Supplementary Questions from Hon. Abeid Ighondo Ramadhani (28 total)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naipongeza Serikali kwa juhudi hizi za kuboresha huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini ikiwemo maendeleo yanayofanyika kwenye hii Hospitali ya Wilaya pamoja na vifaa tiba na upanuzi wa wodi.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Halmashauri ya Wilaya ya Singida inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi wa Idara ya Afya, hasa wauguzi pamoja na madaktari: Je, Serikali ina mpango au mkakati gani wa kuhakikisha inaleta watumishi wa kada hii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana ipasavyo?
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali ilijenga Kituo cha Afya cha Mgori pale ambapo hata wewe ulifika siku ile ulipokuja kuniombea kura; lakini hospitali hii hadi sasa haijaanza kufanya kazi pamoja na kwamba kituo hiki kimekamilika kwa asilimia 100 kwa maana ya majengo; hapana vifaa tiba wala gari la kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba pamoja na ununuzi wa ambulance kwa ajili ya kubebea wagonjwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani kwa ufuatiliaji wa karibu sana katika miradi ya maendeleo katika Jimbo lake hili la Singida Kaskazini ikiwepo miradi hii ya afya. Kimsingi ni kweli tunafahamu baada ya kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali ya kujenga miundombinu ya huduma za afya kwa maana ya Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mpya za Halmashauri, automatically tumekuwa na uhitaji mkubwa pia wa watumishi wakiwemo Waganga, Madaktari pamoja na Wauguzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuweka mipango ya kuendelea kuajiri watumishi hawa ili sasa vituo hivi ambavyo vimejengwa na kukamilika vianze kutoa huduma; na katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imeomba vibali vya ajira kwa ajili ya wataalam hawa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ighondo kwamba pamoja na maeneo mengine kote nchini, Serikali itahakikisha inawapangia watumishi katika Halmashauri ya Singida likiwemo Jimbo hili la Singida Kaskazini ili vituo vya afya viendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Mgori kimekamilika muda mrefu na sasa kinahitaji kupata watumishi kama ambavyo nimeongea kwenye swali langu la msingi, pia gari la wagonjwa na vifaa tiba. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwa ajili ya Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri mpya ambazo zinaendelea kukamilishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakipa kipaumbele sana Kituo cha Afya cha Mgori ili na chenyewe kipate vifaa tiba na kuhakikisha kwamba kinaanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na magari ya wagonjwa, utaratibu wa Serikali tunaendelea kuandaa mipango ya kupata magari ya wagonjwa katika Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri kwa awamu kwa kadri ambavyo tutapata fedha. Hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hicho pia ni kipaumbele na Serikali itakwenda kukitimiza.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyogeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Singida Mjini kupitia Kinyeto hadi Sagala eneo la Kinyagigi linalounganisha Kijiji cha Minyaa na Kinyagigi ilikatika kabisa na wakati wa mvua ilikuwa haipitiki ambapo maji hujaa inakuwa kama bwawa vile. Pia barabara inayotoka Makuro kuelekea Jagwa nayo pia ilikatika kabisa na ilikuwa haipitiki kutokana na utengenezaji wa chini ya kiwango. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha barabara hizi zinapitika wakati wote hasa wakati wa masika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana na mimi wakati wowote kuanzia sasa kwenda kutembelea jimbo zima kuona uhalisia wa barabara zake zilivyo hoi na ambavyo hazipitiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge ameuliza upi ni mpango mkakati wa Serikali wa kusaidia hizi barabara ziwe zinapitika wakati wote. Nimwambie tu Mheshimiwa kwamba Mpango Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakarabati, tunatengeneza na tunaanzisha barabara mpya ili kuhakikisha tunatoa huduma hiyo kwa wananchi kwa wakati wote. Ndio maana katika bajeti ambayo mmetutengea sasa hivi kuna ongezeko la fedha na kazi mojawapo ya hizo fedha zilizoongezeka ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kushughulikia barabara hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara za aina tatu; za lami, changarawe na udongo na zaidi ya asilimia 80 za barabara zetu ni za udongo. Kwa hiyo, lengu letu sisi kwa awamu ya kwanza chini ya Rais wetu wa Awamu ya Sita ni walau tuifikie nchi nzima kwa kiwango cha changarawe kwa asilimia 50. Tukijenga kwa kiwango hicho cha changarawe na tukijenga na madaraja, naamini kabisa huu uharibifu ambao unasababisha hizi barabara zisipitike wakati wote tutakuwa tumeutatua ikiwemo za Jimbo lake la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili la kuongozana naye, naomba kusema kwamba nipo tayari. Bahati nzuri nilishafika Singida Kaskazini, nafahamu miundombinu yake na changamoto zake na nilikwenda wakati ni msimu wa mvua. Kwa hiyo, tutarudi tena tukafanye kazi kwa sababu huo ndiyo wajibu ambao tumedhamiria kuufanya. Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, Serikali baada ya kukamilisha miradi ya maji, hasa vile visima virefu, huanzisha kamati za watumiamaji, lakini kamati hizi zimekuwa zikishindwa kujiendesha na hivyo kufikia mahali kushindwa kabisa kutoa huduma au kufa. Na ningependa kushauri pengine Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wale watumishi wanaotakiwa kuajiriwa na watumiamaji, na hizi kamati, waajiriwe moja kwa moja na Wizara badala ya hizi kamati halafu zile fedha kidogo zinazopatikana zielekezwe kwenye ukarabati na ununuzi wa vifaa?
