Primary Questions from Hon. Alexander Pastory Mnyeti (5 total)
MHE. ALEXANDER P. MNYETI Aliuliza: -
Chanzo cha Maji cha Ihelele kilichopo Kijiji cha Nyanhomango kinasambaza maji katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora: -
Je, ni lini Serikali itapeleka miundombinu ya maji kwenye Kijiji hicho pamoja na vijiji vingine vinavyozunguka chanzo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Nyanhomango kilichopo katika Kata ya Ilujamate, kinapata huduma ya maji katika Skimu yenye chanzo kilichopo katika Ziwa Victoria kwenye bomba la kutoka Mabale kwenda Mbarika. Skimu hiyo inazalisha lita 1,555,200 kwa siku ambapo maji yanayozalishwa yanatosheleza mahitaji ya eneo lote ikiwemo Kijiji cha Nyanhomango. Huduma ya maji inapatikana kwenye vituo 9 vya kuchotea maji na tanki moja lenye ujazo wa lita 135,000.
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Isesa katika Kata ya Ilujamate kinapata huduma ya maji kupitia skimu yenye chanzo cha kisima kirefu inayozalisha lita 116,000 kwa siku ukilinganisha na mahitaji ya kijiji hicho ambayo ni lita 91,100 kwa siku. Skimu hiyo ina vituo 12 vya kuchotea maji na tanki moja lenye ujazo wa lita 135,000.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, Serikali kupitia RUWASA inatekeleza Mradi mkubwa wa Maji Ilujamate – Buhingo utakaonufaisha vijiji 16 vilivyopo karibu na chanzo cha Ihelele. Vijiji hivyo ni Gukwa, Mbalama, Buhunda, Mwagimagi, Kifune, Gulumungu, Lukanga, Nyambiti, Busongo, Ng’hamve, Nyamayinza, Songiwe, Seeke, Buhingo, Kabale na Mwasagela.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2021. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa matenki matatu yenye jumla ya ujazo wa lita 850,000, ulazaji wa bomba kuu kilometa 34.4, mabomba ya usambazaji maji kilometa 35 na vituo vya kuchotea maji 25. Kukamilika kwa mradi huo kutaboresha huduma ya maji kutoka asilimia 73 za sasa hadi asilimia 88 mwaka 2023.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji kwenye Mji wa Usagara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Wilayani Misungwi ni asilimia 73. Katika juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo, katika mwaka 2021/2022, Serikali kupitia Programu ya Lake Victoria Water and Sanitation imepanga kutekeleza mradi wa maji katika maeneo ya Usagara, Buswelu, Kisesa na Buhongwa. Mradi huu utahusisha ujenzi wa vituo vya kusukuma maji viwili, mifumo ya usafirishaji na usambazaji maji yatakayozalishwa na Chanzo kipya cha Maji Butimba, ulazaji wa mabomba makubwa yenye ukubwa wa kuanzia milimita 50 hadi 600 kwa umbali wa kilomita 50, ujenzi wa matanki manne ya ukubwa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo utanufaisha maeneo yote ya Mji wa Usagara ikiwemo Usagara, Fela, Nyang’homango, Idetemya, Ukiliguru, Ntende, Sanjo, Isamilo, Mayolwa, Bukumbi na Kigongo.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya Maji katika Kituo cha Utafiti na Chuo cha Kilimo Ukirigulu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Utafiti na Chuo cha Kilimo Ukirigulu kilikuwa na Skimu ya Maji iliyojengwa mwaka 1965. Chanzo cha maji cha skimu hiyo ni Ziwa Victoria na ina matenki mawili ya maji. Moja lipo Kijiji cha Mwalogwabagole na lingine liko eneo la chuo hicho. Skimu hiyo ina vituo vya kuchotea maji 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu wa mradi kwa ajili ya ukarabati wa skimu hiyo umekamilika na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi 630,733,364 ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji na kutahusisha ulazaji wa mabomba mapya kilometa 40.4 na ukarabati wa matenki mawili katika Kituo cha Ukirigulu na Kijiji cha Mwalogwabagole yenye lita za ujazo 225,000. Chuo cha Ukirigulu pamoja na Vijiji vya Mwalogwabagole, Buganda, Nyagholongo, Ngudama, Nyamule, Mwagala, Nyamikoma vitanufaika baada ya kukamilika kwa mradi na ukarabati wa skimu hiyo na jumla ya wananchi 19,658 watanufaika.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Mwanangwa – Misasi – Kahama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwanangwa – Misasi – Kawekamo – Solwa – Kahama yenye urefu wa kilometa 150, ilifanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kukamilika mwaka 2017 kwa gharama ya shilingi milioni 798.8. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili iendelee kupitika kipindi chote cha mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 2,809.304 zimetengwa kwa matengenezo mbalimbali pamoja na ujenzi wa madaraja saba katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko. Madaraja hayo ni madaraja mawili katika eneo la Mwanzugi, madaraja matatu katika eneo la Mwakitolyo na madaraja mawili katika eneo la Solwa.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi wa kilometa 5.15 kwa kiwango cha lami katika eneo la Kahama kuelekea Solwa. Ahsante.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Mji wa Misasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waaziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti Mbunge wa Misungwi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Misasi ina vijiji Vinne (4) vya Inonelwa, Misasi, Mwasagela na Manawa na vinapata huduma ya maji kupitia visima virefu viwili pamoja na skimu za maji za mtandao wa bomba. Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Kata hiyo ni asilimia 40. Katika kuboresha huduma ya maji katika Kata ya Misasi, Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi unaotoa maji kwenye bomba kuu la Mabale-Mbarika kwenda kwenye vijiji vya Kata hiyo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi huo kutaboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Kata ya Misasi kufikia asilimia 80. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaendelea na upanuzi wa mradi huo ili kuhakikisha wananchi wote wa Kata ya hiyo wanapata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza.