Supplementary Questions from Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (43 total)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa sababu amenihakikishia kwamba mradi unakamilika Machi mwaka huu, napenda sasa kupata kauli ya Serikali kwa sababu bado tuna vijiji takribani 25 pale Biharamulo ambavyo havina umeme, kwa hiyo, labda ningehakikishiwa na Serikali sasa kwamba wakazi wa Biharamulo wajipange kwa ajili ya kusambaziwa umeme kwa sababu jibu ilikuwa tuko low voltage ndio maana hatukusambaziwa umeme katika vijiji vingine. Kwa hiyo, labda nipate kauli ya Serikali kutuhakikishia kwamba vijiji vilivyobaki baada ya kukamilika mradi huu vitaweza kupata umeme pia? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, uniwie radhi sana ili niweze kusimama kwa ajili ya kuongeza majibu na nimesimama kwa sababu hivi karibuni nilitembelea Biharamulo.
Mheshimiwa Spika, Biharamulo wana vijiji takribani 79 na bado vijiji 27. Hivi karibuni pamoja na Mheshimiwa Mbunge nilitembelea vijiji hivyo, tumeshakamilisha matayarisho yote na si kwa Biharamulo peke yake.
Napenda nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba vijiji vyote ambavyo havijapata umeme 2,159 kati ya vijiji 12,268 tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia tarehe 15 mwezi huu ndani ya miezi 18, nimeona nianze na taarifa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa Biharamulo umeme ambao tunajenga ambao kwenye jibu la msingi umeelezwa wa kutoka Geita-Nyakanazi, Nyakanazi-Rusumo na Nyakanazi- Kigoma ni mwarobani kwa kuwapatia umeme wananchi wa Biharamulo na Mkoa wa Kagera na mikoa ya Geita pamoja na Kigoma. Mradi wenyewe peke yake kabla ya kupeleka umeme kwenye mpango wa REA utapeleka vijiji 32 na katika vijiji 32 vijiji saba ni vya Biharamulo, ikiwemo Nyakafundwa, Kalenge, Kasonta pamoja na Nyanyantakala, Mavota mpaka Nakahanyia vyote vitapelekewa umeme.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nitoe shukrani kwa Serikali kwa majibu mazuri kabisa ya kuridhisha kwa ajili ya wananchi wa Biharamulo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Miji ya Nyakanazi, Nyakahura na Nyanza ni miongoni mwa sehemu ambazo zinapanuka kwa kasi katika Wilaya ya Biharamulo lakini bado zina ukosefu wa maji. Naomba kujua au kusikia kauli ya Serikali jinsi gani hawa wananchi wataweza kupatiwa huduma ya maji katika mwaka huu wa fedha au mwaka ujao ili tuweze kuondoa kero hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kata ya Kaniha na Nyantakala zinabeba shule mbili kubwa za boarding pale Biharamulo na shule zile zina uhaba mkubwa wa maji. Naomba kupata kauli ya Serikali ni lini wataweza hata kuchimbiwa visima viwili virefu katika shule zile ili watoto hao waweze kuondokana na adha ya kupata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua vema tatizo la maji lililopo pale Biharamulo. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alikuwa katika Kata ya Nyakahura kwenye ziara yake ya kikazi. Kwa sasa maji toka Bwawa la Nyakahura ambapo vijiji vinne vinapata maji, tunatambua utekelezaji wake unakwenda vizuri kwa vijiji vile vinne.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunafahamu kuna ushirikiano mzuri kati ya RUWASA pamoja na BWSSA. Tayari Serikali inafahamu chanzo kile bado hakitoshelezi kwa sababu ya ongezeko la watu. Tayari Serikali kupitia EWURA imeshatenga fedha za usanifu wa maji kutoka kwenye Mto Myovozi. Lengo ni kuona kwamba eneo lote la Nyakahura linakwenda kupata maji safi na salama ya kutosheleza hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye kwenye Kata ya Nyanza usanifu unaendelea. Pia tutahakikisha maji ya kutosha yanakwenda kupatikana. Tayari kuna chanzo chenye uwezo wa lita 50,000 kwa saa ambapo maji haya yatasaidia sana mpaka kwenye Kata ya Nyanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inatambua umuhimu wa maji mashuleni. Tayari kwenye Shule ya Mbaba kuna kisima kirefu pale kimechimbwa na maji yanapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Nyantakara, mradi umetekelezwa. Pale tuna mradi mkubwa tu ambapo fedha zaidi ya shilingi milioni 300 zimeelekezwa na maji yatafika mabombani muda sio mrefu, haitazidi wiki tatu.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana; na mimi kwa niaba ya wananchi wa Biharamuro ningependa niongezee swali la nyongeza. Wilaya ya Biharamuro ni miongoni mwa wilaya kongwe kabisa za nchi hii lakini ukiingia katika mazingira ya polisi wa Biharamuro wanapoishi, bado wanaishi kwenye nyumba zilizojengwa na Mkoloni pale. Lakini mazingira ya kazi ni magumu wote mnajua kumekuwa na majambazi kule lakini vijana wale wanajitahidi kupambana nao usiku na mchana na hali yetu ni shwari kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maswali niliyonayo ni mawili, ni lini tutajengewa kituo kipya cha Polisi, ikizingatiwa tayari hati iko pale na kiwanja kipo tayari? Lakini pili…
NAIBU SPIKA: Moja tu Mheshimiwa; moja tu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ruhusa yako, nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kukiri tena kwamba bado tuna changamoto hasa kwenye usafiri, makazi na Vituo vya Polisi. Kwa kuwa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tayari wana hati ambayo inawamilikisha wao waweze kujengewa eneo zuri waweze kupata jengo zuri ambalo litatoa huduma za ulinzi na usalama kwa wananchi, nimwambie tu kwamba aendelee kustahimili na mimi nalichukua hili tunakwenda kulifanyia kazi ili tuhakikishe kwamba katika eneo lake wanapata kituo kikubwa kizuri na cha kisasa ambacho kitaendelea kutoa huduma kwa wananchi na wananchi wakaendelea ku-enjoy hiyo huduma ya ulinzi na usalama katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na pesa ambayo tumeipata hiyo shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu majengo yanaelekea kukamilika na tumefikia mwisho sasa, ni nini mpango wa Serikali kutupatia vifaatiba ili majengo haya angalau yaweze kuanza kufanya kazi haraka iwezekanavyo kwenye robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2021/2022?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu hospitali hii bado ni sehemu ya kwanza itakuwa haiwezi kulaza wagonjwa, ni nini mpango wa Serikali kwenye kutupatia ambulance mpya na ya kisasa ili angalau wagonjwa wale ambao hawataweza kupata huduma kwenye Hospitali ya Wilaya waweze kukimbizwa na kupatiwa huduma sehemu nyingine kipindi tunaendelea na kukamilisha ujenzi wa awamu ya pili? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba majengo haya ya Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo yako katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Katika mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kwenda kununua vifaatiba kwa ajili ya hospitali hizi mpya ambazo zinaendelea na ujenzi. Kati ya hospitali hizo, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitatengewa bajeti hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili tunahitaji kuwa na magari ya wagonjwa katika hospitali zetu za halmashauri na mipango ya Serikali inaendelea kufanyika ili kuona namna ambavyo tunaweza tukapata magari hayo na kuyafikisha katika halmashauri hizi. Kwa hivyo, Hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo ni moja ya hospitali ambazo zitawekewa mpango wa kupata gari la wagonjwa ili tuweze kuboresha zaidi huduma za afya katika eneo hilo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza ambayo ningependa kupata majibu yake. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii ni kiunganishi muhimu ambacho kinaunga Chato na Biharamulo kuelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, ningependa kujua sasa kwamba construction period ya barabara hii itakuwa ni miezi mingapi ili nijue na wananchi wale waweze kujipanga kwa ajili ya kuchukua fursa za pale?