Contributions by Hon. Judith Salvio Kapinga (24 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Rehema, kwa kutujalia wote kuweza kuwepo hapa siku ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo wangu…
NAIBU SPIKA: Samahani Mheshimiwa Mbunge kidogo. Waheshimiwa dakika ni tano na kengele itagongwa moja. Karibu Mheshimiwa Judith Kapinga.
MHE. JUDITH KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyotangulia kusema, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Rehema kwa kutujalia kuwepo hapa siku ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo wangu, napenda kumshukuru Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa maono makubwa aliyonayo kwa taifa letu la Tanzania. Namwombea afya zaidi, nguvu zaidi na hekima zaidi ili aweze kutuongoza katika utekelezaji wa maono haya kwa kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuboresha mfumo wa elimu ili kuleta tija kwa wahitimu. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea katika sekta ya elimu, mfumo wetu wa elimu bado unalalamikiwa sana. Sababu kuu ni moja, bado haujaweza kumzalia matunda kijana wa Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia taifa letu lina vijana wengi wenye talanta ambao iwapo mfumo wa elimu ungeboreshwa na kuzingatia teknolojia wangeweza kujiajiri, kuajiri vijana wengine lakini pia wangeweza kuchangia kikamilifu katika pato la taifa. Ndiyo maana leo napenda nijielekeze kuchangia ni kwa namna gani mfumo wa elimu unaweza kuboreshwa na kuzingatia teknolojia ili tuweze kufikia ajira milioni 8 ambazo tumeahidi katika Ilani yetu ya Chama Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tulipokaa hapa ukiangalia ulimwengu matajiri kumi wakubwa duniani saba kati yao wamepata utajiri aidha kwa njia ya mtandao (internet) ama kwa njia teknolojia bandia, sidhani kama ni Kiswahili sahihi ila wenzetu Wazungu wanasema artificial intelligence ama kupitia TEHAMA. Nikitoa mifano michache, ukimwangalia Jeff Bezos tajiri wa kwanza duniani amepata utajiri wake kupitia mtandao wa Amazon wa kununua na kuuza bidhaa anaingiza bilioni 127 kwa saa moja na ameajiri watu si chini ya laki moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia na matajiri wengine ambao ni wadogo, Mark Zuckerberg tajiri mdogo kuliko wote duniani ameajiri watu 52,000 anaingiza mamilioni ya shilingi kupitia mitandao ya jamii tunayoitumia hapa kama WhatsApp, Facebook na Instagram.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia matajiri wengine wadogo kabisa Larry Page, Sergey Brin wote wanaingiza mamilioni ya shilingi kwa saa moja na wameajiri siyo chini ya watu 135,000. Siwezi kuwaelezea wote lakini taswira hii inatuambia teknolojia ndiyo mwarobaini wa changamoto za ajira za vijana wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai kwa Serikali ya chama changu kuweza kuangalia upya mifumo yetu ya elimu ili kuboresha masomo ya sayansi. Ubunifu unaanzia kwenye kujua ABCs za computer. Lazima tuboreshe masomo yetu ya sayansi yazingatie mafunzo ya computer kuanzia elimu ya msingi kwa sababu huko ndiko ubunifu unakoanzia na siyo kusubiria kuwafundisha watoto vyuo vikuu wakati vichwa vyao tayari vimekomaa. Matajiri wote hawa walipata mafanikio kwa sababu mifumo ya elimu iliwaandaa, iliwakuza kiubunifu na iliwasaidia na ndiyo maana wengi wao walivyofika chuo kikuu waliweza kubuni program hizi ambazo zinatatua changamoto za dunia za teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia leo vijana wetu wanaomaliza form four na form six mfumo wa elimu umewasaidia vipi? Mfumo wa elimu unapaswa kumsaidia kijana kwa ujuzi wa kujitegemea kwa ngazi yoyote anayoishia. Kinachosikitisha zaidi vijana wetu wa chuo Kikuu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JUDITH KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, napenda kuipongeza Serikali kwa commitment kubwa inayofanya katika sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kuzungumzia namna tunaweza tukaboresha mifumo ya kutumia huduma za fedha kwa njia za kimtandao. Kama tunavyofahamu, kutokana na changamoto kubwa ya ajira vijana wengi wamejielekeza katika kufanya ujasiriamali wa kimtandao ambao kwa kiasi kikubwa unatumia huduma za fedha za kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za fedha za kimtandao zimewekwa pamoja na sababu nyingine, ili