Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Issa Jumanne Mtemvu (33 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hii hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema lolote na mimi kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mungu sana kwa kunipa nafasi hii. Pili, nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipitisha mimi kuwa mgombea na kunisaidia kushinda kwa kura nyingi sana. Pia nisiache kuwashukuru sana sehemu kubwa ya familia yangu, mke wangu na wanangu kunivumilia katika kipindi cha uchaguzi ambacho kilikuwa kigumu sana. Kwa sababu ya muda niendelee moja kwa moja na nijielekeze katika maeneo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na vipaumbele kadhaa karibu vitano lakini kimoja cha kuimarisha utawala bora wa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma, rushwa na wizi niseme machache hapo. Ni kweli Mheshimiwa Rais amefanya makubwa katika kipindi chake cha Awamu ya Kwanza ya miaka mitano. Tumeona wametumbuliwa watu wengi, tumeona watumishi wazembe ambao wamewajibishwa, taarifa inatuambia takriban watu au watumishi 32,555 walichukuliwa hatua mbalimbali. Pamoja na haya, Mheshimiwa Rais katika ukurasa wa tisa nikinukuu amesema ataboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli katika kipindi cha miaka mitano, watumishi wa umma hawajakaa katika hali nzuri, ukweli hawajaona mishahara lakini hii yote ilikuwa inatokana na jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais alikuwa ana kazi kubwa ya kuona jinsi gani uchumi na hali ya Kitanzania katika mapato inapanda. Tuemona uchumi umepanda takribani kwa asilimia saba kila mwaka. Tumeona Pato la Taifa limepanda kutoka trilioni 94 hadi 139. Tumeona ameweza kudhibiti mfumuko wa bei. Sasa kwa yote haya ninaona kabisa hili ambalo Mheshimiwa Rais anataka kwenda kulitekeleza katika kipindi kijacho kinaenda kuwa bora kwa watumishi wote.

Mheshimiwa Spika, niseme pia juu ya hili la kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Pamoja na mambo mengine lakini liko jambo hili asilimia 10 kutoka mapato ghafi ya Manispaa zetu. Wengi wamesema katika eneo hili, lakini mimi ninaliona pamoja wametamkwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa asilimia 4:4:2; lakini naona kundi la vijana kuanzia miaka 35 na wazee wamesahaulika kabisa. Hao ni kuanzia umri kama wa kwangu na kuendelea. Akinamama kuanzia umri wa ujana hadi wanazeeka wanawezeshwa katika asilimia hizi 10. Inajionesha wazi katika sura za usoni wazee au vijana wanaokuja kuwa wazee watakuja kukosa nguvu za kiuchumi na hali mbaya itakuja kwa wakati huo. Hilo niliona likae hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niseme juu ya fedha hizi zinazotolewa hasa katika kundi la vijana. Sasa tunawapa asilimia nne zao lakini hatuwaoni wanaenda kufanya biashara maeneo gani. Wale vijana wanaowawakilisha wamesema vizuri, lakini mimi nataka kusema katika Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya ya Ubungo hususan katika majimbo haya mawili tumeona upanuzi wa barabara wa njia nane kutoka Kimara mpaka Mlandizi takribani shilingi bilioni 140, Mheshimiwa Magufuli amezielekeza katika ujenzi wa barabara ile na tunatambua hizi fedha ni za ndani. Ni kweli upanuzi huu umetupa taabu sana kwa ajili ya vijana wengi na wafanyabiashara machinga pembeni mwa barabara, leo wanalia sana kuanzia Kimara, Temboni, Stopover, Mbezi yote hata pale Kibamba CCM.

Mheshimiwa Spika, niombe sasa Mheshimiwa Waziri alieleza vizuri. Wakati tunajenga vile vituo vya daladala, vituo vya mabasi basi tutumie sehemu fulani tuanze kuwapunguza hawa wajasiriamali wakiwa wamepata mabanda mazuri kama lile banda pale Mvomero ambalo Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo wakajengewa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nijielekeze kwenye eneo moja la elimu kwa haraka. Wengi wamesema lakini hasa nipongeze sana, lile la King’ong’o ni la kwanza, lakini sasa tayari taarifa inasema yatafanyika mazuri lakini zaidi kutokana na muda niache tu nitajielekeza katika mpango unaokuja niseme vyema juu ya maji na miundombinu yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nitumie nafasi hii kukushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Awali ya yote nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wawili, lakini vilevile na wataalam. Pia nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kweli kwa jinsi ambavyo unatuendesha ndani ya Bunge hili ugeni wangu huu mpaka nafarijika. Kwa muda mchache umenipa nafasi mara nyingi na wananchi wangu wanayaona haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika maeneo machache sana; eneo la kwanza ni eneo la mabonde na mafuriko katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hili ni tatizo sana, hivi pia sasa hivi tunazungumza ni nyakati za mvua kule wananchi wanalia sana. Niliwahi kusema kidogo kwenye eneo hili, lakini niseme tu kwamba mabonde sasa haya, kwanza niipongeze Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu pia, imefanya vizuri sana kwenye eneo la Mto Msimbazi, lakini pia hata kwenye Mto Jide pale ndani ya Wilaya yetu ya Ubungo ndani ya Jimbo la Rafiki yangu kaka yangu Proresa Kitila Alexander Mkumbo upande wa Ubungo, lakini bado tumebakiwa na Mto Mbezi. Naiomba sana Serikali ijielekeze vizuri ili tuone sasa mito hii inapanuka, taasisi zetu zinaondoka sasa na mafuriko. Sasa hivi tayari Shule ya Msingi Msigani pale inaondoka, Shule ya Msingi Matosa inaondoka, kwa hiyo na nyumba nyingi za wakazi wetu zinakwenda. Hivyo ni lazima, kwa sababu dhima yetu mojawapo ni kukuza uchumi pamoja na maendeleo ya watu. Kama watu hawaishi vizuri hawana maisha bora, nyumba bora maana yake tunaweza tukashindwa kwenda kwenye mpango wetu ule wa tatu ambao tumetoka kuujadili siku si nyingi.

Mheshimiwa Spika, miradi ya maboresho ya miji; Waheshimiwa Wabunge wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamezungumza juu ya DMDP II, Dar es Salaam Metropolitan Development Programme II. Ya kwanza ilifanya vizuri sana, tumeona Dar es Salaam inang’aa kwa mataa mengi, Dar es Salaam inang’aa kwa barabara nzuri nyingi. Niseme ukweli Hayati alivyopita tarehe 24 ndani ya Dar es Salaam katika ziara yake alipita pale Jimboni Kibamba na nilipata bahati ya kusema kidogo, katika matatu niliyosema ukweli aliyakubali yote.

Nilisema kitakwimu ndani ya mzunguko wa barabara zinazozidi zaidi ya kilomita 350 ni kilomita tano tu ndiyo zenye lami katika Jimbo la Kibamba. Hii si sawa na ukweli Waheshimiwa Wabunge wengi hasa zaidi ya 40 na Manaibu Waziri na Mawaziri zaidi ya 10 wanaishi kwenye hili Jimbo. Naomba kabisa mnisaidie ndugu zangu Jimbo limekaa kwenye hali mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe na Waheshimiwa Wabunge wamesema huu mradi wa DMDP II naomba utoke huko uliko kama umesimama ili uje utuokoe. Wakati tunaomba kura za Mheshimiwa Rais aliyepo sasa hivi akiwa anagombea kama Makamu wa Rais, lakini na Waheshimiwa Wabunge tulionyeshwa mtandao wa barabara kilomita 107 za ndani ambazo chini ya TARURA kupitia DMDP II na wananchi wakafurahi, wakaona sasa ile hali ambayo ilikuwa inawasababisha wajifungue barabarani kwa sababu ya njia nyingi kuwa za tope, sasa wanaenda kuishi katika maisha yaliyo bora.

Mheshimiwa Spika, niombe sana, huu mradi kwetu ni muhimu sana ndiyo utaenda kuwaokoa wana Dar es Salaam, lakini mpaka sasa tumeshamaliza bajeti yetu ya TARURA katika ngazi ya Mkoa na niliona takriban kilomita 60 zimewekwa pale, nikaanza kufurahi sana, lakini sijui kama kweli kutakuwa na sintofahamu, niombe sana kama patakuwa na nafasi ya Mheshimiwa Waziri kwenye hili, kama anaweza kuligusia kidogo ili tuweze kuona kama kweli hii DMDP II inakuja Dar es Salaam au haiji.

Mheshimiwa Spika, natamani pia niseme kidogo juu ya madeni ya muda mrefu na hasa kwa watumishi wa umma. Profesa wa Moshi Vijijini, mzee wangu alisema vizuri asubuhi, nikasema ananinyang’anya ninalotaka kusema lakini akaelekea upande mwingine kidogo. Niseme kwamba, tunayo shida kwenye hili eneo, mpaka sasa kwa ripoti ya CAG anatuambia zaidi ya bilioni 190 ndiyo deni ambalo lipo mpaka sasa kama madeni ya watumishi; hapo wapo Walimu pamoja na watumishi wengine.

Mheshimiwa Spika, bilioni 190 si nyingi sana, najua kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 tulikuwa na deni au na madeni karibu bilioni 207. Utaona zimepungua kwa bilioni 16, hii niipongeze sana sana Wizara ya Kisekta kwamba imefanya jambo jema, imepunguza bilioni 16 katika mwaka mmoja, kwa hiyo si jambo dogo, wamefanya vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo lakini bado kuna kazi ya kufanya. Asubuhi Profesa alishauri kidogo, anasema tunaweza tukaachaacha barabara kule na nini na ni kweli ndiyo ushauri. Sitaki kuelekea kwenye ushauri wa CAG amesema nini, lakini niwashauri tu, tunajielekeza sana, tunayo miradi mikubwa sana ya mabilioni ya namba na ni mizuri kweli na naipongeza ile miradi yote. Hata hivyo, hebu tutafiti jinsi ya mkakati mzuri wa kuondoa hili deni la bilioni 190, tukiamua kweli tunaenda kuzilipa zote.

Mheshimiwa Spika, hizi bilioni 190 ukiwalipa Walimu na watumishi wa umma, maana yake umepeleka hela mtaani. Ukizilipa bilioni 190, maana yake ile hali ambayo tunaitaka sisi sasa ya kukuza uchumi na kuinua maisha ya watu, kweli yanaenda kuwagonga watu. Hii ndiyo dhamira ya Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, unamwona anataka sasa kuzileta hela mifukoni kwa watu, yaani uchumi wa fedha uende kwenye mifuko ya watu na ndiyo maana ameelekeza hata madeni mengine ya wazabuni na kadhalika yalipwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana ukiona inafaa hili jambo liende na niseme mpaka sasa tunatenga bilioni sita za kulipa madeni, hazitoshi na bilioni nne ndiyo za ndani (own source), lakini bilioni nne ni za maendeleo, hazitoshi tukapunguze katika baadhi ya vifungu katika mafungu mengine huko, tutoe kwenye posho tulete hapa ili hawa watumishi wa umma waweze kulipwa hizi bilioni 190, sioni kama ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kidogo juu ya Dar es Salaam kuhusu mradi huu wa DART, wa mabasi yaendayo kasi, yuko Mbunge mmoja siyo wa Dar es Salaam lakini nimefurahi sana, wanasimama Wabunge wengine na wenyewe wanaisemea Dar es Salaam, ndiyo maana nafurahi uwepo wa Wabunge wengi wanaoishi Dar es Salaam. Kweli ule mradi ni mzuri na najua unaendelea, lakini hata wewe umewahi kusema, miradi hii inayoendelea miundombinu ni ya kwetu Serikali, hebu tuone jinsi gani huduma hizi zitolewe kwa ushindani. Leo tunayo miundombinu mizuri, tumetoka awamu ya kwanza tunaendelea awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu, lakini ukweli mabasi hayatoshi, wananchi wa Dar es Salaam leo wanateseka kwa nini tumezuia mabasi yale ya vituo vya basi kwenda Mjini Kariakoo. Tumezuia tukisema tunaweza kuwamudu wote waingie kwenye mabasi ya mwendo kasi, haiwezekani! Kwa nini tusiseme ya kijani ni ya Serikali, wengine waje na mekundu, wengine waje na ya njano ili tukashindane kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi niombe sana, leo hii barabara imekuwa ni mateso kwa hata wanaochangia kodi yenyewe. Leo kuna wagonjwa wanapata rufaa kutoka Mloganzila wanaenda Muhimbili, lakini unaambiwa hata yale magari ambayo ni ambulance hayawezi kupita kwenye barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni kilio kikubwa kweli, kwa hiyo mgonjwa ambaye sehemu yake ya kodi ndiyo inajenga barabara ile, leo na yeye ili awahi maisha yake apate uhai, inawezekana asipite ile barabara na akafa kabla hajafika kwenye hospitali nyingine! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ninasema si kwa kubahatisha, ndani ya jimbo langu Hospitali ya Mlonganzila iko hapo, na nilipata bahati kuwatembelea Mwezi Januari, na moja ya kikao changu na menejimenti ya pale hiki kilikuwa kilio chao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe kwa jinsi ambavyo utakapoona inafaa tupate maelekezo mazuri, siyo sisi viongozi tupite mule wala siyo wengine, haya magari kwa ajili ya usalama wa maisha ya watanzania waishio Dar es Salama wapite kwenye njia ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi kwa siku ya leo niliona niyaseme hayo ya mabonde, mafuriko, DMDP ll, eneo la madeni ya Watumishi wa Umma na hili la ushauri na maombi juu ya barabara yetu ya DARTS, baada ya kusema hivyo nakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa barua ya tarehe 18.12.2018 kufanya marekebisho ya mpaka kati ya Wilaya ya Ubungo na Wilaya ya Kisarawe. Kazi ilianza tarehe 10.01.2019; walipitia GN Na. 41 ya tarehe 15.02.1974 na ramani yake Na. E1/341/254 iliyosajiliwa kwa Na. 43075 inayoonesha Hospitali ya Mloganzila.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa maelekezo umefanyika kikamilifu, aidha, mapendekezo na ushauri umetolewa ipasavyo. Taarifa hii imewasilishwa kwenye ofisi za Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya kutoa GN mpya na mpaka sasa bado utekelezaji haujafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri ukifika kwenye majumuisho uweze kutuambia juu ya hitimisho ya suala hili ili wananchi wa maeneo haya waweze kupata huduma zinazostahili kwa mamlaka sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika hotuba au bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kama waliotangulia nami nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan na nampongeza wazi kabisa ndani ya sakafu ya moyo wangu kwa sababu ya kazi kubwa anayoifanya, hasa ni katika kutekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022. Pamoja na mambo mengine makubwa ya ulinzi na usalama, lakini kiujumla miradi ya kielelezo ameitekeleza vile ambavyo Watanzania hawakutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mingi Watanzania wanatakiwa waijue ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa SGR ilikuwa takribani asilimia sabini na kitu sasa hivi ni asilimia 95.3 inakwenda vizuri hasa katika vipande vya mwanzo kuanzia Dar es Salaam - Morogoro lakini hata Morogoro – Makutupora hiyo imeenda kwa kiwango kikubwa, lakini mikataba mingi imeendelea katika vipande vilivyobakia.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu JK Nyerere Megawatt 2,115, nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, tumekwenda kule na tumejiridhisha kabisa kazi inakwenda vizuri kama Mheshimiwa Msukuma asubuhi alivyoeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo miradi mingine ujenzi wa bomba la mafuta ghafi, kutoka Hoima Uganda hadi Chongeleani Tanga, tunaambiwa kazi inakwenda vizuri na tumeona ameisaini mikataba ya mwisho.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwisho kabisa ujenzi wa madaraja makubwa na barabara, hii hata kule Dar es Salaam wananchi wa Dar es Salaam wanajua kwamba lipo daraja zuri lile la Tanzanite pale Palm Beach ambalo limekamilika na limeshazinduliwa, lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo aliianza akiwa Makamu wa Rais akaipokea vizuri na sasa ameenda nayo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili hivi eneo la TARURA, lakini vilevile na eneo la ardhi na hasa katika ukurasa wa 142. Upande wa TARURA tunashukuru sana katika kipindi kilichopita tumeona hapa TARURA ilikuwa ina changamoto kubwa na tumelia sana humu ndani mpaka tukaenda kwenye tozo, tukaweka tozo kwenye mafuta ya petrol na diesel ili tuongeze zaidi ya bilioni 396 kwenda kwenye TARURA, zitusaidie kwenye majimbo yetu na Mheshimiwa Rais aliongeza zaidi ya milioni 500 hadi bilioni moja, wengine bilioni moja na nusu kuweza kwenda kwenye majimbo na tumeona kazi nzuri ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni tofauti sana na Dar es Salaam, Dar es Salaam kule tunalia sana na hasa kwenye Wilaya ya Ubungo. Hii Wilaya ipo pembezoni na imesahaulika kwa muda mrefu sana. Barabara kule hakuna kabisa ni vumbi, ni mchanga, vumbi na udongo. Tumelia mara nyingi viongozi wakubwa wakija tunasema lakini ukweli kama nchi inao mpango mzuri wa mradi mzuri ambao tumekuwa tukiambiwa, sisi wawakilishi na wananchi wenyewe mradi wa DMDP III, Dar es Salaam Metropolitan Development Program III. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ya kwanza imekuja tumesema hapa Bungeni, hata mwaka jana nilisema kwenye Bunge la Bajeti. Program ile imesaidia Buza, Kijichi, Sinza na maeneo mengine kuna mataa mazuri kule hadi kule Mburahati. Ya pili imeenda kwenye Mto Msimbazi, nami nafurahi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Hii ya tatu tumeambiwa inakuja lakini hatuioni ikija. Bunge lililopita nilisema hapa, Waziri akisimama atuambie inakuja au haiji, lakini hakuna majibu. Sasa hivi tunaambiwa kuna mtaalam mmoja kakaa nayo zaidi ya miezi mitatu au minne kusaini tu ili tuweze kuona, barabara zaidi ya kilometa 107 za vumbi ambazo wananchi walikuwa wanaamini tukipata ile wananchi wa Jimbo la Kibamba na Ubungo wanaenda kufurahi. Tunaomba sana sana kwenye majumuisho tuambiwe DMDP III ipo wapi inakuja au haiji kwenye bajeti inayokuja.

Mheshimiwa Spika, lipo jambo hapa limezungumzwa kwenye ukurasa wa 42; Ujenzi wa Barabara ya Njia Nane Kimara – Kibaha nilisema juzi kwenye swali langu la msingi tunafurahi sana tunaambiwa zaidi ya asilimia 86 sasa hivi zimekamilika zaidi tu palikuwa na ongezeko la kimkataba kwenye zile kilometa 19.2 Kimara - Kibaha lakini kuna shida. Jambo hili lilitekelezeka kisheria; niliuliza hapa sheria gani ilitumika kuwaondoa wananchi wa pembezoni pale kwenye barabara ya njia nane na kuwavunjia bila fidia? Leo ni kilio kikubwa sana tulijibiwa hapa sheria iliyotumika ni ya mwaka 1932, yaani mwaka 1932 baba yangu Marehemu Mzee Mtemvu kaondoka, babu yangu kaondoka, Alhaji Zuberi Mwinyishee Manga Mtemvu kaondoka, hakuna hapa ambaye aliwahi kuwepo. Bunge hili ndiyo linatunga sheria, leo tunaishi na sheria ya mwaka 1932 kweli? Sheria ya 1932 ndiyo inavunja makazi ya watu?

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe, mwaka 1974/1975 palikuwa na operation vijiji ambayo ilikuwa ina lengo la kuondoa watu ndani ndani kuwaleta pembezoni mwa barabara ambao walijengewa shule, hospitali na kadhalika na kadhalika na vile vile hizi huduma maana yake ilikuwepo ni rasmi, lakini zipo sheria nyingine ambazo zilikuwa zinatumika. Kuna Sheria ya Mipango Miji, kuna Land Act ya mwaka 1999 Na.5, zote hizi zilikuja na kuondoa sheria nyingine zilizopita. Hata mwaka 1989 hati ya Kiluvya ilitolewa na Mheshimiwa Hayati Kawawa aliipokea mwaka 1989, Kijiji cha Kiluvya, sasa na yenyewe pia ilikuwa ni ya uongo. Hii inaleta sintofahamu tunaomba sana tufahamu jambo hili ili wananchi kama kweli walikuwa wana haki na haijafanyika, basi haki yao iende na zaidi ya hili hata palikuwa na kesi… (Makofi)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe mchangiaji Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, pacha wangu kwamba, hili suala la fidia hata wananchi wa Ubungo Kisiwani ambao wanatakiwa wapishe Mradi wa DART wanatakiwa walipwe fidia, lakini hatma yake haijulikani mpaka leo.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naipokea tena ukitegemea ni taarifa ya Profesa ambaye si muda mrefu anaenda kuingia kwenye kilio kingine cha bomoa bomoa kutokea Ubungo hadi pale Kimara walipoanzia kwangu. Pole sana nafikiri sasa utakimbizana na hilo ili lisiwafikie wananchi wako.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jambo la ardhi, katika ukurasa wa 42 wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna muda wengine tunalia juu ya changamoto, changamoto ni kujenga jenga barabara zenye mabonde mabonde na kadhalika na mashimo shimo ya mvua, lakini kuna wakati mwingine ni lazima kama nchi tulilie juu ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Rais alienda kuzindua nyumba za Magomeni Quarter, jambo zuri, nakumbuka zamani nikiwa Diwani pale ndiyo tulianza ule mchakato wa kuvunja vile vijumba na tukaja na malengo yale au mawazo mapana au maono mapana mwaka 2012. Miaka 10 baadaye tunaona Mheshimiwa Rais anaenda kuzindua nyumba maghorofa pale ambapo wananchi na Watanzania wameona, ni leo lazima tuwe na sura hiyo. Leo tuna Tandale kongwe kabisa, leo tuna Magomeni, tuna Manzese lazima tufikie tukajenge majengo ya aina ile.

Mheshimiwa Spika, hili kwenye nchi kadhaa limeshafanyika Misri kule na nchi nyingine, ni jambo jepesi tu, waende kuingia makubaliano na wananchi ambao wanamiliki hati zile katika vile vijumba vyao, wanawapa floor ya chini na floor ya kwanza, floor ya tatu hadi ya kumi wanachukua kama nchi ambayo kimsingi…

MHE. TARIMBA GULAM ABBAS: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni lazima haya yote tunaweza kuyafanya…

T A A R I F A

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Mtemvu kwamba yaliyowafika kwake Kibamba pamoja na Ubungo, yaliwafika wananchi wa Jimbo la Kinondoni mwaka 2015, wamebomolewa wananchi wa Magomeni, wananchi wa Hananasif jumla nyumba 94, lakini mpaka leo haijulikani, hivyo kilio chao na sisi Jimbo la Kinondoni tunacho.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nilinde na ni ukweli.

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja hii ya makazi ambayo nilikuwa naendelea kuizungumza ni lazima tuzingatie Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ambao moja ya malengo yake karibu manne, mojawapo ni kuchochea maendeleo ya watu. Unachocheaje maendeleo ya watu wakiwa maskini, wakiwa wanakaa katika makazi ambayo si bora. Kwa hiyo, naliona hili wenzetu vizuri ni lazima wazingatie kwamba sasa tukaboreshe kama Magomeni tulivyoona twendeni Tandale, Manzese na maeneo mengine ya Magomeni ili tuweze kuukuza mji.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Mtemvu anahoja nzuri sana ya uendelezi wa haya makazi, kwa mfano katika majiji yetu yote Mbeya, Arusha, Mwanza na baadhi ya miji ukiangalia kwa kweli makazi yapo holela holela. Kwa hiyo ana hoja nzuri nai- cement kwa Taifa ili serikali iweze kuichukua.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru itabidi nimalizie hapa hapa tu, lakini haya yote haya wenzetu wamewahi kusema kuna Karl Max aliwahi kueleza vizuri juu ya relationship between population growth and economic development. Kwa hiyo, tuweze kuona, lakini hata Mao Zedong, baba wa China alisema country is greatest wealth is its people tutumie idadi ya watu zaidi ya milioni sita ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kuweza kuongeza mapato na kuweza kuongeza mchango katika pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja iliyo mbele yetu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii iliyowasillishwa na Mheshimiwa Waziri ya Fungu 56 pamoja na Taasisi zake.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kwa haraka kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais nami natambua Dada yangu huyu ana uwezo mkubwa na anafanya kazi vizuri sana. Pamoja na timu yake nzima ya Naibu Mawaziri wawili pia kwa Wataalam Kaka yangu Adolph Ndunguru na Wasaidizi wako au Naibu Makatibu wote watatu.

Mheshimiwa Spika, kwa haraka na kwa kipekee sana nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli wananchi wa Wilaya ya Ubungo, wananchi wa Jimbo la Kibamba tuna kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Wengi wamesema hapa nitakuwa mchoyo wa fadhila hizi za kushukuru kama sitasema dakika moja kwenye muda wangu wa kuchangia.

Mheshimiwa Spika, tumeona mambo mengi sana ndani ya Jimbo la Kibamba, ndani ya kipindi chake kidogo tu tayari ametujengea shule Nne za sekondari, ikiwepo shule maalum ambayo kaleta Bilioni Tatu imejenga shule maalumu ya Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Sita ya Wasichana hili ni jambo kubwa sana. Pia juzi tu tayari siku ya Jumatatu inawezekana tukazindua uanzishaji wa ujenzi wa Chuo cha VETA kule pembezoni kabisa ndani ya Jimbo la Kibamba - Kata ya kibamba, jambo kubwa. Mengine mazuri mengi sana tunaendelea kumsemea Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hotuba iliyowasilishwa hapa nitajielekeza katika maeneo mawili hivi kama muda utaniruhusu, nilikuwa nina zaidi hata ya mambo mawili.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni hili la asilimia 10 limesemwa na wengi. Jambo hili limenihuzunisha sana na limenihuzunisha kwa sababu ya kuona machozi ya Mheshimiwa Rais kwenye nia njema ambayo kama Taifa tulitamani kuona ile ajenda ya kuwainua wananchi wetu kiuchumi inafikiwa, lakini zimetoka fedha, na nikuambie kwa 2022/2023 zilitengwa bilioni 75 kwa ajili ya eneo hili na hizo ni sehemu tu ya fedha za ndani za miradi ya maendeleo karibu bilioni 394 zikasogea kidogo katika eneo hilo la asilimia 10, bilioni 75 kwa nchi nzima, lakini tunaambiwa na CAG katika mwaka huo tu uliokaguliwa 2021/2022 almost bilioni 88.8. maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, maana yake hata zile tunazotengwa za mwaka mzima kwa nchi nzima zinapigwa zote. Ndiyo tafsiri tu ya kihesabu! Kama 2022/2023 tumetenga bilioni 75 lakini 2021/2022 tumetoka kukaguliwa zimepigwa bilioni 88, maana yake asilimia 100 tuliyotengewa imepigwa, hii ni hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, liko jambo hapa kwenye hili, kupigwa tumezoea lakini kuna changamoto kwenye hili. Tunaambiwa vipo vikundi vingine hata havipo, vina fedha nyingi tu. Mimi ninashauri katika eneo hili, kubwa limesemwa na Kamati tumesikia, patakuwa hakuna mahusiano mazuri kati ya Wasimamizi Madiwani lakini na CMT katika maeneo mengi ambayo ukiangalia na analysis imejionesha kwenye Halmashauri nyingi tu ambazo zimeangaliwa au CAG kaziona Tatu zimeaharibu sana.

Mheshimiwa Spika, katika ya milioni 200 karibu milioni 774 ambazo fedha zilitolewa milioni 774 wakajigawia watu wenyewe, miongoni mwa wanakikundi nje ya miradi iliyozingatiwa. Tafsiri yake nini? Unaona Wilaya ya Ubungo ninayotokea mimi milioni 218 zaidi ya asilimia 40, yaani tumeziiba eti! (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nawaona Halmashauri ya Makambako na Geita wanaenda zaidi ya Milioni 172 Makambako, Halmashauri ya Geita Milioni 112, ni nyingi! NI nini hapa nataka kusema? Kanuni zetu na Mheshimiwa Waziri ulizoziweka kwenye kusimamia hii, nikukumbushe tu tunaongozwa na Kanuni ya 24 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya mwaka 2019, tumekubaliana adhabu maana wanaoiba lazima adhabu ziwepo intact, faini ni kati ya shilingi laki mbili na milioni moja au kifungo kati ya miezi 12 na 24.