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuzingatia umuhimu wa Hifadhi ya Chato Burigi na location ya Uwanja wa Ndege wa Geita Chato ulipo, sasa ningependa kujua je, Serikali haioni ni wakati muhimu sasa wa kuijenga barabara hii sambamba na barabara ya Mkingo – Chato kupitia Kaswezibakaya ili iweze kuunganisha Kabindi pale watu wanaokuja waweze kutoka vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba barabara hii imetengewa fedha kwenye bajeti hii na yeye Mheshimiwa Mbunge ni shahidi. Kipindi cha matengenezo kitategemea na hali halisi, lakini cha msingi tu ni kwamba mara bajeti itakapoanza barabara hii itaanza kujengwa, lakini kipindi kitakachotumika itategemea na taratibu za manunuzi zitakavyokamilika, lakini pia na hali ya hewa itakayokuwepo. Kwa hiyo, ni ngumu kusema itachukua muda gani, lakini tutaanza kujenga mara tu bajeti itakavyoanza kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, barabara hii itaendelea kukarabatiwa katika kiwango cha changarawe. Hata hivyo, azma ya Serikali ni kuijenga kwa kiwango cha lami kadri fedha itakavyopatikana ili watalii na watu mbalimbali waweze kupita kwenye hizo mbuga za wanyama na kufika kwenye Uwanja wa Ndege wa Chato. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali, lakini pia labda nieleze kidogo; mnamo tarehe 1 mwezi wa Kumi mwaka jana 2020 tukiwa katika kampeni Waziri Mkuu aliahidi ujenzi wa soko hili pale Nyakanazi na tarehe 11 mwezi wa Pili wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, swali lililoulizwa na Mheshimiwa Neema Lugangira aliahidi pia ujenzi wa soko hili na akataja kabisa ni soko la kimkakati na akataja value yake kama ni 3.5 billion.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu ya Serikali wanasema wanahamasisha Halmashauri ya Biharamulo ili iweze kufanya ujenzi wa soko hili; hili soko limetamkwa, ukisema 3.5 billion kwa Halmashauri ya Biharamulo wajenge soko hili, labda litakaa zaidi ya miaka kumi, kwa sababu uwezo huo hatuna; na ilitamkwa humu ndani ya Bunge: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate commitment ya Serikali kwanza nijue financing ya soko hili itafanyika vipi? Sisi uwezo huo hatuna. Kwa hiyo, nipate majibu ya Serikali kama Serikali kuu itafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu soko hili ni muhimu kwa ajili ya kufungua ukanda wetu na ni soko la kikanda litakalohudumia nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na nchi nyingine zote za Jirani: nipate majibu ya Serikali, ni lini ujenzi wa soko hili utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mkakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha inatekeleza ahadi ambazo viongozi wa Serikali wanaahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Chiwelesa kwa ufuatiliaji mkubwa anaofanya kwa ajili ya maendeleo katika Jimbo lake la Biharamulo Magharibi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli masoko haya ya kimkakati na hasa masoko ya pembezoni ambayo yako katika mipaka ya nchi za jirani na hasa hizi za Kongo, Rwanda na Burundi ni masoko ambayo yana umuhimu sana kuyaendeleza ili yaweze kuleta maendeleo ya nchi, lakini kuwapatia kipato wananchi wanaokaa katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kupitia programu ya ASDP II ambayo pia imeweka ule mfumo wa O and OD ambao ni fursa na vikwazo kupitia utaratibu huo, Halmashauri zinahamasishwa kuangalia vyanzo mbalimbali vya ku-finance mipango yao, mikakati yao katika kuendeleza sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na TAMISEMI tuna mikakati mbalimbali ambayo pia kupitia humo tunaweza kujenga masoko haya kulingana na fedha zinazvyopatikana. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi pia.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Biharamulo tuna vijiji 75. Kati ya vijiji 75 vijiji 25 havina mawasiliano kabisa, kabisa, na bado tuna shida, ukiachilia mbali vitongoji. Sasa ni nini hatua ambayo Serikali imachukua kwa ajili kuweza kuboresha mawasiliano? Ukizingatia watu hawa nao inabidi washiriki mchango wa maendeleo wa nchi hii lakini wameachwa mbali kwa sababu wako katika maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa. Nataka kusikia kauli ya Serikali kuhusu vijiji 25 vya Biharamulo.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra Mbunge wa Biharamulo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ambayo imebahatika na ambayo itanufaika katika mpango wa utekelezaji mradi wa mipakani basi na Biharamulo inaenda kupata miradi takribani sita.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba kipindi kitakapofikia tena cha kuleta bajeti ili tuweze kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata mawasiliano basi aweze kutuunga mkono kuhakikisha kwamba bajeti hii iweze kwenda kujibu mahitaji ya Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo kubwa sana katika eneo hili la hifadhi hii ya Burigi Chato na tunashukuru kwa fedha ambazo zimetolewa na kutoa elimu kwa umma unaozunguka hifadhi ile. Kumekuwa na kesi kubwa sana pale za mifugo ya watu kukamatwa ndani ya hifadhi lakini baada ya kukamatwa zinapopelekwa kesi mahakamani, watu wale wamekuwa wanatozwa fine ya Shilingi 100,000/= kwa kila ng’ombe na wengi wanalipa baada ya kutozwa ile fine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa shida imekuja unatoza fine mahakamani ulikamatiwa ng’ombe 100 unapopewa barua ya mahakama, umeshalipa fedha ya Shilingi Milioni 10 ukarudishiwe ng’ombe wako unaenda unakuta ng’ombe wako 70, ng’ombe wako 80 badala ya ng’ombe waliokamatwa.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya vitendo hivi ambavyo vimesababisha wananchi wa Biharamulo kuteseka na hatimae kupoteza fedha zao na ng’ombe hao ambao wamekuwa wanapotea huko. Nisikie kauli ya Serikali juu ya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwa na kesi pia wananchi wananifuata ninapokuwa Jimboni, saa nyingine wanapiga simu na kwa DC kesi zipo. Mwananchi anakuja analalamika kwamba, Mheshimiwa Mbunge nimekamatiwa ng’ombe wangu 50 bado tuna kesi mahakamani, lakini ng’ombe wangu nimewaona kwenye mnada wanauzwa. Sasa naomba kusikia kauli ya Serikali juu ya hili jambo ambalo limesababisha watu sasa wanaona taabu kabisa na wanatuchonganisha na wananchi. Tukisikia kauli ya Serikali juu ya hili pia hao ng’ombe ambao wamekuwa wanauzwa kwenye mnada je, hatuoni haja ya Serikali kuunda Tume Maalum, kwa ajili ya kwenda kuangalia hivi vitendo vya wananchi kulalamika? Kwamba, ng’ombe wao wanauzwa kwenye mnada na ilhali bado kesi zinaendelea mahakamani.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika,
ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kutoa pole kwa wale wananchi ambao wameendelea kukutana na kadhia hii, ya kudhulumiwa mifugo yao na kumekuwa ndiyo na malalamiko mengi na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walishawahi kunifuata kwamba, kuna baadhi ya wahifadhi wasio waaminifu ambao inapelekea mifugo yao kutotimia kama ambavyo imekamatwa awali.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tunafahamu Sheria za Utumishi wa Umma, watumishi hawa tumekuwa tukiwachukulia hatua wale ambao wanahusika na kadhia hii ikiwemo upotevu wa mifugo. Lakini pia kumekuwa na changamoto ya baadhi ya mifugo ambayo huwa inakufa wakati ikiwa inasubiri kupelekwa Mahakamani kwa maana ya kesi inapochukua muda mrefu Mahakamani inapelekea baadhi ya mifugo kupoteza maisha. Lakini kwa upande mwingine ambao amesema Mheshimiwa Mbunge kwamba mifugo mingine inaonekana iko minadani, basi Serikali itaendelea kufuatilia na wale watumishi ambao wanahusika na changamoto hizi tutawachukulia hatua. Na inapothibitika basi wengine tunawasimamisha kazi na hata kufukuzwa kazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge ambao wana changamoto hii, niwaombe pale kuna mfugaji ambaye amekutana na changamoto hii basi watusaidie kutupa hizi taarifa. Lakini pia niwaombe Waheshimiwa tuendelee kuelimisha hawa wafugaji pia, wakifuga kwa kufuata Sheria na taratibu za nchi ninaamini kabisa kadhia hii tutaipunguza kabisa ama kuimaliza. Ahsante. (Makofi)
MHE. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii.
