Supplementary Questions from Hon. Zahor Mohamed Haji (16 total)
MHE. ZAHOR MOHAMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; je, Serikali sasa iko tayari kutoa taaluma hii baada ya mkanganyiko wa mambo haya kwa upande wa Zanzibar?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; je, lini hili linaweza kuanza kufanyika kwa ajili ya kuondoa huo mkanganyiko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zahor kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ada ya Serikali kutoa taaluma kwa wananchi wake na taasisi mbalimbali, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wote juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anauliza, ni lini? Niseme, Serikali kutoa taaluma kwa wananchi wake ni suala endelevu. Kwa hiyo, tunaendelea kutoa taaluma kwa wananchi.
MHE. ZAHOR MOHAMED HAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba niongeze swali moja la ziada.
Wanasema justice delayed is a justice denied, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari sasa kuongeza uharaka wa jambo hili kwa sababu wananchi wamekuwa wakipata matatizo kwa muda mrefu? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la nyongeza la ndugu yangu pale Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli uharaka upo na kwa sababu ni sehemu ya mchakato wa kupatikana kwa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo hayo, naomba Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tu na muda wa kutosha na ataona kinachoendelea kwa sababu kimsingi Mahakama ya Tanzania iko kwenye mabadiliko makubwa sana katika uwekezaji wake, kwenye majengo ya kutolea huduma. Kwa hiyo hata hili ndio maana tumelitolea maelezo kwamba tunalifanyia kazi na kazi itakwenda kwa kasi sana. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ambayo yamesema kikao chamwisho kilifanyika Agosti, 2021 na katika kikao hicho changamoto 11 kati ya 18 zilipatiwa ufumbuzi.
(a) Je, Serikali inaweza kulitaarifu Bunge sasa mambo hayo ni yapi?
(b) Ni lini Serikali italeta Muswada ili mambo yaya sasa yatambulike kisheria kwamba yapo nje ya changamoto zetu na kila mtu afanye ya kwake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera, kama iifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika changamoto 25, jumla ya changamoto 28 zimeshapatiwa ufumbuzi, miongoni mwa hizo kama ambavyo umenishauri nitampelekea kwa maandishi ili aweze kuziona. Zipo changamoto kwa mfano kulikuwa kuna hoja ya uvuvi katika Bahari Kuu hii ilishapatiwa ufumbuzi, kulikuwa kuna hoja ya mgawanyo wa mapato ilishapatiwa ufumbuzi. Kulikuwa kuna hoja ya mapato yanayotokana na uhamiaji, hii ilishapatiwa ufumbuzi kwa upande wa Zanzibar, kulikuwa kuna hoja ya ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo, kusainiwa kwa mikataba ya miradi ya maendeleo Zanzibar hili limeshapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kusainiwa kwa mkataba ujenzi wa Hospitali ya Mbiguni Zanzibar, ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar, ujenzi wa barabar ya kutokea Chake, Machomanne, Meli Tano kuelekea kwa Binti Abeid kueleka Wete, yote haya na mengine yalishapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mengine kama ulivyoshauri nitampelekea kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuwa jambo hili la Muungano ni jambo ambalo hati zake zimesainiwa zipo na zina nguvu kisheria. Kwa hiyo, nimuambie tu Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu ni jambo ambalo linahitaji ridhaa ya pande zote mbili, wacha tukakae tutakapoona kuna haja ya kuleta kama Muswada basi tutalileta hapa. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningeomba Serikali itusaidie kufahamu.
