Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ng'wasi Damas Kamani (23 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwanza kabisa, nianze kwa kumrudishia shukrani Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Nchi kwa kutupa kibali wote kuwa hapa jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa nafasi ya kipekee kabisa niwashukuru vijana wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia katika Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa imani kubwa waliyonipa ya kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyokwishafanya katika nchi yetu kwa miaka mitano iliyopita. Hotuba aliyoitoa katika Bunge hili Novemba, 2020 inatia matumaini makubwa sana kwetu sisi Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ajira limekuwa changamoto kubwa sana kwetu sisi vijana. Mimi kama mwakilishi wa vijana naomba kuungana na Wabunge wenzangu kulichangia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ajira ni mtambuka na linahitaji juhudi za pamoja za Serikali, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na sisi vijana wenyewe. Pamoja na hayo, jukumu la msingi bado linabaki kwa Serikali kuhakikisha inawezesha sekta binafsi ili kuzalisha ajira nyingi zaidi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kwamba kuna sababu kuu nne zinazochangia pakubwa sana katika tatizo la ajira katika nchi hii. Naomba nizitaje na zitakuwa pointi zangu za msingi jioni ya leo. Kwanza, ni mifumo ya elimu ambayo ujuzi wake hauendani na mahitaji ya ajira; la pili ni vijana kutokuwa na taarifa na takwimu za fursa za biashara na ujasiriamali zinazowazunguka; ya tatu ni sera za vijana na uwezo mdogo wa kiteknolojia; ya nne ni Serikali kutowekeza vya kutosha kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la mifumo ya elimu ambayo ujuzi wake hauendani na mahitaji ya ajira, kwanza kabisa, nianze kwa kuipongeza Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha vyuo vya ufundi katika sehemu mbalimbali. Pia nizidi kuwapongeza kwa kutupa ule mfumo wa competence-based system of education ambapo lengo lake kubwa ni kuwawezesha watoto na vijana wanaosoma kupata ujuzi wa msingi wa maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini changamoto kubwa ya mfumo huu ni kwamba walimu ambao wanatakiwa kufundisha vijana wetu bado hata wao hawajauelewa mfumo huu. Utafiti uliofanywa na wanazuoni wa Chuo cha Sokoine unaonesha kwamba asilimia 86 ya walimu bado hawajaelewa dhima kuu ya mfumo huu na asilimia kama 78 ya lesson plans wanazotumia kufundisha haziendani na mfumo huu wa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea na utaratibu huu kutatufanya tuwe na vijana ambao hawana stadi za kutosha na hawa wakiingia katika soko la ajira, itaongeza changamoto. Ushauri wangu kwa Wizara ya Elimu tuandae utaratibu ambao Walimu na Wakufunzi wataelekezwa upya ili waelewe namna mfumo huu unavyofanya kazi, kwa sababu mfumo huu una faida kubwa ili wao waweze kufundisha vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niungane na Wabunge wengine walioweka msisitizo katika suala zima la elimu ya stadi ya ujuzi ambayo itaendana na mfumo wa sayansi na teknolojia. Katika hili niishauri Wizara ya Elimu ione utaratibu ambao elimu ya usimamizi wa fedha inaweza ikaanza kufundishwa katika shule zetu kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni changamoto sana kama vijana hawa ambao wanatoka mashuleni wanakuja, tunawakabidhi fedha na mikopo mbalimbali kutoka kwenye Halmashauri zetu na Serikali lakini hawana elimu ya usimamizi wa fedha. Kwa hiyo, kama tulivyolifanya somo la historia ili kukuza uzalendo, vivyo hivyo somo la usimamizi wa fedha lianze kufundishwa katika shule zetu kuanzia ngazi ya chini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la vijana kutokuwa na taarifa na takwimu ya fursa za biashara na ujasiriamali zinazowazunguka, ningependa katika suala hili niongelee mikopo ya Halmashauri, almaarufu 4,4,2 na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wa vijana katika Wizara zetu. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuanzisha utaratibu huu na kweli unasaidia vijana, lakini bado kuna changamoto katika utoaji na ufanisi wa mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kuna baadhi ya halmashauri ambazo zinakuwa na mapato makubwa kuliko nyingine. Hivyo vijana ambao wako katika halmashauri zisizo na mapato, wanakuwa na shida kidogo. Tungeangalia utaratibu wa kuweza ku-centralize mfumo huu au Mfuko huu ili vijana wote tuweze kunufaika sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba tuangalie utaratibu wa kuweza kupunguza idadi ya watu katika kundi la watu ambao wanaweza kuwa eligible kwa ajili ya kupata mikopo hii. Kundi la watu 10 ni changamoto kidogo. Tuangalie kupunguza list, wawe watano mpaka watatu ili tuweze kupata ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la Mifuko ya Uwezeshaji katika Wizara mbalimbali; kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hili alisisitiza kwamba Mifuko hii iongezewe ufanisi. Mifuko hii ina changamoto kuu tatu; kwanza, mara nyingi haina fedha; na ile yenye fedha huwa mara nyingi ina urasimu mkubwa katika upatikanaji wa fedha zake; na tatu, vijana wengi hawana taarifa ya namna gani fedha hizi wanazipata. Hivyo, nadhani ni jukumu la moja kwa moja la Serikali kuhakikisha kwamba vijana wanapata taarifa zilizo sahihi za fedha hizi na namna gani wanaweza kuzipata fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza, nimeamua kuanzisha Kongamano la Vijana na Maendeleo kwa vijana wote nchi nzima, litakalofanyika mwaka huu mwezi wa Saba na litakuwa endelevu kwa kila mwaka, ambapo nitaalika Wizara zote na Taasisi zote za uwezeshaji wa vijana ndani na nje ya nchi, ili tukutane na vijana hao na kuwapa elimu juu ya Mifuko hii na fursa zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nawaomba Waheshimiwa Wabunge, pale nitakapokuja kuwaomba ku- support mfumo huu, naomba muwe wepesi ku-support kwa sababu vijana hawa ambao ni asilimia 61.9 wa nchi hii ndio waliokuwa wapiga kura wenu na tuna jukumu la moja kwa moja kuhakikisha tunawasaidia kuwanyanyua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la Sera ya Vijana na uwezo mdogo wa kiteknolojia; namshukuru sana Mheshimiwa Rais na sera yake ya Serikali ya Viwanda. Hii imetusaidia sana katika kuzalisha ajira nyingi. Katika Hotuba yake Mheshimiwa Rais ameweka wazi, viwanda vidogo vidogo kama 8,477 vimeanzishwa kati ya mwaka 2015 mpaka 2020; na jumla ya ajira kama 480,000 zimezalishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi hii bado ni ndogo. Naomba kushukuru sana Wizara ya Kazi na Vijana chini ya Mheshimiwa Jenista, imeanzisha Mfumo wa Green House ambapo itaweka green house hizi katika Halmashauri mbalimbali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi ya kusema, lakini naamini mengine nitayawasilisha kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa yote, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mwaka Mmoja. Nianze kwa kumpongeza Waziri Dkt. Mpango kwa Mpango huu mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama mwakilishi wa vijana nina machache tu ya kushauri juu ya namna gani tunaweza tukashughulikia au kutatua tatizo la ajira. Wote ni mashahidi kwamba kila Mbunge anayesimama ni dhahiri anakerwa na tatizo la ukosefu au upungufu wa ajira kwa vijana. Nina ushauri wa namna mbili tu na ndiyo zitakuwa points zangu za msingi kwa jioni ya leo. Kwanza, ni namna gani tunaweza kutumia Mifuko ya Hifadhi za Jamii kutatua changamoto ya ajira; na pili, namna gani vijana tuafikia uchumi wa kweli wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la namna gani tunaweza kutumia Mifuko ya Hifadhi za Jamii kutatua changamoto ya ajira, nianze kwa kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira kwa kuleta katika Bunge hili Tukufu Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii, mwaka 2018 na Bunge hili Tukufu likapitisha sheria hiyo ambapo mpaka sasa mifuko yetu tunaendelea nayo vizuri. Ni-declare kwamba niko katika Kamati ya Katiba na Sheria ambayo inasimamia mifuko hii. Kwa hiyo, nafahamu namna mifuko hii inafanya kazi na mpaka sasa imefikia wapi. Napenda tu kusema kwamba tusiamini yale tunayosikia kwamba mifuko hii haiko vizuri. Mifuko hii inaendelea vizuri na tunaamini itakwenda kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 ilipotungwa Sheria hii ya mabadiliko ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii, kifungu cha 91(1) cha Sheria ya NSSF kinaruhusu mfuko huu kupokea michango kutoka kwa watu walioko kwenye informal sectors au ajira zisizo rasmi. Watu hawa wanatoa michango ya shilingi 20,000/= tu kwa mwezi ambayo ni sawa na shilingi 650/= kwa siku. Baada ya kupokea michango hii, mtu akishafikisha miaka miwili, anakuwa na uwezo wa kupokea fao ambalo ni aidha atapata vifaa, mashine au mtaji wa kuanzisha kiwanda kidogo. Hii inafanyika kupitia SIDO na Benki shirikishi za mfuko huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama ifuatavyo. Changamoto ya kwanza tunayokutana nayo sisi kama vijana hasa wale ambao tunatoka vyuoni, kwanza anayetaka kuajiriwa katika mfumo ulio rasmi, anapata changamoto ya kukosa uzoefu (experience). Pia yule anayetaka kwenda kujiajiri, hana mtaji na hakopesheki katika benki na taasisi nyingine za fedha kwa sababu hana collateral au dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tukiamua kupeleka utaratibu huu kwenda vyuoni moja kwa moja, tukahamasisha vijana walioko katika vyuo na vyuo vikuu kuweza kupata mchango wa Sh.20,000/= kila mwezi, ambapo kijana huyu atachanga kwa muda wa miaka miwili, mitatu au minne kutegemea na kipindi chake anachokaa chuoni. Akitoka hapo, kijana huyu kupitia benki hizi shirikishi chini ya Mfuko wa NSSF na SIDO anakuwa anaweza kukopesheka aidha mashine, kifaa cha kazi au anaweza kukopesheka kwa mtaji kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Wizara husika ikikaa na kuangalia mpango huu, itakuwa tumepata mwarobaini wa tatizo la ajira kwa vijana wanaotoka katika vyuo na vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, napenda kusema kwamba tutakuwa ndiyo tumeondoa tatizo la ajira kwa upande wao, lakini tutakuwa tumeiongezea nguvu mifuko hii ambayo kwa namna moja au nyingine naweza nikasema ni National Security. Kwa sababu fedha hizi ndizo zinazotumiwa na Serikali yetu kuwekeza katika miundombinu na katika huduma mbalimbali za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, vijana hawa wakienda kujiajiri wenyewe…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, VIJANA, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi. Mheshimiwa Ng’wasi ukae chini halafu uzime microphone. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, VIJANA, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza sanasana Mbunge huyu kijana kwa mchango wake na umahiri mkubwa wa kiushauri anaoutoa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa kwamba kwa hesabu na taarifa niliyonayo kama Waziri wa Sekta kwa sasa, Mfuko wa NSSF ambao unashughulika na private sector, asilimia 100 ya makusanyo, ni asilimia 40 tu ndiyo inayotosha kulipa aina zote za mafao na kubakiwa na asilimia 60 ya makusanyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa asilimia ile 60 ya makusanyo, mimi kama Waziri wa Sekta, kwa kushirikiana na vijana wazalendo kama huyu anayechangia hapa, tukatengeneza kwa pamoja programu nzuri, nadhani ushauri huu unaweza kuwa ni muafaka kabisa wa kutafuta mwarobaini kwa ajili ya kuwahudumia vijana wetu na kutatua tatizo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa taarifa hii kwa kweli ningefurahi kumpa Ubalozi au Champion wa kuwasaidia vijana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, unapokea taarifa hiyo?

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea na nitafurahi sana kuwa Balozi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, tumesikia hapa kwamba kuna changamoto kubwa sana katika mikopo ya elimu ya juu. Mpango huu kama ukifanikiwa, utasaidia vijana hawa wanaotoka vyuoni moja kwa moja kuingia katika mpango wa kujiajiri na kuajiri wengine kuweza kuanza mara moja kurejesha mikopo yao ya elimu ya juu na kuepuka suala zima la riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, llani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 inaahidi kwamba kuna ajira milioni nane ndani ya miaka hii mitano zinatakiwa kuzalishwa. Kwa mpango huu, kama ukifanikiwa, maana yake suala hili la ajira milioni nane linakwenda kuwa rahisi na linakwenda kufanikiwa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, point yangu ya pili inakwenda sambamba na hii, ni namna gani vijana tutafikia uchumi wa kweli wa viwanda? Tunapozungumzia uchumi wa viwanda hasa kwetu sisi vijana ambao ndiyo kwanza tunaanza maisha, hatuzungumzia viwanda vya billions of money au millions of money, a hundred of millions, hapana; tunazungumzia viwanda vidogo vidogo ambavyo kila mtu atakuwa na uwezo wa kukianzisha kwenye chumba chake au kwenye nyumba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vitawezekana tu kwetu sisi vijana kama tukitoa bajeti ya kutosha kwenda kwenye SIDO na TIRDO. Taasisi hizi ndizo pekee ambazo zina uwezo wa kutusaidia sisi kupata mashine zenye efficiency sawa lakini kwa gharama ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mfano wa mfanyabiashara aliyetaka mtambo wa kutengeneza ethanol kwa kutumia zao la mihogo. Mtambo huu huu Brazil na China ulikuwa ni shilingi milioni 850, lakini mtambo huu huu, model ile ile baada ya kuwa studied na TIRDO wametoa mapendekezo ya kuweza kuutengeneza kwa shilingi milioni 150. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Mitambo ambayo tunaweza kuipata katika nchi jirani kwa gharama kubwa, tunaweza tukaitengeneza sisi wenyewe katika nchi yetu kwa gharama ya chini ambayo itatusaidia vijana kuweza kushiriki moja kwa moja katika uchumi wa viwanda na kukuza pato la Taifa. Naomba katika Mpango huu mawazo haya tuyaangalie namna tunavyoyaweka ili sisi kama vijana tupate kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado deni la msingi linabaki kwa Wizara ya Elimu. Vijana tukitoka vyuoni, hata tukitengenezewa mazingira mazuri kiasi gani, kama elimu tuliyopata katika shule tulizosoma haitusaidii au haitu- equip kuweza kuwa na uelewa wa kutosha wa kijamii, maana yake mambo haya yote ni bure. Mama yangu Mheshimiwa Ndalichako nakuamini, naomba sana mpango mfumo wa elimu uangaliwe kwa kushirikisha wadau wakiwemo vijana, nini hasa kinaweza kubadilishwa katika mfumo wetu wa elimu ili vijana watoke shuleni wakiwa na uwezo wa kuishi katika jamii zetu (real societies). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia katika Mpango huu jioni ya leo. Nianze pia kwa kutoa pole kwa familia ya Dkt. John Pombe Magufuli, Watanzania wote, viongozi wote kwa msiba huu mzito ambao ulitutikisa kama Taifa, lakini pia nizidi kutoa pongezi nyingi niungane na Wabunge wenzangu kwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa trend nzuri ambayo ameanza nayo ambayo inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba mchango wangu wa leo nianze kwa kutoa mfano wa mfumo wa familia ya Kisukuma. Wote tunaweza kuwa tunafahamu kwamba sisi Wasukuma tunaishi kwenye familia ambazo ni extended, familia yenye watoto wachache sana ni watoto kumi na kuendelea na familia ambayo ina watoto wengi ndio inakuwa familia tajiri Zaidi katika kile kijijini. Hii ni kwa sababu watoto hawa ndio kama source of labour ndio watatumika wakienda kuchunga, watagawa vizuri majike yatachungwa vizuri, madume yatachungwa vizuri, ndama zitachungwa vizuri jioni zikarudi zimeshiba. Pia kama wakienda shambani watoto hawa wakiungana kwa pamoja maana yake heka nyingi zitalimwa, lakini pia hata kama mtoto wa familia ile akitaka kuoa anajengewa pale pale pembeni ili aoe na yeye azae waungane wote pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana ya kutoa mfano huu ni nini? Asilimia zaidi ya sitini ya wananchi wa Taifa hili ni vijana, lakini nasukumwa kuamini kwamba Serikali haitaki au haijaona umuhimu wa kutumia wingi huu wa vijana wenye nguvu na ambao wako tayari kutumikia Taifa hili kama ambavyo familia ya Kisukuma inatumia watoto wake wengi ili kujipatia zaidi na kuwa tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto yetu kubwa sisi ni ukosefu wa ajira, lakini kwa nini kwa wingi wetu huu, bado Serikali yetu inaweza ikatumia pesa nyingi sana kuangiza mafuta ya kula kila mwaka, wakati kwa mwaka tunaweza kutumia pesa hizi, tumeshaambiwa na Mheshimiwa Kingu na wengine kwamba wapo tayari kutupa maeneo, Serikali ikaanzisha kambi, ikaweka miundombinu, vijana wakawekwa pale wakalima alizeti, wakalima michikichi na namna nyingine zote tukapata mafuta ya kutosha tuka-save pesa za Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaweza tukaamua kutumia vijana hawa hawa katika kazi nyingine nyingi miradi mingi ya kimkakati, vijana ambo wana ari ya kufanya kazi, kulitumikia Taifa hili kuliingizia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna pekee ambayo tunaweza kuweza kufanya hivyo, kwanza kabisa ni kuhakikisha tunakomboa vijana hawa kifikra kwa maana ya kuboresha mfumo wa elimu. Pili, tuwe na national agenda au vipaumbele vya Kitaifa ambavyo tutawaonesha vijana hawa kwamba Taifa letu linaelekea huku na Serikali yetu ikafanya juhudi za makusudi za kuhakikisha kwamba zinawezesha vijana hawa kuendana na vipaumbele vya Kitaifa na mwisho tunakomboa Taifa letu kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la elimu, naomba nitoe takwimu chache tu. Mwaka 2014, wanafunzi wapatao 885,000 walimaliza darasa saba, mwaka 2018 walimaliza form four lakini walimaliza wanafunzi 425,000 na mwaka huo walipomaliza form four wanafunzi 121,251 wakachaguliwa kujiunga na kidato cha sita na vyuo vya ufundi. Hata hivyo, mwaka 2020 ni wanafunzi 84,212 tu ndio wamemaliza, maana yake wanafunzi 725,645 wako wapi ambao walimaliza darasa mwaka 2014 na mwaka 2020 hawakumaliza kidato cha sita wala vyuo vya ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia VETA zetu zote nchi nzima at high capacity zina uwezo wa ku-accommodate watu 150,000 hadi 170,000 tu, wale wengine waliobaki wanakwenda wapi. Pia wote tunakubaliana katika michango yetu Waheshimiwa Wabunge wote tangu mwanzo wa Bunge hili mpaka sasa wame-hint kwamba mfumo wetu wa elimu haumwandai kijana kuweza kubaki kwenye jamii na kuitumikia jamii yake kwa kujiajiri mwenyewe, vijana hao wanaobaki wanakwenda wapi? Ndio huku huku tunazidi kuzalisha magenge ya wezi na majambazi, lakini sisi ndio tumezalisha watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya ili niseme nini, ushauri wangu; kuna mifumo mingi ambayo imeanzishwa na Wizara zetu na Serikali yetu ya kuhakikisha kwamba tuna- remedy suala hili ikiwa ni pamoja na kuanzisha program za internship na apprenticeship, kuwapa watu elimu ya vitendo ili wawe tayari kuingia kwenye soko la ajira. Hata hivyo, Serikali yetu kila mwaka imekuwa inatenga pesa nyingi sana kwa ajili ya mifumo hii. Pesa hii hii ambayo ingeweza kutumika kurudi kwenye mifumo yetu ya elimu, tukaboresha mifumo yetu, tukaanza kuwafundisha watu vitu ambavyo ni relevant kwa mazingira ya Kitanzania na tuka-save pesa nyingi za Serikali zizazotumika kuweka mifumo ya internship na apprenticeship. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi ambayo tumekuwa shuleni tumefundishwa, lakini mpaka leo applicability yake hatujaona kwenye maisha ya kawaida. Hii ni kwa sababu mfumo wetu wa elimu umekuwa static, kitu ambacho walijifunza watu miaka 20 iliyopita, wanajifunza hawa hawa wa miaka ya leo, lakini dunia inabadilika. Ushauri wangu kwa Serikali na Wizara ya Elimu, suala la elimu liwe suala la kubadilika, liwe revolving issue, watu wafundishe vitu ambavyo vinakwenda na muda, kitu alichojifunza jana kilikuwa relevant leo sio relevant tena tuache, tuanze kufundisha watu vitu vinavyokwenda na wakati, ikiwa ni pamoja na elimu ya vitendo ambayo itamsaidia kijana, hata akiamua kwamba siendelei mbele naishia darasa la saba, naishia form four, naishia form six au labda naenda mpaka chou, ana uwezo wa kurudi kwenye jamii, kuitumikia jamii yake akazalisha kujikomboa yeye, familia yake na kujenga uchumi wa nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, nimezungumzia suala la kutengeneza vipaumbele vya Taifa au National Agendas. Nitoe tu mfano leo kaka yangu Kingu amezungumzia suala la Misri na namna gani wamebadilisha kutoka jangwa na kuwa wazalishaji wakubwa sana wa vyakula vingine vingi, land reclamation Egypty ilikuwa ni National Agenda ambayo ilibebwa iwe, isiwe lazima wai- achieve. Nchi zetu za Afrika hasa sisi labda Watanzania National agenda zinakwenda na uongozi unaoingia, hatuja- define agenda zetu sisi kama Taifa labda kwa miaka 20 au 30 kwamba iwe isiwe, inyeshe mvua, liwake jua, sisi tutakwenda na mkondo huu tu mpaka tuhakikishe kwamba tumeufanyia kazi na ume-bear fruits.

