Supplementary Questions from Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima (30 total)
MHE. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa nilipofika ofisini kwa Mheshimiwa Waziri akaniambia kwamba Meko tayari amepima viwanja 840 na akanijulisha kwamba amepima viwanja 4,000 Basihaya. Sasa kwa kuwa Chasimba, Chachui Chatembo na Kasangwe Burumawe, Kissanga na maeneo mengine ni maeneo ya Jimbo la Kawe na yaligubikwa na migogoro ya ardhi, sasa ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakwenda pamoja nami, Mbunge wa Kawe ili tukamalize migogoro iliyodumu kwa muda mrefu? (Kicheko)
WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amempa Mheshimiwa Njau. Pili nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Kawe, Askofu Gwajima, mimi Askofu Gwajima nilikuwa simjui lakini amenitafuta kwa shughuli hizi za kero za wananchi wa Kawe hata kabla hajawa Mbunge, ilinilazimu kutoka kwenye kampeni, kuacha kampeni zangu Isimani kwenda kumsikiliza Dar es Salaam kwa sababu ya hiki. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima….
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mimi najua angeuliza Mheshimiwa Halima ningemjibu, ninyi siwajibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Gwajima tukimaliza Bunge hili, nimepanga ratiba ya kwenda kukamilisha kero za migogoro ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatatua tatizo la Chasimba, Chatembo, Chachui kwa sababu mimi nilifanya kama Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwaonea huruma wale wananchi waliokuwa wafukuzwe. Kwa hiyo tutakwenda pamoja tutakwenda Basihaya, tutakwenda Chasimba na wananchi wanaoishi huko wajue kwamba nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kuhakikisha kwamba jambo hili la kero za wananchi kule sasa linaisha. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza:-
Mheshimiwa Spika, huko Nyakasangwe ambapo kule nyuma kumetokea mauaji kwa sababu ya matatizo ya ardhi. Je, ni lini sasa Waziri atakwenda pamoja nami huko ili tushughulike kuweka mambo ya wananchi sawa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, Askofu Gwajima, kwamba tutapanga wakati wowote tuweze kwenda kwa sababu sasa tuko kwenye bajeti, lakini tutapata fursa nzuri ya kwenda kwenye eneo alilolitaja.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali kidogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, kukamilika kwa Mji Mpya wa Kawe utaongeza shughuli za kijamii kwa wananchi wanaokaa kwenye eneo la Kawe, hasa Mzimuni, Ukwamani na maeneo mengine. Kukamilika kwa Mji Mpya wa Kawe ni kiashiria cha Kawe yetu ijayo kuwa wilaya. Je, ni lini hasa Mji Mpya wa Kawe utakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumjibu Mheshimiwa Askofu Gwajima swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa sababu baada ya kuingia tu Bungeni amekuwa akifuatilia sana mradi ule ili kuweza kuona unakamilika lini ili uweze kupendezesha maeneo yale. Azma ya Serikali hata ilipohamishia Makao Makuu hapa Mji wa Dar es Salaam ulibaki kama mji wa kibiashara. Kwa hiyo, lengo letu kama Serikali pia ni kuhakikisha kwamba mradi ule unakamilika ili ile maana halisi ya kufanya Dar-es-Salaam kuwa mji wa kibiashara na Kawe kuonekana kama satellite town ambayo tumekusudia kuifanya hivyo tumesema mwaka wa fedha unaokuja mradi ule utakwenda kukamilishwa. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi Mheshimiwa Wizara iko makini katika hilo. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza kwa kuwa, karibu wenyeji wote wa Jimbo la Kawe wanajishughulisha na shughuli za uvuvi mdogo mdogo hasa wa mitumbwi na mara nyingi hutokea ajali hasa wakati wa usiku na kuhatarisha wavuvi wetu. Ni lini sasa Serikali italeta Boti angalau Fiber Boat ndogo ndogo, kwa ajili ya kuokoa panapotokea madhila ya namna hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kata ya Msasani, Kata ya Kawe, Kata ya Kunduchi, Kata ya Mbweni, Mbezi pamoja na Bunju yote hiyo ni wavuvi wadogo wadogo wanaotumia mitumbwi na mikopo ya halmashauri haiwapi nafasi kwa sababu ina ukomo wa miaka 35. Ni lini sasa Serikali itakuwa na mpango maalum wa kuwapa mikopo hawa wavuvi ili kusudi kuboresha uvuvi wao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kuhusu usalama wa wavuvi na uokozi pale wanapopata madhila mbalimbali baharini. Serikali kwa pamoja Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kupitia Police Marine lakini na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu zote zinafanya kazi kwa pamoja na hivi sasa ninavyozungumza, tuko katika mkakati wa kuhakikisha kwamba, panapatikana chombo au vyombo ambavyo vitakuwa vikifanya kazi hiyo ya doria na jambo hili linaratibiwa vyema na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hivyo, wananchi wa Kawe na wenyewe wamo katika mpango wa namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, Jambo la pili ni kuhusu mikopo. Mheshimiwa Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe nataka nikuhakikishie kwamba, tumejipanga vyema na katika bajeti yetu ya awamu hii ya 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita ya mama Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema nataka nikukaribishe kwa ajili ya kuhakikisha vikundi na vijana wa pale Kawe waweze kupata mashine za boti lakini vilevile waweze kujiunga katika vikundi vitakavyowasaidia kutengeneza vichanja vya ukaushaji wa samaki na hata kutengeneza mashine za kuzalisha barafu wauziane wao wenyewe kwa ajili ya kuondosha tatizo la upotevu wa mazao. Ahsante.
MHE. ASK. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la Singida Mashariki linafanana kabisa na tatizo la Kata ya Mabwepande katika Jimbo la Kawe, ni lini sasa Serikali itamalizia ile Hospitali ya Jimbo la Kawe katika Kata ya Mabwepande?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni inajenga Hospitali ya Manispaa katika eneo la Mabwepande na mwezi wa tatu tulifanya ziara pale, tulishirikiana na Mheshimiwa Mbunge, iko hatua za mwisho za ukamilishaji na tulishatoa maelekezo kupitia mapato ya ndani wahakikishe hospitali ile inaanza kufanya kazi ndani ya mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya vifaatiba lakini pia kwa ajili ya kumalizia baadhi ya shughuli za ujenzi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Manispaa ya Kinondoni. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja tu la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Kawe lina barabara nyingi sana ambazo zinaunganisha Wilaya na Wilaya kwa mfano, Wilaya ya Ubungo pamoja na Kindondoni huko kwa juu.
Ni lini sasa Waziri atakwenda pamoja nami ili ukaone hali halisi katika Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mara baada ya Bunge nitaongozana na wewe pamoja na wale Wabunge ambao niliahidi katika Mkoa wa Dar es Salaam kuzungukia barabara zote za Mkoa huo, ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam kwenye Jimbo langu la Kawe hasa Kata ya Wazo kwenye eneo la Madale, Kisanga, Mbezi Juu hakuna maji kabisa. Waziri anasemaje kwa habari ya kuwapa maji watu wa Kawe, ni lini hasa Mheshimiwa Waziri? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, brother wangu Gwajima kwa kazi kubwa ya muda mfupi ambayo anaifanya katika Jimbo lile la Kawe. Tarehe 5 Julai nitakuwepo Jijini Dar es Salaam nina mazungumzo na watu wa DAWASA.
