Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Alexander Pastory Mnyeti (23 total)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu hayo ya Serikali yenye kuleta matumaini kwa wananchi wa Lindi Manispaa. Hata hivyo, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Lindi Manispaa tumeshatenga ekari moja na nusu kwa ajili ya ujenzi wa soko hili la samaki, vilevile tuna wavuvi 2,193 ambao wamesajiliwa na wachuuzi wadogo wadogo 470 ambao wanakosa mahali pa kufanyia shughuli zao za biashara. Naomba Serikali itupe majibu ya uhakika na ya kueleweka ya kuwapa wananchi wa Lindi Manispaa matumaini; ni lini sasa mtaanza kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa soko la Samaki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wavuvi kwa kuwakopesha maboti, pamoja na nyavu na injini ili wavuvi hawa sasa waendeleze uvuvi wao kwa vifaa hivi vyenye uhakika na usalama wa kutosha? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza swali lake la nyongeza kuwa tayari Halmashauri ya Manispaa ya Lindi tayari wameshakupata eneo, namwomba baada ya Bunge hili twende na wataalamu pale Lindi tukahakiki hilo eneo na wataalamu na tukishajua eneo hilo lililopatikana lina ukubwa gani na linafaa kwa matumizi hayo, Wizara iko tayari kuanza ujenzi wa soko hilo mara moja.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kuhusu zana. Tathmini tayari imeshafanyika, wataalamu wameshafanya tathmini ya zana gani zinafaa kwa maeneo hayo ya wavuvi, namwomba baada ya hili, kwa sababu tayari kila kitu kimeshafanyika, basi baada ya Bunge hili tuambatane naye kama nilivyosema hapo awali, twende kwa wavuvi hao kuhakiki ni aina gani ya zana zinazohitajika ili Serikakli ione namna ya kuanza kuwakopesha wavuvi hao hizo zana, ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini Serikali itaanza mpango wa kujenga soko jipya la kisasa la samaki katika Wilaya ya Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, swali la nyongeza Mheshimiwa Ndugulile, anataka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko jipya Kigamboni. Ujenzi wa soko jipya Kigamboni utategemea uwezekano wa kibajeti. Kama Serikali itapata bajeti, basi iko tayati kuanza ujenzi wa soko hilo jipya pale Kigamboni, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, swali dogo la nyongeza. Hali ya soko la samaki Tanga ni sawa sawa kabisa na hali ya soko la samaki Lindi; je, ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha linapatikana soko la samaki la kisasa kwenye Jiji la Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge katika swali lake, wako wataalam wanafanya tathmini ya kuyatambua hayo masoko yote nchi nzima. Tunaomba nafasi ili wataalam hao waendelee na tathmini hiyo, na wakishamaliza, Serikali itatoa utaratibu wa namna gani masoko hayo yanakwenda kujengwa katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Miundombinu ya soko la samaki katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ni mibovu na mibaya hasa sehemu ya jiko pamoja na ofisi. Nini mkakati wa Serikali kuboresha miuondombinu hiyo? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, soko la Mikindani ni kama masoko mengine ambayo nimeshatoa maelekezo, kwamba tutatuma wataalam kuja kuangalia upungufu uko wapi, halafu baada ya kuyajua huo upungufu, Serikali iko tayari kuanza kufanya marekebisho ya maeneo hayo. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sasa ni mwaka wa tano tangu 2018 maktaba ilipokamilika, thamani zake ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, maabara ilipanga kukamilika Oktoba, 2022 na kwa sasa imefikia asilimia 35, nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba Wizara ilikuwa inasubiri ukamilishaji wa maktaba na maabara na baada na ukamilishaji huo, Serikali inakwenda kuweka samani zote. Kwa kuwa tayari maktaba imeshakamilika, bado maabara, Wizara ilikuwa inasubiri vyote vikamilike kwa pamoja ili samani hizo zote ziende kwa pamoja. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute Subira, jambo hili tunalifuatilia. Leo jioni tukutane mimi na yeye twende pale Wizarani tufuatilie tuone jambo hili linafika mwisho kwa kiwango hiki, ahsante. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Shirika la CARMATEC limebobea katika kutengeneza mitambo ya biogas; je, Serikali inajishughulishaje na shirika hili karika mambo ya utengenezaji wa biogas?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa nchi ya China inaongoza kwa uzalishaji wa biogas kwa kiwango cha cubic meters 15,000,000 kwa mwaka; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wananchi wetu wakasome wapate ujuzi wa hali ya juu wa kutengeneza biogas; kwanza kwa sababu tunahitaji kufuga zaidi kisasa kuliko kuswaga ng’ombe; na pili itapuguza uharibifu wa mazingira kwa ajili ya mmomonyoko wa udongo unaoletwa na ng’ombe wengi ambao wanachungwa badala ya kufungwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua namna ambavyo Serikali na Wizara yetu inavyoshirikiana na mashirika haya ikiwa ni pamoja na wadau wetu wa China. Wizara imepokea ushauri huo wa Mheshimiwa Mbunge. Tutakwenda kulifanyia kazi jambo hili la mashirikiano yetu na kupeleka wanafunzi wetu kwenda kujufunza nchini China.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, jambo hili tumelichukua na ushauri huu tumeupokea na tutakwenda kulifanyia kazi.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana pia nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa sekta hii ya uvuvi kwenye Pato la Taifa kwa kiwango cha asilimia 1.8, tunakubaliana kwamba mchango huu bado ni mdogo sana, lakini nafahamu kwamba ipo mipango ya Serikali kununua meli kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu. Nataka kufahamu ni stage gani tumefikia kwenye uagizaji wa meli hizi kwenda kuvua kwenye Bahari Kuu?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kujua ni kwa namna gani mipango hii ya Serikali kwenye Wizara hii ya Uvuvi inaishirikisha Zanzibar katika kukuza Uchumi wa Bluu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar. Swali lake la kwanza anataka kujua kuhusu mchango.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mchango huu ni mdogo, mchango wa asilimia 1.9 ni mchango mdogo na ndiyo maana Serikali imekuja na mikakati mbalimbali ambayo itakuja kusaidia sana kuinua kipato hiki. Moja ya mikakati ambayo Serikali imekuja nayo ni pamoja na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. Tunakwenda kujenga Bandari ya Uvuvi pia kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya samaki, pia kufufua viwanda ambavyo tayari vimeshakufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba asilimia 1.9 ni asilimia ndogo na Serikali iko na mkakati wa kufanya kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kufufua Shirika la TAFICO ambalo tayari limeshakufa. Kwa hiyo, tunayo mikakati kama Serikali kwamba mikakati hiyo ambayo tumeiweka tukiitimiza vizuri tunaweza tukaongeza pato kutoka 1.9 kwenda juu zaidi. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira kwamba iko mikakati Serikali inajipanga kwa ajili ya kwenda kuimarisha jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ametaka kujua ni lini ununuzi wa meli hiyo utakamilika. Mchakato wa ununuzi wa meli upo unaendelea lakini umesimama kidogo kwa sababu za kibajeti. Kwa hiyo, mara Serikali itakapopata fedha ununuzi wa meli hiyo utaweza kufanyika mara moja. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya ucheleweshwaji wa mradi huu masika ikakuta mradi umecheleweshwa na mvua za masika, lakini Mkandarasi alichukua muda mrefu sana kuingia site katika kujenga mradi huu na mradi huu unajengwa na Wizara, haushirikishi Halmashauri ambayo wako katika eneo husika la mradi.

Je, Serikali ina mkakati gani kushirikisha kwa ukamilifu Halmashauri ya Nsimbo ili kuendelea kusimamia mradi huu?

