MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO aliuliza: -
Je, nini hatma ya wananchi wa Ubungo Kisiwani waliofanyiwa tathmini ya kulipwa fidia ili wapishe ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo la makazi ya watu la Ubungo Kisiwani lilifanyiwa uthamini na kuandaa jedwali la uthamini lililothibitishwa na kusainiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwezi Aprili, 2022 lenye jumla ya Shilingi bilioni 7.87 zitakazolipwa kwa wananchi 90 wa eneo hilo watakaopisha ujenzi wa Karakana hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia hiyo kwa wananchi 90 na mara zinakapopatikana malipo hayo yatafanyika.