Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana (9 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Hili suala la wastaafu kwa kweli ni kero kubwa katika nchi yetu. Nashukuru majibu ya Serikali, lakini niseme tu Serikali inatakiwa kujitahidi kwenye jambo hili, kwa sababu wastaafu waliomaliza ku-document document zao ambao wapo kwenye maeneo, wanaolia, wanaokwenda kwenye maofisi, wana miezi sita, miaka tano, miaka minne, ni wengi kuliko ilivyo kawaida.

Kwa hiyo, Serikali itafute mfuko thabiti wa kuzingatia mambo haya ili watu waweze kupata fedha zao. Watu wanakufa wanadai fedha, kwa nini mtu ameitumikia nchi, halafu anakufa anadai fedha.

Mheshimiwa Spika, naiomba tu Serikali itengeneze jambo hili liwe nzuri zaidi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu, Serikali ya Awamu ya Sita na hasa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma baada ya kuingia na kugundua kwamba wakati mwingine ucheleweshaji wa mafao hayo ya wastaafu yanatokana na haya malimbikizo ya michango. Michango mingi ambayo inatakiwa ipelekwe na waajiri, imekuwa ikicheleweshwa kupelekwa kwa mazingira ya aina moja ama nyingine. Serikali imekuja na suluhu hiyo ya kutengeneza mfumo ambao utawasaidia wafanyakazi wote kutambua ni lini wanastaafu na haki zao zikoje?

Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha sasa na upande wa pili wa mifuko, tumewaagiza na wameshatekeleza. Kwa mfano, Mfuko wa PSSSF wameshatengeneza mfumo ambao unaitwa PSSSF Kiganjani. Mfumo huo sasa umeshasambazwa na unaendelea kusambazwa kwa wanachama wote. Wanachama ambao wanakaribia kustaafu, wamekuwa sasa wakiwezeshwa kuzitambua haki zao kupitia kwenye mfumo na kuanza kuwasiliana na ofisi zote kabla ya muda kustaafu ili kupunguza hiyo kadhia ambayo imekuwa ikiendelea.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo tumewahagiza Mfuko wa PSSSF na mifuko mingine, kabla ya muda wa kustaafu, wastaafu wote watarajiwa tumeanzisha sasa vikao maalumu mfuko kukutana na wastaafu watarajiwa kuwatambua na kuandaa mafao yao mapema na hivyo kadiri tunavyokwenda kadhia hii itakuja kuondoka na tunapenda wastaafu waweze kupata mafao yao kwa muda unaotakiwa. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anajibu, amesema moja ya changamoto ya kuchelewa kulipwa kwa wastaafu ni pamoja na waajiri kuchelewa kupeleka michango. Wakati jana nimeomba mwongozo, nimepokea message 165, wengine hawajalipwa kuanzia mwaka 2012; lakini kwenye Bunge la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliji-commit kwamba atafanya ziara kwenye vyombo vyote vya habari kuhakikisha wanapeleka michango ili Waandishi wa Habari na watu wengine binafsi walipwe kwa wakati. Sasa nataka niulize, ni lini ataanza hiyo ziara ili Waandishi wa Habari michango yao ipelekwe ili na wenyewe wawe na uhakika, baada ya kumaliza kazi zao wapate stahiki zao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, masuala haya ya haki ya wafanyakazi ni masuala yanayotakiwa kuangaliwa kwa utaratibu mzuri sana. Masuala haya hayafanani tu labda na maamuzi ya mtu, kuamua kukaa hapa, ukae na nani na ufanye nini? Hapana, ni lazima kuyatengenezea utaratibu madhubuti.

Mheshimiwa Spika, naomba kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tumeshaanza hiyo kazi. Kazi ya kwanza tuliyoifanya ni kupata ushirikiano kutoka kwa Waandishi wa Habari, kutambua vyombo ambavyo vimekithiri kwa kutokulipa mishahara na mafao ya Waandishi wa Habari. Kazi hiyo, tumeshaitekeleza na baada ya hapo sasa ndipo tutakwenda kuanza ziara ya kukutana na vyombo hivyo. Huwezi kuanza tu kukutana nao kabla hujapata taarifa.

Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge Serikali inafanya kwa utaratibu, inatengeneza mikakati kusudi utaratibu huo ukianza kuchukuliwa hatua, hatua hizo ziwe zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nina swali moja tu la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile makosa haya ya ukatili wa kijinsia sasa yanaendana na makosa ya kuporomoka kwa maadili.