Kwa kuwa hitaji hili la stendi katika Mji wa Geita ni sawasawa na kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Biharamulo cha kupata stendi ya kisasa pale, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa stendi ya kisasa katika Mji wa Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu ya stendi za kisasa, ujenzi wa barabara pamoja na ujenzi wa masoko vyote ni vipaumbele katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kazi ambayo Serikali tumeelekeza, kwanza halmashauri zifanye tathmini ya uwezo wa mapato yao ya ndani na kuweka kipaumbele cha kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo, zikiwemo stendi za kisasa kwa kutumia mapato ya ndani kwa zile halmashauri zenye uwezo wa mapato ya ndani. Zile halmashauri ambazo hazina uwezo wa mapato ya ndani waandae maandiko ya miradi ya kimkakati ya stendi hizo na kuyawasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara na Mipango ili tufanye tathmini na kutafuta fedha za kuwezesha kujenga stendi za kisasa za kimikakati katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ezra Chiwelesa kwamba, wafanye tathmini Biharamulo waone uwezo wao wa mapato ya ndani, lakini kama hautoshi walete mradi wa kimkakati ili fedha itafutwe kwa ajili ya kujenga stendi ya kisasa pale Biharamulo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la madaraja katika Jimbo la Mbinga Vijijini ni sawa na tatizo la baadhi ya vijiji katika jimbo la Biharamulo. Kwa mfano; Kijiji cha Nemba kwenye Kata ya Nemba kuna Kijiji cha Kisenga kwenda Nyamazina, kuna makorongo makubwa sana watu hawawezi kupita na ni sehemu yenye mazao mengi Lusahunga, Midaho kwenda njia panda, Nyakahura kuna Kalukwete kwenda Msali B na Nyevyondo kwenda Ngara. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa madaraja ili wananchi hao waweze kuunganishwa na hatimaye waweze kupata huduma wanazostahili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ambavyo TARURA inategemewa na Waheshimiwa Wabunge katika kutoa huduma kwenye majimbo yetu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, juzi tuliita wakandarasi wote nchini ambao wanahudumu kupitia TARURA, tuliita Mameneja wa Wilaya ya Mikoa ili kuweza kujipanga vyema kufanya kazi kwa weledi katika kuhudumia barabara za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie tunajenga TARURA mpya. Tumejifunza upande wa TANROADS kwa mfano kwenye masuala ya manunuzi, TANROADS huwa wanaanza mipango yao kuanzia Aprili kwa assumption kwamba haijawahi kutoka Wizara ikapata bajeti pungufu kwa mwaka fedha unaofuata pungufu ya asilimia 60 ya bajeti iliyopita. Kutokana na hilo TANROADS huwa wanafanya mipango ya manunuzi kuanzia Aprili ili inapoanza Julai 1 ya mwaka wa fedha wakandarasi wanakuwa wapo tayari kwenda site kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, utaratibu huo tunauleta ndani ya TARURA na tuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kupitia tozo kwa lita shilingi mia moja tayari TARURA kuna zaidi ya bilioni 322 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye barabara kwenye wilaya zetu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TARURA kuweza kupata Mifuko zaidi ya miwili ambayo tulikuwa nayo, Mfuko wa Tozo tumeona umeanza kutuletea fedha na Waheshimiwa Wabunge tutajipanga vizuri kuhakikisha huduma bora ya barabara za wananchi wetu vijijini na kwenye wilaya zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia kwenye mwaka wa fedha tutakaoleta Bajeti Bungeni hapa, Waheshimiwa Wabunge wataona mabadiliko na tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya upembuzi yakinifu mapema badala ya kusubiri kupata fedha ndiyo TARURA ikafanye usanifu, sasa hivi tutakuwa tunafanya mapema, tunakuwa tuna database, fedha inapopatikana tunakwenda kwenye utendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye swali la Mheshimiwa Ndugu yangu Liuka Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, ametaja barabara ambayo inaunganisha mikoa miwili. Dhamira ya TARURA ni kuvipa vipaumbele barabara kama hizo ni kwa sababu ni barabara za kimkakati. Kwa hiyo, tutabainisha hilo kwenye jimbo lake pamoja na majimbo yote ili kuhakikisha tunapotekeleza fedha inavyokwenda basi hiyo barabara inaleta impact za kiuchumi kwa wanachi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Mahitaji ya uwanja katika Wilaya ya Sikonge ni sawa kabisa na mahitaji, ambayo yapo katika Jimbo letu la Biharamulo ikizingatiwa kwamba Hifadhi ya Burigi, Chato ipo Biharamulo na mageti yote yapo Biharamulo; hata hivyo, tumekuwa na uwanja wetu wa muda mrefu pale eneo la Katoke ambao ungesaidia zaidi kukuza utalii hasa kwa wageni ambao watahitaji kutembelea Hifadhi ya Biharamulo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu: Ni lini mpango wa Serikali kusogeza huduma pale katika eneo la Katoke kwa kukarabati ule uwanja ili uweze kutumika na watalii wanaotembelea hifadhi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru sana Mheshimiwa Engineer Ezra kwa kuwa ni mdau mkubwa wa kuhamasisha utalii katika maeneo ya Burigi Chato; na hili ni eneo mojawapo ambalo tumeendelea kulihamasisha; na kwa bahati nzuri sasa hivi tumeshaanza kupata watalii wengi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka kwamba tuna kiwanja kizuri sana ambacho kimejengwa na Serikali maeneo ya Chato. Uwanja huu ni mkubwa ambao ulikuwa na lengo la kuhakikisha wale watalii wote ambao wanataka kuingia lango la Chato na Biharamulo waweze kufika kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliweka mkakati kwamba pamoja na watalii wengi wanaopita maeneo hayo, wengi wao wakiwa wanunuzi wa madini, basi wanapopita kwenda kununua madini na uwanja wa ndege wa Taifa uko pale, basi ni rahisi kupita maeneo yale na pia kuona vivutio vilivyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, namwomba Mheshimiwa Eng. Ezra awe na subira kidogo wakati tunaangalia mafungu mbalimbali ya kuweza kuboresha eneo hili la Biharamulo – Katoke, tuendelee kutumia huu uwanja wa Taifa uliopo ambao ni mzuri zaidi kwa ajili ya kuwezesha watalii waweze kuingia katika malango haya yote mawili. Ahsante. (Makofi)
MHE ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, lakini kwa idhini yako nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Watanzania ambao wamenifanya ni-trend wiki hii na kauli mbiu yangu ya kuchumba chima. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya pili sasa ninaulizia hii pesa ya shilingi milioni 204 ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya suppliers ambao tayari walikwisha- supply vifaa na leo hii ni miezi 18 wanaidai Serikali. Ninaomba kupata kauli thabiti ya Serikali, ni lini pesa hii itapelekwa ili tumalizane na hili tatizo kwa sababu wanadai zaidi ya miezi 18 baadhi ya watu pale?
Pili, kwa kuwa sasa wananchi wangu wa Biharamulo ambao ni wafanyabiashara wamelazimika kuingia kwenye hali y kuikopesha Serikali bila makubaliano ya mikopo.
Je, Serikali ipo tayari kuwalipa na riba hawa watu ambao wame-supply vifaa na leo wanatakiwa walipwe pesa yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa ruhusa yako naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anajitahidi kufuatilia wananchi wa Jimbo hilo kwa maendeleo na maslahi ya Wilaya yake.
Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji madeni Serikali siku zote ipo katika harakati za kuhakikisha kwamba imelipa madeni ya wadai wote. Zipo taratibu ambazo zinafuatwa za kujiridhisha na kuhakiki madeni hayo ili baadae tuweze kulipa kwa utaratibu.