ziweze kumrahisishia huduma mfanyabiashara. Nafahamu hizi huduma za kifedha za kimtandao zinahusisha tozo ambazo zina kodi ambayo ni muhimu sana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali. Pamoja na dhamira hizo ambazo ni njema sana tozo kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha kwa mitandao ni kubwa mno na hivyo inasababisha vijana wengi wasiweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Leo hii ukiwa unatuma pesa shilingi 5,000/= tu kwa mtandao wa simu gharama yake ni shilingi 750/=, unaweza ukaona ni ndogo lakini ni 15% ya pesa ya mtu. Anayetoa shilingi 50,000/= anakatwa shilingi 2,700/= ni 5.4%; anayetoa shilingi 200,000/= anakatwa shilingi 3,700/= ni 1.9%. Kwanza unaona yule ambaye ni maskini kabisa wa chini ametoa shilingi 5,000/= anakatwa 15% ya pesa yake, yule ambaye anatoa shilingi 300,000/= anakatwa 1.9% ya pesa yake. Sasa hawa vijana ambao wanaanza biashara wataweza vipi kupambana katika soko hili la kimitandao? Hawana ajira, wanaamua kujiajiri kwenye mitandao na gharama zinakuwa kubwa kiasi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiamua kwa mfano leo unaamua kutuma ada kutoka Tigo Pesa kwenda NMB gharama yake kwa Sh.140,000/= unakatwa Sh.6,000/=. Kama una watoto watatu gharama yake ni Sh.18,000/=, kwa uchumi upi wa Mtanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ni kubwa mno, kijana anafanya kazi kwenye mtandao ili apate faida ya shilingi 10,000/= na shilingi 20,000/= lakini yote inaliwa kwenye tozo za huduma za fedha za kimtandao. Naomba Serikali iangalie upya hizi tozo ili ziweze kuleta unafuu kwa vijana ambao wanapambana kwenye mitandao ili kuweza kupata kula yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye huduma za internet, natambua tafiti zinaonesha Tanzania ndiyo ina tozo ndogo kabisa kwenye data, katika ukanda wote wa East Africa, lakini tatizo lipo kwenye upandishaji holela wa huduma za data (internet). Wiki moja iliyopita ukitoa shilingi 8,000/= kwa Tigo ulikuwa unapata GB 16, yaani kesho asubuhi watu wameamka wameweka 8,000/= wanunue GB 16 wanapewa GB tatu, hawajapewa taarifa kwamba huduma gharama yake zinaongezeka. Halafu sasa MB 300 unapata kwa Sh.1,000/= yaani kwa mfanyabiashara uki-post post mbili, hela imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 3,000/= unapata GB moja wakati shilingi 3,000/= ulikuwa unapata mpaka GB 5. Watanzania hawakupewa taarifa ya upandishaji wa gharama hizi yaani kampuni ya mawasiliano anaamka anaamua kupandisha gharama za mitandao kama anavyopenda. Pato la mtu mmoja-mmoja ni shilingi elfu moja na kitu, lakini unamfanya Mtanzania atumie gharama ya shilingi 3,000/= kwa siku kwenye huduma ya mawasiliano, sio sahihi. Naomba Serikali iangalie upya ili inusuri vijana hawa ambao wanatumia mitandao ya kijamii kujipatia kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la pili kutoka mwisho, sisi tunapolipa huduma, tunaweza kulipa huduma kupitia Master Card Visa pamoja na PayPal kulipia malipo nje ya nchi. Leo mimi kijana wa Kitanzania nikiamua kufungua website kutaka kutangaza bidhaa watu wa nje ya nchi waweze kununua kwenye website yangu hawawezi kulipa kupitia Master Card, PayPal, Visa au Credit Card hela iingie moja kwa moja kwenye benki yangu, lakini mimi nina uwezo wa kuwalipa wale wa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vijana tunawahimiza ubunifu, lakini ubunifu wao hauwezi kuwasaidia kwa sababu watu wa nje hawawezikuwalipa kwenye akaunti zao za benki. Naomba BoT na Wizara ya Fedha iangalie suala hili kumnusuru kijana huyu wa Kitanzania na kumwekea mazingira mazuri ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia na mimi ningependa nijielekeze katika mambo mawili. Tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha ukuaji wa uchumi, na tunapohusisha ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa tunaongelea mambo ya msingi sita; yaani uendelevu, uzalishaji, uwekezaji, mashirikiano, usalama pamoja na usawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa kwenye usawa ndipo ambapo ningependa nijielekeze kwasababu ni suala ambalo linahusisha haki na utu wa watu. Na tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha utu na haki za watu. Yaani lengo kuu la maendeleo ya watu ni uhuru na haki za watu; huwezi kutofautisha hayo masuala mawili.
