Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rwegasira Mukasa Oscar (25 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi, lakini juu ya hayo namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilisha uchaguzi. Nawashukuru wapiga kura wa Biharamulo na Watanzania kwa ujumla kwa kukamilisha zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea nina maneno machache ya utangulizi. Siku moja nilikuwa kwenye benki moja ambayo sitaitaja jina, nikakumbana pale kwenye meza ya huduma kwa wateja na mzee mmoja ambaye alikuwa na malalamiko yanayofanana na ya kwangu. Yeye anasema ameweka kadi kwenye ATM, karatasi ikatoka kwamba pesa zimetoka, lakini pesa hazikutoka, nami nilikuwa na tatizo kama hilo. Alipowaeleza wale wahudumu, wakaja kama watano wanaeleza namna ambavyo mfumo wa computer unafanya transaction na maelezo mengi ya kitaalam. Yule mzee akawaambia vijana sikilizeni, mimi kama mteja wa benki yenu nina kazi mbili tu, nina kazi ya kuweka pesa na kutoa pesa. Hiyo habari ya mchakato unakwendaje, transaction system kazungumzeni huko halafu mje na pesa. Kwa nini nasema hivyo? Watanzania hawa ambao wanalitazama Bunge hili nao wana kazi tatu…
MBUNGE FULANI: Hawasikii hao!
MHE. OSCAR R. MUKASA: Vyovyote, watafahamu na watasikia, kuna namna watasikia. Wana kazi ya kufanya kazi, wana kazi ya kulipa kodi na wana kazi ya kudai huduma kwenye sekta mbalimbali basi, hawana kazi nyingine. Kazi hizi za kwamba kanuni iko hivi na nini ni muhimu, lakini mwisho wa siku wao wanataka matokeo.
Leo Mheshimiwa Zitto Kabwe, sijui kama yupo, huwa namheshimu sana, lakini leo amenishangaza. Amefanya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana rafiki yangu Zitto ni Mbunge makini. Nakwambia wewe Mwenyekiti, namheshimu sana Mheshimiwa Zitto, ni Mbunge makini na ninyi mnafahamu; lakini leo na siku chache zilizopita nimeshangaa kidogo na namwomba asiendelee kunishangaza.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Kwamba Ijumaa Bunge lilipoahirishwa nimefanya hesabu ya haraka haraka, nakubaliana kabisa kwamba kazi ya wapinzani ni kuisimamia Serikali na hawakuja hapa kuishangilia, hilo linafahamika kabisa. Hata hivyo, kazi hiyo lazima ifanyike kwa namna ambayo ina maslahi kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ijumaa lilipoahirishwa Bunge, kwa hesabu ya haraka haraka, kwa kutofanya kazi kuanzia saa tano ile mpaka muda uliopaswa kufanywa zimepotea kama milioni thelathini na tatu. Zimepotea kwa sababu mmoja wa Wabunge alitaka kuonesha namna anavyoweza kusoma Kanuni. Ungeweza kuonesha unavyosoma Kanuni, lakini ukawaacha Watanzania salama kwa kutotumia hela yao vibaya. Watanzania wanatarajia matokeo, lakini Wabunge wenzangu wa CCM na mimi nakuja kwenu. Tuna kazi ya kuisimamia Serikali, nje ya Bunge kwenye vikao vyetu na tuna kazi ya kuisimamia Serikali hapa ndani. Kilichotokea Ijumaa na yaliyotaka kutokea leo ni dalili kwamba kazi yetu Wabunge wa CCM hatujaifanya kwa kikamilifu. Huo ndio utangulizi kwa Wabunge wa CCM na Wabunge wa Vyama vya Upinzani. Watanzania wanatarajia matokeo, hawali Kanuni, hawali Sheria. Nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuchangia Mpango wa Maendeleo, napenda kuwa na kipaumbele kimoja ambacho ni mtambuka. Kipengele ambacho ni mtambuka, kwangu ni namna gani jitihada zetu za kukuza uchumi zinaendana na maendeleo ya uchumi. Ni namna gani chochote tulichokiandika kwenye mipango hii kinakwenda kugusa maisha ya mwananchi wa kawaida. Tukijenga reli, tukazungumzia barabara, tukazungumza yote hayo, kama hayagusi maisha ya mwananchi wa kawaida, Watanzania hawatuelewa, tutakuwa tunaimba wimbo wa kila siku ambao hauna tija kwao, wakati wao kazi yao ni kuona maisha yao yanabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano, ukurasa wa 27 wa hiki kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo unazungumzia namna ya kufunganisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu. Wanaonesha dalili hizo kwamba wanataka kusema hivyo, lakini ukienda kwenye maandishi kwa ndani, kwenye maudhui yenyewe, maeneo mengi huoni namna ambavyo Mpango huu unakwenda kugusa maisha ya mtu wa chini kabisa, nitatoa mifano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara, tumezungumza barabara, lakini utaona hapa tunazungumza barabara kubwa tu; za Mikoa, barabara za Wilaya, lakini ndugu zangu nikumbushe kitu kimoja. Barabara kubwa ya lami ina maana, lakini kama kule kijijini anakoishi mwanandhi, ndani Kijiji cha Kalenge, Kijiji cha Kitwazi hakufikiki hata kwa baiskeli, hata kwa pikipiki, maana ya barabara kubwa inapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetarajia tuone namna gani sasa tunaweza kuweka mipango ya kushuka chini. Wakati tunajenga barabara kuu zinazotuunganisha na mikoa umefika wakati sasa hata barabara zile zinazotoka (feeder roads) zinazokuja kukutana na barabara hizo ionekane wazi kabisa kwenye mpango kwamba sasa mwelekeo wetu ni kwenda kugusa mawasiliano ya barabara kwa mwananchi aliye kijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu, ukiangalia kwenye elimu hapa kwenye utekelezaji na kwenye vipaumbele, utaona tunaongelea maabara, madarasa, lakini mwalimu tunasahau kwamba ndiye mfanyakazi wa umma wa nchi hii ambaye anafahamika anapofanya kazi, lakini hafahamiki anaishi wapi. Hatuzungumzii nyumba za walimu, hatuweki mkakati nyumba za walimu miaka nenda rudi, tunazungumza mambo ya maabara. Ni mazuri, lakini ukipita kwa mwalimu utakuwa umegusa mengine yote kwa upana na kwa namna ya kwenda kubadilisha maisha ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara, nimeshangaa sana kwamba pamoja na kwamba nimezungumzia habari ya feeder roads, nashangaa sana kuona kwamba siioni barabara ya kutoka Bwanga kwenda Kalebezo, barabara inayounganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Kagera na nchi jirani ya Rwanda; barabara ambayo inakwenda kwenye Wilaya mama ya Rais anayeongoza nchi hii. Alikuwa mgombea wa Ubunge mara mbili pale Bihalamuro, lakini Mikoa hii ya Geita na Kagera kama haitaunganishwa na nchi jirani kwa kiwango kinachostahili tunaua biashara pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, unaona pale kwenye utekelezaji wanaongelea tu hospitali za rufaa, ni vizuri kabisa. Hata hivyo, hospitali za rufaa bila kuweka nguvu kwenye zahanati na vituo vya afya hatutagusa maisha ya watu. Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ya Dar es Salaam au ya Bugando ni muhimu iwepo lakini haina maana kama mtu hawezi hata kupata mahali pa kupata huduma ya kwanza ili aambiwe nenda rufaa. Ni lazima mpango huu ujikite kwenye zahanati na vituo vya afya kwamba sasa tunakwenda kuwagusa ili wakishindwa kutibiwa pale ndipo waende kwenye hospitali kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujumbe wangu ni kwamba, mipango yote tunayoiweka tuwe na kipaumbele mtambuka ambacho kinasema chochote tunachokifanya lazima kionekane wazi kwamba kinakwenda kugusa maisha ya mtu wa chini, vinginevyo maana yake inapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nawaombea kila la kheri Waheshimiwa Wabunge wa CCM tuisimamie Serikali, lakini na Wabunge wa Upinzani tuibane Serikali kwa namna ambayo inaleta tija kwa wananchi. Nawashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia na mimi kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, nawashukuru Wabunge wenzangu wote kwa kazi tunayoifanya, nakupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha vizuri, ukisikiliza unaona kabisa matumaini kwamba amejipanga kwa maana ya kufikiria na kuweka mkakati, lakini nina haya ya kusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu moja ambayo nadhani ni vizuri tuitazame na inaendana kidogo na msemaji aliyetangulia, Mheshimiwa Waziri uangalie pia namna ya kufanya kitu kinaitwa tathmini ya mambo ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwenye hii mipango uliyoiweka na mambo ambayo yanawezesha utekelezaji wa mipango uliyoweka, SWOT analysis. Kwa sababu yako mambo ambayo pamoja na mipango mizuri ambayo ukiisikiliza hii hotuba unavutiwa lakini yasipofanyiwa kazi hatufanya lolote kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza wakulima wa Wilaya ya Biharamulo, Ngara na Bukombe na jirani huko kwa sababu wote tunawasiliana wanajiandaa, ni kutengeneza mishale sasa hivi kwa sababu wafugaji tarehe 15/06 wanatoka kwenye hifadhi kurudi huku. Kwa hiyo, haya yote tunayoandaa kama hatukabiliani na mambo haya ambayo ni hatarishi kwa mipango hii ni bora tu tukaongeza bajeti kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo itakwenda kutuliza ghasia kuliko kuweka mbolea na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu limekuwa sasa ni jambo la kawaida, unakumbuka Mheshimiwa Waziri, namuomba anayemsemesha Waziri wa Kilimo atupe nafasi kwa sababu tunaongea mambo makubwa. Mwenyekiti naomba unilinde, naongea na kiti lakini Waziri mhusika asikie.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu imekuwa ni kawaida sasa tarehe 27/28 Disemba, sikumbuki exactly tarehe ila wiki ya mwisho ya mwezi wa Disemba, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akiambatana na Naibu Waziri wa Maliasili walikuwa Benako pale mpakani mwa Biharamulo na Ngara kwa sababu tulikuwa tumewaita kwenda kutatua mgogoro kama huo ambao ulikuwa unataka kutokea watu walikuwa wameandaa mishale. Leo pia mimi Mbunge wa Biharamulo badala ya kujadili mkakati sasa najadili namna gani tuzuie mapambano ili baadaye tuje kwenye mkakati, kwa hiyo, hili suala limekuwa la kawaida sasa.
Kwa hiyo, tusipoondokana na hili tunapoteza muda na tunapoteza muda kwa mambo ambayo yako ndani ya uwezo wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nateta na mtu mmoja hapa naambiwa Rwanda ndiyo wanapeleka mzigo mkubwa wa nyama ya ng‟ombe Congo lakini ng‟ombe hao wanatoka Tanzania, Ngara, Biharamulo, Bukombe sasa sisi ni waajabu, wanatushangaa. Kwa hiyo, badala ya kugeuza mifugo hii iwe neema tunaigeuza kwamba ni sehemu ya kuanzisha mapambano kati ya wakulima na wafugaji. Tuondoke hapo ndipo tutaweza kuongea mambo haya kwa maana ya kuweka mikakati na kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza hapa hali huko kwa kweli ni mbaya. Ukizungumza na mfugaji Biharamulo, Ngara, Bukombe sasa hivi hamuwezi hata kuongea lolote ni tarehe 15 imekaribia, tunafanyaje, tuondoke hapo Mheshimiwa Waziri na tunataka tuweke nguvu kubwa kwenye kutatua jambo hili, tumalize tufanye mambo mengine. Wakulima wamechoka, wafugaji wamechoka, Wabunge hatufikirii jambo lingine, unafikiria tu wafugaji na wakulima kila asubuhi, kila jioni. Tunaharibu rasilimali na akili tulizozileta humu Bungeni, tumalize jambo hilo twende kwenye jambo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo za kilimo. Mwezi Disemba nilikwenda kijiji kimoja kinaitwa Ntumagu kiko Kata ya Nyanza - Biharamulo. Nimefika pale kabla sijaongea ajabu wananchi mara nyingi wanapenda tunazungumza halafu nao wanapata nafasi ya kuzungumza, wakasema leo tunaanza sisi. Wakaniambia wewe bwana tunajua umekwenda shuleni, unasema sijui una digrii ya ngapi, Mkuu wa Wilaya tumesikia ana digrii moja, mbili, Mkurugenzi ana digrii mbili, Bwana Shamba alikuja hapa juzi ametuletea mbegu za kupanda wakati sisi mahindi yameshafika kiunoni naye tunaambiwa ana digrii moja, sasa mna digrii zote hizo lakini hamjui mahindi yanapandwa lini ni nini? Wananchi wanashangaa. Nalo tumelisikia kwenye hotuba lakini limekuwa linasemwa tena na tena hata tukiwa na mipango mikubwa sana huku juu kama yale ambayo ndiyo yanawagusa wananchi hayafanyiki yote haya mengine yanapoteza maana yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa yale mambo yanayogusa wananchi tumetaja la kwanza, vurugu za wakulima na wafugaji zishughulikiwe. Mheshimiwa Maghembe anasema ni tarehe 15 anakwenda kuwatoa wafugaji wote kwenye hifadhi, ni jambo zuri kwa sababu hawapaswi kuwa kwenye hifadhi, lakini si tupange? Mkulima anatekeleza wajibu wake, analima mpunga, mahindi, tunanunua tunakula, mfugaji naye anatekeleza wajibu wake, tukienda butchery pale hatuulizi kwamba naomba kilo tano; mbili za ng‟ombe aliyekula hifadhi halafu tatu za ng‟ombe wa maeneo mengine, hatusemi hivyo. Tunaomba kilo tano tunapewa ametimiza wajibu wake. Serikali yenye wajibu wa kuwapanga ili haya yote yafanyike haitekelezi wajibu wake. Kwa hiyo, tunapoteza muda kufikiria migogoro badala ya kwenda kwenye mambo ya mkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni hilo tumesema linagusa wananchi, habari ya pembejeo ambalo tunaomba pamoja na michakato yote zifike kwa wakati. Baada ya kuongea na wale wananchi walioniambia mbolea ya kupandia imefika wakati mahindi yamefika kiunoni nilikwenda kuongea na watu wa Halmashauri, nikakutana na Bwana Kilimo pale. Nilivyomuelezea akanipa story nzuri ambavyo mchakato wa kufikisha hiyo mbolea kwa mwananchi ulivyo, ikitoka hapa inafika pale lakini haya ni maelezo tu, mwananchi hayamsaidii. Kinachomsaidia ni pembejeo kufika kwa wakati ili apande kwa wakati tupate tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda wa wafugaji ambao unajumuisha Biharamulo, Ngara na Bukombe na kwingine wana umoja wao. Wakikupa takwimu utashangaa, wanasema kwa wastani kwa mwezi kuna kodi wanailipa kwa njia ya rushwa kwa hao watu wanaowafukuza kwenye hifadhi ya karibu milioni 30 mpaka 50. Kwa hiyo, kodi hiyo hiyo tukitafuta namna ya kuigeuza iwe halali itatusaidia hata kuwapanga hawa, lakini inatoka kwa mwezi na wenyewe wametunza takwimu vizuri kabisa lakini ni kodi ambayo inakwenda kwa njia ya rushwa kwa sababu watu wanatengeneza tu mazingira kwamba leo tukafanye doria, tutaondoka na milioni 30, kesho tukafanye hivi. Kwa hiyo, tutumie rasilimali tuliyonayo kwa njia ambayo inaleta tija ili kodi hiyo hiyo ilipwe kihalali badala ya kulipwa kwa namna ambayo haifaidishi Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya 30% ya mifugo ya ukanda ule inapata chanjo na hao wafugaji wanasema wao wako tayari hizo huduma zikipatikana wanazilipia tu. Ukiweka mfumo sahihi wa kulipia huduma hizo ina maana una mfumo sahihi wa kuweka takwimu, una mfumo sahihi wa kufuatilia kodi na wao wako tayari kulipa kodi. Hivi tunavyozungumza wafugaji wa ukanda ule wanalipa tu ushuru wa Halmashauri lakini hakuna namna wanalipa kodi ya Serikali Kuu na ukizungumza nao wanasema wako tayari, sasa hiyo potential tunayo mbona hatuitumii? Ukishatatua suala la wafugaji umetatua la wakulima kwa sababu sasa hivi mkulima ambaye angekuwa anafikiria afanyeje kwenye msimu unaokuja anafikiria namna gani atapambana na hawa jamaa watakavyotoka msituni huko kwenye hifadhi tarehe 15/06.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili limekuwa tatizo sugu na sisi wananchi wa ukanda ule tunadhani sasa inatosha. Kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Waziri afanye uratibu na Wizara nyingine zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuambiwa siku moja kwamba tunawafukuza hawa wafugaji kwenye hifadhi kwa sababu wako wengine wanatoka Rwanda, sasa hiyo siyo kazi ya mfugaji wa Tanzania kujua kwamba huyu ni wa Rwanda asiwe hapa ni kazi ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Kwa hiyo, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mambo ya Ndani na wa Maliasili wakae waseme huyu ni mfugaji wa Tanzania afuge, alipe kodi, awekewe miundombinu lakini unakuta kiongozi anasema kabisa tunawafukuza kwa sababu wako wafugaji wa Rwanda, sasa hii siyo kazi ya mfugaji wa Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuzungumza leo kwa niaba ya wananchi wa Biharamulo, lakini nawashukuru Wabunge wote waliotangulia kuzungumza kwa michango yao mizuri sana ya kuisimamia Serikali yetu, Wizara hii ya Elimu, Teknolojia na Ufundi. Kwa namna ya pekee pia nakupongeza Waziri na timu yako kwa kazi nzuri, lakini nina haya ya kukuambia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako makubwa, watu tuna matumaini na wewe Mheshimiwa Waziri, lakini unaingia kwenye Wizara ambayo yako hata madogo ambayo umekuta haiwezi kuyafanya. Sasa una kazi kubwa mbele hapo! Naanza na mfano mdogo tu halafu nitakuja kwenye hotuba yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014 kijana aitwae Kuzima Suedi wa Biharamulo, Shule ya Sekondari Kagango, alikuwa miongoni mwa vijana kumi bora wa masomo ya sayansi Kitaifa. Akafurahi sana na sisi tukafurahi sana! Wizara ikamwalika kwenye Wiki ya Elimu mwaka 2015 hapa Dodoma, akaja mzazi, Afisa Elimu, chereko chereko nyingi! Mgeni Rasmi akatoa zawadi kwa watu wachache, akasema waliosalia akiwemo wa Biharamulo, zawadi yao ya laptop na cheque itawafuata. Mpaka leo ni kuzungushana! Afisa Elimu wa Mkoa, wa Wilaya! Hayo ni madogo tu, nakuja lingine la utangulizi kabla sijaja kwenye hotuba. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii habari ya watoto wetu wa kike wanapopata ujauzito kuondolewa shuleni, nafikiri tusilitazame kwa namna tu ya haki yao ya kusoma, nadhani tulipe picha ya ziada. Hii ni habari ya mfumo dume ambao tunauendeleza kwa kiwango kikubwa sana. Mimi najiuliza jambo moja, linapofanyika lile tendo, ni mmoja tu ambaye masikini matokeo yake yanaonekana hadharani, tumbo linakuwa kubwa. Kungekuwa na utaratibu kila mwanaume anayempa mtu ujauzito naye anavimba nundu tunaona, tungejua na mtu mwingine wa kufukuza; kwamba wa kike anafukuzwa shule, wa kiume kama ni mwanafunzi mwenzake naye anafukuzwa; kama mwanaume ni Mwalimu, ama Mbunge, ama Polisi naye anakamatwa siku hiyo kwa sababu ana nundu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunawaonea hawa kwa sababu sisi ushahidi wa kwamba tumeshiriki kwenye hilo, hauonekani mara moja, mpaka tutafute tafute, tunakaa kubishana jambo ambalo liko wazi. Hebu tuwape haki wanawake! Tutafute namna ya kuwezesha watoto wetu wa kike wasipate ujauzito; hiyo ndiyo kazi ya kwanza, lakini inapotokea bahati mbaya limetokea hilo, tusiwahukumu peke yao. Huo ndiyo ujumbe wangu wa kwanza. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja sasa kwenye mchango. Ukiangalia kitabu cha hotuba pale sura ya kwanza, picha ya kwanza kabisa, umeweka picha ya Mheshimiwa Rais na kuna nukuu ya maneno anayoyasema kuhusu elimu; anamalizia, “Serikali ya Awamu ya Tano, itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa, ni pamoja na kuongeza mkazo katika masomo ya Sayansi. Hiyo ni nukuu. Tunapozungumza hivi, Biharamulo Wilaya nzima, tuna Walimu 560; Walimu wa Sayansi 30; lakini ukiangalia ukurasa wa 19 wa hotuba hii, umeeleza, “katika udhibiti wa ubora wa elimu kwa mwaka wa fedha huu unaokuja, Wizara imepanga kufanya yafuatayo.” Yametajwa mengi pale, lakini sioni mkakati wa kushughulika na suala la Walimu wa Sayansi. Hakuna hata pale! Sasa tunaongea tu nadharia lakini hatuweki mikakati; hatuwezi kutoka hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dunia ya sasa kama tutaendelea na Walimu 30 wafundishe shule 18 zenye wanafunzi 8,900, Walimu 30 wa Sayansi, hatuwezi kutoka tulipo. Inabaki ni jitihada za Afisa Elimu tu kule Biharamulo masikini anahangaika, hivi tunavyoongea ana Walimu wanane wanaojitolea. Amenituma nikuombe uhakikishe kwenye mgao unaokuja kwa sababu ni walimu na wana degree na walishajitolea pale, usiwatoe pale. Usije na ubabe baadaye kwamba sisi tunakupangia uende tunakotaka sisi, wakati wamejitolea mwaka mzima pale kabla wewe hujaweza kulipa. Nitakupa majina uwaweke pale, kwa sababu wameshajitolea na wanaipenda Biharamulo na wana sababu kwa nini walijitolea bila kulipwa wakiwa Biharamulo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije habari ya mitaala. Mwaka 2014 kama siyo mwaka 2015 mlibadilisha mitaala kwa Darasa la Kwanza na la Pili, mkaondoa masomo sita, mkaleta kusoma kuandika; KKK tatu zile. Hivi tunavyozungumza, watoto walio Darasa la Tatu, Walimu wa Kiingereza hawajui wawafundishe kuanzia wapi, kwa sababu walisoma Kiingereza mpaka mwezi wa Tano mwaka 2015, wakiwa la Pili. Mtaala mpya wa Darasa la Tatu unaochukua hali ya sasa, kwamba Kiingereza kianze Darasa la Kwanza haupo. Kwa hiyo, Walimu wanabahatisha tu; na watakaoingia Darasa la Tatu mwaka 2017 wana habari hiyo hiyo. Hatuwezi kufika kwa mtindo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, nina vitabu vitatu; viwili vya sayansi Darasa la Saba; kimoja cha sayansi Darasa la Sita. Nchi hii ukiwa Darasa la Sita ubongo wako una sehemu tatu, ukiwa Darasa la Saba ubongo una sehemu nne. Tutakwenda kweli? Hebu imarisha hivyo vitengo vya ukaguzi, tujue tunawafundisha nini wanafunzi kwa standard na consistence. Tutapanga mipango mikubwa kabisa, ambayo ukisoma kwenye makaratasi inaingia akilini, lakini uhalisia kule chini ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu Wizara, hebu tusikie, Waheshimiwa Wabunge wamesema sana kuhusu Walimu, ni Sekta ya Elimu tu ambayo ukitaka kujenga darasa ni lazima Mtendaji wa Kata amkimbize mwananchi kuchanga, lakini sijawahi kusikia Mtendaji wa Kijji anamfuata mwananchi kumkamata achange pesa ya umeme wa REA. Tumeweka kwenye mfumo. Sijawahi kusikia Mtendaji wa Kijiji anamfuata mwananchi kumkamata achange mfuko wa barabara ili tujenga lami; hakuna! Hata hivyo anachanga na tumeweka kwenye mfumo. Ni darasa tu na nyumba ya Mwalimu ndiyo lazima wakimbizwe na Mtendaji wa Kata, hebu tuondoke kwenye ujima, tutafute tozo kwenye kodi ambazo tutakamata Sekta ya Elimu na mundombinu yake, tushughulike nayo kama Taifa, ndiyo tutaondoka kwenye hali hiyo.
Napenda pia kuongelea kidogo COSTECH, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia. Hebu tuiwezeshe! Tunataka huo ubunifu waanze kuufanya kuanzia kwenye Shule za Sekondari, wawezeshwe waende kule; wawezeshe Walimu kutambua vipaji mapema, namna gani tutashughulika navyo, kikiwa kipaji bado kiko Biharamulo, kiko kidato cha pili, kipaji kiko kidato cha tatu, tunakijua kipo na tunapanga mpango wa kukiendeleza na kukikamata kitakapofika Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kwenye hoja ambayo nilitaka kuisahau kuhusiana na vitabu vyetu mashuleni. Kuna kitabu kimoja nimekutana nacho kwenye shule moja huko, kimoja kinasema tuna sayari tisa, kingine tuna sayari kumi. Sasa mimi nikachanganyikiwa, hawa watoto wakitoka hapo unataka huyu huyu ndiye aje kushiriki kwenye dunia ya sayansi na teknalojia? Haiwezekani na hatutafika kwa mwendo huo, nashukuru. (Makofi)
MHE. OSCAR R. MUKASA: Ni kengele ya kwanza?
MWENYEKITI: Ya pili Mheshimiwa
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, coverage ya civil registration ni ndogo sana hapa nchini, inawezekana ni chini ya asilimia kumi. Kwa nini msitumie watendaji wa Kata na Vijiji kama mawakala wa RITA kwa kuwapa gawio kwa kila kizazi, kifo na ndoa wanavyoorodhesha na kutumia taasisi za utafiti kwa kuhakiki ubora.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya hatukuweza kuona performance report ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha tulionao. Endapo ningepata fursa ya kuona ripoti hiyo, kungekuwa na fursa ya kusema yafuatayo kwa takwimu zaidi. Kuna dalili nzuri kwenye viashiria vya uchumi mkubwa (macro economic indicators), lakini kuna kila dalili kuwa tunaporomoka kwenye micro economic indicators.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ni kwamba mpango wa 2017/2018 pia hauonekani kuzingatia upungufu huu. Mfano, tungeweka nguvu kubwa kwenye viwanda vya kiwango (size) ya kati badala ya vikubwa ingekuwa rahisi kuweka kichocheo kwa sekta ya kilimo kwenye mikoa tofauti tofauti kwa kuzingatia zao la kilimo linalopatikana eneo husika. Tuwe na mtiririko (sequence) sahihi wa nini cha kufanya. Kilimo kifunganishwe na upatikanaji wa umeme na maji, soko la ndani ya Tanzania na soko la Afrika Mashariki litatosha kwa awamu hiyo ya kwanza. Hii pia itaongeza wigo wa walipa kodi, miundombinu (ndege, meli, reli) ili kutanua soko nje ya Tanzania na Afrika Mashariki.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iweke utaratibu wa kushirikiana na halmashauri kwa ajili ya miradi ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kuweka miradi ya kilimo au vinginevyo kwa ajili ya vijana kwenye umbali unaokaribia mita 60 za hifadhi za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya kadhaa ikiwemo Biharamulo zina maeneo makubwa ambayo ni hifadhi za Taifa. Mfano 54% ya eneo la Wilaya ya Biharamulo ni hifadhi za Taifa, kwa sababu hiyo wananchi wanalazimika kutunza hifadhi na mazingira kwa kuwa population density ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya Wizara hii kubaini wilaya zote za aina hii na kukaa nazo na kubuni suluhisho la pamoja kwa maana ya kupata rasilimali fedha pamoja na utashi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongelea vijana kupewa miradi kwenye maeneo karibu na mita 60 za hifadhi ya vyanzo vya maji, lengo ni kuwatumia vijana, wawe walinzi wa vyanzo vya maji wakati wakitekeleza miradi yao katika maeneo jirani na vyanzo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ushahidi kuwa asilimia kubwa ya mkaa unaotengenezwa hapa nchini unatumika katika Jiji la Dar es Salaam na Majiji mengine. Je, Serikali haioni haja ya kuweka tozo kwenye kila gunia la mkaa unaoingia Jiji la Dar es Salaam kutumia tozo hiyo kutoa ruzuku kwa matumizi ya gesi ili wananchi wanunue mitungi ya gesi kwa bei ya chini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Road Fund iwe re-allocated. Kwa sasa asilimia 70 barabara kuu na asilimia 30 barabara za halmashauri, hazitendi haki kwa barabara za vitongojini. Halmashauri zimeishia kuchonga barabara chache sana zinazounganisha kata; vijiji na vitongoji bado sana.

