Supplementary Questions from Hon. Martha Nehemia Gwau (8 total)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza. Je, ni mamlaka gani hasa inayosimamia uingizaji wa zebaki nchini?
Mheshimiwa Spika, lakini kingine, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kutoa elimu ya madhara ya kemikali hiyo ya zebaki kwa wananchi wanaojihusisha na uchimbaji wa madini, hususan Mkoa wangu wa Singida, Ikungi na Wilaya ya Iramba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la kwanza ni mamlaka gani inayohusika na kusimamia uingizaji wa kemikali hizi nchini:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye swali la msingi, ni Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini ili tuweze kufanikiwa kwenye hili ni suala ambalo linahitaji kushirikisha mamlaka mbalimbali. Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba, kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika zitashirikishwa, ili kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti wa kina.
Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili. Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu suala hilo:-
Mheshimiwa Spika, ni swali zuri, na nafikiri iko tayari na kwa sababu tunahitaji kwakweli kutoa elimu pamoja na kudhibiti kwa maana ya kuwasajili watu kama hao wanaoingiza, lakini vilevile kuna umuhimu wa ufuatiliaji, ili zebaki isiweze kuingia kwa njia za panya. Lakini wakati huohuo kwenda kutoa elimu hasa kwenye maeneo ya madini ambayo wanachimba dhahabu, kwenye makaa ya mawe ambao wanahitaji kutumia zebaki. Wakati huohuo kwenye hospitali zetu ambazo vilevile zenaki inatumika, kuhakikisha kwamba, wakati wa ku-despose hivyo vitu vinakuwa disposed vizuri. Vilevile kuwajulisha wananchi namna nzuri ya kutumia, lakini kununua vifaa ambavyo wakati wachimba madini wanapokuwa wanatumia basi kuwe na mashine na vifaa maalum ambavyo vinasababisha hivyo vitu visiweze kutoka na kuingia kwenye jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri swali lake Serikali iko tayari na nafikiri kwa ajili ya kufanya hatua hiyo fedha zinahitajika.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa katika mikoa 12 iliyotajwa ya hizo nyumba, Mkoa wa Singida siyo miongoni mwa Mikoa iliyo na hiyo huduma. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha nyumba hizo katika Mkoa wa Singida?
Swali la pili, kwa kuwa ukatili kwa watoto bado unaendelea siku hadi siku. Je, Serikali imefikia wapi au ina mpango gani wa kuanzisha Vituo vya Kulelea Watoto (ECD Centers) ili kuhakikisha kwamba wazazi wanakuwa wanawaacha watoto kwenye mikono salama? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nehemia Gwau: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kujenga nyumba salama katika Mkoa wa Singida, ni dhahiri kwamba iko mikoa mingi kweli ambayo haina nyumba salama, hapa ni mitano tu inayo, na wizara inafanya jitihada za kuwasiliana na wadau ambao wamekuja kutusaidia katika mapambano haya ya kutokomeza ukatili. Andiko hilo likipita, tutapeleleka hizi rasilimali katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa ikiwemo huko Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kupitia mwongozo huu, tunaomba mamlaka za Mikoa na Halmashauri na wadau walioko huko waone umuhimu wa kuanza kuanzisha nyumba hizi wakati Wizara inakuja kuongezea nguvu. Vilevile kwenye bajeti zinazokuja; mwaka ujao tutaendelea kutenga fedha kidogo katika ngazi zote kwa ajili ya kuchochea ujenzi wa nyumba Salama hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu maelezi ya Watoto, ni kweli, mpango wa Serikali ni kuhakikisha watoto wanalelewa vizuri kwa kuwajengea vituo vya kuwalea na kuwakuza katika maeneo ya jamii. Sasa tuna vituo 200 tumeshirikiana na wadau kuvijenga. Formular ni ile ile, tunahamasisha wadau waliopo kwenye Halmashauri zetu waendelee kujitokeza na kuchangia fedha kwa ajili ya vituo hivi, lakini kwenye bajeti zetu tutatenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi sasa Wizarani tuna kikao kinaendelea cha resource mobilization. Hivyo, tukiipata, tutaanza kuwapelekea wale ambao wameshamiliki na wameanza huku tukiwaelimisha wengine ambao bado hawajaona umuhimu huo, kuamka na kujipanga kwenye bajeti za mwaka unaokuja, ahsante.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Mkoa wa Singida ni jirani kabisa na Mkoa wa Dodoma ambao ndiyo Makao Makuu ya nchi: Je, ni lini Kiwanja cha Ndege Singida kitakamilika ili wananchi wa Singida wapate huduma; lakini pia uwanja huo wa Singida utumike kama uwanja wa dharura kama Dodoma kuna changamoto? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Singida ni mkoa ambao uko karibu na Dodoma na Serikali tayari imeshafanya usanifu wa Uwanja wa Singida ili uweze kujengwa, kwani unaweza ukatumika sana pale ambapo kunatokea changamoto katika viwanja vya Mkoa wa Dodoma, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi kwa kunisaidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya usanifu kukamilika, hatua inayofuata sasa ni kujua mahitaji halisi kwa ajili ya fidia ili hatimaye tuweze kuanza kufanyia kazi huo uwanja. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza: Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa SGR, ambao ni wananchi wa Halmashauri ya Itigi na wananchi wa Halmashauri ya Manyoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Ni lini Serikali italipa Service Levy kutokana na ujenzi wa reli ya SGR kwa hizi Halmashauri ambazo zimepitiwa na reli hii; Halmashauri ya Itigi na Halmashauri ya Manyoni? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia malipo hayo, nataka nimjulishe kwamba mfumo wa utoaji wa ardhi katika eneo hilo umekuwa ukienda sambamba na kulipa fidia. Maeneo ambayo hayajalipwa fidia kwa sasa ni yale maeneo ambayo tuna uchimbaji wa malighafi ya ujenzi ikiwa ni pamoja na Tambukareli, Centre pamoja na Milembela. Maeneo hayo yataendelea kulipwa kulingana na hatua za uthamini zitakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na Service Levy kwa Halmashauri zote mbili kwa maana ya Itigi pamoja na hiyo nyingine ya Manyoni, tulifanya vikao mwaka jana, 2021 kati ya TRC pamoja na Halmashauri zote mbili, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake baada ya kukubaliana ikaonekana kwamba pengine inatakiwa waanze kulipwa shilingi 1,500,000,000 kwa kila Halmashauri moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza, tayari wameshalipwa shilingi 214,000,000 kila mmoja na malipo mengine yataendelea kufanyika kulingana na jinsi tutakavyokuwa tumechimba zile material. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Wilaya ya Manyoni imeshatenga eneo la ujenzi wa chuo cha VETA katika Halmashauri ya Manyoni.
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa chuo hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi kwamba ni sera ya Serikali kujenga chuo katika kila wilaya ikiwemo na Wilaya ya Manyoni. Na kwa vile katika mwaka ujao wa fedha tuna zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 36 basi Wilaya ya Manyoni tutaipa kipaumbele. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Bajeti ya TARURA katika Wilaya ya Ikungi ni ndogo na kwa kuwa muunganiko wa eneo na eneo umekuwa ni changamoto kwa haya madaraja. Je, ni upi mpango wa Serikali katika kujenga madaraja haya ili kuunganisha vijiji, kata pamoja na wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Mtaturu kashawasilisha bajeti ya Madaraja matano ambayo ni Matongo – Mpetu, Misughaa – Ntutu, Misughaa – Kikio, Kimbwi na Lighwa na kwa umuhimu wake na udharura wake na kwa sababu bajeti tayari ipo mezani, tunataka kujua, je, ni lini Serikali itafanya uharaka wa kujenga hayo madaraja ili kuunganisha vijiji na kata hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tukiwasiliana na Mheshimiwa Mtaturu mara kwa mara akinieleza changamoto hizi za miundombinu kwenye jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijibu swali lake la kwanza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba inajenga na inaboresha miundombinu katika maeneo yote nchi nzima. Barabara hizi za wilaya zina jumla ya urefu wa kilometa 144,429 na ni mtandao mkubwa ambao unahitaji bajeti kubwa. Mpaka muda huu tayari Mheshimiwa Rais amehakikisha Bajeti ya TARURA inaongezeka kutoka bajeti ya awali ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 275 mpaka sasa tunavyoongea bajeti ya TARURA ni shilingi bilioni 710.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pale inapotokea dharura, Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki kwa wananchi, kwa maana ya barabara hizi zenye umuhimu na ambazo zinahitajika kujengwa ili ziunganishe kijiji na kijiji na kata na kata. Nimhakikishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanyia kazi ujenzi wa madaraja na miundombinu yote ambayo ni muhimu kwa ajili ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusu madaraja matatu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema bajeti ya dharura imeongezwa kutoka shilingi bilioni 21.2 mpaka sasa imefika shilingi bilioni 52.6, yote hii ni kwa sababu Serikali inataka pale inapotokea dharura, basi inapeleka fedha kwa ajili kushughulikia udharura huo.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nataka kujua ni lini Mradi wa Maji wa Kintinku, Lusilile, katika Wilaya ya Manyoni ambao unahudumia vijiji 11 utakamilika ili wanawake wa Tarafa ya Kintinku wapate huduma ya maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni maelekezo ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba, miradi yote ambayo imekwama kwa muda mrefu inafanyika na kukamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anaendelea kupambana kuhusu mradi huu aendelee kutupatia ushirikiano ili sisi tuweze kutimiza majukumu yetu na kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata maji. Ahsante sana.
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa taarifa za wakopaji ni muhimu kwa financial institutions zote. Je, na hizi microfinance ndogo ndogo nazo zinapeleka taarifa za wakopaji BOT?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ili kuepuka default rate kwa financial institution zetu. Je, BOT wana-update hizo taarifa kwenye credit reference kwa muda gani; kwa wiki au kwa mwezi kwa sababu tunajua wakopaji wanakopa kila siku, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, taasisi zote za fedha kubwa na ndogo zinatakiwa zipeleke taarifa sahihi kwenye kanzidata inayosimamiwa na BOT.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kila baada ya mwezi taarifa hizo zinapokelewa na kusambazwa kwa taasisi zinazohusika. Ahsante.