Primary Questions from Hon. Kenneth Ernest Nollo (16 total)
MHE. KENNETH E. NOLLO Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa GoTHOMIS kwenye zahanati kama ilivyo kwenye vituo vya afya ili kuondoa mwanya wa upotevu wa mapato?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Kieletroniki wa Uendeshaji wa Huduma za Afya (Government of Tanzania Health Operations Management Information System - (GoTHOMIS) ni mfumo wa usimamizi wa uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za wagonjwa na magonjwa, taarifa za malipo ya matibabu, taarifa za madawa na vifaa tiba na taarifa za huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu ulianzishwa mwaka 2016 na kuanza kusimikwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote. Mfumo umeboreshwa na kuunganishwa na mifumo mingine kama Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG), mfumo wa NHIF kwa ajili ya usimamizi wa madai na mfumo wa Kuomba Madawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (ELMIS).
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Februari 2021, Mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika vituo vya kutolea huduma 921, ikiwa ni hospitali 21 za mikoa, hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za wilaya 22, vituo vya afya 385 na zahanati 411. Kazi ya kusimika mfumo huu katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote nchini inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri zimekuwa zikitumia vyanzo vyake vya ndani kusimika mtandao kiwambo na kununua vifaa vingine zikiwemo kompyuta na wataalam wa halmashauri kushirikiana na wataalam wa mikoa katika kusimika mifumo hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya vituo vilivyofungiwa Mfumo wa GoTHOMIS na ambavyo vina miundombinu wezeshi kama mawasiliano ya internet vinatumia moja kwa moja Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) na hivyo kuwezesha wapewa huduma kulipa moja kwa moja benki au kupitia mitandao ya simu na hivyo kuwezesha makusanyo ya vituo kuongezeka na kutumika ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufungaji wa mifumo huu utaendelea kutekelezwa.
MHE. KENETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabwawa makubwa ambayo yatahifadhi maji ya mvua ili yaweze kutumika kwa shughuli za kibinadamu, kilimo na mifugo katika Mkoa wa Dodoma ambao umekuwa haupati mvua za kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Keneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshmiwa Naibu Spika, katika jitihada za kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Dodoma, katika mwaka 2020/2021, Serikali imekamilisha usanifu kwa ajili ya kukarabati Bwawa la Chikopelo lililopo umbali wa kilomita 70 kutoka Bahi Mjini ili kuongeza upatikanaji wa maji katika vijiji sita ikiwemo Mji wa Bahi na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidoka litakalohudumia vijiji saba ikiwemo Mji wa Chemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati na ujenzi wa mabwawa hayo unatarajiwa kufanyika katika mwaka 2021/ 2022, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa malambo sita katika Vijiji vya Mpamwata, Uwekela, Kambia, Nyasa, Kolema Kuu, Kidoka na Palanga katika Wilaya za Bahi na Chemba.
Mheshmiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali ina mpango wa kujenga bwawa la kimkakati katika Kata ya Farkwa ambapo mpaka sasa usanifu umekamilika na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaotakiwa kupisha eneo la mradi wa ujenzi wa bwawa hilo umefanyika kwa asilimia 99. Bwawa hilo lenye mita za ujazo milioni 470 linatarajiwa kujengwa kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Dodoma, Serikali imechimba visima visima nane na kukarabati visima vitatu vya zamani. Kazi ya ufungaji wa miundombinu inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Chumvi katika Kata ya Ilindi, Wilayani Bahi kitakachosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na kutoa ajira kwa wananchi hasa akina mama?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya vipaumbele vya Serikali katika kipindi hiki ni kuhamasisha ujenzi na kuendeleza viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana kwa wingi nchini ikiwemo madini ya chumvi inayopatikana katika Kata za Ilindi na Chali katika Wilaya ya Bahi ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, shughuli za uchimbaji na ukusanyaji wa chumvi Wilayani Bahi, zimeajiri takribani watu 400 hasa vijana na akinamama. Serikali inafanya utafiti wa kujua kiasi cha chumvi kilichopo yaani salt deposit ili utafiti huo ukikamilika utumike katika kuhamasisha wawekezaji katika viwanda vya chumvi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inashirikiana na Wizara nyingine za kisekta ikiwemo Wizara ya Maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika katika eneo hilo na Wizara ya Madini kujua kiasi cha madini ya chumvi kilichopo yaani salt deposit ili kuona kama kitakidhi kiwango cha uzalishaji kinachotakiwa kuendesha na kiwanda hasa kiwanda vya kati.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inafanya utafiti wa teknolojia rafiki ya kuwasaidia wajasiliamali wadogo ili kuzalisha chumvi kwa tija katika eneo la Ilindi, Bahi.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Bihawana – Chali hadi Sanza Manyoni kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hii muhimu huwa haipitiki wakati wa masika?