Mheshimwa Naibu Spika, kwa hiyo kila atakayeingia maana yake ataingia na vipaumbele vyake na vipaumbele hivi ni vyema, lakini labda muda ule ambao tunakuwa tunawapa viongozi wetu ni mfupi. Akiingia mwingine akaingia na lingine maana yake bidii yote, resources zote zilizokwishatumika zinaishia pale, tunaanza na vitu vingine, kitu ambacho tunapoteza rasilimali nyingi. Hata hivyo, wananchi wetu watashindwa kuelewa majukumu yao Kitaifa ni yapi, Taifa letu linatoka wapi linaenda wapi, tujikite wapi na tukiwa na vipaumbele hivi itasaidia sasa Serikali nayo kuhakikisha kwamba inachukua steps za msingi. Let say tumesema sasa hivi ni Serikali ya viwanda na mkondo wetu Kitaifa ni viwanda maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, Serikali itahakikisha kwenye suala la viwanda inaondoa urasimu wote, inarekebisha au kufuta baadhi ya kodi ili wavutike na kuingia kule kwenye viwanda. Tukikaa na mkondo huu kwa miaka 20 maana yake viwanda nchi kwetu, by the time tunabadilisha kwenda kwenye kipaumbele kingine viwanda vimesimima na nchi yetu kwenye suala hilo imekwishakaa vizuri. Kwa hiyo, naomba Serikali ikae chini, iangalie kwamba vipaumbele vyetu ni vipi na wananchi waambiwe na waambiwe majukumu yao na Serikali iji- dedicate kwenye vipaumbele hivyo kuhakikisha inavirahisha kiasi ambacho mwananchi yeyote yule ana uwezo wa kuingia na kufanya kazi katika vipaumbele hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwetu sisi vijana imekuwa changamoto sana kuingia kwenye hizi biashara kwa sababu bado hakuna urafiki wa kukaribisha mtu anayeanza biashara au anayeanza uwekezaji kwenye nchi yetu. Mtu akiingia mtaji wenyewe ame-struggle, amekopa halmashauri, kakopa benki, dhamana inasumbua, lakini akiingia nusu robo tatu yote inatakiwa iende ikalipie leseni, ikalipie kodi na vitu vingine, kwa hiyo tunawakatisha tamaa. Tuki-define vipaumbele vyetu, maana yake mtu anajua sasa hivi kuna urahisi wa kwenda huku, wananchi wote wanajua tunaelekea wapi na nini tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano kutoka kwenye Nchi ya Thailand; ukifika kwenye nchi ile, ukishuka tu Airport unaulizwa hii ni mara yako ya kwanza kufika au wewe ni mwenyeji hapa. Ukisema ni mara yako ya kwanza unaanza kupewa vipaumbele; nchi yetu ina hiki, hiki na hiki , kabla hujaondoka tafadhali tembelea hapa na hapa, maana yake ni uzalendo ambao wananchi wa kawaida wamekwishajiwekea kwa kutambua vipaumbele vya nchi yao wapi inakwenda na wanaitangaza kidunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo machache, la mwisho kabisa nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimwa Rais kwa msimamo mzuri alioutoa katika hotuba yake ya mwisho juu zima ya suala ya bando au mitandao. Vijana wengi pamoja na kuwa ajira ni changamoto, wengi tunatumia sana sana mitandao hii kujiajiri. Tunafanya biashara za mitandaoni, lakini hata pia kwenye kusoma, tunasoma kupitia mitandao, lakini hata kwenye sanaa na michezo, wasanii wetu wanategemea kupitia you tube na namna nyingine zingine zote ndio sisi tukaona kazi zao na kuzinunua. Kwa hiyo kidogo changamoto hii ilikuwa inatupeleka kwenye shida kubwa sana na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na niombe Wizara hii husika basi iliangalie suala hili ili lisije likajirudia tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kukushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nianze kwa ku-declare interest, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na hivyo nianze kwa kuipongeza Wizara hii ambayo imefanya kazi kubwa sana katika kuboresha miundombinu ya mahakama. Mahakama zimejengwa, mahakama jumuishi zinazojali haki za binadamu usawa wa kijinsia na haki za watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, nizidi kupongeza Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya. Tunatambua kwamba, wamekuwa na mifumo mingi ambayo imeanzishwa ikiwemo mifumo ya mitandao, mahakama za kimtandao ambayo itasaidia sana sana wananchi wetu kwenye suala zima la upatikanaji wa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu wa leo kwa kutoa tu ushauri. Langu leo ni ushauri. Kila kinachofanyika kwenye nchi hii ni katika misingi ya sheria na kanuni, maana yake sisi wote tuko hapa leo kwa sababu kuna sheria au kuna kanuni inaturuhusu kuwepo hapa na kufanya haya tunayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa mfano wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali au CAG. Ofisi hii imepewa mamlaka chini ya Ibara ya 143 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ofisi hii kazi yake au jukumu lake kubwa, ni kudhibiti na kukagua mipango yote na matumizi ya pesa za Serikali katika Taasisi zote kuona kama zinatumika kama mipango yote ilivyowekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wote na sisi Wabunge tunakuwa tuna imani kwamba, kila kitu kinakwenda sawasawa pamoja na mipango yote ya pesa mpaka tutakapopokea ripoti hii ya huyu Mkaguzi, ituonyeshe either kuna sehemu pesa hizi hazikutumika vizuri au kuna sehemu zilipelekwa kinyume na utaratibu au kuna sehemu zimetumika vizuri au kuna sehemu labda tunapata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoa mfano huu, lakini sasa nirudi katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Inabidi tujiulize ni chombo gani, Taasisi gani au ni mtu gani mwenye mamlaka ya ku-assess whether sheria tunazotunga kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatekelezwa sawasawa na maelekezo ya sheria hizo. Pia ni Tume gani inayoangalia kwamba, sheria hizi either zinakuwa zinawapa haki wananchi, au zinawakandamiza, au sheria imekuwa short kwa kitu fulani tuiongeze wigo sehemu fulani au tuipunguzie mamlaka sehemu Fulani. Pia tunaweza kuona kwamba, Tume fulani iliyotengenezwa kwa mujibu wa sheria inafanya kazi zake sawasawa au haifanyi kazi zake sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba, jukumu la kutunga sheria lipo ndani ya Bunge hili Tukufu, lakini kuna principle ya natural justice inayosema kwamba, you cannot be a judge of your own case. Ni chombo gani kinachotuonesha kwamba sheria tulizopitisha sisi kama Bunge, zinafanya kazi yake sawasawa au zinafuatwa sawasawa kule nje. Tunatambua kwamba, kuna chombo ambacho ni mahakama, mhimili ulioanzishwa kwa ajili ya ku- enforce sheria hizi, lakini mahakama tunatambua wote kwamba, haiwezi ika-move on its own motion lazima iwe moved na mtu, either kuna mgogoro umetokea au kuna mtu anaenda kutafuta tafsiri ya sheria mahakamani. Vile vile tuangalie je, kuna sheria ngapi ambazo tumezitunga leo hii ni source ya grievance nyingi sana kwenye jamii yetu na si wote tuna nguvu ya kwenda mahakamani kufungua kesi kwa ajili ya kupata tafsiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba, Bunge hili mwaka 1980 lilitunga Sheria ya kuanzisha chombo kinachoitwa The Law Reforms Commission, ambacho kimsingi majukumu yake ni haya sasa; ya kuonesha kwamba, sheria zinazotungwa zinaendelea kuendana na wakati? Au sheria zinazotungwa zinatekelezwa sawasawa wapi tuongeze, wapi tupunguze maana yake kulishauri Bunge na Serikali sheria zetu ziendeje?

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo hiki nasukumwa kusema bado hakijafanya kazi yake sawasawa, aidha kuna upungufu wa bajeti au kuna upungufu kwenye utendaji wa chombo hiki au composition ya chombo hiki. Nitoe mfano, kuna sheria kwa mfano, sheria inayo-deal na Bodi ya Mikopo. Kuna mambo mengi sana ambayo Wabunge wengi wamesimama na kuzungumza juu ya Sheria hii ya Bodi ya Mikopo. Suala zima la kupandisha interest kutoka asilimia nane (8) kwenda 15. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo hiki kingekuwepo hili lilikuwa ni jukumu lake la ku-assess na kuihoji Serikali kwamba, justification ya kutoa asilimia nane interest kwenda 15 imepatikana wapi? Je, kima cha chini cha mshahara wa Kiserikali tukitoa asilimia 15, tukatoa PAYE, tukatoa makato ya NSSF au PSSSF kinamtosha kijana kuweza kumudu maisha yake na ndio maana tukatoa nane kwenda 15? Pia, chombo hiki kingekuwa na mamlaka ya kuihoji Serikali katika utungaji wa sheria hii, ni wapi wamepata justification ya kuweka asilimia sita kama retention fee ya mikopo hii, wakati tunajua kwamba inflation ya pesa yetu katika nchi yetu mwaka 2019 tulikuwa na 3.4 percent, 2020 tulikuwa na 3.2 na mwaka 2021 mpaka Machi tumekuwa na kama 3.2 mpaka sasa Machi mwaka huu, lakini wenyewe tumewekewa asilimia sita kama kulinda thamani ya pesa hii, justification hii imetoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, justification nyingine ya kuweka grace period ya miaka mwili ndio mtu aanze kulipa, je, tumekusanya takwimu za kututosha ili kuona kwamba katika nchi hii kijana akihitimu ana window ya miaka miwili tu atakuwa amepata ajira! Kuna watu wanakaa mpaka miaka saba mpaka 10 hawajapata ajira. Maana yake chombo hiki kingekuwa na uwezo wa kuhoji utekelezaji wa baadhi ya sheria, ikatupa maoni yake na kikawa na nguvu na ripoti hizi zikaletwa Bungeni tukazijadili na zikatumika kama ushauri wa moja kwa moja kuli-guide Bunge na kui-guide Serikali namna gani tunarekebisha sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe mfano wa mfumo mzima wa upatikanaji wa haki hasa kwenye mfumo wa makosa ya jinai. Mahakama zetu zina mamlaka ya kutoa hukumu ya mwisho, lakini hazina mamlaka ya ku-guide namna gani uchunguzi au investigation zinafanyika kule kwenye hizi kesi zetu. Kwa hiyo, unakuta kuna kesi inakaa miaka miwili, mitatu, minne au mitano bado uchunguzi unafanyika, aidha mtu yuko ndani au yuko nje, lakini anazidi kupoteza muda wa msingi wa kuwa anahudhuria mahakamani kila siku na haki yake haijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo hiki kingekuwa na mamlaka ya moja kwa moja kutuonesha kwamba, wapi turekebishe, wapi tuongeze nguvu katika mahakama zetu ili ziweze kusukuma vyombo vya kufanya uchunguzi wa haraka. Chombo hiki kingetuonesha kwamba kwenye sheria labda kuna makosa tuweke time limit investigation, ili iwabane watu wale wafanye uchunguzi kwa muda mfupi ili haki za watu ziweze kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii ni kuonesha kwamba chombo chetu cha Law Reforms Commission kipo na majukumu yake yapo kisheria lakini hakijafanya kazi yake sawasawa. Mmigogoro mingi inayotokea kati ya Serikali na wananchi ni katika utekelezaji wa sheria. Sheria zetu zipo, ndio kuna baadhi zina upungufu lakini zile ambazo zipo sawasawa, labda hazitekelezwi sawasawa huko kwenye jamii zetu. Chombo hiki kingekuja na ripoti ya kila mwaka kama sheria inavyosema, ili kutueleza kwamba sheria hizi ziko hivi, lakini hazitekelezwi na wapi turekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuatilia, ni muda wa miaka mingi sana tangu chombo hiki kitii takwa la kisheria la kuleta ripoti yake kwenye Bunge hili Tukufu. Nimekwenda kwenda Kitengo cha Hansard wameshindwa hata kupata record halisi ya lini ripoti imepokelewa hapa Bungeni, kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Ripoti ya CAG inapokelewa kila mwaka na inatu-guide kama Serikali kuona kwamba wapi mapato yetu hayakwenda vizuri, wapi turekebishe, wapi tufanye vizuri zaidi. Kwa hiyo, naishauri Wizara hii ya Serikali kuangalia namna ya kukifufua chombo hiki, aidha tukifumue tukiweke sawa ili kipate nguvu ya kuwa kinaleta ripoti katika Bunge hili Tukufu, ili tuweze kuona utekelezaji wa sheria unakwenda kama ambavyo sheria zetu zimetungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niipongeze tena Wizara hii, kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake ambao unaendelea kufanyika na tunaamini kwamba kama Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 inavyotuelekeza, hasa katika ukurasa wa 167 upatikanaji wa haki utaendelea kuwepo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii ya kuchangia katika wizara hii, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza wizara hii na watendaji wake wote kwa hatua hii ya utendaji ambayo imefikia lakini pili niungane na Mheshimiwa Eshi kukipongeza Chama changu Cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa kilichopata kule mkoa ni Kigoma katika jimbo la Mwihambwe na Bwihigwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto ya ajira tuliyonayo vijana katika nchi hii, sehemu ya kandarasi ni moja ya sehemu ambazo vijana wengi wamejikita katika kutatua changamoto hii ya ajira. Lakini bado pamoja na juhudi hii wanayoifanya kujiingiza katika sehemu hii wanachangamoto nyingi na changamoto kuu ambayo tunakutana nayo ni ukosefu wa mitaji na ujuzi wa kutosha kujiingiza katika kazi hizi za ukandarasi hasa ukandarasi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inanifanya nijiulize ni lini hasa au Serikali inadhani ni lini hasa tutaendelea kutoa asilimia zaidi ya 70 ya kazi zote ambazo zinazofanyika katika nchi hii kwenda katika makampuni ya kigeni ili hali asilimia kumi tu ya makampuni yaliyosajiliwa ndio ya kigeni hii ni aibu sana. Nadhani ni wakati sasa Serikali ijihoji kwamba tuna mkakati gani wa miaka 2, 3, 4, 5, 10 au hata 50 kwa kuhakikisha kwamba na sisi itafika wakati wakandarasi wa kitanzania watafanya kazi zetu za hapa ndani kwa asilimia 70 na wakandarasi wa nje wafanye kwa asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ilani yetu ya uchaguzi tuliyotumia kuomba kura zaidi ya asilimia 90 ya Wabunge tulioko katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 72 ni kushirikisha kikamilifu vikundi vya wanakijiiji na wananchi pamoja na makandarasi wadogo katika kazi za matengenezo madogo ya barabara kama vile kufyeka nyasi kuzibua mifereji mitaro ya barabara na kufanya usafi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, “pili, kuendelea kuwajengea uwezo wakandarasi wazalengo ikiwemo kuwapatia kazi nyingi zaidi za fedha za mifuko ya barabara na kuwawezesha kupata mikopo ili kushiriki kikamilifu kwenye kazi kubwa za ujenzi wa barabara, madaraja na majengo.” Maana yake tuliwaahidi vijana, hasa wakandarasi, kwamba kazi yetu ndani ya miaka hii mitano itakuwa ni kuhakikisha tunawajengea uwezo wa kushiriki katika kandarasi, hasa kandarasi kubwa, lakini pia kuwasaidia ili waweze kukopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika changamoto hii ya mitaji, kwa kiasi kikubwa imechangiwa na Serikali yenyewe. Tunatambua kwamba kazi hizi ni kazi ambazo zinahitaji mitaji mikubwa na labda wengi wetu hatuna, lakini Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha inatubeba sisi vijana na kutuwezesha hivyo hivyo kushiriki katika kazi hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi yao wamejitahidi, wametuafuta hela huku na huku ikiwemo kukopa katika benki za kibiashara kuingia katika kazi hizi, lakini shida inakuja kwenye vipaumbele vya kulipwa. Kwa vile wageni katika kampuni zao wanakuwa wana-raise invoice kila baada ya mwezi na kudai interest katika invoice zile zisipolipwa kwa muda, Serikali yetu inawalipa wao kama kipaumbele kuliko kuwalipa wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo imekuwa changamoto zaidi ya kuua mitaji ya vijana hawa. Huyu mtu kakopa kwenye benki ya kibiashara, anatajiwa riba kila anavyozidi kuchelewesha malipo; na imefikia hatua mikataba wanayopewa Wakandarasi wetu wa ndani haiaminiki tena kwenye benki zetu na taasisi za fedha. Mtu hawezi kupeleka mkataba ule akapewa pesa ya mkopo ili aje afanyie kazi. Kwa nini? Kwa sababu Serikali haiwalipi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mtu hana hata pesa ya kula, lakini anakwambia anadai Serikalini shilingi milioni 500. Ni kitu cha aibu sana. Wakati makampuni ya nje tunayalipa kwa wakati, wazawa tunawaacha pembeni, inatia mashaka kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili suala la kuhakikisha kwamba tunawashirikisha…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Engineer. Mwanaisha Ulenge.

