Supplementary Questions from Hon. Kenneth Ernest Nollo (20 total)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika,naomba kuuliza swali la nyongeza, kigezo kikubwa cha ufaulu cha wanafunzi kwenda kidato cha kwanza au kwenda kidato cha tano imekuwa ni zile grade aidha A,B,C ambazo zinatumika sasa katika ufaulu, lakini kwenye midterm reviews za wanafunzi hasa mitihani Serikali imekuwa na utaratibu ambao tumeendelea nao nadhani tulirithi kwenye ukoloni kwa kutoa wa kwanza mpaka wa mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limekuwa lina- affect watoto kisaikolojia na mtoto anakuwa na alama A, lakini ni wa kumi na ukimuuliza ulikuwa wangapi darasani anakwambia nilikuwa wa kumi lakini ana A; je, Serikali haioni jambo hili linaathiri watoto kisaikolojia na katika maisha mtu kujiona kwamba yuko grade ya mwisho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nollo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna uhakika sana kama kuwapanga watoto wa kwanza mpaka wa mwisho kuna haribu saikolojia ya watoto bali inaonesha ushindani na namna gani watoto wanaweza wakashindana ili kuweza na yeye kujisukuma kuweza kufika hapo juu, lakini nadhani ni suala ambalo linahitaji kufanyiwa utafiti kwamba je, kupangwa watoto katika utaratibu huo kuna athiri kisaikolojia. Hili naomba tulibebe tukalifanyie utafiti na kama tukiona kama kweli lina tija tunaweza tukaja kutoa majibu mbele ya Bunge lako tukufu.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, swali langu la msingi lilikuwa ni kwamba mfumo huu umeshafika kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kwenye zahanati 400, lakini tunajua nchi hii ina vijiji takribani 12,000, kwa maana hiyo na zahanati hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu la msingi ni kwamba zahanati nyingi sasa hawawezi kukusanya kwa kutumia ule mfumo na kinachotokea ni kwamba kunakuwa na upotevu wa mapato. Sasa swali langu la msingi ni je, Serikali haioni kwamba tutumie mfumo wa kawaida wa makusanyo ya kawaida (POS) ili tutoke kwenye upotevu ambao unaendelea sasa hivi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa dawa, hasa kwa watu wanaotumia CHF, kichecheo kikubwa imekuwa fedha za papo kwa papo, na hiyo inatokana na hii ya kwamba kuna upotevu wa fedha ambazo sasa mtu anakuwa analipa lakini fedha hazionekani.
Kwa hiyo, swali langu liko hapo, kwamba ni namna gani Serikali sasa inakuja kwamba ikiwezekana sisi tutumie POS kwa ajili ya kukusanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili Mheshimiwa.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, connection kidogo, mfumo huu unatumia milioni 14 ku- install…
NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili ya nyongeza, na ndiyo yanayoruhusiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha ukusanyaji wa mapato, matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi lakini pia takwimu za huduma za afya katika vituo vyetu kwa kufunga mifumo ya GoTHOMIS. Na ni kweli kwamba bado kuna zahanati na vituo vya afya ambavyo bado havijafungwa mfumo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Nollo kwamba kazi hii ya kufunga mifumo katika zahanati zetu ni endelevu. Kama ambavyo tunafahamu, hatujamaliza kujenga zahanati kwenye vijiji vyetu, na wala hatujamaliza kujenga vituo vya afya katika kata zetu lakini pia Hospitali za Halmashauri katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo automatically tutaendelea kutekeleza ufungaji wa mfumo huu katika vituo vipya ambavyo vinaendelea kujengwa lakini pia katika vile vituo ambavyo bado havijajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kutumia mfumo wa POS halitatuwezesha kuboresha huduma za afya, kwa sababu lengo la mfumo wa GOT-HOMIS ni kuwa na taarifa za uhakika za magonjwa, matumizi ya dawa, aina ya matibabu yanayotolewa katika vituo. Kwa utaratibu