Mheshimiwa Spika, lakini swali lingine la pili. Serikali ilichimba visima virefu katika Kijiji cha Misinko na Kijiji cha Kitongoji cha Gairo katika Kijiji cha Sagara, lakini baada ya kukamilisha kuchimba visima vile maji yale yalionekana yana chumvi nyingi sana na hivyo hayafai kwa matumizi ya binadamu. Serikali iliahidi kuchukua sample ya yale maji na kuyapima ili yaweze kutumiwa na binadamu, jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.
SPIKA: Sasa swali Mheshimiwa.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuhakikisha kuja na mkakati mbadala wa kuwapatia maji safi na salama wananchi wa vijiji vile? Na hapa ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri angeambatana na mimi twende tukaonje yale maji yalivyo na chumvi na hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abeid Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Kamati za Watumiamaji, hili Mheshimiwa Waziri ameshakuwa akiongea mara nyingi na ameshawaagiza mameneja wote wa maeneo yote ya Mamlaka za Maji pamoja na RUWASA kuona kwamba, wanaajiri vijana wetu wanaotokana na chuo chetu cha maji pale Dar-Es-Salaam, hasa kwenye eneo la uhasibu. Hii ni kwa sababu, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa sana katika hizi jumuiya.
Mheshimiwa Spika, na mfano mzuri uko pale kwenye Jimbo lake Pangani. Palikuwa hakuna mhasibu, waliweza kukusanya labda laki saba tu kwa mwezi, lakini baada ya kumuajiri binti ambaye ni mhasibu, msomi, mwenye profession hiyo sasa hivi wanaweza kukusanya takribani milioni nne na nusu. Hivyo, tunaendelea kutoa wito katika majimbo yote tuweze kushirikiana kuona kwamba, kamati zile tunaruhusu hawa vijana wanaajiriwa.
Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na mishahara yao itoke Serikalini; kwa sasa hivi inakuwa ni ngumu, lakini kwa sababu wao wenyewe wanakusanya fedha za kutosha wana uwezo wa kujisimamia na kuweza kulipana hiyo mishahara. Pamoja na hilo, tayari Mheshimiwa Waziri ametupia jicho la ziada kuona nyakati zile za kiangazi namna gani ya kuweza kuzisaidia jumuiya hizi.
Mheshimiwa Spika, lakini katika suala la maji chumvi kuweza kupatikana baada ya kisima kuchimbwa:-
Mheshimiwa Spika, tayari pia wataalamu wetu wameelekezwa kwenda kusimamia na kuona namna bora ya kuona chumvi hii inaweza ikatibika. Na endapo itashindikana basi, chanzo mbadala cha maji kitaweza kufikiriwa na kutumika katika utoaji maji kwenye jamii.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize mswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kuna baadhi ya vijiji ambavyo vimeachwa katika huu mkakati ambao sasa unaenda kutekelezeka wa vijiji hivi 29, mathalani Vijiji vya Sagara, Itaja, Kinyamwenda, Mwighanji, Itamka, Endesh, Sefunga, Namrama havijaonekana.
Sasa Serikali inampangao gani kuhakikisha vile vijiji vyote vilivyoachwa vionekane sasa katika ramani ili navyo vinufaike na mradi huu?
Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo yameshapatiwa umeme, kuna vitongoji vikubwa vyenye hadhi ya kijiji na taasisi za umma kama vile shule na zahanati, lakini umeme umeishia pale tu center, na hapo hapo kuna maeneo ambayo tayari walishafanya na wiring waliagizwa wafanye wiring na umeme haujafika.
Sasa ningependa kujua Serikali ina mpango gani kuhakikisha maeneo yale ambayo ni makubwa yana hadhi ya kijiji nayo yapatiwe umeme? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna vijiji ambavyo vilionekana vimebaki katika kuchukuliwa kwa awamu ya tatu mzunguko wa pili wa REA, na amevitaja vijiji sita, vijiji vitatu vya Endesh kinyamwenda na Endesh nyengine viko katika mradi wa backbone ambao unatoka Iringa kwenda kupeleka umeme mpaka Namanga, kwa hiyo ule mradi mkubwa umechukua vijiji vitatu ambavyo tutavipatia umeme. Mkoa wa Singida una vijiji saba ambavyo tumeviweka kwenye ule mradi, vijiji vitatu viko Singida Kaskazini na vitaingia kwenye huo mradi na vitachukuliwa na vitapatiwa umeme kufikia mwishoni mwa mwezi Julai.
Mheshimiwa Spika, vijiji vyengine vitatu vinavyobakia vimechukuliwa katika hivyo 26; kama tulivyosema hapo awali kwamba kuna maeneo ambayo yalikuwa yamebaki na takriban vijiji 680 vyote yameingizwa kwenye REA Awamu ya Tatu mzinguko wa pili, na yote yatafanyiwa kazi kwa pamoja ili inapofika Disemba 2022 vijiji vyote Tanzania Bara viwe vimepata umeme.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili ni kweli kwamba kuna maeneo yetu ya vitongoji bado hayajapata umeme, na kama ambayo tunavyokuwa tukisema maendeleo ni hatua taratibu tunawafikia, tulianza kwenye vijiji na tunamaliza Disemba mwakani, kwenye vitongoji tunaendelea kufika na speed yetu ni nzuri na tunamini kwamba muda kabla haujawa mrefu sana, kila kitongoji kitakuwa kimepatiwa umeme.