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Ng’wasi kwamba anachosema ni kitu sahihi. Siyo tu kwamba Wakandarasi hawa wazawa wa ndani wanachelewa kulipwa, lakini pia Wakandarasi wazawa wa ndani hawana jeuri ya kumwomba client interest. Ile 14.7 billion aliyoisema CAG, ile ni ya Wakandarasi wa nje. Wakandarasi wazawa wanaogopa kudai hata interest kwa sababu wanaogopa kukosa kazi kesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo. Naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo inapatikana kwenye kushirikisha hivi vikundi vidogo vidogo vya wananchi kwenye kazi hizi, hasa kazi ndogo ndogo ni kwamba, kwanza hakuna mikataba inayoeleweka wanayopewa watu hawa kabla ya kupewa kazi hizi na wengi wanaishia kukimbiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea na baadhi ya Wabunge wa Majimbo, pesa nyingi wanaishia kulipwa wao kwa sababu wale Wakandarasi wanawapa kazi hizi ndogo ndogo, wanaishia kuwakimbia. Kwa hiyo, nashauri Serikali iangalie utaratibu wa kuweza kuvilinda vikundi hivi vidogo vidogo vinapokuwa vinapewa kazi na wakandarasi wakubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye bidding process; tunatambua kwamba tenda hizi zinatolewa kwa uwazi, watu wanakuwa na uhuru wa ku-bid freely, lakini tukiangalia Wakandarasi wetu wa ndani na wa nje, wa kwetu wako kwenye disadvantage kubwa kuliko wa nje. Kwa sababu wa nje kwanza kabisa wanapewa support kubwa sana na Serikali zao, kitu ambacho hakipo katika kandarasi zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili, watu hawa wana- bid kwa bei ya chini wakiwa wameshajua kwamba upungufu wa ulipaji uliopo kwenye mifumo yetu ikoje na wanategemea faida wataitengeneza kwenye interest, kitu ambacho Mtanzania hana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri ni wakati Serikali iangalie namna gani inafanya juhudi ya makusudi kutekeleza yale tuliyoahidi kwenye ilani yetu kwa kuwapa support, kuwawezesha Wakandarasi wa ndani, kuhakikisha wanawapa kipaumbele kwenye malipo ili waweze kukua na mwisho wa siku basi tuone asilimia za Wakandarasi wanaofanya kazi zetu za ndani ni watu wetu wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, tumeahidi kwenye ilani kwamba tutazidi kuwawezesha kuwapa kazi nyingi zaidi. Hapa kwenye hili, naomba Serikali kuangalia kwa umakini sana tunavyokwenda na hili suala. Sekta binafsi ni ya msingi sana kwenye maendeleo ya Taifa lolote lile, lakini sasa baada ya kuwa kandarasi nyingi za ndani zinasumbua kwenye ufanyaji wa kazi ikiwa ni pamoja na kazi kuishia njiani kwa sababu hawana pesa au wamecheleweshewa pesa, Serikali sasa ime-resort kwenye kutumia taasisi zake binafsi kufanya kazi hizi. Hilo ni jambo jema, kwa sababu najua Serikali haicheleweshi malipo kwenye taasisi zake zenyewe, lakini hii inakwenda kuua wakandarasi binafsi, inaua sekta binafsi ya wakandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, badala ya kuwanyang’anya kazi na kuzipa kazi taasisi za Serikali kama TBA, SUMA JKT, basi tuangalie namna gani ya kuwasaidia kuondoa changamoto walizonazo, ili basi tuendelee kuwakuza na sekta binafsi ikue zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kuna huu mfuko wa kudhamini Wakandarasi wadogo ambao ndiyo Serikali iliuanzisha kwa ajili ya kuwakomboa kwenye suala zima la mtaji, lakini Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mfuko huu una shilingi bilioni 3.9 pekee mpaka sasa tangu uanzishwe na Wakandarasi walio ndani yake ni 1,167. Haitoshi kabisa kuwapa mtaji Wakandarasi hawa kufanya hizo kazi. Kwa hiyo, pia tunaomba Serikali iangalie katika bajeti hii namna gani inaongeza pesa katika mfuko huu ili Wakandarasi wa ndani wengi zaidi wapate kunufaika nao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye hizi kazi; tunashukuru Serikali imefanya kazi nzuri ya kuhakikisha wazawa wanaajiriwa zaidi kwenye kazi hizi za ukandarasi, lakini basi tunaomba iangalie namna gani wahusika wa eneo husika waweze kuwa wanufaika wa kwanza wa zile kazi zinazofanyika kwenye maeneo yao. Kwa mfano, tuna reli ambayo sasa hivi inatakiwa kujengwa kutoka Mwanza kwenda Isaka. Basi watu wa Mwanza na wa kanda ile wawe wanufaika wa kwanza wa tenda na kazi zinazopatikana kutoka katika reli ile, sambamba na maeneo mengine yote. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi ya kusema, nitayachangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa siku, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii. Lakini pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wanafanya kuendelea kuimarisha mahusiano yetu na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kwa kutoa takwimu ndogo iliyotolewa na Benki ya Dunia ambayo inaonesha kwamba kati ya mwaka 2018 mpaka mwaka 2030 idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwenye nchi zenye uchumi wa chini na uchumi wa kati itaongezeka kwa idadi ya milioni 552. Lakini idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwenye nchi zenye uchumi wa juu kwa kipindi hiki hiki, itashuka kwa idadi ya watu milioni 40.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba nadhani ni wakati Serikali yetu, hasa Wizara hii tunayoichangia leo, ikaanza kuangalia ni namna gani tuta-tackle ongezeko hili la watu kwenye nchi yetu ambayo itakuwa ni general kwa Bara letu, lakini pia tutatumia vipi fursa ya upungufu wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwenye nchi za wenzetu ili kuweza ku-facilitate Watanzania kwenda kuziba pengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kuishauri Wizara hii iangalie namna gani inaweza kushirikiana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba ifikapo muda ambao gap hili tunaanza kuliona kwa ukubwa basi watu wetu wa Tanzania wawe na skills za kutosha kuweza kukidhi nafasi hiyo, hasa vijana wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia takwimu hizi hizi zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2050 mazingira ya Kiafrika yatakuwa uninhabitable kwa maana ya mabadiliko ya tabia nchi kama tusipochukua hatua za kutosha kurekebisha shida zilizopo katika mazingira. Maana yake hii pia inaiamsha Wizara hii kuangalia kwamba ni namna gani sasa tunatumia mahusiano yetu ya kimataifa kuhakikisha kwamba watu wetu wanaweza kufaidika na mahusiano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kutaka kujua kutoka kwa Wizara hii ina mikakati gani ya kuhakikisha kwamba ina-scout vya kutosha kupitia Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali, fursa mbalimbali, mikopo na grants ambazo zinaweza zikatumiwa na vijana wetu wa Kitanzania kujinufaisha na mahusiano ambayo tumeendelea kuyajenga kwa gharama kubwa na kwa muda mrefu kati ya nchi yetu na nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni namna gani Wizara hii inajenga hamasa kwa Watanzania hata fursa hizi zinapopatikana wazichangamkie. Lakini si kuwahamasisha tu, bali kuendelea kuwajengea uwezo ili hata wanapopata fursa hizi wazitumikie ipasavyo na kuweza kuifaidisha nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kwamba mahusiano tuliyonayo kati ya nchi yetu na nchi zingine itufaidishe sawasawa na inavyowafaidisha wale tulio na mahusiano nao. Lakini pia sisi vijana wa Tanzania tunategemea sana kupata taarifa ya fursa zote zilizopo katika nchi nyingine kupitia Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni jambo la kusikitisha kwamba hata ukiingia kwenye website ya Wizara hii, fursa wanazoelezea ni zile ambazo zinapatikana ndani ya nchi yetu. Hakuna sehemu ambayo mimi kijana wa Kitanzania nitakwenda kwenye website ya Wizara hii nipate kujua fursa zilizopo nchi nyingine ili mimi niweze kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si tu kuona hizo fursa, hata nione kwamba kuna nini nchi gani, lakini hata niende kwa nani, niende wapi, niwasiliane na nani, ili niweze kupata fursa hizi. Kwa hiyo, sisi kama vijana wa Kitanzania tunaomba Wizara hii iboreshe mifumo yake ya taarifa ili tuweze kupata taarifa ya fursa zote zinazopatikana kule na tuzichangamkie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia Wizara hii iangalie namna gani tunakuza wingi wa watu wetu wanaokwenda kufanya kazi katika nchi za wenzetu ili tuongeze mapato na si mapato tu, tuongeze pia skills, knowledge na technological transfer kutoka kwenye nchi za wenzetu kuja kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama vijana tunasema sawa, pesa tunapata kama mapato, japo hata ukilinganisha remittances tunazopata Tanzania ni tofauti sana na zile ambazo nchi nyingine zinapata. Mfano mdogo mwaka 2018 Nchi ya Egypt imepata kipato cha USD bilioni 28.9 kama remittance kutoka nje. Nigeria mwaka huohuo wamepata dola bilioni 24.3. Wakati nchi yetu ya Tanzania kwa mwaka huo ime-register kipato cha dola milioni 365.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wanaongelea dola bilioni ishirini na kitu, sisi hata bilioni moja hatujafika. Maana yake ni kwamba hatutumii vizuri mahusiano tuliyonayo na nchi nyingine, tunayoendelea kuyajenga kwa kutumia kodi za Watanzania kujinufaisha kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ni wakati sasa Wizara hii iangalie, mahusiano haya tunayoyajenga, je, yana manufaa kwetu? Je, ni mahusiano ya kimkakati? Na kama ni hivyo, basi kuanzia sasa tuanze kutengeneza mahusiano ya kimkakati ambayo tunajua as much as tunawafaidisha wengine na sisi Watanzania tunafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na faida zinazopatikana zimguse Mtanzania, ikiwa ni pamoja basi na kuangalia namna gani tuna-bridge gap ya ajira kwetu kwa kuwachukua watu wetu waende ili wazidi kuturudishia mapato zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuongelei tu suala la mapato, tunaongelea pia suala la technology, suala la knowledge na skills. Nchi za wenzetu wanakwenda mbali kuanza kuchukua watu kuanzia ngazi ya chini wakiwa na umri mdogo kwenda kuwafundisha kwenye nchi za wenzetu ili wapate knowledge na technology waturudishie kwenye nchi zetu. Tanzania bado mpango huo uko chini kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mahusiano tunayoyajenga tunayajenga na nchi husika lakini siyo na Watanzania walioko kwenye nchi husika. Inasikitisha sana kwa mfano nchi ya Finland kwenye Kampuni ya Nokia, zaidi ya asilimia 80 ya ma-engineer walioko pale ni Watanzania, lakini kitu kinachoonesha kwamba hatuna mahusiano nao mazuri ni kwamba mpaka leo hatuna hata kampuni ya simu kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tungekuwa na mahusiano nao mazuri maana yake wangeweza ku-transfer technology hiyo, wakaja hapa na kutupa hiyo teknolojia basi tukazidi kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri na Wabunge wenzangu wengi wameshauri tuwe na database ya kuonesha idadi ya Watanzania wetu waliko nje, na si kuwa na database ya ujumla, database hii tui-cluster kwa maana ya kutenga watu wenye profession fulani, watu wenye kazi zingine kulingana na umuhimu wao ili tujue tunawa-support vipi watu hao na watatuletea nini kwenye nchi yetu, hivyo ndivyo tunavyoweza kunufaika na mahusiano yetu na nchi zinazotuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze, tumefungua Consulate General Lubumbashi, lakini utajiuliza taasisi zipi za Kitanzania au makampuni yapi ya Kitanzania yanasaidiwa na Wizara hii kwenda na yenyewe kufungua au kuanza kufanya kazi zake katika nchi za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua kwamba tuna taasisi nyingi za kifedha, kwa mfano tuna CRDB, NMB, NBC, taasisi ambazo zina nguvu na uzoefu, hata nguvu ya kifedha pia inajitosheleza. Lakini taasisi za kifedha ambazo zinafanya kazi kwenye nchi zingine zote ni taasisi za Kikenya, tuna Equity Bank, KCB na hata Mtanzania akitaka kufanya kazi, japokuwa tuna Ubalozi Kenya, akifika mpakani anaachana na benki za Kitanzania anaanza kutafuta namna ya kufanya kazi na benki za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwape nguvu hata taasisi zetu na zenyewe zisambae kwenda kwenye sehemu mbalimbali ambao tuna mahusiano nayo ili kukuza uchumi wa nchi. Kwa hiyo, bado rai yangu ni kwamba mahusiano tunayoyatengeneza yasiwe mahusiano tu ya diplomacy bali tuwe na faida kwenye mahusiano hayo. Na faida hizi basi tuzitengeneze kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia Wizara hii na Mama yetu Samia Suluhu Hassan, juzi tumempokea mfanyabiashara mkubwa Dangote, hilo ni jambo zuri sana kwa sababu anasaidia kuwekeza na kujenga ajira. Lakini hii iwe ni kama wake up call. Tuna wafanyabiashara wakubwa sana kwenye nchi yetu, namna gani na sisi tunaweza kuwa-promote kwenda kuwekeza na kutambulika kwa ukubwa kwenye nchi zingine kama sisi tunavyowatambua wafanyabiashara wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi kama wamekwenda kuwekeza, je, Serikali ina mkono kwenye uwekezaji wao au wamekwenda kuwekeza kwa nguvu zao wenyewe, na hata baada ya wao kwenda kuwekeza kule, Serikali inawashika vipi mkono. Kwa hiyo haya yote ni mambo ambayo lazima tuyaangalie na tusiwe tu tunakaribisha wawekezaji wa nje kuja ndani bila sisi kutoa wawekezaji wetu wa Kitanzania waende wakawekeze nje, hiyo ndiyo namna ambayo tutakuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika mjadala huu wa Mpango wa Mwaka Mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kuu itakuwa kuwazungumzia wapigakura wetu walio wengi katika nchi hii ambao ni vijana. Changamoto namba moja, ambayo nitaendelea kuipigia kelele ambayo ni ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu, ndani ya muda mfupi ambao ameingia vijana ni kundi ambalo ameendelea kulibeba, ameonekana kutokulisahau na hata katika maamuzi mbalimbali ameendelea kutukumbuka. Kwa hilo tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna mambo machache tu ambayo ningependa katika Mpango huu ambao ni wa mwaka mmoja basi tuyazingatie kwa kuangalia vijana hawa. Kama tunazungumzia asilimia zaidi ya 60 ya watanzania wote ambao ni vijana, maana yake tulitegemea discussion kubwa may be asilimia zaidi ya 30 ya Mpango huu uwe unalenga kuliangalia kundi kubwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwenye hili hasa katika suala hili la ajira niongelee mambo machache. La kwanza, tangu Mheshimiwa Rais ameingia madarakani kwa hii miezi sita kuna ajira nyingi sana zimeshatangazwa zaidi ya ajira 5000, katika taasisi mbalimbali kuna TANAPA, TAKUKURU, POLISI, TRA tunashukuru sana. Kwa hilo, tunashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna vigezo ambavyo vimekuwa vinajumuishwa kwenye qualification za watu wanaotakiwa kuomba ajira hizi, ambazo kwetu sisi vijana tunakiri kusema kwamba zinatutatiza kidogo. Kwa mfano; kuna kigezo cha mtu awe amekwenda National Service au JKT. Tukiangalia katika Nchi yetu, kwanza kabisa nafasi za JKT zinazotangazwa huwa ni chache ukilinganisha na idadi kubwa ya vijana tuliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mbili hata wale ambao wana ule mfumo wa kutoka form six kwenda JKT bado Serikali yetu haiwachukui vijana wote. Kuna baadhi ya miaka vijana wamechukuliwa kulingana na division zao kwamba, mwenye division one na division two peke yake ndiyo watakwenda. Lakini kuna baadhi ya miaka wamechukuliwa vijana kwa alphabetical order ya majina yao. Kwamba, kwenye wale wenye walioanzia A labda mpaka J ndiyo watakwenda wanaobaki wanabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, naona inasikitisha sana kama tukianza kutoa ajira kwa vijana kwa kuwahukumu kulingana na alphabetical order ya majina yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba kwa vile ninaanziwa na N basi ajira fulani fulani nizisahau au kwa sababu nilipata division three, lakini qualification zote ninazo basi ajira fulani fulani nizisahau. Kigezo hiki si sawa na kama Serikali yetu ilikuwa inaona kwamba ni muhimu kutangaza ajira kwa vigezo vya namna hii, basi ingeanza kwanza kutengeneza mazingira ya vigezo hivi ndiyo twende kwenye ajira kulingana na vigezo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadiriki kusema kwamba tukiendelea na vigezo kama hivi tunavunja Katiba yetu hasa Ibara ya 13(4), ambayo inakataza Kitengo chochote cha Serikali au Mamlaka kutoa maamuzi yoyote ambayo yataleta ubaguzi kwa watanzania kwa namna yoyote ile. Kwa hiyo, nashauri kuanzia sasa Serikali yetu iangalie, tunapokuwa tunatoa ajira au fursa kwa vijana wetu, ili wote tuweze kuzi- access kwa usawa basi tuangalie vigezo ambavyo vina maana na ambavyo vina maslahi katika utekelezaji wa ajira hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili ni suala zima la mitandao. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu miezi kadhaa iliyopita, hali ya hewa ilichafuka kidogo baada ya gharama ya mitandao kupanda na akatoa maelekezo kwamba gharama hizo zirekebishwe lakini suala hili lisijitokeze tena. Sisi vijana tunatumia sana mitandao siku hizi kujiajiri, na hii imeipunguzia sana Serikali mzigo wa kutuajiri sisi vijana. Lakini si kujiajiri tu, tunatumia pia mitandao hii kusoma kwa hiyo inachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto iliyokuja ni kwamba baada ya Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo kwamba hali hiyo irekebishwe na isijirudie tena, imeanza kurudishwa kidogo kidogo, kidogo kidogo, mpaka sasa tunavyozungumza imerudi hali ile ile aliyoikanya Mheshimiwa Rais. Nitoe tu mfano kidogo kwamba katika takwimu zilizotolewa na TCRA kwa mfano mdogo tu wa mtandao wa Airtel. Gharama ya MB 1 kwa takwimu za robo mwaka kwa Disemba, 2020 ilikuwa ni shilingi 5/= kwa MB 1 kwa mtandao wa Airtel. Robo iliyofuata ambayo ni Machi, 2021 ilibaki hivyo hivyo shilingi 5/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Juni, 2021 imepanda mpaka shilingi 9/= almost twice na kwa vile tu TCRA hawaja upload taarifa ya robo iliyofuata ambayo inakwisha mwezi Septemba, 2021. Maana yake tunategemea itakuwa imepanda zaidi, ni ngumu sana kwa kijana wa Kitanzania ambaye anategemea mitandao hii kujiajiri. Kutumia gharama kubwa namna hii ambayo haistahimiliki kuweza kufanya shughuli zake na kimsingi, Serikali inakuwa imeshindwa kabisa kumsaidia Mtanzania kijana wa kitanzania kutengeneza mazingira bora ya kujiajiri mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha zaidi ni kwamba Serikali yetu pia ni shareholders kwenye mitandao hii ya simu. Kwa hiyo, ina nafasi kubwa sana pia ya kutusemea na kutusaidia kutengeneza mazingira bora ili vijana tuweze kuendelea kujiajiri kupitia mitandao hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizidi kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na ama kweli ni haki kusema kwamba tumepata mama mtafutaji kweli kweli. Mama atakwenda akirudi anawaambia nimerudi na kijisenti hiki kidogo tutagawana hivi tena kwa uwazi kabisa. Hilo tunamshukuru sana na kwa kweli sisi kama vijana, anazidi kutupa imani ya kwamba miaka hii minne inayofuata itakuwa ni miaka ya neema kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hayo nilitegemea basi, kulingana na fedha hizi za Covid ambazo tumepata, tumepata madarasa 15,000 ya Sekondari, tumepata Shule Shikizi madarasa kama 3000, tumepata ambulance 395. Lakini pia, kwa fedha za tozo hizi hizi kwa maarifa ya Mheshimiwa Rais tunapata pia madarasa mengi sana katika shule zetu za Misingi na Zahanati. Basi nilitegemea katika Mpango huu wa mwaka mmoja wa bajeti unaofuata tungeona basi Serikali yetu kwa kuangalia pia tuliwaahidi wapiga kura, tuliwaahidi vijana hawa ajira milioni 8 tuone ajira ambazo zitapatikana. Hasa za walimu, madereva na wauguzi au watendaji katika Sekta ya Afya zinakuwa reflected katika Mpango huu, hasa kwa mwaka unaofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo nita-subscribe kwa alichokisema Mheshimiwa Kingu jana kwamba, tutatibu kitu kimoja lakini tutazalisha changamoto nyingine ya kutokuwa na ubora. Either katika elimu au katika Afya kwa sababu tutakuwa na madarasa mengi, wanafunzi wengi bila kuwa na watumishi wa kutosha. Ninaomba tukuze imani ya vijana hasa kwa Serikali yetu kwa kuakisi hizi juhudi za Mheshimiwa Rais. Katika Mpango huu tuoneshe namna gani Serikali imejipanga kutangaza ajira za kutosha kwa walimu, kutangaza ajira za kutosha kwa wauguzi na madereva. Ili tuzidi kuiamini Serikali yetu na vijana tujiandae kuweza kukidhi matakwa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nimalizie, wakati Wabunge wengi wanazungumza, wamezungumza juu ya vipaumbele na mimi nikinukuu mchango wangu katika Mpango uliopita wa Bajeti iliyopita, niliomba kwamba ni muhimu Serikali yetu ikaja na vipaumbele ambavyo vitatuongoza katika mipango yote tunayotengeneza. Wabunge wengi wamekwishazungumza kwamba ni matakwa yetu kama wawakilishi wa wananchi tulitaka kipaumbele kiwe Kilimo. Sasa katika kilimo mwaka huu, mwaka 2021 Mpango wa Taifa wa kuwashirikisha Vijana katika Kilimo ndiyo unamalizika na umekwisha malizika Oktoba, 2021. Mpango huu ulikuwa unaanza 2016 – 2021 na kuna observation fulani zimeonekana katika Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya observation hizo ni kwamba kilimo it is not attractive kwa vijana kushiriki katika Sekta ya Kilimo katika Nchi yetu. Sasa nilitegemea kwa vile Mpango huu umekwisha, basi huu Mpango unaofuata wa mwaka huu ungetuonyesha kwamba, sasa tu-test mafanikio ya huu Mpango wa miaka minne uliofanyika wa kuwashirikisha vijana katika Kilimo. Lakini pia una Mpango gani mpya sasa baada ya kuangalia mafanikio ya Mpango huu, wa kuhakikisha kwamba basi kilimo kinaanza kuwa- attract vijana ili wote tuweze kushiriki. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwasi.

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye mpango wetu huu wa mwaka 2024/2025. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya yeye pamoja na wasaidizi wake Mawaziri na Manaibu Waziri, wanafanya kazi nzuri na kubwa kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaongozwa na dira na mipango ya miaka tofauti tofauti. Kuna mipango ya miaka mitano, miaka kumi na tano, miaka 30 na mpaka miaka 60. Hii mipango ya mwaka mmoja mmoja ambayo tunajadili hapa kwenye Bunge kila mwaka ningependa niishauri Serikali walau iwe inangalia mambo current zaidi ili tuweze kuisaidia nchi yetu. Kwa nini nasema hivi, mwaka jana taifa letu limepitia mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi iliyoongozwa kwa ushupavu mkubwa sana na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya mwanzo ya Sensa hii ilitoka Oktoba, mwaka jana lakini mpaka sasa tunapozungumza final report bado haijatoka. Sasa tunazungumza mpango ambao ndiyo wa kwanza tangu tufanye Sensa hii. Sisi kama Wabunge, bila hii final report tunashauri vipi Serikali namna ya kuboresha mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ni muhimu hii mipango ya mwaka mmoja mmoja iangalie vitu current. Tumetumia zaidi ya bilioni 400 kufanya Sensa hii. Sasa, tija ya fedha hizi itaonekana kwa namna gani? Tunatumia ripoti hii kupanga mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya nchi yetu. Naishauri Serikali iangalie namna final report ije ili Waheshimiwa Wabunge waishauri Serikali kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, kwenye Sensa hii tumeona kwamba kuna idadi ya watu kiasi gani, wanawake kwa wanaume kwa kila mkoa. Kuna mikoa yenye watu wengi na kuna mikoa yenye watu wachache. Kwa mfano, Mkoa wa Njombe una watu kama laki nane na kitu tu. Kuna Mkoa wa Dar es Salaam ambao tunaongelea una watu zaidi ya milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango lazima iende tofauti kwa sehemu na sehemu. Pia, ninavyosema tuongelee mipango current, namaanisha; siku Serikali nyingi tumeona, Rais wetu na wasaidizi wake wamesaini mkataba mzuri na mkubwa sana wa Bandari ambao unakwenda kufanya na kuleta mageuzi makubwa sana ya kiuchumi nchini kwetu. Hata hivyo bado mpango wetu haujaweza ku-incorporate zile financial implications ambazo zitaletwa na mkataba huu. (Makof)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pia, kuna mikataba au miradi mikubwa sana ambayo inaendelea kwenye nchi yetu ambayo tunategemea ndani ya miaka hii 2024/2025 ikamilike na itakuwa na financial implications kubwa sana kwenye nchi yetu la. Mpango haujatuonyesha, naongelea kwa mfano, Bwawa la Mwalimu Nyerere, tumekuwa tukisubiri mradi huu kwa muda mrefu na tumepewa matumaini na Serikali yetu na niipongeze sana kwamba mradi huu unakwenda vizuri na unakwenda kukamilika. Faida za mradi huu na financial implications zake tuzione kwenye mipango yetu ili tuone namna gani tunasonga mbele kwanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Prof. Kitila Mkumbo akiwa bado Mbunge alikuwa anazungumzia sana Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Sasa amekabidhiwa kijiti, ninashukuru na kumpongeza kwa sababu nimeona kwamba kwenye mpango wake anaona haja ya Serikali kuanza kufanyia kazi mradi huu. Nadhani kuna haja, tofauti na sentensi hii tu aende mbele zaidi kushauri kama alivyokuwa anashauri akiwa amekaa pale; kwamba ni namna gani anafikiri tuende sasa na mradi huu ili ulete tija kwenye taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ni mzuri sana lakini kwa bahati mbaya ninahisi, kaka yangu Mheshimiwa Prof. Kitila amewasahau vijana kwenye mpango huu. Kwa nini nasema hivi, nizungumzie suala la changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa vijana. Tukiwa tunazungumzia takwimu ambazo zililetwa na Wizara yetu ya Kilimo, ikiwa inaonyesha justification za Mradi wa BBT; ilionyesha kwamba vijana zaidi ya 16 million kwenye nchi yetu, wanawake kwa wanaume wana changamoto ya kupatikana kwa mitaji. Yaani hawana accessibility ya financial institutions zile kubwa kwa maana ya mabenki na hizi ndogo ndogo kwa ajili ya kijipatia mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru na kuiopongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, kwa sababu iliona haja na changamoto hii ikaleta mpango wa 4:4:2 au mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu aliiona changamoto ambazo makundi haya maalum yanapitia kwenye halmashauri zetu na akatoa maelekezo ya mfuko huu. Hiki kitu kilifanyika Aprili mwaka huu, mpaka leo tunavyozungumza ni miezi saba na hakuna hatua ambayo tumeiona kwa macho ikifanyika kuonyesha kwamba kweli mfuko huu utarudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema Justice does not have only to be done. It should be seen to be done. Serikali inatuambia kwamba inafanyia kazi mchakato huu. Ninakataa kuamini kwamba, mfuko huu tayari uko kisheria. Vyanzo vya fedha za mfuko huu zinajulikana lakini maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalikuwa mahususi, fedha hizi zipitie kwenye benki. Haimaanishi tunaanzisha benki mpya ili tukae muda mrefu namna hii, ni benki hizi hizi tulizonazo. Ninakataa kuamini kwamba, Serikali hii yenye wataalam wengi wa kutosha wanaofikiri vizuri, wanahitaji zaidi ya mwaka mzima kuweza kuja na mpango huu kwa ajili ya vijana…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NG’WASI D. KAMANI: … lakini, kitendo cha kwamba mpango huu haujataja jambo hili unamaanisha kwamba vijana tusiwe na matumaini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ng’wasi, samahani kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye pendekezo la Mheshimiwa Rais kutumia benki, in a records taifa letu limewahi kutumia DCB Bank kwenye ya Dar es Salaam na kwenye records hawajawahi kuwa na upotevu wa fedha kwa kiwango ambacho sasa zimepotea. Kwa hiyo, Serikali ina delay lakini ina sehemu ya kwenda kujifunza DCB Bank na kuchukua hatua na kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Ng’wasi, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii na inazidi kuonyesha ni namna gani it is unjustifiable kwa Serikali kukaa muda mrefu namna hii bila kuleta utaratibu hii na vijana wakaendela kutumia fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, kitendo cha Profesa Kitila kutoku-incorporate katika mpango wake namna gani fedha hizi zitaenda kurudi kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ina maanisha kwamba tuondoe matumaini katika kipindi hiki cha 2024/2025 kwamba mfuko huu utarudishwa na fedha hizi zitarudi kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani mpango huu Mheshimiwa Kitila unapokuja kutujibu katika mrejesho wako wa mwisho, utuambie namna gani fedha hizi zinakuja kwenda katika channels zinazotakiwa na ziwafikie walengwa. Mheshimiwa Kitila, kwa nini nasema hivi, vijana wanawake kwa wanaume, ndiyo asset kubwa na nzuri ya nchi yoyote ambayo inajielewa katika dunia hii. Ni kwa sababu vijana ndiyo tunategemea watakuja kuwa wazazi waliobora baadaye, walezi waliobora baadaye, viongozi waliobora baadaye lakini wafanya maamuzi katika taifa hili. Kama tusipoanza kuwawezesha leo, ninaamini tunatishia kesho zilizo salama za taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka kusema kitendo cha kuchelewesha mikakati ya kuhakikisha vijana wanapata mitaji katika nchi hii kina multiplying effects. Effect ya kwanza ambayo mimi ninaiona na immediate kabisa na imepigiwa kelele na baadhi ya watu ni issue ya gambling, tunaiita kamari. Vijana wengi sasa wameishia kwenye kucheza kamari. Na tafiti za msingi zimefanyika kwamba, Kamari iwe ni online, iwe ni hizi tunaita sports betting zote zina implications kwenye psychology ya kijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, implication yake kiutafiti ni kwamba, mtu wa kawaida anatakiwa aonyeshwe namna gani anahitaji kukifanyia kazi kitu ambacho anataka kukipata. Hata maandiko yamesema asiyefaya kazi na asile. Lakini Kamari zinajaribu kumuonyesha kijana kwamba kuna njia nyepesi zaidi za kupata kitu kilichokikubwa zaidi. Changamoto ninayoiona hapa ni kwamba, tunaenda kuzalisha watu ambao wataona kwamba wana haja ya kuona namna ya kurahisisha mazingira yao ya kupata fedha. Mtu huyu ukimpeleka kwenye utumishi wa umma huwezi ukamwambia akae afanye kazi asubuhi mpaka jioni, siku saba, mwezi, miaka ili apate kitu fulani ilhali anaona kuna njia nyepesi ya kuweza kufanya ili apate kitu kilichokikubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naona kwa kuendelea kuchelewesha haya, tuna-multiply effect kubwa sana. Siyo ya leo tu ya vijana wetu lakini kesho ya taifa letu. Nadhani ni wakati sasa tuchukue hatua, tufanyie kazi shida ya upatikanaji wa mitaji kwa vijana pamoja na kupuunguza changamoto ya ajira. Tunajua kwamba Serikali haiwezi ikaajiri vijana wote lakini tukiwapatia mitaji, tukiwatengenezea mazingira yaliyobora; tunaenda kuzalisha taifa lenye vijana ambao kesho taifa letu litakuwa na nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, Profesa Kitila nakuomba, mjadala wetu wa mpango umetanguliwa na mjadala wa Ripoti ya CAG. Nilichangia mwaka jana, nikashauri kwamba tunahitaji kutengeneza sheria mpya ya uwajibikaji wa watumishi wa umma. Lakini kwa sababu mpango huu tunataka tuuone uki-reflect kwenye uchumi wa nchi yetu, na moja kwa moja Ripoti ya CAG ilikuwa inaonyesha namna gani uchumi wetu unadhidi kuathiriwa na matendo ya baadhi ya watumishi wetu, ninadhani kuna umuhimu mpango wako ukaonyesha namna gani unakwenda kufanyia kazi changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kutengeneza mipango ya bajeti ya trilioni 47 tunayoizungumzia sasa ilhali hatujarekebisha changamoto ambazo tumetoka kuzijadili juzi. Maana yake ni kwamba, tunategeneza mazingira yale yale ya viwango vikubwa zaidi kuendelea kupotea kadiri tunavyozidi kuongeza bajeti. Nadhani tutakuwa hatuendi vizuri kama taifa kama tunadhani kutatua changamoto zetu ni kuongeza ukubwa wa bajeti bila kuziba kunakovuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukabaki na bajeti zetu ndogo lakini kama fedha inakwenda kule inakostahili na inatumika vuzuri, bado tukapata maendeleo makubwa kuliko kuwa na bajeti kubwa ambazo zina mianya mingi zaidi inayovuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Ofisi hii muhimu sana. Kwanza, wazee wetu waliwahi kusema kwamba kupanga ni kuchagua. Kwa hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuitenga Ofisi hii ya Rais, Mipango na Uwekezaji kusimama peke yake na kumpa mtu makini kabisa, Profesa Kitila Mkumbo kuisimamia. Namwamini Profesa na naamini kwamba anakwenda kutuongoza vizuri na kuweka mipango ya nchi yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sensa tuliyofanya mwaka 2022 inaonesha kwamba 76% ya Taifa hili ni vijana chini ya miaka 35. Kwa maana hiyo nilitegemea kwamba mipango yote ambayo tunaipanga sasa hivi katika kila sekta kwa asilimia kubwa ni lazima izunguke kundi hili kubwa, 76% ni nyingi sana na katika hili ningependa sana tuangalie changamoto ambayo ni ya kwanza kabisa kwa vijana wa Taifa hili, changamoto ya ajira.

