Answers to Primary Questions by Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana (3 total)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Je, lini Serikali italeta Bungeni sheria mahsusi kwa ajili ya kuwalinda wananchi dhidi ya ukatili wa kijinsia?
WAZIRI KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunazo sheria zinazowalinda wananchi dhidi ya ukatili wa kijinsia ambazo ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16; Sheria ya Ndoa, Sura ya 29; Sheria ya Mtoto, Sura ya 13; Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sura ya 443; na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Sura ya 432. Kwa pamoja sheria hizo zina vifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia. Sheria zote kwa pamoja zina vifungu vinavyoshugulika na makosa ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta ikiwemo Wizara ya Maendeleo, Jinsia, Watoto na Makundi Maalum, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na wadau mbalimbali tunaendelea na uchambuzi ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahsusi ya ukatili wa kijinsia au tuboreshe sheria zilizopo. Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo Serikali itachukua hatua stahiki.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-
Je, lini Serikali itakarabati au kujenga Mahakama mpya ya Wilaya ya Ukerewe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mahakama inaendelea na utekelezaji wa mpango wa kujenga na kukarabati majengo katika ngazi mbalimbali. Aidha, katika ngazi ya Mahakama za Wilaya, bado tuna Wilaya ambazo hatuna majengo na hivyo, kulazimika kutumia majengo ya kuazima kwenye taasisi nyingine kama Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe kwa sasa inafanya kazi kwenye majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Hata hivyo, katika mpango wetu wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, tumepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe katika mwaka wa fedha 2024/2025. Naomba nitumie fursa hii kuishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kutupatia kiwanja kwa ajili ya kujenga jengo hilo.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkalama utaanza?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Mkalama, kama ifuatayo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na kukarabati majengo chakavu. Wilaya ya Mkalama ni moja ya Wilaya nne ambazo kwa sasa bado huduma za Mahakama zinapatikana kupitia wilaya za jirani. Aidha, kutokana na uhaba wa majengo ya Mahakama, majengo haya yanajengwa na kukarabatiwa kwa awamu kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mpango wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkalama unatarajiwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwa sasa tayari maandalizi ya michoro hiyo yamekamilika na zabuni imetangazwa ili kupata mkandarasi wa ujenzi. Hivyo, ujenzi huo kimsingi unatarajiwa kuanza kabla ya mwezi Juni, 2024.