Mheshimiwa Spika, kwa wale ndugu zetu ambao walishatumikia miezi 18 lakini fedha hiyo haijapatikana, tumeshatoa mpaka kufikia Januari mwaka huu tumeshatoa shilingi milioni mia tatu kuja katika Jimbo lako la Halmashauri ya Biharamulo. Katika fedha hiyo mnaweza mkatenga fedha maalum kupunguza taratibu deni la wananchi ambao walitumikia Jimbo hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Biharamulo, tuna ujenzi wa hospitali ya Wilaya pale, lakini ujenzi ule umekwama kwa muda mrefu kwa sababu ya pesa iliyorudishwa Shilingi milioni 204. Hii fedha nimeisema mbele ya Rais akiwa Biharamulo tarehe 8 Juni, na TAMISEMI wakaahidi kwamba wanakwenda kuifuatilia: Ni lini sasa fedha hii italetwa ili tuweze kukamilisha kwa sababu kila kitu kiko tayari pale isipokuwa fedha hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amefuatilia sana suala ya fedha hizi na ameshauliza hapa. Tulikubaliana na Hazina kwa maana ya Wizara ya Fedha, fedha zile ziweze kurejeshwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafuatilia sisi na Wizara ya Fedha, tuhakikishe fedha zinakwenda kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nikijaribu kupitia huku kwenye benki hii, ni takribani miaka 10 sasa tangu benki hii ianzishwe. Ilianzishwa mwezi Septemba, 2012, lakini tunaona ina matawi matano tu. Matawi haya matano yako katika majiji haya makubwa, lakini tunajua wakulima wako kwenye vijiji vyetu na kata zetu ambako tunatoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, kwa sababu Serikali imesema itapanuka lakini based on kupata pesa ya mtaji mkubwa zaidi: Ni nini mpango wa Serikali kuiongezea pesa benki hii hata kupitia hazina ili wakulima wetu ambao wametutuma sisi hapa waweze kunufaika na benki hii ambayo ina miaka zaidi ya 10 lakini haijawafikia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: tarehe 9/6/2022 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa katika ziara ya Mkoa wa Kagera kwenye uwanja wa Kaitaba alitoa maelekezo maalum kwa Serikali ya Mkoa wa Kagera na akai-cite kwamba tumekuwa na shida ya mafuta ya kula katika nchi hii na mpango uliopo ni kuutumia Mkoa wa Kagera ambao una maeneo makubwa ambayo hayatumiki kwa ajili ya kufanya kilimo cha michikichi na kilimo cha alizeti; na ameelekeza tutenge hekta takribani 70,000 mpaka 100,000 kwa ajili ya kutatua tatizo hili: -
Sasa je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kuielekeza benki hii pamoja na kwamba mtaji wao bado ni mdogo, ielekee Kagera ikaungane na Serikali ya Mkoa ili waone wanasaidiaje kutatua tatizo hili la mafuta ya kula? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Eng. Ezra kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza tunalipokea kama ushauri na tunaenda kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili pia tunaenda kulifanyia tathmini tuone kama upo umuhimu wa kuelekea kwa wakati huu; na kwa kuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kunyanyua uchumi katika Mkoa wa Kagera, basi nalo hili tumelipokea na tunalifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, je lini Serikali itajenga Vituo Vya Afya katika Kata za Nyamigogo, Kabindi, Kaniha, na Nyatakala Wilayani Biharamulo? Kwa sababu tuna uhitaji mkubwa wa Vituo Vya Afya katika maeneo hayo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Eng. Ezra Chiwelesa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge na uhitaji wa vituo vya afya tutakwenda kufanya tathmini na kuona uwezekano wa mapato ya ndani kujenga vituo hivyo, lakini pia kutafuta fedha Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga vituo hivyo kama vitakidhi vigezo vile vya kujenga vituo vya afya katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na hasa fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuhudumia vituo vya afya vilivyobaki. Kwa Kituo cha Nemba nashukuru kwa ajili ya vifaa vilivyopokelewa. Hata hivyo, nina swali moja la nyongeza; Kituo cha Afya cha Rukaragata ndicho kinachohudumia Wilaya ya Biharamulo Mjini, kwa sababu hatuna hospitali ya wilaya, kwa sababu hospitali iliyojengwa iko Kata jirani ya Lubungo. Sasa swali, kwa sababu tuna akinamama ambao wanajifungua pale na wanapata shida na hamna jengo la upasuaji na wametuambia tutapata pesa katika mwaka 2023/2024, ni mbali sana kwa sababu akinamama wanaendelea kuzaa na wanahitaji huduma. Sasa kwa sababu Waziri wa Fedha yuko hapa na Waziri ametuambia twende huko mbele, naamini Serikali inaweza ikapata fedha katika vyanzo vingine tukapata hii fedha katika mwaka huu wa fedha. Je, Waziri haoni haja ya kumpa nafasi Waziri wa Fedha aweze kutusaidia kwenye hili ili tuweze kupata fedha hii na akinamama wa Biharamulo waweze kunufaika na hili? Nashukuru.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo kwa swali lake na kwa kweli amekuwa akifuatilia sana wizarani fedha ya hospitali ya wilaya ambayo ni takribani milioni 204, pamoja na hili suala ambalo anasema hospitali yake ya wilaya, I mean kituo hiki cha mjini kinafanyika kama hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe na nimwombe Mheshimiwa Mbunge aridhie tulichukue jambo hili Wizara ya Fedha ili tuwasiliane na wenzetu wa TAMISEMI, pamoja na yeye na Mkurugenzi wake, tuweze kuona namna ya kuliharakisha kwa ajili ya maisha ya Wanabiharamulo kama ambavyo amesema. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi pia.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Ngara ni sawa na tatizo lililoko Biharamulo maana tumeanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya kwa muda mrefu sana, na kuna pesa milioni 204 ilirudishwa, nimeshaiongelea humu zaidi ya mara tano, lakini pia kuna pesa ya bajeti ya mwaka huu milioni 750. Sasa, kwa sababu hospitali hii tumeanza kuitumia tarehe 13 Januari, ila majengo mengine hayajamalizika.
Ni lini mtapeleka pesa hizi ili wananchi wa Biharamulo waweze kutumia Hospitali yao kwa uhuru ili wapate huduma wanayostahili kupata? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupeleka fedha Biharamilo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri kwa awamu, lakini nafahamu kuna fedha ambazo Mheshimiwa Chiwelesa amekuwa akifuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatafutwa, zinapelekwa Biharamulo ili hospitali ile ikamilike ianze kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru Serikali kwa mbolea ya ruzuku lakini kwa kuwa mbolea hii tangu tumepitisha bajeti hapa, maeneo kama ya Kagera ambao tunakuwa na msimu wa kilimo umeshapita na mbolea haikupatikana kwa wakati kwa sababu mawakala hawapo kabisa.
Je, ni nini kauli ya Serikali kwa wananchi hususan wa Wilaya ya Bihalamuro ambao wamekosa kabisa mbolea hii ya ruzuku ili kipindi cha msimu unaofuata waweze kuwa na matumaini ya kupata mbolea hii kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulipata changamoto ya mfumo wa usambazaji, ambao hivi sasa tumeendela kuurekebisha na hivi sasa tumeruhusu pia usajili wa vyama vya ushirika, kuwa kama sehemu ya wasambazaji wa mbolea vilevile na vyama vya wakulima vilivyosajiliwa na pia tutatumia baadhi ya maghala yaliyokuwa katika mradi wa MIVARF kama sehemu ya usambazaji wa mbolea hizi. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi kinachokuja changamoto hii haitajirudia tena, tutahakikisha kwamba mbolea inawafikia wakulima kwa wakati lakini katika maeneo yao walipo pia.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo hili ambalo liko Nkasi na sawa na tatizo ambalo liko Biharamulo hasa tukitegemea kwamba tuna mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyaleta katika Mji wa Biharamulo.
Ni nini sasa kauli ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mradi huo katika mwaka huu wa fedha? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Engineer Ezra, kwa kazi kazi kubwa nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Biharamulo.
Mheshimiwa Spika, namna ya kutatua tatizo la maji Biharamulo ni kuhakikisha tunaanzisha mradi mkubwa wa kutumia Ziwa Victoria na tumeanza jitihada katika maeneo mbalimbali. Nimwombe awe mvumilivu, nadhani kipindi ambacho tutaisoma bajeti yetu tarehe 12 mambo yatakuwa bambam, tuko pamoja. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, labda sasa niseme jambo moja, leo ni mara yangu ya tatu nauliza swali hili hili. Mwaka jana kwenye Bunge la bajeti nilijibiwa hivi hivi. Mwaka huu pia Wizara ya Fedha imenijibu kwamba inashughulikia. Ila nimekuwa disappointed na majibu ya Serikali kwa sababu wanasema Wilaya ya Biharamuo haikufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwennyekiti, nina barua hapa ya tarehe 9 Juni, 2020, copy ninayo na ninaamini kila sehemu ipo. Nina barua hapa ya tarehe 20 Agosti, 2020 copy ninayo na barua ipo. Sasa kinachoshangaza ni kwamba, majibu niliyopewa na Wizara hii hii mwaka jana ni tofauti na majibu ninayopewa leo. Nilikuwa naona kwamba tumeshaenda mbele, lakini majibu nayojibiwa leo wananirudisha nyuma tena. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza, naomba Serikali inipe majibu hapa wananchi wa Biharamulo wakiwa wamesubiria hospitali kwa muda mrefu.
