Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana (4 total)

MHE.DKT. PINDI H. CHANA Aliuliza:-

Serikali imekuwa ikisaidia sana vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nchini kupitia Halmashauri za Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mifuko hiyo ili kutoa viwango vikubwa zaidi vya mikopo?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato kutokana na vyanzo vya ndani vya halmashauri inatolewa na halmashauri zote nchini kutokana na fedha zilizokusanywa na halmashauri kwa kipindi husika baada ya kutoa vyanzo lindwa kama vile fedha za uchangiaji wa Huduma za Afya, ada za taka na ada za Shule za Sekondari Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha kiwango cha mikopo inayotolewa na halmashauri Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzisimamia halmashauri kutekeleza Sheria ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, kuzijengea uwezo Kamati za Huduma za Mikopo za Kata na Halmashauri ili ziwe na ujuzi wa kutosha wa kuanzisha na kuendeleza vikundi vya wajasiriamali pamoja na ujuzi wa kusimamia utoaji na urejeshwaji wa mikopo, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanufaika wa mikopo kabla ya utoaji wa mikopo kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuzielekeza halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza:-

Je, Serikali imejipanga vipi kutafuta Soko la uhakika la zao la mahindi kwa wakulima wa Mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo inatekeleza mikakati mbalimbali ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Viwanda na Biashara katika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo kuwaunganisha wakulima wa mahindi na wasindikaji wa mahindi kwa ajili ya unga na chakula cha mifugo, kuondoa vikwazo na kupunguza gharama za biashara na kupunguza ukiritimba na kuanza kutoa vibali vya kuuza mazao nje bila ya kuwa- charge. Vilevile, Wizara ipo katika hatua za awali kuhakikisha kwamba inaanzisha Idara ya Masoko na sekta binafsi; Serikali kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Mazao mchanganyiko na Serikali kufanya makubaliano ya kibiashara baina ya Tanzania na nchi zenye fursa ya masoko zikiwemo nchi za DRC, Kenya, Sudan ya Kusini, Rwanda, Burundi na kutumia njia mbadala kuhakikisha wasafirishaji wanapata huduma za usafirishaji ikiwemo vibali kiurahisi. Pia Mkoa wa Njombe kuunganishwa na wanunuzi ikiwemo Kampuni ya Silverland ambayo katika msimu wa 2020/2021 imenunua jumla ya wastani wa tani 40,000 za mahindi.

Mheshimiwa Spika, kupitia jitihada hizo, kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Desemba 2020 wakulima na wafanyabiashara wameuza tani 89,725 za mahindi nchini Kenya, Burundi na DRC. Bodi ya Mazao na Nafaka Mchanganyiko imenunua jumla ya tani 24,000 za mahindi kutoka kwa wakulima. Pia, kufikia mwezi Mei, 2020, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) amenunua jumla ya tani 73,000 za mahindi zenye thamani ya shilingi bilioni 48 kutoka kwa wakulima na vikundi mbalimbali kwenye kanda zote nane. Kati ya hizo, jumla ya tani 11,000 za mahindi zimenunuliwa kutoka Kanda ya Makambako inayojumuisha Mkoa wa Njombe ambao ulizalisha tani 332,000 za mahindi katika mwaka wa 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2021, Wizara inaangalia uwezekano wa kuwa na maghala katika nchi zenye masoko makubwa ya mazao ikiwemo nchi za DRC na South Sudan kwa lengo la kuhifadhi na kutangaza mazao ya kilimo na hivyo kuyauza kwa urahisi katika nchi hizo.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Jengo la Utawala la Central Police Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jengo la ofisi zinazotumika kwa sasa kama jengo la polisi la utawala (Central Police) Mkoa wa Njombe lipo katika hifadhi ya barabara kuu iendayo Mkoa wa Ruvuma. Kwa sasa Jeshi la Polisi limeshaomba eneo toka Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa ajili ya kujenga ofisi za utawala na makazi ya askari na Halmashauri imeshatoa hekari 40 eneo la Lunyunyu.

Mheshimiwa Spika, tathmini kwa ajili ya kulipa fidia wananchi walioko eneo hilo imeshafanyika kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe na kiasi cha shilingi 322,000,000 zinahitajika kwa ajili ya malipo ya fidia na kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia hii ili ujenzi uanze mara moja. Nakushukuru.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaunganisha Wakulima wa Mikoa ya Kusini hususan Mkoa wa Njombe na Wawekezaji wa nje na ndani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuwaunganisha wakulima na wawekezaji wa ndani na nje ili kuwa na mfumo endelevu unaowapa fursa ya wote kuwepo na kwa faida ya pande zote mbili. Katika kutekeleza mpango huo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa inaratibu makubaliano kati ya wanunuzi/wasindikaji na wakulima kupitia kilimo cha Mkataba kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa teknolojia, pembejeo pamoja na masoko.

Mheshimiwa Spika, kupitia ushoroba wa maendeleo wa SAGCOT, Wizara imehamasisha wawakezaji Tanzania Agrofood Ltd & Olivado Ltd katika Mikoa ya Njombe na Iringa ambao wameunganishwa na wakulima wadogo na kuwezesha kuongezeka kwa mauzo wa mazao mbalimbali mfano parachichi. Mauzo yameongezeka kutoka tani 3,696 mwaka 2015 hadi tani 7,190 mwaka 2019.

Aidha, bei parachichi pia imeongezeka kutoka shilingi 1,200,000 kwa tani mwaka 2015 hadi shilingi 1,800,000 kwa tani mwaka 2020. Uwepo wa kampuni hizo zinazowahakikishia wakulima soko imekuwa ni chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia program ya Agri-connect inayotekelezwa kwa uratibu wa Wizara ya Kilimo moja ya nguzo zake ni kuunganisha wakulima na wewekezaji katika mnyororo wa thamani. Programu hiyo katika Mikoa ya Kusini ukiwemo Mkoa wa Njombe ambapo mazao ya kipaumbele ni mazao ya bustani, chai na kahawa. Programu hiyo inalenga kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na ya nje.