Mheshimiwa Spika, hebu ona watu wamepiga Milioni 700 unaenda kumwambia adhabu yake ni kukulipa kati ya Laki Mbili na Milioni Moja tumekuwa wapi? Hii ni changamoto kweli! Au Kifungo cha kati ya miezi 12 na 24 mojawapo, lakini wangapi wamefungwa? Mpaka leo hatuoni. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakuamini sana kwenye hili, tuendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais nia yake ya kuona watu wanachukuliwa hatua haraka wachukuliwe hatua haraka na sheria zinakuongoza tu, hata kabla hatujakaa mwezi wa Nane na wa Kumi na Moja kwa maana ya Taarifa ya CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili, utakumbuka sana mara nyingi huwa nachangia sana Wizara ya Afya na mwaka huu nimeomba lakini sidhani kama nitafanikiwa kuichangia, eneo lenyewe leo nimelijua ni la nani. Mheshimiwa Waziri kazungumzia juu ya K tatu, Kupima, Kupanga na Kurasimisha ardhi, kumbe ni jukumu la msingi la Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ubungo Jimbo la Kibamba tunalia hapa kila siku, tumefeli kabisa kwenye jambo la urasimishaji, mara nyingi nimechangia hapa nakuonyesha zaidi ya bilioni tatu zimepotea Mheshimiwa Waziri anashuka mara kwa mara Wilayani lakini tumefanikisha mimi na yeye kukubaliana dhamana ya kwake kama Msimamizi wa Sera ni kutoa Hati, lakini jukumu la Kupima, Kupanga na Kuthaminisha ni jukumu hili ambalo lipo chini ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Bilioni zetu Tatu na zaidi zilishapotea, nimeomba hata Waziri Mkuu aingilie kuzitafuta hizi hela hamna.

Mheshimiwa Spika, nimeshangaa hotuba ya Mheshimiwa Waziri naikuta najua hili janga kalikuta, kuna Bilioni 49.9 kazitamka yeye zimeenda kwenye Halmashauri huko kama revolving kwa jukumu la KKK, na yeye anasema kwenye ripoti amefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 90 ya jambo hilo, lakini CAG sasa wakati anamkabidhi Mheshimiwa Rais anazungumza bilioni 29.9 zaidi ya asilimia 59.6 zimepigwa hazijarudishwa mpaka sasa, eneo hilo hilo katika Bilioni 50 zimetoka, nyuma yake tulitoa Bilioni 46 zaidi ya asilimia 50 hela zinapotea.

Mheshimiwa Spika, ni lazima wenyewe tujionee huruma, wananchi kule Kibamba wametoa wenyewe zaidi ya Bilioni Tatu za kwao, Halmashauri nyingine zinapewa na hela hazirudi, tujitahidi kwenda na Kibamba zile hela wale waliopima kupanga au wameshatoa hela zao laki mbili hadi laki tatu tuone jinsi gani ya kuwasaidia wapate hati zao badala ya kuendelea kuwatesa. Niliona hilo niliweke katika sura hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu na la mwisho ni jambo la TARURA limesemwa na waliotangulia. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, wakati wa reference ya mwaka 2020/2021 tulikuta TARURA inapokea takribani Bilioni 250 hivi, lakini kwa kuingia ule mwaka wa 2021/2022 Mheshimiwa Rais kwa kufikiria kwa kina sana akaona hela haitoshi, Wabunge tukalia hapa akaingiza Shilingi Mia Moja ya tozo ya mafuta ya diesel, petrol na mafuta ya taa ikatuongezea tukafika Bilioni 700. Kwa hiyo, unaweza kumuona Mheshimiwa Rais alituvusha na tukiona kwenye Halmashauri zetu, tumeona kwenye Majimbo yetu mambo mazuri yamefanyika. Kuanzia 2022/2023 ongezeko kutoka pale ni dogo sana lakini hata leo anatamka tena Mheshimiwa Waziri kiasi kilichoongezwa TARURA bado hatuioni ile nia tena ileile iliyoanza, madhara yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, mimi na wewe ni mashahidi hata kule kwenye Jimbo lako la Mbeya, population inaongezeka kwa mujibu wa statistics iliyotolewa sasa hivi ya mwaka 2020, vilevile maombi mengi ya barabara za vumbi kuelekea TARURA ni makubwa sana lakini na mtandao wa barabara wa muda mrefu ni 144,000 lakini za vumbi ni zaidi ya kilomita 130,000 hivi, maana yake hali ni mbaya sana! Nini kinaweza kikafanyika?

Mheshimiwa Spika, tukitaka kujenga barabara zote na akili kubwa tukaipeleka kwa wananchi ambao ndiyo tunawawakilisha, maana yake tukapeleke angalau kwa kilomita 130, 000 zilizobaki hazijawahi kushughulikiwa Milioni 500 tukajenga lami, maana yake unaweza ukaenda ukatafuta Trilioni 65 unazitoa wapi, kama kuanzia leo hatuna nia njema ya kupeleka hela nyingi kama alivyofanya Rais mwaka 2022/2023 kwenda kuogeza zaidi ya bilioni 500 pale kupitia shilingi 100 ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nia yangu ni kuona kama Taifa tunapeleka nia njema ya kujenga barabara za vumbi na changarawe zikawe za lami ili maendeleo haya yaende kwa kasi sana, kuliko yale ambayo tunayaona ni ya kimkakati, miradi ya vielelezo ni vizuri lakini wananchi wa pale Kibamba kule ndani ambao hawawezi hata kupata huduma ya afya kwa sababu ya vumbi na udongo, anashindwa kuweza kuelewa ataenda saa ngapi kwenye reli ataenda saa ngapi kwenye maeneo yenye ndege ataenda saa ngapi kwenye maeneo mengine, kwa hiyo tufungamanishe miradi ya kielelezo na miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, nafikiri nimetendea haki siku uliyonipa na kwa kutumia nafasi hii niunge mkono hoja iliyopo mbele yetu. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa mchana huu nianze kuchangia kwenye Wizara hii, Fungu 67; lakini kabla nitoe pongezi sana kwa hotuba nzuri iliyowasilishwa na kaka yangu Simbachawene. Najua ni kwa msaada mzuri wa mdogo wangu Ridhiwani Kikwete, na ninatambua bila shaka watendaji kwenye Wizara hii ya Ofisi ya Rais Utumishi wako vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu najua ni kumi nimeziweka hapa ili yale ambayo ninayoweza kujaliwa kuyatimiza. Kabla, hii dakika moja lazima niseme vizuri juu ya kazi kubwa ambayo inafanywa na Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kila mmoja anayesimama hapa anajaribu kueleza ni jinsi gani Mheshimiwa Rais anafanya kazi, hatuwezi kumaliza kwa dakika moja. Nakumbuka, na ninawasilisha leo; wananchi wangu wa Jimbo la Kibamba, yupo mzee mmoja mstaafu wiki moja iliyopita aliniandikia barua, akaniambia naomba peleka wazo langu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama anafanya kazi kubwa, ndiye Rais wetu wa kwanza mwanamke, kwa nini tusifikie sarafu yetu ya nchi ikabeba sura ya Mama Samia Suluhu Hassan? Najua tuliwekeana utaratibu na marais wetu huyu ni wa sita, marais wawili tu ndio wanaoonekana, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi. Tufikie maamuzi Rais wetu wa kwanza mwanamke kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naye aingie kwenye sarafu ya fedha zetu, haya si maneno yangu ni maneno ya wananchi wangu toka jimbo la Kibamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia maeneo mawili mpaka matatu muda ukiniruhusu kwa haraka. Eneo la kwanza ni eneo ambalo linahusu utumishi kwa ujumla wake lakini katika idara nataka nizungumze kidogo idara ya uhasibu pamoja na fedha. Kumekuwa na changamoto sana, na nimewahi kuuliza swali la msingi hapa kama mwaka na nusu uliopita juu ya idara hii. Inaonekana idara ya fedha na uhasibu ndicho kiini cha hati safi na hati chafu. Wakuu wa ofisi, kwa maana ya accounting officers wanapopata hati safi wanasifiwa lakini inapopatikana chafu hawa ndio wanaoshikwa; hawa wahasibu na wakaguzi wa fedha walioandaa hesabu, lakini kuna jambo huku ambalo ndilo linasababisha ambalo leo likieleweka tena inawezekana ikalisaidia Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idara hii mara nyingi katika sekritarieti za mikoa na wizara zetu na hizi tunaita idara zinazojitegemea, zote hizi zina wahasibu wakuu; lakini pia kuna vitengo. Sasa wakuu wa vitengo wana changamoto sana. Kwanza wanakuwa hawawi involved vizuri kwenye menejimenti, hilo la kwanza; lakini la pili hawa wote wanakuwa ni ma chief accountants. Ukiwa na tofauti na wakuu wa idara, kwa mfano idara ya rasilimali watu, tuna wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu lakini ziada wana wasaidizi, mkurugenzi utawala, mkurugenzi rasilimali watu, wamegawanyika wawili, wasaidizi hao, lakini unaenda mipango, Mkurugenzi wa Mipango ana wasaidizi, mkurugenzi upande fulani, mkurugenzi upande fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokwenda kwa uhasibu unakuta mhasibu mkuu peke yake; anahangaika na mambo ya malipo, kama payment anahangaika na mambo ya revenue kama mapato, ni jambo gumu na kubwa sana. Mkumbuke tulikotoka tulikuwa tunatumia manual hata kwenye kufunga hesabu, lakini leo unapofunga hesabu Tanzania ndivyo wanavyofunga hesabu Marekani na Uingereza, kwa standard moja. Sasa kwa nini tunaona kazi zao hizi ni ndogo? Kwa hiyo ni vizuri tupandishe hadhi kwenye hizi ziwe idara, muwape wawe wakurugenzi wa fedha na utawala lakini pia wawe na wakurugenzi wasaidizi upande wa fedha na upande wa utawala. Kwa kufanya hivyo tutapunguza sana na kwa kiwango kikubwa hoja za ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mhasibu mkuu yupo peke yake na anafanya kazi peke yake, niliona hilo niliweke hivyo. Na, hata kama hatutaki kwenda kuibadilisha kuwa idara basi mhasibu mkuu kimuundo awe na wasaidiizi. Kuwe na mhasibu mkuu msaidizi kimuundo kwenye upande mmoja wa mapato na upande mmoja wa matumizi. Ikiwa hivyo tutasaidiwa sana kwenye kufunga hesabu vizuri na kuondoa hoja ya ukaguzi. Niliona hilo niliweke katika sura hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu ajira portal, limesemwa na wengine. Mimi mwanzo nilikuwa na mawazo, tuliko toka zamani ilikuwa kila taasisi accounting officer anaweza kuajiri lakini tukaja kwenye huu mfumo mzuri tukajua utatusaidia. Hata hivyo nje kuna manung’uniko mengi sana juu ya jambo ambalo mimi nilijua garbage inn garbage out; kwamba tunachokiingiza process mle iwe ni fair na nje pia tutakutana na jambo zuri, lakini leo mambo ya hovyo tu bado yanatokea kaka yangu Simbachawene. Tunaitegemea ajira portal lakini ukiichungulia, amesema Engineer Chiwelesa, unaona kabila limesimama pale, unaliona kabisa. Si hivyo tu unaona ukanda, na inatokea kwenye ajira portal tunayoiamini lakini ziada inatokea sura za viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwona Mheshimiwa Simbachawene moja kwa moja kwenye matokeo ya wale wanaoajiriwa, unamwona Mheshimiwa Kikwete moja kwa moja, natolea mifano tu. Hii haiwezi kusaidia. Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wakurugenzi ndio sura ya ajira inayotembea. Mimi sitaki tuondoke kwenye ajira portal bali tui-strengthen. Waheshimiwa Wabunge wengi wametoa ushauri, na mimi ni mmoja wapo, kwamba ikibidi twende kwenye majimbo ili mimi wale wanaonitumia message na kadhalika niwaone. Hata kama wataenda kufanya kazi Mbeya, Sumbawanga lakini hawa wanatokea Wilaya ya Ubungo, hiyo itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa haraka. Nimeona hapa, liko jambo la idara ya kumbukumbu na nyaraka za Taifa, nimesoma nikafurahi sana. Humu ndani wenzetu wanatuambia ni kama mradi na fedha walizozipata wamejaribu kutafuta nyaraka kwa kuhoji familia na watu, walimu, waasisi wetu, wanatamkwa waasisi wawili humu. Anatamkwa mhasisi wetu Karume kwa upande wa Zanzibar na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa ujumla ndio waasisi wetu. Lakini changamoto ya humu maandishi yanaonesha historia zao zimetafutwa hata kabla ya uhuru tangu wanasoma na Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vizazi vya mwisho vya kujua historia ya nchi yetu ni sisi. Tukiondoka sisi wajukuu na watoto wetu hawatajua tena kwenye hili, na ndiyo maana wanaenda kwa kuchoka, watajua watu wawili lakini sio kweli. Uhuru wanchi hii umepatikana na wazee wetu tunawajua. Nakutajia na majukumu yao, Kasela Bantu hakuna mtu asiye mjua. Huyu ndiye mwaka 1954 aliyeshawishi kikao cha TANU kifanyike ili kuanzishwa kutoka Tanganyika African Association TAA, iliyoanzishwa 1929-1954. Kuna Abulwahid Sykes tangu mwaka 1929 alikuwa na TAA hadi 1954. Yeye ndiye aliachia kiti akamwachia Mwalimu Julius Nyerere tangu TAA kuanzishwa hadi TANU. Kuna Alhaj Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu katibu Mkuu wa Kwanza wa TANU, kwa nini tunaacha haya? Vilevile kuna mzee Dothan Azizi, Waheshimiwa Wabunge lazima niwaambie, huyu ndiye aliyetoa land rover yake ikatembea kwa ajili ya kutafuta kura za TANU. Si hivyo tu, pia kuna akina Mzee Rupia, Bibi Titi Mohammed; na juzi nilimfurahia sana Mheshimiwa Mchengerwa, na akina mama mmeanza kukubali na kukumbuka kwamba huyu ndiye mama wa Taifa sasa, lakini walisahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri ukija utuambie, hizi nyaraka zenu juu ya wengine wote ambao walisababisha hao wakafahamika. Mimi nataka niwaambie tu wala si success story kama ndugu yangu Chief Kunambi anavyosema, lakini nikikumbuka sana, Mwalimu Nyerere anatoka Pugu alikaa pale mnaita Aggrey kwenye nyumba ya Mwinshehe Manga Mtemvu, babu huyo, akiwa anakunywa kahawa na kadhalika, kwenda Kariakoo Shimoni. Hii nchi lazima watu hawa wafahamike na kutambulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,lakini mwisho sana kwa umuhimu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Watumishi mmewafurahisha, mmeanzisha PEPMIS na PIPMIS, mifumo miwili; ya watumishi na ya public institutions itawasaidia sasa hivi kuna hali mbaya sana. Mimi huwa sipendi kuongelea kwingine kwenye nchi hii. Wilaya ya Ubungo tunayotokea leo kunawazuia sana watumishi ndiyo maana mmeziona issue za mkaguzi wa nje, mambo ya hovyo sana; lakini maana yake kuna watu wameishi mle muda mrefu. Nendeni mkaangalie muone walio overstay muwatoe, si lazima niwataje majina kama Wabunge wengine wanavyofanya hapa, sihitaji kutaja jina la mtu mle ndani kwenye taasisi mimi ninayoiongoza, Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo. Nendeni mkaone shida iko wapi ili muweze kutusafishia mazingira hayo Mheshimiwa Simbachawene.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja iliyopo mezani, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia fungu 48 - Wizara ya yetu hii ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Kwa nafasi hii naweza kuchangia maeneo kama mawili na nikipata muda zaidi nitakuwa na eneo la tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze hapa ambapo ameishia Mheshimiwa Halima kwenye eneo la mgogoro. Kwanza, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoendelea kuwaaminisha Watanzania kwamba gurudumu linaendelea bila kusimama, wazi kabisa. Nitatoa uthibitisho katika maeneo mengi haya ambayo nitachangia. Pia nawapongeza sana Wizara; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mabula na kaka yangu Mheshimiwa Pinda, pamoja na Katibu Mkuu na timu yake ya watendaji, wananendelea kufanya kazi vizuri sana.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza hapa alivyosimama Mheshimiwa Halima juu ya mgogoro wa kule Dar es Salaam, eneo ambalo linaingiliana katika majimbo mawili. Hili linaitwa Shamba la Malolo (Malolo Farm). Kwenye historia, ni kweli shamba hili lilikuwa linamilikiwa na Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC) kwa hati Na. 30 (163) iliyotolewa Tarehe 01 mwezi wa Nne mwaka 1983 ya miaka 99 na eneo hilo lilikuwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa hekta au ekari 4,743.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza tukubaliane, ni kweli shamba lilikuwa la DDC, hilo lazima tukubali, lakini kwa kupumzika na wakawa wamelala, hili Shirika la Maendeleo Dar es Salaam, wananchi wakaingia. Sasa wananchi hawa ni takribani zaidi ya 70,000. Upande mmoja wa Kinondoni zaidi ya 39,000, maana wengi wapo Kibamba katika maeneo aliyoyasema Tegeta A, Goba maeneo ya Msumi yote, lakini na maeneo ya upande wa Kibesa Mabwepande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa upande mmoja watu wana uelewa kidogo hili jambo lililotembea upande wa Kinondoni. Nitumie nafasi hii sana kumpongeza Mkuu wa Mkoa aliyeondoka, Cyprian Amos Makala na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu yangu Abas Zuberi Mwishehe Mwanga Mtemvu. Nisiache kumpongeza sana Mkuu ya Wilaya ya Kinondoni, wamefanya vikao zaidi ya vitatu juu ya hii sintofahamu. Mheshimiwa Waziri umesema, moja ya njia zako za kutatua migogoro ni viongozi kutembelea maeneo yale. Ulitamka kabisa, na hii ndipo ilipopatikana. Maana Mkuu wa Mkoa alipoenda kutembelea kule, ndiyo akaliona hili jambo na akatoa maelekezo ya vikao vianze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa upande wa Kinondoni kwenye watu 35,000 Mheshimiwa Gwajima angekuwepo angesema, na ndiyo maana nampongeza sana. Amekaa vikao vitatu, wamefikia kwenye solution, kwamba walipe fidia kuanzia shilingi 8,000 wakakatana, shilingi 6,500 wakakatana, wamefikia shilingi 4,000 kwa kiako cha juzi. Hiyo ni hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mimi niseme, kwa sababu engagement haionekani wameingia watu wa Ubungo na wakati fulani niliwahi kumwuliza Mheshimiwa Kheri Denis James, Comrade, Mkuu wangu wa Wilaya akaenda Mbulu. Vipi hili jambo? Akasema anaendelea nalo, lakini nilipofuatilia hakuna vikao vya Ubungo ambavyo vimeingia kwenye ile engagement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana, wamefikia 4,000 sawa, lakini kama mtu namiliki kipande cha square meter 500 akalipwa shilingi 4,000 ni shilingi 2,000,000 kule kuna watu wana nyumba za udongo, anatoa wapi shilingi 2,000,000? Kwa hiyo, mimi kama Mbunge wa upande mmoja mwenye watu wengi, hapo mlipofikia kama Serikali ni jambo zuri, mmeangalia consideration ya wananchi wako pale, lakini shamba hilo, hili ni Shirika la Serikali tu. Kwanini isiwe bure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani kwa nini shilingi 4,000? Anaenda kupewa nani? DDC aliyekaa miaka 40 na kuliacha! Hebu mwende mkaone, engagement ya Wilaya ya Ubungo; na hapa nitumie nafasi hii kumwomba sana Comrade Hashim Abdalla Komba, DC bora kabisa, yaani ni DC sijawahi kuona. DC bora kabisa aingie kwenye jambo hili vizuri, tuweze kuona wananchi wa Jimbo la Kibamba upande wa Tegeta A, Goba, upande wa Msumi nzima na upande wa Kibesa, nusu ya Mabwepande. Kwa hiyo, kwa sisi shilingi 4,000 bado ni kubwa, tupunguze au twende na bure kabisa. Hayo ni maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nafikiri hapo utakuwa umenielewa, kazi mmeinza, mmefanya vizuri. Siyo tu ya kulaumiwa, kweli wananchi waliingilia eneo hilo la ekari 4,700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu urasimishaji. Kila nikisimama hapa, lazima niseme hili, na huwa nasema kidogo kwa ukali, lakini leo nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. Tumekaa vikao vingi Dar es Salaam. Sana. Tumekaa vikao vingi Jimboni, umekuwa ukitafuta jinsi ya kutatua jambo la urasimishaji. Urasimishaji limefeli Dar es Salaam. Kweli, lakini nilisikia sehemu tunazungumza, kama huyu, mpeni mpango mmoja wa miaka 10. Kama umefika mwisho, Desemba mwaka huu wa 2023, twende kwenye masterplan. Nikakwambia, hapana, masterplan ina gharama kubwa na ni ngumu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ile tuliyokuwa ya kuwapatia hati kwa gharama nafuu, tuendelee kuwa nayo. Leo umeniambia kwenye page 59, unao mradi wa uboreshaji wa miliki za ardhi (LTIP), Dola 150,000,000 takribani Shilingi bilioni 345, hongera sana, lakini moja na vipaumbele vyako vingi vya kujenga maofisi na kadhalika, namba moja ni kutatua changamoto ya urasimishaji katika maeneo mengi nchini na hasa Dar es Salaam. Nakupongeza sana. Umeenda mbali, unatatuaje? Unasema utaenda kuanza na mitaa 559. Mimi nina mitaa 42 tu. Naamini ndani ya mitaa yako 559, mitaa 42 yote, najua mmeambiana sample na Benki ya Dunia, lakini mpeleke yote 42 ili tutatue tatizo la wananchi wa Jimbo la Kibamba kwenye urasimishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wangu naomba niwaambie, utafiti umepatikana, Mheshimiwa Waziri anaenda nalo vizuri na timu yake ya Wizara, na anawaondoa hofu wananchi wa Kibamba, yale mambo yangu matatu makubwa; maji, barabara na urasimishaji, yote yanapata majibu mwaka huu. Mambo yanaenda vizuri bambam, mambo yanakwenda vizuri Kibamba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Jambo lingine ni uboreshaji wa makazi, ndiyo jambo la tatu nilisema kama muda upo. Naona upo. Nimekuwa nikisema hapa pia kuhusu uboreshaji wa makazi. Nimeangalia taarifa za mapato na maduhuli, bado yako chini, 42% ni chini sana. Waheshimiwa Wabunge wengi waliotangulia kusema, wanne au watano mbele yangu, wameendelea kusisitiza kwamba Mheshimiwa Waziri ongeza mikakati ya kukusanya mapato. Pia ongeza ubunifu wa kuona vyanzo vipya vya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema na juzi kwenye semina yako nilisema lakini nilipata majibu kwa wataalamu ambayo yanaleta moyo. Nitumie nafasi hii tena kumpongeza Mheshimiwa Rais na nilikuwa nasema, nitaendelea kusema, nampongeza kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Samia Housing Scheme, nyumba 5,000 ni jambo kubwa sana, kwa sababu dhamira au dhima ya mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano, ulikuwa ni kuona tunaboresha makazi ya wananchi wetu ili wajiinue kiuchumi. Mama ameionesha wazi, tunabishana wapi hapo? Nyumba 5,000, asilimia 50 zinakaa Dar es Salaam, asilimia 20 zinaenda Dodoma, asilimia 30 katika mikoa mingine. Ndivyo tulivyoambiwa. Jambo la kupongeza sana hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba, hilo mmepeleka pale Kawe, kwenye eneo moja tu, makazi mapya na wananchi wengi watapata, lakini vipi yale makazi holela, makazi ya chini sana ya wakazi wa Tandale? Nimeendelea kusema, mwaka wa tatu nasema hapa; Manzese ni wachache. Ndugu zangu Wakinga pale akina Sanga wanachukua chukua tu pale wanajenga magorofa Manzese. Kuna Vingunguti na majiji mengine, maeneo ambayo kwa kweli yana hali mbaya, kwa nini tusiende tukatengeneza engagement pale ya kutengeneza MoU, mkubaliane na wananchi wanaomiliki vile vinyumba vya urithi, mkachukua mkawaachia chini ya floor ya kwanza ya pili, Serikali ikachukua ya tatu mpaka ya kumi mkaingiza wananchi wengine? Maana yake wananchi sasa watakuwa wanalipa kodi ya majengo, wananchi watakuwa wanalipa mambo mengine, na maisha yao na afya zao zitakuwa zimeboreka na pia miundombinu ya miji itakuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi. Nilisema juzi, mfano kule Lang’ata constituency, Jiji la Nairobi; hili ni Jimbo ambalo alikuwa anaongonza Mheshimiwa Raila Odinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli kulikuwa kuna eneo linaitwa Kibera, nyie wengine mnajua, lilikuwa lina mabati-mabati, hivyo kuliko hata Tandale, leo liko vizuri, twende tuige hivyo. Misri kule, South Africa haya mambo yapo ni gharama ni kweli. Juzi nilijibu, hebu endeleeni ingieni tufanye uchumi wa hewani, nyumba ina miaka 30/40 ndiko kwetu sisi, Magomeni, Manzese, Kariakoo, ndiko kwetu, ndiko kwa wazee wetu. Tuko tayari, njooni mtupe uchumi wa chini wa maduka na floor ya kwanza ya pili, chukueni ya tatu hadi ya kumi, mbona tayari hapo utaongeza mapato Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niliona mwaka huu wa tatu nimesema na ninashauri anza kufanya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umeisha Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naunga mkono hoja ya Wizara hii. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Bismillah! Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ambayo umenipa na mimi nichangie kwenye taarifa hizi za Kamati tatu za PAC, LAAC na PIC. Pia, natamka wazi mimi natokana na Kamati ya Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu wa leo napenda kwanza kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kufanya kazi vizuri na maelekezo yake kwa ujumla wake, Wasaidizi wake wanayafanikisha kwa kiwango kinachofaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maneno ya awali tu, moja, ninayo slogan mwenyewe ambayo nimewahi kui-induce kwa marafiki zangu Waheshimiwa Wabunge wengine, ikiwa inaitwa ‘Kumtenganisha Mheshimiwa Rais na Mafisadi, kumtenganisha Mheshimiwa Rais na wezi!’ Hii ni slogan yangu ya muda mrefu sana. Leo nimefurahi Kaka yangu Mheshimiwa Ole-Sendeka ulipopata nafasi ya kutoa taarifa, ukasema uwatenganishe Waheshimiwa Mawaziri na wezi. Ukarudi chini kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hapa niko tayari kutofautiana na haya maneno uliyoyaweka hapa. Mimi ninaamini Makamisaa wetu tumewapeleka kwenye Wizara mkamsaidie Mheshimiwa Rais, mkatusaidie Wabunge. Ndiyo maana mmekwenda wachache kule. Sasa, tunapofika sehemu na wewe pia tukutenganishe na hawa mafisadi, hao mafisadi tukawaita ni Maafisa Masuuli na Wasaidizi wao, sasa wewe unakuwa uko wapi? Umepewa instruments zote, una uwezo wa kuwafanya vyovyote katika Wizara ambazo mnazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawaomba sana, ninyi pamoja na Wizara zenu mumsaidie Mheshimiwa Rais ili aweze kufikia yale ambayo anayatarajia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafahamu ninayempa taarifa ni mtu anayejua Local Government vizuri sana, ni mtoto wa Local Government. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria zetu za Fedha za Local Government, sisi tuliopo humu ndani ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha za Halmashauri za Serikali za Mitaa, kwa hiyo, mapungufu yote yanayotokea kule hata sisi humu ndani ni sehemu yake. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo....

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa...

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah, taarifa!

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, ninaomba tusikilizane.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Waziri, utaharibu ushirika wa Bunge ....

MWENYEKITI: Mheshimiwa Simbachawene endelea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mtemvu kwamba iko haja, hatuwezi kutenganisha ni lazima wote tuwajibike, haya yanayotokea leo wote tunawajibika. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtemvu endelea na mchango wako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu kwanza ndiyo uwe muhimu lakini kwa heshima kubwa ambazo huwa ninampatia za asilimia mia moja kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtemvu na Waheshimiwa Wabunge, taarifa ni sehemu ya muda wako wa mchango, kwa hiyo, endelea na mchango wako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wana muda wao wa mwisho wa kuhitimisha, ambao watapata nafasi ya kutujibu vizuri lakini kwenye hili ambalo ili nipokee hii taarifa, ninataka kumwambia ni kweli anachokisema, Waheshimiwa Madiwani ni sehemu ya maamuzi kwenye Local Government, vipi kwenye Serikali Kuu? Mimi nimesema hapa ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, siyo Local Government, haya madudu ambayo sijaanza hata kuyasema yanatokea Serikali Kuu, huku sisi ni nani kule kwenye Serikali Kuu? Ni ninyi ndiyo mpo huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa hiyo ni nzuri, lakini kwenye upande mmoja wa local government ambapo ameniambia mimi pia ni mshiriki kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la maneno ya jumla, kwa sababu sijaanza kuchangia, ni heshima kwa chama changu. Haya mambo ambayo yanatokea hivi kwenye kamati zote, heshima ya chama changu kwenye umma (public), mnaitikisa, kwa hiyo, yanatuuma sana. Ziada, ni heshima ya taarifa ya CAG kwa umma. Taarifa zina miaka zaidi ya mitatu au minne, business as usual. Hatuwezi kwenda hivi kama Taifa. Hoja zinakuja, majibu ni changamoto, wananchi wanapokea mwezi wa Tatu, tunakuja kujadili mwezi wa Kumi na Moja, na mambo bado hayaendi, tunaendelea kubishana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujitahidi sana. Waheshimiwa Wabunge wengi wameelekeza au wametamani leo watoke na maazimio au kesho ambayo kwa kweli public itatuelewa. Sasa baada ya maneno yangu hayo ya jumla, nitatamani kuchangia katika maeneo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni Tanoil. Kwenye taarifa humo naona hata nimenukuliwa huko. Ndani ya Kamati, nafikiri hapa nilikaa nao vizuri sana. Kwa sababu wengi wamezungumza kwa ujumla wa changamoto ziliyotokea ndani ya Tanoil, wala sitaki kufika huko. Kwa sababu najua yameshaingia vizuri kwenye Hansard. Nitazungumza eneo dogo ambalo wengi hawajalizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na upungufu wote huo, moja, hakuna monthly reconciliation ambayo ilitusababishia tupate opportunity loss ya shilingi bilioni 1.8. Vile vile zaidi ya tani mbili, shehena mbili za mafuta za thamani ya shilingi bilioni 16.2, ambazo tungeweza kuzipata, tumeshindwa kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni hiyo ya underpricing ambayo watu wameielezea, kwamba underpricing na hii niitolee tu mfano, niwaambie tu vizuri kwamba ipo hivi, mwaka 2022 Tanoil palikuwa kuna bei ambayo, na ndiyo mwaka ambao tumefanya biashara vizuri. Kwa sababu mwaka wa nyuma yake tumefanya biashara kwa miezi miwili tu na ndiyo maana tulikuwa na loss ya shilingi milioni 166, lakini mwaka huu tunazungumzia loss ya Shilingi bilioni 7.8 ni kwa sababu full year (mwaka mzima) tumefanya biashara vizuri, lakini shida hapa imetokea nini? Kuna bei elekezi shilingi 2,610, hiyo ndiyo EWURA. Wao wakaenda kuuza chini ya shilingi 78.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo wanayo, haki ya kupunguza kwa percent kutoka ile base ya EWURA. Kwa hiyo, hiyo ni management standard, hawakuitii, lakini hata ile ya EWURA hawakuitii. Kamati ilihoji juu ya kibali, lakini ikumbukwe sana Chief Internal Auditor wa TPDC, parent company alikiri kuwa walikuwa hawana kibali. Kuna mmoja akasema, sasa kama mpaka watu wanakili kwa sentensi moja, “hatukuwa na kibali na tumefanya.” Sisi bado tunawatafuta hawa? Kwa hiyo, tunawatafuta wa nini? Yyaani mambo yako wazi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya utetezi wao, wakasema walikuwa hawana wataalamu huko siku za nyuma, lakini najua CAG amepata wapi haya? Kuna mmoja alisema kule juu ya kwenye tozo na tuzo, Polisi kule. Kuna sehemu kuna watu, vijana wazalendo sana. Nataka niseme kwa sababu kwenye ripoti ya Kamati yetu tumesema iende forensic audit kule, wakafanye ukaguzi wa kiuchunguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mtaalamu, kijana mdogo mwenye CPA yupo pale, ameenda kuwasaidia kutengeneza hizi hesabu, kaenda kuziona, madudu yote haya kayaona. Wamemwondoa, wamempa akasome magazeti, tena kwa kumuumiza kweli! Hatuwezi kufikia hapa. Hii mifano ipo, amezungumza kule Mheshimiwa Ester Bulaya, lakini ikumbukwe kwenye michango ya nyuma kidogo kaka yangu wa Kigoma Mjini aliwahi kumzungumzia Meneja wa TRA mipakani na baadaye mkamrudisha. Watu wanafukuzana. Mdogo wangu Mheshimiwa Mrisho Gambo, amewahi kumzungumzia hapa Internal Auditor mmoja Arusha, vijana wazalendo ambao tunatamani watusaidie kama Taifa ambapo ninyi mpo huko kama wasimamizi, hamwezi kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hata management mngeshaona kuna kijana kaumizwa, kwa nini katolewa? Mimi ningelikuwa ndio nipo mle ndani kama Kamisaa, huyu ndio angekuwa Manager of Finance au Director of Finance wa pale, kama siyo sehemu nyingine. sasa mnaenda kuwaumiza. Kwa hiyo, hiyo haikuwa na afya sana. Kwa hiyo, natamani sana Mheshimiwa Waziri mfuatilie, yupo mtu kaumia juu ya kutoa siri ya jambo hili. Kwa sababu tunapeleka uchunguzi kule, mtakuja kukuta hasara imeenda mara 12. Siyo Shilingi bilioni saba tu, zaidi ya Shilingi bilioni 60 kwa mwaka ujao, na mtakuja kunikumbuka na kwenye Hansard itabaki kumbukumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili. Ni riba ya shilingi bilioni 113.8 ambayo anadaiwa TANESCO na kampuni ya Pan Africa Energy. Upo mkataba ambao umeingiwa kati ya Pan Africa Energy na TANESCO kwa ajili ya matumizi ya gesi, lakini mkataba huu una-requirement yake ambayo wameekeana, kwamba kila ankara ya mwezi inapozalishwa inatakiwa ilipwe katika muda waliokubaliana. Kutoilipa kwa wakati, maana yake nini? Maana yake kutakuwa kuna riba ya asilimia nne na hii riba inakuja juu ya LIBOR rate. Maana yake ni nini? Kama riba ni asilimia nne na mwaka huo hii London Inter-Bank Offered Rate (LIBOR) itakuwa yenyewe ina-vary, siyo fixed. Kwa sasa ni asilimia 5.1, inasababisha tulipe asilimia 9.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Mkaguzi anaenda kukagua kwa huu mwaka 2021/2022 wa hesabu, zipo ankara 115 hazijawahi kulipwa. Maana yake nini? Maana yake ukiondoa deni halisi ambalo TANESCO analijua la kama Shilingi bilioni 245, tayari ndani yake kuna riba ya Shilingi bilioni 113. Hizi ni fedha nyingi sana. Maana yake kila mwaka ina-accumulate riba ya Shilingi bilioni 11. Sasa shilingi bilioni 11 kwa mwaka hizi fedha, mimi Mbunge wa Jimbo la Kibamba Wilaya ya Ubungo, Wilaya ya Changamoto, ndugu zangu hapa ningekuwa na zahanati ngapi? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mtemvu, malizia mchango wako. Muda wako umeisha.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme ukweli…

MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho Mheshimiwa, muda umekwisha.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaunga mkono hoja, nina ushahuri wa dakika moja. Ni kwamba, tuangalie mamlaka zote za uteuzi, muangalie qualification za watu rather than nepotism ili Taifa hili liweze kwenda mbele. Vinginevyo, hatutaweza kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Mpango huu wa bajeti wa miaka mitano 2021/2022 mpaka 2025/2026 pamoja na mwaka mmoja wa 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vipaumbele vyote ambavyo vimeainishwa, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake kwa ujumla kwa maana nimeshiriki katika kuuona Mpango ulivyowasilishwa kwenye Kamati, kama Mjumbe wa Kamati na nimechangia kwa kina. Kwa sasa nijielekeze katika maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni master plan ya Dar es Salaam kwa ujumla, lakini la pili, jinsi gani tutatumia usimamizi na ufuatiliaji katika miradi, hasa ya kimkakati na mingine kwa maana ya monitoring and evaluation katika miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wachache wa Dar es Salaam wamezungumza kwa ujumla juu ya master plan ya Dar es Salaam na hasa katika maeneo ya miundombinu kama mafuriko na upimaji wa ardhi. Nipongeze sana huu mpango wenyewe, katika page ya 97 wameeleza juu ya mkakati wa kuboresha maeneo hayo ya mabonde, lakini kuboresha pia maeneo ya miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa Dar es Salaam ambayo tuna population yenye makadirio takribani milioni sita kwa kufikia mwaka 2020, lakini tukiwa tunajua hata tax collection haipungui asilimia 80 na hata mchango katika GDP Dar es Salaam inachangia zaidi ya asilimia 75. Kwa msingi huo, tunataka kuona Dar es Salaam inakuwa kama sehemu ya kimkakati sana katika kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko hapa kutafuta fedha siyo kuangalia fedha zinakwenda wapi, tutakuja kwenye bajeti. Hapa mimi naona kama mkakati ukiwekwa vizuri Dar es Salaam inafaa sana kwenda kwenye housing building strategy. Wakati niko Diwani Manispaa ya Kinondoni tulikuwa tuna mpango wa kuondoa nyumba kongwe za Magomeni, takribani nyumba 605, ni mpango wa zaidi ya miaka 8 kuanzia 2012, leo nyumba zimejengwa. Naona mpango huo ungeendelea Dar es Salaam; tuna maeneo kama Tandale, Magomeni, Manzese, tukafanye mipango ya kujenga nyumba ambazo zitatusaidia kuinua uchumi wa watu, lakini tutaweza kuwa ni sehemu ya mapato sasa kwa jinsi ambavyo tutaingia makubaliano na wale wakazi ambao wana ardhi za msingi au ardhi zile ambazo ni za kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kwa haraka ni upimaji wa ardhi. Mpango umesema vizuri una nia ya kupima ardhi nchi nzima, sasa waende kweli kimkakati wapime ardhi. Waipime ardhi ya Dar es Salaam kutokana na population niliyosema, makadirio ni watu milioni sita, tukipima ardhi kwa watu wote hawa, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema nia yake ni nzuri kwenye hili, basi tutaweza kuona jinsi gani mapato tunayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko eneo hili la usimamizi na ufuatiliaji. Tutakubaliana hapa miradi mingi hata hii ya kimkakati bado item au component ya ufuatiliaji haipo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nivumilie dakika moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti …

MWENYEKITI: Nina orodha ndefu Mheshimiwa. Uniwie radhi, ahsante sana.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa maana ya mwaka 2021/2022 – 2025/2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri mapema kwamba mimi ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo, nimechangia mara nyingi katika maeneo mengi. Kwa sasa nitumie nafasi hii kuchangia eneo moja tu ambalo pia nilitumia nafasi kama hii kuchangia Mpango kwa mara kwanza mwezi Februari katika eneo la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kutuwasilishia Mpango mzuri. Pia, nimpongeze Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa jinsi ambavyo waliweza kutuongoza na kufikia mapendekezo hayo ambayo Waheshimiwa Wajumbe wameyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu una maeneo matano ya vipaumbele, lakini binafsi nitajielekeza katika eneo moja la kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Hapa yako mambo mengi ya elimu, afya na kadhalika lakini mimi nimebeba hili la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema sana juu ya eneo la ardhi na hasa upimaji, Mpango wetu ulieleza wazi nia yake ya kupima ardhi nchi nzima. Nia hii wala si mpya sana kwenye Mpango wa Tatu, ilikuwepo pia kwenye Mpango wa Pili. Nikikumbuka sana katika Mpango wa Pili tumeendelea sana kupima ardhi na hapa niipongeze sana Wizara ya kisekta kwa kufanya kazi nzuri sana kitakwimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufahamu vizuri maana halisi ya kupima ardhi ni lazima tujue faida zake. Nitataja chache sana kwa sababu ya muda, tukipima ardhi maana yake tutatambua kisheria umiliki halali wa kipande kilichopimwa, kuongeza thamani ya ardhi, kuongeza usalama wa ardhi, kutumika kama dhamana na zaidi kuondoa migogoro kwa majirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, hizo zikiwa ni sifa chache sana lakini malengo ya upimaji katika kipindi kilichopita cha Mpango wa Pili tumepima vizuri sana. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 – 2019/2020 tumetoka katika upimaji wa karibu viwanja 74,000 mpaka kufikia viwanja 150,000 ni ongezeko zaidi ya nusu yaani mara mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mpango mzuri ambao upo sana ndiyo maana nina wasifia sana, katika kipindi hiki cha Mpango wa Tatu naona sasa wanaelekea kwenye kupima ardhi katika kiwango cha 300,000 mpaka 500,000 kwa mwaka, hili ni jambo kubwa sana. Zaidi nijielekeze na nilisema Februari nchi hii ni kubwa, ina eneo la ardhi kubwa sana lakini toka Uhuru tumeshapima asilimia 25 tu na najua malengo kwa miaka mitano ijayo itakuwa labda kwa ziada ya asilimia 100 maana yake ni mara mbili kufikia asilimia 45. Ni ukweli tukijielekeza sana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watu zaidi ya milioni sita katika makadirio kati ya milioni 61 kwa nchi nzima, unaweza ukaona tuna idadi kubwa na tukiwekeza pale tunaweza tukapata tija sana ya kuinua watu wetu kiuchumi. Tukiinua watu hawa kiuchumi maana yake itaenda sambamba kwa maana ya multiplier effect katika maeneo mengine ambayo yatatusaidia sana kujiinua kiuchumi lakini vilevile kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuseme ukweli, nimepongeza kwa kiasi lakini ipo kazi bado haijafanyika na mimi muda mwingi naipima kazi ya sekta hii katika Mkoa wa Dar es Salaam vis a vis mikoa mingine na nipongeze sana. Trend ya mwaka 2015/2016 – 2019/2020 na hasa miaka miwili ya mwisho utaona Mkoa wa Dodoma vis a vis Mkoa wa Dar es Salaam, nilijaribu kupitapita kitakwimu nikakutana na kitabu kimoja cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri cha mwisho kwa sekta hii 2021, karibu kama ukurasa 170 unaweza ukaona viwanja vilivyopimwa 2018/2019 Dar es Salaam ni 25,490 lakini mwaka huo huo Dodoma imepima 71,571. Kwa mwaka uliofuatia 2019/2020 mpaka Aprili, Dar es Salaam tumepima viwanja 11,125, Dodoma 76,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndipo ninaposhangaa. Ninashangaa kwa kuona kwamba bado hatujaamua kupima ardhi, tungeamua kupima ardhi hii haiwezekani eneo lenye watu milioni sita tunapima ardhi viwanja 14,000. Watu wenye watu takriban milioni mbili wanapima viwanja 70,000 mpaka 75,000. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli pia katika mwaka 2017/2018, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aliwahi kutoa kauli moja nzuri sana juu ya kurasimisha ardhi nchi nzima. Jambo hili lilikuwa ni zuri sana kwa maana katika malengo yale niliyoyasema kama faida ya kupima ardhi utaona huko kuinua wananchi kiuchumi. Alitamani kuona maeneo ambayo yameendelezwa kiholela sasa basi watu waweze kupimiwa bila kubomolewa na baadaye hati zile ziwasaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfano wa kawaida sana, Mkoa wa Dar es Salaam kwenye lile jambo la urasimishaji ambayo nikinukuu kauli ya Mheshimiwa Waziri aliyoitoa tarehe 23 Oktoba, 2017 alisema: “Hatutobomoa nyumba ya mtu bali tutaendelea na urasimishaji wa makazi kwa maeneo yaliyojengwa holela ili yawe makazi rasmi na wananchi wapelekewe huduma muhimu kama vile barabara, umeme na maji. Muhimu wapewe hati miliki ili ziwasaidie kiuchumi na waweze kulipa kodi ya ardhi, lakini nitazuia ujenzi mpya holela katika miji yetu kwa mujibu wa sheria. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi, tarehe 23 Oktoba, 2017”.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo hapa kwa kumalizia dakika zilizobakia. Kitakwimu, urasimishaji huu umekuwa donda kubwa Dar es Salaam kama sample ya nchi nzima. Dar es Salaam katika Wilaya ya Ubungo nikienda Jimbo la Kibamba kwenye Kata sita nabeba kata mbili tu, maana huko kwingine ni nyingi sana, katika kata mbili tu katika nia njema ya kupima ardhi hii ili itusaidie sana kwenda kwenye Mpango wa Tatu, katika makampuni yaliyosajiliwa, kwenye usajili, uthamini, wana mambo kama matatu hivi lakini viwanja vilivyotambuliwa na kupimwa kati ya viwanja 10,000 ndani ya kata moja ya Kibamba ni viwanja 3,000 tu ndiyo vimewekewa mawe, hati ni 20 katika kipindi cha miaka miwili na zaidi. Kata ya Mbezi, katika viwanja vilivyopimwa 33,000 hakuna hati hata moja katika kipindi cha miaka miwili na nusu Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, fedha ni zipi zimechangwa? Kwenye ile Kata ya Kibamba peke yake shilingi milioni 890 wakati Kata ya Mbezi ni shilingi bilioni 2.57, ukizijumlisha ni zaidi ya shilingi bilioni 3 zimechangwa na Watanzania maskini lakini mpaka sana hawajawahi kuona hati ndani ya kipindi cha miaka miwili, haya ni magumu hata kuyatamka. Leo tunasimama tunazungumzia Mpango uje utusaidie kwenda mbele katika kipindi cha miaka mitato 2021-2026. Kwa kweli lazima tuoneshe tuna nia njema kusema haya tunayoyasema ili tuyatende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili halijawahi kwenda sawa, tunatambua wakati tunapeleka urasimishaji upande mmoja watu wanaambiwa wachange fedha zao ili twende sawa wapate hati, kuna upande mwingine zaidi ya halmashauri 27 zimepewa zaidi ya shilingi bilioni 6 hadi 10. Tumeona Kamati ilikuwa Iringa juzi tu na ikakuta zaidi ya shilingi milioni 400 waliyopewa ile halmashauri wameshindwa hata kurejesha, ni revolving lakini wameshindwa kurudisha lakini hawa waliotoa hela zao zinaenda kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana jukumu la Wizara kwenye hili ni kutoa hati siyo makampuni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nitarudi kuongelea sekta hii vizuri sana. Nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie Wizara hii. Mimi nitajielekeza kwenye eneo la tafiti tu, limesemwa na wajumbe wengi lakini na mimi niseme hapa kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwanza muhimu ni vizuri tujue hata nini maana ya tafiti katika elimu ya juu. Mwananzuoni mmoja anaitwa Godwin Kalibao anasema, utafiti unahusisha kukusanya data, habari na ukweli kwa ajili ya kuendeleza ujuzi. Yupo mwingine anaitwa John W. Gasswell anasema, utafiti ni mchakato wa hatua za kukusanya na kuchambua habari ili kuongeza uelewa wetu wa mada na masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwa kina sana na nilimsikiliza vizuri wakati anaendelea kuzungumzia baadhi ya vyuo vyetu kuanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Mzumbe, DUSE na vyuo vingine vya ufundi na zaidi katika eneo la tafiti. Nampongeza kwa sababu kama Serikali pia bado inaendelea kutoa fedha kidogo kwa ajili ya machapisho na tafiti mbalimbali lakini hazitoshelezi. Ukiangalia uhitaji wenyewe kwa takwimu mbalimbali ambazo unaweza ukazipata, mimi nimejaribu sana kwenda kwenye taasisi zetu za tafiti mbalimbali kuanzia NBS na nyingine nyingi, inaonyesha tunahitaji tafiti na machapisho mbalimbali kwa kiasi kikubwa kuliko ambavyo vimewasilishwa katika bajeti ya 2021 hata matarijio ya bajeti yetu tunayokwenda nayo sasa au tunayoianza hii ya 2021/ 2022.

Mheshimiwa Spika, pamoja na faida nyingi za tafiti, kwa muda siwezi kusema yote, zipo faida mbalimbali; moja, ikiwa ni kupata taarifa muhimu kuhusu suala linalotafitiwa; kuongeza hazina za maarifa katika eneo hilo lakini kupima joto la hali, fikra na mitazamo mbalimbali. Pamoja na faida hizi zote katika maeneo ya tafiti hatujafanikiwa kama taifa kwa sababu ya changamoto zilizopo. Changamoto kubwa kama Taifa ni mbili; ya kwanza ni gharama na ya pili ni wataalam wabobezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la gharama nimefurahi sana, Mwenyekiti wa Kamati alivyokuja mbele hapo amesema kwenye eneo hili hatujafanikiwa sana na akatolewa mfano COSTECH wameweka shilingi bilioni 3.8 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na anasema hazitoshi kabisa, sasa hili ni eneo moja tu. Pia Mwenyekiti amesema katika nchi za Ulaya wameweka makadirio ya mchango wa Pato la Taifa liwe ni asilimia tatu ambayo inaenda kwenye utafiti lakini kwenye nchi za Afrika ni asilimia moja. Unaweza ukaona bado kama Afrika tunahitaji kujivuta sana in particular ni Tanzania sisi tupo wapi. Hali yetu bado si nzuri sana katika eneo la gharama.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nijaribu kusema, hili la gharama mara nyingi tumeendelea kutegemea wafadhali ndiyo maana katika bajeti yetu hatuwezi kuiona imeweka kiasi kikubwa kwa ajili ya tafiti. Tunakubali, tunahitaji wafadhali watusaidie tufanye tafiti lakini ukweli hawa wafadhali ili watupe fedha zao tufanye tafiti ni lazima tafiti zitaenda kwa ajili ya majibu yao na hiyo ndiyo changamoto. Hizi tafiti sisi tunazotaka kuzifanya ni za aina mbili tu, tafiti za msingi ambazo wanaziita basic research lakini na tafiti tumizi applied au pure research. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Taifa lazima tujue hizi tafiti za msingi ambazo ndiyo zinatumika kwa muda mrefu, je, tunazo kwa kiasi gani? Hitaji letu ni lipi? Zimepungua kwa kiasi gani? Zinahitaji gharama gani? Tunashindwa kufika hapo. Hizi za muda mfupi ambazo ni tafiti tumizi, tunazo kwa kiasi gani? Mpaka sasa zimetafitiwa kwa kiasi gani katika hitaji lipi la jamii katika maeneo mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, tunapokosekana kwenye eneo hili la tafiti, tunashindwa kujielekeza katika mipango yetu mbalimbali. Mheshimiwa Mpina asubuhi amezungumza juu ya kushindwa kujielekeza kujua kwa sasa tunahitaji elimu ipi? Elimu yenye ujuzi kwa kiasi gani? Watu wafundishwe nini ili wakaombe, wakapate soko la ajira ambalo linafanana na elimu wanayoihitaji? Yote ni kwa sababu ya kukosa tafiti.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo ya kilimo, Mheshimiwa Naibu Waziri mara nyingi anasimama hapa, anatueleza juu ya uhitaji wa mbegu za kisasa na kadhalika. Huwezi kujua hitaji la mbegu kwenye nchi kama hatuna tafiti za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengine ya afya na usalama wa wananchi wetu, ili tuweze kujua yote ni lazima tafiti mbalimbali za muda mfupi na mrefu ziweze kufanyika. Nilisema maeneo mawili ni changamoto. Eneo la pili, ni la wataalam wabobezi. Hao wanaweza kuwa ni wale wenye shahada za uzamivu na umahiri, Ph.D na Masters, lakini zaidi ni hawa za uzamivu Ph.D.

Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa ni shahidi, Mwenyekiti pia kasema, changamoto ya kwanza katika elimu ni upungufu wa wataalam katika vyuo vyetu. Hili wote tunakubaliana kwamba ni kweli, tuna changamoto ya wahadhiri. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ameendelea kueleza udahili wa wanafunzi katika eneo hili la umahiri na uzamivu, kote amesema katika vyuo vyote; nami nimeendelea kuweka pale 28, 34, 18, 64 wanaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukimtafuta Mheshimiwa Profesa Ndalichako ambaye ni mbobezi wa zaidi ya miaka 18 mpaka 20 ni sawa na wale wanaoenda kufundishwa leo! Nataka kusema nini? Nataka kusema, leo tuna changamoto ya ubora wa elimu katika nchi yetu (quality). Katika hili hatupingani. Tunakubali watoto wetu wanakwenda, enrollment ni kubwa katika kipindi cha miaka mitano mfululizo, lakini katika wataalam hakuna ongezeko. Yaani ukitafuta hizi mbili, line moja inaenda katika kuongeza watoto wengi mashuleni kwa kipindi cha miaka mitano… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Issa Mtemvu. Muda hauko upande wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu. Kwanza ninayo kila sababu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, baba Mkwe wangu Mheshimiwa William Lukuvi, maana nimeoa Ilula pale, Semkinywa, kwa hiyo kwangu Mheshimiwa Waziri ni baba Mkwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Angeline Mabula, bila kuacha kuwapongeza Watendaji Wakuu wakiongozwa na Bi. Mary Makondo akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu Kaka yangu Nicholas Mkapa. Nawapongeza sana pamoja na wasaidizi wao kwenye Wizara, kwa kweli mnaendelea kufanya kazi vizuri katika ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nitajielekeza katika maeneo mawili. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 87 hadi 89 inaeleza sana juu ya urasimishaji, kwa maana ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa hati eneo hili, lakini eneo B nitajiekeleza kidogo kwenye mgogoro mdogo uliopo katika Hospitali yetu ya Mloganzila na sio mgogoro ni jinsi ya utatuaji wa jambo lile kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la urasimishaji baada ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini nimpongeze kimahsusi sana baada ya kukubali maana ni mtiifu sana, kukubali maelekezo ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 24 mwezi Februari pale Kibamba wakati anazindua ile Stendi ya Magufuli alitoa maelekezo ya kukabidhiwa hati wananchi wa Jimbo la Kibamba na Wilaya ya Ubungo hati ya takribani ekari 52.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa wa Mheshimiwa Lukuvi alituletea baada ya kufufua mipaka ile hati yenye ukubwa wa ekari 75.2 nampongeza sana, sana Mheshimiwa Waziri. Aliileta ndani ya siku mbili tarehe 26 nikiwepo pale pamoja na Wakurugenzi na Mheshimiwa DC tuliipokea na maelekezo yake. Tumwahidi Waziri tutatekeleza vile ambavyo wanatarajia, hakuna mtu atakula kipande kwa ajili ya kujenga nyumba yake na makazi yake na mkewe au dada yake, tunapeleka maslahi mapana ya wananchi katika eneo lile. Namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze juu ya urasimishaji nimekuwa nikisema hapa na juzi tu tarehe 18 nilikuwa na swali la msingi katika eneo hili na niliongea, lakini leo niseme kwa kuweka vitu sawa, hali ya upimaji ndani ya Wilaya ya Ubungo, lakini hususani Jimbo la Kibamba, ndani ya mitaa yote 43 iliyopo pale, nirudie kusema hali bado si shwari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia yetu ya upangaji, upimaji na umilikishaji tuone wananchi wanaenda kujiinua kiuchumi ndiyo dhamira kubwa na niliwahi kusema hapa hata kauli ya Mheshimiwa Waziri ile ya mwaka 2017 mwezi wa 10 tarehe 23 juu ya kusema jambo hili liende vizuri aone wananchi wanajiinua kiuchumi halijafikia kwenye lengo. Kama sasa tuna hali hii ambayo takribani wananchi 153,000 ambao tayari viwanja vyao vimefikia katika hatua ya upimaji tu wa awali, karibu watu 53 lakini kwa haraka juzi hapa nilijibiwa kwamba takribani viwanja 1,925 tayari vina maombi ya hati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vina maombi 1,900 tuseme 2,000 kutoka 53,000 ambao wameanza au vimeanza kupimwa kwa awali, unaitafuta asilimia hapa huioni ya utija. Taarifa ambazo ninazo kama Mbunge, hati kuandaliwa ni jambo moja, zilizoandaliwa 1,900, lakini hati ambazo zimetoka ni 845 na hii leo niirudie tena, maana Hansard ilikaa vizuri kwenye majibu ya msingi, lakini sio katika maswali yangu ya nyongeza. Hati 845 ndiyo zilitoka kwa wananchi katika mitaa 43 ukigawanya kawaida ukawapa tu kila mtaa hati
19 na point kwa sisi wahasibu tunasema hati 20 kwa kila mtaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kweli takribani mradi ambao umeanza 2013 wa miaka kumi hadi 2023 tumeambiwa leo asubuhi hapa mradi utaenda kuisha 2023, kwa Kibamba pale umeanza 2017 baada ya kauli ya Mheshimiwa Waziri mpaka 2023 tutakuwa na miaka mitano tu, leo tupo chini ya asilimia 10 ya utoaji hati, yale malengo mahsusi yatafikia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka juu ya uwajibikaji wa Mheshimiwa Waziri, lakini najua na nitamwambia anaangushwa sehemu gani. Hali hii ina changamoto nyingi sana, lakini kwenye hili ndiyo maana hawafiki ni kwa kuwa pia kuna shida moja ya mashamba limezungumzwa hapa. Yapo mashamba ambayo kama bado tunaendelea kuchelea kuyafuta hati zake maana yake tutashindwa kufanya upimaji wa jumla wa viwanja vingine ambayo yapo karibu na maeneo hayo. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri na hilo pia anaweza akaja kulizungumza juu ya mkakati, kwa sababu nimeona maelezo yake yapo vizuri kabisa, nia njema ya kupima mashamba, lakini pia na kufuta mashamba ambayo yatakuwa hayana tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili eneo, tunazo changamoto karibu tatu, nne na nitazisema na nilieleza hapa. Huu mpango ni mzuri, sina shaka nao, yenyewe program na nia yake ni nzuri, dhamira yake kwa wananchi ni nzuri sana, lakini bado ipo shida juu ya usimamizi wake. Jukumu la Serikali, jukumu la Wizara wala siyo kupanga, wala siyo kupima, wala siyo kuthamini zile ardhi, siyo jukumu lao kimsingi au kisheria, hili ni jukumu la Mamlaka za Miji pamoja na Sekta Binafsi na wameeleza vizuri kwenye hotuba ya Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Wizara ni kusimamia na kuratibu mambo haya yaende vizuri, lakini lao moja kwa moja ni kuona hati zinatoka ili ile dhima kuu ya jambo hili iweze kufikiwa. Tulivyoanza hili jambo maelekezo ya Wizara kwenye kuratibu yalieleza akaunti zote za urasimishaji zifunguliwe kwa ushirika baina ya mkandarasi na Kamati ya Urasimishaji, kuna shida ikatokea hapo, alivyohusishwa mkandarasi kwenye akaunti zile ndiyo upigaji wa fedha kwenye akaunti za benki ulifanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilieleza juzi tukashindana kwenye figure, hela zimepigwa nyingi leo wananchi wa Jimbo la Kibamba wanalia, lakini wanalia kwa sababu wamekosa majibu. Msimamizi na mratibu akisaidiwa na halmashauri zetu kule hawezi kutoa majibu kwa wananchi waliotoa hela zao. Katika hii hatua ya awali tu, nieleze ukweli, malipo yale ni kati ya 150,000 mpaka 200,000. Ilianza 200,000, mratibu na msimamizi akaona ni nyingi akasaidia 180,000 ikaenda hadi 150,000, watu wamejitahidi kulipa, wapo wanaolipa kidogo kidogo wapo wamelipa kwa ukamilifu, lakini hizi hela zilizolipwa awamu ya kwanza zimepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye baada ya Mheshimiwa Waziri kuliona, ndiyo maana namsifia sana, akaja akawaondoa wakandarasi akaacha timu ya Kamati ya Urasimishaji, sasa mambo yanaenda vizuri na najua hata majibu yale ya msingi ni watu 30,000 tu ambao ndiyo wamelipia ni wale baada ya utaratibu umekaa vizuri. Hoja yangu ilikuja hawa kabla wakati wamehusishwa wakandarasi na wakapiga zile hela, thamani ya fedha za wananchi wa jimbo lile zimekwenda wapi? Tunazionaje? Maana hati hamna na hela zao hawajui zilipokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba juzi hapa kama kweli yule Mtaalam wa Fedha, Mkaguzi wa Fedha na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kama anaweza kuingia hapa, maana nao wana taratibu zao, lakini nafikiria hizi hela ni za wananchi, wananchi wa Serikali hii na hii hapa ni Kamati yetu ya Ukaguzi, I mean Mdhibiti Mkuu (CAG) apewe nafasi kama siyo yeye nani jicho la tatu, kati ya Serikali na wananchi juu ya hela zilizopigwa, ndiyo nia yangu jicho la tatu liende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka sana hizo ni fedha, Mheshimiwa Waziri atatwambia mkakati wa Serikali juu ya jicho la tatu kwenye eneo hili. Hata hivyo, kuna makampuni yanasemekana yamefilisika, makampuni kati ya makampuni 162 ambao walitwambia kwenye taarifa zao wameyasajili kama nchi, lakini yapo makampuni 32 yameingia kwenye mchakato huu ndani ya Jimbo la Kibamba, haya makampuni ni ukweli hayafanyi kazi, lakini yapo makampuni yasiyopungua manne, matano mengine yametamkwa yamefisilika na Mheshimiwa Waziri anajua hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimsifie Waziri amewahi kufika kwenye vikao vyake ndani ya mkoa, ndani ya wilaya na akachukua hatua. Zipo hatua amechukua, hatua mojawapo aliyochukua, nishukuru sana na taarifa yake imesema amechukua hatua, ndiyo maana amefuta leseni za kampuni tatu, lakini amechukua hatua kwa kusimamisha kwa muda makampuni tisa, amechukua hatua kwa kuyapa onyo makampuni 41, lakini amezisimamisha kampuni 15, nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la ziada, hayo tu hayatoshi na mengine amewapeleka TAKUKURU wafanye kazi, hakuna majibu kwa wananchi nini mpaka leo na hapa tunaambiwa mwaka mmoja na nusu ujao mradi unaisha, tusije tukawa kama benki tuambiwe, mlango ukifungwa tunapotaka kwenda kuchukua hela ndani ya benki, je, zikiwa nje tunatolewa? Waliokuwepo ndani wamefungiwa huduma itawaishia watu wa ndani? Watuambie au huo mwaka 2023 Mheshimiwa Naibu Waziri jana amezungumza hapa ikiisha ndiyo tunarudi kwenye utaratibu wa kawaida kule kwa furaha, naomba tupate majibu hapa, huu unaishajeishaje na hela zetu hatujui zilipokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumaliza kwa sababu siwezi kumaliza yote na hata lile la Mloganzila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga hata hivyo.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru, kwa haya machache niliyosema lakini najua dhima itakuwa imeeleweka na Mheshimiwa Waziri atasema vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa kiwango kinachofaa. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie taarifa zetu hizi. Kwanza na mimi nikiri kukubaliana kabisa au kuunga hoja mkono taarifa zote mbili za Wenyeviti wetu wa LAAC na PAC, nikiwa natokea kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Spika, tuliyojadili sana kwenye taarifa zetu kwa kipindi hichi ni taarifa za Ukaguzi wa Kiufanisi. Kuangalia si tu fedha tulizopeleka lakini fedha tulizopeleka zimekuwa na thamani gani au na mchango gani katika miradi ambayo tulikuwa tunaikusudia kama Taifa.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaeleza lolote, nitumie nafasi hii nami kumshukuru sana sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitendea haki sana Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo hususan Jimbo la Kibamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi sana, jimbo lile lilikuwa linakaribia kuzikwa (niseme). Wananchi wa jimbo lile walikuwa wanatamani hata kuhama, wote tu, lakini leo katika huduma za jamii zote; nikizungumzia shule, shule mpya saba; nikizungumzia eneo la afya, hospitali mpya kaijenga Mheshimiwa Rais Mama Samia, lakini shule ya Mkoa wa Dar es Salaam, ile ya shilingi bilioni 4.1 kaijenda ndani ya Jimbo la Kibamba. Pia juzi nimekabidhi ambulance.

Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi, mambo ni mazuri. Yaliyobaki niliwahi kusema hapa, ni machache, lakini mwisho wa siku mambo ni bam bam.

Mheshimiwa Spika, uniruhusu nijielekeze kwenye maeneo machache. Moja, ni eneo la ufanisi wa ukaguzi katika miradi ya maji hasa mijini. Jicho letu CAG amefanya kazi kubwa sana. Pamoja na kazi kubwa ambayo anafanya mwamvuli wetu katika eneo la maji ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, lakini ukweli jicho linamwonesha kuna upungufu mkubwa sana katika usimamizi wa miradi hasa miradi mikubwa.

Mheshimiwa Spika, moja, mipango hamna, taratibu hakuna katika ofisi au hizi mamlaka za maji bila usimamizi wa miradi husika. Hata matumizi ya ufanisi kwenye mitambo tunayowekeza, ile mitambo mikubwa ya gharama kubwa uwezo wa kuitumia hawana. Inawezekana hapa sasa kunahitajika kuwa na mafunzo ya hali ya juu kwa wataalamu wetu ili waweze kuitumia.

Mheshimiwa Spika, katika mamlaka nane ambazo jicho limeweza kuangalia au CAG ameweza kuzipitia unaweza kuona kwa kiwango cha chini kabisa Wakala wa Maji wa RUWASA na SUWASA chini ya 22% kuweza kusimamia mitambo iliyowekezwa. Zaidi ya hilo, kutosimamia kule maana yake imesababisha wananchi katika maeneo yale au halmashauri zile wameshindwa kupata maji ilhali uwekezaji ulikuwa unatosha kabisa wananchi wale waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana, angalau katika zile nane, mbili zilizofanya vizuri ni DAWASA na DUWASA, yaani kwa maana ya 100% hapa Dodoma na kwa 78.5% kwa Dar es Salaam. Kwa hiyo, unaweza ukaona angalau kuna mafanikio katika maeneo hayo. Mapungufu haya yote wanatoa sababu wao. Wana sababu kama tano; moja, ni kukatika kwa umeme, wanasema ni moja ya sababu inayowafanya washindwe kufanikisha usimamizi wa maji na kusambaza maji mijini.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kupungua kwa nguvu za umeme, low voltage. La tatu ni ubovu wa pampu na uchakavu wa miundombinu. Hii sample ilifanyika kwa miaka mitatu 2019/2020 hadi 2021/2022 miaka mitatu, lakini sasa hivi tunavyozungumza, Dar es Salaam Jimbo la Kibamba wana siku ya 34 changamoto ya maji zaidi ya mwezi mmoja watu hawana maji, lakini sababu ni hizi hizi tena, wataalamu wanatuambia low voltage, miundombinu imechukuliwa na maji na sababu nyingine kama hizi pampu Ruvu Juu pale, ndani ya miaka mitatu labda haijatengenezwa.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atoe jicho, aangalie sana, kazi anaifanya kubwa, lakini anaweza kuangushwa na wataalamu wake katika jambo hili. Yaani ninavyozungumza, hatuna maji Dar es Salaam. Jimbo la Kibamba wananchi wa maeneo mengi hawana maji zaidi ya wiki tatu, lakini kuna mmoja alizungumza, Mheshimiwa Mwambe juu ya madeni, baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa madeni ya maji. Zaidi ya shilingi bilioni 43.3 ni madeni.

Mheshimiwa Spika, kwanini hawalipi wakati kwenye bajeti zetu tukipitisha hapa tunaweka token kwenye utility? Shida ni nini? Wanatumia katika matumizi mengine au ni nini? Katika hili tumshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni vizuri na kama ananisikia vizuri, wataalamu wake kama wapo, ni vizuri sasa mkali-reinvest fedha kwa ajili ya utility ili moja kwa moja fungu la 21 – Hazina (Treasure) iweze kulipia madeni haya, kwa sababu hawa watu inaonekana tukiwapa wanatumia kwenye matumizi mengine, lakini tukizifunga, zitaenda kutusaidia katika malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, tunaambiwa eti ni taasisi zile nzito nzito. Kwa sababu mimi niliwahi kuhoji kwenye Kamati, sasa kama ni kwenye taasisi zile nzito, kama majeshi na megine na kadhalika, hizi fedha si ndiyo kwanza tunaweza tukaanza kuwapa wao! Tunampelekea nani? Tukimaliza madeni ya Serikali (public dept), mishahara, tunapeleka kwao. Kwa hiyo, wataweza kulipa madeni. Nafikiri, ndiyo maana nakumbuka zamani tuliambiwa kaa, kaa. Ee, maneno mawili, lakini sijui kama tunaendelea nayo yale maneno mawili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikitoka katika eneo hilo, kuna jambo la Mradi wa DMDP page ya 114 ya taarifa ya Kamati yetu. Nashukuru sana katika ukaguzi wa ufanisi, katika mradi wa DMDP awamu ya kwanza ulifanya mambo mazuri na makubwa na wananchi wengi wa Dar es Salaam wanajua, na Waheshimiwa Wabunge ambao wanakaa Dar es Salaam Kijichi nimeiona lami inatembea, Temeke nzima, Buza na maeneo machache ya Kinondoni kwa maana ya Sinza mataa mazuri, Mburahati na maeneo mengine yote ni DMDP one, tumefaanya kazi nzuri. Zaidi ya US dollar ya milioni 330.3 na zaidi ya milioni 300 hizi tumepata kutokea Benki ya Dunia. Kwa hiyo, tuwashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, upungufu mdogo ambao ninaamini katika nyakati za miradi ambayo inakuja karibuni watafanyia kazi, mfano changamoto ya muda kuongezeka kutoka miezi 15 hadi miezi 26, laini ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi kutoa siku 33 hadi siku 295 miezi 10 unachelewa kumlipa mkandarasi, lazima hata deni litaongezeka.

Mheshimiwa Spika, ziada ni certificate of completion. Unatoa certification ya kumaliza kazi kabla hata kazi haijaanza. Kwa hiyo, nawaomba sana TARURA kupitia hii DMDP, hii DMDP inayokuja sasa, ambayo sisi Dar es Salaam, nafuu imesomwa hapa, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, siasa ya Dar es Salaam ni miundombinu. Hatuna siasa nyingine, nilisema asubuhi. Sisi hatuna siasa ya uvuvi, hatuna siasa ya kilimo, siasa yetu ya msingi ni barabara tu ili uchumi wetu uweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwenye eneo hili anatutendea haki, DMDP ya kwanza ilihusu wilaya tatu; Temeke, Ilala na Kinondoni, sasa hivi ameiongeza Kigamboni na Kibamba au Ubungo ambapo na wananchi wa Kibamba wanaenda kukutana na kilometa 23 hizi vizuri kabisa. Kwa hiyo, niwaambie kabisa, kazi ya Mheshimiwa wenu Issa Jumanne Mtemvu inaendelea kuwasemea Bungeni mliponileta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kidogo sana ni eneo la urasimishaji. Kazi imeendelea kufanywa vizuri katika page ya 131 limesemwa jambo la urasimishaji. Namshukuru sana Mheshimiwa Mabula kwa kuendelea kufanya kazi nzuri akiwa Naibu na baadaye Waziri baada ya Mheshimiwa Lukuvi na sasa mdogo wangu Mheshimiwa Jerry William Silaa, Mbunge wa Ukonga anaendelea kufanya kazi vizuri, anatupa ushirikiano mzuri katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto unazo sana, zimesemwa kwenye taarifa, sitaki kuzisema. Taarifa imesomwa na Mheshimiwa Mwenyekiti, japo changamoto nyingi ambazo zimesababisha, hamjafikia malengo. Mpaka sasa hivi chini ya 10% ndiyo hati nchini mmezipata. Kwa hiyo, nataka niseme, mmekuja kwenye bajeti ya sasa hii iliyopita ya 2023/2024, mlituambia dola za Kimarekani milioni 150 ambayo ni takribani shilingi bilioni 345, na shilingi bilioni 61 zitakuwa ni kwa ajili ya urasimishaji, naombeni mkazitumie.

Mheshimiwa Spika, najua mmeanza kazi kupitia madawati, mmefanya kazi nzuri sana, mnaanza kwa awamu, nendeni mkaharakishe ili wananchi wapate hati.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi naunga mkono hoja ya Kamati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa mafungu yake mawili; Fungu Na. 48 na Fungu Na. 3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia nami nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya kwenye nchi yetu. Ni dhahiri kila Mtanzania anajua kazi inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa haraka nitumie nafasi hii kuipongeza sana Wizara kwa ujumla; kamisaa wetu Mheshimiwa Jerry William Silaa na kaka yangu Mheshimiwa Mizengo Pinda Geophrey, pia nisiache kwa watendaji wakiongozwa na Mhandisi Sanga, Katibu Mkuu; Naibu Katibu Mkuu pamoja na wataalam wao wote. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri ambayo na sisi Waheshimiwa Wabunge tunaithamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nijielekeze kwenye maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni eneo la urasimishaji likienda sambamba na migogoro ya wawekezaji dhidi ya wananchi wetu au ya maeneo. La pili, ni eneo hili ambalo wengi wamelizungumzia. Kuhusu Fungu Na.3 la Tume yetu ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la urasimishaji ni sehemu ambayo katika kipindi changu cha miaka mitatu, na huu wa nne, nimekuwa nikilisema kila tukiwa tunachangia bajeti. Naipongeza sana Serikali, imefikia pazuri, tofauti na tulipoanzia; na hapa mlipofika mpaka leo mmepata mkopo wa Benki ya Dunia wa shilingi bilioni 345 na mmejielekeza nazo kwenye maeneo ya Dar es Salaam huko ili kuondoa migogoro kupitia dawati au Kliniki ya Ardhi. Pamoja na maeneo mengine, huko kwenye nchi yetu, mimi napongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili eneo, Waziri akiwa ni mdau wetu wa Dar es Salaam, pia naomba sana waongeze kasi. Kamati imesema ina shaka juu ya huu mradi wetu wa LTIP kama unaweza kwenda sawa kama tulivyokusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aongeze kasi kwenye madawati hayo ili mpaka tunafikia uchaguzi wetu Dar es Salaam, nami nishukuru sana viongozi wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam wako hapa, wametambulishwa, nashukuru, lakini watambue wazi sasa hivi hii ndiyo agenda yetu Dar es Salaam. Urasimishaji kama hatutoboi na kule nje patakuwa ni balaa. Hili ni jambo jema, nimemwambia tukiwa ndani na tukiwa wawili; na hapa nalisema wazi kwenye Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwa ujumla wake ni hili jambo la usimamizi wa ardhi na wawekezaji. Nchi yetu imefanya sensa kwa zaidi ya mara tano hivi; mwaka 1967, tumefanya tena mwaka 1978. Mwaka 1967 ilikuwa na watu milioni 12, mwaka 1978 milioni 17, mwaka 1988 tukafanya tena tukawa na watu milioni 23, mwaka 2002 tukafanya tena sensa tukawa na watu milioni 34, mwaka 2012 na mwaka 2022 tukawa na watu milioni 61. Kwa sensa ya mwaka 2022 Bara ina watu milioni 59.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kusema kwamba nimeona hoja ya wawekezaji, nami naipongeza sana Wizara, wamekuwa wanayo nia ya kuingiza wawekezaji 151 kutoka nje na wawekezaji 65 kutoka ndani, jumla yake ni takribani maombi 216, amesema Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana. Amezungumza kuwa hawa wa nje wana matarajio ya kumwingizia mtaji wa zaidi ya dola milioni 58.95 au bilioni 152. Hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo kwenye hao wa ndani ambao kwa sasa kwa mwaka huu wamewafikiria maombi yao kama 65 hivi. Kwenye historia ya nchi yetu kuanzia miaka ya 1980 tumekuwa na wawekezaji uchwara. Hizi lugha ngumu sana, nitakuwa najitahidi kujifunza Kiswahili. Nataka nimpe mfano mmoja, tunaye mwekezaji wa tangu mwaka 1984 mpaka 1987 alifika ndani ya kijiji Jimbo la Kibaha Vijijini kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mwakamo hapa, sisi wengine ni Wazaramo, wakati huo huo ni Waluguru; ndiyo humo humo kwetu kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwekezaji huyu ameingia akapewa ekari 200 vizuri tu. Alipopewa ekari 200 amekaa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15, anatoka anawaambia wananchi pale kwamba mimi nina ekari 2,500. Ekari 2500 ni kama vijiji viwili vya Lupunga na Kikongo, hatari sana. Vilevile wapo watu pale ndani ambao walikuwa ni sehemu ya ajira kwenye kulima mchicha kwenye ekari 200, na kesho yake wanakuja kuambiwa kuwa hata wewe tulikununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ni kwamba mwekezaji wa aina hii anafika anaulizwa, onyesha hati, hati haionyeshwi, anawaambia tu kwamba kuna hati. Sasa hebu onyesha pale nilipokuuzia mimi, anasema nilinunua mikorosho, kwangu hakuna mikorosho, nilipewa tu zawadi hata maeneo ambayo hakuna mikorosho, lakini kuna viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata juzi nilikuwa nasema hapa, kuwa nyie viongozi wakubwa, Katibu Mkuu na Waziri ni wa kuteuliwa, kila siku mnabadilishwa, lakini kuna wataalam wetu huku chini ambao ni changamoto. Sasa eneo kama hili nilitegemea RC wangu awe anafika ndani kwenye mashamba ili ajionee. Wanayetaka kumtoa leo ana mti wenye unene wangu, wanayetaka kumwingiza hajawahi kulima hata mchicha, wamempa leo ana miaka 40 ilhali sheria na sera inazungumza miaka 12. Wanasimamia sheria ya wapi? Kwa nini wananchi wanaonewa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiacha hoja hii, nilizungumzia sensa ili uweze kuona kwamba kama mwaka 1978 au 1988 ambapo kulikuwa na watu 23,000, leo watu 59,000 kwa mujibu wa mambo ya ardhi; watu 59,000 ambao ni vijiji viwili anawapeleka wapi hawa? Mheshimiwa Waziri hili analijua vizuri, atarajie kwenda kule akamwokoe Mheshimiwa Mwakamo na akakiokoe Chama Cha Mapinduzi ndani ya Wilaya yetu ya Kibaha Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nilizungumza kuhusu Fungu Na. 3 – Tume ya Taifa ya Mipango. Wengi wamesema lakini mimi nitapenda kusema kwa takwimu. Mimi nimekuwa nikishangaa sana, na hapa nizungumze tu kwamba napongeza ule mradi wa LTIP wa dola milioni 150, takribani shilingi bilioni 345. Pamoja na mambo mengi, mwaka jana tulimwambia Waziri mwenye dhamana aliyekuwepo wakati huo, Mheshimiwa Dkt. Angellina Mabula, tukasema hizi ni fedha nyingi, wameweka mipango mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie, wamekusudia kuingiza takribani vijiji visivyozidi 1,667 kwenye upimaji huu, tena baada ya maboresho, na vijiji hivi kwa thamani ya kupima kijiji kwa shilingi milioni 15, maana yake anatarajia kuweka shilingi bilioni 25, hazizidi hapo. Kwa hiyo, ndani ya hizo fedha zote za mkopo atatuambia hapa hajachukua zaidi ya shilingi bilioni 23, ndizo alizoziingiza kwenye kupima ardhi za vijiji, tutapima kweli!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Olelekeita amemaliza kusema hapa, na Mheshimiwa mwingine ndugu yangu wa Dodoma amezungumzia kuhusu nia njema ya kupima. Kama tungepima, tungetambua wazi kwamba kuna maeneo ya malisho yangehitajika na tungejua ya kilimo, makazi, uwekezaji, miundombinu ya barabara, huduma za jamii na hifadhi za misitu. Mheshimiwa Olelekeita ameuliza ni asilimia ngapi hii? Hatujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, kaka yangu Mheshimiwa Bashe, katika miaka yake miwili ametafuta shilingi bilioni 700 humu ndani. Ameanza na shilingi bilioni 249, mwaka wake wa kwanza tukamwekea shilingi bilioni 700, wa pili shilingi bilioni 900 na huu wa tatu shilingi trilioni 1.1, over seven hundred billion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jerry Silaa, miaka miwili anahitaji shilingi bilioni 120 kupima vijiji 8,400 alivyobakiza 120. Kwa nini yeye akose ndani ya Bunge hili? Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, capacity yake ya kufanya katika kipindi cha mwaka mmoja ni capacity ambayo inaweza ikampa takribani vijiji 1400; na ukimpa kwa shilingi milioni 15 maana yake anahitaji shilingi bilioni kama 20. Sasa katika shilingi bilioni 20 leo wanampa shilingi bilioni tano! Kwa shilingi bilioni tano aliishia kupima vijiji 300. Sasa si ataishia vijiji 400! Tunakwenda wapi? Anahitaji miaka 19.6 au miaka 20 kupima vijiji vyote 8,400 vilivyobakia. Haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge humu ndani kwa nia njema tumsaidie Mheshimiwa Rais, maana siasa ya Chama cha Mapinduzi zipo ndani ya upimaji wa vijiji kutokana na faida ya upimaji wa vijiji hivyo. Tukipima vijiji ndipo tutaona vizuri, hata lile jambo zuri la kilimo la Mheshimiwa Bashe lingeenda vizuri. Tutajua anaishia hapa, wafugaji wanaishia hapa, wawekezaji wanaishia pale, huduma za jamii wanaishia kule, eneo la misitu linaishia pale, malisho yanaishia huku. Tunaanzia juu tunashuka chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwenye vijiji. Kwa mwaka huu apewa shilingi bilioni tano kwa ajili ya maendeleo ili kupima vijiji 400, haimtoshi. Capacity yake ni vijiji 1,100 au 1,400. Tukimpatia shilingi bilioni 20 angalau atatumia miaka mitano kupima vijiji vyote 8,000 vilivyobakia. Hili ni jambo la msingi na jambo la muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nitumie tena nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kumwona yeye kama kamisaa anayetufaa kwenye Wizara hii. Anaendelea kuwa na macho makubwa ya kuona dira ya Taifa inakotaka kwenda. Tunaendelea kumwombea dua Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu ampe karama kubwa, aliyonayo iongezeke mara dufu na Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia hija na haja ya kuendelea kutuhudumia katika kipindi kinachokuja 2025/2030,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ISSA J. MTEMVU: …tupo kwa ajili yake na tutahakikisha kura zote zinakwenda kwake. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi, naunga mkono hoja kwa asilimia zote. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2021. Kabla sijachangia, nitumie nafasi hii kwanza nami nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kupiga kazi yenye mfano wa kutukuka kabisa kwenye nchi yetu, Afrika na dunia nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza kwa jinsi ambavyo amefanya uteuzi ulio mzuri. Katika jambo hili tulilonalo muda huu, ni uteuzi alioufanya juu ya Daktari Mheshimiwa Mchemba Lameck kuwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mhandisi Masauni na wale Makatibu Wakuu na Makatibu Wakuu Wasaidizi wawili. Kwa kweli wanaisaidia Wizara hii ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni-declare kabisa, ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti. Natumia nafasi hii kumpongeza sana Mwenyekiti wetu, kaka yangu Mheshimiwa Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini akiwa pamoja na Makamu Mwenyekiti wetu CPA Omar Kigua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo machache ambayo nitajaribu kusema. Eneo la kwanza ni sehemu ya tano ya mikopo, dhamana na misaada, Sura ya 134. Hapa marekebisho yamefanyika kwa kuweka kifungu kipya cha 13(b), lakini marekebisho haya kwenye Muswada yamefanyika ili kuruhusu Serikali kuweza kudhamini kampuni zetu au taasisi za Umma ili ziweze kukopesheka, lakini dhamana yetu tuliyoiweka pale ni katika kiasi cha share tunazozimiliki katika kampuni husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema. Hata kwenye sheria iliyopita siyo kwamba Serikali ilikuwa haiweki dhamana. Ilikuwa inaweka dhamana kwa kiwango cha asilimia 70 ya mkopo wote ambapo hiyo taasisi au hiyo kampuni inaenda kuchukua. Asilimia 70 tu ya mkopo wake wote, lakini sasa tumebadilisha tunaenda kuweka share zetu ambazo tunazo pale ndiyo kiwango ambacho tunakubali kuwekea dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme ukweli, kwenye hili CAG kwenye ripoti ya miaka mitatu mfululizo 2018/ 2019 na 2019/2020, amekuwa akisema juu ya kutokuwa na maadili timilifu, kutokuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, kutokuwa na nidhamu hata pale tunapokopesheka kusimamia mikopo tuliyopewa au dhamana na Serikali.

Kwa hiyo, nasema hili, kwa sababu pia umekuwa ushauri wa Kamati juu ya kuona jicho letu likae vizuri pale wakati tunatoa dhamana hizi ili zitusaidie tusije tukaenda chaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maangalizo ya msingi kabisa, maangalizo kama inflation (mfumuko wa bei), tukishatoa au tunataka kutoa dhamana, tuangalie hilo jambo. Muhimu sana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo issues za international pandemic. Umeona katika miaka miwili mfululizo tumedhuriwa sana na jambo la Covid 19. Kwa hiyo, kuna mambo kama haya lazima macho yetu yawe vizuri ili tusije tukaliingiza Taifa kwenye deni kubwa ambalo likishindwa kulipika linaenda kwenye deni la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niseme jambo hilo. Jambo la pili la marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Mifumo ya Malipo Sura ya 437. Hapa Marekebisho ya Muswada wa Sheria tumefanya katika Kifungu 46 (a) na dhumuni lilikuwa ni kuweka tozo katika kila muamala wa kutuma au kutoa fedha kwa kiasi kinachotofautiana tofautiana. Maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tumeweka wazi kabisa itakuwa ni shilingi 10 mpaka shilingi 10,000. Asubuhi hapa yupo mmoja amejaribu kutoa mfano na niuweke sawa. Alisema, kuna mtumaji na mpokeaji na mfano akaweka shilingi 10; ikitumwa kwa zamani, ina-charge shilingi 360; ikitumwa leo, ina-charge karibu 560. Huyo ni mtumaji; lakini mpokeaji wa leo, kwenye kutuma ile atapokea kwa shilingi 1,450 maana yake kuna hela ya kutolea, lakini kwa leo itakuwa imeongezeka 1,650. Yaani kuna maongezeko ya shilingi 200. Hapa ikawa ni issue sana asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, dhumuni letu kwenye hili ni kuongeza wala tusiwe na mashaka juu ya kuongeza shilingi 200, ndiyo lilikuwa dhumuni letu, lakini nini implication ya kuongeza? Naomba niseme, sababu ya kuongeza Watanzania na wana-Kibamba wasikie; moja, ilikuwa iweze kutusaidia kwenye elimu ya juu. Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa, katika mwaka 2019/2020 takribani watoto 11,000 wamefaulu na wameshindwa kwenda shule, lakini ametenga takribani shilingi zisizopungua bilioni 70 kuwasaidia watoto wa aina hii na ndio nia yetu sisi Wabunge wote. Tunaona watoto wetu wanafaulu wanashindwa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie, mimi sio wa zamani sana kwa umri wangu, lakini wakati mimi ninasoma, kufaulu ni kuchaguliwa tu, lakini wako wengi katika watoto 200 wanaenda 18 wengine wote wanaitwa wamefeli, lakini wala Serikali ilikuwa haihangaiki kuongeza madarasa, wala kutafuta hela nyingine za watoto wasome, lakini leo hii Serikali sikivu imesikia hii Awamu ya Sita, inaona jinsi gani kila mtoto anayefaulu apelekwe shuleni. Hii ni pongezi kubwa kwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, lakini pongezi kabisa kwa Waziri mwenye dhamana na timu yake yote kwa jinsi ambavyo wamejipambanua kuona watoto wetu wanaenda shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo eneo hilo tu, imetusaidia hata katika eneo la afya. Takribani shilingi bilioni 123 baada ya haya mambo kukusanywa, shilingi 10/= wakilipa kwa transfer au kuhamisha miamala hadi 10,000/= kuna shilingi bilioni 123 upande wa afya. Zinaenda kufanya nini? Watanzania wasikie, wananchi wa Jimbo la Kibamba wasikie. Kuna maboma karibu 10,000 ya vituo vya afya na zahanati, ambayo yamekaa huko hayajaisha. Kila Mbunge atapelekewa maboma 10. Hii ni faida kubwa, haiwezi kutokea bila fedha. Fedha ni lazima ziwe za kwao, zitokee ili waweze kuhudumiwa katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niliseme hilo, lakini lipo jambo lingine. Kwenye ushuru wa muda wa maongezi, kwa haraka, shilingi 10 hadi shilingi 200 implication ni ile ile. Hapa kazi kubwa imefanyika na wananchi wajue, wale wadau tuliowahi kukutananao wengine wanasema kuna hasara, shilingi 500 hadi shilingi 1,000 ni watu zaidi ya asilimia 94. Sisi tunasema sawa. Kama shilingi 500/= hadi shilingi 1,000 ndio wako asilimia 94 ya watumiaji, sisi tunaenda pale pale tukaweke hata shilingi 5. Eeh, shilingi 500 ya muda wa maongezi, hadi 1,000 sisi tunaweka shilingi 5 ili kila Mtanzania aone pinch ya kutaka kuona barabara nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesema Jimbo la Kibamba nje ya barabara zetu zile za juu pale kilometa tano, nyingine zote za udongo, watapataje barabara ya morrum? Kilometa 3,101; kilometa 319 zote ni za vumbi na udongo. Lazima walipe hata shilingi 5/= kama siyo shilingi 10/= ili tuweze kuyapata haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Sehemu ya Kumi na Nne, Sehemu ya Tisa na Sehemu ya Ishirini ya Sheria ya Bandari, Sura ya 116, Sheria ya Wakala wa Meli, Sura ya 415 na Sheria ya Mawasiliano, Sura ya 172. Ninataka kusema nini? Wengi wamesema hapa, tunayo TASAC, tunayo TCRA na tunayo TPA. Zote hapa, nimefurahi sana, Mheshimiwa Waziri umebeba hizi vizuri. Tumeenda kupeleka fedha zao zote zile mbichi kabla hawajatumia kwenye mfuko maalum pale BOT, lakini kuna maangalizo. Jambo ni zuri, tukasema tunawatangulizia miezi miwili halafu baadaye mwezi mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hapa na nilisema na kule, tujaribu kuwapelekea miezi mitatu mitatu wakajisimamie kutokana na changamoto nyingi walizonazo. Mbili kwenye nyingi ambazo wanazo kwa mfano wa TPA, tayari wameingia MoU wao na watu wa reli ili waone jinsi gani mashehena yanatoka kwenda kwenye bandari kavu. Sasa tukiwasimamia sana kwenye kufanya approval za fedha, zitatuletea shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni usafiri wa Dar es Salaam. Tunaona kuingia na kutoka bandarini ni changamoto sana ya foleni. Wana mipango mizuri kama bandari kuona jinsi gani wanatengeneza barabara zile, sasa hela tunawashikia tuzitoe kwa wakati ikibidi ili waweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kumalizia ni eneo la Sheria ya Ardhi, Sura ya 113. Nimefurahi sana, niliongea hapa wakati nachangia bajeti; na nimsifie sana, nilimwita Baba yangu Mkwe, Mzee Mheshimiwa Lukuvi, amefanya vyema. Tulikuwa tunaongelea premium hapa, ilikuwa asilimia 2.5 kuipunguza kwenye upimaji wa kawaida, lakini 1% kwenda chini kwenye upimaji wa urasimishaji. Zote kaziondoa 2.5% na ile 1% kupeleka 0.5%, pongezi sana Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii na Naibu wako, ni wasikivu kweli. Ninawashukuru. Maana yake nini? Wananchi sasa wanaenda kupata hati. Hati ambayo ni dhamana ya Serikali, dhamana ya Wizara kutoa Hati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zile kampuni zilikuwa zinaishia kupima na kuthaminisha tu, ambapo mlipunguza kutoka shilingi 200,000 hadi shilingi 150,000. Nyie sasa mmefanya vyema, mkatoe hati kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mhesimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja bajeti ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie...

NAIBU SPIKA: Samahani Mheshimiwa Issa Mtemvu kabla hujaanza kuchangia, Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, saa tano na nusu Mheshimiwa Spika anawaita kwa ajili ya kikao hapa lounge.

Mheshimiwa Issa Mtemvu, endelea.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara ya Maji, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Kibamba. Nitumie nafasi sana kuwapongeza viongozi wenye dhamana ya Wizara hii ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri, lakini pia dada yangu Maryprisca kwa kufanya kazi vizuri pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Sanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema mara nyingi hapa Dar es Salaam ina mafanikio makubwa sana kwenye suala la maji na taarifa zetu zote Mheshimiwa Waziri Mkuu amewahi kutuambia hapa, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa mara nyingi sana amekuwa akisema takwimu zaidi ya asilimia 92 Dar es Salaam ina maji. Nawapongeza sana, lakini nimekuwa nikisema hizo asilimia zilizobakia Dar es Salaam ni za Jimbo Kibamba. Kibamba kuna shida kubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi imeenda mingi sana ipo pale Kibamba imeenda kwa kaka yangu Mheshimiwa Jafo kule, mradi mzuri kabisa zaidi ya asilimia 97 umetoka Luguruni Kibamba. Umeenda kwa kaka yangu Profesa Kitila Alexander Mkumbo, akinamama wametuliwa ndoo kichwani kule Ubungo, lakini wananchi wa Jimbo la Kibamba wanaendelea kuteseka.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi iliyopo pale ambayo inaendelea nishukuru sana upo mradi mkubwa sana unatoka changanyikeni unaenda Bagamoyo lakini lipo tanki kubwa la lita milioni 5.6, liko pale Tegeta A, hili likitengenezwa vizuri, linaenda vizuri, likikamilika na usambazaji wa mabomba Kata nzima ya Goba wanaenda kupata maji salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi tunaoulilia sasa, ambao Hayati alipita mchakato ulikuwa tayari unaendelea, lakini akasema mfanye kwa dharura ni tanki kubwa pale Mshikamano, Kata ya Mbezi, mpaka sasa halijaanza, Mheshimiwa Waziri akija naomba nifahamu vizuri ni lini tanki
hili pale Mshikamano lisaidie wananchi wote wa Makabe, wananchi wa Msakuzi, wananchi wa Mpiji Magoe, wote waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri niliisikiliza, mmoja wa mradi uliotamkwa ni pale Kata ya Kwembe Kinyazi A, unazungumza milioni 33, mradi ule umekamilika mwezi Februari, ni ukweli hakuna kitu kama hicho. Bahati nimemwomba Mheshimiwa Waziri kwenda baada ya bajeti yake kupitishwa na amekubali na barua ipo mezani kwake, tutaenda tutafika pale ataona watu wanaendelea kunywa maji ya chumvi, lakini maji ya njano, maji mabaya kabisa ndani ya Kata ya Kwembe au eneo la Kinyazi A.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme juu ya changamoto kubwa katika Kata ya Kibamba maji yapo changamoto ni usambaji wa mabomba. Ipo miradi midogo midogo zaidi ya kumi na mbili toka mwaka 2020 mwezi Machi, bajeti iliyopita tena ya juzi yake ya mwaka 2019/2020 mpaka leo katika mabomba haya maji hayatoki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika Wilaya ya Ubungo, upande wa Jimbo la Ubungo, kwa bahati tulikuwa wote. Nafurahi sana kaka yangu Rwemeja pale anafanya kazi vema, lakini katika hili wanisaidie kutoa mabomba, yasambazwe kwa wananchi hawa niliotamka katika kata nyingi ili waweze kupata maji salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo kama Kibwegere, Kwembe, Msingwa, Malamba Mawili, Ukombozi na Msumi na kule Kibesa mbele ya Mpiji Magoe kwenda Mabwepande, kule kunataka tusambaze mabomba tu il mtu aweze kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua bado dakika moja au na nusu, nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri, katutengea bilioni 25, usambaji wa maji katika maeneo ambayo hakuna maji Jijini Dar es Salaam. Naomba hizi hela alizozitenga Waziri, hajasema zinakuja Kibamba ameweka kwa ujumla wake, asilimia 92 tayari Dar es Salaam, hakuna maji Kibamba, tupeleke Kibamba ili wananchi wapate maji salama na nyenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nikushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Maji kwa asilimia zinazotosha kwa sababu wananchi wanaenda kupata maji salama na ya kutosheleza. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwa hizo dakika tano. Sitoacha kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya wizara hii ya fedha na Mheshimiwa Naibu Waziri wake na watendaji wote wa wizara hii kwa kazi nzuri waliyofanya kutuletea taarifa hii ya hotuba ya bajeti na hali ya uchumi wa nchi yetu ambayo imeeleweka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nitajielekeza katika maeneo machache na hasa katika mazingira ya Sera ya Mapato pamoja na Sera ya Matumizi. Katika Sera ya Mapato pamoja na kuendelea kutekeleza mpango mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji wa viwango Mheshimiwa Waziri ametuelekeza eneo la mapato ataliangalia sana kwenye maeneo ya kodi, tozo na ada mbalimbali na hapa ndiyo nataka kusema, moja ikiwa ni kodi ya majengo sura 289.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka sana nakubaliana sana, zilikuwepo option nyingi sana, lakini hii moja aliyoichukua Mheshimiwa Waziri yakutumia mifumo ya LUKU ni moja ya utaratibu mzuri sana kati ya taratibu nyingi ambazo zingeweza kuwepo. Na hii kwa sababu ameona uchumi wa sasa unakwenda na teknolojia ya TEHAMA kwa hiyo, akaona ni vizuri tuelekee na njia hiyo nami nampongeza sana. Lakini pia limesaidia wale ndugu zetu wa Chama chetu cha Mapinduzi walikuwa wanatumika vibaya sana katika eneo hili bila tija yoyote kwa hiyo sasa kwa njia hii wanaenda kupumzika na fedha nyingi tutazipata katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia eneo la Ukaguzi wa Umma sura 418, Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa nia ya Serikali kupeleka CAG akakague makampuni yetu yale ambayo Serikali ina HISA chache minority interest ni jambo zuri, lakini linachangamoto kwa haraka. Moja ya changamoto; linaweza likatuletea shida kwenye uwekezaji, hizi minority interest tulizonazo kwenye makampuni yale, yale makampuni yana utaratibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili ambalo ni changamoto; ni katika eneo la Bodi ya Directors, yale yanasimamiwa na bodi zao, bodi zao zina taratibu zake, kwa hiyo nia yetu nzuri kupeleka CAG akafanye kazi mle, lakini hebu tuone kama hizi bodi zao zina uwezo wa kupeleka KPMG na wengine wengi priest house Water, Beroke and Tuch na wengine hebu tuone katika maangalizo hayo ili tuweze kwenda sambamba. Lakini tunajua mpaka sasa CAG mwenyewe hajaweza kukamilisha asilimia 100 ya ukaguzi wa yale ambayo yanatakiwa kwa Mujibu wa Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema pia maeneo mawili ya mwisho katika eneo la mapato, moja ni eneo hili la ushuru wa barabara na mafuta, jambo nzuri sana tumeelekeza shilingi mia kwa petrol na diesel sisi tunalifurahia kwa sababu tunaenda kuongeza fedha takribani bilioni za kutosha ambazo zitaenda kutusaidia kwenye barabara zetu za TARURA. Na hii lazima niwaambie wananchi wa Kibamba wafurahie hili walifurahiye jambo hili. Kwa sababu barabara za jimbo lile ndiyo barabara changamoto kwa Mkoa wa Dar es Salaam bilioni hizi zaidi ya 399 zikiongezwa mule maana yake TARURA watapata fedha na fedha zaidi ya bajeti waliokuwa wamewekewa awali, sasa wananchi wategemee barabara zao zitapitika kwa wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo tozo ya posta na mawasiliano hii ni shilingi 10 hadi shilingi 200 hii nataka niwaambie wananchi wangu waielewe vizuri sana hii inatija na itatusaidia sana, itatusaidia kwa sababu fedha hizi zinaenda kuongeza bajeti ya maji na ndiyo Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia 92 za mafanikio katika wizara, lakini asilimia 8 hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikisema hapa hizi ni shida ambazo ziko ndani ya Kibamba, sasa wakikubali kulipa hizi shilingi 10 hadi 200 maana yake tunaenda kuongezewa zaidi ya bajeti iliyokuwa imepangwa katika wizara hii na maji yanaenda kupatikana vizuri ndani ya Kibamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upande wa sera ya matumizi kwa haraka, nitasema kidogo hapa juu ya fedha zinazotumika mwisho wa mwaka kuzibakiza ndani ya Sekretari zetu za Mikoa kama tulivyokuwa tumeomba sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge jambo nzuri na mimi nalikubali, linamaangalizo. Sheria iko vizuri sheria ya fedha Ibara ya 29(1) hadi (5) inazungumzia unspent amount katika mwisho wa mwaka wa fedha ni vizuri zirudishwe katika mfuko mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunasema hazitorudi so zimekwenda kwa kuchelewa vizuri lakini regulation ikatueleze vizuri na ije hapa kwenye Bunge lako Tukufu ili tuweze kuweka vizuri muda sasa ambao itaendelea kubaki kule ili baada ya muda fulani ikishindwa maana ilikuwa tarehe 15 kabla ya mwaka kufungwa watoe taarifa kwa Pay Master General, sasa itaongezwa zaidi hata ya mwezi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia inaleta sura ya kutumia vibaya hizi hela ndani ya deposit, vizuri regulation ikija hapa tuiunge mkono katika mazingira ambayo yatasaidia utimilifu wa nidhamu na maadili ya matumizi ya fedha za Serikali. Najua muda ni mdogo sana lakini niseme vizuri juu ya jambo la DMDP II Dar es Salaam nimeliona Mheshimiwa Waziri kalisemea vizuri ametenga dola za Kimarekani milioni 120. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naomba niunge mkono hotuba ya Waziri na bajeti ya Serikali ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Malizia sentensi ametenga milioni 120…

MHE. ISSA J MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Dollar za Kimarekani kwa ajili ya Mto Msimbazi na kutengeneza guidon katika hili, lakini wajielekeze sasa kuna Mto Mbezi kuna shida sana Mheshimiwa Waziri katika bakaa utakayokuwa nayo najua re-allocation zinawezekana utusaidie na Mto Mbezi ndani ya Jimbo la Kimbamba nakushukuru sana kwa kuniongezea dakika moja hii ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2022/2023. Nitajielekeza katika maeneo mawili tu muda ukinifaa sana; eneo la mapato katika sehemu ya mawasiliano na eneo lingine ni mwenendo wa riba hapa nchini na hasa eneo ambalo halijazungumzwa na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya; sehemu kubwa wamesema wengine, lakini kwa jinsi anavyotuheshimisha kwenye majimbo yetu.

Pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana kwa usikivu kama ambavyo nimeendelea kusema, Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi nzuri ya usikivu anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru sana Mheshimiwa Spik ana Naibu Spika. Kwa kweli sisi tunaendelea kujifunza sana kila siku na kila wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Kamati ya bajeti mimi nikiwa ni Mjumbe wa Kamati inayoongozwa na kaka yetu Mheshimiwa Daniel Sillo na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Omari Kigua, tunaamini Waheshimiwa Wabunge wameiona na wameipongeza, nasi tumefarijika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mchango wangu, katika eneo hili la makampuni ya simu, kuna changamoto sana. Tunakubali sana kwamba eneo hili la mobile sectors limechangia sehemu kubwa sana kwenye nchi yetu. Kwa uchache sana, katika kipindi cha miaka miwili wamechangia takribani Dola za Kimarekani milioni 441, takribani shilingi trilioni moja za Kitanzania. Vilevile wana mchango kwenye GDP takribani asilimia 5.2 na ziada ya mchango wao kwenye ajira kwenye sekta hii ni takribani watu 1,500,000. Hii ni karibu asilimia 2.6 ya idadi ya watu wetu wote wa takribani watu milioni 60 hadi 64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo hapa ambalo nataka kusema na kubwa ni eneo linaloonekana kuna upotevu mkubwa sana wa mapato katika eneo la mawasiliano. Liko jambo ambalo ukiliangalia kwenye takwimu za miaka karibu nane, tisa; mwaka 2013 hao wenzetu kwenye sekta hii waliwahi ku-declare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa average revenue per user; kiwango cha mtu moja moja katika kipato anachokipata kwa haya makampuni; kwa mtu mmoja kwenye idadi ya watu wote, ilikuwa ni takribani dola 5.5, kama 12,000 hivi. Katika kipindi hiki cha miaka miwili iliyopita, wame- declare tena punguzo takribani dola 2.3, yaani kama shilingi 5,000 au shilingi 6,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali linakuja hapa. Huo wakati ambao wanasema hayo kwa mtu average revenue per user ni 12,000, tulikuwa hatuna data wala tulikuwa hatuna mambo ya kuhamisha miamala ya kifedha. Leo tunajua wote idadi ya watu ni zaidi ya asilimia takribani milioni 60, 64. Nao wanasema takribani watu asilimia 42 ya population nzima wameji-engage kwenye mobile service. Sasa unaiona siyo chini ya milioni 30, lakini punguzo hili linatoka wapi kama leo tume-engage kwenye data, kwenye mobile transfer (miamala ya fedha)? Iko shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nimejitembeza kwenye nchi kadhaa kwenye jambo hili, nikakuta takribani nchi saba ziligutuka juu ya wizi mkubwa au upotefu wa mapato makubwa katika eneo hili, wakafanya Forensic Audit. Nchi kadhaa, mimi nitataja chache sana; baada ya kufanya Forensic Audit wamekuta upotevu mkubwa sana wa mabilioni ya namba. Hizi ni nchi kama Ghana, Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi na nyingine nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwepesi, nchi nyingi zimeanza kufanya ukaguzi huu kuanzia mwaka 2003. Ndugu zetu Kenya na Uganda walifanya mwaka 2003. Uganda walifanya mwaka 2009. Hawa walikuta upotevu wa zaidi ya asilimia 300, increase; na waliweza kurudishiwa fedha zilizopotea kwa Kenya tu ni zaidi ya shilingi bilioni 600; kwa Uganda ni zaidi ya shilingi bilioni 600 na yenyewe.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa haraka, Ghana ambao juzi, mwezi wa Nane mwaka 202,1 wamefanya Forensic Audit kwenye data na mobile money transfer na wamemaliza juzi tu, wamekuta upotevu wa zaidi ya asilimia 300; Dola za Kimarekani milioni 418, hizi ni takribani shilingi trilioni moja za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, sisi huwa tunachelewa sana. Leo Serikali ikaone inayo sababu ya kwenda kufanya Forensic Audit kwenye miamala hii kwenye haya makampuni yetu ya simu. Ni ukweli, wanafanya kati ya miezi mitatu hadi sita, wala siyo muda mrefu, watakuja kutuambia kwenye Bunge lako hapa ni kiasi gani tumeokoa kwenye declaration zao za revenue kila mwaka? Ni kiasi kikubwa sana tunapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika chache kama nitaweza, niseme kidogo juu ya eneo hili la mwenendo wa riba. Maeneo mengi wamesema BoT imefanya kazi nzuri, Serikali imeingiza shilingi trilioni moja ili kupunguza zile riba na mambo mengine. Nataka kusema kuna wizi mkubwa hapa, nitumie tu hiyo lugha. Katika eneo hili wananchi wanaumizwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu viwili vinaitwa: moja, credit life insurance na nyingine ni takeover loans penalties. Niseme kwa haraka hili la kwanza, tutagundua Waheshimiwa Wabunge wote, tukichukua mkopo tunakatwa credit life insurance at once. Mkopo utachukua wa miaka mitano, lakini tunakatwa bima ya miaka mitano mara moja. Huu ni wizi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikilisema hili, linaenda sambamba na suala la takeover loans penalties. Hawa Waheshimiwa Wabunge hapa wamechukua mikopo inawezekana kwa asilimia 13 au 14, lakini kuna benki nyingine zinatoa mikopo kwa asilimia 12. Katikati ya mwaka, katika mkopo wangu wa miaka mitano unapoamua kuuhamisha, unau-takeover, unau-liquidate pale, unauhamisha kwenye benki nyingine, kwa sababu ya faida ya difference of interest rate. Wanaku-charge asilimia tatu hadi tano bila wewe kujua. Hii ni kitu kibaya sana. Maana yake customer wanaumizwa na haki yao ya msingi ya kuhamisha mkopo wao kwa faida ya interest rate walizoziona kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili, sana ni mambo mawili; moja, atoe clear directive kwamba hakuna penalty ambayo inastahili kulipwa wakati mteja anahamisha mkopo wake. Hili muhimu sana, itawasaidia Watumishi wa Umma, itawasaidi Waheshimiwa Wabunge na wengine na wengine wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hizi insurance, kama nimechukua mkopo unanikata miaka mitano kwa mara moja, leo nauhamisha mwaka wa pili, napeleka kwenye benki nyingine, naenda kukatwa insurance tena, wakati wewe umechukua yote ya miaka mitano. Kwa nini isifanywe kwa pro-rata; miaka yako miwili chukua, nikihama miaka mitatu kwenda benki nyingine, kule nikakatwe makato yale yale ambayo nilikuwa nimeshayapeleka kwenye benki ya awali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Huo ulikuwa mchango wangu wa leo. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie sekunde hii moja kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 42, lipo jambo linazungumzwa na Kamati juu ya Daraja la Tanzanite. Daraja hili ni furaha ya Tanzania kupata mkopo wa dola milioni 121, shilingi za Kitanzania kama bilioni 243. Hili ni daraja zuri lakini tunatambua umuhimu wa daraja lile limekuwa ni mbadala wa daraja lililokuwepo siku zote pale ambalo limekuwa likisaidia wananchi, lakini vilevile palikuwa na foleni kubwa.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba hili siyo daraja la kwanza kupatikana kwenye nchi yetu. Dar es Salaam lipo daraja lingine zuri Kigamboni ambapo mwaka 2015 lilijengwa chini ya Shirika letu la NSSF kwa shilingi bilioni 214 tofauti ya bilioni kama 30 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wengine waliotangulia kusema leo kwamba tunaendelea kuwa na mshangao juu ya faida zote ambazo zinaonekana juu ya daraja lile. Daraja la Kigamboni toka limejengwa kama mbadala wa wananchi wa kule tayari limewekewa tozo, wananchi wale upande mmoja walikuwa wakilipa tozo za kawaida vilevile daraja lilipokuja kuwa mbadala wakaendelea kulipa tozo. Sababu kubwa ilikuwa ni fedha zetu wenyewe kutoka katika Shirika letu la NSSF ambalo limewekeza pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la sasa hivi ni mkopo ambao tunajua bilioni 243 linaenda kuwa deni la Serikali, deni ambalo kila Mtanzania ana nafasi ya kulilipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sababu kama mbili tu au tatu za kutofautisha watu wa Kigamboni na lile daraja la pale na wale watu wanaopita, kuna hali kama mbili. Moja, ni umasikini. Ukiangalia upande wa Kigamboni, viashiria vyote vya kimasikini vipo kule. Hali ya umasikini, hata matumizi ya kaya kwa siku, utaweza kutofautisha na watu wa Oysterbay, Masaki na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama waliotangulia walivyosema na kushauri, ni vizuri. Mimi nishauri katika eneo hili; kama Kigamboni katika nyanja zote hizo mbili, madaraja yote mawili, wanalipa tozo, basi na huku walipe tozo. Option ya pili, kama ni lazima sana, au sisi ambao hatujui kwa huku hawalipi na kule wanalipa, basi wananchi wa upande wa kule kwenye kaya nyingi za masikini wasilipe tozo katika upande mmoja; na upande wa daraja waendelee kulipa yale magari yanayopita. Inaweza ikawa ni njia nzuri ya kusaidia malalamiko makubwa ya watu wa Dar es Salaam na wananchi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze sana kwenye upande wa TARURA. Wakati wa nyuma hapa kidogo katika kutafuta mapato kwa ajili ya barabara zetu vijijini na mijini chini ya TARURA, tuliingiza tozo ya mafuta (petroli na dizeli) shilingi 100/=, tukatarajia kupata shilingi bilioni 322. Ni kweli katika fedha hizo mpaka sasa zimeshatumika, zimetolewa takribani 43%, jambo zuri na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha hazitoshi. Mpaka juzi hapa, Bunge letu hapa likatoa kauli, TARURA waje na tathmini ya nchi nzima kwa kuokoa hali ya barabara zilizoharibika. Tathmini imekuja na Kamati imeeleza, takribani shilingi bilioni 119 wanazihitaji, lakini shilingi bilioni 119 wanazitoa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 wamepangiwa shilingi bilioni saba na nyongeza ya shilingi bilioni moja ambayo wametoa katika reallocation ya ndani ambayo kwa kuongezea wamefikia shilingi bilioni nane. Hii ndiyo dharura kwenye bajeti ambayo tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona hali ya hatari ambayo tunayo kwenye barabara zetu. Sasa Kamati inaeleza, ongezeko ni shilingi bilioni 111, zinatoka wapi? Maana yake nini? Zinaenda kudhuru bajeti iliyopitishwa na Bunge hili. Shilingi bilioni 111 ni fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwa sababu hatuwezi kuendelea hivi kudhuru bajeti ambazo tunakaa kama Taifa tunapitisha, lakini leo tukafanye reallocation between votes, tukanyang’anye katika mafungu mengine ya Wizara ili tuweze kufanya jambo la dharura katika hili. Sasa, nini cha kufanya? Kuna mambo mawili: Moja, katika eneo hili ni vizuri tupeleke fedha zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye bajeti yetu inayokuja 2022/2023 kama dharura; eneo la pili kwa sentensi moja, ni kutafuta vyanzo vingine. Dar es Salaam kule tunahitaji GN…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia malizia.

MHE. ISSA J. MTEMVU: …ije haraka ili tuweze kutatua barabara za ndani kama ilivyo miji 45 katika mikoa mingine ambavyo wametatuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Nyongeza ya Bajeti ya Mwaka 2021/2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye jambo hili.

Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kweli bila kusema maneno mengi mama anaupiga mwingi kama taarifa ya Kamati yetu inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli pongezi zangu nizimalizie kwa sehemu mbili moja Wizara ya Fedha wamekuwa wasikivu, wizara hii kupitia Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Chande, lakini pia wakiongozwa na Katibu Mkuu Emmanuel Tutuba kwa kweli ni wasikivu wameendelea kufanya kazi vizuri na kamati lakini mpaka kufikia katika makubaliano haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukweli hata Kamati yetu wenyewe nimpongeze sana Mheshimiwa Daniel Sillo, Mwenyekiti wetu wa Kamati lakini na Makamu Mwenyekiti CPA Omar Kigua wanatusimamia vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo tuko hapa nakubali kabisa hoja hii na naomba Waheshimiwa Wabunge wakubali kuidhinisha hizi trilioni 1.3 iweze kupata nyongeza ya ukomo wa bajeti ya mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, tulikuwepo hapa tukaidhinisha bajeti ya mwaka 2021/2022 ya shiingi trilioni 36.6. lakini ni ukweli nyongeza hii ya trilioni 1.3 inatupekeka kwenye ukomo wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022 kuwa trilioni 37.98. Hili ni jambo la kisheria chini ya Sheria ya Bajeti ambayo imesomwa kifungu cha 43(3), lakini vilevile, na Katiba yetu Ibara ya 137 Katiba ya nchi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni jambo lipo kwa mujibu wa Sheria ni jambo ambalo ni kubwa na ni zuri kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, mkopo huu umesemwa kwenye Kamati, mkopo huu ulikuwa uwe na riba ya asilimia 1.5 lakini kwa jinsi ambavyo mama yetu amekuwa anao uwezo wa ushawishi mkubwa imeenda kutolewa hii riba ya 1.5 mpaka sifuri. Sasa mkopo huu hauna riba yoyote, lakini si hivyo tu mkopo huu mrejesho wake uwe wa miaka mitatu, lakini ameweza kujadiliana mpaka mrejesho (payback period) imeongezwa mpaka miaka mitano. Hili ni jambo kubwa lakini lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukweli leo Watanzania wote wanajua juu ya mkopo wa trilioni 1.3; kila mmoja ukimwambia anajua, hatusemi ya nyuma walikuwa wanajua, lakini kuna uwazi mkubwa sana ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita. Tumpongeze sana Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini matumizi; si kawaida leo kila Mtanzania na wale wananchi wa Kibamba wanajua maana ya trilioni 1.3; kwenye eneo la afya zimepelekwa zaidi ya shilingi bilioni 466, Watanzania wanajua zaidi ya ICU 67 zinaena kupelekwa huko, lakini kuna ambulance za advance karibu 20 lakini ninaambiwa na ambulance basic za kawaida karibu 253, si jambo dogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye elimu wamesema wengine leo madarasa 15,000; madarasa 12,000 ya kawaida ya sekondari, lakini madarasa 3,000 ya shule za msingi shikizi; si jambo dogo ndani ya madarasa hayo wananchi wa Wilaya ya Ubungo wanajua madarasa 151 yameenda katika Wilaya ya Ubungo; katika Jimbo la Kibamba madarasa 104 si kitu kidogo Mbunge wao ameyatembelea yote, ameyaona yote na kwa kweli namshukuru sana Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaambiwa viko VETA 26 kwenye Wilaya zote na VETA kubwa za Kimkoa sita; si jambo dogo hizi zikikamilika wananchi wa kibamba katika eneo tuliopewa na Mheshimiwa Rais tunaenda kupata kwenye bajeti ya 2022/ 2023 VETA mpya kwa sababu zilizokuwa zinajengwa zote zitakuwa zimepata fedha na sasa zitakuwa zimekwenda mpya na sisi tunaomba wananchi wa Kibamba kupewa VETA nyingine. Hii ni kazi kubwa alizozifanya Rais na kufungua hizi fursa katika majimbo mengine. (Makofi)

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Jerry Silaa.

T A A R I F A

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa mzungumzaji na Bunge lako taarifa siyo Jimbo la Kibamba peke yake, kwenye Jimbo la Ukonga jumla ya madarasa 129 sawa na shilingi bilioni 2.5 zimejengwa na wananchi wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu malizia mchango wako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, hayo ndiyo mambo makubwa ya Mama Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais bora kabisa, Rais bora Afrika na duniani ndiyo maana hayo mambo unayaona katika kila jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nasema la maji; zimepelekwa shilingi bilioni 139.4 lakini ukweli wananchi wa Wilaya ya Ubungo Jimbo la Kibamba wanajua kwenye zile shida za maji tumeshasaini mkataba wa shilingi bilioni 5.4 pale Mshikamano. Sasa tunataka nini watanzania wanataka nini wanaenda kuyaona maji, shida ya maji inaenda kuisha katika muda mfupi mambo ya utalii Covid-19 ilituletea shida kwenye utalii lakini zimepelekwa fedha za kutosha karibia bilioni 90.4, sasa hivi mambo yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kumaliza ni kweli tunalo ombi hapa la shilingi bilioni 693 kama nakisi sehemu ya pengo katika bajeti yetu tuliyokuwa tunaenda nayo ili kujazia tunaomba Waheshimiwa Wabunge mkubali kukopa kiasi hiki katika mkopo nafuu wa shilingi bilioni 693 ili mambo yazidi kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie kwenye ripoti hizi ambazo zimewasilishwa ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitasema kidogo kwenye ripoti ya PAC katika eneo ni moja tu la usimamizi wa mikataba na athari zake katika matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamejadili katika eneo hili kwa kugusia jinsi gani mikataba kwenye nchi yetu haiheshimiwi; jinsi gani mikataba ambayo imefungwa vizuri pasiposhaka na wataalamu wetu, kwa maana ya wanasheria wabobezi (land lawyers) ikija katika usimamizi wake inaleta shida katika nchi yetu. Mifano iko mingi, michache tutaisema lakini mingine imesemwa na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ripoti ya CAG ametoa mifano mingi sana ya jinsi mikataba ilivyoshindwa kusimamiwa vizuri mpaka fedha za umma zimepotea nyingi sana. Nitasema mifano kama miwili;

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na mikopo mingi sana ambayo imekuwa inakuja baada ya makubaliano ya nchi yetu na mashirika ya kimataifa. Pamekuwa na mradi mikubwa ambao ulikuwa unaendeshwa chini ya TANROAD, Mradi wa Uwezeshaji wa Biashara na Uchukuzi Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni huzuni sana, fedha tunazikopa nje, nyingi sana. Kama ambavyo tunaendelea kukopa fedha nyingi, na mimi nakubaliana kabisa na taratibu za kukopa, na hasa hii mikopo ambayo Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa awamu ya sita ambaye tunaenenda naye. Mikopo mizuri yenye tija na isiyo na riba kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo masharti ya kimkataba ambayo pale ambapo tunakubaliana kuchukua mikopo mikubwa kwa ajili ya kufanya miradi hasa ya barabara ambayo imetolewa na CAG; katika mradi huu niliotamka, Mradi wa Uwezeshaji wa Biashara na Uchukuzi Kusini mwa Afrika, palitokea malipo ya ada isiyo na tija ya ada ya huduma ya kifedha ya zaidi ya dola za kimarekani laki moja na ishirini na tisa mia tisa na sitini na nane. Hizi ni takriban milioni mia tatu na hamsini, zilipotea tu, na tulifikia tukalizilipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tulizilipa? Tulipewa mkopo fulani mkubwa ambao ulituambia mpaka kufikia tarehe 30 Julai, 2013, miaka kadhaa, zaidi ya kumi ilitakiwa tuwe tumekamilisha miradi husika. Lakini kwa sababu ambazo, inawezekana design ya mradi ilikuwa na changamoto, na sababu zingine ambazo hazina mantiki kabisa tunashindwa ku-meet yale masharti ya kimkataba. Matokeo yake nini; hii ilitokea, bakaa ya fedha ambayo imekopwa; katika bakaa yoyote ambayo ulitakiwa uitumie kwa kipindi fulani na ukashindwa kukitumia makubaliano ya mkataba ni kwamba utakatwa robo ya tatu ya asilimia moja ya kiasi ulichoshindwa kutumia. Hii ni aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikabaki Dola za kimarekani milioni kumi na saba laki tatu ishirini na tisa mia moja themanini na nne na nukta kama ishirini, na taarifa ya Kamati inatuambia hivyo. Ukitafuta robo tatu ya aslimia moja ya fedha hizo dola milioni 17 unapata dola 129,698.90, zaidi ya milioni mia tatu na hamsini; na tukazilipa, tunalipa tu halafu tumetulia. Aliyesababisha damage hii kama nchi hakuna chochote alichofanyiwa na hakuna lolote lililoendelea, business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu; mfano mwingine CAG anatuambia wa kushindwa kusimamia mikataba yetu ambayo wenyewe tumeiingia, kulikuwa kuna ongezeko la gharama za fidia ya kiasi cha shilingi bilioni 22.35, na hii ni kutokana na kutolipwa kwa kaya 1,125.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1997 Wizara iliyokuwa ya Uchukuzi na Mawasiliano Iliingia na Mkandarasi Mshauri kuhusu jinsi gani ya kuongeza Airport yetu Julius Nyerere International Airport. Katika ule mchakato wa kuongeza kulikuwa na kaya nyingi sana zilitakiwa zilipwe mabilioni. Kiukweli niishukuru Serikali yangu Sikivu, kwa kiasi fulani ilifanikiwa kulipa.

Mheshimiwa Spika, lakini ni ukweli pia katika mwaka ule kwa sababu za kibajeti hatukufanikiwa kuwalipa wote au kulipa fidia zote, tukabakiza wananchi 1,125, ripoti ya CAG inatuambia hivyo. Wale wananchi walitakiwa kulipwa bilioni saba za Kitanzania; lakini tangu mwaka huo hadi tathimini ya mwisho inafanyika mwaka 2020 unaweza ukaona hakuna chochote kilicholipwa wakati wote. Msimamizi wa mkataba hayupo na hajui kama kuna watu aliwaacha pending hajamalizana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kanuni ya 13 (3) ya Kanuni za Ardhi, Uhakiki na Thamani ya Fidia na Ardhi ilibidi wajielekeze kwenye kufanya tathimini upya ili kujua bilioni saba zimeongezeka kiasi gani, zile za wale watu wetu 1,125 ambalo ni jambo jema, ni takwa la kikanuni. Tulipoenda wakasema riba ni asilimia sita, tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2019, lakini ilibidi riba iongezeke, ikatupeleka mpaka wakafanya uthamini wa mara kwa mara. Ilikuwa jambo jema sana ili wananchi wetu wasionewe, ikatufikisha kwenye 29,768.029,951 zaidi ya bilioni 22; nataka kusema jambo hapo. Si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tumefika wakati tunasema tuna mradi X tunataka kuutekeleza kama nchi, huu wa kufungua airport yetu wakati huo tulifikiri ni jambo jema. Maana yake mhandisi mshauri alishasema pana idadi ya watu hawa, tunajua maeneo ya pale, lakini hawa watu wanatakiwa walipwe kiasi hiki. Kama tunakwenda maana yake tuko tayari kwa fedha za ndani na fedha za nje. Sasa kama tumekaa kutoka bilioni saba hadi bilioni 29, tunaambiwa na CAG, bilioni ishirini na mbili nukta kadhaa ni deni mpaka sasa tunavyoongea, sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamesema hapa, hii ni kiashiria kibaya sana. Wataalamu wetu wanakaa wanajua kuwa wanatakiwa wasimamie mikataba ile lakini hawaisimamii kwa wakati lakini wanaacha. Je, wanaacha kusudi ili riba iongezeke? Au wanakuwa na sababu zipi? Sasa tumetoka billion saba hadi bilioni 29. Bilioni 22 linakuwa deni.

Mheshimiwa mwenyekiti, hii sio sawa; fedha za Watanzania zinapotea. Bilioni 22 tungezipeleka kwenye Jimbo la Kibamba. Leo mimi ninalia maji hayatimii, barabara hazipo chini ya kilomita tano za TARURA na TANROAD hakuna. Huduma nyingine ni changamoto sana. nimpongeze sana Mama Samia anatusaidia sana, tunaona huduma nyingine za afya na elimu zinakuja, lakini tunashida kubwa bado. Maji hatuyaoni maeneo mengi, na ninasema kila siku, barabara bado sana, idadi ya watu Dar es salaam ni zaidi ya milioni nne na nusu. Sasa, hivi tunafanyaje? Sio sawa, lazima tuiseme.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hizo sababu mbili za kushindwa kusimamia mikataba ya nchi yetu vizuri. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi nichangie huu mpango wetu, Mpango wa Tatu wa maendeleo katika nchi yetu. Pamoja na muda nisiache kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na kuendelea kumpa moyo mkubwa kabisa kwamba kazi anayoendelea kuifanya kwenye nchi haina mfano na tunaendelea kumuombea kwa Mungu aendelee kumpa afya njema ili Watanzania waweze kuendelea kuona matunda yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitasema jambo moja tu ambalo Serikali imeanza kulifanyiakazi lakini naona hatuendi nalo kwa speed nalo ni eneo la usimamizi wa maafa nchini. Nikitambua tayari Kifungu cha 35 cha Sheria ya Bajeti Sura ya 439 kinaeleza wazi juu ya kuanzishwa kwa Mfuko huu, lakini ukweli Serikali hapa kupitia Kamati ya Kudumu ya Sheria na Katiba Mwezi Febuari 14, 2022, Kamati iliwasilisha hapa juu ya Mapendekezo ya Muswada wa Sheria kwenye jambo hili. Septemba mwaka huu 2022 Waziri Kaka yangu Simbachawene naye aliwasilisha Muswada wa Sheria wa Usimamizi wa Maafa Nchini, ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba bado Mfuko huu aujaanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti. Lazama tukubaliane inawezekana umuhimu wenzetu hawajaujua bado. Kwa nini tunahitaji kuharakisha mfuko huu kupatikana? Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge, juu ya majanga mengi nchi ambayo tumewahi kuyapata katika kipindi cha miaka kadhaa. Mwaka 1996 Tarehe 21, Mei, tulipata maafa makubwa kupitia MV Bukoba, wananchi wanajua. Ni kweli kupitia taarifa ya Jaji Robert Kisanga tuliweza kupoteza wananchi wetu, watoto wetu, wazee wetu 391 dhidi ya waliookolewa 114 tu, unaweza ukaona hili ni janga!

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu ni juzi tu MV Spice tarehe 10 Septemba 2011, zaidi ya maiti zilipatikana 243 lakini waliokutwa hai ni 900 tulipoteza hawakupatikana kabisa zaidi ya 1,370 hata kupatikana. Niwakumbushe tena kwa haraka kupitia maji tu Bahari na Maziwa ajali kubwa ya MV Skagit mwaka 2012 wananchi zaidi ya 222 walipoteza maisha, kuna MV Julius mwaka 2017 pia MV Nyerere mwaka 2018 ambayo ilikuwa inatokea Bungarara kuelekea kwenye Kisiwa cha Ukara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya majanga ni makubwa kama nchi. Tumepoteza ndugu zetu wengi, nini maana ya Mfuko huu? Mfuko huu utatusaidia pale ambapo haya majanga ambayo yameendelea nimeyataja ikijumuishwa hata hiyo ya juzi ya ndege, tungeweza sasa hapa kuona fedha za haraka za dharura ambazo zingeweza kusaidia hata kupeleka Jeshi letu la Navy la Uokoaji, katika maeneo ya kimkakati na tukaweza kuwawezesha kupitia Mfuko huo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile moto. Masoko yetu mengi, Soko la Kariakoo tumelikarabati kwa Billion 32, Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda pale kukarabati tu, Soko la Mwanjelwa - Mbeya, Soko la Ilala kwa Naibu Spika lakini hata Mwenge zaidi ya bilioni 50. Madhara yake ni nini kama hatuna Mfuko huu? Madhara yake mpango wa kama huu na bajeti zetu tunazoziweka kila mwaka zinaenda kuharibiwa, maana yake yale tunayotarajia kuyafanya activities zinazotakiwa kufanywa haziwezi kufanyika. Kwa sababu dharura imekuja hatujajipanga nayo tunaenda kuchukua hela maana yake ni activities nyingine zinaweza zisifanyike. Kwa hiyo, ni maombi yangu sana Mfuko huu ninajua nia na dhamira ya Serikali ndiyo maana tumeanza na sheria basi tuelekee kwa sababu ndiyo nia yake kwenda kuanzisha Mfuko huu tukaanzishe haraka ili tuweze kufika sehemu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mengi watu wanayajua. Mlima Kilimanjaro zaidi ya siku 15 tumeshindwa kuuzima hata ule moto ni hatari, haya madhara yake ni makubwa karibu hata manne, moja ni uchumi wa nchi yetu lakini la pili ni mapato watalii hawawezi kuja leo kwa haraka lakini vilevile ina-distort hata ile goodwill ambayo tunayo kama nchi ndani ya vivutio vyetu hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ajali hizi zinawapa umaskini watu wetu. Amezungumza role model wangu, Mheshimiwa Kaka yangu pale Mheshimiwa Hasunga, kwamba ni ukweli mpango wetu unazungumzia juu ya dhima ya kuona maendeleao ya watu wetu. Sasa kama watu wetu wanakufa na hatuna mipango ya dharura kutengeneza Mfuko wao hili dakika ikifikia pale tunachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka, leo tunafanya nini kwa sasabu hatuna mfuko huu? Tunaenda Fungu 21 tunachukua hela pale haiwezekani, hatujawahi kuukuta ule Mfuko lile Fungu 21 lina hela muda wote. Kwa hiyo, ni vizuri na ni muhimu sana tufike sehemu tuone umuhimu wa Mfuko huu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye moja ya hoja iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Bajeti. Nikitambua mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, naona nichangie katika kipengele kimoja tu kwenye ukurasa wa 50 wa ripoti ya Mwenyekiti au ripoti yetu kwenye eneo la mikopo hii ambayo sisi kama nchi tunaifurahia jinsi gani Rais wetu anaipambania. Kabla ya kufanya hivyo, nitumie nafasi hii sana kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoendelea kufanya kazi kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mikopo ambayo imezungumzwa katika ripoti yetu kuna huu mkopo wa (ECF- Extended Credit Facility) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa IFM wa Dola za Kimarekani Bilioni 1.04 au sawa na Shilingi za Kitanzania Trilioni 2.4. Kuna shida, Kamati inasema ina shaka juu ya malengo kama yanafikiwa, labda niwapitishe lengo kubwa kwenye mkopo huu wa trilioni 2.4 ambalo ni dirisha la pili na niwakumbushe ni dirisha la pili ambao tumepata, tofauti na lile dirisha la kwanza ambalo tulipata zile (RCF - Rapid Credit Facility) au UVIKO 19 hizi fedha ni 2.4 trillion. Fedha hizi tulizichukua kwa sababu ya lengo, lengo kubwa lilikuwa ni kupunguza urali kwa ujumla, urali wa nchi yetu katika yale ambayo tunaweza badala ya ku-import, tukaweza kuzalisha ndani na tofauti na hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kinachotokea ni changamoto kubwa sana. Ukiangalia ufanisi wa Mkopo huu mpaka sasa mkopo huu umetolewa mwezi Agosti ambao unatakiwa katika masharti yake utatolewa kwa awamu saba kwa vipindi vya miezi arobaini, lakini mpaka sasa ambapo ni dirisha linakuja mwezi wa Tatu mwakani kwa maana ya baada ya tathmini, lakini taasisi zote hizo ambazo zimepewa au maeneo yote ya kipaumbele matano, eneo la kilimo, uvuvi, nishati maji, nishati umeme, bado hakuna hata moja lililofika asilimia 30. Hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tunategemea Shilingi bilioni 760, tunaambiwa kwenye Kamati ndiyo tunatarajia tupewe ndani ya mwaka mmoja na tumepewa kwa awamu mbili; ya kwanza shilingi bilioni 349, sasa hivi tulitarajia kabla hao Wazungu hawajaja kutufanyia tathmini ili watupe second tranche, maana yake tulitakiwa tufike hata asilimia 60 au 70 sasa tuko chini ya asilimia 28.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakutajia kwa uchache. Eneo la kilimo, ECF kilimo, wametumia asilimia 28. Yaani fedha waliyopangiwa ni shilingi bilioni 40 wamepata shilingi bilioni 11; eneo la uvuvi, Fungu 64 katika bajeti ya shilingi bilioni 60 wamepata shilingi bilioni 1.1, yaani asilimia 1.9. Eneo lingine kama kilimo katika vipaumbele vitano wamefanya vitatu tu na vyote chini ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuonesha nini? Kama tumewapa kilimo eneo la umwagiliaji katika Fungu 5, shilingi bilioni 215, wamepewa chini ya shilingi bilioni 42. Sasa tunataka kujiuliza, hawa jamaa wakija kutufanyia tathmini ili tupate second tranche tutaweza kufanikiwa? Swali lingine unajiuliza, hivi mama anavyoenda kupata haya madirisha, anaenda anakutananayo kwa bahati mbaya au tayari wataalamu mnakua mnasema tunahitaji jambo fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani hela inapatikana ndiyo mnaanza kujipanga katika ofisi zenu. Maana kama nchi lazima tujue sasa, shida ni nani? Shida ni nyie wasimamizi, makamisaa wetu katika Wizara? Shida ni nini? Manunuzi? Shida ni nini? Kwa nini hatusogei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe kwa haraka, inawezekana hii ni tabia. Tunaambiwa palikuwa na dirisha la kwanza la RCF au UVICO 19, tuliambiwa mambo mengi sana. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Watanzania wanajua ni ile shilingi bilioni 600 na kitu ambayo ilienda kujengea madarasa 15,000 yakiwepo 12,000 na 3,000 ya shikizi. Mambo mazuri yalionekana pale, lakini hela nyingine ziko wapi? Mambo mengine ni yapi? Tunaona moja moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa, nataka niwakumbushe; na ndiyo maana hatutekelezi hii mikopo tunayopewa. Tuliambiwa tungeweza kuwa; hela iliyoenda afya Shilingi milioni 263, tena afya kwa upande wa Wizara, nyingine zilienda TAMISEMI, lakini lengo lake lilikuwa ni kununuliwa magari 503. Yako wapi? Ndani ya magari hayo; Land Cruiser Hard Top 262, basic ambulance 373, advance ambulance 20, ziko wapi? Ndiyo maana nazungumzia malengo ya mikopo yetu, ni kweli toka mwezi Juni, 2022 tuliambiwa yangeanza kuja magari hapa ambulance, mpaka leo hakuna? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dirisha la pili hili tunaendeleanalo. Changamoto za utendaji kazi chini ya asilimia 30. Rais wetu, mama yetu, ataenda atakutana na dirisha la tatu, mtamwingiza chaka tena achukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwakumbushe. Tuna shida kama Taifa. Katika bajeti zetu za Serikali za kila mwaka, bajeti ya 2022/2023 ni ya shilingi bilioni 41 tumesema hapa, lakini fedha za maendeleo zinazowekwa ni takribani shilingi trilioni 15.1. Kama shilingi trilioni 15.1 tunaendelea kufurahia Shilingi trilioni 1.3, RCF tunafurahia shilingi trilioni 2.4 tena tunazifurahia, na ni kweli, ni vizuri na tunazifuatilia, kwa nini hatufuatilii shilingi trilioni 15 zile za maendeleo katika kila mwaka, kwanini hatuzifuatilii? Katika kipindi cha miaka mitano, maana yake ni zaidi ya shilingi trilioni 60. Kama nchi tumeziweka katika maendeleo, lakini hakuna follow up. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida. Tumesema hapa kwenye Kamati, shida ya Sheria ya M&E, tuliomba sera ije hapa tutunge sheria ya monitoring and evaluation ingeweza kutusaidia kama nchi kuweza kufuatilia fedha zetu nyingi zinazoshuka chini. Leo shida yetu tunafurahia mikopo, nami naifurahia, mama yangu anaitafuta, lakini zile hela zetu tunazoziweka katika maendeleo, zetu wenyewe Shilingi milioni 14 hadi 15 mbona hatuzifuatilii na zinapotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tungeweza kuweka ring fence kwenye hela fulani tukawapelekea TARURA wenye kilometa 144,000 mtandao wa barabara. Wote hapa tunajua, tuna barabara za vumbi tunatamani ziwe changarawe au lami, kwa nini tusipeleke fedha nyingi tukazitolee macho kwenye barabara zetu za ndani za TARURA? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Taifa, lazima tujitathmini sana. Mikopo tunaitaka, lakini vilevile na fedha zetu za ndani za maendeleo tuzitolee macho kwa kutungiwa sheria. Ije hapa sera, tutunge sheria ya monitoring and evaluation ili tusimamie fedha zetu zote zinazoshuka chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie kwenye wizara hii. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Jumaa Aweso Mbunge na Naibu Waziri dada yangu Mahundi na watendaji wao wote wa wizara hii ya Maji, Fungu 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukweli kazi wanayoifanya ni kazi kubwa ni kazi ya kizalendo nchi yetu ni kubwa. Miradi inayohitajika ni mingi na maji hayana Subira. Mwananchi uweze kumwambia usubiri maji kesho au kesho kutwa hali ya maji ni muhimu kupatikana kwa wananchi wetu kwa haraka na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Nampongeza kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Mwaka 2021/2022 nilizungumza hapa, nikalia kwa muda sana na nikasema kwenye maswali yangu ya msingi naya nyongeza mliyonipa nafasi ya kuuliza, juu ya tanki ya mradi mkubwa pale mshikamano ambao utakuja kuwa majibu ya sehemu kubwa ya Jimbo la Kibamba. Mheshimiwa Rais alisikia kupitia mwamvuli wake Mheshimiwa Waziri, alifika jimboni mwezi wa nane mwishoni mwaka jana na kusaini mkataba ule hadharani mbele ya wananchi wa Jimbo la Kibamba na tayari kazi ile kubwa inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimshukuru sana, kwamba fedha zilizokopwa za tirioni 1.3 za UVIKO zilipelekwa zaidi ya bilioni 139 za maendeleo katika Wizara ya Maji fungu 49, na bilioni 2.5 zilitolewa kwenda Kibamba kwa ajili ya mradi huu wa mshikamano. Nikushukuru sana Mheshimiwa Rais na kwa usikivu wa waziri wako kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli, panakuwepo na mazuri mengi lakini vile vile na changamoto huwa zipo. Nifurahi tu, nifurahi kwa maana kimbilio la ukosefu wa fedha linaweza likatamkwa katika njia nyingine kama UVIKO ilienda kuongezea 139, lakini kila mwaka tunawapangia au tunawapitishia almost bilioni 680 katika Wizara hii. Lakini za maendeleo ni takribani bilioni 646 lakini walivyoongezewa na hizo 139 zikafika takriban bilioni 785, bajeti ya mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupanga na kupata ni vitu viwili tofauti hawa wanabahati sana wamepanga wamewekewa hizo lakini wamepokea takribani bilioni 743 ambapo taarifa ya Waziri inasema ni asilimia 95. Hii ni pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais pia sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama tunapata kile tulichokipanga kwa nini sasa miradi haitekelezeki kwa wakati? Kwanini miradi haitekelezeki kwa wakati? Wananchi wa Jimbo la Kibamba wanaendelea kulia na mimi huwa nalia hapa mwakilishiwao. Kibamba ndiyo imelisha Ubungo yote Jimbo la Ubungo kaka yangu Profesa Kitila Alexander Mkumbo yupo hapa. Lakini Kibamba ndiyo inalisha Pugu, kila siku nasema, I mean Kisarawe hadi na huko Pugu; mradi mkubwa umeenda Kibamba – Kirasawe, asilimia 95 wananachi wa kule kwa kaka yangu Jafo wanakunywa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawana maji Jimbo la Kibamba. Tunaambiwa hapa asilimia 86 katika miji, nafurahi hiyo ni takwimu ya jumla na uwiano au average. Lakini ukienda specific Kibamba natamka tu maeneo machache na Mijini, na Waheshimiwa Wabunge hapa zaidi ya 50 wanaishi kwenye Jimbo la Kibamba na Mawaziri zaidi ya 15 wako. Ipo siku nitawataja kwa majina ili muweze kuona umuhimu wa Jimbo lile. Mimi nasema ni Dar es Salaam Vijijini, mkubali ni Dar es Salaam Vijijini kwa sababu wanahitaji attention kubwa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, maeneo ambayo ni maarufu na wananchi wanayajua na humu wote wanajua. Nasema Mpiji Magohe, Msumi, Msakuzi yote Kaskazini na Kusini hakuna maji kabisa. Vilevile, maeneo machache ya Kwembe, King’azi A nimezungumza watu wanakunywa maji machafu ya visima, machafu ya rangi na Mheshimiwa Waziri anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, leo nilisema sitosema sana. Kazi mpaka sasa inafanyika. Sisemi kwamba hafanyi. Ipo miradi mitatu nimesema ukiondoa Mshikamano wa Mheshimiwa Rais, mradi wa Kitaifa. Nimesema mradi wa Kitopeni upo kwenye taarifa zao. Tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri tangu mwezi wa nane kwamba mwezi wa 12 tungepata hii miradi mitatu, ambayo ni Kitopeni, Mradi wa Mabwepande kule kwa Askofu Gwajima namuibia maji kwenye Tanki la Malolo kuja kilometa 8.2 hadi Mpiji Center kujazia pale Kidesa mpaka leo miezi sita imeongezeka. Christmas tutaenda na Waziri kunywa pale maji, hakuna miezi sita imeongezeka. Tenki pale kutokea Kwembe Kati kuelekea King’azi AB na Kilimahewa tumewaambiwa wananchi pale, tumeenda na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mbunge. Leo hawa viongozi ninaowataja hawawezi kwenda watapigwa mawe. Hawawezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tumeahidiwa mimi na wewe, kwa nini tunadanganywa? Mpango mzuri ulionao ni kuongeza uwezo na kutoa mafunzo mazuri kwa Watendaji wako wa ndani kwa ajili ya kazi za extension na distribution zifanyike kwa wakati. Kama bado uwezo mdogo, muone jinsi na mikakati ya dharula kuiokoa Dar es Salaam maeneo ya pembezoni. Mimi nimekusifia kazi unaifanya vizuri kama kijana mwenzangu lakini kama unaangushwa, sisemi unaangushwa na Ruemeja; anafanya kazi mpaka mnamuongezea na Tanga, Korogwe, Same na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi niaombe sana, leo siwezi kumaliza kusema, jicho la Serikali lijielekeze Kibamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. ISSA J. MTEMVU: …vinginevyo mtamuondoa Mheshimiwa Mtemvu Kibamba na siasa itaendelea kuwa ngumu sana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Fungu 49 - Wizara ya Maji ya Ndugu yangu Comrade Aweso. Nisiwe mchoyo wa fadhila ya kuwapongeza sana. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya na ni ukweli Wananchi wa Kibamba wanajua kabisa kazi kubwa ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo letu la Kibamba. Ni kwa sababu maelekezo yake pia yanapokelewa vizuri na hawa ndugu zetu ambao wanatafsiri maelekezo, Ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, Waziri na Naibu wake, dada yangu Mheshimiwa Maryprisca Mahundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema, mwishoni kwenye shukrani. Sasa anayo timu nzuri hapo Wizarani, sina shaka kabisa juu ya Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Sadiki Kemikimba na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Cyrpian Luhemeja, kaka yangu anao wasaidizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni shuhuda nimekwenda ofisini kwa Waziri mara nyingi na nyingine ambayo amenikutanisha na menejimenti yake yote juu ya changamoto ya Jimbo za Kibamba, lakini leo nieleze kidogo juu ya mafanikio ya Mheshimiwa Rais katika miaka yake miwili. Naingia hapa Jimbo la Kibamba lina changamoto chini ya asilimia 30 maji wanayapata, kabisa. Wananchi wengi hawana maji, wanapatapata maji pale barabarani, kwenye matanki makubwa Luguruni kwenye mita 20 au 30, lakini leo ninavyozungumza tayari Mheshimiwa Rais alikubali kilio changu humu ndani cha kujenga Tanki la Mshikamano kwa bilioni 5.4, lakini alitumia fedha za UVIKO bilioni 2.5 akazileta. Katika zile bilioni 139, bilioni 2.5 akasema mpeni Kibamba hata tanki lake la Mshikamano liweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tanki limeshajengwa limezinduliwa na wananchi wanaendelea kuunganishiwa maji, lakini pongezi nyingine kwa Mheshimiwa Rais, upo mradi wa zaidi ya bilioni 65 kutoka World Bank. Mradi wa chuo kikuu kuelekea Bagamoyo, lakini tumefaidika na tanki la Tegeta A, ujazo wa tanki ile milioni tano, tayari tanki limekamilika. Wananchi wa Goba yote wanaendelea kuunganishiwa maji. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, sana kwa jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo mimi na Waziri hata jana nilimwomba niende na akanialika kwenye menejementi yake yote, yote kueleza changamoto mbili ambazo nijue kama amezifanyia kazi au bado. Moja ni wananchi wetu wa Msumi, Kata ya Mbezi, wananchi hawa ni wengi, ndio Jimbo lile lina watu 650,000, jimbo la tano Tanzania nzima kuwa idadi ya watu na wananchi ni wengi kweli, lakin hawana hata chanzo cha maji. Nimshukuru kwa majibu aliyonipa. Tayari wameelekeza fedha katika matanki mawili ya Mshikamano na Tanki la Tegeta A kuunganisha nguvu ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili watengeneze matanki mawili ya bilioni 13.6. Nawashukuru sana. Najua sasa wananchi wa Mbezi, eneo la Msumi lote linaenda kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho lenye changamoto ni King’azi A, nimezungumza hapa miaka miwili mfululizo kwenye Hansard ipo. Niliwahi kusema viongozi watapigwa mawe humu, lakini leo Waziri amenipa majibu. Katika eneo lile kuna eneo linaitwa Bangalo Kilimahewa, eneo la kwao, watu wa DAWASA, sasa hivi wanaelekeza bilioni 42 pale. Sasa faida yake nini? Mradi mkubwa chini ya Benki ya Dunia, wananchi wa Kibamba, King’azi A na B wanaenda kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wananchi wa Bangulo, Kinyerezi Jimbo la dada yangu, lakini kuna wananchi wa Kinyerezi, Majohe, Pugu Kipunguni, Ukonga, tunaona mradi mkubwa unaenda kuwasaidia watu wa Dar es Salaam, wananchi wa majimbo matatu. Nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Aweso, sina sababu ya kusema mengine, ni kumpongeza kama kijana, anaendelea kuonesha vijana wakipewa nafasi wanavyoweza kufanya kazi. Nampa pongezi sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli katika muda nilionao baada ya hilo, Mheshimiwa Waziri taarifa yake yote kwa nafasi aliyonayo eneo lake ni maji safi na majitaka, lakini eneo hilo la majitaka halizungumzi vizuri sana kwenye taarifa zake kwa nyakati zote. Najua wameelekeza mitambo mizuri ya kubebea uchafu ule katika maeneo machache, lakini nimwambie takwimu zinavyosema kwenye taarifa yake, kwamba mpaka sasa ana kilometa 1,385 kwa mwaka uliopita mpaka sasa hivi 1,416. Huo ndio mtandao wa kilometa za maeneo za maji taka, lakini ameweza kuwaunganishia wateja 53,000… (Makofi)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa Saashisha.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa kaka yangu taarifa tu kwamba, ni kweli eneo hili la maji taka limesahaulika. Hapo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna eneo wanamwaga majitaka, eneo la Swaswa. Serikali imejenga barabara nzuri mbele na nyuma na majumba yamejengwa mazuri ya ghorofa, lakini yale majitaka usiku yanatoa harufu kali, hawayatibu vizuri. Kwa hiyo, nilikuwa nampa taarifa kwamba ni kweli, watazame na eneo hili. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mtemvu, unapokea hiyo taarifa?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea na mchango wangu eneo hili, inawezekana ni gharama sana, sijui lakini niwashauri kwa sasa. Kwa sensa ya mwaka 2020, tumefikia takribani watu milioni sita ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, majumba mengi yamejengwa ya maghorofa Kariakoo na maeneo mengine, lakini ukweli miundombinu ya majitaka haijawekwa vizuri. Sasa niwashauri kwa sababu nyumba nyingi za Kariakoo zinajiunganishia katika mifumo ya maji taka katika mifereji ya majisafi, kwa hiyo ni changamoto, lakini kuna eneo lingine ni mfumo wa majitaka usiotumia chemba, jinsi unavyofanya kazi. Wanaweza kutoa elimu hii kwa watu wengi sasa hivi wanavyojenga, wajenge mifumo ile ya maji taka ambayo haihitaji kutumia chemba inaweza pia ikatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna jambo hili ni changamoto sana, taka ngumu pia kutupwa kwenye vyanzo vya maji. Dar es Salaam hii hali mbaya na sasa niwaambie kipindupindu kimeanza kuingia, yote hii ni kwa sababu hatujajielekeza vizuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri achukuea na wataalam wake, eneo hili la kwake la pili, nashangaa sana hizi Wizara, nitakuja kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inakaa kwenye ardhi, makazi inaacha. Hili la kwake la maji na mambo ya taka, maji yuko vizuri, taka anaziacha. Ajielekeze huko vizuri, najua ameanza lakini aongeze nguvu, nina imani sana atafanikiwa kama alivyofanikiwa kwenye maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi, naunga mkono bajeti hii ya Wizara ya Maji kwa asilimia zote. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia bajeti yetu ya Serikali iliyowekwa mezani na kaka yangu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba pamoja na Naibu wake ndugu yangu Chande.