Mheshimiwa Mbunge nikuombe uwepo katika kikao kile na moja ya maelekezo ya haraka tutakayoyafanya ni kuhakikisha wananchi wa Wazo wanaenda kupata maji kwa haraka. Ahsante sana.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Jimbo la Kyerwa la maji, linafanana sana na tatizo la Jimbo la Kawe; na kwa kuwa ndugu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso alikuwa na mradi unaotokea Ruvu Chini mahali ambapo amejenga matenki Mabwepande, Bunju A, Tegeta, Salasala na maeneo mengine ya Jimbo la Kawe; na mradi huu ulitegemewa mwisho wa mwaka Desemba uwe umeshakamilika ili watu wapate maji, lakini mpaka leo Madale, Nakasangwe, Kisauke, Mabwepande, Tegeta hazina maji: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa mradi huu utakamilika ili wananchi wangu wa Jimbo la Kawe wapate maji? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo la Kawe. Kwa kweli maeneo ya Mabwepande yamekuwa na changamoto kubwa sana na tunaona kazi kubwa inayofanywa na DAWASA. Naomba baada ya saa 7.00 tukutane, tufanye mawasiliano na Mkurugenzi wa DAWASA ili tuweze kutia nguvu kwa pamoja na mradi ule uweze kukamilika na wananchi wa Mabwepande waendelee kupata huduma ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya barabara za Katavi yanafanana sana na matatizo ya barabara ya Kawe. Nataka kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri; barabara ya Bagamoyo – Tegeta imejengwa hapo katikati haina mitaro kabisa na matokeo yake inasababisha mafuriko kwenye maeneo ya Basihaya, DAWASCO na Boko; ni lini sasa Mheshimiwa Waziri utakwenda pamoja na mimi uone jinsi ambavyo TANROADS wamejenga bila mtaro kabisa na inasababisha mafuriko ambayo yanahatarisha maisha ya wananchi? Ni lini Mheshimiwa Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie mara baada ya kumalizika kwa Bunge tutaambatana naye kwenda kutembelea barabara hii. Ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza; barabara ya Bunju B, Msitu wa Mabwepande mpaka Mbezi Mwisho ilipandishwa daraja kutoka TARURA kuingizwa TANROADS na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Gwajima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema barabara hii ilikuwa inahudumiwa na TARURA na kwa kuwa imepandishwa daraja naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge kuwa katika kipindi hiki cha bajeti tuweze kuhakikisha kwamba barabara hii imeingia kwenye mpango ili tunapoanza utekelezaji wa bajeti inayofuata barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kama Mheshimiwa Rais alipoipandisha na kuhakikisha kwamba inajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASK. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Rais alipofika Bunju B, aliahidi kwamba barabara ya Bunju B kupitia Mabwepande itajengwa kwa kiwango cha lami; je, unaweza kuwahakikishia wananchi wa Mabwepande kwamba itawekwa kwenye bajeti ijayo 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri na mimi nimeitembelea hii barabara na kama alivyoomba iwepo kwenye bajeti Bunge hili ndiyo litaamua hiyo barabara ipitishwe kuwa kwenye bajeti, lakini sisi kama Wizara tunategemea kuipendekeza iwepo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Tegeta – Bagamoyo imejengwa na TANROADS na kuna sehemu ambayo hawajaweka mitaro kabisa, inasababisha mafuriko katika maeneo ya Basihaya na Tegeta: -
Mheshimiwa Spika, ni nini tamko la Wizara juu ya ku-repair eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala aliloliongelea la kusababisha mafuriko kwa sababu ya ujenzi wake kwa sababu ya barabara zimeinuka, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumelichukua na ninaomba kutumia nafasi hii nimwagize Meneja wa Barabara wa Dar es Salaam aende akafanye study ya nini Wizara tufanye ili tuweze kuondoa changamoto hii kwa wananchi. Ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali za kujenga minara, badala ya kuijaza Tanzania na utitiri wa minara, ni lini sasa itakuja na teknolojia ya kutumia mnara mmoja ili kuepusha nchi nzima kuwa na utitiri wa minara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari teknolojia ya kutumia mnara mmoja inatumika hapa nchini. Tunaita core location, core location maana yake kwamba Tigo inakuwepo pale pale, Airtel inakuwepo pale pale, Voda inakuwepo pale pale, kampuni zote zinakuwepo pale pale. Changamoto inayokuwepo ni katika maslahi ya hizo kampuni wanapo- share wanaona kama vile wananyang’anyana wateja. Kwa hiyo, hii ni changamoto ambayo inawahusu mobile network operator moja kwa moja, ambapo wao ndio wanaweza kuamua kwamba waende ku-share ama kutoku-share, kulingana na maslahi ya kibiashara zaidi. Ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Pamoja na majibu mazuri ya Mhehimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kitambulisho cha NIDA kinamthibitisha mtu kwamba ni Mtanzania, inakuwaje sasa wakati mtu anakwenda kutafuta hati ya kusafiria (Passport), anaombwa vitu vilevile alivyokuwa anaombwa wakati anaomba hati ya kusafiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kufanya hiyo namba ya Kitambulisho cha Taifa kuwa hiyo hiyo namba ya TIN na kuwa hiyo hiyo namba ya mita ya umeme kwa watu ambao wana nyumba zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali la Mheshimiwa Dkt. Askofu Josephat Gwajima maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika wakati tukawa tuna mdadisi mtu mara mbilimbili maana yake tumemdadisi kwenye NIDA pia tunamdadisi tupate maelezo yake kwenye hati ya kusafiria, suala kubwa hapa tunataka tujiridhishe. Kwa hiyo inabidi lazima tufike wakati tumhoji ili tuweze kujiridhisha kwa sababu hali za mifumo zinabadilika lakini na hali za binadamu pia zinabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kitambulisho ambacho alikuwa nacho, kwa sababu vitambulisho pia vina-expire date, vinakuwa na date of issue, kwa hiyo tunataka tujiridhishe kwamba ni yeye na labda alipotokea na mazingira mengine, kwa hiyo, kubwa hapa huwa tunataka kujiridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lake la pili ameuliza Je, Serikali haioni haja ya kusema sasa tuunganishe mifumo. Hilo ni jambo jema na tunalichukua ni wazo zuri kwenda kulifanyia kazi kwa sababu siyo Tanzania tu, zipo nchi ambazo tayari zimeshafanya huo mfumo na zinatumia NIDA na kitambulisho kingine. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Matukio ya ujambazi, watu kupigwa, panya roads kwenye maeneo ya Kawe, Kunduchi na maeneo mengine yamezidi sana. Sasa ni nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali ya nyongeza la Mheshimiwa Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia suala hili, kuna wakati ameongea kwenye YouTube tumeona, lakini baadhi ya taarifa hazikuwa kweli sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ujambazi nakupigwa ni ni jukumu la msingi la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na hususani Jeshi la Polisi. Nadhani mmemsikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, IGP na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Tumeahidi kushughulika na vijana hawa, tumesema wakitu-beep sisi tutawapigia. Kwa hiyo, kwa tahadhali hiyo, tunaomba watafute kazi nyingine ya kufanya badala ya uhalifu wanaofanya dhidi ya binadamu kwani hatutauvumilia. Ahsante.
MHE. ASK. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mradi mkubwa wa maji unaotokea Ruvu Chini kukamilika lakini baadhi ya Kata za Jimbo la Kawe kama Mbezi Juu hazina maji kabisa. Nini kauli ya Serikali?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kubwa mradi ule mkubwa tumeshaukamilisha na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika wiki ya maji alikuja kuuzindua, kazi iliyobaki ni suala zima tu la usambazaji. Kwa hiyo, kikubwa tutaongeza kasi juu ya usambazaji maeneo haya ya Mbezi Juu na maeneo mengine kuhakikisha kwamba wanapata huduma ya majisafi na salama.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nusu ya Jimbo la Kawe kwa maana ya Msasani, Masaki, Oysterbay, Kunduchi, Mbweni, Kawe, Bunju, Sea Cliff na Coco yote iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuendeleza hii michezo ya Bahari kwa ajili ya afya, burudani na kipato cha watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, je, utakubali Jumapili hii tuandamane pamoja tukafungue Ligi ya Rede kwa michezo inofanyika katika Jimbo la Kawe? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuchukua nafasi hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Josephat Gwajima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kwa kuona fursa kubwa iliyopo katika mchezo wa soka la ufukweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, soka la ufukweni katika nchi hii limeanzishwa rasmi mwaka 2014 na ni kwa miaka tisa tu ambayo tumekuwa tukilifanya, lakini limeonyesha kuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa tuko Namba Tano kwa Bara la Afrika kwa soka la ufukweni na Namba 42 kwenye rank za FIFA za kidunia kwa soka la ufukweni, namba ambazo hili soka letu la kawaida hatujawahi kuzifikia na pengine itatuchukua muda mrefu kidogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na TFF kwa kushirikiana na Serikali, kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye michezo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wanao