Supplementary Questions from Hon. Maimuna Salum Mtanda (48 total)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Jimbo la Newala Vijijini linakabiliwa na uhaba mkubwa wa upatikanaji wa dawa kwa wananchi wake. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na suala hili? Uhaba ule unachangia kwa kiasi kikubwa sana wananchi kushindwa kujiunga na mpango wa CHF iliyoboreshwa kwa sababu wamekatishwa tamaa na mpango wa awali, wakienda vituoni hawapati dawa hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Jimbo la Newala Vijijini linakabilishwa na uhaba mkubwa pia wa watumishi, hali ambayo inazorotesha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi. Ni lini Serikali itapeleka watumishi wa afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma inayostahili kama wananchi wengine? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka kipaumbele kuhakikisha vituo vyetu vya huduma kote nchini vinakuwa na dawa za kutosha. Ndiyo maana katika kipindi cha miaka mitano, bajeti ya dawa ya Serikali imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 271 mwaka 2020. Hii ni jitihada kubwa sana ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata dawa za kutosha vituoni.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusisitiza, kwanza kuhakikisha Halmashauri zinasimamia ipasavyo mapato ya uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu. Nasi Waheshimiwa Wabunge ni sehemu ya Madiwani katika Halmashauri zetu, kumekuwa na changamoto ya usimamizi wa makusanyo ya fedha za uchangiaji ili ziweze kuongeza mapato ya vituo na kuboresha dawa katika vituo vyetu. Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu na kuboresha upatikanaji wa dawa nchini kote lakini katika Halmashauri ya Newala Vijijini.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uhaba wa watumishi, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele cha hali ya juu sana katika kuboresha upatikanaji wa watumishi katika vituo vyetu. Mipango iliyopo ni pamoja na kuendelea kuajiri na ushahidi unaonekana. Katika kipindi cha miaka mitano, zaidi ya watumishi 14,000 na mwaka jana madaktari 1,000 wameajiriwa katika vituo vyetu mbalimbali. Zoezi hili la kuajiri watumishi wa afya ni endelevu na Serikali itaendelea kuajiri ili kuboresha huduma za afya katika nchi yetu.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jimbo la Tandahimba pamoja na Newala Vijijini lina changamoto ya upatikanji wa vifaatiba pamoja na vitenganishi hali ambayo wakati mwingine inasababisha akinamama wanaojifungua kwenda kutafuta kadi za kliniki mitaani. Je, upi mpango wa dharura wa Serikali wa kunusuru hali hiyo ya upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na vitendanishi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Jimbo la Newala Vijijini lenye Kata 22 lina vituo vitatu tu vya kutolea huduma za afya hali ambayo inaleta changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Jimbo la Newala Vijijini ili wananchi wale wapate huduma za afya kama ambavyo inahitajika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya katika vituo vya afya kwanza kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vifaatiba, vitendanishi lakini pia ununuzi wa dawa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu tunaoendelea nao Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba na tayari shilingi bilioni 15 zimekwishanunua vifaatiba na vimekwishapelekwa kwenye vituo vya afya vya awamu ya kwanza na awamu ya pili. Kiasi cha shilingi bilioni 11 kiko katika hatua za manunuzi na mara moja vifaa hivyo vitanunuliwa na kupelekwa kwenye vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, kituo cha afya katika Jimbo la Newala ni moja ya vituo vya afya vilivyojengwa katika awamu ya tatu na ya nne na hivyo vituo hivi vitakwenda kutengewa fedha za ununuzi wa vifaatiba katika mwaka wa fedha 2021/ 2022. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwamba vituo vyake hivi vya afya vitawekewa mpango wa kununuliwa vifaatiba ili viendelee kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na idadi ya vitu vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini, ni kweli Serikali inatambua kwamba bado kuna uhitaji mkubwa wa vituo vya afya katika kata za Jimbo la Newala Vijijini na nchini kote kwa ujumla na ndiyo maana katika mwaka wa fedha ujao ambapo Mheshimiwa Waziri atawasilisha Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunatarajia kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya katika kata za Jimbo hili la Newala na nchini kote kwa ujumla. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili litaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Wazir nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara Miyuyu - Ndanda kimekuwa kimetengewa fedha mara kwa mara za matengenezo ya kawaida, lakini fedha hizo hazitibu shida iliyoko kwenye mlima pale na barabara ile ni barabara ambayo inatumika kwa wagonjwa kutoka Wilaya za Newala na Tandahimba wanaopata rufaa kwenda Hospitali ya Ndanda. Hali ya pale ni mbaya, ni mlima kumbwa na korongo kubwa kiasi kwamba inahatarisha usalama kwa watumiaji wa barabara ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata kauli ya Serikali. Ni lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ile hasa kipande kile ili wananchi wanaotumia hospitali ya Ndanda kama hospitali ya Rufaa waweze kupata urahisi wa kufika hospitalini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo la Newala Vijijini, zimesababisha athari kubwa sana ya barabara kukatika magari hayapiti, hata pikipiki zinapita kwa shida, kwa mfano barabara kutoka Malatu Shuleni - Namkonda hadi Chitekete, barabara ya Maputi - Meta, barabara ya Likwaya Nambali, barabara ya Mtikwichini - Chikalule, barabara ya Mtikwichini - Lochino na Chikalule.
Mheshsimiwa Naibu Spika, upi mpango wa Serikali wa kupeleka fedha kwa ajili ya dharura ya kutengeneza barabara hizo ambazo kwa sasa hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge aliuliza eneo korofi la Mlima Miyuyu mpaka Ndanda na amesema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha, lakini bahati mbaya tatizo hilo limekuwa halitatuliki, kwa hiyo, alikuwa anaiomba Serikali ni lini itajenga lami katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu peke ninachoweza kumuhakikishia ni kwamba kutokana na ombi alilolileta na sisi Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutakwenda tufanye tathimini na baada ya hapo tutaleta majibu ya eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sehemu ya pili barabara ambazo amejaribu kuzitaja Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini anafanya kazi hii kwa nia njema ya kusaidia wananchi wake wa Jimbo la Newala, ameainisha maeneo mengi sana na kutaka mpango wa dharura na lenyewe nimuhakikishie kwamba Serikali tumesikia na kwa sababu katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha yakiwemo hayo maeneo ambayo ameyaainisha, lakini Serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta vyanzo vingine.
Kwa hiyo kulingana na bajeti itakavyopatikana na sisi tutaakikisha kabisa kwamba tunatatua matatizo ya wananchi wa Newala na maeneo mengine ya Tanzania. Kwa hiyo, ahsante sana Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yako na nikupongeze kwa kazi nzuri kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza; kwanza nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nataka kujua namna ambavyo Wizara ya Mambo ya Ndani inashirikiana na Wizara ya TAMISEMI wenye shule kuhakikisha kwamba matukio haya sasa yanakoma kwa sababu, yamekuwa yakisumbua mara kwa mara katika shule zetu hasa za mabweni. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunao ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na TAMISEMI na hata hawa watu wa Wizara ya Elimu katika kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi kubwa ya majanga ya moto na majanga mengine hasa katika maeneo ya shule na maeneo mengine. Tayari tumeshakuwa tunakaa vikao mbalimbali, tumeshapanga mipango mbalimbali ambayo ni mikakati ya kuhakikisha kwamba tunapunguza haya majanga.
Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa asiwe na wasiwasi juhudi zinaendelea kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba tunapunguza haya majanga kwa kiasi kikubwa. Nakushukuru.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante. Naomba kuiuliza wizara maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tatizo la maji kwenye Jimbo la Newala Vijijini limekuwa ni sugu, wananchi wa Newala Vijijini wanakunywa maji ya kuokota ambayo wanaokota kipindi cha mvua, maji ambayo huwa yanaoza na yanatoa harufu. Lakini tunacho chanzo kikubwa cha Bonde la Mitema ambalo Serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa bonde lile litatua kabisa changamoto za maji kwa sababu maji yaliyopo katika bonde lile yana mita za ujazo zipatazo 31,200 lakini mahitaji ya wananchi wa Newala, Tandahimba pamoja na Nanyamba kwa siku ni mita za ujazo 23,441.
Je Serikali imejipangaje kuhakikisha inaweka fedha za kutosha katika bonde la Mitema ili tatizo la maji liweze kukoma na wananchi waweze kupata maji ya kutosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika kituo cha Mto Ngwele kulikuwa na tatizo la pump house pamoja na transformer. Lakini bahati nzuri Januari mwaka huu pump house imerekebishwa na TANESCO wameshapelekwa pale transformer iko pale haijafungwa hadi leo hii ikaweza kusukuma maji. Nini kauli ya Serikali kwasababu wananchi wanaendelea kutaabika kupata maji wakati transformer iko pale wanashindwa kuifunga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwanza nakupongeza sana wewe ni Mbunge wa Jimbo, mwana mama Hodari na umekuwa ukifuatilia kwa uchungu sana masuala la maji ili kuokoa kina mama wenzako kuhakikisha wanatuliwa ndoo kichwani kama ambavyo wizara tunakesha, tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba kina mama lazima tuwatue ndoo kichwani na maji yapatikane umbali mfupi kutoka kwenye makazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake namba moja anauliza fedha za kutosha kuwezesha bonde la Mitema. Hii ni moja ya kazi ambazo tumeagiza RUWASA waweze kushughulikia, hii itafanyika ndani ya mwaka wa fedha ujao na kuona kwamba tuanze kuuona usanifu unakamilika na kila kitu kinakwenda vizuri ili maji yaweze kupatikana kwenye chanzo cha uhakika. Wakati tuna hitimisha bajeti yetu nimeongelea suala la Newala hata mimi ni mwana mama nisingependa kuona watu wanaendelea kutumia maji ya kuokota kwa karne hii na tumshukuru Mungu tumempata Rais mwana mama ambaye kiu yake kubwa ni kuona kina mama wanatuliwa ndoo kichwani. Mheshimiwa Mbunge Maimuna hili tutashirikiana kwa pamaja kuona kwamba tunakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusiana na transformer ambayo ipo pale. Sisi kwa upande wa wizara yetu tuliweza kushughulika na pump house na imeshakamilika. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Nishati kuona kwamba sasa ile transformer inakwenda kufungwa haraka iwezekanavyo ili matumizi ya umeme kwenye kusukuma maji yakaweze kufanyika na watu wakanufaike na mradi ambao umeshakamilika.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza kwamba, katika Jimbo la Newala Vijijini, kuna Mradi wa Maji wa Mnima Miuyu, mradi huu ulikuwa ni wa miezi tisa, ulikuwa ni mwaka 2018 na hadi leo hii haujakamilika. Je, ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Jimbo la Newala Vijijini waweze kupata maji ya uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Naomba kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ambayo utekelezaji wake umeanza na ipo katika process, yote lazima itakamilika kadri fedha tunavyozipata na kadri ya muda ulivyopangwa. Hivyo nipende kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, namna ambavyo amekuwa akizungumza nasi mara kwa mara, tuendelee kuwasiliana kwa karibu na tutakwenda pia kuona kazi imefikia wapi na kazi itakamilika kadiri inavyotakiwa.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali hadi Mtama yenye kilomita 74 ndiyo barabara pekee inayofungua mji wa Newala na maeneo mengine kuelekea Dar es Salaam hadi kuja huku Dodoma. Nakubaliana na Mheshimiwa Waziri kwamba fedha zitatengwa kwa awamu lakini ikumbukwe kwamba wilaya hii ni ya muda mrefu tangu 1952 hadi leo haina barabara ya uhakika. Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha ili barabara hii iweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na changamoto za ubovu wa hii barabara wafanyabiashara wengi wa usafirishaji wanakwama kupeleka vyombo vyao vya usafiri kwa hofu ya uharibifu wa vyombo vyao na wananchi wanateseka na usafiri kwa sababu ya ubovu wa barabara. Je, Serikali haioni kwamba inarudisha nyuma jitihada zake za ajira kupitia sekta zisizo rasmi hasa usafirishaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi barabara hii ni kweli ni ya muhimu sana kwa mkoa wa Mtwara ambayo inaunganisha mkoa wa Lindi. Lakini kwa kulitambua hilo Wizara ya Ujenzi kupitia TANROAD inajenga maeneo korofi yote kwa kiwango cha lami na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba maeneo mengi korofi yamejengwa kwa kiwango cha lami na hata katika mwaka huu wa fedha tunaoendea kuna fedha imetengwa kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami yale maeneo yote korofi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, ambalo linafanana hili jibu la kwanza kwa sababu ya kutambua ule ubovu kwenye hii barabara ndiyo maana sasa TANROADS Mkoa wa Mtwara unafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika muda wote na kuhakikisha kwamba maeneo korofi yote yanawekewa lami ili barabara hii iweze kupitika muda wote wa mwaka ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Chanzo cha maji ya Mitema ambacho kipo katika Jimbo la Newala Vijijini kina maji ya kutosha kiasi kwamba kama uwekezaji wa fedha utakuwa wa kutosha, tatizo la maji katika Jimbo ya Newala Vijijini, Newala Mjini, Tandahimba na baadhi ya Kata za Nanyama zitaondokana na shida ya maji. Je, ni lini Serikali itawekeza fedha za kutosha katika chanzo cha maji cha Mitema ili kuondoa kadhia ya maji kwa wananchi wa maeneo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Newala Vijijini. Lakini pia nimpongeze sana, juzi tuliweza kukutana pia na Mheshimiwa Mbunge wa Newala Mjini, baba yangu, mzee wangu, Mheshimiwa Kapteni Mkuchika, juu ya Mradi huu wa Makonde. Ni mradi wa muda mrefu sana ambao umekuwa na maneno mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie nikiwa mwenye dhamana ya Wizara ya Maji, Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mahususi kwa ajili ya Watanzania, waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Juzi tumekaa kikao baada ya mazungumzo yale, maelekezo ambayo tumeyatoa ni kwamba mradi ule tunakwenda kuuanza, iwe jua iwe mvua, ili wananchi wa Newala waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali kuhusiana na barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali hadi Mtama yenye kilometa 74.23 ambayo imeshajengwa kwa lami kwa kilometa 22.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba commitment ya Serikali ni lini itatafuta fedha kutoka kwa wadau wengine wa maendeleo ili barabara kipande kilichobaki kiweze kukamilishwa kwa kiwango cha lami kwa sababu Serikali imekuwa ikitenga fedha kidogo, inajenga kilometa tatu tu kwa mwaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupata jibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY
K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hii barabara aliyoitaja ya Amkeni kwenda Kitangali, tumekuwa tukitenga fedha kidogo kwa ajili ya ujenzi, lakini yote hii ni kutokana na uwezo wa bajeti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kujenga barabara, siyo hii tu bali ni barabara zote, kwamba kadri fedha inavyopatikana, basi Serikali itaongeza fedha. Ndiyo maana hata tukitangaza barabara pengine kilometa tatu, lakini fedha ikipatikana Serikali hatusiti kuongeza bajeti kwa ajili ya kuendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na barabara hii, kadri fedha itakavyopatikana, Serikali itazidi kuongeza kiasi cha fedha. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii, Vituo Vya Afya cha Chihangu pamoja na Mkwedu muda mrefu havina wodi za kulaza wagonjwa.