(b) Je Serikali ina mpango gani wa kuinua tuta la barabara katika eneo la Chali ili liweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Bihawana – Chali hadi Sanza Manyoni ni barabara ya Mkoa inayojulikana kwa jina la Bihawana - Chidilo – Chipanga – Chali Igongo ambayo ina urefu wa kilomita 69, ambayo inaunganisha Wilaya za Bahi na Manyoni kupitia Sanza. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 shillingi milioni 759.252 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, sehemu (b) kuhusu kuinua tuta eneo la Chali, Serikali imefanya kazi zifuatazo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2019/ 2020, Serikali imejenga kalavati kubwa na kuinua tuta lenye urefu wa mita 500. Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Serikali imejenga makalavati makubwa mawili na kuinua tuta lenye urefu wa mita 100. Vilevile, katika mwaka wa fedha huu wa 2021/2022, Serikali imepanga kunyanyua tuta lenye urefu wa mita 500 ambapo mkataba wa kazi hii upo katika hatua za kusainiwa. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha uzalishaji wa madume bora ya ng’ombe Wilayani Bahi ili kuleta tija kwa wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuimarisha mashamba yake ya uzalishaji wa madume bora ya Mabuki, Mwanza; Kitulo, Njombe; na Sao Hill lililopo Mkoani Iringa ili yaweze kuzalisha madume mengi na bora kwa lengo la kuyasambaza kwa wafugaji wote wanaohitaji ikiwa ni pamoja na wafugaji wa Wilaya ya Bahi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya teknolojia ya uhimilishaji katika kuboresha kosaafu za ng’ombe ili kuwa na kundi la mifugo yenye tija katika kuzalishaji nyama na maziwa na hivyo kukidhi mahitaji ya soko.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kuleta mikataba ya madini na nishati ijadiliwe Bungeni kabla ya kuingia makubaliano na wawekezaji?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi Sura ya 450 kifungu cha 5 inatoa wajibu wa Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, katika utekelezaji wa jukumu lake la kuishauri Serikali linaweza kuitisha mikataba inayohusu masuala ya utajiri na rasilimali za nchi na kuweza kupitia kwa lengo la kuishauri Serikali na kutoa azimio la kuondoa masharti hasi katika mikataba. Takwa hili la sheria linazingatia misingi iliyowekwa na sheria, kwamba mikataba au makubaliano yaliyoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji yanazingatia haki, usawa na nia njema kwa pande zote na kuzingatia maslahi ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiwasilisha mikataba kupitia kamati za kudumu za Bunge na Kamati kuzitolea maelekezo na ushauri kutoka kwa sekta husika. Pale Kamati husika inapoona umuhimu wa kufikisha mkataba mbele ya Bunge lako Tukufu maelekezo hutolewa na kwa kuzingatia Sheria husika.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setilaiti?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwa na Setilaiti, hivyo, mwaka huu wa fedha Serikali imeanza utaratibu wa awali utakaowezesha kuunda na kurusha setilaiti angani. Ili kuwezesha kufikia azma hiyo, Serikali tayari imeandaa andiko dhana na kuunda timu ya wataalam watakaoshauri aina ya setilaiti tutakayorusha angani itakayoendana na mahitaji halisi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi kisha kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. KENETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja la kudumu kwenye Mto Mzizima ili barabara ya Kigwe hadi Chipanga Wilayani Bahi iweze kupitika mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia TARURA Wilaya ya Bahi, imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 620.23 kwa ajili ya ujenzi wa daraja (box culvert) lenye urefu wa mita 34. Ujenzi wa daraja hili umeanza tarehe 20 Februari, 2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 19 Agosti, 2022 na ujenzi wa mradi huu umefikia asilimia 30. Kazi hiyo inafanywa na Mkandarasi Ravji Construction Ltd.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo utaifanya barabara ya Kigwe – Chipanga kupitika wakati wote na hivyo kuondoa kero ya wananchi kutumia muda mwingi wa kusubiria maji ya mto yapungue ili wavuke na kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuwa na Sera ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwenye Mikoa ya Kanda ya Kati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Kilimo ya Taifa ya mwaka 2013, inatambua umuhimu wa kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo. Kupitia sera hiyo, maeneo ya
