Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abeid Ighondo Ramadhani (38 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Ni Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili niwashukuru wananchi wangu wa SIngida Kaskazini kwa kuniamini na kunipa fursa ya kuja kuwakilisha sauti zao katika Bunge letu hili tukufu. Nikishukuru pia Chama changu cha Mapinduzi kwa imani yake kwangu na mimi naahidi kama nilivyowaahidi kwamba sitawaangusha, nitawatumikia kwa unyenyekevu mkubwa na kwa uaminifu wa kutosha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukifuatilia mjadala, Wabunge wengi wanazungumzia jambo la TARURA, barabara, afya, maji na kilimo. Haya mambo ndiyo yanayogusa maisha ya Mtanzania. Naomba sana tuzingatie hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo na yenyewe ilijikita kwenye haya haya na mimi siiiti hotuba, naiita yale yalikuwa ni maelekezo. Tuichukue hotuba ile tuitazame neno kwa neno, tuchukue hayo maelekezo itoshe tu kusema Mheshimiwa Rais alitupa maelekezo sisi Wabunge pamoja na Mawaziri na alisema hebu msiogope. Amesema fanyeni maamuzi chukueni hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu naomba ujielekeze zaidi kwenye kushauri kwa sababu mengi yamesemwa, suala la TARURA ni msiba, ukienda vijijini hakuna barabara ni mapalio. Sasa sisi tumechoka kupita kwenye mapalio. Wabunge hapa wanazungumza maisha halisi yaliyoko kule kwenye field. Tumechoka kupita kwenye mapalio, ninashauri kama hii TARURA haipewi fedha ifutwe! Kwa sababu hizo ni kodi za Watanzania, majengo wanayojenga kila Wilaya nchi hii hata lile jengo lao pale Wizarani hizo ni kodi za Watanzania. Hizo fedha badala ya kutumiwa kwenye mafuta, jengo na kwenye viti na mishahara, hizo fedha zichukuliwe zipelekwe zikatengeneze barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kwa uchache kwenye jimbo langu tu kwenye hili eneo la TARURA kilometa 800 za barabara wanapewa shilingi milioni 600, utatengeneza nini hapo? Si vichekesho hivi? Naomba hili jambo lichukuliwe, Serikali iliangalie tuanche kurudia rudia mambo sio kila siku tunazungumza jambo hili. Kurudia rudia ina maana hawa Wabunge hawaaminiki wanapolalamika suala la barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa pia nizungumzie eneo la viwanda. Mheshimiwa Rais dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha tunakuwa na uchumi wa viwanda na uchumi wa viwanda hatuwezi kuuona endapo sekta ya viwanda haijawa connected na sekta za uzalishaji. Itakuwa ni ndoto! Tuhakikishe tunaelekeza nguvu zetu zote kwenye eneo la uzalishaji. Tuangalie kwenye kilimo, tuangalie kwenye uvuvi, tuangalie kwenye ufugaji, huko ndiko tunakuta Watanzania wengi na ndio wanaozalisha na hao ndio wanaoweza kutuletea raw materials zinazohitajika kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sisi leo natoleo mfano tu mdogo kwenye eneo la mifugo, ngozi inaoza na mimi ambaye ni mfugaji mtoto wa mkulima tunahitaji tuone yale mazao kule vijijini yanakuwa processed, yawaajiri Watanzania. Tunalalamika suala la ajira, tunamuajiri wapi Mtanzania kama hatujajikita kwenye eneo la viwanda? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ighondo.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba haya machache niliyoyazungumza nione yakitekelezwa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii angalau niseme mawili matatu kwenye mjadala huu wa Wizara hii ya Maji. Awali ya yote, kutokana na muda naomba nitambue kazi nzuri inayofanywa na watendaji pamoja na Mawaziri wa Wizara hii. Kwa mantiki hiyo, niishukuru Serikali kwa miradi mikubwa ya maji ambayo imekwishakamilika na inatoa maji hivi sasa kwa upanuzi mkubwa wa njia za maji pamoja na miundombinu katika Kijiji cha Halunyangu, Kijota, Mgori, Mangida, Mughamu pamoja na Msisi. Miradi hii kwa kiwango kikubwa imeondoa adha kwa wananchi ambao walikuwa wanapata tabu kweli kweli wanapohitaji huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii nashukuru na naipongeza Serikali kwa kutupatia fedha kwa ajili ya miradi mikubwa minne ya maji. Kijiji cha Mwighanji, Mitula, Migugu na Ughandibe. Hatua hii ni nzuri sana na naomba sana Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika kwa wakati kama ambavyo imepangwa. Kwa mazingira hayo, naomba sasa DDCA, ambao ni Wakala wa Uchimbaji Visima vya Serikali wafike mara moja kwa ajili ya kuanza kazi ili wananchi wetu waondokane na adha ya kupata taabu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitambue pia mchango wa wadau, taasisi binafsi kwenye upatikanaji wa maji katika Jimbo la Singida Kaskazini. Naomba nitambue Shirika la Rehema Foundation, Silver Crescent ya kutoka Nchini Uturuki ambao kwa kushirikiana na Mbunge tangu aanze kazi miezi sita sasa amefanikiwa kukarabati visima 23 ambavyo vilikuwa vimekufa kabisa lakini na kuchimba visima virefu vinne katika Kijiji cha Kinyamwenda, Makuro, Maghandi na Itamka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi kubwa katika hili, visima vile vinatoa maji ya kutosha kuanzia lita 10,000 kwa saa moja. Ni ombi kwamba maji haya yasambazwe. Naiomba Wizara kwa kushirikiana na RUWASA, maji hayo yasambazwe ili yawafikie wananchi wengi kwenye vijiji vingi badala ya kubaki pia yanatolewa kwenye centre tu ile pale kilipo kisima.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa sasa ambayo naiona kwenye miradi mingi ya maji, Singida Kaskazini pamoja na maeneo mengine ni suala la ufuatiliaji. Ufuatiliaji ni tatizo kubwa sana. Unakuta kisima kimetengenezwa leo kinakaa miaka 20 hakijawahi hata kutembelewa siku moja kuangaliwa changamoto zake. Kwa hiyo, visima vingi vimekufa. Mathalani, visima hivi 23 ambavyo mimi Mbunge kwa kushirikiana na wadau tumevikarabati, vilichimbwa mwaka 1980 na Shirika la TCRS. Kwa hiyo, niombe sasa Wizara ya Maji wawe na tabia ya kufuatilia miradi, ku-cross check…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Lah! Naunga mkono hoja ingawa bado nilikuwa na mengi ya kusema hapa. (Makofi)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa walau nichangie katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri ya Bajeti Kuu ya Serikali, kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uchapaji kazi wake mzuri, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu yake nzima iliyochakata bajeti hii ambayo hivi sasa tumeiona imetupa vipaumbele vikubwa kadhaa ikiwemo kwanza kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimepewa kipaumbele namba moja na hasa hasa kwenye maeneo ya umwagiliaji pamoja na pembejeo za kilimo. Hapohapo ile miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ndio tunasema inaenda kukomboa uchumi wa nchi yetu Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, haya mambo kwa kweli tunayo kila sababu ya kumpongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye tunasema ndiye mbeba maono ya nchi yetu kuelekea 2025. Nimuombee Rais wetu afya njema na tumpe moyo, tumtie moyo Rais wetu kwa kazi hii anayoifanya ili aendelee kututumikia Watanzania wenzake kwa moyo na kwa upendo wa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nilete shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, siku ile nilipoomba barabara ile ya Singida - Ilongero nimshukuru Waziri wa Ujenzi aliahidi kunipa kilomita 10 za lami, lakini na yeye Waziri wa Fedha akaniambia bwana tunaenda kutafuta fedha kwa barabara nzima iwekwe lami, hiyo ahadi tunaishukuru wananchi wa Singida Kaskazini lakini tunatarajia sasa tuone utekelezaji. Tunatarajia tuone utekelezaji kuanzia mwaka huu wa fedha kama Waziri Mbarawa alivyosema lakini hata wewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama ulivyoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu kubwa ya leo pamoja na mazuri mengi niliyoyaona kwenye bajeti hii ikiwemo suala la wanafunzi wa elimu ya vyuo vya kati kusoma for free kwa mikopo kutoka Serikalini, kwa kuondolewa ada lakini pia kwa kuendelea kutoa ruzuku kwenye mbegu kwenye mbolea na pembejeo za kilimo. Nina mambo machache ambayo ningependa kuyawasilisha kwa ajili ya kuyafanyia kazi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuna suala la ule mfumo wa electronic stamp (ETS). Mfumo huu ni mzuri lakini umekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau kwamba una gharama kubwa, yule mwekezaji anayetoa hii huduma imekuwa kidogo ina malalamiko kutoka kwa wadau. Kwa hiyo, niombe Serikali ichukue fursa ya kukutana na yule mdau ili kupunguza zile gharama ili wale wananchi wanaopata hii huduma wapate huduma hii kwa urahisi.

Pili, zile stamp zilizopo kwenye chupa za maji kwenye soda na kadhalika zimekuwa zina malalamiko kwa hiyo niombe Serikali ikae na yule mwekezaji waweze kuondoa zile gharama ziwe za kawaida kwa ajili ya kupunguza hata gharama pia za maji kwenye matumizi ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme moja kubwa leo kwenye eneo la kilimo hususani zao la alizeti. Wenzangu wamezungumza sana wanaotoka Mikoa ya Kati, alizungumza sana Mheshimiwa Yahaya Massare jana amezungumza pia Mheshimiwa Kunti Majala asubuhi ya leo lakini na Wabunge wengine wanaotoka kwenye maeneo yanayozalisha Alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022, 2022/2023 Wizara ya Kilimo, Waziri Mkuu kwa ujumla wake wametuhamasisha sana kulima alizeti, tunashukuru tumeona pembejeo za kilimo, tumeletewa mbolea, mbegu zenye ruzuku lakini hatua hizo zimewezesha kwa kiwango kikubwa kuongeza tija kwenye uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alizeti imelimwa kwa kiwango kikubwa sana nchini, kuanzia Iringa, Singida Kaskazini, mpaka kule Maluga, Kiomboi kule ndani kule Shelui wanakolima alizeti, wamelima sana alizeti na sasa hivi pale barabarani tunakopita pale Maluga unaona alizeti ni nyingi kweli kweli, ukienda Iramba ndani kule Mkoa wamelima sana alizeti kwa wingi, nyingi kwelikweli nawapongeza sana wa Singida, Wanasingida, Watanzania kwa ujumla wanaozalisha alizeti. Niwapongeze na watu wa Ilongero, Mudida na kule kwingine kote walioitiia wito wa Serikali kwa kulima na kuzalisha alizeti kwa wingi, wameipokea kauli mbiu wamepokea kauli za viongozi wao kuhakikisha wanazalisha sana alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida inakoanzia ni wapi? Kwa masikitiko makubwa sana, kwa majonzi makubwa sana, sasa hivi tunavyoongea hapa bei ya gunia moja la alizeti ambalo lina ujazo wa kilo sitini mpaka sabini ni shilingi 25,000 umeuza sana 35,000. Kwa kweli ni masikitiko makubwa sana kwa mfumo huu, hili tatizo limeletwa na sisi tunaoagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu ambayo naiheshimu sana na kwa kweli suala la kilimo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo mimi niliinadi mwaka 2020, wakati tuko kwenye Uchaguzi Mkuu, kwamba tunakwenda kukipa kipaumbele kilimo na tunaenda kuki-modernize kiwe cha kisasa, kwenye ukurasa wa 33 kuendelea mpaka huko inakoenda kwamba Serikali ya CCM inakwenda ku-modernize kilimo. Sasa ku-modernize kilimo maana yake ni kuhakikisha hata kwenye masoko yetu, sisi wenyewe tu-export nje ya nchi, siyo tu import. Nashangaa inawezekanaje tuwe tunaagiza mafuta ya kula nchini wakati tuna mawese, tuna alizeti, karanga na pamba. Sisi ndio tunatakiwa tupeleke mafuta ya kula nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kunti alizungumza vizuri sana asubuhi kuhusu eneo la alizeti. Naomba mchango wake nami niutambue kwenye eneo la alizeti. Naomba Mheshimiwa Waziri kwenye eneo la alizeti, katika suala la kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, hii tunailetea nchi yetu laana. Tunawaumiza wakulima wetu, tunawaumiza wananchi wetu ambao maisha yao yanategemea kilimo. Mwananchi amelima kutoka mwezi wa Kumi na Moja mpaka leo Mwezi wa Sita ndiyo anaenda kuuza. Almost seven months yuko kwenye kilimo anahangaika kuzalisha, unakuja kumwambia leo unamwagizia mafuta kutoka nje. Hii siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali yangu ifanye mambo mawili. La kwanza kwenye hili, ili kumsaidia mkulima, kumsaidia mwananchi wa kawaida wa nchi yetu, la kwanza tuhakikishe ile nakisi iliyopo, tunasema mahitaji yetu ya ndani ni tani 650,000, lakini tuna uwezo wa kuzalisha tani 300,000, basi tusiagize hivi sasa. Tusubiri wakati tunapoona nakisi kule mwishoni ndiyo tuagize, lakini tuagizie kwa kutumia vibali kulingana na upungufu uliopo. Sasa hivi ni soko huria, ukimwambia mtu agiza, aneleta zaidi ya hizo. Anaweza kuleta tani 1,000, tutawezaje kudhibiti hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana twende kwa takwimu. Tuangalie kwanza tuna viwanda kiasi gani vinavyozalisha mafuta? Vina uwezo gani? Tuangalie na uzalishaji tunaoufanya, kweli hii nakisi tunayosema ya tani 350,000 ndiyo iko hivyo hivyo? Maana yake wenzetu wanapoambiwa walete, wanaagiza mpaka wanakuja kuua soko letu la mazao ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana Waziri anisikie na Serikali kwa ujumla, kwamba kuendelea kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi ni kuendelea kumdidimiza mkulima ambaye maisha yake asilimia 100 yanategemea hiyo mbegu ya alizeti, yanategemea kilimo, hana mshahara, hana kitu kingine chochote kinachomwingizia mapato kwenye maisha yake. Anategemea apate dawa, apate ada ya watoto wake, na kila kitu kwenye maisha yake anategemea alizeti au mazao. Sasa sisi tunavyoendelea kuagiza kutoka nje, tunamnyanyasa, tunamuumiza huyu mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye eneo la alizeti, kuagiza mafuta kutoka nje, naomba Serikali ilisikie hili na kulifanyia kazi. Serikali ifanye tafiti, kwa nini sisi mpaka leo tunaagiza mafuta kutoka nje ya nchi wakati ardhi yetu ukianzia Kigoma uende mpaka Pwani, kote unakutana na alizeti. Ukianzia Ruvuma mpaka Arusha kote tunalima alizeti; tunalima chikichi, tunalima pamba, inakuaje mpaka leo sisi ni waagizaji wa mafuta kutoka nje? Tuna hujuma? Hatufanyi kazi ipasavyo? Tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili Mheshimiwa Waziri alichukue, ninashukuru kwamba hata yeye ni mkulima namba moja, hata kwenye hotuba yake hapa alisema amesoma kwa kupitia mifugo, amesoma kwa kupitia kilimo, kwa sababu kilimo na mifugo vinaenda pamoja. Naamini hili ninalolizungumza analielewa kaka yangu doctor, tunatarajia baadaye awe Profesa. Sasa Uprofesa huu tuulete kwenye maisha halisi ya wananchi wale waliotuzaa sisi wakatusomesha mpaka leo tuko hapa. Mheshimiwa Waziri … (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: …tunatarajia nao wapate manufaa na matunda.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ramadhani kuna taarifa. Iko wapi taarifa?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Kuchauka.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa. Nampa taarifa mzungumzaji, anachangia vizuri sana. Nami ninazo taarifa kutoka kwa wakulima wanasema, katika kuagiza haya mafuta humu, kuna watu wananufaika, ndiyo maana wanaendelea kuagiza. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ramadhani Ighondo, unapokea hiyo taarifa?

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshaunga mkono hoja, lakini pia anachokizungumza Mheshimiwa Kuchauka ni kweli. Hili eneo la kuagiza mafuta ndiyo linalowatesa wananchi kwa sababu kuna watu wananufaika na wametundika mirija yao, wanawatesa wananchi wenzangu kule Singida Kaskazini, Iramba, Mkalama pamoja na maeneo mengine kwa sababu ya fursa wanazozitumia za kuagiza mafuta kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninashukuru. Naunga mkono hoja. Naomba hili moja kubwa la leo la eneo la mafuta ambalo nimezungumza, lichukuliwe na Serikali na lifanyiwe kazi, ahsante. (Makofi)
The Finance Bill, 2022
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Serikali kwa usikivu wake wa kupokea na kufanyia kazi maoni yetu Wabunge na kisha kufanyia marekebisho baadhi ya maeneo yaliyoletwa kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano; kuondoa 3.5% kama kodi ya magari makubwa na mabasi ya abiria na kutokuondoa 5% kwenye 10% ya fedha za mikopo kwa ajili makundi maalum kwenye mapato ya ndani ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri Serikali kuwekeza ipasavyo kwenye sekta za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili iweze kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa msiba uliowapata kwa kuondokewa na mwananchi mmoja, Mzee Salimu Isango baada ya gari waliyokuwa wanasafiria kutoka Ng’amu kundumbukia kwenye Mto katika Daraja la Mwakiti. Nawapa pole na niwaambie kwamba Mpango huu wa Taifa wa Miaka Mitano umesema kwamba utajikita katika uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Kwa hivyo, daraja hilo naamini litatengenezwa na litaepusha vifo vinavyoendelea kutokea hasa kipindi hiki cha mvua maji yanapokuwa yamejaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuzungumzia eneo la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Msiba mkubwa uliopo kwa vijana wa Kitanzania hivi sasa pamoja na wasomi wote wanaopita vyuoni kwa kupata mkopo huu ama mikopo hii ya elimu ya vyuo vikuu ni tofauti na matarajio ambayo yaliwekwa kwenye mfuko huu. Serikali ilikuwa inalenga kuwakomboa wananchi wake maskini lakini kinachotokea hivi sasa watoto wa kimaskini wanaonufaika na mkopo wa elimu ya juu pindi wanapomaliza masomo palepale wanakabwa wanaambiwa waanze kulipa mkopo bila kujali amepata ajira pale pale anageuka kuwa mdaiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kama sisi tumelenga kuwakomboa Watanzania, jana umemkopesha kwa sababu ni mtoto maskini aliyeshindwa kujisomesha. Kesho baada tu ya kumaliza masomo hajapata kazi umeshambana. Kwa maana hiyo hapa Serikali badala ya kuwasaidia watu wake imegeuka sasa inafanya nao biashara. Kitu ambacho ni hatari sana kwa maisha ya Watanzania na kwa elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu changamoto ya ajira ilivyo kubwa hivi sasa. Tunasahau hapohapo, badala ya sisi kujikita kuwasaidia hawa vijana ili watoke waende wakafanye kazi hata kwa kushirikisha Sekta Binafsi, sisi tunawakaba hapohapo bila kujali changamoto wanazokutana nazo na mazingira magumu ya elimu tunayoyaona sisi wenyewe hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba hii bodi badala ya kujikita kwenye kuwabana watoto hawa kwa kuwadai mikopo hii warudishe pindi wanapomaliza masomo, iwape muda wa kulipa madeni yao. Pia riba zipungue, riba zimekuwa kubwa sana kwenye eneo hili.

MWENYEKITI: Jitambulishe wa taarifa. Mheshimiwa Naibu Waziri endelea.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Ibara ya 178 ya Sheria ya Bodi ya Mikopo inawapa nafasi wahitimu kurejesha mikopo baada ya miaka miwili. Marekebisho hayo yalifanyika mwaka 2016 ikaondoa kipindi cha mwaka mmoja na hivi sasa marejesho yanafanyika baada ya miaka miwili na ilipitishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ighondo, pokea taarifa hiyo.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, lakini tatizo ni riba kubwa zilizopo kwenye hii mikopo, tupunguze riba hii. Mwanafunzi anapoanza kulipa ule mkopo alipe lile deni alilokopa na huu mkopo usiwe na riba, ndiyo hoja kubwa ninayotaka kuisimamia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa retention, ule mkopo unaongezeka kadri muda unavyokwenda, ndiyo kitu ambacho mimi nataka nikiombe hapa; badala ya huyu mtu kuja kulipishwa riba alipe ule mkopo, principle aliochukua, ndiyo hoja kubwa ambayo naiomba Serikali ichukue hili na iliangalie kwa makini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo watoto hawa wanaomaliza vyuo wapate kazi, tushirikishe sekta binafsi. Tushirikishe sekta binafsi hawa watoto waende wafanye practical, wafanye mazoezi, hata Serikali inavyotangaza ajira kile kipengele cha uzoefu wa miaka 15 mtoto huyu atafaulu.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu kumpa taarifa mzungumzaji kwamba licha ya riba bado muda wa miaka miwili ambao umetengwa ni wa karibu sana. Hapa asubuhi umetupa testimony ya mtoto aliyemaliza Mzumbe, ana takribani miaka sita hajapata ajira, sasa baada ya miaka miwili unaanza kumwambia atoe laki moja, anazipata wapi wakati hana ajira. Kwa hiyo hilo nalo Serikali iweze kuli-consider.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nampa hiyo taarifa. Ahsante.

