Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zuena Athumani Bushiri (38 total)

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya miradi kutokukamilika kwa wakati. Nini kauli ya Serikali kwa wakandarasi ambao hawamalizi miradi yao kwa wakati na kuchelewesha huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kumekuwa na wimbi kubwa sana la wizi wa miundombinu ya umeme, mfano kule Moshi Manispaa, katika Kata za Soweto, Boma Ng’ombe, Barabara ya Bonite pamekuwa na wimbi la vijana ambao wanaiba miundombinu hii. Je, Serikali hii inachukua hatua gani kudhibiti uharibifu huu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kuhusiana na miradi ambayo haijakamilika ni kwamba, kwanza ifikapo Disemba mwaka huu 2021 miradi yote ambayo siyo ya REA III round II itakuwa imekamilika kwa maana ya REA II na REA III round I itakuwa imekamilika.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa na changamoto kidogo zilizopelekea miradi hii kuchelewa, sababu mojawapo ikiwa ni kwamba ni vile vifaa ambavyo vilikuwa vinaagizwa nje ya nchi vilichelewa kufika kwa sababu ya lockdown za wenzetu kule kushindwa kuleta vile vifaa kwa wakati. Shida nyingine ilikuwa ni maeneo mengine miundombinu kuharibiwa na mvua kali na hivyo watu wakashindwa kukamilisha kazi zao kwa wakati. Hata hivyo, tumejiwekea utaratibu na tunawaahidi Watanzania kwamba ifikapo Disemba mwaka huu hakutakuwa kuna mradi wowote wa REA III round I au REA II ambayo inaendelea, itakuwa yote imekwisha. Miradi ambayo itakayokuwa inaendelea ni ya REA III round II ambayo nayo Disemba mwakani itakamilika.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mambo haya hayajitokezi tena, Serikali ilielekeza kwamba vifaa vyote vipatikane hapa nchini na kweli vinapatikana. Hiyo inatuongezea speed ya kufanya kazi hizi na kuzimaliza mapema.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo Serikali imelifanya ni kuhakikisha sasa inatoka kwenye kufanya kazi hizi kwa mtindo wa goods na kuziweka kwenye works, kwamba mtu atalipwa baada kukamilisha kipande fulani cha kazi ambacho anatakiwa kukifanya na hiyo inatusaidia kusimamia vizuri maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo Serikali imelifanya, tumehakikisha sasa tunakwenda kila kanda na kila mkoa kuweka msimamizi wa miradi yetu ya REA, akae kule masaa 24 akimsimamia mkandarasi anayefanya kazi kuhakikisha kwamba kazi inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, tumehakikisha kwamba, wale wakandarasi wanaokwenda kwenye maeneo yetu tumewakabidhi kwa Waheshimiwa Wabunge ili na wenyewe wawe wasimamizi namba moja wa kuhakikisha kila siku wanawaona site na pale ambapo panatokea hitilafu ya kuwa mzembe mzembe, basi taarifa hizo zinatufikia mara moja. Tunaamini njia hizo zitatusaidia.

Mheshimiwa Spika kwenye jambo la pili; jambo la wizi siyo la mtu mmoja kulikemea, tunawaomba wenzetu tuendelee kushirikiana, sisi kama Wizara tunawapa support kubwa sana wakandarasi wanapotoa taarifa za kuibiwa, tunasaidiana nao moja kwa moja kuhakikisha kwamba tunafuatilia, kuhakikisha tunawachukulia hatua wale walioiba miundombinu. Pia tunaweka mikakati mingine ya ziada ya kuwasaidia wale wakandarasi kuweka vifaa vyao katika godown za TANESCO ili angalau viwe katika usalama zaidi.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumewaelekeza, wao ndiyo wenye wajibu wa kuhakikisha mali hizo haziibiwi ili wafikishe mizigo ile na kazi ifanyike kwa wakati. Tunaamini kufikia Disemba mwakani, jambo la kupeleka umeme REA III round II litakamilika kwa muda uliopangwa kwa mujibu maelekezo ya Serikali. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia swali la nyongeza. Changamoto iliyoko Jimbo la Kilolo ni sawa na changamoto iliyoko katika Hifadhi ya Same ambayo katika hifadhi hiyo barabara kuu inapita kuelekea katika Jimbo la Same Mashariki. Katikati ya Hifadhi hiyo, hakuna mawasiliano ya simu, jambo ambalo linapelekea vijana wengi kwenda kufanya mambo ya kiukorofi, kuteka baadhi ya magari na kuwapora wananchi mali zao. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba inajenga minara ya simu maeneo hayo ili endapo ukorofi kama huo vijana wataufanya, waweze kutoa mawasiliano kwa ajili ya kutetea haki yao? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina mpango wa kuhakikisha kwamba tunapeleka mawasiliano katika maeneo ya mbuga na hifadhi ili kuhakikisha kwamba maeneo haya yasiwe na changamoto tena kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ilianza kama zahanati mnamo mwaka 1920 ikapandishwa daraja ikawa Kituo cha Afya mwaka 1922, ikapandishwa daraja ikawa Hospitali ya Mkoa mwaka 1956, mwaka 2011 ikapanda daraja kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hii inahudumia Wilaya zote saba za Mkoa wa Kilimanjaro, lakini ina upungufu wa Madaktari Bingwa hususani upande wa wanawake.