Je, ni lini Serikali itaenda kujenga wodi katika Vituo hiyo vya Afya vilivyoko Jimbo la Newala Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini kama ifutavyo: -
Mheshimiwa Spika, vituo vyetu vya afya vingi havina wodi za wazazi pamoja pia na wodi za wagonjwa wengine, kama vituo hivi ambavyo Mheshimiwa Maimuna Mtanda amevitaja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuna mpango wa kuhakikisha vituo vyote ambavyo havina majengo toshelezi tunakwenda kujenga majengo hayo kwa awamu ili yaweze kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Mnivata-Tandahimba-Newala-Masasi kilometa 160 tunafahamu kwamba fedha zake zimepatikana na kipindi cha mvua karibia kinaanza.
Je, ni lini sasa ujenzi utaanza rasmi wa barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii inafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, taratibu zote za zabuni na kuandaa zimeshakamilika. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zote za manunuzi zitakavyokuwa zimekamilka, barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Ni lini bonde la Maji la Mitema ambalo lipo Jimbo la Newala Vijijini ambalo lina maji ya kutosha litafanyiwa kazi ipasavyo ili wananchi wa Newala, Tandahimba na Nanyamba waweze kupata maji ya uhakika kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna, Mbunge wa Jimbo la Newala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mikoa ya kusini tunakwenda kuinufaisha na miradi yetu mikubwa ya Mto Ruvuma pamoja na maeneo yote ambayo yanatupatia maji ya kutosha. Hivyo bonde la maji la Mto Mitema nalo lipo kwenye mikakati yetu na kuona kwamba maeneo yote ya Newala tunakwenda kuondokana na maji ya kuokota na maji aina zote ambayo hayafai kwa matumizi ya wanadamu. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Je, Serikali imejipangaje kuhusu masoko ya ndani na nje ya nchi ili wakulima walime wakijua kwamba masoko watapata baada ya mazao kuvunwa?
Swali la Pili, kwa kuwa hali ya hewa ya Tarafa ya Chilangala, kwa leo hii imebadilika siyo kama ile miaka ya 1970 na 1980 wakati zao hili linalimwa. Je, Serikali imejipangaje kwenda kutoa elimu kwa wakulima hawa ili waweze kulima kilimo chenye tija? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtanda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, Wizara kupitia TARI - Naliendele na Mlingano, sasa hivi wanafanya mapping ya soil na kuweza kutoa elimu kwa wakulima kutokana na ekolojia ya maeneo husika na hili zoezi ni on going, tutakapoanza program ya soya katika Mikoa ya Kusini, TARI Naliendele moja ya jukumu lao la msingi itakuwa ni kutoa elimu kwa wakulima ili tuweze kupata tija, na ndiyo maana tunaanza eneo dogo la Wilaya ya Newala Vijijini and then baada ya hapo mwaka unaofuata wa 2023/2024 kulifanya hili zao kuwa ni zao la tatu katika Mikoa ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko changamoto masoko ipo hasa kwa mazao ambayo siyo ya msingi ya chakula kwa binadamu, kama mazao ya korosho na mazao mengine. Kwa hiyo, hatua ambayo tunaifanya kama Serikali sasa hivi na mtaona mwaka kesho, ni Serikali kuweka nguvu kubwa katika kuongeza thamani kwa mazao ambayo tunayazalisha ndani ya nchi na kuwasaidia private sector ambao wamewekeza katika maeneo hayo kuwapa nguvu na kuwasaidia infrastructure development ili waweze kuongeza thamani katika mazao yetu na kuhakikisha kwamba tunapata zile international certification ili tuweze kumaliza hayo matatizo.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Katika Jimbo la Newala Vijijini kuna changamoto kubwa ya mawasiliano hasa katika kata za Chitekete, Makukwe na baadhi ya vijiji vya Nambali na Mkomatu.
Je, ni lini Serikali italeta mawasiliano katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa jimbo la Newala Vijijini lina changamoto, na mimi nilishafika kule; lakini Jimbo hili baadhi ya kata tuliziingiza katika utekelezaji wa miradi wa Special Zones and Border,s lakini vile vile baadhi ya kata tumeziingiza kwenye Mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Pamoja na hayo yote Mheshimiwa Waziri pia amepanga timu moja ya kuzunguka na kujiridhisha katika maeneo ambayo yana changamoto kubwa ili tuyapatie kipaumbele, tunaamini kwamba timu hiyo itakapoleta majibu ya tathmini Waheshimiwa Wabunge tutaweza kuwahudumia kwa sababu ni dhamira ya Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Naomba kuiuliza Serikali;
Je, ni lini vijiji 63 vilivyopo katika Jimbo la Newala Vijijini ambavyo havijawahi kuona umeme kabisa vitapatiwa umeme ili nao wawe wanufaika wa nishati hii muhimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mhehsimiwa Mwenyekiti, wakandarasi katika Mkoa wa Mtwara na Lindi wako kazini wananendelea. Tumehimizana na wakandarasi walio katika maeneo hayo na kufatiliana nao kwa wakati ili kuhakikisha kazi yao inakamilika. Kama nilivyosema, ile kazi ya nyongeza na ya awali itakamilika mwezi Disemba mwaka huu 2023.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika,nakushukuru kwa kunipatia nafasi.
Ni lini Serikali itajenga karakana ngumu katika Chuo cha VETA kitangali karakana ngumu ambazo ni uselemala na welding kwa sababu karakana hizo hazipo katika chuo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika chuo chetu cha Kitangali kuna upungufu wa karakana na mimi nilishafika pale, nilifanya ziara mwaka jana kuweza kwenda kuona eneo lile na nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge katika bajeti tutakayoiandaa ya mwaka 2023/2024 tunakusudia kuhakikisha kwamba maeneo yale ambayo kuna upungufu wa karakana ikiwemo pale Kitangali pamoja na Mikumi kwa Mheshimiwa Londo tunatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa karakana kwenye maeneo hayo.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANROADS ilikuwa na utaratibu wa kujenga kwa kiwango cha lami maeneo ya vilima korofi ili kurahisisha mawasiliano ya barabara hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami eneo korofi la kilima cha Miyuyu - Ndanda ili kurahisisha mawasiliano ya usafiri kwa wananchi wa Newala wanaoenda kutibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tulishawaagiza Mameneja wote wa TANROADS na kazi hiyo imeshafanyika kuainisha maeneo yote korofi ikiwemo na maeneo haya ya vilima ambavyo viko katika Wilaya ya Newala. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vilima hivyo vitajengwa kwa kiwango cha lami ili isiwe tatizo la wananchi kupata mawasiliano kipindi cha mvua. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini Serikali ilituhakikishia kwamba kwa msimu wa 2022/2023 pembejeo zitafika kwa wakati kwa sababu upuliziaji baadhi ya maeneo huanza mwezi Mei. Kwa takwimu ambazo Mheshimiwa Waziri amezitoa, ukiangalia sulphur imefika tani 1,600, bado tani 23,400 lakini viuatilifu vya maji hadi sasa vimefika lita 730,724 bado lita 770,000. Je, Serikali imejipangaje ili kutokurudi kule ambako mwaka jana tulipata changamoto sana ya upatikanaji wa mapema wa pembejeo hizi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, Taasisi ya TPRA ime-test baadhi ya pembejeo ambazo zimefika na kukuta kuna changamoto ya baadhi ya kutokidhi vigezo na kwamba pembejeo hizo zirudishwe zilikotoka. Je, Serikali inatuambiaje hizo pembejeo hazitarudi kwa mlango mwingine kwenda kwa wakulima? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu viuatilifu ambavyo vimekuwa na mashaka kwanza nilihakikishie Bunge lako siyo viuatilifu vya msimu wa 2022/2023, bali ni viuatilifu ambavyo vilikuwa procured kwa ajili ya msimu wa 2021/2022 na sasa hivi kama Serikali tulichokifanya, viuatilifu vyote ambavyo vilikuwa vina mashaka juu ya ubora vinakusanywa na kuhifadhiwa katika ghala moja katika Mkoa wa Mtwara chini ya usimamizi wa Serikali. Kwa hiyo nataka nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba viuatilifu hivi havitarudi kwa mlango wa nyuma kwenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, kuhusu viuatilifu ambavyo vimeshafika ni ukweli kwamba mwaka jana tulikuwa na tatizo na mwaka jana tenda ilitangazwa mwezi Aprili lakini msimu huu tenda tulizitangaza toka mwezi Januari na mpaka sasa mahitaji ya viuatilifu asilimia 50 ya mahitaji ya viuatilifu vya maji tayari viko Mkoa wa Mtwara na hivi vingine tunatarajia vitafika late tarehe 30 Mei na vitashushwa katika Bandari ya Mtwara.
Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na niwahakikishie wakulima wa korosho, wote watapata viuatilifu vilivyokuwa allocated kwa wakati bila shaka. Pia mwaka huu tumeongeza idadi ya viuatilifu vya maji ili kumpa mkulima matumizi ya viuatilifu vya maji zaidi kuliko matumizi ya sulphur ambayo kwa utafiti wa TARI Naliendele matumizi ya viuatilifu vya maji ni bora zaidi kuliko sulphur na ndomana mwaka huu tumetoa idadi kubwa ya viuatilifu vya maji. Kwa hiyo nataka nimhakikishie Mbunge na wakulima wa korosho kwamba hatutakuwa na matatizo tuliyo experience mwaka jana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pamoja na majibu hayo, kuna vituo vya afya ambavyo viko mbali sana na Hospitali ya Wilaya kiasi ambacho inakuwa shida kwa wagonjwa kupelekwa katika hospitali hiyo. Kwa mfano, Kituo cha Mtambaswala ni kilomita 70 kutoka Hospitali ya Wilaya, Kituo cha Nanyumbu kilomita 40, Kituo cha Michiga kilomita 30; kwa hiyo, kwa umbali huo, naomba kupata commitment ya Serikali kwa sababu kama tutagawa equally kwa Halmashauri zote, kuna vituo vya afya ambavyo vitakuwa havifanyiwi kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba pia kupata majibu ya Serikali: Ni lini Kituo cha Afya cha Mkwedu ambacho kipo katika Jimbo la Newala Vijijini kitapelekewa gari kwa ajili ya wagonjwa kwa sababu kituo kile kinahudumia kata zaidi ya tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Vituo vya Afya vya Mtambaswala, Nanyumbu viko mbali sana kutoka Hospitali ya Halmashauri na Serikali inatambua kwamba vituo vya mbali sana vinahitaji kupata magari ya wagonjwa. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametupa fedha TAMISEMI kwa ajili ya kununua magari 407. Magari ya wagonjwa 195 kwa kila halmashauri na halmashauri hii ya Nanyumbu itapata na magari 212 kwa ajili ya usimamizi wa huduma za afya katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaona tutakuwa na magari zaidi ya hayo, lakini tutaendelea kutoa kipaumbele kwenye vituo vya mbali zaidi ili vipate magari yakiwemo vituo hivi vya afya.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mkwedu, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatafuta fedha ili tuweze kupeleka gari la wagonjwa. Nafahamu kituo hiki kiko mbali sana na kinahudumia wananchi wengi. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwakunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuiomba Serikali je, haioni haja ya kufanya review ya Wakandarasi waliopewa kazi ya REA III, Round II kwa sababu wengi wanasuasua akiwemo yule aliyepewa kazi katika Jimbo la Newala Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ipo changamoto kubwa sana ya kuchelewa kwa miradi ya REA na sababu iliyopo ni kwamba mikataba ambayo REA imeingia na Wakandarasi ni mikataba ambayo inaweka bei fixed. Bahati mbaya katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, gharama ya vifaa hasa alluminium na copper duniani imepanda kwa asilimia zaidi ya 137. Kwa hiyo, jambo ambalo Serikali imefanya ni kutafuta bajeti ya ziada kufidia ongezeko la bei za vifaa hivyo na hadi sasa tumeongea na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili kufungua mikataba na kuirekebisha kwa kuzingatia mabadiliko ya bei hizo na tunaamini kabisa kwamba hivi karibuni tutafanikiwa na miradi ile ambayo inakwamakwama kutokana na kutopatikana kwa vifaa itaendelea na hili ni kwa nchi nzima.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kuongeza posho kwa usimamizi wa mitihani, kwa sababu zoezi la usimamizi wa mitihani ni gumu wakati mwingine linagharimu ustawi wa maisha ya msimamizi husika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda Mbunge wa Newala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Hivi sasa taratibu za usahihishaji wa mitihani tunakwenda kubadilika kwa sababu tunakwenda kwenye e-marking. Tumeanza kwa mitihani ya Darasa la Saba na sasa hivi tuko kwenye pilot ya mitihani ya Ualimu na baadae tutakwenda kwenye mitihani ya Form Four na Form Six. Kwa hiyo kwanza tutapunguza sana gharama za Walimu kusogea kwenye maeneo yale ambayo tunasahihisha mitihani badala yake mitihani itakuwa inasahihishwa huko huko Mikoani.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo wakati tunakwenda kuboresha mifumo hii ya usahihishaji wa mitihani vilevile tunakwenda kuboresha na posho zile za wasahihishaji wa mitihani na wale wataokuwa wanasimamia mitihani hii. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi hili tayari liko kwenye bajeti zetu na linakwenda kukaa sawasawa. Nakushukuru sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Swali langu kwa Wizara ni kwamba, Mkoa wa Mtwara na Barabara yake ya kiuchumi kilometa 210 kutoka Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi ambayo tayari imeshajengwa kilometa 50 na fedha zimeshapatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika muda mrefu, lakini kila tukiuliza tunaambiwa Serikali ipo kwenye mchakato wa manunuzi. Sasa tunataka kujua, ni lini mchakato wa manunuzi utakamilika ili barabara hii ya kiuchumi ianze kujengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Newala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara ya Mnivata – Tandahimba – Newala hadi Masasi, kilometa 160 ipo kwenye taratibu za manunuzi. ADB wameshakubali, tumepata no objection; kwa hiyo, kinachoendelea sasa hivi ni taratibu za kawaida za manunuzi na hasa tunapokuwa tunashirikiana na wenzetu wahisani kwamba, tutakapokamilisha lot hizi mbili, zitaanza kujengwa. Tuna uhakika kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha huu, shughuli nyingi zitakuwa zimeanza katika hiyo barabara, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itajenga shule za sekondari katika kata ambazo wanafunzi wake wanatembea umbali mrefu kwa mfano Chilangala, Mkomatuu ambazo ziko katika Jimbo la Newala Vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tunafahamu na kutambua kwamba shule hizo zimejengwa tunashukuru, lakini mkakati wa kupeleka walimu ukoje kwa sababu shule hizo mpaka sasa haijapelekewa Walimu wa kufundisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la je, ni lini Serikali itajenga shule hizi kwenye kata zilizosalia? Dhamira ya Serikali ni kujenga shule katika kila kata ya nchi yetu na hii ilikuwa ni awamu ya kwanza tu. Hata hivyo, niwatoe mashaka Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwenda kwenye awamu ya pili ya kujenga shule hizi za kata na muda si mrefu wataanza kuona shule hizi zikijengwa katika halmashauri zote 184 katika nchi yetu. Kila halmashauri itapata walau shule moja kwenye awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, Mkakati wa Serikali. Wabunge ni mashahidi, wameona namna gani Serikali hii ya Awamu ya Sita imetangaza ajira zaidi ya 21,000 kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Angela Kairuki ya kuajiri Walimu na watumishi katika Sekta ya Afya. Hii yote ni kwenda kuhakikisha kwamba Serikali inaziba mapengo haya ya Walimu ambao wanahitajika kwenye maeneo haya. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Jimbo la Newala Vijijini lina vijiji zaidi ya 60 ambavyo havijapatiwa umeme. Je, ni lini Mradi wa REA, mzunguko wa pili, utaenda kumaliza tatizo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, unaendelea na tunatarajia utakamilika ifikapo Desemba, 2023. Katika Jimbo la Newala Vijijini napo mradi huu utatakiwa ukamilike na vijiji vyote vilivyopo vitapata umeme.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina shule moja tu ya sekondari ya kidato cha tano; lakini inazo shule mbili ambazo zina sifa ya kuwa kidato cha tano, Shule ya sekondari ya Mpotola na Shule ya Sekondari Makukwe, lakini tuna shindwa kwa sababu hatuna mabweni au hosteli.
