Primary Questions from Hon. Martha Nehemia Gwau (6 total)
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza:-
Je, ni kiasi gani cha Zebaki kinaingizwa nchini kila Mwaka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019 kiasi cha Zebaki kilichoingizwa nchini kilikuwa ni tani 24.42, ambapo mwaka 2020 kilikuwa ni tani 22.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba zebaki ni kemikali inayotakiwa kudhibitiwa kwasababu ina madhara ya afya ya binadamu kama vile kusababisha upofu, kutetemeka viungo, kupoteza kumbukumbu, kuharibika ngozi, tatizo la ini na figo.
Mheshimiwa Spika, hivyo basi Serikali, kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti uingizaji wa Zebaki kwa kuwasajili wale wanaoingiza Zebaki nchini na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba za kuwahifadhi waliofanyiwa ukatili ikizingatiwa kuwa ukatili kwa watoto na wanawake umeongezeka?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa kuwahifadhi waliofanyiwa ukatili (kujenga nyumba za kuwahifadhi waliofanyiwa ukatili), Serikali imeandaa Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Nyumba Salama wa Mwaka 2019, kwa ajili ya manusura wa vitendo vya ukatili pamoja na wahanga wa biashara haramu wa usafirishaji wa binadamu. Lengo ni kuweka mazingira wezeshi kwa uanzishaji huduma ya nyumba salama kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na kwa watoto hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hadi kufikia June 2023 jumla ya nyumba salama 12 zimeanzishwa na kusajiliwa katika Mikoa ya Arusha, Kigoma, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma hii kwa mujibu wa Mwongozo wa mwaka 2019.
MHE. YAHAYA O. MASSARE K.n.y. MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -
Je, Serikali haioni kuna haja ya watoto wachanga kutumia Bima za Afya za Mama zao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa kukitokea changamoto kwa wazazi wenye bima wanaojifungua watoto wao kushindwa kupata huduma hasa kwenye vituo vya huduma za afya vya sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya alishatoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha watoto wachanga wenye uhitaji wa huduma wanapata huduma za afya bila kikwazo chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuelekeza Watendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na vituo vyote vya huduma za afya nchini kuhakikisha watoto wanapata huduma kwani Mama yupo na kadi yake inayoonesha ushahidi wote kuhusu mtoto husika na ni mtoto wa ngapi kwenye familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaasa wazazi na viongozi wa hospitali husika kukomesha kabisa matukio ya kughushi nyaraka ambayo pia ndiyo yanapelekea kuwepo na usumbufu wakati mwingine. Naomba kuwasilisha.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua usafiri wa Reli kutoka Dodoma kwenda Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) ina mpango wa ufufuaji na ukarabati wa miundombinu ya Reli ya Kati yenye kiwango cha Meter Gauge. Aidha, TRC inaendelea na ukarabati na uboreshaji wa Njia Kuu kutoka Dar es Salaam - Isaka ambapo kwa awamu ya kwanza uboreshaji umefanyika kutoka Dar es Salaam hadi Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa awamu ya pili, Serikali ina mpango wa kuboresha kipande cha Tabora – Isaka ikiwemo kukarabati kipande cha Dodoma – Manyoni kwa maeneo yaliyobaki wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza. Vilevile, Serikali inafanya tathmini ya ukarabati wa njia ya reli ya Manyoni – Singida ili kuimarisha shughuli za kiuchumi kupitia usafiri wa reli kwa kuunganisha ukanda huo.
MHE. MARTHA N. GWAU K.n.y. MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga madaraja kwenye Barabara za Misughaa hadi Kikio na Matongo hadi Mpetu – Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa vivuko na madaraja katika Jimbo la Singida Mashariki. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya shilingi milioni 435 zimetumika katika ujenzi wa madaraja katika Barabara ya Mpetu – Matongo - Misughaa – Msule - Sambaru, Mungaa – Ntuntu - Mang’onyi na Lighwa – Ujaire. Utekelezaji wake umefikia asilimia 90. Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imeweka katika mpango wake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya shilingi bilioni 1.11 kwa ajili ujenzi wa madaraja katika Wilaya ya Ikungi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Barabara za Misughaa - Kikio na Matongo - Mpetu kuna uhitaji wa jumla ya madaraja matatu ambayo ni Daraja la Mto Matongo lenye urefu wa mita 65, Daraja la Mto Isanja lenye urefu wa mita 45 na Daraja la Mto Siuyu lenye urefu wa mita 30. Kutokana na ukubwa wa madaraja haya usanifu wa kina unahitajika kufanywa. TARURA imeanza kutekeleza kazi ya usanifu wa madaraja haya kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi wake.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -
Je, kuna Kampuni ngapi nchini za kutoa taarifa za mikopo (credit reporting company) zinazoangalia hali ya kifedha ya mkopaji na uwezo wake wa kulipa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 imeipa Benki Kuu mamlaka ya kuanzisha na kusimamia kanzidata ya taarifa za wakopaji (credit reference system), kutoa leseni na kusimamia kampuni binafsi za kuchakata taarifa za mikopo.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa, Benki Kuu imetoa leseni kwa kampuni mbili za kuchakata taarifa za mikopo. Kampuni hizo ni Creditinfo Tanzania Limited na Dun & Bradstreet Credit Bureau Tanzania Limited. Ahsante.