Contributions by Hon. Simai Hassan Sadiki (17 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi kuwa mchangiaji katika bajeti hii ya leo. Natumia nafasi hii kuwapongeza sana watendaji wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulihakikishia Taifa hili linapata maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ningependa ujikite zaidi katika suala zima la uendeshaji sekta ya utalii. Duniani kote wataalam wa utalii wanapozungumza suala zima la utalii wanaainisha vitu vitano wanaita A5; kuna vitu vitano ambavyo ndivyo uti wa mgongo wa utalii. Kitu cha kwanza ni amani na utulivu tuliokuwa nao; Kitu cha pili ni vivutio duniani kote ambavyo vinapelekea watalii kwenda kutembelea; Kitu cha tatu miundombinu inayoweza kufikika katika sekta hiyo na kitu cha nne ni good service. Katika suala la good service Tanzania bado hatujakuwa more advance; na Kitu cha tano ni suala la promotion and marketing.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mimi zaidi nitajikita katika suala zima la promotion and marketing. Tanzania takriban tupo nchi ya pili kwa kujaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii duniani. Nchi ya kwanza Brazil, lakini cha kushangaza na cha kusikitisha sisi bado hatujajiwekeza zaidi katika kutangaza biashara hii. Ukiangalia duniani kote utalii siku zote unaletwa na matamasha, maonyesho pamoja na festivals, lakini sisi Tanzania mpaka hii leo tuna matamasha yasiyozidi manne wakati wenzetu Brazil wana matamasha yasiyoshuka 58. Ukija nchi kama Spain wana matamasha 48 na Uingereza wana matamasha 54.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusitarajie sana kutangaza utalii wetu kwa kutegemea zaidi labda Tanzania Safari Channel ya TBC, inawezekana hata hiyo TBC hata Dubai watu hawawezi wakaisikia. Unapoangalia channel kama vile CNN pamoja na Sky News utaona utaona nchi za wenzetu kama vile Belarus, Bulgeria wameweka clip zao ndogo ndogo kuonyesha jinsi gani nchi zao zilivyokuwa na vivutio vingi vya utalii. Tuangalie mfano nchi ya Jirani hapa hii wanayoita Rwanda ni nchi ndogo sana, tumewazidi kwa vivutio vingi sana vya kitalii, lakini wao wanatumia bajeti kubwa katika kuwekeza katika sekta hii. Wameweza kuisaini Memorandum of Understanding na timu kama ya Arsenal, unapoangalia jezi za Arsenal mkononi hapa wameandika visiting Rwanda. Kwa hiyo wanatumia bajeti yao katika kuitangaza hii sekta nzima ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru sana ndugu zetu Simba, kama wenzetu wengi walivyokwisha kuelezea, wakati ambapo walipoenda kushiriki hizi ligi za klabu bingwa barani Afrika walijaribu sana kuitangaza Tanzania. Hata hivyo, lazima tukubali utalii wetu wa Afrika hususan Tanzania unategemea zaidi watalii kutoka Magharibi mwa Ulaya pamoja na nchi za Amerika na Nordic countries, sasa huko Simba bado hawajaweza kufika. Kwa hiyo, lazima tutafute njia nyingine za kuweza kuwekeza kama vile tunaweza kutangaza utalii wetu katika ligi kubwa kama vile ligi za Bundesliga Uingereza kule pamoja na nchi nyingine kama vile Ufaransa tukiwa tuna clip zetu za kuweza kututangaza tunaweza kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Tanzania tumebahatika kuwa na vyanzo vingi vya maji, lakini Watanzania bado hatujaelimishwa namna gani tunaweza kuvitumia vyanzo vya maji kama ni sehemu moja ya utalii. Katika vyanzo vya maji tuna uwezo wa kupata utalii wa water sport, hauhitaji gharama nyingi wala hauhitaji bajeti kubwa ukilinganisha na utalii wa aina nyingine. Tanzania tuna visiwa ambavyo havitoshuka 220, havishuki hapo, lakini duniani kote utalii ambao una thamani zaidi ni utalii wa kivisiwa, lakini ukitizama huku kwetu sisi visiwa hatujaweza kuviorodhesha kama ni sehemu ya kitalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wanatumia visiwa kama sehemu ya kitega uchumi, lakini sisi badala ya kujaliwa neema hiyo tutumie kama ni sehemu ya kitega uchumi tunaenda katika migogoro. Nimpe mfano Mheshimiwa Waziri; kuna kisiwa kimoja kinaitwa Latham Island ambacho kwa jina maarufu tunaita tunaita Fungu Mbaraka, watembezaji wa watalii wanapotoka kule Zanzibar kwenda kuangalia kile kisiwa pale wakiwa na wageni mara nyingi wanazuiliwa sana, kumekuwa na malalamiko ya aina yake kwa watu wa TMA (Tanzania Marine Authority) kwa kushirikiana na fisheries, wanakuwa wanawazuia kwa sababu wana leseni za kibiashara kutoka Zanzibar. Wanafanya kitendo kile hali ya kwamba wale watembeza wageni wanao wageni na wageni wanafahamu kile kinachozungumzwa, hii inatuharibia, sisi sote tunajenga nchi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwa kuongezea kuna suala zima la miundombinu. Utalii ni sekta ambayo haiwezi ikajitegemea yenyewe lazima inategemea sekta nyingine. Mtalii anapotoka kwao haji hapa na embe, haji hapa na wali katika hotpot, wala haji hapa na gari ya kutembelea, anatarajia aje hivyo vitu avikute hapa. Cha kusikitisha sehemu nyingi ambazo zimepitiwa na sekta hizi za utalii wanafanya biashara…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kuweza kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji katika ripoti hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mawaziri wote pamoja na Wizara zao na Serikali kwa ujumla kwa kuwa na nia safi kabisa ya kutunga sheria kulingana na mazingira na mabadiliko ya nchi na dunia kwa ujumla yanayoendelea kutokea kila siku. Ni ukweli usiopingika Tanzania ni kama sehemu moja wapo ya dunia ni wazi hatuwezi kuishi bila kufuata sheria na kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hata kama Bunge hili tutaazimia kwamba tuondoe sheria zote za nchi hii, bado tutaendelea kuishi katika zile scope za sheria za kimaumbile, kwa sababu binadamu toka azaliwe anaongozwa na sheria. Kwa maana hiyo hii inaonesha wazi umuhimu wa sheria katika maisha ya binadamu ni sawasawa na umuhimu wa maji hatuna namna ya kuweza kuziepuka sheria na kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la msingi kabisa la kuzingatia katika utunzi mzima wa sheria tuelewe ya kwamba sheria siku zote ndizo ambazo zinakuja kuonesha ule uhalisia wa maisha ya wananchi yaliyowazunguka, kwa hiyo, sheria zinatakiwa na sheria ndizo zitakazokuwa zinaongoza maisha na matendo halisi ya nchi na raia wanaoishi katika sehemu hiyo, lakini suala la kujiuliza; je, ni kwa namna gani sheria hizi zinaakisi na zinafikia malengo halisi ya utunzi wa sheria zilizokuwa bora?
Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli sisi kama Kamati tumeweza kupitia sheria nyingi na kusema kweli niipongeze Serikali kwa kazi wanazoendelea kuzifanya, lakini changamoto haziwezi zikakosekana, utaona kwamba mantiki walizokuwa nazo Wizara na Mawaziri wetu katika utunzi wa hizi kanuni na sheria ni nzuri na unaweza kuikuta kanuni ile kwa asilimia 100 inawezekana inakidhi matakwa na mahitaji ya jamii husika, lakini ikakosa ubora kutokana na kipengele kimoja tu au vipengele viwili ikaitoa maanani sheria yote ikaonekana haina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika utaratibu huu ni vizuri zaidi kwa watunzi wa kanuni na sheria kuzingatia mazingira na matakwa halisi ya sheria na jamii nini inachohitaji kwa wakati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano ningependa sana nilizungumzie ule usawa na uhalisia wa sheria na kanuni tulizoweza kuzipitia na mazingira halisi ya Watanzania tunayoishi. Nichukulie mfano ukiangalia mfano Sheria Ndogo ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Halmashauri ya Itigi kipengele namba 14(3) kinaeleza wazi kwamba abiria yeyote atakayetupa taka nje ya basi la abiria basi itachukuliwa kosa hilo limefanywa na dereva, kondakta au mmiliki wa basi hilo, ukiangalia mantiki ya kutunga hiyo sheria unajua wazi kwamba lengo ni kuweka usafi wa mazingira katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la usafi wa mazingira katika nchi ni suala la Kikatiba ni wajibu wa kila mtu, ukiangalia Ibara 27(1) ni wajibu wa kila Mtanzania kuweka mazingira safi na salama. Tunajua dhamira ilikuwa ni nzuri lakini nani wa kuadhibiwa? Hakuna utaratibu duniani kosa lifanywe na mtu ‘A’ baadaye aende akaadhibiwe na mtu ‘B’ hiyo sheria itakosa maana, hivi kweli kosa kafanya abiria itakuwaje aende akaadhibiwe kondakta au mmiliki wa basi? Kwa nini? Tutoke na tukimbilie kumtafuta mmiliki wa basi, wakati mmiliki wa basi, dereva au kondakta katekeleza majukumu yake kuhakikisha usafi unadumu na unatekelezeka katika gari yake pengine kaweka dustbin na vifaa vingine vitakavyoweza kusababisha usafi usitoke nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini abiria mwenyewe tu akaamua kufungua kioo akatupa taka nje, leo hii unaenda kumkamata nani dereva, uwajibikaji katika sheria na usawa uko wapi? Sasa ukiangalia katika mazingira kama hayo haitokuwa hiyo sheria ina uhalisia katika utekelezaji, kwa sababu ni mwiko katika sheria kuadhibiwa mtu kwa kosa ambalo hakustahiki kuadhibiwa nalo hakuna kitu kama hicho duniani na haya itakuwa tuseme kwamba Tanzania tunatunga sheria za kwamba aliyefanya kosa mtu mwingine baadaye anakwenda kuadhibiwa mtu mwingine maana yake lile lengo la sheria halitofikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu lengo la sheria ni kumfanya yule ambaye amefanya kosa kupata adhabu ili kutoa funzo kwa wengine wasirejee makosa kama yale, sasa leo kosa kafanya baba umeenda nyumbani baba umemkosa unamkamata mama na watoto haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ikiwa katika nchi hii tukitunga sheria za namna hiyo, tusema kwamba tunatunga sheria kwamba anayefanya kosa siye anayehusika moja kwa moja katika adhabu tunazidiana kwa niaba hivi kweli nchi inaweza kutawalika, sio kweli kabisa kitu cha namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kusema kweli katika hali kama hii tuangalie ile mantiki ni nini na kipi kinachotakiwa kufanywa ili sheria zetu ziweze kusadifu mazingira halisi na kugusa wale walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliishie hapo nchi yetu kwa asilimia kubwa raia wake ni wakulima na wafugaji. Wakulima wanaishi sana katika sehemu za kijiji, vijiji vingi ndivyo ambavyo unaweza ukawakuta wakulima; ukienda katika Ibara ya 4(1) ya sheria ndogo ya Ada na Ushuru ya Halmashauri ya Itigi utaona wameweka baadhi ya masharti ambayo yanawataka wakulima wanapotaka kulima lazima wafuate kalenda ya Halmashauri, sio wazo baya lakini unajiuliza how come inaweza kutekeleza hii sheria kwamba sisi sote tulime kwa kufuata kalenda ya Halmashauri, ipo wapi hiyo kalenda ya Halmashauri. Namna gani una uwezo wa kuifuata wapi ipo, je, ni namna gani mwananchi anauwezo wa kuielewa imeandikwa, imebandikwa sehemu, imetangwazwa yaani unapatwa na maswali mengi ambayo yanauwezo wa kukosa majibu katika application yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuiandika ni rahisi, tamu kumeza, lakini ngumu kutafuna yaani kuitamka tu hivi kuiandika inawezekana kuwa rahisi, lakini namna gani katika utekelezaji wake ndipo shida inapokuja. Unaposema kwamba tufuate kalenda ya Halmashauri, tukienda katika aspect za utekelezaji kilimo unaweza ukakuta katika mazingira tuliyokuwa nayo mtu analima vile anavyojisikia, hakuna mtu anayelazimishwa kwamba bwana wewe uende ukalime analima kwa wakati wake na anavuna kwa wakati wake. Sasa ukisema kwamba tufuate hiyo kalenda, hiyo kalenda unapata maswali inaanzaje katika mazingira kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu analima yeye mwenyewe anavyojisika, anavuna yeye mwenyewe anavyojisikia, lakini hakuna sheria hata moja inayoenda kumlazimisha mtu kwamba lazima alime kwa eneo la ukubwa wa kiasi fulani, kwa maana hiyo itakuwaje tuki-impose kifungu cha sheria kinachotaka wakati wa kulima lazima ufuate kalenda ya Halmashauri, haiwezekani, itakuwa hilo ni jambo gumu. Unajiuliza hivi Halmashauri wana kalenda ya mvua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake unaweza ukajiuliza mvua wanakalenda nayo wanajua ni exactly wakati gani mvua ina uwezo wa kunyesha. Hivi katika mazingira ya kawaida tunayoishi wale raia wa kawaida vijiji huku hivi taarifa hata hawana leo hii mnamtungia sheria za namna hiyo tunajua mantiki ni nini, lakini tuangalie ule uhalisia wa hiki kitu ambacho tunachotaka kwenda kukisimamia, pengine tukikosa kukiwekea mazingira mazuri basi hata utekelezaji wake utabakia katika maandishi tu lakini uhalisia utakuwa haupo kwa sababu kuna mazingira mengine mtu analima pengine kutokana na kipindi hiki nalima mazao haya na ardhi yangu nalima hiki hana kalenda huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwingine anaweza akasema kwa kipindi hiki nina uwezo wa kufanya jambo moja, mbili, tatu au ana uwezo wa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji, hili kalenda ya Halmashauri ina nafasi gani katika suala hilo, lakini ukiachilia hapo katika wakulima vile vile kuna suala la wafugaji Ibara 3 ya hiyo kanuni na hiyo vilevile haikuacha imewekea masharti ambayo ni magumu kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hiyo kanuni inamtaka mfugaji yeyote atayekuwa anafuga wanyama katika Halmashauri ya Itigi ni lazima idadi ya mifugo itaamuliwa na Halmashauri, Halmashauri ndio itakayokupangia wewe, wao ndio mabwana wakubwa itakupangia idadi ya mifugo utakayotakiwa kufuga. Kiukweli kabisa ukisoma hiyo sheria unajua mantiki ni nini tunajua kabisa ni matumizi bora ya ardhi pengine, lakini ukienda katika application vipi inaweza kutekelezeka, vipi inaweza ukaenda kum-control mfugaji amenunua eneo lake huko kijijini anafuga kuku wake, wewe utampitiaje mfugaji mmoja mmoja wa kuku halafu um-control. Hivi kweli inaweza kutekelezeka mtu anafuga kuku wake, njiwa, kwa