Primary Questions from Hon. Condester Michael Sichalwe (15 total)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kutatua migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi wa Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi katika Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba. Migogoro hii imetokana na uuzaji holela wa ardhi uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji katika kata hizo.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua migogoro hiyo, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Momba imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 38. Kati ya migogoro hiyo, migogoro 34 tayari imetatuliwa na migogoro minne ipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu rasmi wa kisheria katika uuzaji na ukodishaji ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji katika Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosha. Upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani Momba ni wastani wa asilimia 59.07 kupitia visima vifupi (16), visima virefu (43), skimu za usambazaji maji (17) na matanki ya kuvunia maji ya mvua (3). Katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani Momba, Serikali inatekeleza miradi ya maji katika Vijiji 13 vya Nkangamo, Itelefya, Mbao, Mkonga, Papa, Masanyinta, Kasamu, Samang’ombe, Lwatwe, Ivuma, Kapele, Mkutano na Kalungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zinazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matanki saba (7) yenye ujumla ya ujazo wa lita 600,000, ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilomita 32, vituo vya kuchotea maji 66 na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji umbali wa kilomita 72. Utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022. Kukamilika kwa miradi hiyo kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji. Serikali itaendelea kutenga fedha za utekelezaji wa miradi mwaka hadi mwaka ili kumaliza tatizo la maji katika Jimbo la Momba na kufikia lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka, 2025.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwanunulia mitambo ya kisasa na kuwapa mikopo wanawake ambao wanazalisha pombe za kienyeji?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nakushuru. Kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshiniwa Condester Michael Sichalwe Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uzalishaji na uuzaji wa pombe za kienyeji unaofanyika vijijini na katika baadhi ya maeneo ya mijini. Kwa sasa Serikali haijaanzisha mpango wa kuwanunulia mitambo ya kisasa na kuwapa mikopo wanawake wanaozalisha pombe za kienyeji. Hata hivyo, wanawake wajasiriamali wataendelea kupata mikopo kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya mikataba ya minara ya simu kati ya kampuni za simu na Kijiji cha Namuchinka Kata ya Kapele?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Namchinka kina minara miwili iliyojengwa na Kampuni ya Tigo na Halotel. Minara hiyo imesimikwa katika ardhi inayomilikiwa na watu binafsi na siyo kijiji. Hivyo, watoa huduma hulipa malipo ya pango la ardhi kwa wamiliki hao kulingana na makubalino katika mikataba waliyoingia.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu nitoe maelekezo kwa watoa huduma wote kuhakikisha kuwa wanashirikisha Serikali ya Wilaya na Kijiji wanapotaka kujenga minara ya mawasiliano katika Kijiji husika ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza ya namna hii. Vilevile, watoa huduma wahakikishe waingie mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali za Vijiji ili kuwa na ulinzi wa uhakika katika minara ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nitoe rai kwa wananchi kuwa wazalendo na kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wakati wa ujenzi na ulinzi wa miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa endelevu kwenye maeneo yetu.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, Serikali haioni kuna haja ya nchi yetu kurudi COMESA?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 19 zilizokuwa mwanzilishi wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) mwaka 1994. Tanzania ilijitoa katika COMESA mwaka 2000 kwa sababu ilikuwa ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo baadhi ya nchi za jumuiya hizo pia ni wanachama wa COMESA.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kujitoa kwa Tanzania kulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa nchi haitaathirika kiuchumi, kwani bado ni mwanachama wa EAC na SADC na kuwa lengo ni kulipunguzia Taifa gharama hasa michango ya wanachama.
Mheshimiwa Spika, tutakumbuka kuwa, mwaka 2008 nchi za COMESA, EAC na SADC zilikubaliana kuanzisha Utatu. Hivyo Tanzania inaendelea kushirikiana na COMESA kupitia Utatu huu (COMESA – EAC - SADC Tripartate Arrangement). Aidha, mwezi Septemba, 2021, Bunge lako Tukufu liliridhia Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA). Kuwa sehemu ya Utatu wa COMESA – EAC - SADC, na kuridhiwa kwa Mkataba wa AfCFTA kunaifanya Tanzania kuendelea kushirikiana na nchi za COMESA. Ahsante sana.