Ni lini fedha hii inapelekwa? Yaani lini siyo nyuma wala mbele lini, date, kabla ya mwisho wa bajeti hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili tuna pesa milioni 376 kwa ajili ya vifaa tiba ya hospitali hii. Sasa, leo ni mwezi wa tano, mwaka wa fedha unaisha. Kwa hiyo tusiletewe hii fedha mwezi wa sita katikati tukaambiwa inatakiwa itumike kwa haraka. Pamoja na hii nijue fedha ya vifaa tiba inakuja lini, na utaratibu wake ukoje kama kama inachelewa tunairudisha au tunabaki nayo? Majibu mawili tu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanya kazi kwa kufuata kumbukumbu ambazo zinaoneshwa katika mafaili yetu lakini katika document mbalimbali za Serikali. Na sisi tumefuatilia Wizara ya Fedha na Mipango; pamoja na kwamba Mheshimiwa Mbunge una hizo barua inawezekana ziliandikwa lakini hatuzioni Wizara ya Fedha na Mipango, na suala lilikuwa sio kuandika barua ilikuwa barua zifikishwe Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa hiyo, kama waliandika kwa ku-back date, ili kuweza kutengeneza mazingira hayo sisi hatujazipata hizo, na tungezipata nikuhakikishie Serikali Sikivu ingezifanyia kazi. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunachosema hapa ni sahihi na tunaendelea kusema vitu sahihi katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na lini fedha hizi zinapelekwa katika mwaka huu wa fedha tayari mmepata milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Biharamulo. Mwaka ujao wa fedha mmepata milioni 750 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Kwa hiyo, hapa ni wazi kwamba Serikali inaendelea kupeleka fedha na hospitali inaendelea kujengwa. Hitaji la wananchi ni hospitali na Serikali ina commitment kubwa kuhakikisha hospitali inaendelea kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na milioni 376 za vifaa tiba utaratibu upo wazi tunatepeleka fedha Bohari Kuu ya Madawa (MSD) na itanunua vifaa vile ambavyo imeorodheshwa na halmashauri vitaletwa kwa ajili ya huduma hizo. Nikuhakikishie tu, kwamba MSD inakwenda vizuri sana, vifaa vitakuja huduma zitaendelea pale Biharamulo.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba nifanye masahihisho kidogo, kituo kinaitwa
Rukalagata, Kata ya Biharamulo Mjini, kingine ni Kalenge Kata ya Kalenge na kingine ni Nyabusozi Kata ya Nyabusozi.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba 2022 nilisimama hapa ndani nikiongelea Kituo cha Rukalagata kwamba hakina jengo la upasuaji na bahati nzuri nikajibiwa na Waziri wa Fedha kwamba nilete maombi maalum na wao watanitengea pesa kwa sababu hospitali ya Biharamulo Mjini imejengwa lakini iko nje ya Mji kwa hiyo watu wa Biharamulo Mjini hawapati huduma. Barua yetu ilitoka Tarehe 14 siku tatu zilizofuata…
SPIKA: Swali lako Mheshimiwa Ezra ni lipi?
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Swali la kwanza je, hii barua ilishapokelewa na imefika kwa Waziri wa Fedha? Je, status ikoje, kama haijafika naomba niikabidhi hii barua.
Pili, napenda nishukuru kwa sababu nimeambiwa vituo viwili vitafanyiwa kazi. Ni hayo tu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimepokea marekebisho, pili kwa kuwa barua iliwasilishwa na Halmashauri ya Biharamulo kwenda Wizara ya Fedha, Ofisi ya Rais -TAMISEMI tutafanya mawasiliano ya karibu na Wizara ya Fedha baada ya maswali hapa na tuone kama barua imeshafika na tuone hatua za utekelezaji ili ahadi ya Serikali ya kuleta fedha hiyo iweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, pili, hivi vituo vya afya viwili ambavyo vimetengewa shilingi milioni 500 ni vile kati ya vituo vya afya vitatu ambavyo Halmashauri mtaona kipaumbele ni vipi vianze ili tuanze kukarabati na kuanza kutoa huduma hizo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini barabara ya Katoke – Nyamirembe itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, kwani ipo kwenye bajeti ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhandisi Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja tumeitengea bajeti kwa ajili ya kuanza maandalizi kuijenga kwa kiwango cha lami na tuna hakika kwamba hata katika bajeti itakayokuja tumependekeza hiyo barabara ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na umuhimu wa Serikali kukuza utalii hususani katika mbuga yetu ya Burigi – Biharamulo, naomba kujua ni lini sasa uwanja wa ndege wa Biharamulo sasa utakarabatiwa ili uweze kuwa kiungo muhimu cha kuleta watalii katika eneo letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiwelesa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Kiwanja cha Ndege cha Biharamulo ni miongoni mwa viwanja 11 ambavyo tumevitengea fedha na kwa kiwanja cha Biharamulo pekee tumetenga takribani Milioni 400 kwa jili ya ukarabati kiwanja hiki cha Biharamulo. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, na especially commitment ya Serikali kwamba Mradi huu wa Maji ya Ziwa Victoria unaanza katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024. Lakini kama ulivyosema, utekelezaji wa miradi ya maji kwa Biharamulo uko asilimia 65 sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba, umesema mmetuwekea 2.8 kilometa mtandao. Sasa kwa sababu maji yanakuja, naomba ufanye commitment, kwa sababu sasa bahati nzuri leo najibiwa na Waziri mwenyewe, angalau uniongezee kilometa tatu nyingine waweze kusambaza mabomba zaidi pale mjini ili maji yatakapofika yawafikie wananchi wengi zaidi. Swali la kwanza hilo, naomba tu commitment.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mradi huu wa Maji wa Ziwa Victoria tulikuwa tumeahidiwa pia kutoa maji Ziwa Victoria tupite katika Kata za Nyamigogo, yale Kabindi, Nyabusozi, Nemba yaende Nyantakara yafike mpaka Nyakanazi katika kata ya Lusahunga. Sasa ni lini mradi huu wa kutoa maji za Ziwa Victoria katika line hii ya kuyapeleka mpaka Nyakanazi utatekelezwa na Serikali kwa ajili ya wakazi wa Buharamulo na hususan Nyakanazi, center kubwa inayokuwa pale?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na kipenzi cha Wanabiharamulo, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Nimhakikishie kwamba Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha Wanabiharamulo wanapata maji. Kwa hiyo, juu ya ombi lake la kuongeza mtandao, tupo tayari kutoa fedha kwa ajili ya uongezaji wa mtandao wananchi wake waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni juu ya ujenzi huu wa mradi mkubwa. Ujenzi wa mradi huu chanzo tunachukua pale eneo la Chato na ni miongoni mwa miradi ya miji 28 na mkandarasi amekwishapatikana, advance payment imekwisha tolewa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba safari moja huanzisha mwingine, uanzaji wa mradi huu ndiyo tunakwenda kukamilisha ujenzi wa mradi wa Biharamulo, ahsante sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Biharamulo kijiografia ni eneo kubwa sana na tumekuwa katika scarcity hiyo ya watendaji kwa muda mrefu sana. Sasa kwa sababu umesema tayari maombi yetu mnayo.
Swali la kwanza; je, ni nili tutapatiwa kibali tuweze kuajiri watendaji ku-cover zile nafasi ambazo zimebaki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kama unavyojua Wilaya ya Biharamulo sasa population yetu ni watu 457,114. Jimbo hili ndilo linaloongoza kwa idadi kubwa ya watu kwa Mkoa wa Kagera, lakini kijiografia pia ni Jimbo kubwa zaidi lina vijiji 79, kata 17 lakini zilizotawanyika sana.