MWENYEKITI: Malizia kwa sentensi moja Mheshimiwa Ramadhani kwa sababu muda umekwisha.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda pia angalau kwa uchache nizungumzie kidogo kwenye eneo la viwanda…

MWENYEKITI: Bahati mbaya umechelewa. (Kicheko)

Ahsante sana Mheshimiwa Ighondo.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nami nianze kwanza kwa kuwapongeza Mawaziri na Naibu Waziri wote waliochaguliwa ama walioteuliwa katika awamu hii ya Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo mawili matatu, lakini naomba nianze na hili la viwanda na hapa naomba Waziri wetu wa Fedha anisikilize kwa makini kwa sababu kwanza yeye ni kijana mwenzangu lakini ni mtu ambaye amekabidhiwa jukumu la kwenda kukomboa uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye eneo la viwanda ndugu zangu wabobezi katika mausala ya uchumi watanisaidia lakini katika pitapita zangu, uchumi wa viwanda, nchi iliyoendelea kiviwanda inatakiwa iwe na sifa kuu chache. Kwanza, tunatakiwa tu-export manufactured goods. Pili, tunatakiwa tu-import raw materials, tu-import malighafi kutoka nje kuja kulisha viwanda vyetu huku nchini lakini tuingize teknolojia. tukirudi kwenye uhalisia wa uchumi wetu Tanzania hii kitu inaenda kinyume, yaani kichwa chini miguu juu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazingira haya, kweli tunaweza kufikia ule uchumi tunaosema wa viwanda? Juzi tu hapa, tena sio juzi na hilo tatizo liko hivi sasa, mahindi ya Tanzania yamezuiliwa pale mpakani Kenya. Mimi nilifikiri kama tungekuwa smart Watanzania tungefurahi suala lile, tunatakiwa sisi tupeleke kule nje unga siyo kupeleka malighafi. Tunatakiwa sisi tu-export manufactured goods, sisi tuzalishe, tu-process tuhakikishe tunalisha viwanda vyetu hapa nchini, kule tupeleke bidhaa zilizotengenezwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Ziwa wanalalamika hapa kila siku, pamba, pamba, ngozi kwa nini tunatoa malighafi hivi kwenda kuwakuzia wenzetu uchumi wakati sisi wenyewe tunahitaji bidhaa hizi kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani? Ninatarajia katika Mpango huu tunaozungumza hivi sasa, Mawziri wetu, Waziri wa Viwanda, Waziri wa Fedha, Waziri wa Biashara na Uwekezaji mtutoa hapa tulipo twende hatua inayofuata kwa kuhakikisha bidhaa na mazao tunayozalisha humu ndani, tunaya-process wenyewe, tunapeleka nje bidhaa zilizokwishatengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasikia tuna viwanda vya viatu vya ngozi hapa nchini, lakini nashangaa tunafurahia kweli kuvaa viatu vya China. Hatuwatendei haki wakulima wetu na wazalishaji wetu wa ndani kuhakikisha kile tunachowahubiria kila siku zalisheni, kweli wanazalisha lakini kwenye eneo la finishing tunashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtaalam mbobezi wa uchumi, leo tunasema upele umepata mkunaji, basi kamalize kazi ndugu yangu tunategemea matokeo makubwa sasa. Tuwasaidie vijana wetu basi na wao wapate ajira kupitia sekta zetu za viwanda. Serikali haiwezi kuajiri ikawamaliza Watanzania wote, sasa hivi vijana wako mtaani wanasubiri ajira, utawaajiri wapi? Lazima tuanzishe viwanda vya kimkakati, lazima tuhakikishe raw materials zilizopo nchini zinafaidisha Watanzania hasa kwenda kwenye viwanda vya kwetu humu ndani sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kwenye eneo la kilimo mashaka bado ni makubwa. Nizungumzie tu maeneo machache ambayo nina uzoefu nayo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini. Sisi ndiyo wazazlishaji wakubwa sana wa alizeti, haya mafuta mnayokula hapa yametoka Singida Kaskazini mimi ndiyo nazalisha kule pamoja ndugu zangu. Gunia la alizeti iliyozalishwa limefungwa vizuri la kilo 100 ni Sh.40,000 mpaka Sh.50,000 lakini mbegu ni Sh.60,000 au Sh.70,000, tutamkomboa lini huyu mkulima? Tuleteeni pembejeo, mbegu na ziuzwe kwa bei affordable kwa kila Mtanzania. Hata hizi kelele tunazopiga kwenye viwanda watu watazalisha tupapeleka viwandani. Sasa hivi ndugu zangu kule Singida Kaskazini wameiacha alizeti kwa sababu bei ya mbegu ni kubwa, tu- subsidize mbegu, pembejeo ili wakulima waweze ku-afford kwa kiwango tunachofahamu cha hali za wananchi wetu kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la tatu ambalo linaendana sasa na haya masuala viwanda na kilimo ni lazima miundombinu iwe mizuri kwenye eneo la kuzalisha mpaka processing kama ni viwanda. Tulizungumza sana barabara zetu sasa hivi mvua zimenyesha zimeharibu kwelikweli barabara hazipitiki. Sidhani kama kuna Waziri hapa anayetokea Dar es Salaam maeneo ya Magogoni pale, wengi mnatoka vijijini kama ninakotoka mimi, mnafahamu hali halisi ya mazingira ya mwananchi wa Tanzania, tutengenezeeni miundombinu ya barabara za vijijini hata hizi zinazounganisha mkoa na mkoa na wilaya na wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo barabara moja kubwa pale inayotoka Singida Mjini kwenda Haydom, ile ndiyo roho ya uchumi wa Singida Kaskazini. Barabara hii ni ahadi ya viongozi wa kitaifa kuanzia Rais Mstaafu Hayati Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Naomba basi, tusiwadhalilishe viongozi hawa, tekelezani hizi ahadi ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo barabara inatoka Singida Mjini - Kinyeto – Kinyagigi – Meriya – Maghojo - Sagara nayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani hivi sasa. Naomba barabara hii nayo itengenezwe kwa kiwango cha lami kwa sababu sisi kwa uzalishaji wetu wa alizeti ninaowaambia hapa ndiyo tunaowalisha kwa mafuta, hatuwezi kuwaletea sokoni kama barabara ni mbovu. Ndiyo tunaozalisha vitunguu kwelikweli lakini hatuwezi kuvikisha sokoni kama barabara ni mbovu. Naomba kwa kupitia Mpango wetu huu wa Maendeleo tuione miundombinu ni kipaumbele na tuhakikishe tunawasaidia wakulima wetu katika eneo lao la uzalishaji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kwenye utawala bora kidogo…

NAIBU SPIKA: Hiyo ni kengele ya pili Mheshimiwa Ramadhani.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima yako naomba nusu dakika, inanitosha, naomba kuzungumzia suala la maslahi ya Madiwani.

NAIBU SPIKA: Sasa jambo jipya tena hilo Mheshimiwa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi angalau na mimi niseme machache kwenye mjadala wa Wizara yetu ya Elimu ambayo ni Wizara muhimu kwelikweli kwa mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuipongeza na kuishukuru Serikali; nampongeza sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake muhimu sana ya kuondoa ile asilimia sita kwenye mikopo ya elimu ya juu. Kitendo hiki ni cha kiungwana na kwa kweli nampongeza sana. Vilevile nimpongeze Waziri wa Elimu kwa kuondoa ile asilimia kumi iliyokuwa inatokana na penati kwa maana ya wanufaika kuchelewesha mkopo ule kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa hatua hii hapa imeonyesha ni kwa kiwango gani inamjali Mtanzania wa chini, yule maskini, kwa sababu mikopo hii lengo lake ni kuwakomboa watoto wa kimaskini wa Kitanzania ambao hawawezi kukopeshwa na mtu yeyote yule isipokuwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe mikopo hii sasa tupanue wigo tuipeleke kwenye ngazi za chini, kwenye ile elimu ya kati, vyuo vya kati, VETA vyuo vingine vya ufundi tumesha-train graduates sasa naona kwa kiwango fulani, mpaka tumeshindwa kuwaajiri na wenyewe wako mataani kila mahali. Naomba sasa tuelekee na huku kwenye hii elimu ya kati ambao ndio wanaofanya kazi moja kwa moja, tena hawa ukiwapa mkopo leo hii, ndani ya miezi mitatu anakwenda kufanya kazi moja kwa moja, kama ni fundi atapaua, atajenga ukuta, atapata fedha atakuja kurudisha huu mkopo.

Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie sasa kwenye elimu ya kati nao wanufaike na hii mikopo na ikumbukwe hivi sasa tuna shule hizi za sekondari karibu kila kata. Kwa hiyo sio wote wanaoweza kwenda vyuo vikuu, turudi huku chini huku nao wanufaike na mikopo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapohapo niombe sasa huu mpango wa Vyuo vya VETA, nilishaongea sana na Waziri wa Elimu mara kadhaa, aipe kipaumbele Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Jimbo la Singida Kaskazini katika kupata Chuo Cha VETA. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, vijana wana wito mkubwa sana wa kwenda kusoma mafunzo ya ufundi, lakini hakuna chou, vilivyopo ni mbali, havifikiki, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri akija hapa niombe commitment yake, aniambie ujenzi wa Chuo cha VETA Singida Kaskazini ni lini utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja hapa naomba nichukue nafasi hii kulisema, kwa sababu tukiendelea kunyamaza tutakuwa hatuitendei haki nchi yetu. Nchi yetu imeweka rasilimali nyingi sana kwenye elimu, vyuo vikuu vya kutosha, vyuo vya kati na shule za sekondari na hata za msingi. Nataka nitoe masikitiko yangu makubwa sana, sisi hapa Bungeni mara kadhaa tumekuwa sasa vinara wa kubeza juhudi hizi na kuonyesha elimu haina umuhimu. Hili jambo kwa kweli, naomba tulichukulie umakini na twende kwa tahadhari.

Mheshimiwa Naibu Spika, statement tunazozitoa sisi Wabunge humu Bungeni hata wakati mwingine utanisamehe, hata kiti, kwamba elimu ya darasa la saba ni ya muhimu kweli kuliko wasomi maprofesa. Hii statement sio nzuri, sio kwamba napuuza darasa la saba, hapana, naheshimu sana mchango wao na naheshimu sana umuhimu wao kwenye nchi yetu, lakini naomba twende kwa tahadhari, tusije tukafika mahali tukapuuza elimu, tukapuuza taaluma, tukapuuza wataalam, tutalidhalilisha Taifa hili. Tutafika mahali tutaangamiza Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuanzia leo baada ya hotuba hii, tuache kabisa kejeli kwenye taaluma, kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba pia nizungumzie upungufu wa Walimu kwenye shule zetu za misingi na sekondari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, mambo machache muhimu naomba yazingatiwe kama ifuatavyo; kwanza bajeti ya kilimo iongezwe kwani kiasi cha fedha kilichotengwa kwa sasa hakiwezi kukidhi kuleta mageuzi kwenye kilimo.

Vilevile mpango mkakati wa kuongeza uzalishaji wa alizeti katika mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu uliozinduliwa Singida hivi karibuni na Waziri Mkuu utekelezwe kwa vitendo na uwe endelevu, isiwe ni jambo la mwaka huu kwa sababu ya upungufu wa mafuta, lakini liwe endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kuhusu posho za Madiwani; naipongeza sana Serikali kwa utaratibu iliopendekeza wa kuwalipa Madiwani kupitia Serikali Kuu na moja kwa moja kwenye akaunti zao. Ushauri ni kwamba ni vyema kiwango wanacholipwa kiongezeke kutoka shilingi 350,000 hadi shilingi milioni moja au 700,000 kwa mwezi kwani Diwani ndio msimamizi wa miradi yote ya maendeleo inayokwenda kwenye kata yake ambayo ni ya mamilioni ya fedha, kumuacha Diwani akilia njaa huku anasimamia miradi mikubwa ya maendeleo haileti picha nzuri. Anaweza kushawishika kuhujumu au kuingia kwenye upigaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Diwani ndio msimamizi wa wataalam wote kwenye kata yake. Anahitajika awe vizuri kiuchumi ili aweze kuifanya kazi hii kwa ukamilifu. Pia Diwani ndio anaishi na jamii, matatizo yote yanaelekezwa kwake, akiwa na posho ya milioni moja ataweza kusaidia jamii na kuisemea ipasavyo Serikali hapo kwenye eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi laki moja kwa Maafisa Tarafa; napongeza sana hatua hii ya Serikali kuwapatia shilingi laki moja Maafisa Tarafa kila mwezi. Hata hivyo kumejitokeza manyanyaso kutoka kwa ma-DAS wakisema kuwa sasa watasitisha kuwapa posho za mafuta ya pikipiki na matengenezo (OC) kati ya shilingi 50,000 hadi shilingi 250,000 au mafuta ya petroli lita 50 walizokuwa wanawapatia Maafisa Tarafa hapo awali.

Naomba katika majibu ya Waziri alitolee ufafanuzi jambo hili na kukemea kauli na matendo wanayoanza kuoneshwa na ma-DAS dhidi ya Maafisa Tarafa kuwa watasitisha kutoa zile walizokuwa wanawapa. Naomba hii ifahamike na itajwe na Waziri kuwa ni ku-top up ile posho waliyokuwa wanapewa ili kuboresha utendaji kazi wao. Jambo hili limejitokeza kwa Wilaya ya Singida ambapo Maafisa Tarafa wameanza kutishiwa/kuacha kupewa posho/ oc waliyokuwa wanapewa hapo awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji na jinsi anavyoendelea ku-fit katika nafasi yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili nizungumzie changamoto za barabara zilizopo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mchache, itifaki ya shukrani na pongezi naomba izingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda moja kwa moja kwenye mchango wangu, nizungumzie barabara mbili, tatu, ambazo ni muhimu kwelikweli kwa maisha na uchumi wa wananchi wa Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na barabara hii ya kutoka Singida – Haydom kupitia Mji mdogo wa Ilongero ambao ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya na inapita katika Mji mdogo wa Mtinko na Kata ya Modeda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni ahadi toka Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi. Nakumbuka wakati huo niko darasa la tatu, mzee Mwinyi alikuja pale Ilongero akaombwa barabara hii akaahidi akasema nitaijenga. Amemaliza amekuja aliyefuata mzee Mkapa naye alifika Ilongero pale akaahidi hii barabara, lakini hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati tunaomba kura, Rais, Hayati Dkt. Magufuli, alifika Singida Mjini na akaahidi hii barabara. Kama haitoshi, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alifika Ilongero na akaahidi kwamba hii barabara tunaijenga kwa kiwango cha lami. Na kwa matokeo hayo kura zilipigwa nyingi kwelikweli kwa CCM.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo, kuna taarifa; Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampa taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na Waziri Mkuu kutoa hiyo ahadi, lakini Waziri Mkuu kwenye Jimbo lake kuna barabara tatu zote hazifikiki, kwa maana ya kwamba Liwale – Ruangwa, Nachingwea – Ruangwa na Nanganga – Ruangwa; zote hazifikiki kwa lami.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu ya muda mfupi ambao kila Mbunge anao wa kuchangia tujitahidi taarifa tunazozitoa basi ziwe za kumuongezea kile anachochangia; Mheshimiwa Ighondo, malizia mchango wako.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na masikitiko hayo ambayo nimeyaeleza naomba basi hii barabara sasa itengenezwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa uchache kwamba angalau imeonekana kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa 42, kwamba inakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu. Basi niombe sana kwa heshima na taadhima, nitaongea kwa lugha ya upole sana leo, sitafanya sarakasi kama alivyosema Mheshimiwa Flatei, lakini ninaomba hii barabara itengenezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hizi fedha kwanza ni kidogo, niliona ni shilingi milioni 100, milioni 100 kwa kilometa 93 kusema kweli siyo haki, siyo sawa hata kidogo. Barabara ambayo imeahidiwa na viongozi wote wa Kitaifa tangu uhuru mpaka leo tunaipa kamilioni 100, hili kwa kweli naomba litazamwe na ninamuomba Waziri nitaishika shilingi yako hapa; ongeza fedha hapa, fedha ziongezeke kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza barabara hii inakwenda Makao Makuu ya wilaya, lakini pili, ndiyo roho ya uchumi wa Wanasingida Kaskazini; vitunguu, mafuta ya alizeti mnayoona, asali na maziwa yote, hii barabara ndiyo roho ya uchumi wao. Niombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa nipe majibu sahihi, vinginevyo hatutaelewana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara nyingine ya Ilongero – Ikhanoda – Ngamu; hii barabara iliua. Kuna daraja pale la mchepuko, maji yalizidi baada ya mvua kunyesha yakafunika daraja likajengwa daraja la dharura, daraja lile liliua mtu, sasa naomba daraja hili na lenyewe lijengwe. Tuhakikishe linainuliwa ili kuepusha vifo vinavyotokea kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ile ambayo niliisema kwenye swali la nyongeza ya Singida – Kinyeto – Sagara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani. Naomba hii barabara nayo ijengwe kwa kiwango cha lami.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja lakini Kiwanja cha Ndege cha Singida hakionekani kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba na chenyewe akisimama akisemee. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wa maandishi kama ifuatavyo kuhusu changamoto za kimaendeleo jimbo la Singida Kaskazini; kwanza tatizo la upungufu mkubwa wa watumishi katika Idara ya Elimu Msingi ina upungufu wa walimu 1097, Idara ya Elimu Sekondari ina upungufu wa walimu 151 na sekta ya afya ina upungufu wa watumishi 542.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utawala; Halmashauri ina upungufu watumishi 47; Watendaji wa Vijiji 24 kati ya 84 na Watendaji wa kata sita, jumla ni upungufu wa watumishi 2867.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kuwe na msawazo, Mikoa na Halmashauri zenye upungufu wa asilimia 50 na kuendelea zipewe kipaumbele katika kupatiwa watumishi. Halmashauri ya Wilaya ya Singida ni muhanga wa tatizo hili. Naomba sana ipatiwe watumishi hawa.

Pia naomba fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Ngimu ambapo boma lina miaka 14 sasa (boma lipo usawa wa linta). Pamoja na zahanati ya Pohama ambayo iko lenye linta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vifaatiba katika Hospitali ya Wilaya Ilongero na Vituo vya Afya Mgori na Msange. Pia ambulance nne kwa mchanganuo ufuatao; moja kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Ilongero, moja kwa ajili ya Kituo cha Afya Mgori, moja kwa ajili ya Kituo cha Afya Msange na moja kwa ajili ya Kituo cha Afya Makuro.

Kuhusu TARURA iendelee kuongezewa fedha katka Wilaya ya Singida DC iweze kujenga daraja la Mgori ambalo ni drift huuwa watu, daraja la Mpambaa na kuboresha barabara za makao makuu ya Wilaya na za miji midogo ya Ilongero, Ngamu, Msange na Mtinko.

Pia ni ushauri kuwa zabuni za barabara zitangazwe kuanzia mwezi aprili ili ziweze kutekelezwa wakati wa kiangazi (mwezi Julai hadi Novemba).

Mheshimiwa Mwenyekiti,napendekeza maslahi ya Madiwani yaboreshwe, walipwe mshahara wa kila mwezi usiopungua shilingi milioni moja. Pia walipwe posho za vikao kwa uwiano sawa kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri eneo la manunuzi liboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii angalau niwasemee wananchi wenzangu ambao kwa asilimia 95 ni wakulima katika Jimbo langu la Singida Kaskazini. Uhai wa wana Singida Kaskazini unategemea sana zao la alizeti, lakini kilimo hiki wamekuwa wakilima kwa jembe la mkono jambo ambalo limeshindwa kabisa kutuletea tija ya uzalishaji wa zao hili kama ambavyo ingeweza kuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa zao la alizeti kuanzia kupanda mpaka kuvuna ni miezi mitatu tu lakini mkulima anakosa kulima kiwango cha kutosha kwa sababu ya changamoto hasa hasa za vitendeakazi. Zana za kilimo, mbegu pamoja na mitaji. Nikuombe sana na niiombe Serikali, Wizara hii watuletee mbegu na mbegu hizi ziwe kwa bei ya chini ili wakulima waweze kumudu gharama. Haiwezekani kilo mbili ziuzwe shilingi 60,000 na zaidi halafu gunia moja lije liuzwe 50,000. Hii inamuumiza sana mkulima na inampotezea muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama haitoshi niombe sasa Serikali tuhakikishe kwamba tunaleta kilimo cha irrigation, cha umwagiliaji. Katika Jimbo la Singida Kaskazini mabwawa matatu yameungana imekuwa ziwa. Niombe sasa maji haya yatumike ipasavyo kwa kuleta miundombinu ya umwagiliaji ili vijana waliojitokeza waliohamasika kutumia maji haya walime hata wakati wa kiangazi. Bwawa la Masoqeda, Kisisi, yameungana yamekuwa ni ziwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana maji haya Serikali iyatumie ipasavyo kwa kuhakikisha vijana wanapelekewa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuongeza tija katika uzalishaji wa alizeti na hata viwanda vilivyopo pale viweze kupata raw materials ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasahivi viwanda vinakosa malighafi kwa sababu tunazalisha kwa kiwango kidogo sana na kwa mwaka huu alizeti haijalimwa kwa sababu ya kukosekana mbegu na bei kuwa ndogo. Kwa hiyo, watu wanaamua waende kwenye mazao mengine na kuachana na alizeti. Ndiyo maana mnaona mwaka huu mafuta yamepanda bei na yameadimika kabisa. Kwa hiyo, niombe sana eneo hili litazamwe kwa jicho tofauti sana. Nashukuru kwamba zao la alizeti limeingizwa kwenye yale mazao ya kimkakati, basi isiwe ni kwenye makarasha tu. Yaende kwenye utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongee kidogo kuhusu zao la kitunguu ambalo ndilo hasa sisi watu wa Singida tunalima kitunguu bila kutumia madawa. Ni kilimo cha asili kabisa, unapanda kitunguu, unavuna bila kutumia dawa. Kitunguu hiki hakijawekewa mkakati, ni mkulima mwenyewe anahangaika kwa nguvu zake binafsi, hakuna mkono wa Serikali hata kidogo. Sisi tunaishia tu kujivunia kwamba watu wanalima lakini hatuwasaidii. Tuhakikishe tunawapelekea hawa watu mbegu. Subsidies zipelekwe kwenye mbegu lakini pia tuwape vijana mitaji waweze kuongeza tija, waweze kuzalisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa spika, lakini hapo hapo eneo la masoko, soko la kitunguu lipo lakini shida ni utaratibu mbovu unaopatikana pale sokoni. Mkulima anapopeleka zao lake sokoni utaratibu ni mbovu anaishia kuteseka madalali wajanja wajanja.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, sasa ni vyema utaratibu mzuri uwekwe ili watu hawa nao wanufaike na kilimo chao hiki wanachoteseka nacho muda mrefu. (Makofi)

SPIKA: Ahsante.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa haya machache. Naunga mkono hoja lakini niiombe Serikali itusikie haya tunayoyazungumza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali ilitoa mwongozo kuwa shule za Serikali na binafsi zisitishe bweni kwa madarasa ya tano, nne hadi chekechea lakini hadi sasa kuna shule zimeendelea kulazimisha watoto wa madarasa haya kukaa bweni. Jambo hili linaleta mashaka na wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wetu hususan suala la maadili ambapo hivi sasa kuna ukatili mkubwa dhidi ya watoto wadogo hususan mashuleni. Natolea mfano wa Shule ya Msingi na Elimu ya Awali ya Ndameze iliyopo mkoani Kigoma. Ni vyema Serikali ifuatilie utekelezaji wa agizo ililotoa ili kulinda usalama wa watoto wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni upungufu wa watumishi hususan walimu na idara ya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Jimbo la Singida Kaskazini, upande wa walimu tuna upungufu wa walimu 900 na zaidi na upande wa afya tuna upungufu wa watumishi 316. Ni ombi kubwa kuwa katika ajira zilizotangazwa, Halmashauri ya Wilaya ya Singida nayo ipatiwe watumishi hawa, na upande wa utawala pia tunao upungufu mkubwa wa watendaji wa kata na vijiji.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine naomba fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa boma la Kituo cha Afya Ngimu ambalo limekaa miaka 14 sasa. Pia ukamilishaji wa jengo la OPD la Kituo cha Afya Kinyagigi ambapo wananchi wameshapaua, kilichobaki ni umaliziaji tu ambao makadirio ni shilingi milioni 100 tu. Aidha katika Hospitali ya Wilaya tunaomba kupatiwa standby generator ambalo litasaidia wakati umeme umekatika. Mara kadhaa umeme unapokuwa umekatika wagonjwa wamekuwa wakipata tabu hususan wanapojifungua na wale wanaohitaji kupumua kwa mashine.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipatia fursa hii angalau na mimi niwasemee wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusiana na suala hili muhimu sana la nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara na hasa Waziri Kalemani kwa usikivu wake mwingi sana tunapokuwa tuna mahitaji kwake, tukiwa na shida mbalimbali kwa kweli, amekuwa msikivu na anatusikia. Namuomba aendelee kuwa mnyenyekevu na asipandishe mabega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie mambo machache matatu makubwa, umeme wa REA, umeme wa upepo Mkoani Singida na ule umeme mkubwa unaotoka Namanga – Arusha – Singida. Kwa upande wa REA, kata zangu tano hadi sasa hazijaguswa kabisa na umeme hata nyumba moja zinakaa gizani, lakini unakuta kata imezungukwa, wamegusagusa kwenye centres za kata lakini maeneo ya jirani yameachwa.