Swali la pili, Serikali inachelewesha malipo ya Mkandarasi, Mkandarasi anashindwa kutekeleza mradi kutokana na kukosa kulipwa pesa. Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi pesa zake ili aweze kukamilisha mradi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza miradi hii ni miradi ya Serikali, haijalishi mradi unatekelezwa na Wizara ama unatekelezwa na Halmashauri, miradi hii yote ni ya Serikali. Miradi hii inapokuja huku kwenye Halmashauri maana yake mamlaka zote za Serikali zinapaswa kushiriki katika kutekeleza mradi huo, kwa sababu miradi hii haimaanishi kwamba inapojengwa na Wizara ni kwamba Serikali nyingine haihusiki, Hapana! Sasa hii ni dhana ya uelewa katika Halmashauri zetu kwamba miradi inapokuja kwa namna moja au nyingine ni lazima watumishi wa Halmashauri washiriki kwa namna moja ama nyingine katika kusimamia mradi huo ili kuleta tija na ubora wa miradi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua namna ya ucheleweshaji wa malipo. Malipo ya Serikali yoyote yanalipwa kulingana na certificate ya utekelezaji wa mradi alipofikia huyo Mkandarasi. Serikali inalipa fedha kutokana na certificate alizo-raise ambazo zinatokana na kazi aliyoifanya kwa kiwango hicho na huyu mkandarasi mpaka sasa ameshalipwa zaidi ya asilimia 70 ya malipo yake kwa sababu jumla ya shilingi milioni zaidi ya 270 amekwishalipwa kati ya milioni 510.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mkandarasi huyu anakwenda vizuri na ukiona mradi unachelewa ni kwa sababu ya upatikanaj wa fedha lakini ni pamoja na kwamba kazi anayoifanya ndiyo itakayo-determine analipwa fedha kiasi gani, kwa hiyo, huyu analipwa kulingana na kazi anayoifanya. Naomba kuwasilisha.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa. Ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo jitihada kubwa ambazo zilishafanywa huko nyuma na wananchi kupitia utaratibu wa Vijiji vya Ujamaa na nguvu za wananchi kuhakikisha kwamba wanachimba mabwawa katika kipindi cha nyuma. Hapa miaka ya 90 mpaka 2000, Serikali iliweza kuchiba baadhi ya mabwawa, lakini mabwawa yale ni kama yalitelekezwa na baadaye yakawa yameharibika. Kuna uhitaji ama umuhimu wa kuyafufua yale mabwawa ambayo yalichibwa nyakati hizo, kabla ya kuweka mkakati wa muda mrefu ule wa kujenga mabwawa haya.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mabwawa yaliyopo katika maeneo hayo yanafufuliwa kwanza?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natumia nafasi hii kumpongeza sana Mbunge wa Kishapu, Mheshimiwa Boniphace Nyangindu, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufatilia namna ambavyo wafugaji wake wanatakiwa wawe na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyouliza swali lake la msingi, ni kweli kwamba Serikali ipo na mipango mingi ya kufufua mabwawa yote yaliyokufa. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge hili tutatuma wataalam kuja kufanya tathmini katika jimbo lake. Tujue tathmini hiyo, mabwawa yako mangapi na yanahitaji nini ili Wizara kamaSerikali Wizara iweze kutuma namna ya kuyafufua haya mabwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua mabwawa ambayo yanahitaji kufufuliwa na Serikali yapo maeneo mengi. Serikali tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge Serikali imejipanga vizuri. Tukishapata kujua gharama za shilingi ngapi inatakiwa kwenda kuyafufua hayo mabwawa tupo tayari kwenda kuyafufua mabwawa hayo kwenye Jimbo la Kishapu. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro mikubwa kati ya wafugaji na wakulima. Ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu wakulima wa Kata ya Lumesule wana mgogoro mkubwa na wafugaji wa eneo hilo. Hii imepelekea kuhatarisha hata maisha yao. Hivi ninavyozungumza wakulima wako katika hali mbaya sana ya usalama kati yao na wafugaji.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri upo tayari mara baada ya kuahirishwa Bunge letu kesho kutwa, mimi na wewe tukafuatana tukaenda kwenye Kata husika kutatua mgogoro uliopo kati ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama Wizara iko tayari kuambatana naye baada ya Bunge hili. Wizara iko tayari kuandamana na Mheshimiwa Mbunge. Tuko tayari kwenda kuona mgogoro huu na kuutafutia ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla Wizara haijaenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu Serikali hii ni kubwa, wapo viongozi ambao wanapaswa kuanza kuhangaika na migogoro hii kabla Wizara haijafika huko. Yupo Mheshimiwa DC, nitoe wito sana, Mheshimiwa DC na wataalam wote waliopo huko wa Mifugo na Kilimo kwenda kutatua mgogoro huu kabla Wizara haijafika huko kutafuta ufumbuzi wa kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ina Wataalam wa Kilimo na Mifugo, ina Mheshimiwa DC ambaye ni Kamisaa wao. Tunaomba kabla Wizara haijafika huko nitoe wito kwa wakuu wote waende kutatua mgogoro huu kabla hatujafika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni lini tathmini hiyo itakamilika ili Watanzania wafanye kazi zao kwa ufasaha ili kuleta tija? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, kwa kuchelewesha kukamilisha taratibu hizo hatuoni kwamba tunawanyima Watanzania fursa katika kumiliki rasilimali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba mchakato wa kubadilisha sheria ama kanuni ni mchakato unaofanyika mara kwa mara. Kama nilivyosema mwaka 2019 mchakato huo ulifanyika tukabadilisha sheria mbalimbali, mwaka 2020 tukabadilisha. Kwa hiyo, sheria ambazo zinaonekana pengine ni kandamizi kwa wadau wa uvuvi, Serikali iko tayari kuendelea kuzibadilisha mara kwa mara kadri ya mahitaji.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini zinaendelea kulingana na sheria, jiografia na uhitaji wa maeneo husika. Lengo la Serikali hasa ni kuhakikisha kwamba sheria zinazotumika kumsaidia huyu mvuvi ama mtumizi wa sekta hiyo kurahisisha shughuli zake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tathmini zinaendelea. Sheria ambazo ni kinzani na mahitaji ya watumiaji wetu, zinaendelea kubadilishwa siku hadi siku kama ambavyo zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara. Kwa hiyo, wataalamu wanaendele kufanya tathmini, lakini sio tu wataalam wa Wizara, ni pamoja na watumiaji wa sheria hizi wanaendelea kufanya tathmini siku hadi siku kama ambavyo sheria na kanuni zimekuwa zikibadilika, naomba kuwasilisha. (Mkofi)
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ni kweli Serikali ilisitisha zoezi hili la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kieletroniki mwaka jana 2022, Novemba tarehe kama hii, ili kuipa Wizara kufanya tathmini ya upungufu. Kutokana na umuhimu wa zoezi la utambuzi wa mifugo ambacho ndicho kinachoweza kuondoa migogoro kati ya wafugaji, na kusababisha mifugo kuhamahama na kuingiliana pamoja na wizi wa mifugo; changamoto ambayo iko kwa wafugaji wadogo zaidi kuliko wa mashamba makubwa, ambapo ufugaji kule uko salama na idadi yake inafahamika: Ni lini sasa Serikali itafanya zoezi hili kwa wafugaji wa kawaida na wadogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kuna changamoto ya takwimu ya uhakika ya mifugo. Ni lini Serikali itafanya sensa ya mifugo ili tuwe na takwimu halisi ya mifugo katika nchi yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nianze na hili la hereni kwamba ni kweli Serikali ilisitisha na sasa mwaka mmoja umepita. Serikali imesitisha baada ya zoezi hili kulalamikiwa sana na wadau, hasa wafugaji wadogo wadogo. Sasa Serikali ilichokifanya ni kuainisha changamoto zile ambazo wafugaji wanazilalamikia na kutafuta majawabu sahihi. Baada ya kupata hayo majawabu sahihi, na kwa kuwa zoezi hili lilizuiliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulichokifanya Wizara ni kumwandikia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba sasa tunashughulikia changamoto zote ambazo wafugaji wameziainisha, kwamba majibu yake sasa tayari tunayo na Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari amesharuhusu tuendelee na zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba zoezi hili litaanza mara moja, hivi punde kadiri ambavyo maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yalivyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili amelisema hapa kuhusu sensa. Ni kweli kwamba sensa hii huwa inafanyika kila baada ya miaka mwili. Sensa ya mwisho ilifanyika mwaka wa fedha 1920 na mwaka huu sasa tutafanya sensa 2023 kwa ajili ya kubaini idadi halisi ya mifugo tuliyonayo katika Taifa letu. Sensa hii tunashirikiana na watu wa NBS, wanaoshughulika na masuala ya takwimu kuhakikisha kwamba takwimu tunazozipata zinalenga kwenye kuleta tija katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ziwa Tanganyika, Wilaya Nkasi hakuna vizimba hata kimoja . Ni lini Serikali mtapeleka vizimba Wilaya ya Nkasi hasa Jimbo la Nkasi Kusini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la namba