sababu hiyo sheria ukija kutafsiri hilo neno wanyama, wanyama inajumuisha mjumuiko mpana zaidi maana yake ngo’mbe, kuku, bata, njiwa hata kunguru na mende pia vilevile ni Wanyama. Kwa sababu sheria imejumuisha, je, ana uwezo wa kufuga na nani? Ni binadamu na mende siku hizi wanafugwa na binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namna gani ukiangalia unaweza kuchukua kama ni vitu vidogo vidogo lakini ukiangalie yule anayeiandika anaenda kuisimamia ni tofauti, sasa yule anayekwenda kuisimamia inawezekana akaja na mtazamo tofauti na yale malengo yaliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa masuala kama hayo ni vizuri yakawa under control, ni vizuri kwakuwa hizi sheria nyingi za Halmashari zinazotungwa takribani zote zinakuwa zinafanana sasa ili kuepuka matatizo kama haya ni vizuri watunzi wetu wa sheria wakawa wanaangalia ile mifumo inayoongoza katika utungaji bora wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kuweza kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji jioni hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie fursa hii kuwapa pole sana wananchi wa Jimbo la Kijini pamoja na wananchi wa Jimbo la Nungwi, hasa katika Vijiji vya Kidoti, Tazari na Kilimani kutokana na athari za upepo mkali ulioharibu nyumba na mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali yangu tukufu ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona namna ya kuweza kuwafariji wananchi wale waliopata majanga yale ikizingatiwa kwamba upepo ule ni miongoni mwa athari za mabadiliko ya tabia nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, mchango wangu ninapenda kuuelekeza moja kwa moja katika suala zima la maadili, mila, sinka na taratibu za Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani muda huu tuliokuwa nao nchi zote zimeweza kugawika katika makundi mawili; zipo nchi zinaokubaliana na masuala ya ushoga, ndoa za jinsia moja, lakini zipo nchi pia ambazo zinapinga vitendo hivi. Hofu yangu ipo kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na hatua tunazochukua juu ya kukabiliana na suala hili. Kusema kweli bado hatujachukua hatua za kuridhisha na kuonesha u-serious wetu kama tunavyokuwa serious katika kupambana na majanga mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano; yakitokea maradhi ya kuambukiza nchi za jirani utakuta ghafla Serikali inaanza kuchukua jitihada za kufunga mipaka kuzuia wageni kuingia katika nchi hizi ambazo wageni wanatoka katika nchi ambazo zinasadikika kuwa na maradhi hayo. Lakini hali iko tofauti katika suala hili la ushoga. Changamoto tunazozikuta kutokana na suala hili, sisi tuliopitiwa na majimbo ambayo yamezungukwa na utalii ni kubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani, na ni muumini wa kila siku; Tanzania tumekuwa na sheria nyingi zinazoweza kutosheleza kukabiliana na hali hii ya ushoga. Lakini changamoto inakuja katika suala zima la usimamiaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ninapenda nitoe mfano, Jimbo langu la Nungwi ni jimbo la kitalii na ilivyojengeka au ilivyoaminika ni kwamba sehemu kubwa zinazoendesha biashara hizi za ushoga, za ndoa za kiume, ni sehemu ambazo zimepitiwa na sekta ya utalii. Kinachonihuzunisha, unaweza kuwakuta maaskari wanatoka nje ya Nungwi, wanatoka sehemu tofauti na Zanzibar kukiwa kuna sherehe au hali yoyote katika mazingira ya Nungwi unaweza ukakuta maaskari wapo wengi wanakuja kwa ajili ya kutunza mazingira ya pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha ni kwamba badala ya kwenda kufanya doria katika matukio waliopangiwa wale maaskari unaweza kuwakuta maaskari wamekwenda kuzongea na kuwanyang’anya waendesha bodaboda bodaboda zao na kuzipeleka kituo cha polisi kwa ajili ya mazungumzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonisikitisha maana ya hiki ninachokizungumza kinatuweka na masuala mawili mazito. Inawezekana kwa Tanzania yetu ya kileo suala la waendesha bodaboda kukosa helmet likaonekana kwamba lina athari kubwa zaidi kuliko suala la ushoga.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
T A A R I F A
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nilikusudia nieleze kuhusiana na hatua ambazo Serikali kwa ujumla wake imechukua kuhusiana na changamoto hii ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumza kwenye hotuba ya bajeti yangu kwa kirefu, lakini naona huu ni mchango takribani wa pili umekuwa ukiishutumu Serikali juu ya hii kadhia ambayo inaendelea duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ambayo nataka kutoa ni kwamba kwanza, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali kupitia kauli mbalimbali za viongozi wetu kuanzia Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mara kadhaa wamelizungumzia na wameonesha hisia zao na hasira juu ya matatizo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hatua ambazo tunachukua kama Serikali, zinaratibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, atakuja kueleza mwenyewe. Lakini kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa kama Wizara ambayo inasimamia usalama wa nchi hii na utekelezaji wa sheria hizo, kuna mambo mengi ambayo tumeyafanya ya kimkakati. Hofu yangu ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wasidhani kwamba Serikali haichukui hatua kwenye jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi; kuna masuala ambayo yanahusu usimamizi wa sheria kwa upande wa Jeshi la Polisi, kuna watu wengi ambao wanahusika katika mambo kama haya wameshachukuliwa hatua mbalimbali, na wengine wapo katika uchunguzi. Kuna hatua za kiuhamiaji kwa wale ambao wanajihusisha na masuala haya wanaotoka nje ya nchi kupitia taasisi mbalimbali, hatua hizo za kiuhamiaji vilevile zimeshachukuliwa za kiuhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hatua za kitaasisi kupitia taasisi mbalimbali ama jumuiya zinazojishughulisha na mambo haya, tunashirikiana vizuri na Mheshimiwa Waziri, Dkt. Gwajima, ambaye anasimamia NGOs na mimi nasimamia jumuiya za kiraia, kushughulika na taasisi na jumuiya hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hatua ziko nyingi sana. Niombe Waheshimiwa Wabunge pale ambapo nitakuja kusoma hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tutaeleza kwa kina.
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, waelewe tu kwamba Serikali iko very serious na tatizo hili na hatua nyingi zinachukuliwa na pongezi kwa jitihada zao ambazo wanaendelea.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuchangia hoja yangu; naipokea taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea, maaskari wamekuwa waki-deal zaidi na waendesha bodaboda, kitu ambacho kinawapa hofu Watanzania juu ya ukubwa wa waendesha bodaboda kukosa helmet na suala la ushoga. Kitu kinachotia hofu zaidi ni kwamba hivi kuna ugomvi gani baina ya vijana wetu wa bodaboda na maaskari polisi? Lakini hivi kuna uswahiba gani uliopo kati ya baadhi ya maaskari na wale wanaojihusisha na vitendo vya ushoga? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni maisha, tuwasome kisha tuwasomeshe kwa vizazi vyetu. Mwanadamu amekuwa akinywa pombe zaidi kuliko maji safi na salama kwa afya yake. Mwanadamu amekuwa akiwatupa na kuwatelekeza viumbe ambao amevizaa yeye mwenyewe wakati kuku na bata wanaendelea na utaratibu wao uleule wa kuwalea na kuwa na mapenzi kwa watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanadamu wamekuwa na tabia ya kutaka kuzaa na wale waliowazaa au watakaowazaa lakini simba wanaendelea na utaratibu wa kuwafukuza watoto wao wanapofikia umri wa balehe na kuwataka waende wakajitegemee ili kuepusha tu kuzaa na wazazi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote hapa ni wazazi, sote ni walezi na sote tuna familia. Mzazi na mlezi wa kweli ni yule anayeguswa na changamoto za mtoto wa mwenzake. Katika hili wanyama tangu walipoumbwa hawajawahi kubadilisha tabia zao lakini binadamu tumebadilika na kuwa na tabia za kinyama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mashekhe, mapadre, wanaendelea kupaza sauti kukemea ushoga na vitendo hivi vinavyoambatana na mambo hayo, Serikali iko bize zaidi katika kukusanya mapato na tozo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijifanya hatuyaoni haya, tunayafumbia macho, badala yake tukiacha kudumisha mila na kuendekeza nguvu zaidi katika kukusanya mapato kwa wahisani na wawekezaji ambao baadhi yao hawana tija.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miaka michache tutakuwa na chanzo kipya cha kukusanya mapato kupitia mashoga.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, taarifa hiyo iwe fupi tafadhali.
T A A R I F A
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba tumekuwa tukipigana vita kubwa sana katika kuhakikisha tunatunza maadili ya nchi hii na vizazi vyetu; tumekuwa tukiongea sana. Jambo ambalo nimeliona ni kwamba ufuatiliaji wa nini Serikali inafanya kwa Watanzania wengi na wawakilishi wao siyo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeimba mpaka nyimbo za don’t touch here, here and there kama vile tunachekesha, ni kupeleka hamasa hiyo, tumetengeneza SMAUJATA, Jeshi la
Jamii la Wazalendo, wako kule wanafanya maandamano… Kilimanjaro jana…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, yote hiyo ni kuamsha, na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepeleka barua kwamba agenda hii iwe ya kudumu kwenye mabaraza yetu ya halmashauri ya Madiwani na Kata.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachangia.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Simai, endelea na mchango wako.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningelipenda niendelee na hoja yangu nakusisitiza kwamba kama tutaendelea kuwa busy zaidi katika masuala ya kukusanya mapato kuliko ku-deal na mila na desturi za Kitanzania basi tujiandae Watanzania kuwa na chanzo kipya cha kukusanya mapato kupitia mashoga kwa sababu kasi ya ushoga inaongezeka kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile maana ya…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji katika hotuba ya bajeti ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Wizara ambayo ipo mezani kwetu tunayoijadili leo ni Wizara inayoenda kugusa hali halisi za watanzania kwa jina lingine kule mitaani hii tunapenda kuita Wizara ya kitoweo kwa sababu Mifugo na Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakupongeza sana kwa bajeti yako kwa kiasi fulani imefanya kazi na imejibu hoja kwa kiwango kikubwa ambacho Wabunge tulitarajia kusikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri wewe ni rafiki yangu sana na urafiki wetu umekuja kutokana kwamba wewe unatoka eneo linalotoka wavuvi na mimi natoka maeneo yanayotoka wavuvi kule Zanzibar. Lakini ni ukweli kabisa sina lengo la kuzuia shilingi kwa namna yoyote ila wakati ambapo utapoweza kuwasilisha bajeti hii na kuja kutuhutubia kwa mara ya mwisho kufunga hotuba yako ukishindwa kutuelezea yale matarajio ambayo Wabunge sisi tulitarajia kuyasikia yawepo katika hotuba yako basi sisi tutaacha kujadili hotuba yako baadaye tutakuja yale ambayo wananchi wametutuma tuje tuyazungumzie hapa kwasababu wao ndio wanapenda wayasikie hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu bora ambazo zimejaaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji katika Bara la Afrika, Tanzania tumebahatika kuwa na mito mingi, kuwa na bahari kuu kuwa na maziwa mengi tu inasemekana hata chanzo cha mto Nile kinapatikana Tanzania na ndio maana nchi za jirani zetu zinazotuzunguka kama vile nchi za Malawi, Kongo, Zimbabwe zinategemea sana kupata samaki wao kupitia Tanzania kwa mfano Kongo na Malawi ni wafanyabiashara wakubwa sana wa dagaa kwa nchi ya Tanzania naizungumza hii kwasababu ya kuonesha jinsi gani umuhimu wa sekta hii ya mifugo ilivyo kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake dagaa kwa kiasi kikubwa hata akinamama na wavuvi wadogo wadogo wana uwezo wa kuifanya hii shughuli, licha ya umuhimu wa sekta hii lakini bado sisi kama Serikali hatujawa serious katika kuwekeza na kutafuta wawekezaji watakaoweza kuja kui-support sekta hii na sina doubt na utendaji wa Mawaziri. Kwasababu wakati mwingine tunaweza kuwabebesha mzigo mkubwa Mawaziri nimejifunza kitu leo Waziri wa Uvuvi na Mifugo unatuwasilishia bajeti katika bajeti iliyopita utekelezaji wake maana yake fedha iliyokuja katika utekelezaji wa miradi ya bajeti ni asilimia 3.3 katika miradi ya maendeleo lakini kwenye mishahara asilimia 66. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi haya tunayoyapanga kwenda kutekeleza kama fedha usipopewa unakwenda kutekeleza nini, maana yake wakati mwingine tuna uwezo wa kumbebesha lawama mtu ambaye hastahili ingawa sio lengo, sasa kama kweli tunataka kunyanyua mifugo yetu kama kweli tunataka kuendeleza sekta ya uvuvi ni lazima Serikali tuangalie utaratibu wa kuwawezesha wavuvi wetu, hivi sheria na hizi taratibu za uvuvi ambazo zinaonekana kwamba ni kikwazo kwa wavuvi wadogo na wavuvi wakubwa hakuna haja ya kuendelea nazo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo hii unaweza ukatunga sheria ukamwambia mtu usivue sehemu fulani, nyavu fulani usitumie kuvua lakini ukashindwa kumpa mbadala wake hakuna anayependa kufanya uhalifu lakini mazingira wakati mwingine yanalazimisha na sheria ngumu zikachangia katika hayo. Mheshimiwa Waziri Serikali ione haja ya kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo za uvuvi itafute njia na ikae na wawekezaji watakaoweza kuisaidia sekta hii ya uvuvi watakaoweza kuwapatia wavuvi wetu vifaa vya uvuvi kama vile mashine, na pembejeo nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wavuvi wetu wanavua uvuvi ambao ni wa holela mtu anatoka anakwenda kuvua lakini hajui wapi anapokwenda anakwenda kubahatisha hajui samaki wapi anakwenda kuwakamata huku tutoke kwenye njia hizi za local sasa hivi twende na utaratibu unaokubalika tulingane na wavuvi wenzetu wa dunia za nchi nyingine. Katika hili nioneshe mfano mmoja nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa jitihada kubwa anazozifanya kupitia sera ya uchumi wa bluu lazima tumpongeze kwa hilo. Yeye sasa hivi ameshaandaa takribani boti 557 kwenda kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo na vi-holi vile vya kuvunia mwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali kama hii wananchi wamekuwa wanavua maji madogo samaki wengi tunawaacha katika uvuvi wa maji marefu au bahari kuu lakini kule watafikaje? Vyombo wanavyotumia ni mtumbwi, mtumbwi hauwezi ukautumia kwa uvuvi wa maji marefu au uvuvi wa bahari kuu na ndio maana unasikia kesi nyingi zinakuja, Mamba kala Mtumbwi na abiria aliyekuwepo ndani yaani huu ndio ukweli ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu sasa katika mazingira kama hayo ndio tunasema tunawathamini na kuwa-support wavuvi wetu sasa katika suala hili bajeti ya killimo ipo vizuri kwasababu asilimia kubwa imewagusa wananchi wadogo lakini sekta nyingine ipi inayowagusa wananchi wadogo na wakombozi wa maskini, ni sekta hiyo ya uchumi wa bluu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wale watu ambao wanaonekana hawana ajira watu ambao wanaharakati wanaona kwamba bamba gumu kwa upande fulani wa kimaisha wanajikita katika sekta hizi ya uvuvi na mifugo. Maana yake na sisi kama Serikali tuwatafutie njia sahihi tukae na tujue tunawa-support vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikwambie kitu kimoja tujifunze kutoka kwa wenzetu nchi kama Norway iliyokuwepo Bara la Ulaya ni miongoni mwa nchi zinazojulikana kama Nordic Countries hii nchi inazalisha gesi nyingi nchi hii inazalisha mafuta mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kiukweli asilimia 70 ya uchumi wao inategemea uvuvi kwanini, wao wamewasaidia wavuvi wao na wakaipa thamani inayostahiki sekta hii ya uvuvi. Mheshimiwa Waziri katika hili unapozungumzia suala la zima la uvuvi, kilimo, ufugaji maana yake unazungumzia vitu tofauti na mazingira yatatofautiana, kwa kule Zanzibar sisi sekta ya uvuvi ndio mkombozi wetu, kwa sababu ardhi yetu sisi ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watu. Lakini kwa huku upande wa bara kilimo lazima kitakuwa na tija na kitapewa support kubwa sasa sisi tunategemea hii sekta ya uvuvi zaidi ikilinganishwa na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali kama hii Mheshimiwa Waziri kumekuwa na changamoto kubwa mno kwa wavuvi wetu hususani katika masuala haya ya hawa wanaohusika na huu uvuvi wa bahari kuu, changamoto za leseni ni bei kubwa mno Mheshimiwa Waziri kwa maskini, leseni za uvuvi wa bahari kuu maana yake ni changamoto kwa wavuvi, lakini isitoshe suala la kuwachaji mara mbili wavuvi wanaotoka Zanzibar regardless aina gani ya uvuvi kwa sababu vyombo vile wanakuwa wamevikatia leseni wanapokuja huku wanachajiwa tena leseni, matatizo kama haya ni masuala ya kukaa na kushirikiana na wale wenzenu wa Zanzibar kutafuta zile changamoto kuondosha hili migongano isiyokuwa ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri najua Wizara yako ukiangalia waajiriwa wengi sio rasmi na hii ningependa unipatie ufafanuzi kitu kimoja Mheshimiwa Waziri, kuna suala zima la mvuvi na changamoto zinazowakabili lakini research fupi niliyoifanya kwamba changamoto hizi zinatokana kwamba wewe na Wizara yako humjui mvuvi ni nani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ninazungumza na kama sio kweli basi ningeomba unifafanulie hakuna sheria ya Tanzania hii inayomtafsiri moja kwa moja maana ya mvuvi ni nani, naizungumza hii kwa hoja yangu. Hapa unaomba fedha kwenda kuwasaidia wavuvi unaomba fedha hizi kwenda kuwasaidia wavuvi lakini wavuvi ni nani wakati hatuwatambui katika sheria, umeweka tu katika sheria taratibu za uvuvi ukaweka aina za uvuvi lakini hakuna maana leo hii inapotokea fursa za mikopo…
MWENYEKITI: Malizia sentensi yako Mheshimiwa.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja inapotoka fursa za mikopo zinaenda kwa wafugaji na wawindaji wa paa zile nyavu badala ya kwenda kuwindiwa baharini kwa sababu mtu leo atoke na mshipi aende kuingia chomboni utahesabu kama ni mvuvi kwa mujibu wa sheria zenu. Sasa hizi fedha badala ya kuomba kwenda kuwasaidia hawa wavuvi tuletee yaani omba fedha hizi kwa ajili ya kurekebisha kwanza angalau hizi changamoto ndogo ndogo zinazotokana na… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashirikia kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kuweza kunipa fursa hii ya kuchangia katika hoja ya leo. Sambamba na hilo, natumia fursa hii kumpongeza sana Waziri na Naibu wake pamoja na Kamati zao zote kwa kubwa wanazozifanya. Hakika Watanzania tunajivunia kuwa nao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kulifanya Taifa hili la Tanzania kuwa au kufikia hatua ya kukamilisha ufuataji wa misingi ya Utawala Bora, Haki, Usawa wa Kijinsia katika uwajibikaji, ni lazima tuhakikishe kwamba wananchi wa Taifa hili wananufaika na rasilimali zao sambamba na kutekelezewa mahitaji yao na Serikali yao wanayoitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna masikitiko makubwa mno kwa wastaafu wetu. Wafanyakazi wa Taifa hili wanakuwa na wasiwasi mkubwa sana juu ya mafao yao mara baada ya kustaafu kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa mfano mmoja. Kuna watu wamestaafu kazi toka mwaka 2003, hadi hii leo tunapozungumza bado hawajapatiwa mafao yao ya kustaafu kazi hiyo. Mimi Jimboni kwangu kuna mfano mzuri, kuna watu mwaka 2004 walipewa hadi cheque za kwenda kuchukua malipo yao lakini kufika kule katika Taasisi inayohusika mtu anaambiwa jina la mwisho limekosewa. Kwa mfano, naitwa Simai Hassan Ali, limeandikwa Simai Hassan Ally, ile Y ya mwisho tu. Kitendo cha kurekebisha cheque hiyo mpaka hii leo tuna miaka si chini ya 18 bado kurekebisha cheque haijarekebishwa. Kitendo ambacho kinakuwa kinaleta manung’uniko na masikitiko makubwa kwa wastaafu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ningependa kuzungumzia suala zima la watu wanaohusika na mitandao. Kuna mapato makubwa sana ambayo Serikali hii tunayaacha. Ni lazima Wizara ya Fedha ipitie tena VAT, lazima wapiti tena hao watu wanaohusika na wanaofanya masuala ya miamala ya kifedha mtandaoni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna vyanzo vingi sana na kuna pesa nyingi sana ambazo sisi tunazipoteza pindi kama tutazisimamia fedha hizo basi tuna uwezo wa kupata hata madawati ya kushughulikia shule zote za nchi hii. Tuna uwezo wa kuendeleza miundombinu mingi tuliyokuwa nayo. Kiukweli kabisa, watoa huduma hizi za kifedha kupitia mitandao kusema ukweli kodi wanayolipa ni tofauti sana na faida wanayoipata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nisingependa kuizungumzia faida yao lakini tuangalie ule uhalisia wa kile ambacho wanakipata kupitia Taifa hili na kile tunachowalipisha sisi. Sisi tunahitaji Bodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Sambamba na hilo, tunaelewa kwamba Wizara ya Fedha ndiyo Wizara inayosimamia uchumi wa nchi hii chini ya usimamizi wa BoT. Wakati huo huo, BoT ndiyo mhusika mkuu wa thamani ya fedha wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kitu cha kusikitisha BoT wakati inapoweka vigezo vya kiuchumi wanapenda sana kuangalia upande mmoja tu wa Tanzania Bara, hawaangalii sana vile vigezo vinavyotumika kule Tanzania Visiwani. Kwa mfano, Tanzania Bara wanatoa kipaumbele kwenye masuala ya kilimo, mazao kama vile karanga, korosho lakini Tanzania Visiwani tuna mazao ya kimkakati kabisa ambayo ni pekee kabisa. Ukiangalia tuna uzalishaji mkubwa wa karafuu, tuna uzalishaji wa mwani, tuna utalii lakini sasa wakati ambapo hatuvipi tija kupitia BoT, hatuvi-promote vitu hivi kusema ukweli inakuwa inaleta ukakasi na masikitiko makubwa kwa upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tuelewe sisi sote ni nchi moja lakini tuna mifumo miwili. Licha ya kwamba tuna mifumo hiyo miwili tofauti, ila pesa yetu na uchumi wetu unakuwa unasimamiwa na BoT, BoT ni kitu ambacho kinasimamia maslahi ya pande hizi zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika kusimamia hilo, kama ntakuwa sikosei ni lazima sasa imefikia wakati Wizara ya Fedha ije isimamie vizuri ule mradi unaoitwa JSFC (Joint Sterling Financial Committee) kitu ambacho kinakuwa kinajumuisha taasisi zote za kifedha baina ya Tanzania visiwani na Tanzania Bara. Tutakuwa tunapata ule uwajibikaji wa pamoja na kuondoa malalamiko kwa upande mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ningependa sana nizungumzie suala la microfinance na BoT. Tanzania tuna malalamiko makubwa kwa vijana wetu kwa kukosa ajira lakini kusema kweli matangazo mengine na maagizo mengine yanapokuwa yanatoka wananchi wanakuwa wanaa msikitiko makubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuchukulie mfano kitendo cha BoT, kwa upande mmoja inawezekana walikuwa sahihi lakini upande mwingine kuzuia haya masuala ya Bureau de Change na kutoa agizo kwamba masuala ya ubadilishaji fedha lazima yafanyike katika Taasisi za Kibenki za Serikali inakuwa ni mtihani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna sehemu nyingine tuna uwezo wa kuzikosesha uchumi wake mkubwa katika halmashauri kwa mfano Halmashauri za Arusha na Visiwa vya Zanzibar. Tunategemea sana mapato yetu kupitia hii Sekta ya Utalii lakini sasa tunapokuwa tunapoziruhusu hizi benki chache kuweza kutoa huduma hizi za ubadilishaji wa fedha inakuwa inaleta ukakasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali yetu sisi kuna siku za kazi na siku zisizokuwa za kazi. Kwa mfano, siku ya Jumapili hakuna kazi. Sasa inakuwa ngumu kwa mtalii anapokuja hapa kumwambia kwamba anataka kwenda kubadili pesa, kumwambia leo Jumapili hakuna kazi. Kwa maana hiyo, siku hiyo mtalii itabidi alale na njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ningependa nizungumzie issue za siri za Kibenki kwa wawekezaji. Kumekuwa na malalamiko makubwa sana kwa wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa kwamba, Taarifa zao za Kibenki mara nyingi zinakuwa wazi. Serikali mara nyingi kupitia hizi Taasisi za Kibenki wanakuwa wanaziiingilia ndani hizi taarifa za wawekezaji hawa kitu ambacho kinakuwa kinaivunjia sifa na hadhi nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitakuwa kitu cha busara kwa akaunti za wawekezaji wakubwa, wafanyabiashara maarufu kwamba hata muuza dagaa ana uwezo wa kukuambia akaunti ya mwekezaji fulani ina kiasi gani. Hii inakuwa sio kitu kizuri. Lazima tuwe na utaratibu wa kuhifadhi siri za benki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna nchi kama vile Dubai, Uswiss, wao hata kama Serikali basi inapokwenda kudai documents kwa masuala ya makampuni makubwa yanayowekeza katika nchi ile inakuwa ni shida kupewa kwa sababu wameingia makubaliano na makubaliano hayo ni ya kimkataba yanaongozwa na siri. Maana yake ni kuwa Benki ni issue ya siri kwa kuzingatia tu kwamba pesa hizo zinazokuwa zimo humo zitatumika kwa maslahi ya Taifa na kwa utaratibu ambao haukiuki misingi ya nchi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna tatizo jingine hapa. Imefikia hatua kwamba Tanzania kweli tunataka mpaato ya nchi yetu kwa ajili ya kuongeza mishahara kwa wafanyakazi…
SPIKA: (Kicheko)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji jioni hii ya leo. Napenda kutumia fursa hii kuipongeza sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuja na bajeti ambayo Watanzania waliokuwa wakiililia kwa muda wa miaka mingi sana. Sambamba na hilo napenda kutuma pongezi za pekee kwa Waziri wa Fedha kwa kuja na bajeti iliyokusanya mawazo ya wananchi. Hiki kinadhihirisha wazi kwamba yeye mwenyewe ni mshabiki na mpenzi namba moja wa wananchi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa leo, ningependa sana nijikite sana katika masuala ya kilimo. Kwa mujibu wa wasilisho la Waziri wa Fedha, ukiliangalia kwa undani kabisa utabaini kwamba sekta ya kilimo ndio sekta ambayo inaendesha uchumi wa nchi hii. Sekta hii ya kilimo ndio sekta pekee inayowaajiri Watanzania wa kila aina. Hata hivyo, cha kusikitisha licha kwamba sekta hii ya kilimo kuwa ni driving sekta ya uchumi wa nchi bado haijawa na mchango mzuri katika pato Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siri ya mafanikio ya uchumi unaotokana na kilimo ni kuwepo kwa viwanda. Kuwepo kwa viwanda ambavyo vitakuwa vinasindika na ku-process mazao ya kilimo vitatusababishia sisi kuweza ku-control uchumi na mazao yetu yatakuwa na thamani ndani na nje ya Taifa hili. Kwa sababu tukiwa na viwanda vingi ambavyo vina uwezo wa ku-process mazao yetu tutaepuka ile biashara ya kupeleka mazao, malighafi nchi za nje na badala yake tutakuwa tunapeleka products zinazotokana na mazao yale ya mashamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukubali kwa miaka mingi sana, kilimo hakikuwa kikiwekwa kipaumbele kinachostahiki. Ndio maana hakikuwa kikichangia kwa asilimia kubwa katika uchumi wa Taifa hili. Labda niseme kuna mtaalam mmoja Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe pale, Profesa Aida alisema kwamba mchango wa Serikali katika sekta ya kilimo bado ni mdogo sana, tena ni wa maneno matupu kuliko vitendo. Kwa sababu kasi ya kupunguza umaskini bado haijatekelezwa kwa mujibu wa vile tunavyotarajia.