huo hatuwezi kupata taarifa hizo kwa kutumia mashine za POS. Kwa hiyo naomba nimuhakikishie kwamba kama nilivyotangulia kusema tumeshafunga katika vituo 921 nchini kote, na kila mwaka wa fedha tunaendelea kufunga mifumo hii na tutaendelea kufunga ili viendelee kutoa huduma bora zaidi za afya katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali pili, changamoto ya upatikanaji wa dawa kwa baadhi ya vituo. Ni kweli Serikali imeendelea sana kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyetu vya huduma. Ukilinganisha hali ya upatikanaji wa dawa mwaka 2015 na 2020/2021 tumepanda kutoka wastani wa asilimia 75 kwa dawa muhimu mpaka wastani wa asilimia 80 hadi asilimia 85 kwa dawa muhimu. Lengo la Serikali ni kufika angalau asilimia 95 kuelekea asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaombe Waheshimiwa Wabunge; kwamba sisi ni sehemu ya Madiwani katika Halmashauri zetu, sisi ni wawakilishi wa wananchi katika Halmashauri zetu. Tuendelee kushirikiana na Serikali kusimamia ukusanyaji wa mapato ya uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu na kuhakikisha dawa zile kama ambavyo Serikali tunasimamia kwa karibu zinatumika na kuwafikia wananchi wote wakiwepo wanachama wa CHF. Kwa hiyo naomba nimuhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili litaendelea kuboreshwa.
MHE. KENETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu la msingi ilikuwa ni kwamba Mkoa wa Dodoma unapata mvua kidogo lakini kumekuwa na upotevu mkubwa wa maji kipindi mvua inavyokuwa inanyesha.
Lengo la swali langu ni je, Serikali ina programu gani mahsusi, acha hii ya kudonoa donoa, programu mahsusi ya kuanza kukinga maji ambayo yanapotea kwa kiasi kikubwa kwa miaka nenda rudi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; tunajenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Lakini, mradi huu ni mkubwa unapita kwenye mabonde na mito mingi. Je, Serikali kupitia Wizara ya Fedha, Kilimo na Wizara ya Ujenzi haioni kwamba tuongeze sehemu ya mradi ule kwa ajili sasa ya kuweka mabwawa na kutengeneza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo badala ya fedha nyingi zinajenga kwenye reli lakini mradi ule hauna pact ambayo ingeweza kusaidia kwenye Sekta ya Kilimo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mahsusi wa Serikali kutumia maji ya mvua kama nilivyoelekeza, tuna mpango wa kuchimba mabwawa ambayo yataweza kuvuna yale maji na yatasambazwa kwa wananchi wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na ujenzi wa reli ya kisasa. Pamoja na kwamba hii ni nje ya Wizara yangu nipende tu kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba reli hii ni ya thamani kubwa sana na ni ya manufaa makubwa kwa wananchi hivyo, kila suala lina mkakati wake na umuhimu wake. Masuala ya mabwawa kuongezwa, sisi kama Wizara ya Maji tutashughulikia. Licha ya kwamba mradi huo wa reli manufaa yake yataendelea kuzingatiwa. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli ya uchimbaji chumvi kwenye kata ya Ilindi imekuwa ni ya muda mrefu na Halmashauri tumepanga mwaka ujao wa fedha tuweze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga jengo ambalo sasa tutahitaji tupate mashine kwa ajili ya kiwanda kianze.
Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari aambatane na mimi baada ya Bunge hili ili kwanza akaone eneo lile na ikiwezekana kama alivyosema sasa SIDO waweze kutusaidia kiwanda kile kianze?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, Serikali imesema kwamba Kata ya Chali na Kata ya Ilindi ni kata ambazo zina chumvi pale, lakini pamoja na ile kumekuwa na tatizo la upatikanaji wa maji kwa sababu ya chumvi Kata ya Ilindi haina maji kabisa kila sehemu maji yana chumvi na Kata ya Chali nayo haina maji ina sehemu moja ambayo ina chanzo cha maji, lakini Serikali imekuwa inaahidi haijatekeleza mradi ule.