Mheshimiwa Spika, nazungumza haya kwasababu uhuru na haki ya mtu unahusisha uhuru wa kipato. Tunapojadili mpango huu ni muhimu sana kuweza kuweka baadhi ya mambo sawa, ambayo yanashika uhuru wa kipato cha mtu; na uhuru wa kipato cha mtu mara nyingi unalindwa na Sheria na taratibu za nchi.
Mheshimiwa Spika, ningependa nijielekeze hapa kwasababu zipo Sheria ambazo zinakandamiza uhuru wa kipato cha mtu, inawezekana kukawa na changamoto, na hapa ningependa nijihusishe specifical katika Sheria ya Uhujumu Uchumi, nafahamu imeongelewa sana lakini ningependa niweke mkazo hapa. Kwa ambao hawafahamu Sheria hii ya Uhujumu Uchumi na Utakatishaji Fedha ilikuja baada ya tukio la Septemba 11; pale ndipo ambapo Sheria hii ilisisitizwe iweze kuletwa katika mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla, ndipo na hapo sisi tukapata sheria hii. Lakini tulipokosea nchi nyingi za Afrika pamoja na Tanzania tulipata mapokeo ya sheria hii bila ya kuangalia mazingira yetu ya ndani.
Mheshimiwa Spika, na vile vile tulipopata sheria hii hatari zaidi hatukuwa na uzoefu na kujadili ama kuendesha mashtaka haya, na hivyo tukajikuta tunapokonya haki za watu za dhamana, lakini vile vile tukapoka mali za watu kwa kudhania, kwamba sheria inaruhusu ilhali kimsingi ilikuwa labda ni tafsiri mbaya ya sheria ama sheria hazikukaa sawa ama matumizi mabaya tu ya nafasi pamoja na madaraka ya watu waliodhaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu makosa mengi katika sheria zetu za Tanzania yana dhamana; ukiangalia wizi, ukwepaji wa kodi ni makosa ambayo yana dhamana lakini ilivyokuja sheria hii dhamana ikanyimwa. Hata hivyo, watafsiri wetu wa sheria wametufelisha sehemu moja, makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha ni matokeo ya makosa ya msingi yaani leo hii umeiba ama unatuhumiwa kwa ukwepaji kodi, mpaka ukwepaji kodi uwe- establish ndipo pale utaweza kujua, je, ukwepaji kodi ulisababisha utakatishaji wa fedha? Ndipo hapo unamhukumu mtu kwa kosa la kuhujumu uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu makosa haya ya utakatishaji wa fedha ni vigumu sana kuya-prove wenzetu wa DPP wakaamua warahisishe Maisha. Moja, kwa sababu ni ngumu sana ku-prove sasa wanaamua pale kwenye kosa lako la msingi ambalo lina dhamana akuwekee na money laundering ili likose dhamana. Pili, kwa sababu halina dhamana utawekwa rumande sasa pale ndiyo wanakuja na negotiations (pre-bargaining) anakwambaia sasa hapa kuna shitaka hili na kwa sababu mashtaka haya yana sifa ya kukukalisha rumande miaka na miaka, mtu uko frustrated unawaza biashara zako, unawaza familia yako, unamuwaza mke au mume wako utakosa ku-negotiate ili uweze kutoka? Uta-negotiate tu na hapo ndipo ambapo watu wanapokwa mali zao kwa taratibu ambazo siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema utaratibu huu ni unyang’anyi tu wa bila silaha, tunapokonya watu kwa taratibu ambazo zingeweza kutafsiriwa ili ziweze kurahisisha watu wetu walinde kipato chao na utu wao. Kwa hiyo, haya masuala ya hii sheria, naomba sana Serikali yangu sikivu iangalie upya na inawezekana sheria haina matatizo ila tafsiri ya sheria kwa watendaji wetu iangalie mazingira ambayo tutalinda utu na kipato cha watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo napenda nijielekeze nalo ni kuhusiana na masuala la mawasiliano na teknolojia. Inawezekana nikaonekana kama mlalamikaji lakini napenda nisisitize hapa. Kwanza napenda niishukuru Serikali yangu Sikivu, tulipozungumza masuala ya mabando ilisikia ikatoa maelekezo na tunashukuru sana. Hata hivyo, bado naomba Serikali iangalie masuala ya mabando ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi. Vijana wengi wanatumia huduma hizi, toka mwezi wa kwanza tunalalamika huu ni mwezi wa nne masuala haya hayajafanyiwa kazi, tunapewa tu matamko lakini vijana wengi zaidi ya milioni 23 wanatumia mitandao ya simu kwa ajili ya shughuli zao, tunaomba tuangaliwe. Unapewa