Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maimuna Salum Mtanda (24 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa ridhaa yako kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa ridhaa ya kupeperusha bendera katika Jimbo la Newala Vijijini. Pia nipongeze na kuishukuru familia yangu kwa support wakati wote wa uchaguzi hadi sasa. Kipekee pia niwashukuru wapigakura wa Jimbo la Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Novemba, 2020 pamoja na ile ya 2015. Ni hotuba ambazo nimepitia zote, hotuba ambazo zina maono, hotuba ambazo kwa namna ya kipekee, hasa ile ya 2015, ilipotekelezwa pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilikifanya Chama Cha Mapinduzi kutembea kifua mbele wakati wa Uchaguzi wa Mwaka 2020. Nina imani hotuba hii ambayo ameitoa 2020 tukiitekeleza hivi inavyotakiwa 2025 itakuwa ni kuteleza kama kwenye ganda la ndizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi, tumeyaona. Amesimamia vizuri miundombinu katika nchi hii kuanzia afya, barabara, elimu na sekta nyingine zote. Tunampongeza sana kwa kile ambacho amekifanya kwa kusaidiana na wasaidizi wake ambao ni Mawaziri wetu. Hata hivyo, zipo changamoto kadhaa ambazo zikisimamiwa na kutekelezwa ipasavyo nadhani nchi hii itasonga mbele sana zaidi ya hapa ambapo tupo sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanazalisha kwa kiasi kikubwa zao la korosho, zao ambalo linaipatia nchi hii uchumi na fedha nyingi za kigeni, lakini kuna changamoto ya barabara yetu ya kiuchumi, barabara ambayo inatumika kupitisha zao la korosho kutoka kwenye maeneo ya wakulima kuelekea bandarini. Barabara ile imeshaombewa muda mrefu lakini haikamiliki. Ni barabara ya kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi hadi Nachingwea. Barabara ile hadi sasa imekamilishwa kwa kiwango cha lami kwa kilometa 50 tu. Niombe wenzetu wa Ujenzi kuharakisha ukamilishaji wa barabara ile ili mazao ya wakulima yapate kusafirishwa kwa urahisi kuelekea bandarini, lakini pia kuvinusuru vyombo ambavyo vinasafirisha mazao hayo kuelekea bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ambayo ipo Jimbo la Newala Vijijini imehamia mwaka jana katika eneo lake jipya la utawala. Eneo lile halina jengo la utawala na kwenye hotuba tumeelezwa na kusisitizwa suala la utawala bora. Utawala Bora ni pamoja na kuwepo na maeneo ya watumishi kutendea kazi, lakini Halmashauri ya Wilaya ya Newala haina jengo la Utawala. Niombe wahusika na wasimamizi wa masuala ya utawala kwa maana ya TAMISEMI watuangalie kwa jicho la pekee ili watumishi wale wapatiwe jengo la utawala nao wafanye kazi katika mazingira yaliyoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Newala Vijijini kuna changamoto ya maeneo ya kutolea huduma ya afya. Zipo kata 22 lakini ni kata tatu tu ndizo ambazo zina vituo vya afya. Naomba Mheshimiwa anayesimamia afya atuangalie kwa jicho la kipekee tupate vituo vya afya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana kwa kupunguza kiasi kikubwa cha migogoro iliyokuwa na Maafisa Ardhi wasio waaminifu ambao walikuwa wanagawa ardhi moja kwa zaidi ya watu wawili, changamoto hii ilikuwa kubwa sana katika baadhi ya maeneo ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo bado kuna baadhi ya changamoto za ardhi ikiwemo moja, mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kati ya eneo la Mpanyani karibu na Nangoo. Kutokana na mgogoro uliopo ambao haujapata suluhisho, msimu wa korosho unapowadia Halmshauri hizi mbili hugombania wapi kwa kwenda kuuza korosho zao, kila Wilaya huvutia kwake ili wapate mapato. Mgogoro huu umechukua muda mrefu tunaomba utatuliwe.

Pili, katika Kijiji cha Chilangala eneo la Mbwinji, watu wa Mamlaka ya Maji (MANAWASA) wamechukua ardhi ambayo wanakijiji walikuwa wamelima mazao yao ya chakula na biashara bila kulipa fidia kwa wananchi husika wa Chilangala kwa ajili ya mradi wa maji. Changamoto hiyo imezua mgogoro mkubwa kwa wananchi wa Chilangala ambao hawajajua hatma ya ardhi yao iliyochukuliwa. Tunaiomba Wizara ya Ardhi iingilie kati ili wananchi wa Chilangala walipwe fidia ya ardhi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Serikali imeanza kufanya sensa ya utambuzi wa nyumba vijijini zenye hadhi angalau ya kudumu kwa miaka 15, nyumba zilizojengwa kwa udongo, saruji na kuezekwa kwa bati ili ziweze kulipa pango la nyumba. Pamoja na lengo zuri la Serikali la kudhibiti mapato lakini malalamiko yaliyopo kwa wananchi wa kipato kidogo ni namna watakavyopata fedha za kulipia pango kwa kuwa wapo baadhi yao wamejengewa nyumba hizo na watoto wao au ndugu zao. Lakini wapo wanaolalamika kwa kuwa walijenga nyumba hizo kipindi bei ya zao la korosho ikiwa nzuri, lakini kwa hali iliyopo sasa wanapata wakati mgumu ni namna gani watakwenda kulipia pango hilo katika mazingira ya sasa ambapo bei ya mazao haijatulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu 2011 - Ofisi ya Ardhi Mtwara ilijiwekea mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria mbalimbali za ardhi katika Halmashauri tisa za mkoa huo kufikia Juni, 2021. Hadi kufikia Mei 15, 2021 Ofisi ya Ardhi Mkoa imefanikiwa kutoa elimu kwa Halamshauri za Masasi, Nanyamba na Nanyumbu pekee huku muda uliobaki ni mwezi mmoja tu. Je, ni nini kimekwamisha zoezi hilo kusuasua ukizingatia kuwa muda wa mpango umebaki mwezi mmoja tu? Je, upo uwezekano wa Ofisi ya Ardhi Mkoa kumaliza zoezi la utoaji wa elimu katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya Afya. Kipekee sana nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kweli amekuwa akitekeleza na kupeleka fedha nyingi sana kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, namshukuru yey pamoja na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kama nilivyotangulia kusema, Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wamepeleka fedha nyingi kwenda kutekeleza miradi ya hospitali, vituo vya afya, zahanati, kujenga shule na mambo mengi yanafanyika katika maeneo yetu, nasi sote ni mashahidi wa yale ambayo yanatekelezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nini matarajio kama nchi? Matarajio ni kuona kwamba miradi ile inatekelezwa kikamilifu na inakuwa na thamani ya fedha iliyopelekwa katika hayo maeneo. Kwa bahati mbaya sana katika baadhi ya maeneo, hasa kwenye Halmashauri za pembezoni, ili miradi ile iende ikakamilike vizuri, lazima kuwe na rasilimali watu wa kutosha. Ila kwa bahati mbaya Halimshauri zetu za pembezoni kuna upungudu mkubwa sana wa rasilimali watu kiasi ambacho utekelezaji wa miradi ile unakuwa chini ya kiwango. Ukienda unakosa watu wa manunuzi, unakosa ma-engineer, unakosa wahasibu na mambo kadha wa kadha. Kwa hiyo, matokeo yake miradi mingi inatekelezwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Spika, labda nikupe mfano wa uchache au upungufu wa watumishi katika baadhi ya Halmashauri. Ukienda kwenye ripoti ya CAG, ziko Halimashauri nyingi ambazo zimebainisha upungufu wa watumishi ikiwemo Kasulu DC, kuna uhaba wa watumishi 163 sawa na 52% tu. Ukienda Nanyamba Mji kuna upungufu wa watumishi 932; ukienda Halmashauri ya Kilwa, walimu peke yake, kuna upungufu wa walimu 735; Ukienda Newala DC kuna upungufu wa watumishi 1,087 waliopo ni 1,088 tu; ukienda kwenye maeneo mengi kwenye kata hakuna Maafisa Maendeleo ya Jamii, sehemu ambayo tunapeleka fedha nyingi sana zile za mikopo ya 10% lakini hakuna wasimamizi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ukienda katika baadhi ya Halmashauri hakuna Wakaguzi wa Ndani, hawapo. Pia Maafisa Manunuzi kwenye Halmashauri zetu nalo ni changamoto, wengi waliopo ni wale walioazimwa na Halmashauri na wanakosa sifa. Sasa matokeo yake ni kwamba miradi mingi, kwa sababu hawa watumishi ambao tunawakosa ndio ambao wangtakiwa kusimamia miradi hiyo kwa ukamilifu, miradi imekosa thamani halisi ya fedha kama vile ambavyo tulikuwa tunatarajia.

Mheshimiwa Spika, rasilimali watu ndiyo uti wa mgongo kwenye utendaji wa hizi Halmashauri. Kwa mfano, umepeleka fedha hiyo asilimia 10 ili iende kwenye hayo makundi ya akina mama, vijana, pamoja na watu wenye ulemavu, lakini hakuna mfuatiliaji kule. Zile fedha zinaenda kuzama, kwa sababu zitapelekwa, lakini nani wa kuwaelimisha? Hayupo. Nani atasimamia? Hayupo. Kwa hiyo unakuta fedha nyingi zinapotea.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 ni Shilingi bilioni 47.1 hazijarejeshwa. Hizi ni fedha nyingi ambazo zingefanya kazi nyingi sana katika Halmashauri zetu. Ukirudi miaka mitano nyuma, ni zaidi ya Shilingi bilioni 100 zimeshindwa kurejeshwa, zimezama.

Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba Halmashauri na wale ambao tuliwatarajia waende tukawainue kiuchumi wanakosa kuinuliwa kiuchumi kwa sababu hizo fedha ambazo tulitarajia zirudi zikawasaidie watu wengine hakuna mtu wa kuelimisha na kutoa elimu ya kutosha pamoja na usimamizi wa hayo makusanyo kule kwenye maeneo ya kata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye suala la manunuzi, kama ambavyo Mjumbe ambaye ametangulia kusema, fedha nyingi katika Halmashauri zetu zinaenda upabde wa manunuzi, lakini hakuna watu wa manunuzi. Kwa hiyo, unakuta Mkurugenzi anakwenda kumwazima; natolea tu mfano, mwalimu, mtu ambaye hana sifa ya kutosha kwenye eneo hilo, ndiye anaenda kusimamia manunuzi. Ukienda kwenye ripoti ya CAG, kiasi kikubwa cha fedha kimepotea kwa sababu ya kukosa watu wenye sifa wa kusimamia manunuzi ya Umma. Wanafanya manunuzi lakini hayafuati taratibu na kanuni ambazo zimeandaliwa na PPRA.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kukosekana kwa ma-engineer katika Halmashauri zetu; tulienda kwenye Halimashauri mojawapo kwenye mkoa huu ambao tupo, tulimkuta mtu ambaye alikuwa anasimamia ujenzi wa bwalo pamoja na bweni, alikuwa ni Mwalimu. Kwanini alikuwa anasimamia Mwalimu? Amewekwa pale kwa sababu ya ukosefu wa engineer pale Halmashauri. Kwa hiyo, kawekwa yeye. Tulikuta miradi ile kwa kweli ilikuwa inasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kwa sababu fedha hizi zinatokana na kodi za wananchi, lakini lengo ni kutoa huduma kwa wananchi pale ambapo miradi itakamilika vizuri. Naiomb Serikali basi, ijitahidi kuajiri watumishi ambao wataenda ku-cover gap lililopo kwa sasa ili miradi iwe na thamani ya fedha ambazo zinapelekwa kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine, nilizungumzia suala la upungufu wa walimu katika baadhi ya maeneo, vile vile, ukosefu wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nao ni mkubwa. Naiomba Serikali ifike mahali sasa tuajiri watumishi ambao wana utashi wa kuishi kwenye maeneo husika au wale ambao wanatoka kwenye maeneo yao. Kwa sababu ipo changamoto kubwa, mtumishi anapoenda kwenye eneo ambalo jiografia yake inakinzana na yeye, anakaa kwa muda mfupi, anataka kutoka. Nafahamu kwamba Tanzania ni yetu sote, kila mmoja anatakiwa kuishi popote, lakini ipo hiyo changamoto sana ambayo tunai-experience site. Mtu anaenda kuripoti na anataka arudi, matokeo yake upungufu hauishi kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuweke muda maalum kwa mtumishi kuhama, yule ambaye amepata ajira. Muda ambao haupungui miaka mitatu ili angalau tu-retain wale ambao wapo. Otherwise haya maeneo ya pembezoni ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yataendelea kubakia bila kuwa na watumishi na hali inazidi kuwa mbaya kwa sababu lengo ni watumishi wawepo ili huduma zikaweze kutolewa ipasavyo. Watumishi wanapokosekana, huduma pia zinakosekana.

Mheshimiwa Spika, lingine naomba pia Serikali ibaini upungufu kwa kila Halmashauri za pembezoni, ili wakati wa kutoa ajira, basi kipaumbele kiwe ni yale maeneno ambayo yana upungufu mkubwa. Kwa sababu haiwezekani kila siku baadhi ya maeneo watumishi wanakuwa wachache. Imekuwa kama ni wimbo, kuna maeneo yana watumishi wengi na mengine yana watumishi wachache. Sasa hao ambao ni wachache, utoaji wa huduma inawawia pia vigumu. Kwa hiyo, tufanye Sensa ya makusudi, tubaini hali ilivyo ili linapokuja suala la ajira, basi watumishi wapelekwe au tutoe kipaumbele katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limejitokeza kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021, ni tatizo la fedha kutopelekwa benki zinazokusanywa kwa mfumo wa POS. Hii ni changamoto kubwa na imejitokeza katika maeneo mengi. Kwa mwaka 2020/2021 peke yake ni Shilingi bilioni 17 hazikupelekwa benki. Tafsiri yake rahisi tu ni kwamba hizo fedha zimeingia kwenye mifuko ya watu, lakini zingekuwa zimewekwa benki zingefanya mambo ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, sasa tunakwamisha kwa sababu kwenye bajeti Kuu ya Taifa inabajetiwa pia na fedha zinazotokana na makusanyo kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, unakuta bajeti kuu ya Taifa haitimii kwa sababu kuna fedha huku nyuma ambazo zimewekwa kwenye mifuko ya watu ambao siyo waaminifu. Naiomba Wizara ambayo inasimamia TAMISEMI kuweka mfumo ambao ni madhubuti utakaodhibiti hili suala za fedha kutopelekwa benki.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi siyo za leo kwa sababu huu ni mwaka wa pili, kw sababu ni za mwaka 2020/2021, Shilingi bilioni 17 hazijaenda benki hadi leo. Wamechukuliwa hatua gani ambao wamehusika? Mpaka sasa baadhi ya maeneo unakuta bado. Kesi nyingi ziko TAKUKURU, wengine wamepelewa Polisi, lakini kile ambacho tulikuwa tunataraji, kwa sababu lengo letu lilikuwa tupate zile fedha zikatoe huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, inachelewesha pia utoaji huduma kwa wananchi kwa sababu fedha zimeingia kwenye mifiuko ambayo siyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba TAMISEMI, ule mfumo wa kielektroniki wa TAUSI uanze kufanya kazi ili tuweze ku-monitor haya mambo mengine amabyo yanaweza pia kurekebishika.