Mheshimiwa Spika, kwenye vitongoji TANESCO ni jukumu lao la kila siku wanaendelea kupeleke kwenye maeneo yetu, na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unapoingia kijijini utafika pia kwenye vitongoji na pia miradi yetu mingine ikiwemo densification ambayo tunatarajia ianze mwezi wa 10 itachukua walau sehemu ya vitongoji ili zoezi
hilo la kupeleka umeme kwenye vitongoji liweze kukamilika na wananchi waweze kupata umeme, ahsante.
MHE. ABEID I. RAMADHANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri yenye natumaini ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri anatuambia kwamba mkataba umeshasainiwa tangu Oktoba, 2021 ambapo utachukua mwaka mzima mpaka 2022 mwishoni. Kwa nini sasa upembuzi yakinifu uchukue muda mrefu hivyo kwa kilomita 93 tu wakati tayari fedha zipo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa hadi sasa sijaona chochote kinachoendelea katika barabara hii, Waziri yuko tayari kuongozana nami hadi site kwenda kuona na kusimamia utekelezaji wa kazi hii uanze ipasavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhan, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kilomita 93.3 ni kilomita nyingi na tunachofanya siyo tu upembuzi yakinifu ni upembezi yakinifu na usanifu wa kina ambao ndiyo utatoa sasa gharama ya hii barabara itahitaji kiasi gani. Kwa hiyo, baada ya hilo nadhani pengine kwa bajeti itakayofata ndiyo sasa tutakuwa tumepata gharama ili kuanza kuingiza kwenye mpango kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge ambao barabara hii inawahusu, mara baada ya kikao hiki cha Bunge nitatembelea Mkoa wa Singida kwani natambua barabara hii inaunganisha Singida, Manyara hadi Simiyu.
Kwa hiyo, nimejipanga kutembelea hii barabara, Mheshimiwa Mbunge awe tayari kwamba tutaongozana kuangalia hii barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nitoe pia shukrani zangu za dhati kwa hatua hiyo iliyofikiwa ambapo sasa wanyama kama vile tembo, twiga, swala na wengineo wameongezeka sana. Sasa naomba kuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je ni kwa namna gani sasa wananchi wanaozunguka msitu ule wameshirikishwa ikiwa ni pamoja na kupewa elimu ili kuepusha migogoro na migongano isiyokuwa na lazima inayoweza kujitokeza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, je, Serikali inatoa commitment gani wakati wa kutoa tangazo sasa la kuumiliki ule msitu, kupeleka mizinga ili wananchi waone fursa yaani wanufaike na zile fursa zinazotokana na huo msitu ili nao wawe sehemu ya kuutunza huu msitu? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi ni kwamba Serikali tumeendelea kupongeza Serikali za Vijiji, Wilaya na Mikoa kwa hatua ambayo wamefikia kwamba maamuzi waliyoyafanya kwanza ni mazuri; lakini pia nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumeshakamilisha tangazo na kuwa na GN ya eneo lile basi tutaanza kuelimisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo kuangalia na kuona faida za kuhifadhi huo msitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia faida nyingine zinazopatikana katika maeneo hayo ikiwemo kuhamasisha wananchi kujiendeleza na faida ya ufugaji nyuki ili kuweza kupata zao la asali lakini kwa wakati huo huo tunaweza tukaendelea kutangaza utalii na likawa eneo mojawapo la kuhamasisha watu kwenda kutembelea katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika hizi zote ni faida kwa wananchi na watarajie kwamba watafaida nae neo hili kwa sababu uhifadhi ni moja ya maeneo ambayo tunaendelea kuhamasisha nchini kote. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipatia fursa. Pamoja na majibu haya ya Serikali ningeomba kujua, kwa kuwa mradi huu ni muhimu sana katika nchi yetu, pia umechukuwa muda mrefu sana bila kukamilika. Je, Serikali sasa ina mkakati gani mahsusi na wa ziada wa kuhakikisha mradi huu unaanza uzalishaji mara moja. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema Mkandarasi tayari amepatikana kwa ajili ya majadiliano lakini tumepata changamoto ndogo ya yeye kuhitaji vitu ambavyo havikuwemo kwenye masharti ya tenda ya zabuni. Tumeshafikia mwisho na msimamo wa Serikali ni kwamba hakutakuwepo na Government Guarantee kwenye mradi huu, bali akubaliane tufanye vile tulivyokubaliana tangu mwanzo.
Mheshimiwa Spika, akikubali Januari tutaanza kufanya kazi hii na asipokubali, Serikali sasa ishaamua kuendelea mbele na Zabuni hii mpya ili tuweze kuhakikisha tunampata Mkandarasi wa kufanya kazi hii kwa wakati. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Singida imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa VETA na uhitaji ni mkubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa ajili ya chuo hiki.