mbili, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Bwawa la Kacheche la kunyweshea mifugo pamoja na ujenzi wa majosho mawili Chala B, Kata ya Chala pamoja na Kijiji cha Kitosi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na hili la vizimba, tumeshatoa maelekeza kwamba mvuvi yeyote ama mwananchi yeyote ambaye ana shida na vizimba ama boti au nyenzo zozote zinazohusiana na uvuvi, aombe haraka iwezekanavyo milango ipo wazi kwa Watanzania wote. Kwa kweli Mheshimiwa Rais, ametufungulia njia kama mnavyokumbuka Tarehe 30, aligawa kule Mwanza vizimba na boti za kutosha na Wizara ipo katika mchakato wakutafuta vizimba vingine ili kuwagawia wananchi watakaohitaji kwa awamu ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuhamasisha Wananchi wake wenye uhitaji. Tupo tayari kupeleka Ziwa Tanganyika na tayari tumeshaanza Ziwa Victoria na kwa kweli vijana wote na wavuvi wote wenye shida na wenye uhitaji wa nyenzo za uvuvi Serikali ipo tayari kuwagawia. Ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili, kuhusiana na lini bwawa litakamilika na majosho. Hapa katikati tulisimama kidogo kwa sababu ya upatikanaji wa fedha. Mara tu Serikali itakapopata fedha tutakwenda kukamilisha ujenzi wa majosho hayo. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka katika Wilaya yake tumemtengea jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki katika eneo hilo. Tukapopata fedha nyingine tutakwenda kukamilisha ujenzi wa majosho hayo na mabwawa ambayo yapo katika Wilaya yake, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninashukuru kwa kunipa fursa na mimi niulize swali la nyongeza. Kwanza, ninashukuru kwa huduma tuliyoipata miundombinu katika Ziwa Victoria. Wilaya ya Ilemela asilimia 87 ni eneo la maji, na wanawake na vijana wengi wanashughulika na mazao ya samaki hususani dagaa lakini miundombinu yao ya kukausha samaki si mizuri hasa kwa afya ya binadamu. Ni lini Wizara itasaidia kuweka miundombinu kwa ajili ya kukausha samaki kwa wafanyabiashara hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema kwamba Serikali imeshaanza na katika Ziwa Victoria tumeshaanza kuwasaidia Wavuvi namna ya kuvua zile samaki lakini pia kuhifadhi samaki. Hili wazo la Mheshimiwa Mbunge tumelichukua tutakwenda kulifanyia kazi kuwasidia Wavuvi wakanda ya ziwa. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye orodha ya masoko ya Samaki yatakayojengwa katika mpango ambao ameusema Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni pamoja na Nyamikoma, Jimbo la Busega. Mpaka sasa soko hili halijaanza kujengwa na imebaki miezi minne kukamilika kwa mwaka wa fedha. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa soko hili la Nyamikoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza ujenzi wa Soko Nyamikoma mara tu fedha zitakapokuwa zimepatikana. Tayari Serikali imeshaanza ujenzi wa masoko katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tunduma, Muleba, Momba, Ludewa, Busega, Nkinga na Kalambo. Kwa hiyo, mara tu tutakapopata fedha Serikali itaanza ujenzi haraka sana iwezekenavyo katika Kijiji cha Nyamikoma. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na naishukuru Serikali kwa kuchimba Bwawa la Kihumbu. Sasa nataka kuuliza, kwa sababu bwawa limechukua muda mrefu kidogo pamoja na kwamba jitihada zipo.

Je, ni lini sasa hilo bwawa litakamilika ili wananchi watumie maji ya bwawa hilo na mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli bwawa halijakamilika; Serikali tayari imeshakutana na mkandarasi na imeshampa deadline juu ya lini bwawa linatakiwa kukamilika na tayari tumeshakubaliana. Mara tu mkataba utakapokuwa umekamilika bwawa hilo litakuwa limekamilika na atatukabidhi Serikallini kwa ajili ya kuendelea kulitumia.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Manyoni Magharibi ni mbaya, eneo lile ni kame. Pamoja na juhudi hizi za Serikali, sasa Naibu Waziri haoni umuhimu wa kuongeza kasi ya kupeleka mabwawa zaidi pamoja na majosho katika Jimbo la Manyoni Magharibi ili kuwasidia wakulima wetu pamoja na wafugaji ambao mifugo yao inapata tabu kwa kipindi cha kiangazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Singida Kaskazini katika bajeti ya mwaka 2023/2024, Serikali ilitupatia miradi ya majosho manne katika Kijiji cha Minyenye, Ghalunyangu, Muhamo na Mangida. Kwa bahati mbaya fedha hazikuja kwa ajili ya kutekeleza miradi hii pamoja na kuwa wananchi tayari walishaanda upande wa nguvu kazi.