MB 300 kwa Sh.2000 unafanya biashara, vijana huku ndipo tulipokimbilia kwa sababu mfumo wa elimu haujaweza kutusaidia. Sasa kwa mantiki kama hizi tunasaidiwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TCRA imetoa tamko kwamba ikifika Mei Moja vijana zaidi ya 90,000 wanaosajili line wawe wana vibanda, leseni na TIN namba. Anasajili line kwa Sh.1000 na anapata wateja kwa kusambaa huku mtaani leo hii unamwambia awe na kibanda wateja atapata wapi? Airtel inawalipa vijana hao zaidi ya shilingi milioni 700 ikilipa kima cha chini lakini inalipa mpaka shilingi bilioni 1 kwa vijana 30,000 lakini wanaenda kukosa kazi hawa. Naomba Serikali yangu iangalie mambo kama haya ili vijana wa Taifa hili wasiwe frustrated na mazingira ya kibiashara. Naomba Serikali yangu ituangalie sisi vijana ambao tunalipenda Taifa letu na tunafanya kazi kwa juhudi kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunivumilia na kunipa dakika za ziada. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa sasa hivi Tanzania na dunia nzima tumesimama katikati ya mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamebadilisha yataendelea kubadilisha namna tunavyoishi, namna tunavyofanya kazi na namna tunavyoshirikiana na watu wengine. Huko tunakoelekea, kwa namna ambavyo mabadiliko ya teknolojia yanatokea, haina shaka kwamba kwa ujumla maisha yetu yatabadilika kwa kasi ambayo tusiyoitarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunakumbuka, tukiangalia hapa tulipo na tulipotoka, mapinduzi ya kwanza ya viwanda namna ambavyo yalikuwa yanaendeshwa, yalikuwa yanatumia njia ya maji pamoja na mvuke, yaani water na steam power. Mapinduzi ya pili yali-advance kidogo yakawa yanatumia electronic power; mapinduzi ya tatu yakaenda yakawa yanatumia electronics and information technology. Hapa tulipo sasa hivi yame-advance kiasi cha kwamba tunatumia mchanganyiko wa nguvu kazi yaani za mikono, kidijitali na mbinu za kibaiolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya ili niweze kueleweka kwamba hapa tulipo tuko katika nyakati ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya dunia na mabadiliko yanayoenda sasa hivi kwa kasi ambayo yanatokea haijawahi kuwa recorded toka dunia imeanzishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema pia ili tuone umuhimu wa kuwekeza katika masuala ya teknolojia, sayansi pamoja na uvumbuzi, lakini hatutaweza kufanikiwa kwa sababu masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia, uvumbuzi, mawasiliano na habari hayajawekwa pamoja katika nchi yetu, yaani yameparanganyika. Yapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini masuala ya information na communication na ICT yako kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu kama tunavyofahamu ni dubwana kubwa namna hii, masuala ya sayansi na teknolojia, hayawezi kuendelezwa pale kwa kasi ambayo sisi tunaitaka na ndiyo maana leo hii nataka nishauri Serikali yangu sikivu. Wakati umefika sasa tu-centralize masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia, uvumbuzi, habari na mawasiliano kwenye sehemu moja. Sehemu sahihi ni Wizara hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba kwa nini tu-centralize leo? Ni kwa sababu tunapaswa kujisuka upya ili tuweze kwenda na kasi ambayo dunia inaenda. Lazima tukae kwenye mstari ambao the rest of the world wapo. Leo hii tulipokaa hapa nchi 24 duniani zimeshaweka makubaliano ya kumaliza matumizi ya mafuta ya petroli kuanzia mwaka 2025, ina maana watakuwa wanatumia magari ya umeme ama magari ya gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tulitakiwa tuwe tuna mkakati wa kutuwezesha sisi kuungana na dunia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwekeza kwa wataalam ambao wanaweza kubadilisha mifumo yetu ya magari kwenda kwenye mifumo ya magari aina ya umeme na gesi. Haya yote hayawezekani kwa sababu mambo yote haya yamekuwa decentralized. Hakuna sehemu moja ambapo tunaweza