Je, ni lini Serikali itatuunga mkono kutujengea hosteli ili tuanze kidato cha tano na cha sita katika shule hizo mbili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda Mbunge wa Newala vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu na yeye, kwamba Serikali imesikia na imepokea hayo maombi na itayafanyia kazi kwa kadri ambavyo tunatafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa hiyo huduma ya kidato cha tano na sita na Watanzania wote kwa ujumla, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, suala la upembuzi yakinifu limechukua muda mrefu sana, ndiyo kwanza saa hizi Serikali imejipanga kuanza kutenga fedha.
Je, Serikali haioni kwamba ujenzi wa bandari katika mwambao wa Bahari ya Hindi ungerahisisha sana na kupunguza suala la ukosefu wa ajira kwa wananchi wa Tanzania, hususan wa Mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mkoa wa Mtwara unalima mazao ya mihogo, njugu, mbaazi, nazi, mazao ambayo yanahitajika sana kule Comoro. Je, Serikali haioni kwamba kama kungekuwa na meli hii uwepo wake ungechechemua sana uchumi wa watu wa Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imechukua muda mrefu kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na ulianza tangu mwaka 2019 na 2021. Hii ilikuwa ni kwanza lazima ilitakiwa tujiridhishe – na huu ulikuwa upembuzi yakinifu wa awali – tujiridhishe kiasi cha mzigo utakaotoka Mtwara kwenda Comoro ili tujue ni aina gani ya mali na ukubwa wake, ambaye Serikali kwayo itakwenda kujenga ama kutengeneza.
Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo, kwa kuwa katika Mwaka wa Fedha ujao tumetenga fedha sasa kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa kina wa mwisho ili tupate uhalisia wa aina gani ya meli hii.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili; Serikali inatambua juhudi za wakulima wa Mtwara, hususan wale wote ambao wanalima mazao mbalimbali. Na kuna kila sababu ya kwamba wawe na meli inayosafirisha mazao yao kutoka Mtwara kwenda Visiwa vya Comoro.
Mheshimiwa Spika, na kwa jitihada hizo, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ziara aliyoifanya Ufaransa, ndiyo maana meli hizi sasa zimeshaanza kuja nchini, hususan katika Kampuni ya CMA, CGM pamoja na UFL Express, maana kwamba Mtwara itakuwa hub, na Nchi jirani kama Comoro, Mozambique pamoja na Malawi watakuwa wanachukua mizigo pale kwenda maeneo yao, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini pia naishukuru Serikali kwamba kuna mradi mkubwa wa Makonde ambao wametupatia fedha unatekelezwa kwenye Wilaya yetu ya Newala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi lilihusu Jimbo la Newala Vijijini. Kumbuka kwamba Newala ina Majimbo mawili ambayo ni Newala Mjini na Newala Vijijini, kwa hiyo swali lilikuwa specific kwa Newala Vijijini. Sasa kwa kujumlisha hivi tutashindwa kupata uhalisia wake wa tatizo hasa ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa, pamoja na yote yaliyojitokeza, kwenye Jimbo la Newala Vijijini kuna Mradi wa Maji wa Mnima – Miyuyu ambao umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2018, na mradi ule ulikuwa ni wa miezi tisa. Mpaka sasa utekelezaji wake ni asilimia 65 tu. Pia changamoto ambayo inasababisha mradi huu kutokamilika ni kukosekana kwa fedha. Fedha zilizokuwa zimetengwa ni bilioni 1.3, zimelipwa milioni 614 tu. Je, ni lini Serikali itamaliza fedha zilizobakia ili wananchi wa Newala Vijijini waweze kupata maji?
Swali la pili, kwenye Vijiji vya Mkudumba, Mnyengachi, Mnyambe, Mnima, Bahati, Mikumbi, Mkongi, Namangudu, Nangujane, Chilende, Mkoma, ‘two’ pamoja na Lihanga kuna miradi ya maji ambayo inatekelezwa. Lakini miradi ile ina changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili miradi hii ikamilike? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Miyuyu tatizo ni fedha na swali lake la pili tatizo pia ni fedha. Naomba niwe nimepokea masuala haya ya Newala Vijijini na nitafanyia kazi mimi mwenyewe kwa ukaribu kuhakikisha fedha zinakwenda na kazi inakamilika kwa wakati.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii. Nina swali la nyongeza. Jimbo la Newala vijijini maeneo yake mengi yanakosa mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itakuja kujenga minara katika jimbo lile ili mawasiliano yaweze kuboreshwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri, mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tumeshafanya ziara katika jimbo lake na maeneo ambayo yalikuwa na changamoto, Serikali iliyachukua na tayari yameingizwa kwenye utekelezaji wa miradi 758 ambapo kata 713 zinaenda kuguswa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi bali awe na subira wakati utekelezaji ukiwa unaanza, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii. Jimbo la Newala Vijijini lina jumla ya walimu 475 kati ya walimu 787 wanaohitajika kuwepo.
Je, ni lini Serikali itapeleka walimu 312 ambao ni upungufu katika Jimbo la Newala Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa Kada ya Elimu na pia imeendelea kupeleka walimu katika Halmashairi ya Newala Vijijini lakini tunatambua kwamba bado kuna upungufu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba kadri Serikali itakavyokuwa inaajiri walimu, tutatoa kipaumbele katika Halmashauri ya Newala Vijijini. Ahsante.
