MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa sana Barani Afrika. Ni lugha ya pili kwa kuzungumzwa na watu wengi Barani Afrika na pia ni kati ya lugha kumi zinazozungumzwa sana duniani. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Kiswahili kinakuwa bidhaa hasa wakati wa kuchangia diplomasia ya uchumi na kuwa fursa ya ajira kwa Watanzania? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye leo ametupa uhai wa kukutana hapa na kuendelea na shughuli zetu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, pili, niungane nawe kuwakaribisha Waheshimiwa Wabunge wenzetu kutoka Baraza la Wawakilishi kuungana nasi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibuni sana, tutawapa ushirikiano wa hali ya juu na kwa kweli mtasaidia sana kuchangia yale muhimu na kuishauri Serikali na sisi Serikali tupo tayari kupokea ushauri wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Baba Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kiswahili sasa kimepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa kwenye mataifa mengi duniani na wala siyo kuzungumzwa tu pia hata matumizi yake yameongezeka. Tumeanza kuona nchi mbalimbali kubwa duniani zikiandaa vipindi vya Kiswahili kwenye redio na kwenye magazeti yao. Hii ni ishara kwamba Kiswahili chetu sasa kinakua duniani kote.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kutengeneza fursa hata kwa Watanzania ambao ndiyo wenye Kiswahili? Kiswahili hiki hapa nchini kinazungumzwa na makabila yetu karibu yote na ndiyo lugha ambayo inatuunganisha Watanzania. Tumeanza kusambaza Kiswahili hiki kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki, tumeona nchi zote za Afrika Mashariki zinazungumza lugha hii. Wote ni mashahidi tumeona jitihada ambazo zimefanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kusambaza Kiswahili kwenye Nchi za Ukanda wa Kusini (SADC) pale ambapo amekutana na Marais mbalimbali kuwahamasisha na sasa tumeona Kiswahili kimeanza kufundishwa kwenye nchi zao, kwa hiyo, Kiswahili kinazidi kupanuka.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, Kiswahili nacho kinaenda mbali zaidi, utaona Ujerumani, Marekani, Uingereza na Mataifa mengine makubwa yanaendelea kutumia Kiswahili. Sisi kama Serikali tumeweza kuwasiliana kupitia Balozi zetu, kila Balozi tumeiagiza kwenye nchi ambazo Balozi yupo kuanzisha kituo cha kujifunzia Kiswahili. Malengo yetu ni kupanua matumizi ya lugha ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapowafikishia Mabalozi na kufungua vituo na kuwafanya wananchi wa nchi husika kujifunza Kiswahili hapo sasa tumeingiza kwenye diplomasia ya Kiswahili. Kwa kuwa sasa Kiswahili kinapendwa duniani kote na kinazungumzwa na nchi nyingi sisi Watanzania sasa tuna fursa ya kuwa walimu wazuri kwenye nchi hizo kwenye vituo vyetu vya kufundisha Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kuwa walimu kwenye nchi hizo tayari tunafungua fursa za kiuchumi kwa kuajiri Watanzania kwenda kufanya kazi kwenye nchi hizo. Watanzania wakishapata ajira tunajua kodi kidogo inarudi nchini na tunaboresha uchumi wetu wa ndani. Kwa hiyo, tutatumia diplomasia hii kukuza uchumi wa ndani na hasa kwa kutoa fursa ya Watanzania kuajiriwa kwenye maeneo hayo kuendeleza kuboresha Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali moja. Tumekuwa na tatizo sugu la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika Shule za Sekondari na huu wimbo umekuwa wa muda mrefu sana: Je, ni nini sasa mkakati wa kudumu wa Serikali, kuondoa upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika shule za Sekondari?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Baba Askofu, Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vilevile tunao upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwenye Shule zetu za Sekondari. Tunapoelekea kutekeleza Sera hii mpya ya Elimu, eneo hili tumeliangalia. Tumeanza kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi kutoka Shule za Msingi na kuelekea Sekondari na kuhakikisha kuwa tunapata wafaulu ambao pia na wao tunawapeleka kwenye Vyuo vya Ualimu ili kupata taaluma ya ufundishaji wa masomo ya sayansi tuweze kupata walimu ambao watakuja kufundisha tena elimu hii kuanzia ngazi zote za msingi na sekondari ili tuweze kuongeza idadi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, mkakati uliopo ni ule ambao nimeueleza awali kwamba kupitia vibali tunavyopata kutoka kwa Ofisi ya Rais, tunatoa nafasi zaidi ya ajira za walimu wa masomo ya sayansi. Kwa mfano, ajira ya mwisho ya walimu 4,000, nafasi 2,500 zilikuwa za walimu wa masomo ya sayansi na nafasi 1,500 zilikuwa za walimu wa masomo ya Arts. Kwa hiyo, hii ilikuwa inatoa mwanya kwa mwalimu yeyote aliyehitimu mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi kupata ajira ili kuongeza nguvu ya ufundishaji kule kwenye shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati huu utaendelea na utakuwa endelevu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa pamoja na Wizara ya Elimu wanaendelea kusimamia hili kwa karibu ili kuondoa upungufu mkubwa uliopo kwenye masomo ya sayansi, ahsante sana.