Mheshimiwa Spika, katika mipango yetu ni muhimu tukawaelekeza vijana kwamba nchi hii inakwenda wapi na wao waendeje. Ni muhimu kwa sababu sidhani kama kuna afya kuliacha kundi hili lijiindee katika karne hii ya 21 kuji-surprise na kuwa na kesho ambayo hawaitambui; kwenda na kutegemea kwamba tutaikuta kesho na tutapambana nayo tutakavyoikuta, sitegemei hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Katika nchi yetu sasa hivi kuna maeneo matano ambayo tunayaona kulingana na projections zake, utashi wa viongozi wetu na maendeleo ya sekta hizo, kwamba ni sekta ambazo zitaendelea ku-boom kwa miaka 20 mpaka 50 inayofika. Kuna sekta za utalii, viwanda, kilimo, uchukuzi na sekta ya uchimbaji. Nategemea katika mipango yetu tuoneshe ni namna gani tumejipanga kulielekeza kundi hili kubwa. Kwanza katika namna ya uelimishaji wake kwenda ku-tackle mabadiliko watakayoyakuta katika sekta hizi, lakini pili kuangalia namna gani tuna wa-groom kuendana na mabadiliko ya nchi hii katika sekta hizi.

Mheshimiwa Spika, leo hii tunaongelea biashara katika eneo huru la Afrika ambapo Afrika nzima, nchi zaidi ya 50 zitakuwa na soko huru la pamoja. Lazima katika mipango yetu tuoneshe ni namna gani tunakwenda kuwa-groom vijana wetu kupambana na uhuru huu ili kuweza kunufaika na eneo hili huru la biashara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ni lazima Wizara hii ituambie, je, inafurahishwa na vijana ambao wanatoka katika vyuo na vyuo vikuu vyetu katika nchi hii? Kama sivyo, je, tunaingiaje katika mpango wao wa kuweza kutuinua na kutuweka sawa ili leo hii tunapokuwa tunaongelea dira ya mpaka mwaka 2050 tuone namna gani vijana tunafika 2050 tukiwa imara?

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Profesa, anatuonesha namna ambayo amechukua maoni sehemu mbalimbali za nchi hii kwenye Dira hii ya 2050, waliotoa maoni haya 80% ni vijana kati ya miaka 15 mpaka 35. Hii inaonesha kwamba moja, vijana wanataka sana sana kushiriki kwenye kushauri namna Serikali na nchi yao inavyoenda na mbili, wanapenda na wao wahusishwe kwenye mipango ya nchi hii. Kwa hiyo naiomba sana Ofisi hii katika kupanga mipango yake na namna inavyoshauri sekta mbalimbali, isilisahau kundi hili muhimu sana la vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, nizungumzie sekta ya kilimo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Leo hii tunakwenda kuzungumzia sekta ambayo tunaitengea zaidi ya trilioni moja kwenye bajeti, kwa hiyo ni lazima tuonyeshe ni namna gani sekta hii inakwenda kutusaidia kuzalisha zile ajira milioni tatu zilizokuwa zimeahidiwa tangu mwanzo. Tuna Miradi kama ya BBT, naomba sana katika mipango yetu tuoneshe ni namna gani tunakwenda kushusha Mradi wa BBT kwenda kuwa localized kwenye wilaya na mikoa yetu. Hii itatuondolea sana changamoto na malalamiko ya vijana wengi kwamba wameachwa nje ya mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna maeneo ambayo yalikwishatolewa maelezo na Mheshimiwa Waziri Mkuu yatengwe kwenye kila halmashauri zetu ili kuhakikisha kwamba vijana wanapewa maeneo hayo kujiendeleza wao wenyewe. Maeneo haya yatumike kwenye miradi hii ili vijana kwenye wilaya zetu na mikoa yetu, waende kunufaika huko moja kwa moja na ndipo tutakapoona hizi ajira milioni tatu zinazalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunazungumzia bajeti ya trilioni moja kwa ajili ya sekta hii. Naamini, tusije tukafanya kilimo cha kizamani. Ili tufanye kilimo cha kisasa ni lazima tuuangalie ugani kwa namna ya tofauti sana. Napendekeza tuanzishe mamlaka ya ugani kama tulivyoanzisha TARURA na RUWASA, ili kusudi mamlaka hii ishuke mpaka vijijini kwenda kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kulima kibiashara na kujiongezea thamani ya mazao wanayoyazalisha. Hivi ndivyo ambavyo tunaweza kwenda kweli kukomboa kilimo chetu na kukiweka kwenye value sawasawa na bajeti tunayoitengea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inabidi vilevile tuwekeze kwenye value addition, lazima tuwekeze kwenye viwanda. Kwenye hili nilikwishashauri ndani ya Bunge hili Tukufu, kwamba ni lazima tutoe incentive kwa Watanzania wanaotaka kuanzisha viwanda katika Serikali zingine za nchi hii tofauti na Dar es Salaam na Pwani. Baba wa Taifa alikuwa na maana kubwa sana kuanzisha viwanda katika kila sehemu kulingana na mazao au na vitu vinavyopatikana kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kitu hatari sana kuona viwanda vyote vya nchi hii, almost 80 percent, viko sehemu moja. Siku maeneo haya yakipatwa na emergency yoyote, maana yake ni kwamba uchumi wa Taifa hili utayumba kwa kiasi kikubwa. Lazima tuoneshwe mipango na incentive gani watatoa kwa Watanzania. Iwe ni incentive za kikodi au mapunguzo ya thamani ya vitu kadhaa ili kusudi waweze kuanzisha viwanda na processing industries katika sehemu mbalimbali za nchi kwa ajili ya kusaidia wale wanaozalisha kule kule waweze kuona tija ya maendeleo haya ya miundombinu ambayo tunafanya kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa pia kushauri, leo hii sisi watu wa Kanda ya Ziwa, tuna Ziwa Victoria. Sasa, ni lazima tuone mipango ya kutumia ziwa hili kuondokana na kwanza, shida ya maji na pili tuwe na scheme za umwagiliaji za kutosha. Ni aibu sana kwa sisi ambao tuna maji ya Ziwa Victoria kuanza kuja humu Bungeni na kulia changamoto ya maji. Tunalia na changamoto ya kwamba, kipindi cha kiangazi hatuwezi kulima ilhali tuna ziwa. Tunaweza kutengeneza irrigation schemes. Lazima kwenye mipango yetu Waziri atupe mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha maeneo haya yanazalisha kwa wingi kulingana na rasilimali tulizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina zaidi ya 51% ya Ziwa Victoria, kwa hiyo ni lazima tujue ni kwa namna gani tunakwenda kulitumia ili kukuza uchumi wetu hasa wa maeneo ambayo yanazunguka eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, kwenye sekta ya nishati nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu ameonesha dhima na nia ya moja kwa moja ya kufanya Watanzania tuanze kutumia nishati safi. Katika hili nampongeza sana. Nampongeza pia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Watumishi wote wa Wizara kwa scheme waliyoifanya ya kugawa mitungi ya gesi katika sehemu mbalimbali. Nawapongeza kwa sababu nimefuatilia katika bajeti watakayoileta katika Bunge hili Tukufu wamekwenda mbele zaidi, kuona ni namna gani tutapeleka nishati ya gesi asilia vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunagawa mitungi ya gesi lakini si Watanzania wengi watakaokuwa na uwezo wa kwenda ku-refill mitungi ile ikiisha. Ni lazima tutafakari namna gani tutakuwa na uendelevu wa project hii, hasa kwenye jamii za ufugaji. Wao tayari nishati ya kuzalisha hii gesi asilia wanayo ya kutosha na gharama yake ni nafuu. Tutenge bajeti twende tukawekeze huko ili tuwe na uendelevu wa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa economies of scale; nilitegemea, kwa sababu sasa hivi kuna matumizi makubwa sana ya hii nishati safi, basi angalau gharama ya gesi ingeshuka kulingana na matumizi yake makubwa. Naomba sana pia kwenye mipango tuliangalie hili la namna gani ya kushusha nishati hii ya gesi ili wengi waweze kuipata kwa wepesi. Kwa sasa hivi inatumika kwa wingi na kwa economies of scale, naamini kwamba tunaweza tukashusha. Tusije tukaishia ku-mobilize Watanzania kutumia nishati safi, lakini tukapandisha faida na kuwanufaisha watu kadhaa; wakati tungeweza kushusha na kufanya Watanzania wengi zaidi wakatumia nishati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya mwisho ni kwenye suala zima la uwajibikaji na utawala bora. Kwenye hili nampongeza sana Profesa kwa sababu katika hotuba yake, ameelezea misingi 10 ambayo ataisimamia kwenye Ofisi yake. Msingi namba nane amesema nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na msingi namba 10 amesema ni kusimamia mipango tutakayoipanga na kuitekeleza. Kwenye hili amenipa imani kubwa sana. Nimwombe sana Profesa ili tuweze kufikisha au kufikia kule tunakopanga kufikia ni muhimu sana tukaimarisha nidhamu katika matumizi ya fedha za umma. Kwa kufanya hivyo tu ndiyo itatuwezesha kufikia huko, kwa sababu tukiendelea kupanga mipango mizuri lakini fedha ambazo zinaenda kutimiza mipango hiyo hazifiki kule zinakotakiwa, naamini tutakuwa na mkwamo mkubwa sana katika mipango hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya dharura kuhusu kuongezwa kwa umri wa waombaji wa ajira za Serikali
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kuniunga mkono katika hoja hii ambayo ina maslahi mapana sana na makubwa kwa vijana na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wastani wa vyuo vyetu nchi nzima vinatema vijana au wahitimu kuanzia 100,000 mpaka 300,000 kwa mwaka. Wote tunajua kwamba, vijana hawa hawawezi kumezwa wote kuingia katika ajira Serikalini. Wote tunajua kwamba ni ukweli usiopingika tumekuwa na muda mrefu kidogo ajira za Serikalini zimekuwa hazitangazwi na kutolewa. Tumshukuru tu Mheshimiwa Rais kwamba tangu ameingia madarakani amejitahidi kutoa ajira nyingi kuwameza vijana hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna principle moja inaitwa Legitimate Expectations au Matarajio Halali. Vijana hawa wanaotoka katika vyuo vyetu, ambao Serikali yetu imetumia fedha nyingi sana kuwasomesha wanatoka wakiwa na matarajio halali kwamba Serikali itawapokea, kuwa-groom na kuwaingiza katika system zake ili nao waendelee kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu hatuna hifadhi za watu binafsi, hifadhi zote ni za Serikali. Maana yake ni kwamba, kila aliyeenda kusoma kozi hii ajira yake pekee ni Serikalini. Leo hii tunatoa mwanya wa mwaka mmoja, maana yake tunawaambia wahitimu wote waliohitimu katika kozi hizi kwamba, asipopata kazi ndani ya mwaka mmoja wa kuhitimu kwake asahau, aende akatafute kazi nyingine. Hiyo siyo haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri. Mtu akisoma vizuri, straight, ameanza mwanzo mpaka mwisho bila kuweka gap, ndiyo atamaliza na umri wa miaka 24, lakini wote tunayafahamu mazingira yetu, uhalisia wetu tunaufahamu. Mtu kwa sababu zozote anaweza akapata gap ya mwaka mmoja au miwili hajaenda chuo whether anatafuta ada au mazingira yoyote yale. Maana yake huyu mtu atamaliza kusoma akiwa haajiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini hii siyo haki kwa vijana wetu bado. Kama walivyozungumza Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunao mwanya wa kuongeza umri ili kuweka muda ambao mtu kwa umri wake na fitness yake anaweza kufundishika kwa mafunzo haya na akafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tumesoma pia description ya kazi anazokwenda kufanya mtu. Tumeona kwenye udereva, sawa udereva kinachohitajika mtu haendi kubeba magogo, udereva ni kuendesha gari tu. Hata kama anakwenda kuendesha katika sehemu isiyo na barabara, kuendesha ni kuendesha na haya mafunzo ambayo wamesema wakishawachukua hawa watu wanakwenda kuwapa, yanatosha kabisa kum-equip huyu mtu kwenda kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kushukuru kwa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze tu kwa kuishauri Wizara hii juu ya migogoro kati ya wafugaji na wahifadhi. Wabunge wengi, hasa wa majimbo ya maeneo ambayo shughuli kuu ni ufugaji na wanapakana na hifadhi wamezungumza juu ya madhara mengi sana yanayotokana na migogoro hii kati ya wafugaji na wahifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili tu ya kushauri kwa Wizara hii. Kwanza naomba Wizara hii ifanye upya tathmini na upimaji wa hifadhi zao na waweke upya mipaka yao. Tuache kutumia mipaka ya zamani, kuna ramani tunaambiwa sijui mwaka themanini, mwaka wa ngapi, miaka kama ishirini, thelathini iliyopita. Tuache kutumia kutumia ramani hizi, tufanye upimaji mpya kwa sababu tayari kuna mabadiliko makubwa sana yamekwishafanyika kwenye ramani hizi na watu wamekwishaishi kwenye baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya vijiji Wabunge wake humu ndani unakuta kijiji chote ni eneo la shoroba au eneo la hifadhi. Kwa hiyo tukitumia ramani za zamani maana yake hata kuna baadhi ya Wabunge humu wananchi wao wote wame-trespass. Kwa hiyo tufanye upimaji upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upimaji huo basi kama ambavyo maeneo ya hifadhi yako landlocked na GN kwenye sheria zetu, basi na sisi maeneo ya vijiji, maeneo ya kulima na maeneo ya ufugaji yawe landlocked hivyo hivyo ili tuanze kuiwajibisha Wizara hii pale ambapo na wao wanyama wataingia kwetu na sisi tuwajibishwe pale ambapo wananchi wetu wataingia kwao. Kwa hiyo ulinzi wa kisheria uwe kwa pande zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na mzungumzaji aliyepita juu ya hili suala la usafirishaji wa viumbe hai kwenda nje. Nianze tu kwa kusema kwamba kama ilivyooneshwa kwenye wasilisho la Mheshimiwa Waziri, Wizara hii inachangia asilimia 21 ya GDP ya nchi hii. Kati ya asilimia hizi 21, asilimia 17.6 zinatokana na utalii peke yake na asilimia 80 ya suala hili la utalii kwa maana ya hii 17.6, inatokana na utalii wa wanyama. Maana yake ni kwamba watalii wengi wanakuja kwenye nchi yetu kwa sababu tuna wanyama mbalimbali ambao wangependa kuwaona, aidha, kwa sababu wa kwetu ni tofauti sana au hawapatikani kwenye sehemu nyingine ya dunia hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sambamba na hayo, Wizara hii inachangia asilimia 25 ya fedha zote za kigeni zinazoingia katika nchi yetu, lakini vijana milioni 1.6 wameajiriwa katika sekta hii ya utalii ikiwa ni pamoja na madereva, tour guides, hotelini na sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kwamba hili ni suala la kizalendo; tukiruhusu wanyama wetu ambao wanapatikana kwa upekee kabisa kwenye nchi yetu, wakapelekwa katika nchi zingine, maana yake tunasema watalii hawatakuja tena kuangalia wanyama hawa, lakini pia hawatakuja tena kwa shughuli zozote za kiutafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatutakuwa tu tumeathiri hii asilimia 17.6 ya pato letu la ndani, bali tutakuwa tumeathiri hizi ajira milioni moja na laki sita za vijana wa Kitanzania ambao wanategemea utalii kama shughuli kuu ya uchumi katika maisha yao. Pia tutakuwa tumeathiri biashara ya Shirika letu la Ndege la ATC ambalo tumetumia fedha nyingi sana kulifufua mpaka sasa. Vile vile, tutakuwa tumeathiri sekta binafsi ya hoteli, usafirishaji, yote haya yataathirika kwa kiasi kikubwa kama tukiruhusu usafirishaji wa wanyama kwenda nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, hebu tutafakari, kama ingekuwa madini, kwa mfano gold, inaweza ikapandwa na ikaota kama mti, tunategemea wale watu wangeendelea kuja kuwekeza kwetu? Wangechukua wakaenda wakapanda wakaendelea na mambo yao. Sasa hivyohivyo wanyama leo hii tukiruhusu waende wakazalishwe kwingine maana yake species ambayo tungetaka wale watalii waje kuiona kwa upekee katika nchi yetu itapatikana sehemu zingine zote duniani. Hakutakuwa na haja ya mtu kufunga safari. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Haya, naona jirani anataka kumpa taarifa, Mheshimiwa Asia Halamga.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Kanda ya Kaskazini tunategemea sana utalii na kipindi hiki kifupi cha COVID-19 kimeathiri sana uchumi, hasa uchumi wa vijana wa Kanda ya Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi zimeahidiwa ajira zaidi ya milioni nane za vijana zitakazotokana na masuala ya utalii na masuala mengine ili kuweza kufikia ajira milioni nane. Naamini kabisa tukiruhusu wanyama wakatoka nje ya nchi, hatuwezi kufikia kwa sababu nchi zingine hazitakuwa na sababu ya kuja katika nchi yetu ya Tanzania. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Naona huo ulikuwa ni mchango wa Mheshimiwa Asia Halamga kwenye hii Wizara kuliko taarifa. Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, malizia mchango wako.

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa anazungumzia sekta ya madini wakati bado nchi yetu haijapata nafasi ya kutosha kuwekeza huko alisema kama bado hatujawa tayari kuwekeza na madini haya yakawafaidisha Watanzania, basi tuache uwekezaji huu ili uje uwafaidishe Watanzania pale ambapo tutakuwa tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama bado Watanzania hatujawa tayari kutumia wanyama wetu vizuri ikatuletea tija, kuliko kukubali tuwasafirishe kwenda nje, tuwaache ili tutakapokuwa tayari wawafaidishe Watanzania wenyewe. Rai yangu tulinde ajira hizi za vijana ambazo zinakwenda kupotea, tulinde mapato haya ambayo tutayapoteza kama tukiruhusu suala hili likaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, napenda tu kuchangia kwenye suala zima la misitu. Tunaishukuru sana Serikali yetu, imekuwa ikiweka mkazo sana kwenye upandaji wa miti, misitu ya Serikali na misitu ya watu binafsi. Hata hivyo, changamoto kubwa kwenye sekta hii ya misitu imekuwa ni uchomaji moto wa misitu. Wote tunakubali kwamba kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa mazingira ambao umesababisha mabadiliko ya tabianchi yanayotuathiri nchi na hata dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wamejitolea kwa rasilimali zao wenyewe kupanda misitu kwenye mikoa mbalimbali ya nchi hii ambayo inatusaidia. Kwanza inaisaidia Serikali kutunza mazingira; lakini pili, inasaidia sana katika suala zima la kuleta mvua na kusaidia kwenye kilimo ambacho zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania tunakitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye misitu ya Serikali nafahamu suala hili la moto ni changamoto, lakini wao wana watu ambao wanawasaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

NAIBU SPIKA: Sasa naona umeishia neno wanasaidia, malizia sentensi yako.

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwenye misitu ya Serikali wao wana vijana wao ambao Serikali imewaweka kwa ajili ya kusaidia kulinda moto, kitu ambacho mtu binafsi hana rasilimali hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba Wizara hii itafakari upya namna gani wawekezaji wanaowekeza kwenye misitu nao wanalindwa kwenye suala hili la moto, ikiwa ni pamoja sasa na Serikali kuona kama inaweza kusaidia kuweka walinzi hawa kwenye misitu ya watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia katika ripoti za Kamati hizi tatu muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa leo utajikita katika wizi, upotevu, ubadhirifu na ufujaji wa fedha katika halmashauri zetu. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na katika moja ya majukumu ya Kamati yangu ni pamoja na kuangalia namna fedha zinavyotumika kuendesha miradi mbalimbali na kuleta maendeleo kwa wananchi katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mengi ambayo yamesomwa kwenye ripoti yetu naomba tu ni-highlight machache. Kuna suala zima la kubadili miamala katika mfumo bila kufuata utaratibu na katika halmashauri ya Ubungo tuna hasara ya Shilingi Milioni 21.3; Kigamboni, Bilioni 10.8; Ilemela, Bilioni 8.7. Katika matumizi ya fedha mbichi; Ubungo tuna Milioni 196.3, Kigamboni Milioni 47, Ilemela milioni 627, lakini hii ni bila kuzungumzia fedha ambazo zimelipwa kwa mkandarasi bila kuwa ametoa ushahidi Milioni 356, fedha ambazo zimelipwa kwa kazi ambayo haijafanyika Ilemela Milioni 138 na Fedha ambayo imelipwa zaidi ya kiwango kilichokuwa kinadaiwa Milioni 237.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nimeyataja haya? Nimeyataja ili Bunge lako Tukufu na wananchi wajue viwango vya fedha tunazozungumzia. Katika hizi halmashauri tatu tu ripoti yetu inaonesha ni zaidi ya Bilioni 20 zinaoneshwa kwenye ripoti ya CAG zina mashaka na hazijaeleweka namna ya matumizi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoshangaza zaidi ni kwamba, watumishi wanaohusika katika wizi, ubadhirifu au uzembe huu wanafanyiwa yafuatayo: -

(i) Wanapewa barua za onyo;

(ii) Wanahamishwa kupeleka katika halmashauri zingine;

(iii) Wanaanza kufanyiwa uchunguzi na cha kushangaza zaidi baadhi ya watumishi bado wapo katika halmashauri wakati bado wanafanyiwa uchunguzi; na

(iv) Wengine wanapelekwa Polisi au TAKUKURU na hawa ni wachache, lakini bado haitoi justification kuwapeleka watumishi hawa Polisi au TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi kwa sababu ripoti ya CAG ina uzito wa kuweza kutumika kama ushahidi mahakamani. Kwa hiyo, maana yake hawa watu walitakiwa wafikishwe mahakamani na hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, inakuaje leo hii Mheshimiwa Rais anazunguka sehemu mbalimbali kutafuta fedha kuhakikisha wananchi wanaletewa maendeleo, fedha zinamwagwa kwenye halmashauri zetu ili watu tupate maendeleo. Fedha hizi tulitakiwa tuzione zina-reflect kwenye mzunguko wa fedha kwa wananchi, lakini hatulioni kwa sababu kuna uzembe, wizi na upotevu mkubwa unafanyika kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, humu Wabunge wengi sana kwenye simu zao wana soft cope za CV zimejaa watu wanaomba watafutiwe ajira, wana hard copy mafaili yamejaa wanaomba watafutiwe ajira. Hizi ajira zinatoka wapi kama fedha ambazo zinapelekwa kwenye halmashauri zetu kwenye jamii zetu zitumike kuleta maendeleo, kuzalisha ajira, kufanya uwekezaji zinaibiwa na zinaingia kwenye mifuko ya watu.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Taarifa.

MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii darasa moja fedha zimeenda kwenye halmashauri zetu Milioni 20 kwa darasa moja, darasa la vioo la...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa subiri kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda nimpe taarifa tu dada yangu mchango wake ni mzuri sana kwa kusisitiza kwa kweli Serikali, hawa waliothibitishwa na CAG ni majangili, ni majambazi wanatakiwa wakamatwe mara moja haraka, tena wakaishi mahabusu huko. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kamani, taarifa hiyo.

MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii huko mitaani vijana wanakosa hata shilingi laki mbili ya kuanza kujiajiri kuanzisha kitu kidogo tu, lakini kuna watu kwenye halmashauri zetu wamejilipa pesa. Pesa ambazo hazina idadi wamejilipa na ikithibitika kwamba wameiba wanaambiwa warudishe taratibu kwa muda ambao haueleweki ni muda gani. Hii naiona kama ni mikopo ambayo mtu anaamua kujipa isiyo na riba, isiyo na muda siku akiamua kumaliza kulipa anajilipa. Hii sio haki na haikubaliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia sisi kama Wabunge, Madiwani na Mheshimiwa Rais hatutakubali mwaka 2025 tusulubiwe na wananchi kwa sababu hatujaweza kutatua changamoto zao, lakini fedha zilikuja na baadhi ya watu wali-mismanage fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hapana, hapana, hapana, hatutakubali. Ninachoomba ushauri wangu, Serikali iangalie namna, ituletee mabadiliko ya Sheria katika Bunge hili na Wabunge najua ni wazalendo tutapitisha mabadiliko hayo, tuangalie upya mfumo wa uwajibikaji katika utumishi wa umma. Hatuwezi kuwa watu wanafanya makosa kama haya, viwango vikubwa vya fedha kama hivi tunaishia kuwapa onyo au kuwahamisha hapana. Kuna vijana wengi sana mtaani ambao wangeweza kufanya kazi hizi, ni wazalendo basi tuwaondoe watu hawa tuwape wale vijana kazi wafanye.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano mdogo, leo hii tuna project ya vijana chini ya Wizara ya Kilimo, building a better tomorrow imepewa bilioni tatu tu kwa hatua ya mwanzo ya kuandaa hekari laki na sitini kutengeneza miundombinu kwa ajili ya kuwaweka vijana waanze kufanya kazi. Kama Shilingi Bilioni tatu inaweza kufanya kazi kwenye mikoa mitatu tu hizi Bilioni 20 tungepeka Tanzania nzima tungefanya nini kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wananchi wa kawaida kwenye Sheria zetu, The Penal Code, Section ya 265, mwananchi wa kawaida akikutwa na kosa la wizi regardless ya kiwango hata kama ni kuku, anapewa adhabu ya mpaka miaka saba kufungwa, lakini hawa watu wanaoiba kutumia numbers, wanaiba kutumia mifumo yetu, mabilioni ya fedha, tunawapa onyo na kuwahamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haikubaliki. Naomba sheria ije tuifanyie marekebisho na kama inashindikana, kusiwe na double standard; basi na wananchi wanaoiba nao tuishie kuwapa onyo au waishie tu kuwashauri ili nao wawe sawa na sisi. Vinginevyo nasema fedha ya umma lazima itumike kuleta maendeleo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata nafasi leo ya kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nina machache tu ya kusema. Siku ya leo nitazungumzia mambo mawili, na muda ukiruhusu nitakwenda kwenye la tatu. Nitazungumzia suala la uzalendo kwa vijana, suala la maadili kwenye nchi yetu na muda ukiruhusu nitazungumzia utaratibu wa ujazaji wa nafasi za ajira zinazotangazwa Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la uzalendo kwa vijana; kwanza kabisa, naomba kwa niaba ya vijana wote Watanzania, tufikishe salamu zetu za pongezi na shukrani za kutosha kabisa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu tangu ameingia madarakani Mheshimiwa Rais amekuwa nasi bega kwa bega, changamoto zetu amezivaa, amekuwa anazi-address kila siku na kuwasisitizia watendaji wake pia kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Tumekuwa na malalamiko ya muda mrefu sana sisi vijana kwamba tukianza biashara tunakuwa na msururu wa taratibu nyingi na urasimu mkubwa sana kabla ya kuja kusimama kwenye biashara zetu. Mheshimiwa Rais ameliona hili, na siku za hivi karibuni kupitia Waziri Viwanda na Biashara, ameondoa malipo ya kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kijana aneyeanza biashara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizi za Mheshimiwa Rais, tangu alipoingia katika kiti chake, kahakikisha anatulea sisi vijana na kutuaminisha kwamba tunaye mtu anayetuunga mkono katika juhudi zetu za kuchangia katika kujenga Taifa letu. Hata hivyo, bado tuna changamoto moja kubwa sana ambayo inatishia moyo wa uzalendo kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha pale ambapo vijana tunakuwa tunajifunga mikanda, shime kujenga nchi yetu pamoja na mazingira na changamoto zote tunazokutana nazo, halafu tunaona kuna baadhi ya watendaji ambao sisi vijana tumewaamini kupitia nafasi mbalimbali Serikalini, kufanya kazi yao kutuletea maendeleo kwa kodi tunazolipa, wanaiba pesa hizo na badala yake tunashindwa kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata neno la Mungu limesema kwamba “toa boriti katika jicho lako, ndipo utoe boriti katika jicho la mwingine.” Tunapataje nguvu au Serikali itapata wapi legality ya kumwambia kijana uwe mzalendo, ukipewa nafasi fanya kazi na ujenge nchi yako ilhali kuna baadhi wamepewa nafasi hizo na wanayoyafanya tunayaona.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii vijana wanaohitimu tunawalaumu, kwamba kijana anahitimu, anataka ndani ya mwaka mmoja ama miwili aendeshe Range, ajenge ghorofa. Tunawalaumu, lakini haya hatujayatoa from no where, tunawaona. Kuna vijana wadogo, leo hii unamwona kapata kazi TRA, kapata kazi bandarini, mwaka mmoja ana ghorofa. Unaniambiaje mimi nisifanye yale kama anayoyafanya yule? Tunaua Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana sio Taifa la kesho tu, ni Taifa la leo. Kama tunataka vijana waendelee kuwa wazalendo, waendelee kuijenga nchi hii, tujenge nchi ambayo miaka 100, miaka 200 itasimama ikiwa na uchumi imara, tunahitaji mabadiliko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishauri katika Bunge lililopita kwamba Serikali ituletee mabadiliko ya sheria ili tukuze uwajibikaji katika utumishi wa umma. Hawa wanaofanya mambo haya, tuwawajibishe. Leo hii kijana akiona kwamba mwizi au anayefanya ubadhilifu amewajibishwa, hata yeye kesho anazidi kuona kwamba Taifa linamlinda, Taifa linam- support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahenga walisema, “mtoto wa mhunzi asiposana, hufukuta.” Maana yake ni nini? Maji hufuata mkondo. Sasa kama Serikali inatuonesha mkondo huu, kesho vijana watafuata mkondo upi? Tunaomba, tunaomba, tunaomba; haya yanayoendelea kule nje hayana afya kwa vijana, hayana afya kwa Taifa, hayana afya kwa kesho yetu iliyo salama. Tunahitaji mabadiliko ya sheria na tunahitaji hatua za haraka zichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la maadili, wamezungumza Wabunge wenzangu hapa waliotangulia. Kuna kitu ambacho kinaendelea kwenye jamii yetu kinatushtua. Kimsingi kinatishia hata kesho ya nchi yetu na kinahusu bara zima kwa ujumla. Mapenzi ya jinsia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua kwamba kujihusisha na mambo haya, moja ya effect yake kubwa zaidi ni kukosekana kwa uendelevu wa vizazi. Hakuna kizazi kinachoweza kuendelea kwa mapenzi kati ya mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke. Mimi nitawarudisha nyuma kwenye historia. Karne ya 19, moja ya vitu vilivyoisaidia Europe ku-develop kwa kasi ilikuwa ni kitu kinachoitwa demographic revolution. Ongezeko kubwa la idadi ya watu, lakini ripoti za IMF na World Bank zinatuonesha nchi ya China imefika hapa ilipofika sababu kuu, ikiwa ni wingi wa watu walionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mambo haya yanaletwa, siyo kwamba wenzetu hawaoni juhudi za ukombozi ambao Bara la Afrika linajitahidi kufanya ili kufika mbele na kujiondoa katika lindi la umasikini tulionao, ni wazi. Pia ripoti ya World Bank inaonesha, Africa is the youngest continent. Maana yake ni nini? Afrika ndiyo bara pekee lenye nguvu kazi kubwa zaidi kuliko mabara mengine yote duniani. Afrika ndiyo ina vijana wadogo zaidi kuliko mabara mengine huko duniani. Maana yake miaka 10, 20, 30 ijayo Afrika leo haitakuwa hapa ilipo. Tuna vijana wenye nguvu na wenye uweledi wa kufanya kazi. Uchumi wetu utakuwa umeimarika, umeimarika, umeimarika zaidi. Kimsingi hicho ni tishio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamechangia kwa maana ya kwamba hii ni tishio tu kwa maadili yetu, lakini mimi naenda mbele nasema, hili ni tishio dhidi ya ukombozi wa kiuchumi ambao Afrika na Tanzania inajaribu kufanya. Ni ukweli usiopingika kwamba sisi Watanzania zaidi ya asilimia 80 tunategemea kufanya kazi za ngumu ili kujipatia kipato, lakini tafiti zinaonesha kwamba kibiolojia, watu wanaojihusisha na mambo hayo, hasa wanaume wanapungukiwa na nguvu ya kufanya kazi kwa zaidi ya asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta. Miaka 20 ijayo tutapata wapi vijana wa kufanya kazi za nguvu za nchi hii, kuijenga nchi hii? Tunahitaji hatua za haraka zichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa kwa sababu Mheshimiwa Rais amezungumza, Mheshimiwa Makamu wa Rais amezungumza, Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumza, Wabunge mbalimbali wamezungumza, viongozi wetu wa dini wamezungumza, Watanzania kila sehemu wanazungumza, kwa nini hatua hazichukuliwi? Sheria ipo wazi, hiki kitu ni criminal offence. Mheshimiwa Saashisha alisoma hapa sheria ndani ya Bunge hili, kwamba ni miaka 30 ukionekana umefanya mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo kesi ya nani atamfunga paka kengele? Kwa nini? Kwa sababu watu hawa wanajinasibu, na wako wazi hata kwenye mitandao ya kijamii. Kwa nini hatuoni hatua zikichukuliwa? Tunahitaji kuona hatua za haraka zinachukuliwa kunusuru vizazi vyetu, kunusuru nchi yetu lakini kunusuru uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, lakini siyo kwa umuhimu mdogo, nitaongelea suala la utaratibu wa ujazaji wa nafasi za ajira kwenye nchi yetu. Tunashukuru sana tangu Mheshimiwa Rais ameingia madarakani, ametangaza nafasi nyingi sana za ajira na vijana wengi wamejipatia ajira. Kwenye hilo tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tuna walakini kidogo katika utaratibu unaotumiaka kujaza nafasi hizi. Kwanza kabisa, tukiangalia ratio ya applicants kwa nafasi zile ambazo zinazozatangazwa, inaonesha namna gani tuna tatizo kubwa sana la ajira kwenye nchi yetu. Tunaipongeza Wizara kwa sababu tulitoa maoni nayo ikapokea, ikaanzisha vituo mbalimbali ambapo watu sasa wanaweza kwenda kufanya interview tofauti na zamani ambapo lazima waje sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja ni kwamba, unakuta zinahitajika nafasi 100, lakini idadi ya watu wanaoitwa kwenye interview unakuta ratio yake ni hata 50:1. Unajiuliza, kama hawa watu kwenye ku-apply walitoa vyeti vyao, wali-submit vielelezo vyote vilivyotakiwa. Kwa nini waitwe watu wengi kiasi hiki kwa nafasi chache ilhali tunajua fika kwamba hawa vijana wana changamoto huko waliko? Wengi hata akiitwa hata kwenye kufanya interview wanakwambia hata nauli sina, sijui nitafikia wapi? Sijui nitakula nini kwa hizi siku ninazoenda kufanya interview?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta nafasi moja wanaigombania vijana 50. Kuna haja ya kufanya hayo? Pili, vijana hawa wakifika kwenye interview, kumekuwa na tendency; unaambiwa interview inaanza saa 3.00, lakini vijana watakaa pale mpaka saa 8.00 hamna interview iliyofanyika. Hawajui wala hawajapewa utaratibu wowote. Kwa nini kama Serikali inakuwa imejiaandaa kufanya interview na kusaili vijana hawa, kwa nini wasijipange, utaratibu ufanyike, vijana wafanye interview warudi majumbani? Inakuwa ni kama hawajajipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, tumeambiwa kwamba mnafanya interview, kuna baadhi yenu wanawekwa kwenye kanzidata ili nafasi nyingine zikija, wasifanye tena usaili wachukuliwe kwenye kanzidata. Hilo ni jambo zuri, lakini lazima tuwe na transparency. Vijana watajiuliza kwamba tuna uhakika gani kwamba hawa waliowekwa sasa hivi ndiyo wale waliokuwa kwenye kanzidata? Tuna uhakika gani kwamba hawa hawajachukuliwa kutoka mifukoni mwa watu wakawekwa kwenye nafasi zile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali. Naomba, kama kuna kanzidata, iwe wazi, kila mtu ajue kwamba mimi kwenye kanzidata ni Na. 3, zikitangazwa nafasi 10 maana yake na mimi nimo; zikitangazwa nafasi 20 nami nimo, au simo nasubiri kipindi kijacho, ili kuondoa sintofahamau kwa vijana kwenye suala hili la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu tangu aingie madarakani kati ya vitu ambavyo ameviweka kama maeneo yake ya vipaumbele ni katika kuhakikisha kwamba anaifungua Nchi yetu kwa wawekezaji wa nje, kuhakikisha anakuza uwekezaji wa ndani na kuhakikisha anakuza diplomasia ya uchumi katika Nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba nitumie fursa hii kuipongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara. Kwa sababu kazi inayofanyika ni kubwa na matokeo yake tunayaona, hotuba iliyosomwa ya bajeti ya Wizara hii inatia matumaini.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia nilivyokuwa nimepanga kuchangia, nimevutiwa sana na mchango alioutoa Mheshimiwa Mtenga juu ya changamoto ya viwanda vya chumvi katika Mkoa wake wa Mtwara na Lindi na ningependa tu wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kutujibu hapa atueleze nini mkakati wa Serikali au Serikali ina mpango gani katika ku–control vibali vya uingizaji wa chumvi nchini, kwa sababu tukiacha hili eneo wazi hatuhatarishi tu viwanda hivi lakini tunahatarisha ajira nyingi sana za vijana…

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ng’wasi Kamani kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Biteko.

TAARIFA

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge ninaomba tu kutoa taarifa kwa msemaji na kwa Bunge, kwamba vibali vya kuingiza chumvi nchini vilisimamishwa na Waziri wa Viwanda na sisi Wizara ya Madini tunaotoa vibali toka tumekubaliana na Wizara ya Viwanda kusitisha uingizaji wa chumvi ili tukubaliane namna gani tutumie chumvi ya ndani kabla ya kuagiza ya nje, hatujawahi kutoa kibali chochote na hakuna kibali kinachotolewa hadi sasa. Kwa hiyo, nilitaka tu wakati anachangia awe na comfort hiyo na Bunge liwe na comfort kwamba Serikali inafanyia kazi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Dotto Biteko, nilimsikia Mheshimiwa Nyongo akisema asilimia 70 ya chumvi inaagizwa. Amesema asilimia 70, wewe unasema haiagizwi kabisa, yaani mmesitisha uagizaji ama mimi ndio nimechanganya? Si unazungumzia chumvi. Mheshimiwa Nyongo taarifa uliokua unampa Mheshimiwa Mtenga ilikuwa inasema, tunaagiza asilimia ngapi?

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba mahitaji ya chumvi kwa mwaka Tanzania ni tani 250,000. Tunaingiza asilimia 70 ya mahitaji hayo na wakati nchi ina uwezo wa kuzalisha chumvi tani zaidi ya 300,000 kwa kutumia source zote tulizonazo. (Makofi)

SPIKA: Haya, ahsante sana. Mheshimiwa Doto Biteko, hiyo taarifa sasa iko sahihi ili nimuulize sasa yule anapokea taarifa yako, kwamba vibali havitolewi na yule anasema asilimia 70 inaingia. Au ilikuwa inaingia kabla hamjaweka hilo katazo.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Nyongo nimemuelewa ni kwamba mahitaji ya chumvi ni tani 250,000 ambayo namba imepanda kidogo. Lakini sisi tunaagiza chumvi asilimia 70 wakati tuna uwezo wa kuzalisha zaidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nyongo ana justify kwamba hatuna sababu ya kuagiza kwa sababu uwezo wa kuzalisha uwezo wa kuzalisha chumvi ndani ni mkubwa kuliko kuagiza nje na ndicho nilichokuwa natoa taarifa kwa Mheshimiwa Kamani.

SPIKA: Swali langu ni kwamba hiyo asilimia 70 tunaingiza ama hatuingizi?

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, hiyo asilimia 70 ndio tunayo import kwa ajili ya kuja ku-blend chumvi ambayo tunayo ndani wakati tunayo ndani inayozidi kiwango hicho.

SPIKA: Haya pengine mwenye hoja ameelewa, Mheshimiwa Ng’wasi Kamani unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naipokea, lakini nitumie fursa hii kutoa rai kwa Serikali kama tayari takwimu zinaonesha kwamba tuna uwezo wa kuzalisha chumvi ya ndani kwa kiwango kikubwa hata kuliko kile tunachohitaji katika mahitaji yetu. Naiomba sana Serikali utaratibu huu wa kufuta vibali hivi basi utiliwe mkazo ili viwanda vya ndani vya chumvi vipate kuzalisha na ajira za vijana na wakina mama wa Tanzania tuendelee kuzilinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya kwanza itakuja kwenye suala la chuma; Imekua miaka mingi sana na Wabunge wengi sana wamechangia suala la Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Silengi kuujadili mradi huo kwa sababu naamini Serikali imesikia inaendelea kulifanyia kazi kwa sababu imekua ni jambo la muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka tu Serikali itueleza katika nchi yetu Mungu ameibariki na chuma inapatikana sehemu nyingi sana na katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ametuonesha kwamba katika mwaka huu wa fedha wanampango wa ku-deal na Liganga na Mchuchuma na Chuma kilichoko Maganga Matitu. Lakini kuna chuma kipi Handeni Tanga, kuna chuma kipo Mayamaya Dodoma, kuna chuma kiko maeneo Hondusi Morogoro lakini Wizara haizungumzii mambo haya. Tunaona kila leo kuna magari ya Dangote yanatoka katika maeneo yale ambako wachimbaji wadogo wadogo wanachimba chuma zinasafirishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali nitaomba ije itupe majibu, je, imekwishafanya tathmnini ya viwango vya chuma vilivyoko katika maeneo haya? lakini wachimbaji wadogo wadogo wanachimba hii chuma na kupakia na zinaenda nje. Je Serikali inafanya tathmini ya kiasi gani cha chuma kinatoka? Lakini Serikali inapokea mapato au maduhuri kiasi gani kutoka kwa wachimbaji wale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano katika Wizara ya Madini, miaka ya nyuma Wizara ya Madini ilikuwa imetoa kipaumbele kikubwa sana na guidance kubwa kwa makampuni makubwa ya wachimbaji, ikasahau wachimbaji wadogo. Leo hii Wizara ya Madini imeamua kuwa incorporate wachimbaji wadogo na tuona ni namna gani mapato kutoka Wizara ya Madini yameongezeka.

Mheshimiwa Spika, ninaomba pia Wizara hii iangalie mfano huu kutoka katika Wizara ya Madini. Tuna wachimbaji wadogo wa chuma wanaochimba na chuma hii inatoka, itueleze ni kwa nini chuma hii inatoka bila kuchakatwa. Ni kwa nini hatujaja na mpango mkakati wa kuwa guide hawa wachimbaji wadogo ili na wao waweze kutuongezea pato na Mheshimiwa Waziri katika taarifa yake ametuonesha mahitaji ya chuma yalikuwa kutoka tani 200,000 na sasa tunaenda kwenye tani 1,000,000 na tuna project kubwa sana za Serikali zinazofanyika za kimkakati zinazohitaji chuma.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kila chuma iliyoko katika nchi hii tukiiutumia ivilivyo na Serikali ikaangalia. Kuacha tu katika hii project moja ya Liganga na Mchuchuma ambayo nayo inatakiwa iendelee kufanyiwa kazi lakini tuangalie na chuma zingine zilizoko katika maeneo mengine ili tusipoteze mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuja pia katika suala la NDC, NDC imeanzishwa zaidi ya miaka 60 sasa katika Nchi yetu. Ningependa pia katika majibu ya Serikali Mheshimiwa Waziri aje atuambie NDC mpaka sasa ina leseni ngapi? Na leseni ngapi zinazofanya kazi na ngapi hazifanyi kazi, wapi tumefeli na wapi tunatakiwa kurekebisha. Ili kusudi tuweze kuisaidia NDC kufanya kazi yake vizuri na iendelee kulipa maduhuri inayotakiwa kulipa katika Serikali.