Je, Waziri wa Maji yuko tayari vilevile naye aweze kufanya ziara kwenye Kata ya Ilindi na Kata ya Chali ili aweze kuona shida inayowakabili wananchi wa kata hizi kutokana uwepo wa chumvi ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema lengo la Serikali ni kuona tunahamamisha ujenzi wa viwanda vingi nchini ili kutumia malighafi tulizonazo, kwa hiyo, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Nollo ili twende kuangalia kwanza sehemu yenyewe ilivyo, lakini pia tuweze kupata taarifa sahihi na kuweza kuanza michakato ya kuona namna gani ya kuvutia wawekezaji katika kujenga kiwanda au viwanda katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili, ni kweli, kwa sababu kama alivyosema eneo lile lina chumvi kwa hiyo maana yake maji mengi yatakuwa ni ya chumvi. Serikali kupitia Wizara ya Maji najua wana mipango mingi, basi tutashirikiana na Wizara ya Maji ili kuhakikisha tunaona namna gani ya kuwasaidia ndugu zetu wa Bahi ili waweze kupata maji safi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na umuhimu wa barabara hii Wabunge wengi waliopita upande wa Bahi na upande wa Manyoni, wamekuwa wanaulizia kuhusu umuhimu wa barabara hii na majibu ya Serikali yamekuwa ndiyo hayo, kwamba, tunatafuta fedha kwa ajili ya usanifu yakinifu na ile nyingine aliyoisema.
Mheshimiwa Spika, sasa, tena niulize hapo: Je, ni lini fedha ya upembuzi yakinifu itapatikana? Maana yake ndiyo hayo hayo miaka yote. Sasa ile ya upembuzi yakinifu na ile nyingine, ni lini fedha itapatikana? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwenye majibu ya sehemu (b) nilikuwa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri afanye ziara ili aweze kupata uhakika kabisa na alichokijibu hapa. Mimi mwezi wa Nne nilikesha pale, barabara ilijifunga na kinachojibiwa hapa sicho kilichofanyika. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili hebu akafanye ziara aweze kuona na mwenyewe awe na picha halisi ya eneo lile.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni lini? Serikali mwaka huu wa fedha imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza kazi hii. Suala la kutembelea, hilo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, niko tayari kutembelea hilo eneo kwa sababu ni eneo hili hili tu. Nitakapokuwa nakwenda Kaskazini, basi nitapita barabara hiyo na nitamjulisha ili tuweze kukagua pamoja naye hiyo barabara. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Katika Wilaya ya Mpwapwa kuna idadi kubwa sana ya mifugo, lakini changamoto yetu kule ni ukosefu wa mfumo rasmi wa upatikanaji wa madawa kwa ajili ya kutibu mifugo yetu. Wafugaji kule wanategemea sana walanguzi ambao wakati mwingine wamewauzia dawa feki na zimewasababishia hasara. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu rasmi wa kuhakikisha kwamba wafugaji wetu wanapata dawa za kutibu magonjwa ya mifugo katika maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kwenye vitengo vyetu vya Baraza la Veterinary Tanzania na TMDA kwa pamoja tunafanya operations za mara kwa mara za kufuatilia dawa zisizo na viwango. Kwa mwaka jana tulikamata na hatua za kisheria zilichukuliwa na mwaka huu pia vile vile Mkoani Mwanza tayari yuko mzalishaji na msambazaji wa dawa feki ambaye tumemkamata.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wetu sasa kupitia Baraza hili ni kuhakikisha kwamba udhibiti wa dawa hizi unaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuzalisha dawa nyingi zaidi zilizobora kupitia viwanda vyetu vya hapa nchini pamoja na kiwanda cha Serikali kilichoko pale Kibaha kwa maana cha TVI ili wafugaji wetu waweze kupata uhakika wa chanjo na dawa zenye kukidhi viwango.