Mheshimwia Naibu Spika, katika suala zima la kilimo kuna masoko mengi mno duniani. Kuna masoko Nchi za Asia, kuna masoko ya mahindi Nchi za jirani zetu kama Kenya. Bunge hili lina nafasi ya kipekee katika kujadili hotuba na bajeti pamoja na sera za uchumi wa Taifa hili. Katika majadiliano hayo ni lazima tujadili kwa kuangalia vizuri sana faida na hasara zilizokuwemo katika kila bajeti na mpango. Isipokuwa bajeti na mpango iliyowasilishwa juzi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kiuhalisia kabisa vinakwenda sambamba na uhalisia na wananchi wa nchi hii na vinakwenda kujibu matarajio ya wananchi wa kipato cha chini ambao ni wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna masoko mengi mno duniani, bado hatujaweza kuyatangaza mazao yetu ndani ya nchi na nje ya nchi Kimataifa. Tukiweza kuzitumia vizuri balozi zetu, ukiangalia takwimu za balozi zetu tulizokuwa nazo na ukiangalia matunda na mazao tunayozalisha katika nchi hii, basi utaona bado balozi hazijafanya kazi tunayoitarajia kufanywa. Lazima imefikia hatua Serikali ikae na wakulima, ikae na mabalozi wajue namna gani wana uwezo wa kuyatangaza mazao yetu katika nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia takwimu za Balozi zetu tulizkuwa nazo, na ukiangalia matunda na mazao tunayozalisha katika nchi hii, bado utaona bado Balozi hazijafanya kazi tunayoitarajia kufanya. Lazima ifikie hatua Serikali ikae na mabalozi wajue namna gani wana uwezo wa kuyatangaza mazao yetu katika nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke katika mazao ya kilimo, niende katika sekta ya ufugaji. Tanzania hii ni nchi ya pili kujaaliwa kuwa na mifugo mingi Barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia. Ingawa Ethiopia wana mifugo mingi kutushinda sisi, lakini ardhi yao ni ya jangwa, ni kame. Hawana maeneo safi ya ulishia mifugo ukilinganisha na sisi. Tanzania hii kila unapopita ni ardhi ya kijani. Tuna sehemu nyingi za kulishia mifugo, ardhi yetu imejaaliwa kila aina ya neema, rutuba na baraka lakini bado tunashindwa na nchi kama Ethiopia na Sudan kusafirisha mazao yanayotokana na wanyama. Kuna soko kubwa sana katika nchi za Asia, hususan Arabic Countries, kuna soko la ng’ombe mbuzi na kondoo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia kitakwimu, Ethiopia na Sudan ambao ardhi yao ni jangwa, wao wanasafirisha sana mazao ya nyama kuliko sisi. Sasa kitu kama hiki kusema kweli inakuwa inaaibisha sana Taifa hili la Tanzania. Ni kitendo cha ajabu mno, mbuzi au ng’ombe anayetoka Sudan kwenda katika soko la Kimataifa ashinde bei kuliko mbuzi anayetoka Tanzania ambaye kuna kila aina ya neema ya malisho ya wanyama. Ni kitendo cha aibu sana kwamba Tanzania hadi hii leo tunaagiza nyama, tunakula sausage za ng’ombe au mbuzi na kuku wanaotoka Brazil wakati sisi ndiyo ambao tulitakiwa tu-process nyama hizi kusafirisha, lakini sisi tunapokea kutoka nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Wizara ya Fedha mkae na sekta ya ufugaji mwangalie hili tatizo. Tutumie hizi fursa, tusitarajie kwamba kuna neema nyingine zaidi ambazo za kutunufaisha kama hizi. Kwa sababu kilimo na ufugaji ndizo zinazowagusa moja kwa moja maisha ya masikini wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke hapo niende nikazungumzie suala zima la mabadiliko ya tabianchi. Juzi katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri wa Fedha alizungumza kitu ambacho kilituvutia sana sisi Watanzania hususan Watanzania Visiwani. Nafasi ya Zanzibar na mgawanyo wa Zanzibar katika masuala yanayokuja, pesa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Mheshimiwa Waziri alisema kwamba wametenga fedha kwa ajili ya kwenda ku-support kingo za mito Wilaya ya Kaskazini A. Ni wazo zuri sana kwa sababu Zanzibar kwa kiasi kikubwa sasa hivi kuna mabadiliko na kuna athari kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo tungependa Mheshimiwa Waziri aende mbele zaidi, kwa sababu sisi Zanzibar hasa huko Kaskazini A hatuna hata mto unaosafiria hata kwa mtumbwi. Sisi ukiangalia bahari inatulea zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda maeneo ya Nungwi, mwanzo wa kisiwa, ukienda Kaskazi bahari inakula kisiwa, ukienda Magharibi bahari inakula kisiwa, ukienda Mashariki bahari inakula kisiwa. Tulitarajia zaidi kwamba Mheshimiwa Waziri ataacha hiyo process, maana inaonekana kwamba tafiti iliyofanyika labda haikuzingatia wapi iende. Bahari ina athari kubwa zaidi kuliko hiyo mito. Mito ya Zanzibar ni mito ambayo ikinyesha mvua dakika mbili, ikikata hakuna tena mito. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hili lifanyiwe kazi kwa sababu mabadiliko ya tabianchi, kule Kaskazini A visima vingi sana mwanzo vilikuwa vinatoa maji safi, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi maji yanapatikana katika visima vile ni maji ya bahari. Sasa hayo ndiyo mambo ya kwenda kuyashughulikia kuliko hizo kingo za mito. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazo zuri na kwa mujibu wa haya ambayo kayaelezea Mheshimiwa Waziri naona iko haja ya kukutana na hawa Wabunge wa Kaskazini kuweza kumpa ile picha halisi ya yale malalamiko yetu yanayotukabili kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja mia juu ya mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kuweza kunipa fursa ya kuchangia jioni hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zimetungwa kwa ajili ya ku-regulate human conduct sasa kwa kawaida sheria yeyote inakuwa inaongoza matendo halisi ya mwanadamu, sheria nazo katika utungwaji wake zimekuwa zimekuwa zimewekewa misingi maalum itakayoongozwa katika uandishi wake au maandalizi yake. Sheria Ndogo inapokuwa inaenda kinyume na utaratibu wa Katiba, sheria inapokuwa inaenda kinyume na utaratibu wa Sheria Mama maana yake sheria hiyo inakosa uhalisia katika matumizi yake. Sheria inapokosa uhalisia katika matumizi yake moja kwa moja itakuwa ni batili na haina uhalali wowote kisheria katika kuitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini, siyo kitu cha busara kwa changamoto zinazojitokeza katika utunzi na uandaaji wa Sheria Ndogo kuletwa hapa Bungeni kila mara na kuweza kujadiliwa. Matatizo haya na changamoto hizi zinazojitokeza takribani Mabunge ya miaka yote kasoro zinazojitokeza ni zilezile. Kamati ya Sheria Ndogo inachukua jitihada za msingi kuisisitiza Serikali juu ya kuzidisha umakini kabisa wakati wanapoandaa hizi sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala linalosikitisha zaidi katika utungaji wa sheria hizi siyo halali kwa Bunge hili kutaka Sheria Ndogo hizi kuingizwa hapa kabla ya kuanza kutumika huko hii ni kwa mujibu wa Tafsiri ya Sheria (The Interpretation of Law Act), Kifungu Namba 37 na 38 (1) maana yake sheria inapokuja hapa Bungeni kuijadiliwa kwanza inakuwa tayari imeshatumika huko kwa wananchi kama wananchi kuumia tayari wameshaumia sana, sasa tutakapokuwa tunakosa u-serious wakati tunapoandaa hizi sheria maana yake nini, moja kwa moja tunaenda kuangamiza wananchi ambao ndio walengwa halisi zinazokoenda kuwasimamia katika utumikaji wa hizi sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Sheria Ndogo kukosa uhalisia ni tatizo moja kubwa sana. Nakupa mfano sheria nyingi zilizokuja Bungeni kipindi hiki cha Bunge la Mkutano wa Tatu na la Bunge la Mkutano wa Nne zimekosa uhalisia katika matumizi. Nakupa mfano, kuna Sheria Ndogo ya kudhibiti ombaomba ya Wilaya ya Chunya iliyotungwa mwaka 2021 ukisoma hiyo sheria tafsiri yake inaweka wazi inatafsiri ombaomba kwa kumtambua kama mtu ambaye kaanza na ulemavu kitu ambacho ni kinyume kabisa na utaratibu wa Katiba. Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano inahamasisha umoja, mshikamano na usawa kwa binadamu, lakini ukiisoma hiyo sheria kwa undani zaidi utakuja kubaini kwamba ubaguzi ni sehemu inayopewa kipaumbele. Nakupa mfano, ukiangalia Kifungu cha 10 katika hiyo sheria kinasema wazi kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ana mamlaka ya kumfukuza ombaomba kumrejesha Wilaya alikotoka na katika Mkoa alikotoka kwa kumkabidhi kwa Katibu Tawala wa Mkoa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia mantiki ya hicho kifungu ni nini, unaweza kujiuliza hivi Mkurugenzi anapopata mamlaka ya kumrejesha ombaomba kwao hivi maombaomba wote wanaoenda Chunya maana yake Chunya hakuna ombaomba au sehemu nyingine ndizo zenye kutoa ombaomba na kupeleka Chunya hiyo moja, lakini unaweza kujikuta kwamba sheria hii mantiki yake ya kutungwa ni nini, tunaelewa hypothetically tunajua mantiki yake ya kutungwa ni nini, lakini lazima izingatie mahitaji ya watu kwa sababu suala la ombaomba siyo Tanzania tu, tunapokuja kumtungia sheria kwamba ombaomba, tumeshamuita ombaomba leo hii tunatengeneza sheria tukimkamata tunampiga faini ya Shilingi Laki Mbili maana yake nini, sasa huyu ombaomba au ni mtu mwenye uwezo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombaomba duniani kote wapo hata kule Marekani, ombaomba wapo tofauti ni majina tu, sisi tunawaita ombaomba kule wanaita nini homeless people! maana yake unga wa ngano, chapati ya unga wa ngano na andazi vyote ni kitu kimoja vinatumia jamii ya unga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho kinaonyesha wazi kwamba sheria hizi haziendani na uhalisia halisi wawatanzania soma Sheria ya Uvuvi (The Fisheries Regulatory Act, ya 2009) utaona wazi kwamba hii sheria haiakisi mahitaji ya wananchi walio chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano, ndani ya hiyo Kanuni hiyo unakuja kukuta kwamba miongoni mwa sifa ambazo mtu anatakiwa awe nazo wakati anapoamua kusafirisha samaki nje ya nchi, anatakiwa awe na certificate of incorporation sambamba na hilo awe na article na Memorandum of Association ya kampuni. Haya ni masuala ya kampuni ideological tunaimani kwamba once the company is registered become legal entity lakini kuna tofauti uhalali tunaoipa kampuni kutekeleza majukumu ya kibanadamu tunaiweka kwa misingi ya kwamba iwe na uwezo wa kushtaki na kushtakiwa. Lakini hatuwezi tukamchukua binadamu kuwa na hadhi sawa na kampuni vitu hivi ni masharti ambayo hayawezi yakatekelezeka kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapoweka mazingira haya lazima tuangalie wale watu wa tabaka la chini. Sheria hii imeenda mbali zaidi cha kushangaza zaidi kwamba wavuvi wamewekewa kina maalumu cha kuweza kuvua tuchukulie mathalani Ziwa Tanganyika lina maji ambayo hayatashuka mita 50, kina cha kwenda chini, lakini sheria ile imeweka mipaka mwisho uvuvi kuvua ni mita 20 kitu ambacho vipi nyavu zao zitakuwa zinavuta hawa samaki wa juu juu tu. Katika mita 150 ambazo zinatakiwa zivuliwe, wewe unaweka mita 20 wewe unayeweka mita 20 maana yake umeacha samaki katika mita 130 hizo umeziacha huru sasa hawa samaki wanauwezo wa kwenda sehemu yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba lile ziwa Tanganyika sisi tuna-share na wenzetu nchi kama vile Congo, sasa tunaposema tunawaacha wale samaki sisi, tumejitungia sheria ngumu, sheria ambazo haziwezi kutekelezeka, Congo wao wakienda kule wao watawavua, samaki siku zote hasubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki kwanza hana passport atakapotaka kwenda Kongo, kwamba aende akakate passport, aende akaonane na uhamiaji ndipo aende kule, yeye ana uwezo wa kwenda hajijui sasa hivi yuko wapi anaingia wakati wowote na kutoka wakati wowote. Sasa tujaribu kuweka sheria ambazo ni rafiki kwa wananchi wa tabaka la chini, kwa sababu siku zote tunaposema tunapomuwekea mtu sheria rahisi basi inakuwa rahisi kuzifuata, lakini ukiamua kumuwekea sheria ngumu utamuona yule mtu adui. (Makofi)
MWENYEKITI: Malizia sentensi yako.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana kuzingatia mahitaji halisi ya utungwaji wa sheria. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kuweza kunipa fursa ya kuwa mchangiaji siku hii ya leo. Mchango wangu mimi nitauelekeza zaidi katika kuangalia utekelezaji wa Maazimio ya Bunge yaliyotolewa wakati wa Mkutano wa Tano, Sita na Mkutano wa Saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ieleweke ya kwamba Bunge ndicho chombo kinachohusika katika utaratibu wa kutunga sheria za nchi hii. Ila, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kipengele namba 97 (5), sambamba na Sheria ya Tafsiri ya Sheria (The Interpretation of Law Act) Bunge hili limepewa mamlaka ya kukasimu mamlaka yake kwa taasisi nyingine za Serikali ili kuweza kutunga sheria. Kwa hiyo ni wajibu wa Bunge kuhakikisha mamlaka ilizozikasimu kwa idara au taasisi nyingine zinatumia mamlaka hayo kama inavyostahili. Ili kutimiza wajibu huo, ni jukumu la Bunge kufuatilia kwa karibu namna taasisi au Wizara hizo zinavyotumia mamlaka hayo. Kwa maana ya kwamba au kwa maneno mengine ni kwamba Bunge haliishii katika kuainisha au kubainisha tu dosari zilizotekea katika kanuni au sheria kwa njia ya maazimio, isipokuwa linatakiwa lifuatilie kwa karibu namna maazimio hayo yalovyoenda kutekelezwa na Wizara husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tulijaribu kufanya ufuatiliaji wa karibu sana wa Maazimio ya Bunge. Ni ukweli kabisa usiopingika kwamba tuliweza kubaini mambo mengi mno. Kuna Wizara ambazo zimeweza kukamilisha utaratibu mzima wa kutekeleza Maazimio ya Bunge yaliyotolewa. Nisingependa nizizungumzie Wizara hizo kwa sababu hizo zimetekeleza wajibu na taratibu zilizowekwa na Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna Wizara nyingine ambazo zimejaribu kutekeleza Maazimio ya Bunge kwa kiwango fulani; kwa maana ya kwamba wapo katika michakato hawajakamilisha utekelezaji wote. Ila, cha kusikitisha ni kwamba muda tuliotoa, kwa sababu tuzingatie sheria hizo ziliwasilishwa hapa na maazimio hayo yalitolewa hapa tangu wakati wa Mkutano wa Tano na wa Sita maana yake ni muda mrefu. Kutokukamilisha kwao kwa utekelezaji wa Maazimio ya Bunge maana yake nini, sheria zile bado zinaendelea kuwakandamiza wananchi kule chini. Wananchi bado wanaendelea kulalamika. Tunawaomba waweze kukamilisha jitihada zile za ukamilishaji wa Maazimio ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linalohuzunisha zaidi ni kundi la tatu. Kamati ya Sheria Ndogo katika ufuatiliaji wa Maazimio ya Bunge ilibaini wazi kwamba zipo Wizara ambazo hazijatekeleza hata kwa kiwango chochote Maazimio ya Bunge hili. Ni jambo ambalo linasikitisha sana. Masuala tumeweza kuyapitisha katika Bunge hili, yakajadiliwa katika Bunge hili, sote kwa umoja wetu tuliokuwepo hapa tukatoka na azimio moja. Leo hii unaita Wizara mbele ya Kamati kujibu kwanini wameshindwa kutekeleza azimio hili, wanakwambia kwamba Bunge wakati linaazimia halikuwa sahihi na usahihi wake badala ya kukaa sisi tuliona upo hivi; kitu ambacho kilitakiwa kifanyike hata kabla ya kuletwa kama azimio; kwa sababu kabla ya kuletwa azimio tunakutana na Wizara, tunakutana na Serikali kujadiliana, tunakutana nao kubadilishana nao mawazo, tunaleta hapa kama ni azimio. Inakuwaje yale tunayo yaazimia Bunge bado yaendelee kuwa na mjadala kwa Wizara za Serikali? Hii inasikitisha sana na inawezekana Serikali inafanya hivi kwa kuwa katika kanuni zetu za kudumu za Bunge wanajihisi pengine hatuna kipengele cha kuweza kuwaadhibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine kama maamuzi ama Maazimio ya Bunge hayakutekelezwa, inawezekana kanuni zetu zipo wazi, hazisemi kitu gani kitafuta kwa Waziri au kwa Wizara ambayo haikutekeleza Maazimio ya Bunge. Labda tubadilike na tuige kwa wenzetu. Wenzetu wao wana utaratibu kwamba kama maazimio yaliyotolewa na Bunge kwa Wizara fulani na Wizara badala yake haikutekeleza maazimio hayo basi bajeti yao haiwezi ikajadiliwa mpaka waende wakakamilishe. Labda tuende katika mfumo huo. Kwa sababu chombo hiki kieleweke ni chombo ambacho kina ukubwa wa aina yake, ni chombo ambacho kina umuhimu wa aina yake na kina hadhi na heshima, sawa sawa na Mihimili mingine ya dola. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifurahishwa sana juzi na kauli ya kaka yangu Mwiguli Nchemba. Kusema kweli alinifurahisha sana aliposema kwamba chombo hiki akiwa anaashiria Bunge, chombo hiki kina nafasi kubwa sana. Hakina jukumu la kujadili matukio tu, lakini kina wajibu wa kuishauri Serikali namna gani ya kuweka utaratibu wa kuhakikisha Watanzania wanaondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana nisieleweke nini ninamaanisha, lakini kiukweli kabisa duniani kote sababu kubwa ya umaskini inaanza na kuwa na kanuni na sheria mbovu. Yule tunayemwita maskini, maana yake ni maskini kwa mujibu wa sheria, yule tunayemwita tajiri, huyo ni tajiri kwa mujibu wa sheria. Tanzania tumekuwa na maskini wengi kwa sababu tumekuwa na kanuni nyingi na sheria nyingi ambazo zinahubiri zaidi umaskini kuliko utajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa na utaratibu wa kuendelea kutunga sheria ambazo zaidi zinaenda kuwakandamiza watu wa tabaka la chini, tukitunga sheria za ku-deal zaidi na masuala ya mafungu ya mihogo, basi tusitarajie kwamba lengo na dhamira ya Serikali ina uwezo wa kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa Bunge kazi yake kubwa ni kutunga sheria na kuzipa mamlaka nyingine kukasimu madaraka hayo, na tumekasimu madaraka kwa halmashauri zitunge sheria lakini halmashauri zinatunga sheria kinyume na taratibu. Ieleweke kwa mujibu wa taratibu za kisheria yeyote anayetoa mamlaka ya kufanyika jambo fulani basi jambo hilo likifanyika inahesabika sawa sawa limefanywa na aliyetoa mamlaka hayo. Bunge limetoa mamlaka kwa halmashauri kutunga sheria, halmashauri zimetunga kanuni mbovu, maana yake Bunge limehusika katika kanuni hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msisitizo wangu kwa upande wa Serikali, nashauri tuzidishe umakini kwa taasisi zetu, kwa Wizara zetu, wakati ambapo tunaenda kutekeleza Maazimio ya Bunge; lakini vile tuzidishe umakini wakati ambapo tunakaa na kutengeneza sheria mpya. Kwa sababu sheria ndogo hizi za halmashauri ndizo automatically, directly zinaenda kugusa maisha ya Watanzania… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo katika hotuba hii muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa letu na kwa Muungano wetu.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Kaka yangu Mheshimiwa Suleiman Jafo kwa kuja Jimboni kwangu na Wilayani kwangu kuja kunitembelea katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Bila shaka Mheshimiwa Waziri uliweza kuona uhalisia wa athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika Kijiji cha Nungwi na Matemwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kunako tarehe 26 Julai, 2021, Wizara ya Madini ilikutana na Wizara ya Maji na Nishati ya Zanzibar, kukaa na kujadili baadhi ya mambo. Licha ya kwamba, taasisi hizi mbili siyo za kimuungano, lakini kwa nini zimekaa na kujadili mustakabali wa Watanzania? Sababu kubwa ni kulinda na kudumisha mahusiano yaliyokuwepo baina ya pande mbili hizi za Muungano.
Mheshimiwa Spika, hii inatupa picha ya wazi kwamba, kuna masuala mengine ambayo yana maslahi mapana kwa Watanzania hata kama siyo ya kimuungano yanaweza kujadiliwa kwa maslahi ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Mkoa wa Kaskazini Unguja, hususan katika Vijiji vya Pwani Mchangani, Kijini na Jimbo la Nungwi kwa ujumla ni vijiji ambavyo vimetawaliwa na ukame. Ukame ambao unasababishwa na maji ya bahari kuvamia maeneo yale, kitu ambacho wananchi wa kule wamekuwa wanapata shida kubwa katika kuyatafuta maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, jambo lile limesababisha wananchi wa maeneo yale kuathirika kwa sababu ya kimaumbile kwa upande wa maji, vilevile wameathirika kutokana na athari nyingine za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ione haja ya kukaa na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuandaa miradi maalum ya kwenda kunusuru maisha ya wananchi wa maeneo yale. Kwa sababu, suala la mabadiliko ya tabianchi ni suala la kimuungano na suala la mazingira siku zote lina element ya masuala ya kimuungano, wale wananchi kwa kuwa wameathirika na sababu za kimazingira na athari zinzotokana na mabadiliko ya tabianchi hakuna haja ya kusema labda kwa nini yazungumziwe masuala ya maji katika suala ambalo ni la kimuungano? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hali kama hii maji ya maeneo yale yameathirika kutokana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. Mwanzoni historia inaonekana wazi kwamba tulikuwa tunapata maji safi na salama mnamo mwaka 2010, nafikiri Wizara ya Muungano na Mazingira ilitupa miradi kwa kuona ule uzito, lakini miradi ile imeshakuwa michache kulinganisha na ongezeko kubwa la wananchi wa maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ziara yako uliyokuja wananchi wanatarajia mambo makubwa mno kutokana na ziara yako, lakini bado wana hamu ya kukuona unarejea tena na tena kwa sababu athari zile mkiendelea kukaa kimya bado zinaendelea kuathiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu cha msisitizo kikubwa Wizara hii ione haja na kila sababu ya kufanya mambo mawili kupitia miradi hii ya kimuungano.
Mheshimiwa Spika, kwanza Zanzibar kuongezewa fungu kwa sababu, athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi licha ya kwamba, huku maeneo ya Ukerewe na maeneo mengine zinapatikana, lakini athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi zinaonekana katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, hata kule Pemba kulikuwa na mabonde 18 wananchi wa kule walikuwa wanalima mihogo, mbaazi, kunde, lakini leo hii hatuzungumzii tena maeneo yale yote yameshaliwa na bahari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ndio maana nasisitiza…
(Hapa kuengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji )
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami kuweza kunipa fursa hii ya kuchangia katika hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Ikumbukwe ya kwamba hii ni Wizara Mama ni Wizara ambayo imebeba suala zima la ulinzi wa raia pamoja na mali zao, kwa hiyo uhai wetu, usalama wetu unategemea zaidi ufanisi na uwajibikaji katika majukumu ya Watendaji wa sekta hii.
Mheshimiwa Spika, kuna nchi duniani hazina Jeshi lakini hakuna nchi iliyokuwa haina Polisi, Magereza, Uhamiaji pamoja na Zimamoto na Uokozi ila cha kusikitisha ni kwamba bado Jeshi hili hatulithamini na kulipa hadhi inayotakikana. Hivi mpaka leo bado tunang’ang’ania kuendeleza kujenga kuwa na wingi wa vituo wakati maaskari huku wanakabiliwa na changamoto nyingi? Maaskari wanalalamika hawana sehemu za kukaa, Askari wanalalamika vifaa vya utendaji kazi, maaskari wanapata changamoto kubwa wanapostahiki mafao yao, thamani yao iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sioni sababu na wala sioni haja ya kusema kwamba tunaenda kupiga marufuku suala zima la Jeshi la Polisi au maaskari wengine kutoa michango wanapoenda masomoni wakati tunashindwa kuwajengea nyumba na kuwarekebishia maisha yao. Kwa sababu Askari wanaoenda masomoni ni wachache zaidi ukilinganisha na wale wanaokosa makazi na suala la makazi kwa maaskari ni la kila siku, lakini suala la masomoni ni suala miezi miwili miezi mitatu wamemaliza! Sasa hili fungu ningeomba liondoshwe lipelekwe huko kunakojengwa nyumba za makazi za maaskari.
Mheshimiwa Spika, wakati juzi ninazungumza hapa nilipouliza swali langu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwamba Nungwi kuna ukosefu wa nyumba za maaskari, akatoa agizo kwa wawekezaji na wahisani wanaomiliki nyumba maeneo yale wawapangishe maaskari wale. Sasa najiuliza hivi Nungwi kodi chumba kimoja kile chumba kimoja tu kinaweza kufika Shilingi 100,000 hadi Shilingi 150,000 hivi ni Askari gani ana uwezo wa kulipa hizo gharama si tunawatengenezea mianya ya kuchukua rushwa kabisa? Suala hili naomba liangaliwe kwa kituo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mafunzo kwa askari ni jambo muhimu lakini lazima tuwafundishe Askari kufanya kazi kulingana na mazingira, sambamba na hilo lazima wakati tunapogawa hawa maaskari na kuwapeleka vituoni tuwapeleke kwa mujibu wa taaluma na ile sehemu wanayoenda.
Mheshimiwa Spika, hapa napenda nizungumze kitu kimoja lazima ieleweke sana na Mheshimiwa Waziri, kuna maeneo tuliyo nayo hayafananii, Zanzibar hii tuna maeneo yamekabiliwa zaidi na sekta nzima ya utalii ambapo raia unaweza ukawakuta inawezekana ni wachache zaidi kuliko hao wageni wanaokuja. Sasa changamoto inakuja mgeni anapokuwa na kesi yake au anapokuwa na changamoto yake aende kituo cha Polisi unakuta maaskari wanapenya kwa mlango wa nyuma kwa sababu hawajui kiingereza. Kiingereza chao kikubwa photo man sasa photo man inaendaje? Sasa hayo mafunzo unayotoa isiwe ya kupiga kwato tu, lazima na lugha ifundishwe mtenge vitengo maalum katika maeneo kama yale Mheshimiwa Waziri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, hili suala la mafunzo kwao ni suala moja la msingi vinginevyo tutaliaibisha Jeshi letu la Polisi lakini tutaibisha mitaala yetu ya elimu ya Tanzania. Katika hili napo Mheshimiwa Waziri nisipopata majibu ya msingi huenda nikazuia Shilingi yako Kaka yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la ajira sekta yako ina asilimia kubwa ya masuala yanayohusika na Muungano, Zanzibar tuna asilimia 21 au watu 21 ndiyo wanaotakiwa kuajiriwa? Kwa sababu hizi nafasi hatuzioni zinapokuja, zinakuja Zanzibar tunasikia lakini wachache mwisho wa siku unakuja kukuta labda watu watatu, watu wanne kutoka sehemu nyingine na ubaya wa mambo, hii yote inasababishwa kwamba ajira hizi zinapitia Makao Makuu haziji kwa Mikoa na ndiyo maana Wabunge wengi wanalalamika kwamba zinapokuja ajira bora zipite Majimboni lakini sisi tusiende Majimboni tuzipeleke hizi ajira kunako Mikoa kwa sababu miongoni mwa sifa ili uajiriwe katika sekta hizi basi uwe na cheti cha JKU umepita JKU au JKT, sawa wanapotafuta watu wawe wanapita Mikoani hizi nafasi zinakuja Mikoani lakini sasa nyinyi wakati tayari watu wameshamaliza mafunzo mnataka kuajiri hamzingatii kigezo cha Mikoa na ndiyo maana unakuta Jeshi letu letu lina sura ya sehemu moja na Wabunge wengine wanalalamika. Suala hili lazima tuliangalie kwa makini sana.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuwa mchangiaji. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Marais wetu; Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Taifa hili. Baada ya utangulizi huo, napenda nianze kwa kusema kwamba, vitu vyote duniani vina mipaka, lakini hakuna kitu kinachoweza kuunganisha dunia, mataifa, mabara na nchi kwa ujumla isipokuwa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, athari za kimazingira hazitegemei wapi uharibifu wa mazingira umefanywa. Uharibifu wa mazingira unaofanywa na wanadamu ndio unaosababisha athari za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia iko busy katika kupambana zaidi na masuala haya ya mabadiliko ya taibanchi. Kwa kuzingatia hivyo, jambo hili linatupa picha wazi kwamba, issue ya mazingira ni issue ya world, cross cutting issue, siyo suala la Taifa moja, wala siyo suala la sekta moja katika nchi ambayo inastahiki kuchukua hatua. Ni lazima sisi kama nchi kila Wizara ichukue nafasi katika kukabiliana na masuala haya, kama tulivyo. Kwa sababu kila Wizara inachukua jitihada kwa njia moja au njia nyingine bila kuhusika katika uharibifu wa mazingira. Kwa nini tushindwe kuchukua jitihada za msingi kwa kila Wizara katika Serikali hii kuweza kupambana na kuweza ku-control masuala ya uharibifu wa mazingira?