Miamala ya simu kwa kutumia fedha. Utumiaji kutoka Mtandao mmoja kwenda mwingine haufanyi kazi, fedha nyingine za wananchi zinapotea na watu wa kampuni wanatoa maelezo tu lakini fedha zinapotea Tunashukuru kwa ujenzi unaoendelea katika barabara ya Bwanga – Kelebezo. Hata hivyo kasi inaendelea kuwa ndogo, vile vile Mkandarasi haweki alama barabarani na hivyo kusababisha ajali.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa maabara kwenye vituo vya afya iwe kipaumbele. Kwa Biharamulo DMO anatoa pesa mfukoni mwake kulipa watu watatu wenye vyeti vya taaluma ya maabara ambao wanafanya kazi kwa kujitolea. Watu hawa hawalipwi mshahara, wanalipwa posho na DMO kutoka kwenye mshahara wake. Naomba waingizwe kwenye ajira na wabakizwe pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa CHF kwa wajawazito wa Wilaya ya Biharamulo, tutafikiwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, PLHIV na walemavu wajumuishwe kwenye asilimia kumi ya Halmashauri inayokwenda kwa vijana na wanawake. Haya ni makundi maalum zaidi, wakipata pesa hizi zitawasaidia kufanya shughuli za kiuchumi na hivyo kuweza kulipia CHF.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tutafute tozo fulani kisha fedha hiyo izungushiwe (Ring Fencing) kama REA, vinginevyo tunajidanganya. Hali ya maji huko vijijini ni mbaya kuliko mnavyodhani. Ni aibu!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Nyakalura uliigharimu Serikali shilingi bilioni moja lakini mpaka leo hakuna maji. Harufu ya rushwa kwenye mradi huo iko wazi, chukueni hatua, wananchi wanalalamika. Mji wa Kabindi unakua kwa kasi na sasa idadi ni takriban 25,000, hakuna maji kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na pia namshukuru Mungu kwamba amenipa fursa na ametupa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa na mimi napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango na timu yake kwa kazi nzuri, nasema ni kazi nzuri kwa vigezo vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ukisikiliza hotuba yake hata ukisoma kwa kiwango kikubwa utakuta mambo mengi ambayo ameyasema mule ni mambo ambayo sisi wenyewe Wabunge tulishauri hapa. Tuliyapigia kelele sana mwaka jana, tukayapigia kelele sana humo katikati na nataka kusema mimi ni mmoja ya watu ambao amethibitisha kwamba nilikuwa nakosea, Waingereza wanasema ameni- prove wrong. Mwaka jana nilitoka hapa na fikra kwamba Mheshimiwa Mpango hasikilizi, lakini mwaka huu ameni- prove wrong anasikiliza, kwa hiyo, hicho kigezo cha kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo cha pili, kwa sababu amesikiliza, utagundua kwamba mengi aliyoyasema kwa kweli hata wasikilizaji, wananchi wetu huko vijijini kabla hata hawajaona habari ya utekelezaji itakuwa vipi kwa sababu hiyo ni hatua nyingine lakini angalau kwa hatua ya kwanza wanaona bajeti hii ni ya kwetu. Akishindwa kutekeleza hiyo ni habari nyingine sisi tutamwambia kama Wabunge lakini kwa hatua ya kwanza wanaona kabisa hii bajeti ni ya kwetu sisi ndiyo walengwa. Kwa hiyo, nampongeza na timu yake kwa mambo hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wanasema kufanya vizuri haitoshi tunatakiwa kufanya vizuri zaidi. Yapo mambo ambayo bado sikubaliani na Mheshimiwa Mpango. Maisha ya binadamu ukijaribu kuweka vipaumbele ni jambo gani la kwanza ambalo hilo lisipokuwepo uhai wake hautakuwepo, la kwanza ni hewa ya kupumua ambayo kwa bahati nzuri ama mbaya hiyo haipo kwenye bajeti.

Pili, ni chakula na la tatu ni maji yaani ni afadhali Watanzania wote tutembee uchi hapa lakini tuna maji na tuna chakula. Hivyo ndiyo vipaumbele kwamba hewa ndiyo ya kwanza, huwezi kuongelea nguo wala viwanda kama hakuna hewa, imechafuliwa, ina gesi yenye sumu haiwezekani…

TAARIFA ....

