MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali imefikia wapi taratibu za ujenzi wa Barabara ya Mtwara Pachani kwenda Lusewa – Magazini mpaka Nalasi – Tunduru? Maana Mwenyekiti mmoja wa kijiji…
SPIKA: Mheshimiwa hiyo ni barabara moja?
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ndiyo, ni barabara moja, ila inapitia kwenye Kata za Lusewa - Magazini...
SPIKA: Haya, uliza swali lako sasa.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Mtwara – Pachani – Nalasi ambayo inapitia katika kata hizo?
Mheshimiwa Spika, juzi nilielezwa na Mwenyekiti wa Kijiji kimoja kwamba mwezi wa Nne niwe nimeanza kuijenga barabara hiyo au watanishughulikia. Je, Serikali inawaeleza nini? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa...
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ngoja kwanza. Mheshimiwa Mbunge maelezo ya sehemu ya pili ya swali lako kidogo yatakuwa nje ya utaratibu wa yale anayoweza kujibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa hiyo, ili umweke sehemu nzuri, hebu mwulize swali lako kwa yale anayoweza kuyajibu yeye kama Naibu Waziri wa Ujenzi. Ile sehemu ya pili mwondolee ili asilazimike kukujibu.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali imefikia wapi kuhusu utaratibu wa kuijenga barabara ya Mtwara - Pachani mpaka Nalasi – Tunduru ambayo inapita kwenye Kata za Mkongo, Ligera, Lusewa, Magazini mpaka Tunduru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna uhitaji mkubwa sana wa kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami. Tulichofanya kama Serikali, kwanza ni kuisanifu barabara yote wakati tunatafuta fedha kuijenga hiyo barabara ambayo ina urefu wa kilomita 300.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tulichomwahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, wakati tunaendelea kutafuta fedha, maeneo yote korofi katika hiyo barabara ambayo huwa yanaleta changamoto tutahakikisha kwamba tunayaimarisha kwa kuyajenga kwa zege ama lami ili wananchi hao wasikwame wakati Serikali inatafuta fedha. Hivyo, mpango huo upo, ndiyo maana tumefanya usanifu kwa barabara yote, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali na nina maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa mpango huo na ninatambua kuna vivuko vingine vinafanyiwa maboresho kama kivuko cha MV Nyerere na kadhalika. Vivuko hivi vikishakamilika au vikihamishiwa Ukerewe kunatakiwa kuwe na magati ambayo yatasaidia vivuko hivi kutua, lakini sioni dalili zozote za maandalizi ya magati kwenye eneo la Gana, Kakukuru, Lutale wala Ilugwa. Ni nini mkakati wa Serikali kuanza maandalizi ya magati kwenye maeneo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwenye bajeti ya mwaka 2024 tulitenga pesa kwa ajili ya kujenga mabanda ya abiria kusubiri kwenye eneo la Bugolola, Bwisya pamoja na Bukimwi lakini sioni kazi yoyote inayoendelea. Ni nini mpango wa Serikali kujenga mabanda haya ya abiria kusubiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala haya ya vivuko na hasa katika Jimbo lake la Ukerewe ambalo linaunganisha sehemu kubwa na vivuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magati, eneo hili ambalo nalisema ni sehemu ambayo kivuko kipya kinakwenda. Kwa hiyo, tunachofanya sasa hivi, ni usanifu ili kujenga magati ambayo yatahudumia katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vivuko vyote ambavyo vinafanya kazi, na tunajenga vivuko vipya, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba tayari magati yanaendelea kujengwa na yapo kwenye hatua za mwisho kabisa. Kwa hiyo, sasa hivi tunachofanya katika maeneo haya ambayo ni mapya, sasa hivi tupo kwenye usanifu ili tuweze kuanza kujenga magati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika swali lake la pili kuhusu mabanda, tumetenga bajeti katika mwaka huu 2025, wakati tunaendelea na ujenzi wa vivuko vipya. Pia tuna mpango wa kujenga mabanda, na kazi hii Wizara imeipa TBA ambao wapo mwishoni kabisa kukamilisha usanifu wa mabanda kwa sababu haya mabanda hayafanani kati ya kituo na kituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mpango huo upo na tupo hatua za mwisho za usanifu na baada ya hapo tutaanza ujenzi pia wa mabanda ili kutoa huduma katika maeneo hayo ya vivuko. Ahsante. (Makofi)