Naomba commitment ya Mheshimiwa Waziri; je, Halmashauri ya Wilaya ya Singida nayo imo katika kupata chuo hiki? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhani, Mbunge wa Singida, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Singida ninachofahamu kuna Chuo cha VETA cha Mkoa wa Singida ambacho kipo katika Wilaya ya Singida. Kwa hiyo, maadam tuna chuo cha VETA cha Mkoa ambacho kipo katika Wilaya ya Singida, hatuwezi tena kwenda kujenga chuo kingine katika Wilaya hiyo hiyo. Kwa hiyo, kile Chuo cha VETA cha Mkoa wa Singida ndicho ambacho kitatumika kama chuo cha Wilaya ya Singida. Nakushukuru sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru natambua juhudi hizo za Serikali, lakini kituo hicho cha polisi cha Kinyagigi ni kidogo, lakini pia kiko umbali mrefu kutoka yalipo majengo ya Serikali ikiwemo jengo la halmashauri, hospitali ya wilaya, benki pamoja na huduma za mahakama.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha polisi chenye hadhi ya wilaya katika mji wa Ilongero?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kituo cha polisi kilichopo katika Mji wa Ilongero ni chakavu, hakina gari wala nyumba za watumishi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha huduma za kipolisi katika kituo hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kituo cha polisi hadhi ya wilaya nadhani ni jambo la kuhitaji tafakuru na niko tayari kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Wilaya ya Singida ina kituo cha ngazi ya wilaya, kinachotafutwa hapa ni kituo cha ngazi ya halmashauri. Sisi tunafahamu sote huwezi ukawa na OCD wawili ndani ya wilaya moja, lakini pale ambapo halmashauri ile itakuwa wilaya itakuwa rahisi ku- determine kwamba tunampeleka OCD and therefore anakuwa na ofisi yake, lakini tunatambua umuhimu wa kujenga kituo chenye hadhi kuliko hiki cha Daraja la C kwa sababu ni kituo kidogo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tutawasiliana kupitia Jeshi la Polisi tuone uwezekano wa kujenga kituo kikubwa kidogo kinachoweza kutekeleza majukumu zaidi ya kituo cha Daraja C.
Mheshimiwa Spika, kuhusu uchakavu tumesema tutaendelea kufanya ukarabati wa vituo vilivyo katika hali mbaya kutegemea uwepo wa fedha. Kwa mwaka huu nitaja juzi hapa baadhi ya vituo na kadri ya hali ya fedha itakavyoruhusu eneo hili la Ilongero litazingatiwa katika bajeti zetu, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya kutia matumaini ya Serikali awali ya yote kwanza nitoe pole kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini kufatia ajali mbaya iliyotokea juzi na kuuwa wananchi wanne hapo hapo na majeruhi 20 lakini hawakuweza kupatiwa matibabu kwa wakati na ipasavyo kwa sababu ya kukosa vifaa tiba katika hospitali zetu. Lakini...
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge ngoja tuelewane vizuri, kwanza ni kipindi cha maswali, pili unaongeza hoja hapo kwamba hawakupatiwa matibabu, hiyo ni hoja nzito sana, unao ushahidi ama huna? Kama huna hebu jielekeze kwenye maswali ondoa hiyo habari nyingine kabisa, kwa sababu tusije tukahama kwenye maswali tukaelekea kuanza kushughulika na hiyo hoja kwamba walifariki kwa sababu hawajapatiwa matibabu, hiyo ni hoja nzito sana kuletwa hapa Bungeni.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, maswali yangu mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, ni lini tutapatiwa ambulance katika hospitali hizi ili kurahisisha huduma kwa wananchi wetu wanaopata magonjwa mbalimbali na mengine ya ghafla kama ajali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini sasa Serikali itapeleka watumishi wa kutosha katika vituo hivi vya afya pamoja na hospitali ya wilaya ili waweze kutoa huduma kwa wakati na ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ambulance katika bajeti inayokwisha mwaka huu tarehe 30 Juni, Serikali imetenga magari ya wagojwa 195 na kila halmashauri itapata gari la wagonjwa ikiwepo halmashauri ya Singida ambayo tutapeleka kwenye hospitali hii. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba suala hilo tayari linafanyiwa kazi na gari ya wagonjwa itapelekwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na watumishi ni kweli tuna upungufu wa utumishi, lakini Serikali imetoa kibali tayari hivi sasa vijana wanaendelea kuomba ajira ya watumishi wa kada mbalimbali za afya 7,612 na miongoni mwa watumishi hao watapelekwa katika Wilaya ya Singida.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona.
Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara inayotoka Singida Mjini – Ilongero – Mtinko mpaka Haydom kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ighondo, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Singida – Ilongero inayoelekea Hydom tupo tunakamilisha usanifu wa mwisho. Tulifanya usanifu wa awali lakini sasa hivi tupo tunakamilisha usanifu na baada ya kupata hiyo detail design ndiyo sasa mipango ya kuijenga kwa kiwango cha lami itaanza.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi kwanza nitoe shukrani na pongezi kwa majibu mazuri na ambayo yanaenda kutoa matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini ambao wanasubiri skimu hizi kwa hamu kubwa.
Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Skimu ya Msange wananchi wanatumia mfumo wa mafuta, yaani diesel, kwa ajili ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji na tayari wananchi wameshatuma maombi kwa ajili ya kubadilishiwa mfumo kwenda…
SPIKA: Swali.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, je, Serikali iko tayari sasa kuwasaidia wananchi kubadilisha mfumo kutoka kwenye generator ili waepuke mafuta mengi na sasa watumie umeme?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna Bwawa la Mgori pamoja na Kisisya ambayo yamejaa tope na mifumo ya umwagiliaji imeharibika;
Je, Serikali iko tayari sasa kwenda kuyafufua mabwawa haya ili yaweze kuwasadia wananchi kuongeza kipato katika kilimo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo itakaa pamoja na Wizara ya Nishati ili kuhakikisha wanafanikisha jambo hili kuondoa wananchi kutoka kwenye generator kwenda kwenye umeme. Kwa hiyo, hilo tutakaa pamoja ili kulifanikisha hilo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Bwawa la Mgori na Kisisya ambayo yamejaa tope na yanahitaji kufufuliwa, nimhakikishie tu, kwamba nimezungumza na Waziri wa Kilimo na Wizara ya Kilimo itawatuma wataalam wake waende kufanya tathmini ili waweze kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hiyo, ahsante sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; lakini pia naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, changamoto iliyopo hapo Ikungi ni sawa sawa na iliyopo katika Jimbo la Singida Kaskazini katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo tulisha wasilisha maandiko kwa ajili ya kupatiwa soko la kisasa katika mji wa Melya njia panda ya Melya lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.