MHE. MAIMUNA SALUM MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwamba asilimia kubwa ya wakulima wa zao hili ni wanawake, je, mkakati wa kutoa elimu pia kuwahusisha wanaume ili na wao waweze kujiongezea kipato kupitia zao hili ukoje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa product itokanayo na zao la mwani ni muhimu sana kwa afya ya wananchi wote wakiwemo wanaume pamoja na wanawake. Je Serikali haioni haja sasa ya kutumia Vyombo vya Habari kuujulisha umma umuhimu wa zao hili ili wananchi wengi waweze kulilima na kupata mazao au kupata ajira zitokanazo na zao hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua umuhimu wa zao hili na jitihada mojawapo ya sasa na mkakati ambao tulionao katika maeneo ambayo yanazunguka Ukanda wa Pwani na wamekuwa wakituona maeneo mbalimbali ni kutangaza kwa makundi yote mawili wanawake na wanaume kuhakikisha wanashiriki katika zao hili la mwani. Kwa hiyo kazi hiyo tunaifanya na tutaongeza jitihada kuifanya ili ongezeko la watu wanaojihusisha na shughuli hizo wawe wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutumia Vyombo vya Habari, sasa hivi tumekuwa tukifanya ukiangalia TBC kuna vipindi vinavyohusisha kilimo cha mwani, lakini tutaongeza mara dufu zaidi ili tutanue wigo mpana ili vyombo vya Habari viweze kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo jambo hilo tumelipokea na tutalifanya, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kwanza tunaishukuru lakini nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ili barabara hii ilete ile tija ambayo imekusudiwa ni vyema ikakamilika kwa haraka ili kunusuru maisha ya wananchi pamoja na mali zao. Ni upi sasa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha barabara hii inatengewa fedha za dharura ili iweze kukamilisha ujenzi kwa haraka iwezekanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, jiografia ya Wilaya ya Newala kila upande ambao utaingilia unakutana na vilima vikali. Kwa mfano Nadimba Chiwata, Mikumbi, Mpanyani, Mkoma II Chimemena, Lihanga Chikalole. Ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba barabara hizi ambazo nimezitaja zinajengwa angalau kwa kiwango cha changarawe? nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mtanda la kwanza la mpango wa dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekwishakusema katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali katika mwaka wa fedha huu ambao tupo sasa tumeutekeleza ilitenga shilingi milioni 825 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Mwaka wa fedha tunaoenda kuuanza mwezi Julai 2023/2024 TARURA imetenga shilingi bilioni moja na tayari bado matengenezo haya yanaendelea na yapo asilimia 52.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kuhakikisha kwamba hii bilioni moja inaenda haraka katika Jimbo la Newala Vijijini kwa ajili ya kutekeleza kipande cha barabara ambacho kimetengwa kwa utekelezaji wake ili wananchi waweze kupita kwa sababu barabara hii inaunganisha Jimbo la Ndanda na Jimbo la Newala Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mwambe na Mheshimiwa Mtanda wamekuwa wakifatilia sana barabara hii. Nikienda kwenye swali lake la pili la barabara hii ambayo inapita Nandimba, Chiwata ambayo inatoka Newala Vijijini kuelekea Masasi tutaendelea kutafuta fedha na kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara hii na kipaumbele kikiwa katika maeneo ya vilima vikali.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa nafasi hii nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sasa Serikali haioni kwamba kuna haja ya kubadilisha sheria iliyopo ambayo inawanyima haki watoto wale kwa sababu wanaachwa wakiwa wadogo sana, wachanga, kiasi kwamba inaweza ikawasababishia vifo kwa kukosa uangalizi wa karibu wa mama?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kwamba, Serikali sasa haini kwamba kwa kumnyima hizo haki mama yule ambaye amejifungua mtoto njiti wa siku zile za nyongeza kunaweza kukamsababishia matatizo ya afya ya akili ambayo itagharimu tena Serikali kumtibia matatizo ya afya ya akili ambayo yatamfanya asifanye kazi yake ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la kubadilsha sheria nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sheria zipo, miongozo ipo na taratibu zipo. Changamoto inayotokea labda ni ile ambayo naweza kusema kwamba kuna baadhi ya Waajiri ambao kwa roho mbaya tu wanaamua kuwanyima hawa wazazi wanaopata watoto njiti. Lakini kwa upande wa sheria na zote zimeelezwa wazi, na mimi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, lakini pia kutoa maelekezo kwa waajiri wote kwamba inapotokea mama amepata mtoto njiti na mazingira yanafahamika, watoto wanatakiwa kulelewa katika kangaroo basi ni wito wangu kwamba waongozwe pia na ubinadamu katika yale mamlaka ambayo wamepewa ili waweze kuwapa nafasi wazazi wakalee watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili katika maeneo ambayo kinamama may be labda wanakumbwa na hili tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliita kwamba tatizo la afya ya akili; nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali inayoongozwa na mwanamama Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali wakinamama Watanzania, inawajali watoto wa Tanzania lakini pia inatambua na kuheshimu na kulea afya za akili za Watanzania. Kwa hiyo nataka nikuhakikishie kwamba kama panapotokea matatizo hayo Mheshimiwa Rais ameishatoa maelekezo lakini pia na sisi tuwe chini yake tunamsadia, tumekwishapewa maelekezo na tunachotakiwa kufanya ni kuwaonea huruma wazazi hawa na kuwapa nafasi ili waende wakalee watoto wao ambao wamezaliwa katika mazinguru magumu kama hayo yaliyotajwa. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENNEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yanayotolewa na Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete nimesimama kwa sababu ya uzito la suala la watoto njiti. Wazazi wao wanapotakiwa wakimaliza siku 84 katika likizo ya uzazi, na bila shaka wote tunakubaliana kwamba siku 84 kwa mtoto aliyezaliwa njiti anakuwa bado hajaimarika sawa sawa; na unjiti unatofautiana, wengine wanazaliwa na miezi sita, wengine wanazaliwa miezi saba, wengine wanazaliwa miezi nane wanakuwa hawajakamilika uumbaji unakuwa bado unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo chama/NGO inayohusiana na masuala ya kusaidia watoto njiti, wamekwishaleta malalamiko mengi sana Serikali. Sasa leo nataka nionyeshe mahala ambapo Waheshimiwa Wabunge tusaidiane katika kuona kama tunahitaji kweli kubadilisha sheria au sheria iliyopo inajitosheleza kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Kanuni za Utumishi wa Umma ya Mwaka 2009 Kanuni ya pili, H16 mnaweza mka-google hata nikimaliza kujibu swali mtapata maelezo yanayosema; “Except in cases of illness or other cases of emergence” yaani kwenye kesi hizi mtumishi ana haki ya kuomba extension of leave. Sasa tunajaribu kuona kama inatosha au haitoshi Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu kundi hili ni kweli mtu akizaliwa anapofariki inaumiza sana na wengi humu tumezaliwa tukiwa njiti. Hatujisemi tu humu lakini tusingeangaliwa kwa zaidi ya siku 84 tungekuwa hatupo leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuipitie hiyo Kanuni halafu Waheshimiwa Wabunge wale wenye maoni, watatuletea maoni kama inatosha au haitoshi? (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, VETA Kitangari inahudumia majimbo mawili; Newala Mjini pamoja na Newala Vijijini, kwa hiyo, inasababisha usafiri wa wanafunzi kutoka kwenye maeneo yao kwenda katika eneo VETA ilipo ni mbali. Ujenzi ambao umetajwa na Serikali hauhusishi bweni la wavulana katika VETA hii.
Je, ni lini Serikali itaweka kwenye mpango ujenzi wa bweni la wavulana katika VETA ile ya Kitangari ili kuleta urahisi wa usafiri?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; linahusu watumishi, katika fani za umeme, ushonaji na uhazili, kuna mwalimu mmoja mmoja kiasi kwamba akipata dharura wanafunzi wale hawasomi.
