Primary Questions from Hon. Issa Jumanne Mtemvu (19 total)
MHE. ISSA J. MTEMVU Aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza kikamilifu Waraka Na. 3 wa mwaka 2015 kuhusu Muundo wa Kada ya Uhasibu na Ukaguzi wa Ndani?
(b) Je, ni lini Kitengo cha Uhasibu na Fedha katika Wizara na Sekretarieti za Mikoa zitapewa hadhi ya kuwa Idara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima pamoja na afya njema. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa imani yake aliyokuwa nayo kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, nijibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Waraka Na. 3 wa mwaka 2015 kuhusu Muundo wa Kada ya Uhasibu na Ukaguzi wa Ndani ulianza kutekelezwa mwezi Julai, 2018 kwa kutenganisha Kada ya Maafisa Hesabu na Wahasibu. Kwa mujibu wa muundo huo mpya Wahasibu na Wakaguzi ni wale ambao wana CPA na wale wasio na CPA wanatambulika kama Maafisa Hesabu na Maafisa Ukaguzi.
(b) Mheshimiwa Spika, kuhusu kupandisha hadhi vitengo vya uhasibu na fedha katika Wizara na Sekretarieti za Mikoa kuwa idara, katika kuandaa miundo ya taasisi, vigezo kadhaa hutumika ili kufikia maamuzi ya kuwa Idara, Vitengo na Sehemu. Kwa kuwa miundo hii hufanyiwa marekebisho mara kwa mara kwa kushirikiana na wataalamu wa miundo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na kujadiliwa katika ngazi ya maamuzi, ni mategemeo yetu kwamba Serikali itakapoona kuwa Kitengo cha Uhasibu na Fedha kinakidhi vigezo vya kuwa idara, kitapewa hadhi hiyo.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa Hati katika Mradi wa Urasimishaji kwa Wananchi wa Kata za Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani, Goba na Saranga?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Kurasimisha na Kuzuia Makazi Yasiyopangwa Mijini, programu ambayo ilianza 2013 na inakwenda kwisha 2023 katika maeneo mbalimbali nchini. Kuanzia mwaka 2015, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipanua wigo wa kushirikisha sekta binafsi kufanya kazi za urasimishaji ambapo jumla ya kampuni 163 za upangaji na upimaji ardhi zilisajiliwa zimewezesha kuandaa michoro ya urasimishaji 3,832 na jumla ya viwanja 1,638,062 katika mamlaka za upangaji 134. Kampuni hizi zinafanya kazi kwa kuingia mikataba na wananchi kupitia Kamati za Urasimishaji za Wananchi Nchini na kuratibu wa mamlaka za upangaji kuchangia gharama za urasimishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata sita za Saranga, Mbezi, Goba, Kwembe, Msigani na Kibamba, jumla ya wananchi 30,216 wamechangia gharama za upangaji na upimaji kati ya wananchi 147,299 waliotegemewa kuchangia. Aidha, Kampuni za urasimishaji kwa kushirikiana na Serikali zimeandaa michoro ya Mipangomiji 384 yenye viwanja 141,881 ambapo kati ya hivyo, viwanja 8,316 vimepimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na kutoa hati katika viwanja 8,316 ambavyo upimaji wake umekamilika katika Kata ya Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani, Goba na Saranga ambapo mpaka sasa kuna jumla ya hati 1,754 zilizoandaliwa kati ya maombi 1,925 yaliyowasilishwa. Serikali pia imekwishaandaa ankara 2,889 na kusambaza kwenye mitaa ya Kata hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna changamoto ya wananchi kutolipa ankara zao kwa wakati ili kuchukua hati zilizoandaliwa. Hivyo tunawasihi wananchi wa maeneo hayo kulipia gharama za umilikishwaji ili waweze kupewa hatimiliki. Vilevile kampuni zilizopewa kazi ya urasimishaji kukamilisha kwa wakati kazi walizopewa kwa kuzingatia mwongozo wa urasimishaji uliotolewa na Wizara. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukaimu muda mrefu kwa watumishi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Sekretarieti za Mikoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uwepo wa Watumishi wanaokaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu na uchambuzi uliofanyika unaonesha kuwa, watumishi 1,496 wanakaimu nafasi za uongozi katika Taasisi mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Wilaya na Sekretarieti za Mikoa. Kati ya hao, watumishi 332 wanakaimu nafasi zao wakiwa na vibali halali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi na Watumishi 1,164 wanakaimu nafasi zao bila ya kuwa na vibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi, Aidha, Kati ya watumishi hawa 1,164 ambao wanakaimu nafasi bila vibali vya Katibu Mkuu Utumishi, jumla ya watumishi 543 hawana ºifa za kukaimu nafasi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kutatua changamoto hii, ofisi yangu imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kukusanya taarifa za maafýsa Waandamizi na Wakuu 7,008 katika Utumishi wa Umma wakiwemo watumishi wanaokaimu nafasi hizo ili wafanyiwe upekuzi kwa ajili ya kujaza nafasi wazi za uongozi na zinazokaimiwa kwa muda mrefu.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Mbezi Shule – Mpiji Magohe – Bunju kupitia Mabwe Pande na Kibamba Njia Panda – Mpiji Magohe kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa J. Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mbezi Shule – Mpiji Magohe – Bunju kupitia Mabwe Pande ni barabara inayotambulika kwa jina la Mbezi Victoria – Mpiji Magohe hadi Bunju yenye urefu wa kilometa 25; na barabara ya Kibamba Njia Panda – Mpiji Magohe inatambulika kwa jina la Kibamba Shule hadi Mpiji Magohe ambayo ina urefu wa kilometa 8.7.