Je, Serikali haioni haja ya kuboresha sheria hii iliyopo sasa ili kuchanganya tiba ya makosa haya yanayotokana na kuporomoka kwa maadili? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nijibu swali la nyongeza kuwa Serikali inaona haja ya kuboresha sheria hizi, hivi sasa tupo katika mchakato wa kupitia taarifa maalum ya masuala ya maadili.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka katika Bunge hili tulizungumza sana kuhusu masuala ya maadili, masuala ya mahusiano ya jinsia moja. Nimeshaunda timu maalum pale Wizarani na wanaandaa taarifa kuona namna gani sheria hizi tuendelee kuziboresha. Kwa hiyo, haja ya kuboresha ipo na ndiyo jukumu la msingi la Bunge. Kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kazi ya Bunge ni kurekebisha sheria, kwa hiyo, suala la kuangalia kama ipo haja au haipo kwa kweli, nichukue nafasi hii kusema tu kwamba, hilo ndilo jukumu la msingi kabisa la Wizara yangu na tunaendelea kuangalia namna gani tuendelee kuziboresha sheria zetu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Karagwe imeathirika sana na ukatili wa kubakwa watoto kuanzia miaka mitatu mpaka nane, wakati huu ambapo sheria haijatungwa, hatua zipi za haraka zitachukuliwa ili kunusuru kizazi hiki?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, si kwamba sheria haijatungwa, ni kwamba sheria tunazo mbalimbali za masuala ya ukatili, lakini swali la msingi lilitaka sheria zote hizi za masuala ya ukatili wa kijinsia ziwe kwenye sheria hii moja. Sheria ya Mtoto inaelezea masuala ya ukatili kwa mtoto, Sheria ya Ndoa inaelezea ukatili ndani ya masuala ya ndoa. Pia tunayo Sheria ya Kanuni ya Adhabu, huko nyuma tulikuwa na Sheria ya Masuala ya Kujamiiana na yale yote makosa ya kujamiiana (Sexual Offence Act.) tukaingiza kwenye Penal Code. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, sheria tunazo na kifungu 131 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinaelezea vizuri kabisa masuala ya ukatili.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwamba, yako maeneo kuna ukatili wa watoto. Nichukue nafasi hii kusema tu kwamba, maeneo yote ambako kuna ukatili wa watoto kwanza tunaomba taarifa zifike katika vituo vyetu vya Polisi na vituo vyote vya haki jinai. Tunayo sheria hata ya kumlinda mtoa taarifa, tunaita Whistleblowers Act. Kwa hiyo, Sheria hii ya Penal Code hivi sasa ipo na kwa kweli, inakidhi haja pale ambapo mtoto amefanyiwa ukatili tena chini ya miaka kumi, sheria inaeleza wazi kabisa ni kifungo cha maisha.

Mheshimiwa Spika, hoja ilikuwa ni kuzichanganya sheria zote ziwepo kwenye sheria hii moja. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa na kumpongeza kwamba, kujali watoto ni suala la msingi sana, lakini pia sheria zilizopo kwa kweli kwa sasa zinakidhi haja ya makosa haya ya ukatili wa kijinsia. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza niipongeze Serikali kupitia Wizara kwa kutupatia pesa za kujenga Mahakama ya Mwanzo Ilangara, ujenzi unaendelea, lakini kwa mpango vilevile wa kutupatia pesa kwa ajili ya kujenga Mahakama kwa mwaka huu, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, kiwanja kilichopatikana kiko mbali na maeneo wanayoishi wananchi na kuna eneo ambalo linatumika sasa linalomilikiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na yuko tayari kulitoa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Wizara iko tayari kujadiliana na kukaa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili eneo hili lenye ukubwa wa mira za mraba zaidi ya 3,300 liweze kutumika kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo? Nashukuru.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, eneo ambalo tunakwenda kujenga hii Mahakama ya Ukerewe lipo Airport, Kata ya Mkirizya, na tayari tathmini imeshafanyika na wananchi wamekwishafidiwa kwa ajili ya ujenzi. Sasa suala analolisema Mheshimiwa kwamba, kuna kiwanja kingine tuone namna gani ya ku-shift na huku tumeshalipa fidia kwa wananchi tayari kwa ujenzi, inaweza ikawa ni changamoto.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba nilichukue tulifanyie kazi kama tunaweza ku-shift, maana kule wananchi wameshafidiwa tayari kwa kujenga, sasa ku-shift mahali pengine inawezekana kukawa na masuala ya gharama na kadhalika, ikawa changamoto, lakini hata hivyo naomba nilichukue.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali yanayotia moyo, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Wananchi wa Mkalama wamepoteza sana haki zao kwa kuamua kuachana na kesi kwa kukosa uwezo wa kwenda wilaya ya jirani kupata haki yao; na kwa kuwa bajeti yetu ni cash budget; je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha kwamba mgao wa kwanza tu wa bajeti hii unakwenda Mkalama kuondoa tatizo hili ambalo limewasumbua sana wananchi wa Mkalama? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kimsingi Serikali iko makini na ujenzi wa Mahakama hii ya Mkalama. Hivi sasa kupitia Mkurugenzi tumeshalipa fidia, eneo lile kulikuwa na makaburi ikabidi kulipa fidia na kumwelekeza Mkurugenzi ahamishe makaburi. Kwa hiyo, tayari masuala ya compensation (fidia) yamekamilika na Serikali inatambua kabisa umuhimu wa huduma za mahakama kwa wananchi wetu (utawala wa sheria).