MHE.KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya maeneo yanayolalamikiwa katika nchi zenye utajiri wa mafuta ya gesi ni kukosekana kwa utawala bora katika kuwa na uwazi kwa mikataba hii kwa umma; je, ipi mikakati ya Serikali katika kuenzi jitihada za kufikia lengo hili la kuwa na uwazi wa mikataba kwa ujumla katika umma wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili pamoja na kwamba mikataba imekuwa inakuja bungeni kupitia Kamati; je, Serikali haioni kama kuna umuhimu wa kubadilisha utaratibu huu ili kuwe na utaratibu ambao Bunge litaweza kuona kwa maana ya Bunge zima hata kuwe kwa kipindi cha mwisho wa mwaka ili waweze kuona ni maeneo gani ambayo Serikali imeingia mkataba na waweze kupata uelewa wa pamoja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nollo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwazi katika mikataba upo na kimsingi kwa sababu muuliza swali ni sehemu ya Wabunge na Kamati za Bunge zimeundwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa Kibunge, zinapopata nafasi ya kupitia mikataba hii huwa ni kupunguza lile jambo katika mazingira ambayo yanaweza upotofu wa jumla katika suala la mikataba. Hivyo basi mikataba inapojadiliwa na Kamati za Bunge ni kisheria kabisa unakuwa tayari maelekezo yanayotolewa na Kamati zile yanakuwa ni halali na ni sawa kufikishwa mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu lile suala la kubadilisha mfumo, ni Bunge hili lililokaa na likaweka utaratibu huo, na ni Bunge hili hili linaweza likabadilisha mfumo. Hivyo basi ni jambo ambalo ningemshauri Mheshimiwa Mbunge kutoa hoja ili sasa vyombo vinavyohusika katika kubadilisha mifumo viweze kuchukua nafasi yake. Lakini kwa namna tunavyokwenda kwa sasa ni jambo ambalo linazingatia taratibu na sheria tulizojiwekea. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Nina swali dogo la nyongeza kwamba nchi ya Uganda, siku ya jana tarehe 6 imekuwa ni nchi ya 12 katika Afrika kurusha Setilaiti yake angani. Setilaiti ile imeundwa kwa kupitia vijana ma- engineer wa Uganda wakishirikiana na nchi ya Japan na Kituo cha Anga cha Marekani: Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha program hii ya kuanza kufundisha vijana wetu kwa kushirikiana kama ilivyofanyika Uganda ili tuweze kupata setilaiti ambayo itaundwa na Watanzania halisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nchi za Afrika mpaka sasa tuna setilaiti 41 na kuanzia mwaka 2016 ni setilaiti takribani 20 ambazo tayari zimekuwa angani. Katika hizo setilaiti 41 ni tisa tu ambazo zimekuwa designed, manufactured na baadaye kupelekwa angani ambazo zina asili ya Kiafrika.
Mheshimiwa Spika, bado tuna maeneo mengi ya kuendelea kujifunza, lakini kama nilivyojibu katika swali la msingi, Mheshimiwa Rais siku ya tarehe 8 Februari wakati akiwa na kikao kazi na Wakuu wa Mikoa, alielekeza Wizara yetu ili tuone umuhimu sasa wa kuwa na setilaiti yetu. Tayari Wizara yetu imeshaunda timu ya wataalam ambao watakuja kuishauri Serikali aina ya setilaiti itakayoendana na mahitaji ya Watanzania. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Skimu ya Kongogo ni moja ya skimu ambazo ziliwekwa kwenye bajeti ya 2022/2023; je, Serikali imefikia wapi katika kuanza utekelezaji wa ujenzi wa skimu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Skimu ya Kongogo ipo katika bajeti ya mwaka huu na hatua ambayo tumeifikia, mkandarasi ameshapatikana na muda wowote kuanzia hivi sasa atakwenda kuanza utekelezaji wa ujenzi wa skimu hiyo.