mpango mkakati wa miaka mitano, ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha kwamba soka la ufukweni linafundishwa mashuleni na vyuoni na kila Mkoa ambao una fukwe kuweza kuwa na ligi yake kwa ajili ya soka la ufukweni. Lengo ni katika kipindi cha miaka mitano hii inayofuata tuwe na wachezaji angalau 10,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeanzisha mazungumzo na JKT na wadau wengine kadhaa ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji kwa ajili ya soka la ufukweni. Pia, kumekuwa na mashindano ya Copa Dar es Salaam ambayo yanazishirikisha nchi mbalimbali kama Burundi, Uganda, Comoro, Ushelisheli na Malawi, mwaka huu tuna mpango wa kuwaalika Kenya, Oman, Morocco na Senegal. Kwa hiyo, tutakuwa na Ligi ya Soka la Ufukweni yenye nchi Tisa, ambapo ni wazi kabisa itaongeza Pato la Taifa lakini wachezaji wetu wengi watashiriki na itatoa ajira za moja kwa moja na ajira nyingi nyingine zinazozunguka mchezo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, najua Askofu utakuwa na maono, umengundua kama Jumapili ninao muda na tutaambatana mimi na wewe kwa ajili ya kwenda kuanzisha Ligi yako ya rede pale Jimboni Kawe. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Barabara ya Tegeta – Basihaya – Bunju mpaka Bagamoyo katika Jimbo la Kawe imejengwa bila mitaro ya maji. Kwa sababu hiyo, husababisha mafuriko makubwa sana kwenye maeneo ya Nyaishozi, Tegeta, Nyamachabes. Sasa, ni lini Serikali itajenga mitaro ya maji kuepusha hatari kwa wananci kwa sababu ya mvua zinazoendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Askofu Gwajima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua katika kipindi hiki mvua imeendelea kubwa sana kwa Jiji la Dar-es-Salaam na eneo alilolitaja kwa kweli limeathirika kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja yote ya Basihaya, Msikitini, DAWASA na Nyaishozi yalikuwa yamefanyiwa design yaanze kujengwa kabla, lakini kwa kuwa tuna Mradi mkubwa wa BRT IV maeneo haya yatakuwa ni sehemu ya ujenzi wa Mradi huo wa BRT IV.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Jimbo la Kawe, tulichokifanya, tutawahusisha na tumehusisha pia TARURA ili wakati wa kujenga pia hiyo mitaro na wenzetu wa TARURA tusije tukajenga halafu kuwe na changamoto kwenye barabara zetu, kwa hiyo nao watahusika. Mkataba uko tayari kusainiwa. Kwa hiyo, muda wowote kazi ya ujenzi kwa BRT IV itaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini? Inawezekana hata ikawa Juni tukasaini huo mkataba. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASKF. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba barabara ya kutoka Bunju B mpaka Mabwepande ijengwe kwa kiwango cha lami katika Jimbo la Kawe: Ni lini Serikali itatimiza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Bunju B – Mabwepande – Magohe – Mapigi hadi Kibamba, ni moja ya barabara ambayo sasa hivi inafanyiwa usanifu. Siyo tu ahadi ya viongozi, lakini tunategemea ndiyo itakuwa altering ya barabara za Mji wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, ipo kwenye mpango na tunavyoongea sasa hivi Washauri Wahandisi wako kazini wanafanya usanifu, ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa sababu ya wingi wa mvua zinazonyesha katika Jiji la Dar es Salaam, barabara nyingi zilizo chini ya TARURA katika Jimbo la Kawe zimekatika vipande vipande.
Ni nini mpango wa Serikali ku-repair barabara hizi ili wananchi waweze kupita na kuondoa usumbufu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gwajima la barabara za Dar es Salaam kukatikakatika kwa sababu ya mvua, tunaenda kuanza kutekeleza Bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa Wakala wa barabara ikiwemo Dar es Salaam. Mheshimiwa Mbunge naye ni shahidi kwamba hivi karibuni wamesaini mkataba kwa ajili ya uanzishwaji wa mradi wa DMDP II ambao utakwenda kuwa mwarobaini wa barabara hizi mbovu za Jiji la Dar es Salaam kwa kujenga mifereji na kuhakikisha barabara pia zinapitika wakati wote.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniruhusu niulize swali moja la nyongeza.
Ni lini Serikali itajenga barabara ya mwendokasi yaani BRT - 4 ambayo kipande kikubwa kinaanzia Mwenge - Makongo Sekondari, Lugalo Jeshini, Mbezi Beach, Tegeta kwa Ndevu, Nyaishozi mpaka Basihaya ambayo pia itaondoa mafuriko yanayoikumba Basihaya kwa kujenga mitaro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge wa Kawe kwamba barabara aliyoitaja iko kwenye BRT - 4 ambayo itaanzia Maktaba itakuja Mwenge mpaka pale Daraja la Kijazi hiyo itakuwa ni Lot ya kwanza; na Lot ya pili itaanzia Mwenge – Tegeta mpaka kuja huku DAWASA.