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba tangu Wilaya Mpya ya Mkalama imeanza, huduma zilikuwa bado zinatolewa kwenye Wilaya jirani ya Iramba tangu mwaka 2012. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari michoro imekamilika na kabla ya Juni, katika bajeti hii ambayo tunayo, tunatarajia kuanza hii kazi. Kama ulivyosema, mara pesa itakapopatikana, basi tuweke kipaumbele. Hilo tutalihakikisha tunalizingatia.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kwamba Wilaya ya Kishapu itajengewa Mahakama ya Wilaya; ni lini ujenzi huo utaanza katika Wilaya ya Kishapu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi Mahakama ya Wilaya ya Kishapu ni miongoni mwa zile Mahakama ambazo ziko katika mpango mkakati wa kujengwa mwaka 2024/2025. Tunaishukuru sana Kamati ya Katiba na Sheria imepitisha pesa na hatua ya Mahakama ya Kishapu na yenyewe ipo katika maandalizi ya mchoro na Maandalizi hayo yameshakamilika na mzabuni ameshatangazwa ili kupata mkandarasi wa ujenzi.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali ilionesha kwamba inaenda kujenga Mahakama yenye hadhi ya kiwilaya katika Wilaya ya Tarime. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi tunazo Mahakama za Mwanzo takribani 72 ambazo tuna mpango mkakati wa kuzijenga. Pia, tunazo Mahakama za Wilaya takribani 42 ambazo na zenyewe zipo katika mkakati, ikiwemo na Mahakama ya Tarime. Kwa hiyo, nimhakikishie, kutokana na characteristics za Tarime, pale lazima Mahakama iwepo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kadiri fedha itakavyopatikana Tarime ni miongoni mwa vipaumbele vyetu. Kwa hiyo, Tarime ni lazima ipewe Mahakama haraka sana. (Kicheko/Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nakushukuru sana wewe na Bunge zima kwa jinsi mlivyonichukulia na mlivyonipenda na mlivyonihifadhi mpaka leo Mshua nimeingia ndani ya Bunge lako. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, majengo ya Mahakama yapo ya kutosha tunashukuru, lakini kuna wananchi wengi bado wanapata shida na usumbufu kufuatilia kesi zao ambazo zinapigwa danadana kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itatengeneza hotline au kitengo maalum kwa watu wanaopata shida, wanaofuatilia kesi zao indefinitely kesi ndogo ndogo kama za upangaji, mtu kapanga nyumba halafu hataki kuhama, wala hataki kulipa? Lini Serikali itawasaidia wananchi hawa kuondoa kero yao hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, wanasema a.k.a Mshua. Suala la kuwa na hotline kama alivyosema ni jambo la muhimu, na tayari Mahakama ina hotline. Wale ambao wanadhani kesi zao zimecheleweshwa, wanaweza kupiga simu na kuweza kujua taarifa zao.

Mheshimiwa Spika, wakati unatembelea Mahakama walikuonesha hiyo namba ambayo wananchi wanaweza kupiga kuulizia kuhusu kesi. Kwa hiyo, tayari kama anavyosema, hotline tunayo. Pia Mahakama hivi sasa tumepunguza backlog hadi kufikia asilimia nne. Tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, ameteua Majaji. Hivi sasa Majaji wameongezeka na Mahakama zetu zimejitahidi kutekeleza kesi kwa haraka sana kwa sababu hivi sasa tunatumia teknolojia (e-Case Management) ili kuhakikisha kesi haziendi muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la Mheshimiwa ni la msingi na hivi sasa tuna-fast track kesi zisichukue muda mrefu. Tukichukulia Mahakama za Mwanzo huwa hazizidi miezi sita. Ndani ya miezi sita Mahakama za Mwanzo nyingi wanakuwa wameshamaliza shauri, inabaki zile ambazo zinaenda kwa appeal, Mahakama za Wilaya au Mahakama Kuu na Mahakama za Rufaa. Kwa hiyo, mkakati wa kupunguza backlog unaendelea.