Mheshimiwa Spika, mathalani Kata ya Ughandi yenye Vijiji vya Senenemfuru, Laghane, Damisinko, haijaguswa hata kidogo. Upande wa huku Msisi angalau wameguswaguswa upande wa Mashariki Ntinko, kuna baadhi ya maeneo yameguswa, lakini kata iko katikati kwa nini hata vijiji vya jirani visipate umeme?

Mheshimiwa Spika, Kata ya Itaja ambayo iko barabara kuu, Arusha Road, vijiji vyake hata kimoja havijapata umeme, lakini kuna vijiji vya jirani ambavyo vina umeme. Kwa nini sasa wasingekuwa wanaunganisha vijiji kulingana na jiografia?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Vijiji vya Ngimu, Bohama, Mbwighanji, Lamba, Kinyagigi, Makuro, Mkenge, Matumbo, Poku, Ghalunyangu, Mwalala, Migugu, Minyenye, Ikiu, Mwarufyu, Mdhae, Mwasauya, Sefunga, Ndwamoghanga, Unyampanda vipatiwe umeme. Nashukuru kwamba tumepatiwa huyu mkandarasi at least tunapata matumaini na wananchi wetu wanapata moyo, wamefurahi sana; nimewajulisha kwamba, tumepata mkandarasi sasa mtulie umeme unakuja utekelezaji basi uwe ni ule ambao tunautarajia. Naomba hawa wakandarasi wawasikilize viongozi wanapowaelekeza anzieni hapa, wawe wasikivu sio wawe miungu watu, watusikie tunapowaomba at least yale maeneo ya vipaumbele wayafanyie kazi. Naomba haya malalamiko sasa yasirudierudie tena kwa sababu umeme ndio maisha ya Watanzania, umeme ni uchumi. Tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda, utawezekanaje bila umeme? Vijana wetu wana shughuli mbalimbali zinazohitaji umeme, kuchomelea, kunyoa, watafanyaje hizi shughuli bila umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikirudi kwenye umeme wa upepo Mkoani Singida, mradi huu una miaka zaidi ya sita hivi sasa na mkandarasi alishaweka kila kitu chake pale field lakini hadi sasa ameshindwa kupewa go ahead ya kuendelea kutekeleza mradi huu na unapita katika vijiji nane vya jimbo langu. Niombe sasa Waziri atakapokuja hapa ku-wind up atupe commitment ya kuanza kwa mradi huu ili angalau wananchi wa vijiji vile nane wapate matumaini ya kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huu umeme mkubwa unaotoka Namanga – Arusha – Singida, una Kilowatt 2000 ni umeme mkubwa ambao ungeweza kuondoa kabisa tatizo la umeme nchini lakini hadi sasa hatujajua muendelezo wake unakuwaje. Kwa hiyo, niombe pia Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa atupe commitment kuhusu eneo hili ili tupate umeme kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nimuombe Mheshimiwa Waziri, mimi ninayeongea hapa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini nakaa gizani umeme hamna nyumbani kwangu, Waziri haoni aibu? Nimeshamueleza mara kadhaa, nimeshamueleza hata DG wa REA, Meneja wa Kanda hata wa mkoa wameshindwa kunisikiliza. Jamani, sasa kama Mbunge hasikilizwi mwananchi wa kijijini kule ataweza kusikilizwa? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza Benki ya Kilimo iweke kipaumbele kukopesha wafugaji hasa wadogo na wa kati.

Mheshimiwa Spika, Wizara na taasisi husika zilizo chini ya Wizara ziendelee kutenga maeneo ya kufugia na maeneo ya malisho, mifugo ni mingi kuliko rasilimali ardhi, malisho, maji, na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupata vitalu vya kufugia katika Ranchi za Taifa usiwe mgumu kama ilivyo sasa. Wizara iweke utaratibu rafiki kwa wananchi wanaohitaji vitalu wasipate vikwazo na vikatisha tamaa.

Mheshimiwa Spika, Serikali iweke ruzuku kujenga vituo vya maziwa na viwanda, kama inavyojenga masoko, stendi za mabasi, vituo vya afya, na kadhalika; kwa nini hawajengi vituo vya maziwa na viwanda?

Mheshimiwa Spika, wafugaji wa ng'ombe wa asili wako tayari kubadilika na wao kujaribu kufuga kisasa, shida ni upatikanaji wa ng'ombe bora wa maziwa ukitaka hata ng’ombe 100 utazunguka nchi nzima hupati, Serikali iwekeze zaidi kwenye uhimilishaji na kuagiza mitamba nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali ijenge masoko ya kuuzia maziwa au vituo vya kuuzia maziwa maana si salama kiafya, wauza maziwa wanapanga maziwa chini, pia Serikali inakosa mapato mengi kupitia utaratibu huu mbovu uliopo hivi sasa. Asilimia 90 ya maziwa yanayozalishwa nchini karibu lita bilioni nne kwa mwaka huuzwa katika mfumo usio rasmi na kuikosesha Serikali mapato. Tunaomba Serikali iwekeze kujenga mifumo na miundombinu ya kukusanya na kuuza maziwa mpaka vijijini kama ilivyo kwa sekta ya nyama kila kona kuna butchery.

Mheshimiwa Spika, Serikali iwekeze sana kwa vijana na wanawake ili sekta ikue na kuwa endelevu.

Pia Serikali itenge bajeti kubwa ya kuhamasisha kulima na kuhifadhi malisho na maji kwani bila kufanya hivyo wafugaji wataendelea kuhamahama kwa kufuata yalipo malisho na maji na kuendelea kuharibu mazingira. Tupeleke mashamba darasa kila kijiji kuhusu majani ya malisho ya ng’ombe kuepuka ufugaji wa kuhama hama.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ambayo ipo mbele yetu. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kuwa uwasilishaji mzuri na pia hata Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Kawawa, naye amewasilisha vizuri na kimsingi taarifa hiyo imesheheni na mawazo yaliyopo kwenye taarifa ile kwakweli hata sisi kama Kamati tuliyajadili na tumeyaafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninasimama hapa kutoa mchango wa ziada kuhusu hoja hii ya Azimio la kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika ya Kuzuia na Kupambana na Tatizo la Ugaidi Duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo mimi nataka kulisema, la kwanza kabisa ni umuhimu wa maisha, umuhimu wa uhai ambao Mwenyezi Mungu ametuzawadia. Hatupaswi kabisa ku-compromise na uhai ambao ni zawadi pekee tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Sasa tunapoona mtu anacheza au anafanya utani au anachezea maisha ya mwanadamu asiyekuwa na hatia hakuna mtu hata mmoja atakayefurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, Azimio hili ama Itifaki hii lengo lake ni kwenda kuhakikisha linalinda uhai wa mwanadamu. Na hasa sisi watanzania ambao tumekuwa ni nchi ya amani kwa kipindi kirefu, kisiwa cha amani, sasa yanapokuja matukio kama haya ya ugaidi yanaondoa kabisa ile heshima ya uhali ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwanza niwaombe Wabunge wenzangu waunge mkono hoja hii, waunge mkono Itifaki hii iweze kuridhiwa ili sasa nchi yetu iweze kuhakikisha inanufaika na zile faida ambazo wenzangu wanazisema zinazotokana na Itifaki hii. Na kimsingi Itifaki hii imeshasainiwa na nchi nyingi. Nchi zipatazo 45 zimesaini ikiwemo Tanzania na nchi 21 zimeridhia. Kwa hiyo, sisi sasa tunaenda kuwa nchi zaidi ya 22 ambazo tayari zimesharidhia- adopt hii Itifaki kwa lengo la kuhakikisha tunabadilishana uzoefu, tunabadilishana taarifa kama ambavyo wenzangu wamesema katika kupambana na tatizo hili la ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunavyofahamu panapokosekana amani hata shughuli za kibinadamu za kiuchumi hazifanyiki. Huwezi Kwenda kufanya kazi huku ukiwa na mashaka ukiwa huna uhakika na uzima na usalama wa mazingira uliyonayo. Ndiyo maana kuna watu hapa akiona mende ana mashaka hawezi tena hata kutoka, anakuwa na wasiwasi sasa hapa tunazungumzia suala la ugaidi adui ambaye humuoni, hujui ni wakati gani atatekeleza tukio. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuhakikishe tunaliridhia azimio hili ili tuweze kunufaika na faida zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kwenda kuridhia Itifaki hii itaisaidia nchi yetu kuhakikisha inachukua hatua za lazima za haki za msingi za binadamu dhidi ya vitendo hivi vya kigaidi. Vilevile itasaidia kuhakikisha nchi yetu inazuia uingiaji na utoaji wa mafunzo kwa vitendo vya kigaidi ama vikundi vya kigaidi vinavyojihusisha na haya masuala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo inaenda kuipa nchi yetu sasa nguvu, tena kwa kushirikiana na nchi zingine, kupambana na vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na matendo ya kigaidi. Pia itasaidia kuainisha, kutambua na kuzuia ama kukamata fedha na mali zinazotumika katika masuala haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi, kama tunavyofahamu, mwenzangu mmoja amesema ni organized crime. Ni watu ambao wameungana. Kwa hiyo, inawezekana nchi ziko sehemu nyingine, Ulaya na kadhalika, zinakuja huku kwa njia zisizofaa, kuja kutumika kigaidi. Kwa hiyo, hii itifaki inakwenda kusaidia katika kuzuia fedha haramu za namna hiyo ambazo zinakuja kuhatarisha maisha yetu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kusisitiza na kuwaomba Wabunge wenzangu, tuone umuhimu wa itifaki hii na kuhakikisha tunaungana kwa pamoja, tunairidhia ili iende kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itasaidia kuanzisha pia vituo vya Kitaifa ndani ya nchi yetu kwa ajili ya kubadilishana na kupeana taarifa za makundi ya kigaidi kwa wakati na shughuli za kigaidi katika ngazi za kikanda na hata Kimataifa. Kwa hiyo, tufahamu kwamba inawezekana kuna taarifa zimepatikana nchi fulani au eneo fulani, sisi hatuna, lakini taarifa hizo zinataka kuathiri nchi yetu, kwa hiyo, sasa tunakwenda kupata uhuru ule ama uwezekano rahisi wa kupata taarifa kutoka sehemu nyingine ambazo zingekuja kutuathiri sisi huku nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo hili in a nutshell ukizungumzia faida mahususi za itifaki hii, kwanza ni kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na kuwepo kwa amani na usalama. Kama ambavyo tumesema kule mwanzo kwamba jambo la kwanza ni amani na usalama katika nchi yetu. Sasa panapokuwa na usalama, ndipo shughuli za kibiashara na za kiuchumi zitafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna uwekezaji tunaoweza kupata kama nchi yetu ina viashiria vya ugaidi ambavyo tulishawahi kuona hata huko nyuma. Watalii hawawezi kuja. Kukishakuwa tu na taarifa zozote kuhusiana na masuala ya ugaidi, watalii hawawezi tena kuja. Kwa hiyo, hii sasa inakwenda kutuwekea uhakika wa utalii na hata wageni na wawekezaji wa sekta mbalimbali katika nchi yetu katika kuhakikisha tunaimarisha uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia ushirikiano, itaipa nchi yetu uwezo wa kushirikiana na nchi wanachama katika kulinda amani na usalama. Hii ndiyo ambayo tunasema inaenda kuhakikisha uhai ama kulinda mali za watu pamoja na maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nalo ni la muhimu ni kuhakikisha tunakwenda kubadilishana utaalam na masuala ya misaada ya kiufundi. Sisi tuna limitation, kuna wenzetu wengine ambao wame-advance, kwa hiyo, tunaporidhia hili, ina maana tunaenda kushirikiana na wenzetu wengine ambao wame-advance, wana utaalam na pia ufundi uliopo ili tuweze kushirikiana, tuutumie katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nasema hii inaenda kuisaidia nchi yetu; kama unavyofahamu, kumekuwa na taarifa nyingi kwamba kuna watu wanasema watuhumiwa wengi wa ugaidi wanakamatwa, wanakaa muda mrefu magerezani, wanashikiliwa, wanateswa. Kwa hiyo, hii pia inakwenda kutusaidia, na nchi inakwenda kupata namna ya ku-deal na zile kesi za watuhumiwa wa masuala ya ugaidi kwa urahisi. Badala ya kukaa muda mrefu magerezani, hii inakwenda kutusaidia pia katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa. Pia hata kuwarudisha wale walioko nje, walioko Tanzania wa nchi nyingine waende kwenye nchi zao, Watanzania walioko nje warudishwe kwa ajili ya kufuata taratibu za kisheria ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kuridhia itifaki hii kwa pamoja ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama na inaepukana na masuala haya ya kuishi kwa hofu na mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Nami nichukue fursa hii kwanza kwa kuanza kuwatakia heri Waislam wote ambao wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, na niombe kwa Mwenyezi Mungu atupokelee funga zetu na dua zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kupongeza uwasilishaji mzuri wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini pia niwapongeze vijana wenzangu hawa; Waziri pamoja na Manaibu Waziri wote wawili. Ni vijana wachapa kazi, nami nasema upele umepata mkunaji. Kazi kubwa kwenu ni kuingia field, kutokukaa ofisini, njooni mtukute kule Singida Kaskazini mwone kazi nzuri tunayoendelea kuichapa kule ambapo kimsingi inatokana na uwezeshaji ambao nyie mnaoufanya huku Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima ya kipekee naomba nichukue fursa hii kuwasilisha shukrani na pongezi nyingi za wana Jimbo la Singida Kaskazini kwa fedha nyingi walizoletewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi wa yale mabilioni tuliyosema ya Mheshimiwa Samia. Nashangaa watu wanasema fedha za UVIKO; zile siyo fedha za UVIKO, yale ni mabilioni ya Mheshimiwa Samia. Naomba hilo lirekebishwe. Tumepata fedha nyingi ambazo zimetuwezesha kujenga madarasa 67, Shule Shikizi pamoja na Sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza mwaka huu, wanafunzi wote wameripoti shule kwa awamu moja, tena wakiwa wamekaa kwenye madawati. Tumepata madawati zaidi ya 2,500, sasa haya kwa mwaka huu hata wazazi wamehamasika kuwapeleka watoto wao shuleni. Maana watu walikuwa wanahamasisha watoto wasiende shule. Mtoto anafaulu lakini anaambiwa asiende shule kwa sababu mzazi anabanwa kwenye michango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu, kwa haya mabilioni ya Mheshimiwa Samia, kwa kweli tunapaswa tumpongeze sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa matrilioni ya fedha. Kwa mazingira haya, wananchi wa Singida Kaskazini wameniomba nije hapa na zawadi kwa Mheshimiwa Rais. Wamesema wanampa Rais zawadi ya dumu 10 za asali; wanampa dumu 10 za mafuta ya alizeti; lakini wanampa na kuku wa kienyeji 50 wa Singida ili wakati anakunywa supu hii ya kuku wa kienyeji, huku anawafikiria kuwaletea zaidi na zaidi ili kuhakikisha wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitaje mambo machache ambayo yamefanyika pamoja na hayo madarasa. Tumepata fedha kwa ajili kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambayo tumepata fedha kwa ajili ya ICU na vifaa vingine muhimu. Mimi hili nimelitazama kwa heshima ya kipekee na ndiyo nasema sasa hapa kuna umuhimu wa kuunga mkono juhudi hizi ili tuendelee kuwatumikia wananchi wetu ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha kwa ajili ya shule sekondari mpya shilingi milioni 470, Kata ya Kinyeto katika Kijiji cha Mkimbii, hili linaenda kukomboa watoto wetu ambao walikuwa wanakosa elimu kwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, kwenye barabara tumepata mamilioni ya fedha. Kwa mara ya kwanza tumepata bajeti mara tatu ya kawaida, tulikuwa tunapata shilingi milioni 600; mwaka huu wa fedha tumepata shilingi bilioni 2.2. Sasa barabara zinatengenezwa na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kidogo kwamba, kuna madaraja mawili yanakula watu kila mwaka. Kuna daraja la Mgori na daraja la Pambaa. Madaraja haya naomba yafanyiwe kazi, yajengwe, yanyanyuliwe; wametengeneza zile drift, sasa maji yanapopita juu; juzi hapa katikati daraja la Mgori, mama wa watu amekwenda kujifungulia pale darajani, maana alishindwa kuvuka wakati anakwenda hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana jambo hili lifanyiwe kazi, tuhakikishe miundombinu yetu ya barabara inakaa vizuri na haya madaraja yakanyanyuliwe. Hapo hapo kwenye barabara, kuna suala hili la barabara za Miji Midogo pamoja na Makao Makuu ya Halmashauri za Wilaya. Serikali hii imetuletea shilingi bilioni mbili na mamilioni mengine mengi kujenga jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumepata fedha nyingi sana, lakini barabara zake zile ni mbaya na pia tunahitaji tuboreshe miundombinu zaidi. Hatuwezi kuwa na jengo zuri lakini barabara ni mbaya. Kwa hiyo, naomba sana Mawaziri waje watujengee mbiundombinu ya barabara katika hii Miji Midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la Madiwani linalozungumzwa hapa. Posho kwa ajili ya Madiwani; Diwani ndiyo kiungo, ndiyo msimamizi wa mamilioni haya tunayoyazungumza, shilingi trilioni 1.3, Msimamizi Mkuu alikuwa ni Diwani kule chini. Sasa unakuja kumpa posho ya shilingi 300,000; hivi nikikupa wewe Mwenyekiti hapo, itachukua hata masaa mawili bado ipo mfukoni? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, bajeti hii iwe ni mkombozi wa Mheshimiwa Diwani. Yeye anasimamia wataalam, wana mamilioni ya fedha wanalipwa. Wataalam kwa kiwango cha chini wana Degrees ambapo unakuta mshahara wake ni shilingi 700,000; shilingi milioni moja na kuendelea. Diwani analipwa posho ya shilingi 300,000; anaweza kumsimamia mtaalam huyu? Hebu tuache utani kwenye hili eneo. Mheshimiwa Waziri, usipoangalia katika hili, nitashika shilingi yako, tumkomboe Diwani. Tutunze heshima ya hawa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kwa heshima ya kipekee, kwenye eneo la afya, nashukuru sana tumepata Vituo vya Afya viwili vinavyofanya kazi, lakini kuna Kituo cha Afya ambacho tumepata kile cha Makuro. Naomba sasa tupate vifaa tiba. Hospitali ya Wilaya ile nzuri tuliyoipata, Wilaya ya Ilongero, haina vifaa tiba, haijaanza kufanya kazi; ya Msange hakuna vifaa tiba, Mgori hakuna vifaa tiba. Hata hii Makuro tunayoikamilisha sasa, haina vifaa tiba. Naomba sana tupate vifaa tiba ili angalau sasa isiwe ni white elephants, zianze kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hapo hapo, nawasilisha ombi sasa kwa Mheshimiwa Waziri. Kuna boma la Kituo cha Afya cha Ngimu, lina miaka 14 sasa, ni boma karibu limechakaa. Nakuomba sana sana, mwaka huu katika bajeti hii nione ukiniletea fedha kwa ajili ya kukamilisha lile boma la Kituo cha Afya lililokaa miaka na miaka halijapauliwa pamoja na lile la Kohama. Yamekaa miaka nenda rudi, wananchi wamejitolea kwa kuuza kuku wao, lakini sisi tumeshindwa kuwapokea, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri kwa heshima kubwa sana ulitazame hili kwa heshima ya kipekee na uniletee fedha Mheshimiwa na uje wewe mwenyewe uone ile hali ilivyo, jinsi wananchi wanavyopata taabu kule mabondeni kwenye bonde la ufa, wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya Mheshimiwa Waziri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekwisha! Ahsante sana, naunga mkono hoja. Ila upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ni mkubwa sana, hasa walimu, sekta ya afya na utawala. Naomba pia mnitazame kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa angalau na mimi kuwasemea wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya. Pia nitangulize shukrani zangu nyingi sana kwa Waziri wetu Pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifana kuhakikisha nchi yetu inapata maji. Na hapa lazima tutambue juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kusema kweli hata ukifuatilia hotuba yangu yam waka jana kwenye wizara nilikuwa mkali sana na nilisikitika kwa ile hali ya wananchi wetu kunywa maji pamoja na Wanyama. Lakini mwaka huu nitakwenda kuzungumza kwa kutoa shukrani na pongezi kwa kazi kubwa ambayo imefanyika kwa kipindi hiki kifupi cha miaka hii miwili au huu mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Singida Kaskazini tumepata miradi mipya yam aji 15 ambayo inatafikisha asilimia 67 ya upatikanaji wa maji endapo miradi itakamilika ipasavyo, ambapo tumepata visima 15 vyenye thamani ya shilingi milioni 420 kila kimoja katika Kijiji cha Ntondo, Kwae, Sekotoure, Kinyamwenda, Msikii, Mwalala, Poku, Igauri, Mwakiti, Itamka, Mkenge, Makuro, Misinko, Msimihi na Maghandi. Maeneo haya sasa yanaenda ya kupata uponyaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nichukue fursa hii pia kuwapongeza watendaji wa Wizara ya Maji, kwa maana ya RUWASA pale Mkoani. Meneja wa Mkoa pamoja na Meneja wa Wilaya pamoja na staff wao kwakweli wanatupa ushirikiano sana katika kuhakikisha jamii yaw ana Singida inapata maji safi na salama wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru pia wadau wa Sekta Binafsi wanaoshirikiana na Serikali kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji, wakiwemo World Save International, World Division pamoja Silver Crescense ya kutoka Uturuki ambao wametusaidia kukarabati na kuchimba visima vipya vipatavyo 44 katika vijiji mbalimbali vya Jimbo letu la Singida Kaskazini. Kwa hiyo, ninaendelea kuwashukuru na kuwaomba waendelee kutupa ushirikiano kuhakikisha kila mtu katika Jimbo letu la Singida Kaskazini anapata maji safi na salama wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende kwenye kuwasilisha changamoto chache ambazo ninaomba sana Mheshimiwa Waziri azingatie na kuhakikisha tunazipatia ufumbuzi ili tuendane na hii kasi ambayo nimeizungumza hapa tunayoitarajia, ya kupata maji safi. Moja ya changamoto kuna vijiji ambavyo tuliwahi kuchimba maji lakini kwakweli maji haya yanapatikana ya chumvi na si salama kwa binadamu. Kwa hiyo, maeneo yale yanahitaji tupeleke bomba. Mojawapo ni kijiji cha Gaiye kitongoji cha Gairu katika kijiji cha Sagara pamoja na kijiji cha Mangida tumechimba visima kadhaa lakini maji hayakupatikana. Kwa hiyo maeneo haya nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tuende tukafanye usambazi kutoka kwenye kile chanzo cha Sagara ambacho kina maji ya kutosha; lakini tu hatujatandika mabomba niombe sana tufanye usambazaji tuwapelekee hawa wananchi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siku nilienda kuomba kura pale walinipa maji ya chumvi. Tafsiri yake ni kwamba yale maji kama yanafaa nami niyanywe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikukaribishe siku moja na wewe uje haya maji uone kwamba kuna shida. Kwa hiyo, nikuombe ushirikiano tuwasambazie maji na wala si umbali mrefu ni kama kilometa moja tu ambayo wala si gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nimetaja miradi mikubwa sana ya maji hapa, nikiacha ile minne ambayo tayari imeshakamilika. Ule mradi wa Wamitura ambao una thamani wa Shilingi milioni 565 kuna ule mradi wa Mweghanji shilingi milioni 565, ule mradi wa Ndibeshi Shilingi 565. Miradi hii ina gharama kubwa lakini changamoto kubwa ipo kwenye usimamizi. Idara yetu ya RUWASA hawana vitendea kazi hata gari hawana. Unampa mtu mradi wa shilingi billions of money lakini namna ya kuusimamia kufika pale kwenye field hawana uwezo huo kwasababu ya vitendea kazi.

