engineer, wale ndiyo wanakuwa wasimamizi wakuu wa yale mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana, mara nyingi sana wanapata lawama lakini baadae wanapokuja kufuatilia utakuta kada hii hawana kosa jamani, kuna watu pale nyuma yake ndiyo wanakuwa na makosa hayo. Kwa hiyo niombe kada hii tuimarishe, tuwatafutie semina vizuri, wapokee kazi ambayo imeingia iliyokuwa upande wa pili na tuwaimarishe jamani, kwa kweli tuwaimarishe, wanatumia pesa nyingi ya nchi yetu, wanatakiwa wapewe kazi na muongozo ulio imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa 2024/2025 tunaona kwamba kuna vipengele hapa, kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu, kuendeleza rasilimali watu na vitu kama hivyo. Kipengele hiki cha nne kuchochea maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Lindi asilimia kubwa kuna kazi mbili zinazofanyika, wananchi wengi ni wakulima, wananchi waliobaki asilimia kubwa ni wavuvi. Nikija kwenye suala la wakulima hiki kipengele cha nne kinachosema kuchochea maendeleo ya watu, kule Mkoa wa Lindi mpaka majirani zake mwaka huu itakuwa ni shida sana. Kuna huyu mnyama tulishapiga kelele mara nyingi sana kwenye Bunge lako, huyu mnyama anaitwa tembo, kiukweli wananchi wa kule wanakufa, wanauawa na huyu mnyama, wakienda mashambani kulima mazao yanaliwa, watoto wengi wanashindwa kwenda shule, hata hao waliolima ni wachache, wengi wameshindwa kulima, hata hao waliobarikiwa wakaweza kulima mazao yote yanaliwa na tembo. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa
MWENYEKITI: Mheshimiwa Chinguile, taarifa.
TAARIFA
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge anazungumza vizuri, hata kule kwenye Jimbo la Nachingwea mwananchi ameuawa mara ya mwisho tarehe 17 Juni, mwaka huu kwa hiyo hali siyo nzuri sana. Naomba kuunga mkono anachokizungumza.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chinguile, Mheshimiwa Pathan.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Sasa hali iliyoko ni njaa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja sijaongea kabisa. Hali ni mbaya na sheria zilizopo sasa hivi Maliasili kifutajasho heka moja mtu unamlipa laki moja, halafu pamoja na kwamba kifutajasho wanalipwa laki moja bado hata vifutajasho vya mwaka jana wananchi hawajapata. Hali ni mbaya sana, tuwakumbuke wananchi wetu, hali siyo nzuri jamani. Huyu mnyama tumewashauri kutengeneza solar electric fence hata kwenye sehemu chache, tunaomba Serikali itusaidie. (Makofi)