Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maimuna Ahmad Pathan (15 total)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Katika hali halisi hiyo pesa iliyotengwa 1.5 kwa ujenzi wa barabara ya lami ni ndogo sana na upembuzi yakinifu umefanyika muda mrefu sana.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza pesa angalau hata kidogo, watutengenezee hata kilometa 30 tu, kwa mwaka huu, halafu na zile zitakazobakia waongoze pesa kwa mwaka ujao watutengenezee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hela iliyotengwa ni hela ndogo kulingana na urefu wa barabara, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii fedha iliyotengewa ni fedha ya awali kwa ajili ya mobilization na kadri fedha itakavyoendelea kupatikana kwa jinsi Serikali itakavyopata, itazidi kuongezewa ili kujengwa kwa kiwango chote.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii inatakiwa ijengwe katika kipindi cha awamu yote hii ya miaka mitano. Kwa hiyo, kadri fedha itakavyoendelea kupatikana basi barabara hii tunahakika kwamba itajengwa yote kwa kiwango cha lami, kwa maana ya Masasi, Nachingwea hadi Liwale. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, huoni kwamba kuvua samaki usiku wakiwa wamelala unaweza ukavua samaki hata wale ambao hawajalengwa? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali itabadilisha au itafanya marekebisho ya kanuni ya mwaka 2020, kipengele cha 66(b)(b), 66(f)(f), 66(g)(g) na kipengele 128(1) ambacho kina faini ambayo haitekelezeki kwa wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nitoe ufafanuzi katika suala hili la kuvua samaki usiku. Kuvua samaki usiku kuna uwezekano wa samaki wale wadogo kuwa karibu zaidi ya kina 50 kuliko wale samaki wakubwa, lakini pia uvuvi wa kutumia ring net unasababisha kuchukua mazalia ya samaki pamoja na mayai ambayo yanaweza yakaondoa uvuvi endelevu katika mazalia ya samaki na hivyo kufanya maeneo haya yasiwe endelevu kiuchumi na kiuvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la lini Serikali itabadili kanuni; mchakato wa kanuni hizi unaendelea, hivyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Bunge, muda ukifika zitakuja kwenye kamati husika na kanuni hizi zitafanyiwa marekebisho, ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Lindi sasa hivi kuna gesi ambayo tunategemea itakuwa inawekezwa pale.

Je ni lini Uwanja wa Ndege wa Lindi Mjini utatatengenezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pathan, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Lindi upo kwenye mpango, na katika bajeti hii upo kwenye mpango wa kuanza taratibu za kuujenga. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa jibu zuri ambalo nimelipata: -

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati upi ambao imeuweka wakati mwingine isijirudie kukaa muda mrefu bodi za wataalam kutokuwepo?

Mheshimiwa Spika, Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imejiandaa na imeweka mipango, mikakati na taratibu maalum ambazo zitakuwa ni suluhisho sahihi la kutokuwa na muda mrefu wa kuunda ama kuteuwa bodi hizo. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya kutoka Masasi - Nachingwea kwenda Liwale ni barabara ya mkakati: Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja inaanzia Mtwara - Mnivata - Newala hadi Masasi, ina urefu wa kilometa 210. Kilometa 50 atakubaliana nami zimeshajengwa; na tunavyoongea sasa hivi, tupo kwenye hatua za mwisho, African Development Bank wanaijenga hiyo barabara; na kuanzia mwezi Tisa ama wa Kumi hii barabara itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa zote 160. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, Serikali ina mikakati gani endelevu ambayo itakuwa imejiwekea ili kuepusha migogoro hii ambayo inapelekea wananchi wetu kuuana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni hatua gani zinachukuliwa na Serikali kwa wale wanaobainika kusababisha migogoro hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kufanya jitihada mbali mbali za kuhakikisha kwamba ina suluhisha migogoro hiyo ikiwemo kuendelea na programu za kupanga, kupima na kumilikisha lakini pia kuendelea kupanga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha mipango yote inaendelea kupangwa katika maeneo hayo.

Pia, kushirikiana na mamlaka za upangaji, tumeendelea kuelimishana na kupanga bajeti kuhakikisha kwamba maeneo yote vijiji yanaendelea kupimwa na kupangwa ili kuondoa malalamiko ya wananchi ikiwemo migogoro hii inayoendelea katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali la pili lililoulizwa na Mheshimiwa Maimuna Pathan, juu ya hatua gani zinazofanyika kwa wale ambao wanaendelea kufanya fujo, jeshi letu la polisi limejidhibiti katika kuhakikisha kwamba watu wote wanaofanya matatizo au kuendeleza fujo katika maeneo yetu wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tunajua ugonjwa huu unawasumbua akina mama wengi sana wakati wa kujifungua.