Je, sasa ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge kwamba, mabwawa ambayo yaliahidiwa kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka wa fedha wa bajeti bado haujaisha. Namhakikishia kwamba, jinsi ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unapatikana, tutakwenda kuyajenga hayo mabwaka kama ambavyo bwawa tulilokwishalikabidhi tayari limekwishajengwa katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kuongeza kasi ya ujenzi wa haya mabwawa, ni kweli kama nilivyokwisha jibu kwamba, tumeshakabidhi bwawa la kwanza na Serikali sasa inaendelea kutafuta fedha zingine kwa ajili ujenzi wa mabwawa mengine. Tunakiri kwamba, Wilaya ya Itigi ni miongoni wa wilaya kame ambazo zinahitaji kuongezewa mabwawa na majosho kwa ajili ya kuisaidia mifugo yetu iliyoko katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea kufuatilia na inaendelea kutafuta namna ambavyo inaweza kusaidia ujenzi wa mabwawa katika Wilaya hii ya Itigi, ahsante. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kuuliza ni lini sasa Serikali ina mpango wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mashimba Ndaki, alipokuja kwenye Jimbo la Msalala na kuahidi bwawa la kunyweshea mifugo.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Mashimba Ndaki, Mheshimiwa Waziri wa Mifugo Mstaafu ambayo aliitoa katika Jimbo la Msalala, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ahadi za viongozi wote walizokwishazitoa tunazo kama Wizara. Tuna database muhimu ya ahadi hizo. Nimhakikishie, mara ambapo tutapata fedha kwa ajili ya utengenezaji wa mabwawa hayo tutakuja kujenga katika Jimbo lake la Msalala. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Wilaya ya Liwale tulipata shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga bwawa pale Kijiji cha Kimambi lakini wale wataalamu badala ya kujenga bwawa walijenga Karo. Ni nini kauli ya Serikali juu ya ufisadi ule?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, concern ya Mbunge tumeshaipokea na tayari Wizara inajipanga kupeleka wataalam kwa ajili ya uchunguzi wa jambo hili. Mara tutakapojiridhisha kwamba kuna tatizo katika mradi huo tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za utumishi. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nimshukuru Mheshimiwa kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Kata hizo Nane zina jumla ya wananchi 26,582. Je, kwa idadi hiyo ya boti mbili Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Serikali inatakiwa iongeze boti?

Swali la pili, wavuvi wa Jimbo lile wana changamoto nyingi na wana maoni mengi ambayo wangetamani wakae na Mheshimiwa Waziri. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kutangulizana na mimi baada ya Bunge hili kwenda kukaa na wavuvi wa Jimbo la Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la ugawaji wa boti lilianza kwa zoezi la awali Mheshimiwa Rais amekwishatoa maelekezo kwamba tuangalie maeneo yote yenye uhitaji wa kuongeza boti hizo na tayari tumeshaainisha maeneo ambayo yana umuhimu wa kuongeza boti na sasa Wizara iko tayari kuongeza boti kulingana na mahitaji ya maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kuwatembelea, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kamonga kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana shida za wananchi wake na kuwatatulia, kwa kadri hiyo na sisi Wizara tuko tayari kufika katika eneo lake kwenda kuzungumza na wavuvi hao kuona namna sahihi ya kutatua changamoto wanazopitia wavuvi hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya vyuo katika taasisi hizo kama vile Mtwara–Mikindani, Kibirizi–Kigoma, Gabimori–Rorya mameneja wake wamekaimu kwa kipindi kirefu sana kuanzia miaka saba mpaka kumi na moja;

i. Je, Serikali haioni inafifisha malengo ama maelekezo ya Chama cha Mapinduzi katika vyuo hivyo kutoa mafunzo kwa sababu havina mameneja wa kudumu?