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine ambalo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali amelibainisha kwenye Hesabu ya 2020/2021, nalo ni suala la vitendea kazi kwa watumishi. Nimeongea hapa kuhusu Maafisa Maendeleo ya Jamii, lakini pia tuna ma-engineer wanaosimamia miradi, tuna wahasibu, wakusanya mapato, wanahitaji vitendea kazi ili waweze kufika kwenye maeneo ambako wanaweza kutoa hizo huduma au kukusanya mapato. Halmashauri nyingi hazina vitendea kazi kwa watu hao. Unakuta internal auditor yupo pale, anatakiwa kumkagua Mkurugenzi, Mkurugenzi hampi usafiri; kwa sababu akimpa usafiri, maana yake anaenda kumtafutia yeye changamoto. Kwa hiyo, hapewi usafiri, kiasi kwamba sasa unakuta kazi ya internal auditor inakuwa ngumu sana, namna gani atafika akakague miradi ili aje abainishe yaliyopo huko site? Anashindwa kwa sababu hana vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara tuangalie Halmashauri, tuwawezeshe waweze kufika kwenye maeneo. Engineer yupo, anatakiwa akakague miradi, na sasa hivi miradi ipo mingi kwenye kata zetu, lakini engineer yupo Halmashauri, hana usafiri wa kumfikisha huko site. Matokeo yake sasa, kwa sababu yeye hawezi kufika kwa wakati, basi ana-delegate, anawaambia walioko site kama ni watu wa Afya, kama ni watu wa Elimu au nani, wasimamie hiyo miradi wao, lakini wao tukumbuke kwamba hawana ujuzi wa majukumu ambayo wanapewa. Matokeo yake ni miradi inazidi kuharibika kwa kukosa vitendea kazi vya kuwafikisha maeneo mbalimbali ya kusimamia miradi kule site. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine niseme kidogo ni suala la wahasibu. Nilitangulia kusema kwamba wahasibu ni wachache, lakini unakuta maeneo mengine wahasibu hawa wamepitwa na wakati, kwa maana ya kwamba mifumo inabadilika kila siku ya ufungaji wa hesabu za mwaka, lakini wahasibu hawa hawana mafunzo ya namna ya kufunga hesabu hizo za mwaka. Matokeo yake inapofika ufungaji wa hesabu za mwaka wanapita, wanahaha kwenye maeneo mbalimbali kutafuta watu wa kuwafungia hesabu zao. Ni suala ambalo linapoteza fedha nyingi za Halmashauri, kwa sababu wangekaa kwenye vituo vyao wakafunga wenyewe hesabu zao ingepunguza hizo gharama za kupita wanazunguka kutafuta watu waweze kuwafungia hesabu zao za mwaka. Kwa hiyo, hili ni tatizo ambalo lazima Wizara zinazosimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa walione, waone namna nzuri ambayo watatoa mafunzo kwa wahasibu ili waendane na utaratibu na mfumo mpya unaotumika sasa wa ufungaji za hesabu hizi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, wengine ambao wanafanya wao wenyewe, wanasema poteleambali tunafanya, unakuta hesabu zao ni mbaya, hata CAG anashindwa kuisoma hiyo hesabu ya Halmashauri husika na matokeo yake wanaipa hati ambayo siyo yenyewe, lakini ni kwa sababu tu ya upungufu wa ujuzi kwa wahasibu ambao wapo katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia naishukuru Wizara ya Fedha kwa uwasilishaji mzuri wa Mpango wa Miaka Mitano inayokuja kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Mpango huu, tuna maana kwamba ni mwelekezo wa Serikali kwa miaka mitano ijayo. Sasa ili kuutendea haki Mpango huu na yale matarajio tunayoyatarajia yaweze kupatikana vizuri, kuna mambo lazima yaboreshwe ikiwemo rasilimali watu, lazima iwepo, miundombinu iboreke na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza wenzetu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa sababu wametuwezesha na kutuelewa sisi Wananewala kwa kuwaendeleza na kuchukua majengo ambayo yalikuwa ya NDF ili kuwa VETA. Sisi Wananewala tuna kiu kubwa ya kupata ajira kwa vijana wetu, kwa hiyo, tukawakabidhi wenzetu wa Wizara ya Elimu majengo ili yatumike kama VETA na vijana wetu wakapate ujuzi, waweze kujiajiri wenyewe na kisha maendeleo ya watu yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema, lakini majengo yale yatatumiwa na Wilaya zaidi ya moja kwa maana ya Tandahimba, hakuna VETA, ni majirani zetu, watatumia pale; Masasi kwa maana ya Lulindi, hawana VETA, watatumia pale na Wananewala. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ituongezee au itujengee mabweni ili wanafunzi watakaoenda kusoma pale wapate elimu na ujuzi unaotosheleza bila kuhangaika, mwisho wa siku wakapate wao wenyewe kujiajiri na maendeleo ya nchi yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili maendeleo yaweze kupatikana, lazima miundombinu iboreshwe hasa barabara. Wananewala Vijijini wana barabara yao ambayo inaunganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa maana ya Wilaya ya Lindi Vijijini na Newala; barabara ya kutoka Mkwiti – Kitangali hadi Amkeni. Barabara ile ni ya vumbi, lakini ikiboreshwa kwa kiwango cha lami, tuna uhakika kabisa kwamba mawasiliano yatakuwa rahisi, watu watafanya biashara, watakuwa wanasafiri kutoka eneo moja na kwenda eneo lingine na kujipatia fedha ambazo wataenda kuendeleza maisha yao na kuachana na hali ambayo wanayo kwa sasa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ambayo inasimamia ujenzi, kwa sababu tunataka kuboresha au kuleta maendeleo ya watu, basi itujengee barabara ile kwa kiwango cha lami ili nasi maendeleo yetu yaweze kupatikana kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchangiaji ambaye amezungumzia suala la utafiti kwa vyuo vyetu vya kilimo, ni muhimu sana. Utafiti wa mazao ni muhimu sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze fedha kwenye vyuo vya utafiti ili waweze kufanya utafiti wa mara kwa mara ambapo watakuwa up to date na hali ya mabadiliko ya mazao yetu kwa kadri inavyojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanamtwara tunalima korosho ambazo zina magonjwa mbalimbali; ni kama binadamu, magonjwa yanabadilika kila leo. Kwa hiyo, tusipowekeza kwenye utafiti wakulima wetu wakapata kujua aina ya magonjwa ambayo yanajitokeza kwa wakati huo kupitia watafiti wale wa TARI Naliendele, nadhani tutakuwa hatufanyi chochote na uzalishaji wa zao la korosho utakuwa unapungua kadri ya siku zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niunganishe na Maafisa Ugani. Tunaomba Maafisa hawa wawepo kwenye vijiji vyetu, kwa sababu sasa hivi tunavuna lakini kiholela…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja, lakini tunaomba tupatiwe Maafisa Ugani ili wakawasimamie wakulima wetu ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa mara nyingine naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, kwanza Halmashauri nyingi zinakosa ma-engineeer wa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa hali inayosababisha miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango. Mfano katika Halmashauri ya Newala ina maafisa mchundo wanne, engineer mmoja na hakuna mkadiriaji majengo. Athari ya hali hii ni kwamba miradi inayotekelezwa kwa force account mara nyingi inaponunua vifaa kwa jumla (bulk procurement) ukadiriaji unakuwa na mapungufu mfano wengi hununua vifaa vingi vinavyobakia hali inayoleta ubadhirifu wa fedha za umma.

Pili ni kuhusu miundombinu chakavu nikianza na afya; vituo vya afya vya Chihangu na Mkwedu; tuna vituo vya afya viwili ambavyo ni kongwe na chakavu; havina wodi za kulaza wagonjwa.

Kuhusu uchakavu; Kituo cha Afya Chihangu paa lake linavuja sana hali inayoleta ugumu kwenye utendaji kazi kwa watumishi na wagonjwa pia.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu; shule nyingi za msingi ni za muda mrefu na zimechakaa sana. Mfano ni shule zifuatazo; Nakahako (paa linavuja) namadarasa matatu ni mabovu inabidi yavunjwe hayakarabatiki; Shule ya Msingi Mtanda; Mtongwele; Nambudi; Mpotola; na Bahati (vyumba vichache). Pia Majembe Juu; Chinle; Lihanga na Mahoha.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina upungufu mkubwa wa nyumba za watumishi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa haya ambayo amekuwa akiyatenda. Kwa kweli anatupeleka kuzuri na sisi wote ni mashahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wote waliotuletea Mpango huu, Mawaziri wote pamoja na Wasaidizi wao, Mpango ni mzuri na nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Mpango kuna mambo mbalimbali na shabaha nyingi zimewekwa, lakini naanza na ile ya elimu, nimeangalia kwenye Mpango wa 2024/2025 ambapo kiashiria kimojawapo kinasema ni viashiria vya maendeleo ya watu, lakini kwenye shabaha inasema kuchochea na kuboresha ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizidi kusoma zaidi kwenye Mpango kumeonesha namna ambavyo kule nyuma tulikotoka kuanzia 2012 hadi 2022 udahili wa wanafunzi ulivyoongezeka kwenye Nyanja zote kuanzia Elimu ya Msingi udahili umeongezeka kutoka asilimia 94.6 hadi asilimia 113.2 mwaka 2022, hiyo ni kuanzia mwaka 2012. Kadhalika na sekondari tunashukuru sana udahili huu umeongezeka kwa sababu ya jitihada mbalimbali ambazo zimefanywa na Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwekezaji katika Sekta ya Elimu ni mkubwa sana, ujenzi wa vyumba vya madarasa umeongeza, maabara zimeboreshwa, ujenzi wa mabweni lakini pia elimu msingi bila malipo bado inaendelea kutolewa hadi leo. Kwa hiyo ni kiasi kikubwa sana cha fedha ambacho kinaenda kwa ajili ya kuimarisha Elimu yetu kuanzia ngazi ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo kwa sababu uwekezaji kwenye Sekta ya Elimu ni mkubwa, tunategemea outcome ya wanafunzi hapo mbele na wenyewe waje wanafunzi ambao wameiva ukizingatia kwamba kuna kuchochea na kuboresha ubora wa elimu. ubora wa elimu ni pamoja na kuwa na Walimu wa kutosha ili kuweza kufundisha vizuri na wanafunzi wapate elimu bora mwisho wa siku Taifa liwe na kile ambacho tulikusudia tukawekeza kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye Mpango wetu sijaona, nashukuru kwamba zipo ajira ambazo huwa zinatolewatolewa, lakini kwa uwekezaji huu lazima tuwe na mkakati wa dhati wa kuhakikisha Walimu wanapatikana watakaoenda sambamba na idadi ya wanafunzi tulionayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wanahangaika ukienda shule za pembezoni hakuna Walimu, Walimu ni wachache sana kiasi kwamba wanafunzi wengine anaenda anamaliza siku hapati Mwalimu, kesho anarudi tena, anakosa Mwalimu, inasababisha pia hata utoro, Kwa hiyo ili kudhibiti hali hii lazima tuwe na mkakati wa dhati utakaoendana sambamba na uwekezaji ambao Serikali imekuwa ikifanya katika Sekta ya Elimu, lakini pia tuwapunguzie wazazi mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchache wa Walimu, wazazi wengi sasa hivi wamekuwa wakilipia Walimu wao ili wawafundishe watoto wao. Kwa hiyo kulipia kunamwongezea mzazi gharama ya Elimu, kwa hiyo niombe sana Serikali ili tupate output nzuri ni lazima tuwekeze na uwekezaji hatuna kwa kukwepea lazima tuajiri, tuweke mikakati ya dhati katika kuajiri Walimu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona katika kupitia Mpango wetu ni upande wa kilimo. Naomba ninukuu kwamba; “Kuanzia huko nyuma hadi kufikia mwaka 2000 mauzo ya bidhaa zetu kwenye kilimo, mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi yametawaliwa na usafirishaji wa malighafi bila kuongezea thamani. Hali inayosababisha ukuaji wa uchumi kutoendana na kasi ya kupunguza umaskini na ajira hususani vijijini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nime-base tu kwenye kilimo, hili ni la kweli, lakini niishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu imeendelea kuboresha Sekta ya Kilimo kwa namna mbalimbali, lakini hili la kuongeza thamani bado tunatakiwa kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao yetu ni kweli kabisa tunasafirisha au tunauza yakiwa ghafi hali ambayo inatupunguzia sana mapato Serikalini lakini kwa Mwananchi mmojammoja na hali ya umasikini sasa imeendelea badala ya kuwa inapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kwa sababu thamani hii tutaipata kupitia viwanda vidogovidogo vingi, hivyo, Serikali ijikite katika Mpango wa namna ya kufufua viwanda ambavyo vimekufa hususani Viwanda vya Korosho. Ukienda kwenye maeneo mbalimbali yanayozalisha korosho mathalani ukienda Mtwara, Newala na Masasi kuna Viwanda vya Kubangua Korosho vilijengwa huko nyuma. Sasa hivi vile viwanda havifanyi kazi matokeo yake bado tunauza korosho ghafi ambazo hazina afya sana kwa mkulima. Kwa hiyo niombe sana ufufuaji wa viwanda vyetu ufanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali pia upande wa kilimo kwenye zao la korosho wamekuja na mpango wa kujenga Kiwanda kikubwa cha Korosho, industrial park kule Nanyamba, lengo la kiwanda kile ni kuhakikisha kwamba korosho zitakazozalishwa zinaenda pale zinabanguliwa, tunasafirisha sasa na kuuza korosho ambazo tayari zimeshaongezeka thamani. Kwa hiyo ni mpango mzuri ambao kama utasimamiwa sawasawa utatutoa sisi hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko yangu tu kidogo ni kwamba naona kuna changamoto, pamoja na Mpango mzuri wa Serikali kujenga kiwanda hiki, uzalishaji wa zao la korosho unazidi kupungua, kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais kwamba ametuletea pembejeo, ambazo wakulima wamezitumia lengo lilikuwa kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametangulia hapa Mheshimiwa Mhata, ametaja mwaka 2021 Tanzania nzima tuliuza tani laki tatu, lakini 2022 tani laki moja na themanini na mbili, mwaka huu hatujui tutauza tani ngapi? Sasa najiuliza tu peke yangu kwamba tumeshaweka mkakati wa kujenga kiwanda kikubwa pale Nanyamba kwa ajili ya korosho, sasa tusipofanya utafiti wa kubaini ni nini kinaangusha au kinaporomosha zao letu la korosho nadhani kiwanda kile hakitaleta tija ile ambayo tulikuwa tunaifikiria. Tukumbuke kwamba ni uwekezaji mkubwa sana ambao umefanyika, kwa hiyo niiombe sana Serikali, kwenye Mpango huu tuweke kipengele cha kufanya utafiti wa anguko la zao la korosho. Iwepo kabisa, ili tukishafanya utafiti tukagundua, basi uwekezaji wetu utaenda vizuri kama vile ambavyo tunatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tunaweza tukafanya utafiti, lakini akina nani watashuka kule chini, niombe pia mkakati wa kuajiri Maafisa Ugani ambao wataenda kufika mpaka ngazi ya vijiji kule chini ili kuinua uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo uwekezaji wa viwanda ambao tunao utaleta tija kwa Taifa lakini pia utainua uchumi wa mkulima mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kwenye kipengele cha Sekta ya Usafirishaji hususan reli ya kusini. Usafirishaji ndio ndio uti, tunaweza tukalima, tunaweza tukavuna, tunaweza tukafanya chochote, kama hatuna means nzuri ya usafiri, mazao, madini na bidhaa zozote hazitafika kule ambako tunatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba Serikali imewekeza sana kwenye Bandari ya Mtwara, zaidi ya bilioni 168 zimewekezwa Bandarini, lengo Bandari ile ifanye kazi vizuri ili ilete tija kwa Taifa hili. Nasikitika tu kwamba pamoja na kuweka kule sijaona kwenye Mpango ujenzi wa reli hii ya kusini. Leo hii ukienda Mtwara makaa kutoka Mchuchuma kule Liganga yanasafiri kwa njia ya barabara yanaharibu barabara kiasi kwamba tutakuwa tunatengeneza kila siku. Kwa hiyo niwaombe sana wenzetu wa Wizara kwenye Mpango huu tuwe na mkakati wa dhati wa kujenga reli kutoka Mchuchuma na matawi yake ya Liganga hadi Mtwara ili tuweze kusafirisha bidhaa kwa kupitia reli na kupunguza uharibifu wa barabara ambao unajitokeza siku hadi siku.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi, lakini pia niendelee kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na wale wote waliosaidia kuandaa hotuba ile. Nimeipitia hotuba yake, lakini naomba nami nichangie baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la watumishi, ambao ni walimu. Nilipata kusikia kuhusu ajira mpya za walimu kwamba sasa hivi Wizara imeweka mpango kwamba anayeomba ajira ya walimu anataja sehemu ambako anatakiwa kwenda kufanya kazi. Yaani kwenye application, katika maombi yake anaandika, mimi nataka kwenda sehemu fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo ni zuri, lakini linaweza kuwa na changamoto kwa upande mwingine kwamba kuna maeneo hali yetu, maeneo yetu tunayafahamu, kuna maeneo miundombinu ni hafifu kiasi kwamba hayatapata watu wa kuomba moja kwa moja. Katika mazingira hayo kuna maeneo yatanufaika, yatapata watu wengi na kuna maeneo yatakosa kabisa watu wa kuomba kutokana na hali ya kijografia. Kwa hiyo, naomba tuangalie upya, wazo ni zuri kwamba litapunguza ile hali ya mtu akishapangiwa eneo, anakwenda kuomba abadilishwe, lakini italeta athari kwa upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la uhaba wa walimu katika maeneo yetu. Sasa hivi nchi yetu iko kwenye uchumi wa kati, lakini tunataka tutoke hapo. Katika hali hiyo ni lazima kujiimarisha kuwekeza katika elimu ili hivyo ambavyo tunavitarajia viweze kwenda vizuri. Kuna uhaba mkubwa sana wa walimu katika shule zetu hasa za msingi pamoja na sekondari. Maeneo mengi ambayo yameadhirika ni yale ambayo yapo remote sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukija kwenye Jimbo la Newala Vijiji, kutokana na umbali kati ya kijiji na Kijiji; na sera yetu ni kwamba kila kijiji kiwe na Shule ya Msingi, unakuta jumla ya wanafunzi katika Shule ya Msingi kwenye shule fulani iliyopo katika kijiji fulani haizidi 100. Hesabu zinazopangwa kwa ratio ya mwalimu na mwanafunzi ni mwalimu mmoja na wanafunzi 45. Kwa hiyo, unakuta shule hiyo; mathalani shule yenye wanafunzi 80 au 90 inakuwa na walimu wawili tu, lakini ina madarasa kuanzia awali mpaka la Darasa la Saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu hao wana mzigo mkubwa sana. Kwa hiyo, naomba tuangalie, sawa ratio ni hiyo, lakini naiomba Wizara na kuishauri iangalie upya maeneo yale ambayo yako mbali lakini yana uchache wa wanafunzi ili angalau walimu waweze kuongezwa kwenye maeneo hayo na watoto wapate stahiki yake ili Tanzania ya viwanda iweze kuendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naiu Spika, ukienda kwenye afya, kuna uchache pia wa watumishi katika maeneo hayo. Unaenda kwenye Dispensary unakuta mtumishi ni mmoja, anahudumia watu wote; wajawazito awapime yeye, wagonjwa wa Malaria awatibu yeye, kila kitu ni yeye.