Mheshimiwa Spika, ningependa pia Mheshimiwa Waziri katika majibu yake aje atueleze, tumeona mikakati mingi na kwa hilo nawapongeza ya kuweza kuwakuwa wawekezaji wadogo ndani ya Nchi yetu. Kwa namna moja ama nyingine naweza nikasema bado Wizara hii haina wivu na wafanyabiashara wake wa ndani, Wizara hii haina wivu na wawekezaji wadogo wa ndani kwa sababu wawekezaji hao na wafanyabiashara wanapitia changamoto nyingi na mara nyingi Wizara hii imekuwa ikirudi nyuma kuwaachia Wizara zingine ziweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii wafanyabiashara kule nje hata wakipata usumbufu kutoka TRA bado Wizara hii itasema hapana hayo ni mambo ya Wizara ya Fedha sisi tunakaa pembeni. Leo hii wafanyabiashara wetu wanachajiwa hela ya kodi kabla ya miezi sita ambayo ndio takwa la sheria. Wizara hii itakuambia inakaa nyuma haya ni mambo ya TRA, mambo ya Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wizara hii ianze kuwa na wivu na wafanyabiashara wake ianze kuwa na wivu na wawekezaji wa ndani. Wawekezaji wa nje tunawapenda, wanatupa fursa za ajira, wanatupa mapato kama nchi lakini fimbo ya mbali haiui nyoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji Wizara hii ije mkakati kama tunavyolinda wawekezaji wa nje, kama tunavyopambana kuhakikisha wanakuja kwa wingi, tuendelee kuwalinda wa ndani ili waweze ku-maintain ushindani. Tuwape nafuu za kikodi tuwajengee mazingira yaliyo salama ili kesho na keshokutwa mfanyabiashara katika eneo lake la kazi akiona Afisa wa Serikali anakuja kumtembelea wasitishike kama wanavyotishika sasa hivi. Waone hawa ni marafiki zao wanataka kuwanyanyua wanataka kuwasaidia katika hili Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine nilitaka kuishauri Serikali sasa hivi zaidi ya asilimia 70 ya viwanda vilivyoko katika nchi yetu viko maeneo ya Dar es Salaam na Pwani. Je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango wa kutoa incentive kwa wawekezaji wa ndani na nje ili kuweza kuanzisha viwanda vingi zaidi katika maeneo mengine ya nchi? Baba wa Taifa aliona umuhimu wa jambo hili na ndio maana walianzisha viwanda vingi sana katika maeneo mbalimbali ya nchi, mikoa mbalimbali kulingana na mazao au vitu vinavyozalishwa katika mikoa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii viwanda hivyo vingi vimekufa kwa sababu ya ubinafsishaji na wale waliobinfsisha viwanda hivi, wamekiri wenyewe hata wengine wameandika vitabu kwamba kuna sehemu walikosea. Sasa Serikali inajifunza nini ili kutusaidia kwanza kufufua viwanda hivi turudishe viwanda katika mikoa mingine ili tuweze ku-balance maendeleo lakini mimi naamini pia ni hatari sana kwa Taifa letu kama tukifanya viwanda vyote viwepo Dar es Salaam na Pwani tu. Hiyo ni ngumu sana tunatishia kwanza migration watu wote wa Nchi nzima wahamie Dar es Salaam na Pwani lakini pili maendeleo yatakuwepo kule kuliko sehemu zingine zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Waziri atatuambia hapa kwamba pamoja na kwamba Nchi yetu ni consumers wakubwa sana wa vitu vingi sana kutoka nchi za wenzetu. Ni kwa nini makampuni haya makubwa ya manufacturing yanaanzisha franchise na branches zake katika nchi za wenzetu zinazotuzunguka na hawaji hapa kwetu.

Mheshimiwa Spika, pia tulikuwa na sehemu za ku-assemble scania katika Nchi zetu na matreka. Viwanda hivyo vimefungwa, vimepelekwa katika nchi za wenzetu. Kuna shida gani katika nchi yetu inayofanya wawekezaji wakubwa badala ya kuleta makampuni haya ku-assemble mali zao hapa inapeleka katika nchi jirani na sisi tunakosa fursa hizo.

Mheshimiwa Spika, nilishawahi kuishauri Serikali, tuna uhitaji mkubwa sana wa kuiwezesha TiRDO na SIDO zetu kama tunahitaji kwenda katika uchumi wa viwanda. Leo hii SIDO katika bajeti iliyopita ilitengewa 1.9 bilion lakini mpaka tunavyozungumza imepewa milioni 400 tu. Hatuwezi tukafika katika uchumi wa viwanda kama TiRDO na SIDO tusipoziwezesha inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye wizara hii Muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita. Rais wetu Dkt. Samia suluhu Hassan, tangu alipoingia madarakani kati ya sekta ambazo aliziangalia kwa jicho la tatu ni sekta hii ya elimu. Mapema Kabisa alitoa msimamo wake na maelekezo kwamba anataka maboresho yafanyike lakini hakuzungumza tu alienda kwa vitendo. Ametenga fedha nyingi amakwenda kuboresha maisha ya wanafunzi vyuoni, ameongeza wigo wa elimu bila malipo. Kwa hiyo, sisi vijana na watanzania kwa ujumla tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa maboresho haya ambayo ameyafanya kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri wewe pamoja na Wizara nzima, Naibu Waziri wetu, Katibu Mkuu na watu wako wote tunawashukuru sana na kuwapongeza. Kwa sababu rasimu hii ya maboresho ambayo mmetuletea kwa kweli inatia moyo. Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu sana cha watanzania kwa ujumla na hata Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, kwamba tuna maboresho ya haraka sana yanahitajika kufanyika kwenye mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru hata Sera yetu ya elimu bado na yenyewe ina recognize kwamba tunayo changamoto kwenye mfumo wetu wa elimu. Hii rasmu ambayo mmetuletea imekuwa exhaustive, inatia moyo kwamba tukienda kweli katika utekelezaji huu na mkiendelea ku-incorporate mawazo ya Wabunge wengi ambayo wanaendelea kutoa basi naamini kesho yetu ni bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia kwenye masuala machache tu, la kwanza; nilishauri katika mchango wangu wa kwanza nilipoingia Bungeni hapa kwamba, tunahitaji kuwa na agenda ya Kitaifa. Nitoe mfano kwenye nchi za wenzetu kwa mfano China, wao walikuwa na agenda kwamba ifikapo mwaka 2025 wangependa industrial product zote asilimia 75 zinazokuwa consumed duniani zote zitoke China na kwa kiasi kubwa nasema wamefanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunazungumzia Tanzania ya viwanda, tukizungumzia kilimo, kiwanda kinachozalisha watu ambao wanakwenda kwenye sekta hizi ni Wizara hii ya Elimu ndio inatutayarishia watu hawa. Nafikiri kwa namna ambavyo tumeandaa hii rasmu yetu na kwa namna ambavyo na quote mwanzo kabisa wa sera ambayo ni rasimu inasema “Serikali imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025” na inasema inatarajia kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya watanzania walioelimika na kupenda kujieleimisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mawanda mapana sana tusiogope kuota. Tunapenda Tanzania tuione wapi ili Wizara hii ya Elimu itusaidie kuandaa watu hao. Tunapenda Tanzania leo hii tukizungumza duniani kama tunataka nini tuje tukipate Tanzania na wizara hii ndio wakati wake huu na hasa muda huu ambao tunafanya mapitio mtuandalie watu wa kwenda katika mlengwa huo. Kama tunasema tunataka Tanzania ya viwanda tunatakiwa tuanze kuanzie level ya chini kuanda watu hawa ili mwisho wa siku tuone Tanzania kweli ikielekea huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana na wala hatutakuwa tumeji–stretch sana tunatia hatari ya kuwa jacks of all trades and master of none. Lazima tuweze ku–master. Sasa hivi Afrika inaongelea eneo huru la biashara Afrika. Lazima tuseme sisi Tanzania tukinda katika hii free movement of good, free movement of people tunataka Tanzania tuwe na speciality ipi? Ndio wakati sasa hivi wa kuandaa kupitia mabadiliko hata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; niombe sana sana Wabunge wengi wamechangia sana juu ya suala la lugha. Lugha yetu ya kitanzania ni lugha ya kiswahili na ni lugha ambayo tunaipenda we are very proud na lugha yetu lakini ni lazima tuangalie mabadiliko ya kidunia tunayoenda nayo. Sasa hivi tunakwenda kwenye dunia ambayo ni free movement of people, sio Afrika tu lakini dunia nzima kwa ujumla. Sasa tuki-incorporate lugha ya kiswahili peke yake tunamtenga mtanzania na dunia nyingine. Ni muhimu sana. Tuendelee kuitunza lugha yetu lakini tuendelee kuangalia lugha ambazo zitamfanya mtanzania aende katika dunia nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze kwa sababu katika rasimu hii mmekwenda mbali. Mmetoka katika debate ya Kiswahili na kiingereza mmekwenda kwenye kiarabu, kifaransa na kichina. Niwapongeze kwa sababu huko ndiko dunia inakotaka twende, kwenye hilo mmefaulu. Niombe mmesema anaetaka kufundisha kiswahili aombe kibali aruhusiwe anaetaka kufundisha kiingereza aombe kibali aruhusiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunahitaji kufanya marekebisho katika hayo. Kwa sababu kama tunataka tuifungue Tanzania na kimsingi hii ni direction amekwisha tuonesha Mheshimiwa Rais anataka Tanzania tusikae kama kisiwa twende duniani. Sasa tukisema tu kwamba kuna baadhi ya wanafunzi watafundishwa kiswahili peke yake tunawatenga watu hawa na hawawezi kwena duniani, nadhani katika hili tuliangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika marekebisho haya tunayofanya stakeholder namba moja ni mwalimu. Yaani hatuta achieve chochote kama tusipoangalia maboresho katika hali za walimu. Wabunge wengi wamezungumzia katika kuboresha hali zao za kufundisha na mazingira yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko concerned zaidi kama tunapokwenda kwenye mabadiliko haya ambayo kwa kiasi kikubwa sasa yanakwenda kumfanya mwanafunzi aweze kupambana na mazingira yake. Je, anaemfundisha kwenda kupambana na mazingira yake yuko well equipped kumfundisha mwanafunzi ili akitoka akapambane na mazingira yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu tulianzisha mfumo wa competence based lakini as we speak mpaka leo less than 40 percent ya walimu walioko wameweza kupewa elimu ya kutosha kuweza kurudisha hizo knowledge kwa wanafunzi. Je, tunapokwenda kufanya maboresho haya, walimu tulionao wanakwenda kupata hizo knowledge kwa mfumo upi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, bado tuna upungufu mkubwa sana wa walimu. Tumewekeza sana kwenye miundombinu, tumewekeza sana kwenye kuboresha mazingira ya wanafunzi kusoma lakini bado tuna upungufu mkubwa sana wa walimu. Kama ambavyo tuliifanya agenda ya kitaifa kwamba tunatenga bajeti ya kutosha kwenda kuongeza madarasa, tunatenga bajeti ya kutosha kwenda kuongeza madawati, ningependa pia tuifanye agenda ya makusudi kwamba tunatenga bajeti ya kwenda kuongeza idadi ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna sekta inayoweza kusimama kama kiwanda kinachotuzalishia wataalamu hakitasimama na kiwanda hiki si kingine ni Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kutia msisitizo. Nashukuru kwa sababu rasimu hii imeanza kuonesha msisitizo wa mafunzo ya TEHAMA kuanzia level ya chini kabisa elimu ya awali mpaka mwisho. Lakini sasa dunia ya leo inakwenda kwenye information technology zaidi, dunia ya leo inakwenda kwenye artificial intelligence. Ni muhimu sana kuanzia elimu ya chini tuanze kuwafundisha wanafunzi wetu information technology. Tena sio vile vitu vya awali ambavyo tulikuwa tunajifunza mwanzoni kwamba, label hii ni CPU, hapana. Tunahitaji kwenda ndani zaidi kwa sababu dunia ndiko ilikofika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kimsingi the future is closer than we think. Kwa sababu wenzetu sasa hivi wanakwenda ku–substitute kabisa binadamu kuweka mashine. Sasa sisi tunawaandaaje watu wetu kwamba tunakwenda kuwa substituted tuanze kutumia mashine. Ni lazima tuangalie kwa karibu sana na napenda tusiweke msisitizo huu vyuoni tu, tuanzie kwenye elimu ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe tu data ndogo, mwaka 2015 wanafunzi waliokuwa wanamaliza shule za sekondari walikuwa ni wanafunzi milioni 1,648,000+ lakini mwaka 2019 sasa hivi wamemaliza wanafunzi milioni 2,185,000 hawa ni wanaomaliza elimu ya sekondari. Lakini wanaotoka vyuoni, mwaka 2015 walitoka wanafunzi 65000 tu kutoka milioni 1,600,000 wakatoka vyuoni wanafunzi 65,000, 2019 kutoka milioni 2.1 wakatoka vyuoni wanafunzi 87,000 hao zaidi ya wanafunzi milioni mbili wako wapi? Maana yake tumewaacha kwenye level za chini. Kama tunaanza kuwekeza lazima tuwekeze kuanzia level ya chini ili yeyote anayeweza kuishia chini basi atoke akiwa na skills za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzunguzmia wanafunzi wetu Watoto wa kike. Tulipitisha hapa katika Bunge lako Tukufu Sheria ambayo inatoa adhabu ya miaka 30 kwa watu ambao watawapa ujauzito Watoto wetu wa kike ambao wako shuleni. Sheria hiyo ilikuwa ni nzuri na na malengo yalikuwa ni mema. Lakini Sheria ile pia ilipata resistance kwa kiasi fulani kwa sababu wanaharakati waliona kwamba tunatoa adhabu upande mmoja wakati wakosaji wanaweza kuwa wawili au huyu binti akijifungua basi huyu bwana yuko gerezani hivyo huyu mtoto atalelewa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema kwamba tulishindwa kuangalia kitu kingine ambacho kingeweza kuwa matokeo ya jambo hili. Kitu hicho ni kama kifuatacho;