MHE.CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, lini Serikali itafufua Mradi wa Chumvi Ivuna – Itumbula Momba?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Chumvi cha Itumbula kilichopo Kata ya Ivuna Wilaya ya Momba kilianzishwa na wananchi ambao wameungana pamoja kutoka Kijiji cha Ivuna na Itumbula ili kuanzisha mradi wa kuzalisha chumvi kwenye bwawa la maji ya chumvi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua juhudi na jitihada za Wananchi wa Kijiji cha Itumbula na itahakikisha kuwa kiwanda hicho kinaanza uzalishaji. Serikali imeshatoa Shilingi milioni 120 kwa kuelewa kuwa ni mradi wa kimkakati lakini pia Halmashauri ya Wilaya ya Momba imetoa shilingi milioni 50 ili kusaidia katika kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Spika, aidha mikakati ya Serikali ni kuhakikisha tunahamasisha wawekezaji wengine kuwekeza katika kiwanda hicho.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, ni lini changamoto ya maji ndani ya Jimbo la Momba litatatuliwa?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua adha ya maji wanayopata Wananchi wa Wilaya ya Momba na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 miradi ya maji ya Msangano-Naming’ongo, Isanga - Kakozi na Tindingoma - Mlomba inaendelea kutekelezwa na itahudumia vijiji 11 vya Msangano, Nkala, Makamba, Naming'ongo, Yala, Ipata, Ntinga, Chindi, Isanga, Kakozi na Mlomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kupitia chanzo cha maji cha Mto Momba ili kuhakikisha wananchi katika vijiji vilivyobaki Wilayani Momba wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua migogoro kati ya Wananchi na maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kutatua migogoro baina ya hifadhi na wananchi. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kufanya tathmini ya aina, chimbuko na namna ya kutatua migogoro husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inasimamia misitu minne ya hifadhi katika wilaya ya Momba. Misitu hii ni Isalalolunga, Isalalo, Ivuna North na Ivuna South ambayo kimsingi haina mgogoro na wananchi. Katika kuimarisha ulinzi na usimamizi wa hifadhi hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu zikiwemo kuweka alama za kudumu za mipaka, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii, kuondoa wavamizi na kuchukua hatua za kisheria kwa wahalifu.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa ithibati kwa baadhi ya pombe za kienyeji ambazo zimekidhi viwango?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Mwezi Oktoba, 2022 jumla ya leseni 43 za ubora zimetolewa kwa bidhaa mbalimbali za pombe za kienyeji zilizokidhi viwango na maombi mengine mapya 22 yapo kwenye hatua mbalimbali za tathmini kuelekea kwenye kupata ithibati ya ubora. Aidha, Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania itaendelea kutengeneza viwango vya pombe za kienyeji kwa kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza, nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha zoezi la kuwasha umeme kwenye vijiji vilivyosalia katika Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote visivyo na umeme vitafikiwa na huduma ya umeme. Mradi huu unahudumia vijiji 42 vilivyosalia katika Jimbo la Momba ambapo kati ya hivyo vijiji 22 vimekwishawashiwa umeme na vijiji 20 kazi mbalimbali zinaendelea. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2023. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHWALE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaongeza geti lingine ndani ya Jimbo la Momba kutokana na geti la Tunduma kuzidiwa katika kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichwale, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kurahishisha biashara kati ya nchi ya Tanzania na Zambia na kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katika Kituo cha Tunduma, Serikali inaendelea kuchambua na kutathmini taratibu zilizopo ili kuona kama kuna uwezekano wa kuongeza Kituo cha Forodha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuondokana na changamoto ya msongamano wa magari ambapo Januari, 2021 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliingia makubaliano na Mamlaka ya Mapato ya Zambia yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi. Hatua hizo ni pamoja na: -
i. Kuunganisha mfumo wa TANCIS wa TRA na mfumo wa ASCUDA World wa Zambia ili kuiwezesha Idara ya Forodha Zambia kupata taarifa za shehena ya mzigo husika kabla kuwasili mpakani; na
ii. Serikali ya Zambia kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara na eneo la kuegesha magari kupitia ufadhili wa Trademark East Africa (TMEA).
