Primary Questions from Hon. Salim Alaudin Hasham (10 total)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA - K.n.y. MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani kutengeneza barabara za Ulanga na kutenga bajeti ya dharura ili TARURA iweze kukarabati barabara mara tu zinapoharibika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia TARURA ya Halmashauri Ulanga usafiri ili kuongeza ufanisi katika kazi zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alaudin Hasham Salim, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Serikali imeongeza fedha za matengenezo ya barabara kutoka shilingi milioni 471.49 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi shilingi 671.49 katika mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 42.4. Aidha, Serikali imekuwa ikitenga 5% ya bajeti ya fedha za matengenezo ya barabara kwa ajili ya kazi za dharura. Kupitia fedha za dharura, TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga imejenga madaraja ya Epanko na Ikangao kwa gharama ya Shilingi milioni 64.5 katika mwaka wa fedha 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya magari kwa ajili ya usimamizi wa miradi ya barabara na uendeshaji wa ofisi za Mameneja wa TARURA katika Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga. Wakala una magari 192 yaliyopo katika hali nzuri kwenye Mikoa na Halmashauri, magari 107 mabovu na magari 15 katika Ofisi za Makao Makuu.
Katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA imetenga shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ununuzi wa magari 26 na pikipiki tisa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA imeidhinishiwa shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya ununuzi wa magari 30. Magari hayo yatapelekwa kwenye Halmashauri mbalimbali ambazo hazina magari na Halmashauri ambazo hazina Magari kama Ulanga, zitapewa kipaumbele. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Ifakara – Mahenge utaanza kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alaudin Hasham Salim, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ifakara –Mahenge ni sehemu ya Barabara Kuu ya Mikumi, Kidatu, Ifakara, Lupiro, Mahenge/Malinyi, Kilosa kwa Mpepo, Londo hadi Lumecha yenye urefu wa kilometa 547 ambayo inaunganisha Mikoa ya Ruvuma na Morogoro. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ilikamilika mwaka 2018 kwa lengo la kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa ujenzi wa Daraja la Magufuli lenye urefu wa mita 384 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilometa 9.142 umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Ifakara – Lupiro – Mahenge utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami zikiendelea, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara husika ili ipitike majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vtuo vya kutolea huduma za afya Wilayani Ulanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Alaudin Hasham, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kuongeza bajeti katika Wilaya ya Ulanga na nchini kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya dawa katika Halmashauri ya Wilaya Ulanga imeongezeka kutoka shilingi milioni 337.49 (Serikali Kuu, fedha uchangiaji huduma na Mfuko wa Pamoja wa Afya) mwaka 2015/2016 hadi shilingi milioni 475.53 mwaka 2020/2021. Upatikanaji wa dawa muhimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga umeongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2015/2016 hadi kufikia asilimia 82.2 mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi bado kuna changamoto ya upungufu wa baadhi ya dawa na vifaa tiba vituoni. Serikali itaendelea kuboresha bajeti na usimamizi wa bidhaa hizi ili kuondoa changamoto hiyo.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. ALAUDIN H. SALIM aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali mpya ya Wilaya ya Ulanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alaudin Hasham Salim, Mbunge wa Jimbo la Ulanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ina Hospitali ya Wilaya Ulanga ambayo ni kongwe na chakavu. Serikali itafanya tathmini ya hospitali hiyo ili kufanya maamuzi ya kuikarabati katika bajeti ya mwaka 2023/2024 au kuweka mpango wa kujenga hospitali mpya. Ahsante.
MHE. ALAUDIN H. SALIM aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafungua barabara ya kimkakati inayotoka Mahenge mpaka Liwale kupitia Malinyi, Mlimba, Njombe na Songea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alaudin Hasham Salim, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara inayotoka Mahenge kwenda Liwale ni Mahenge - Mwaya – Ilonga – Liwale ambapo sehemu ya Mahenge hadi Ilonga imefunguliwa na inapitika majira yote ya mwaka. Hata hivyo, kutoka Ilonga kwenda Liwale hakuna barabara kwa Mwalimu Nyerere na itahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu wa awali kuona iwapo inakidhi vigezo vya mazingira kabla ya kufunguliwa.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga kwa kwango cha lami barabara ya kutoka Ifakara hadi Mahenge?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Alaudin Hasham, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Ifakara Kibaoni hadi Mahenge Mjini yenye urefu wa kilometa 55.4 ni sehemu ya Barabara ya Ifakara – Mahenge– Malinyi – Kilosa kwa Mpepo
– Londo hadi Lumecha yenye urefu wa kilometa 435 ambayo Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa EPC+F. Uchambuzi na tathmini ya zabuni za kumpata Mkandarasi na Mwekezaji atakayetekeleza mradi huu zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Juni, 2023, ahsante. (Makofi)
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
Je, lini serikali itajenga skimu za umwagiliaji katika Jimbo la Ulanga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Alaudin Hasham, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Skimu za Euga, Ulanga, hekta 440, Minepa, Ulanga, hekta1,800 na Lupilo, Ulanga, hekta 3,000. Mara baada ya zoezi la upembuzi yakiniffu kukamilika skimu hizi zitaanza kujengwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Hospitali mpya ya Wilaya ya Ulanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ilianza kutoa huduma mwaka 1905 kama Kituo cha Afya na baadaye kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali. Aidha, hospitali hii ni miongoni mwa hospitali kongwe 50 ambazo Serikali ilizifanyia tathmini, kwa ajili ya ukarabati mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imetenga shilingi bilioni 27.9 za ukarabati wa hospitali kongwe 31 zilizobaki ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Ulanga, ambayo imepokea shilingi milioni 900 ambapo ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali unaendelea, ahsante.
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza: -
Je, lini Serikali itatoa majibu juu ya umiliki wa Msitu wa Hewa ya Ukaa uliopo Kituti hadi Mgolo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 23 cha Sheria ya Misitu kimeweka utaratibu wa uanzishaji na usimamizi wa maeneo ya misitu kisheria. Kupitia Tangazo la Serikali Na. 783/2022, Wizara ilikamilisha taratibu za awali za kutoa notisi ya siku 90 za nia ya Serikali ya kuanzisha rasmi Msitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga. Kwa sasa Wizara inakamilisha taratibu za kisheria za kuanzisha msitu huo ambao utakuwa chini ya umiliki wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza:-
Je, lini Serikai itajenga Barabara ya Ifakara – Malinyi – Namatumbo – Mahenge Mjini hadi Lupiro kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshasaini mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo – Lumecha kwa utaratibu wa EPC + F. Kwa kawaida, ujenzi wa barabara kwa utaratibu wa EPC + F unahusisha kufanya usanifu wa barabara kabla ya kuanza ujenzi. Kwa sasa mkandarasi ameanza na anaendelea na usanifu wa kina. Aidha, Serikali na wakandarasi wanaendelea na taratibu za kupata fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa miradi yote ya EPC + F ikiwemo barabara hii, ahsante.