MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa fursa ulionipatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu na kwa sasa kuna changamoto kubwa ya kupanda kwa bei ya pembejeo nchini na hii ipo kwenye pembejeo zinazohusu mazao mbalimbali ikiwemo mahindi. Suala hili limekuwa tatizo kubwa kwa nchi nzima lakini pia kwenye mikoa yetu ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo na Mufindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfano mbolea ya DAP kwa maeneo ya kule kwetu ni zaidi ya shilingi 100,000 wakati huo bei ya mahindi ni karibu shilingi 5000 yaani inakuhitaji ubebe karibu debe 20 za mahindi ili urudi na mfuko mmoja wa mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni upi mkakati wa Serikali wa muda mrefu na muda mfupi katika kutatua changamoto hii ambayo ni kero kubwa sana kwa wananchi wetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi tunapata tatizo kubwa la upatikanaji wa mbolea; tatizo hili sio la Tanzania tu ni duniani kote kwa sababu uzalishaji umepungua sana. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha tunapata mbolea ya kutosha zinaendelea na mwezi mmoja uliopita nilikuwa na Waziri wa Kilimo nchini Morocco ambako pia kuna kiwanda kinazalisha mbolea nyingi inayosambazwa karibu duniani kote na tumegundua kwamba mahitaji ni makubwa mno na kwa hiyo hata bei zake nazo zimepanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bei ya mbolea sasa duniani kote iko juu lakini mpango wa muda mfupi ambao tumeutumia ili kupata mbolea angalau iweze kushusha bei ni kutoa ruhusa kwa wafanyabiashara kuingiza mbolea hapa nchini. Tunaamini kwa kuleta mbolea kwa wingi na kwa ushindani inaweza ikasaidia kidogo kupunguza bei badala ya bei hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge inaweza kuwa bei ya chini ya kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama njia ya muda mfupi sisi wenyewe hapa nchini tumeazimia kutoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza viwanda vya kutengeneza mbolea hapa. Mpaka leo hii tuna kiwanda kimoja tu kile cha pale Minjingu lakini bado tunazalisha kwa kiwango kidogo sana. Tumefanya jitihada za kupata wawekezaji kutoka nchi jirani ya Burundi na nimepata fursa ya kwenda kukutana na mwekezaji kulekule nchini Burundi tumezungumza na amekubali kuja hapa na tayari tumempa eneo hapa jijini Dodoma na ameanza hatua nzuri ya kuanza kuchimba msingi na ujenzi wa kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini uzalishaji mkubwa unaofanywa pale Burundi akija kuzalisha hapa tatizo la upatikanaji wa mbolea litakuwa limepungua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwasihi sana wakulima kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada za kila namna kuhakikisha upatikanaji wa mbolea unakuwepo kwa kiwango kikubwa ili kupunguza bei ambazo mkulima anaweza kumudu kuipata na kuendelea na kilimo chake huku tukiwasiliana na nchi ambazo zinazalisha mbolea ili tuweze kupata mbolea kutoka maeneo yote. Kwa hiyo, tumetoa fursa kwa wafanyabiashara na pia Serikali kupitia Wizara ya Kilimo wanaendelea kuhakikisha kwamba tunapata mbolea ya kutosha kutoka nchi rafiki. Hizi zote ni jitihada za kuhakikisha kwamba tunapata mbolea na ikiwezekana tupate mbolea itakayoanza msimu huu wa kilimo. Huo ndiyo mpango wa muda mfupi na muda mrefu ambao tunautumia kwa sasa. (Makofi)