Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (17 total)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza:-
Je, ni kwa kiasi gani eneo la EPZ lililotengwa na Mamlaka ya Bandari Mkoani Mtwara kwa ajili ya uwekezaji limetumika kwa shughuli iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ujenzi wa Bandari Huru ya Mtwara (Mtwara Free Port Zone) unahusu ujenzi wa sehemu maalum ya Bandari yenye gati na sehemu ya ugavi kwa ajili ya kuhudumia Sekta za Mafuta na Gesi. Madhumuni ya kuanzishwa kwa Eneo la Uwekezaji katika eneo la Bandari Huru ya Mtwara ilitokana na hitaji la makampuni yanayotoa huduma kwa Makampuni yanayofanya shughuli za utafutaji wa Gesi na Mafuta katika mwambao mwa Pwani ya Nchi za Tanzania, Kenya na Msumbiji ambayo yalikuwa yanahitaji kuwa na kituo cha ugavi (supply base) karibu na Bandari ya Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Eneo la Mradi wa Uwekezaji lenye ukubwa wa jumla ya hekta 110 katika Bandari Huru ya Mtwara (Mtwara Free Port Zone) linaendelezwa kwa awamu. Katika awamu ya kwanza, eneo la ukubwa wa hekta 10 limeendelezwa kwa asilimia mia moja kama ilivyopangwa. Shughuli za utekelezaji wa mradi huo zimehusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ndani na nje (offsite and onsite infrastructure) ikiwemo barabara kwa kiwango cha lami, umeme na mfumo wa usambazaji wa majisafi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uendelezaji wa miundombinu katika eneo hilo kukamilika kwa asilimia mia moja (100%), kwa sasa shughuli za uwekezaji katika eneo hilo zinaendelea vema na makampuni matatu (3) yanafanya shughuli hizo za uwekezaji.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Viwanda vya General Tires na Pharmaceutical Industries Ltd. ili kuongeza ajira na upatikanaji wa dawa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Bisahara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na viwanda mbalimbali nchini vikiwemo viwanda vya matairi na dawa ili kuchochea uchumi wa nchi kwa kuzalisha bidhaa na ajira. Kiwanda cha matairi kinachojulikana kama General Tire kilichopo katika Jiji la Arusha ni moja ya kiwanda kikubwa cha matairi katika ukanda wa Afrika Mashariki. Uzalishaji katika kiwanda hicho ulisimama mwezi Agosti, 2007 baada ya kukosa fedha za kujiendesha, husasan fedha za kununua malighafi. Hivyo, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukifufua kiwanda hicho ili kufikia malengo ya Serikali kujitosheleza kwa mahitaji ya matairi nchini, kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza matairi kutoka nje na kuzalisha ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) iliunda Timu ya Wataalam ili kufanya tathmini juu ya njia bora ya kuendesha kiwanda hicho. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa mitambo na teknolojia iliyopo imepitwa na wakati na hivyo ikashauriwa kuwa mashine na mitambo ya kisasa ifungwe ili kuleta tija na ufanisi katika uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia NDC inaendelea kutafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kuwekeza teknolojia mpya katika kiwanda hiki hususan ya kisasa kuendana na mahitaji ya bidhaa za matairi zilizopo sokoni. Tayari utaratibu wa kutangaza zabuni umefanyika ili kumpata mbia wa kufufua Kiwanda cha Matairi Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo na Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Mkakati wake, viwanda vya dawa ni moja ya viwanda vya kipaumbele ikizingatiwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kuagiza dawa kutoka nje ya nchi kwa mwaka, ajira zinazopotea pamoja na umuhimu wa kuzalisha dawa kwa ajili ya usalama wa wananchi wake. Hivyo, Wizara inaona kuna umuhimu mkubwa wa kuharakisha kufikiwa kwa maamuzi ya kesi inayoikabili Kiwanda cha TPI na pia kwa kuzingatia kuwa Serikali inamiliki hisa asilimia 30 katika Kiwanda hicho ili kuruhusu mara moja kuanza kwa uzalishaji wa dawa. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-
Je, ni lini upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Ilovo utakamilika, na kwa kiasi gani upanuzi huo utaenda sambamba na kuondoa kero ya Mizani na Vipimo vya Sucrose kwa wakulima wa Miwa?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kinaendeshwa na Kilombero Sugar Company Limited, Kampuni hii inamilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Ilovo Sugar Africa yenye asilimia 75 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye asilimia 25 katika hisa hizo. Katika kutekeleza sera ya Serikali ya kujitosheleza kwa mahitaji ya sukari nchini ifikapo mwaka 2025, Kampuni ya Kilombero Sugar itatekeleza mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kwa gharama ya shilingi bilioni 571.6.