Mheshimiwa Naiu Spika, kama binadamu anachoka, wakati anapochoka, anakuja mgonjwa ambaye anatakiwa apatiwe huduma ya haraka, naye ana mlundikano mkubwa wa wagonjwa, anashindwa. Anaposhindwa, mgonjwa analalamika kwamba sijapata huduma ipasavyo; lakini siyo kwamba kwa matakwa ya yule ambaye yuko pale anatoa huduma, ni kwa sababu ya uchache wa watoa huduma katika eneo lile, wagonjwa hawapati matibabu stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara iangalie eneo hili ili wananchi wapate huduma ipasavyo. Ukienda kwenye Jimbo la Newala Vijijini hali ya Watumishi wa Huduma za Afya ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ukosefu wa bei za uhakika kwenye mazao mchanganyiko hasa Mbaazi, Njungu pamoja na Mihogo. Wananchi wanajitahidi sana kulima, lakini mazao hayo hayapati bei. Matokeo yake kule kwangu Newala vijijini wanaamua kuhama makazi yao, wanaenda mikoa ya jirani kulima ufuta angalau ambao una nafuu ya bei. Matokeo yake, maendeleo ya Newala Vijijini yanazidi kuzorota; na kwa sababu wazazi wamehama, wanaondoka na watoto wao na kwa hiyo, kunakuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi na mimba zisizotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo iangalie suala la bei ya mazao mchanganyiko kwa jicho la kipekee ili wananchi watulie kwenye maeneo yao waweze kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la TARURA ambalo jirani yangu Mheshimiwa Cecil ameliongea. Hali ya barabara zinazohudumiwa na TARURA kule kwetu siyo nzuri sana. Hatuwalaumu wao, lakini tatizo ni fedha chache ambazo zipo katika mfuko huo. Barabara nyingi hazipitiki. Wakulima ambao wanazalisha mazao yao pembeni au walioko pembeni mipakani mwa Newala na Wilaya jirani wakati mwingine wanashindwa kusafirisha hasa zao la Korosho kutoka kule wanakolima kuleta kwenye maeneo yao ili wauzie kwenye vyama vya msingi ambavyo viko kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake Jimbo la Newala Vijijini kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu ya barabara nzuri, linajikuta linapoteza mapato kwa sababu wanalazimika kwenda kuuza mazao yao kwenye wilaya na vijiji vya jirani hatimaye tunakosa mapato. Hasa ukienda Kata ya Mikumbi; barabara ya Mikumbi - Mpanyani haipitiki, barabara Namdimba - Chiwata haipitiki, barabara Mkoma - Chikalule haipitiki na barabara nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana suala la TARURA liongezewe mapato ili barabara ziboreshwe na Jimbo la Newala vijijini liweze kupata kile ambacho kinatarajiwa kutokana na mazoa yanayolimwa na wananchi wa jimbo hilo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Nianze kuwapongeza Waziri na timu yake lakini pia nimpongeze Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa hotuba yake. Kipekee, niishukuru Serikali pamoja na Wizara kwa kutupatia fedha shilingi bilioni moja sisi Newala Vijijini kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, Wizara ya Afya inakabiliwa na changamoto nyingi sana hasa kwenye maeneo yetu. Nianze na suala la ukosefu wa nishati ya umeme katika yale maeneo ambayo huduma za afya zinatolewa lakini hawajafikiwa bado na miradi ya umeme au pia mradi wa REA nao haujafika, kuna changamoto kubwa sana katika utoaji wa afya katika maeneo hayo. Katika maeneo mengi unakuta kuna zahanati zinatumia solar ambazo hazikaguliwi kiasi kwamba zinakufa matokeo yake wagonjwa wanaokwenda kupata huduma pale wanakosa huduma ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, akina mama wajawazito muda wa kujifungua haupigi hodi au hauchaguzi wakati mwingine wanakwenda kupata hizo huduma nyakati za usiku matokeo yake kituo kina giza lakini mama mjamzito anatakiwa ajifungue hapo. Inambidi mama mjamzito pamoja na uchungu alionao awashe tochi yake ya siku ammulikie mtoa huduma anayemsaidia kwa wakati huo. Mimi ni mzazi najua uchungu ulivyo, napata shida sana wakati mwingine wa kutambua namna gani mama huyu anaweza kumulika tochi amsaidie mzalishaji wakati yupo kwenye maumivu makali. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara iangalie kwa jicho la kipekee maeneo kama hayo ili ufumbuzi upatikane akina mama wapate huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dunia sasa hivi imekumbwa na magonjwa mengi ya milipuko ikiwemo suala la Corona. Wanaotoa huduma katika maeneo yetu ni madaktari wetu tunatambua lakini sijaona mkakati wa Serikali wa kutafuta PPE ya kuwakinga madaktari wanaokwenda kutoa huduma kwa wagonjwa. Matokeo yake madaktari wana-risk maisha, wananunua PPE wenyewe, kama hana uwezo anaingia kichwa kichwa kwenda kutoa huduma. Hii ni changamoto kubwa na tunawakatisha tamaa. Namuomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja yake aje na mpango mkakati wa namna gani atawasaidia madaktari kuwapatia PPE ili waweze kuwahudumia wagonjwa bila kupata shida au kuwa na hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nami niungane na wenzangu kuongelea yale makundi yaliyobainishwa katika Sera ya Afya kwamba watapatiwa huduma za afya bure. Hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imebainishwa kwamba wazee zaidi ya miaka 60 watapata huduma bure, akina mama wajawazito pamoja na watoto chini ya miaka mitano. Hata hivyo, suala hili limekuwa ni kinyume kila ukienda kwenye mikutano sijui kama ni kwangu peke yangu unakutana na kero hiyo. Wazee wanalalamika hawapati vitambulisho matokeo yake wanashindwa kupata huduma ya afya. Sasa hawaelewi wapo kwenye dilemma, je, kilichoongelewa katika Ilani ilikuwa ni kwa ajili ya kuombea kura au kweli Serikali ilikuwa na nia thabiti ya kuwasaidia wazee hawa? Niombe sana Serikali pamoja na Wizara ijipange vizuri wazee wabainishwe wapewe zile kadi wapate huduma za afya kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilivyoeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la akina mama wajawazito limekuwa ni changamoto kweli kweli, kuanzia kadi za kliniki wanatakiwa wanunue wao wenyewe. Kadi ya kliniki ambapo ndiko tutaona maendeleo ya ukuaji wa mimba yake anatakiwa anunue lakini tumeshaji nasibu sisi kwamba tutawapatia huduma za afya bure. Kwa hiyo, inaleta mkanganyiko sana kwa sababu akina mama hawapati hizo huduma bure wala Watoto. Kwa hiyo, tunapokwenda tukasema kwamba huduma zinatolewa bure tunakuwa hatueleweki. Niungane na wenzangu Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja tunaomba uje na mpango mkakati utueleze namna gani au nini kauli ya Serikali kuhusiana na kundi hili la wanufaika wa huduma bure za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niungane na wale walioongelea suala la CHF Iliyoboreshwa. Mkakati ulikuwa mzuri lengo la Serikali lilikuwa zuri lakini wale waliokata kadi kwa ajili ya kupata hizo huduma hawapati …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imegonga.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iangalie na kufuatilia ili kulinda afya ya watoto wadogo wanaokwenda kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo. Wapo baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo ambao wamepata vibali isivyo halali kwani nimeshudia watoto wakirundikwa kwenye vyumba visivyokidhi haja kiafya wakati wa mchana wanaposubiri wazazi kuwafuata. Wanarundikwa kwenye vigodoro, wanalazwa kama samaki. Fuatilieni vituo hivyo hususani mkoa wa Dar es Salaam, hali si rafiki.

Mheshimiwa Spika, watoto hawa wengi ni kati ya mwaka mmoja hadi miaka minne, lakini cha kushangaza vituo hivyo vinachanganywa na watoto wa umri wa miaka mitano hadi sita wanaotakiwa wawe pre-school. Matokeo yake ni watoto wadogo wanaweza kulawitiwa na hawa watoto wenye umri usiotakiwa kuwa kwenye hivi vituo vya kulelea watoto. Tunaomba Maafisa Ustawi wa Wilaya wafuatilie na kukagua kwa kushtukiza vituo hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi, awali ya yote niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa uwasilishaji pamoja na timu yake yote. Lakini pia Kamati; lakini kipekee kabisa niipongeze Serikali kwa mwaka huu wa 2021 kwa kupeleka michezo ya UMITASHUTA pamoja na UMISETA katika Mkoa wa Mtwara kwa sababu kwa kufanya hivyo inafungua milango ya fursa kwa Wana Mtwara, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye mchango, Tanzania wote tunatambua kwamba imekuwa ikishiriki mara nyingi kwenye michezo mbalimbali ya kitaifa pamoja na kimataifa. Kuna wakati huwa tunafanya vizuri, lakini kuna wakati hatufanyi vizuri sana. Lakini ukiangalia ni kwa nini hatufanyi vizuri sana kuna sehemu kuna gap.

Mheshimiwa Spika, Tanzania pamoja na Serikali yake kwa ujumla imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika maandalizi ya michezo ya UMISETA, pamoja na UMITASHUTA jambo ambalo ni jema kwa sababu tunataraji wanamichezo hawa ambao wanaenda kucheza michezo ya kimataifa watokane na maandalizi ambayo yanafanyika katika michezo ya UMISETA pamoja na UMITASHUTA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukianglaia Serikali inatenga shilingi 600 kwa wanafunzi wa shule za msingi kila mwanafunzi mmoja kwa ajili ya maandalizi ya UMITASHUTA na shilingi 1,500 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari, ni jambo jema tunawashukuru na kwa kweli wanafunzi wanahamasika na wanafanya vizuri. Niwapongeze TFF kwa sababu wakati wa michezo hiyo wamekuwa wakiwabaini wanafunzi wanaofanya vizuri wanawaweka kwenye database yao pamoja na CHANETA na watu wa basketball.

Mheshimiwa Spika, lakini pale michezo ambayo inashindanishwa ni mingi ipo pia michezo ya ndani wale wa michezo ya ndani sijaona mkakati madhubuti wa Serikali kuwashirikisha au kuwachukua katika database yao ili waweze kuwatumia baadaye. Nishauri sana Serikali kwamba michezo ya ndani ni sehemu ya michezo na yenyewe ichukuliwe kwa uzito wake Watoto wale nao wapate kushiriki katika michezo mingine hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wale wanafunzi wanaomaliza wanaoshiriki michezo ya UMISETA pamoja na UMITASHUTA wakishamaliza shule hakuna wanakoelekea, wamejitahidi wamefanya vizuri, wamemaliza masomo yao wanarudi wanakaa nyumbani hakuna muendelezo wa michezo kwa wanafunzi wale. (Makofi)

Sasa swali la kujiuliza ni kwamba Serikali iliwekeza kwa kiasi kikubwa, wanafunzi wakajitoa, maandalizi yakafanyika, lakini mwisho wa siku fedha za Serikali ambazo zimeenda kuwekeza katika michezo hiyo hazileti tija kwa sababu wanafunzi wanapomaliza hakuna wanakoelekea tena ukiondoa wale wachache wa football, netball pamoja na basketball.