Je, huoni kwamba iko haja ya Serikali kutupatia usafiri kwa ajili ya watendaji wa vijiji na kata ili huduma za wananchi ziweze kufika kwa haraka zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la kwanza la Mheshimiwa Ezra Chiwelesa, la lini kibali hiki cha ajira. Nikirejea majibu yangu ya msingi, tutatoa vibali hivi kadri ya bajeti itakavyoruhusu, lakini tayari Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imeshapata watendaji wa vijiji 20 katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023. Kwa hiyo, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge Serikali inatambua upungufu huu na inaendelea kulifanyia kazi na muda si mrefu mtaona watendaji hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali la pili la usafiri. Wote humu ndani ni mashahidi katika awamu hii ya sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kwa mara ya kwanza kuanza kutoa pikipiki kwa watendaji wa kata zetu zote nchini. Tayari walikuja Dodoma hapa na wakakabidhiwa pikipiki hizo. Na zile kata ambazo bado zimesalia kuna baadhi ya Wakurugenzi ambao wameanza kununua kwa mapato yao ya ndani na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wetu. Kwa hiyo niwatake tena Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatenga fedha ya kununua usafiri kwa ajili ya watendaji wa kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na inaporuhusu bajeti basi hadi kwa watendaji wa vijiji, lakini mpaka sasa Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kupunguza upungufu huu wa usafiri.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Geita - Nyakanazi na Nyakanazi - Rusumo kuna baadhi ya wananchi wa Biharamulo ambao wanapitiwa na mradi ule katika Kata nne za Rusahunga, Kaninha na Nyakahula nao pia bado hawajalipwa pesa zao za fidia. Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha malipo hayo kwa baadhi ya watu ambao walikuwa hajalipwa pesa zao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fidia ya Geita - Nyakanazi tayari Serikali ilishatenga fedha bilioni sita na tayari fedha bilioni 5.9 zilishalipwa kwa ajili ya wananchi na wananchi waliobakia ni wananchi 49 tu, tunaamini taratibu zikikamilika na wao wataweza kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Nyakanazi -Rusumo pia Serikali ilishatenga fedha bilioni 3.8 na tayari bilioni tatu ilishalipwa, wananchi waliobakia ni 39 tu. Nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kwa sababu fidia hii imekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, tutafuatilia kuhakikisha kwamba kidogo kilichobakia kinaweza kukamilika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHILEWESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Hospitali ya Wilaya Biharamulo tulianza kutoa huduma tarehe 13 Januari, tukapata usajili tarehe 20 Februari. Lakini mpaka sasa tangu tume-apply maombi kwa ajili ya kutoa Huduma za NHIF kwenye hospitali yetu hatujapata kibali wala hatujapata majibu kutoka NHIF. Ni nini kauli ya Serikali juu ya wakazi wa Biharamulo wanaotumia hospitali ile kwa sababu wamekosa haki yao ili hali wanazo kadi na wana kila kitu kinachohusu NHIF. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimeanza kumjua Mheshimiwa Mbunge kwa yeye kupigania hii hospitali yake. Kwa hiyo, kwa kweli sisi kama Serikali hatutakubali kazi uliyofanya kwa nguvu kubwa kwa miaka miwili wananchi wasiweze kupata huduma. Kwa hiyo, namwagiza Mkurugenzi wa NHIF Taifa nampa siku tatu Hospitali yako ya Biharamulo ipate Mfuko wa NHIF.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mabenki mengi hapa nchini bado yana uhaba wa fedha tofauti na Mheshimiwa Waziri ulivyosema. Hali ambayo imepelekea sasa hivi wafanyabiashara wengi wa Soko la Kariakoo, hawa wadogo wadogo na wengine wakubwa wanapata shida ya kupata pesa za kigeni, kiasi kwamba CRDB in a day sasa hivi huwezi kupata zaidi ya dola 1,000 na mabenki mengine kama NMB na NBC huwezi kutoa zaidi ya dola 500 kwa siku. Kitu ambacho kama mtu anahitaji kutuma pesa nyingi nje ina mchukua muda mrefu sana kuzunguka kwenye benki mbalimbali kukusanya hela na haruhusiwi ku-change hizo hela;
Je, sasa ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha tunawapeleka wafanyabiashara katika dreams zao za kupata fedha za kigeni ili waweze kufanya shughuli zao za biashara vizuri bila kukwama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kihalisia Nchi zetu zimekuwa zinafanya trading kubwa sana na Nchi za Asia ikiwemo China, India na Uturuki pia, lakini wafanyabiashara wa Tanzania wanalazimika kubadilisha pesa zao kuwa kwenye shilingi kupeleka katika dola na wanapofika kwenye yale Mataifa wana-change tena kutoka kwenye dola kupeleka kwenye pesa za wale mataifa;
Je, sasa wanakuwa wanapata hasara ya exchange rate hapo, hamuoni kwamba iko hajia ya Serikali ya Tanzania kuongea na mataifa haya makubwa ambayo tunafanya nayo biashara na tunatembelea kwa kiasi kikubwa na uanguko wa dola hasa zinaposhindwa kupatikana, wakaturuhusu tukaanza kufanya exchange rate ya pesa za nchi zao; kwa mfano anaenda China akaondoka na Yuan akiwa hapa hapa akifika kule asipate usumbufu wa kubadilisha kwenye dola halafu watoke kwenye dola warudi kwenye pesa ya Mataifa yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Chiwelesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, tayari Serikali imechukua hatua kadhaa ili kupunguza au kuondoa changamoto hiyo. Kwa hiyo naomba nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, hivi karibuni changamoto hiyo imeondoka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, shauri lako Mheshimiwa Engineer tumelichukua na tunalifanyia kazi. Ninachotaka kukuambia, hivi karibuni tumeanza mazungumzo na India katika shauri ambalo umelitoa na Nchi nyingine tutaenda.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kulikuwa na ujenzi wa vituo vikubwa vitatu vya forodha, kipindi inajengwa Vigaza kulikuwa na cha Manyoni halikadharika kulikuwa na Kituo cha Nyakanazi Biharamulo ambacho kilikuwa kimeshaanza kujengwa na tayari majengo yako pale, lakini kimetelekezwa kile kituo na kiko chini ya Wizara ya Fedha.
Sasa nilitaka kujua ni lini ujenzi wa Kituo cha forodha Nyakanazi Biharamulo ambacho kilishaanza ujenzi utafufuliwa ili uweze kukamilika kwa manufaa ya Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ezra kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kilikuwa na mgogoro kati ya Mkandarasi na upande mwingine lakini tumechukua hatua na ninacho mhakikishia Mheshimiwa Mbunge, hivi karibuni tutapata mwafaka wa jambo hilo na kituo hicho kitaendelea na ujenzi kama kilivyopangwa.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, tuna barabara inayounganisha Mikoa ya Kagera na Geita kutokea Katoke – Buharamulo kwenda kwenye Bandari ya Nyamirembe, na tuliahidiwa kwamba ingeanza kufanyiwa ujenzi mwaka huu wa fedha. Sasa tunaelekea ni mwezi wa tano sasa hivi imebaki miezi miwili hatujaona mkandarasi site.
Ni lini sasa barabara hii itaanziwa ujenzi ili wananchi wale waweze kuanza kuitumia ikiwa katika kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyamirembe – Katoke inatoka kwenye Bandari ya Nyamirembe ambayo tayari imeshakamilishwa na lengo ni kuunganisha hii bandari na Biharamulo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ipo kwenye mpango na imeshaombewa kibali ili iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tatizo la usafiri kwa Kituo cha Polisi cha Mavota ambacho kinahusika na ulinzi wa mgodi wa Biharamulo Gold Mine ni kubwa. Tuna kituo pale, lakini hakuna usafiri hata pikipiki.
Sasa ni lini labda Serikali itatusaidia kupata hata usafiri wa pikipiki mbili/tatu ili tuweze kuimarisha ulinzi juu ya wawekezaji ambao wamewekeza katika mgodi ule wa Mavota?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vituo vingi vya polisi havina usafiri wa uhakika, hasa vituo vilivvyo kwenye ngazi ya kata na kwenye maeneo mahususi kama haya ya migodi. Pengine nitumie nafasi hii kueleza kwamba katika mwaka wa fedha huu na ujao tuna magari zaidi ya 300 ambayo yatapatikana na sehemu ya magari hayo ni ku-support usafiri kwenye vituo mbalimbali vya polisi. Sasa pengine niwasiliane na Mbunge kuona uhitaji wa usafiri wa pikipiki katika kituo hiki ili tushirikiane kuzungumza na wadau waweze kutoa fedha kuwezesha ikiwa mpango wa Serikali wa magari hayo utachelewa kufika. Nashukuru.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wakati wa Bunge la Bajeti niliahidiwa shilingi milioni 500 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya Kalenge na Nyubusozi wilayani Biharamulo. Ni lini pesa hiyo itatumwa ili huduma hiyo iweze kufanyika kwa ajili ya wananchi wa Biharamulo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Vituo hivi vya afya ambavyo viliahidiwa katika Bunge la Bajeti, ni sehemu ya kipaumble cha Serikali katika kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha na kuzipeleka ili ujenzi uweze kufanyika. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mbunge uwe na Subira kidogo wakati Serikali inatafuta fedha na mara fedha zikipatikana kwa awamu tutahakikisha kwamba tunaanza ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mwaka 2022 niliuliza swali hapa ndani ya Bunge nikajulishwa kwamba nilete andiko kwa ajili ya ujenzi wa Stendi ya Wilaya ya Biharamulo. Pia kwenye miradi ya kimkakati wa Mkoa wa Kagera kwenye bajeti ya mwaka huu 2023 tuliwasilisha pia. Sasa, naomba kujua ni lini ujenzi wa Stendi ya Wilaya ya Biharamulo utaanza ili wananchi wa Biharamulo waweze kupata huduma hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri ya Biharamulo kwa kuwasilisha andiko la maombi ya Mradi wa Ujenzi wa Stendi ya Halmashauri na nimwambie tu kwamba baada ya mawasilisho hayo Serikali inaendelea kupitia maandiko yale kufanya tathmini ya vigezo. Pia sambamba na hilo, kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, mara fedha zikishapatikana na baada ya kupitia andiko hilo na kujiridhisha na vigezo, fedha itatafutwa kwa ajili ya kujenga stendi hiyo ya Biharamulo, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa condition hii ya kupita JKT na Serikali imekiri kwamba uwezo wa kuwachukua watu wote haupo lakini recently tumekuwa tunaona ajira nyingi zinazotangazwa zimeweka kigezo cha kwamba kijana awe amepita JKT. Kwa hiyo vijana wengi wanatamani waingie kwenye hizi ajira lakini kigezo cha kupitia JKT kinawanyima fursa na hawatendewi haki;