Niombe sana tuwasaidie hawa watu wapate magari, wapate vitendea kazi ili waweze kufika kwenye maeneo ya kazi kwa wakati na kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na eneo la jumuiya za watumia maji amezungumza Mbunge dakika mbili tatu zilizopita kuhusu uwezo mdogo alionao wakifedha hata kitaalamu. Tunategeneza miradi ya kutosha ya fedha nyingi lakini kwenye eneo la uendeshaji tunakwama. Niombe wale watalamu wawili mhasibu pamoja na fundi hawa wawe ni waajiriwa wa Serikali pamoja na fundi hawa wawe ni waajiriwa wa Serikali na walipwe na Serikali ili tuweze kuwa- manage, na tuweze kuwafuatilia na kuwasimamia ipasavyo. Hii itasaidia kwenye ufanisi kwa maana ya efficiency ya hii miradi pamoja na kudumu iweze kudumu ili kuendelea kuwahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningeomba pia Wizara wanisaidie, hasa Mheshimiwa Waziri ni kwenye kuongeza upanuzi wa miradi. Hii miradi ambayo nimeitaja hapa kumi na tano ni miradi minne tu ambayo itafanyiwa usambazaji. Niombe sana hii miradi iongezewe fedha ili tuweze kufanya upanuzi hata yale maeneo mengine ambayo hayajafikiwa tunaweza tukayafikia kwa kufanya upanuzi, kwa maana ya kuweka mtandao wa bomba kwenye maeneo ambayo hayana maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kuna vijiji ambavyo tumeomba kwa Next budget vijiji ambavyo vinashinda kubwa sana ya maji na havina mradi wowote kijiji cha Semfuru, Ndugwira, Ikiu, Kibaoni na kule Mukulu Mheshimiwa Waziri ulifika siku ile ulivyokuja tuliwaahidi wananchi na walifurahi sana. Kwanza ujio wako pale ulipokuja walifurahi na ulivyowaahidi maji kwakweli walifurahi zaidi. Sasa wameendelea kunikumbusha Bwana Mheshimiwa Waziri alituahidi kisima hapa vipi? Kwa hiyo, sasa niwasilishe tena ombi hili kwako Mheshimiwa Waziri angalau basi nawao wapate maji yale siku ukienda sasa tuyanywe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kuwasilisha hili lakini pia kwenye maeneo kuna miradi ambayo tayari inafanya kazi mathalani mradi wa maji pale mji mdogo wa Ilongero ambao ndiyo makao makuu ya halmashauri. Ule mradi ni wa muda mrefu unachanzo cha uhakika cha maji, lakini shida ni maji yale yapo maeneo machache hata maeneo ya karibu tu hayapati maji. Kwa hiyo, niombe tufanye upanuzi kwa kuongeza miundo mbinu kama vile kujenga matanki pamoja na mabomba ili wananchi wapate maji ipasavyo. Pale vilevile kuna watumishi wa Serikali wanakwenda makazini asubuhi wanarudi wamechoka wanahitaji wapate maji salama na yakutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana mradi huu wa Ilongero pamoja na ule wa Mji mdogo wa Ngamu ifanyiwe upanuzi wa kutosha ili wananchi wengi wapate maji; kwa sababu pengine inaweza ikatupunguzia hata adha ya kuhangaika kuchimba visima vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niombe pia, kwenye hizi jumuiya za watumia maji kuna shida moja ambayo naiona, kwamba hawa wananchi wale wakata risiti wale wanatumia zile risiti za mkono stakabadhi ni vyema wangekuwa na zile EFD Machines ambazo kwanza zitaepusha upotevu wa fedha lakini pia zitasaidia hata kufuatilia mapato yanayopatikana ambapo wakati mwingine miradi hii inaharibika tunashindwa kuikarabati. Kwa hiyo, niombe sasa ni vyema watu hawa wapatiwe EFD machine kwaajili ya kuhakikisha tunadhibiti mapato yanayopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya mimi niwasilishe sana taarifa yangu hii lakini niendelee kuiomba Wizara kuhakikisha kwamba hii miradi ambayo wameahidi kututekelezea mwaka huu ichimbwe kwa wakati na fedha zije kwa wakati ili next time nikija hapa Mheshimiwa Waziri tuwe tunapongezana tu si kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nishukuru sana, niwasilishe hotuba yangu. Ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ramadhani Ighondo Abeid.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa angalau nitoe na mimi mchango wangu katika hii sekta muhimu ya kilimo na pia niwasemee wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini ambao kwa asilimia kubwa wanategemea kilimo katika maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kutoa pongezi na shukrani nyingi sana kwa Waziri wa Kilimo pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutoa angalau bajeti ya shilingi bilioni 751 kwa ajili ya kilimo. Hii ni hatua kubwa lakini hatua ya pili ni utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa hatua yake ya kufika Jimboni kwangu Singida Kaskazini. Mheshimiwa Waziri alifika katika bonde kubwa na zuri sana la umwagiliaji pale Msange, akaenda Mughamu na akatuahidi kwamba sasa tutakwenda kupona kwa kutuletea mradi mkubwa wa umwagiliaji katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, project ile tayari imeshafika hatua kubwa ya feasibility study survey na bwawa pamoja na eneo lenyewe la mradi liko tayari kwa maana ya mashamba, kikubwa sasa tunachosubiri ni fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ile kazi iweze kuanza. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aendelee kulimulikia macho kwa karibu sana eneo lile ili kuwakomboa ndugu zako wale wa Singida Kaskazini ambao walifurahi sana siku ile ulipokuja wakaona kabisa kwamba upele sasa umepata mkunaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo na pamoja na ujio wa Mheshimiwa Waziri alienda kwenye maeneo machache sana mawili tu ya umwagiliaji katika Jimbo la Singida Kaskazini, lakini yako maeneo mengine ambayo tungependa sana afike ili aje aone na kutupa moyo aweze kuwahamasisha Wanasingida Kaskazini kwa kilimo cha umwagiliaji. Kuna maeneo kama vile Mtambuko mabwawa makubwa yana maji muda wote wa mwaka, lakini hayatumiki ipasavyo kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Bwawa la Masoweda, Kisisi kuna Mikuyu na Endeshi, maeneo haya ninaomba sana nimuombe Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla wayamulike eneo la Mkoa wa Singida kwa kiwango kikubwa ni kame, lakini tumepata baraka hii ya water bodies ambazo yapo muda wote. Niombe sana maeneo haya yatazamwe ili yaweze kuwasaidia na kuwakomboa wananchi wetu ambao kwa kiwango kikubwa wanategemea kilimo, lakini kilimo chenyewe siyo cha uhakika kwa sababu wanategemea mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo niipongeze tena Wizara na hasa Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea mbegu hizi za kisasa za alizeti. Tunaipongeza sana Serikali na ni hatua nzuri lakini kwa upande wa Mkoa wa Singida mbegu hizi hazijafanya vizuri sana kwa sababu ya mvua. Mbegu zimekuwa za bei nzuri lakini sasa mvua imetuangusha ndiyo maana nasisitiza kwenye eneo la umwagiliaji ili hizi mbegu ambazo tumepewa kutoka shilingi 35,000 kwa kilo sasa hivi ni shilingi 3,500 lakini hazijaweza kutusaidia sana kwa sababu ya kukosekana mvua ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisisitize kwenye hizi mbegu ufanyike utafiti sasa tupate mbegu zinazohimili ukame, zinazochukua muda mfupi na zinazotoa mazao mengi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia pembejeo zingine, tumepata mbegu nashukuru na naendelea kuomba huu mpango uendelee na uboreshwe. Lakini kwenye eneo la pembejeo ninaomba sasa tujielekeze kwenye mbolea. Mbolea hivi sasa mathalani Urea mfuko mmoja ambao ulikuwa unauzwa shilingi 60,000 leo unauzwa shilingi 110,000; DAP ambayo ilikuwa inauzwa shilingi 75,000 leo inauzwa shilingi 110,000 ni gharama kubwa sana kwa mkulima hii. Haiwezi kumsaidia na hatuwezi kuwakomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali iweke ruzuku kwenye mbolea na pembejeo zingine za kilimo, madawa mengine, viuatilifu lakini pia hata matrekta leo tumeona jeshi la kilimo hapa Bungeni wamepewa pikipiki, wamepewa mpaka vishikwambi, lakini mkulima anatumia jembe la mkono. Haiendani, tunataka hivi vitu viende sambamba tumboreshee mazingira mtendaji kwa maana ya mtumishi, msimamizi lakini hata mkulima naye pia tumtazame, tumboreshee mazingira yake ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, sana, sana tuhakikishe tunaondoka kwenye jembe la mkono, jembe la asili ambalo halijatupa tija tangu tumepata Uhuru tunalima na jembe la mkono mpaka leo tunalalamika njaa, tunalalamika hatutoshelezi kwenye uzalishaji ni kwa sababu hatujawekeza ipasavyo kwa mkulima. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekuacha, lakini malizia.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, niombe sana kwenye eneo la upungufu wa watumishi hasa Maafisa Kilimo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini tunavyo vijiji 84, kata 21 lakini tuna Maafisa Ugani na Kilimo ni 13 tu. Kwa hiyo, niombe sana vijiji vingi havina Watendaji, havina Maafisa Ugani hawa, wataalam kwa hiyo, wakulima wanajilimia hawana mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, ninayo mengi na nitayawasilisha mengine kwa maandishi. Niombe sana Wizara hii next time iongezewe muda. Muda wa dakika tano hizi hatuwezi kuishauri Serikari ipasavyo, tutaishia kupitiapitia tu juu juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninashukuru sana na ninaunga mkono na ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi nichangie katika mjadala huu wa Wizara ya TAMISEMI.

Kwanza, nami nichukue fursa hii kwanza kupongeza utendaji mzuri wa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake Naibu Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu na Makatibu Wakuu, kwa kweli tunayo imani kubwa na tunawaomba waendelee na moyo huo wa utendaji mzuri ambao tunauona. Vilevile pia nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambae kwa kiwango kikubwa anatuheshimisha bajeti hizi kwa kipindi hiki akiwa madarakani miaka miwili sasa, tunaona jinsi ambavyo zinaelekea kwenye maisha halisi ya mwananchi, kwenye maeneo ambayo ndiyo tunamkuta Mtanzania, kwenye elimu, afya, kwenye barabara ndiko tunako mkuta mwananchi halisi wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kuwapongeza Waislam wa Mkoa wa Singida ambao jana walifanya maandamano kupinga suala la zima la mmong’onyoko wa maadili hapa nchini, ambayo hivi sasa tunaona kuna nia ovyo inayofanywa na baadhi ya watu kutaka kuteketeza kizazi, kuteketeza maisha ya mwananchi au maisha ya binadamu ambayo ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nawapongeza sana Waislam wale wa Mkoa wa Singida pamoja na Viongozi wa Dini kwa ujumla hapa nchini hata Mkoa wa Singida Maaskofu nao wametoa matamko na wamesema kwenye maeneo yao, nawaomba waendelee na moyo huo na wasiache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Spika, ambaye pia alitoa mwongozo kuhusu suala hili hapa nchini na naomba Serikali ichukue hatua wasibaki kujitafuna na kumung’unya maneno wakati tayari wanayo mamlaka ya kushughulika na tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upande wa eneo la afya kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini. Kwa nafasi ya kipekee sana nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwa fedha nyingi ambazo ametupa kwenye eneo la afya kwenye Jimbo la Singida Kaskazini. Tunayo Hospitali ya Wilaya na sasa ina vifaatiba na kazi inaendelea kufanyika, pia tunavyo Vituo vya Afya, Kituo cha Afya cha Makuro nacho kimeanza kufanya kazi Tarehe 03 Machi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa kwa kipindi hiki kifupi tumeshajenga zahanati Tisa na baadhi zinafanyakazi ikiwemo ya Mwachambia, Unyampanda pamoja na zahanati ya Mwakichenche. Ninaipongeza Serikali kwa eneo hili, ninaomba bado ninayo maeneo ya changamoto kuna Boma la Kituo cha Afya pale Ngimu, hili boma lina miaka 14 sasa, ameishafika Katibu Mkuu wa CCM ameona na amepita pia Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa ameona na alitoa machozi baada ya kuona nguvu kazi za wananchi zimepotea kwa muda mrefu lakini Serikali haijawapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na timu yake walione hili. Eneo lile ni tense liko kwenye mazingira magumu ya Bonde la Ufa wananchi wanateseka kupanda Milima kufuata huduma za afya mbali. Naomba Serikali iwapokee wananchi hawa, iwaokoe mama zetu wanaoteseka wakati wa kujifungua. Watoto wanaohangaika na huduma za afya pamoja na Wazee wasiyoweza kutembea, niombe sana Serikali ilichukue hili na nione kwenye bajeti hii fedha zije zijenge Boma lile la Kituo cha Afya (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kituo cha Afya Kinyagigi nalo naomba fedha pamoja na boma la zahanati pale Sagara naomba nako fedha zije pamoja na Mwakichenche pale Minyenye. Eneo hili la afya ninaiomba Serikali itupatie ambulance, kuna umuhimu mkubwa sana tupate ambulance kwa sababu maeneo haya kama nilivyosema tumepata zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ya Wilaya hakuna ambulance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye eneo la TARURA ninashukuru sana kwa fedha ambazo zimekuja kwenye eneo la barabara mpaka sasa tunapokea Shilingi Biloni 2.2 kwenye miundombinu ya barabara upande wa TARURA. Ninaomba fedha ziendelee kuja na TARURA iendelee kuongezewa fedha lakini na wao waendelee kuboresha madaraja, waendelee kuboresha mitaro ile ya kutiririsha maji, wafanye kazi kwa ufanisi value for money tunataka tuone fedha zinazokuja zifanyiwe kazi ipasavyo ili kuondokana na kero ambayo wananchi wamekuwa wakiipata kwenye eneo la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili specific naomba nizungumzie ile barabara inayotoka pale njia panda Mgori kwenda Mughunga mpaka Mukulu, Nduamughanga barabara kipande cha kilomita 25 kutoka Nduamughanga kwenda Mukulu ambapo ndiyo tunakutana na Wilaya Chemba, eneo lile ni baya, lina madaraja Saba ni eneo fupi sana kilomita 25 lakini ni maporomoko, mito naomba sana barabara hii ipate fedha za ziada mwaka huu ili iweze kutengenezwa na madaraja yale yaweze kuimarishwa ili kuwaunganisha wananchi wale na wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie maeneo ya Miji yanayokua. Mji wa Ilongero ambapo ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri hakuna barabara hata kidogo, niombe sasa tupatiwe fedha kwa ajili ya kuboresha barabara za ule Mji ili uweze kuwahudumia wananchi ipasavyo wanaotoka Kanda zote za Wilaya ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe madaraja mahusisi, daraja la Mpambano nashukuru limepatiwa fedha Shilingi Milioni 650 kupitia ule mapango wa Mama wa World Bank lakini sasa niombe fedha kwenye daraja la Mgori, daraja lile limekuwa likiua watu, wananchi wamekuwa wakizama pale na limekuwa likikata mawasiliano ya wananchi hasa wakati wa mvua. Niombe sasa tupatiwe fedha na kwenyewe tukalijenge lile daraja. Kama haitoshi daraja lile la pale linalounganisha Minyaa na Mwanyonye daraja lile ni baya limekuwa likitutesa, naomba nako tupatiwe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu ninashukuru kwa fedha za mradi wa BOOST shule mbili za msingi tumepata lakini niombe sasa ujenzi wa nyumba za Walimu pamoja na vyumba vya madarasa lakini na madawati. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abeid, muda wako umeisha ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana ninaunga mkono hoja lakini naomba next time mtupe muda wa kutosha angalau dakika kumi na kuendelea. Ahsante sana. (Makofi
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia katika mjadala wetu huu muhimu wa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwanza kwa kuwapongeza Watendaji wa Wizara hii kwa kuanza na Mheshimiwa Waziri ambaye kwanza amepewa majukumu haya kwa muda mfupi uliopita, nadhani haizidi hata mwenzi mmoja lakini anaonekana kuyamudu vizuri majukumu yake na hata hotuba yake ilikuwa nzuri pamoja na Naibu wake pia ni kijana mwenzetu tuna imani naye, kwa hiyo tunawatakia kila la kheri kwenye utendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Katibu Mkuu wa Wizara naye ni kijana mwenzetu, tunaamini kwamba kwa upya wao huo, tunatarajia mambo mengi mazuri yanaenda kutekelezeka kwa maana ya kwamba utakuwa ni utumishi usiozingatia mazoea, siyo utumishi unaofanya kazi kwa mazoea, tunataka creativity tunataka tunaone mambo mapya tunayoyazungumza hapa yanafanyiwa kazi na tunataka tuone mabadiliko, waboreshe utumishi, waboreshe utendaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo kubwa moja ambalo lilikuwa kwenye moyo wangu kuhusu mafao kwa wastaafu hasa hasa kwenye eneo la kikokotoo. Ninamshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambae aliridhia kikokotoo hiki kutoka kwenye asilimia 25 kwenda kwenye asilimia 33. Jambo hili bado lina manung’uniko kwenye eneo la utekelezaji, watumishi hasa wastaafu bado wana malalamiko kwenye kiwango wanachopewa cha mafao lakini pia kumekuwa na usumbufu mkubwa baada ya kuunganisha ile mifuko ya jamii liliyokuwa mitano kwenda kwenye mfuko mmoja uliobaki, hivi sasa kumekuwa na malalamiko mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi anakwenda pale ile filling system ya taarifa zake ni mbovu, anaambiwa wewe ulikuwa LAPF sisi PSSF hatuna taarifa zako, anakwenda anaambiwa nenda rudi, hivi na ni watu wazima wazee tunaotarajia waheshimike na wahudumiwe ipasavyo, ninaomba tuhakikishe tunaboresha huduma kwa wastaafu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kile kiwango ambacho kiliridhiwa walipokaa waajiri, Serikali pamoja na kile Chama cha Wafanyakazi kwamba iwe asilimia 33 bado jambo hili watumishi hawajaridhika nalo walio wengi. Naomba niwe very sincere nizungumze kile kulichopo moyoni mwangu na sisi tuko kwa wananchi, tunaishi na wananchi hawa wanaostaafu ndiyo wanarudi wanakuwa wapigakura wetu na tuna watarajia waje watupigie kura 2025 watampigia kura Mheshimiwa Samia watatupia kura na sisi wote tulioko hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana jambo lirudiwe tena liende kwenye majadiliano liangaliwe upya, yale malalamiko mapungufu taliyopo yakafanyiwe kazi, wastaafu wanapata taabu, naomba lifanyiwe kazi mapungufu yaliyopo yatatuliwe ili wastaafu hawa nao waweze kunufaika na waweze kuishi vizuri maisha yao ya ustaafu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili jambo la ajira ambalo tumekuwa tukulizungumza sana hapa Bungeni ambao ni mjadala mkubwa hivi sasa. Kwenye eneo la ajira hapa tuna wataalam bobezi hapa, wakiwemo walimu wetu waliotufundisha vyuo vikuu, walitufundisha kuajiri kwa kuzingatia sifa kwa kuondokana mambo ya nepotism, tuzingatie bureaucratic systems, kwa kuajiri kupitia nepotism mambo ya udugu, kufahamiana huyu ni mtoto wa fulani, huu ni ushamba, huu ni utumishi wa kishamba, mtu mshamba ambae hajastaarabika ataenda kumuangalia ndugu yake badala ya kuzingatia sifa. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakemea kabisa wale wanaoajiri watu kwa kuangalia nyuso badala ya kuangalia sifa walizonazo, hili tutaliepuka endapo tutaenda kuondokana na kufanya interview kwa face to face huu utaratibu uliopo hivi sasa wa kuwakusanya Watanzania kutoka Mtwara, kutoka Katavi kutoka Mwanza huko Kagera, kutoka sijui wapi Ukerewe, kuwalete Dodoma kuja kufanya interview ni mambo ya kishamba haya (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende sasa kwenye kuzingatia TEHAMA, sasa hivi wenzetu wanaajiri kwa kutumia kompyuta. Kama watoto walienda Vyuo Vikuu kwa ku-apply kwenye kompyuta huko vijijini mwao, kwa nini wasifanye hizi interview au wasi-apply kazi kwa kupitia kompyuta hukohuko waliko kwenye maeneo yao tuepuke gharama, tuepuke usumbufu, tuwasaidie Watanzania hawa masikini wanaotaka kujikomboa kwa kutumia vyeti vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu utaratibu wa kuajiri hivi sasa naomba tuzingatie kompyuta, tu-computerize mifumo yetu. Tunaweza kufanya interview kwenye Mikoa yetu ukawa ni utaratibu ambao uko fair, ukam-accommodate kila mtu, tena kwa kuzingatia sifa zao. Kama tuliwaita vyuoni kwa kutumia kompyuta tena hukohuko kwenye vijiji wanakotoka kwa nini leo tunapotaka kuwaajiri tunashindwa kutumia kompyuta, kwa nini hatuaminiani shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye eneo la ajira hizi kelele hazitaisha endapo tutaendelea na ule ukale wa utaratibu tunaoutumia kwenye ajira. Malalamiko yataendela kuwepo, tutaendela kulaumiana bila sababu. Kwa hiyo, ninashauri hapa pamoja na kutumia hizi TEHAMA pia tuunde timu ya kushauri. Tunao wataalam, tunao watu bobezi Maprofesa wasomi wazuri, kwa nini hatutaki kutumia watu hawa watushauri ipasavyo ili tuweze kuboresha utumishi, tuweze kupata watumishi wazuri wanaoweza kwenda kukutumikia ipasavyo kwenye utumishi wetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine..

MWENYEKITI: Mheshimiwa...

MHE. ABEI R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu watumishi. Tuna vijana wanatembea na bahasha mitaani mpaka wanachoka, viatu yaani wanatembea kama vile vichaa, hata nguo wanashindwa kufua, hawana sabuni hawana nini, lakini tunalalamika tunao upungufu wa watumishi tatizo liko wapi? Kwa nini tunashindwa kuajiri watumishi wanaotosha wakatumikia watu wetu kule vijijini?

