Supplementary Questions from Hon. Abdi Hija Mkasha (5 total)
MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni muda gani tangu Jeshi la Polisi lifanye tathmini ya ukarabati wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ilifanyika mwaka jana, 2023. Nami nimhakikishie Mheshimiwa Mkasha, kwa sababu, liko kwenye bajeti ya 2023/2024, mara fedha hizo ambazo tayari zimeombwa Hazina zitakapotoka, kituo hiki kitaanza kukarabatiwa. (Makofi)
MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza ambalo lina sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Naomba nitoe taarifa katika hili Bunge kama ndani ya Wilaya yetu ya Micheweni bahati nzuri Ofisi ya Uhamiaji tunayo lakini kubwa ni suala zima la makazi kwa wale askari wetu. Je, ni lini ujenzi huu utaanza?
(b) Je, Waziri yupo tayari kufuatana nami ili twende akajionee uhalisia wa hali ilivyo katika eneo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ujenzi wa majengo haya ya makazi ya Askari wa Uhamiaji katika Wilaya ya Micheweni itaanza katika mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari tumetenga shilingi 1,250,000,000 ili kazi ianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kuongozana na Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari kuongozana naye kwenda Micheweni baada ya Bunge la Bajeti, kwa hiyo, asiwe na wasiwasi. ahsante sana, (Makofi)
MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali dogo moja la nyongeza. Je, ni lini Serikali itafunga kamera za usalama katika Miji ya Pemba ikiwemo na Wilaya ya Micheweni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdi Hija Mkasha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwa upande wa Pemba, tayari kamera zimeshafungwa kwenye Mji wa Chakechake, Mkoani pamoja na Wete. Vilevile, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, tumetenga fedha kwa ajili ya kumalizia maeneo yaliyobaki ikiwepo Mji wa Micheweni.
MHE. ABDI HIJA MKASHA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiboresha Kituo cha TEHAMA kilichopo Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilitekeleza mradi wa ujenzi wa vituo 11 vya TEHAMA, Unguja na Pemba ambapo kwa kila wilaya kimejengwa kituo kimoja kwa madhumuni ya kuwapa fursa wananchi wa Zanzibar kujifunza na kutumia TEHAMA kwa ajili ya manufaa yao wenyewe ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni. Kituo cha TEHAMA Sokoni kilichopo Wilaya ya Micheweni ni miongoni mwa vituo hivyo ambapo kinaendelea kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali kuhusu kukiboresha kituo husika kilichopo katika Wilaya ya Micheweni, inaashiria kuwa ipo changamoto. Hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi itafanya tathmini ili kujua mahitaji halisi ya kituo hicho kwa lengo la kufanya maboresho yanayohitajika. (Makofi)
MHE. ABDI HIJA MKASHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imekiri kuwepo kwa changamoto katika kituo kile; je, ni lini itaharakisha kwenda kufanya tathmini hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika kituo kile kuna vijana ambao wanajitolea, je, Serikali ipo tayari kuwafanyia mpango angalau wa kupata posho ya kuweza kujikimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza, ninampongeza sana Mheshimiwa Abdi Mkasha kwa kufuatilia maslahi ya vijana ambao wako pale tayari wanafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, tayari sisi kama Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Tanzania Bara tulishafanya sehemu yetu kupitia UCSAF na tayari tumeshakabidhi kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara hii ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Hivyo, ninapenda tu kukwambia kwa sababu tunafanya kwa ushirikiano basi nitawasiliana na wewe na kuona namna njema ya kukukabidhi kwa wenzetu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili waweze kufanya haya wote mawili; kuharakisha katika maboresho, lakini vilevile kuangalia maslahi ya vijana. (Makofi)