Mheshimiwa Spika, matokeo tunatarajia mradi huu ni kuwa na Kiwanda cha kisasa, ambacho kitakuwa kikubwa mara nne kuliko cha sasa, kuongeza uzalishaji wa sukari mara mbili kutoka tani 127,000 za sasa hadi tani 271,000 kwa mwaka. Kuongeza mara tatu matumizi ya miwa kutoka kwa wakulima wadogo kutoka tani 600,000 hadi tani milioni 1.7 na kuongeza zaidi ya mara tatu idadi ya wakulima wanaouza miwa kutoka wakulima 7,500 hadi 15,000 mpaka 16,000. Mazungumzo kati ya wabia kuhusu mradi huu yamekamilika na utekelezaji wake utaanza mwezi Juni, ambao ni mwezi huu na unatarajiwa ukamilike mwezi Julai mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu yake ya pili ya swali, Serikali inatambua changamoto ya kero ya mizani na upimaji wa ubora wa miwa kwa wakulima wa miwa huko Kilombero. Katika kutatua changamoto hii, Serikali inalenga kuwa na mizani huru tofauti na ya sasa, ili tuwe na wapimaji huru na nimeshawaelekeza Work and Measures Agency wafanye utafiti kuona uwezekano wa wao wenyewe kupima, badala ya kupima na Kiwanda cha Kilombero. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, ni fursa gani za uwekezaji zinapatikana Tanzania?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba uniruhusu nitumie dakika moja tu kutoa shukurani. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyonipa kumsaidia katika ofisi yake katika eneo la mipango na uwekezaji. Nimuahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa bidii na utii wa hali ya juu kwake, kwa Serikali yake, kwa nchi yetu na kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa ushirikiano ambao ulinipa nikiwa Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati yako, nakushukuru sana lakini niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano na niwaombe wanipe ushirikiano katika hatua hii ambayo ninayo kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naomba sasa nijibu swali namba tano la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali. Naomba nitaje sekta tano tu kwanza, katika sekta ya kilimo tunazo fursa za uwekezaji katika kuongeza thamani ya mazao. Tunayo pia fursa ya kilimo katika mazao ya kipaumbele kama vile mafuta ya kula, sukari na ngano. Tunazo pia fursa katika eneo la utalii hasa katika ujenzi wa hoteli na makazi, tunazo fursa katika eneo la viwanda hasa katika viwanda vinavyolenga uzalishaji wa mbolea, dawa za mifugo na binadamu, nguo na mavazi na bidhaa za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati na gesi tunazo fursa za uwekezaji katika kuzalishaji nishati, katika uvunaji wa gesi na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi. Tunazo pia fursa katika eneo la madini hasa katika maeneo ya utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani ya madini.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-
Je, ni miradi mingapi ya kimkakati imejengwa katika Wilaya ya Ileje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ikiwemo ya uwekezaji wa madini, kilimo, biashara na uvuvi ambayo ina mchango mkubwa katika mapato ya Wilaya hiyo. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na:-
(i) Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira.
(ii) Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Bwelui wa megawati 4.7 wenye thamani ya shilingi 19,675,520,200.