MHE. OSCAR R. MUKASA: Haya, tuendelee Mheshimiwa Mpango na mambo ya msingi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi, kwanza kabisa ni hewa ambayo haipo kwenye bajeti. Pili, chakula na tatu ni maji halafu mengine yote pamoja na umuhimu wake yanafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama ukurasa wa 8 mpaka wa 9 wa Kitabu cha Hali ya Uchumi, anasema hivi Mheshimiwa Mpango kwamba Pato la Taifa lilitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 lakini limekua kwa asilimia saba badala ya
7.2 na akafafanua kwamba ziko sekta ambazo ndiyo zimechangia tusifikie lengo hilo na sekta mojawapo ni kilimo ambayo ilitarajiwa kuchangia kwa asilimia 2.9 lakini ikachangia kwa asilimia 2.1, amesema vizuri pale. Ukiangalia vipaumbele vya bajeti sasa kilimo kimeguswa kwenye shamba moja la miwa. Sasa mimi nikakaa najiuliza pamoja na kwamba sipingani na shamba la miwa kwa sababu nadhani anakwenda kujibu ile habari ya ukurasa fulani hapo hapo anasema, moja ya mazao ambayo tulilazimika kuleta kwa wingi kutoka nje ya nchi mwaka jana ni sukari, nafikiri anakwenda kujibu hilo, lakini nilitarajia kilimo kwa ujumla wake kipate kipaumbele. Hata kama huwezi kuwa na majibu ya matatizo yote lakini lazima kwenye vipaumbele vya Kitaifa vilivyo kwa ngazi ya bajeti tofauti na ngazi ya Wizara moja moja lazima kilimo kitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukurasa wa 11 wa hali ya uchumi pia anasema; mfumuko wa bei wa mwezi wa Aprili, 2017 ulikwenda juu ya wastani ya mwaka wa mfumuko wa bei, ukaenda 6.4 badala ya 5.2 ambayo ni wastani kwa sababu kulikuwa na hofu ya upungufu wa chakula kwa sababu watu waliona msimu wa mvua unachelewa. Hii yote inakuonyesha namna gani tunahitaji kujikita siyo tu kwenye kilimo tunapaswa kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kama unavyofahamu hatujawahi kutumia potential yetu ya kilimo, uwezo wetu wa kilimo cha umwagiliaji kwa kiwango kinachostahili. Kwa hiyo, nilitarajia kwenye vipaumbele vya ngazi ya Kitaifa, vya ngazi ya bajeti kuu siyo ngazi ya sekta moja moja habari ya angalau kilimo cha umwagiliaji kionekane ni kipaumbele. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango nimeshangaa sana kutoona kipaumbele cha kilimo zaidi ya shamba moja la miwa kwenye bajeti kuu, naomba ufanye mapitio kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya maji sasa ambayo imepelekea mtu akatoa taarifa hapa, sina matatizo na taarifa hiyo lakini mimi nilikuwa najikita kwenye mantiki kama mantiki umeiona nakushukuru, kama huioni bahati mbaya nitakuelekeza baadaye. Biharamulo leo tunavyozungumza, katika vijiji 80 vya Wilaya ya Biharamulo huwezi kuhesabu vijiji zaidi ya 15 au 16 ambavyo ukienda kuongea ajenda

nyingine tofauti na maji watakusikiliza. Leo Mji Mdogo wa Kabindi pale mpaka watu jana nilikuwa nazungumza nao wanapanga kufanya maandamano wanasema kwamba sasa hali ni mbaya. Tunaomba Mheshimiwa Mpango hebu weka hii habari ya maji, Wabunge wamesema mengi sitaki kurudia, habari ya maji hebu tuifikirie Kitaifa na kimkakati. Hii habari ya kuiacha kwamba ni suala la kudonoadonoa kila Mbunge anakwenda anakimbizana na Waziri wa Maji anampa msaada kimradi kimoja, kisima kimoja na vitu kama hivyo haitatufikisha. Kwa taarifa za kitafiti zilizopo habari ya kutafuta maji inachukua zaidi ya asilimia 40 ya muda wa Watanzania wa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali kwa sababu wanahangaika kwenda kutafuta maji ya kutumia nyumbani kwao na kwa ajili ya maisha ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo kwenye hotuba yake ukurasa wa 31 na yeye aliorodhesha pale vipaumbele akavitaja, cha kwanza anasema, kuboresha mfumo wa utafiti wa utoaji wa matokeo ya utafiti kwa wadau, kuimarisha usimamizi kabla na baada ya mavuno, kuimarisha upatikanaji na utumiaji wa pembejeo, zana za kilimo na vitu kama hivyo, kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo, kuratibu na kuboresha matumizi endelevu ya ardhi, kuunda na kupitia sera, kuwezesha uwezeshaji wa sekta binafsi na kuimarisha uratibu, ufuatiliaji na tathmini. Nililazimika kwenda huku maana yake nilidhani inawezekana kwenye bajeti kuu tumesahau hii habari ya umwagiliaji kwa sababu ndiyo itatutoa, tunazungumzia hapa habari ya ukame mpaka mfumuko wa bei unapanda nikasema ngoja nirudi kwa Waziri wa Kilimo inawezekana yeye anaongelea umwagiliaji lakini na yeye hasemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna tatizo na tumuombe Waziri wa Fedha, uzito wa suala la kilimo kwa upana wake uliotolewa hapa hautoshi. Kwa hiyo narudia, moja, suala la muhimu kabisa kwa binadamu ni pumzi ambayo wewe huna mamlaka nayo kwenye bajeti isipokuwa kama itatokea uchafuzi wa hali ya hewa inawezekana ikakuhusu.

Pili, ni chakula tunaomba utoe uzito unaostahili kwenye chakula na tatu ni maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unasimama hapa kutujibu tunaomba utuambie mustakabali wa kilimo kwa upana wake na tusisahau hii ndiyo sekta ambayo inaajiri Watanzania angalau asilimia 65. Ninyi Kitaifa mnaongelea asilimia lakini Biharamulo unaongelea asilimia 90 mpaka 92 wote wanajihusisha na kilimo. Kwa hiyo, tunaomba utakaposimama hapa Mheshimiwa Waziri utuonyeshe ni namna gani unaingiza suala la maji na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye habari ya makinikia maana naona kwa wiki hii usipoongelea makinikia unaweza kuwa upo tofauti kidogo kwa sababu kuna statistical normality na ideal normality kwamba ukienda kule kwa watu wafupi Congo sijui wanaitwa kabila gani, wote ni wafupi wewe ni mrefu. Statistically pale wewe ni abnormal, wao statistically ni normal kwa sababu ndiyo wengi ila ideally wewe uko kawaida wao wako abnormal. Kwa hiyo, lazima niongelee makinikia na mimi nitayaongelea kwa sentensi chache tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vita kuna mambo kadhaa lakini makubwa matatu ambayo mimi nataka kuyasemea. Moja, kuna lengo (goal) yaani mnalenga nini, mbili, kuna mkakati (strategy), mnajipangaje kwa ujumla na kwa upana wake na tatu kuna tactics (mbinu). Sasa kwamba lengo letu ni kushinda hii vita ya kwamba tumenyonywa miaka mingi siamini kama kuna Mtanzania ambaye hana lengo hilo, lakini kwa ngazi ya mkakati hiyo ndiyo ngazi ambayo yuko Rais. Rais anachotaka kufanya, mimi nimemsikiliza, nimemfuatilia unamuona huyu mkakati wake ni kutafuta namna gani siku tukikaa meza moja na hao tushike upande wa mpini na wao washike makali au angalau tuwe na meza moja, ndiyo mkakati alionao ukimsikiliza na ukimfuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiwasikiliza wengine wanaochangia unaona kwamba kila mmoja anataka kuchangia kwa ngazi ya tactics (mbinu) ambalo ni jambo zuri lakini kwa bahati mbaya mtu anataka kuchangia kwa ngazi ya tactics (mbinu) lakini anafikiri ili mbinu yake ionekane imesaidia ni lazima abomoe mkakati, sasa hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wana falsafa wanasema, ukiwa na mkakati mzuri bila mbinu utakuwa na mawazo mazuri bila utendaji, lakini ukiwa na mbinu nzuri bila mkakati ni vurugu. Ndiyo maana hapa unaona mwingine anasema haya tunajenga nyumba, wewe bomoa tofali hili badala ya wote kusema jenga. Kwa hiyo, tutambue kwamba lengo letu ni moja, Rais yuko kwenye ngazi ya mkakati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko kwenye ngazi ya mbinu, kwa hiyo, kila mtu atoe mchango wake wa mbinu ambayo hailengi kubomoa mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Awali ya yote namshukuru Mungu kwa afya. Pili nawatakia kila la kheri ndugu zetu Waislam ambao wameanza mwezi Mtukufu. Pia nataka kuwapa pole wananchi wa Biharamulo kwa adha inayoendelea huko, sasa hivi ni vurugu tupu baina ya wafugaji na wakulima baada ya hii habari ya mifugo kutolewa hifadhini bila mpango, lakini hiyo tutaisema baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa maana ya hotuba nataka kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima kwa sababu kuna kazi wamefanya ndio maana tupo hapa, vinginevyo tungekuwa hatuwezi hata kujadili, kwa hiyo nawapongeza kwa kazi, lakini tunayo mambo ya kusema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nitakwenda haraka haraka kwa sababu ya muda nina mambo kadhaa. Ukurasa wa 73 wa hotuba Wizara inazungumzia mafanikio kwa mwaka uliopita na moja ya mafanikio hayo ni kupunguza madeni ya wazabuni na wakandarasi. Wamesema wengi sana waliotangulia, lakini nataka kuweka msisitizo hapa, tunaomba Wizara iwatazame hawa wazabuni na wakandarasi kama sehemu au kama mawakala ambao mbali na kufanya kazi zao ndio wanatusaidia kuwezesha mzunguko wa pesa huko kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, mama mmoja ambaye ndiye analisha shule zetu za sekondari karibu 20 zote pale, huyo ni mfano tu, wako wengi pale wafanyabiashara wa Biharamulo wanaodai pesa na sasa wanaelekea kufilisika. Huyu namchukulia kama mfano, analisha shule lakini hivi tunavyozungumza anaidai Serikali milioni kama 400, imefikia hatua sasa mabenki yanataka kukamata magari yake, lakini watu binafsi wengine ambao wameshamsaidia wao tayari wamekamata magari na rasilimali, amesimama kabisa, yaani ni muda siyo mrefu tunamuingiza kwenye umaskini, tunamaliza mtaji wake wakati ni mtu yeye na wenzake wanashiriki kuwa kama mawakala wa kutusaidia kuzungusha pesa pale, akilisha watu 20 kuna watu anawaajiri pale kwenye kiwanda chake, wanabeba mahindi wanapeleka kwenye mashine, wanapakia kwenye gari, wanasambaza, ni ajira zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa hatumtazami yule mfanyabiashara peke yake, tunatazama mzunguko mzima. Tunaomba mlipe uzito ili haya madeni tuyalipe hata kama hamuwezi kulipa yote angalau sasa naomba Mheshimiwa Waziri tuone namna gani kila mmoja angalau anapunguza ule mzigo ili magari yake yaruhusiwe, mashine zake ziruhusiwe kuendelea, vinginevyo anasimama kabisa na wote waliomzunguka ambao wanapata uchumi kupitia yeye wanasimama kabisa, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimeangalia ripoti moja hapa ya Benki Kuu inazungumzia annual growth of banks credit to major economic activities, mengi yamesemwa pale katika chati mojawapo. Interest yangu iko kwenye habari ya kilimo, inaonesha mwezi wa Tatu mwaka huu growth ni minus 9.2 ukilinganisha na 11.2 chanya ya mwaka jana mwezi wa Tatu mwaka 2016.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ikanikumbusha nilikwenda siku moja Benki ya Kilimo pale, nimepekela kampuni moja ya binafsi ambayo tunataka itusaidie kushughulika na wakulima wa Biharamulo. Benki ya Kilimo wanatuambia tuna mikoa kadhaa ya kuanzia Kagera haimo, sasa nikawa nashangaa ni namna gani sasa! Hili ndio jambo ambalo linakwenda kushughulika na Watanzania asilimia 80 ambao ndiyo wakulima lakini bado tunalifanya kwa maeneo madogomadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie hapo namna gani wale ambao tuna nia ya kuleta watu watusaidie kwenye uwekezaji wa kilimo tutasaidiwa, kwa sababu benki hii wanatuambia kuna maeneo wanaanza mengine tusubiri. Tusubiri wakati hii ndio ajira ya asilimia 80 ya watu wetu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nataka kugusia kidogo habari ya sekta binafsi, MKURABITA, Hernando De Soto alisema nafikiri ni 2003 kama sikosei mwanzoni mwa 2000 kwamba asilimia 98 ya business transaction kwenye nchi hii zinafanyika nje ya mfumo, kwa hiyo hazilipi kodi na asilimia 90 kama sikosei, figure hizo nitaangalia vizuri, za land property (mali ardhi) iko nje ya mfumo hailipi kodi. Hilo tulishalifanyia uchambuzi kwa kusaidiana na Hernando De Soto ndio ikazaa MKURABITA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, mbona hatuoni mrejesho wa kila tunavyosoma bajeti wa namna gani sasa, MKURABITA imeondoa kwa mwaka mmoja idadi kadhaa ya Watanzania waliokuwa nje ya sekta inayotambulika imewaingiza kwenye sekta, hivyo, hata Waziri wa Fedha atuambie kwa kuingiza hawa sasa tumeingiza nguvu ya kikodi ya kiwango fulani ili mtu akiweza kufuatilia kwa miaka mitano tunaona tunakwenda wapi, naomba maelezo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne; wenzangu wamegusia, kuna habari ya kukusanya kodi, habari ya kupeleka hela kwenye Halmashauri lakini kuna habari ya kasi ya kuzitumia. Nina mfano mahususi hapa, tuliomba pesa kwa ajili ya maji ya Biharamulo Mjini kutoka Wizara ya Maji, tunashukuru wametupa milioni 200 mwezi wa Kwanza, mpaka leo tunavyoongea mwezi wa Tano huu unakwisha mambo yanakwenda taratibu kama kinyonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza leo na RAS wa Kagera na mtu wa Mamlaka ya Maji Bukoba Mjini, anasema mwanzo kulikuwa na ubishani kati ya Watendaji wetu wa Halmashauri na Mkoani, kwamba Halmashauri wanataka wafanye wao, hawa wanasema haiwezekani hizi hela zitapotea. Hiyo process tu ya kubishana imetumia miezi miwili. Tunaomba Waziri aje na mfumo ambao pamoja na kuzipeleka na kuzisimamia kwa maana zimefanya nini, tuwe na mfumo wa kutazama kasi ya kuzitumia kwa sababu inachangia sana kwenye kukwamisha maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, nimesoma hotuba ukurasa wa 76, tunasema moja ya majukumu ya Wizara; kuweka utaratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini, kufanya tathmini ya miradi ya kuondoa umaskini ngazi ya Vijiji na Wilaya. Hii sasa naleta habari ya ng’ombe na mifugo kule kwenye hifadhi, kwenye muktadha wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kilio cha wafugaji Kanda ya Ziwa na jana nilikuwa Biharamulo ni kwamba tunavyozungumza ng’ombe 11,000 wametaifishwa kwa maana ya kwamba tunawaondoa kwenye hifadhi kwa sababu hawastahili kuwa kule, sina tatizo na hilo. Mimi sio mmoja wa Wabunge wanaotaka ng’ombe wakae hifadhini, lakini swali langu ni kwa nini hatuoni hii kama ni fursa ya kiuchumi? Kwa nini hatujaribu kukaa na wafugaji na wakulima tukawaonesha fursa tulizonazo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nimewahi kusema hapa, nimesaidiwa na UNDP wamefanya tathmini ya uwekezaji kwenye Wilaya ya Biharamulo baada ya kutuambia kwamba sisi ni maskini wa pili. Wakasema mambo mengi lakini nitasema moja tu, asilimia 54 ya eneo letu liko kwenye hifadhi, asilimia 46 ya eneo letu ndio la uzalishaji, lakini hilo asilimia 46 asilimia kubwa ya kutosha ni underutilized, hatujapanga, ardhi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza na Mifuko ya Hifadhi, dada yangu Mheshimiwa Jenista hapa nataka nimshukuru sana, akatukusanyia mpaka Mifuko ya Hifadhi, wakaja viongozi wa Chama cha Wafugaji, wakakaa wafugaji wako tayari, tumefanya tathmini kuna mifugo kama milioni moja kiwango cha chini. Wakasema kila kichwa kichangie elfu 50 tukaona hiyo bilioni 50, tuungane na Mifuko ya Hifadhi tutengeneze viwanda kule, tutengeneze ranchi ndogo ndogo kwa sababu ripoti zinasema tuna underutilized ardhi yetu, tuwaondoe kwa namna ambayo hawatakaa kwenye hifadhi lakini hawataleta vurugu kwa kuwatoa kwenye hifadhi kuleta Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza Biharamulo hatukuwa na migogoro ya wafugaji na wakulima lakini leo badala ya akili ya Mbunge na akili ya watu wengine kuwekeza kwenye kutafuta uwekezaji tunawekeza kwenye kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo haikuwepo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri amesema kwenye ukurasa wa 41 habari ya ubia wa sekta binafsi mpaka wana Tume maalum, watusaidie sasa. Wakati maliasili na kilimo hawajaliona hilo au wanaliona, lakini wanakwenda taratibu waje wao na jicho la uwekezaji ili tukatatue mgogoro wa wafugaji, hifadhi na wakulima kwa jicho la uwekezaji kwa sababu inawezekana, wafugaji na wakulima wapo tayari lakini sisi viongozi ndio tunawagombanisha kwa kutofanya kazi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 75, Mheshimiwa Waziri ameongelea majukumu ya Wizara ya kubuni na kusimamia utekelezaji wa sera ya uchumi, ndio mambo haya. Uchumi tusiuangalie huku juu tu, twende huko Wilayani watusaidie, tunazungumzia kuondoa umaskini lakini Biharamulo leo tunaongeza umaskini. Mimi pale sasa hivi hotuba pekee ninayopaswa kutoa pale ni kuzungumzia mifugo tu, siwezi kuongelea maji, siwezi kuongelea nini, kuongelea wakulima na wafugaji. Hebu...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Benki Kuu inaonesha kushuka kwa kiwango kikubwa kwenye mikopo ya mabenki kwenye shughuli muhimu za kiuchumi mfano mkopo kwa watu binafsi 4.9% kwa mwezi Machi, 2017 ukilinganisha na 37.2% kwa mwezi Machi, 2016, mawasiliano na usafiri 21.6% mwezi Machi, 2017 ukilinganisha na 27.4% ya Machi,2016 na kadhalika. Je, mwelekeo huu unatupeleka wapi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na namshukuru Mungu kwa uhai na afya na ninaendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kunipa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ujumla wake, lakini kuna maeneo ambayo inabidi tuseme. Biharamulo hivi tunavyoongea sasa hivi, kuna kilio kikubwa sana cha wakulima wa pamba. Wakulima wa pamba wameingia kwenye dimbwi ambalo hawajui na hatujui tunatoka vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dawa kwa ajili ya kupambana na wadudu, tunaambiwa wanaletewa dawa aina ya Duduall, Duduba na Bamethrin. Dawa hizi hazifanyi kazi, kabisa na kuna maoni mara tatu. Wataalam wetu wa kilimo wa Halmashauri ya Wilaya pale wanasema tatizo la kwanza ambalo wanadhani ndiyo linasababisha hili inawezekana ni kukosekana kwa mwendelezo wa upatikanaji wa dawa kwa sababu mkulima anapotakiwa kuweka dawa kwenye pamba wiki ya mbili, lakini labda anatakiwa wiki ya nne apate dawa nyingine isipokuja kwa wakati hao wadudu wanajenga usugu.

