Primary Questions from Hon. Tarimba Gulam Abbas (12 total)
MHE. TARIMBA G. ABBAS Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kazi ya ujenzi wa mradi wa Mto Msimbazi ambao umetajwa katika Bajeti ya mwaka 2021/2022?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge wa Jimbo la kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali na Benki ya Dunia inatarajia kufanya majadiliano ya mapendekezo ya awali ya mradi mwezi Desemba 2021 na kusaini mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 120 ifikapo mwezi Machi 2022 na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2022 baada ya kukamilisha masharti yote ya kutekeleza mradi.
Mheshimiwa Spika, huu ni mradi wa kukabiliana na mafuriko katika bonde la Mto Msimbazi. Mradi huo kwa sasa upo katika hatua za maandalizi ambapo usanifu wa miundombinu husika pamoja na nyaraka muhimu kwa ajili ya masuala ya mazingira na fidia zinaandaliwa.
Mheshimiwa Spika, Kimsingi mradi huu utahusisha pia ujenzi wa daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390; Upanuzi wa mto kwa upande wa chini kuanzia barabara ya Kawawa hadi daraja la Salander ili kuruhusu maji ya mvua kwenda baharini kwa haraka;
Mheshimiwa Spika, Uimarishaji wa kingo za mto msimbazi katika maeneo korofi kwa upande wa juu katika maeneo ya Tabata na Kinyerezi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo;
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa vitega mchanga na vituo vya kuhudumia mto kwa ajili ya kupunguza kiwango cha mchanga kinachotuama eneo la chini la Mto Msimbazi;
Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa matuta kwa upande wa chini wa mto Msimbazi (kuanzia Daraja la Selander hadi Barabara ya Kawawa) yatakayoruhusu matumizi mbalimbali ya ardhi ikiwemo City Park eneo la Jangwani pamoja na maendeleo ya makazi maeneo ya Mchikichini, Sunna na Hananasif; Program za kuboresha usimamizi wa takangumu katika Kata 18 zinazozunguka bonde la Mto Msimbazi; na Kurudishia uoto wa asili katika maeneo yenye mikoko, maeneo yenye ardhi oevu, pamoja na misitu ya Pugu na Kazimzumbu, Wilayani Kisarawe.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mto Msimbazi ambao umeainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira; kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas Mbunge Jimbo la Kinondoni naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inatekeleza mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project) kwa mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza DFID, inatekeleza programu ya Tanzania Urban Resilience Programme ambayo imelenga kuzisaidia halmashauri na Serikali Kuu katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuanzia, programu itaanza kutatua changamoto zinazolikabili Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari DFID imeshatenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 20 kwa ajili ya Bonde la Mto Msimbazi. Pia Benki ya Dunia, kupitia mradi wa DMDP, imekubali mkopo wa nyongeza wa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba Gulam Mbunge wa Kinondoni:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kubadili eneo la bonde la Mto Msimbazi kuwa eneo la uwekezaji na fursa mbalimbali. Ili kufikia azma hiyo, usanifu wa mradi huo umekamilika. Utekelezaji wa mradi utaanza baada ya kupata idhini ya Serikali kuhusu matumizi ya fedha hizo za mkopo kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ili kupunguza athari za mafuriko kwa sasa, kipande cha Mto Msimbazi cha daraja la Jangwani kinafanyiwa usafi wa mara kwa mara na wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Utoaji wa leseni za biashara kwa biashara ndogo za maduka katika Manispaa ya Kinondoni umekuwa na changamoto kutokana na wafanyabiashara hao kutokuwa na Tax Clearence kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Je, ni kwa nini Serikali isiiagize TRA kwenda mitaani na kubaini biashara hizo na kuzisajili kwa lengo la kurahisisha utoaji wa Tax Clearance ili leseni ziweze kutolewa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto zinazopelekea wafanyabiashara kutopatiwa Tax Clearance ambalo ni takwa la kupatiwa leseni ya biashara, ni pamoja na wafanyabiashara hao kutosajiliwa na kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN Number).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto hii kwa wafanyabiashara, Serikali imeongeza kasi ya zoezi la usajili wa walipakodi katika jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na kampeni ya mlango kwa mlango ili kutatua changamoto zinazowakabili walipakodi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kodi, kuwatambua walipakodi wapya na kuwasajili. Lengo la kampeni hii ni kurahisisha zoezi la usajili wa walipakodi kwa kuwasogezea karibu huduma hii wafanyabiashara wote nchini, kwa kuwafuata katika maeneo yao ya biashara badala ya kuwasubiria waje katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili maalum limeanza mwezi Agosti, 2021 katika mikoa yote ya kikodi katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Manispaa ya Kinondoni na litaendelea nchi nzima. Ni matumaini ya Serikali kuwa zoezi hili litaongeza idadi ya walipakodi waliosajiliwa na hivyo kurahisisha upatikanaji wa tax clearance ili leseni za biashara ziweze kutolewa kwa uharaka zaidi. Ahsante.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 ni fedha kiasi gani kwa ajili ya vijana, akinamama na watu wenye ulemavu zimekopeshwa na kurejeshwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa mikopo inayotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia mikopo hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2020 Serikali kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ilitoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 133. Katika kipindi hicho jumla ya shilingi bilioni 92.21 sawa na asilimia 69.32 zilirejeshwa kutoka kwa vikundi vya wanufaika.