Je, kwa wale ambao walikuwemo kwenye mfuko wa TASAF lakini hawaku–qualify kuondoka lakini hawakurudishwa tena kwenye mfuko huu kwenye muda huu? Tafadhali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zahor Haji, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa walengwa ambao walikuwemo kwenye mpango wa TASAF lakini baadae ikaonekana hali zao zimeimarika na kutolewa haijazuiwa wao kurudishwa kwenye mpango wa TASAF pale ambapo watakuwa wameshuka chini ya vile vigezo ambavyo vimewekwa vya mtu kuonekana ana hali nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba nitakaa na Mheshimiwa Zahor Haji ili tuweze kuona ni namna gani wataalamu wetu wa TASAF wanaweza kwenda pale Mwera na kuangalia hizo kaya ambazo zilitolewa na ziweze kurudi katika mpango wa TASAF.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza; la kwanza, je, Serikali inatambua kwamba tabia hii inafanyika katika jimbo langu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Je, Serikali sasa iko tayari kulifanyia kazi hii ili kuondokana na tatizo hili kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali inatambua juu ya tabia za baadhi ya viongozi au wananchi wanaoshiriki katika kuhakikisha kwamba wanawanyima watu haki zao. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa kutambua hilo Serikali imejidhatiti kuhakikishi kwamba inachukua hatua zote husika na pale inapotokea wananchi wanashindwa kwenda kushtaki basi na sisi pia kama wawakilishi wa wananchi tunaruhusiwa kufikisha vilio katika ofisi hizo mbili ikiwemo mkurugenzi na ofisi ya makamu wa pili wa Rais kama nilivyoeleza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba haki za watu wote wanaostahiki kuingia katika mfuko wa TASAF zinapatikana.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Serikali kwa jibu lake lakini pia wamekuwa wanasiasa. Mimi ombi langu ni hili; kwa sababu hili siyo jambo la kupanga ni jambo la dharura, na tumeliuliza zaidi ya miaka mitatu humuhumu ndani majibu ndiyo hayahaya, ombi langu ituambie Serikali.
a) Je, ni lini imeamua au itaamua kulishughulikia jambo hili kwa dharura?
b) Je, ni lini sasa Serikali itashirikiana seriously na Serikali ya Zanzibar ili kuwaondolea maafa watu wetu wa Mwera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera kutoka Zanzibar kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari ziko hatua mbalimbali ambazo zimeshachukuliwa kama hatua za dharura kwa sababu ya jambo hili la utokeaji wa haya maafa. Na hapa nataka nichukue fursa hii nimpe pole sana Mheshimiwa Zahor kwa haya matukio ambayo yanatokezea mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha Serikali kuunda kamati zinashughulikia maafa ambazo zipo kwenye ngazi tofauti, zikiwemo ngazi za shehiya na ngazi za wilaya ni miongoni mwa hatua madhubuti ambayo imeshachukuliwa. Katika jibu la msingi tayari tumeshaeleza kwamba, kupitia bajeti hii ya mwaka ya fedha huu 2023/2024 tutahakikisha kwamba tunakwenda kushughulikia maeneo yote ambayo yanakabiliwa na maafa kama haya likiwemo Jimbo la Mwera na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka tu nimwambie Mheshimiwa kwamba kuna baadhi ya mambo tayari tumeshayaelekeza. Serikali imetoa maelekezo kupitia Serikali ya Jamhuri na Serikali ya Zanzibar, kwamba kwanza watu waendelee kupewa elimu, ngazi za shehiya, halmashauri, wilaya, mikoa zitoe elimu kwa wananchi. Elimu ya kwanza, wananchi wasijenge kwenye mabonde, wasijenge kwenye maeneo ambayo maji yanatuama. La pili, wananchi wasitupe taka chafuzi, taka ngumu, taka zidishi kwenye maeneo ya mitaro, mwisho wa siku inakwama, halafu maji hayaendi yanasababisha mafuriko. La tatu, wajenge kwenye maeneo ambayo yameshapimwa. Lengo na madhumuni wajenge kwenye maeneo salama waepukane na maafa kama haya, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru Serikali kwa jibu. Pamoja na kwamba jibu hili limejibiwa kisiasa zaidi kuliko tatizo lilivyo, ningeomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini sasa Serikali au Wizara itakuwa Serious Kujibu matatizo yetu ambayo yanaongozwa na Sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kwa sababu imeonekana Sheria hii inafanya kazi zaidi kwenye upande mmoja lakini kuwaathiri Wabunge wa Majimbo kwa upande wa Zanzibar. Je, Serikali sasa haioni iko haja ya kuwaandikia wenzetu wa Zanzibar ili waache kuvunja Sheria iliyotungwa na Bunge hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tuko serious katika kufanya kazi zetu. Tupo serious kufanya kazi zetu kwa mujibu wa sheria na taratibu zote zilizowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inayafnya kazi kwa upande