Mheshimiwa Spika, barabara hizi ni sehemu ya barabara ya Mzunguko wa Nje wa jiji la Dar es Salaam (Outer Ring Roads) inayoanzia Bunju – Mpiji Magohe – Kibamba – Pugu Kajiungeni – Mzinga – Tuangoma mpaka Kigamboni ambayo ina urefu wa kilometa 61.
Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika mpango wa kujenga barabara hizi kwa kiwango cha lami. Katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 jumla ya Shilingi milioni 600 zimetengwa kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya mzunguko wa nje inayoanzia Bunju – Mpiji Magohe – Kibamba – Pugu Kajiungeni – Mzinga – Tuangoma mpaka Kigamboni na mzunguko wa ndani inayoanzia – Mbezi Mwisho – Kifuru – Banana – Kipara hadi Kigamboni. Taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri wakufanya kazi hiyo zipo katika hatua za mwisho za uchambuzi wa zabuni. Mara baada ya kazi hiyo kukamilika, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutatua mgogoro wa bomoabomoa wa nyumba za wananchi zilizokuwa pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kibamba ulioanza mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka 2017/2018, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sekta ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam iliondosha nyumba na mali za watu zilizokuwa zimejengwa kinyume cha sheria ndani ya eneo la hifadhi ya Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kibamba ikiwa ni maandalizi ya kupanua barabara hiyo toka njia mbili hadi njia nane ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 1932 pamoja na Kanuni zake za mwaka 1955 na marekebisho yake Na. 13 ya mwaka 2009, imeainishwa kwamba upana wa hifadhi ya barabara hiyo kuanzia Kimara Stop Over hadi Kibaha (TAMCO) ni mita 121 kutoka katikati ya barabara kila upande. Hivyo, nyumba na mali zote zilizokuwa ndani ya eneo hili walikuwa wako ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kinyume na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuwaondoa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha utekelezaji wa mradi huu lilifanyika kwa kufuata Sheria ya Barabara na hadi sasa Serikali haina mgogoro wowote na wananchi walioondolewa ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kutatokea mgogoro kati ya wananchi wa eneo la Kimara hadi Kibamba kuhusiana na bomoa bomoa ya nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro kinyume na sheria, mgogoro huo utatatuliwa kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, kuna Mkakati gani wa kukabiliana na mafuriko katika Mto Mbezi yanayosababisha uharibifu wa miundombinu ya shule na makazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazotokana na mafuriko katika mito yetu nchini ukiwemo Mto Mbezi. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali imeandaa Mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam wa Mwaka 2021. Mwongozo huu unalengo la kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kusafisha tope na mchanga kwenye mito na mabonde ili kuruhusu uwepo wa mtiririko mzuri wa maji kuelekea baharini ili kuepuka athari za mafuriko.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kumhakikishia Mbunge kuwa, itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mwongozo ili kutatua changamoto ya mafuriko katika mito na mabonde yaliyopo katika Mkoa wa Dar es Salaam ili kukabiliana na madhara ya mafuriko na kuhakikisha miundombinu ya shule na makazi ya watu yanaendelea kuwa salama. Nakushukuru.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia Pori tengefu la Mabwepande kama chanzo cha mapato?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha Pori la Akiba Pande linaendelea kuwa kitovu cha utalii katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani kuwa chanzo cha mapato, Serikali imetumia kiasi cha shilingi 710,789,122 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya utalii zikiwemo public camp site Mbili katika eneo la Msakuzi na Jomeke na Picnic Site Mbili eneo la Bwawani na Crater pamoja na ujenzi wa uzio wa bustani ya wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hiyo imekamilika na imeanza kutumiwa na watalii ambapo kwa sasa shughuli mbalimbali zikiwemo mbio za Marathon, nyama choma festival, utalii wa kutembea kwa miguu na kuendesha baiskeli, upigaji picha na matamasha mbalimbali vimeanza kutumika.