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tafiti zinaonesha kuwa watoto wa kike wana invest zaidi kwenye kutokuonekana na mimba kuliko kuonekana na mimba. Kwa maana ya kwamba watoto wa kike sasa hivi wanatumia vidonge vya uzazi wa mpango, watoto wa kike wanatumia vidonge vya kutoa mimba ili asionekane na mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiangalia katika hii rasimu mpya uliyotuletea hakuna elimu ya kujitambua. Tumesahau kumuelimisha mtoto wa kike, kujitambua kuwa na self-awareness, kuwa na self-respect ili asiweze kuingia katika vitendo hivyo ku–begin with. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama tuna risk sana kuwa na wanawake ambao watakuwa na matatizo ya cancer za uzazi, watoto ambao hawana maadili japokuwa mimba hatuzioni. Ninaomba sana katika hii rasimu mpya ambayo tunaitengeneza tuiangalie upya ili tuweke elimu ya kujitambua turudishe watoto wa kike katika maadili ya kitanzania, turudishe watoto wa kike katika kujitambua kwamba hili jambo si sahihi kuanzia mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana niweze kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya kilimo, Wizara muhimu sana kwa ustawi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote katika Wizara hii ya kilimo kwa sababu tangu ameingia madarakani ameonesha utashi wa moja kwa moja wa kumkomboa mkulima, kumuondoa mkulima wa kitanzania kutoka katika kuwa mtu ambae tunamtoa sadaka pale ambapo tunapata changamoto bila kujali tunamuumiza kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niende moja kwa moja kwenye ninachotaka kuzungumzia. Nitazungumzia huu mradi wa BBT au jenga kesho iliyo bora ambayo kimsingi inaangalia zaidi ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mbunge mwakilishi wa Vijana na nimeingia katika Bunge hili kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi na ahadi namba sita ya mwanachama yeyote wa Chama cha Mapinduzi, ni kujielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa maslahi ya wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya Mheshimiwa Bashe, kuja na jambo hili la Mradi huu wa BBT nilichukua jukumu la kujielimisha na kugundua jambo hili si jipya. Watu wengi waneweza kuona ndoto za Mheshimiwa Bashe na wasaidizi wake ni kama Ndoto za Alinacha au Hekaya za Abunuwas lakini sisi sio wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo hayo yalianza kufanyika katika Nchi ya Malaysia mwaka 1956, chini ya mradi ulioitwa FELDA au Federal Land Development Authority. Mradi huu kadri tunavyoongea leo unachangia asilimia 18 ya GDP ya nchi hii. Leo hii tunapozungumza ni moja ya mradi ambao unamiliki sekta kubwa sana ya uzalishaji katika nchi hiyo, ni mradi ambao umeifanya Malaysia iwepo katika nchi ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa palm oil duniani. Lakini ni mradi ambao umekwisha ondoka katika kupewa grants za Serikali na leo hii tunazungumza unapewa mikopo na Benki ya Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe, kwa sababu pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la watu wasio na imani na mradi huu hajarudi nyuma. Nimpongeze kwa sababu amechukua initiative ya kutuamini vijana na wanawake wa Kitanzania kwamba tukishikwa mkono na kuwezeshwa na Serikali, tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme nasikitishwa sana kwa sababu kama sisi Wabunge ambao ni wawakilishi na kwenye majimbo yetu tuna vijana, sensa iliyofanyika mwaka 2022, inaonesha zaidi ya asilimia 34 walioko katika nchi hii ni vijana lakini sisi Wabunge hatuwaamini vijana, nani atuamini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si jipya na katika haya nina machache ya kushauri na ninaamini tukienda pamoja Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Rais, pamoja na wasaidizi wao tunakwenda kufanikiwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la recruitment, namna ambavyo vijana hawa wamepatikana. Yalitolewa matanzangazo na vijana waliomba kupitia mitandao na takwimu zinaonesha zaidi ya vijana 20,000 waliomba. Lakini wengi wa hawa walioomba wanatokea katika Jiji la Dar es salaam kuliko majiji mengine au mikoa mingine ya nchi hii. Hii inaonesha kwamba ilikuwa kama survival for the fittest. Watu wa Dar es salaam wana mtandao kwa karibu zaidi ndio maana wameweza kuomba wengi zaidi na kuchaguliwa kwa wingi zaidi. Kwa hiyo, nimuache Mheshimiwa Bashe na wasaoidizi wake, kipindi kijacho wanapokuja kuchukua vijana hawa wahakikishe wanawachukua vijana kwa namna ambayo itatoa fursa sawa kwa vijana wote wa nchi hii kuweza kuomba na kupata fursa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee mimi niombe, mashamba haya yanapoanzishwa basi wajitahidi kuhakikisha kwamba yanaanzishwa katika kanda zote za nchi hii na hawa vijana wanapokuwa posted wawe posted katika Kanda zao. Tukiwapeleka mbali kama tunavyofanya sasa hivi ina risk vijana kuweza kutelekeza mashamba yale na kurudi nyumbani pale mambo yanapokuwa magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana tuhakikishe kwamba tunakuwa na mashamba haya katika kanda mbalimbali lakini hata kule tusipoweza kuanzisha mashamba haya, basi tuanzishe vitalu nyumba ili tutoe fursa sawa kwa vijana kushiriki katika kilimo kutoka kila sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto moja wapo kubwa zaidi katika mradi huu ni suala la ardhi. Wenzetu wa Malaysia waliweza kwa sababu inamiilikiwa na Crown. Kwa hiyo, wenyewe ilikuwa ni rahisi sana kwa Mfalme na wasaididzi wake kutoa ardhi na kuwapa watu. Kwetu sisi jambo hili ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naomba sana pale ambapo wizara inakuja kutujibu, ituambie namna bora ambayo inafikiria itaweza kutumia ardhi ndogo tuliyonayo kuwasaidia vijana wengi ambao wanazidi kuongezeka siku kwa siku. Takwimu za Sensa zinaonesha pamoja na kwamba asilimia 34 ni vijana lakini asilimia 44 ni wale walio chini ya miaka 18 na hawa tunawategemea ni vijana wa kesho. Wizara ije utuambie ni namna gani inafikira kutumia ardhi ndogo tuliyonayo ambayo haiongezeki, kuwasaidia hawa tulio nao na hawa ambao wanakuja ku-graduate na kuwa vjana wa kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unaonekana utakwisha mwaka 2030, ninaiomba sana Wizara, iangalie namna ya kutengeneza uendelevu wa huu mradi. Kama kule ambako tumejifunza wao wameanza tangu mwaka 1956, mpaka leo tunavyozungumza mradi huu upo na unaendelea na umejenga mabilionea wengi sana kutoka Malaysia. Naomba pia Serikali iangalie namna gani ya kuendelea kutengeneza uwezekano wa Mradi huu kuendelea hata baada ya mwaka 2030 ili vijana wa Kitanzania waendelee kunufaika, vijana wa Kitanzania waendelee kuvutiwa na kilimo, waendelee kuweza kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa naomba kwa vile bajeti inayotumika au iliyotengwa katika mradi huu ni kubwa lakini bajeti kubwa zaidi imeenda kutengeneza foundation. Nilikuwa naishauri Wizara iangalie namna ya kupeleka mradi huu kwanza kwa mwanzo katika mikoa ambayo ina vyanzo vya maji vya uhakika ili tuweze kupunguza gharama za mwanzo za mradi na fedha nyingi zaidi iende kutumika kwa vijana moja kwa moja kuliko kutengeneza miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Mheshimiwa Bashe, aangalie namna ambayo ata-link mradi huu na vijana wanaotoka vyuo na vyuo vikuu na a–link na vijana wanaotoka JKT ili kuweza kutumia mashamba haya kuweza kuwasaidia vijana hawa ambao tayari Serikali imekwishatumia fedha nyingi kuwaelimisha, tayari Serikali imekwishakutumia fedha nyingi kuwapa mafunzo hawa JKT na wao waje walisaidie Taifa lao waweze kuwa na kesho iliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niombe, changamoto kubwa ya mkulima wa kitanzania ni suala la soko, niombe sana katika mradi huu Mheshimiwa anapokuwa anaangalia namna ya kutengeneza basi ahakikishe vile vyote vinavyozalishwa vinaweza kupata soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nakuomba sana… naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kupata nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/2024. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo anayoifanya katika nchi yetu. Niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara. Kazi mnayofanya ni kubwa na Mungu aendelee kuwatia nguvu ya kulitumikia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa sababu ni sikivu na inasikiliza sana maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge wengi walilalamika juu ya faini za bodaboda na zilipunguzwa kutoka 30,000 mpaka 10,000. Mimi leo nakuja mbele yako kuomba sasa Wizara na Serikali waangalie pia faini zinazochajiwa katika bajaji za mizigo. Bajaji za mizigo zinachajiwa faini ya shilingi 250,000 kwa kukosa stika ya usafirishaji. Hii imekuwa ni kwa sababu bajaji hizi kwenye sheria zimewekwa kwenye class moja na malori ya mizigo. Ni kitu cha ajabu sana kuweka kifaa kinachonunuliwa shilingi milioni tano mpaka sita kwenye class moja ya malipo sawa na kifaa kinachonunuliwa zaidi ya milioni 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wa LATRA alitangaza kwamba sasa watu hawa waanze kuchajiwa faini ya shilingi 25,000 lakini jambo hili halitekelezwi na watendaji wa chini na hii ni kwa sababu ya mapungufu yaliyoko kwenye sheria. Mimi niiombe Serikali kama tulivyosikia kilio cha waendesha bodaboda tusikie kilio cha waenda bajaji za mizigo. Hawa ni vijana wanaotaka kujikomboa, wanaotaka kujikwamua, tuwashike mkono. Shilingi 250,000 ni fedha nyingi tupunguze fedha hii ifike shilingi 25,000 na tu-reflect mapungufu haya kwenye sheria zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia Serikali kwa sababu ilisikia kilio cha wafanyabiashara hasa wa soko la Kariakoo kwenye kero mbalimbali walizokuwa wanapitia kwenye biashara na mengi yamerekebishwa; mimi niwapongeze sana. Hata hivyo niiombe Serikali yetu, changamoto zilizoelezwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ni changamoto ambazo wanazipitia wafanyabiashara sehemu zote nchi nzima. Kero walizozieleza wafanyabiashara wa Kariakoo ni kero ambazo wanazipitia wafanyabiashara almost wote nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusisubiri wafanyabiashara wa sehemu nyingine pia wagome ili twende tukatatue changamoto hizo. Mimi naomba yale mliyoyafanya kwa wafanyabiashara wa Kariakoo yaende yakafanyike kwa wafanyabiashara wengine wote nchi nzima. Tutoe mafunzo na maelekezo kwa watumishi wetu wa TRA, lugha wanazotumia na approach wanayotumia kwa wafanyabiashara wetu si rafiki sana, waende wakarekebishe ili wafanyabiashara na TRA waanze kufanya kazi kwa harmony na kwa amani kujenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kati ya vitu ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kuwa anasisitizia ni namna gani ambayo tunaweza tuka-widen tax base kwenye nchi yetu ili tusiumize wale wachache wanaoendelea kutuchangia na kutusaidia katika kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina jambo la kushauri, kuna kitu kinaitwa carbon credit, alizungumza Mheshimiwa Kakoso. Wilaya ya Tanganyika peke yake kwa vijiji nane tu inalipwa takribani bilioni nne mpaka tano kwa malipo haya ya carbon credit. Sasa hivi dunia inakoelekea hot topic ni climate change, mabadiliko ya tabianchi; na itaendelea kuwa hot topic kwa sababu ndiko tulipo na ndiko tunakoelekea. Sasa, kwa nchi kama za kwetu za uchumi wa chini tutaendelea kuwa wahanga wakubwa wa mabadiliko haya ya tabianchi. Namna gani tunaweza kufaidika na wale wanaochafua mazingira kutusaidia na sisi kuweza ku-deal na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kupitia hiki kitu kinachoitwa carbon credit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hi kuna nchi, nitolee mfano nchi ya Ghana, kwa miezi sita tu kuanzia Juni mpaka Desemba 2019 wamepokea malipo ya dola za kimarekani milioni 4.9 kwa carbon payment, miezi sita tu; na wao wamelipwa fedha hizi kwa hekta milioni sita tu za misitu. Takwimu katika nchi yetu zinaonesha kwamba sisi tuna hekta milioni 48 za misitu. Kama tukisema tunaanza ku-tap malipo katika carbon credit za misitu hii hekta milioni 48 naamini tunakwenda kukusanya fedha nyingi sana. Kuliko kuendelea kuongeza kodi kwa wale walipa kodi wachache kuendelea kuwaumiza kuna namna nyingine ya kuongeza tax base kwa kupokea fedha kutoka katika rasilimali ambazo tumeshapewa na Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa kinara wa mfano wa namna gani tunaweza yukaongeza mapato kupitia rasilimali zetu kwenye Royal Tour. Sisi twende mbele zaidi, tuunge mkono juhudi zake, tutumie hizi carbon credit kuzalisha mapato kwa ajili ya kuendelea kuleta maendeleo na kukabili matokeo mabaya au matokeo hasi ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuchangia katika Bunge hili na nitaendelea kusema; kwamba hatuwatendei haki wakandarasi wazawa wa ndani. Ripoti ya CAG inaonesha kila mwaka kwamba wakandarasi hawa hatuwalipi kwa wakati. Lakini ni uhalisia, hawa watu wako katika majimbo yetu, tuna malalamiko ya kutosha. Lakini kubwa zaidi wale ni vijana wenzangu na hivyo nina jukumu la kuwasemea. Nilisema na nitaendelea kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekwishakutoa maelekezo, tutoe kipaumbele kuwalipa wakandarasi wa ndani. Hawa ni wazalendo, fedha tunazowalipa zinabaki hapa ndani, mzunguko wake unabaki hapa ndani, wanaajiri Watanzania wenzetu. Tusiendelee kufilisi Watanzania wenzetu kwa kuchelewa kuwalipa ilihali hawa watu wana malipo kwenye commercial banks. Ninaomba sana Serikali twende tukaangalie suala hili tuwalipe kwa wakati wakandarasi wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mimi niende kwenye fedha za 4:4:2. Ukurasa wa kumi wa bajeti yetu unaonesha kwamba Serikali iko katika mchakato wa kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais, na pale tutakapokuwa tayari kukamilisha utaratibu wa kupitishia fedha hizi benki utakuja kutupa taarifa. Mimi niwapongeze sana kwa hatua ambazo mnaendelea nazo. Nina machache ya kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanakwenda kuchukua fedha katika halmashauri zetu, fedha hizi za 4:4:2 hawakujua kwamba benki zipo, walijua; lakini walikwenda kule kwa sababu kuna changamoto kadha wa kadha kwenye kupata fedha kwenye benki zetu. Kuna changamoto za muda, ukiritimba, gharama, kuna rushwa na nyingine nyingi. Mimi niiombe sana Serikali, inapokuwa inaangalia namna gani ya kupitishia fedha hizi tuangalie pia namna ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi, ili hawa watu ambao tunataka tuendelee kuwawezesha kiuchumi kupitia sasa kwenye benki zetu tuhakikishe tunaendelea kuwajengea mazingira yaliyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana issue ya gharama, kuna gharama kubwa sana na usumbufu mkubwa sana kwa mtu kwenda ku-apply mkopo benki. Cha kwanza tusiwaengue maafisa maendeleo moja kwa moja, tuendelee kufanya kazi kwa karibu sana kati ya benki ya maafisa maendeleo. Pili benki sasa tunakwenda kuzipatia mtaji ambao wao hawana hata ile cost of funds, tunakwenda kuwaongezea capital kupitia hizi fedha za 4:4:2. Niwaombe sasa ikiwezekana zile gharama za mikopo benki wazibebe wenyewe, wasiwabebeshe vijana wanawake wala watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe sana suala la muda, vijana wengi pia hawana dhamana, benki nyingi zinahitaji dhamana, tuliangalie suala hili. Kule kwenye halmashauri zetu walikuwa wanatubeba kwa nafasi zetu kama tulivyo. Leo hii Mheshimiwa Bashe anajaribu kuanzisha BBT ili tusaidie vijana kumiliki ardhi tupate dhamana kuingia benki. Sasa niombe sana hizi fedha zinapopitishiwa benki tuwe makini na kale kautaratibu ni jambo zuri, lakini tuhakikishe pia hatuumizi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zuri, mimi nampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ni kweli kulikuwa na changamoto nyingi, CAG ameonesha upotevu mkubwa uliokuwa unatokea kwenye halmashauri zetu. Tunaamini fedha hizi zikipita huku zinakuwa na ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe kuwepo na timu za watu ambao wataendelea kuwa-monitor hawa vijana. Hata kama wakishapewa hizi fedha waendelee kuwafatilia ili wahakikishe kwamba fedha hizi zinazaa na zinakuwa na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia Mheshimiwa Rais nimpongeze sana na nimshukuru kwa sababu alitenga fedha shilingi bilioni 20 ili kuhakikisha mikoa ya Kanda ya Ziwa inaweza kunufaika na rasilimali ziliozoko katika Ziwa Victoria. Walikuja watu wa wizarani tuliunda vikundi vya vijana katika Mikoa ya Mwanza, Kagera, Simuyu, Geita na Mara. Vikundi viliundwa vikawa vetted tukaandika maandiko, maandiko yakaenda Wizarani, yakapitiwa yakafanyiwa vetting watu wa Wizarani wakaja wakatoa mafunzo kwa vijana na mwisho wa siku ikaja list ya vikundi ambavyo vime-qualify kupata fedha na idadi ya fedha ambayo vikundi hivyo watapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza cha kushangaza tarehe 13 Juni wamekuja tena watumishi wa Wizarani kule Mwanza kuzungumza na vijana; na badala yake wamekuja kutuambia mambo ambayo ni tofauti kabisa na vile tulivyokuwa tumekubaliana. Vikundi hivi vilitakiwa vianze kufuga samaki kwa njia ya vizimba kwenye Ziwa Victoria. Kwenye makubaliano ya Mwanza vikundi hivi kwenye fedha zile milioni 130 kwa kila kikundi, vilitakiwa vipewe vizimba, samaki, chakula pamoja fedha kwa ajili ya kufanya doria na kutunza vile vizimba kwa miezi nane ili baada ya hapo fedha hizi waweze kuzirejesha, na fedha hizi zilikuwa zinapitia TADB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza wamekuja watumishi wa Wizara kuja kuwaambia vijana kwamba tofauti na walivyokuwa wamekubaliana, kwamba venders wa hivi vizimba, chakula cha Samaki na vifaranga itakuwa ni makubaliano kati ya vijana na Wizara; na fedha ile hawatapewa vijana itaenda kulipwa kwa wale venders moja kwa moja; na jambo hilo vijana wamekubali. Changamoto inakuja watumishi wa Wizara wamkuja kuwaambia vijana kwamba wao wenyewe ndio watakaochagua venders. Wao ndio watachangua venders wa vizimba, Samaki, na chakula. Lakini experience inatuonesha kwamba watu wengi wameshaanza kufuga Samaki kwa vizimba na wamefeli. Wamefeli kwa sababu ya uduni wa ubora wa vizimba, uduni na udumavu wa vifaranga pamoja na chakula kisicho bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii watu Wizara wanakuja kutuambia tutafanya haya, kama hamtaki acheni. Je, hii ndiyo lugha ambayo Mama Samia amewatuma kuja kuwaambia vijana? Hii ndiyo lugha ambayo Mama Samia ametoa bilioni 20 ili vijana waje waambiwe hivyo? Leo hii vipi kuhusu hivi vizimba vikiletwa na havina ubora? Je, vifaranga vikiletwa na vikadumaa au chakula kisicho na ubora. Mikopo hii wanabebeshwa vijana wao ndio walipe, wanalipaje vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka ni kwamba makubaliano ya mwanzo yabaki vilevile. Vijana wakae na kujadiliana venders na Wizara ili wale watakaoridhia ndio wapewe tender ya kuleta hivyo vitu ili hata mwisho wa siku hivi vitu vikiwa si bora vijana waweze ku-own makosa yao na kulipa fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia vijana wamekuja kuambiwa na watumishi wa Wizara kwamba hatutalipa tena fedha kwa ajili ya doria, fedha za kujikimu kwa kila kijana kwa hii miezi nane wakati mnafatilia huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea mradi wa miezi nane, vijana wakati wanafatilia mradi huu watakuwa wanatumia nini? tunatishia vijana kuweza kutekeleza miradi hii ili kwenda kutafuta fedha za kujikimu. Lakini fedha hizi hawapewi bure ziko ndani ya mikopo ambayo maandiko ya wizara yalikuwa yameshakubalia kuwapa fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki ni kitu ambacho soko lipo. Mwanza sasa hivi as we speak wanaboresha airport iwe ya kimataifa. Tuna Daraja la Magufuli ambalo linatusaidia kutoa Samaki kupeleka nchi za jirani. Tuna SGR ambayo pia itatusaidia kusafirirsha bidhaa hizi kwa wepesi. Tuna viwanda vingi sana vya minofu ambavyo mpaka sasa malighafi haitoshi. Zao hili tunaloenda kutoa kwenye Ziwa Victoria wala soko lake halina mashaka. Kwa nini Wizara inapata kigugumizi kutoa fedha hizi kwa vijana kama tulivyokuwa tumekubaliana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zinasema fedha hizi milioni 130 kwa kila kikundi zimetoka, hizi fedha ambazo Wizara sasa inasema hazitowapa vijana zimeenda wapi? tunahitaji tuambiwe na hii lugha ya kuwaambia vijana kwamba tutafanya hivyo la sivyo kama hamtaki acheni, basi acheni kwa sababu mnawatengenezea vijana bomu la kuwapa miradi ambayo itashindwa kuwa sustainable. Leo hii tunatengeneza vile vizimba vya zaidi ya milioni 60 mpaka 100 kuweka ndani ya Ziwa Victoria halafu unamnyima kijana milioni mbili tatu ya kijikimu ili kukifatilia kile kizimba. Leo hii mtu anatakiwa kukodi boti ya kwenda kufanya doria za ulinzi na kulisha wale Samaki shilingi 60,000 mpaka 80,000 kwa siku ndani ya miezi nane kijana anapata wapi hizi fedha? Atapata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwatengenezee mazingira vijana ya kuonekana wao hawawezi kufanya kazi, tusiwatengenezee mazingira vijana ya kuonekana wao si wasikivu na wala si wachapakazi. Vijana wanayo nia tuwashike mkono na tufate maelekezo kama Mama Samia anavyotaka. Tusimchonganishe Mama na Vijana wake, hatutakubali. Vijana tumemwelewa Mama tutampigia kura kwa nguvu 2025 kwa sababu tunajua chote anachokifanya ni kuhakikisha vijana wa Tanzania tunanufaika na matunda ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nitafurahi sana kama Mheshimiwa Waziri akija katika kuhitimisha hoja yake akatupa majibu vijana wa mikoa hii mitano. Kwamba hii project itaishia wapi na nini kinaenda kutokea kwenye zile fedha ambazo Wizara imetuambia kwamba haitazileta ilihali tunajua zimetoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba, Watanzania wanaishi kwa haki, demokrasia, umoja na wanaishi kulingana na sheria zinavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nitakuwa nipo sahihi nikisema kwamba, mwanahaki za binadamu namba moja Tanzania kwa sasa ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hili kwa kweli amefanikiwa kwa ukubwa sana, ameanzisha Tume ya Haki Jinai ambapo maoni ya Watanzania yamechukuliwa na yanafanyiwa kazi. Bunge hili hili tumepitisha Sheria za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, tunaendelea kufanya mabadiliko mbalimbali ya sheria kuhakikisha kwamba, demokrasia na haki za binadamu Tanzania zinaendelea kulindwa. Naipongeza sana Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaendelea kufanya kuhakikisha kwamba Watanzania wote haki zao zinalindwa na kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mchango wangu wa leo utajikita kwenye Fungu Namba 59 la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. Tume hii imeanzishwa chini ya Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura Na. 171 ambayo tulianzisha tangu mwaka 1983. Kati ya majukumu makuu kabisa ya Tume hii, ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, inaziangalia na kuzitazama Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziendane na mazingira ya wakati huo na kuhakikisha kwamba, zinaendana na mabadiliko endelevu ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka uliopita taarifa zinatuonesha Tume hii ilitengewe shilingi bilioni 5.1, lakini mpaka tunavyozungumza Tume hii imepewa fedha kwa 53% tu ambayo ni sawa na shilingi bilioni 2.6. Changamoto ya ukosefu wa fedha katika Tume hii ya Kurekebisha Sheria ndiyo ambayo inatufanya mpaka sasa tunakuwa na sheria nyingi ambazo zimepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria nyingi sana amezitaja Mheshimiwa Noah, akionesha kuna Sheria ya Ndoa ambayo mpaka sasa haijarekebishwa na Bunge hili, kuna Sheria za Ardhi ambazo zina migogoro, kuna Sheria za Wanyamapori ambazo zina migogoro kwa wananchi. Sheria hizo zingeweza kubadilishwa kwa wakati kama tungeipatia fedha za kutosha Tume hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili naomba kushauri, tuipatie fedha za kutosha Tume hii ili mabadiliko yafanyike kwa wakati. Nitatoa mfano, leo hii kwenye Sheria zetu za Utumishi wa Umma, tuna mifumo ambayo ni centralized. Tumeianzisha mifumo hii kwa sheria za zamani na sera tunayoitumia sasa pia ni ya muda mrefu sana, sheria hii imeshakuwa na upungufu mkubwa sana kulingana na mazingira tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna mfumo centralized wa kupata waajiriwa wote Serikalini. Ajira zinatangazwa, watu wanaomba na tunakuwa na mfumo mmoja wa kuchakata nafasi hizi za ajira, lakini tumeona na tafiti mbalimbali zimefanyika zinazoonesha Tanzania ya sasa inahitaji mfumo decentralized. Inahitaji ajira zinapotangazwa zishushwe kwenye maeneo yetu, kama ni mikoa au wilaya ili watu wote Watanzania waweze kugawana nafasi hizi za ajira kwa usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa Sera yake ya Elimu Bure na kwa kuendelea kuongeza mikopo kwenye elimu ya juu. Sasa hivi hakuna mkoa usio na wasomi, hakuna wilaya isiyo na wasomi, hakuna kata isiyo na wasomi. Wasomi wametapakaa kila sehemu. Tunahitaji mabadiliko ya sheria na sera zetu ili zinapotangazwa ajira zishushwe kwenye mikoa na wilaya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano, kuna nafasi hapa zimetangazwa kama nafasi 46,000 tukigawana kwa mikoa 26 tunapata karibu kila mkoa nafasi 1,700. Kwa Mkoa wangu wa Mwanza ambao una wilaya saba tukigawana hizo nafasi 1,700 kila wilaya inaondoka na nafasi zaidi ya 250. Itakuwa ni ngumu sana kwa kijana yeyote au mtu yeyote aliyeomba ajira kulalamikia mfumo wa upatikanaji wa ajira ilihali hata kama hajapata yeye anajua katika wilaya yake au kata yake kuna watu kadhaa wamepata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itatuondolea sana migogoro mingi kati yetu sisi na wale ambao tunawaongoza. Pia, katika hili hili la kurekebisha sheria, nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona kwamba kuna haja ya kufanya mapitio katika ile mikopo ya 10%. Naipongeza sana Serikali katika bajeti ambayo imesomwa na TAMISEMI hapa wiki iliyopita, wametuambia kwamba tunarudisha ile mikopo ya 10% kwa halmashauri kadhaa kwa mfumo mpya na halmashauri nyingine kwa mfumo ule ambao utaangaliwa kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hii tuliipitisha kwa Sheria ya Bunge. Tunahitaji Sheria iletwe hapa Bungeni ili tubadilishe kuruhusu mikopo hii kuanza kupitia benki. Leo hii tumetoa tamko hapa lakini tutakuwa challenged tunapitiaje benki bila kurekebisha sheria? Tutenge fedha kwa Tume hii ya Kurekebisha Sheria ili walete mabadiliko ya Sheria ya Fedha katika halmashauri zetu tuweze kuanzisha huu mfumo mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumekuwa tunapiga kelele sana kwamba, tunahitaji sheria iletwe kwa ajili ya kuwapa kipaumbele wale wanaojitolea katika halmashauri zetu wapewe kipaumbele pale ambapo ajira zitatangazwa. Sheria hii imekuwa ya muda mrefu sana tunajua itakuja lakini haiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa Wizara hii na chini ya Tume hii iangalie sheria tulizonazo izirekebishe ili mtu yeyote anayeomba kujitolea kupata mentorship kwenye ofisi zetu, kwanza waruhusiwe. Kwa sababu kwa mfumo uliopo sasa hivi, mtu anaomba kujitolea kama vile anaomba kulipwa mshahara. Anaomba kufanya kazi bure, anaomba kujitolea kwa muda wake, lakini ataongeza pia uzalishaji na utoaji wa huduma lakini wanapata usumbufu sana. Tuletewe sheria watu waruhusiwe kujitolea, lakini wale wanaojitolea wapewe kipaumbele kwenye ajira zinapotangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya yatawezekana kama tukiiwezesha Tume hii ya Kurekebisha Sheria chini ya Fungu hili 59 kupata fedha zake kwa asilimia zote 100. Sheria zetu zianze kuendana na mazingira tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, misingi ya umoja, amani na uhuru tuliyonayo katika nchi yetu hii ilijengwa, haikutokea tu na ilijengwa kuanzia katika ngazi za familia. Tuna haja ya kuilinda sana taasisi ya familia. Kwa takwimu zilizopo sasa hivi inaonekana kwamba divorce rate kwenye nchi yetu inaongezeka kwa kasi na ni kwa kasi ambayo inatia mashaka ya ustahimilivu wa taasisi hii ya familia. Moja ya sababu ambazo zimeonekana zinaongeza rate ya divorce au talaka kwenye nchi yetu, ni umbali wa waajiriwa wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baba ameajiriwa Mwanza, mama kaajiriwa Mpanda, mama kaajiriwa Mara, baba kaajiriwa Rukwa. Hii ndiyo inaongeza wingi wa talaka. Kama tunataka kuhakikisha watoto wetu wanalelewa katika malezi bora tuhakikishe kwamba misingi ya mila na tamaduni zetu katika nchi hii zinalindwa, tuhakikishe kama Serikali inalinda taasisi hii ya familia. Tupitishe sheria hapa, tuzipitie sheria zetu za utumishi ili kuwepo na misingi inayobana utumishi wa umma katika kulinda familia. Kama baba ameajiriwa Mwanza hata kama ni wilaya tofauti, mama naye asogezwe karibu ili kulinda familia na taasisi hii kuhakikisha kwamba tunakuwa na kesho ya watoto wetu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya mimi pia kupata kuchangia juu ya Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2021, ambao lengo lake kuu ni kuhakikisha kwamba lugha ya Kiswahili inakuwa lugha ya sheria katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa lugha yetu ya Kiswahili kama ilivyowasilishwa katika maoni ya Kamati ni lugha ya Taifa na ni lugha ambayo ilikuwa na msingi mkubwa sana katika kutuunganisha kupigania Uhuru. Kwa hiyo lugha hii inajenga dhana nzima ya uzalendo kati yetu sisi Watanzania na kuzidi kuitangaza na kuitangaza nchi yetu katika nchi zote za kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ametangulia kusema msemaji aliyepita kwamba kigezo cha Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kujua kusoma na kuandika. Lugha ya kiingereza ni lugha ambayo tumeipokea, ni lugha ya kimapokeo kutoka katika nchi zingine, kwa maana ya kwamba kigezo cha kujua kusoma na kuandika kinajumlisha tu kujua lugha yetu ya Taifa. Hivyo sheria zikiletwa kwa lugha ya Kiswahili katika Bunge hili tukufu na amini hata sisi Wabunge tutapata nafasi nzuri zaidi ya kusoma sheria hizo, kuzielewa na kuweza kuzichangia kwa manufaa mazima ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukipitisha pia sheria hii na kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kisheria hii nayo itakuwa inajumlisha kabisa haki ya Mtanzania kuweza kuelewa mambo yote yaliyomzunguka, wote tunafahamu kwamba kila kinachofanyika katika nchi yetu kinafanyika kwa misingi ya sheria, kama Mtanzania hata pata nafasi ya kusoma sheria na akazielewa kwa sababu anashindwa kuelewa lugha iliyotumika kuziandika sheria hizo maana yake moja kwa moja tunamzuia Mtanzania huyu kuelewa haki zake na wote tunafahamu kwamba ignorantia juris non excusat kwamba ignorant of law is not an excuse. Sasa Watanzania wasipoelewa lugha zao maana yake tunaweza moja kwa moja kuwakosesha haki zao za msingi kabisa za kuendelea na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kama tulivyoeleza katika ripoti ya Kamati sisi hatutakuwa wa kwanza kuifanya lugha yetu ya taifa kuwa lugha ya kisheria. Nchi mbalimbali zimekwisha fanya hayo na ikawezekana mabadiliko yanachukua muda na gharama lakini naamini faida kubwa tutakazozipata za kiuchumi na hata za haki na usawa katika nchi hii zita-justify matumizi mazima ya lugha yetu ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa kusema haya naomba Bunge hili Tukufu lipitishe mabadiliko haya ya sheria. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia katika Muswada huu muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali yetu ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Project hizi kubwa ya kimkakati ambazo zitasaidia sana katika maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu umekwisha sainiwa na Muswada huu ni moja tu ya takwa la mkataba huu ili kufanya sheria zetu ziendane na utekelezaji wa mkataba huu. Ni vyema pia watanzania wakifahamu kwamba katika Project hii ya Bomba la Mafuta, mafuta haya si ya kwetu Tanzania, sisi tunachotoa kama watanzania tunatoa light of passage maana yake tunatoa ardhi yetu ili bomba hili litoke Uganda kuja mpaka Tanga kwa ajili ya usafirishaji kwenda katika pande zote za dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafaida nyingi sana ambazo sisi vijana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutafaidika nazo ukiachana na kwamba rasilimali hii si ya kwetu. Kwanza kabisa tutapata ajira nyingi sana inakadiriwa ajira 6000 mpaka ajira 10,000 zitazalishwa katika bomba hili, lakini ifahamike wazi kwamba asilimia 80 ya bomba hili zipo Tanzania, maana yake ni kwamba hata zaidi ya asilimia 80 ya ajira hizi possibly tukisimama vizuri Serikali maana yake ajira hizi zitatoka kwa watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu katika mkataba huu basi Serikali yetu ihakikishe inasimamia sana sana regulation zetu za Local Content ili kuhakikisha watanzania ndiyo wafaidika wa kwanza wa ajira zote hizi. Fursa nyingi sana tutapata katika mkataba huu, tutapata nafasi za usafirishaji na kusafirisha watu na mizigo, ajira katika huduma za ulinzi, ajira katika kuzalisha na kuuza mazao ya vyakula na mifugo, huduma za kupika vyakula na kutoa vinywaji baridi, kuna huduma za malazi ya hotel na kuhifadhi wageni, kuna vifaa vya matumizi ya ofisini, kuna huduma za kuuza mafuta ya petrol na diesel na nyingi nyingi hizi zote ni ajira ambazo vijana wa watanzania tutafaidika nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali katika mkataba huu niwaombe sana Serikali ili sisi vijana wa Tanzania tuweze kufaidika na fursa zote zitakazopatikana katika mradi huu, usimamizi madhubuti unatakiwa, maana yake Serikali ifanye juhudi ya makusudi ya kusimamia ikiwa ni pamoja na kuweka maelekezo kwamba watanzania wawe wanufaika wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Muswada huu kuna marekebisho mengi sana ya Sheria ambayo yanatoa mwanya, kwa sababu Mkataba huu ni wa Kimataifa kwetu sisi watanzania kuweka equal grounds za bargaining za ajira kwetu sisi na watu wa Kimataifa. Lakini Serikali yetu ikisimama kidete maana yake watanzania kwa sababu bomba hili zaidi ya asilimia 80 ziko Tanzania maana yake tutakuwa wafaidika au wanufaika wakuu wa ajira zote zinazopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niiombe Serikali sisi, vijana wa Tanzania hatukuwepo wakati miradi kama TAZARA au TAZAMA inafanyika, maana yake ni kwamba hatuna experience ya kutosha ya miradi mikubwa yenye nature kama hii. Niiombe Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha inatumia mradi huu kuwa kama ground ya vijana kujifunza ili sisi tunapokuwa tunaendelea kama nchi kupata miradi mikubwa kama hii basi watanzania tusiwe nyuma tuwe tumekwisha jifunza tumepata uzoefu wa kutosha namna ya kusimamia namna ya kutekeleza miradi hii, ili tuendelee kutekeleza miradi yetu sisi wenyewe watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika suala zima la CSR, CSR si katika kujenga tu majengo ni pamoja na technology au knowledge ambayo watu hawa au kampuni hii inaweza ikatuachia vijana watanzania tukaendelea kurithishana vizazi na vizazi ili miradi hii ya kimkakati inapoendelea kufanyika basi tunaendelea kuisimamia kama wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, 2022
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia katika Muswada huu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 1 wa mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kuipongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kwanza kabisa kwa kutuletea Muswada huu kwa lugha ya Kiswahili ikiwa ni namna mojawapo ya kutekeleza matakwa ya Sheria iliyotungwa na Bunge hili Tukufu. Pia niweze kusema kwamba maafa ni jambo linalotokea kwa dharura, tunakuwa hatuja-foresee mambo haya na Muswada huu kama walivyotangulia Wabunge wenzangu umekuja kwa muda muafaka.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa sababu ya issue muhimu sana ya mabadiliko ya tabianchi na maafa nayo yamekuwa mengi. Kwa hiyo, sheria hii kwa utungaji wake na tukienda kuitekeleza vizuri hasa ukizingatia sheria hii imekuja kuangalia, namna ya kuwasaidia wananchi moja kwa moja kuanzia ngazi ya chini, naamini tunaweza kupunguza majanga makubwa sana yanayowapata wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuli-convince Bunge hili Tukufu kuipitisha sheria hii kwa hoja zifuatazo: Kwanza, ni juu ya issue ya urasimu wa kamati zilizoundwa katika sheria hii. Katika sheria iliyofutwa kamati hizi zilikuwepo baadhi na baadhi sasa zimeundwa, lakini bado urasimu ulikuwa mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali imepokea maoni ya Kamati, imepunguza urasimu kwa maana ya wingi wa Wajumbe na utaratibu unaotumika kuunda Kamati hizi. Pia, kwa namna ya pekee namwomba Mheshimiwa Waziri kwa kutumia Ibara ya 39 ambayo inampa nguvu ya kwenda kutengeneza Kanuni, basi aangalie namna ambayo Kamati moja haitazuia Kamati nyingine kutekeleza majukumu yake pale ambapo maafa yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hilo tutakuwa tumesaidia sana kupunguza bureaucracy kwa sababu tusipoweka kifungu hiki italazimisha kama hizi kamati fulani haijakaa, nyingine haiwezi kukaa. Hii italeta madhara makubwa ukizingatia majanga yanaongelea right to life (haki ya kuishi) ambayo ndiyo haki ya msingi zaidi ya mwanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili naomba niongelee suala la kuheshimu haki za binadamu za Mtanzania hasa Ibara ya 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mapendekezo ya kwanza kabisa ya sheria iliyokuwa imeletwa na Serikali katika Kamati ya Bunge hili Tukufu ilikuwa inampa nguvu Waziri, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kutumia mali za mwananchi wa kawaida (private/individual) mali yoyote ile wakati wa majanga bila kuwa imeongelea suala zima la fidia. Nashukuru sana Serikali imepokea maoni yetu na imeondoa mali za watu binafsi na sasa Serikali itatumia mali za Umma pekee katika majanga ili kuokoa wananchi kwa wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, naipongeza sana Serikali kwa sababu katika sheria hii imeweka inclusion ya Wizara zote ukizingatia kwamba suala la majanga hatuchagui whether litatokea kwenye maji, litaathiri chakula, litahusu moto, litaathiri miundombinu; kwa hiyo, imeweka WIzara zote ili kuhakikisha kwamba majanga yanapotokea kila Wizara kwa namna yake na kwa nafasi yake inahusika kutoa nafuu kwa wananchi kwa namna inavyowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nigusie tu pia suala la mfuko. Mchangiaji aliyepita amezungumza kwamba katika sheria iliyopita kulikuwa kuna ulazima wa Bunge hili kutenga fedha kwa ajili ya mfuko huu wa maafa. Naweza kusema kwamba section 29 ya sheria inayopendekeza kufutwa ilikuwa ndiyo imeongelea mfuko huu, lakini sources of funds za mfuko huu ilikuwa based on pure donations. Maana yake ni kwamba ilikuwa ni pale ambapo watu watachanga kwa upendeleo wao, ndiyo watu waweze kuhudumiwa kwa fedha zile katika mambo ya maafa.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa sababu katika sheria hii mpya iliyoletwa imeweka ulazima katika kila mwaka wa bajeti Serikali kupitia Bunge hili Tukufu kutenga fedha kwenda katika mfuko huu na fedha hizi zitumike siyo tu katika kukinga maafa, lakini kupunguza madhara ya majanga na maafa pale yanapojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizi, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri katika Kanuni zetu ambazo amepewa nguvu ya kutunga chini ya Ibara ya 39 ya Sheria hii, azingatie pia mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, cha kwanza, nashauri sana katika Kanuni hizi ahusishe suala zima la relief in loan repayment schemes, kwa maana ya unafuu wa malipo ya mikopo ya wananchi wetu. Serikali yetu katika utungaji wa sheria hii imechukua study kutoka katika nchi kama ya India na South Africa; na wenzetu wameenda mbali sana, wame-provide kwenye sheria zao kwamba yanapotokea majanga inatambua kwamba wananchi ndio waathirika wakubwa na wananchi wengi wanatumia fedha kutoka katika taasisi mbalimbali ambazo wanazipata kwa njia ya mikopo kuwekeza katika maisha yao ya kawaida na hivyo majanga yanapojitokeza kunakuwa na disturbance kwenye namna yao kwanza ya kujipatia kipato na hivyo katika kurejesha mikopo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali iangalie namna ya kuonesha katika kanuni ni namna gani wananchi hao wataangaliwa ikiwa ni pamoja na Serikali sasa kuona inawekaje kwa vile yenyewe kupitia Benki Kuu ndio wasimamizi wa taasisi za fedha, inaelekeza kwamba watu hao wapewe nafuu fulani fulani aidha ya muda au msamaha fulani ili tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha pili, nilikuwa nashauri kuwe na maboresho katika Shirika letu la Bima ya Taifa. Tumesema kwamba Bunge hili litatoa fedha au litatunga sheria au katika kupitisha bajeti litatoa fedha kwa ajili ya mfuko huu. Nachelea kusema kwamba, mfuko huu ni kwa ajili ya muda ule ambao majanga yanatokea, lakini baada ya majanga wale wanaachwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza kusema kwamba ni muhimu sasa Serikali kupitia Wizara zinazohusika kuangalia namna ya kuboresha Shirika letu la Bima ili kwanza, tuwape elimu wananchi kwa umuhimu wa kukata bima katika mali zao; pili, tuangalie namna, ikiwezekana kutoa ruzuku kwenye Shirika hili ili Bima za mali za wananchi hasa wa kipato cha chini ziweze kukatwa kwa bei ndogo. Hii itaipunguzia sana Serikali mzigo mkubwa pale ambapo majanga yanatokea kwa namna ya kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba Bunge hili Tukufu kupitisha Sheria hii kwa sababu inakwenda kutusaidia sana wakati wa majanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 2) Act, 2022
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kama walivyotangulia kusema Wabunge wenzangu Muswada huu umekuja na marekebisho ya Sheria Tatu, nikianza na Sheria yetu ya kwanza ambayo inahusiana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu naungana moja kwa moja na Wabunge wenzangu waliotangulia kusema kwamba tunashukuru sana kwa sababu Serikali imeona unyeti wa jambo hili na nachelea kusema kwamba mambo haya usafirishaji haramu wa binadamu na biashara ya madawa ya kulevya waathirika wakubwa zaidi ni vijana.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali imeona haja ya kuongeza adhabu kwenye mambo haya hasa hasa haya ya usafirishaji haramu wa binadamu. Nami kwa kutoa tu mawazo yangu kwa sababu kuna mazingira ambayo Serikali imekwishaona ya kujirudia kwa makosa haya, kwamba mtu anahukumiwa mara ya kwanza anapewa adhabu, mara ya pili anarudia tena ya tatu na Zaidi, ninaomba tuone namna ya kuweka adhabu ya kifungo cha maisha bila mbadala wa faini ili tuweze kudhibiti watu hawa, kwa sababu biashara hii inakwenda ku-determine moja kwa moja haki za binadamu za watu wetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala zima la mabadiliko ya Sheria hii inayohusiana na Udhibiti wa Madawa ya Kulevya nami niungane na Wabunge waliotangulia kuipongeza Serikali kwamba, bado inaendelea kuangalia namna mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunadhibiti biashara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikinukuu takwimu zilizotolewa kwenye taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2021 ya nchi yetu iliyotolewa na Tume yetu ambayo inatoa taarifa kuanzia mwaka 2021 mpaka Juni 2022, taarifa hii inaonesha kwamba kwa miaka karibu Tisa tangu mwaka 2012 mpaka 2021 kumekuwa na uongezeko mkubwa sana wa kilo za madawa ya kulevya hasa heroin yanayokamatwa kwenye nchi yetu. Kuongezeka huku cha kushangaza hakuendi sambamba na kuongezeka kwa watuhumiwa wanaokamatwa. Maana yake ni nini, watuhumiwa wale wale wanaokamatwa idadi ile ile ongezeko dogo sana au pungufu dogo lakini kiwango cha dawa zinazokamatwa kinaongezeka. Nitoe mfano takwimu za mwaka 2021 zinaonesha kwamba watu 588 wamekamatwa wakiwa in possession ya heroin, madawa ya kuleya aina ya heroin na takwimu hizi zinaenda sambamba na zile takwimu za mwaka 2014 ambapo watu 584 walikamatwa.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 watu hawa 584 walikuwa na kilo 400 za heroin wakati mwaka 2021 watu hawa hawa 588 walikuwa na kilo zaidi ya 1,500 ya heroin. Mimi naomba kui-challenge Serikali wao wametoa sababu kwenye taarifa yao kwamba hii inasababishwa na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya wananchi na Tume yetu na vyombo vyetu ambayo imesaidia kupatikana taarifa kwa wepesi zaidi na hivyo wamekamata kiwango kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, hii ingekuwa ni sababu pekee nadhani tungekuwa tumeona ongezeko la watu sambamba na ongezeko la kilo, sasa hii mimi nachelea kusema inatuonesha kwamba kunaweza kuwa na watu wale wale ambao adhabu zetu zinawapa nguvu ya kurudi kwenye jamii na kwa vile tumesha-establish na Wabunge wenzangu wamesema kwamba hii ni biashara ambayo ni organized imepangwa vizuri kimkakati na inafanyika kwa watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha, maana yake wanapata nguvu ya kufanya zaidi wanapata uwezo mkubwa zaidi wa kifedha na hata udhibiti wao nadhani unakwenda kuwa mgumu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ongezeko hili la kilo nyingi zaidi za dawa za kulevya zinaashiria ongezeko la idadi ya watu ambao wanaathiriwa na dawa hizi za kulevya. Kama Serikali inaamini kwamba kuanzisha mahabusu private kwa Tume hii ya kuwa ina-handle watu hawa inakwenda kupunguza idadi ya kilo hizi na hivyo kupunguza idadi ya waathirika, mimi naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia. Lakini tu nitoe pendekezo langu na ushauri wangu kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba naunga mkono hatuwezi tuka- ignore ukweli kwamba bado rasilimali fedha ni tatizo. Bado ni kweli kwamba kuna mahabusu ambazo bado tunahitaji ziwepo lakini hazipo kwa sababu za kibajeti, bado tunahitaji vituo vingi zaidi vya Polisi lakini havipo kwa sababu ya changamoto za kibajeti, hivyo kama tumeamua kwenda kuanzisha mahabusu hizi ninaishauri Serikali iangalie kwanza na kutoa kipaumbele kwa Mikoa mikubwa ya kimkakati ambayo takwimu zinaonesha kwamba ina mzunguko mkubwa wa biashara hizi ili sasa tuanze kudhibiti kule na kadri rasilimali fedha zinavyozidi kupatikana basi tuende na sehemu zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia wakati tunaanzisha mahabusu hizi tusisahau suala zima la haki za binadamu ili mwisho wa siku tusije tukazitumia hizi sasa kama kichaka, watu wakiingia kule akija kutoka tumemsahau. Tumeona kwamba hata kuna kipindi Mheshimiwa Rais alipiga kelele kwamba Majeshi yetu ya Polisi kuna namna yanatumika kuvunja haki za binadamu, basi hebu tuendelee kuhakikisha kwamba tuna-withhold haki za binadamu ili hizi mahabusu zetu ziendelee kuwa zinaangalia haki hizi.