Je, hatuoni sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kuondoa kigezo cha kupita JKT mpaka pale itakapokuwa tayari kuwahudumia watu wote ili ushindani uweze kuwa sawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba lalamiko hili limeshasikika, na kama tulifufatilia Taarifa ya Tume ya Jinai ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na ni pendekezo linalofanyiwa kazi na Serikali. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo Serikali ilitenga shilingi bilioni nane kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya takribani 20 ambavyo havitoi huduma kama vituo vya afya kamili na miongoni mwa vituo hivyo Wilaya ya Biharamulo tulitengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya kukarabati Vituo vya Afya vya Nyabusozi na Kalenge, lakini mpaka sasa pesa hiyo haijatoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali kwa sababu mwaka wa fedha unaisha na sijaona pesa hiyo ikiwa imepelekwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu awali, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaboresha huduma za afya msingi. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba Serikali ipo kazini na ndiyo maana kwanza ilianza kutenga bajeti. Kwa hiyo mimi na yeye tutakaa na tutazungumza tuone mkwamo upo sehemu gani.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali italeta pesa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukamilishaji wa Vituo vya Ndabusozi na Kalenge kama ilivyoahidiwa katika bajeti ya mwaka huu tunaoendelea nao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, vipo vituo vya afya ambavyo vilipokea shilingi milioni 250 na ujenzi wake haujakamilika kwa sababu tunahitaji shilingi milioni 250 nyingine. Kwa hiyo, vituo vyote, vikiwemo hivyo vya ndani ya Jimbo la Biharamulo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Chiwelesa kwamba Serikali ina mpango mkakati wa kupeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo vya afya, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 20 Desemba, 2016, Serikali ilisaini Mkataba na Kampuni ya Motor Van kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Nyakanazi kwa thamani ya shilingi bilioni 25. Ujenzi ulianza lakini baadaye ukasimama na Kituo hicho kimetelekezwa na miundombinu ile iliyokuwa imefanyika mwanzo yote inaharibika sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kauli ya Serikali, ni lini umaliziaji wa Kituo kile utafanyika ili pesa walipa kodi ambayo ilikuwa imewekezwa pale iweze kukamilika na hatimaye thamani ile ambayo tulitarajia kuipata watu wa Biharamulo tuipate kupitia kituo kile? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni la kiutawala na ni utekelezaji wa mradi ambao unafuata mtiririko wa fedha. Nimelipokea tutaongea na wenzetu wa Mamlaka ya Mapato pamoja na Wizara ya Fedha ili kuweza kuhakikisha kwamba fedha zinafuata mtiririko ili kuweza kukamilisha mradi uliotajwa.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na taratibu zile kwa mfano nafasi za majeshi na vitu vingine ambavyo watoto wanapatikana kwenye maeneo yetu ya majimbo. Baada ya usaili kutoka kwenye wilaya, anafika mkoani mkoa wanawarudisha, wanaambiwa huyu ana kovu, sijui ana nini, kumekuwa na vigezo vingi sana watu wa mkoa wanadhulumu watu wa wilaya.
Mheshimiwa Spika, sasa tulikuwa tunaomba nafasi zipelekwe wilayani hasa zile ambazo hazihitaji vigezo zaidi ya Form Four. Wakishatoka wilayani waende moja kwa moja kwenye training kwa sababu wanapofika mkoani, watu wa mkoani wanakuwa na nafasi za kuchomeka watu wao na watu wetu waliotoka kwenye wilaya wanaachwa. Tulikuwa tunaomba hilo lizingatiwe, ni hilo tu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana, nadhani huo ulikuwa ni ushauri, kwa hiyo, utachukuliwa halafu wakaupime kwa sababu hapo mwishoni umemaliza vizuri, lakini vigezo lazima vizingatiwe. Tukisema kutakuwa hakuna vigezo kwa sababu tu watu wametoka mahali, itakuwa changamoto, ila mwishoni umemaliza kwamba unatoa ushauri wa namna ambavyo wafanye hili zoezi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri naamini umeupokea huo ushauri.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Ahsante sana, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nishukuru kwa ajili ya ujenzi wa hizi shule ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja na bado nyingine za sekondari zimepatikana pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukiangalia rekodi ya Sensa ya Mwaka 2022 Jimbo la Biharamulo ndiyo linayoongoza kwa idadi ya watu kwa Mkoa wa Kagera that means tuna watoto wengi sana ambao bado wanahitaji huduma. Kwa hiyo, ni nini mpango wa Serikali kwenye kutuletea vyumba vya madarasa vingine kwa ajili ya maeneo mengine ambayo bado yana watoto wengi wasiyoipata hiyo huduma kwa Shule za Msingi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia watoto hawa wanapofaulu kwenda Sekondari kwa sababu ni wengi bado wana uhaba wa vyumba vya madarasa na pia wanapoelekea Sekondari. Kwa sababu ni Wizara hii hii na ni jambo hili la vyumba vya madarasa naomba kusikia pia kauli ya Serikali juu ya watoto wanaofaulu kwenda Sekondari Wilaya ya Biharamulo waweze kuongezewa vyumba vya madarasa ili wapate accommodation nzuri wanapoenda sekondari. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ya uwakilishi anayoifanya. Lakini kuhusiana na swali lake la kwanza napenda nianze kukumbushia msingi mzima wa ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi ni kuhakikisha kwamba Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na fees code centralization, yaani zinaweza zenyewe kujitegemea kwa maana kutafuta mapato na kuweza kuendeleza miundombinu ya msingi. Kwa sababu jukumu la msingi la kutengeneza miundombinu mbalimbali liko kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lakini tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Miradi ya BOOST kwa ajili ya Shule za Misingi na Mradi SEQUIP ameleta fedha nyingi sana kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na ndiyo maana kila mwaka Serikali imekuwa ikituma fedha katika huu Mradi wa BOOST kwa ajili ya kwenda kuongeza madarasa katika shule zetu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika muktadha wa swali lake yeye kwa maana ya Shule za Sekondari. Sasa kwenye swali lake la pili katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 kupitia Mradi wa SEQUIP Serikali imeleta jumla ya shilingi milioni 584.2 kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Lusahunga, lakini pia imeleta jumla ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya nyumba za walimu. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikileta fedha kila mwaka wa fedha kuhakikisha kwamba inaongeza nguvu pale ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa tayari zimeanza na zenyewe kuunga mkono au kujenga miundombinu hii muhimu katika Sekta ya Elimu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kuhakikisha inaboresha miundombinu ya Sekta ya Eilimu na pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Naibu Waziri amekiri kwamba, ili uhamisho uweze kufanyika lazima kuwe na programu ya kubadilishana, lakini recently katika Wilaya ya Biharamulo tumekuwa tunapokea barua za uhamisho wa watumishi kutoka TAMISEMI bila hata halmashauri kuhusika na chochote.
SPIKA: Mheshimiwa swali, swali, swali.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, sasa uko tayari kutoa kauli ya kusimamisha uhamisho wowote ambao umetokea TAMISEMI moja kwa moja kuja Biharamulo bila programu ya kubadilishana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mimi na yeye tutakaa na tutafanya ufatiliaji kuona tatizo alilolisema katika jimbo lake ili tuweze kuchukua hatua stahiki, lakini msimamo wa Serikali ndiyo huo kwamba, uhamisho unapofanyika, mwalimu anapotoka katika kituo kimoja lazima awe amepatikana mwalimu mwingine wa kuja kuziba pengo lake. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nipongeze kwa hatua hizo kubwa ambazo zimefanyika za uwekezaji huo mkubwa wa Kituo cha Nyakanazi na hatimaye kuweza kutuondolea tatizo la kukatika katika kwa umeme, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Nyakanazi tulikuwa tunapata mradi wa umeme unaotoka Biharamulo kwenda Mkoa wa Kigoma au tunauita Kigoma – Nyakanazi ambao ulikuwa na vijiji 32, vijiji saba vikiwa Wilaya ya Biharamulo katika Kata za Kalenge na Nyanza na vijiji 25 Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa katika Wilaya ya Biharamulo, hivyo vijiji saba vya Kata za Kalenge na Nyanza mpaka sasa baada ya kumalizika mradi ule ni wateja wangapi wameunganishiwa umeme kutokana na vijiji hivi saba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mradi huu mkubwa wa kutoka Geita kuja Nyakanazi na kutoka Rusumo kuja Nyakanazi ulipitia maeneo ya watu na walistahili fidia. Nadhani mwaka jana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati akiwa Biharamulo tuliomba wale watu ambao hawajalipwa pesa zao waweze kupatiwa pesa zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kusikia kauli ya Serikali, mmefikia wapi na maandalizi ya kuwalipa pesa wale waliokuwa wamepitiwa na ule mradi ili sasa kwa sababu umeme unawaka na walipisha maeneo yao wao waweze kupata haki yao ya kulipwa fidia ambayo imechukua muda mrefu sana, wale waliokuwa wamebaki wachache kama 32? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, Engineer Ezra Chiwelesa kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatetea wananchi wa Biharamulo na ninaomba kujibu maswali yake kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji saba vilivyopo katika Kata za Kalenge pamoja na Nyanza mpaka sasa tumeshaunganisha wateja 615 na kwa sababu kazi hii ni endelevu, tunaendelea hivyo kadiri wananchi wanavyofanya wiring tunaendelea kuwaunganisha na umeme. kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kazi hii inafanyika vizuri sana na REA kwa kushirikiana na TANESCO.