Kwanza nitumie nafasi hii sana kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nilikuwa nanukuu hapa sentensi iliyoandikwa na Kamati ya Bajeti, ikanipendeza sana; niinukuu; “Napenda nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuonesha kwa vitendo nia yake thabiti ya kuondolea Watanzania umaskini na kuwaletea maendeleo. Aidha utu wake katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii umekuwa ni msingi imara katika kutekeleza kauli yake mbiu ya kazi iendelee.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maneno ambayo kila Mtanzania hawezi kuyabishia. Ni maneno sahihi ambayo anastahili kupewa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ziada nimpongeze pia Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa jinsi wanavyoendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza yale ambayo ameahidi kuwafanyia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka kwa sababu ya muda nitajielekeza kwenye maeneo machache tu. Jambo la kwanza lilisemwa wakati tunachangia bajeti za kisekta, Wizara ya Afya; suala la urasimishaji. Nipongeze sana Serikali katika hatua sasa hivi iliyofikia ninao mkopo wad ola milioni 150, takribani bilioni 345 ambao utaenda kusaidia maeneo mengi kwenye eneo la Wizara hii ya Ardhi. Niombe sasa, utekelezaji huu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ujielekeze kule, kama wenyewe walivyosema, fedha zitoke ziende zikamalizie mgogoro wa urasimishaji ndani ya mitaa iliyopo ndani ya Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara ya kisekta inasema itatatua mitaa 559 mimi nina mitaa 42 hivi; kwa hiyo ipo tayari kwenda kumaliza. Mwakani naamini wakati tunapitisha bajeti yetu ya Serikali sitoongea tena mambo ya ardhi. Nina imani sana mambo mazuri yatafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine niipongeze tena Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni eneo la barabara. Tumepiga kelele humu kwenye bajeti za kisekta; lakini hata hii bajeti kuu imeeleza vizuri juu ya barabara kubwa za kimkoa, kiwilaya na miradi mingine itakayoendelea. Kule ndani ya Jimbo la Kibamba barabara za chini ya TARURA na DMDP tayari, tunaishukuru sana Serikali. Tumeshasaini na wakandarasi na washauri (consultants); vilevile na stakeholders, tumefanyia Dodoma na Dar es Salaam. Leo wananchi wanajua kwamba miradi inaenda kutekelezwa kuanzia mwezi wa nne mwakani. Barabara ya Kingongo inaenda kutengenezwa kwa lami, tunaendelea. Barabara ya Msumi kilometa nane inafungua kutoka Madale hadi Stendi ya Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kwa Shija kilometa 4.2, pia na Barabara ya Konoike kule ambako kuna tenki kubwa la mshikamano ambalo tumejengewa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo mambo ni mazuri. King’azi – Malamba Mawili kilometa mbili za lami zinaanza mwezi wa nne kwa hiyo hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Barabara, niliuliza swali la nyongeza asubuhi. Kuna ahadi nyingi. Bajeti yako inasema moja ya vigezo ukiondoa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na mambo mengine lakini ahadi za viongozi wa kitaifa ni eneo ambalo linazingatiwa. Hili nimesema asubuhi chini ya asilimia 50 embu tukaliangalie ili tuendelee kuwaheshimisha viongozi wetu hawa. Wanakwenda kutembelea maeneo wakitoa ahadi zitelekezeke. Ni vizuri sana kuangalia zote za miaka ya nyuma muweze kuzitengea fedha na kuzitekeleza zile ahadi za viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la maji. Mheshimiwa Waziri taarifa yako imesema na yenyewe vizuri, niendelee kuwapongeza. Dar es Salaam Jimbo la Kibamba mambo ni mazuri na tunaendelea kuunganishiwa maji. Lakini shaka yangu, wakati wa kiangazi tunakosa maji ya Ruvu ambayo ni tegemeo katika miaka tangu tunapata uhuru. Leo population ni kubwa, zaidi ya watu milioni 5.4. Haiwezekani wakategemea chanzo kimoja, tunajua tumewekeza kwenye Bwawa la Kidunda basi niombe sana utekelezaji wake uende haraka ili sasa wananchi hawa katika mikwazo ya vipindi vigumu tuendelee kuwapatia maji safi na salama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Wizara yetu hii Fungu 98.

Awali ya yote na mimi nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoendelea kufanya nchini, lakini pia nimshukuru sana nakumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima lakini pia na watendaji wakiongozwa na Balozi Mhandisi Aisha Amour; Mheshimiwa Aisha Amour Katibu Mkuu wa Wizara hii ya ujenzi hasa sekta ya ujenzi, kwa kweli ni mchapakazi mkubwa, mimi binafsi namtambua amekuwa RAS wangu nikuwa Mhasibu Mkuu wake Mkoa wa Kilimanjaro, kwa hiyo lazima niseme ukweli kwa jinsi ambavyo umeaminika ninajua sasa utakwenda kutusaidia katika Wizara hii kutuvusha kwa changamoto ambazo wengi wameendelea kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo na hasa nimempongeza Mheshimiwa Rais mahususi sana na lazima niseme kwa nini kwa sababu ya barabara yetu ya njia nane upanuzi wa barabara ya njia nane inayotoka Kimara mpaka Kibaha kilimeta 19.2 ambayo imeenda sambamba na madaraja ya Kibamba pale Kiluvya na daraja la Mpiji, tunamshukuru sana na Watanzania wengi, Wabunge wengi hiyo barabara ni ya kitaifa na wameiyona. Mheshimiwa Rais ana sababu za kushukuliwa katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tumezungumza sana mambo ya Dar es Salaam, Waheshimiwa Wabunge wengi katika barabara hizi, wanatamani ziende kule zikaunganishe Wilaya, Mikoa na kadhalika zibebe mazao na mambo mengine ili yaende kwa wale walaji. Lakini leo nataka niwaambie kwa nini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Dar es Salaam? Kwa sababu sensa ya mwisho ya mwaka 2012 ilituambia tuna takribani ya watu milioni 4.2 lakini sasa hivi kuna maoteo ya makadirio ya watu au kadirio la watu la zaidi ya milioni sita kama Dar es Salaam na hii ni zaidi hata ya Afrika Mashariki katika majiji mengi pia zaidi sio tu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa nini Dar es Salaam? Ni kwa sababu ndio Jiji linalokuwa kwa kasi sana, miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi duniani, lakini kwa nini Dar es Salaam, Dar es Salaam ndio lango linaloongoza kwa kuingiza na kuondoa watalii yaani kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Rais juu ya jambo hili ambalo amelifanya Dar es Salaam ndio lango la hawa watalii sasa. Kuingia na kutoka, kwa hiyo wananchi hawa na Waheshimiwa Wabunge mjue Dar es Salaam katika umuhimu wake huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kodi ni zaidi ya asilimia 85 kama kodi ndio inapatikana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, lakini zaidi contribution ya Dar es Salaam kwenye GDP tunaambiwa kwa research ya mwaka 2020 iliyofanyika zaidi ya shilingi trilioni 25.3 zinapatikana Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na hilo sasa niende kwenye hoja zangu mahususi, utanielewa sasa kwa nini nalilia Dar es Salaam. Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022 Dar es Salaam ukiondoa barabara kubwa hiyo ambayo nimeitamka ya kitaifa ziko barabara za kimikoa na sio nyingi, nikizitamka katika bajeti ya 2021/2022 ilitamka barabara ya Kibamba - Kisopwa - Kwembe - Makondeko kilometa 14 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kilichofanyika hivyo barabara kilometa 14 tu ndani ya Kibamba, lakini kuna barabara ya njia panda Matosa - Goba kwenda Matosa mpaka njia ya highway barabara kubwa kilometa sita. Katika kipindi cha miaka mitano mpaka leo tunamtafuta mkandarasi amepewa kilometa moja; miaka mitano na barabara hii ni muhimu kwa wananchi wa pale na wengi hapa wanapita na Wabunge wengi wanaishi pale kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Goba - Njia Nne kuelekea Matosa mpaka inatoka kwenye barabara ya njia nane hakuna kinachofanyika miaka mitano. Tuombe sana jicho la huruma liendelee kwenda pale kilometa tano; wenzetu wanaongea kilometa 100, 78, 304 ni kilometa sita hakuna kinachofanyika Dar es Salaam kweli ndani ya umuhimu wote nilioueleza huu mambo yote haya ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kweli tunawaombeni sana mtuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa la utekelezaji wa ahadi za Rais na viongozi wakuu, walisema mwaka jana kwenye bajeti ya mwaka jana Waheshimiwa Wabunge walisema kama nchi lazima tuone tunapoalika viongozi wetu wakubwa wanakuja kwenye mikoa yetu, kwenye majimbo yetu tunatamani kuwaomba vitu, na tukiwaomba wananchi wanajua leo amekuja mfalme na yapo maneno mengi ya kiswahili ambayo yanatumika juu kuenzi na kuheshimu wa ujio wa viongozi wa kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi wa kitaifa anafika anaahidi hakuna kinachotekelezwa, lakini hata taarifa ya Waziri haituambii utekelezaji wa maelekezo na maagizo ya viongozi wa nchi imetekelezeka kwa asilimia ngapi. Kwa upande wa TAMISEMI, TARURA na sasa hivi ninatoka kwenye Kamati ndani, wameeleza hata utekelezaji wao umefikia asilimia 85 ya maelekezo au maagizo ya viongozi wa kitaifa, huku ni ngapi, hamjasema, tunataka kujua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua ninayoisema ya pale ndogo tu ya tarehe 25 Februari, 2019 nimepata bahati ya kusema na watu wanajua niliomba barabara ya kwanza, junction ya Makabe kwenda Msakuzi kutokea Mpiji Magohe kilometa tisa tu, lakini barabara ikaunganishwa na barabara inaitwa Kwa Yusufu kwenda Mpiji Magohe hadi Mabwepande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na barabara ya tatu inatoka Njia Nane kwenda Njia Panda ya Shule kuelekea Kibwegere mpaka Mpiji Magohe, jumla ni kilometa 37. Wakati fulani niliuliza swali la msingi hapa nikaambiwa sasa ipo na imewekea hela na inaendelea kutengenezwa. Leo bajeti ya 2022/2023 lugha inayozungumzwa hapa upembuzi yakinifu, upembuzi wa kina sijui na mambo haya ya kitaalam taalam, mimi mhasibu hata sijui hayo maneno yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaenda mbele tunarudi nyuma hoja ambayo itatoka leo hapa kwamba wananchi wataniuliza tuliambiwa na Hayati barabara hizi angetamani hela zitolewe kwingine zijengwe kwa haraka na azione zikiisha, ndani ya siku saba akafariki. Leo ujanja ujanja mtupu kama vile aliyetoa ahadi ni Rais sio taasisi. Ahadi ilitolewa na taasisi ya Uraisi tunaombeni sana msisababishe viongozi wakashindwa kuja tena, tunaombeni mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliona niliseme vizuri Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha utuambie ndani ya Jimbo la Kibamba barabara chache hizi za kilometa 37 unaziachia kilometa ngapi na sio maneno ya kiahandisi ambayo unaendelea kutujazia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli mimi leo nilisema sitaki kusema maneno mengi dakika tano zinanitosha, ziada niombe tena naomba kwa heshima Wizara hii ituonee huruma sio leo kila siku niseme maji niseme watu wa Kibamba, nizingumze ardhi kesho kutwa nitasema Kibamba ya shida, nizungumze uchumi wa watu wa shida Kibamba tunaombeni msaada ili tuheshimishe, tuhemishe Chama chetu cha Mapinduzi chenye nia njema na Watanzania na Watanzania wanavyokipenda na kukipa kura nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kusema haya yaliyo machache, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya uteuzi mzuri wa dada yangu Dkt. Angeline Mabula kuwa Waziri mwenye dhamana na Wizara hii ya Ardhi na Makazi, lakini pamoja na hilo pia kwa ndugu yangu rafiki yangu, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete kuwa ni msaidizi wa Mheshimiwa Mabula. Lakini nitambue kazi nzuri inayofanya na Wizara, kwa maana ya watendaji wao wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitasema kidogo tu kwenye eneo ambalo mara nyingi nikipata nafasi nalisemea kama kuikumbusha Wizara na eneo lenyewe ni jambo la urasimishaji. Mjumbe mmoja kule upande wa pili alinyanyuka akaweka kibwagizo tu kwamba wananchi wanatakiwa waelewe sana nini maana ya urasimishaji na akatoa mfano yeye anatoka Tabora lakini akasema hasa kule Dar es Salaam, mimi nikapiga makofi hapa mawili matatu nilitaka kumwambia ni kweli tunatamani kujua maana ya urasimishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hiki ni kidonda kisichopona, hili kwetu ni tatizo, mwaka jana nilisema hapa, nilisema tukatofautina tofautiana na Mheshimiwa Waziri akiwa Naibu Waziri, moja kwenye swali la msingi lakini baadaye hata wakati nachangia kwenye fungu hili. Hoja yetu pale tunajua na huku imesemwa kwenye ukurasa wa 43 urasimishaji kwa ujumla katika jukumu la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, sehemu kubwa ni jambo la mamlaka zetu za Miji na Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunatambua kule Dar es Salaam jambo hili wamepewa makampuni kufanya na Mamlaka za Miji haya makampuni tunaanzia hapa, yameletwa na kupewa ithibati kwa kuwa scanned na Wizara yaani wananchi wetu kule so tu wamepokea makampuni au walikaa wenyewe wakasema aje huyu au aje yule, Wizara mliangalia makampuni yale, lakini mwisho wa siku mkasema sasa nendeni mkaingie katika Halmashauri zenu za Miji na Halmashauri na Halmashauri za I mean katika miji yetu ili wafanyekazi na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa tatizo, mwaka jana nilisema wizi mkubwa, makampuni yametuibia, fedha nyingi tukatofautiana hapa, lakini mimi nakumbuka Naibu Waziri amekuja juzi tu, kabla ya kuwa waziri wakati mdogo tu kabla hajawa Waziri ameona, kwamba kama tumetofautiana figure, lakini zaidi ya bilioni nane aliziona kabisa kwamba iko shida sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukweli nitumie nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Kheri Dennis James, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo nampongeza kwa sababu amechukuwa hatua za awali lakini amepata ushauri baada ya kutembelewa na Mheshimiwa Waziri kwamba tufike sehemu, yale makampuni baadhi yake wakasimamishwa, lakini bado hoja yangu fedha za wananchi ziko wapi, mwaka jana nikasema jicho la tatu lije, hata kama CAG nikawashauri mleteni ili ajue hela za wananchi ni kwa kiasi gani zimeibiwa hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwaka jana tuliambiwa mradi huu wa miaka kumi unaenda kuisha mwezi Oktoba 2023; mwaka 2023 ni kesho kutwa sisi bado hela tumepoteza mabilioni ya hela, lakini dhima inasemwa humu, lakini dhima ya kupima, kupanga na kutoa hati, ni kuboresha maisha na uchumi wa wananchi sasa sisi tunafanya nini tunaendelea kuwa maskini hati hatuna, ardhi yenyewe tunakuwanazo kwa shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kwa haraka; nimeona hapa wewe ni shahidi inazungumzwa miji shilingi bilioni 45.7 huku amesema kama bilioni hamsini hivi zinapelekwa kwenye Halmashauri 25, kwa ajili ya jambo hili hili la kupima kupanga na kumilikisha ardhi, wakati mwaka jana nilisema kila mwaka zinawekwa zinaenda huko, shilingi bilioni 50 wengine wanapewa kwa jambo lile Dar es Salaam inaachwa tena, kwa hiyo wananchi wanatoa wenyewe na wana hali mbaya na zinaibiwa na hatufanyi chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mim niwaombe sana Mheshimiwa Waziri nataka nikushauri na katika hili naomba uniruhusu nimwomba na Waziri Mkuu aliingilie jambo hili na aje Kibamba kwenye Jimbo lile na Wilaya nzima ya Ubungo aone anatutatuaje, pelekeni chukuweni jukumu ile hela yote iliyopota fanyeni ninyi ndio imepotea kwenu kwa sababu mlileta ninyi yale makampuni. Wapelekeeni zile demand kwa ajili ya kulipia hati tu, ile ndio wadaiwe wale wananchi ambao wameibiwa zile fedha na yale makampuni mliyoyaleta ninyi huo ndio ushauri katika eneo hilo. Nafikiri nitakuwa nimeeleweka siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mlonganzila pale miaka ya nyuma kidogo wananchi watakumbuka tumepeleka pale hospitali ya Mlonganzila kulikuwa wananchi wanaishi katika lile eneo zaidi wa wananchi 2500, eneo lile ambalo kuna Hospitali ya Mlonganzila, lakini mimi nishukuru sana Serikali zetu zote hizi ziliona hiyo sababu ikawalipa mali zao, iwe mazao na nyumba zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu ya eneo hili baada ya tathimini kubwa ilionekana la Tanganyika Packers basi wakati ule namkumbuka alikuwa Angellah Kairuki alifika na wakakubaliana kama neno la Serikali kwamba tutawalipa kifuta machozi shilingi milioni mbili kwa kila ekari mwaka 2015/2016 mpaka leo, sijui ni kwa sababu tulikuwa tunaenda kwenye uchaguzi wa 2015 hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo mlikumbuke, muende kule wananchi kule wanalia mkalipe kile kifuta machozi mlichokiahidi cha shilingi milioni mbili kwa kila ekari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya mwisho dogo juu ya kuboresha miji ya Dar es Salaam kama maendeleo katika maeneo ya Tandale nilishalisema wakati nachangia Waziri Mkuu, maeneo ya Manzese, maeneo ya Magomeni kama tulivyofanya Magomeni quarters tubadilishe uchumi wa Dar es salaam ili maisha ya watu yawe bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara yetu hii muhimu kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana kwa usimamizi mzuri wa kamisaa wetu Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Hassan Chande, lakini niwapongeze sana watendaji wakiongozwa na wakuu wetu watatu hawa; Emmanuel Tutuba - Katibu Mkuu wa Wizara hii, pamoja na Naibu Makatibu Wakuu wawili; kaka yangu Lawrence Mafuru na dada Jenifa Omolo, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziada nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kazi anayoendelea kufanya ni lazima tuseme, anafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri juu ya eneo la usimamizi wa sera za kiuchumi, uchumi jumla na akatuambia ni ukweli mambo makubwa ambayo yametusaidia sana ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kuendelea kubaki kwenye asilimia 4.9 ukilinganisha na asilimia 4.8 kwa mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, kubwa sana ni kuwezesha shughuli mbalimbali baada ya UVIKO-19 kurejesha ile hali nzuri ambayo tulidhurika katika muda ule ambao watu mnakumbuka tulivyoingia kwenye UVIKO-19. Lakini ziada ya hapo pia kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu. Haya ni mambo makubwa na ni ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Ndio amesababisha tukaendelea kuwa stable kama nchi katika hali ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili hivi, na muda ukiniruhusu eneo la tatu.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni madeni; nitumie nafasi hii kumpongeza tena kama wenzangu waliotanguliwa kusema, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutoa shilingi bilioni 772.87 kuweza kulipa madeni mbalimbali. Madeni ya wakandarasi zaidi ya shilingi bilioni nne, wazabuni zaidi ya shilingi bilioni 81.6, watumishi nje ya mishahara shilingi bilioni 25.7, watoa huduma shilingi bilioni 52.7 na madeni mengineyo zaidi ya shilingi bilioni 608.51, jumla yake ni takribani shilingi bilioni 772; siyo jambo la kawaida, ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, taarifa inatuambia yapo madeni mengine ambayo yako chini ya Msajili wa Hazina, yapo madeni ya mashirika na taasisi za umma ambayo yanatakiwa kulipwa na Msajili wa Hazina; hapa shida ipo.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wenzetu hasa wa sekta binafsi, wanajitahidi sana kujiinua kiuchumi kwa kukopa na kadhalika ili waweze kusaidia kutoa huduma Serikalini. Lakini Watanzania wengi wanakufa, wafanyabiashara wenzetu hawa wanaumia. Leo nataka nikwambie mfano mdogo sana, mwaka 2005 kampuni moja na hii niliwahi kuwasilisha hata kwenye Kamati Kampuni moja, NICOS ilifanya kazi na TRL wakati ule wa kampuni tanzui ile HSC sijui. Toka wakati huo, mwaka 2005, ikalipwa mara moja, mbili, baadaye mgogoro, mwaka 2009 mahakamani, mwaka 2014 hukumu ikatoka mumlipe pamoja na riba na gharama zake zote za mahakama. Mpaka leo mwaka 2022 miaka saba, kimya, hakuna cha kulipa wala kujibu barua.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho wa siku leo, baada ya kubanana sana watu ndio wanataka kwenda tena mahakamani kusema hatujaridhika na hukumu ya mahakama ya miaka nane, siyo sawa. Huyu ni Mtanzania. Sasa huyu ni mmoja, je, Watanzania wangapi ambao wamekopa na leo wamefilisika kwa sababu ya kushindwa kulipwa madeni yao?

Kwa hiyo, niliona ni vizuri jambo hili wenzetu mliangalie kwenye sura ambayo itawasaidia Watanzania waweze kujiinua kiuchumi badala ya kuweza kuanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme jambo la pili; wengine wamesema pia kuhusu Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor). Taarifa yetu inajieleza sana juu ya taarifa ya Mkaguzi wa Ndani kuelekezwa kwenye Kamati ya Ukaguzi (Audit Committee), na tukazungumza pale idadi ya watu watano, lakini tungetamani sana ili kuondoa inpairness, wawili watoke ndani watatu watoke nje. Ushauri mzuri nami naunga mkono kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha, ukiangalia Taarifa ya CAG sehemu kubwa hasa kwenye LGAs, kwenye taarifa kule kwenye Halmashauri zetu, shida ikitokea kule kwenye Taarifa ya CAG anakwenda kubebwa Internal Auditor, Mhasibu na Mweka Hazina, hakuna wengine wanaobwebwa. Lakini furaha ikija kwenye taasisi ya kupata hati safi anapigiwa makofi Mkurugenzi na wasimamizi wao ambao ni Sekretarieti za Mikoa; hii ni shida. Jicho letu liende vizuri, niliwahi kushauri humu mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natoa experience, nimetumika kwenye Sekretarieti za Mikoa. Kuna mtu anaitwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Regional Chief Internal Auditor), hana kazi, hana kazi. Na kwa nini hana kazi, anahitajika akitumika huyu naamini CAG atakwenda kufurahi kufanya kazi zake vizuri na ata-rely on the work of internal auditors. Vinginevyo, kama alivyosema Mheshimiwa Subira, siyo lazima, sheria haimlazimishi external auditor aka-rely kwenye kazi ya internal auditor, akikuta internal control iko vibaya anaachana nayo, anakuja na ya kwake.