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu wa mwaka jana Mkoa wa Dodoma hatukupata mbegu za mtama mfupi lakini vile vile mbegu ya alizeti hatukupata na nataka kupata majibu ya Serikali. Serikali ina mkakati gani kwa msimu unaokuja ili kwanza tupate uhakika wa mbegu ambao tumekuwa hatupati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la jingine la pili ni kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba yapo mabwawa saba ambayo miongoni yatajengwa Dodoma. Je, mabwawa hayo ni yapi na yataanza kujengwa lini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza la kuhusu mbegu za alizeti na mtama mfupi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu ujao wa kilimo wakulima wa Mkoa wa Dodoma pia watanufaika na utoaji wa mbegu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu mabwawa. Katika jibu langu la msingi nimetamka mikoa mitatu kwa maana ya Tabora, Dodoma pamoja na Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa ambayo tunayo mpaka yanaendelea hivi sasa ni mabwawa ya Msagali pale eneo la Mpwapwa, Bwawa la Membe ambalo litakuwa lina uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo milioni 12 lakini vile vile Lyamalwaga ambayo iko Nzega, vile vile Kongogo ambayo iko Bahi na mengine akiyataka kwa orodha nitamtajia yote katika Mkoa wa Dodoma, kwa sababu ya muda naomba niyataje haya machache. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Pamoja na demokrasia yetu ya uwakilishi nchi zilizoendelea wamekuwa na utaratibu wa kupokea hoja za wananchi za kimaendeleo na pale wanapoziona zina maana mwananchi huyo huitwa kuja kutetea hoja yake na ambayo inaweza kutumika kwa ajili ya kuendeleza eneo husika, jambo hili limeendelea kufanyika katika nchi nyingi zilizoendelea.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi karibuni Serikali imesitisha utoaji wa asilimia kumi kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. Kwa kuwa jambo hili lina maslahi mapana ya nchi yetu. Je, Serikali haioni haja ya kuruhusu kwamba sasa wananchi watoe maoni kuhusu jambo hili, namna bora ya kuweza kulitekeleza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Nollo ni kwamba wananchi wanapewa fursa ya kuhudhuria Mabaraza ya Madiwani na kusikiliza mijadala ambayo inaendelea, kama kuna hoja mahsusi kwa mwananchi au ana idea yoyote ambayo anataka kuiwasilisha anaweza akaonana na Mwenyekiti wa Halmashauri, akazungumza nae na kumpa wazo hilo, kisha Mwenyekiti wa Halmashauri anawasilisha lile kwa wenzake ambao ni Baraza la Madiwani, wakiona inafaa anaalikwa yule mwananchi ili aweze kutoa presentation mbele ya Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huo upo, kwa hiyo niombe tu wananchi wa kule Bahi na maeneo mengine, kuhakikisha kwamba kama kuna mwananchi ana idea nzuri ya kusaidia jamii na Halmashauri, basi awasiliane na Mwenyekiti wa Halmashauri ili Mwenyekiti wa Halmashauri aweze kuongea na Madiwani wenzake na kumkaribisha mwananchi huyo katika Mabaraza ya Madiwani kwenda kufanya presentation. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, Nchi ya Iran ina miaka 56 ya ubalozi hapa nchini, lakini nchi ya Pakistani ina miaka 40 ya ubalozi hapa nchini.
Je, Serikali haioni muhali kidiplomasia kwa miaka yote hii kutokufungua ubalozi kwenye nchi hizi mbili?
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine, swali la pili, kama nilivyosema kwa wingi wa miaka ya balozi hizi ambazo ziko hapa kwetu nchini na Serikali kwa kufanya tathmini kwa miaka 56 na miaka 40. Je, commitment yake ni lini sasa itafungua balozi kwenye nchi hizi mbili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na kwamba, nchi yetu haina ofisi za ubalozi nchini Pakistan na Iran, lakini hata hivyo tumekuwa na ushirikiano mkubwa na tumekuwa tukishirikiana katika nyanja mbalimbali. Tuna mikakati mingi ya kuendeleza uhusiano huu na mmojawapo ni kuanzisha tume za pamoja za kudumu za ushirikiano kati ya Tanzania na Pakistan na Tanzania na Iran. Kwa Iran tayari hiyo ipo na kwa Pakistan tayari tumeshaanza mchakato huo na tayari tumewasilisha rasimu ya makubaliano hayo na ipo upande wa Ubalozi wa Pakistan tukisubiri majibu yao.