Je, Serikali inatoa commitment gani kwa ajili ya kujenga soko hilo la kisasa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi?
Swali la pili, Mji wa Ikungi pamoja na Singida Kaskazini hazina stendi zinazoeleweka za kisasa kwa ajili ya magari kuingia na kutoka. Je,Serikali sasa itajenga lini stendi hizo kwa ajili ya kupendezesha miji yetu lakini pia hata kuingizia mapato halmashuri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Igondo Ramadhani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ambayo pia iko katika Jimbo la Singida Kaskazini Halmashauri ya Singida la kukosa soko, na niwapongeze Halmashauri ya Singida kwa sababu tayari kweli walishawasilisha andiko mkakati kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa Ikungi pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwamba Serikali inaendelea na uchambuzi wa maandiko yale kuona kama yanakidhi vigezo vya kuwa miradi ya kimkakati ili fedha ziweze kutafutwa kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na changamoto ya stendi ya mabasi, Serikali imeshaweka mpango kazi kwenye halmashauri zetu zote kuanza kuainisha maeneo ambayo yanatakiwa kujenga stendi lakini pili kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani pamoja na Serikali kuu kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga maeneo hayo. Kwa hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Stendi hizo zinajengwa, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Katika Jimbo la Singida Kaskazini Kijiji cha Kinyeto na Ilongero kuna bwawa la Ntambuko ambalo wananchi wanapata shida...
SPIKA: Swali lako.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali italeta kivuko katika bwawa la Ntambuko linalounganisha Kijiji cha Itamuka, Ilongero na Kinyeto?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tumelichukua hilo na TEMESA watakwenda kufanya study ili waone kama kivuko kinaweza kikajengwa kwenye hilo bwawa alilolisema kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa pande hizo mbili. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Serikali imekuwa na utaratibu wa kuagiza mafuta ya kula nchini, ambayo yameua kabisa soko la mafuta ya alizeti ambayo Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara walihamasisha sana ulimaji wa alizeti. Sasa ni lini Serikali itaacha utaratibu huu ili kulinda bei ya mafuta na alizeti hapa nchini? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli msimu huu kidogo bei ya alizeti imeshuka kwa mkulima. Tunafahamu kwamba mkulima akiuza alizeti chini ya shilingi 900 mpaka ikafika shilingi 700, maana yake anapata hasara. Kama Wizara, tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya fedha kupitia upya maamuzi tuliyoyafanya mwaka 2022 ya ku- reduce tax ya import ya refined palm oil mpaka kufika asilimia 25, kuiangalia impact yake na athari yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nataka niliambie Bunge lako tukufu, import substitution strategy tuliyofanya kama Serikali na ninyi Waheshimiwa Wabunge ya kusaidia kuwekeza kwenye alizeti, ukiangalia report ya BoT ya mwezi huu wa Machi iliyotoka, inaonesha kwa kiwango gani hatua tulizochukua zimepunguza importation ya mafuta ya kula kwa wakati huu wa uzalishaji wa mafuta ya alizeti yameongezeka.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hatutaruhusu zao la alizeti kufa kwa sababu Serikali inachukua hatua mbalimbali na tutapitia changamoto hizi zilizojitokeza kwa mwaka huu wa fedha ili kuweza kumlinda mkulima na kuhakikisha nchi inajitosheleza mafuta.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa upembuzi yakinifu sasa umekamilika je, Serikali iko tayari sasa kutenga fedha kwenye bajeti hii tunayoijadili hivi sasa ya 2023/2024 kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi wa barabara hiyo ambayo inakwenda mpaka makao makuu ya halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili je, Serikali sasa iko tayari kufanya upembuzi yakinifu kwa kipande kinachounganisha barabara hii cha kutoka hapo Ilongero makao makuu ya halmashauri kupitia Ighanoda kwenda ngamu kilomita 27.1 ambayo inatuunganisha na Wilaya ya Hanang Mkoa wa Manyara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba tumeshakamilisha usanifu wa hii barabara na sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha. Na nataka nisiji-commit hapa, kwamba kama bajeti tumeshatenga, lakini itategemea na upatikanaji wa fedha, kwa sababu baada ya kukamilisha usanifu kazi inayofata ni kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami; na ndiyo hiyo dhamira ya Serikali kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu barabara aliyoitaja ambayo inaanzia Ilongelo hadi Ngamo ni barabara fupi kama kilomita zisizozidi 27. Naomba nimuagize Meneja wa Mkoa afanye tathmini ya gharama kwa ajili ya kuanza kufanya usanifu kwa barabara hiyo, halafu aipeleke Makao Makuu kwa ajili ya kufikiria kuiweka kwenye mpango wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa hicho kipande cha barabara cha Ilongelo kwenda Ngamo, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu haya ya Serikali. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa soko hili pamoja na stendi ni hitaji kubwa la Wananchi wa Singida Kaskazini. Je, ni lini hasa Serikali itakamilisha hiyo tathmini ili kuweza sasa kutoa nafasi kwa miradi hii kuanza kutekelezeka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa halmashauri imeanza kutenga fedha kidogo kidogo lakini hazitoshi. Je, Serikali sasa ina mkakati gani mahsusi ya kuhakikisha inatumia vyanzo vingine vya fedha kuhakikisha ina supplement ili kukamilisha miradi hii kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba soko na stendi hii ni hitaji kubwa la wananchi na Serikali inatambua hili na ndio maana imeelekeza ifanyike tathmini. Tumewaalekeza Halmashauri hii ya Singida ihakikishe inakamilisha tathmini ndani ya miezi mitatu na kuleta maandiko hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili yaweze kupitiwa na kufanyiwa maamuzi.