MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza:-
Je, lini Kituo cha Polisi Micheweni kitakarabatiwa ili kiendane na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdi Hija Mkasha, Mbunge wa Micheweni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ilifanya tathmini kwa ajili ya kubaini kiwango cha uchakavu na gharama za ukarabati wa jengo la Kituo cha Polisi Micheweni na kubaini kuwa jumla ya shilingi milioni 65 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zimetengwa kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024. Mara fedha hizo zitakapopokelewa, zitatumwa katika kituo hicho ili ukarabati wake uanze kufanyika, nashukuru.
MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Nyumba za Askari wa Jeshi la Uhamiaji Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imekamilisha taratibu za kufunga mikataba ili kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi sanjari na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Uhamiaji Wilaya Micheweni. Gharama ya utekelezaji wa mradi huu ni kiasi cha shilingi 2,695,937,724.80, ikijumuisha gharama za mkandarasi kiasi cha shilingi 2,549,937,724.80 na mshauri elekezi kiasi cha shilingi 146,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilisha taratibu za ununuzi, tayari Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi 1,250,000,000 ili kuanza utekelezaji wa mradi huu. Aidha, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake, ahsante sana.