Mheshimiwa Spika, lingine, nchi yetu inapenda kuwa na balozi nyingi sana nchi za nje, lakini ni muhimu sana kufanya tathmini, kama nilivyoeleza hapo mwanzo, ili kujua tija hasa ambazo tutapata katika nchi hizo. Pia hali ya kifedha inaporuhusu nafungua hizo balozi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bwawa la Chikopelo linategemewa na Kata za Chali na Kata ya Nondwa. Bwawa hili limekuwa na uwezo wa kutunza maji msimu wote, hata hivyo lina changamoto ya kupungua kwa kina kutokana na kujaa kwa matope.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati bwawa hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine dogo ni kwamba Kilimo cha Zabibu ni kilimo kinachotegemewa hapa Mkoa wa Dodoma hata hivyo kilimo hiki bado kinategemea kwa kiasi kikubwa mvua. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili tuanze kupata umwagiliaji kwa ajili ya kilimo na kupata tija? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu Bwawa la Chikopelo. Katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kiambatisho namba 13 tumelitamka Bwawa la Chikopelo kati ya mabwawa ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi mwaka ujao wa fedha. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge na Kata za Nondwa alizozitaja na maeneo ya jirani kuwa bwawa hili linakwenda kufanya kazi na wananchi watanufaika kwa kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu zabibu, tunatambua kwamba Dodoma ni kati ya eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa sana wa zabibu hapa Tanzania na hivyo kuna umuhimu pia wa kuunganisha zao hili na kilimo cha umwagiliaji. Kwa kuanzia tunao tayari mfumo wa umwagiliaji katika eneo letu la Chinangali ambapo tunalo shamba kubwa la umwagiliaji kwa ajili ya kilimo cha zabibu. Sambamba na hilo hata hili Bwawa la Chikopelo pia na lenyewe tutaangalia ikolojia yake kama ita-support kilimo cha zabibu pia tutaunganisha mifumo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kwamba tumetamka hapa tunakwenda kuchimba visima 150 kila Halmashauri nchi nzima hivyo wakulima wa bahi pia watanufaika na visima hivi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji cha zabibu.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Nataka tu nijue Serikali inatumia kigezo gani? tofauti ya 27,000 na shilingi 300,000 ni kubwa mno je, Serikali haioni hebu ije na mkakati wa kuona kiwango fulani ambacho kitakuwa kina rationale nzuri kwa wote wanaokaa mjini na wale wa vijijini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kuliwahi kuwa na viwango tofauti tofauti vya kuunganisha umeme. Sasa kwa maneno machache niseme tulipata kipindi fulani mradi wa kupeleka umeme vijijini na ulikuwa unafanyika bure kwa watanzania wote waliyokuwa wanakidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ule mradi ulikuwa wa mfadhili na mfadhili akasema hawezi kutoa bure, kwa hiyo, tutakubaliana kwamba basi mwananchi alipie VAT ambayo kipindi hicho VAT ilikuwa ni shilingi 27,000 ndiyo genesis ya shilingi 27,000 ilipoanzia. Kwa hiyo, tumekwenda nayo kwa utaratibu huo mpaka sasa na Serikali sasa ndiyo inafanya mchakato na upembuzi mpana zaidi ili kuona kama tunaweza tukawa tuna viwango tofauti tofauti kwa misingi tofauti tofauti kama hii 27,000 ilikotokea kipindi hicho ilikuwa kuunganisha, ilikuwa 150,000 nadhani sasa asilimia 18 au 20 nadhani VAT ilikuwa asilimia 20 ikawa ni shilingi 27,000 ndiyo genesis ya shilingi 27,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi ni shilingi laki saba, laki sita mpaka laki saba. Kwa hiyo, inapungua kwenda laki tatu kulingana na ruzuku ambayo inayotolewa na Serikali kwenye maeneo ya mijini na maeneo ya vijijini au kwenda shilingi 27,000. Nashukuru.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri mwelekeo wa Serikali kutafuta scholarship ni katika maeneo gani hususan ambayo inataka wanafunzi wetu waende kusoma. Vilevile ukiangalia idadi ya wanafunzi 400 kwa Taifa hili ni kidogo sana ambao wamepata scholarship. Je, mpango wa Serikali ni upi hasa wenyewe makusudi kutafuta scholarship nje ya nchi ili iweze kuongeza idadi ya Watanzania wengi waweze kwenda kusoma nje ya nchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, ingawa amezungumzia maeneo mawili ambayo kipaumbele ni vipi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba nchi hizi zinapotoa ufadhili kwenye hizi scholarship ni nchi zenyewe ndizo ambazo zina-detect, zinazoamua kwamba kozi gani ziende zikasomewe; lakini maeneo mengi sana yamekuwa ni maeneo ya Udaktari pamoja na Uhandisi. Pia naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka ujao wa fedha, sisi kama Serikali kwanza tumeviagiza vyuo vyetu vikuu viweze kuandaa au kupendekeza maeneo ambayo wanafunzi wa Kitanzania watakwenda kufanya masomo yao nje ya nchi.