(iii) Mradi wa Ujenzi wa Soko la Kimataifa la Isongoole.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ya Kimkakati kuilingana na fursa zinazopatikana nchini kwa lengo la kukuza uchumi, nakushukuru.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, madai ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliidhinishwa na kulipwa kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 39 wa mwaka 2006. Serikali iliamua kuwalipa wastaafu hao kwa kuzingatia Sheria za Pensheni za Jumuiya hiyo, sheria na taratibu za fedha, maridhiano ya mwaka 1984 na Sheria Na. 2 ya mwaka 1987, pamoja na Hati ya Makubaliano ya Septemba, 2005 na Hukumu ya Mahakama Kuu ya tarehe 21 Septemba, 2005.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miongozo tajwa hapo juu Serikali iliandaa utaratibu wa kuwalipa wastaafu na mirathi kwa waliofariki wapatao 31,831 kwa mujibu wa Hati za Makubaliano. Zoezi hilo lilifanyika kwa kipindi cha miaka minane kuanzia Julai, 2006 hadi Novemba, 2013 lilipofungwa rasmi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kulipa pensheni za kila mwezi kwa wastaafu ambao hawakuwa kwenye mpango wa kuchangia ambao walirejeshwa na kusajiliwa katika daftari la malipo ya pensheni ya kila mwezi. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Septemba, 2023 Serikali imeshalipa shilingi 1,075,289,494.12 kwa wastaafu 1,744.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kulipa pensheni kwa wastaafu wanaostahili kulingana na sheria, kanuni na taratibu za malipo ya Serikali na si vinginevyo, nakushuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ujenzi wa viwanda vya maziwa katika Mkoa wa Arusha hutangazwa kupitia makongamano ya uwekezaji yanayoratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Vilevile, Kituo hiki huandaa safari na mikutano ya uwekezaji nje ya nchi ambapo hutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji wa viwanda vya kusindika maziwa katika Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji nchini, Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwekeza nchini kwa kutumia malighafi zilizopo katika maeneo yetu husika, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ujenzi wa viwanda vya maziwa katika Mkoa wa Arusha hutangazwa kupitia makongamano ya uwekezaji yanayoratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Vilevile, Kituo hiki huandaa safari na mikutano ya uwekezaji nje ya nchi ambapo hutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji wa viwanda vya kusindika maziwa katika Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji nchini, Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwekeza nchini kwa kutumia malighafi zilizopo katika maeneo yetu husika, nakushukuru.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua na kutangaza maeneo ya uwekezaji Mkoani Kigoma?
NAIBU WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati wa Serikali ni kuendelea kuzitangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini zikiwemo zinazopatikana Mkoani Kigoma. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuandaa makala maalum (documentary) ya kutangaza maeneo ya uwekezaji katika Mkoa wa Kigoma, pia, kufanya makongamano ya kimataifa ya biashara na uwekezaji, ambapo kongamano la kwanza lilifanyika mwaka 2019 na la pili lilifanyika mwaka 2022. Aidha, mwezi Mei, 2024, Mkoa wa Kigoma unatarajia kufanya Kongamano la tatu la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutangaza maeneo ya uwekezaji kupitia ziara za viongozi wa Kitaifa ndani na nje ya nchi na kupitia ofisi zetu za balozi zetu, nakushukuru sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaachia maeneo yaliyotwaliwa na EPZA ambayo hayapo kwenye mipango ya matumizi ili wananchi wayatumie?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetwaa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanzisha Kanda Maalum za Kiuchumi. Maeneo hayo yapo katika hatua mbalimbali za utwaaji na uendelezaji. Katika kuendeleza maeneo hayo Mamlaka huandaa Mpango Kabambe ili kuainisha matumizi mbalimbali ya maeneo hayo. Hivyo, maeneo yaliyotwaliwa na EPZA bado yapo kwenye mpango wa matumizi yaliyokusudiwa.