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itatenga fedha baada ya kufanya tathmini, itatenga fedha kwa ajili ya kuongeza nguvu za kukamilisha ujenzi wa stendi lakini pia soko ambalo linahitajika, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu haya mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza je, Serikali sasa ina mpango gani mahususi wa kuwapatia wakulima nchini zana za kisasa za kilimo hususani matrekta ambapo sasa hivi tunaona wananchi wetu wanatumia jembe la mkono katika maeneo mbalimbali?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani mahususi wa kufanya kilimo cha umwagiliaji kuwa ni ajenda ya kitaifa ambapo wananchi wetu sasa waweze kulima mara mbili kwa mwaka kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua. Tuna maeneo mengi yenye maji kama Singida Kaskazini, lakini bado hayajatumiaka ipasavyo. Tunaomba mkakati mahsusi wa Serikali kuhusu ku–mechanize kilimo chetu.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge kuhusu zana za kilimo kama alivyosema tunaendela kufanya mageuzi katika matumizi ya zana za kilimo za kisasa ili wakulima wetu waweze kuzalisha kwa tija na hivi sasa tunashirikiana na CARMTEC na Shirika la TEMDO katika kuja na teknolojia mbalimbali na zana mbalimbli za kusaidia katika uzalishaji katika sekta hii ya kilimo. Lakini kubwa kuliko yote ni kwamba tunakwenda kuanzisha mechanization hub katika ikolojia mbalimbali za nchi yetu ya Tanzania kikanda ili wakulima wetu pia waweze kutumia fursa hiyo ya kuweza kutumia mitambo hiyo ya kukodisha badala ya mkulima kwenda kukopa trekta huko ana ekari mbili na kuingia gharama kubwa, tunaweka vituo hivi kwa ajili ya ukodishaji wa zana za kilimo za kisasa.
Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu mipango mahususi katika eneo la umwagiliaji, kama nilivyokuwa nikisema hapa ndani ni dhamira ya Serikali kuhakikisha ya kwamba tunatekeleza kwa dhati kabisa eneo hili la umwagiliaji kwa kuweka mipango madhubuti na mkakati mkubwa hivi sasa ni kuhakikisha scheme zetu zote za umwagiliaji nchini zinafanya kazi, lakini hatua kubwa na ya kwanza ni kuhakikisha kwanza tunaweka vyanzo vya uhakika vya maji ili scheme hizo ziweze kufanya kazi na wananchi waweze kuhudumia mashamba yao zaidi ya mara moja ndani ya mwaka mmoja.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii nzuri na muhimu sana, naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba muda mwingi Wabunge wako hapa Dodoma kwa shughuli za Kibunge na kama unavyofahamu Mbunge wakati wote anafanya kazi za wananchi. Lakini kwa hapa Dodoma Wabunge hawana ofisi, ofisi zao zimekuwa ni magari, ukienda kwenye gari unakuta amerundika makabrasha mengi ambayo angepaswa kuwa na ofisi ili aweze ku-attend issues mbalimbali za kibunge.
Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea ofisi Wabunge hapa wawapo kwenye shughuli zao za Kibunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameleta mapendekezo, na kila mapendekezo yanahitaji bajeti, tunahitaji kwanza kufanya tathmini na kuona uwezekano wa utekelezaji wa jambo hilo. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tumepokea jambo hilo, tutakwenda kulifanyia tathimini, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mhehimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi, pamoja na majibu yao ya Serikali lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini sasa fedha hizi ambazo amezitaja Mheshimiwa Waziri zitaletwa kwaajili ya kuboresha miundombinu ya vituo hivi vya polisi vya Mtinko na Ngamu pamoja na kujenga vile vingine vya Msange na Ngimu maana yake tayari maeneo yapo?
Swali la pili nataka nijue, Serikali sasa inamkakati gani wa kujenga kituo cha polisi cha hadhi ya Wilaya katika Mji wa Ilongero ambao unakuwa kwa kasi unawatu wengi, lakini pia na kwa sasa ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya kwa hiyo, unahitaji usalama, huduma na pamoja na kwamba kituo hicho sasa eneo hilo linanyumba za polisi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili nyongeza ya Mheshimiwa Ighondo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja lini fedha? Bahati nzuri tumeshafanya tathimini tumepata shilingi milioni 46.4 zinahitajika kwaajili ya kukamilisha ukarabati huo, lakini katika mwaka huu wa fedha kama tulivyosema tutaendelea kutoa fedha kwa awamu kulingana na upatikanaji wake. Niombe kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mwaka ujao tunachukua commitment ya kuweka fedha hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mkakati wa kujenga kituo cha polisi cha hadhi ya Wilaya niseme tu kwamba Wizara pamoja na Serikali kwa ujumla kuhakikisha tunajenga kituo chenye hadhi ya wilaya kwenye Makao Makuu ya Wilaya sasa hii ni Wilaya ya Singida ambayo OCD anaofisi yake lakini tutakachoweza kufanya ni kuimarisha vituo vya polisi ngazi ya kata na tarafa ili viweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi badala ya kila jimbo kuliwekea kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya. Nashukuru.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Manyoni Magharibi ni mbaya, eneo lile ni kame. Pamoja na juhudi hizi za Serikali, sasa Naibu Waziri haoni umuhimu wa kuongeza kasi ya kupeleka mabwawa zaidi pamoja na majosho katika Jimbo la Manyoni Magharibi ili kuwasidia wakulima wetu pamoja na wafugaji ambao mifugo yao inapata tabu kwa kipindi cha kiangazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Singida Kaskazini katika bajeti ya mwaka 2023/2024, Serikali ilitupatia miradi ya majosho manne katika Kijiji cha Minyenye, Ghalunyangu, Muhamo na Mangida. Kwa bahati mbaya fedha hazikuja kwa ajili ya kutekeleza miradi hii pamoja na kuwa wananchi tayari walishaanda upande wa nguvu kazi.