Kwa hiyo, niombe Serikali sasa iwe na mkakati madhubuti wa kuhakikisha wale wanafunzi wanaomaliza shule wanachukuliwa au wanaendeleza michezo yetu mbalimbali ili baadaye iweze kutuletea tija katika Taifa katika fani hiyo ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niongelee pia suala la utamaduni; hii ndiyo Wizara ambayo inasimamia kwa ujumla masuala yote ya utamaduni, utamaduni kwa maana ya vyakula, maadili na mambo yote yale ambayo yanakusanyika huko, lakini tumeona mmomonyoko mkubwa sana wa kimaadili sasa hivi katika nchi yetu. Niiombe Wizara kwa sababu ni Wizara ambayo ina vyombo vya habari; ina television pamoja na magazeti na redio kwa kupitia vyombo vyake vya habari waanze kurejesha au watoe elimu kuhusiana na suala la maadili katika nchi hii, hali iliyoko ni mbaya hata Mheshimiwa Rais alisema wakati anaongea na wazee wa Dar es Salaam, mwanafunzi au kijana amekaa kwenye kiti, lakini hampishi mama mjamzito wala wazee na hiyo inatokana na mmomonyoko wa maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutumie vyombo vyetu tulivyo navyo kutoa elimu ili suala la maadili liweze kuendelezwa katika nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna Mtanda.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, maeneo ya utalii katika Wilaya ya Newala nikianza na utalii; Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba mtume tume ya wataalamu waje Jimbo la Newala Vijijini kuona maeneo mazuri ya utalii yaliyopo Jimbo la Newala Vijijini katika Kata ya Chilangala ambako kuna maporomoko mazuri sana ya utalii katika Mlima Miyuyu.

Aidha kwenye Jimbo la Newala Mjini lipo Shimo la Mungu eneo zuri kabisa la utalii. Tunaomba mje muwekeze katika Wilaya ya Newala kwenye masuala ya utalii.

Pia Wilaya ya Newala kuna kivutio kizuri sana cha utalii wa utamaduni wa Kimakonde kuanzia ngoma na vyakula. Katika Jimbo la Newala Vijijini katika Kata ya Mchemo huwa kuna maadhimisho ya siku ya utamaduni wa Kimakonde, tunaomba Wizara yako ituwezeshe kuimarisha sherehe hizo, pia mje mjionee siku hiyo maalum. Kama Wana-Newala tupo tayari kushirikiana nanyi katika kila hatua.

Mheshimiwa Spika, changamoto kati ya TFS na wananchi wa Kata ya Chilangala; naomba kuuwasilisha kwenu mgogoro unaofukuta kati ya wananchi wa Kata ya Chilangala na TFS ambapo mwezi Aprili mwananchi mmoja amefariki katika harakati zitokanazo na mgogoro wao kutotatuliwa hali iyoleta kadhia hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Nishari.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nitoe pongezi nyingi kwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati pamoja na watendaji wake wote. Pia niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuasisi suala la mradi wa umeme vijijini kwani umepunguza kwa kiasi kikubwa sana kero ya umeme ambayo ilikuwa inavikumba vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jimbo la Newala Vijijini. Wote tunajua kwamba umeme ni ajira, biashara, ulinzi lakini pia ni afya. Jimbo la Newala Vijijini lina jumla ya vijiji 107, kati ya vijiji hivyo ni 54 tu ndiyo vyenye umeme, vijiji 53 havina umeme sawa na asilimia 49.53. Kuna Kata sita katika hivyo vijiji 53 ikiwemo Kata ya Chitekete ambayo Mbunge mimi natoka haina umeme niko gizani. Kata nyingine ni Nakahako, Mpwapwa, Nandwahi, Mkoma 2 na Nambali, kata hizi hazina kabisa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ujazilizi wa vijiji vile ambavyo mradi wa REA umepita. Mheshimiwa Waziri una kazi kubwa ya kufanya kwa sababu kama walivyotangulia kusema katika vijiji ambavyo umeme umepita vingi wanauona umeme umekaa kama kamba ya kuanikia nguo, haujashuka kwenye nyumba za wananchi. Ukienda Kata ya Mdimba inahesabika kwamba ina umeme lakini Mdimba pale ambapo ndipo Makao Makuu ya Kata umeme haujashuka kabisa na ni kero kubwa wanasumbua kila siku. Tunashukuru tumepata mkandarasi, niombe sana Mheshimiwa Waziri msimamie kwa karibu kwa sababu hali iliyopo inahitaji usimamizi otherwise ile miaka miwili ambayo tumejipangia kwamba vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme kwa hali iliyopo Newala Vijijini tunaweza tusifanikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtwara sasa ameshusha neema ya madini. Tumesikia kuna graphite kule Chiwata ambayo na mimi pia inanigusa kwa namna moja au nyingine. Ili mradi ule uweze kufanyiwa kazi vizuri tunahitaji umeme wa uhakika. Kulikuwa na mpango ule wa kujenga power station ya megawatt 300 pale Mtwara, tunaomba wakati unakuja kuhitimisha hoja yako utuambie mpango hule umefikia wapi kwa sababu kupitia mpango ule tutakuwa na uhakika kwamba umeme wa kutosha utapatikana na miradi mingine mikubwa ya maendeleo kama viwanda pamoja na machimbo vitaendeshwa bila bugudha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia na mimi niongelee suala la kukatikakatika kwa umeme, hali ilikuwa mbaya sana kwa Mkoa wa Mtwara lakini niishukuru Serikali ilifanya juhudi kubwa sasa hivi umeme unakatika lakini nafuu hipo. Watu wa TANESCO Makao Makuu, watu wa Kanda, TANESCO Wilaya waliweka kambi kuhakikisha kwamba tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Mtwara linapata ufumbuzi.

Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba tulikwambia suala hilo na wewe ukalifanyia kazi na tunashukuru ulikuja ukaona ile hali ukatuma hiyo timu ikaja kuhakikisha kwamba suala la kukatikakatika kwa umeme basi linaisha Mkoani Mtwara. Niendelee kukuomba juhudi ziendelee kufanyika ili kukomesha kabisa suala la ukatikaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambayo ameendelea kuipa fedha Wizara ya Kilimo ili kuongeza uzalishaji katika mazao mbalimbali yakiwemo ya chakula na biashara, lakini pia niwapongeze pia viongozi wa Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuisimamia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu zao la korosho kwa upande wa viatilifu; tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutupatia pembejeo bure kwa wakulima wetu. Naomba Serikali isimamie ubora wa pembejeo zinazopelekwa kwa wakulima wetu. Zipo dosari chache za kiutendaji kutoka kwa wasambazaji wetu, kufuatia ripoti ya Tume iliyoundwa kuchunguza mwenendo mzima wa zao la korosho, yapo maelezo ya dawa isiyostahili kwenye zao la korosho ambayo msimu uliopita walipewa wakulima. Sumu ambayo ni kwa ajili ya maua ya rose na mbogamboga wamepewa wakulima wa korosho. Matokeo ya dawa za namna hii ni kuharibu mimea na kuathiri uzalishaji. Tunaomba dawa ile kwa mamlaka yenu wakulima waarifiwe wasiitumie na zoezi hili lifanyike mapema kwa kuwa huu ndio msimu wa maandalizi ya mashamba.

Mheshimiwa Spika, kuhusu waatalam wetu tulionao site (Maafisa Ugani) wapewe mafunzo ili nao wajue namna ya kutumia viatilifu vinavyoletwa kwenye maeneo yao. Wengi hawajui, hali inayowafanya wakulima kulima kwa mazoea. Rejea maelezo ya taarifa ya Ripoti ya Tume iliyoundwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mfumo wa TMX niiombe Serikali isimamie vizuri mfumo huu ili ulete tija kwa wakulima. Tusiruhusu watu wenye maslahi binafsi kuuingilia mfumo huu, isije wakaja wale wanunuzi wahuni waliokuwa wanajimilikisha makampuni zaidi ya kumi kwenye mtindo wa kulaza sanduku wakijifanya ni watu tofauti kumbe ni mnunuzi mmoja yule yule ndiye anajifanya makampuni kumi. Tuwe makini tusije tukaharibiwa na wajanja wachache.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mjengeko wa bei ya korosho, naiomba Serikali ijitahidi kututafutia masoko ya uhakika ya kununua mazao yetu. Aidha, suala la tozo katika bei ya korosho liangaliwe upya kwa sababu tozo nyingi zinaathiri malipo ya mkulima moja kwa moja. Mfano tunaposema shilingi 110 ya gunia analipia mnunuzi, sio sahihi kwa sababu mwisho wa siku kimsingi anayelipia ni mkulima.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uhakiki wa idadi ya miche ya mikorosho kwa wakulima; zoezi limegubikwa na sintofahamu nyingi. Wengi hawajakwenda mashambani wamekadiria tu, matokeo yake ni kutotosheleza kwa pembejeo tunayowapatia.

Mheshimiwa Spika, hitimisho, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia chochote kuhusiana na bajeti ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya pamoja na wasaidizi wake wote. Kwa kweli, ametuheshimisha sana wanawake wa nchi hii, wanawake sasa hivi wamekuja juu, wamepata ujasiri mkubwa, lakini yote hayo ni kutokana na mwongozo wake vile anavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri na timu yake yote, kwa namna ambavyo wameandaa bajeti. Bajeti ni nzuri, bajeti ambayo inawagusa wananchi wote wa nchi hii, kuanzia wakulima, wafanyakazi, wafugaji, pamoja na watumishi wote. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa namna ambavyo mmepokea maoni ya Wabunge, hatimaye mmeweka kwenye bajeti suala la fedha za Madiwani pamoja na Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa, kulipwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muhanga wa Madiwani. Katika Jimbo langu la Newala Vijijini, Madiwani waliomaliza muda wao wanadai Halmashauri posho zao, mpaka leo hawajapata. Kwa hiyo, sasa hii ni tiba, tunashukuru na tunatumaini kwamba Madiwani sasa watafanya kazi kwa moyo, watakuwa na ari kubwa kwa sababu wanajua unapofika mwisho wa mwezi watapata posho zao bila shida. Sasa katika hilo, nami nashauri kwamba tuangalie pia zile posho angalau ziongezeke kidogo kwa sababu kiasi kile kwa kweli ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye masuala muhimu, masuala ya ukusanyaji wa mapato. Natambua kabisa nchi hii ina miradi mikubwa ya Kitaifa inayotekelezwa ambayo inahitaji fedha nyingi. Pia ipo miradi katika Halmashauri zetu ambayo nayo inahitaji fedha za kutosha, lakini kuna Madiwani ambao watalipwa posho kupitia Serikali Kuu, kuna Maafisa Tarafa, kuna Watendaji wa Kata, fedha hizi ukiangalia zinatakiwa zikusanywe ili hii miradi pamoja na hizi posho ziweze kupatikana. Kama hazitakusanywa vizuri, kwa usimamizi imara, haya ambayo yamewekwa kwenye bajeti yanaweza yasitekelezeke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tuweke namna nzuri ya ukusanyaji wa mapato ili yasivuje, tuweze kutekeleza miradi yetu kwa ufanisi mkubwa. Naomba nitoe mfano mdogo. Kupitia Ripoti ya CAG hii ambayo ameitoa ya mwaka 2019/2020 kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 ambazo zilikusanywa nje ya mfumo kupitia katika vyanzo mbalimbali vya mapato. Sababu ambayo CAG ameitoa ni kwamba fedha hizi zilipita nje ya mfumo kwa kukosekana kwa mashine za POS. Pia kulikuwa na fedha nyingine ambazo zilikuwa zinatumika, zile fedha mbichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana haya, matatizo ya POS tujiimarishe sasa, tuhakikishe tuna vifaa vya kutosha ambavyo vitaenda kutumika kila eneo linalohusiana na ukusanyaji wa mapato yetu ili malengo yetu yakapate kutimia vile ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, naipongeza sana Serikali kwa kuamua kwa dhati sasa kuanza mpango wa utoaji wa huduma za afya kwa maana ya Bima ya Afya kwa wananchi wote. Ni jambo jema kwa sababu Taifa ambalo litakuwa na wagonjwa wengi, basi halitaweza kuzalisha vile ambavyo tunatarajia. Kwa hiyo, kupitia mpango huu ni matumaini yangu kwamba wananchi watakuwa na afya bora, watafanya kazi zao vizuri na hatimaye Taifa litaweza kujipatia fedha nyingi katika kutekeleza miradi. (Makofi)