Mheshimwa Naibu Spika, vile vile kama nilivyoeleza katika swali la nyongeza ni kwamba, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo tumekuwa tukifadhili baadhi ya scholarship kwa kupata partial mikopo kwa ajili ya vijana wetu ambao wanakwenda kusoma nje. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wetu kama Serikali na tutaendelea kufanya hivyo wakati upatikanaji wa fedha utakapokuwa mzuri. Nakushukuru sana.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali hususani kwanza kufanya upembuzi yakinifu na baadaye utekelezaji wa bajeti 2023/2024.
Swali langu nilitaka niulize Serikali Mkoa wa Dodoma umekuwa unapata mvua kidogo, lakini pamoja na mvua kidogo tumekuwa na maji mengi ambayo yanapotea; je, nini ni mkakati mahususi hasa katika kuongeza mabwawa haya ya skimu hizi za umwagiliaji kutoka kwa Serikali ukoje? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge hii imekuwa ni hoja yake na ameisema sana hapa Bungeni na sisi Wizara ya Kilimo kwenye bajeti inayokuja tulizingatia hilo. Tuna ujenzi wa mabwawa makubwa mawili katika Wilaya ya Chamwino eneo la Membe na Msagali Mpwapwa, kama sehemu ya kuanzia katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na-reserve kubwa ya maji ili tuweze kufanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru sana Serikali kwa ahadi ya kunipatia madume 20 ya ng’ombe katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza. Kiasi hiki cha madume 200 ambayo Serikali inanunua ukilinganisha na idadi ya ng’ombe tuliyonayo ni hatua kidogo sana. Kwanza, hata hayo madume yenyewe tunayachosha kwa maana ya wingi wa majike yaliyopo. Je, Serikali haioni kwamba badala ya kununua madume 200 tuongeze tufike angalau hata 1,000 ili nchi nzima katika maeneo ya wafugaji tuweze kupata madume mengi na kwa uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Dodoma tuna Kituo cha Utafiti wa Malisho pale Mpwapwa na hapa Kongwa, lakini ukija katika Wilaya yangu ya Bahi kwenye kata za wafugaji ukianzia pale Chifutuka, Chipanga na Chikora, hakuna hata nyasi moja ya utafiti ambayo imeletwa katika wilaya yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa vituo hivi ambavyo vina miaka mingi, lakini taarifa zake na matunda yake hayafiki katika wilaya zinazovizunguka? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hili la madume 200. Ni kweli madume 200 ni wachache na mpango wa Serikali ni kuongeza kadri ya upatikanaji wa bajeti. Tunamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari kuongeza madume hao kadri ambavyo bajeti inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la nyasi, tayari wataalam wetu wanaendelea na utafiti katika maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mara tu utafiti utakapokamilika, basi mbegu za nyasi bora zitakwenda katika Jimbo lake la Bahi. Kwa sasa watafiti wetu wanafanya utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwa ni Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine, na Bahi pia watafika kwa ajili ya kukamilisha utafiti huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakuja Bahi kwa ajili ya kukamilisha utafiti huo na majibu yatakapopatikana, wataalam wetu wako tayari kutoa elimu kwa wafugaji wetu ili waweze kutumia nyasi hizo zinazotakiwa. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Zipo halmashauri ambazo zina uwezo wa mapato na zina uwezo wa kuajiri walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kugatua suala la ajira ya walimu liende kwenye halmashauri ambazo wanaweza wakaajiri na wakaweza kuwalipa walimu badala ya kusubiri mgao wa kitaifa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na mambo mengine inasimamia suala la ugatuzi kwa maana ya D by D na inapenda sana kuona halmashauri zinaweza kuwa na uwezo na ubunifu wa kutengeneza mapato makubwa ya ndani na kuweza kujiendesha zenyewe. Kwa hiyo, mawazo ya Mheshimiwa Mbunge ni mawazo mazuri, tunayachukua sisi kama Serikali, tutayachakata na tunaamini kwamba yataweza kutekelezeka.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini vile vile nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema zoezi hili la Serikali kuhamia Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kwamba taasisi 65 zimeshahamia hapa Dodoma, lakini mwisho kabisa wa taasisi zote kuhamia Dodoma ni lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Makao Makuu ya Nchi ambako viongozi wengi wa Serikali wanafanya kazi ni lazima kuwe na makazi yao rasmi. Je, ujenzi wa makazi rasmi ya viongozi wa Serikali utaanza lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, napokea pongezi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini mwisho wa taasisi za Serikali kuhamia Dodoma, kama nilivyojibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Kenneth Nollo kwamba tunaendelea na uchambuzi. Taarifa itakapokamilika, tutawaambia ni taasisi ngapi zimeshahamia na ngapi zimebaki. Tunatarajia mwaka 2025 taasisi zote ziwe zimeshahamia Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili, kwanza naendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri. Nimhakikishie kwamba Serikali ilianza ujenzi wa nyumba za viongozi kuanzia mwaka 2021/2022. Kupitia Wakala wa Majengo (TBA) tulijenga nyumba 20 na Septemba, 2023 nyumba 150 za watumishi zilizinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuko kwenye zoezi la kupanga eneo ambalo tumelitwaa kwa ajili ya kujenga nyumba za viongozi wa Serikali na watumishi. Sasa hivi tuko kwenye hatua ya kujipanga kwa kupitia hao wenzetu wa TBA watuainishie vizuri, na tutakuwa na ekari 4,654. Tumetwaa eneo kati ya Mji wa Serikali Mtumba na Ikulu hapo kwa ajili ya kujenga nyumba hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaendelea vizuri na uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba na kila jambo linaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwatoe mashaka na niwakaribishe sekta binafsi, ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ili hatua ya manunuzi kuanza inatakiwa kwamba kazi iwe imeshatangazwa kwenye hatua za manunuzi, lakini bado haijatangazwa. Swali langu linabaki pale pale, ni lini Serikali inaanza ukarabati?
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza; Umoja wa Wakulima pale Bahi walikopa Benki - NMB na bahati mbaya yakatokea mafuriko na deni lile limekuwa likiongezeka na Wizara ilionesha interest ya kumaliza mkwamo wa deni lile. Je, ni lini deni hili linaenda kumalizwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba kama tulivyojibu katika jibu la msingi ni kwamba tayari feasibility study imeshafanyika na sasa tuko katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi na nimthibitishie tu katika mwaka huu wa fedha jambo hili litakuwa limekamilika na tutamkabidhi mkandarasi site baada ya kumaliza hizi hatua za manunuzi. Kwa hiyo, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko kazini na hili jambo litaenda kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu deni ni kwamba tunashosubiria sisi ni fedha tu na baada ya hapo tutalipa. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunalifahamu jambo hili na ndiyo maana Serikali tumekuwa tukilifuatilia kila wakati, ahsante sana. (Makofi)