Je, Serikali inasema nini kuhusu kuongeza madaktari bingwa wa Hospitali hii kwa sababu huduma stahiki wananchi wa Kilimanjaro hawazipati kutokana na ukosefu wa madaktari na madaktari bingwa?

Kutokana na miundombinu hii iliyoanza tangu mwaka 1920 ni kweli kabisa hospitali ile imechoka, mazingira…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kujenga majengo ambayo yana hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mzuri sana hasa kwenye eneo la hospitali hiyo, lakini kwa ufuatiliaji wake mzuri hasa kwenye huduma ya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kuhusu Madaktari Bingwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mawenzi hospitali hiyo mpaka sasa ina ma-specialist, tisa lakini specifically idara anayoisema Mheshimiwa Mbunge ambayo inahitajika kuwa na Madaktari Bingwa wanne ina Daktari Bingwa mmoja. Kwa hiyo, ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge wakati tunajipanga kwa mwaka huu kwa maana ya ajira za mwaka huu Hospitali ya Mawenzi itakuwa mojawapo ya hospitali za kipumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sivyo tu kwamba kuna ma-specialist tisa, lakini kuna baadhi ya Idara kama Idara ya Mifupa ambayo haifanyi vizuri sana, tutaenda kufanya kazi kubwa kwenye kuboresha hasa kuweka kwenye vifaa, lakini kuelekeza utawala wa hospitali ili usimamie vizuri eneo hili liwe kufanya kupunguza rufaa kwenda KCMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pilli ni kuhusu miundombinu kwamba hospitali ni ya muda mrefu na kuna majengo ambayo yamechakaa na mengine kabisa hayafai kutumika. Ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema na baada yeye kuja Wizarani, Mheshimiwa Waziri wa Afya alituma timu wiki mbili zilizopita, wameshakwenda Mawenzi na sasa wako kwenye hali ya kuangalia yale majengo ambayo hayafai kabisa na michoro imeanza kuchorwa ili kuja na mawazo ya namna gani tunaweza kuboresha hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini kuna suala la ardhi pembeni ya Hospitali ya Mawenzi kuna ardhi ya Manispaa ambayo tunaweza tukafikiria namna ya kushirikiana na Manispaa kama inawezekana, lakini ukiangalia ramani yamwaka 1959 Hospitali ya Mawenzi na ukiangalia mabadiliko ya 2009 utaona kuna maeneo fulani ya hospitali hiyo ambayo vilevile hayaonekani kwenye ramani nayo yatashughulikiwa kuhakikisha sasa tunaenda kuja na mkakati ambao hospitali hiyo itaboreshwa vizuri sana, ahsante sana.
(Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ukweli usiopingika kwamba ni barabara ambayo haipitiki kipindi chote cha mvua. Ni barabara ambayo inaleta manufaa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa madini ya jasi ya Makanya yanalisha viwanda vya Tanga Cement, Twiga Cement, Moshi Cement, Doria Arusha na nchi za Rwanda na Burundi na kuiingizia Serikali mapato. Serikali haioni haja ya kuiboresha barabara kwa kuitengea fedha ili iweze kufanya kazi muda wote na kuongeza mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika machimbo haya wako wanawake ambao wamewekeza kule ambao wamepata fursa ya kuendesha biashara ya mama lishe na biashara ndogondogo. Je, Serikali haioni kwamba kwa kusimama kwa machimbo haya kutokana na barabara korofi wanawake hawa wanadhoofika kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza maswali mawili ya msingi kabisa ambayo yana nia njema ya kuwasaidia wanawake wote wa Same mpaka Mkoa mzima wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza la msingi ambalo ameuliza hapa, amesema barabara hii haipitiki na ameomba Serikali tutenge fedha. Kwa kuwa maombi haya yametoka kwa mtu ambaye ameshakuwa kiongozi ndani ya chama na ni maombi muhimu sana,
nimwambie tu kwamba tutatuma wataalam wetu wa Ofisi ya Rais, TARURA, waende katika eneo hilo wakafanye tathmini ya kina na kuileta ofisini ili tuone namna ambavyo tunaweza tukasaidia barabara hii iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amesema kwamba kusimama kwa machimbo ya jasi kunasababisha uchumi kwa akina mama kuyumba na kuomba watu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusaidia ili barabara hiyo iweze kujengwa. Kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba tutahakikisha barabara hiyo inatengenezwa na inapitika kwa wakati wote kuhakikisha tunasaidia akina mama hao wanaoendesha biashara zao maeneo yale lakini vilevile tunawasaidia wananchi wa Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo Unguja na Pemba yanafanana sawa na matatizo yaliyopo katika Kituo cha Polisi cha Gonja Maore. Kituo hiki kilijengwa tangu mwaka 1958, kilijengwa kipindi cha Mkoloni. Nyumba zake zote zimechakaa sana, Kituo cha Polisi kimechakaa sana, miundombinu yake hasa maeneo ya toilets hayafai. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kufanya ukarabati katika nyumba hizo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kweli naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba Wizara inatambua uchakavu wa vituo na makazi ya askari katika maeneo mbalimbali nchini. Ndiyo maana tumesema tunafanya tathmini ili kuona kiwango cha uchakavu, tuandae mpango kabambe wa kukarabati vituo hivi. Kwa hiyo, Kituo cha Mheshimiwa Mbunge cha Gonja Maore tutakifuatilia ili kuona katika mwaka ujao nini tunaweza kufanya kukirekebisha kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa Gonja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mwembe – Mbaga – Mamba ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Hayati Rais Dkt. Magufuli?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwembe – Mbaga ambayo iko Same ni barabara ambayo iko kwenye miinuko. Tulichokifanya kwa sasa, kabla ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami ni kuainisha maeneo yote korofi na yenye miinuko ili tuweze kuyadhibiti na yaweze kupitika kwa mwaka wote, na baada ya hapo Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kufanya feasibility study na usanifu wa kina ili kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, tafiti zimefanyika Kitaifa, Je, ni maeneo gani ambayo yanaonyesha baada ya kufanya tafiti kwamba zoezi hili liko kwa wingi nchini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tunachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba katika kila watoto 20 mmoja anakutwa na tatizo hilo, maeneo yote ya nchi wamekuwa wapatikana watoto kama hao kwa sababu matatizo mengine yanatokana na maambukizi au wakati mwingine inaweza kuwa mama ana damu aina fulani na mtoto ana damu aina fulani ambayo wakati mwingine ikichanganyikana inasababisha tatizo hilo. Wakati mwingine inatokana kwamba wakati mtoto yuko tumboni kwa mama anakuwa na damu nyingi, chembechembe nyekundu nyingi za damu, kwa sababu tumboni kwa mama anatumia hewa oxygen ambayo ni ile ya mama, kwa hiyo ni lazima awe na chembe chembe nyingi za damu.