Mheshiiwa Mwenyekiti, sasa hapa naomba nitoe rai kwamba, kwa sababu tumeshaweka huo mkakati, tuandae namna ambayo wale wanaokwenda kukusanya fedha za Bima ya Afya au watakaosimamia ujazaji wa fomu za Bima ya Afya wapatiwe mafunzo maalum, kwa sababu sasa itasambaa nchi nzima tofauti na ilivyo sasa hivi kwamba wanaopata huduma ya Bima za Afya ni wachache kuliko tunavyotarajia kama Taifa kwamba sasa watu wote wanakwenda kupata hizi huduma za Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naongea hivyo? Naongea hivyo kwa sababu ukienda kwenye Ripoti ile ya CAG, alibaini madai ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1 ambayo Bima ya Afya yanaidai Serikali kwa sababu tu ya changamoto ya zile kasoro za ujazaji wa fomu. Sasa ukiangalia wanaopata hizo huduma sio wengi kiasi hicho, lakini fomu ambazo zina shida ya kulipwa fedha zake ni zaidi ya shilingi bilioni 2.1. Je, Watanzania wote watakapoingia kwenye huo mfumo, ni kiasi gani cha kasoro kitasababisha upotevu wa dawa kwa kiasi kikubwa? Kwa hiyo, naomba sana mafunzo yatolewe, watu wawe na ujuzi wa kujaza zile fomu ili changamoto hizi zisije zikajitokeza kule tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza tena Serikali, kwa kweli katika bajeti hii imeweka mambo mengi sana kuhusiana na masuala ya kilimo. Ukienda kwenye kilimo cha mihogo wameweka namna ambavyo watasimamia mazao ya mihogo, lakini pia hata kwenye korosho. Sasa changamoto yangu ni viwanda. Katika nchi hii kuna baadhi ya viwanda havifanyi kazi sawasawa. Kule kwetu Newala ambako tunazalisha korosho kati ya tani 20 hadi 30 kwa mwaka hatuna kiwanda cha uhakika cha kubangua korosho ili kuithaminisha korosho hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kiwanda cha Agrofocus, hiki kimebinafsishwa, lakini tuna kiwanda cha Micronox; kiwanda hiki kimepewa mtu ambaye uwezo wake tunadhani ni mdogo kwa sababu, kwa mfano msimu uliopita hakuwa na malighafi. Inaonekana hakuwa na fedha, kwa hiyo, yale ambayo tulitegemea tuyapate kutokana na kiwanda hiki yanashindwa kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vile wakati vinafanya kazi kule Newala, zaidi ya asilimia 80 ya waliokuwa wanafanya kazi pale ni wanawake. Sasa hivi viwanda havifanyi kazi, wanawake wamekaa chini, wanashindwa kuwasaidia akina baba, wanashindwa kutimiza majukumu yao. Naiomba sana Serikali, nimeangalia pia kwenye bajeti sijaona mkakati wa dhati wa namna ya kuinua viwanda vile vikaweza kufanya kazi kuanzia msimu unaofuata. Kwa hiyo, changamoto hii maana yake bado ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna taarifa kwamba kulikuwa na mnunuzi kutoka nje alitaka kununua kiwanda kimojawapo na Serikali ina taarifa hiyo. Naomba basi Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kufanya majumuisho utuambie hatima ya ununuzi wa kiwanda kile imefikia wapi? Hii itawasaidia wananchi wa Newala kujiajiri kupitia ubanguaji wa korosho wanazozizalisha kwa wingi katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo linaleta changamoto kubwa katika Mikoa au Wilaya ya Newala kwa ujumla ni suala la barabara. Wilaya ya Newala ipo Kisiwani, haina hata barabara moja ya lami kati ya wilaya na wilaya au wilaya na mkoa inayofika Wilaya ya Newala. Barabara zote ni za vumbi, lakini ni wakulima wazuri sana wa korosho na mihogo. Kwa hiyo, usafirishaji wa mazao yao ni changamoto kubwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Serikali ilikuwa kuunganisha barabara za mkoa na mkoa kwa kiwango cha lami. Wilaya ya Newala inaunganisha Mkoa wa Lindi kupitia Mtama kwenda Mtwara, lakini barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali mpaka Mtama yenye kilometa 74 ni ya vumbi. Tunaishukuru Serikali imeshajenga kwa kiwango cha lami kilometa 22. Tunaomba Serikali iboreshe barabara hii, ijengwe kwa kiwango cha lami sasa ikamilike ili wananchi wa Newala ambao wanapata huduma zao nyingi katika Jiji la Dar es Salaam nao waweze kutumia barabara hii ikiwa katika mazingira mazuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai ambayo ametupatia. Lakini kipekee niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa wasilisho zuri la hotuba ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi ambayo imefanya jitihada kubwa, ya kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ambayo ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu. Wamefanya hivyo, tumeshaona, wote ni mashahidi. Ukienda Mkoa wa Dar es Salaam utakuta Daraja la Tanzanite lakini pia kuna Flyover mbalimbali, na katika maeneo mbalimbali Serikali yetu imejitahidi kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Sababu ya kufanya hivyo ni kuchochea maendeleo ya wananchi na mtu mmoja mmoja kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, niende sasa kwenye sekta hiyo ya usafiri na usafirishaji katika Mkoa wetu wa Mtwara. Tuna kilio cha muda mrefu cha barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi, kilomita 210. Tunaishukuru Serikali kwamba tarehe 25 Novemba, 2021 ilisaini mkataba wa mkopo wa shilingi bilioni 268 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika; tunashukuru kwa hilo. Sasa, ni yapi matarajio ya wananchi ambao wameteseka muda mrefu? Wananchi wanatumia gharama kubwa sana za nauli kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa sababu ya ubovu wa barabara. Kwa hiyo, wanachotarajia wananchi hivi sasa baada ya kusaini mkopo ule ni kuona ujenzi unaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kusini wameshaumwa na nyoka na sasa wakiona jani hushtuka, bado hawajaamini kama kweli barabara ile pamoja na kusaini mkopo itajengwa. Hii ni kwa sababu ahadi nyingi zilishapita huko nyuma, tukaelezwa pia na idadi ya wakandarasi, ambao wanakwenda kujenga barabara hizo, lakini ilipita na ahadi hizo ziliyeyuka. Sasa, leo tumeshapata hizo fedha, tunachotarajia sisi wananchi wa Kusini ni kuona kwamba barabara ile ya kiuchumi, ambayo inasafirisha zao la korosho linaloipatia nchi hii fedha nyingi za kigeni; ni barabara hiyo sasa kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kujengwa kwa barabara ile kuna manufaa sana. Kwanza kutachochea maendeleo ya Bandari ya Mtwara ambayo Serikali imewekeza fedha nyingi lakini matumizi yake hadi sasa sio ya kuridhisha. Lakini vilevile kutokana na barabara na Bandari ile maendeleo ya wana Kusini hasa wa maeneo ya Mtwara yatachangamka, kutakuwa na kima mamalishe watapika pale Bandarini na pia wauzaji wa bidhaa mbalimbali nao watauza kwa sababu bandari sasa itakuwa active.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya miundombinu ya usafiri katika Mikoa ya Kusini kwa ujumla bado si nzuri, sio nzuri kabisa kiasi kwamba umasikini unazidi kuongezeka kwa wananchi badala ya kutoweka. Sasa hivi barabara ya kutoka Newala kwenda Amkeni – Kitangali – Mtama; barabara ile hata wale waliokuwa wanapeleka mabasi yao hawapeleki tena. Mabasi yanayopita kwenye njia hizo yameharibika, mabasi ni mabovu hayamalizi safari. Kwa hiyo, wananchi wanazidi kudidimia wafanyabiashara hawawezi kupeleka magari yao kwa sababu, wanakwenda kuangamiza hayo magari yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, effect ya hivyo ni kwamba uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unazidi kudorora. Niiombe sana Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi ifanye kweli, miundombinu ile iboreshwe ili uchumi wa wananchi wale nao upate kuchangamka.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya Mtwara iko mingi lakini hiyo mingi haitekelezeki. Kulikuwa na suala la reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay, tuliambiwa kwamba mwaka 2019 Juni mkataba ungesainiwa wa ujenzi wa reli ile lakini mpaka leo hakuna kinachoeleweka. Lakini pia, kuna Mtwara Development Corridor, imesemwa sasa hivi imepotea. Haya mambo yakiendelea hivi tunazidi kuwapoteza watu ambao wangezalisha chakula lakini pia tungepata manufaa makubwa sana kama ile miundombinu ya usafiri ingeweza kuboreshwa. Tunazo tani nyingi tu za makaa ya mawe kutoka Mchuchuma ambayo yangepita kwenye reli kwenda kwenye Bandari ya Mtwara. Hii kwa sasa haiwezekani kwa sababu reli hiyo haijajengwa hadi hivi tunavyoongea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la bandari bado ni kizungumkuti. Pamoja na Serikali kuwekeza fedha nyingi, kitu pekee ambacho kilikuwa kinapita kwenye Bandari ile ni korosho peke yake. Sasa korosho ina msimu, si muda wote. Sasa hivi tunamshukuru Dangote kwamba cement yake anataka kupitishia kule. Lakini basi tuchangamshe na hivi vingine ili Bandari ile ilete manufaa ambayo Serikali imeikusudia kwa wananchi wa Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kuhusu suala la umeme. Umeme si anasa, umeme ni ulinzi kwa sababu wote tu mashahidi kinachoendelea nchi jirani ya Msumbiji wote tunakifahamu. Lakini wananchi wa Newala, hasa wa Newala vijijini wako gizani. Newala vijijini ina vijiji 107 lakini ni vijiji 33 tu ndivyo vyenye umeme. Vijiji 74 havina umeme. Sasa, vijana wetu wanajiajirije kama hakuna umeme katika maeneo yao? Lakini je, ulinzi na usalama wa wananchi wa Newala ukoje kama wanaishi gizani mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali ilituletea mkandarasi tangu Agosti mwaka jana, anaitwa Central Electrical International Limited. Lakini tangu akabidhiwe mradi mwaka jana Agosti, kati ya vijiji 74 ambavyo havina umeme amevipitia mpaka leo hii vijiji 21 tu. Na hivyo 21 si kwamba ameshasimamisha nguzo, bado mpaka leo sasa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kweli anafanyakazi kubwa pamoja na wasaidizi wake wote. Nimshukuru pia Waziri wa Afya kwa wasilisho zuri ambalo amelifanya pamoja na wasaidizi wake wote. Uchumi wa nchi yetu ukuaji wake unakwenda sambamba na masuala ya afya kwa wananchi wake. Kwa hiyo, kama afya haitatiliwa mkazo maana yake hata zile juhudi ambazo tunazifanya za kukuza uchumi wa nchi yetu hazitaleta matunda ambayo tunayatarajia. Kwa hiyo, afya ni kitu muhimu tuwekeze tuisimamie ili tuweze kupata tija ile ambayo Taifa inalitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende sasa kwenye changamoto. Changamoto ya kwanza kama ambavyo wametangulia kusema waliotangulia ni suala la uhaba wa watumishi katika kada za afya. Maeneo mengi hasa ya pembezoni watumishi wa kada hii ni wachache hali ambayo inaleta changamoto katika uletaji wa huduma zenye ufanisi katika maeneo hayo. Kwa mfano, ukienda kwenye Jimbo la Newala Vijijini tunao watumishi 119 tu ambao ni sawa na asilimia 19 ya mahitaji wa watumishi wa afya wanaohitajika katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala Vijijini. Hii ni hatari kubwa kwa sababu kuna watu wanafanyakazi ambazo hawajasomea. Kutokana na uchache huo utamkuta Nesi anaandika dawa huyo huyo akachome sindano ni hatari, tunahatarisha usalama wa wananchi wa Jimbo la Newala na maeneo mengine ambayo yana shida kama za Newala Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine inaleta uchonganishi kati ya wananchi na Serikali kwa sababu wananchi wanaohudumiwa wanaongea vibaya kwa sababu tu wanakosa huduma stahiki, lakini shida kubwa ipo kwenye uchache wa watumishi waliopo katika maeneo hayo. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu unafanya kazi kubwa sana kazi nzuri inaonekana umepata kibali cha kuajiri watumishi zaidi ya 10,000. Naomba sana angalia sana maeneo yale ambayo yana uhaba mkubwa wa watumishi ili na wao wakaweze kupata huduma kutokana na watumishi ambao watapelekwa katika maeneo yao ikiwemo pia na Newala Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni uchache wa nyumba za watumishi wa kada ya afya. Sawa, watumishi wako wachache lakini hawana maeneo ya kuishi hawana nyumba za kuishi. Ugonjwa hauchagui muda wala dakika sasa kama mtumishi yuko mbali anapatikana mbali, anamuhudumiaje mwananchi ambaye amepata shida eneo X ambalo ni mbali kutoka pale anapoishi? Lakini hata hivyo hizo nyumba chache zilizopo kwa mfano ukienda kwenye Jimbo la Newala Vijijini, tuna mahitaji ya nyumba 184 lakini tuna upungufu wa nyumba 140. Zipo nyumba 44 katika hizo nyumba 44 ni nyumba nne tu ndizo ambazo zina nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyumba ni chakavu hazistahili kwa kweli kuishi watumishi wale wakati mwingine wanakata tamaa, kwa namna ambavyo wanaishi yale maeneo ambayo wanatoka kwenda kuhudumia wananchi wetu. Nimuombe sana Waziri na timu yake tuangalie miundombinu ya nyumba kwa watumishi wetu wa Idara ya Afya ili na wao waishi sehemu nzuri na salama wapate moyo wa kwenda kutuhudumia, ili kupata ufanisi baadaye wa zile fedha ambazo Serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kupeleka huko lakini inakutana na watumishi waliokata tamaa ambao wanashindwa kutoa tiba vizuri kutokana na mazingira ambayo wanaishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo hilo haliko Newala Vijijini peke yake liko pia Newala Mjini liko pia na maeneo mengine ya Mtwara. Suala lingine ni mahitaji ya vifaa tiba pamoja na vitenganishi katika Jimbo la Newala Vijijini tunazo zahanati tatu ambazo zimekamilika, tunayo zahanati ya Mpwapwa, tunayo zahanati ya Nakahako, tunayo zahanati ya Hengapano. Zahanati zile tunaishukuru Serikali imesaidia kukamilisha maboma zimekamilika, tunaomba sasa kupatiwa vifaa tiba ili zikaweze kutoa huduma kwa wananchi wetu. Pia tunayo majengo ya OPD na maabara katika Hospitali ya Wilaya nayo tunayaombea dawa pamoja na vifaa tiba, ili ikaweze kutoa huduma katika maeneo ambayo yanahitajika kutoa huduma hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninalo pia linalohusiana na MSD niombe sana MSD iwe na dawa wakati wote ili kuondoa mkanganyiko kwa sababu, zahanati pamoja na hospitali zinapoomba dawa basi ikute MSD ina dawa kiasi ambacho haitagharimu tena suala la kwenda kutafuta Alternative Way ya kupata hizo dawa. Kuchelewa kupatikana kwa dawa kunaigharimu sana maisha ya wananchi wetu kiasi kwamba wengine inawezekana tungeweza kuokoa maisha yao, lakini kwa sababu dawa hazipatikani vituoni kutokana na ukosefu wa dawa kwenye MSD inakuwa ni changamoto ambayo wananchi wengi wanakwenda kupata shida jambo ambalo lingeweza kutatuliwa kama MSD ingekuwa na dawa wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuomba katika Kituo chetu cha Mkwedu ambacho kipo katika Jimbo la Newala Vijijini, tunayo Ultrasound iko pale lakini haina mfanyakazi/mtaalam tulishaomba muda mrefu. Pia Makamu wa Rais alishatoa maagizo mtaalam apelekwe pale mpaka leo tunavyoongea mtaalam hajapelekwa kile kifaa kimekaa pale kama mapambo hakifanyi kazi, wakati uhitaji wa wananchi wa kutumia kifaa hicho ni mkubwa sana sasa inasababisha kero na inawezekana pia kikaenda kuharibika kwa sababu hakitumiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi yake ya uhai, pia nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hasssan kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya wote tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya nasi tutawapa ushirikiano, tunaomba tu yale ambayo tutakuwa tunajadiliana basi ya ninyi mpate kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hii tunaona kabisa maeneo mengi ya pembezoni, Halmashauri za pembezoni Tanzania nzima zina upungufu mkubwa sana wa watumishi ukilinganisha na maeneo mengine, Serikali inaenda kuajiri Sekta ya afya na elimu watumishi 21,000, ombi langu kwa TAMISEMI pamoja na afya ni kuona kwamba tupange idadi ya watumishi hawa kulingana na uhitaji wa maeneo husika, siyo kusambaza tu kwasababu kila mmoja apate, kuna maeneo hali ni mbaya huduma haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Newala imepokea zaidi ya Bilioni 8.5, nini matarajio ya wananchi? Matarajio ya wananchi ni kuona kwamba thamani ya fedha iliyotolewa inafanana au inaenda sambamba na huduma inayopatikana katika maeneo husika, hilo ndiyo tarajio kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto ambayo inazifanya Halmashauri zetu zishindwe kufikia katika utoaji wa huduma iliyo bora. Mfano, ukienda kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala, upande wa afya watumishi mahitaji ni 526 waliopo ni 172 upungufu ni 354, hali ambayo inaleta malalamiko kati ya watoa huduma na wahudumiwa, kwa sababu kunakuwa na msuguano wale wahudumiwa wanaona hawafanyiwi ipasavyo lakini wakati mwingine ni kutokana na uchache wa watumishi waliopo, wanashindwa namna ya kujigawa ili waweze kutoa huduma ipasavyo. Kwa hiyo, niombe sana watumishi wa kada ya afya wapelekwe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Newala ili wakaweze kutoa huduma kwa wananchi kulingana na fedha ambazo Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali imekuwa ikizitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda elimu - Elimu ya msingi upungufu wa walimu ni 327 kwenye uhitaji wa 787. Kwa hiyo, unaona kwamba walimu waliopo msingi wanapata kazi kubwa sana, mzigo ni mkubwa wa ufundishaji na ikumbukwe kwamba mwalimu ili akafundishe lazima aandae somo, sasa Mwalimu huyu anafundisha Darasa la Kwanza, Darasa la Pili mpaka Darasa la Saba anawezaje kuandaa masomo yote, vipindi vyote ili akaweze kufanyakazi inayostahili. Kwa hiyo, tuangalie kwa jicho la pekee namna ambavyo upungufu huu unaathiri utoaji wa elimu iliyo bora kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekondari pia hali ni hiyo hiyo. Mzigo wa walimu ni mkubwa, mwalimu anafundisha Biology kuanzia kidato cha kwanza, cha pili, cha tatu cha nne. Fikiria mzigo ambao anaubeba, hajasahihisha bado, ukiacha kuandaa lazima asahihishe aone kazi ambayo imefanywa na mwanafunzi kama inaendana na kile ambacho amekifundisha, kwa hiyo unakuta mzigo anaobeba ni mkubwa kuliko hali halisi, kuliko uwezo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa fedha zile za elimu bila ada, inapeleka kwa wanafunzi hawa kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita sasa. Lakini kwa sababu ya hali ya upungufu wa walimu uliyopo inalazimika jamii kutafuta walimu wa kwao ili wakawafundishe watoto wao ku - cover lile gap, lakini wale wanaowafundisha hawatoki mikono mitupu lazima wazazi wachangishane, wawalipe walimu wale. Sasa katika mazingira hayo unakuta wazazi wanalalamika kwamba tunabebeshwa mzigo mkubwa na kwamba ile fedha ambayo tunaipeleka hawaioni ile thamani yake kwa sababu tu ya uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watumishi wa kada ya ualimu wangekuwepo wala hilo gap lisingeonekana. Niombe sana tupeleke walimu katika Halmashauri hizi za pembezoni. Pia tunao Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata, Jimbo la Newala Vijijini lina Kata 22 lakini ina Maafisa Maendeleo ya Jamii Wanne tu. Maafisa Maendeleo ya Jamii hawa ndiyo ambao wanaenda kusimamia zile fedha asilimia 10 inayoenda kwenye Halmashauri, kama hawapo nani atasimamia, matokeo yake fedha zinashindwa kurudishwa kwa sababu hakuna ufatiliaji.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwa mchango wako.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Kilimo. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niwapongeze Wizara kupitia Waziri wa Kilimo na timu yake yote kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya kwa manufaa ya nchi yetu. Niwapongeze pia Wizara kwa ruzuku mbalimbali katika mazao ya kilimo ambayo wameendelea kuitoa. Lakini pia niwapongeze kwa kurudisha export levy katika msimu wa mwaka jana; export levy ambayo ni msaada sana kwa wakulima, hasa wa korosho ambako ndiko zao lenye export levy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nimeenda kuangalia miongoni mwa malengo ya Wizara ni pamoja na kupunguza umasikini kwa asilimia 50 kwa wakulima ifikapo 2030. Ni wazo zuri, ni mpango mzuri. Lakini napata shida kidogo; ni namna gani tutafikia kupunguza umaskini kwa wakulima hawa kwa trend ambayo tunaenda nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kurudisha export levy kwenye zao la korosho tulifarijika sana, na tunaendelea kushukuru; faraja yetu ilikuwa ni kwamba, kumbe sasa zile tozo mbalimbali ambazo zinapunguza kiasi cha fedha ambazo mkulima wa korosho anapoenda kuuza zao lake zinaenda kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunashukuru kwamba tunapata pembejeo kwa ile asilima 50 ambayo inaenda kwenye tasnia ya korosho; lakini ile 50% ambayo inaenda kwenye mfuko mkuu wa Serikali tuombe sasa. Ili mkulima asibebeshwe mzigo mkubwa au apate bei ambayo italeta manufaa kwake na kupunguza umaskini, kama ambavyo tumetarajia kuupunguza, basi tunaomba zile tozo kwa mfano za CBT, TARI, task force zichukuliwe na Serikali ili mkulima anapoenda kuuza korosho yake basi aweze kupata angalau kitu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikorosho gharama ambazo mkulima anazitumia kuanzia kuandaa mashamba, palizi na shughuli zote mpaka aje kuvuna gharama zake ni kubwa mno. Gharama zile zinamfanya mkulima azidi kudidimia siku hadi siku. Kwa mfano kuna mwaka ambao korosho bei ilipanda kidogo kwenye soko, ikafikia kwa kilo shilingi 3,000 hadi 4,000. Ukienda yale maeneo ambayo yanalima korosho hali ilikuwa nzuri tulichangamka, watu walijenga nyumba bora na walikuwa wanapeleka watoto shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi imekuwa ni kinyume, wakulima wa korosho wamedidimia kwa sababu gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana, hali ambayo inazidi kudidimiza. Ndiyo maana nachelea kwamba, je kweli tutaweza kupunguza hiyo asilima 50 ya umaskini kwa hali ambayo tunaiona sasa hivi? Lazima mkakati wa dhati uwepo wa kuhakikisha kwamba zao hili linaenda kumuinua mkulima. Bila mkakati wa dhati itakuwa ni hadithi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ili kuthaminisha korosho hizo sasa hivi akina mama wengi wanabangua korosho zao ili wauze zikiwa katika hali ya thamani kubwa zaidi, lakini wanakosa namna ya kupata masoko. Korosho wanazo, wanamuuzia nani wanashindwa. Niombe, Serikali itakapokuja kuhitimisha ituambie mkakati wa kuwasaidia wakulima ambao wanabangua korosho zao ukoje ili wapate masoko. Wanashindwa branding, korosho zinabakia ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Serikali imetuambia kwamba, hadi kufikia Aprili 2023 imepeleka Marekani tani 74.19 zilizobanguliwa zenye thamani ya shilingi milioni 455.7, ni jambo zuri la kushukuru. Lakini sasa tuone ni namna gani Wizara itabeba, badala ya wabanguaji wakubwa peke yake tuwafikie wale wabanguaji wadogo ambao na wenyewe wanatamani siku moja korosho zao walizobangua wanaziuza na wana uhakika wa soko. Lakini pia wanauza hata huko nje. Wizara tukifanya hivyo tutakuwa tunawasaidia sana wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tunashukuru kwamba Serikali ilitupatia pembejeo za ruzuku kwenye msimu uliopita na kule nyuma pia. Lakini msimu wa mwaka jana, baada ya kuona changamoto zilizojitokeza kwenye msimu wa mwaka 2020/2021 mwaka jana Wizara ilitoa mwongozo wa namna ya ugawaji wa pembejeo zile za ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo ule ulileta shida kidogo katika utekelezaji wake. Nishauri Wizara, kwamba tunapoandaa miongozo hii tujaribu kushuka kulechini tukaone hali halisi. Mengi yanatendeka kwa kukaa mezani, hatujui uhalisia ulivyo kule chini kwa wazalishaji wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo ule badala ya kumnufaisha mkulima halisi wa korosho ambaye tulimtegemea ulienda kuwanufaisha wale ambao walikuwa wananunua kangomba. Wananunua ndio wao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ashante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachania kwa maandishi naunga mkono hoja. Ahsante (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuchangia machache yanayohusiana na masuala ya maji.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli, kazi anayoifanya ni kubwa na sisi Watanzania na sisi Wanamtwara na sisi Wananewala tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema sisi Wanamtwara, sisi Wananewala? Ametoka kuongea hapa Mheshimiwa Hokororo akautaja Mradi wa Maji ule wa Makonde ambao ni mradi wa muda mrefu, uliasisiwa na watu wa Finland muda mrefu, ukachoka, ukawa hauhudumii wananchi ipasavyo, mabomba yalishachoka sana. Awamu kwa awamu tukawa tunaomba fedha ili mradi huu ukapate kuboreshwa, lakini ilishindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso amefika Newala akaliliwa na wazee, yeye mwenyewe ni shahidi, kwa kero ya maji ambayo wananchi wa Newala walikuwa wanaipata, lakini tunashukuru sana Serikali ikatupatia bilioni 84.7 kupitia Mradi wa Miji 28. Kwa kweli, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fedha tumezipata. Matarajio ya Wananewala, Wanatandahimba na watu wa Nanyamba ambako mradi huu unapita ni kwamba, wanachotaraji ni kuona mradi unatekelezwa ipasavyo, unatoa maji, ili wananchi wa maeneo niliyoyataja sasa na wenyewe waanze kutumia maji ya bomba, maji yaliyo safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupeleka fedha hizo tunajua kazi zimeshaanza, maeneo ya kujenga matanki yameshaanza kusafishwa kwa kila eneo. Kwa mfano Newala, Newala Mji, pale Nambunga, Newala Vijijini, Nanda, Tandahimba, lakini pia na kule Nanyamba, tunatakiwa kuweka usimamizi wa dhati pamoja na kupeleka fedha kama usimamizi hautakuwepo, tija ya mradi hatutaipata. Sisi tunategemea kwamba, ifikapo Juni, 2024 wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huu waanze kunufaika na mradi huu, lakini tukiacha kusimamia ipasavyo matokeo hatutayaona. Ipo miradi ambayo tunaishuhudia kwa macho haisimamiwi ipasavyo, matokeo yake ni kwamba, huduma kwa wananchi hazifiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mradi ukasimamiwe, lakini kusimamiwa huko kutategemea wale watu wa Makonde hawana gari la uhakika la kufuatilia huu mradi kwa uhakika. Niiombe Wizara, nilisikia kulikuwa na tetesi ya kupatiwa gari, watu wa Makonde wapatiwe gari ili waweze kusimamia vizuri mradi huo ukalete manufaa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa lazima niongee kwa sababu, kupata fedha bilioni 84 kwa mkupuo sio jambo rahisi. Ni kazi kubwa sana ilifanyika mpaka na sisi tukawa wanufaika wa mradi huo. Mradi huu ili ukafanye kazi itakayoonekana vizuri na wananchi wote waweze kupata maji, ukienda kwenye Jimbo la Newala ipo miradi mingine ambayo kama itakamilika na kufanya kazi vizuri, basi tija ya mradi mkubwa huu itaenda kuonekana kwa wepesi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Mlima Miuyu, upo unatekelezwa katika Jimbo la Newala Vijijini. Mradi huu ni wa muda mrefu. Ulikuwa ni mradi wa miezi tisa kuanzia mwaka 2018/2019, lakini mpaka leo haujakamilika na haujakamilika, inawezekana kuna changamoto za wakandarasi, lakini Wizara pia, hawajawakamilishia fedha. Mradi ulikuwa wa bilioni 1.3 lakini fedha ambazo zimelipwa ni milioni 614 pekee. Niiombe sana Wizara itafute kwa nini fedha hazijaenda, kama shida iko kwa wakandarasi tuwasimamie wakandarasi wetu, kama shida ni ya Wizara, Wizara pelekeni fedha na waje watuambie ni lini fedha zitaenda. Mradi wa miezi tisa wa 2018 mpaka leo tunaongea, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu pamoja na mimi mwenyewe kwenye maeneo yetu, hatujawahi kuona maji ya bomba. Sasa hii miradi ambayo imeshaanza kwenda angalau basi, ikasimamiwe vizuri. Kwa kiasi fulani nashukuru kwenye huu Mradi wa Miyulu, angalau msimu wa mwaka jana, kaingazi cha mwaka jana, ile pressure kali, fedha ambazo tulikuwa tunalipa kule nyuma kwa ndoo ya lita 20 kulipa kwa shilingi 2,000, msimu wa mwaka jana ilipungua kwa sababu, angalau hii miradi kidogo ilikuwa inaanza kutoa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Mheshimiwa Waziri asimamie, kumbe inawezekana, mambo mengine ni masuala tu ya umeme, mara umekatwa, ukiuliza kwa nini fedha hazikupelekwa umeme ukirejeshwa maji yanatoka. Niombe sana, tusimamie, tuone tija ya miradi ambayo inakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za kutopatikana kwa maji ni nyingi, ukienda leo Jimbo la Newala Vijijini pamoja na Newala Mjini, kuna miradi ambayo haikamiliki kwa wakati kwa sababu tu ya ukosefu wa maji. Mradi unapelekewa fedha, wananchi wako tayari kutoa nguvu zao, wanahangaika kumaliza maji kwenye visima. Kule kwetu kwa sababu ya changamoto ya maji kila nyumba inayojengwa inakua na kisima, tunavuna maji, lakini maji yale kwa bahati mbaya hayatibiwi, tunayatumia hivyohivyo, ni yale maji ya kuokota, ndiyo maji ambayo sasa inapotokea miradi kwenye kijiji wananchi wanajikusanya wanaenda kuchukua maji yao kwenye visima wanaenda kutekeleza miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine yale maji yanaisha, kwa hiyo miradi unakuta haitekelezeki kwa wakati sahihi kwa sababu ya ukosefu wa maji. Tunakuja tunawalaumu sana Wakurugenzi wetu lakini wakati mwingine wana changamoto hiyo ya maji. Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie, maji Newala sasa ije ibadilike historia, mmeshaanza kuandika hiyo historia kwa kupeleka fedha nyingi, tunaomba sana wananchi wa Newala nao wanataka kuondokana na kero ya maji, kuondokana na kero ya maji ya kuokota kwa kupatiwa maji ambayo yatatoka kwenye mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi mingine midogomidogo kwenye maeneo yetu. Miradi ambayo ikienda nayo kupelekewa fedha basi changamoto kubwa sana tutakuwa tumeipunguza Mheshimiwa Waziri wetu. Kwa mfano, kuna mradi wa usambazaji wa maji wa vijiji vya Mkudumba – Mnyengachi na Mdimba – Mnyambe – Mnima na Bahati. Pia upo mradi mwingine ambao unajumuisha Vijiji vya Mikumbi, Mkongi, Nyamangudu, Nangujane, Chirende, Mkomato pamoja na Lihanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ipo kwenye mpango lakini tunaiombea sana ipate fedha. Kukamilika kwa miradi hii kutakuwa na sura nyingine ya Newala, sura ya Newala haitakuwa ile ambayo tumeizoea siku zote. Kuna watu wanarudi Newala wanakataa kufanya kazi kwa sababu ya shida ya maji. Mtu anafika Newala unatumia maji kwenye kile kikopo, kinaitwa kidosho, anapewa kile aoge, hawezi. Atakaa siku ya kwanza, mwezi wa kwanza anaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni afya, maji ni uhai, magonjwa mengi yanatokana na ukosefu wa maji. Tunaipa Wizara ya Afya mzigo mkubwa wa kutibia wagonjwa, magonjwa ambayo kumbe yangeweza kuzuilika kama maji safi na salama yangeweza kupelekwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuombe sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na mtani wangu Mheshimiwa Mahundi, chondechonde, tunaomba usimamizi na upelekaji wa fedha uende ili wananchi wa Newala wapate maji, tuigeuze Newala, maji Newala ni shida kwelikweli. Kila mtu atashangaa kama watayaona maji Newala kwa hali ya Newala jinsi ilivyo miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mvua zimeanza kukata tumeshaanza kupata hofu, kwa sababu kuna maeneo mvua hazikunyesha vya kutosha kwenye maeneo hayohayo ya Newala, kwa hiyo hata visima vyao vile vya asili havina maji. Kwa hiyo hapa sasa hivi mvua inavyoanza kukata tunaanza kupata hofu. Hivi sasa hivi mvua imekata tutaishije kwa miezi yote mpaka masika yaje, kwa sababu masika ndiyo mkombozi wetu, lakini kwa dunia ya sasa ilivyo kutegemea masika peke yake hapana Mheshimiwa Waziri. Tunaomba tuondokane na suala la kutumia visima, tuondokane na maji ya kuokota, wakati sasa umefika nasi tufaidi, tuone raha ya kutumia maji ya bomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi yako, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia afya. Kipekee nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. Na katika Wizara hii amefanya mengi sana makubwa ambayo mengine yanaendelea kukamilika na mengine yanaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kipekee kukutakia heri sana wewe binafsi kwa ule mchakato ambao uko mbele yako, na Insha Allah Mwenyezi Mungu ataleta heri, kwa sababu Waswahili wanasema iliyonona inaanzia miguuni; huku Tanzania umenona, hongera. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri mwenye dhamana aliyewasilisha hotuba yake pamoja na viongozi wake wote wanaomsaidia kazi; hongereni sana, hotuba ni nzuri.