huu wa Mfuko wa Jimbo iko Sheria inayosimamia Mfuko wa Jimbo. Lakini ipo Sheria inaitwa Zanzibar Revenue Administrative Act. Sheria ambayo inasimamia na imetoa mamlaka kwa halmashauri na Mabaraza ya Miji kutoza ama kukata kodi kutokana na sehemu ya fedha zinazoingia kwenye halmashauri zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko serious na kutokana na u-serious tulionao tunakwenda kutatua changamoto zote ambazo zinakabili Mfuko wa Jimbo hasa katika Jimbo la Mwera na maeneo mengine yote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, nimwambie Mheshimiwa kwamba tuko tayari kama ushauri wake alivyosema kwamba tuandike barua lakini nataka nimfahamishe tunavyo vikao vinavyohusika na kujadili changamoto hizi na majadiliano yote yanayohusiana na Mfuko wa Jimbo. Vikao ambavyo vinaanza katika ngazi nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tayari tumekwishaandaa kikao kazi ambacho tunakwenda kukaa viongozi wa halmashauri zote, viongozi wa mabaraza ya miji, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais ili lengo na madhumuni na Wabunge wote tuweze kuelezana hizi changamoto zinazogusa Mfuko wa Jimbo hasa kwa upande wa Zanzibar.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya ziada. Namshukuru Waziri kwa jawabu lake zuri lakini ningeomba sasa Serikali ituambie, kwa sababu vijana wanapata tabu sana kupata malipo yao, Je, ni lini Serikali itaruhusu mifumo kama ya PayPal ili watu waanze kulipwa fedha zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zahor kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya PayPal haijaomba leseni. Mara tu itakapoomba leseni na kukidhi vigezo vya kisheria basi Serikali itaruhusu kampuni hiyo kutoa huduma nchini.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri anipe majibu; je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ili mambo yote ambayo yameondolewa kwenye changamoto za Mambo ya Muungano yaonekane kwenye Sheria? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Zahor kwa kazi nzuri anayoifanya Jimboni lakini pia kazi anayoifanya katika kutaka wananchi wajue na wapate taaluma juu ya masuala yanayogusa mnasaba wa Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kikao chetu cha tarehe 6 Disemba, 2022, miongoni mwa ajenda ambayo iliibuka katika kikao kile ni namna gani changamoto zilizokuwa zimeshatatuliwa tukaziweka katika legal document. Miongoni mwa kazi ambayo tuliwapa tulitoa maelekezo kwa wanasheria wetu wa pande zote mbili za muungano waende wakakae wakaone namna ya kuweza kuanza mchakato huu ili lengo na madhumuni tuweze kuyaingiza katika legal document. Hii itasaidia kizazi kijacho kuyatambua haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo, kazi inafanyika, wanasheria tumeshawapa kazi na watakuja kutuletea majibu na hili jambo la kuifanya ikawa kwenye document ya kisheria inakwenda kufanyika, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nina mambo mawili. La kwanza, naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu ya kujipanga kupambana na maafa ambayo kwa kweli sote kama Taifa tumeyaona. Tunawashukuru na tunawaomba waendelee kujipanga zaidi kwa sababu mambo haya ni ya kujirudia na hasa ukizingatia mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea na sote tunashuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwangu ni ushauri. Naomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu mambo ya majanga ni mambo ambayo yasiyotabirika, na yanahitaji mafunzo na uwezo kwenye taasisi zake zote, na kwa sababu ni kazi zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya Bara na Zanzibar, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, basi ione namna nzuri inavyoweza kuwasaidia wenzetu kwa upande wa pili ili nao waweze kujipanga vizuri kwa kuweza kukabiliana na maafa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea pongezi za Mheshimiwa Zahor, nasi tunaendelea kumpongeza lakini pia tunampa pole kwa maafa yaliyotokea kule Jimboni kwake Mwera. Tunamhakikishia kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu tuko imara na tutaendelea kujipanga zaidi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo la pili kuhusu ushauri, tumepokea ushauri wake. Kwa kuwa masuala haya pia yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza, nasi Ofisi ya Waziri Mkuu tuna vikao vyetu vya mashauriano tunapitia Ofisi ya Makamu wa Pili, tutaendelea kuboresha ushirikiano huo ili kuendelea kuwafikia wananchi katika maeneo yote katika nchi yetu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kuishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya ziada.