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati dunia ipo katika kupambana na uharibifu wa hali ya hewa na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi sisi tukiwa kama Taifa, bado sioni haja na kujigamba kwamba tunachukua jitihada za kutosha katika kukabiliana na hali hii. Kwa sababu, sisi kama Taifa kupitia chombo hiki kitukufu, Bunge, leo hii tunajadili suala la mazingira na Muungano kwa kuchanganya vitu viwili kwa pamoja, wakati vitu hivi ukiviangalia, concept ta mazingira ndiyo inayobeba agenda ya dunia nzima sasa hivi. Concept ya Muungano maana yake ni masuala ya nchi mbili. Leo hii tunajadili kwa kutumia kutwa moja, sijui kama kweli tunachukua jitihada za kutosheleza kukabiliana na hizi effects. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwenda kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, miradi yake haitakiwi kutekelezwa kwa kutumia bahati katika majimbo. Tunatakiwa tuangalie ule uhalisia, wapi effects zinaonekana waziwazi na kwa muda gani? Sisi kama Taifa hatuwezi kwenda kumshughulikia mgonjwa aliyekuja hospitali aliyejikata wembe wakati anakata kucha, kisa kaja mwanzo, tukamwacha mama mjamzito ambaye amefika hospitali muda huu akiwa anagaragara kutokana na uchungu wa kutaka kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana gani? Sisi Nungwi hali ni mbaya. Mkoa wa Kaskazini kiujumla athari za mabadiliko ya tabianchi siyo jambo la kufumbia macho. Bahari, upepo, visima kujaa maji ya chumvi vinaangamiza sana Jimbo la Nungwi, Kijini na hata maeneo ya jirani. Nakumbuka mwaka jana niliuliza swali dogo la nyongeza kuhusiana na hatua mtakazoweza kuchukua kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maeneo ya Nungwi, Mheshimiwa Naibu Waziri, Muungano na Mazingira alijibu kwamba, katika bajeti ile ya 2021/2022 watatenga fungu la kwenda kujenga kuta pale, lakini cha kusikitisha, bajeti ilipita na hakuna hata moja lililofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alikuja Jimboni kwangu Nungwi, kaka yangu Mheshimiwa Jafo. Baada ya kuja tukaenda kukagua, lakini nasikitika mpaka leo hii bado sijaona jitihada zilizochukuliwa. Nimwambie kitu, ziara yake ilitupa matumaini sana, lakini ilikuwa aniambie tu ukweli kwamba alikuja zaidi kama ni holiday. Nikamwandalia life jacket angalau aende kuogelea na makasa na makobe kule, kama wanavyofanya watalii wengine. Kwa sababu, tulitegemea ziara ile itazaa matunda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku watu wanaohusika na suala la Muungano na mazingira wanakuja eneo la Nungwi, wanapima kwa kamba, wameshakuja kupima kwa GPS, kwa tape, kila aina ya vipimo wanakuja, lakini hakuna kimoja kinachofanyika. Sasa bora tuambizane kwamba eneo lile tulihifadhi kwa ajili ya utafiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi, ili wale wananchi tuwaondoe, tuwape ardhi sehemu nyingine kama Mwanza, Kagera, tuwatafutie sehemu ya kuishi ili pale tukatumie kwa rasilimali hiyo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu, Mheshimiwa Selemani Jafo, na ninafikiria watu wa Muungano na Mazingira kwa upande wa Zanzibar wananisikia; chonde chonde, umesoma bajeti lakini bado halijakuwemo. Maeneo yale yanatuathiri vibaya sana, yanatudhalilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, upo, wewe ni msikivu sana. Shauriana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Zanzibar ni Visiwa ambavyo vinaathirika kwa asilimia kubwa kutokana na staili ya mabadiliko ya tabia nchi kwa sababu tumezungukwa na bahari. Misaada inayokuja, uhisani unaokuja, ni vizuri tukaelekeza nguvu zetu kule kwa sababu athari zake zinaonekana waziwazi, hususan Nungwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chonde chonde kaka yangu, nakuomba kupitia Serikali hizi Tukufu, Serikali sikivu. Twende tukatekeleze ujenzi wa ukuta kuzuia bahari isiendelee kutuathiri maeneo ya Nungwi na vitongoji vyake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu, Mheshimiwa Jafo, nakumbuka katika bajeti iliyopita vilevile kuna suala la mfuko wa jimbo. Kuna fedha za mfuko wa jimbo tulipitisha hapa kama sote majimbo ya Tanzania kwa kuongezewa. Lakini kinachosikitisha ni kwamba mpaka leo hii majimbo ya Tanzania Visiwani tunapiga zogo. Bado hatujaongezewa chochote. Fedha zile zipo kwa ajili ya kwenda kuipa support miradi ambayo haikupata fungu katika bajeti. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Haikupata fungu…
NAIBU SPIKA: Taarifa, taarifa Mheshimiwa Simai.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaelewa sana tatizo analolizungumza Mheshimiwa Simai la fedha za mfuko wa jimbo. Naomba tu nimpe taarifa na kumhakikishia kwamba Serikali imeshalifanyia kazi na muda si mrefu kadhia hiyo itakuwa imeshatatuliwa kupitia Wizara ya Fedha, na Waheshimiwa Wabunge wote wa Zanzibar watapatiwa fedha hiyo. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante; Mheshimiwa Simai, taarifa hiyo.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo, ahsante sana. Lakini fedha hizi tukumbuke kwamba zipo kwa ajili ya kuchochea maendelea ambayo ni miradi ya wananchi ambayo haikuwa kipaumbele katika miradi iliyotengewa fedha kwa ajili ya bajeti. Sasa niiombe Serikali tuharakishe mchakato huu wa mfuko wa jimbo na sisi Wazanzibari tupate hiyo haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji leo hii. Awali ya yote natumia fursa hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais wa Zanzibar, kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kuwatumikia wananchi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba, miongoni mwa majukumu mama na ya msingi ya Kamati ya Sheria Ndogo, ni kufanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zinazowasilishwa Bungeni pamoja na kuangalia utekelezaji wa Maazimio ya Bunge. Miezi michache iliyopita nyuma, Bunge hili tukufu liliazimia jumla ya dosari 83 ziende zikarekebishwe kutokana na athari zinazowakuta wananchi. Wakati Kamati ya Sheria Ndogo ilipofanya mapitio ya utekelezaji wa maazimio yale, imebaini kwamba kumekuwa na dosari 19 ambazo zimeshindwa kurekebishwa licha ya kuwa baadhi ya Wizara husika tayari walikuwa wameshatangaza marekebisho yao katika Gazeti la Serikali. Ukiangalia ndani, dosari zile hawakuzirekebisha kama ilivyoazimiwa na Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawa na kusema kwamba, 22.89% ya Maazimio ya Bunge yaliyotolewa toka tarehe 8 Februari, 2023 hadi kufika tarehe 14 Agosti, 2023, wakati Kamati ya Sheria Ndogo ilipokutana katika vikao vyake vya kupokea taarifa ya utekelezaji, maazimio hayo hayakuwa yametekelezeka. Miongoni mwa Wizara ambazo tulibaini zimeshindwa kutekeleza maazimio hayo kwa kiwango ambacho Bunge liliazimia, ni Wizara ya TAMISEMI. Tulikuja kubaini walikuwa na dosari 16 ambazo wameshindwa kuzitekeleza. Wizara ya Madini na wao walikuwa na dosari tatu ambazo zimeshindwa kutekelezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inatupa picha gani? Jambo hili la kushindwa kutekeleza Maazimio ya Bunge inatoa taswira kwa wananchi kwamba, Wizara hizi zimeshindwa kutii maagizo ya Bunge au zimeshindwa kutekeleza kwa sababu ya kuona kwamba Bunge hili halina nguvu na mamlaka ya kuwalazimisha wao kutekeleza jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitendo ambacho hakiwezi kuvumilika, kuacha kutumika kwa dosari hizi katika mazingira ya kawaida, kwa sababu kuendelea kutumika kwa dosari hizi ni sawa na kuyakumbatia madhara yanayotokana na dosari ya sheria hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wa dosari ambazo Bunge liliazimia ziende zikarekebishwe lakini hazikuweza kurekebishwa. Unaposoma Sheria ya Usafi wa Mazingira ya Wilaya ya Misungwi ya mwaka 2023, Ibara ya 22(2), Kifungu hiki kimekuwa na mkanganyiko mkubwa sana wa adhabu, unapoenda kusoma kifungu cha 36(1). Kifungu cha 22(2) kinatoa adhabu ya jumla kwa mtu yeyote yule atakayekiuka masharti yoyote ya Kifungu cha Sheria. Kinatoa adhabu ya kupigwa faini isiyozidi shilingi 200,000 au kifungo kisichozidi miezi 12. Mkanganyiko unatokea utakapoenda kusoma Ibara ya 36(1) ya Kanuni hii ambapo hicho kipengele kinasema; “Mtu yeyote atakayefanya kosa lolote katika sheria hii, atapigwa faini isiyopungua shilingi 200,000 au kifungo kisichopungua miezi sita.”
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mkanganyiko katika utekelezaji wa adhabu unaotokana na sheria. Kwa sababu, wakati ambapo wananchi wanaenda kuadhibiwa kwa sheria hii, changamoto itakayotokea ni kipengele gani cha sheria kifuatwe. Aidha, 36(1) au 22(2). Huu ni mkanganyiko usiokuwa wa lazima na mkanganyiko huu unaendelea kuwepo na kuwaathiri wananchi, kwa sababu tu ya mamlaka inayohusika kushindwa kutekeleza Maazimio ya Bunge, kwa sababu, Bunge tayari walishawaelekeza waende wakaondoe dosari hizi lakini hawakufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili ndiyo chombo cha uwakilishi wa wananchi, haliwezi na halitoweza kuacha mamlaka yake ya kutengeneza sheria, yatumike kwa namna itakayoweza kuwakanganya wananchi katika kutekeleza majukumu yao. Dosari yoyote inayotokana na athari ya kushindwa kutekeleza au kushindwa kutekeleza kwa muda Maazimio ya Bunge, haikubaliki kuachwa kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili ndiyo chombo cha wananchi, lakini pia ndiyo sauti ya wananchi. Ikiwa kama ndiyo sauti ya wananchi, Bunge haliwezi kukaa kimya kwa zile dosari ambazo zinaendelea kuwaumiza wananchi wetu. Ndiyo maana Bunge hili lilitoa maazimio ya kwamba, dosari hizi 19 ziondoshwe ili zisiendelee kuleta madhara kwa wananchi. Kusema ukweli hakuna hata kimoja kilichofanyika, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni uoni wa Kamati kwamba, Bunge hili litazuia utumikaji wa dosari hizi 19, zilizokuwemo katika Sheria Ndogo kumi ili zisiendelee kutumika kwa wananchi, kwa sababu, kama Bunge hili litaachilia kuendelea kutumika kwa dosari hizi, ni sawa na Bunge hili kuridhia kuendelea kukumbatia athari zinazowapata wananchi zinazotokana na Sheria hizi Ndogo. Vile vile, itatafsirika ya kwamba Bunge hili limekubali mamlaka yake iliyokasimu kwa mamlaka nyingine zakutunga sheria, zitumike kinyume na utaratibu unaokusudiwa ambao ndiyo dhamira halisi ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo chochote kinachotokana na madhara yanayotokana na dosari hizi ambazo Bunge limedhamiria ziondoshwe, hakitavumiliwa na hazitaachwa kuendelea kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kitu kimoja kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla, si udhaifu katika maisha kukubali kukosolewa, kuambiwa na kuelekezwa kwa maslahi ya wengi au wachache, ikiwa jambo lina maslahi kwa Taifa hili. Ni kweli kabisa makosa tunayo katika kuelekezana. Wengine wakali, wabishi na wengine wagumu kuelewa. Kibaya zaidi, wapo miongoni mwetu. Kupata mawazo yao, fikra zao, akili zao pamoja na elimu yao, zionekane hakuna wa kuzipinga kutokana na jinsi wao walivyoelimishwa. Kitendo cha kuwakosoa au kuwaelekeza, kwao wao ni sawa na udhaifu ambao Mungu kawajalia na hawakustahiki kuwa nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge ndicho chombo chenye mamlaka ya kusimamia utungaji wa sheria zote za nchi hii. Kitendo cha kukasimu mamlaka yake kwa Wizara nyingine, haimaanishi kwamba Bunge halikuwa na uwezo wa kutengeneza sheria hizo, lakini limetekeleza majukumu yake ya Kikatiba ya kukasimu madaraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, leo hii ni vizuri tukaazimia na kuzitaka Wizara ambazo zimeshindwa kutekeleza Maazimio ya Bunge hili tukufu, zirekebishe kasoro hizo mara moja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake mkubwa aliouonesha jana, licha ya kwamba Dar-es-Salaam Young Africans walipoteza mchezo, lakini hakurudi nyuma aliweza kuweka mzigo mezani kama alivyoahidi. Pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa kudumisha misingi ya haki na utawala bora katika uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa lolote raia ili ajulikane kwamba yeye ndiye mwananchi wa Taifa hilo hakuna kinachomtambulisha zaidi ya kitambulisho. Kitu kinachoshangaza katika Taifa letu hili mambo ni tofauti. Kumekuwa na ukakasi mkubwa katika upatikanaji wa vitambulisho vya uraia, vitambulisho vya Mtanzania. Mheshimiwa Waziri ningependa sana Kaka yangu utakapokuja hapa kuhitimisha ni lazima utueleze mkakati wa Serikali mlionao juu ya upatikanaji wa vitambulisho vya Mtanzania. Kama siyo hivyo, mimi sitaondoka na shilingi, lakini nitaondoka na mshahara wote na mamilioni yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo linaendelea sasa hivi, kule Zanzibar tunapozungumzia suala la upatikanaji wa leseni za udereva ni tofauti sana na huku. Zanzibar ili upate leseni ya udereva wanaohusika na masuala ya leseni ya udereva ni mawasiliano. Maana inawezekana mawasiliano wakaidanganya Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini Tanzania Bara ili upate leseni ya udereva ni lazima upite kwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi wao ndiyo wanaotoa leseni za udereva. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na zoezi la unyang’anyaji wa leseni za udereva kwa madereva hata kama wameendesha miaka 20. Unajua napata suala kitu kimoja, leseni walizokuwanazo zinathibitisha wazi kwamba wao walikuwa na leseni, lakini kwa nini wanyang’anywe leseni? Sifa gani waliyoikosa? Kama kumrejesha darasani kwa nini msimrejeshe wakati ule ambapo alikuja kuomba leseni, mumrejeshe sasa hivi kakosa sifa gani? Je, kapunguza uwezo wa kuona au kigezo kipi mnachotumia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nimkumbushe Kaka yangu Mheshimiwa Masauni na Mheshimiwa Jumanne kwamba, mwaka jana niliuliza swali hapa Bungeni kuhusiana na ujenzi wa nyumba za Askari kule Nungwi na upanuzi wa kituo cha Polisi. Majibu niliyojibiwa ni kwamba, mnawaruhusu wananchi waliozunguka maeneo yale waweze kukodisha nyumba zao ili Askari wale wapate sehemu ya kukaa. Kusema kweli, nilikaa nikatafakari mara sita, hivi kweli askari tunamtakia mema? Turuhusu raia aende akamkodishe tena maeneo ya Nungwi ambayo ni maeneo ya uwekezaji? Chumba kimoja unaweza kukodi kwa laki, je, leo Askari ana familia nyumba moja atakodi kwa shilingi ngapi? Kwa mshahara gani anaoupata atakaoweza kujikimu kama siyo kumtengenezea misingi ya rushwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi, ulikataa kupanua nyumba za Askari, ulikataa kupanua eneo la Kituo cha Polisi, kinachonisikitisha na kinachonihuzunisha, umeenda kuchukua kituo changu cha afya Nungwi na kuweka Askari Utalii, hili jambo halikubaliki. Hili jambo halikubaliki! Kituo cha afya kile wananchi walikuwa wanakitegemea sana, kuweka Askari wako katika maeneo yale kumesababisha usumbufu mkubwa. Kama ulishindwa kujenga vituo vya polisi basi ilikuwa huna haja ya kwenda kung’ang’ania kituo cha afya, mlitumia njia moja mkatuchezea mchezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuliuliza kwa nini kituo chetu kimefungwa? Hoja mkasema kwamba, kituo kile mashimo yake ya choo yamejaa, ninachotaka niulize wale Askari wako wanajisaidia wapi? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, sababu ya pili ukaniambia kwamba, pindi ikinyesha mvua katika maeneo yale maji yanaingia mpaka ndani yanaweza kusababisha maradhi juu ya wagonjwa, hivi Askari wao wana kinga juu ya maradhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuelewe ya kwamba, kabla ya kuanzishwa Polisi Utalii, Nungwi sisi tulikuwa na Polisi Shirikishi, Polisi Jamii. Polisi Jamii walikuwa wanafanya kazi kubwa mno kwa sababu, ulinzi wa kwanza wa raia na mali zao unategemea zaidi wananchi wanaozunguka maeneo yale. Leo hii mmetuletea Askari Utalii, sipingani nao, Rais alianzisha kile kikundi kwa lengo mahsusi na lengo madhubuti kabisa, lakini leo hii kimebadilika kikundi kile, kimekuwa ni kikundi cha manyanyaso, kimekuwa kikundi cha wala rushwa, kimekuwa ni kikundi ambacho kinasababisha shaghalabaghala, zogo, kafara, sijui hata kitu gani kwa wananchi wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine lazima tukae tutafakari sisi kama Taifa, hivi tuseme Askari Jamii wakiwezeshwa hivi wanaweza kushindwa kweli kulinda fukwe zao? Hivi Askari Jamii tukiwapatia vifaa kuna haja gani ya maeneo yale yanayozunguka fukwe kuleta Askari Utalii kulinda beach?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Uhifadhi lilikuwa na dhamira nzuri kuanzishwa, kama nilivyotangulia kusema, lakini sasa hivi Mheshimiwa Waziri, wanalichafua Jeshi letu la Polisi. Misingi na utaratibu wa uchukuaji wa rushwa na kunyang’anya kwa kutumia nguvu imekuwa mtihani katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja, wakati mlipokuja kujenga kituo Nungwi, wananchi waliamini kwamba mtawalinda raia na mali zetu, lakini kumbe mmekuja kutuwinda raia na vitu vyetu. Mmekuja kuwawinda raia na wasio kitu, kwa sababu vituo vya Polisi vimekuwa vina-base zaidi kuwaweka ndani wale watu masikini. Masikini wananyanyasika. Kile Kituo cha Polisi pale Nungwi kimekuwa kikitumika na watu kuonesha mamlaka waliyokuwa nayo. Watu wanaweza kuwekwa ndani kituoni, lakini sababu za msingi hazijulikani. Tunaongoza kwa kuwa na unreported case. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi kinachonisikitisha, unaleta kesi za watu wanaohusika na dawa za kulevya; wananchi wetu wanajitolea kuwaonesha maaskari nani na nani anayehusika na dawa za kulevya, kumbe tunawatafutia kula! tunaleta ripoti leo, kesho mtu huyo katoka. Halafu anakuja kukutajia, sasa nimeambiwa na afande moja, mbili, tatu. Kusema kweli tunalikosesha uaminifu Jeshi letu la Polisi na tunaliondolea ushirikiano baina ya raia wema na Jeshi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati walala hoi, waendesha bodaboda na wavuvi wananyanyasika; wakati hawa wanalia; cha kushangaza, wauza unga, wavuta bangi na wanaokwepa kodi za Serikali, wao wanalindwa pamoja na kuhifadhiwa. Tunaelekea wapi? Mara ngapi Kituoni kwetu Nungwi tunapeleka watu ambao wanahusika na tuhuma mbaya lakini mnawaachia? Mheshimiwa Waziri mimi nimekuwa nikikutumia messages mara nyingi juu ya mwenendo mzima wa Kituo cha Polisi, Nungwi, lakini hakuna moja linalotekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazuia mshahara wa Mheshimiwa Waziri kama hajanipigia msasa kituoni kwangu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Simai. Malizia sekunde 30.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji jioni hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufanya kazi ni suala la kikatiba na ni haki ya kila mtu au raia wa nchi hii, katika kuifahamu na kuifafanua nadharia hii ndiyo maana Serikali ilipoona kwamba haina ajira za kutosha za kuajiri vijana na wananchi wote iliamua kurasimisha baadhi ya biashara zikiwemo biashara za bajaji na bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge na Kaka zangu Makamanda, wakati mwingine busara na hekima umuhimu wake huishinda sheria. Ndugu zetu hawa bodaboda ni ulezi wetu huu; sisi tukiwa kama viongozi ni lazima tuwalee. Bodaboda wana viongozi wao, bodaboda wana usajili wao na wanavyo vituo vyao na vinaeleweka. Namna bora ya kusimamia haki na heshima kwa vijana hawa, ni vizuri sana na ipo kila sababu ya kutumia viongozi wao na kuwapa elimu juu ya usimamizi wa misingi bora ya utekelezaji wa sheria bila ya shuruti, hususan katika masuala yanayohusu barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwapa elimu itakuwa ni bora zaidi kuliko kila wakati Jeshi la Polisi kushughulika nao kwa njia za kufanya hizi doria za kuwashtukiza, kwa sababu doria hizo mara nyingi zinakuwa siyo za kujenga, badala yake tunawajengea usugu vijana wale. Kazi rahisi ilikuwa ni kuwapa elimu juu ya sheria za barabarani, lakini tunapita njia ngumu kwa mambo yaliyorahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine ukamataji wanaofanyiwa vijana wale unakuwa siyo wa halali na unashusha hadhi na heshima na utu wa mtu. Ieleweke kazi ya bodaboda ni kazi kama ajira nyingine na jamii ya bodaboda ni jamii ambayo ni sawasawa na jamii ya wafugaji, tunatofautiana katika majukumu na mazingira ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona Askari wanaenda kukamata bodaboda kwa kuvizia na kwa kunyatianyatia au kwa kushtukiza, basi jua kuna kasoro katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi. Ukiona taratibu za uvamizi wa vituo vya bodaboda zimekithiri basi elewa kwa wenye kuelewa wataelewa kwamba kuna hitilafu katika mifumo ya ufuataji wa misingi ya utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke ya kwamba dhamira ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwenda kujenga vituo katika maeneo ya vijiji na Kata, kushusha vituo katika maeneo ya wananchi ni kuhakikisha wanawashirikisha wananchi katika dhana nzima ya Posili Jamii au Polisi Shirikishi. Utaendaje kuitekeleza dhana hii wakati una mkakati wa kupanga doria za kushtukiza? Hatimaye wananchi hao wakiwa wanabugudhiwa na hizo doria usitarajie kwamba wananchi hao watatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja, nina mfano mzuri wa matukio mengi sana hususan kule Kaskazini maeneo ya Nungwi. Bahati kule ukuaji wa miji umeongozeka na panapokuwa na ongezeko la ukuaji wa mji basi vijana na biashara ya bodaboda inakuwa inakithiri. Vijana wangu wa maeneo yale wamekuwa hawana furaha wala hawaifurahii kazi ile ya bodaboda kutokana na adha na bugudhi za Jeshi la Polisi, kwa misingi gani? Wakati mwingine utakuta Jeshi la Polisi wanawavizia, wanajificha kabisa katika vichaka ili wawakamate hali ya kwamba hawana sare ama uniform. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine unaweza ukawakuta Jeshi la Polisi linakusanya vyombo vyao hali ya kwamba vyombo viko maskani vijana wametulia, wanavichukua na kuvipeleka katika Kituo cha Polisi, baadae kituo kile kinageuka kuwa karakana badala ya kuwa kituo cha kushughulikia raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kwa kusema kwamba unapohisi Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuvizia vizia na linafanya kazi kwa kudowea dowea hawa raia maana yake kuna kasoro katika Jeshi la Polisi. Kuna kasoro kubwa ndani ya Jeshi la Polisi kwa watendaji wadogo wanaoenda kusimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine Jeshi la Polisi lina kawaida ya kuwakimbiza bodaboda, bodaboda kasajiliwa, chombo chake kinaeleweka na kijiwe chake kinaeleweka, kuna haja gani ya kumkimbiza wakati wana viongozi wao? Kitu ambacho kimekuwa kikisababisha migogoro na ajali nyingi barabarani, wakati mwingine tunawalaumu vijana, lakini hata Jeshi la Polisi kwa misingi hiyo kwa sababu wale vijana hawana pa kusemea, tunakuwa tunawabebesha lawama zisizokuwa za msingi. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Simai muda wako umekwisha ni kengele ya pili.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nami kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji jioni hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini pili ningependa niseme machache sana katika Wizara hii. Waswahili husema; “Chenye thamani hutunzwa na kulindwa.” Nilichokuwa nataka kujua ni kipi chenye thamani zaidi kati ya fedha za kigeni, chakula na maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa kama Taifa tumekuwa na taratibu za kuhifadhi hela za kigeni ili kutakapotokea mtikisiko wa upungufu wa fedha za kigeni hizo, sisi kama Taifa tuwe nazo, lakini kwa upande wa chakula tukiwa kama Taifa tumekuwa na utaratibu wa kuhifadhi chakula ili baa la njaa linapoikabili Taifa au Mataifa mengine duniani sisi tuwe na chakula akiba hata kama ni cha miezi miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa chakula au upande wa dona si kila mtu ana uwezo wa kutumia dona, inatumiwa na watu wachache. Inawezekana Taifa hili linatumia chakula hiki au mtu huyu amepigwa marufuku kutumia chakula fulani, lakini hakuna daktari hata mmoja atakayekupiga marufuku katika utumiaji wa maji. Kwa maana gani, hakuna mtu anayetumia mafuta kama mbadala wa maji. Katika hili ningependa niweke sawa kidogo, kwanza fursa hii kuishukuru sana hii Wizara kupitia kwa Mheshimiwa Waziri na Kamati yetu ya Bunge kwa kuona katika ripoti yao wameweka msisitizo juu ya umuhimu wa kuharakisha mchakato wa ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji hongereni sana. Nini tufanye ili kuonesha sisi kama Taifa tunayathamini na kutoa mchango katika suala zima la maji? Nitakuwa na michango mitatu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni lazima tufanye rejea ya Sera ya Maji, sera ambayo itaenda kuweza msisitizo juu ya elimu kwa umma kuhusiana na umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji. Inawezekana Serikali ipo katika mchakato wa kufanya mapitio au maboresho ya Sera ya Maji lakini ipo haja ya kuharakisha mchakato huo ili Sera hiyo izidi kuweka umuhimu kwa umma juu ya umuhimu wa maji. Umma ufahamu maji yana umuhimu gani. Lazima twende mbali zaidi kutokana na hali ya mabadiliko ya tabianchi tuliyokuwa nayo sasa hivi lazima sera iangalie na iboreshe namna gani miundombinu ya maji itakavyojengwa kwa kukabiliana na athari nzima za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nalo ni la kisera; Sera yenyewe sasa itamke wazi kwamba maji ni uhai na maji ni usalama ya Taifa, kwa sababu Maisha yetu sote viumbe yanategemea maji. Viwanda vikubwa na vidogo uendeshaji wake unategemea maji, kilimo pamoja na mifugo vyote vinategemea maji. Hata hiyo nishati ya umeme kwa vyanzo vyake asilimia kubwa vinategemea maji. Sasa upungufu wa maji ukitokea basi tutaanza kushuhudia mtikisiko wa usalama katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mdogo tu palipotokea upungufu wa vyanzo vya maji vinavyopeleka Dar es Salaam basi mtikisiko wa usalama ulianza kuonekana kwa baadhi ya maeneo. Maji yakipungua au ukame wa maji ukatokea basi mtikisiko katika sekta ya mifugo na viwanda au na kilimo lazima utatokea tu. Ndiyo maana nasema, nasisitiza maji ni usalama wa Taifa na hakuna mbadala wa maji. Maji si sehemu ya siasa ni sehemu ya Maisha ya Mtanzania na mwananchi yeyote wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo litakuwa ni la mwisho katika mchango wangu ni lazima sasa Serikali iwekeze katika sekta nzima ya maji. Ni lazima Serikali iwekeze hasa kibajeti katika usimamizi wa rasilimali za maji, kuhusu njia sahihi na za kisasa pamoja na kuweka ushirikishwaji wa wananchi katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji hii ndiyo dawa tosha. Tusitarajie licha ya kwamba Serikali itawekeza huko lakini uwekezaji huo lazima uende mbali zaidi katika kujenga miundombinu ya kuhifadhi na kusambaza maji kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusitarajie kwamba...
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Anatropia.
TAARIFA
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji pamoja na juhudi unazotaka Serikali ielimishe wananchi juu ya kuhifadhi maji, kuna halmashauri leo zimeweka Sheria kwamba yale maji yanayoifadhiwa pamoja na visima wanavyochimba kwa ajili ya kupata maji wawe wanalipia tozo hivyo visima.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Simai unapokea Taarifa?
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea, pamoja na yote hayo tusitarajie wala tusiruhusu sekta binafsi kwamba hiyo ndiyo iende ika-control uwekezaji katika masuala ya maji. Serikali haina jinsi lazima iwekeze kwa kiasi kikubwa katika changamoto hii. Tutakapoiruhusu sekta binafsi iingie huko maji yataenda kuwa bidhaa baada ya kuwa huduma na sisi tunachotaka maji yasimame kama ni huduma badala ya kuwa bidhaa hiyo itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini chakusikitisha kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Bashiru kasema hapa kwamba bajeti sasa hivi tumeanza kulega lega. Bajeti ya mwaka jana imekuwa ni kubwa ukilinganisha na bajeti ya mwaka huu, wakati ambapo ilitakiwa bajeti ya mwaka huu iwe ni kubwa zaidi maradufu kuliko bajeti ya mwaka jana. Kwa changamoto hizi ninazozisema na umuhimu ninaouona hakuna sababu ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo hususani katika suala la umwagiliaji iwe...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: ...ni kubwa halafu bajeti ya Wizara ya Maji iwe ndogo haiwezekani wakati Wizara ya Maji ndiyo inayo-control masuala na vyanzo vyote vya maji. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, nakushukuru sana.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji. Kamati ya Sheria Ndogo imekuwa ikikutana kwa vipindi tofauti kwa lengo la kufanya uchambuzi na kuangalia utekelezaji wa Maazimio ya Bunge yaliyokuwa yakitolewa Bungeni hapa katika hatua mbalimbali zilizofikiwa. Ni lazima tukiri ya kwamba licha ya kuwepo kwa jitihada nyingi zinazofanywa na Wizara pamoja na Halmashauri zetu katika kutunga Kanuni hizi ili kuhakikisha kwamba Kanuni hizi wanazotunga haziendi kuleta shida kwa wananchi katika matumizi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imebaini kwamba yapo matatizo ambayo kila mara tumekuwa tukiyazungumza Bungeni hapa bado yameendelea kujitokeza ingawa si kwa wingi kama katika miaka michache iliyopita. Kitu cha kusikitisha zaidi ni kwamba Kamati imebaini zipo baadhi ya Sheria ndogo zimeweka masharti au maudhui ambayo yanapingana na Katiba ya nchi hii au Sheria Mama za nchi hii, jambo ambalo limekuwa likikosesha uhalali kanuni hizi katika utumikaje wake, kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katiba ndiyo Sheria Kuu ambayo imeweka masharti ya kufuatwa na sheria zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria zote zinazotungwa na Bunge na Sheria Ndogo zote zinazotungwa na Mamlaka yaliyokasimiwa na Bunge ni Sheria halali za nchi hii kwa mujibu wa Sheria ya Tafsiri ya Sheria Ibara ya 36(1), kwa hiyo ni lazima ziakisi Ibara ya 64(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inazilazimisha Sheria zote za nchi hii kufuata misingi halisi ya Katiba kama ilivyokwishaelekezwa kwa kusema kwamba bila kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar, kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanzania, Zanzibar yasiyokuwa ya Muungano Katiba hii itakuwa na nguvu kwa Jamhuri nzima ya Muungano na Sheria nyingine yoyote kama itaweka masharti yatakayokinzana na Katiba hii, Katiba itakuwa na nguvu na Sheria hiyo itakuwa batili kwa kiwango ilichokuika Sheria hiyo, kwa kiwango ilichokiuka Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, utukufu wa kauli hii ya Katiba huwezi kuikuta katika Sheria nyingine yoyote ya nchi hii, kipengele hiki huwezi kukikuta hii inaonyesha ule upekee wa Katiba na inatofautisha Katiba, nguvu za Katiba na Sheria nyingine hususan Sheria Mama na Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea mbali zaidi, leo hii wakati tunafanya uchambuzi wa Kanuni, Kamati hii imebaini kwamba zipo baadhi ya Halmashauri zimetunga Sheria ambazo totally moja kwa moja ukizisoma unajua kwamba hawakuzingatia masharti ya Katiba. Kwa mfano, unapoenda kusoma Sheria ya usimamizi na udhibiti wa mifugo ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya 2024 iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali katika Tangazo la Serikali Namba 38 la Tarehe 19 Januari, 2024 basi ukiisomsa ile Kanuni Ibara ya 26(s) utakuta kwamba Kanuni ile inapiga marufuku kwa Watanzania vitu vya msingi ikiwemo uhuru wao wa kujishirikisha na harakati ya vyama vya siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeenda mbali zaidi ikapiga marufuku hata utaratibu wa mfugaji kuhusika katika harakati za kisiasa hata kupachika bendera katika maeneo yao, totally kwa mujibu wa Sheria ile, kwa mujibu wa Kanuni ile mfugaji hatakiwi kuhusika. Imesema kwamba mfugaji yoyote atakuwa ametenda kosa ikiwa atafanya shughuli yoyote ya kisiasa, narejea tena, mfugaji atakuwa amefanya kosa ikiwa atafanya shughuli yoyote ya kisiasa ikiwemo kupandisha bendera maana yake nini? Hiyo kauli ukiitizama unajua mantiki yao ni nini, lakini shida ya hii statement haikujitosheleza, haikuainisha ni maeneo yapi ambayo mfugaji amekatazwa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida inakuja na siku zote napenda kusema kwamba wakati mwingine sisi tunaotunga sheria inawezekana tukawa ndiyo chanzo cha tatizo, lakini wakati mwingine mtafsiri sheria inawezekana akwa ndiyo chanzo cha tatizo, lakini kuna wakati anayeenda kusimamia Sheria inawezekana akawa ndiyo chanzo cha tatizo. Katika yote haya umakini na uelewa wa pamoja vinahitajika kuzingatiwa kwa hali ya juu pamoja na ushirikishwaji na mahusiano ya karibu baina ya wanaotunga sheria, wanaotafsiri sheria na wanaoenda kuzisimamia sheria vinginevyo mtunga sheria atakuwa na tafsiri yake, msimamizi wa sheria atakuwa na tafsiri yake, lakini kibaya zaidi kwa msimamiaji wa sheria atakapokuwa na tafsiri yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho kitatupelekea kushindwa kufikia malengo ya zile sheria ndogo tunazozitunga. Katika mazingira kama haya unapozungumza mfugaji kwamba hatakiwi kuhusika na shughuli za kisiasa maana yake wewe moja kwa moja unaenda kumvunjia uhuru wake Kikatiba. Ukisoma Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 20(1) inamruhusu mtu yoyote kujihusisha katika harakati za kisiasa, sasa hii kanuni ilitakiwa iende mbali zaidi kwa kusema tu kwamba, labda hatakiwi kupachika bendera za siasa katika maeneo ya mifugo hapo kidogo ingekuwa imekaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuiacha wazi kama hivi ilivyo huko kwa watafsiri sheria inaweza ikaleta shida na baadaye tutashindwa kufikia lile lengo halisi ambalo tumelikusudia na itaondosha ile misingi ya utawala bora pamoja na kwenda kuondosha kabisa misingi ya kidemokrasia ambayo Mama yetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kila siku anaipigania katika Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea mbele zaidi tumebaini vilevile Kamati hii imebaini kwamba zipo baadhi ya Kanuni ambazo zimetungwa zinapingana na Sheria Mama. Utakapoenda kusoma Sheria Ndogo ya Mazingira ya Wilaya ya Kibondo Tangazo la Serikali Namba 920 lililotoka tarehe 22 Disemba, 2023 section ya 16(e), ukienda kusoma hii Kanuni ya Mazingira unakuta wamepiga marufuku kwa mtu yoyote aliyekuwa ndani ya basi atakapoingia katika stendi ya mabasi iwe nje wakati anaingia au anatoka anapokuwa katika Halmashauri tu akiwa ndani ya basi anakatazwa kutupa taka ngumu katika maeneo ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua dhamira yao nini, tunajua lengo lao nini, ni kuhifadhi mazingira, lakini sasa unapotunga Sheria kisha ukaitaja taka ngumu hiyo utakuwa unapongana na Sheria Mama ya nchi hii kwa sababu unaposema taka ngumu, ukiitaja taka ngumu peke yake umeacha ombwe kwa maneno ya Makamu Mwenyekiti wangu akitumia Kipemba unaacha ombwe, sasa ukisema kwamba ni marufuku kutupa taka ngumu, lakini je, atakayetupa taka laini utamhukumu kwa sheria gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake unajikuta umeacha taka ngumu, umeacha taka laini na taka nyinginezo kwa sababu Sheria ya Mazingira ya Nchi hii inafahamu kuna taka laini na taka laini na taka nyinginezo pamoja na taka ngumu, sasa unaposema taka ngumu peke yake maana yake bado utakuwa unakiuka misingi halisi ya utungaji wa Sheria Mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika yote niendelee kuwashukuru sana kama alivyokwishasema Makamu Mwenyekiti wangu, zamani tulikuwa tuna msururu mkubwa wa changamoto hizi za sheria ambazo zinaletwa pale, lakini sasa hivi kusema kweli tunatumia muda mwingi, lakini makosa unayoyabaini ni machache mno na hii inaonyesha taswira halisi ya namna Wizara pamoja na halmashauri walivyokuwa serious katika kutekeleza yale maazimio na wakati wa kutunga hizi Sheria Ndogo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji. Kwanza, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anazozifanya. Pili, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi pamoja na Wizara yake kwa jinsi wanavyofanya kazi. Hakika Watanzania wanaziona na wataziheshimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba, ieleweke ya kwamba ardhi siyo utajiri. Ardhi na rasilimali ardhi ni msingi mkuu wa uhai wa Taifa pamoja na wananchi wake. Pia, sisi kama wanandamu, msingi mkuu wa uhai wetu ni uhai. Tunayo haki ya kuishi na tunayo haki ya kumiliki mali ikiwemo ardhi. Hata hivyo, haki hii ya kumiliki ardhi na haki hii ya ardhi imekabiliwa na changamoto nyingi mno. Kwa sababu ya muda nitazungumza kwa uchache sana mambo matatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza linaloikabili ardhi yetu ni changamoto ya ongezeko la idadi ya watu. Mara baada ya kupata uhuru, ukiunganisha idadi ya watu wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani hatukufikia hata milioni 10. Hata hivyo, baada ya miaka 60 ya uhuru idadi hiyo imekuwa ni zaidi ya mara tano au sita zaidi kwani tumekuwa si chini ya milioni 60. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inaleta picha kwamba, mahitaji ya ardhi kwa shughuli za kiuchumi kwa maendeleo ya watu yameongezeka. Hata hivyo, licha ya ongezeko kubwa la watu ardhi tuliyokuwa nayo ni ileile bado haijakua. Kwa hiyo, inaonesha wazi kwamba kasi ya ongezeko la watu iko mbele zaidi ya kasi ya upangaji wa miji tuliyokuwa nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili linalofanana na hili kwanza ni upanukaji wa miji kiholela. Hata yale maeneo ambayo yalikuwa yakitumika kwa ajili ya shughuli za kilimo sasa hivi yamekuwa miji. Yale maeneo ambayo yalikuwa yanatumika kwa shughuli za ufugaji sasa hivi yamekuwa miji. Upanukaji huu wa miji kiholela usiozingatia mipango bora ya matumizi ya ardhi unaweza ukaleta shida kitu ambacho unaweza ukazidisha thamani ardhi na ikawasababishia shida kwa wanyonge. Upanukaji wa miji uliopo sasa hivi hauendani sambamba kabisa na upangaji wa miji yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni hili jambo la kiulimwengu la athari ya mabadiliko ya tabianchi. Huwezi ukazungumzia maendeleo ya nchi, huwezi ukazungumzia athari au changamoto zinazoikabili ardhi bila kuzungumzia athari ya mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili Tanzania. Hii ni kwa sababu yale maeneo mengi ya fukwe, kando za mito na milima sasa hivi yameliwa. Maeneo ya kilimo kumetokea ukame, wananchi wafugaji wamehama maeneo yao wamehamia maeneo mengine na baadaye migogoro imetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suluhisho la changamoto zote hizi tatu nilizozisema ni kuwa na Sera na Sheria bora. Niipongeze sana Serikali kwa kuanza mchakato mpya wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Ardhi pamoja na Sheria zake. Hata hivyo, katika hili ni vizuri tukajifunza utaratibu uliokuwepo kwa waliotunga Sera na Sheria kwa wakati ule wa utawala wa Marehemu Mzee Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, mchakato wake ulikuwa ni tofauti sana na huu ambao tunauendesha sasa hivi. Yaani haukuwa mchakato wa kawaida kawaida hivi. Mchakato ule ulitoka hadharani ukawashirikisha wananchi. Mheshimiwa Rais alitengeneza Tume Maalum ya kushughulikia ardhi ambayo ilikuwa chini ya usimamizi wake yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tume ile ilitembea Tanzania nzima ikahoji watu, watu wakasikilizwa, wakashirikishwa na wakatoa maoni yao. Baadaye sasa maoni yale ndiyo yaliyotumika baada ya kuchakatwa yakatengeneza hizi Sera na Sheria ambazo tunazitumia sasa hivi. Hata hivyo, hofu yangu na wasiwasi wangu niliokuwa nao kwa huu mchakato unaoendelea sasa hivi ni juu ya ushirikishwaji wa wananchi mwamko bado ni mdogo mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana hata wananchi hawajui nini kinachoendelea. Tukiendelea kunyamaza kimya bila kuwashirikisha wananchi inaweza kuja hoja tukatoka na sera na sheria ambazo zimetungwa katika meza. Sera ambazo zina uwezo wa kuwapa watu maneno ya kusema kwamba Serikali imetunga Sera dhidi ya wananchi au imetunga sheria dhidi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukumbuke kwamba Serikali ni taasisi na umma ndiyo nchi. Ardhi ni mali ya umma na siyo mali ya Serikali. Kwa hiyo, Serikali lazima iwahusishe wananchi katika masuala yote yanayohusu ardhi. Ni lazima Serikali iende chini kwa wananchi kuhusiana na huu mchakato. Wananchi wao ndiyo watakaosema kwa mujibu wa changamoto zilizopo sasa hivi, vipi viwe vipaumbele vya Sera yetu ya Taifa, vipi viwe vipaumbele vya sheria zetu tunazotarajia kutunga. Hata hivyo, tumeanza huu mchakato ingawa mchakato wa mwaka 1995 ulikuwa na kasoro zake lakini kitu cha msingi na kujivunia ni ule ushirikishwaji wa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeanza mchakato, lakini lile vuguvugu ni dogo mno ukilinganisha na miaka ile. Jambo hili la utungaji wa Sera na Sheria za Ardhi ni jambo zito na linahitaji mijadala ya Kitaifa. Kama tulivyokuwa na Tume ya Haki Jinai, basi umefikia wakati kwa sasa hivi ingekuwa ni kitu cha busara na hekima tukawa na Tume ya Haki Ardhi kutokana na unyeti wa jambo lenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendeleze kwa kusema kwamba, migogoro inayoendelea kuibuka ni mingi. Wakati wa wasilisho la Kamati walielezea changamoto ambazo zinaendelea kutokea hususan katika masuala ya ulipaji wa fidia ilihali utaratibu wa Sheria za ulipaji wa Fidia za Ardhi na mambo mengine upo wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utaratibu unatutaka wazi kwamba, unapokwenda kuchukua ardhi ya mtu kwa matumizi ya umma kama ni Serikali, lipa fidia. Hata hivyo, kabla ya kulipa fidia lazima utafanya tathmini ambayo tathmini hiyo ndiyo itakayokwenda kukuongoza wewe katika utaratibu wa kulipa fidia. Ikifika miezi sita, kama umeshindwa kulipa fidia maana yake kutakuwa na ongezeko au riba. Hata hivyo, leo Serikali tumekuwa tunafika hata miaka 10 bila kulipa fidia na ardhi hizo tayari tunakuwa tumezichukua. Maana yake nini? Tuna uwezo wa kusababisha umaskini kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sheria iko wazi, itakapofika zaidi ya miaka miwili maana yake ile tathmini iliyofanyika mwanzo inakufa na uende ukafanye upya kwa sababu ardhi ni mali ambayo haijawahi kushuka bei. Utajiri wa mwanzo na thamani ya mwanzo ya mwanadamu inatokana na ardhi. Taifa lolote lile mipaka yake inalindwa kutokana na ardhi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)