Mheshimiwa Spika, nina mchango katika maeneo machache. Mchango wangu wa kwanza unakwenda kwenye suala la kukatika katika kwa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Niishauri Wizara kutafuta namna nzuri ambayo tatizo hili la kukatika katika kwa umeme litakwenda kukomeshwa kwa sababu linaathiri kwa kiasi kikubwa sana uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika hilo, hata kwenye Mkoa wa Mtwara suala la kukatika katika kwa umeme limekuwa sasa kama ni la kawaida. Lakini kipekee niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri, amekuwa msikivu, juzi tulikaa naye kikao yeye pamoja na wataalamu wake wote kwa saa zaidi ya mbili kwenye jando – maana lile tunaliita jando, na mambo ya jandoni hayasemwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, yale ambayo tumejadiliana yanayowenda kutekelezwa kwenye Mkoa wa Mtwara ili ku-rescue hali ya kukatika katika kwa umeme basi mkayasimamie. Na nishukuru kwamba zoezi lile nimesikia wameshaanza na kuna wengine wameniambia wanaondoka kesho wanakwenda kukaa huko wiki nzima. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri kilichobakia ni usimamizi wa yale ambayo tumekubaliana ili suala la kukatika katika kwa umeme na kuunguza vifaa vya watu liende likapotee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ninapoongea ukienda Mkoa wa Mtwara sasa kumedorora kwa sababu wafanyabiashara wengi vifaa vyao vimeharibika kutokana na tatizo hilo la kukatika katika kwa umeme, uwekezaji hakuna na watu wana hofu hiyo. Kwa hiyo yale ambayo mnakwenda kuyatenda, ikiwemo pia na kupeleka grid ya Taifa kwenye Mkoa wa Mtwara ikitokea Tunduru – Masasi kwenda Mahumbika, ni jambo ambalo litakwenda kuleta urahisi wa upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Mtwara ili sasa uwekezaji na uchangamfu wa mkoa, kwa maana ya kiuchumi, uende ukatekelezwe. Kwa hiyo nawatakia kila la heri katika usimamizi wa hilo ili Taifa liendelee na wananchi wapate uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni suala la REA. Niwaombe Wizara, wenzetu wa afya wana model, ukienda kwenye hospitali zao kubwa wametenga, wale wagonjwa mahututi wana namna yao ya kuwatibu na wagonjwa wengine wa kawaida wana namna ya kuwatibu. Sisi Mtwara kwa suala la REA tuko mahututi. Kwa hiyo niombee treatment ya Mtwara kwenye suala la REA ichukuliwe kama special case, ikasimamiwe. Tukiwasimamia wakandarasi hali ya upatikanaji wa umeme nadhani itakwenda kuwa nzuri.