Lakini kuna malalamiko kutoka kwa wakulima hao, wakulima wanasema wanapokwenda kwenye maduka binafsi wakachukua dawa kwenye maduka binafsi mbali na hii dawa inayoletwa na Bodi ya Pamba dawa hii inafanya kazi. Hiyo ni hypothesis inayoonesha kwamba inawezekana kwenye dawa inayopita kwenye Bodi ya Pamba kuna uchakachuaji na wamefikia hatua ya mbali wakulima wakafanya utafiti wao wenyewe (wakulima wa Biharamulo wana akili sana) kuna tuhuma kwamba wakulima hawa hawatumii vizuri dawa ndiyo maana haifanyi kazi. Wakamtafuta Afisa Ugani wakampeleka kijijini, pale Kijiji cha Kagondo, Kata ya Kabindi wakamwambia chupa ya dawa hii hapa changanya mwenyewe weka kwenye shamba mwenyewe. Akafanya hivyo mtaalam wakaenda siku inayofuata wakakuta wadudu sio tu wapo, inawezekana wameanza kuota na macho wanatazama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasubiri wiki moja wakaenda wakatazama. Wadudu wapo! Wakasubiri wiki tatu, wakamuita na Afisa Ushirika akaja kutazama, wadudu wapo! Kwa hiyo, kuna tatizo. Inawezekana kuna uchakachuaji wa dawa kwenye Bodi ya Pamba kwa sababu wakulima hawa wakienda kuchukua dawa kwenye maduka binafsi inaonekana dawa ile inafanya kazi. Sasa tuna maswali mawili.

Swali la kwanza, tunatatuaje tatizo kwa msimu unaofuata? Lakini swali la pili, tunawafidia vipi wananchi hawa kwa sababu Bodi ya Pamba ambayo ni taasisi ya umma ndiyo imewaletea dawa na tuna sababu kwanini tunataka kudai fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji wa pamba kwenye msimu juzi ulikuwa hekta 500 kwa Wilaya nzima, msimu jana heka 900 na msimu huu heka 2,800 na mwaka jana msimu uliopita wameuza wamepata jumla ya kilo milioni sita. Kwa hiyo, uzalishaji umepanda sana kwa sababu ya uhamasishaji na wananchi walikuwa na matumaini sasa ya kuondoka kwenye umaskini. Msisahau Biharamulo ndiyo Wilaya ya pili kwa umaskini nchi hii kwa kipato cha ngazi ya kaya, mnafahamu. Sasa kama kupitia kilimo ndilo eneo ambalo wananchi wanaweza kujiinua lakini Serikali na vyombo vyake havitimizi wajibu wao ina maana tunakaa kwenye mzunguko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama ukurasa wa 29 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna ushahidi kabisa wa kitu kinaitwa The know-do gap. Tunachojua ni moja lakini tunapokwenda kwenye field hatufanyi hiyo moja, tunafanya mbili. Anasema kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba moja ya matatizo yanayosababisha kilimo kisiwe moja ya nyanja zetu ambazo zinatuinua kiuchumi ni, kuna habari ya ukosefu wa utafiti, ukosefu wa pembejeo, ametamka Waziri Mkuu, tunafahamu lakini hatufanyi! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza wananchi wangu wakulima wamenipigia simu wameniambia chupa mbili za hii dawa ya Duduall ambayo imekuwa inatumika kama ushahidi. Tunaiomba Serikali iende ikafanya tathmini ya hiyo dawa tuone kama je ni kweli kuna uchakachujai ama ni tatizo lile lile la ucheleweshaji wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri Mkuu tufanye tunachoamini ambacho tumeandika kwamba tunavyoshindwa kufanya huduma ya ugani kwa wakulima ni moja ya sababu kubwa ya kilimo kinakuwa hakina tija kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 27, Mheshimiwa Waziri Mkuu anataja kabisa kwamba tutaweka mkazo kwenye mazao matano yakiwemo pamba lakini ukurasa wa 32 anasema; “tumeamua kwa dhati kusimamia sekta ya kilimo.”

Sisi huko kwetu Kagera kuna msemo unasema wakati mnakula chakula cha mchana au usiku pale, mtoto ambaye ni mroho ama mlafi unamuona wakati wa kunawa. Kwa hiyo, kama Waziri Mkuu anatuhakikishia sasa anaweka kwa dhati tunaomba aanze na Biharamulo, twende tukatazame hizo dawa ambazo tumetunza sample, twende tutazame tuone tatizo liko wapi, tatizo liko kwenye uchakachuaji, kukosa consistency ya kuleta dawa ama tatizo liko wapi? Hiyo ndiyo itakuwa alama sahihi kwamba huyu mtoto anayenawa sasa hivi vizuri hatakula kwa ulafi. Nakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee habari ya Waziri Mkuu amesema ukurasa wa 38 na 39 habari ya madini. Tunatambua Mheshimiwa Rais anaendelea na utaratibu wa kuunda ile Kamisheni. Tunaomba twende kwa kasi kwa sababu wananchi wa Biharamulo tumepata maeneo ya uchimbaji wa madini pale, tunahitaji kupata leseni, tumeshajipanga. Huu muda unavyokwenda tunaendelea kupoteza ile momentum na tutakosa fursa ya kufanya kazi yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo viwanda. Mheshimiwa Mwijage yuko hapa. Nimeona kwenye ukurasa wa 35 wa hotuba ya Waziri Mkuu tunasema viwanda 3,000. Naomba tusiiweke too general tuzungumze kwenye hivyo 3,000 vingapi ni vikubwa, vingapi ni vya kati na vingapi ni vidogo, lakini pia twende mbali zaidi, tutafute utaratibu wa incentive, namna gani mtu unamvutia. Unajua kuwekeza kiwanda Dar es Salaam kwa sababu ya baadhi ya miundombinu na kuwekeza kiwanda Biharamulo kuna tofauti! Tukiwawekea hawa private sector incentive kwamba akiwekeza Biharamulo kuna zawadi fulani ambayo anaipata kikodi ili apunguze maumivu kwa sababu ya habari nyingine za miundombinu ya aina mbalimbali itamfanya aende kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ikitokea na mimi Mbunge au Mkuu wa Wilaya, mtu yeyote kutoka Biharamulo akawezesha kupata wadau ambao wataweka kiwanda pale Halmashauri nayo ipate incentive namna gani Halmashauri itapata incentive kikodi badala ya ushuru kwa sababu tunajua vyanzo vingi vimehamishwa kutoka kwenye Halmashauri kwenda Serikali Kuu. Tukienda namna hiyo tutapata namna sahihi ya kuwezesha hata kule ambako kimiundombinu ni vigumu watu kwenda, lakini ukiwawekea uvutiaji watakwenda na mambo yatakaa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo niongelee uwezeshaji wa makundi maalum. Naomba tuwakumbuke Watanzania wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Ni kundi maalum ambalo linashiriki kwa kiwango kikubwa kwenye ile habari ya 90-90-90. Asilimia 90 ya watu wanaodhaniwa kuwa na virusi vya UKIMWI wapime, asilimia 90 ya waliopima watumie dawa na asilimia 90 ya wanaotumia dawa watumie vizuri ili ifubae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakitumia dawa vizuri siyo faida ya kwao peke yao ni faida ya umma mzima. Anapokuwa ametumia dawa kwanza anaondoa utegemezi wa kiuchumi kutoka kwa umma mzima kwa sababu ana uwezo wa kufanya kazi, lakini kama unampa uwezeshaji anaweza akapata Bima ya Afya yeye na familia yake wasiwe na utegemezi. Pia hiyo ni namna moja ya kufanya prevention kwa sababu mnajua prevention is better than cure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo hili la walimu wa sekondari kutolewa sekondari kwenda shule ya msingi, najua ni dharura na Mheshimiwa Ndalichako naamini ananisikia na nilimwambia kidogo kule kwenye Kamati, naomba nisisitize. Nafahamu ni dharura, lakini ni kwa kiwango gani hili tunalifanya kwa muda mfupi lisiwe endelevu? Kwa sababu likiwa endelevu hili halina tofauti na ile habari ambayo nakumbuka nimewahi kumwambia Waziri, jamaa mmoja alienda kwa fundi wa kitanda akamwambia nitengenezee kitanda cha nne kwa sita, fundi akakosea akatengeneza nne kwa tano. Jamaa alivyokwenda kupima pale akakuta miguu inazidi anamuuliza fundi, tufanyaje? Fundi anasema hapa njia rahisi kabisa ya mkato ni kukata miguu ili kitanda kitoshe. Tukienda namna hiyo kwa muda mrefu, kwamba kazi yetu itakuwa ni kurudisha walimu wa sekondari shule ya msingi kuna mzunguko ambao tutaingia, walimu wa sayansi haitatokea siku watoshe.

Moja; sample chupa mbili za nusu lita ziko Biharamulo; moja anayo Extension Officer wa Kata ya Kabindi, moja anayo Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika.

Mbili; naamini na ninadhani, utaniongoza ni kazi ya mnyororo wa Serikali kuhakikisha zinatoka huko zinakuja huku kwa sababu ziko mikononi (hasa hiyo moja iko kwa Afisa wa Kilimo), lakini jambo la tatu narudia na utatazama Hansard. Nimesema hypothesis ni tatu, moja; kukosa consistency ya kupeleka dawa ndiyo kunasababisha wadudu wasiwe, mbili, dawa inayoletwa na Bodi ya Pamba haiui kwa sababu wananchi wanasema ukienda kwenye maduka binafsi wanayopata inaua. Tatu, kuna hypothesis kwamba wakulima hawatumii vizuri ndiyo maana walimleta Afisa Ugani wakamthibitishia na yeye yupo aletwe pamoja na sample. Maana ya hypothesis ni kwamba hujajibu mnatakiwa kufanya kazi mjibu kipi ndiyo kinasababisha. Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Itabidi twende mwendo kasi maana dakika tano hizi hazitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ada na inavyostahili nawapongeza sana Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, Katibu Mkuu naye anafanya kazi nzuri sana, inaoneka watu tunamsahau na timu yake pia, kwa kweli kazi inaoneka. Mimi ni mmoja wa watu ambao binafsi nikijaribu kufuatilia unaona kabisa kwamba sasa kuna mahali tunakwenda kwenye sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna mwanafalsafa mmoja anasema dunia yetu siyo mbinguni na kufanya vizuri haitoshi ni lazima tufanye vizuri zaidi. Kwa hiyo, mnafanya vizuri lakini lazima tufanye vizuri zaidi. Sasa nasema yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba ya Waziri, ukurasa 127, kiambatanisho namba tatu, anapoongelea upatikanaji wa dawa, kuna majedwali pale yanazungumzia kila Wilaya asilimia 80, 90 na mambo kama hayo lakini kwa wastani kitaifa anasema upatikanaji ni asilimia 87, ni jambo zuri. Hata hivyo, hii maana yake ni kwamba katika kila watu 10 unaokutana nao wametoka hospitalini pale, tisa watakuambia tumepata dawa tuliyoandikiwa, kitu ambacho uhalisia kule chini sio kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wasiwasi wangu ni kwamba inawezekana Bohari ya Dawa kusukuma madawa kule wilayani ndio asilimia 87 lakini upatikanaji wa dawa kwa maana ya kutoka pale ilipo kumfikia mgonjwa sio tunachokiona kinachofanana na hii 87. Biharamulo pale ukizungumza na watu kumi wanaotoka Hospitali ya Wilaya pale, ukasimama tu nje, watu watano mpaka sita wana malalamiko ya dawa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ujumbe wangu ni kwamba umefanikiwa sasa kusukuma dawa kwenda kwenye hospitali zetu lakini ukashughulike na kituo cha tiba na mgonjwa ili upatikanaji wa dawa uwe kwa mgonjwa. Kuna habari ya committed supply na actual supply. Kwa hiyo, tuone namna gani mgonjwa anapata dawa hiyo hatua inayofuata. Naomba hata CAG aende mbele zaidi afike hapo na kwenda hatua ya pili kwa sababu lazima twende kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anasema kuna shilingi kama bilioni mbili za Mfuko wa CHF hazieleweki zimefanya nini huko kwenye maeneo yetu, sio maneno yangu ni CAG. Kwa hiyo, naomba tutazame kwenye ukurasa fulani hapa kwenye hotuba unazungumzia CHF iliyoboreshwa inakwenda kutatua habari ya mipaka ya tiba kwa kutumia CHF kuondoka nje ya Halmashauri lakini hiyo haijibu matumizi ambayo hayaeleweki ya pesa ambayo tayari watu wamechanga. Wananchi wakisikia habari sisi inatuwia ngumu kuwahamasisha waendelee kujiunga na CHF. Tunaomba muende hatua ya ziada zaidi ya kuongelea CHF iliyoboreshwa kuwaondolea mipaka ya matumizi ya ile bima yao lakini ukatazame ni kwa nini pesa hizo hazitumiki kama zilivyopangiwa, anasema CAG sio maneno yangu hayo twende kinachofuata kwa sababu tunakwenda kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Biharamulo tuna vituo vya afya vitano lakini katika vituo hivyo ni kimoja tu ambacho kina mtaalamu wa maabara tena ambaye sio wa kiwango cha Laboratory Technician ni Laboratory Assistant. Maana yake kwenye vituo vya afya vyetu vyote pale hawa madaktari wetu waganga wasaidizi wanapiga ramli yaani hata mtu akisema nina dalili za malaria hawezi kwenda kupima, inabidi mganga apige ramli ndio ajue hii ni malaria ama ni nini. Tunaomba tuangalie ni namna gani tutakwenda chini hasa kwenye zile huduma ambazo ni lazima na zinamsaidia yule mganga kufanya tabibu zake kama anavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 57 mpaka 58 kwenye hotuba ya Waziri anaongelea makundi ambayo yanahitaji msamaha na anataja walemavu, familia zenye migogoro, wakimbizi, waathirika wa pombe kwamba hao ndio wanafikiriwa pale.