Kwa hiyo, akitoka nje akizaliwa baada ya saa 24 zile chembechembe nyekundu zinaanza kuondoka kwa maana ya kupasuka zinapoanza kuondoka sasa inasababisha hilo tatizo lakini ni la kawaida kwa sababu anapofika sehemu yenye oxygen nyingi basi chembe chembe zile nyekundu hazihitajiki inabidi ziondoke. Hivyo ni kwamba, kila mahali hilo tatizo linaonekana, jambo la msingi ni kujua katika kila watoto 20 mmoja anaonekana ana hilo tatizo.(Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Mwanga haina mapato ya kutosha, je, Serikali haioni umuhimu wa kuisaidia halmashauri hii ili kujenga uzio katika shule hii muhimu ya wasichana ambayo inapata adha kubwa sana kutokana kutokuwa na uzio, usumbufu, changamoto ya wanyama pamoja na miti kuharibika wakati ambapo ndiyo inaoteshwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Athuman Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeielekeza Halmashauri ya Mwanga na natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge anajua, sawa kiwango chao bado sio kizuri sana. Sasa hivi sisi kama Serikali tumekuwa na mipango mingi ikiwemo kumalizia miundombinu ili wanafunzi wetu waweze kukaa katika maeneo salama ambayo yatawasaidia wao waweze kuwa na ufaulu mzuri katika masomo yao. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tulipokee kwa mipango ya baadaye ili tuweze kuja kulifanyia kazi baada ya kumaliza hili jukumu la kwanza ambalo tumejipangia kama Serikali.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa, nina swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kilimanjaro ni mojawapo ya Mikoa ambayo ina uhitaji wa magari ya polisi hasa magari ya doria; je, Serikali ina mpango gani Mkoa wa Kilimanjaro kupata magari katika awamu hii ya kwanza ya magari 78 ambayo yanaingia nchini mwezi Aprili? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutokana na jitihada zake anazochukua za kuhangaikia Mkoa wake wa Kilimanjaro basi tumepokea mapendekezo yake na tutahakikisha kwamba magari haya yakija tutaangalia uwezekano vilevile tuweze kupeleka Mkoa wa Kilimanjaro. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Januari, 2008 Serikali ilituma wataalam kwenda kupima udongo katika vijiji hivyo vinne vya Mheza, Mpirani, Kadando na Maore; wananchi wanalipata matumaini makubwa sana, lakini mpaka sasa hivi hakuna kitu chochote kinachoendelea; nini kauli ya Serikali kwa wananchi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; zao la mpunga ni zao la biashara ambalo wananchi wengi wanategemea katika maeneo hayo kwa ajili ya chakula pamoja na biashara ili kujikwamua kiuchumi.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wakufanya uharaka wa wa kuwajengea skimu hizo ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza; kazi kubwa ambayo tuliifanya kama Serikali ni kuhakikisha tunaipitia miradi yote ya umwagiliaji na kujua changamoto zake.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili ilikuwa ni kwenda katika utengaji wa fedha ili kuweza kutatua changamoto hizo. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba pamoja na huo mwaka alioutaja, lakini tumeielekeza Tume ya Taifa ya Umwagaliaji kwa ajili ya kwenda kufanya upembuzi yakinifu ili miradi hii ijengwe katika kiwango ambacho kitakuwa kinakidhi mahitaji na mwisho wa siku tusirudie kulekule tulipotoka kurekebisha skimu hizi mara kwa mara.