Swali la kwanza, kwa kuwa suala la utafiti ni suala linalochukua muda, je, Serikali inaweza ikawaambia wananchi ni lini wanategemea kumaliza utafiti huu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu mifumo ni jambo kubwa, je, Serikali iko tayari kuendelea kutoa taaluma zaidi kwa wadau ambao wanasumbuka sana na mifumo hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zahor, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tathimini hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 ambao unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge lako Tukufu ndani ya mwaka huu na Bunge hili la Bajeti.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Serikali kupitia taasisi zake imekuwa na utamaduni na imekuwa na desturi ya kutoa mafunzo siku hadi siku kwa wadau wanaostahiki, ahsante sana.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya ziada. Swali la kwanza, pamoja na mipango mizuri ya Serikali kwenye hoja ya kupambana na mazingira, je, Serikali haioni sasa iko haja ya kubadilisha mkakati kwa sababu athari za mazingira zimekuwa kubwa kuliko mikakati yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa maeneo mengi ambayo Serikali imekuwa ikisema kwamba inajenga ukuta lakini bado yanaendelea kuathirika, je, Serikali iko tayari kufuatana nami kwenye Jimbo la Mwera ili wakaone athari kubwa za mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Zahor, kama alivyouliza. Kwanza tunakubaliana naye kwamba tuko tayari kuungana naye kwenda kwenye Jimbo lake ili kuangalia athari za mazingira zilizopo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, siyo kweli kwamba athari ni kubwa ambazo zinatokea na kwamba labda mikakati yetu haiendani pengine na utatuzi wa changamoto hizo. Kwanza nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeendelea kuwa na ushirikiano mkubwa wa Kimataifa na kikanda katika kuweka mipango mikakati na madhubuti ambayo inaelezea changamoto zilizopo tunazozipata za mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hivyo, ipo mikataba ambayo kama nchi tunaitekeleza. Kwa mfano, Mkataba wa Kimataifa wa kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi na vivyo hivyo kuna Itifaki za Kyoto ambazo tumekaa na kukubaliana namna ambavyo tunaziangalia zile athari. Zaidi ya hapo, kwa ndani ya nchi hii mikakati ambayo nimeieleza, ni mipango ambayo tunaitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia mikataba ya kimataifa tuliyoiingia, tunapata usaidizi wa kifedha na usaidizi wa kitaalamu. Vilevile kwa kutumia wataalamu wetu hapa ndani, tumeendelea kutatua changamoto hizi na ndiyo maana unaona sasa athari zilizotokea za Global warming zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi katika kubadilisha na kuleta mvua nyingi zilizokithiri, pepo kubwa na mafuriko ambayo yamekuwa yakisababishwa kama athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania tumeendelea kuwa sehemu nzuri na salama katika rekodi za East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga, na tayari tunatekeleza mikataba ya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya kimataifa na kikanda. Pia ndani ya nchi kuweka mipango ambayo itasaidia kutokupata athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na kwamba Serikali imeendelea kutoa taaluma au elimu kwa wananchi mbalimbali kwa vyombo mbalimbali, je, Serikali imefanya tathmini kujua ni kiasi gani elimu hiyo inawafikia na inawasaidia wnanchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa sababu, Jimbo la Mwera ni jimbo la vijijini na athari kubwa inatokea kwenye mambo haya ya mazingira ambayo Mheshimiwa Waziri anasema wanatoa elimu. Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri, physically, pamoja na wataalam wake wanaweza kwenda kusaidia kutoa elimu wao wenyewe? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la kaka yangu, Mheshimiwa Zahor, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuweka record sawa; kaka yangu, Mheshimiwa Zahor, ni mzoefu sana, wakati anamsaidia Makamu wa Rais wakati ule alifanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, naomba kumpa maua yake kwa kazi kubwa aliyoifanya katika upande wa muungano na upande wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa tathmini, hivi karibuni tutatoa taarifa yetu ya mazingira ambapo, naamini utakapofika Mwezi Juni tutakuwa tumepata taarifa ambayo iko very comprehensive. Nina imani kwamba, baada ya taarifa hii tutaona tathmini ya hali ilivyo kwa maeneo hayo yote. Kwa hiyo, tusubiri mpaka Mwezi wa Sita, Siku ya World Environment Day, taarifa hii itatoka kwa lengo la kujua tathmini ya athari za mabadiliko ya tabianchi na athari za kimazingira kwa maeneo mbalimbali iko vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la kutoa elimu; naomba nilichukue hili kwa sababu, nina dhamana ya Muungano. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka huwa naenda katika majimbo yao kutembelea miradi ya Mfuko wa Jimbo na mambo mengine. Hili tunalichukua, tutaona namna bora zaidi kwa kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza, kule Zanzibar, kuona jinsi tutakavyofanya ili kuwafikia wananchi wa Mwera kwa ajili ya upatikanaji wa elimu. Ahsante sana.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninaishukuru Serikali pamoja na majibu mazuri, bado inaonekana public haielewi vizuri mambo haya ambayo Serikali inasema yamepatiwa ufumbuzi. Je, Serikali kwa kuanzia kwetu sisi Wabunge iko tayari kutuletea maandiko hayo hasa ya machapisho ili na sisi tuwe sehemu ya hao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je Serikali iko tayari kuendelea na mkakati huu kwa sababu bado inaonekana taaluma inayotolewa na Serikali ni tofauti inayotolewa na wenzetu kule ambao wanapotosha jamii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Zohor kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tumejitahidi sana katika kuieleza jamii juu ya suala zima la umuhimu wa Muungano pia tumejitahidi sana kuieleza jamii juu ya changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye Muungano huu kupitia njia tofauti kama tulivyoeleza katika suala la msingi. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari kuongeza juhudi ama jitihada ili wananchi waweze kupata zaidi elimu ya Muungano na waweze kunufaika na waendelee kuutunza Muungano huu kupitia njia tofauti kama tulivyozieleza.
Mheshimiwa Spika, hata ukitazama Muungano huu, changamoto tulizotokanazo na tulizonazo sasa ni tofauti maana sasa zimebakia changamoto nne ambazo muda wowote tunakwenda kuzimaliza.
Mheshimiwa Spika, tupo tayari kuwapatia Waheshimiwa Wabunge, hivyo vitabu ambavyo tumevieleza pamoja na machapisho. Nataka nitoe maelekezo hapa kupitia Mkurugenzi wa Muungano na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Muungano katika Ofisi ya Makamu wa Rais wahakikishe kwamba Waheshimiwa Wabunge ndani ya wiki inayofuata ndani ya vishikwambi na maeneo mengine iwe tayari wameshapata machapisho hayo na vitabu hivyo ili waweze kunufaika na kujua changamoto zilizotatuliwa, nashukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwamba wamefanya kazi nzuri ya kuliona hili. Je, Serikali sasa haioni haja ya kwenda mbali zaidi, kwa sababu hata nyuzi ya kiatu ya Askari bado ni silaha. Serikali haioni sasa kuwaachia vyombo vyetu vya ulinzi fursa kamili ya kuwa na msamaha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ushauri wake umepokelewa, kwa sababu amesema huoni haja ya kutanua wigo. Tumepokea ushauri huo na tutaufanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwamba wamefanya kazi nzuri ya kuliona hili. Je, Serikali sasa haioni haja ya kwenda mbali zaidi, kwa sababu hata nyuzi ya kiatu ya Askari bado ni silaha. Serikali haioni sasa kuwaachia vyombo vyetu vya ulinzi fursa kamili ya kuwa na msamaha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ushauri wake umepokelewa, kwa sababu amesema huoni haja ya kutanua wigo. Tumepokea ushauri huo na tutaufanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)