Mimi nikafikiria tuna 10% ile ya akina mama na vijana kwenye halmashauri na tumewapa wale kwa sababu ni makundi maalum lakini yako makundi maalum zaidi, walemavu na watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI hawa wana mahitaji zaidi, ni makundi maalum, maalum ndani ya maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute namna ambavyo na wenyewe tuwajumuishe kwenye ile 10% waangaliwe kwa upekee waweze kufanya shughuli za uzalishaji, waweze kununua bima na waweze kupata tiba lakini ukimfikiria kwenye msamaha mpaka mtu aliyeathirika na pombe, mpaka mkimbizi, wakati mlemavu hujamfikiria, nadhani vipaumbele vyetu vinakuwa sio sawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, we must go out of the box, si sawa kwa mifugo kukaa hifadhini lakini ni wajibu wa Serikali kuwapanga wakulima na wafugaji ili watumie vizuri maeneo walionayo na hivyo kutolazimika kuingia hifadhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichopo Wizara na Wakuu wa Mikoa wamejikita kwenye operesheni na kufilisi bila kuiona hii kama fursa ya kugeuza mitazamo ya wafugaji na kushirikiana na wawekezaji ili mifugo iwe fursa. Mfano, Wilaya ya Biharamulo 54% ya eneo ni hifadhi, 46% maeneo ya watu, hata hivyo 46% is under-utilized kwa kuwa haikupangwa. Tujipange na inawezekana tuachane na mambo ya operesheni haya kwani yanaishia kutengeneza mianya ya kuonea watu na rushwa. Fikeni Biharamulo muwasikilize wananchi itawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maliasili na Utalii ni Wizara moja lakini kuna idara au mashirika mbalimbali kama TANAPA, Misitu, Ngorongoro, TAWA na kadhalika. Watumishi wanalalamika kuwa tofauti ya mishahara ni kubwa mno hata kwa watu wenye vigezo vinavyofanana. Wanaolalamika ni wa Serikali Kuu na Idara ya Wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi niungane na wenzangu wote kumpongeza Waziri na timu yake kwa kazi nzuri japo tuna maeneo ya kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, mwezi Februari sikumbuki tarehe nilikuwa na swali hapa kwa Wizara hii kuhusiana na kumomonyoka kwa matumizi ya lugha ya kiswahili ambako kwa kweli kunakithiri na pia hali ya kuchanganya lugha. Imefikia hatua hivi sasa kwenye vyombo vya habari msanii ama mtu yeyote ameitwa pale anazungumza Watanzania wote wanasikiliza, watoto wanaojifunza afadhali sisi tayari tulishapa misingi, unasikia anasema nyimbo hii niliitunga mwaka jana, mwingine anasema, tena watangazaji wa soka wale, kwa mfano anasema timu ya Lipuli imetoka sare na timu ya Polisi kwa hiyo wameshindwa kupata matokeo. Wakati tunafahamu kwamba matokeo ni ama kushinda ama kushindwa ama kutoka sare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna maudhui yanabadilishwa ambayo kwa kiwango kikubwa kwa hawa watoto ambao wanakua sasa tunashindwa kujua tunawafundisha hii version mpya ya kiswahili ama tunaendelea na ile ya kwetu? Wakati huo huo Waziri kwenye ukurasa wa 25 anaongelea kiswahili kuwa bidhaa, ukurasa mwingine sikumbuki anasema ni lugha ya kumi katika lugha 6,000, hizo zote ni sifa ambazo zitakamilika endapo tutakuwa na jitihada za dhati za kutunza kiswahili.

Nafahamu kwamba kwenye kukua kwa kiswahili katika maeneno mapya yanayokuja nayo ni sehemu ya kukuza lakini iwe guided. Naamini kuna wataalamu wetu ambao wanaweza kutuongoza ili hata sisi ambao walau tunajua kile tulichofundishwa miaka hiyo tufahamishwe rasmi sasa kwamba imebadilishwa siku hizi ni nyimbo hii sio wimbo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri wakati ananijibu mwezi Februari alisema kuna sera inakuja nikafurahi sana. Nilitarajia hotuba hii isheheni hiyo mikakati ya sera na iongelee kwa uzito kwa sababu hili jambo linakera.

Tunaomba tuzungumze kiswahili fasaha ili hiyo habari kwamba ni bidhaa, ni lugha ya kumi kweli iwe na tija vinginevyo tutaishia kuiandika tu hapa, hiyo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, siku moja nilihudhuria mechi ya soka ya Simba na nafikiri ni Polisi Morogoro ilikuwa mwaka jana au mwaka juzi sikumbuki vizuri na mabadiliko hayajafanyika. Lile gori la uwanja wa Jamhuri Morogoro upande wa Polisi nafikiri ni Kaskazini, goalkeeper akidondoka kuna shimo pale unaweza usimuone tena refa anaweza akamtafuta. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapo ndipo tunatoa klabu bingwa ya Tanzania ikacheze na National Al-Ahly, tunajidanganya. Core function ya soka ni pale kwenye pitch. Tunazungumza habari ya corporate, ni sawa lakini business kubwa kabisa ya soka ni kwenye pitch. Hivi kwa nini msikae na hizo corporate tukatafuta namna ambavyo kila timu inavyopanda daraja tunaweka mkakati wa pamoja wa kibiashara na kijamii tunapata uwanja, pitch ile hata kama hakuna jukwaa. Huwezi kutoa klabu bingwa kwenye uwanja ule wa Morogoro ambao goalkeeper akidondoka humuoni ikaenda kucheza na National Al-Ahly au Zamalek, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza sana Ndugu yetu Malinzi kwa mambo anayoyafanya, anafanya mazuri tu lakini yako ya msingi. Kwa mfano, amezuia hapa juzi, kuna watu walitaka kuleta fujo, mpira unachezwa uwanjani, ukishindikana mezani, ukishindikana maandamano, haiwezekani! Acha watu wacheze mpira uwanjani, wewe simamia, lakini Malinzi rudi kwenye core function mpira unachezwa kwenye pitch tukose majukwaa lakini pale tucheze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye hotuba sikumbuki ukurasa wa ngapi kuna vituo 56 vitaanza vya kukuza soka la watoto, tuondokane na hii Dar es Salaam, Mwanza na Arusha syndrome. Kuna wachezaji wa mpira kutoka maeneo mengine kwa mfano Biharamulo kuna vipaji.

Waziri atuhakikishie namna gani ata-distribute tupate kituo Biharamulo, Mtwara na sehemu nyingine habari ya Dar es Salaam, Arusha achana nayo, vipaji vipo vijijini. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye suala la sanaa, nimesoma ukurasa fulani hapa unasema kwenye kukuza sanaa lilifanyika kongamano/warsha Kisarawe kwenye shule moja. Jamani lazima tuangalie coverage, tukisema hili ni tukio moja Kisarawe halitatusaidia kuna mambo hayahitaji hata bajeti. Hivi tukihakikisha kwenye curriculum ya shule ya msingi kuna siku moja kwa wiki au kila baada ya wiki mbili, mwalimu mmoja ametengenezwa vizuri anawaandaa watoto wanacheza ngoma za kienyeji, anafanya tathmini, anawaelekeza, hakuna bajeti ni wale wale. Kwa hiyo, tutafute coverage kubwa siyo lazima kila wakati bajeti ni pesa kuna bajeti ya muda tu na bajeti ya kuandaa walimu kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya soka, pia kuna habari ya UMISETA. Wakati huo UMISETA ilikuwa inatengeneza watu kwa sababu nguvu kubwa ilikuwa inawekwa sasa hivi tunaisikia UMISETA passively yaani unaisikia juu juu tu. Ndiyo maana hata hawa akina Samatta wanatokea kwa ajali tu, hata hawa Serengeti Boys kama alivyosema msemaji mmoja aliyetangulia ni ajali. Kuna hatari ikawa wanatoka huko amepata sifa kubwa TFF kazi wameifanya, lakini baada ya hapo hutaona jambo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa habari ya kwenye ligi kuu ya soka kama alivyosema msemaji mmoja aliyetangulia. Tutafute namna gani ya kulinda vipaji vyetu, wazo limetolewa hapo, tuhakikishe kwa mfano kwenye first eleven katika dakika zote tisini kuna walau under twenty wa Tanzania kwenye kila mechi inayochezwa ya Ligi ya Vodacom. Amesema Mbunge mmoja hapa naomba kusisitiza, hiyo ndiyo namna ya kulinda. Pia tutafute namna ambavyo hata wale wachezaji saba waliosajiliwa kutoka nje ya nchi tuwalete ili watuongeze nguvu ligi yetu iwe na mvuto zaidi, lakini sio lazima wote watano wawe kwenye mechi moja, uwa-limit kwamba wale wageni kuna limit fulani ili wa ndani nao wapate fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, mchango wangu ni huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa kwenye Mabaraza ya Ardhi, Vijiji na Kata, ni vurugu na mambo ya ajabu. Mfano, hukumu inampa ushindi mtu kwa kuwa alileta mashahidi wengi kuliko upande wa pili. Wananchi wanazungushwa sana katika rufaa hawapewi hukumu mpaka anakata tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeruhusu makampuni binafsi ya upimaji waweze kushirikiana na Halmashauri zetu kibiashara/Huduma. Watendaji wa Halmashauri bado hawataki kushirikiana na Makampuni hayo mfano ni Halmashauri ya Biharamulo. Tunaomba uharakishwaji wa utatuzi wa migogoro mikubwa ambayo nimeorodhesha tayari. Mfano Mgogoro wa Jeshi na Kijiji cha Rwebya unasumbua sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kutupa afya, nawashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kutoa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri na timu nzima, kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kwa hiyo nafahamu kwa kina nini kinaendelea. Anafanya kazi nzuri ingawa ni wazi lazima tupate maeneo ya kusema ili kufanya kazi iwe nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na pongezi. Pongezi ya kwanza ni kuhusiana na ujenzi wa nyumba za walimu. Biharamulo kwenye shule zenye mazingira magumu nimepata shule mbili, Shule ya Sekondari Katahoka ujenzi unaendelea, Shule ya Sekondari Nemba tumepata mgao lakini naona kuna kuchelewa kidogo, naomba tufuatilie ili tuende kwa kasi. Lakini naomba tuzitazame shule nyingine mbili moja ni Nyakahura Sekondari mpakani kabisa kule na Ngara na Karenge Sekondari hali yake ni mbaya sana. Tunashukuru kwa tulichopata, lakini tunaomba tuzitazame hizo mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, napenda kupongeza suala moja ambalo ni la Kitaifa, hili la Bodi ya Mikopo. Ukiangalia takwimu zinaonesha kabisa mwaka 2015/2016 mwaka ambao Serikali ya sasa iliukuta tayari umeanza, urejeshaji wa mikopo ulikuwa shilingi bilioni 32, lakini 2016/2017 tukaenda shilingi bilioni 116; 2017/2018 tumekwenda shilingi bilioni 130. Ni kazi nzuri kwa kweli, inaonesha kabisa namna gani tunafanya kazi nzuri kwa upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba naomba tutafute namna ya kimkakati zaidi ya kuweza kuboresha zaidi kwenye eneo hili kwa sababu tumeshaonesha tunaweza. Nadhani inawezekana kabisa tukaondoka kwenye Bodi ya Mikopo tukaibadilisha ikawa Higher Education Loan Fund ili ubunifu ukae vizuri zaidi na mianya ya kutapakaa na kuwa na mambo mengine ya kufanya zaidi kuweza kusimama yenyewe iweze kuwa mingi zaidi na wawe na ile autonomy ya kutosha zaidi watafanya kazi vizuri. Hili ni eneo ambalo kwa kweli napongeza lakini tutafute namna ya kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie habari ya ubora wa elimu nikihusianisha na hii habari ya shule za Serikali na shule za binafsi. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbatia, ameisema vizuri sana leo muda mfupi uliopita, kwamba jamani hizi shule zote ni za kwetu na zote zina mchango wa kutosha kwenye kutoa elimu ya nchi hii kwa watoto wetu. Kwa hiyo, tuna wajibu wa kuwasikiliza na kuwasaidia lakini pia tuna wajibu wa kuwasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na upande wa kuwasikiliza. Ilitokea mjadala mwaka jana nakumbuka na wote mnaukumbuka wa habari ya shule za private hizi, wanatoa mitihani mtoto anapotaka kutoka kidato kimoja kwenda kingine, mitihani ndani ya shule na wanaitumia kama kigezo cha kumwambia asiendelee ama arudie. Ni wazi nakubaliana na msimamo wa Serikali, kwamba tukilifanya jambo hili kiholela itakuwa ni hatari, kwamba haujui, huwezi kupima kwamba shule “X” imetumia kipimo gani na shule “Y” imetumia kipimo gani, ni vizuri tukawa na kipimo kimoja ili tuweze kujua nani anafanya nini na kwa manufaa yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili, naiomba Wizara pia kuacha bila kupima nayo ni hatari, tutafute namna ambayo kila mtu asipime kiholela, lakini tuwe na namna ambayo tunawapima hawa watoto wajue kwamba nisipofanya bidii nitashindwa kutoka kidato cha kwanza kwenda cha pili na ule umri mnafahamu ni umri ambao bado wako kwenye hali ambayo wengine hawajielewi, kama hatuna namna ya kupima tunawaacha kiholela, matokeo yake ndiyo tunapata matokeo mabovu sana huko mbele, kwa hiyo naomba hilo Serikali tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili ni upande wa kuwasimamia. Mimi nina mawili, mtanisamehe wenzangu ambao kwa bahati nzuri ama mbaya ni wamiliki wa shule, nalisema hili kwa nia njema tu. Kuna hili suala la shule inachagua watoto kwenda kidato cha kwanza kutoka darasa la saba “A” zote ili matokeo ya kidato cha nne yakitoka ionekane yeye alifaulu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijawahi kuona hospitali ambayo Mheshimiwa Waziri naona hanisikilizi, sijawahi kuona hospitali ambayo mtu akienda daktari anaangalia anasema wewe ninavyokuona unachechemea naomba hapa usije kabisa unaweza ukafia hapa! Ni kazi ya hospitali kwenda kuchukua mtu hata aliye hoi kwa sababu ni kazi yako kutibu.