Kwa hiyo, nimuondoe hofu yakwamba kazi inaendelea kufanyika hivi sasa ni kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu ili tujenge mradi huu kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uharakishaji wa jambo hili; na sisi tunafahamu ya kwamba moja kati ya mazao makubwa ambayo tunayategemea sana ni mazao ya mpunga kwa ajili ya chakula na hivyo tutahakikisha kwamba tunaharakisha zoezi hili ili wakulima wa maeneo hayo waweze kulima kwa wakati na mwisho wa siku tuisaidie nchi yetu ya Tanzania kupata chakula cha uhakika.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Manispaa ya Moshi kumekuwa na matukio mengi sana ya kuungua masoko, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba manispaa haina ya magari ya kutosha ya kuzimia moto tunategemea magari kutoka TPC. Hivyo basi husababisha mali za wananchi kupotea. Je, ni lini Serikali itanunua magari ya kuzimia moto katika Manispaa ya Moshi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Bushiri amekuwa akifuatilia kwa karibu masuala ya Kilimanjaro kuhusiana na Zimamoto, Polisi na mambo yote yaliyo chini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mhehimiwa Spika, tunafahamu kama tulivyosema katika hotuba yetu iliyosomwa na Waziri wiki iliyopita maeneo mengi yana changamoto ya magari, lakini katika bajeti ijayo tumetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari, tutayapeleka kwenye maeneo strategic maeneo ya kimkakati ambayo yamekuwa yanakumbwa na tatizo la namna hii. Hata hivyo, uwepo wa magari tu si suluhisho la kudumu, bali utayari wa wananchi kukabiliana na mambo haya, lakini vile vile kinga dhidi ya majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya KIA - Sanya Juu ambayo ilikuwa ni ahadi ya Hayati Mheshimiwa Rais Magufuli?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tuweze kusoma bajeti yetu. Naamini tutakuwa tumefanya mapendekezo ya nini kifanyike kwenye hii barabara ya KIA - Sanya Juu, ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Njoro II, Rombo, ili kuwatua akinamama wa Rombo ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu tunaendelea na utekelezaji wake; na kadiri tunavyopata fedha, Mheshimiwa Mbunge wewe ni shahidi, tunaendelea kupeleka fedha ili mradi huu ukamilike, kwa sababu lengo la Serikali ni kuona akina mama tunawatua ndoo kichwani.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafsi ya kuuliza swali la nyongeza.

Manispaa ya Moshi tunazo Kata ambazo ziko katika maeneo ya Majengo Kiusa na kota hizo zimechoka sana na ni za miaka mingi sana. Wako wapangaji ambao wameishi pale mpaka sasa hivi wana wajukuu na vitukuu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha kota hizo au hata kama kuna uwezekano wa kuweza kuwauzia? Aahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu ssali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la pili kwenye majibu yangu ya nyongeza kwa Mheshimiwa Kapinga, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, awamu hii ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan; moja, ameshatoa maelekezo kwamba, pale ambapo mnaweza mkafanya na sekta binafsi, basi kuna haja ya kufanya hivyo. TBA kwa jinsi muundo wake ulivyokuwa, sasa hivi iko kwenye kubadilishwa ili iweze kufanya na private sector ili maeneo yote yale ambayo yalikuwa na quarters zilizochoka tuangalie uwezekano wa kuongea na wenzetu wa sekta binafsi ili kuharakisha kujenga majengo kwa ajili ya kutoa huduma kwa watumishi na viongozi wa Tanzania hii, ahsante. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro kuna kata ambazo hazina mawasiliano mpaka wananchi wapande juu ya miti ndio wapate mawasiliano ; na kata hizo zina changamoto ya kuvamiwa na Tembo mara kwa mara.

a) Je, nini kauli ya Serikali ya kuwasaidia wananchi hao kupata mawasiliano ili wanapopata matatizo waweze kutoa taarifa?