Je, Serikali haioni haja sasa ya kuongeza huduma za tija kwenye Hospitali za Mikoa ya Kusini?
NAIBI WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inaongeza, na unapozungumzia kusini ndio maana kuna Hospitali ya Kanda ya Mtwara Kusini kule, ambayo kwa kweli inajengewa uwezo mkubwa kama hospitali zingine za kanda. Moja kutoa huduma lakini pia kujenga uwezo kwa hospitali za upande huu kwa chini ili waweze kutoa huduma hiyo. Pia kwa muda wa miaka hii miwili vimejengwa vituo 862; na kati ya hivyo 421 vimewekewa sehemu za kupasua akina mama ili kuwanusuru na hili jambo. Tutaendelea kufanya hivyo ili kuweza kuwanusuru akina mama. Kwa hiyo kuna mkakati wa nchi nzima si suala la Kusini peke yake.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini barabara ya kutoka Masasi kwenda Liwale kupitia Nachingwea itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale ni kati ya barabara saba ambazo zilichaguliwa kuingia kwenye mpango wa EPC+F; na tunavyoongea sasa hivi upande wa ufundi zimeshakamilishwa ziko kwenye upande wa fedha sasa ya kufanyiwa tathmini.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante. Viwanja hivi vilitumika kwa kupigania uhuru Kusini mwa Bara la Afrika. Je, ni nini tamko la Serikali hasa kwamba viwanja hivi lini vitawekwa lami vyote viwili?

Swali pili, Je, ni lini wananchi waliotwaliwa maeneo yao kwa ajili ya kuongeza eneo kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea watalipwa fidia zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni lini vitajengwa viwanja hivi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo hayo kwamba katika bajeti ya mwaka huu Kiwanja cha Lindi kimetengewa ama tumetenga takribani bilioni 2.5 na fedha hizi zitatumika kwa ajili ya Mkandarasi Mshauri ambae ataandaa document kwa Ajili ya kutangaza viwanja hivi ili viweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, suala la pili anataka kuja ni lini wananchi watalipwa fidia. Ni kweli tathmini imekwishafanyika na mwezi Machi daftari ambalo limeshaandaliwa kwa ajili ya malipo liliwasilishwa kwa Mthamini Mkuu na Mthamini Mkuu ataleta Wizarani na Wizara tutapeleka Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hawa katika kiwanja hiki cha Nachingwea. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; je, ni lini Serikali itatoa pesa au kutenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Kilwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; vifaa vilivyopo kwenye Chuo cha VETA Lindi Mjini ni vya kizamani sana; je, Serikali haioni haja ya kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya Lindi Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha jibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba vyuo hivi vinajengwa katika Wilaya 64, na Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zinajengewa, na tayari tumeshapeleka shilingi milioni 228 kule Kilwa, na usimamizi wa chuo kile kinachojengwa pale unafanywa chini cha Chuo chetu cha FDC ambacho kipo katika Wilaya hiyo ya Kilwa.

Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, lakini niwaondoe hofu wananchi wa Kilwa, hata pale Kilwa napo ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zinajengewa vyuo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili, amezungumza suala la vifaa; ni kweli tukiri kwanza katika vyuo vyetu vya zamani tulikuwa na vyuo 45 vya zamani ikiwemo na hiki cha Lindi, lakini tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa utashi wake na maono yake, katika kipindi hiki kifupi tumeweza kukamilisha vyuo 29 na hivi sasa tunakwenda kujenga vyuo vingine 65, vyuo 64 katika Wilaya na kimoja cha Mkoa. Hivi sasa Serikali inafanya tathmini kwa vyuo vile vyote 45 vya zamani na hivi 29 ambavyo tulijenga katika mwaka uliopita wa fedha, tathmini ya vifaa pamoja na mitambo mbalimbali kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia. Kwa hiyo, tuko njiani kupeleka vifaa hivyo.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni lini tathmini hiyo itakamilika ili Watanzania wafanye kazi zao kwa ufasaha ili kuleta tija? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, kwa kuchelewesha kukamilisha taratibu hizo hatuoni kwamba tunawanyima Watanzania fursa katika kumiliki rasilimali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba mchakato wa kubadilisha sheria ama kanuni ni mchakato unaofanyika mara kwa mara. Kama nilivyosema mwaka 2019 mchakato huo ulifanyika tukabadilisha sheria mbalimbali, mwaka 2020 tukabadilisha. Kwa hiyo, sheria ambazo zinaonekana pengine ni kandamizi kwa wadau wa uvuvi, Serikali iko tayari kuendelea kuzibadilisha mara kwa mara kadri ya mahitaji.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini zinaendelea kulingana na sheria, jiografia na uhitaji wa maeneo husika. Lengo la Serikali hasa ni kuhakikisha kwamba sheria zinazotumika kumsaidia huyu mvuvi ama mtumizi wa sekta hiyo kurahisisha shughuli zake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tathmini zinaendelea. Sheria ambazo ni kinzani na mahitaji ya watumiaji wetu, zinaendelea kubadilishwa siku hadi siku kama ambavyo zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara. Kwa hiyo, wataalamu wanaendele kufanya tathmini, lakini sio tu wataalam wa Wizara, ni pamoja na watumiaji wa sheria hizi wanaendelea kufanya tathmini siku hadi siku kama ambavyo sheria na kanuni zimekuwa zikibadilika, naomba kuwasilisha. (Mkofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuwapongeza viongozi wa TANESCO Mkoa wa Lindi na Kanda ya Kusini, kuna Mkurugenzi wa Kanda Eng. Makota, kuna Meneja wa Mkoa wa Lindi Eng. Kahinda na mameneja wa Wilaya zote Mkoa wa Lindi wamejitahidi sana kubadilisha hali ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Grid ya Taifa inapita katika Wilaya zote za Mkoa wa Lindi na Mtwara ili kuondoa adha hii ya umeme?