Sasa kazi ya shule ni kufundisha watu, naomba tuwe na utaratibu ambapo katika watoto mia unaotaka kuchukua wewe shule ya private, chukua 30 cream, chukua 30 wa kati, chukua 40 siyo waliofeli kabisa lakini ile ngazi inayofuata, waliofeli kabisa tuwaache, lakini tuwe na namna tuchanganye ili hata ukija kusema umefaulu tunajua ulifanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tunakupa wenye “A” zote halafu unakuja unasema mimi nimekuwa wa kwanza, tutafute utaratibu, tuchanganye ili tupime kwa usawa na kila mmoja apate fursa ya kufundishwa. Vinginevyo na hospitali nazo ukienda unachechemea zaidi unaambiwa wewe usiingie bwana utatufia hapa ni kazi yao kukutibu, wakishindwa watakupeleka mahali ambapo kuna ujuzi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kusimamia kwenye hizi shule za private ni habari ya likizo. Mtoto humuoni mwaka mzima wanasema mwezi wa sita hawaji, mwezi wa 12 hawaji, haiwezekani, hata kuja kusalimia wazazi ni sehemu ya shule. Hebu angalia shule za Seminari za Katoliki, wale ukikutwa unasoma saa ya michezo unafukuzwa kwa sababu unafundishwa kutumia muda wako wa kusoma vizuri ili muda wa kula uutumie vizuri, muda wa kucheza uutumie vizuri, lakini ndiyo wanaongoza kufaulu kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna shule yaani mtoto haonekani mwaka mzima wanasema wana masomo maalum! kuja nyumbani kuzungumza na wazazi ni sehemu ya shule, tunaomba usimamie Mheshimiwa Waziri, hizi shule zote ni za kwetu, tusimamie wasome, saa ya kucheza wacheze, saa ya kula wale, saa ya kusoma wasome, likizo waje nyumbani, ni sehemu ya shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongelea pia ukurasa wa 112, ameongelea Chuo cha Mkwawa, kuna shilingi bilioni mbili pale inapelekwa kwa ajili ya maabara ya kompyuta na vitu kama hivyo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kama nilivyosema, nimeshuhudia mwaka huu tumekwenda Mkwawa pale. Serikali imepeleka pesa pale ya kujenga ukumbi wa mikutano lakini mambo yanayoendelea ni maajabu ni ubadhirifu mtupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tubadilishe namna ya kusimamia pesa hizi. Tutakuwa tunafurahi hapa kwamba imekwenda bilioni mbili lakini kama usimamizi haukai vizuri mwisho wa stori ni kutumbua watu kutafuta nani ameiba ambayo haitusaidii, tutafute namna ya kusimamia kabla hazijaibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu lakini nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wake wote kwa kuandaa bajeti lakini kwa kufanya kazi nzuri. Kuna maeneo yenye upungufu, lakini natambua kuna kazi imefanyika vinginevyo Taifa lingekuwa limesisimama kabisa. Kwa hiyo, nawapongeza kwa kazi iliyofanyika lakini nitasema maeneo yale ambayo hayako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, langu la kwanza mahsusi ni wigo wa walipa kodi, ndipo tatizo langu lilipo. Mwaka 2004, kama siyo 2005, Fernando de Soto’s ambaye Waziri anamfahamu vizuri kuliko hata mimi, alishiriki kuandika MKURABITA, alisema zaidi ya asilimia 90 ya shughuli za kiuchumi kwenye nchi hii zinafanya kazi nje ya sheria na shughuli za kijasiriamali asilimia 98 zinafanya kazi nje ya sheria na mbili tu ndiyo ziko ndani ya sheria. Alisema pia mali zetu kama ardhi na vinginevyo, asilimia 11 pekee ndiyo ziko ndani ya mfumo, kwa hiyo, ndiyo zinalipa kodi. Kwa hiyo, tuna wigo mkubwa sana wa mali na shughuli za uchumi ambazo ziko nje ya sheria hazilipi kodi. Kwa wakati huo alithamanisha shughuli za kiuchumi na mali ambazo ziko nje ya uchumi na hazilipi kodi, ilikuwa ni karibu mara kumi zaidi ya pesa yote ya nje, Direct Foreign Investment inayoingia nchi hii toka tumepata uhuru mpaka mwaka huo. Unaona kwamba ni uchumi mkubwa sana uko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilileta hili kwa muktadha wa sasa, nakumbuka tarehe 25 Machi, kama sikosei, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akiwa Morogoro, moja ya kauli zake alikuwa anawakemea TRA kufanya kazi kwa kuwa- harass wafanyabiashara. Naamini kabisa na ni wazi hakuwa anazungumza hivyo kwa maana ya kwamba tusikusanye kodi, lakini ukitafsiri hiyo ni kutafuta namna gani watu walipe kodi lakini wigo uwe mpana, tutafute kupanua ili watu walipe kiwango ambacho kila mtu anakimudu na kwa sababu ni wengi, tutapata tija zaidi kwa maana ya kodi na hakutakuwa na haja ya kukimbizana. Hiyo ndiyo tafsiri rahisi kabisa ya alichokuwa anakisema Mheshimiwa Rais. Sasa nikawa nafikiri hebu tujikite kwenye kutanua wigo wa kodi, ndiyo moja ya matatizo makubwa yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mmoja umetokea juzi hapa, mimi nimetafakari sana hii habari ya kupima samaki kwa rula. Nikawa nafikiri hivi habari ya samaki, ni kweli tunahitaji kusimamia sheria kwamba samaki wavuliwe pale ambapo wana viwango lakini hii habari ya kutanua wigo wa kodi na kusimamia sheria kwenye sekta mbalimbali tunahitaji kuviweka kwenye muktadha sahihi wa kila sekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nafikiri njia rahisi ni kutafuta namna ya ku- balance kati ya ufugaji wa samaki ili isaidie, watu wasijikite zaidi kuvua kwenye maziwa na bahari, wavue huko wanakofuga. Hii itakuwa imetibu mambo mawili; amezuia kila mtu kwenda kule lakini ameanzisha ajira ambako tutapata kodi, watu familia zao maisha yatakwenda na tutapata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata habari ya mifugo, tumepiga kelele sana watu wa Kanda ya Ziwa. Nilisema na ninasema tena. Mimi sio mmoja kati ya watu wanaotetea mifugo wakae hifadhini lakini ni mmoja wa watu ambao sielewi kuwaondoa tu hifadhini ili kukidhi sheria, lakini hatutumii hiyo fursa kubadilisha hii mifugo ikawa ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kuna habari hapa imesemwa ya kugonga wale ng’ombe mihuri, nafikiri Mheshimiwa Rais wakati anatoa agizo hilo alikuwa analenga ni namna gani tujipange. Siyo lazima tukae kwenye kugonga mihuri, kwanza tunaharibu ile ngozi, tunapunguza thamani. Teknolojia sasa hivi iko juu, tena hapa hapa Tanzania, ukienda Sokoine tu hapo, Chuo Kikuu cha Kilimo, ng’ombe anamezeshwa chip, anatembea na chip yake, ukikaa kwenye kompyuta unamwona, unawahesabu ng’ombe 8,000 wako Biharamulo, akifa au akichinjwa unaona taa imezimika, unampa Afisa Ugani wako namna ya kudhibiti wa kwake, unajua nani kachinjwa, nani hajachinjwa, ni rahisi. Hebu tutafute ubunifu ambao utadhibiti watu wasiwe na ng’ombe wengi, lakini umedhibiti na umeweza kurasimisha na kutengeneza ajira na wigo wa kodi. Tupanue wigo wa kodi Mheshimiwa Dkt. Mpango, tatizo langu liko hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye habari ya upangaji wa mipango yetu, haikai vizuri sana hapa, ingekaa kwenye Wizara ile ya Mipango, lakini ngoja niiseme ataona atakavyoiunganisha, ni habari ya sensa. Sensa yetu ndiyo inayotupa idadi ya watu ili kujipanga. Inafahamika duniani na hata sisi tunafahamu na Waziri anafahamu sensa ina upungufu, tena hasa ya kwetu ambayo mara nyingi kuna watu wanakimbia kwa sababu tofauti tofauti, tunashindwa kupata idadi kamili. Sensa iliyopita inasema Dar es Salaam ni watu milioni tano, lakini kwa hesabu ya kawaida tu, hata ukikaa ukiangalia, pale siyo milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, watu wa NIDA wanaoandikisha vitambulisho vya Taifa, ukiangalia idadi ya namba waliyoandikisha mpaka sasa Wilaya ya Temeke peke yake ambayo wanaanzia umri wa miaka 18 kwenda juu na tukikumbuka demografia inasema kwamba umri wa miaka 18 kwenda chini ndiyo watu wengi, ndiyo base, ukilinganisha idadi hiyo ya umri wa miaka 18 kwenda juu na idadi ya sensa inayosema kwa Temeke, ni vitu viwili tofauti. Tutafute tuwe na idadi sahihi ili tuweze kutekeleza mipango yetu na majibu yapo hapa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Machi, 2018 nilikwenda Mkoa wa Songwe kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa pale. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe ametengeneza Daftari la Wakazi la kielektroniki, mnaweza ku-check hata kesho, akikaa mezani anaweza akabonyeza button anakwambia leo wanafunzi ambao hawakwenda shule watoro ni wangapi, siku hiyo hiyo real time. Mkoa wa Songwe, nchi hii, siyo nchi nyingine. Hebu tutafute namna gani twende tujifunze pale, watu wa NBS wakae watazame…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. OSCAR R. MUKASA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI:
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, kwa mara nyingine na kwa uendelevu, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii tena, lakini nakushuru pia kwa kutuongoza vizuri hapa na kwenye kazi zetu zote za kila siku.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wachangiaji wote waliochangia taarifa yetu. Wachangiaji kwa ujumla walikuwa 35 lakini waliogusia taarifa yetu ni wachangiaji 10 ambao ni utashi mkubwa kabisa wa kisiasa kuonyesha kwamba Bunge letu wanatoa kipaumbele kabisa kwenye masuala ya UKIMWI ndiyo maana wametoa michango kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee pia nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wamezungumza; wamezungumza vizuri sana, unaona kabisa utashi wa kupokea kwa kufanyia kazi mapendekezo yetu mara pale ambapo yatakuwa yamepokelewa na Bunge lako Tukufu kwamba ni maazimio ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa namna nyingine tena naishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Tunaposema Serikali, tunamshukuru Mheshimiwa Rais na timu yake nzima, kwa sababu takwimu zinasema, preverence ya kwanza kabisa ya masuala ya UKIMWI nchi hii nafikiri ni mwaka 1992 au 1995, utanirekebisha, ilikuwa ni asilimia 7.2, lakini leo tunaongelea asilimia 4.7. Maana yake ni kwamba, pamoja na kwamba kazi bado ni kubwa mbele yetu, lakini kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia, lakini kuna jambo moja ambalo ni vizuri tuliweke sawa ili tuwe na uelewa wa pamoja. Kuna Wabunge wamechangia vizuri sana kuhusu Mfuko wa Taifa wa UKIMWI, lakini unasikia kwenye maneno yao kuna mwelekeo wa uelewa kwamba kazi ya mfuko wa UKIMWI ni kwenda kuwalinda tu wale ambao wameambukizwa, lakini kumbe kuna Majimbo mawili hapa kwenye habari ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni asilimia 4.7 ambao wameshaambukizwa; hawa tunataka tuhakikishe maisha yao yanaendelea kuwa mazuri kiafya, kiuchumi na kijamii, lakini kuna asilimia 95 ambayo haijaambukizwa, hawa tuna kazi ya kuwalinda wasiambukizwe. Kwa hiyo, kuna hizi constituency zote mbili. Kwa hiyo, mtazamo wetu wa mapambano ya UKIMWI ni vizuri ukaenda kwenye Majimbo yote hayo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nilitaka nigusie Sheria ya UKIMWI kwa ufupi tu. Wamesema vizuri Mheshimiwa Waziri na unaona utashi wa kushughulika na hilo jambo la marekebisho, lakini niseme kwamba msingi wa kwa nini Kamati na sauti ya jamii inaomba marekebisho haya, misingi ni miwili mikubwa. Msingi wa kwanza ni takwimu kwamba maambukizi mapya ya UKIMWI kwa sasa kwa mujibu wa takwimu zetu wenyewe asilimia 40 iko kwa vijana wa miaka 15 mpaka 24 na miongoni mwa hao, asilimia 80 ni vijana wa kike. Kwa hiyo, huko ndiko maambukizi yapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bila kujali kwamba kuna habari ya migongano ya sheria, wameolewa na nini, lakini ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya maambukizi yako kwa vijana wa umri ule. Kwa hiyo, ni muhimu sana twende kutazama kule kuna nini? Kwa hiyo, huo ni msukumo wa kwanza wa marekebisho ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msukumo wa pili ni msukumo wa dunia kwa ujumla. Sasa hivi wanasema 90, 90, 90 na Tanzania pamoja na kazi nzuri ya kutoka preference ya asilimia 7.2 mpaka 4.7 sasa, lakini bado kwenye 90 ya kwanza hatufanyi vizuri, tuko asilimia 52. Kuna uwezekano ikafika 62 kwa sababu ya mambo ya kitakwimu yanafanyika, tutapara report hivi karibuni. Kwa hiyo, asilimia 52 bado haitoshi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, duniani huko watu wamechukua measure mbili kubwa; umri, kwamba watu wenye umri ambao maambukizi ni makubwa waingizwe kwenye kupima kwa hiari, lakini na self testing. Kwa hiyo, tuna misukumo miwili mikubwa ambayo ni muhimu tukaenda nayo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, misukumo hii inakuja na jambo lingine kwamba tuna kazi ya kuhakikisha kwamba Mfuko wa Taifa wa UKIMWI unaanza kusimama wenyewe. Ni kweli ni kazi ambayo haiwezi kukamilika ndani ya miaka michache lakini ni muhimu kazi hiyo ianze. Mfano, ni kwamba kuna taarifa zisizo rasmi lakini kwa bahati nzuri zitakuwa rasmi hivi karibuni; hivi tunavyozungumza wafadhili wanakwenda kupunguza asilimia 23 ya pesa ya UKIMWI inayokuja nchi hii kwa sababu yoyote ile, lakini ni kwamba zinakwenda kupungua. Kwa hiyo, huu ni msukumo ambao unatufanya tunahitaji Mfuko wa ATF upate tozo maalum uweze kusimama wenyewe, vinginevyo tutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano hapa; duniani huko, kuna watu wanafanya endowment fund. Sasa hivi pesa yote ya UKIMWI inayokuja nchi hii, asilimia 60 inakwenda kununua supplies. Unavyosema supplies ni sindano, gloves, na kadhalika. Yaani vifaa vya kusaidia mapambano dhidi ya UKIMWI. Asilimia kubwa ya vifaa hivyo ni vile ambavyo tukiwekeza wenyewe vinaweza vikatengenezwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukitengeneza endowment fund, utashirikisha sekta binafsi, utatafuta hizo pesa za UKIMWI, zinatingia kwenye mfumo wa kiuchumi, kwa hiyo, zitajibu haja ya uchumi na haja ya masuala ya UKIMWI. Kwa hiyo, tunaomba tusisitize sana kwenye ATF na endowment fund ili tuweze kusimama wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Utumishi; Mzee Mkuchika namwomba kwa dhati kabisa, Wizara hii ndiyo ina dhamana ya kusimamia Sheria ya UKIMWI mahali pa kazi. Kuna baadhi ya Wizara tumezungumza nazo, unaona kabisa kwamba mtazamo wa kwamba ni jukumu lao, upo mbali sana, wanadhani ni jukumu la TACAIDS. Kwa hiyo, hapa naoimba tuweke msukumo kwenye Wizara ya Utumishi kuzisimamia Wizara nyingine kwa kazi hiyo, lakini tuboreshe kitengo cha ndani ya TACAIDS ambacho kinapaswa kutazama hizo Wizar nyingine ili waweze kuwasimamia kwa nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Madawa ya Kulevya ni muhimu sana. Sheria inafanya kazi vizuri, tumesikia mifano hapa, ni mfano Tanzania kwa maana ya utekelezaji wa sheria, lakini sheria ambayo inafanya kazi nje ya sera ni wazi itakuwa na upungufu. Tunaomba ile kasi iongezwe ili jambo hilo lifanyike mara moja halafu tumalizane nalo na kasi iwe kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako Tukufu likubali maazimio yetu kwamba ni maazimio ya Bunge ili baada ya hapa sasa Serikali ipate maelekezo ya kufanya kazi kwa kasi na nguvu zaidi kwa ajili ya kupiga hatua.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa namna ya pekee namshukuru Mungu kwa nafasi hii na nawapongeza Wenyeviti wote wawili wa Kamati hizi kwa kazi nzuri kabisa. Kimsingi kwa kiwango kikubwa sana binafsi nakubaliana na mapendekezo yao lakini nina mambo machache ya kuchangia. Miongoni mwa mambo ambayo kwa upande wangu, naona ni mafanikio ya juu kabisa ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli toka imeanza, ni lile jambo la uchumi jumuishi. World Economic Forum ilitangaza Tanzania kwamba ndio nchi inayoongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi kwa mwaka 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa kwamba ni uchumi ambao mbali ya kujali saizi yake au unafanyaje kazi, kwa uzuri kiasi gani, unajumuisha watu wengi wa makundi yote kwenye nchi husika, hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulileta kwenye muktadha wa leo, juzi tarehe sita nilimsikia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli akisihi mahakama zetu mhimili wa mahakama, kwamba sasa wakati umefika wa kuanza kuhakikisha kwamba sheria zetu sasa zinaandikwa na kufanyiwa kazi kwenye mahakama kwa lugha ya Kiswahili. Kwa nini naona hilo ni jambo zuri, mtafiti mmoja amefanya utafiti mwaka 2014 hapa Tanzania anasema miongoni mwa Watanzania milioni 54, asilimia 90 wanaongea Kiswahili na asilimia nne wanaongea Kiingereza nne tu na waliosalia ndio wanaongea zile lugha za kienyeji kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria yetu ya Tafsiri za Sheria kifungu cha 84 kina vifungu vitatu, cha kwanza kinasema the language of the laws of Tanzania shall be written in English or Swahili, kwamba itakuwa kwa Kiingereza ama Kiswahili na pale ambapo hizo version mbili zinagongana, ile version ambayo ndio original sheria ilitengenezwa kabla ya kutafsiriwa ndio itatumika, lakini pale ambapo zilitungwa zote kwa pamoja Kiingereza kitapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo swali langu ni kwa nini tunapambana kujiondoa kwenye utegemezi wa mambo ya kiuchumi na mengine lakini hatutaki kuondoka kwenye utegemezi wa mambo ambayo yanatupa nafasi ya wananchi wetu kushiriki vizuri pale wanapotaka haki zao, kushiriki vizuri pale ambapo wanatakiwa kujieleza, kushiriki vizuri pale ambapo hata kama anasimamiwa na Wakili mahakamani, pamoja na kwamba hana uwezo wa kufanya tafsiri ya kisheria, lakini angalau awe na fursa ya kuelewa Wakili wake anasema nini mwenendo wa Wakili wake unakwendaje kwa maana ya hoja. Hiyo inakuwa ni sehemu ya kupata ile haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 71 ya Katiba ni mfano ambapo kifungu kile kinatoa masharti ya ni namna gani mtu atapoteza nafasi ya Ubunge. Kuna tofauti kwenye version ya Katiba ya Kiingereza na ya Kiswahili, ambapo kifungu ambacho kinasema kwamba yoyote ambaye
samahani niangalie kidogo hapa, kifungu (e)Iwapo Mbunge atachaguliwa ama kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais ni moja ya masharti ya ibara hiyo kwamba atapoteza Ubunge, lakini version ya Kiingereza ya ibara hiyo inaongea kitu kingine. Kwa hiyo suala hili limeshatokea mahakamani, ukatokea mtafaruku, sio mtafaruku wa maana ya kukosea nini kinasema pale, lakini mtafaruku wa maana kwamba kilichoandikwa upande huu ni tofauti kabisa na kilicho upande huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahakamani wanatoa haki ya Katiba ya Kiswahili kwamba ndio iwe ya kwanza kufanyiwa rejea kabla ya ile ya Kiingereza kwa sababu Katiba yetu ilitungwa kwa Kiingereza kama version ya kwanza kabla ya kutafsiriwa. Ushauri wangu niiombe Serikali hebu tufanye mabadiliko tulete hadhi ya lugha yetu, lakini na fursa ya watu kushiriki kwenye haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, katika ukurasa wa 41 wa ripoti ya Kamati ya Katiba na Sheria, wanasema moja ya mapendekezo yao ni usimamizi wa utoaji haki nchini kwamba ni jambo la muhimu sana na wameeleza pale. Nimewahi kushuhudia Biharamulo miongoni mwa mahabusu ambao wamewekwa gerezani pale kwa muda mrefu kabisa, nilipata fursa siku moja nikaingia gerezani pale, nikazungumza na baadhi yao kila mmoja akasema jambo lake. Nikagundua kwamba kulikuwa na mambo ambayo mengine hata sikuwahi kudhani kama yako dunia hii, lakini nikachukua fursa nikamwomba Waziri wa Sheria wakati huo Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alifanya kazi nzuri sana akaja na DPP pale wakasikiliza watu kwa siku moja tu, kuna mahabusu 40 waliondoka mle gerezani kwa sababu ukaaji wao mle ulikuwa kwa kweli huko kinyume cha sharia, wengine hata zile hati za kuwafutia mashtaka zimeshatolewa miezi sita iliyotangulia lakini watu wako mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwe na utaratibu mbali na hii ambayo Mbunge anaweza kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Sheria na DPP kwenda, tuweke utaratibu wa kimfumo wa kuhakikisha tunaweza tukafanya checks and balances za mambo kama haya kwa sababu kuna watu wako kule chini hana mahali pa kusemea, anaminywa haki yake, anakaa miaka miwili, mitatu bila sababu ya msingi na ushahidi Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe nilikwenda nae katika Gereza la Biharamulo, waliondoka watu 40 kwa yeye na DPP kukaa na kuwasikiliza watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya Kamati ya Sheria Ndogo, katika ukurasa wa sita yapo mambo ambayo wanalalamika, wanasema kumekuwa kuna tatizo la sheria ndogo kwenda kinyume na sheria mama au sheria nyinginezo za nchi, lakini kuna matatizo ya sheria ndogo kuwa na makosa ya uandishi, matatizo ya sheria ndogo kutozingatia misingi ya uandishi, kwa mfano hansard zinaonesha wamewahi kupata report ambayo sheria mama inasema kosa fulani adhabu yake ni shilingi 100,000, sheria ndogo kule imekwenda imefanya kitu kwenye muktadha ule unasema 300,000 kwa sababu ya makosa ya uandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo unaweza kuona ni kosa la uandishi kwenye karatasi, lakini huko kwenye field haya mambo yanaumiza watu. Tunaomba tujue namna gani Wizara inayohusika watachukua hatua kwa sababu kumbukumbu za Bunge zinaonekana kwa Kamati hii haya ni malalamiko ambayo yamekuwa yanajirudia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru na naunga mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuturuhusu kufanya hii shughuli leo, lakini nitumie fursa hii kuendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kunipa imani na kunivumilia kwenye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka niipongeze Serikali, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya, lakini kwa maana ya bajeti hii, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anayoifanya, Mheshimiwa Jenister, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Manaibu wao; Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa, hongereni sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo mawili; Sekta ya Afya kama iliyoelezwa kwenye kitabu cha hotuba ukurasa 56 mpaka 62, lakini nitagusia kidogo suala la UKIMWI na mwishoni nitaja mambo mawili matatu yanayohusu Biharamulo mahususi ambayo mengine ni dharura na mengine ambayo yamekuwa yanatusumbua kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 56 mpaka 62 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu, kinaongelea Sekta ya Afya na kuna mahali kinasema vizuri kabisa kuhusu mafanikio ambayo nimeyapongeza na ninaendelea kuyapongeza. Kwa mfano, miundombinu ya huduma za afya kumeongeza vituo vya tiba kutoka vituo 7,678 mpaka vituo 8,119. Maana yake ni kwamba tunaendelea kupeleka huduma za afya kwenye maeneo ambayo zinaweza kutolewa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu kwenye hilo, twende mbali zaidi. Ukisoma ukurasa huo wa 56 mpaka 62 ingawa kichwa cha habari kinasema “Afya”, lakini kwa kiwango kikubwa tumejikita kwenye tiba, ambapo tiba tunaihitaji, lakini tunahitaji sana kwenda kwenye afya kwa ujumla. Afya inaanzia kwenye kuzuia/kukinga lakini kuelimisha watu ili hata hayo mahitaji ya Vituo vya Afya na vifaa tiba, hata kama yanaongezeka yasiendelee kuongeza kwa kasi, ifikie mahali sasa tunashughulika na tiba kwa wale ambao wanaumwa, lakini kwa kiwango kikubwa tunazuia watu wasiugue. Kwa namna hiyo tutakuwa tunatumia zaidi pesa yetu inayozalishwa na sekta nyingine za uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hapa kitabu cha ikama ya Wizara ya Afya wanaita Staffing Level for Ministry of Health and Social Welfare kwa 2014 - 2019 ndiyo kinatumika mpaka sasa. Wameweka pale Staffing Level kwa ngazi ya zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukiangalia pale, karibu asilimia 80 ya watumishi ambao wamewekwa pale kwenye Kituo cha Afya ni watumishi wa tiba. Mtumishi wa Kinga ni mmoja tu, wanamwita Community Health Worker or Social Welfair Assistant ambapo hao wengi wote wa tiba wanaelekezwa kabisa, kwa mfano, Clinical Officer anaambiwa kwa siku ataona wangonjwa 40, Mphamasia anaambiwa kwa siku atafanya prescription 40 na Nesi anaambiwa kwa siku ataona wagonjwa 30. Huyu mtu, Community Health Worker kazi yake anaambiwa to link person between community and the dispensary. Hata ile dhana ya kwamba sasa huyu naye anapaswa tumwekee kipimo kwamba kwa siku atatembelea nyumba kadhaa ahakikishe kuna sehemu ya kunawa mikono, kaya zina vyoo na mambo kama hayo ili nguvu yetu iwe kwenye kinga zaidi kuliko tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Afya ili iweze kuleta majibu kwa maana ya afya kwa ujumla, mapendekezo yangu ni kwamba sasa taratibu tuanze kuondoka kwenye kuwekeza tiba peke yake, tuanze kwenye kinga. Nafahamu kwenye upande wa kinga, kwa mfano, upande wa chanjo tunafanya vizuri sana. Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimeshafika zaidi ya asilimia 95 kwenye kuchanjwa watoto wetu. Vile vile kuna kinga za magonjwa mengine kama ya kuhara, magonjwa mengine ambayo yanasabishwa na tabia tu za wananchi kule vijijini, hatujawekeza vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ule mzigo wa magonjwa kwenye zahanati zetu, ukiangalia burden of diseases profile, utakuta kuna sehemu kubwa ni magonjwa ya kuambukiza ambayo yanazuilika. Malaria ni wazi hilo ni tatizo la Kitaifa, lakini unakuta magonjwa ya kuhara kwenye zahanati yanachukua namba mbili ama namba tatu. Kwa hiyo, mzigo ni mkubwa sana, ni magonjwa ambayo ukielimisha watu tu kidogo, akanawa mikono kabla kula, akanawa mikono baada ya kula, akahakikisha kuna choo kizuri, ule mzigo utapungua na ile nguvu ya pesa tutaipeleka kwenye maeneo mengine ambayo ni ya uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee UKIMWI. Tuna tatizo mpaka sasa kwamba asilimia 93 ya pesa ya mwitikio wa UKIMWI kwenye nchi hii ni kutoka kwa wafadhili. Tumesikia hivi karibuni, wametanga wenzetu Wamarekani kwamba asilimia 23 ya fedha hiyo inaondoka kwa mwaka huu. Ambapo ukiipeleka kwenye thamani ya fedha Kitanzania ni shilingi bilioni 282. Ni fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri tuendelee kuwa tegemezi, lakini namna nzuri ya kujitoa kwenye utegemezi ni kuanza kuwekeza kwenye mfuko wetu wenyewe, Mfuko wa AIDs Trust Fund. Uwezo huo tunao na mifano tunayo, tumefanya hivyo kwenye REA, tumefanya hivyo kwenye maeneo mengine, tutafute namna kukanza kusimama…