b) Je,ni lini Serikali itadhibiti Wizi wa fedha za wananchi kwa kupitia simu kwa kuwa tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa sana katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuwena Athuman Bushiri, Mbunge Viti Maalumu Kilimanjaro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zuwena kwa kazi kubwa ya kuwatetea wana Kilimanjaro katika masuala ya mawasiliano. Mheshimiwa Zuwena alifanya Ziara katika Tarafa ya Jipendae, na akatujulisha Serikali na tukapokea malalamiko hayo ambayo ni changamoto, na Serikali tukayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kata ambazo Mheshimiwa Zuwena amezitaja, Kata ya Kwakoa, Kilya, Tohora pamoja na kata ya Kibisini tayari zimeingizwa kwenye utaratibu wa kupatiwa huduma za mawasiliano. Lakini katika eneo ambalo linaenda katika lango la Hifadhi ya Mkomazi pia nalo Serikali inatarajia kuingia mkataba na TTCL ili iweze kufikisha huduma ya mawasiliano katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwas wali la pili, Serikali haiwezi kupuuza malalamiko ya wananchi. Suala la wizi kwenye masuala ya simu na fedha za wananchi katika mitandao ya simu, nipende kusema jambo moja. Huduma ya mawasiliano ina wadau watatu, kuna watoa huduma, kuna watumiaji wa huduma na kuna Serikali. Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba watoa huduma wanatoa huduma katika mazingira rafiki, lakini na watumiaji wa huduma wanapata huduma ambayo inaendana na haki ambazo wanazitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa maelekezo kwa TCRA kufanyia kazi malalamiko ya wananchi ili kujiridhisha na changamoto jinsi ambavyo ilivyo na kuhakikisha kwamba tunatoa majibu kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Daraja la Makulu Villa ni daraja linalounganisha Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Same, lakini daraja hili limekuwa na changamoto kubwa kwa kuwa wakulima na wafugaji wanashindwa kufanya biashara zao. Je, Serikali imejipanga vipi katika kujenga daraja hili ili kuwasaidia wananchi hawa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kuhusu Daraja la Makulu Villa ambalo linaunganisha Halmashauri ya Simanjiro na Same kwamba ni changamoto na linakwamisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi, wakulima na wafugaji, naomba Serikali tulichukue hili na tutafanya tathmini kuona uwezekano wa kuweka mpango kwa ajili ya ujenzi au ukarabati wa daraja hilo, ahsante. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuwakosoa au kuwasaidia wananchi hawa ambao ni Maaskari wetu wanaofanya kazi usiku na mchana ambao wanaishi katika mazingira magumu sana, kwa kuwa nyumba zao zinavuja na miundombinu imechoka sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami kwenda eneo la tukio akaone hali halisi ya makazi ya maaskari wetu wanavyoishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani kuwa Serikali inatambua uchakavu wa Vituo vya Polisi lakini pia inatambua uchakavu wa nyumba za makazi kwa ajili ya askari hawa. Aidha, Serikali inatambua juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi katika ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge, kwa sasa tunaenda kuzitafuta shilingi bilioni 3.6, zitakapopatikana tunaenda kuanza ujenzi wa nyumba hizo, lengo na madhumuni ni Askari wetu waweze kuishi kwenye mazingira mazuri. Aidha, nimwambie tu kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, tupo tayari kuambatana naye kwenda mpaka kwenye eneo ili kukagua na kuona uchakavu huo na kuona namna ya kuweza kuwasaidia, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Sita kwa kuiona barabara ile kwa kuwa imekuwa na changamoto kubwa sana. Naishukuru Serikali kwa kuingia mkataba wa kutengeneza barabara ile ya Mkomazi – Kisiwani – Same. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja tu la nyongeza. Kuna maeneo ambayo yalitengenezwa kwa kiwango cha lami, kilometa tano, tatu na tano tena; katika Kata ya Ndungu zimetengenezwa kilometa tano, katika Kata ya Maore zimetengenezwa kilometa tano na katika Kata ya Kihurio zimetengenezwa pia kilometa tano…