kipaumbele ya kuongeza tija ni pamoja na kuimarisha utafiti, kuongeza upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo (mbegu, mbolea na viuatilifu), kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji, kupima udongo, kuimarisha matumizi ya zana bora za kilimo na kuimarisha huduma za ugani katika kanda zote za Ikolojia nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza miradi ya umwagiliaji katika Mikoa ya Kanda ya Kati – Dodoma, Singida na Tabora kwa kujenga mabwawa saba na skimu za umwagiliaji kumi; uimarishwaji wa Vituo vya Utafiti vya Tumbi, Makutupora na Hombolo; usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima; na uimarishwaji wa huduma za ugani ikiwa ni mkakati katika utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya Taifa ya Mwaka 2013.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuweka utaratibu kwa wananchi kuwasilisha Hoja Binafsi mbele ya Mabaraza ya Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Halmashauri, Mwananchi wa kawadia hawezi kuwasilisha hoja binafsi katika Vikao vya Baraza la Madiwani kwa kuwa tayari yupo mwakilishi wake katika kikao hicho ambaye ni Diwani wa Kata husika.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, lini Serikali itafungua Ofisi za Balozi katika nchi za Iran na Pakistan?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua ya kufanya tathmini ya kuangalia uwezekano wa kufungua ubalozi katika nchi za Iran na Pakistan. Tathmini hiyo inayofanyika, inajumuisha pamoja na mambo mengine, kuangalia fursa za kiuchumi ambazo nchi yetu itanufaika nazo kwa kuzingatia mwongozo wa Sera ya Mambo ya Nje uliojikita katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi na tija katika matumizi ya fedha za Umma. Taarifa ya Tathmini hiyo itawasilishwa kwa mamlaka husika pindi itakapokamilika.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Tanzania inawakilishwa nchini Iran na Pakistan kupitia ubalozi wetu ulioko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Ahsante sana.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Mtitaa Wilayani Bahi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Umwagiliaji Mtitaa iliyopo katika Kijiji cha Mtitaa, Kata ya Mtitaa Wilayani Bahi, ilijengwa kupitia Mpango Shirikishi wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji (PIDP) katika mwaka wa fedha 2002/2003 na kuanza uzalishaji mwaka 2003/2004. Skimu hii pia ina miundombinu ya bwawa dogo la kuvuna maji msimu wa mvua na zao linalolimwa ni Mpunga. Skimu ina jumla ya hekta 107 na ina jumla ya wakulima 215.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za ukarabati wa skimu za Bonde la Bahi ikiwemo skimu ya Mtitaa ambazo zimeharibiwa na mafuriko ili kuzirudisha kwenye uzalishaji.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati kwenye skimu ya kilimo cha mpunga iliyopo Kata ya Bahi, Wilayani Bahi kwani miundombinu yake imechakaa sana na kupelekea upotevu wa maji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu katika skimu ya kilimo cha mpunga iliyopo Kata ya Bahi, Wilayani Bahi ili kujua gharama halisi ya ukarabati. Aidha, fedha kwa ajili ya ukarabati huo zitatengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha Madume Bora ya Ng’ombe Wilayani Bahi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Mabadiliko ya Sekta ya Mifugo wa Miaka Mitano Kuanzia Mwaka 2022/2023 hadi Mwaka 2026/2027. Aidha, kupitia mpango huo, uboreshaji wa mbari za ng’ombe unafanyika kupitia matumizi ya madume bora na uhimilishaji ambapo kwa upande wa madume, Wizara imesambaza bure madume bora ya ng’ombe wa nyama 366 kwenye vikundi vya wafugaji katika halmashauri nane ili kuzalisha mifugo yenye tija zaidi ile ya asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Wizara kwa sasa ni kusambaza madume bora ya ng’ombe kwa vikundi vya wafugaji ili kuboresha mifugo yao badala ya kuanzisha vituo vya madume. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara imepanga kununua madume bora 200 yatakayosambazwa kwa vikundi vya wafugaji, wakiwemo wafugaji wa Halmashauri ya Bahi ambao watapewa madume 20. Naomba kuwasilisha.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, lini zoezi la kuhamia Dodoma litakamilika na Taasisi ngapi zimeshahamia Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma lilianza rasmi mnamo mwaka 2016. Hadi sasa jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali Kuu, Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na taasisi 65 wameshahamia Dodoma na wanaendelea kutekeleza majukumu yao wakiwa Makao Makuu ya Nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma kwa kuzingatia mpango kazi maalum na ujenzi wa awamu ya pili wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi utakaohitimishwa ifikapo mwaka 2025.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ukarabati wa Skimu za Umwagiliaji zilizopo Kata ya Bahi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu zilizopo katika Bonde la Bahi. Bonde hilo lina jumla ya hekta 5,000 na linajumuisha Skimu za Nguvumali, Bahi Sokoni, Mtazamo, Matajila na Welela. Kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa skimu hizo umekamilika na skimu hizo zipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu za Mkakatika na Makulu katika Bonde la Bahi ili kuongeza eneo la umwagiliaji.