ii. Je, Serikali itakapokamilisha mchakato huo wa kujaza hizo nafasi kwa muundo uliokamilika tangu Novemba 2022, iko tayari kuwalipa mameneja hao wanaokaimu akiwemo meneja wa Mtwara-Mikindani aliyokaimu kwa miaka 11 kwa nafasi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza sana dada yangu Agnes kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana chuo hiki na kwa kweli kama Wizara tunatumia nafasi hii kumpongeza sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia habari hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kweli kwamba kuna makaimu katika vyuo vingi vinavyohusiana na masuala ya uvuvi. Napenda kutumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba makaimu hao sasa watakwenda kuthibitishwa, wale wenye vigezo. Jambo hili liko kwenye upekuzi na upekuzi upo katika hatua za mwisho namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba linakwenda kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili alilosema kuhusu mameneja waliokaimu kwa muda mrefu taratibu za kiutumishi zinafahamika. Kama watakuwa na sifa za kulipwa basi watalipwa, Serikali iko tayari kuwalipa na kama watakuwa hawana sifa za kulipwa basi hawatalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa majosho matano. Nina swali moja tu la nyongeza. Nataka kujua kama Wizara inajua kwa uhakika katika vijiji vyetu vyote 114, mahitaji ya majosho ni kwa kiwango gani, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli kwamba Wizara ina Database ya kujua wapi panahitajika josho lipi, kwa size gani na kwa umuhimu gani? Pia, Mheshimiwa Mbunge kama anaona kuna sehemu ambapo sisi kama Serikali tunapaswa kwenda kujenga josho, alete taarifa zake tuweze kufanyia kazi kwenye maeneo hayo. Hata hivyo, mpaka sasa database ya vijiji ambavyo majosho yanatakiwa kujengwa, Serikali ina hiyo database, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na nina maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia Wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu zana na nyenzo za uvuvi kama vile nyavu, boti na vizimba, kama ilivyofanya hivi karibuni kwa wenzao wa Lake Victoria?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uvuvi haramu ni chanzo kikubwa cha kuzorotesha uchumi wa Samaki; na Maafisa Uvuvi wa hapa nchini na hata kule Nyumba ya Mungu, wameweka mkazo kwenye kuwakamata wavuvi na kuwapiga faini badala ya kutoa elimu endelevu ya namna bora ya kufanya uvuvi: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchukua hatua kupambana na hali hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili la kwanza. Kwanza ugawaji wa nyenzo za uvuvi kama boti, nyavu na kadhalika, kama ambavyo Mheshimiwa Rais alifanya juzi kule Mwanza, Ziwa Victoria, hii ni fursa kwa Watanzania wote kwenye maziwa na mabwawa mbalimbali, wanaruhusiwa kuchukua nyenzo hizi kwa njia ya kukopa kupitia TADB, benki yetu ya kilimo ambapo ukiwasilisha andiko lako vizuri kwa kupitia wataalamu wetu, unaweza kupata ushauri na baadaye ukakopeshwa nyenzo hizo ukafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ni fursa kwa Watanzania wote ikiwemo wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, kwanza nikupongeze sana kwa ufuatiliaji na namna ambavyo unaendelea kufuatilia. Umekuwa msumbufu sana kwenye hili. Tunakupongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kweli tupo tayari kukupa ushirikiano ili wavuvi wako waweze kupata nyenzo hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba Maafisa Uvuvi kazi yao ni kuhakikisha wanasimamia shughuli za uvuvi kwenye maeneo yao pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi wetu. Natoa wito na rai kwa Maafisa Uvuvi wote nchini kuhakikisha kwamba wanajikiza zaidi kwenye kutoa elimu na kusimamia shughuli za uvuvi na siyo kujigeuza kuwa Maafisa Masuuli na Maafisa wa Mapato, kukatisha ushuru na mambo mengine ambayo hayawahusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatoa wito kwa Maafisa wote kwamba sasa wajielekeze kwenye kazi yao ya msingi ambayo wanatakiwa kufanya kwenye maeneo yao huko wanakofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)