SPIKA: Swali lako Mheshimiwa.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Je, Serikali sasa kupitia mkataba huu itabomoa ile lami ambayo imetengenezwa ambayo imeanza kuchakaa au itaendelea na ile ile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri, Mbunge, Viti Maalum, Mkoa wa Kilimanjaro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza napokea hizo pongezi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuhusu suala lake la maeneo ambayo tumeyajenga, wakati hizi barabara zinajengwa kwa vipande vipande yalikuwa ni maelekezo kutokana na wananchi wa maeneo hayo yalivyokuwa korofi, lakini pia kwenye miji midogo waliomba viongozi na wakatoa maelekezo barabara hizo ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa vipande vipande.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na wananchi ambao wanahusika na hiyo barabara, usanifu uliofanyika, hayo maeneo yameshakuwa yamechakaa na hayaendani na usanifu wa sasa. Kwa hiyo, maeneo yote yale yatafumuliwa na yatajengwa upya, isipokuwa kuna kilometa tano na kitu ambayo inaendela kujengwa, hiyo ndiyo ianendana na usanifu wa sasa, lakini maeneo yote ya zamani yatafumuliwa na kujengwa upya, ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Makanya – Ruvu ambayo inakwenda kwenye machimbo ya gypsum? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni barabara ya kimkakati ambayo inaenda kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Siha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikijibu hapa, kwa maeneo ambayo tumeona jitihada za Halmashauri na wananchi katika ujenzi wa vituo vya polisi ni kipaumbele cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Jeshi la Polisi kuwaunga mkono ili kukamilisha. Tutaangalia katika mipangilio yetu namna ambavyo tunaweza tukapata fedha kupitia ama vyanzo vya fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu au fedha za tuzo na tozo kuwaunga mkono wananchi wa Siha kukamilisha kituo chao cha Polisi, nashukuru.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA Wilayani Rombo kwa kuwa Halmashauri imeshatoa eneo na wataalam wa ardhi wameshafanya uchambuzi na kuona linafaa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zuena kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa vyuo 68 vya wilaya zilizobaki, Rombo ni miongoni mwa Wilaya ambayo inakwenda kujengewa chuo hicho. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kazi kule Rombo tayari imeshaanza. Tumefanya geo technical, topographical, environment impact assessment, na tayari tumeshatambua eneo na shughuli zimeshaanza katika mwaka huu wa fedha.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama za Mwanzo hasa zilizopo Vijijini ambazo miundombinu yake imechakaa sana, ikiwepo Mahakama ya Gonja Maore, Jimbo la Same Mashariki katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mahakama nyingi za mwanzo zilijengwa katika mfumo ambao ni wa kizamani sana, na kwa sasa tunaendelea kuziondoa zingine katika sura kabisa ya Mahakama ulivyo sasa ili tujenge Mahakama nyingine nzuri zaidi. Kuhusu ukarabati kwa zile ambazo tunaziangalia kama zinaweza zikarekebika hizo ndizo tunaziwekea mpango wa kwenda kuzifanyia ukarabati na zoezi hilo linaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Gonja, Mahakama za Mwanzo kama nilivyoeleza kwamba tutazipitia nazo kuangalia namna ambavyo tunaweza tukazifanyia kazi. Ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naomba niulize swali; je Serikali haioni haja ya kurejesha huduma hii katika halmashauri sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara imejipanga vipi kudhibiti janga la moto katika masoko nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Bushiri kama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja; kuhusu umuhimu wa kurejesha huduma hizi halmashauri, naomba nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba huko nyuma huduma hizi zilikuwa zinatolewa na halmashauri, baada ya kuthibitika kwamba weledi na uwezo wa halmashauri kutekeleza jambo hili ni changamoto ikaamuriwa huduma hizi zirudi Makao Makuu na ndiyo ikaimarishwa hili Jeshi la Zimamato na Ukoaji. Kwa hiyo kama tunazungumza kurejesha itabidi tufanye tathimini kujiridhisha leo ule uwezo ambao haukuwepo miaka kumi iliyopita kama umekuwepo na hivyo kuona umuhimu wa kurejesha hizi huduma.

Hata hivyo, wananchi wanao hudumiwa wapo kwenye halmashauri na wengi ni wafanyabiashara ni wazi kwamba bajeti ya zimamoto ni changamoto, hivyo halmashauri zinatakiwa kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa ili askari wetu waliopangwa kwenye maeneo hayo wavitumie vifaa hivyo kuzima moto kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, swali la pili juu ya namna ya kudhibiti majanga ya zimamoto yanayozidi kuongezeka; nakiri kwamba yapo ndiyo maana nimebainisha mikakati hapa itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za zimamoto na ukoaji ikiwa ni pamoja na mafunzo, lakini vilevile elimu kwa umma na kuzingatia weledi katika ujenzi wa majengo yetu. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama za Mwanzo hasa zilizopo Vijijini ambazo miundombinu yake imechakaa sana, ikiwepo Mahakama ya Gonja Maore, Jimbo la Same Mashariki katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mahakama nyingi za mwanzo zilijengwa katika mfumo ambao ni wa kizamani sana, na kwa sasa tunaendelea kuziondoa zingine katika sura kabisa ya Mahakama ulivyo sasa ili tujenge Mahakama nyingine nzuri zaidi. Kuhusu ukarabati kwa zile ambazo tunaziangalia kama zinaweza zikarekebika hizo ndizo tunaziwekea mpango wa kwenda kuzifanyia ukarabati na zoezi hilo linaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Gonja, Mahakama za Mwanzo kama nilivyoeleza kwamba tutazipitia nazo kuangalia namna ambavyo tunaweza tukazifanyia kazi. Ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Siha ina vijana wengi sana ambao hawajapata nafasi ya kuendelea na masomo ya juu.