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga majengo ya viwanda kuwapangishia wawekezaji wazawa ili kuongeza idadi kwani gharama za kuanzisha kiwanda ziko juu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Sera za Serikali katika uwekezaji ni kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maendeleo ya viwanda. Serikali ina jukumu la msingi la kutwaa, kupima na kupanga matumizi ya ardhi, wakati sekta binafsi hukaribishwa na kuhamasishwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya viwanda. Utaratibu huu umeshaanza kuzaa matunda ambapo hadi kufikia Desemba jumla ya kongani kubwa tatu za viwanda zimejengwa kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-
Je, Serikali ina Mkakati gani wa kufanya utafiti maalum katika Mji wa Tunduma ili kubaini ni namna gani unaweza kuchangia kukuza uchumi wa nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango, hususan kifungu cha 6, pamoja na majukumu mengine, Tume ya Mipango ina jukumu la kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo Tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia hili, Tume ya Mipango imejipanga kufanya tafiti mbalimbali na kuratibu tafiti zitakazofanywa na taasisi nyingine za umma na binafsi kwa lengo la kubaini fursa za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, hivyo, Serikali, kupitia Tume ya Mipango, itafanya tafiti mbalimbali kubaini fursa za maendeleo katika miji ikiwemo Mji wa Tunduma kwa lengo kubaini ni jinsi gani mji huu na miji mingine nchini inaweza kuongeza kasi ya maendeleo na kuchangia kukuza uchumi wa nchi, ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaachia maeneo yaliyotwaliwa na EPZA ambayo hayapo kwenye mipango ya matumizi ili wananchi wayatumie?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetwaa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanzisha Kanda Maalum za Kiuchumi. Maeneo hayo yapo katika hatua mbalimbali za utwaaji na uendelezaji. Katika kuendeleza maeneo hayo Mamlaka huandaa Mpango Kabambe ili kuainisha matumizi mbalimbali ya maeneo hayo. Hivyo, maeneo yaliyotwaliwa na EPZA bado yapo kwenye mpango wa matumizi yaliyokusudiwa.
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga majengo ya viwanda kuwapangishia wawekezaji wazawa ili kuongeza idadi kwani gharama za kuanzisha kiwanda ziko juu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa Sera za Serikali katika uwekezaji ni kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika maendeleo ya viwanda. Serikali ina jukumu la msingi la kutwaa, kupima na kupanga matumizi ya ardhi, wakati sekta binafsi hukaribishwa na kuhamasishwa kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya viwanda. Utaratibu huu umeshaanza kuzaa matunda ambapo hadi kufikia Desemba jumla ya kongani kubwa tatu za viwanda zimejengwa kwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanzisha utekelezaji wa mpango wake wa kuanzisha vituo maalum vya masuala ya uwekezaji na masoko kwa wanawake kila kata?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha kanda maalum za kiuchumi katika mikoa mbalimbali nchini. Lengo kuu la kuanzisha maeneo haya ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa nchini na kukuza mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani na pia kuzalisha bidhaa zinazoagizwa nje kwa soko la ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendeleza maeneo haya kuna sehemu zitatengwa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati (SME’s) wakiwemo wanawake na vijana ili waweze kuanzisha viwanda vya kuchakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya soko la ndani na nje. Aidha, maeneo haya yatatumika kama incubators kwa maana ya atamizi ili kukuza wajasiriamali wadogo. Nakushukuru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE K.n.y. MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:-
Je, ni Miradi mingapi ya kimkakati imetekelezwa katika Wilaya ya Tunduru?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika Wilaya ya Tunduru kama ilivyo katika wilaya nyingine na miradi hiyo ipo katika sekta zote; sekta ya elimu, Sekta ya afya, nyumba na maeneo mengine. Kwa mfano, katika Wilaya ya Tunduru, anafahamu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na ukarabati mkubwa wa ukarabati mkubwa wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa vituo vya afya na kadhalika. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti katika Mji Mdogo wa Mtambaswala ili kubaini ni namna gani unaweza kuchangia uchumi wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Mipango imejipanga kuhakikisha kuwa upangaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo unazingatia tafiti za kisayansi na ushahidi wa kitakwimu. Katika kutekeleza hilo, Tume ya Mipango imeanza zoezi la utafiti kuhusu uchumi wa mipakani (border economies) katika miji mbalimbali kwa lengo la kubainisha fursa, changamoto na namna miji hiyo inavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwemo Mji wa Mtambaswala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa utafiti huu kutawezesha upatikanaji wa takwimu na taarifa sahihi kuhusu uchumi wa mipakani zitakazosaidia katika mipango ya maendeleo ili kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na agenda za kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.