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji kwamba badala ya kuongeza bajeti kwenye UKIMWI ashauri wananchi waache uasherati. (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mukasa.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa naiachia kiti, kitaona inaendaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mifano kwamba Tanzania kwenye baadhi ya maeneo tumeendelea kusimama wenyewe na jambo hili la UKIMWI ni jambo ambalo linatoa platform, ni jambo mtambuka ambalo linasababisha magonjwa mengine yote ikiwemo TB, Hepatitis hata Kisukari sasa hivi, mtu ambaye ana tatizo la upungufu wa kinga, anakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kufariki kutokana na magonjwa mengine kwa sababu ya kuwa na upungufu wa kinga. Jambo ambalo linahusu maisha yetu tena kwa upana huo ni vizuri sana na ni muhimu sana Serikali ikafahamu kwamba tuanze sasa kutafuta namna ya kusimama wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo matatu ya Biharamulo; moja jana jioni Askari wa SUMA JKT wamemuua mwananchi mmoja wa Kijiji wa Mavota kwa tuhuma kwamba aliingia kwenye eneo ambalo hapaswi kuingia. Naomba Serikali, Waziri wa Nishati kama yuko hapa, Waziri wa Ulinzi watusaidie kuangalia hali kama hii, kama inaanza kujitokeza tena, ni kweli hatuwaambii wananchi wetu wavunje sharia, lakini taratibu za kuwadhibiti pale ambapo wanaonekana wamevunja sheria zinafahamika. Huko nyuma jambo hili lilikuwa kubwa sana, tukalikabili likawa limeisha, lakini sasa inaonekana linataka kurudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee habari ya ulinzi na usalama Biharamulo; jana na wiki kadhaa zilizopita yameanza kurudi matukio kwa kasi ya majambazi kuvamia maduka, majambazi kuteka magari, jambo ambalo lilikuwa linatuathiri siku za nyuma kwa sababu ya sisi kuwa mpakani na nchi jirani ambazo zina watu wanaoingia bila utaratibu likawa limedhibitiwa kwa kiwango kikubwa hasa kwa kuweka kikosi maalum pale Nyakanazi, lakini kwa wiki chache zilizopita inaonekana ile hali ya zamani ambayo ni mbaya inaanza kurudi kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali waangalie jambo hili kwa sababu wananchi wa Biharamulo sasa hali kama ile inavyojirudia kwa kiwango kikubwa, tunashindwa kufanya shughuli zetu za uchumi, tunaishia nguvu zetu zote kuweka kwenye mambo ya kiusalama. Kuna migogoro ya Jeshi na Vijiji, Kijiji cha Rusabya, Kabukome na Kalebezo, nimesikia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi asubuhi analiongelea kwa ujumla, lakini ujumla huo, umekuwa unachukua muda mrefu sana. Tunaomba Serikali, hizo Wizara zimepewa kazi ya kwenda kutazama, hebu tumalize kazi hiyo, kwa sababu kule wananchi kule wamesimama hawafanyi shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa mara nyingine nampongeza Waziri Mkuu na timu yake, kwa kazi nzuri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kipaumbele cha juu kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa hii nafasi ya kufanya shughuli ya leo. Pia nawashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kuniunga mkono, lakini kwa namna ya pekee napenda kuipongeza Serikali, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye Sekta hii ya Afya mambo yanaonekana, lakini Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile na wasaidizi wenu Katibu Mkuu na wengine wote tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushahidi uko wazi, mimi nitatoa ushahidi mmoja kwamba mkononi kwangu nina ripoti, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Institute for Health Metrics and Evaluation, moja ya mambo ambayo wamepima ni habari ya maternal mortality kwa watoto wa chini ya miaka mitano na infants wale chini ya mwaka mmoja, inaonesha kabisa takwimu ziko wazi hapo kwamba hatujafika tunapotakiwa kufika, lakini tunakwenda vizuri kulingana na matarajio namna wanavyopima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza sana, lakini tumesikia hapa, Mheshimiwa Mbunge mmoja amesema namna ambavyo Wizara hii inapata pesa kidogo ukilinganisha na mahitaji ambalo sio jambo zuri, lakini hata Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Ndugulile na timu yao, kwa kweli wamejitahidi sana kuratibu wadau wengine wa nje ya Serikali. Ndiyo maana mambo mengine yanakwenda, ukipata fursa ya kuwa nao karibu utaona hilo na kweli huwa linanitia moyo sana, naona mwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme mawili ya Biharamulo; moja tunashukuru tumejengewa Kituo cha Afya Nemba, lakini kinaleta mahitaji kwa sasa tutafanya upasuaji pale wa akinamama wajawazito, wale wanaohitaji upasuaji, tunahitaji ambulance, jiografia ya Biharamulo ni ngumu sana kwa sasa tuna Kituo Nyakahura na Nyakanazi ambavyo ni mbali sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, tunahitaji wataalam wengine wa dawa za usingizi, yako matukio kadhaa ya upungufu yanayosababisha vifo vya akinamama kutokana na upungufu wa wale wataalam wa dawa za usingizi. Tuna Madaktari, ama MD mmoja ama wawili, wako kwenye hivyo vituo, lakini kwa sababu watu wa usingizi hawatoshi, mara nyingine ucheleweshwaji inakuwa haiwezekani kufanya upasuaji kwenye Kituo cha Afya na safari ya kwenda Biharamulo Mjini kwa ajili ya upasuaji inakuwa ndefu inasababisha vifo. Hayo ndiyo mahitaji yetu mawili makubwa kwa Biharamulo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije suala la Kitaifa, pamoja na pongezi na kazi nzuri inayofanyika yako maeneo ya kuboresha. Ukitazama ripoti hii hii ya Institute of Health Metrics and Evaluation, inasema kwa mwaka 2017 wamelinganisha 2007 na 2017, hii ni taasisi maarufu sana duniani na inaheshimika, wame-rank wameweka uwiano, wamepanga ule uzito wa sababu za vifo kwenye nchi yetu hii. Katika sababu hizo, ziko ambazo zinatokana na UKIMWI, TB, Malaria lakini hata na magonjwa ya kuhara ni miongoni mwa sababu kumi za vifo ambavyo zinachukua uzito wa juu. Metrics

Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu za vifo, kabla ya wakati, yaani zile pre-mature death wame-rank mambo hapo, kuna tuberculosis, lakini kuna protein energy malnutrition, mambo ya utapiamlo, mambo yanayozuilika kabisa na sababu za ulemavu, inayoongoza kabisa ni dietary iron deficiency na ukiangalia zaidi kwenye ripoti yao wanasema, vifo pamoja na ulemavu kwa pamoja sababu inayoongoza ni malnutrition, utapiamlo, yaani nchi hii tuna tatizo kubwa la utapiamlo, pamoja na kufanya kazi vizuri sana huko kwenye tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa, nijikite zaidi kwenye utapiamlo huo, Sera ya lishe nchi hii, imepitwa na wakati, toka mwaka 1992. Kwa bahati mbaya, ilikuwa inatazama zaidi mchango wa lishe kutoka kwenye Sekta ya Afya, haitazami mchango wa lishe kutoka kwenye sekta nyingine, hili ni tatizo. Tunaomba tufanye mapitio ya Sera, kama asilimia, tatizo linaloongoza kwa habari ya vifo na ulemavu kwa pamoja, namba moja ni utapiamlo wala sio kipindupindu, sio jambo lingine wala sio malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima twende kwenye Sera yetu, tuone namna gani sekta zote zitaingia. Nakumbuka mwaka jana, waliwaita Wakuu wa Mikoa hapa, nikaona wanaweka sahihi, lilikuwa ni jambo zuri, lakini nikawa najiuliza hivi hizi sahihi zitatusaidia, kama hatuna framework? Pia sijasikia ushahidi wowote kwamba hizo sahihi zimesaidia, wameleta improvement, ni kwa sababu lazima likae kimfumo, tuzialike Sera zote kisera na tunaomba katika hili, ikae Sera ya Lishe sio kuchukua habari ya lishe kuiweka kwenye Sera ya Afya, kwa sababu hili jambo ni mtambuka na kubwa. Naomba kusema kwamba hili tutalipigia kelele sana. Tunaomba Sera ya Lishe ije haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usafi; moja ya sababu zinazosababisha vifo, ukichanganya vifo na ulemavu kwa pamoja, ni habari ya wash, mtu anatoka kujisaidia hanawi mikono, anakuja kumsalimia mwenzake na hapa ukiangalia kama mtu angekuwa anapima watu tunavyosalimiana, hapa kwa mikono lakini asilimia zaidi ya sabini ngapi hawanawi mikono baada ya kujisaidia. Hili linahitaji elimu tu na wamesema Wabunge wengi hapa, twende kule kwenye zahanati na vituo vya afya tuweke wahudumu wa afya wa kwenda kuelimisha vijijini wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye Ikama ya Watumishi wa Afya wanayo ya zahanati inasema Clinical Officer kwa siku aone wagonjwa 40. Mtu wa madawa kwa siku ahudumie prescription 40, lakini ikifika kwa yule Community Health Worker inasema aunganishe tu kituo na kijijini, haimpi kwamba leo katazame vyoo saba ukatazame wangapi wameweka sehemu za kunawa, twende huko, tuondoke kwenye tiba sasa tumeshafanya vizuri, twende kwenye afya. Watanzania wanahitaji Afya, nimesikia watu wanawapongeza Madaktari na mimi nawapongeza, lakini ifikie hatua, tuanze kupongeza, tunawapongeza Mabwana Afya, wamehamasisha sasa huku hatuharishi, kwa sababu ukiangalia hapa inasema asilimia 2.7 ya wananchi nchi hii hawana vyoo kabisa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kutoa mchango wangu. Lakini kwa namna ya juu kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufaya kazi hii; na ninawapongeza Wizara, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na timu yenu nzima, hongereni kwa kazi mnayofanya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani, miongoni mwa mambo ambayo iliyafanya kwa nguvu kubwa kabisa ni kuweka amri ambazo zilisaidia kwenye utekelezaji wa sheria kwenye mambo ya hifadhi ambayo ilihusiana na mifugo, kwa sababu ilikuwa inaingia kule, lakini pia na habari ya uvuvi. Ni jambo zuri, kwa sababu sheria ni namna tu mlivyokubaliana namna ya kuishi na namna ya kuhusiana lakini amri ndiyo lile karipio linalotoka kwenda kuhakikisha watu wanafuata sharia; kwa hiyo hilo nalipongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, mimi ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba sasa tumepata muda wa kutosha wa kuweka amri ili sheria zitekelezwe na ushahidi uko wazi, kwamba sasa amri zinaanza kuzaa matunda. Nitatoa mfano wa Biharamulo; Biharamulo ni Wilaya ambayo asilimia 46 ya eneo lake ni eneo lililohifadhiwa; kwa maana ya Burigi, Biharamulo na Kimisi; kwa hiyo asilimia 54 ya eneo iliyobaki ndiyo kwa ajili ya shughuli nyingine za uchumi, nasema nyingine kwa sababu uhifadhi nao ni shughuli ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu hiyo, kwa sababu ya kitovu hicho cha hizo hifadhi tatu, wakati wa zile vurugu za kuondoa mifugo kutoka kwenye hifadhi ili habari ya uhifadhi iende vizuri Biharamulo ilikuwa ni kitovu cha mapambano kati ya hifadhi na wafugaji, ilikuwa vurugu kubwa sana. Lakini sasa mimi ni mmoja wa mashahidi kwamba ni kweli kuondoa wale ng’ombe hifadhini kumeanza kuleta tija.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa mmeona kuna picha ilikuwa inatembea kwenye mitandao, kuna ndovu mmoja amegongwa na gari barabarani, nafikiri ni upande wa Karagwe, hiyo ni ishara kwamba wanyama hawa tunaowahifadhi wameanza sasa kuwa wengi na sasa wanaanza kuonekana hata kwa ngazi hiyo. Lakini faida hiyo tunayoipata upande wa hifadhi hebu twende na upande wa pili, upande wa wafugaji nako tutafute sasa kwenda hatua ya zaidi baada ya amri sasa tuanze kuwekeza kwenye mambo ambayo yataongeza tija.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka kabla ya zile vurugu za hifadhi na wafugaji mimi nilikuwa nimepata fursa ya kuongea na mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii; walikuwa tayari kuja kukaa na Chama cha Wafugaji Ukanda ule wa Wilaya za Biharamulo, Ngara, Karagwe, Chato, Muleba, ili kuona ni namna gani eneo dogo tulilonalo la asilimia 54; kwa sababu tunafanana wilaya hizo; litatumika kwa tija.