Je, Serikali ina mpango gani katika hivi vyuo 36 na yenyewe kupata nafasi ya kujenga Chuo cha VETA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge Viti wa Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwamba ujenzi huo unakwenda kwa awamu, kwa hiyo kuna maeneo tutayafikia na kwa vile tutaweka vigezo, cha msingi tutaangalia ule uhitaji mkubwa katika maeneo tutakayoyaainisha. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwenye hili, kwa vile Wilaya ya Siha ina uhitaji mkubwa na vijana pale ni wengi kwa vyovyote vile Wilaya ya Siha tutaipa kipaumbele, nakushukuru sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa ujenzi wa soko hili ulitokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa ni Makamu wa Rais; na kwa kuwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara wananchi wa Rombo walikumbushia ahadi yao: Je, nini kauli ya Serikali kuhusu ujenzi wa soko hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, shilingi milioni 75 ni fedha ndogo sana katika ujenzi huu. Je, Serikali kwa nini isiweke ujenzi wa soko hili katika miradi ya kimkakati ili kutimiza ahadi ya viongozi hawa wawili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba ahadi za viongozi wetu wa kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa kuwa ni kweli fedha ambayo imetengwa ni kidogo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rombo kufanya tathmini ya kina na upembuzi yakinifu wa gharama zinazohitajika, kwa ajili ya ujenzi wa soko hili na kuziwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuona kama fedha itatoka Central Government au wanaweza kugharamia kwa mapato ya ndani, ahsante. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Holili - Tarakea kwa kuwa kumekuwa na msongamano mkubwa sana katika barabara ya Rombo ambayo inabeba malori mengi, inachukua malori yanayopeleka mchanga katika nchi ya Kenya? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri, Barabara hii ya Holili – Tarakea, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuona ni namna gani ambavyo bajeti imetengwa kwa ajili ya kupanua barabara hii ili iweze kupitika wakati wote.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule ya Sekondari Kwambegu iliyoko Kata ya Mahore ambalo ni hitaji la wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapandisha hadhi shule hii iliyopo Kata ya Mahore. Kama nilivyokuwa nikimjibu Mheshimiwa Kapinga kwamba, ni kwa mujibu wa sheria na taratibu zile zilizopo; ni lazima kwanza iwe imekidhi vigezo ambavyo vimewekwa. Hivyo basi, nimatake Mkurugenzi wa halmashauri husika kuweza kuanza kufanya tathmini hii na kisha Mkaguzi kwenda kuona kama vile vigezo vimetimia na kuweza kuomba kwa wenzetu wa Wizara ya Elimu kuweza kupandisha hadhi shule hii. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na migogoro kati ya Kata ya Makanya Ruvu na Makanya Bangalala ya muda mrefu. Je Serikali ina mpango gani wa kumaliza migogoro hii ya ardhi? Ahsante.
SPIKA: Hizo kata ziko wapi Mheshimiwa?

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Same, Jimbo la Same Magharibi.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli wiki iliyopita nilipita Bangalala na Makanya na Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi Mheshimiwa David Mathayo. Tayari nimeunda timu ndogo itakwenda Bangalala na Makanya tarehe 07 ya mwezi huu na baada ya kuniletea taarifa nitafika tena kwenda kutoa majibu ya mgogoro huu ambao umekuwa ukiwasumbua wananchi kwenye mipaka yao.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya cha Umbwe hakina maabara, OPD na mortuary.

Je, ni lini Serikali itajenga vitu hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, vituo vingi vya afya hapa nchini hasa vile vilivyojengwa miaka ya nyuma vina upungufu wa baadhi ya majengo. Ndiyo maana Ofisi ya Rais TAMISEMI imefanya mapping ya vituo vyote kote nchini na kuvitambua vituo ambavyo vina majengo pungufu ya yale ambayo yanahitajika kwa ajili ya vituo vya afya kikiwemo kituo hichi cha Umbwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo hivi pamoja na hiki kituo kipo kwenye mpango na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza majengo hayo ili viwe na majengo ili viwe na majengo yale yanayohitajika kwa ngazi ya kituo cha afya.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Moshi ina vijana wengi sana ambao wanahitaji elimu ya ufundi. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika halmashauri hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwia Mwenyekiti, ninaomba nijibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kujibu kwenye maswali ya msingi kwamba kwa sasa baada ya kukamilisha ujenzi wa vile vyuo 25 vya awamu ya kwanza katika wilaya 25 na hivi 64, tutakuwa hatuna wilaya ambayo haina Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba kunawezekana kukawa na umbali wa namna moja au nyingine lakini ninaamini pale Moshi tuna Chuo cha VETA ambacho kiko pale Moshi, ni chuo cha mkoa, lakini vilevile kina-save kama chuo cha wilaya, lakini kwenye zile wilaya nyingine za pembezoni, ukienda Rombo, ukienda Hai, ukienda Siha, kote kule tumejenga Vyuo vya VETA na yale majimbo ambayo hayana vyuo tunakwenda kujenga shule za ufundi ku-complement pale ambapo Chuo cha VETA kimekosekana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji katika Kata ya Kimochi, Moshi Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipokee changamoto hii kwanza nikaielewe kwa kina ili tuweze kuifanyia kazi kulingana na uhitaji wake. Nakushukuru sana.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Kituo cha Afya cha Tarakea kitaboreshwa ili kiweze kutoa huduma ya upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge, amefuatilia mara kadhaa na sisi kama Serikali kazi yetu ni kupokea maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya kwenda kutengeneza mipango na bajeti kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, Kituo cha Afya cha Tarakea tumekichukua Mheshimiwa Mbunge, tutakiwekea mpango kwa ajili ya ukarabati. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Maore, Kijiji cha Muheza, Kitongoji cha Nandululu tembo wameingia na kubomoa miundombinu ya maji, hivyo wafugaji hupata shida sana kwa ajili ya mifugo kupata maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kujenga miundombinu hiyo ya maji ili kutatua tatizo hili?

Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuongozana na mimi kwenda kuona hali halisi ilivyo katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ninatambua kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Mbunge Zuena Bushiri katika kufuatilia masuala ya mifugo hususani katika Mkoa wake wa Kilimanjaro. Nimwondoe shaka, jambo lake nimezungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na amenithibitishia kwamba jambo hilo wanaliweka katika mpango wa kuhakikisha linajengwa kwa dharura kupitia visima ambavyo Bunge lako Tukufu lilipitisha katika Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyopitishwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuongozana, nimthibitishie tu kwamba nimzengumza na Mheshimiwa Mnyeti pamoja na Mheshimiwa Ulega wamesema watakuwa tayari watakaporudi, wapange tu muda gani wafike katika hayo maeneo ambayo umeanisha yana changamoto, ahsante.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa, Mfuko wa Jimbo ulipeleka shilingi milioni saba ukaendelea kujenga uzio huo na ikawapa wananchi matumaini makubwa sana kutokana na changamoto iliyopo katika kituo hicho cha afya kwa wagonjwa kuibiwa nguo wakati wameanika, chupa za chai pamoja na simu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili kumaliza changamoto hii ya ujenzi wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vituo vyetu hivi vya afya vinakuwa na usalama, ikiwemo kujenga uzio kwa ajili ya kuzuia changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa kupeleka fedha za Mfuko wa Jimbo pia na Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kwa kuendelea kupeleka fedha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumeshaelekeza Manispaa ya Moshi, wataendelea kutenga fedha kwa awamu na kuhakikisha kwamba uzio huu unakamilika mapema sana iwezekanavyo, ahsante. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha afya cha Gonyaza kilichopo Kata ya Suji - Same Mashariki ni kituo ambacho kinahudumia watu wengi sana na kutokana na jiografia yake ya milima, wananchi wanapata shida sana, lakini kituo hicho kinasuasua katika ujenzi wake. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya uwakilishi anayoifanya. Naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaimarisha utoaji wa huduma ya afya msingi na inafanya hivyo kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ikiwemo ya ujenzi wa vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya msingi kama hospitali, zahanati pamoja na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kituo cha afya alichokitaja Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba Serikali itahakikisha kituo hiki kinakamilika na kinaweza kupatiwa vifaa na vifaatiba pamoja na watumishi wa kada ya afya ili kiweze sasa kuanza kutoa huduma za afya.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Moshi ina vijana wengi sana ambao wanahitaji elimu ya ufundi. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika halmashauri hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwia Mwenyekiti, ninaomba nijibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kujibu kwenye maswali ya msingi kwamba kwa sasa baada ya kukamilisha ujenzi wa vile vyuo 25 vya awamu ya kwanza katika wilaya 25 na hivi 64, tutakuwa hatuna wilaya ambayo haina Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba kunawezekana kukawa na umbali wa namna moja au nyingine lakini ninaamini pale Moshi tuna Chuo cha VETA ambacho kiko pale Moshi, ni chuo cha mkoa, lakini vilevile kina-save kama chuo cha wilaya, lakini kwenye zile wilaya nyingine za pembezoni, ukienda Rombo, ukienda Hai, ukienda Siha, kote kule tumejenga Vyuo vya VETA na yale majimbo ambayo hayana vyuo tunakwenda kujenga shule za ufundi ku-complement pale ambapo Chuo cha VETA kimekosekana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Kata ya Karansi kumekuwa na matukio ya mauaji ya mara kwa mara. Mnamo mwaka 2016 aliuawa baba mmoja katika Kata hiyo na mnamo mwaka 2022 mwanamke mmoja alichinjwa. Je, Serikali inaongea nini au inawaambia nini wananchi wa Karansi, katika kuwasaidia ili kuepukana na matukio mazito kama hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Kata hiyo hiyo kumekuwa na matukio ya uhalifu yakiongezeka sana kutokana na idadi ya wananchi waliopo. Hivi karibuni katika mwezi wa Tatu mwaka huu 2024, na mwezi huu wa Nne yamevunjwa maduka manne ya wafanyabiashara na mali za thamani ya zaidi ya shilingi milioni 48 zimepotea. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kujenga kituo kidogo cha Polisi ili kuwasaidia wananchi katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Zuena Bushiri, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii taarifa nimeipokea sasa kwamba kuna mauaji yalifanyika katika Kata hiyo, nitafuatilia kujua ni watu gani waliohusika, lakini pia ni hatua gani zilichukuliwa na Serikali kwa mauaji yaliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; Jeshi la Polisi limesambaza Askari Kata ili kushirikiana na wananchi na kuboresha ulinzi shirikishi katika maeneo yote na kuboresha doria ili kudhibiti masuala yote ya uhalifu katika Kata zetu na vijiji vyetu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mbunge awasihi wananchi wa Kata ya Karansi kushirikiana na Askari ili kuboresha doria katika maeneo yote ili Kata hiyo na Kata nyingine ziendelee kuwa salama, ahsante. (Makofi)