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli utakamilika pamoja na kuhakikisha Kituo hiki kinafanya kazi kama kilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Mabasi cha Magufuli kinachoendelea na ujenzi katika eneo la Mbezi Luis kilianza ujenzi Januari, 2019 kwa mkataba wa miezi 18, hivyo ujenzi ulipaswa kukamilika Julai, 2020.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi aliongezewa muda wa ujenzi hadi Juni, 2022 kutokana na kuchelewa kutolewa kwa msamaha wa kodi wa vifaa vya ukamilishaji wa ujenzi huo.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2022, kiasi cha shilingi bilioni 53.09 sawa na asilimia 94.73 zilikuwa zimelipwa kukamilisha ujenzi. Aidha, tarehe 14 Machi, 2022, Serikali imetoa msamaha wa kodi na sasa Mkandarasi anaendelea na manunuzi ya vifaa ili kazi ya ujenzi iendelee na kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2022. Kukamilika kwa kazi hizo kutafanya kituo hicho kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Misamaha ya VAT inayotolewa inaleta tija kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha misamaha ya kodi inakuwa na tija katika uchumi na jamii kwa ujumla, orodha ya bidhaa na vifaa vinavyostahili msamaha wa kodi inaandaliwa, kuhakiki orodha ya bidhaa na vifaa, kuhakikisha mwombaji anajaza fomu maalum inayothibitisha ununuzi wa bidhaa au vifaa husika pamoja na kufanya kaguzi za mara kwa mara dhidi ya misamaha iliyotolewa ili kuthibitisha iwapo matumizi ya bidhaa au vifaa vilivyosamehewa kodi vimetumika kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutekeleza matakwa ya kisheria husika katika ufuatiliaji na tathmini ya misamaha ya kodi ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ili kuhakikisha kuwa misamaha ya kodi inatolewa kwa kuzingatia sheria na inatumika kama ilivyokusudiwa.
MHE. ISSA J MTEMVU aliuliza: -
Je, nini mkakati wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka baadhi ya maeneo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 2.1. 2 cha Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la mwaka 2008 na Kanuni D.6 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani wa wazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako kuwa, Serikali haitoi ajira kwa kuzingatia maeneo. Waombaji wote wa kazi Serikalini huchukuliwa kuwa na haki sawa na hivyo wote hupimwa na kuchujwa kwa vigezo vinavyofanana bila upendeleo wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahimize Watanzania wote wenye sifa stahiki kutoka maeneo yote nchini wajitokeze kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa na Mamlaka zinazoshughulikia ajira nchini ili waweze kushindana na waombaji wengine.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kujenga kivuko cha juu barabara ya njia nane eneo la Magari Saba Mbezi ili kulinda uhai wa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, eneo la Magari Saba, eneo la Mbezi, limekwishawekwa kivuko cha pundamilia (zebra crossing) kwa wapita kwa miguu ili kuwawezesha watumiaji wa barabara hiyo kuvuka kwa usalama katika eneo hilo, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, ni lini Wananchi wa Mpiji – Magohe, Kibesa, Msumi, Makabe, Msingwa, Ukombozi na Goba watapata majisafi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa Miradi ya Maji ya Changanyikeni - Bagamoyo, ujenzi wa matenki ya maji katika maeneo ya Mshikamano, Tegeta A, Malolo na mradi wa usambazaji maji kusini mwa Dar es Salaam ambapo kukamilika kwa miradi hii kutawezesha wakazi wa maeneo ya Mpiji-Magohe, Kibesa, Msumi, Mbezi, Makabe, Msakuzi, Msingwa, Ukombozi, King'azi, Malamba Mawili, Msingwa, Kipesa Mapwepande, Mpakani na Goba kupata huduma ya majisafi, salama na ya kutosheleza.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kutenga sehemu kwa ajili ya shule ya sekondari katika Pori Tengefu Mabwepande lililopo Kibesa, Jimbo la Kibamba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba Pande lenye ukubwa wa kilometa za mraba 15.39 limetengwa kwa sababu kuu zifuatazo; kufyonza hewa chafu (carbon sink) inayotokana na shughuli za kibinadamu ili isisababishe madhara kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, na kuhifadhi mimea na viumbe hai wengine kama wadudu na wanyamapori ambao ni muhimu katika kuhakikisha mifumo ikolojia ya maeneo husika inaimarika na kutoa huduma za kiikolojia. Aidha, eneo hilo pia linatumika kwa shughuli za utalii na kwa sasa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya pori hilo ili kuvutia watalii wengi na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.
Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo na kuzingatia kwamba eneo hilo ni dogo, Wizara haioni busara kuendelea kumega eneo hilo kwa shughuli za kijamii.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Sport Arena katika Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali namba 252 la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na mpango wa ujenzi wa Sports and Arts Arena katika Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma yenye thamani ya jumla ya Shilingi za Kianzania bilioni 550 kwa ushirikiano wa Serikali na Wadau. Wizara imeshakamilisha hatua za awali za kutengeneza michoro ya Arena hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vikao vya mashauriano baina ya Wizara na Mkoa wa Dar es Salaam vinaendelea ili kukubaliana sehemu ya ujenzi wa viwanja hivyo. Eneo la Luguruni lililopo Manispaa ya Ubungo lenye ukubwa wa ekari 10.5 ni kati ya maeneo yanayotarajiwa kupendekezwa kwa ujenzi wa mradi huo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, ujenzi utaanza mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya malipo ya fidia kwenye miradi ya barabara za TANROADS zinazopita kwenye makazi ya watu Kibamba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao mali zao zinaathiriwa na miradi ya ujenzi wa barabara hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007. Wananchi wote ambao mali zao ziko nje ya eneo la hifadhi ya barabara wanalipwa fidia na wale ambao mali zao zimo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara hawastahili kulipwa fidia. Hii ni kwa wananchi wote nchi nzima ikiwemo na wananchi wa Jimbo la Kibamba, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, lini ujenzi wa Vibanda vya Wajasiriamali pembezoni mwa Barabara ya Njia Nane Kimara hadi Kiluvya utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS,) imekamilisha Usanifu wa Vibanda 950 vya Wajasiliamali vitakavyojengwa pembezoni mwa Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya. Zabuni ziko katika hatua ya uchambuzi (evaluation) na ujenzi unatarajiwa kuanza Mwezi Desemba, 2023 na utekelezaji wake unakadiriwa kuchukua muda wa miezi sita, ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, ipi kauli ya Serikali juu ya kutokamilika kwa Miradi ya Maji katika Jimbo la Kibamba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa miradi mitatu ya usambazaji wa maji kutokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Bagamoyo (2B-2F), Mshikamano na Kitopeni ambapo miradi hiyo inanufaisha wakazi wapatao 210,876 wa Jimbo la Kibamba.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji Kusini mwa Dar es Salaam (Bangulo) ambapo utekelezaji wake umefikia 25% na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024. Mradi huo ukikamilika utanufaisha wakazi wapatao 271,863 wa Jimbo la Kibamba.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukamilisha utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Jimbo la Kibamba.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -
Je, hadi sasa Serikali ina madeni kiasi gani ya watumishi wa umma yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2024 madeni ya watumishi wa umma yaliyohakikiwa na kukidhi vigezo vya kulipwa yanayohusu likizo, uhamisho na kusafirisha mizigo baada ya kustaafu yalikuwa na jumla ya shilingi bilioni 285.1. Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya madeni yenye ujazo wa shilingi bilioni 55.9 yamelipwa. Aidha, Serikali itaendelea kulipa madeni ya watumishi yasiyo ya kimshahara kila mwaka kwa kuzingatia taarifa ya uhakiki wa madeni.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza:-
Je, upi mkakati wa Serikali wa kukabiliana na matumizi ya mkaa na kuni nchini ili kulinda mazingira?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Mtemvu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kuanzia mwaka 2024 hadi 2034 ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia. Mkakati huu unalenga kuhakikisha angalau 80% ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mkakati huu unalenga kupunguza gharama za nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, kuimarisha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uhakika ya nishati safi ya kupikia, kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia, pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)