Kwa hiyo, tutakuwa na wakandarasi wawili; lot ya kwanza ndiyo hiyo na lot ya tatu itakuwa ni mkandarasi ambaye atajenga majengo.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tarehe 30 Juni, 2023 siku ya Ijumaa pale DAWASA tunakwenda kusaini mikataba hiyo ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya BRT - 4, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa asilimia 75 ya mafuta ya kupikia yanatoka nje ya nchi na kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kupikia kilichopo katika Kata ya Wazo kinaitwa Family kimefungwa.
Je, Mheshimiwa Waziri ataambatana pamoja na mimi baada ya hapa ili kujua ni sababu gani kiwanda hicho kimefungwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Mchungaji Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali sasa hivi mkakati wetu ni kuhakikisha tunajitolesheza kwenye mafuta ya kula. Kwa hiyo kama kweli kuna kiwanda ambacho kimefungwa na mimi kama Naibu Waziri kwenye sekta inayohusu viwanda, nitaambatana na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuona changamoto gani zinakikabili hicho kiwanda ili kiweze kuendelea kuzalisha mafuta ya kula ili kupunguza changamoto hii ya mafuta ya kula nchini, nakushuru sana.
MHE. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Kawe, katika Wilaya ya Kinondoni lina mtandao mkubwa wa barabara kuliko majimbo yote ya Dar es Salaam; je, Serikali inaweza kusema ina mkakati gani kuongeza nguvu kuongeza barabara kutengeneza kupitia DMDP awamu ya pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kwamba tunatambua ukubwa wa Jimbo la Kawe kama ilivyo katika majimbo mengine na tunatambua umuhimu wa kuongeza bajeti. Na katika mradi DMDP moja ya vigezo ambavyo umezingatia ni pamoja na ukubwa wa maeneo. Kwa hiyo, mgawanyo utalizingatia ukubwa wa maeneo husika, ahsante sana.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mvua nyingi zinazoendelea katika Jiji la Dar es Salaam mito mingi imejaa na kumwaga maji kwenye nyumba za wananchi; na watoto wengi wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya mito hiyo na imehatarisha maisha ya watu na nyumba za watu.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kusaidia kudhibiti mito hii isiharibu maisha ya watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mto Nakasangwe, Mto Tegeta, Mto Mbezi, Mto Ndumbwi na Mto Mpiji miaka miwili iliyopita ilikuwa na upana wa mita 50 tu leo ina upana wa mita 100.
Je, Waziri utakubali kwenda pamoja na mimi ukaione mito hii wewe mwenyewe na utafute ufumbuzi wa kudumu wa kudhibiti mito hii kwa ajili ya kuokoa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Askofu Gwajima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kumpa pole sana Mheshimiwa Gwajima kwa kuingiliwa kwa maji katika maeneo yale, mito mingi imefurika. Lakini pia nachukua fursa hii kumpongeza sana mpaka jana usiku nilikuwa naangalia kwenye vyombo vya habari yupo Kawe anawasaidia Wananchi, anashirikiana nao katika janga hili la kuingiliwa kwa maji. Nataka kuchukua fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wote ambao wameathirika na mvua kwa njia moja au nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mipango ya dharura ambayo tunakwenda kuifanya kama Serikali kuhakikisha kwamba tunatatua hii changamoto ya kufurika kwa mito na maziwa na maeneo mengine ambayo yanajaa maji yanaathiri wananchi; kwanza ni kwenda kutafuta fedha kuhakikisha kwamba tunajenga kuta ambazo zitazuia maji yasiingie kwenye makazi ya wananchi. Pili tutahakikisha tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajue athari za mvua na athari za kukaa kwenye mabonde, na pia wajue namna ya kuweza kuondoka mapema kabla mvua hizi hazijaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti vilevile, tunakwenda kuishirikisha jamii kwenye masuala ya usafi wa mito, mitaro na maeneo mengine ambayo yanakwamisha maji yasiende mwisho wa siku yanasabisha maafa. Kubwa ni utekelezaji wa Sheria ile ya mita 60 kama ilivyozungumzwa katika Kanuni ile ya 191 ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa jambo hili na kazi kubwa anayoifanya Dkt. Gwajima nipo tayari kwenda Jimboni Kawe