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ramadhani Ighondo muda wako umekwisha.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja ninaomba tuajiri watu wakatumikie nchi, vijana wasomi wapo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote, nianze pia na mimi kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Abdallah Ulega, kijana mwenzetu na uzuri namfahamu, alikuwa Youth League, ni committed person, very humble, understanding; kwa hiyo, naamnini hapa Wizara imepata mtu sahihi pamoja Naibu wake. Ni kwamba tunakwenda kutekeleza hivi vitu tunavyovizungumza ambavyo tumeviona kwenye hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa, tunatarajia tuone mambo mazuri ya kisomi, ya kitaalamu na wayashushe mpaka kule chini ambako wanatukuta sisi wafugaji ambao hatujui kusoma wala kuandika. Kwa hiyo, watafute namna sasa, kutumia elimu zao hizi nzuri waweze ku-match na sisi wanakijiji ili tuweze kwenda sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu ku-declare interest, mimi ni mtoto wa mfugaji, nimesoma kwa kutumia mifugo hii. Kwa hiyo, ni sekta muhimu ambayo kimsingi namwomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yake, waitazame kwa jicho la karibu, watumie nafasi ambazo wamepewa na Mheshimiwa Rais, amewaamini vizuri, nasi tuna imaninao kubwa, kuhakikisha hii Wizara inakuwa na tija kwenye pato la Taifa letu na hasa wananchi walioko kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuzungumzia masuala machache ya jimboni kwangu yanayohusu sekta hii, halafu nitazungumza mambo ya jumla ya kitaifa. Kwenye eneo la malisho pamoja na majosho, hasa majosho; kwa kule jimboni kwangu ninashukuru nilipata miradi katika ule mwaka wa fedha unaoisha, majosho manne katika Kijiji cha Muaghamo, Mangida, Minyenye na Makuro. Kwa masikitiko makubwa, hii miradi haikuweza kutekelezeka kwa sababu ya ule utaratibu wa Wizara, kwamba, wanakuwa na zile fedha, mpaka waone josho limetengenezwa na wakandarasi. Wakandarasi watengeneze kwa kutumia nguvu zao, ndipo waje walipwe. Sasa huu utaratibu umekuwa siyo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri utaratibu huu, ingekuwa wanapeleka Halmashauri kwa sababu Halmashauri tunazo kila eneo na ni Government entity inayosimamia mambo haya na tunaiamini. Kwa hiyo, fedha hizi ziende pale ili wale wakandarasi waweze kupewa wafanye kazi kuliko kuzi-own huku juu, utaratibu unakuwa ni mrefu na mgumu, na siyo rahisi kufikika. Naomba huu utaratibu urahisisishwe ili nipate haya majosho manne ambayo ilikuwa niyapate. Pia, nashukuru kwa miradi ya majosho mengine manne ambayo naenda kupata kwa mwaka huu unaokuja wa fedha katika Kijiji cha Mukulu, Unyampanda, Ughandi na Mughunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye zile center atamizi. Ofisi ya Waziri Mkuu walikuja wakati ikiwa chini ya Wizara hii ya Mifugo. Ni kwamba, wangetuletea center kwa ajili ya kituo atamizi kwenye Kijiji changu kimoja cha Nkwaye, lakini mpaka sasa sijaona kinachoendelea. Center hii ingekuwa ni nzuri kwa vijana, kwa ajili ya kurithisha mafunzo mazuri, endelevu ya kisasa kwa wenzao wengine. Sasa sijaona kinachoendelea. Naiomba sasa Wizara walichukue hili, ili nione sasa kile kituo cha ufugaji bora utekelezaji ufanyike ili vijana wetu waweze kupata hii elimu, waweze kuwapa na wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu biashara hii inayofanyika ya ng’ombe. Wafanyabiashara wengi walikuwa wanapata leseni na vibali vile vya kusafirishia mifugo kule kule wilayani na wakati mwingine mkoani, lakini sasa hivi Wizara imelimiliki hili zoezi, wafanyabiashara mpaka waje Wizarani. Sasa inawapa taabu, kwa hiyo, ufanyaji wa biashara ya mifugo umekuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Wizara ibadilishe huu utaratibu ambao upo hivi sasa, irudi kwenye ule utaratibu uliokuwa wa mwanzo, uliokuwa unawawezesha wafanyabiashara wetu wa mifugo ku-access hizi leseni kwenye maeneo yao kuliko kuwapa taabu ya kuwafuata watendaji wetu huku Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la muhimu sasa kwenye sekta hii, katika sekta za muhimu katika nchi yetu huwezi kuiondoa mifugo, huwezi kuondoa uvuvi pamoja na kilimo. Hizi ni production sectors ambazo ndiyo zinatakiwa ziwe sekta za msingi za uzalishaji na zitazamwe kwa jicho la karibu kwa ajili ya kumsaidia Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nchi hii nimeitembea kidogo, kuanzia Bukoba, nimeenda mpaka Zanzibar. Katikati hapo ukipita huwezi kuacha kuona mfugo. Ukianzia Mbeya mpaka uende Arusha, huwezi kuacha kuona mfugo. Sikitiko langu kubwa ni kwenye eneo la bidhaa za mifugo, tumezipuuza. Hakuna viwanda. Hakuna kiwanda cha nyama, wala kiwanda cha maziwa. Vipo vichache. Kwanza tulikuwa na viwanda vile vya zamani; kulikuwa na Tanganyika Packers ambayo leo inatumika kwenye mahubiri. Hivi kweli tunaweza tukafika kwenye point hii ya kuidhalilisha sekta hii ambayo inawasaidia wananchi wa Tanzania zaidi ya milioni 60 leo? Tunaacha mifugo inateseka, ngozi inatupwa. Eti leo sisi tuna- export ngozi kwenda kuliwa Nigeria na Ghana. Ndiyo tumefilisika kwa kiwango hiki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, watendaji wa Wizara hii pamoja na Serikali, twende tukamkomboe mwananchi wa Tanzania kwa kutumia hii sekta ya mifugo. Nasikitika eti leo naambiwa ni asilimia saba sijui tano, kwenye pato la Taifa ndiyo inatokana na mifugo. This is joking! Hapa tunatania, hatujawa serious bado. Naomba sana, turudi kwenye viwanda vile vilivyokuwepo vya kusindika nyama. Nakumbuka tulikula nyama ya kopo wakati huo, lakini leo hakuna. Nyama ikikaa siku mbili buchani, unakuta imeharibika, ndiyo tunaumwa matumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungekuwa tunaweza kuweka viwanda vile vya ku-process nyama, iwekwe kwenye kopo; maziwa, products za ng’ombe, za mifugo; leo hii tungeongeza thamani ya mifugo yetu, tungeingiza pato kubwa la Taifa kwa kupitia mifugo hii. Hata Singida tulikuwa tuna kiwanda cha kusindika nyama ya ng’ombe. Leo hii naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kusimama uniambie, kiwanda cha ng’ombe Singida, status yake ikoje? Naomba hiki kiwanda kirudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sisi tunafuga; tuna ng’ombe wa kutosha, central zone hii kwa ujumla wake tuna mifugo ya kutosha; Shinyanga, na kadhalika, tuweke kiwanda pale Singida cha ng’ombe na mbuzi ili tuweze kuinua kipato cha Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu sana, ni eneo la malisho ya mifugo. Katika eneo ambalo hatujaitendea haki kabisa sekta hii ya mifugo ni eneo la malisho. Naomba sana, tuache kuwadhalilisha wafugaji wetu. Kwa kuwa, tumeshaona wananchi wetu wengi ni wafugaji, nasi tupo kwenye kutengeneza sera na mifumo, tuwatengenezee utaratibu mzuri wa malisho. Majani haya ambayo tumesema ni ya malisho ya mifugo yetu, tuyapeleke mashamba darasa kwenye kila Kijiji, kwenye kila kata. Kwa nini myaache huko Dar es Salaam au Dodoma? Wafugaji hawako Dar es Salaam. Wafugaji na wakulima wako vijijini, tuwafuate waliko tuwapelekee hii huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi suti tuzipeleke kule vijijini ili tukaishi maisha wanayoishi wenzetu kule chini kwenye grassroot. Tutawatendea haki, wakulima wetu wataacha kumangamanga, kutafuta malisho huku na kule. Kila siku tunaona migogoro ya wakulima na wafugaji, haitaisha kama hatujaweza kuwapa wafugaji wetu malisho huko kwenye maeneo yao. Yale maeneo ambayo yalipimwa, Mheshimiwa Waziri mlipima maeneo, mliyarasimisha maeneo vizuri kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninayo mambo mengi hapa nitayawasilisha mengine kwa maandishi, lakini naomba sana haya ambayo nimeyazungumza yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii adhimu kabisa kwa ajili ya kutoa mchango wangu muhimu katika Wizara hii ya Kilimo ambayo ndio maisha ya watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya, wanalengo na nia nzuri ya dhati na very serious kwa ajili ya kukomboa na kuleta revolution, kuleta mageuzi, mapinduzi ya dhati ya kilimo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu baadae utanipigia kengele kwa sababu nina mambo mengi ya kusema hapa. Sasa nataka nitoe sababu za kwa nini nataka kuunga mkono bajeti ya Wizara hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Singida Kaskazini, sababu yetu ya kwanza ya kuunga mkono bajeti hii, ni ruzuku ya mbegu ambayo tumepata latika jimbo langu. Tulipata tani 67,000 na wananchi wametumia mbegu ya alizeti iliyo bora na mwaka huu mavuno yatakuwa mengi kuliko miaka yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata ruzuku ya mbolea ambayo katika jimbo langu tumepata tani 239. Pia tukapata pikipiki 13 za Maafisa ugani kwenye kila kata, kata13 out of 21. Hii ni sababu moja wapo kubwa ya sisi kuunga mkono hoja hii. Pia, pikipiki zile kwa Maafisa Ugani zilikuja pamoja na vitendea kazi vingine ambavyo vilisaidia kupima afya ya udongo n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kubwa la muhimu katika wilaya yangu kwa nini tunaunga mkono hoja hii, nina miradi mikubwa miwili ya umwagiliaji katika Jimbo la Singida Kaskazini. Mradi wa Musange na Mradi wa Mohamo, ambayo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imeonekana katika ukurasa wa 228. Nashukuru hotuba ya Mheshimiwa Wizari, nimeipitia vizuri, nimeona amevitaja katika ukurasa wa 228 kwamba kazi inakwenda kukamilika na wanachi wataanza kunufaika. Kazi ya upembuzi yakinifu inakwenda kukamilika na mabwawa yale yanategemea kuanzia mwaka 2023 sasa yatakwenda kuanza kazi. Hizi ni sababu kuu nne za kuja kusema hapa kwa niaba ya wananchi wa Singida Kaskazini, kwa nini tunaunga Mkono bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo kutoa maoni ama mapendekezo na changamoto ambazo zipo kwenye eneo hili. Kwanza, kwenye mbolea. Mheshimiwa Waziri, ile mbolea naomba wafanye packaging ya kuanzia kilo tano, kumi, ishirini hadi hamsini ili na wakulima wadogo nao wanufaike. Kwa sababu tunapoweka ile packaging kubwa inawalenga wakulima wakubwa tu lakini wale wakulma wadogo wadogo wa bustani na nini wanakosa fursa hii. Hivyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, alichukue hili na alifanyie kazi mwakani tumletee majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa mbolea na mbegu ninaomba vile vituo vya kugawa hizi mbegu visiwe tu sehemu moja, viende mpaka kwenye kata zetu, viwafikie wananchi kuwapunguzia gharama na usumbufu mwingine usiokuwa wa lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu ni kwenye hizi irrigation schemes. Kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini, tunayo maeneo mengine ambayo ni ya muhimu yana maji na ni mazuri kwa kilimo. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri, nilipouliza swali langu hivi karibuni katika Bunge hili, kwenye eneo la Mradi wa Mgori tayari Maafisa wa Wizara ya umwagiliaji wamekwisha fika ninampongeza na ninashukuru sana kwa hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kweli wakati wa utambulishpo pale asubuhi, nimeona wanatambulishwa Maprofesa, ni kweli nimeona these people are serious na kweli ni wasikivu na wanatekeleza kile wanachoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, bado kuna maeneo mengine ya maji katika jimbo langu ambayo yanahitaji scheme kama hizi. Kuna Bwa la Kisisi, Bwawa la Masogweda, kuna Bwawa la Ntambuko, kuna Bwawa la Mikuyu maeneo haya tunaomba Mheshimiwa Waziri, uyachukue tena hawa ni jirani zako, Nzega na Singida Kaskazini ni majirani na ni ndugu. Nikuombe na maeneo haya uyatazame tupate miradi katika maeneo haya ili na wenyewe wanufaike na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni eneo la bei ya alizeti. Alizeti imelimwa sana mwaka huu kwa sababu ya hamasa nzuri ya Waziri na hata Waziri Mkuu alipokuja Singida, lakini cha ajabu na cha kusikitisha leo hii bei ya alizeti imeshuka. Leo hii bei ya gunia la alizeti ni 30,000, 40,000, kilo moja shilingi 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia nataka nikuambie hapa leo, sasa hivi wakulima wataenda kuihama alizeti, watahamia mazao mengine kwa sababu ya changamoto ya bei. Bei ya alizeti ni mbaya, wananchi wanaomba tuache kuagiza mafuta kutoka nje. Kama tumeshindwa kuacha kuagiza basi tuweke kodi, tuweke VAT ili mafuta yale yanapoingia yasiwe na fursa kubwa kuliko mazao tunayozalisha sisi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeitikia wito, tumeitikia agenda hii ya kuhakikisha alizeti inatoa mafuta na tunazalisha mafuta katika nchi yetu lakini tunaomba mtupokee msituache peke yetu tuanze kuteseka. Lakini hilo la masoko na bei liende hata kwenye eneo la kitunguu. Sisi Mkoa wa Singida tunalima sana Kitunguu, ndio uti wa mgongo wa maisha ya watu wa Singida. Shida inakwenda kwenye mnyororo ule wa soko, kuna msemaji amezungumza hapa kuhusu tatizo la madalali. Kuna madalali, sijui kuna ushuru, sijui kuna vitu gani, vitu vingi, bei yenyewe hamna, gharama ni kubwa, tumuokoe mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu tuna eneo zuri kwa ajili ya kujenga soko pale njia panda ya Merya. Mheshimiwa Waziri, ninaomba na Serikali inanisikia katika hili, sio tu Waziri wa kilimo, Serikali inisikie kuanzia TAMISEMI, Viwanda na Biashara, njooni mtujengee soko pale kwa ajili ya kuhakikisha Mkoa wa Singida tunaendelea kuimarisha na kuboresha kipato cha nchi yetu katika eneo la zao la Kitunguu ambalo zao hili kwa Singida ni zao la Kimataifa. Kwa sababu Singida wanakuja watu kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudani mpaka Rwanda wanakuja Singida kwa ajili ya kufuata kitunguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri pamoja Serikali kwa ujumla walichukue hili. Tuboresheeni yale mazingira ya uuzaji na ufanyaji wa biashara katika zao hili la kitunguu. Lakini eneo hilo hilo bado tatizo la rumbesa lipo, tuendelee kuikomesha tatizo la rumbesa ya kitunguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni eneo la matreka, niombe sana tu–modernize kilimo chetu. Ni kweli kabisa wananchi sasa wameitikia kulima na wako tayari kufanya kazi. Shida kubwa tunayokutana nayo ni mazingira, hivi tutalima kwa mkono mpaka lini? Hebu tuhurumieni, niombe sana pembejeo za kilimo hasa matrekta tuyalete vijijini na yawe na masharti nafuu wananchi waweze kukopa. Mwenyewe nilienda hapo Mfuko wa pembejeo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abeid, ahsante sana. Malizia muda wako umekwisha.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mengine mengi nitawasilisha kwa njia ya maandishi. Ninaunga mkono hoja, Waziri achape kazi tunaimani nae. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza kuhusu miradi ya umwagiliaji Jimbo la Singida Kaskazini, Bwawa la Mgori limejaa tope na halina miundombinu ya umwagiliaji. Naishukuru Wizara kwa kutuma timu ya wataalam kuhakikisha bwawa hili linafanyiwa kazi ili liweze kusaidia uzalishaji kwani ni eneo lenye ardhi nzuri kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya mahindi, vitunguu karanga na alizeti. Bwawa hili litanufaisha hekta 1000 endapo litapatiwa miundombinu ya umwagiliaji.

Aidha, katika Jimbo la Singida Kaskazini tunayo Mabwawa ya Ntambuko, Kisisi, Masoghweda, Endesh na Mikuyu ambayo yanafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji endapo yatawekewa miundombinu yake. Pia ardhi yake ni nzuri kwa uzalishaji wa mazao anuai hasa mahindi, alizeti, vitunguu na mbogamboga. Naiomba Wizara iyatembelee na kuyafanyia upembuzi yakinifu na kuyajengea miundombinu yaweze kutumika kwa umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ina upungufu wa watumishi 93 wa Idara ya Kilimo, naomba kupatiwa watumishi ili kazi ziweze kufanyika ipasavyo; idara iwezeshwe usafiri wa gari ili iweze kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kilimo kwa urahisi. Gari lililopo ni kuukuu na ni bovu. Pia tunalo shamba la mbegu lenye hekta 600; naomba Wizara iweke mkakati wa kuzalisha mbegu za mazao hususan mahindi na alizeti ili kuepuka gharama kubwa tunazopata kusafirisha mbegu kutoka maeneo ya mbali.

Mheshimiwa Spika, zao la pamba lirejeshwe katika mkoa wa Singida kwani tunacho Kiwanda cha Pamba Mkoani Singida ambacho kinahudumia mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa utendaji kazi mzuri, pia watendaji akiwamo Katibu Mkuu Balozi Aisha.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba kuwasilisha kilio cha wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusu barabara ya kutoka Singida - Ilongero - Haydom. Barabara hii ni ahadi ya viongozi wote wa Kitaifa ambao hufika Ilongero kuanzia Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi Rais aliyepo madarakani alipokuwa Makamu wa Rais alifika Ilongero akaahidi kuhakikisha barabara hii inawekwa lami.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha hata katika bajeti hii ya leo barabara hii haipo katika mpango. Ni miaka 60 ya Uhuru leo Wana-Singida Kaskazini wanalia, wanateseka, wanataabika, wanakarahika na mateso ya hii barabara.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri aipe kipaumbele barabara hii muhimu kwa uchumi wa Wana-Singida, ni roho ya uchumi wa Wana-Singida Kaskazini. Ni barabara ya msaada mno lakini imekuwa longolongo miaka nenda-rudi, na mimi Mbunge nimechoka matusi ya wananchi. Naomba lami katika hii barabara katika bajeti hii ya mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, naomba tupate walau kilometa kumi za lami katika barabara hii hadi makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika Mji Mdogo wa Ilongero. Watumishi hivi sasa hawakai kwa kukimbia mateso ya barabara hii hususan wakati wa masika na rasta zinazokera na kuharibu magari ya watu.

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja ya bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi hadi nione fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii muhimu sana kwa maisha ya Wana-Singida Kaskazini. Nataka nione kilometa kumi hadi katika Mji wa Ilongero.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alifika jimboni kwangu Singida Kaskazini Kitongoji cha Mukulu, Kata ya Mughunga mwishoni mwa mwaka 2021 na kuwaahidi wananchi wa kitongoji hicho kuwa atawajengea josho la mifugo. Wananchi wale walifurahi sana kwa ahadi hii ya Serikali kwa sababu wanapata taabu sana kuogesha mifugo yao ukizingatia ni jamii ya wafugaji na maisha yao yote yanategemea mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kuhusu ahadi hii kwani wananchi wananikumbusha mara kwa mara na wanaisubiri huduma hii kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Wizara kuanzisha viwanda vya kusindika nyama. Ni muhimu sana kuanzisha viwanda maeneo ya Singida, Dodoma, Shinyanga, Arusha na maeneo yanayofuga ng'ombe kwa wingi ili kuongeza thamani ya mifugo yetu na kuweza kuuza nyama nje ya nchi hususan Visiwa vya Comoro ambavyo vinategemea sana nyama kutoka Tanzania badala ya kusafirisha ng'ombe walio hai, tuweze kusafirisha processed meet.

Pia ni muhimu kuanzisha viwanda vingi vya maziwa nchini, jambo hili litainua uchumi wetu na kuajiri vijana wetu waliopata mafunzo mbalimbali hususan katika fani husika ya uzalishaji, usindikaji, masoko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza sana suala la josho la mifugo kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini Kitongoji cha Mukulu ambacho hakina kabisa huduma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii muhimu sana kwa ajili ya kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu sana ambayo ndiyo chanzo cha uhai wa mwanadamu.

Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri kwa utendaji wake mzuri, pamoja na Naibu wake na watendaji wake Wizarani, mikoani na mpaka wilayani.

Mheshimiwa Spika, sisi kule mkoani Singida katika maeneo ambayo tunajivunia kwamba kweli yana watendaji makini ambao kusema kweli wanatupa ushirikiano wa kutosha ni Meneja wa RUWASA wa Mkoa pamoja na kwangu wilayani. Kwa kweli nadhani ni labda wametengeneza hivyo wamekuwa trained kwa sababu MheshimiwaWaziri yuko hivyo basi hata kule chini pia tunapata hivi vionjo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji hawa wasibadilike, waimarike, waendelee kuwa humble, waendelee kuwa imara katika utendaji na sisi tuko tayari kushirikiana nao.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba kwanza nitoe shukrani nyingi sana pia kwa Mheshimiwa Rais, kwa ile mitambo aliyotuletea katika mikoa yetu ya kuchimba maji. Katika maeneo ambayo tunaona jambo hili ni la muhimu na kweli limetufaa ni Mkoa wa Singida hasa Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, katika kumbukumbu zangu hotuba yangu ya kwanza kwenye Wizara hii nilisema hapa wazi kabisa hapa kwamba, sisi Singida tunakunywa maji na fisi kwa sababu ya shida kubwa ya maji tuliyokuwa tunapata. Wananchi walikuwa wanakesha, usiku wa wa mane akina mama walikuwa hawalali, ndoa zilikuwa zinayumba kwa sababu mama ule muda anaotakiwa kuhudumia ndoa usiku yeye anaenda kusubiri maji kwenye mito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo hii, kwa kupitia ule mtambo wa mama ule alilotuletea mkoani Singida, na kwa wilayani kwangu kwa Jimbo la Singida Kaskazini umeshatuchimbia visima vinavyopata vitano mpaka hivi sasa. Nimechimba maji katika Kijiji cha Nduhila ambapo huo mradi utakwenda kufanyiwa usambazaji wa zaidi ya Kijiji cha Nduhila. Kupitia mtambo huu tumepata katika Vijiji vya Makuro, Mkenge, Matumbo na bado kazi inaendelea kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa mazingira kama haya siwezi kuacha kumshukuru na kumpongeza Rais wetu kwa kazi hii kubwa, kwa sababu sisi katika Imani tunasema ukichimba kisima unakuwa umetoa sadaka inayoendelea hata kama ukifa. Kwa hiyo hapa Mheshimiwa Rais ametenda wema na ametoa sadaka ambayo itaishi milele, haitamfuata hata kesho atakapokuwa hatupo hapa duniani.

Mheshimiwa Spika niishukuru sana pia kwa miradi 15 ya maji ambayo tutapata katika Jimbo langu la Singida Kaskazini, ambapo kupitia gari hili alilotuletea Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ninaamini tutapata visima katika Vijiji vya Ntondo, Nkwaye, Sekouture, Kinyamwenda, Msikii, Mwalala, Nongwa Mpoku, Igauli, Mwakiti, Itamka, Mkende kama nilivyoisema, Makuro, Nyisinko, Isimihi na Kijiji cha Mahandi.

Mheshimiwa Spika, haya ni maeneo ambayo kwa kweli wananchi walikuwa wana kiu ya maji ya muda mrefu lakini sasa watapata maji na hivyo watakata ile kiu. Jambo kubwa ninaloliomba hap ani kwamba, hii miradi itekelezeke kwa wakati ili wananchi nao waionje hii keki ndogo ya Taifa lao, waonje ule utamu wa maji ambao wamekuwa wakiukosa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, vilevile niombe kuwasilisha changamoto chache zilizopo kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini ili Waziri atusaidie wananchi wetu nao waendelee kufurahia. Jambo la kwanza kuhusu usambazaji wa maji katika miji midogo; nikianza na mji wa Ilongero ambayo ni Makao Makuu ya Halmashauri. Huu mji hivi sasa ni populated, umeshakuwa na idadi kubwa ya watu na bado watu wanahamia. Una huduma muhimu za kijamii, una Hospitali ya Wilaya ambayo inahitaji maji muda wote.