Kuhusu swali la pili la fidia, ipo katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni Geita – Nyakanazi. Kwa Geita – Nyakanazi malipo ya Serikali yaani statutory compensation tayari imeshafanyika kwa wananchi wote, ambacho kimebaki ni top up compensation ambapo mkandarasi anatakiwa kuongeza ili waweze kulipwa kwa viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaambiwa mshauri elekezi anatarajiwa kuja hivi karibuni ili kuweza kufanya survey pamoja na masuala mengine ya kiutendaji ili wananchi hawa waweze kumaliziwa ile top up compensation ya mfadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipande cha Rusumo – Nyakanazi kulikuwa na wananchi 1,024 na wananchi takribani 986 wameshalipwa fedha shilingi bilioni 3.7 na wannchi waliobaki ni 38 tu ambapo wanadai shilingi milioni 81.02. Wananchi hawa hawajalipwa kwa sababu ya changamoto za mirathi na migogoro mingine, lakini fedha zao zipo na kadiri ambavyo wataweza kukamilisha taarifa zao na kuweza kumaliza migogoro na kukamilisha taratibu za mirathi watapatiwa fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, fedha za wananchi hawa zipo, taratibu zikikamilika hawa 38 waliobaki katika kipande cha Rusumo – Nyakanazi na wenyewe watalipwa fedha zao, ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini labda nitoe maelezo kidogo kabla ya kuuliza maswali. Majibu yanasema kila Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kuomba, lakini ninachojua kwenye hili, Jeshi la Uhifadhi si kila Mtanzania mwenye sifa, ila ni aliyeandaliwa na familia yake mwenyewe kwa sababu, they don’t train them, wazazi wanawaandaa halafu baada ya hapo wanabaki ku-compete kwa ajira. Kwa hiyo, si kila Mtanzania ni baadhi ya watu ambao wameandaliwa na wazazi wao.
Mheshimiwa Spika, sasa maswali yangu ni mawili. Swali la kwanza; ndani ya Bunge hili tuliondoa kigezo cha JKT, kwa ajili ya ajira hizi za majeshi na maeneo mengine ambayo yalikuwa yana demand kigezo cha JKT, lakini kwenye hili Jeshi la Uhifadhi kumekuwa na kigezo cha miaka 25. Sasa kigezo hiki una-train mtu kwa pesa ya mzazi mwenyewe halafu huna uwezo wa kumwajiri, huwezi kuajiri wote uliowa-train na hawana sehemu ya kuajiriwa kwa sababu, wao kazi yao wamejifunza kulinda wanyama na nini? Sasa inafikia stage hujawaajiri wote, leo unamwambia aliyevuka miaka 25 huwezi kumwajiri, ilhali tayari ameishakuwa trained, ni mwanajeshi yule. Kwa sababu, ame-train-niwa kutumia silaha na vitu vingine. Sasa je, hamuoni iko haja ya kusimamisha mafunzo yao haya kwanza, waajiri wote walio mtaani ambao wazazi wametoa pesa, wameuza viwanja wakawasomesha, ili waweze kuajiriwa wote waishe kwa sababu, waliwa-train wao na hamna sehemu ya kuwapeleka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa sababu, wanajiita jeshi na experince ya majeshi mengine kama Magereza, Polisi, Jeshi la Wananchi, Uhamiaji na mengine yamekuwa hayawa-demand wazazi ku-train watoto, ili nyie muweze kuwaajiri, yamekuwa yanachukua watoto fresh from school, wanawa-train wenyewe, wakishamaliza ku-train wanawaajiri wao wenyewe moja kwa moja. Je, hawaoni na wao iko haja ya kufuata mfumo ule, kuliko kutesa wazazi ku-train watoto ambao wanakuja kuajiriwa kwenye majeshi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Chiwelesa kwa pamoja:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana wewe binafsi, tarehe 2 Septemba, uliruhusu hoja binafsi ya Mheshimiwa Ng’wasi Kamani ijadaliwe ndani ya Bunge hili. Kupitia mjadala ule, Serikali tulivuna mawazo, hekima na busara kubwa sana kutoka kwenye Bunge lako. Mawazo ambayo ndani ya Serikali kwa sasa tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, waiamini Serikali yao. Tuliyapokea maoni yale, tunayafanyia kazi, lakini vilevile vyuo hivi ndani ya Taasisi za Uhifadhi chini ya Wizara yetu vinahudumia Sekta pana ya Maliasili na Utalii, ambaye ni Mwajiri Mkuu kwenye Sekta hii; anaweza kuonekana kwamba, ni Serikali, lakini kwa kiasi kikubwa Sekta Binafsi inaajiri kwa kiwango kikubwa vijana wetu. Halmashauri zetu zote nchini Maafisa Wanyamapori wanatokana na vyuo hivi, kwa hiyo, kusema kwamba, ajira zinazotokana na vyuo vyetu hazipo, nadhani siyo sawa sana.
Mheshimiwa Spika, vyuo vyetu vimetoa wahitimu ambao wanaajiriwa kwenye Sekta Binafsi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za Kimataifa na ambao wamekwenda kwenye Taasisi za Kimataifa wamefanya kazi nzuri sana inayoliletea sifa Taifa letu. Nirejee kusema tunaliomba Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge watuamini jambo hili tunalifanyia kazi ndani ya Serikali. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Idea ya Mheshimiwa Mbunge, mpaka kuuliza swali hili ni kwamba, sisi kama viongozi na kama Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi wa mambo ambayo yanaendelea huko mitandaoni.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utapeli mkubwa sana kwa wananchi, lakini kwa sehemu kubwa watu wanaporipoti taarifa zimekuwa zinahitajika zitumwe TCRA na TCRA ndio waweze kurudisha polisi. Sasa hicho kitendo kinachukua muda sana, kwa sababu unavyoongelea utapeli leo hatuongelei wale watu waliopo mijini au kwenye majiji makubwa. Utapeli unafika mpaka vijijini na sehemu ambazo hakuna hata hayo mawasiliano saa nyingine inachukua muda mrefu sana.
SPIKA: Mheshimiwa mchango umetosha. Swali.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, sasa swali. Je, hatuoni kwamba, ili kuweza kuboresha mawasiliano na kusaidia Watanzania ambao wanapata dhuluma baadhi ya majukumu hasa ku-access information za wahalifu zingewekwa kwenye majeshi ya polisi tu ili mtu anapoibiwa polisi waweze kupata access ya haraka kumhudumia kuliko kuanza kupeleka information mpaka zirudi huku?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni swali moja tu hilo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa kupitia Mwakilishi wake Mheshimiwa Engineer Chiwelesa.
SPIKA: Ngoja. Hamwakilishi yeye ameuliza kwa niaba yake. Kwa hivyo, unamjibu yeye, kwa sababu hili ni swali la nyongeza, unamjibu yeye. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ezra, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli sisi kama Wizara tunafahamu hili na tunalishughulikia kwa umakini sana. Kwa taarifa tu Tanzania ni nchi ya pili Afrika katika usalama wa kimtandao. Hii inaonesha Wizara ipo makini na tunashughulikia haya yote ambayo yanaendelea mitandaoni.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi tumelipa hii kazi kupitia Unit yake ya Cyber Crime Unit. Kwa hiyo, si kwamba, Jeshi la Polisi halishughuliki moja kwa moja, lakini maboresho tutaendelea kuyafanya kadri ya ushauri mzuri ambao Waheshimiwa Wabunge, wanaendelea kutupatia.