Mheshimiwa Spika, pia tuendelee kutoa mafunzo kwa watumishi wetu wanaohusika kwenye suala zima la ku-handle haya madawa ya kulevya ili waendelee kuwa na uadilivu, waendelee kuendana na kasi ambayo Serikali yetu inaona kwamba ni muhimu tuende nayo ili tupunguze changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami kwa hoja hizi naomba kuliomba Bunge lako Tukufu kupitisha mabadiliko haya kwa sababu ya tija kubwa inayokwenda kuwa nayo kwenye jamii. (Makofi)
The Prevention and Combating of Corruption (Amendment) Act, 2024
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Miswada hii muhimu, lakini mchango wangu wa leo nitajielekeza zaidi katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Mheshimiwa Rais, kutumikia katika Wizara hii muhimu. Pia, nampongeza sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na viongozi wengine wote ambao wameendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuhudumu katika kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze pia kwa kuipongeza Serikali kwa sababu lengo la Muswada huu ni kuhakikisha kwamba inaendelea kuipa nguvu PCCB kulingana na malengo kabisa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba anaondoa rushwa katika nchi yetu. Naipongeza Serikali kwa sababu kuna vifungu ambavyo leo hii mimi naliomba Bunge lako Tukufu litusaidie kupitisha marekebisho haya ili kuiongezea nguvu PCCB kwenda kufanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha Saba kinarekebishwa ili kuongeza wigo wa PCCB katika kufanya kazi zake. Sheria iliyokuwepo ilikuwa inaipa mamlaka PCCB kufuatilia makosa yale yaliyo chini ya sheria hiyo pekee. Sasa tunaomba Bunge hili lipitishe marekebisho haya ili kuongeza wigo wa makosa ambayo Taasisi hii ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inakwenda kushughulikia kuunganisha makosa mengine ambayo yapo katika sheria nyingine zote. Hii itaendelea kuiongezea mikono na kuipa nguvu taasisi hii muhimu ili iendelee kutusaidia kuondokana na adui rushwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia kwa marekebisho haya kwa sababu Kifungu cha 10 kinalenga kuharakisha utaratibu wa kushughulikia kwa misingi ya Kimahakama watu wanaokutwa au wanaoshitakiwa na makosa haya ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua kwamba kuna muda mrefu ambao kesi zinakaa Mahakamani kwa sababu tu ya technicalities, kesi inakaa miaka mingi sana. Huku nje jamii inajua kwamba kuna mtu anashitakiwa kwa makosa ya rushwa labda hata ushahidi wake ulikuwa ni wazi na kila mmoja ana ufahamu lakini kwa sababu ya technicalities kesi hizi zinakaa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha kwamba tunapunguza hizi technicalities ili makosa haya yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kukamilika. Kwa hiyo, hii itatusaidia pia kuongeza imani ya wananchi wetu kwa Serikali yetu, lakini pia kwa Mahakama zetu kwa sababu wananchi wanapenda kuona pale ambapo kuna makosa yanafanyika hata ya ubadhirifu na rushwa yanafanyiwa kazi kwa haraka. Naipongeze sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali kwa mapendekezo ya mabadiliko ya kifungu cha 15, 16, 17, 18 na 20 katika sheria tuliyokuwanayo. Lengo pia la vifungu hivi ni kuhakikisha kwamba tunaongeza wigo wa kuwapa adhabu wale wanaokutwa na makosa haya ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria iliyokuwepo ilikuwa inaruhusu mtu anapokutwa na hatia ya makosa haya ya rushwa, chini ya sheria hii faida zozote zile ziwe ni za fedha au za kinamna nyingine yoyote kutokana na rushwa, basi kama ni fedha zinataifishwa na kurudishwa Serikalini katika mamlaka husika ili asiweze kunufaika kwa namna yoyote na vitendo vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mabadiliko ya sheria yanaongeza wigo sasa wa namna Serikali inapoweza kushughulikia proceeds hizi za uhalifu huu ambao mtu anaweza kuwa amefanya, na kimsingi kama nilivyosema mwanzo inaongeza imani kubwa sana ya wananchi kwa Serikali hata kwa Mahakama zetu na vyombo vya haki kuona kwamba mtu anapokutwa na makosa haya, basi asiweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jamii zetu, watu wanaamini kwamba wanaweza wakafanya kosa, ukikamatwa utatumikia kama ni kifungo cha miaka mitatu, minne, mitano na ukitoka, basi utazikuta fedha zako zile ulizozipata kwenye ubadhilifu au rushwa. Sasa Sheria hii imezidi kutuonesha kwamba pale unapokutwa na makosa haya, basi yale manufaa unayoyapata yataondolewa kwako na kurudishwa katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wale waliochangia mwanzo katika maoni katika Kifungu hiki cha 25 kinachozungumziwa kuhusu rushwa ya ngono. Mapendekezo yaliyokuwa yameletwa na Serikali yetu kimsingi yalikuwa yanakwenda kumkandamiza na kumnyamazisha kabisa mhanga wa rushwa hii ya ngono. Wote tunafahamu kwamba ili mtu atoe rushwa anajikuta hana option nyingine yoyote na anaamini kwamba bila kutoa hiyo au bila kulazimika kufanya hivyo, basi anaweza asifanikiwe kile anachokihitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wanaotoa rushwa hizi za ngono kitakwimu ni wanawake na hii pia ni form nyingine ya ukatili wa kijinsia. Leo hii tukiweka vifungu ambavyo vinanyamazisha au vinampa adhabu mhanga wa rushwa ya ngono anapokuja kutoa taarifa kwa namna moja au nyingine tunahalalisha vitendo hivi vya rushwa ya ngono kwa sababu watu hawatakuja tena kutoa taarifa wanapotendewa vitendo kama hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi au zaidi ya 99% yeyote anayekubali kutoa rushwa ya ngono sio kwamba anapenda, hapendi, ni udhalilishaji uliopitiliza. Rushwa ya ngono ina hasara nyingi kuliko hata rushwa ya fedha. Kuna uwezekano wa kupata maradhi. Mtu anaweza akapata ujauzito, mtu anaweza kupata emotional torture ambayo atakaa nayo kwa miaka mingi, lakini ni udhalilishaji wa utu na uvunjifu wa haki za binadamu uliopitiliza. Kwa hiyo, siamini kwamba kama mtu analazimika kufanya kitendo hiki naye basi tumpe adhabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, pamoja na kuona spirit ya Kamati ambayo naipongeza sana kwa kweli imetoa maoni ambayo Watanzania wengi tunayo vichwani mwetu, pia, naipongeza Serikali kwa sababu imeonesha nia ya kukubaliana na maoni ya Kamati ambayo pia naamini ni maoni ya Wabunge wengi na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu nafikiri ni wakati sasa wa kuendelea kuimarisha au kuboresha mifumo ya utoaji wa taarifa katika vitendo hivi vya rushwa ya ngono ili kuwalinda sasa hawa wahanga. Pia tuendelee kuhakikisha kwamba wale wanaotolewa taarifa za vitendo hivi vya rushwa ya ngono wanafanyiwa kazi au kushughulikiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwepo na mara kadhaa kuna clip hata za watu fulani zinavuja kwenye mitandao ambao wanakuwa wanahitaji rushwa ya ngono kwa watu ambao wanahitaji kitu kutoka kwao, lakini jamii haijulishwi namna gani vitu vinafanyiwa kazi. Inashusha pia imani ya watu kwamba hata nikienda kuripoti vitendo hivi labda havifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kama ushauri, kuangalia namna ya kuendelea kuvishughulikia vitendo hivi ili kuvipunguza na ikiwezekana kuviondoa kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naipongeza sana Serikali kwa sababu naamini kupitishwa kwa mabadiliko haya itakuwa ni mwanzo mzuri sana pia wa kupunguza ubadhirifu wa fedha na mali za umma lakini kuongeza uadilifu katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Naliomba Bunge hili Tukufu kupitisha mabadiliko haya kwa kura zote ili twende kuyafanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)