Je, lini Serikali itapeleka walimu katika fani hizo, angalau mmoja mmoja, ili kuleta ufanisi na usomaji mzuri kwa wanafunzi katika VETA Kitangari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtanda, Mbunge wa Newala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, kwamba katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi milioni hizo 666 na katika fedha hizi tayari tumeshapeleka milioni 304 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa baadhi ya majengo. Kwa hiyo nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli ujenzi wa bweni ukawa bado kutokana na fedha iliyopelekwa. Lakini naomba nimhakikishie fungu lililobaki kati ya ile milioni 666 tutakapopeleka fungu hili la pili, ujenzi wa bweni hilo utakuwa umeanza na tutaendelea nao kwa kadri ya fedha tutakavyokuwa tunapeleka.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili la watumishi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu; Mheshimiwa Rais alitoa kibali cha kuajiri watumishi 514 katika mwaka huu wa fedha na mpaka sasa tumeshaajiri watumishi 169. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na eneo la Newala lakini tunafahamu tuna vyuo vya zamani na tuna vyuo vipya 25 vile vya Wilaya, vinne vya Mikoa tunakwenda kuwapangia walimu maeneo haya ili kuhakikisha kwamba taalum hii inaweza kutolewa katika maeneo hayo kwa uhakika, nakushukuru sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kupata nafasi.
Nilitaka kujua ni lini Serikali itatafuta fedha kwaajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Amkeni – Kitangali kwenda Mtama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina azma ya kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami lakini kinachotegemea ni upatikanaji wa fedha na bajeti itakavyoruhusu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakavyopatikana barabara hii pia itaingizwa kwenye mpango ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nami niulize swali moja la nyongeza.
Barabara ya kutoka Mtama – Kitangali hadi Amkeni – Newala, yenye urefu wa kilometa 74 ipo kwenye zoezi la Upembuzi Yakinifu, ni lini zoezi hili litakamilika ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, suala la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ni suala ambalo linategemeana na aina ya barabara yenyewe. Kwa hiyo, mandhari tumeanza tunategemea kwamba, usanifu kwa urefu wa kilometa hizi 74 haziwezi kuzidi mwaka lakini namshawishi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunategemea ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanza usanifu utakuwa umekamilika wa hii barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naipongeza Serikali kwa kufanya zoezi la kuhakiki na kubaini wazee hao ambao hawana uwezo. Pia, pamoja na kuwabaini, Serikali ikawapatia vitambulisho vya ICHF kwa ajili ya kupata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni kwamba pamoja na kupewa hivyo vitambulisho, wakienda kwenye maeneo ya kupata huduma za afya wanaishia kutangatanga kwa sababu hawapati dawa.
Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wazee hawa sasa watapata dawa bila matatizo?
Swali la pili; huko nyuma kulikuwa na slogan ilikuwa inasema” Mpishe Mzee Kwanza” sasa hivi slogan hiyo imeanza kupotea, wazee wanahangaika, wakienda kupata huduma sehemu nyingine hata hospitali na maeneo mengine, hakuna anayejali.
Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunarudi kwenye mkakati ule wa mwanzo wa kuhakikisha wazee wanapishwa ili kupata huduma kwanza ili wakaendelee na mambo yao mengine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hawa wazee kwenda kwenye vituo vya huduma za afya pamoja na vitambulisho vyao wanakuwa hawapati huduma, tutafanya ufuatiliaji kwa sababu huenda wako watu ambao hawawathamini wazee hawa waliotambuliwa kuwa hawana uwezo kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na Wizara Mama ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tutashirikiana na Mabaraza ya Wazee yaliyopo nchini kote ili kufuatilia na kupata maoni ya wazee hawa wasiopata hizo huduma ni kwenye maeneo gani hasa, kwa sababu vipo vituo vya afya vingine vinafanya vizuri sana. Huenda ni baadhi ya maeneo ambayo tutayafuatilia tuyaibue na tushirikiane na Mheshimiwa Waziri wa Afya kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili la kampeni ya “Mpishe Mzee, Mzee ni Tunu Apate Huduma”, kama kuna mahala pameanza kusinzia pia tutafanya ufuatiliaji maana kampeni hii ni endelevu na tuliianzisha mwaka 2021 na imeendelea vizuri mwaka 2022. Sasa kama kuna mahala panalegalega, napeleka tu salamu kwa wale wanaotakiwa kufanya kazi hiyo wakiwemo Maafisa Ustawi wa Jamii wakishirikiana na Wakuu wa Vituo kupitia Waziri mwenye dhamana ya afya, tutafanya ufuatiliaji ili kuiinua tena kampeni hiyo. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Nami naomba niulize swali moja.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya watumishi wa afya wanaohitajika katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala ni 624, waliopo mpaka sasa ni 119 sawa na asilimia 19, na tuliopata juzi ni 38 tu, upungufu bado upo; je, Serikali inasema nini kuhusu kujaza nafasi za watumishi katika kada ya afya kwa Halmashauri ya Jimbo la Newala Vijijini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, jinsi ambavyo bajeti itaendelea kuruhusu, maeneo kama hayo ambayo anayasema Mheshimiwa Mbunge yataendelea kupewa kipaumbele. Utaona wakati wa application wa hizi nafasi zilizotangazwa, umeona kabisa yameainishwa maeneo ambayo wanaruhusiwa watumishi ku-apply na wametajiwa kabisa utaenda hapa, utaenda hapa. Tutaendelea kusisitiza kabisa maeneo yenye upungufu zaidi yanapotokea kibali ndiyo yapewe kipaumbele. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Barabara ya kutoka Mtama – Kitangali kwenda Newala Jimbo la Newala Vijijini inapitika kwa shida kwa sababu ya ubovu wa barabara ile kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuwanusuru wananchi wa Newala na hali ambayo ipo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Mtama – Newala ni kweli barabara hii Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiomba muda mrefu kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuitengeneza barabara hii kwa kiwango cha changarawe. Kwenye vipaumbele vya Wizara ya Ujenzi tutaangalia namna ya kuanza kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana kwa kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kufahamu mkakati ambao Serikali inao katika kuajiri watumishi ambao sio walimu. Kwa mfano, pale chuoni hakuna matron, hakuna patron, hakuna dereva wala wapishi, mkakati ukoje ili huduma ziweze kutolewa kwa ukamilifu katika chuo kile?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kupitia majibu ambayo Serikali imeyatoa, imeonesha kwamba fani ziko tatu, na ni kweli fani tatu tu ambazo zinatolewa kati ya fani nyingi ambazo tunatarajia zitolewe ili wanafunzi wengi au wananchi wengi wapate nafasi ya kupata ujuzi. Mfano, hakuna fani ya mafundi magari, hatuna fani ya ujenzi, hatuna fani ya uunganishaji wa vyuma pamoja na mabomba. Mpango wa Serikali wa kuongeza fani nyingine ukoje ili kuwakwamua wananchi wa Newala ambao wanahitaji fani hizi ili waweze kujiendeleza kimaisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna kuhusiana na suala la watumishi wasiokuwa walimu, naomba nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Maimuna kwamba kunapo mwezi wa Tatu mwaka huu, 2024 tayari tulishatangaza nafasi za watumishi wasiokuwa walimu kwa vyuo vyetu vyote vya VETA. Kwa hiyo, mara tu baada ya mchakato huu kukamilika, baadhi ya watumishi watakaopatikana tutawapeleka katika chuo hiki cha Kitangari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuhusiana na suala la kuongeza fani, Mheshimiwa Maimuna nadhani anafahamu kuna maboresho ambayo tunaendelea pale kwa maana ya ujenzi wa mabweni na ukarabati wa karakana pamoja na madarasa. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha kwanza miundombinu na baada ya uboreshaji huo wa miundombinu, utaratibu wa kuongeza fani sasa tutaweza kuufanya ili uweze kuendana na miundombinu iliyopo katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kumwuliza Naibu Waziri wa Ujenzi: Ni lini Serikali itatafuta fedha ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya Amkeni – Kitangali hadi Mtama kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoanisha Serikali inaitambua. Tutakamilisha kwanza kufanya usanifu wa kina halafu baada ya hapo, Serikali itatafuta fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itafanya ukarabati na upanuzi katika Kituo cha Afya Mkwedu kilichopo Jimbo la Newala Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba twende tukakifanyie tathmini kituo hiki cha afya katika Halmashauri ya Newala Vijijini ili tuweze kuona kiasi cha fedha kinachohitajika na tuweke mipango ya kwenda kukarabati, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la ku-mobilize resource katika Barabara ya Mnivata – Newala – Masasi limechukua muda mrefu na barabara haipitiki. Je, ni lini ujenzi rasmi wa lami utaanza ili wananchi wapite vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza uzuri wa hiyo barabara inafadhiliwa na wenzetu wa African Development Bank na tunafanya ufuatiliaji. Kitu ambacho nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge ni kwamba katika kipindi hiki cha mvua na hasa mvua ambayo imezidi, imekuwa zaidi ya wastani, kwa hiyo, kwenye miundombinu ya barabara imekuwa ni ngumu sana kufanya kazi za barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kuna changamoto yoyote ya mobilization kwenye hiyo barabara, tutafuatilia tuone kama kuna changamoto yoyote, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa sababu Mradi wa Maji wa Makonde ni mradi ambao ni wa muda mrefu, Serikali mwaka 2022 ilituchimbia visima kwenye Kijiji cha Mpalu na Lochinu kwenye Jimbo la Newala Vijijini, lakini visima vile havijasambaza maji mpaka kwa wananchi. Je, ni lini Serikali itapeleka miundombinu ili yale maji kwenye visima yafike kwa wananchi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, visima vyote ambavyo tumeshavichimba na tumesha-test, tumeshafanya pump test, tunaenda kuhakikisha kwamba sasa tunaenda kujenga a point source kwa ajili ya wananchi kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naishukuru Serikali kwamba imeona umuhimu wa uwanja ule kwa sababu ni uwanja ambao ulitumika kukomboa nchi za Kusini mwa Afrika na ule ni miongoni mwa viwanja hivyo. Kwa hiyo, nataka kujua kama Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kwenda Newala ili kuona hali ya uwanja ule?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba, ni zaidi ya miezi mitatu sasa imepita tangu mkataba wa jengo la abiria kwenye uwanja wa Mtwara usainiwe, lakini mkandarasi hajalipwa advance payment ili ujenzi huo uanze. Je, ni lini Serikali italipa advance payment ili ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa Mtwara uanze kujengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali napokea shukurani, na ninaomba shukrani hizi ziende kwa Rais wetu mpendwa ambaye anajenga viwanja takribani nchi nzima. Pia, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kutembelea eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amezungumza kuhusiana na jengo la abiria Mtwara. Serikali katika awamu ya kwanza imefanya kazi kubwa ya kujenga runway katika uwanja wa Mtwara, kuweka taa za barabarani, maegesho, na kadhalika. katika hatua ya pili Serikali imeshasaini mkataba wa takribani shilingi bilioni 67 ambapo tunajenga jengo la abiria, control tower, jengo la zimamoto, hali ya hewa, na kadhalika. Vilevile, hivi ninavyozungumza tayari mkandarasi amekabidhiwa site na ujenzi unaanza mara moja.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ni lini zoezi la upembuzi yakinifu kwenye Barabara ya Mtama – Kitangali – Newala utakamilika ili ujenzi kwa kiwango cha lami uanze kwenye barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, upembuzi na usanifu wa kina unategemea mkataba wenyewe na kazi yenyewe ilivyo. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunategemea utakamilika kwa mujibu wa mkataba. Kama kutatokea changamoto zozote ama kama kuna changamoto zozote Mheshimiwa Mbunge ameziona, basi tuwasiliane ili tuweze kuzitatua, lakini tunategemea utatekelezwa na kutimizwa kwa mujibu wa mkataba. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza Serikali kwa majibu mazuri ambayo wameyatoa lakini nataka kufahamu tu kwamba, yapo maeneo mengi katika nchi yetu ambayo yanafaa sana kwa ufugaji wa nyuki. Ninashukuru wamesema wanaanza mikakati ya kuelimisha Watanzania, lakini naomba niulize; swali la kwanza; ni upi sasa mkakati ambao Serikali imejiwekea ili wale wananchi ambao wanaishi kule vijijini wapate kwa uhakika elimu hii ili ilete manufaa kwa wafugaji wa nyuki wanaoishi vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Newala Vijijini ili aone namna ambavyo mazingira yetu ni mazuri kwa ufugaji wa nyuki na kuleta hamasa kwa wananchi wa Newala Vijijini? Nakushukuru (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumekuwa na mipango mbalimbali ya kutoa elimu kwa wananchi na kama mnavyofahamu kwenye kila Halmashauri tunao Maafisa Nyuki. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwajengea uwezo ili waweze kutoa elimu hiyo. Vilevile, kupitia makongamano ambayo tumekuwa tukiyaandaa tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi na pale ambapo kuna vikundi ambavyo vinahitaji kupatiwa elimu, tumeweza kuwasaidia Maafisa Nyuki waliopo kwenye Halmashauri zetu kuweza kutoa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa wananchi kujiingiza kwa nguvu kubwa katika ufugaji wa nyuki, kwa sababu biashara ya asali na bidhaa zinazoambatana nazo ni kubwa na hivi karibuni Serikali imefanya jambo kubwa. Tumeweza kupata soko kubwa kule Nchini China ambalo kwa mwaka wanahitaji tani 38,000,000. Kwa hiyo, hii ni fursa kwetu sasa kuweza kuchangamkia soko hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Newala kuona jinsi ambavyo tunaweza kushirikiana, kuhamasisha ufugaji wa nyuki na biashara hii katika eneo hilo.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ni lini zoezi la upembuzi yakinifu kwenye Barabara ya Mtama – Kitangali – Newala utakamilika ili ujenzi kwa kiwango cha lami uanze kwenye barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, upembuzi na usanifu wa kina unategemea mkataba wenyewe na kazi yenyewe ilivyo. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunategemea utakamilika kwa mujibu wa mkataba. Kama kutatokea changamoto zozote ama kama kuna changamoto zozote Mheshimiwa Mbunge ameziona, basi tuwasiliane ili tuweze kuzitatua, lakini tunategemea utatekelezwa na kutimizwa kwa mujibu wa mkataba. Ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa. Ni lini Serikali itajenga nyumba za walimu katika shule za Sekondari za Jimbo la Newala Vijijini ili kuwapunguzia umbali walimu ambao wanakaa mbali na shule? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga nyumba za walimu kupitia taratibu mbalimbali na kupitia utaratibu wa program. Kwa mfano programu ya GPE, TSP na kupitia mradi wa SEQUIP Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba inatenga fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatambua kwamba jukumu lote la kujenga nyumba za walimu haliwezi kutekelezwa na Serikali kuu peke yake. Ndiyo maana tunasisitiza na Halmashauri zenyewe ziweze kutenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani na Wakurugenzi waweze kufanya tathmini sahihi ya kujua uhitaji wa nyumba hizi za walimu ili kwa pamoja kupitia miradi hii inayotoka Serikali Kuu na kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa pamoja tuweze kushirikiana kuhakikisha kwamba walimu wanajengewa nyumba za kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa muktadha huo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu Tanzania nzima lakini pia hususan katika Mkoa na Jimbo analotoka Mheshimiwa Mbunge.