Primary Questions from Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato (4 total)
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa vibali kwa Vyuo Vikuu vyenye upungufu wa Wahadhiri ili viweze kuajiri Wahadhiri wapya?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa Wahadhiri katika Vyuo Vikuu vya Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekua ikitoa vibali vya ajira kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2018/ 2019 hadi 2020/2021, Serikali ilitoa vibali vya nafasi za ajira mpya za Wakufunzi na Wahadhiri Wasaidizi 333 katika Vyuo Vikuu vya Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Wahadhiri Vyuoni, Wizara yangu inaendelea na jitihada za kuomba vibali vya ajira za Wahadhiri kutoka Wizara yenye dhamana na Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Sambamba na hilo, pia upo utaratibu wa kuwahamisha watumishi wenye sifa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kwenda Vyuo Vikuu na kuwajengea uwezo ikiwa ni pamoja na kuwasomesha kozi za muda mfupi na mrefu. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawalipa Wahadhiri wote nchini malimbikizo yao ya miaka ya nyuma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali hulipa malimbikizo ya watumishi wote wa Serikali wakiwemo Wahadhiri baada ya kujaza fomu za malimbikizo (arrears clearance forms). Mara baada ya mtumishi kukamilisha kujaza fomu hizo na kuwasilishwa, madai yao hupelekwa Ofisi ya Rais, Management ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na baadaye Hazina kwa ajili ya malipo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Septemba, 2022, Serikali imelipa jumla ya Sh.1,172,429,710 kwa ajili ya malimbikizo ya Wahadhiri. Serikali itaendelea kulipa malimbikizo ya Wahadhiri kulingana na bajeti ya fedha kwa mwezi na mwaka husika.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabweni kwenye shule za wasichana wanaosoma masomo ya sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika shule za bweni. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali imetoa Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa shule 10 maalumu za sekondari za wasichana za masomo ya sayansi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita. Ujenzi huu ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule 26 ambazo kila Mkoa utajengewa shule moja kupitia mradi wa SEQUIP.
Mheshimiwa Spika, mradi huo unahusisha ujenzi wa mabweni tisa katika kila shule na kila bweni litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 120. Aidha, kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Sekta ya Elimu, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati mabweni ili kuongeza nafasi zaidi za wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Sita.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka kipaumbele cha ujenzi wa mabweni kwa shule za kidato cha tano na sita na kwa wanafunzi wote wa kike na wakiume, kwa kuwa wanafunzi wote wana changamoto.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza miundombinu ya Vyuo Vikuu nchini kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) itajenga Chuo Kikuu kipya cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Butiama chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 5,620. Vilevile Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa wa Lindi kitakachokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 360, Kampasi mpya ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili wanafunzi 11,000, Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo cha Mizengo Pinda Mkoa wa Katavi wanafunzi 2,500, Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya Kampasi ya Rukwa wanafunzi 3,000. Vilevile, mradi wa HEET utafanya ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika Mikoa ya pembezoni ikiwemo Mikoa ya Kagera, Tanga, Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Ruvuma, Manyara na Singida.
Mheshimiwa Spika, mradi huo kwa ujumla unatarajia kuboresha Taasisi za Elimu ya Juu 19 kwa kujenga Hosteli 34 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 9,042, vyumba vya mihadhara 130 vitakavyokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 27,254, maabara na karakana zitakazokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 7,850, kumbi za mikutano ya Kisayansi 23, miundombinu ya mashambani pamoja na Vituo Atamizi 10. Nakushukuru sana.