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na makubaliano hayo, Serikali kwa upande wa Tanzania imefanya yafuatayo: -
i. Uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Forodha ambacho kimesaidia taasisi zote za Serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka; na
ii. Serikali kupitia ufadhili wa TMEA imenunua scanners tatu ambazo ni baggage scanner, body scanner na cargo scanner. Aidha, baggage scanner na body scanner zinafanya kazi na cargo scanner inatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Julai, 2022, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuweka Kituo cha Forodha Kakozi Momba ili kuunga mkono jitihada za kujenga Soko la Mazao la Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ina utaratibu wa kupitia na kufanya tathmini ya sehemu zote ambazo zinaweza kujengwa ofisi kwa ajili ya ukusanyaji kodi. Utaratibu huu unazingatia uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa pindi ofisi hizo zitakapofunguliwa kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwenendo wa kukua kwa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kakozi Momba na mipaka mbalimbali hapa nchini. Aidha, maeneo yatakayokidhi vigezo vya kujengwa ofisi za forodha kulingana na tathmini hiyo, taratibu za uanzishwaji wa ofisi hizo zitaanza kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali watu na fedha. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Momba lina jumla ya Vijiji 72 ambapo mpaka sasa vijiji 30 vinapata huduma ya Majisafi na Salama kupitia miradi ya maji ya bomba. Katika kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma ya maji, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi ya Maji katika vijiji 12 vya Muungano, Ipata, Ntinga, Chindi, Makamba, Naming’ongo, Yala, Isanga, Kalungu, Lwatwe, Samag’ombe na Kakozi kwa gharama ya shilingi bilioni 9.45. Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeanza kazi ya utafiti wa maji chini ardhini na uchimbaji wa visima virefu katika vijiji 16 vya Mkutano, Nzoka, Chilangwi, Itumba, Miunga, Mfuto, Machimbo, Mpwinje, Njeleke, Isunda, Chafuna, Msungwe, Sante, Siliwiti, Chole na Mtungwa ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 kwa shilingi milioni mia sita. Kukamilika kwa uchimbaji wa visima hivyo kutawezesha usanifu wa miundombinu ya usambazaji, kufanyika katika mwaka wa fedha 2024/2025 na utekelezaji wake kuanza. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -
Je, lini Kimondo cha Ivuna kitarejeshwa nchini na kutumika kama kivutio cha utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa kimondo kilichoanguka Kijiji cha Ivuna, Mkoa wa Songwe mwaka 1938 kikiwa na ujazo wa tani 0.0077 sawa na asilimia 0.0044% ya kimondo cha Mbozi kilichopo katika Kijiji cha Isele Mkoani Songwe chenye tani 16.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Kimondo cha Ivuna kinahifadhiwa kwenye Makumbusho ya Historia ya Asili iliyo katika Mji wa London Nchini Uingereza. Aidha, Wizara kwa kutambua umuhimu wa malikale zilizochukuliwa nchini kabla na baada ya uhuru kwa sababu mbalimbali kikiwemo Kimondo cha Ivuna, imeunda Kamati ya Kitaifa inayoratibu namna bora ya kurudisha au kunufaika na malikale hizo zilizopo nje ya nchi. Kamati inafuatilia taarifa zake ili kuweza kuishauri Serikali njia sahihi za kukirudisha.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaboresha Mpaka kati ya Zambia na Tanzania, ili kudhibiti njia za panya ambazo mazao na bidhaa nyingine hutoroshwa bila kulipiwa kodi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, katika kudhibiti utoroshwaji wa mazao na bidhaa katika mipaka ya Tanzania na Zambia, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA) ziliingia makubaliano yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi. Utekelezaji wa hatua hizo ni pamoja na:-
(i) Mfumo wa Uondoshaji Mizigo wa TANCIS umeunganishwa na Mfumo wa ASYCUDA World wa Zambia, ili kubadilishana taarifa na kurahisisha taratibu za uondoshaji mizigo;
(ii) Serikali imesimika midaki za kukagua mizigo inayobebwa na abiria pamoja na magari;
(iii) Serikali ya Zambia kupanua barabara na eneo la maegesho ya upande wa Nakonde, ili kupunguza msongamano upande wa Tunduma; na
(iv) Kuendelea kubainisha vihatarishi vilivyopo katika magari ya mizigo yanayopita Mpaka wa Tanzania na Zambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja hatua hizo, Serikali kupitia TRA inaendelea kuimarisha doria, kwa ajili ya kudhibiti maeneo yote ya mpaka wa Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kulinda mapato ya Serikali. Ahsante sana.