Je, sasa ni lini Serikali italeta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hii ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge kwamba, mabwawa ambayo yaliahidiwa kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka wa fedha wa bajeti bado haujaisha. Namhakikishia kwamba, jinsi ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unapatikana, tutakwenda kuyajenga hayo mabwaka kama ambavyo bwawa tulilokwishalikabidhi tayari limekwishajengwa katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu kuongeza kasi ya ujenzi wa haya mabwawa, ni kweli kama nilivyokwisha jibu kwamba, tumeshakabidhi bwawa la kwanza na Serikali sasa inaendelea kutafuta fedha zingine kwa ajili ujenzi wa mabwawa mengine. Tunakiri kwamba, Wilaya ya Itigi ni miongoni wa wilaya kame ambazo zinahitaji kuongezewa mabwawa na majosho kwa ajili ya kuisaidia mifugo yetu iliyoko katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea kufuatilia na inaendelea kutafuta namna ambavyo inaweza kusaidia ujenzi wa mabwawa katika Wilaya hii ya Itigi, ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, ninashukuru kwa maelezo mazuri ya Serikali ingawa hayajajibu swali langu la msingi kwamba ni lini maeneo haya ya utawala yatagawanywa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari vikao vya wilaya kwa maana ya DCC pamoja na RCC vimeshakaa na kuleta mapendekezo Serikali. Kwa hiyo, nilitegemea nipate majibu sahihi hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa imebainika kwamba kuna gharama kubwa sana zinatumika katika kuendesha shughuli za Serikali kwenye kusimamia miradi, lakini kutokana na ukubwa wa maeneo haya Serikali ina mpango gani? Haioni haja ya kuongeza fedha kwa ajili ya usimamizi wa miradi kwenye maeneo yetu haya ikiwemo vyombo vya usafiri?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, sote Waheshimiwa Wabunge, ni mashuhuda kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana ya kujenga miundombinu ya majengo ya utawala kwa maana ya Ofisi za Halmashauri, Ofisi za Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Vijiji na Kata, kazi hiyo bado inaendelea haijakamilika. Ndio maana Serikali imeweka kipaombele kwanza kukamilisha majengo ambayo tayari yanajengwa ili yatoe huduma vizuri. Baadaye tutakwenda kuanzisha maeneo mengine ya utawala ili tuhakikishe kwamba maeneo yaliyoanzishwa yanatoa huduma ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu uhitaji na ukubwa wa kijiografia ya maeneo haya. Mara Serikali itakapoanza kutoa kipaumbele katika kuanzisha maeneo mapya ya utawala tutawapa kipaumbele Halmashauri hii ya Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ukubwa wa maeneo na kuongeza gharama ya usimamizi wa miradi ni kweli. Ndio maana Serikali inaendelea kupeleka vifaa vya usimamizi yakiwemo magari, pikipiki na kadhalika. Ninamhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia mapato ya ndani tutaweka kipaumbele kwenye yale maeneo ambayo yana maeneo makubwa zaidi ya kijiografia na Serikali kuu tutaendelea kufanya hivyo, ahsante sana.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Wananchi wa Kata ya Kinyagigi Jimbo la Singida Kaskazini wamejitolea nguvu zao na kuweza kujenga kituo cha afya, kwa maana ya jengo la OPD na baadhi ya majengo, lakini bado kunahitaji gharama za ukamilishaji ambazo ni shilingi milioni 100.
Je, Serikali sasa haioni haja ya kuwasaidia wananchi hawa ili kumaliza jengo hilo ili kituo hicho kianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza niwapongeze Wananchi wa Kata ya Kinyagigi ambao wamejitolea nguvu zao na kujenga majengo haya. Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatafuta fedha aidha kupitia mapato ya ndani ya halmashauri au Serikali kuu kwa ajili ya kupata hii milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kujua pamoja na kupata hii miradi, lakini utekelezaji wake hadi sasa bado haujafanyika. Kwa hiyo, ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia utekelezaji utaanza?