Mheshimiwa Spika, tunacho kisima pale, lakini sio cha kudumu sana, tunahitaji maji kwenye miji midogo kama vile kuna masoko, kuna huduma nyingine. Katika huu mji kuna mradi pale unaitwa Uyanjo lakini umezidiwa. Naomba upanuzi kwenye huu mradi, ili uweze kuwafikia wananchi wengi ambao wanahamia kwenye ule mji, wanaojenga, sasa hivi kuna ujenzi wa hali ya juu unaendelea, kwa hiyo, niombe maji ya kutosha na ya kudumu, hivyo, upanuzi ufanyike, ili wananchi wengi wapate maji.

Mheshimiwa Spika, Mji Mdogo wa Mtinko. Ule mji una mradi wa maji, lakini mji ule maji yanayotoka pale ni ya chumvi. Kwa hiyo, niombe tupate teknolojia ya ku-purify yale maji ili yaweze kuwa matamu, kama haiwezekani basi tutoe maji kwenye miradi ya jirani, ili maji yale yawe matamu. Tunaumia, sasa hivi unaona meno yangu pamoja na kwamba, ni mazuri, lakini yanakuwa ya njano, tunakunywa maji ya chumvi, tunaharibiwa meno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wazungumzaji wa kutoka Mkoa wa Arusha, kule watu wanaharibika viungo wanakuwa walemavu kwa sababu ya maji. Sasa shida yetu sisi Singida ni maji ya chumvi, kwa hiyo, niombe sana kuwe na teknolojia ya ku-purify maji, ili yaondoe kero hii, lakini hili niunganishe hapa katika Kitongoji cha Gairu kilichopo Kijiji cha Sagara; pale maji yapo, lakini ni ya chumvi mno, yaani ukinywa ni zaidi ya chumvi hiyo unayoifahamu.

Mheshimiwa Spika, niombe sana badala ya kuchimba kisima katika lile eneo, tutoe maji kwenye Kijiji cha Sagara, kipo chanzo cha kudumu, kizuri, kina maji ya kutosha. Tutoe maji kule juu tuyashushe, ni umbali wa kama kilometa mbili au almost two kilometers, nadhani haziwezi kuzidi hapo. Ni rahisi kusambaza maji kutoka kwenye chanzo cha Sagara kuliko kuchimba kisima kipya kwa sababu, tutakapochimba itakuwa ni chumvi tena. Nimeona kwenye bajeti kwamba, tunacho kisima pale, lakini nashauri badala ya kuchimba kisima tupeleke maji kutoka chanzo cha Kijiji cha Sagara ambacho maji yale ni matamu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia miji midogo, ukiwemo Mji wa Ngamu. Mji wa Ngamu una maji, lakini naomba usambazaji ufanyike ili wananchi wengi wapate huduma ile.

Mheshimiwa Spika, kuna eneo lingine na maeneo ambayo tumekuwa tukichimba maji, lakini hayatoki. Mfano Kijiji cha Mangida, alikisema pia Mheshimiwa Aysharose, Kijiji hiki tumechimba maji zaidi ya mara tatu, lakini maji hayatoki, lakini kuna vijiji jirani ambavyo vina maji na ni maji ya kutosha. Mathalani sasa hivi wanapata maji kutoka Mradi wa Kijiji jirani cha Sefunga.

Mheshimiwa Spika, niombe tufanye extension kwenye huu mradi, lakini pia hata Kijiji chenyewe cha Mangida kina maji, lakini yako mbali kidogo kama kilometa mbili. Tuyatoe maji pale, kuna mradi ambao ni wa muda mrefu umechakaa, ni wa tangu Nyerere wenyewe wanasema, kuna yale matanki yale wanasema ya Mjerumani, liko tanki kubwa sana pale, tuyavute maji kutika ule mradi, mengine tuyatoe pale Sefunga, wale wananchi waache kuteseka.

Mheshimiwa Spika, hakika wananchi wa Mangida wanateseka mno kwa shida ya maji. Niombe sana hii iwe ni mara yangu ya mwisho kuitaja Mangida kwa suala la maji, niombe sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili kama ni special case atuletee maji pale kwenye kile Kijiji. Nimeona pia kuna mradi wa kisima pale, si sawa kuchimba pale maji kwa sababu, tumekuwa tukichimba hayatoki.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni Kijiji cha Mwokulu. Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika pale wakati ule walivyokuja, akaahidi pale kwamba, atatusaidia kisima pale, niombe sana atuletee kisima pale, ili wale wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ni gari. Halmashauri yangu ya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Kengele ilishagonga Mheshimiwa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja, RUWASA Wilaya yangu hawana gari naomba wapatiwe gari, usafiri, wanateseka mno wamekuwa kama digidigi. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nami fursa jioni ya leo niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii na hasa kuwasemea wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusu miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuhakikisha anawahudumia Watanzania ipasavyo hususan katika eneo hili la ujenzi wa miundombinu ya usafiri na barabara na mambo mengine hapa nchini kwetu. Pia nimpongeze kwa ukamilishaji wa Ikulu ya nchi, na sasa tunasema nchi iko Dodoma. Kwa hiyo, naomba pia nitumie fursa hii kulisema hilo, kwa sababu ni jambo ambalo kwa miaka nenda rudi lilikuwa mishipa katika nchi yetu. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti, hotuba yake na utendaji wake mzuri pamoja na Manaibu wake wote wawili, Katibu Mkuu na Watendaji kwa ujumla, bila kumsahau Meneja wa TANROADS kule mkoani kwetu Singida, ni mtu very humble, msikivu na pia ni mfuatiliaji, ni mpokeaji wa simu zetu tunapokuwa na changamoto, maana yake sisi kule barabara zetu nyingi ni za vumbi, kwa hiyo, simu ya Meneja wa Mkoa ni iko ubavuni kila dakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama jioni ya leo, naomba nizungumzie jambo kubwa moja kwa muda wangu wote. Barabara inayotoka Singida Mjini inakwenda Njuki - Ilongero ambapo ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida, inakwenda Mtinko hadi Haydom. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara na vilevile ni kiungo pia cha ile barabara inayokwenda mpaka Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba angalau upembuzi yakinifu wa barabara hiyo umekamilika, lakini kwa masikitiko makubwa, nataka niseme tu wazi hapa kwamba mimi nitaondoka hapa nikiwa na machozi na majonzi makubwa nikiwarudishia wananchi wenzangu kilio kule kwamba hatujapata hata kilometa moja ya lami kwenye hii barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze umuhimu wa hii barabara. Kwanza inakwenda kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ambapo kuna watumishi zaidi ya 3,000 walioko pale Makao Makuu ya Wilaya, wanaitumia hii barabara kila siku zaidi ya mara tatu, lakini wanapata shida kwa sababu ya ubovu, ina mashimo. Kama haitoshi, barabara hii inakwenda kwenye Hospitali ya Wilaya iliyoko pale Ilongero, lakini mpaka kesho hii barabara ni mbovu, ni mashimo matupu, watu wanapata shida. Kama haitoshi, barabara hii inawahudumia wananchi wanaokwenda Hospitali ya Haydom, ukanda wote huu wa kati; Mkalama, Jimboni kwangu Singida Kaskazini, Hanang, wote wanakwenda kwenye hii Hospitali ya Haydom, tunapata huduma kule, lakini ni mavumbi, mashimo. Sasa sijui tuongee lugha gani ili mtuelewe leo ndugu zangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inakwenda kwenye hospitali moja muhimu sana ya St. Carolus iliyopo pale Mtinko Mji Mdogo, lakini kila tukizungumza hapa hamtuelewi. Kama hiyo, haitoshi hii barabara iko kwenye ukanda wa uzalishaji mazao makubwa ya biashara na ya chakula, yanapita kwenye hii barabara. Vitunguu tunavyovisema hapa, vinapita kwenye hii barabara, alizeti inapita kwenye hii Barabara, mpaka na hawa kuku tunaowala hapa kila siku wanapita kwenye hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha kusikitisha zaidi, hii barabara ni ahadi ya tangu wakati wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Amekuja Mzee Mwinyi pale Ilongero akaahidi akasema tutaijenga kwa lami, amekuja Hayati Mkapa akaahidi hii Barabara, tena wanakujaga kuombea kura pale. Wanaombea kura hii Barabara. Amekuja Mzee Kikwete ameombea kura hii barabara, amekuja Hayati Dkt. John Magufuli, alisema kabisa tutakuja, tutaweka lami kwenye hii Barabara. Hata Rais wetu wa hivi sasa ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, alikuja akaahidi akasema tutawawekea lami barabara hii. Kigugumizi kiko wapi? Shida ni nini kwenye hii barabara mnatutesa namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii barabara mwaka huu ionekane kwenye bajeti, tuweke lami hii barabara. Kama imeshindikana, tupeni basi kilometa hizi kumi ziende mpaka Makao Makuu ya Halmashauri, watumishi wanakimbia, wanakataa kukaa ofisini. Kila baada ya miezi miwili, anaripoti, wanaondoka, au nitoe machozi hapa ndiyo ninyi muone naongea ya kueleweka hapa? Nitoe machozi? Au nipande juu ya hii meza? Tatizo ni nini? Kwa nini hamtuelewi wananchi wa Singida Kaskazini tunapowaeleza kuhusu hii barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara isipoonekana, nisipoona hata kilomita kumi angalau ifike kwenye Makao Makuu ya Halmashauri, Mheshimiwa Waziri nachukua mshahara wako, tutakutana na wananchi kule Singida Kaskazini. Utaenda kuwaeleza mwenyewe, kwa nini hutupi fedha kwenye hii barabara. Kama mna mpango mwingine labda mtuambie leo. Sisi tunalipa kodi, tena wananchi wa Singida Kaskazini ni waaminifu kweli kwenye Serikali hii, ni wapigakura waaminifu kweli kwa Serikali hii ya CCM, tunaomba mtupe hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba chonde chonde tupate lami kwenye hii barabara. Nami leo hii naomba iwe ni mara ya mwisho kuzungumzia barabara ya Singida – Ilongero - Haydom. Baada ya hapa naomba sana nisizungumze tena kuhusu hii barabara. Nimechoka, nimeuliza maswali ya msingi, maswali ya nyongeza, majibu yanakuja ya pinduapindua kila siku. This will be my last time to talk about this road. Naomba niongee Kinyaturu ndiyo mtanielewa, maana yake Kiswahili hamnielewi. Naomba niongee Kinyaturu hapa pengine Waziri utanielewa. Niongee Kinyaturu hapa? This will be my last time to talk about this road. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Singida Kaskazini wamechoka kudanganywa kuanzia, Hayati Nyerere! Sasa ninyi mnataka kuwafanya viongozi waliopita kuwa ni waongo! Marehemu ni waongo kweli! Ina maana viongozi wa nchi hii wakubwa ni waongo! Tekelezeni ahadi za viongozi wa kitaifa wanazoahidi wanapokuja kwenye maeneo yetu. Viongozi wanapokuja wanapoongea na wananchi, sisi ndio tunaachiwa mizigo tunaowawakilisha. Tunaambiwa ninyi mbona hamwaambii viongozi? Sisi ndio…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii barabara iwekwe lami. Mheshimiwa Waziri amenisikia, tena Waziri wa Fedha na wewe uko hapa, nakuomba sana brother, tusaidie hela, hela!

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Lete hela ile Barabara tuweke lami punda wapiti vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Wananchi wanateseka, lakini Mheshimiwa Waziri kesho Shilingi yako naondoka nayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya, lakini pia kwa usikivu mkubwa sana, Waziri huyu amekuwa msikivu pamoja na Naibu wake, tunapokuwa na changamoto mbalimbali kwa kweli huwa wanatusikiliza kwenye Kamati na hata nje ya Kamati na mimi naendelea kuwaomba kwamba, tabia hiyo waiendeleze wasibadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi yake nzuri anayoifanya katika kuitangaza nchi yetu kimataifa na lazima tukubali kwamba Tanzania sio kisiwa, nchi yetu sio kisiwa kwa hiyo, lazima tu-interact, lazima tujue fursa zinazopatikana nje ya nchi yetu na lazima tuzichangamkie. Kwa hiyo, Rais wetu anapofanya juhudi hizi za kwenda huku na kule lazima tumtie moyo na lazima tumuunge mkono. Na kimsingi kwa yeye ambaye ndio tunasema ndio first diplomat yale anayoyafanya kule watendaji lazima wayachukue na wayatafsiri katika maisha na katika mazingira ya nchi yetu na fursa zinazopatikana kule lazima wazitafsiri katika mazingira halisi ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa lazima twende mbali kidogo, mimi nilikuwa nataka nijikite kidogo kuelezea faida tunazozipata ama ambazo tumeshazipata kama nchi kufuatia ziara alizofanya Mheshimiwa Rais wetu nje ya nchi na hapa nilitaka pia niombe jambo moja, Waziri labda atakapo-wind up atanisaidia, pale tunaposema mama yetu, tunapomtambua Mheshimiwa Rais kama mama, yes I real appreciate she is our mother, ndio mama yetu, ni mlezi wetu, lakini kama kiongozi wa nchi nilikuwa najaribu kujiuliza mwenyewe kwa nini tusimuite Mheshimiwa Rais wa nchi au Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuitofautishe na mama; ndio ni mama kwa kuwa ni mama yetu ni mlezi wetu, lakini tumtambue kwamba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Nitaomba hili kidiplomasia ikiwezekana Mheshimiwa Waziri hapa atupe muongozo sahihi. Ni mama yetu, Mheshimiwa Rais wetu anapenda tumtambue kama mama, lakini kimamlaka imekaaje? Kwa nini tusitambue kwamba huyu ni Mheshimiwa Rais kwa title yake kama Rais kwa nafasi yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli mfano Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje wewe ni mama, tuseme mama yetu Waziri wa Mambo ya Nje? Mimi nadhani tumtambue Mheshimiwa Rais kwa nafasi yake ya Urais. Tuiheshimu ile mamlaka aliyonayo kama mkuu wa taasisi ya Urais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikizungumzia kwa uchache faida ambazo nchi imepata kufuatia ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi; kwanza tumepata miradi mingi sana ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali, kwenye sekta mbalimbali. Tumepata miradi mingi kwenye sekta ya afya, kwenye sekta ya kilimo, kwenye maji, kwenye elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tumeona tumepata vyumba vya madarasa zaidi ya 15,000 nchi nzima. Haya yalikuwa ni matokeo ya ziara za Mheshimiwa Rais alipokwenda kutembelea nje ya nchi yetu ama kutembea nje ya nchi yetu, lakini pia tumepata wawekezaji kwenye sekta mbalimbali waliokuja nchini baada ya Mheshimiwa Rais kwenda wameona fursa ambazo nchi yetu inazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi utalii umeongezeka, watalii wameongezeka na tunafahamu sekta ya utalii inavyoiingizia nchi yetu kipato au pato lililotokana na watalii ni fedha nyingi tunazopata kwa hiyo, lazima tuendelee kuyatafsiri mambo haya katika mazingira halisi sasa ya Kitanzania, ili watu waone umuhimu wa ziara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumepata mikopo ya riba nafuu kutoka nje ya nchi, lakini pia kufungua mahusiano ya kidiplomasia ya nchi yetu na nchi nyingine. Tunafahamu hapa katikati mambo yalikuwa magumu kidogo, lakini sasa hivi tunaona mahusiano yalivyokuwa mazuri, tunapata wageni, tunapata wawekezaji, diplomatically nchi yetu sasa hivi iko vizuri kiuchumi na hata kijamii. Kwa hiyo, lazima tuyathamini mambo haya na tuendelee kuyasema na tuendelee kumpa moyo Mheshimiwa Rais katika ziara hizi anazozifanya na watendaji sasa wayachukue mambo haya, wayatafsiri katika mazingira yah uku chini ili wananchi waendelee ku-support na kuelewa haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na moja ya fedha za miradi ambazo tumezipata, ametangulia kusema Mheshimiwa chumi hapa, kuna fedha ambazo tumezipata zinaelekezwa kwenye miradi mahususi. Mathalani zile ambazo zinakwenda kujenga, kuna fedha hizi ambazo tumepata Euro milioni 450 sawa na shilingi za Kitanzania trilioni 1.17 zinazotoka Umoja wa Ulaya. Fedha hizi zinakwenda kwenye kutekeleza ujenzi wa viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini, kuboresha hata ule uwanja wetu wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere - Terminal II pale, uwanja wa Kigoma wa ndege, uwanja wa Shinyanga na vingine nchini. Kwa hiyo, vitu hivi tusipovieleza hapa haya anayoyafanya mama hayawezi kueleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hili ambalo ni la hizi barabara, kuna barabara kubwa nne ambazo zinaenda kuboreshwa; kuna barabara hii ya Iringa – Msembe kilometa 104; kuna barabara ya Songea – Rutukila kilometa 111; barabara ya Rusahunga – Rusumo kilometa 92; kuna barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi kilometa 201. Hizi fedha ni nyingi na hizi barabara ni muhimu kwa uchumi wan chi yetu, hatuwezi kuzungumza uchumi kama hatuna miundombinu mizuri ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nilifikiri niliseme hili ili hasa watendaji wa Wizara na hata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo ahsante, kengele ya pili.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, japo muda umekuwa mdogo, lakini na viwanja vyetu vilivyoko nje ya nchi huko viendelee kujengwa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi fursa angalau nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii muhimu ya nishati katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, yale maonesho ya nishati waliyotuletea pale kwa kweli yametujibia maswali mengi mbayo pengine tungeyaleta hapa na ingetuchukua muda mrefu kuzungumza, lakini tuliutumia ule muda vizuri kwenye mabanda yale kwa hiyo tumepata majibu sahihi. Ni ombi langu sasa yale ambayo tuliambiwa yakafanyiwe kazi siyo kwamba baada ya bajeti kupita sasa waka-relax waje watuletee mabanda tena mwakani. Tunataka kazi kule field, mambo yaonekane tuwashe umeme vijijini mwetu kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika moja ya mambo ambayo mimi ningeenda kuuliza isingekuwa yale maonesho ilikuwa ni vile vijiji ambavyo vilisahaulika kwenye ile survey ya mwanzo ama list ya mwanzo ambayo iliorodheshwa ya vijiji ambavyo vinaenda kupatiwa umeme. Kwangu nilikuwa na vijiji Tisa ambavyo ni Mdilu, Mwasauya, Mwakincheche, Itamka, Mwigh’anji, Endeshi na Sefonga lakini vijiji hivi tayari vimeingizwa. Ninachoomba sasa na wenyewe survey ikafanyike ili nao wapate matumaini na wao sasa kupata umeme, maana yake mpaka sasa hakuna kilichofanyika pamoja na kwamba tayari vimeshaonekana kwenye orodha kwamba watapatiwa huduma hii ya umeme. Kwa hiyo, ile kufanya survey itaonyesha kwamba kweli sasa kazi inaenda kufanyika na wao wanaenda kuwasha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ni la muhimu sana tunalolipata kule kwa wananchi ni ile kilomita moja. Kwamba umeme unakwenda kilomita moja tu kwenye Kijiji sasa ile haikidhi haja, ni eneo dogo sana. Ninashukuru sana Mheshimiwa Waziri katika presentation yake amesema kwamba kuna timu ambayo inaenda kukaa na kufanya utafiti zaidi, kufanya tathmini ili kuongeza angalau iongezeke iende hata kwenye kilomita tatu mimi naona hiyo ni sawa, angalau kilomita tatu itafikia kukidhi vigezo au kukidhi kuwapatia wananchi wengi huduma hii. Ukizingatia vijiji vyetu ni vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwangu nina vijiji vikubwa unakuta Kijiji kimoja kina vitongoji mpaka vinafika zaidi ya kumi. Mathalani Kitongoji cha Sokoine kikubwa kina hadhi ya Kijiji, Songa kina hadhi ya Kijiji, Kwaye na Mapinduzi na vina huduma za Taasisi za Umma, vina shule, vinavyo hospitali wakati mwingine na vina shughuli za kijamii zinazoendelea zinazohitaji umeme. Lakini kwa sababu tumesema ni Kijiji basi umeme unapelekwa pale Kijijini tu kwenye center jamii iliyo kubwa inaachwa haijapata huduma. Kwa hiyo, ninashauri na ninapendekeza maeneo haya kiwango kile cha kilomita moja kiongezeke ili wananchi wetu waneemeke na hii huduma. Na ni-appreciate kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi nadhani ipo kwenye top three za rural electrification kwa hiyo ni hatua muhimu na sisi tunaiunga mkono lakini ifanyike iendane na wakati ili sasa tuonde na hili tuende kwenye programu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la muhimu ambalo hili nadhani TANESCO walichukue. Kuna wananchi ambao wamepeleka maombi, wameshajaza fomu, wamefanya wiring muda mrefu wengine zaidi ya miezi sita lakini mpaka kesho hawajawahi kuunganishiwa umeme. Wakienda wanaambiwa mara generator sijui limefanyaje, mara waya sijui nguzo zimefanyaje, mwananchi hataki kujua habari za nguzo yeye anataka umeme uwake. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zetu wa TANESCO kwa kuwa tuliowana hata siku ile tuliwaeleza haya, mlitusikia basi naomba haya malalamiko yaondoke, wananchi waliyofanya wiring waunganishiwe umeme ili waache sasa na wao kulalamika, waneemeke na hii huduma. Mathalani pale Kijiji cha Mughamu na Kinyasatu ni zaidi ya nyumba 40 wamefanya wiring lakini hawajapata huduma, pale Miangae, Kinyeto wamefanya wiring muda mrefu lakini hawajapa huduma. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri ulichukue hili angalau tuwapatie watu hawa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru tena pia katika hii programu inayoendelea kwangu nilikuwa na vijiji 31 ambavyo vilihitaji umeme lakini kwa habari njema ni kwamba katika programu inayoendelea sasa hivi kuna vijiji nane ambavyo vinaenda kuwasha umeme kabla ya Tarehe 15 ya mwezi huu. Mimi nalipongeza sana Shirika letu la TANESCO, naipongeza sana Wizara, hata Mkandarasi wa ile Central Electrical ambae anasimamia mradi huu kule Jimboni kwangu, mpaka Tarehe 15 amenihakikishia kwamba vijiji nane vinakwenda kuwashwa umeme. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri siku hiyo uje tuambatane na wewe tukawashe umeme tukaone taa pale zikiwaka, vijana wakifurahi, wakipokea fursa hii kwa mikono miwili na kwenda kuchangamkia sasa fursa za viwanda na mambo mengine yanayohitaji umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo vinaenda kuwashwa umeme nawaomba wananchi wangu wajiandae ni Kijiji cha Muhango, Kijiji cha Mvae, Kijiji cha Kinyagigi, Kijiji cha Munkhola, Soghana, Mwanyonye na Kiyunadi hawa ninaomba sana Mheshimiwa Waziri ujiandae ili siku hiyo ikifika tuondoke mimi na wewe mguu kwa mguu tuhakikishe umeme unawaka kama ambavyo nimeahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na la mwisho kabisa ni umeme wa upepo pale Singida. Walizungumza nadhani wasemaji wawili waliotangulia hapa kuhusu huu umeme wa upepo. Nchi yetu ina uhitaji mkubwa sana wa umeme na tunafahamu gharama kubwa tunayotumia kupata umeme. Sasa kuna huu umeme wa upepo ambao unapatikana Singida, investment yake wala siyo kubwa, lakini kuna Kampuni ambayo imejitokeza muda mrefu zaidi ya miaka tisa sasa ya Upepo Energy mpaka leo tunaambiwa majadiliano yanaendelea, mazungumzo yanaendelea ile michakato tunayolalamika kila siku, mara mchakato na maneno matamu matamu kwa nini hili jambo halifiki mwisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana hili jambo sasa lifike mwisho umeme huu wa upepo utakwenda kutupatia megawati 100; lakini huyu mzabuni yeye anasema ana uwezo wa kuzalisha hata megawati 300, kwanini apewe megawati 100 tu apewe tender hii ya kutosha ya megawati azalishe umeme wa kutosha ili nchi yetu inufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, megawati 300 itapunguza tatizo kwa kiwango kikubwa sana, lakini pia kuna ule umeme wa solar pale Kititimo wa megawati 45 kwa nini hizi project hazikamiliki tender zake? Niombe sana Waziri atakaposimama aniambie tatizo hapa ni nini mpaka mchakato wa kazi/project hii isikamilike na mradi huu wa upepo kwa upande wangu kwenye Jimbo langu unakwenda kunufaisha vijiji nane ambavyo ni Msikii, Kinyamwenda, Itaja, Kinyamwambo, Miipilo, Kinyagigi na Mwanyonye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme huu ukikamilika haya maeneo yatapata umeme hata hatutahangaika na REA ambayo tunasema inakwenda kilometa moja, huu utapanua wigo utakwenda hata maeneo mengine.

Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa na yeye ni kijana mwenzangu atanisikia na yeye kwanza ni msikivu, ni mtu ambaye ni mzalendo. Kwa hiyo, niombe sana alichukue hili atakaposimama hapa aniambie nini sasa kinakwenda kufanyika kuhusu project hizi mbili; huu upepo energy pamoja na ule wa solar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya niunge mkono hoja na niwasilishe ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ABEID M. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa mchango wangu wa maandishi katika Wizara hii muhimu ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza mawaziri wa wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na zaidi nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa mstari wa mbele kuitangaza nchi yetu na vivutio tulivyonavyo hususan kupitia Royal Tour.

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu kuna msitu wa Mgori ambao unamilikiwa na wananchi kupitia Serikali za Vijiji na Halmashauri ya Wilaya ya Singida, hata hivyo wananchi hawa wapo tayari kuukabidhi msitu huu kwa Wizara ili uwe ni msitu wa Hifadhi ya Taifa ambapo hatua kadhaa zimeshanyika kukamilisha mchakato huo.

Ningependa wakati Waziri anafanya majumuisho aniambie ni hatua gani iliyofikiwa maana ni muda sasa tangu jambo hili limeanza kufanyiwa kazi. Ningependa kuona jambo hili linafikia mwisho ili msitu huu uweze kulinufaisha Taifa letu na pia wananchi wetu waweze kunufaika ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile ningependa kuishauri Wizara kuvitangaza vivutio vyetu ipasavyo na kuiboresha safari Channel TV inayotumika kutangaza vivutio vyetu. Ninashauri wawepo watangazaji bobezi katika channel hiyo, pia Balozi zetu zitumike ipasavyo kutangaza vivutio vyetu na kuhamasisha watalii wengi kuja nchini ili nchi yetu ipate watalii wengi.

Mheshimiwa Spika, namalizia kwa kusisitiza Mheshimiwa Waziri anipatie mrejesho kuhusu umiliki wa msitu wa Mgori mchakato wa Serikali kuuchukua mmefikia wapi? Kwa nini unachukua muda mrefu namna hii?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ABEID R. IGHODO: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa mchango wangu wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya ya kuiheshimisha nchi yetu katika sekta ya utamaduni, michezo na sanaa na kuwapongeza Waziri na Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mkubwa ni kuhusu kufanyika kwa matamasha ya utamaduni; Wizara ione namna bora ya kuendelea kuenzi utamaduni wa Mtanzania. Kwa mfano leo tarehe 6 na 7 Juni, 2022 Mkoani Shinyanga linafanyika Tamasha la Utamaduni wa Msukuma pamoja na kuzindua Kijiji cha Makumbusho ambapo itakuwa sehemu ya kupata historia ya eneo hilo kuanzia utawala wa kimila na desturi za Wasukuma. Sasa ni vyema Wizara ikatambua jitihada za Mkoa wa Shinyanga kwa kuwa imetekeleza kwa vitendo agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuandaa matamasha ya utamaduni lakini pia iwe ni chachu kwa Mikoa mingine kuweza kufuata mfano huo ili na maeneo mengine nayo yawe na vijiji vya makumbusho na itaweza kuwa kama sehemu ya utalii ambapo itasaidia kwa wananchi kujua asili ya makabila na historia zake, lakini pia itasaidia kuongeza vyanzo vya mapato kutoka kwa watu watakaotembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nashauri ili kuenzi utamaduni wa Mtanzania, itengwe siku au wiki ya utamaduni kwa nchi nzima ambapo mikoa yote itatumia vijiji ambavyo vitajengwa kwa kushirikiana na machifu ili Taifa liwe na siku ya kuenzi utamaduni wake. Lakini pia katika kukazia siku hiyo kuwe na sehemu ambayo itakuwa ya kitaifa ambapo kila mwaka mnaweza kufanya mzunguko (rotation) ili liwe na ladha tofauti.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuweke utaratibu wa kuandaa au kuchapisha vitabu vya kihistoria ambavyo vitaonesha asili ya kila sehemu kwa wakati huo na namna utawala wa kimila ulivyokuwa ili kuongeza wigo wa utalii kupitia fasihi andishi kwa kuwa vitabu hivyo vitakuwa vikielezea utamaduni wa kila mikoa.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa niweze kuchangia katika hotuba hizi mbili za Wenyeviti wa Kamati muhimu za Kudumu za Bunge. Kwanza naanza kumpongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mhagama, kwa kuwasililisha vizuri Hotuba ya Kamati lakini na ile ya TAMISEMI chini ya Mheshimiwa Dennis Londo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kuchangia maeneo machache. La kwanza kabisa, naomba kuanza na hili la Maslahi na Posho za Waheshimiwa Madiwani pamoja na Viongozi wa Serikali za Mitaa. Ukifwatilia mjadala wa hapa leo kwenye hizi Kamati, hasa ya TAMISEMI, utasikia sauti za Waheshimiwa Wabunge wakilizungumzia jambo hili. Mimi kipekee, naipongeza sana Serikali, katika Awamu hii ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza kuhakikisha kwamba Mheshimiwa Diwani anapata fedha yake, ile posho yake bila kukopwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani walikuwa wakikopwa posho zao lakini hivi sasa angalau wana uhakika wa kupatiwa fedha zile kwa sababu zinalipwa moja kwa moja na Serikali Kuu. Hii ni hatua kubwa na kwa mantiki hiyo, ninaiomba Serikali yangu ya CCM, iendelee kuwa sikivu na iendelee kumtazama mwananchi mnyonge hasa huyu Mheshimiwa Diwani pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji na Mtaa ambaye yeye ndiye ana-deal moja kwa moja na Miradi ile ambayo sisi tunaipitisha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye ndiye anaishi na wananchi kila siku, changamoto zinazojitokeza kwenye jamii yetu yeye ndiye anahangaika nazo. Kwa mazingira hayo, ninarudi tena kuiomba Serikali yetu hii ya CCM ambayo ni sikivu sana, imsikie tena Diwani kilio chake cha kumwongezea ile posho inayompa ya shilingi 350,000 kwa mwezi. Posho ile ni ndogo, ukiangalia hata currency tu ya nchi sasa hivi, ukiangalia mfumuko wa bei, thamani ya shilingi hivi sasa, kwenye matumizi ya kawaida tu, shilingi 350,000 ni fedha ndogo sana haikidhi mahitaji ya mtu mzima ambaye tunasema ni kiongozi, tena anasimamia Wataalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Diwani anamsimamia mtu ambaye ni graduate kwenye eneo lake lakini yeye analipwa shilingi 300,000. Hawezi kuwa na sauti, hawezi kuwa na confidence, anasimamia miradi ya mamilioni ya fedha lakini yeye analipwa shilingi 300,000, hawezi kuwa na confidence. Ndiyo unakuta hapo na yeye anaingia katikia ku-temper kuhakikisha na yeye anapata chochote kwenye miradi tunayoipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, endapo ataongezewa kutoka hii shilingi 300,000, ifike hata basi shilingi milioni 1kama kule Zanzibar. Ikishindikana hiyo basi hata nusu yake, apate hata shilingi 700,000, aweze kukidhi, kumudu, kukidhi maisha yake ya kila siku. Naomba hili, Serikali yangu hii iweze kulichukua hili na kulitazama, huko tunakoelekea kwenye bajeti hii inayokuja hata ile nyingine, kabla ya kwenda kwenye uchaguzi unaokuja, angalau Mheshimiwa Diwani awe ameongezewa kiasi fulani kwenye posho yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, naomba kuambatanisha na suala la ukubwa wa maeneo yetu ya utawala hasahasa kata na vijiji. Tunazo kata kubwa kwelikweli, ninayo Kata moja inaitwa Ughandi, ni kubwa inakaribia jimbo, ninayo Kata ya Mtinko, kubwa kwelikweli, nina Kata ya Makuro, Ngimo, mpaka kule kwa jirani zangu kule Mkalama kuna Kata inaitwa Mwangeza, kutoka mwanzo wa kata kwenda mwisho wa kata ni kilometa 70. Kata ya Ibaga, ni Kata kubwa yenye vijiji tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, haya maeneo naomba sana Serikali yangu hii, itusikie, iende kuyagawa, tupelekeeni Watendaji wa kata, tupelekeeni Watendaji wa Vijiji ili tumuhudumie mwananchi. Kumfuata Mtendaji wa Kata kutoka kilometa 70, ni umbali mkubwa ukiangalia na hali za maisha za wananchi wetu. Naomba sana tulitazame hili jambo kwa ukaribu ili tuweze kuleta tija kwenye kazi tunazozifanya za kuwahudumia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia upande mwingine wa Bajeti hizi tunazozipitisha hapa. Tunapitisha bajeti tunasema ziende zikatekeleze miradi ya maendeleo, lakini fedha haziendi kwa wakati kwa hiyo, utekelezaji wa miradi haufanyiki kwa wakati. Wakati mwingine, tunapitisha fedha lakini hakuna kabisa utekelezaji. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, tubadilishe utaratibu, fedha tunazopitisha hapa ziende kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaleta manung’uniko kwa wananchi mathalani hapa kwenye Bajeti hii iliyopita, nilitoa machozi hapa nikililia barabara yangu ile ya Singida – Ilongero Makao Makuu ya Halmashauri, mpaka hapa tunakwenda kwenye bajeti nyingine, fedha hazijaja. Hii inaleta hata mashaka kwa wananchi kule kwamba huenda tumedanganywa lakini kama fedha zingekuja kwa wakati, leo hii tungekuwa tunaifurahia Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, Serikali ihakikishe fedha tunazozitenga hapa kama Waheshimiwa Wabunge, ziende kwa wakati zikatekeleze ile miradi ya maendeleo, kuna Kituo cha Afya pale Changimu, mpaka leo fedha hamna wakati tulishakubaliana fedha ziende. Kwa hiyo, niombe tunapopitisha vitu hapa, vitekelezeke kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la upungufu wa Watumishi kwenye maeneo yetu, kwenye Sekta ya Afya, Elimu, Utawala, Walimu. Tuna kilio kikubwa sana kwenye maeneo yetu kuhusu Upungufu wa Watumishi, niombe sana…

MWENYEKITI: Ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Abeid.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, huu muda ni mchache sana, ile programu ya Dr. Samia Legal Aid Campaign ambayo imepelekwa kule na Mheshimiwa Rais wetu kutoa msaada wa Kisheria kwa wananchi wetu kule masikini, ishuke iende mpaka kwenye vijiji, iongezewe manpower. Watumishi wale wanasheria wa Halmashauri waende mpaka kule kwa wananchi vijijini ili hii programu iwe na manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa na mimi nitoe mchango wangu katika mapendekezo haya ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali yetu kwa mwaka unaokuja wa Serikali wa 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe Mheshimiwa Rais wa Mabunge yote ya dunia hii, hongera sana tunayo imani kubwa sana na wewe na dunia imeona. Ushindi huo umeonesha kwamba Bunge hili ni Bunge bora kabisa katika Mabunge ya Dunia, kwa hiyo nakupongeza na nakutia moyo tuko pamoja na wewe.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambae ameona umuhimu wa hii mipango kuwa na Wizara, leo tuna Wizara ya Mipango ambayo inaongozwa na Profesa mbobezi kabisa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo damu ya Singida hiyo, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanavyosema wenzangu hapa ninyi hapo mapacha wawili mmekabidhiwa eneo nyeti sana, mmekabidhiwa uchumi wa nchi ili mtuokoe, mtuvushe mtutoe hapa tulipo tusonge mbele kiuchumi, nchi yetu isonge kiuchumi. Ninayo imani kubwa na ninyi na ninao uhakika mtatusaidia na mtahakikisha nchi yetu inabadilika kiuchumi. Nimpopngeze pia Rais wetu tena kwa miradi mingi ambayo ametuletea kwenye maeneo yetu, katika tangazo ulilotoa la yale magari na mimi Jimbo langu tumepata gari la kubebeba wagonjwa ambalo nimekuwa nikiliimba sana hapa Bungeni mara kadhaa, leo namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu ametusikia hivyo wananchi wetu wanaenda kupata nafuu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu na hii isiishie hapo, tuendelee kufanya hivyo ili kuendelea kuokoa maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, agenda yangu kubwa hapa ni sekta ya mifugo ambayo imekuwa ni agenda hot sana hapa Bungeni na kwenye nchi yetu kwa ujumla. Kimsingi bado hatujawa na mpango mkakati kwa ajili ya kuepusha wafugaji nchini kuwa digidigi katika nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa ni watu wa kukimbia kimbia, kufukuzwa fukuzwa isivyo halali. Sasa mimi hapa nilikuwa najaribu kutazama, hivi hatujaona bado athari zinazotokana na migogoro kati ya wafugaji na wakulima hadi tunapoteza maisha ya wananchi wetu. Hatujaona athari kwenye jamii zetu kati ya wafugaji na hifadhi, bado hatujaona athari iliyopo kati ya wafugaji wakati mwingine na Kambi za Jeshi. Hawa watu bado hatujaweka mkakati ipasavyo, mkakati madhubuti wa kuhakikisha nao wanafanya kazi zao vizuri na kwa uaminifu. Naomba kwa Mpango huu tulionao sasa wa mwaka huu tunaokwenda wa fedha 2024/2025, niombe sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo atuletee mkakati wa kuhakikisha wale wazazi wake waliomsomesha kwa kuku, kwa ng’ombe waache kukimbia kimbia.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu wengi tuliopo hapa Bungeni tumetoka vijijini na wengi tumetokana na mifugo kama siyo mifugo basi ni kilimo, tuwatazame hawa watu. Wale mshahara wao ni ng’ombe, mshahara wao ni mbuzi, tunapokosa mipango mikakati ya kuwawekea mazingira mazuri tunawaumiza wanateseka, mwisho wa siku wanakuwa ni maskini wa kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana eneo hili liletewe mikakati endelevu ya kudumu ili watu hawa wafanye kazi zao kwa staha, wafanye kazi zao ipasavyo ili waingize katika Pato la Taifa inavyosapwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa ufupi sana kwenye eneo la viwanda ni muhimu sana tuje na mkakati wa kuongeza thamani kwenye mazao yetu kwa kupitia viwanda. Tuje na viwanda ambavyo vinakwenda kule kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nchi hii haina vijiji tena umeme unapatikana kila kijiji cha nchi hii bado maeneo machache tu, ninaomba sana umeme huu usitumike kuwasha tu nyumbani, utumike kwa ajili ya viwanda, hili litawezekana endapo sisi tutaacha kusafirisha malighafi zetu kuzipeleka nje. Tuhakikishe tunakuwa na processed goods ambazo tutazipeleka nje, tupeleke bidhaa nje badala ya kupeleka raw material nje ya nchi, hii itaongeza kwanza fursa za uwekezaji na itaongeza hata ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tutoke hapa tusiwe kila siku tunaongea hayo hayo tunayarudia, Waziri afanye research, Wizara hii ya Mipango ifanye research, waajiri watu wazuri kwa ajili ya kufanya tafiti kwenye maeneo haya ya uwekezaji, viwanda, ili tuondokane na masuala haya ya kila siku tunakuja hapa tunalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuna mifuko, tunasema tunayo mifuko kila mahali lakini ngozi zinatupwa, ngozi zinaharibika, ngozi hazina thamani ni kwa sababu tumeacha viwanda vyetu vya bidhaa za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna mkakati muhimu sana ambao tunatakiwa tuuzingatie na tuurudie, mkakati wa kuhakikisha yale maeneo ya uzalishaji. Leo tunasema hapa tuna kiwanda, maeneo kama ya central zone tuna mazao tunayoyazalisha, tuhakikishe tuna viwanda vyake, ametoka kusema hapa Mheshimiwa Keneth Nollo wa Bahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Magharibi wanayo mazao wanayoyazalisha tuweke viwanda vinavyofanana na mazao wanayoyazalisha hii itarurahisishia sisi kuhakikisha mazao yetu tunaya-process kwenye maeneo husika na tunatoa tunapeleka nje ya nchi bidhaa badala ya kupeleka raw materials.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine la muhimu ni kuendelea kuimarisha na kuboresha miundombinu ya usafirishaji. Bado tunayo changamoto kubwa sana ya miundombinu ya usafirishaji, barabara zetu hasa zile za vijijini ambapo ndiko tunapotoa kule raw materials, tunapotoa bidhaa bado hatujaweza kuziboresha ipasavyo, ninashauri tuendelee kuziboresha barabara zetu za vijijini, SGR yetu pia tuendelee kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

MWENYEKITI: Haya asante sana, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipatia na mimi fursa angalau na mimi nitoe mchango wangu kwenye bajeti yetu hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba lakini pia na utendaji mzuri akishirikiana na naibu wake pamoja na Wizara kwa jumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mimi niseme pia kwa uchache, niipongeze Serikali na Wizara kwa mapendekezo ya kuja na mkakati wa kubana matumizi kwa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kuepuka upotevu wa mapato ya Serikali kwenye mambo ambayo hayana msingi. Mathalani kwenye kuachana na ununuzi ule wa transaction or procurement na kuboresha mfumo wa manunuzi wa umma (TANePS). Haya mambo yatasaidia sana Serikali yetu kuepuka upotevu mkubwa wa mapato ambayo yanakwenda kwenye njia ambazo si zenyewe. Pia nipongeze ili hatua ya kutokuinyima halmashauri kwa kosa la hati chafu badala yake tujikite kwenye kushughulikia ama kuchukua hatua kwa wale watumishi ambao wamesababisha hati chafu. Hii inaenda kuwapa haki wananchi wetu ambao walikuwa wanakosa fedha zinazokwenda kwenye miradi ambazo zilikuwa zinanyang’anywa halmashauri ama wananchi wananyang’anywa bila kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende kwenye jambo lingine la muhimu la force account. Ninataka kushauri, Serikali isije ikaachana mfumo wa force account kwasababu mfumo huu ni wa muhimu sana na umesaidia sana kukamilisha miradi mingi ya Serikali kwa gharama nafuu. Mpango huu umekuwa na uwazi mkubwa kwasababu mradi unapokwenda mahali unakuwa na kamati za wahusika zinazoundwa. Kuna kamati za manunuzi, mapokezi na, matumizi. Zote hizi ni kwa lengo la kuhakikisha tunabana mianya ya upotevu wa fedha ama rasilimali za Serikali. Lakini hapohapo mfumo huu umetusaidia sana kupunguza gharama za bei ambazo zimekuwa kubwa tofauti na ambavyo kama tungeenda kwa wazabuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja alifika Naibu Waziri kule kwenye jimbo langu akakuta sink moja la choo linauzwa shilingi 97,000, ambalo lingeuzwa kwa shilingi 20,000 au 18,000. Lakini ubao mmoja unaotoka kule Mafinga uliuzwa Singida kwa bei kubwa; ubao wa 2/6 uliuzwa shilingi 18,000 badala ya shilingi 4,500. Hii ni kwa sababu ya force account ambayo inatoa ushirikishwaji kwa Serikali, kwa maana ya wananchi, ku-bargain na fundi anayefanyakazi. Lakini pia jambo hili linawaajiri mafundi wetu wadogo wadogo, linatoa ajira kwa mafundi wa kawaida kule vijijini ambao hawawezi kuanzisha kampuni. Kwa maana hiyo unaongeza mzunguko wa fedha vijijini kwa wananchi mtaani lakini. Lakini pia mfumo huu unahamisha ile ownership ya miradi kwa wananchi wetu. Wananchi wanaona hii miradi ni ya kwao badala ya kuja kukuta mradi umeota hawajui umetokea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, mimi ningeshauri, kuna miradi ambayo wanaweza wakapewa wakandarasi kama hivi tunavyoona kwenye SGR, hapo huwezi kumpa mtu wa force account. Miradi mikubwa ile ya barabara unajenga barabara inatoka Tanga kwenda Singida hiyo lazima umpe mkandarasi mradi wa barabara unaotoka Singida–Hydom kwenye mpaka Simiyu, hiyo huwezi kumpa mtu wa force account, lazima umpe mkandarasi. Kwa hiyo, tusije tukawadharau, tusije tukawapuuza mafundi wetu kwa kupitia hii force account, tutakuwa tumewaumiza sana na tutaiumiza pia Serikali kwa upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, mimi nilitaka nizungumzie pia umuhimu wa kuimarisha sekta za uzalishaji, kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuhakikisha tunazalisha ipasavyo kulisha viwanda vyetu vya ndani. Nimeona hapa Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi za kuingiza bidhaa kutoka nje. Hii inaenda kuua viwanda vyetu vya ndani. Ingepaswa uongeze kodi, kama ulivyoweka kodi kwenye mawigi ongeza kodi kwenye kucha na kope ili haya mambo yasiletwe kutoka nje unaua viwanda vya ndani, hamasisha uzalishaji wa ndani ili wananchi wetu waweze kujikita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza viwanda vitaleta ajira na vitaongeza pato la ndani. Huwezi kukusanya kodi kwenye wigi unaacha eneo muhimu la kilimo. Imarisha kilimo, ufugaji na uvuvi; na hapa nchi yetu itapata, kwanza ajira wananchi wetu watapata ajira lakini pia utahamasisha uzalishaji wa zile raw materials zinazotakiwa ziende viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,tulikuwa tuna viwanda; ningedhani hapa tungejikita kurudisha viwanda vyetu vile vya nyama. Tulikuwa na viwanda vya nyama Shinyanga na Tanganyika Packers. Leo vile viwanda ni maghala na vingine vinatumika kwenye vitu ambavyo siyo kabisa. Ninashangaa sana, sisi badala ya kuhakikisha kama nchi tunajikita kwenye uwekezaji mkubwa tunakimbilia kwenye vitu vidogo vidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana tuisaidie nchi kwa kuhakikisha tunaelekeza uwekezaji mkubwa, tuhamasishe na wawekezaji wakubwa ili tuinue, tuokeo, na tufufue uchumi wetu, tuachane na hivi vitu vidogo vidogo hivi, petty issues, ambavyo kwakweli havitaweza kuisaidia Serikali yetu na nchi yetu. Tutawezaje kujenga miradi mikubwa ambayo tunasema ile inatakiwa itengeneze uchumi wetu kwa kuvipuuza puuza hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kushauri sana Serikali, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hakikisha unakuwa na eneo diplomasia ya uchumi, uwe na wachumi wazuri, bobezi, watumie wakushauri ni namna gani tunaweza kufufua uchumi wetu na kuachana na haya mambo madogo madogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nimeona kuna pendekezo la kuongeza kodi kwenye mabasi na kwenye magari makubwa malori kutoka kwenye 2.5 million kwenda 3.5; hapa si sawa, unaenda kuua kabisa wajasiriliamali; hapa unaenda kuwaua wajasiriliamali. Nikuombe sana, wamazungumza Waheshimiwa Wabunge wengine. Naomba na mimi niongeze na nisisitize, usitake kuwaua wajasiriamali hawa ambao wamejikita huku kwenye usafirishaji. Nikuombe hiyo iliyokuwepo ada ile ibaki vilevile, usiipandishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye eneo la kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji hapa nchini. Sisi tumejikita sana periodic maintenance za barabara. Kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kwenda kukarabati barabara zetu. Ningeshauri tuachane na barabara za vumbi twende sasa kwenye barabara za changarawe. Hili jambo limetupotezea fedha nyingi sana kila mwaka. Tunategeneza barabara zilezile kwa fedha nyingi niombe sana tuachane na…

(Hapa kengele ililia kuashiriakwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kengele ya pili hiyo.