Swali la pili, gesi kwa asilimia kubwa inatoka Mkoa wa Lindi na Mtwara lakini wenyeji wa Mkoa wa Lindi na Mtwara mpaka sasa hivi wanatumia kuni na nishati ya mkaa kupikia. Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuwasaidia kuwapelekea umeme wananchi wale ili tuweze kulinda mazingira ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya Wizara na Serikali kwa ujumla nipokee pongezi kwa ajili ya hawa watendaiji wa TANESCO ambao wanafanya kazi nzuri na wanajitahidi kuhakikisha kila eneo kwa kweli huduma ya umeme inakuwa ya kuimarika. Niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi Serikalini na wizarani na wenzetu wa TANESCO tutaendelea kuhakikisha jambo hili tunalifanyia kazi kwa sababu ndio kazi yetu ambayo mmetuamini nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la pili kwa sababu Mkoa wa Lindi tayari unayo miundombinu ya umeme, tutakapokuwa tumefikisha Grid pale Masasi au Tunduru tayari Mikoa yote na Wilaya zote za Mkoa wa Lindi zitakuwa zimepata umeme wa Grid ya Taifa. Kitakachoendelea kufanyika ni kuendelea kusambaza umeme kwa kutumia miradi yetu ya REA kwenye vijiji na vitongoji ili kila mwananchi sasa aweze kupata umeme. Kwa hiyo, miradi hii mitatu mikubwa niliyoisema itakapokuwa imekamilika na Gridi itakuwa imeingia Mkoa wa Lindi na tayari kila wilaya itapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la pili kama tunavyofahamu sote Serikali imeanza sasa jitihada kubwa sana za kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia ambayo ni pamoja na gesi asilia, gesi za viwandani lakini pia na umeme, na katika maeneo yote ya Lindi na Mtwara tutaweka nguvu za ziada na jitihada kuhakikisha, zile nyumba chache ambazo tayari zimeunganishwa na gesi ya asili basi zinaongezeka kutoka kwenye idadi iliyopo kwa miradi ambayo tumeipanga kwenye bajeti inayokuja ili wananchi wengi zaidi waweze kutumia gesi asilia na hii mitungi mingine ya kawaida ya kuweza kupata nishati safi ya kupikia.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita nilitoa ushauri kwa Serikali kwa kuweka solar electric fence kuzunguka maeneo yote ambayo yana mbuga za wanyama. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuchukua ushauri huo ili kuepuka wanyama kutoka kwenye mbuga za wanyama na kuzunguka hovyo, kuzurua na kuleta maafa na kuharibu mashamba ya watu kwa Watanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, fidia zinazolipwa kwa wahanga ni kidogo sana, haziendani na hali halisi ya sasa; je, Serikali haioni haja ya kuongeza kiwango cha fidia zinazotokana na uharibifu wa wanyamapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, maswali haya yameendelea kujitokeza katika Bunge lako hili, lakini swali la kwanza linalohusiana na kuweka electric fence, tayari Wizara imeshaanza mkakati huo na kuna maeneo ambayo tumeyatengea bajeti tutaanza kuweka fence kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye hili la pili la fidia, tayari mlishatupa maekekezo kupitia sheria hii na tuko kwenye hatua za mwisho. Kwa hiyo, tutaileta na tutafanya marekebisho ili kiwango hiki kiweze kuongezwa. (Makofi)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea kuelekea Liwale kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Pathan, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea kwenda Liwale Serikali imetenga bajeti kwenye bajeti ambayo imepitishwa kuanza na eneo la Masasi kwenda Nachingwea. Kwa hiyo, barabara hiyo tuna hakika itaanza utekelezaji kwa kiwango cha lami kwa mwaka fedha tunaoenda kuuanza sasa. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante, swali langu la kwanza la nyongeza ni kwamba Kikosi cha 41 KJ Nachingwea pia kuna maeneo yalitwaliwa na Jeshi. Ni maeneo ambayo wazee wetu waliyatunza miaka mingi sana.
Je, Serikali haioni haja ya kuwalipa fidia wazee hao?

Swali la pili, kwa kuwa wazee waliyatunza maeneo yote hayo kwa muda mrefu na ilikuwa ni tegemeo kwa maisha yao. Je, Serikali haioni haja kweli ya kuwalipa hata kifuta jasho kidogo ili maisha yaendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa swali la msingi nililolijibu inaonesha kwamba hakuna mgogoro, lakini kwa swali la nyongeza aliloliuliza Mheshimiwa Mbunge Pathan, naomba nilichukue ili kuelekeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Kikosi cha 41 KJ, walifuatilie na kuleta taarifa stahiki ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Nashukuru. (Makofi)