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiweke ulazima wa hitaji la kisheria kuwa Taxpayer Tax Audit ifanyike kila mwaka badala ya kusubiri miaka mitatu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438 kifungu cha 45 imeainisha mamlaka ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya ukaguzi au uchunguzi wa masuala ya kodi kwa walipakodi wote, wakati wowote na sio kwa kuzingatia muda wa miaka mitatu isipokuwa ni pale tu inapoonekana kuna viashiria vya upotevu wa mapato ya Serikali ili kukomboa kodi ambayo haijakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa viashiria hivyo ni Pamoja na: -Mwenendo usioridhisha wa ulipaji kodi; Mlipakodi kutokufuata Sheria za kodi; aina ya biashara au shughuli ya kiuchumi anayofanya mlipakodi husika; na suala lingine lolote ambalo Kamishna Mkuu ataona ni muhimu ili kuhakikisha kuwa kodi stahiki inakusanywa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa ili kupunguza ulazima wa Kamishna Mkuu kufanya uchunguzi na ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipa kodi ni muhimu walipakodi wote kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kodi iliyopo. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu majengo yaliyopo maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 45 lililoulizwa na Mheshimiwa Tarimba Abbas Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba majengo yote yaliyosimama yaendelezwe kwa kikamilifu kama ilivyoainishwa kwenye milki zao na vibali vya ujenzi ili majengo hayo yasitumike kwa matumizi yasiyofaa.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, nini juhudi za Serikali kuweka mifumo rafiki ya kurahisisha ufanyaji wa biashara ili kuvutia zaidi uwekezaji nchini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya maboresho ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria, kuweka mifumo ya kielektroniki, kufuta au kupunguza tozo na ada kero, kuondoa muingiliano wa majukumu katika baadhi ya taasisi, kuunganisha mifumo ya kielektroniki katika taasisi mbalimbali ili iweze kuwasiliana, kuweka miongozo na taratibu za utoaji huduma katika mamlaka za udhibiti, kuanzisha vituo vya pamoja vya kutoa huduma, kusogeza huduma karibu na watumiaji, kuboresha mifumo ya ukaguzi wa pamoja, kuweka utaratibu wa ukaguzi unaozingatia vihatarishi, kujenga uwezo katika mamlaka za uthibiti na kuweka taratibu na kanuni za kujidhibiti. Nakushukuru.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kufanya mapitio ya tathmini kwa wananchi wanaopisha mradi wa kuboresha Bonde la Mto Msimbazi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kufuatia malalamiko ya wananchi yaliyojitokeza kuhusu uthamini wa mali katika eneo la Bonde la Mto Msimbazi, Serikali kupitia Wizara yangu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kufanyia kazi malalamiko hayo kabla ya kuidhinishwa kwa taarifa za uthamini. Aidha, zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi litafanyika baada ya malalamiko hayo kupatiwa ufumbuzi.
MHE. MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawaongezea TARURA bajeti ili barabara za ndani ya Jimbo la Kinondoni zijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Jimbo la Kinondoni lilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 2.38 ambazo zilitekeleza matengenezo ya barabara ya jumla kilometa 26 za lami na changarawe na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya kilometa 0.52. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 32 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 1.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Jimbo la Kinondoni lilitengewa bajeti ya shilingi bilioni 4.87 kwa ajili ya kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara zenye jumla ya kilomita 26.52, ambapo matengenezo ya kawaida ni kilomita 24.32 na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa 2.2 ambapo utekelezaji wake unaendelea na umefikia asilimia 70. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 29 ya bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuiongezea fedha TARURA kwa ajili ya kuongeza mtandao wa barabara za lami katika Jimbo la Kinondoni na maeneo mengine kwa kadri ya upatikani wa fedha.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuondoa sharti la kukopa kwa vikundi mikopo inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeunda Timu ya Kitaifa kwa lengo la kupitia na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuratibu na kusimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Timu hiyo imekalimisha jukumu hilo na kukabidhi taarifa Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea na uchambuzi na mapitio ya taarifa na pindi itakapokamilika taarifa rasmi itatolewa kwa Umma juu ya utaratibu wa mikopo ya asilimia 10 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiongeze kundi la wanaume kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEM naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290 Kifungu cha 37A ya mwaka 2018 na Kanuni za Usimamizi na Utoaji wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 na Kanuni za Marekebisho za mwaka 2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria hii, mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa ajili ya kuwezesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata mikopo isiyo na riba kwa kuzingatia kwamba makundi haya hayawezi kupata mikopo katika taasisi zingine za kifedha kwa sababu ya kukosa dhamana na uwezo mdogo wa kumudu riba ili waweze kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia utoaji wa mikopo hii kwa mujibu wa sheria na kanuni. Aidha, makundi mengine ambayo siyo walengwa wa mikopo hii wanashauriwa kupata mikopo kupitia taasisi zingine za fedha zinazohusika na utoaji wa mikopo. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -
Je, nini kauli ya Serikali juu ya Bima za Afya kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kuhusu Bima ya Afya kwa Watoto ni kuwaomba Watanzania wote, viongozi wote, kisiasa, kidini na kimila kuwa suluhu pekee ni sisi wote kuungana na Serikali katika kuhamasisha umma kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote pale utekelezaji utakapoanza, naomba kuwasilisha.