MHE. ABEID R. IGHONDO:… kutengeneza barabara za vumbi twende kwenye barabara ya changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na mengi, ninakushukuru kwa nafasi, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kusema mawili, matatu kwenye sekta hii muhimu sana ya nishati katika nchi yetu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa utendaji wake mzuri. Pia, niseme tu ukweli Mheshimiwa Dkt. Doto ni mchapa kazi, ni mtendaji na ni mtu ambaye ni msikivu kwa kusema kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilikuwa naongea naye akaniambia bwana hizi kazi wakati wowote (usiku wa manane) unasikia simu kuna jambo limetokea huko inabidi uachane na mambo yako yote ukaanze kushughulika na masuala ya dharura. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Doto tunakupongeza sana pamoja na timu yako yote akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri na Menejimenti yote kwa ujumla. Hata kule mkoani kwetu meneja wa mkoa yule anatupa ushirikiano wa pamoja na wilaya kwa ujumla, tunafanya nao kazi kwa kushirikiana. Kimsingi Wizara hii ipo karibu na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, pamoja na Wizara kwa ujumla kwa kukamilisha kwa kiwango kikubwa sana Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambalo tunasema ndiyo inaenda kuwa ndiyo tiba ya tatizo la umeme hapa nchini. Tulikuwa na janga kubwa la mgao wa umeme, sasa ule mgao tuseme ni kwamba umeondoka imebaki tu sababu za kiufundi. Kwa hiyo, hii inatupa matumaini makubwa sisi Wabunge ambao tupo moja kwa moja kwa wananchi kule. Likitokea tatizo anayepigiwa simu ni Mheshimiwa Mbunge bwana mbona mnakatakata umeme, lakini sasa hivi hilo tatizo halipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweka connection moja kwa moja Bwawa hili la Mwalimu Nyerere na nataka niseme hapa kwamba, Bwawa la Mwalimu Nyerere ni neema kubwa sana kwa Watanzania, kwa sababu linaenda kutuhakikishia uhakika wa uzalishaji wa umeme. Kwa hivyo, hata tunaposema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, hata wawekezaji sasa watakuwa na uhakika wanapoleta investment zao hapa. Wanakuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme. Kwa hiyo, niendelee kusema kabisa kwamba kusitokee watu wanabeza beza hili Bwawa, ooh mara sijui kulitokea nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa hapa niunganishe na kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali ya maji kutokana na mvua kubwa ikiwemo kule Hanang na yale maporomoko yaliyotokea kule Mbeya kwa Mheshimiwa Spika. Hata nadhani leo tumepata taarifa kule Mikocheni Njia ya ITV pale, maji yamefunga barabara yaani yamefurika imekuwa kama kabwawa hivi. Sasa kule nako kuna bwawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba hizi mvua zimekuwa excessive mwaka huu na ni masuala ya hali ya hewa. Kwa hiyo watu lazima waelewe, tusifike mahali tukaanza kubeza juhudi zinazofanywa na Serikali kwa ku-connect na mvua, mvua haiwezi kuzuilika. Hii mvua ni ya Mungu, hatuwezi ku-connect utendaji wa Serikali na mvua. Nitumie nafasi hii kuwashauri Watanzania wenzagu, pale tunapoona jambo zuri linafanyika tuliunge mkono na tulipongeze. Kama tunaona jambo halipo sawasawa tushauri kwa busara na kwa utulivu. Tusiwe tunaongeaongea vitu vingine ambavyo havina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hapa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri anapaswa kujielekeza sasa hivi kwenye sekta hii ya umeme ni kuhakikisha tunajikita ama tunajielekeza kwenye miundombinu ya umeme. Haiwezekani ikafika mahali sijui kuna transformer imesababisha umeme umekatika mahali ikawa ni kelele nchi nzima, hapana. Hivi ni vitu vya kawaida ambavyo ni vya kitaalamu (technical) ambavyo inapaswa Wizara wawe navyo karibu. Nguzo imedondoka mahali au imekatika inaleta kelele ambazo hazina tija. Kwa hiyo, lazima tujikite kwenye vitu hivi vya kitaalamu (technical) ili kuhakikisha tunaondoa malalamiko yasiyokuwa na tija ambayo kuna watu wanaingia humo humo wanaanza kupandikiza chuki ambazo wala hazina msingi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye kuzungumzia mambo mahususi kwenye jimbo, ambayo hata wenzagu wamezungumzia kwenye maeneo yao. Kwanza, ni umeme kwenye taasisi za umma, umeme unafika mahali lakini unakuta taasisi fulani imeachwa jirani pale, shule, zahanati, msikiti ama kanisa. Ni vyema na niombe sana Wizara wajikite kuangalia haya maeneo, ni muhimu sana wapatiwe umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule kwenye jimbo langu kuna Shule ya Msingi Nkwae, Idang’adu, kuna Hospitali pale Misinko, kuna Ughandi kwenyewe, kuna Mfumbu, Mjura, Ikumese, Mpambaa, Shule ya Msingi Kafanabo, Chifu Gwao Shule Shikizi, Shule ya Sekondari Mikiwu na Zahanati ya Malolo. Haya maeneo yapatiwe umeme kwa sababu hayapo mbali, umeme haupo mbali, lakini unakuta ni nguzo moja wanaambiwa hamna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri TANESCO wanapoona REA wameishia mahali wao wafike. Wasiwaache REA pekee yao wawaunge mkono kwa nguzo moja ama ikiwezekana kuwe na programu mahususi ya kuhakikisha maeneo yale ambayo REA wameishia na TANESCO nao wasaidie. Hii inaleta malalamiko wakati mwingine hata wananchi tu wa kawaida, umeme upo pale nguzo moja inakuwa ni shida, umeme hamna. Wanaambiwa bwana hapa sisi tumeishia hapa, sasa hii inaleta shida na wananchi wetu hawamjui REA, hawajui nani, wao wanajua ni Serikali. Kwa hiyo, ni vyema kukawa na coordination ya kutosha ili kusiwe na malalamiko yasiyokuwa na msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ule umeme wa kwenye vitongoji, tulikuwa tumeahidiwa kupata vile vitongoji 15, huu Mradi bado haujatekelezwa. Kwa hiyo, niishauri sasa Serikali watuletee huu mradi lakini pia kwa sasa tusiishie kwenye hivyo vitongoji 15, wa-extend waongeze huo wigo ili wananchi wengi wapate umeme. Kule kwangu kuna vitongoji ambavyo vina size ya vijiji, ni vikubwa kama vijiji. Naomba sana, kitongoji kile, tunaita Kijiji kivuli cha Mukulu wapatiwe umeme. Pale Nkwae Kijiji cha Ikiwu wapatiwe umeme, Mlimani nao wapatiwe umeme, Mburi, Ng’ongoamwandu nao wapatiwe umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kumalizia, naona umewasha mic, kwenye suala la gharama, wale wananchi wetu ambao wapo tunasema peri urban, vijiji lakini ni kama aina fulani ya kamji. Sasa hivi wanaambiwa walipe shilingi 320,000…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, hitimisha tafadhali.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Niombe ile shilingi 320,000 ifanyiwe re-thinking hata kama haitakuwa shilingi 27,000 basi ishuke itoke huko ije hata kwenye shilingi 50,000…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: … ili iwe affordable kwa wananchi wetu. Baada ya kusema haya, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Naomba na mimi pia nichukue fursa hii kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri lakini pia na kwa hotuba yake nzuri inayoonesha dira ya muelekeo mpya na mzuri wa Sekta yetu hii ya Mifugo na Uvuvi. Pia, nishukuru kwa upande wa Jimboni kwangu tuna shida kubwa ya watumishi wa Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi. Tulipata watumishi 14 kwa ujumla wake lakini bado tunayo changamoto ya watumishi wengi wapatao 93, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri uendelee kututazama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata pia vitendea kazi zikiwemo pikipiki nane lakini bado tuna upungufu wa pikipiki 17 kwa hiyo bado tunaendelea kukulilia utusaidie. Pia, huko nyuma tulikuwa tunapata hizi dawa za kuogeshea mifugo, kwa hiyo niendelee kuomba sasa hii huduma iendelee kupatikana kwa sababu mwaka huu hatujapata ile yenye ruzuku. Tunaomba Mheshimiwa Waziri uendelee kutuona katika Wilaya yetu tuendelee kupata dawa za kuogeshea mifugo katika majosho yetu kwa sababu mfugo unapokosa afya hata tija yake inakosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikukumbushe ile ahadi ya majosho 10 ambayo Waziri alituahidi siku ile alivyofika kule kwenye Kijiji cha Mwinkulu, alipokuja kwenye ile timu ya Mawaziri Nane pamoja na hiko Kijiji chenyewe cha Mwinkulu. Alituahidi kwamba angetupatia majosho 10 lakini ile kazi bado haijafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mkubwa ningetaka kujikita kwenye maeneo makubwa kama mawili, matatu hapa. Eneo la kwanza ni kuhusu maeneo ya malisho. Nashukuru sana Wizara imejitahidi kutupa mbegu, imejitahidi sana kupeleka mbegu za malisho na kuleta mbegu mpya kwa ajili ya malisho ya mifugo. Hii ni hatua kubwa lakini bado kuna changamoto kubwa ya maeneo yenyewe ya malisho. Hapa nataka niishauri Serikali, Wizara ianzishe mashamba kwa ajili ya malisho ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee mchango wa Mheshimiwa Kunambi. Amechangia vizuri sana kwenye eneo la kuwekeza kwenye maeneo ya malisho. Malisho ya mifugo kwa sasa ni biashara, wafugaji wanahitaji malisho, wanahitaji majani lakini majani hayapatikani. Watu wengi wanaamini kwamba malisho ni ya Mungu, majani ni ya Mungu lakini majani yenyewe hayaonekani. Ndiyo maana unaona kila mahali sasa hivi kuna migogoro, utakuta migogoro ya wafugaji na wadau wengine wanaohitaji ardhi. Kwa hiyo kumekuwa na shida kubwa kwa sababu hatujawekeza ipasavyo kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaangalia tu kwa tathmini ndogo au kitakwimu. Mkulima au mfugaji akitaka kupanda eka moja ya majani, yeye kazi yake kubwa pale ni kuwa na mbegu, kulima na kupanda. Mavuno yake mpaka mwisho atajikuta robota moja la majani ni shilingi 3,000. Sasa kwa mazingira kama hayo akitoa robota 300 tu anapata shilingi 900,000 lakini ukilima heka moja ya mahindi ukapata gunia 10, gunia moja ni shilingi 40,000, unapata shilingi 400,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona kwamba ukilima majani faida yake ni mara mbili zaidi na yanahitajika yana wateja. Kwa hiyo natoa wito hapa kwa Serikali na sisi ambao ni wazalishaji wa majani tuwekeze kwenye eneo la mashamba ya malisho ya mifugo na hasa hapa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa umeleta mbegu nyingi basi nikuombe uwekeze kwenye eneo la mashamba sasa. Tushushe chini kwenye wilaya zetu, kwenye ma-ranch ili wananchi wanaofuga waweze kupata hii huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Kamati pia imeeleza kuhusu kuanzisha mamlaka kamili ya mifugo pamoja na mamlaka kamili ya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ighondo...

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi kama unavyoona TRA...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ighondo, ahsante

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA, RUWASA na kadhalika na huku pia tuweke hili ili kuwe na tija kwenye ufuatiliaji na usimamizi wa Sekta hii ya mifugo. Nakushukuru kwa nafasi na naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
The Fair Competition (Amendment) Bill, 2024.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia kuhusu Miswada yetu hii ambayo ipo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambaye kimsingi ndiyo mtekelezaji wa mambo haya maana yake tunapotunga sheria yeye pamoja na Serikali wanaenda kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, mahsusi kabisa nianze na haya marekebisho ya Kifungu Namba 16A cha Sheria ya MSD, hapa lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu marekebisho haya yanakwenda kusaidia MSD kuongeza wigo wa uwekezaji hasa katika viwanda vinavyozalisha vifaatiba pamoja na dawa. Tunafahamu gharama kubwa ya dawa pamoja na vifaatiba hapa nchini kwa hiyo haya marekebisho yanakwenda kuiongezea wigo sasa mpana wa MSD kufanya uwekezaji ambao kwa kiasi kikubwa marekebisho haya yanaenda kusaidia kupunguza gharama za matibabu, gharama za dawa, bei za dawa zitapungua hapa lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ule Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 ambao unahusu Muswada wa Sheria ya Uhamiaji, Sheria ya mambo ya Diaspora pamoja na mambo yaliyomo humo ndani, hapa Mheshimiwa Rais wetu kama Mwanadiplomasia namba moja aliona umuhimu mkubwa sana alipoenda kuongea na diaspora kule, akaona umuhimu wa kuona namna ya kuweza kunufaika, ama nchi yetu kupata fursa ya wenzetu wale ambao wameenda huko nje wakapata fursa kule waweze kupewa hadhi maalum ili waweze kuongeza tija katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, hapa napo nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali kwa kuja na mapendekezo haya pia mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Utawala, Katiba na Sheria tumekuwa na majadiliano marefu na mapana ya kina kuhusu jambo hili na kimsingi tumekubaliana Serikali na Kamati zimekubaliana lakini ni maeneo machache tu ambayo yanahitaji kuboreshwa kama ilivyoonekana.

Mheshimiwa Spika, kwanza kuna suala hili la ile sera yetu ya ardhi, masuala ya ardhi yawekwe vizuri ili sasa ile special status inapokuja ikianza utekelezaji wake iweze kuendana na sheria zetu za ndani za nchi yetu. Pia kwenye ile sera yetu ya mambo ya nje ambayo tunasema inakwenda kwenye diplomasia ya uchumi iweze sasa na yenyewe ku-fit mazingira yetu ya ndani ya nchi lakini na mazingira ya nchi za wenzetu kule nje.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais hapa na niseme kwamba hapa Serikali kwa maana ya Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Ardhi na ya Mambo ya nje washirikiane ili haya mapendekezo waliyokuja nayo na maoni ya Kamati ambayo tumeshauri yafanyiwe kazi kwa haraka ili tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, diaspora wetu kuna watu ambao ni wataalam wabobezi wa mambo mbalimbali, kuna madaktari, kuna mainjinia, lakini hatuwatumii hapa nchini kwa sababu walishaenda huko, wamepata uraia kule na Sheria zetu zinawabana, kwa hiyo tunapowapa hii hadhi maalum tutapata kipato kikubwa kutokana nao.

SPIKA: Mheshimiwa Ighondo nieleweshe vizuri.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kama nimepitia vizuri taarifa ya Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kwamba hiyo sehemu imeondolewa siyo? (Makofi)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ni kweli imeondolewa lakini tumesema kwamba kuna vitu ambavyo Serikali inatakiwa ivifanyie kazi irudishe, kwa hiyo ndiyo nilikuwa nashauri sasa itakaporudisha yale maoni ambayo Kamati imeyafanyia kazi na imesema yaletwe yasichukue muda mrefu ili itakapoyaleta sasa yale maono ambayo Mheshimiwa Rais alikaa na wale diaspora akawaahidi kwamba ata-include yale maoni yao yafanyiwe kazi yasichelewe ili ile ahadi ya Mheshimiwa Rais itimie kwa wakati. Ilikuwa ni hilo Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Wazo lako zuri maadam Kamati baada ya kushauriana na Serikali ndicho ambacho kimekubalika basi tuipe Serikali muda, sasa tukiiambia tena isichelewe ikileta Bunge lijalo na likawa pale pale na wewe ni Mjumbe wa Kamati mkairejesha tena itakuwa balaa, kwa hiyo tuipe muda Serikali maana unasema usiwe muda mrefu sasa watajua uwe muda gani.

Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa maelezo yako mazuri na ndiyo hasa line ambayo mimi nipo huko.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo la usafirishaji wa binadamu pia hapa naipongeza Serikali kwa marekebisho ambayo wameyaleta, haya pia yatasaidia kulinda hadhi ya watoto wetu ambao huwa wakati mwingine wanakwenda huko nje wanapata matatizo, kwa hiyo sasa kutakuwa na utaratibu wa namna gani tunaweza tukachukua hatua inapotokea haya matatizo yamejitokeza, kwa sababu wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuweza kuwahudumia ama kuchukua hatua kwa matatizo yanayojitokeza wakiwa huko kwenye nchi za wenzetu.

Mheshimiwa Spika, kimsingi ninaendelea kupongeza na kushukuru na kuunga mkono maoni yote yaliyowekwa na Kamati, sina mambo mengi ya kusema kwa jioni hii nilikuwa na hayo machache, niombe kuunga mkono na kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2) Act, 2024
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia kuhusu Miswada yetu hii ambayo ipo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambaye kimsingi ndiyo mtekelezaji wa mambo haya maana yake tunapotunga sheria yeye pamoja na Serikali wanaenda kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, mahsusi kabisa nianze na haya marekebisho ya Kifungu Namba 16A cha Sheria ya MSD, hapa lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu marekebisho haya yanakwenda kusaidia MSD kuongeza wigo wa uwekezaji hasa katika viwanda vinavyozalisha vifaatiba pamoja na dawa. Tunafahamu gharama kubwa ya dawa pamoja na vifaatiba hapa nchini kwa hiyo haya marekebisho yanakwenda kuiongezea wigo sasa mpana wa MSD kufanya uwekezaji ambao kwa kiasi kikubwa marekebisho haya yanaenda kusaidia kupunguza gharama za matibabu, gharama za dawa, bei za dawa zitapungua hapa lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ule Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 ambao unahusu Muswada wa Sheria ya Uhamiaji, Sheria ya mambo ya Diaspora pamoja na mambo yaliyomo humo ndani, hapa Mheshimiwa Rais wetu kama Mwanadiplomasia namba moja aliona umuhimu mkubwa sana alipoenda kuongea na diaspora kule, akaona umuhimu wa kuona namna ya kuweza kunufaika, ama nchi yetu kupata fursa ya wenzetu wale ambao wameenda huko nje wakapata fursa kule waweze kupewa hadhi maalum ili waweze kuongeza tija katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, hapa napo nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali kwa kuja na mapendekezo haya pia mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Utawala, Katiba na Sheria tumekuwa na majadiliano marefu na mapana ya kina kuhusu jambo hili na kimsingi tumekubaliana Serikali na Kamati zimekubaliana lakini ni maeneo machache tu ambayo yanahitaji kuboreshwa kama ilivyoonekana.

Mheshimiwa Spika, kwanza kuna suala hili la ile sera yetu ya ardhi, masuala ya ardhi yawekwe vizuri ili sasa ile special status inapokuja ikianza utekelezaji wake iweze kuendana na sheria zetu za ndani za nchi yetu. Pia kwenye ile sera yetu ya mambo ya nje ambayo tunasema inakwenda kwenye diplomasia ya uchumi iweze sasa na yenyewe ku-fit mazingira yetu ya ndani ya nchi lakini na mazingira ya nchi za wenzetu kule nje.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais hapa na niseme kwamba hapa Serikali kwa maana ya Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Ardhi na ya Mambo ya nje washirikiane ili haya mapendekezo waliyokuja nayo na maoni ya Kamati ambayo tumeshauri yafanyiwe kazi kwa haraka ili tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, diaspora wetu kuna watu ambao ni wataalam wabobezi wa mambo mbalimbali, kuna madaktari, kuna mainjinia, lakini hatuwatumii hapa nchini kwa sababu walishaenda huko, wamepata uraia kule na Sheria zetu zinawabana, kwa hiyo tunapowapa hii hadhi maalum tutapata kipato kikubwa kutokana nao.

SPIKA: Mheshimiwa Ighondo nieleweshe vizuri.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kama nimepitia vizuri taarifa ya Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kwamba hiyo sehemu imeondolewa siyo? (Makofi)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ni kweli imeondolewa lakini tumesema kwamba kuna vitu ambavyo Serikali inatakiwa ivifanyie kazi irudishe, kwa hiyo ndiyo nilikuwa nashauri sasa itakaporudisha yale maoni ambayo Kamati imeyafanyia kazi na imesema yaletwe yasichukue muda mrefu ili itakapoyaleta sasa yale maono ambayo Mheshimiwa Rais alikaa na wale diaspora akawaahidi kwamba ata-include yale maoni yao yafanyiwe kazi yasichelewe ili ile ahadi ya Mheshimiwa Rais itimie kwa wakati. Ilikuwa ni hilo Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Wazo lako zuri maadam Kamati baada ya kushauriana na Serikali ndicho ambacho kimekubalika basi tuipe Serikali muda, sasa tukiiambia tena isichelewe ikileta Bunge lijalo na likawa pale pale na wewe ni Mjumbe wa Kamati mkairejesha tena itakuwa balaa, kwa hiyo tuipe muda Serikali maana unasema usiwe muda mrefu sasa watajua uwe muda gani.

Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa maelezo yako mazuri na ndiyo hasa line ambayo mimi nipo huko.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo la usafirishaji wa binadamu pia hapa naipongeza Serikali kwa marekebisho ambayo wameyaleta, haya pia yatasaidia kulinda hadhi ya watoto wetu ambao huwa wakati mwingine wanakwenda huko nje wanapata matatizo, kwa hiyo sasa kutakuwa na utaratibu wa namna gani tunaweza tukachukua hatua inapotokea haya matatizo yamejitokeza, kwa sababu wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuweza kuwahudumia ama kuchukua hatua kwa matatizo yanayojitokeza wakiwa huko kwenye nchi za wenzetu.

Mheshimiwa Spika, kimsingi ninaendelea kupongeza na kushukuru na kuunga mkono maoni yote yaliyowekwa na Kamati, sina mambo mengi ya kusema kwa jioni hii nilikuwa na hayo machache, niombe kuunga mkono na kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)