kushirikiana na Wananchi kuhakikisha kwamba tunawasaidia katika kuondokana na hii changamoto ya uingiaji wa maji katika makazi yao, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, nakumbuka tulisaini Mkataba wa Barabara ya Mwendokasi inayoanzia Mwenge – Tegeta – Basihaya. Je, ni lini barabara hiyo ambayo Mkataba wake tumeshasaini itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba tu kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri siku ya kusaini hiyo barabara mimi mwenyewe nilishiriki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua iliyopo sasa hivi iko kwenye zile hatua za awali, yaani mobilization kwa ajili ya kuanza kuijenga hiyo barabara. Wakandarasi tayari wako wanafanya mobilization kwa ajili ya kujenga, yaani maandalizi ya awali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo, ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba Barabara ya kutoka Bunju B kwenda Mabwepande mpaka Ubungo ijengwe kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu, lakini Mheshimiwa Gwajima na Waheshimiwa Wabunge kama wanavyofahamu sasa hivi kuna ukatikaji wa mawasiliano ya barabara na madaraja kote nchini, kipaumbele namba moja ni kuhakikisha tunarudisha mawasiliano haya ili shughuli za uzalishaji kiuchumi na kijamii ziweze kuendelea. Kwa hiyo barabara hizi ikiwemo hii barabara ambayo Mheshimiwa Gwajima amekuwa akiifuatilia kwa karibu tumuahidi yeye pamoja na wananchi kwamba kadri fedha zitakavyopatikana na yenyewe tutaiweka kwenye vipaumbele. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kuniruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza; matumizi ya artificial intelligence kwa maana ya ufahamu bandia (akili mnemba), tayari yameshaanza kutumika hapa nchini kwetu. Tarehe 27 Januari yalifanyika majaribio ya mwalimu kufundisha akiwa Kibaha akafundisha Shule ya Dodoma na limefanyika jaribio lingine la daktari akiwa Dar es Salaam akafanya upasuaji Zanzibar na ukafanikiwa.
Je, hatuoni sasa kwamba introduction ya artificial intelligence inawaondolea watu ajira zao kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; matumizi ya roboti yanalenga kutatua tatizo la upungufu wa watu duniani. Nchi za Magharibi duniani ambapo roboti inatokea watu ni wachache, huku kwetu bado tupo na watu wengi sana. Itakuwaje tutakapofika wakati, mwalimu roboti, daktari roboti na rubani roboti; tutawapeleka wapi watu ambao tunawa-train leo.
Je, Serikali imejiandaa kujua cha kufanya baada ya roboti kuwa zimechukua ukanda wa ajira zote? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na kumpongeza Naibu Waziri na Wizara ya Elimu kwa majibu mazuri na maandalizi mazuri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya sayansi na teknolojia na ubunifu duniani yametupitisha kwenye mapinduzi kadhaa ndiyo maana tuna mapinduzi ya kwanza ya viwanda, mapinduzi ya pili, mapinduzi ya tatu na sasa tupo mapinduzi ya nne na kuna nchi zimeanza mapinduzi ya tano na ya sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mapinduzi yaliyotokea yamekuwa na sifa zake na katika hizo sifa kumekuwa na faida na hasara ya kila mapinduzi kutoka mapinduzi mamoja kwenda mapinduzi mengine. Yapo ambayo yameleta faida, lakini pia yameleta hasara. Tukianza mapinduzi ya kwanza kuna watu walipoteza kazi na kuna watu walipata kazi; mapinduzi ya pili, kuna watu hivyo hivyo walipoteza kazi na kuna watu walipata kazi. Tunafaidikaje au tunapataje hasara inategemea na namna tulivyojipanga na kujiandaa kwa mapinduzi hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mapinduzi ya nne yanajulikana, namna mnavyojiandaa, mnajiandaa kwa kuwa na mifumo mizuri ya sheria kwa maana ya legal framework, kuwa na sera, sheria na kanuni ambazo zitasaidia kuwalinda watu wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mnakuwa na taasisi zitakazosimamia hayo mapinduzi na ya tatu, mnakuwa na uwekezaji kwenye hayo mapinduzi ili mtoke salama. Sasa Serikali imejipangaje? Kwanza, tumpongeze Rais Samia kwa maono yake ya kuanzisha Wizara inayoshughulikia TEHAMA, kwa sababu alipoingia madarakani akaianzisha Wizara. Kazi ya Wizara ni kuziandaa hizo sheria, kuandaa hizo taratibu, lakini pia kuziandaa taasisi na uwekezaji ili Taifa letu lipate faida katika matumizi ya akili bandia badala ya kupata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilihakikishie Bunge lako na Bunge lina wajibu wa kuhakikisha sheria zinatungwa, taratibu zinawekwa ili wale watakaopoteza ajira kuwe na namna ambayo watashughulikiwa. Pia, tuliandae Taifa letu kwamba haya mabadiliko yana fursa ndani yake na ndiyo maana tunawafundisha watoto wetu, tunaandaa vyuo, tunaelimisha jamii ili tusipitwe kwa sababu haya mapinduzi hayakwepeki, lazima tujiandae kwenda huko mbele. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii gesi asilia (CNG) sasa inatumika kwenye gari nyingi, je, hamuoni kuwa sasa ni wakati mwafaka wa kufungua vituo njiani ili mtu anapokuwa anasafiri kutoka Dar es Salaam kuja hapa kuwe na vituo maalumu kabisa vya gesi asilia ambako mtu anaweza kujaza kwenye gari lake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima. Ni kweli kwamba Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi tumeanza mkakati wa kutafuta namna ya kuwa na vituo kwa gari binafsi kuanzia Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa awamu ya kwanza. Tayari tumekwishaanza kuwa na mkakati huo na tayari wadau wa sekta binafsi wameshaanza kujitokeza kwa ajili ya kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo barabarani kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma. Hata kwa upande wa magari ya Serikali tayari TPDC imeanza kuongea na Bohari za GPSA ili kuongeza vituo vya CNG kwenye hivi vituo vya bohari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili pia hata magari ya Serikali nayo yakiwa yamekwishabadilishwa yaweze kujazwa gesi kutokea Dar es Salaam – Dodoma ambapo ndiyo njia kuu ya magari haya kwa kiasi kikubwa yanapopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa pande zote mbili za magari binafsi pamoja na magari ya Serikali tumekwishaanza kulifanyia kazi suala hili ili kuongeza idadi ya magari ambayo yanatumia CNG, ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wetu wa Jeshi la Wananchi Tanzania Bima zao zinawaruhusu kutibiwa katika hospitali za Jeshi peke yake, na hospitali hizi za Jeshi haziko kila mahala nchini. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa ku-extend bima zao ili waweze kutibiwa kwenye hospitali zingine pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake ni la msingi sana na kwa sababu linahusu Wizara mbili, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Afya tunalichukua na tunaitana mara moja kulijadili hilo ili kuweza kurahisishia Jeshi letu kupata huduma kwa urahisi. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kawe lina mashina zaidi ya 1,000 na takribani kila shina lina barabara sita na huu ni mzigo mkubwa. Serikali ikitumia utaratibu wa kawaida inaweza isiweze kumaliza mzigo wa barabara hizi.
Je, Serikali ina mpango gani wa ziada wa kumaliza Barabara hizi ambazo ni karibu elfu sita na kitu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli tunamwona jinsi gani anavyotembelea maeneo mbalimbali kutazama na kuleta msukumo katika kuhakikisha wananchi wake wanapata barabara zilizo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kwamba Serikali inatenga fedha katika Manispaa ya Kinondoni shilingi bilioni saba kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi za TARURA, lakini pia Manispaa ya Kinondoni ipo katika Mradi wa DMDP II ambao ni mradi wa jumla ya USD milioni 438. Mradi huu utaenda kusaidia sana katika kurekebisha barabara katika jimbo lako.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa sababu ninyi mkiwa kama sehemu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni mmeweza kununua mitambo kupitia mapato ya ndani; mmenunua wheel loader, grader na excavator ambazo sasa hivi zipo katika hatua ya clearance na wiki ijayo mitambo hii itakuwa imetoka. (Makofi)
Sasa ninawapongeza kwanza, lakini ninachukua nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwagiza Mkurugenzi, mara tu mitambo hii itakapotoka iingie site, ifike katika Jimbo la Kawe, ianze kuchonga barabara ili wananchi waweze kupata barabara nzuri kabisa. (Makofi)