Mheshimiwa Spika, sasa liko jambo hapa, ni la kimuundo tu na nitoe mfano, Sekretarieti hizi chini kule, kutoka kwenye Sekretarieti za Mikoa kuna mtu anaitwa Katibu Tawala Msaidizi - Local Government. Huyu mtu ana vi-organ pale, yuko autonomous kabisa, katengeneza mtu wa fedha na katengeneza internal auditor, lakini hawa watu ni ma-junior sana, ma-junior in such a way kwamba hawawezi kwenda kusimamia kazi ya wakubwa wao chini. Haiwezekani kuna ma-internal auditors ambao ni Wakuu wa Idara wanakwenda kusimamiwa na senior auditor ambaye anatoka kwenye kitengo cha Katibu Tawala Msaidizi - Local Government. Kwa nini wakati kuna Chief Internal Auditor hana kazi, hawezi kushuka chini anaishia kufanya kazi kwenye ofisi za ma-DAS tu, ndiyo anakagua. Sasa huo u-chief wa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nashauri ni vizuri mkatengeneze muundo ili uboreshwe mumpe majukumu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Mkoa aweze ku-oversee kazi za ma-internal auditors ambao kimsingi hata kwenye ikama zenu yule ni bosi wa ma-internal auditors wa Local Government. Kwa hiyo utaona ile seniority inaweza ikaenda vizuri. Na mwisho wakitoka na taarifa kimkoa basi ni vizuri sana ninavyoona internal auditors wanaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa dakika moja ni contingency fund (CFE).

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, kengele ilishagonga.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi hili niliache, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye nchi yetu. Pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini ni lazima tuendelee kuwapongeza juzi tu tumetoka kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kwenye sekta ya Wizara yake ya Fedha kazi ambayo wanaendelea kufanya kama Wizara pamoja na watendaji wao. Kwa hivyo, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili, matatu kwa haraka jambo la kwanza ni lile ambalo limesemwa na wengi la asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo hapo kwenye asilimia 10. Wengine wanajaribu kutofautisha kati ya Miji yenye mapato makubwa na halmashauri nyingine. Mimi natoka Dar es Salaam unakotoka wewe, kwenye Wilaya yetu ya Ubungo tunasema asilimia 10 bado tunaweza tukasema ina asilimia 50 kwenye mafanikio na nimewahi kusema humu ndani. Tunatamani kujua uhakiki na tathmini ya ujumla katika kipindi chote ambacho asilimia 10 imefanya kazi, hiyo itatupa matokeo. Niliomba hapa TAMISEMI wakafanye hili jambo, leo tungekuwa tunajua kwa nini tano, ingekuwa wanatuambia vizuri kwa nini wanazipunguza, tumefanikiwa kwa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu humu ndani bado zipo taarifa nyingi zimeshapotea fedha nyingi katika hizo asilimia 10. Sasa tunakuwa katika mazingira ya kwamba hatuwezi kufanya maamuzi, je, ni kweli tukubali zipungue au tubaki hapo hapo au tuongeze kama wengine ambavyo wanaona? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko jambo tumezungumza juzi na nilikuwa na swali la nyongeza juu ya vijana wengi zaidi ya miaka 35, akinamama wameingizwa katika umri ambao hauna mpaka. Vijana kundi la akinadada wapo katika umri wao katika ujana na pia na wanawake, lakini vijana mwisho miaka 35. Tunajua wajasiriamali hapa ambao tunawazungumza wengi ni zaidi ya miaka 35 mpaka 40 ndio wengi na huo ndio ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiona azma hii ya kuhamisha asilimia tano ni kama vile, wanakwenda kuwatafuta wajasiriamali ambao wengi wamezidi miaka 35. Kwa hiyo, kama huo ndio muono ni jambo jema, lakini inaweza kubaki 10. Katika halmashauri zenye uwezo, ninayotokea mimi nikikubali kwamba 10 zibaki, lakini jambo hili lenye nia njema na wajasiriamali wa zaidi ya miaka 35 waongezewe hiyo tano. Kwa hiyo, ningefurahi kabisa ingeenda hata asilimia 15, kumi zingebaki na tano zingeongezwa, lakini kwa nani wakafanye tathmini. Wale wenye mapato madogo waachwe vile walivyo, wenye mapato makubwa waende kwenye 10 wajumlishiwe na tano ziweze zikawasaidie au hiyo miundombinu ya hao wengine. Ziada kwenye hili niwaombe sana hebu tukaongeze/tukafungue ule umri pale kwenye hii mikopo, tukaufungue ufike miaka 40 inaweza ikatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye asilimia 10 kuna shida moja ambayo hatuizungumzi. Wananchi wengi wanalia, wapiga kura wetu wengi wanalia. Tunazungumzia asilimia 10 (4:4:2) au hiyo (2:2:1) kwa wajasiriamali wenye biashara, lakini wale ambao wanataka kuanza biashara hatuwataki kabisa na ambao ndio wengi. Sasa hao wanataka kuanza biashara, wanataka mtaji mdogo na sisi hatuwezi kuwapa, tunasema lazima uanze na biashara, ndio maana kuna udanganyifu sasa. Wanatafuta duka la mtu wanakwenda watano, 10 wanasema tukae humu kwako, ili iweze kuja kwa mtu mmoja wakagawane vipande vipande, hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Maafisa Biashara, tunao wengi tu katika kila halmashauri yupo, ana kazi gani kama hawezi kutoa elimu juu ya kuanza biashara na akaweza kuisimamia biashara iliyoanza? Uoga wetu ni nini kama nchi? Uoga wetu ni nini katika hili? Ione hii, tushauri Wizara katika bajeti yetu hii, hebu tuone jambo hili, tufungue pale miaka 40, lakini tukaone mitaji hii inayotolewa iende kwa kuanza biashara na sio kwa mwenye biashara. Inasababisha kuwa na manung’uniko makubwa makubwa sana na fedha zinakwenda kwa watu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo la asilimia 10 hapa naweza nikachomeka jambo ambalo limezungumzwa sana na watu. Kuna jambo la mapato dhidi ya matumizi kwenye halmashauri zetu. Mdogo wangu Mheshimiwa Gambo hapo kaisema katika njia fulani kaifananisha Dar es Salaam na mimi ndio maana naamua nirudi hapo. Ni kweli tunayo hayo mapato, lakini nasema hata hayo mapato ambayo tunayapata ya ndani bado ni madogo kwa sababu, ipo kauli ya Serikali ambayo huwa inatolewa au mpaka sasa imeshawahi kutolewa kwamba matumizi ya Waheshimiwa Madiwani kwenye allowances au hizo capacity building ili waweze kwenda kutoa hamasa ya kukusanya mapato inatolewa kauli moja tu halmashauri zote posho zitafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo hapo Wazii ametamka mwenyewe kuna halmashauri zaidi ya 19, kukusanya tu wanakusanya shilingi 500,000,000, huyu mwingine anakusanya shilingi 8,000,000,000, unasema wote wakatumie shilingi 200,000 tunawezaje hivyo? Hatuwezi kufanana, kama tunatofautiana kwenye kuzitafuta, tutofautiane pia kwenye kuzitumia. Hili ni jambo muhimu sana, inakatisha tamaa. Leo Waheshimiwa Madiwani wanalia kwa sababu wanafananishwa na kule kwa ndugu yangu Tunduru, hakusanyi, hana uwezo wa kukusanya, lakini Ubungo nakusanya. Hivyo, kama nakusanya waacheni Madiwani waendelee kutafuta mianya mingine iliyopotea ili waongeze mapato zaidi lakini na wenyewe waone au wapewe hizi capacity building tofauti kutokana na wanavyokusanya na sio kufananishwa kwa sababu tunatofautiana jinsi ya kutafuta. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la TARURA, ukurasa 25 wa taarifa unasema vizuri na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, zipo tozo nyingi ambazo zimeingia na kutoka. Tumeingiza mwaka jana ya simu, lakini tumeitoa haraka, kwa hiyo tuliingiza ili ikapunguze gharama za smartphone ili tuweze kupata fedha kupitia bando na vitu kama hivyo na data, lakini ujanja ujanja wa wafanyabiashara wamekataa kupunguza. Mwaka huu nimfurahie sana Mheshimiwa Waziri ameirudisha tena, tunakwenda sawa, tukikupa ili twende sawa unakataa tunarudi tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo la tozo ya mafuta fuel levy, jambo hili limebaki hivyo hivyo na limetusaidia, kwenye bajeti ya barabara unaweza ukaangalia kabla ya tozo Mfuko wa barabara peke yake kwenda TARURA zile asilimia 30 ulikuwa unapeleka shilingi bilioni 243.15, lakini baada ya Mheshimiwa Rais kuona umuhimu wa kuweka tozo, imekwenda kuongeza shilingi 322.16. Unaweza ukaiona imekwenda ku-double ukiondoa vyanzo vingine vya barabara ambavyo vinatupeleka kama Shilingi Bilioni 781, lakini tayari shilingi bilioni 600.66 kama asilimia 66 zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zimeshatoka. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mtemvu.

MHE. JUMANNE I. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa leo nimeyasema hayo machache, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja kuhusu Halmashauri za Miji na Wilaya Kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kutatua Tatizo la Upungufu wa Magari ya Zimamoto pamoja na Vifaa Vinavyotumika Kuzima Moto na Uokoaji
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu juu ya hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Tarimo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Tarimo kwa hoja hii ambayo binafsi imenisumbua kwa muda mrefu sana, hata nilivyoingia asubuhi nikamuwahi kumwambia hongera sana na nitapata bahati ya mimi kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nikushukuru wewe kwa kuniona nje ya utaratibu na mwongozo wa kikanuni, lakini ukatupa nafasi kama alivyosema Mheshimiwa Michael Mwakamo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda niseme tu tafsiri ya kwanza ya Jeshi letu la Zimamoto, kwenye taarifa amejaribu kuisema kwamba kabla ya mwaka 2007 tulikuwa tuna taratibu hizi ndani ya halmashauri zetu, lakini Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaundwa kufanya kazi chini ya Sheria Namba 14 ya mwaka 2007 (Fire and Rescue Force Act). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majukumu ya msingi sana lazima tuyafahamu, moja, ni kuzima moto na kuokoa maisha na mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani pamoja na majanga mengineyo.

Mheshimiwa Spika, sasa katika upana huu wote hatuoni jeshi hili likiwa na majukumu yote manne haya kama niliyoyasema. Tukiangalia haraka na maono ya wananchi dhidi ya jeshi lenyewe unaweza ukamuona yupo tu kwenye eneo la kuzima moto, lakini humwoni kwenye mafuriko, majanga ya barabarani na majanga mengine ambayo nimejaribu kuyasema hapa kama vile matetemeko ya ardhi na kadhalika. Kule Kagera yalitokea, lakini na maeneo ya hapa Dodoma hatukuwahi kuwaona.

Mheshimiwa Spika, niseme naunga hoja mkono katika mapana ya kwamba pawepo na MoU kati ya halmashauri na Jeshi la Zimamoto. Pia na mimi hapa niwe very specific ishuke chini, lakini katika zile halmashauri za miji na majiji zenye uwezo zikaisaidie bajeti ya zimamoto kwa sababu kwa Serikali Kuu peke yake kwa majukumu haya niliyoyasema yote kwa majukumu haya kwa mujibu wa sheri inayounda zimamoto, haiwezi kuutekeleza. Kwa hiyo, wakisaidiwa inawezekana wakaweza kufanikisha lakini wale wasio…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, muda wenyewe jamani.

SPIKA: Mtajuana na ninyi huko ni majirani. Kwa hiyo, mtajuana baadaye. Mheshimiwa Mtemvu kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mwandabila. (Makofi)
TAARIFA

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninataka nimwambie kwamba yeye anatoka halmashauri ya mjini Dar es Salaam, haya mambo ya ununuzi wa haya magari ya fire inawezekana. Kama halmashauri ya Mji wa Tunduma imeweza kununua, wenyewe Dar es Salaam wanashindwa kitu gani? Ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mtemvu, Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, hajanielewa tu hoja yangu, ninaona kaunga mkono tu ambacho nilikuwa nakisema, sikukataa kwamba halmashauri za miji na majiji makubwa ziweze kusaidia bajeti kuu ya Serikali kununua ili hawa wadogo wasinunue na ndicho alichokuwa ananiambia nyie mnaweza. Ni kweli tunaweza katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, niweze kukwambia kwa haraka tu, katika majanga haya kama majukumu ya jeshi hili limeshindwa kutokana na vifaa, mimi ninatoa mfano tu mafuriko. Katika kipindi hiki cha mafuriko ndani ya jimbo langu nimepoteza watoto wawili, lakini jinsi gani ambavyo nilikuwa ninajaribu kushirikiana na jeshi hili, lilikuja tu na maji na magari yake, lakini jambo lenyewe ni mafuriko, hawakuja na vifaa vingine.

Mheshimiwa Spika, siku tatu wananchi wa pale wa jimbo lile tulikaa kwenye maji tunatafuta katika njia zetu za local, lakini na wenyewe wakaja wakatuunga mkono kwenye kutembea na fimbo. Tukawauliza je, mngekuwa na mbwa si angenusa kwenye vichaka vilivyojifunika?

Mheshimiwa Spika, huwezi amini, ndani ya muda mdogo baada ya siku kumi akapatikana yule mtoto ndani ya kichaka ambacho hakipo hata zaidi ya meta 200. Kwa hiyo, wangekuwa na mbwa ingetusaidia.

SPIKA: Haya, ngoja twende vizuri. Mheshimiwa muda wako umeisha lakini unayo hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge?
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ninayo hoja hii.

SPIKA: Uko nayo?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kifungu (b) yake umeisoma inasomeka namna gani? Muda wako ulikuwa umeisha. Kwa hiyo, huu unaotumia ni wa kwangu. Fungua tu, halafu soma (b) yake anasema nini. Au ni kusomee? Au umepapata?

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nisaidie, ninaona hitimisho. Juu ya hitimisho (b) ... (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Spika, haya, (b) yake inasomeka hivi na anasema; “Serikali ilete Bungeni Muswada wa Sheria utakaoweka utaratibu wa kuwezesha halmashauri za miji na wilaya kuingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ya kununua magari ya zimamoto na vifaa vya uokoaji. (Makofi)

Haya, ahsante sana, ni hapo nilitaka nikusomee.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na kwa hiyo, ninaiunga hoja mkono ya Mheshimiwa Tarimo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza na mimi naanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa uhai na leo kupata nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kwenye kutatua changamoto hii ya maji na upatikanaji wake nchini. Pia, nampongeza sana mdogo wangu, rafiki yangu, Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Kundo, Katibu Mkuu wetu, dada yangu, Mwajuma Waziri pamoja na viongozi wote kwa maana mnaisimamia taasisi yenu na idara zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siachi kuwapongeza sana watu wangu ninaofanya nao kazi kwa karibu kwa maana ya DAWASA, kaka yangu Kiula Kingu, Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASA, na dada yangu Everlasting Lyaro ambaye ni Afisa Mahusiano wa DAWASA. Kwa kweli, umeweza kutuunganisha Wabunge wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu nyingi sana ni kwa Mheshimiwa Rais, nilisema juzi wakati nachangia kwa Waziri Mkuu, kwa sababu ya mambo makubwa ambayo ameyafanya, lakini kwa sababu ya muda nitasema tu kwa haraka kwa kutaja. Ndani ya muda huu wa miaka yake mitatu tayari tumeona ma-tank karibu mawili na jingine jipya linajengwa Tegeta A, lenye ujazo wa lita 6,000,000 ambalo linasaidia Goba yote na maeneo machache ya Mbezi, Mshikamano na Mbezi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, lipo tank la Kitopeni maeneo ya Mbezi, Makabe na sehemu ndogo ya Msumi A. Sasahivi linajengwa tank kubwa la ujazo wa lita 9,000,000 kule Bangulo, Ilala, ambalo litasaidia Kusini yote ya Dar es Salaam kwa hiyo, mimi napongeza sana juhudi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, niseme kidogo juu ya eneo la bajeti. Eneo hili limesemwa na wachangiaji wengi na mimi kwa fani yangu siwezi kupita bila kueleza jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko sana, sijui kama miradi itakuja kutimia huko mbele, miradi ambayo imeainishwa humu ya zaidi ya trilioni 1.8 hadi mbili dhidi ya bajeti ya shilingi milioni 627 ambayo imepitishwa kwa Mwaka 2024/2025 tofauti na bajeti iliyopita ya Mwaka 2023/2024 ya shilingi bilioni 756.2. Tofauti yake ni shilingi bilioni 128.4 ambayo ni chini kwa asilimia 17, hii siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziada sitaki kusema mapungufu hayo kwenye fedha za OC (Other Charges), nizungumzie za maendeleo. Kwa Mwaka 2023/2024 zilitengwa shilingi bilioni 695.83, lakini sasa hivi kwa Mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 558.1 tofauti ya shilingi bilioni 137.7, amesema Mwenyekiti wakati anaizungumzia Taarifa ya Kamati. Ipo chini kwa asilimia 18, hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati kwa kukubaliana nayo imetoa mapendekezo na lugha yake imekuwa ngumu kidogo. Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukajikuta tunashindwa kwenda kukubalina na hii bajeti katika kumsaidia Waziri wa Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, lakini mimi nataka niseme au kuchangia na kuchochea juu ya taarifa ya Kamati. Kupungua huku kwa shilingi bilioni 137 tunashangaa ni kwa nini dhidi ya mpango uliopo ambao ni mzuri kufikia ile asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haiendi bure, tunajua mpango huo pia, umeathiriwa sasa hivi na El-Nino na mvua nyingi. Tunashangaa, hapa palikuwa na maboresho makubwa ya miundombinu dhidi ya kupungua kwa fedha. Je, hiyo miundombinu itarudije? Siyo hivyo tu, ni vizuri tujue kuna faida au ushauri tupate wapi hizi fedha zilizoondoka shilingi bilioni 137?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema Kamati, ni vizuri, moja tunaweza tukaenda kwenye Hati Fungani, wala siyo jambo baya. Tunaweza tukajikuta Watanzania wengi wana fedha wakawekeza na kutapata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limeshauriwa na kamati ni shilingi 50 ya Mfuko wa Maji ikaongezwa au ikabaki palepale, lakini kupunguza gharama nyingine kutoka kwenye zile ambazo tunazitoza sasa hivi, lakini ushauri wa ziada kwenye eneo hilo ni lazima ikumbukwe tuna madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 300 ambayo yana-exist hadi sasa hivi na ni lazima yalipwe. Kwa hiyo, kwa kila hali tunatamani Waziri wa Fedha kesho uje na mawazo ya kutafuta fedha nyingine, ili tuzirudishe pale zile shilingi bilioni 137 zilizoondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulizungumza hilo niseme kidogo katika uchimbaji wa visima. Nimefurahi, tungeweza kujiuliza ni kwa nini visima? Swali gumu lingekuwa tunaondoka kwenye majisafi na salama sasa tunarudi kwenye maji ya chumvi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni visima kwa sababu, kama nchi kuna wakati tunaingia kwenye vipindi vigumu vya ukame. Vile visima vinaweza vikatusaidia zile nyakati ambazo hatuna majisafi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu nimefurahia sana. Sasa hivi navitaka hivyo visima haraka hata kesho asubuhi vikachimbwe kule Msumi Centre, Msumi Darajani, Mpiji maeneo ya kwa Mvungi, maeneo ya CCM ya zamani na maeneo ya Torino. Vilevile maeneo ya Msingwa Mpakani Kata ya Saranga, maeneo ya Msigani pale Manzese na kwa Mama Nipe ni muhimu sana. Sisi tunavitaka sasahivi visima hivi pamoja na hiyo miradi mizuri ambayo inakuja baada ya mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la kumalizia ombi letu kwa sasa ambalo tuliliomba sana ni mabomba, distribution ya mabomba. Miradi hii tayari ina vifaa vya maji nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ukija kujumuisha hapo naomba useme, nimeona kwenye bajeti yako fedha za ndani shilingi milioni 214 na za nje shilingi bilioni 6 kwenye eneo la kuendeleza miradi ya Dar es Salaam, utoe commitment hapa ili mabomba yapatikane ya aina zote wananchi wapate maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Mradi wa Msumi ulieleza hapa swali langu la msingi juzi lilijibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri bilioni 13.9 zipo, nimeingia kwenye bajeti nakuta bilioni moja kuunganisha chanzo cha Ruvu Juu na Ruvu Chini ukija uniambie 13.9 zinapatikana wapi kwenye bajeti yako?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho ushauri nikuombe ukija hapa uniambie huu mradi unaondelea wa uuzwaji maji kwenye magari ambao nimeeleza humu ndani ni changamoto na ndiyo maana labda wananchi wanafikiri mabomba hatuletewi kukamilisha miradi aliyowekeza bilioni nyingi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Awamu ya Sita...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja ya taarifa hii au Hotuba wa Wizara ya Maji, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria za Fedha Namba 13 wa Mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, nikiwa mmoja wa mjumbe wa Kamati ya Bajeti tumejadili vizuri jambo hili Muswada huu ukiwa ni Muswada muhimu kwa maudhuhi yake yote.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema lolote nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli tunaendelea kusema, Mama anasikia kwa haraka sana na anatoa maelekezo kwa haraka sana kwa ajili ya utekelezaji wa mambo mengi sana ili aweze kwenda kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Rais ni kwa sababu ameona kuwa kuna kila sababu ya kurekebisha sheria kadhaa ili kuvutia wawekezaji kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na ya kielelezo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile Muswada huu unakuja kuonesha ukweli juu ya Mheshimiwa Rais ambaye anaonesha kwa vitendo juu ya namna bora ya kutanzua vile vikwazo vilivyopo wakati tunatekeleza miradi yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na sehemu tano au sheria ndogo ndogo tano ambazo zipo ndani ya Muswada huu mimi nitajielekeza katika maeneo mawili. Moja ni Sheria Ushuru wa Bidhaa Sura ya 147. Hapa tunarekebisha kifungu cha128 ambacho Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Fedha anapata idhini ya Baraza la Mawaziri katika kusamehe ushuru kwenye bidhaa ambazo zitatumika kwenye miradi hii maalum na mahiri maalum. Marekebisho hayo yametusaidia kwenda kwenye hili jambo ambalo wengi wamejadili, kupandisha ushuru wa bidhaa za mvinyo kutoka takriban Shilingi 2,466 mpaka shilingi 5,600, jambo hili limekuwa ni muhimu sana. Umuhimu wake mkubwa ni kwamba unaenda kuinua kilimo chetu cha mvinyo, wengine tumesema tongwa, wengine tumezungumza lugha nyingine.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa sana ni kilimo chetu cha zabibu na vilimo vya aina hiyo kuweza kupata nafasi. Ni ukweli hatujafikia tu kusema 5,600 kutoka 2,466, tumeangalia kwenye nchi kadhaa za Afrika Mashariki kama comparative. Nchi nyingi zimetokea kati ya 5,000 mpaka 5,500, ambapo unaweza ukaona kwetu kwa kuwa Shilingi 2,400 na kitu ilikuwa inaweza ikasababisha hata wawekezaji wengi ambao wako hapa wakaweza kuchukua au kununua mali ghafi za mvinyo kutoka nje ya nchi. Jambo ambalo ulikuwa ni hatari sana kwa wakulima wetu na kwa muktadha mzima wa viwanda vyetu ambavyo vinachakata zao hili. Kwa hiyo, kama wazo na Kamati ilivyoshauri na kukubali mawazo ya Serikali au mapendekezo ya Serikali kwenye Muswada huu kwa kweli niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mlione hili kuwa ni jambo muhimu kwa muktadha mkubwa sana wa kuweza kuinua viwanda vyetu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini ni lazima, wengi wamesema, katika jambo hili kuna maangalizo kadhaa. Kinywaji hiki cha mvinyo ni luxury, wengine wanatumia kama dawa. Kwa hiyo, suala la ubora ni suala la ambalo hatuwezi ku- compromise, ni lazima ubora ukazingatiwe sana, hili wengi wamesema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni uzalishaji (production) kwenye volumes. Kama mfano amezungumza sana Mheshimiwa aliyemaliza kusema ameweka kwenye asilimia 30 na 70. Ni hatari kama tutakuwa kama Taifa sasa bado tukawa tunazalisha chini ya asilimia 50, halafu wakati kabla hatujabadilisha sheria hii ilikuwa tunapata kutoka nje zaidi ya asilimia 50, itakuwa ni hatari. Niombe sana Wizara ya Kilimo imepewa bajeti kubwa sana, zaidi ya mara nne katika miaka miwili hii iliyokwisha. Tangu bilioni mia mbili na hamsini na kitu mpaka bilioni mia tis ana kitu. Kwa kweli walione jicho lao likajielekeze katika eneo hili. Tunabadilisha Muswada wa sheria huu katika kifungu hiki lakini tayari fedha ziko nyingi Mama Samia kashajielekeza Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana mjielekeze kwenye kuweka mikataba ambayo hatuwezi kurudi nyuma. Tukaone ubora wa bidhaa hizi lakini vile vile tukaone uzalishaji unakuwa mkubwa ili tusiweze kuona tunadhurika kutokana na mabadiliko haya ambayo tumeyadhamiria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie kidogo juu ya Sheria ya Ushuru wa Mafuta wa Barabara (The Road Fuel Tolls Act, 2022). Hapa tunabadilisha Kifungu Namba Nane ili pia kumpa Mheshimiwa Waziri mamlaka ya kusamehe ushuru wa mafuta kwa miradi ya uwekezaji mahiri na mahiri maalum. Si jambo baya, ni jambo zuri lakini tuendelee kuangalia. Uzoefu mwingi katika maeneo mengi sehemu ambayo tumepata hasara kama Taifa ni eneo la msamaha wa mafuta, wengi wamesema migodini na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, lakini nishukuru sana Kamati ya Bajeti imeliona na imetoa mapendekezo kadhaa kwenye eneo hili. Na kubwa ni katika mapendekezo kadhaa, na ni vizuri tufahamu. Pendekezo la kwanza tumeangalia muda, pawepo na muda maalum. Tunajua miradi inaendelea kutekelezwa. Pamoja na kuangaliwa miradi hii tujue ili tukiifuatilia tunajua kabisa. Ndani ya mwaka mmoja tuweze kuangalia tumenufaika jinsi gani katika miradi hii mahiri na mahiri maalum ambayo inatekelezwa. Tukiacha wazi maana yake inawezekana miradi imekamilika halafu watu wakawa wanatupiga kupitia msahaha huu ambao tumeuweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile tunatambua kama nchi tunatumia mfumo mmoja wa kuagiza mafuta (bulk procurement system). Ni mfumo mzuri tumewahi kuujadili ndani ya Kamati vizuri kabisa, na kama nchi tunaona bado tunafaidika na mfumo huo wa kuangiza pamoja. Sasa, inabidi tutofautishe mafuta yapi yanakuja katika mfumo huo wa pamoja na mafuta yapi ambayo yanakuja kwa ajili ya miradi maalum na mahiri maalum. Ni vizuri sana, ni muhimu. Kama tutatumia vinasaba sawa, kama tutatumia utaratibu wa uuzaji sawa, lakini ni jambo muhimu sana ili watu wasije wakapitia kwenye upenyo huo kwenda kutuumiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshauri pia kuweka mifumo ya usimamizi ili kuzuia matumizi mabaya ya mafuta ya miradi. Ni vizuri mifumo ikawekwa mapema, hata Mheshimiwa Waziri amesema kwenye taarifa yake, kwamba wanampango wa kufuatilia kwa karibu sana mafuta haya yanavyoingia. Mimi ninaona kwa umahiri na umakini wa Mheshimiwa Waziri kwenye jambo hili atatia nguvu sana na jicho kubwa na watalaam wake ili tusiweze kuanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo niseme juu ya maoni ya jumla. Kamati imeshauri sana misamaha ya kodi hii lazima iangaliwe kwa Pato la Taifa. Ndani ya mpango wetu wa miaka mitano tunaoendelea nao tumekubaliana wenyewe na tumejiwekea wenyewe kwamba misamaha ya kodi isizidi asilimia moja; hili ni jambo zuri. Sasa, Kamati inatoa ushauri kuwa wakati umefika twende tukafanye tathimini ya kina tuweze kuona mpaka sasa kwa misamaha yote ambayo imetolewa nchini imekaa vipi, ina ubora kiasi gani, tumefanikiwa au hatujafanikiwa; na kama haijazidi imezidi asilimia moja au haijazidi asilimia moja? Hili ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona ni muhimu sana nichangie katika maeneo hayo mawili, na nitumie nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu waweze kuridhia Muswada huu wa Sheria Namba 13 wa Mwaka 2022 uweze kupita bila kikwazo chochote kwa maslahi mapana ya nchi yetu na wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)