Mheshimiwa Spika, la pili kuna baadhi ya maeneo mengine ambayo pia yana changamoto ya mawasiliano ikiwemo Kata ya Maghojoa, Kinyagigi, Kinyeto na katika Vijiji vya Minyaa na Kimbii. Ni lini sasa Mheshimiwa Waziri anaweza akanipatia miradi ya minara katika maeneo haya ili wananchi wetu waache kutaabika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ameuliza ni lini utekelezaji utaanza? Tunatarajia mwaka ujao wa fedha maeneo haya yote uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunakuja kuyafanyia tathmini na kuweza kuyapatia huduma, lakini katika Kata hizi za Kinyeto na kata nyingine ulizozitaja UCSAF inakuja kufanya tathmini na lengo ni kuhakiki uhitaji halisi, ni lazima huduma iweze kufikia maeneo haya yote. Kadiri tutakavyopata fedha kuanzia mwaka ujao wa fedha tutahakikisha wananchi nao wanapata huduma nzuri ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuku kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nashukuru kwa majibu hayo, japo naamini kwamba Mheshimiwa Waziri ama Serikali itakubaliana nami kwamba tatizo hili la mmomonyoko wa maadili nchini ni kubwa kuliko hatua ambazo tunachukua. Sasa naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kuhakikisha tunachukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na masuala haya ya mapenzi ya jinsia moja pamoja na mashirika ama watu wanao-support ama wanaosaidia kuenea kwa jambo hili hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kutunga sheria ya kudhibiti masuala ya mapenzi ya jinsia moja hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ni kosa la jinai kwa Kifungu Na. 154 cha Sheria, na Kanuni za Adhabu Sura ya 16 inatambua mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kosa hilo ataadhibiwa kifungo cha miaka 30. Ikithibitika na mtendewa aliridhia kufanyiwa kitendo, basi atahusika na kosa hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, sheria na kanuni na adhabu zipo. Kinachotakiwa ni kufanyiwa marekebisho. Bunge la Kumi na Mbili, Mkutano wa Kumi na Moja, Kikao cha Sita aliagiza Serikali kushirikiana na Tume ya Sheria kuhakikisha kwamba tunafanya utafiti kwa kushirikiana na Tume ya Sheria ambayo mabadiliko yatakayofanyika yafikishwe katika Bunge lako Tukufu. Tume inaendelea na kazi hiyo, na mara baada ya kumalizika, Muswada huo utaletwa Bungeni ili kujadiliwa na kupitishwa. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni lini sasa Serikali itaanza rasmi ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya kutoka Singida Mjini - Hydrogas - Ilongero ambayo tuliahidiwa hapa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara ya Singida – Ilongero nadhani kilometa 10 au 12 zimeshapata kibali cha kutangazwa. Kwa hiyo, muda wowote zitatangazwa ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; nakiri kwamba tumepokea standby generators katika Hospitali ya Wilaya na Kituo cha Afya Mgori. Majenereta haya bado hayajaanza kutumika kwa kipindi kirefu sasa kutokana na kukosekana vile vibanda vya kuweka standby generators. Je, ni lini Serikali itaweza kujenga hivyo vibanda ili haya majenereta yaweze kutumika na kule kwenye Vituo vya Afya vya Mgori na Makuro ambavyo havina?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vyote vilivyopo katika Jimbo la Singida Kaskazini havina vyumba vya kuhifadhia maiti. Je, ni lini Serikali itajenga mortuary ili kuepusha usumbufu unaotokea pindi inapotokea dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwamba, Mheshimiwa Rais ameshapeleka fedha, majenereta yamenunuliwa kwa ajili ya hospitali ya wilaya na vituo vya afya. Kazi yake ni kujenga kibanda kwa ajili ya kuweka jenereta, ili wananchi waanze kupata huduma. Kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, namwelekeza kwamba ndani ya siku 45, mwezi mmoja na nusu, ahakikishe amekamilisha ujenzi wa vibanda hivyo na majenereta hayo yafungwe yaanze kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu majengo ya kuhifadhia maiti. Serikali inaendelea kutafuta fedha na kujenga miundombinu hiyo katika vituo vyetu kwa awamu. Pia, tunaendelea kusisitiza kwamba, mapato ya ndani ya halmashauri yatumike kwa ajili ya kujenga baadhi ya miradi ikiwemo majengo haya muhimu katika jamii zetu ya kuhifadhia maiti. Kwa hiyo, halmashauri ianze kufanya tathmini hiyo, lakini kama uwezo hautaruhusu, basi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itaunga mkono juhudi ambazo watakuwa wameanza utekelezaji wake. Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu haya ya Serikali, naomba kuuliza; kwa kuwa, Serikali imekiri uwepo wa tatizo hili ambalo linasababisha pia kupotea kwa ubora wa mafuta haya ya alizeti na tathmini siyo mkakati, Serikali sasa ina mkakati gani mahususi ikiwa ni pamoja na kuzielekeza halmashauri kujenga vibanda vya kutunza ubora wa bidhaa hii ambayo ni chakula ili pia kutunza afya za walaji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kumekuwa na changamoto ya kushuka kwa bei ya mafuta ya alizeti pamoja na alizeti yenyewe panapokuwa na uzalishaji mkubwa. Ni upi mkakati wa Serikali ili kutoa bei elekezi isiyoyumba panapokuwa na uzalishaji mkubwa wa alizeti ili kumnufaisha mwananchi wa chini kabisa ambaye kazi yake kila siku ni kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua changamoto hiyo na tunafanya tathmini ili sasa tuandae mkakati wa kurekebisha changamoto hiyo kutokana na evidence ambayo tutaipata baada ya kufanya tathmini ya kimazingira.
Mheshimiwa Spika, suala hili ni jumuishi, kwanza linahusisha wafanyabiashara wenyewe, na pia linahusisha halmashauri na viongozi wa halmashauri hizo, wilaya, mkoa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifahamu hilo na inalichukulia very serious, ili tuweze kulifanyia tathmini na kuweka mkakati ambao unakubalika kwa pande zote za wafanyabiashara, wateja, pamoja na Serikali.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na changamoto ya bei ya mafuta ya alizeti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu mafuta ya alizeti yanauzwa kwa soko huria, lakini Serikali imeendelea kutengeneza mazingira na kuweka mazingira bora zaidi kwa ajili ya bei nzuri zaidi ya alizeti na pia ya mafuta. Kwa hiyo, Serikali imepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge na tutayafanyia kazi pale inapowezekana ili tuweze kuboresha zaidi bei ya mafuta ya alizeti, ahsante.