Mheshimiwa Spika, nitolee mfano tu wa Jimbo la Newala Vijijini. Kwenye huu Mradi wa REA III Round Two, kulikuwa na vijiji 76. Kati ya vijiji 107 vya Newala Vijijini, vijiji 76 ndivyo vimlivyoingia kwenye mkataba na mkandarasi ambaye yuko site. Na mkataba ule ulikuwa ni wa August, 2021. Mpaka sasa status ilivyo vijiji 17 tu ndivyo ambavyo vimepata umeme, vijiji 17 viko kwenye process, vijiji 42 bado hawajafikiwa; na deadline ya mradi huu ni December mwaka huu. Sasa naona kama mzigo uliobakia ni mkubwa sana. Tusipowasimamia hawa watu watatuangusha, vijiji vile hawatapata umeme, tutapinduka 2024 bila ya kuwa na umeme. Niombe sana Wizara ikawasimamie.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wana suala wanasema wanaomba LC kutoka Serikalini, wapeni LC isije ikawa ndiyo kisingizio chao. Wapeni na wasimamieni kwa sababu nilicho-study kwa muda mrefu wa mkandarasi wetu ni kwamba anakosa usimamizi ule wa karibu. Kwenye mchezo wa mpira tunasema man to man – twende tukafanye man to man kwenye huu Mradi wa REA kule Newala Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, athari ya kutokuwa na umeme ni kubwa sana. ukienda leo tunazo shule za sekondari kwenye Jimbo la Newala Vijijini, lakini wanajifunzaje TEHAMA kama hawana umeme? Kwa hiyo wale watoto watamaliza bila ya kuwa na knowledge ya TEHAMA kwa sababu tu ya ukosefu wa umeme, lakini huku tumeshawapatayari miradi wakandarasi. Kwa hiyo ili tuokoe kizazi hiki cha watoto ambacho ni cha kidijitali, lazima umeme ukafike shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Wizara ya Elimu imetenga fedha na imeendelea kuboresha miundombinu ya VETA Kitangali. Tumetangaza kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwamba tutaoa ajira zaidi ya 8,000 ifikapo 2025. Ajira hizi zinatoka kwenye sekta iliyo rasmi na isiyo rasmi. Mategemeo yetu ni wale wanaotoka VETA wakajiajiri kwenye sekta zisizokuwa rasmi. Watoto wale wanajifunza useremala, uchomeleaji na mapishi mbalimbali; vyote hivyo vinategemea umeme. Leo hii wanamaliza hawana kwa kwenda ku-practice kile ambacho wamejifunza kutoka kwenye chuo cha VETA. Maana yake ni kwamba tunawekeza fedha nyingi kuwafundisha watoto hawa lakini tija yake haionekani kwa sababu wanakwenda kwenye maeneo ambayo umeme hakuna, kwa hiyo application ya knowledge waliyoipata inakuwa haionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunamshukuru Rais sisi Wananewala, Tandahimba na Nanyamba, ametuletea fedha shilingi bilioni 84.7 kwa ajili ya mradii mkubwa wa maji ambao sasa hivi umeanza kutekelezwa. Karibuni, ikifika 2024, Juni huko mradi unakwenda kukamilika; tutasukumaje maji yawafikie wananchi kama hatuna umeme wa uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niiombe sana Wizara, tunashukuru kwa yale ambayo mmekuwa mnayabuni kila siku, lakini tukasimamie suala la ufikaji wa umeme katika vijiji vyetu. Tumeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna kipengele cha kupeleka kwenye vitongoji 15 kila jimbo kufikisha umeme. Newala Vijijini naogopa, kwa sababu kama vijiji mpaka leo havijafikiwa, hivyo vitongoji vitafikiwa kesho? Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na timu yako, mna kazi ya kufanya Newala Vijijini. Bahati nzuri tumeshakueleza kwa kina na wewe unatambua pamoja na management yako, ni kusimamia sasa tuone utekelezaji wa yale makubaliano, yaende yakatekelezwe kwa vitendo ili uchumi wa wananchi wa Newala Vijijini pamoja na Mtwara kwa ujumla, kupitia sekta ya umeme, ukaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninataka kuliongea kidogo; tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa suala lile la LNG pale Lindi. Uwepo wa mradi ule mkubwa utachechemua kwa kiasi kikubwa sana uchumi wa watu wa Kusini. Kwa sababu kama mradi utaanza kutekelezwa, akina mama wanaolima mbogamboga watakwenda kuuza, na mambo mengi sana ambayo yanategemea upatikanaji wa nishati ile kwa ajili ya uzalishaji wa uchumi kwa wananchi wa Mtwara na Lindi, kwa kweli yatakwenda kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe tu Wizara, kwamba tusimamie utekelezaji ili miradi hii ikaweze kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili ilishagonga Mheshimiwa Mtanda.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi; naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii, Nimshukuru pia Mwenyezi Mungu, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri. Pamoja na yote namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kile kitendo ambacho amekifanya kutukwamua sisi watu wa Mtwara kutokana na barabara yetu ya kiuchumi ya Mnivata – Tandahimba – Newala – Masasi. Mheshimiwa Rais amepeleka zaidi ya bilioni 234 kwa ajili ya barabara ile ambayo ilikuwa kwenye ilani kwa muda mrefu na haitekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye bajeti, niipongeze sana Wizara kwa wasilisho zuri, lakini zipo changamoto ndogo ndogo ambazo zinatakiwa kuangaliwa. Kwenye ile bajeti kuna aya inayozungumzia suala la sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo. Kilimo ni uti wa mgongo; na tunatambua kabisa watu wetu wengi wanaishi vijijini wanategemea kilimo kwa ajili ya kustawisha maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambayo inawakumba wakulima wetu. Kwa mfano, ukienda mikoa ile ambayo inalima zao la korosho kumetokea na utaratibu mwaka huu wa kufanya sensa wa miche ya mikorosho. Wakulima wametekeleza agizo hilo, lakini sasa wakati wa kutoa zile pembejo ambao unafuatana na zile sensa, mambo yamekuwa magumu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo baadhi ya kata ambazo vijiji vyake, kwa mfano, ukienda Kata ya Maputi ambayo ipo Jimbo la Newala Vijijini, kati ya vijiji sita vya kata ile, vijiji vitatu havimo kwenye mpango. Vile vile, ukienda Kata ya Mnyambe, Kata ya Malatu, hizo zote zina–miss kuwemo kwenye utaratibu wa kupata pembejeo kwa sababu ya mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Wizara kuangalia utaratibu mzuri ambao wakulima watapata pembejeo kwa wakati kwa sababu msimu wa upuliziaji wa zao la korosho ni sasa. Inapotokea mkulima hayupo kwenda kurekebisha inachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, tutapishana na wakati. Badala ya wakati wa upuliziaji, upuliziaji utapita, kwa hiyo yale manufaa ambayo tumeyapanga kwamba tunataka kukusanya mazao, tutakosa kupata kile ambacho tulikuwa tunakitarajia. Kwa hiyo, niombe sana hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye upande wa elimu; kuna mambo mengi. Tumeona sasa hivi namna ambavyo Serikali inapeleka fedha nyingi kujenga madarasa. Tunashukuru na kwa sasa madarasa mengi yanakwenda yakiwa na madawati yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna changamoto ambayo imejitokeza kwenye yale madarasa ya zamani. Madarasa mengi ya zamani watoto wanakaa chini, hakuna madawati. Ili umwandae vizuri mwanafunzi lazima akae sehemu nzuri ya kujifunza na kujifundishia. Mwanafunzi anapokosa dawati, hawezi kujifunza vile ambavyo tulikuwa tunatarajia. Kwa hiyo niombe, mwaka 2026 kulikuwa na mkakati ambao ulizilazimisha halmashauri kuhakikisha kwamba madawati yanapatikana. Baada ya mkakati ule hapakuwa tena na shinikizo lingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu halmashauri inakumbana na changamoto nyingi kutokana na mambo ya kifedha, lakini kama hatutaweka msisitizo, wanafunzi wataendelea kupata shida ya namna ya tendo la kujifunza na kujifundishia kwa sababu wengi wanakaa chini, tunawasababishia afya zao kuteteleka kwa sababu anajikunja tangu asubuhi mpaka jioni, zoezi la mwaka mzima, tutawasababishia wanafunzi wetu vibyongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, tunayo misitu yetu ambayo inasimamiwa na watu wa Maliasili, tuone namna ambayo tunaweza kupata magogo tukapeleka yakatengenezwa madawati ambayo yatakwenda kusaidia shule zetu. Nafahamu upo utaratibu, lakini watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakae pamoja na watu wa TAMISEMI, waone namna ambavyo changamoto hii inaweza kwenda kutatuliwa ili wanafunzi wetu wapate sehemu ya kukalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasafirisha magogo kwenda kuyauza nje, sawa tunapata fedha lakini je, afya na ustawi wa wananchi wetu na watoto wetu tunauweka wapi? Tunapotengeneza mazingira ambayo yatasababisha magonjwa, tunazalisha kitu kingine ambapo tutakwenda kutafuta fedha kwa ajili ya kuwatibu, kitu ambacho kingekuwa solved kama wanafunzi hawa wangekaa katika mazingira mazuri ya kusomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hivyo tu, kuna suala la usafi binafsi. Tunafahamu hali za wananchi wetu ni ngumu. Mtoto anakaa chini, asubuhi anaondoka yuko vizuri, msafi, lakini anaporudi jioni ana vumbi amechafuka kwa sababu amekaa chini tangu asubuhi mpaka jioni. Kwa hiyo, kuna vitu vingi vinatengenezwa hapo, lakini source inakuwa ni ukosefu wa madawati katika madarasa yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku kwenye mafuta, fedha zile ambazo amezitoa ambazo angalau zimeshusha kidogo bei ya mafuta hapa nchini tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya ninawaomba wazidi kuongeza nguvu ili tuweze kuyaona manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia suala la gesi asilia. Mtwara Gas Plant ina jumla ya visima 11 ambavyo vinauwezo wa kuzalisha megawatt 22 za umeme kwa siku. Lakini kati ya visima hivyo visima Tisa ni vya muda mrefu ni vya kati ya 2006 na 2007 na life span ya mashine hizo ni miaka 10. Kwa hiyo, utaona kwamba muda wa mashine hizo umeshapita kiasi kwamba uzalishaji wa umeme umekuwa ni wa chini sana. Tunaomba Wizara ijipange kutafuta replacement ya vile visima Tisa ambavyo ni vya muda mrefu ambavyo pia vinaiingizia Serikali gharama kwa sababu ya matengenezo yasiyoisha kwa sababu muda wake pia umeshapita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kupata commitment ya Serikali ni lini mradi wa megawatt 300 ambao unatakiwa kwenda kujengwa kule Mtwara utaanza? Nimeona kwenye hotuba ya Waziri imewekwa lakini hii si mara ya kwanza inawekwa, imewekwa muda mrefu sana kila wakati inawekwa lakini haitekelezwi. Kwa hiyo, tunaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie ni lini hasa ujenzi wa megawatt 300 Mtwara utaenda kuanza kwasababu unafaida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa Mtwara haujatulia, umeme unaofika Mtwara ni mdogo, pamoja na Mtwara tunazalisha gesi lakini umeme wetu unaoingia pale ni mdogo sana unakatika kila wakati. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atuambie ujenzi halisi wa megawatt 300 utaanza lini Mtwara? Anapokuja kuhitimisha hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane pia na mzungumzaji aliyepita aliyezungumzia suala la REA katika maeneo yetu. Ni kweli kabisa Wakandarasi wa REA walipewa kazi ile mwaka jana kati ya Agosti na Septemba, kipindi kile mfumuko wa bei haukuwa mkubwa kama ulivyo sasa hivi, mfumuko umeanza karibuni, sasa wanakuja na kisingizio cha kwamba vifaa vimepanda bei, walikuwa wanafanya nini kipindi chote ambacho kimepita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Jimbo la Newala Vijijini kwa mfano, ambako mkandarasi anayeitwa Central Electrical International Limited amepewa kazi ya kuweka umeme katika Jimbo la Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba, Newala lakini Mkandarasi yule kwakweli tumechoka kwa sababu ufanyaji wake wa kazi haueleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Jimbo la Newala Vijijini, Vijiji 107 ndivyo ambavyo vipo kwenye Jimbo lile lakini ni vijiji 33 tu ndivyo vyenye umeme, Mkandarasi amepewa scope ya kazi anaifahamu lakini ninavyoongea sasa hivi amefika Kata mbili tu ambazo zina vijiji 11 hali ambayo inatia wasiwasi kwamba je, ikifika Desemba 2022 kweli atakuwa amemaliza vijiji vyote 74 ambavyo havina umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri nakuomba Kaka yangu msimamie Mkandarasi aliyepewa kazi Mtwara, Tandahimba, Nanyamba na Newala afanye kazi kwa juhudi ikiwezekana usiku na mchana, kwa sababu watu tupo gizani, lakini umeme huu unamanufaa makubwa sana kama utawafikia wananchi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wanashindwa kujiajiri kwa sababu hawana umeme, kungekuwa na umeme wangeuza ice-cream, wangechomea ma-gate wangefanya kazi mbalimbali lakini wanashindwa kwa sababu umeme haupo. Nasi tumeahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutaongeza ajira zipatazo zaidi ya 8,000 kufikia 2025 lakini ajira hizi zingine zinatokana na sekta binafasi ikiwemo hii ya umeme kwamba vijana wangeweza kujiajiri wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Waziri wetu asimamie umeme ufike kwenye vijiji kupitia REA ili wananchi wale nao waweze kunufaika waone matunda yanayotokana na kazi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo maeneo niliyotaja ambayo yapo gizani yanapakana sana na nchi jirani nchi ambayo hali yake tunaifahamu, nimeshaongea hapa umeme huu si luxury umeme ni ulinzi ukiondoa suala zima la kazi lakini umeme ni ulinzi utatulinda kwa kuwepo kwake. Kwa hiyo, tunavyofanya hawa Wakandarasi waliopewa kazi wanaenda polepole wanahatarisha usalama wa raia wa maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo umeme unaofika maeneo ya Mtwara na Lindi ni mdogo sana, kule tunafahamu kabisa kwamba ndiko gesi asilia inakotoka kwa wingi kutoka kule Msimbati, Songosongo gesi hii inaenda kuchakatwa Kinyerezi inarudishwa kule. Kwa hiyo, umeme taunaopata ni mdogo sana. Tulitaraji miradi hii wananchi wanaotoka katika maeneo yale wai-own wao wenyewe kwa maana ya kwamba waone manufaa yanawafikia moja kwa moja. Tuliambiwa kwamba watapata umeme wa majumbani lakini kiasi ambacho kimefika cha matumizi ya umeme majumbani ni kidogo sana, ni kidogo mno na sijui mradi ule umeishia wapi kwa sababu ulikuja mara moja tumeona kimya mpaka leo. Naomba sana Serikali kupitia Waziri mjipange muhakikishe umeme huu unawafikia wananchi wa Lindi na Mtwara, waone manufaa ili wawe walinzi wazuri wa miradi hii kwa sababu inatoka kule kwao watusaidie kulinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni gridi yetu ya Taifa umeme huu ukienda unaishia Tunduru Gridi ya Taifa kule ipo Tunduru, kwa hiyo, umeme unaofika Masasi kupitia gridi ya Taifa hauna nguvu. Niombe sana Serikali ione uwezekano wa kujenga sub-station maeneo yale ya Masasi ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika kwa sababu kuna kukatika katika sana kwa umeme kutokana na umbali unakotoka umeme hadi kuwafikia walaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini Mheshimiwa Waziri anapokuja aje na majibu ambayo nimeyaomba niyasikie anatujibuje. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami nitoe mchango wa mawazo kuhusiana na bajeti ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi za dhati kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na timu yake yote ambao wamewasilisha bajeti yao vizuri, bajeti ambayo imesheheni mambo mengi ambayo yanaenda kulisukuma Taifa hili katika maendeleo ya dhati.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kile ambacho amekifanya kwenye maendeleo ya kilimo kwa msimu ambao umeisha. Tulipitisha bajeti iliyopita ya 2023/2024, fedha ziliongezwa kwenye kilimo na tumeona mikakati mingi ambayo Serikali imeifanya ikiwemo ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na mengine mengi ambayo yataleta tija kwenye kilimo chetu, ukizingatia kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika pongezi hizo, nitoe mfano wa kile ambacho Serikali imekifanya. Kwa mfano, wakulima wa zao la korosho katika nchi yetu ya Tanzania, kwa msimu wa 2023/2024 Serikali ilijitahidi kutoa pembejeo bure kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji kama vile ambavyo iliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, tunashukuru sana kwamba kwa mfano kwenye zao hilo la korosho uzalishaji umeongezeka kidogo tofauti na msimu wa mwaka 2022/2023. Msimu huu wa mwaka 2023/2024 kutokana na kutolewa kwa pembejeo ambazo zilikuwa bure, ongezeko lipo. Tunaishukuru sana Serikali kwa sababu hali ya wananchi wetu katika mifuko ilikuwa ni ngumu na hivyo wasingeweza kupulizia. Wananchi wengi wanaolima korosho katika nchi hii wamenufaika na pembejeo zile, na zao la korosho uzalishaji angalau umeongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mtwara, ukienda kwenye Chama Kikuu cha Ushirika cha Watu wa Tandahimba na Newala (TANECU) kwa msimu wa mwaka 2022/2023 uzalishaji ulikuwa ni tani 33,000 peke yake, lakini kwa msimu huu wa 2023/2024 zimeongezeka tani 33,000 na kufanya uzalishaji kuwa tani 74,000. Tunaishukuru sana Serikali kwa sababu hali hiyo isingefikiwa. Hicho ni chama kimoja tu, ikija kuunganishwa kwa Tanzania nzima kwa zao la korosho, basi tutaona ongezeko litatofautiana sana na lile la msimu wa mwaka 2022/2023. Tunaishukuru Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ongezeko hilo, nashukuru pia kwenye hotuba ambayo tumeletewa iliyopo mbele yetu, ukienda aya ya 46 inasema: “Pamoja na mambo mengine Serikali itahakikisha kilimo kinakuwa na faida kwa kuhamasisha uongezaji wa thamani kwenye mazao na upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.” Tunashukuru sana kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee hapo. Pamoja na uzalishaji kuongezeka, hili ambalo Serikali imelisema la kutafuta thamani ya mazao pamoja na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi, ndipo changamoto ilipo kwa wakulima wetu wengi; na mazao mengi yanakwama kwenye masoko. Ukienda kwa watu ambao wanazalisha mpunga, wanazalisha mpunga mwingi lakini unakuta wanakwama kwenye bei. Ukienda kwenye korosho, halikadhalika, uzalishaji ndio huo, lakini kwenye bei inakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, msimu huu ambao umeisha, huu wa mwaka 2023/2024 changamoto ya bei imekuwa ni kubwa mno kwenye zao la korosho, bei iko chini. Pamoja na bei kuwa chini, kuna utitiri wa tozo ambazo zinamkumba mkulima wa korosho. Naiomba Serikali yangu tukufu ambayo inasikia, ijaribu kutafuta namna ya kupunguza tozo kwa sababu mkulima anachopata ni kidogo, lakini tozo zimekuwa nyingi kiasi kwamba sasa kile anachokipata pamoja na udogo wake chote kinaishia kwenye tozo. Kwa hiyo, kunakuwa na tofauti kubwa kati ya zile gharama za uzalishaji kuanzia palizi, upuliziaji mpaka kuja kuvuna na kile ambacho mkulima akienda kuuza anakuja kukipata kama take home.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iangalie, ikae chini itafakari suala la tozo ili mkulima apate angalau kitu ambacho kitamfariji, kwa sababu sasa hivi kwa kweli imekuwa ni chanagamoto kubwa. Hapo niseme tu, lawama kubwa tunaibeba sisi ambao ni wawakilishi wa wananchi. Kwa hiyo, Serikali iendelee kututafutia masoko na pia kuangalia hizi tozo kwani zimekuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zao la korosho kunakatwa Export Levy. Export Levy ilivyokatwa, tunashukuru baadhi ya matunda tumeanza kuyaona ikiwemo na pembejeo. Basi naiomba Serikali ifanye kitu ambacho Export Levy itakuja kumnufaisha mkulima wakati anauza zao lake kwa sababu kwa kweli hali imekuwa siyo yenyewe. Hali hii ni kwa sababu sisi bado tunategemea kuuza korosho ghafi, hicho ndicho ambacho tunakwama nacho. Uuzaji wa korosho ghafi ndiyo unaotufikisha hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua jitihada za Serikali za kuweka mpango wa kutengeneza au kuanzisha industrial park ambayo itachakata korosho zote hapa ndani na hatimaye tuuze korosho ambazo siyo ghafi tena, lakini, hiyo ni long term plan. Short term plan lazima tuitafute. Masoko ya korosho yanatafutwa kipindi msimu tayari umeshatangazwa wa kuuza korosho. Kwa hiyo, inakuwa kama kuna uharaka fulani, matokeo yake tunaenda kuangukia kwa wanunuzi ambao wanatulalia kwenye bei. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sababu imeshaweka kwenye mikakati kutafuta masoko ya bidhaa zake za kilimo, basi ifanye mapema kabla ya msimu kutafuta wanunuzi. Kwa sababu, kama itafanyika mapema, ule uharaka haraka ambao mara nyingi hauna baraka utapotea na mkulima yule ataenda kunufaika na soko la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niongelee suala la maji. Nashukuru sana Serikali yetu inafanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba suala la maji linafikia hatua nzuri. Katika Sera yake ya Maji inasema ifikapo 2025, basi kwa wale ambao wanaishi mijini wapate maji safi na salama kwa asilimia 95 na wale ambao wako vijijini wapate maji safi na salama kwa asilimia 85 ifikapo 2025. Katika kufikia hilo, tunaona juhudi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya ili kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanapatikana kwa wananchi wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu kulikuwa na mradi wa miji 28. Mradi ule ulisuasua sana, lakini bahati nzuri ukasainiwa mwaka juzi, 2022 na umeanza utekelezaji katika baadhi ya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wananewala ni wanufaika wa huo mradi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Kengele ya pili hiyo.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Pia naomba kipekee kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya yeye pamoja na wasaidizi wake wote akiwemo Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Viongozi wote wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi hizo zinaambatana na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa lile ni kubwa, lakini linataka kututoa Watanzania hapa tulipo, kutupeleka katika hatua nyingine zaidi ya kiuchumi. Ni bwawa kubwa ambalo kama tutalitumia vizuri, manufaa yake tutayaona na tumeanza kuyaona kwa sababu umeme umeshaanza kuzalishwa. Shukurani kwa Viongozi wa Chama na Serikali ambao mmesimamia bwawa lile.