Mheshimiwa Spika, unakuta mkulima ana eka kumi, analima tatu, eka saba hazitumii lakini anasema hizi ni za kwangu. Lakini hapo kuna fursa ya kuweka uwekezaji ambapo utapata zile nyasi nzuri za ng’ombe kutumia, kwa hiyo kwanza ukaongeza mahusiano mazuri kati ya mfugaji na mkulima, lakini ukaweka namna ambapo hata wote wawili wanaweza kushiriki kwenye ushuru na kodi kwa mfumo ambao ni rasmi.

Mheshimiwa Spika, wakati mifugo ipo hifadhini ilikuwa ni kukimbizana tu, wanakimbizana, wanatoa rushwa, wanaleta kesi na nini. Mimi nimezungumza sana na hiki chama cha wafugaji; pesa iliyokuwa inazunguka kwenye kesi na rushwa, hiyohiyo ukiigeuza ikawa kodi ni uchumi mkubwa sana. Sasa nakuomba Mheshimiwa Mpina, hebu tuanze na ukanda ule kama mfano, njoo tukuelekeze, tunaongea vizuri na chama cha wafugaji. Bahati nzuri wakishakuwa na chama ni fursa kwamba wana sauti moja, njoo tuzungumze tuondoke kwenye hiyo hatua, tumeshafanya vizuri kwenye hatua ya sheria na amri, sasa twende kwenye hatua ya tija ya hizo sheria na amri zianze kuchangia kwenye uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimefurahi, kwenye hotuba yako, sikumbuki ni ukurasa wa ngapi, umezungumzia namna ambavyo sasa nyama tunayoleta kutoka nje ya nchi imeanza kupungua, na ninadhani huo ndiyo uwe mwelekeo. Juzi mimi nimemsikia Mheshimiwa Rais anatoa maelekezo kwamba baadhi ya watu, hasa viongozi wa Serikali, pamoja na kuwa na laini nyingine za simu;nataka nitumie kama mfano; lakini lazima wawe na laini za TTCL kwa sababu wao ndiyo wadau wakubwa wa hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu mmoja akawa anaona kwamba ni jambo limekaa vibaya, lakini mimi nikajiuliza; nina ndugu yangu aliwahi kufanya kazi Airtel, alikuwa ananiambia wao kwa mwezi Airtel wanawapa airtime kwa ajili ya mawasiliano. Na jana nikamuuliza hivi ilitokea siku moja Airtel wakakupa airtime ya Tigo wakati wewe unafanya kazi Airtel? Akasema hapana. Kwa hiyo hiki kinachofanyika mimi nafikiri ndio mwelekeo. Hebu tutafute kuinua mambo ambayo kwanza ni ya Umma halafu twende upande wa pili, siyo kwamba Private Sector tuiue.

Mheshimiwa Spika, sasa niilete kwenye muktadha wa ufugaji. Ukiangalia viatu, mikanda, mabegi tunayotumia hapa Watanzania ni uchumi mkubwa sana unazunguka. Jana nimemsikia Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema tutafute soko nje, lakini mimi nasema tuanze na soko la hapa, hebu starve yale mambo ya nje weka nje huko, tuhakikishe hapa mikanda, viatu, mabegi tunatumia hapa. Tuki-starve supply kutoka nje, hapa soko liki-starve wawekezaji watafanya kazi nzuri, na muwape support, itafikia hatua hata ng’ombe wako akipotea unakuta ameshachunwa watu wanakwenda kutengeneza mikanda kwa sababu mikanda haitoshi, utakuwa umetengeneza soko la hapa.

Mheshimiwa Spika, lakini tuwasaidie na wafugaji sasa; jambo lingine katika ile niliyosema kuongeza ubora; hebu tuondoke kwenye habari ya ng’ombe, kuna mtaalam mmoja alikuwa ananiambia hapa kwamba sio kila ng’ombe ambaye nyama yake itakuwa nzuri, nyama inawekwa inavutwa hivi kama mkanda, ng’ombe anafugwa miezi 18, 16 ni nyama. Sasa sisi hapa unakuta ng’ombe ana miaka tisa, yaani tangu azaliwe anakuja kuchinjwa siku ya graduation ya Form Four ya binti au kijana aliyezaliwa wakati ng’ombe ananunuliwa. Kwa hiyo tutafute namna ya kuanza ku-transform ili habari ya nyama iwe ya kiwango hicho. Utaacha kununua nyama kutoka nje kuleta Serena na kwingine na mambo mengine kama hayo.

Mheshimiwa Spika, nimeskia hapa, kwenye ukurasa fulani hapa, sikumbuki, tutaona, inasema asilimia 20 ya wafugaji wa nchi hii ndio wana access na extension services (huduma za ugani); lakini hata miongoni mwa hao asilimia 20 ni tija ndogo sana inayopatikana pamoja na huduma za ugani. Na hii inaashiria kwamba mambo aliyokuwa anasema Mheshimiwa Dkt. Nagu kama mfano, kwamba mara kuna dawa feki na vitu kama hivyo, inawezekana kweli yapo. Kwa sababu hata katika hiyo asilimia 20 ambayo wanapata huduma za ugani bado tija haipatikani, na hii nimeipata kwenye ripoti ambayo ni ya Serikali inaitwa Tanzania Livestock Modernization Initiative.

Mheshimiwa Spika, tumeona idadi ya ng’ombe inaongezeka, kwenye hotuba wanasema milioni 30 mpaka 32; mbuzi milioni 18, nadhani ni milioni, nafikiri niko sahihi; kondoo wanaongezeka. Lakini twende hatua ya zaidi, kutoka kwenye idadi kwenda sasa kwenye tija ya hiyo idadi. Namna gani sasa; hebu tuingize wawekezaji waende watengeneze ranchi ndogondogo kwenye maeneo ambayo wakulima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Oscar Mukasa.

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwa namna ya pekee kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupa afya na uhai na tunaendelea kumwomba atusaidie kwenye hili dhoruba ambalo linaikumba dunia kwa sasa. Napenda pia nichukue nafasi hii kwa kuendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono kwamba tunaendelea kufanya shughuli za maendeleo. Tatu niipongeze Serikali; Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa; na Mawaziri wote kwa kazi nzuri. Kazi ni nzuri, ni wazi hakuna mtu anaweza akamaliza matatizo yote duniani kwa miaka mitano. Kwa hiyo tunachoangalia hapa ni hatua imepigwa na imepigwa kwa kiasi gani, kwa hiyo nawapongeza kabisa tumesikia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeainisha kabisa kazi zilizofanyika.

Mheshimiwa Spika, mahususi kwa Biharamulo lakini pia inagusa Taifa zima, naipongeza Serikali kwa ule mpango wa kuja na miradi ya kimkakati kwenye halmashauri. Sisi Biharamulo ni moja ya halmashauri za Wilaya ambazo tulifaidika na jambo hilo na tumepata mradi wa ujenzi wa maegesho ya maroli kwa sababu pale Nyakanazi njiapanda ya kwenda Kigoma, Rwanda na Kahama ni mradi mkubwa sana maegesho ya maroli na stendi kubwa ya mabasi na soko, mradi mzuri sana. Hata hivyo, napenda kutoa wazo hapo kwamba awamu inayofuata hebu Serikali tujikite kwenye wazo zuri la miradi ya kimkakati, hebu tutumie mashirika kama haya ya hifadhi kama ya NSSF na mengine, kuyaunganisha na halmashauri ili sasa miradi hii iwe, sawa ipo ya upande wa huduma, lakini sasa twende kwenye upande wa uzalishaji, kwa sababu ukiangalia stendi ya mabasi na maroli ni mradi wa huduma, halmashauri itapata kipato, lakini tukienda kwenye miradi ya uzalishaji nafikiri tutafungua fursa zaidi.

Mheshimiwa Spika, Biharamulo ni kitovu cha wafugaji na mnakumbuka vita ya hifadhi na wafugaji center mojawapo ilikuwa ni Biharamulo, tuna wafugaji wengi na sasa hivi baada ya hii kampeni ya kuondoa wafugaji hifadhini, wafugaji bado hawajapata namna sahihi ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Kwa hiyo hii miradi ya kimkakati, tukiyaunganisha na haya mashirika ya hifadhi ukatumia hiyo fursa ukatengeneza kitu ambacho kinabadilisha ule ufugaji wao unakwenda kibiashara zaidi, nafikiri kuna nafasi pale tutatoka kwenye huduma tunaenda kwenye uzalishaji, kwa hiyo nawapongeza Serikali lakini ni vizuri tukaenda mbele zaidi tukaongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nigusie pia ugonjwa wa Corona maana yake ndio suala la sasa, ni vizuri kuligusia kidogo. Nianze kwa kujaribu kuweka kumbukumbu sawa, nimemsikia Mheshimiwa Sugu akiunganisha imani na sayansi, nataka kuseme tu kwamba, sayansi ni zao la elimu na elimu ni moja ya mapaji ya Roho Mtakatifu, kwa hiyo sayansi na elimu ni matokeo ya imani. Sasa kinachosemwa hapa sio kwamba watu kuwa na laissez faire, watu wajae Kanisani bila utaratibu, lakini pia sio kwamba kama wengine wamefikia hali ya kufunga Makanisa na sisi tufunge, hata kama hatujafikia, sisemi hatujafikia lakini tuipe nafasi Serikali na Serikali wafanye kazi yao ya ku- control, ku- balance vizuri panic na laissez faire, nafikiri ndio kazi kubwa ambayo Serikali tunatakiwa kufanya.

Mheshimiwa Spika, kwenye Corona hapo hapo pia ningemwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, nampongeza sana kwa kazi nzuri inayoendelea sana kabisa, lakini hebu kama alivyosema tujaribu kuwashauri kuliko kuwashambulia na kuwawekea presha, naomba tuongeze kidogo nguvu kwenye ile multisectoralapproach ya kupambana na corona kwamba sio suala la afya kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio amelichukua.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu ilizuia ilifunga shule ambayo ni hatua ya awali nzuri kabisa, lakini hivi tunavyoongea kuna mahali watoto wanakwenda kufanya masomo ya ziada tuition, sasa hilo ukimsubiri Mheshimiwa Waziri wa Afya utachelewa, kuna Wakuu wa Mikoa tuwaambie wafanye kazi yao , kuna Mawaziri wanaohusika wafanye kazi yao, wazuie hiki kitu. Hatua ya kwanza wameshafunga shule, watu waelewe kwamba tumefunga shule ili kuwaondoa watoto kwenye hatari kwa sababu wao sio rahisi kufuata maelekezo, lakini sasa kama huko nyuma watu wanawapeleka kwenye masomo ya ziada, ina maana hata hii jitihada ya kwanza ya kufunga shule unaipunguzia nguvu yake.

Mheshimiwa Spika, ushauri kwa Serikali nzima of course kupitia Wizara ya Afya, sasa hivi nimeona kwenye Mtandao hapa wasilisho zuri kabisa la Wizara ya Afya linaonyesha ramani ya case zetu ziko wapi, wapi una wale contacts unaotafuta kwa wingi vizuri kabisa Dar es Salaam, Arusha, Kagera na Zanzibar, maana yake ni kwamba tunatarajia kwa ramani hii Dar es Salaam na Arusha nguvu ya kupamba tuisikie ni tofauti kuliko kwingine kwa sababu hatuwezi kufanana. Kwa hiyo tujaribu namna ya huu mtawanyiko wa ramani ambao tunaupata kutoka kwa watalaam tusaidie kufanya mambo yetu kwa kusukuma kwa ngazi ya utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nizungumzie kidogo namna ya kutumia rasilimali kidogo tulizonazo kwa tija kubwa zaidi. Najua Serikali tunafanya hivyo kwenye maeneo mengi, lakini kuna eneo moja ambalo ningeomba nilisemee. Nilipata fursa ya kwenda Chuo Kikuu cha Teknolojia Nelson Mandela Arusha, Chuo Kikuu kile tofauti na Vyuo Vikuu vingine, Vyuo Vikuu vingine vyote kazi yake ni ile academic excellence yaani ubora kwenye taaluma lakini Chuo Kikuu kile zaidi academic excellence wanakwenda kwenye ubunifu, wanafanya ubunifu kila Master’sdegree inayotoka pale au Ph.D lazima itoke na ubunifu wa jambo fulani ambalo linakwenda kutatua tatizo kwenye jamii, lakini wanakwama kwenye pesa za uwatamizi wa ubunifu huo.

Mheshimiwa Spika, vile vile wanakwama kwenye namna gani tunaweza tukachukua ubunifu uliofanyika pale kuuleta kwenye mazingira ya viwanda na mazingira ya sera ili ubunifu huo utumike kwa Taifa zima; kwa mfano, wana ubunifu wameufanya wa teknolojia inaitwa non filter, Mtanzania kijana ametengeneza chombo cha maji kinachuja uchafu wote, sasa ameshindwa kuchuja chumvi, lakini uchafu mwingine wote wote anauchuja na maji yanaweza kuwa safi na salama na wamepata tuzo ya WHO na kwingineko wanatambulika kidunia. Sasa tutafute namna ya kimfumo ambapo sisi watunga sera tunaweza kuwa tunakwenda kule kuwa na appetite ya kujua kule kuna nini na kuchukua kuingiza kwenye sera. Kwa mfano hili la maji lina faida kwa Wizara ya Afya na kwa Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, kuna utafiti hapa unaonyesha vifo vya watoto kwenye nchi za Afrika Mashariki vimepungua, lakini vingepungua zaidi endapo tungekuwa tumeshughulika kwa kiwango kikubwa zaidi tulichonacho sasa kwenye habari ya maji ya kunywa ya watoto na vitu kama hivi. Pia ninao utafiti mwingine wa watu wa maji wanasema mpaka sasa hii informal access ya maji ni kubwa zaidi kuliko formal. Kwa hiyo huyu mtu mwenye teknolojia hiyo Nelson Mandela ukimtengenezea mazingira watunga sera tukaenda, tukawa appetite ya kwenda kuchukua ubunifu na kuingiza kwenye sera, watu wengi zaidi hata kama sio wote watapata fursa ya kupata maji salama ya kunywa na kutumia na hivyo itakuwa kazi ya wanasayansi ni kufanya ubunifu, sisi ni kuchukua na kutengeneza mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tukiwa na chombo independent kidogo kinaongozwa labda na Rais mmoja mstaafu ambaye bado ana nguvu ya kukimbiambia, kina Makatibu Wakuu wawili wa nguvu, kina Wabunge wawili, watatu, halafu Spika labda ni mlezi, kinatengeneza appetite ya kwenda kwa wabunifu kuchukua mambo ya kupandisha kwenye policy, basi itatusaidia sana na nchi hii itabadilika na kutumia rasilimali kidogo tulizonazo kwa ajili ya kupata matoke makubwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja naomba kuwasilisha. (Makofi)