Mheshimiwa Spika, ni rai yangu kwa Watanzania wote kuendelea kutunza miundombinu ile hasa wale ambao wanatoka maeneo jirani yenye mito inayoingiza maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, tuendelee kutunza vyanzo vyetu ili mradi wetu uwe endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue pia fursa hii kumshukuru Naibu Waziri Mkuu pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati, kwa jitihada kubwa ambazo wamezifanya katika sekta hii ya nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Newala Vijijini kwa mfano, tunavyo vijiji 107, lakini wakati naingia ni vijiji 31 tu ndivyo ambavyo vilikuwa na umeme. Leo ninapoongea, vijiji 35 tayari vimeshawashwa umeme, vijiji 13 vimeshawekewa transformer bado kupimwa umeme uwashwe, vijiji 25 vinaendelea na kazi katika hatua mbalimbali. Ni vijiji vitatu tu ndiyo ambavyo bado na ninaamini kwa jitihada na namna ambavyo Waziri na timu yake wanafanya kazi, basi vijiji hivi navyo vitafikiwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na shukrani hizi, katika mradi huu wa REA naomba, hivi vijiji ambavyo nimezungumzia ni vile ambavyo vimefikiwa na kilometa moja tu ya ujenzi wa umeme. Kwa hiyo, maeneo mengi ya taasisi kwa mfano, shule, zahanati, nyumba za ibada, zote bado hazijafikiwa na mradi huu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lengo ni kumfikishia mwananchi huduma na kumpunguzia mzigo, naiomba Serikali, zile kilometa mbili ambazo zinaenda kujengwa katika kila kijiji, basi tusimamie zijengwe kwa haraka ili taasisi nilizozitaja zipate umeme na wananchi waweze kuhudumiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, leo hii unaenda kwenye zahanati ambayo imejengwa vizuri, kwa mfano kule Newala Vijijini kuna zahanati ya Namangudu, zahanati nzuri kabisa ya kisasa haina umeme. Sasa mama anaenda kujifungua, anamulikiwa kwa mwanga wa simu, hapana! Siyo sawasawa, kwa sababu Serikali inasema kuongeza kilomita mbili itakuwa ni jambo la haraka. Naomba tumsimamie mkandarasi aliyepewa kazi ili kazi hii ikakamilike haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ipo changamoto nyingine ya kukatikakatika kwa umeme hasa Mkoa wa Mtwara. Naomba sana, najua Serikali inafanya jitihada kubwa, imeshaleta mtambo wa megawati 20, tumeona umeme upo, ila shida ni miundombinu. Ninaiomba Serikali isimamie miundombinu ili umeme ule usikatikekatike sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, najua zipo jitihada nyingine nyingi tu. Kwa mfano, wameshafunga baadhi ya maeneo auto recloser ili kupunguza umbali wa kusafirisha umeme. Naomba tuisimamie kwa haraka ili umeme usikatike maeneo mengi kwa wakati mmoja. Najua ni gharama, lakini inawezekana kwa sababu tumeshaamua, basi tufanye hima umeme uwafikie wananchi, na tupunguze hii adha ya kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba long term plan iwe ni kuufikishia Mkoa wa Mtwara na Lindi umeme kutoka gridi ya Taifa. Mpaka sasa umeme haujafika Gridi ya Taifa. Tunajua Serikali inayo mikakati ya dhati ya kufikisha umeme, lakini naomba usimamizi wa haraka zaidi na tupeleke pesa ili tupate Gridi ya Taifa kwa Mkoa wa Mtwara kutokea kule Songea kama ambavyo mmetuahidi na wananchi wetu wa Mtwara - Newala waweze kufanya uwekezaji mkubwa sasa. Wengi wanashindwa kuwekeza katika maeneo yetu kwa sababu ya ukosefu wa umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda Newala unakutana na viwanda vya korosho vimekaa tu kama maghala ya kutunzia bidhaa, lakini inawezekana sababu mojawapo ya wale wawekezaji kushindwa kuendelea kubangua korosho ni kukatikakatika kwa umeme. Kwa hiyo, naiomba Serikali isimamie tupate umeme kutoka gridi ya Taifa ili uwekezaji Mkoa wa Mtwara ukawe wa uhakika na kuinua kipato cha wananchi wake. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)