tukajisuka kama nchi na kwenda katika kasi ambayo dunia yote inaenda leo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni rai yangu kwa Serikali ya chama change, ni wakati umefika tu-centralize sayansi, teknolojia, uvumbuzi, mawasiliano na habari kwenda kwenye Wizara hii ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kasi ambayo sisi tungeitamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia kwa mfano leo, kuna nchi kadha wa kadha zinanufaika na startup program za vijana kwa sababu wamejisuka na system yote imekuwa centralized. Leo South Africa wanaingiza takribani 1.3 trillion kwa startup program 10 tu za vijana. Imagine pesa ambayo Serikali yao inapata kama wana startup programs 100. Kenya tu hapo wamewekeza kwenye startup programs na wanapata zaidi ya USD milioni karibia 300 kwa program 10 tu. Sisi tunaweza kufanya haya; startup programs chini ya COSTECH hazijipambanui zaidi kiuchumi kwa sababu hazijaweza kusukwa ipasavyo kwa mifumo ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema vijana wa Taifa hili watapata ajira zile milioni nane kwa urahisi kama tukiwekeza kwenye masuala ya teknolojia na hizi startup programs. Kwa sababu startup programs 10 tu zina uwezo wa kuajiri mpaka vijana 1,000. Sasa imagine una startup program 100. Ndio maana naendelea kusisitiza, ni wakati umefika kujisuka upya masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia na uvumbuzi yawe centralized hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya ICT iko chini ya Wizara ya Mawasiliano lakini Sera ya Sayansi na Teknolojia, tena ya siku nyingi, iko Wizara ya Elimu. Sera ya Uvumbuzi mpaka leo mwaka 2021 hatuna Sera ya Innovation kwenye Taifa letu. Ndiyo maana nazungumzia habari ya ku-centralize masuala haya ili yaweze kufanyiwa kazi katika sehemu moja na tuweze kupiga kasi. Trust me not, ikifika 2025 hapa tutatafutana kwa sababu dunia inaenda kwenye kasi ambayo haijawa recorded sehemu yoyote ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye masuala yanayohusiana na ma-bundle. Kumekuwa kuna malalamiko kwa walaji wengi kwamba ma-bundle wanayotumia yanaenda kwa kasi mno. Inawezekana ikawa ni matumizi, lakini kuna tatizo sehemu. Wizara ilielekeza haya makampuni ya simu yaweze kuweka mita zinazoonyesha utumiaji wa ma-bundle, lakini tatizo linakuja kwenye speed ya ma-bundle ambayo tunauziwa. Hizi zinaitwa MPDS hazijawekwa wazi. Kuna makampuni wanatutoa speed ya 3 - 5 MPDS, lakini sasa ma-bundle tunayouziwa, leo Vodacom akinipa mimi bundle la 2GB na Tigo akinipa bundle la 2GB inawezekana la Vodacom likaisha kabla ya Tigo kwa sababu haijawekwa kwamba bundle la 2GB ambalo ninapewa inabidi liwe la speed gani, MPDS ngapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana watumiaji wa mtandao mmoja wanalalamika kuliko watumiaji wa mtandao mwingine, kwa sababu hatuna hata kipimo na hatuwezi ku- trap matumizi ya mitandao yetu. Ndiyo maana leo unaweza ukanunua 2GB ikaisha. Ni haki kwa Mtanzania kulalamika kwamba bundle langu linaisha kama upepo, kwa sababu hatuambiwi speed ya ma-bundle tunayotumia ni MPDS ngapi; na ni vigezo gani vinatumika? Kwa hiyo, labda ifike kipindi tuuziwe ma-bundle kwa mantiki ya speed basi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaambiwa Watanzania ni nchi ya nne kwa ma-bundle rahisi Afrika; lakini sasa kama bundle langu nanunua kwa bei rahisi napewa GB1 sawa, baada ya saa moja, nanunua tena GB1, hiyo ni rahisi in terms of quantity or in terms of speed? Kwa hiyo, ifike mahali sasa Wizara ituangalie hapa; kuna jambo hapa kwenye masuala ya ma-bundle. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wangu wa pili naomba nizungumzie kuhusu masuala ya matumizi ya internet. Naipongeza Serikali, watumiaji wa internet wameongezeka mpaka kufikia milioni 29, lakini nachelea kusema kwamba watumiaji hawa kwa kiasi kikubwa ni watumiaji wa mijini. Sisi kule kwetu Mbinga Kata 29 na vijiji 117 hatuna internet. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani vijiji vyote 117 tunahangaika, mpaka tufike mjini ndiyo tuweze hata kutuma document ama kufungua document kwenye simu. Naomba Waziri wakati anakuja hapa, atueleze sisi wananchi wa Mbinga Vijijini ni lini tutatatuliwa matatizo yetu ya internet? Leo hii kata zote 29 na vijiji 117, jamani naomba Waziri atuambie sisi wananchi wa Mbinga Vijijini tutafanyaje? Maana sasa tunakosa cha kufanya. Tunaomba tuangaliwe tupate na sisi 3G kwa sababu vijana wengi wako kule vijijini, siyo kwamba vijijini hamna vijana ambao wamesoma. Wanataka kuuza kahawa zao kwenye mitandao, wanataka kuuza unga wao kwenye mitandao, tuletewe na sisi kule ili tusije kufanya kazi mjini tukae kule kule kwetu tuuze biashara zetu kule kule tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunafahamu kwamba mawasiliano ya simu ndiyo maisha siku hizi, lakini kata saba hata kupiga simu huwezi. Kata hizo, naomba niweke kwa record; Kitura, Kipololo, Ngima, Mhongozi, Ukata, Amanimakoro, Kihangimauka; na hapa Mheshimiwa Waziri
nataka nikupe taarifa nitashika shilingi, naomba utuambie ni lini kata hizi zitapata mawasiliano ya simu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu vijana katika Taifa lolote duniani ndiyo wadhamini wa Maendeleo wa Taifa hilo yaani they are the trustees of prosperity in the nation. Lakini vilevile vijana katika Taifa lolote ni zawadi kwa Taifa hilo na ndiyo maana kuna msemo unaosema wazee watatangaza vita, lakini ni vijana watakaoenda mbele kupigana au kufariki yaani all the men declare war, but it is the youth must fight and die. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nusu ya watu wote duniani yaani asilimia 50.5 ni vijana chini ya miaka 30; nasema haya kwa sababu Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siyo Rais wa wastani hata kidogo, she is not an average president anafahamu na anatambua vijana wa Taifa hili ndiyo waliobeba mustakabali wa Taifa hili kwa namna moja ama nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatambua makali yetu ya Taifa ya kesho yatazimwa na vijana wa Taifa hili na ndiyo maana juzi katika mkutano wake wa vijana aliahidi mkeka utakaokuja utasheheni na kupambwa na vijana wa Taifa hili. Ila sasa hapa tunamuomba Mheshimiwa Rais aharakishe kwa sababu wananchi mtaani wanalalamika kwamba nazi zimepanda bei (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema maneno haya kwa sababu Rais anafahamu nguvu ya vijana na ndiyo maana tarehe 15 alituita pale Mwanza kuongea na sisi na kutupa moyo na kutupa muelekeo wa Taifa hili. Ndiyo maana nasema kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan she is not an average president at all, anatambua kwamba vijana ndiyo walioikamata dunia hii, kwa hiyo, kwa mantiki hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mkutano ule, tunasema kwamba sisi kama vijana ametuthamini kweli kweli, sisi kama vijana ametupenda kweli kweli na sisi kama vijana ametujali kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama vijana tunamuahidi kufanya kazi kwa kuwa ametupa ari ya kufanya kazi, ametupa nguvu, lakini vilevile ametupa hamasa ya kuendelea kum-support kwa kila jambo atakalolifanya kwa sababu mambo anayotufanyia sisi vijana wa Taifa hili ni ya mfano na tunatiwa moyo kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba kwa bajeti hii ya Serikali ambayo ipo mbele yetu Rais wetu Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi kweli kweli na ninataka niseme hapa kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaenda na trend za dunia inavyoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani kwa lugha moja ama nyingine anaongea lugha moja na ulimwengu wote kwa ujumla na ningependa niwape mfano mmoja; wakati sasa hivi dunia inaenda kwenye deployment ya mtandao wa 5G ambao unaenda kuongeza global economic value ya USD trilioni 13.1 lakini inaenda kuongeza ajira takribani milioni 22.1. Juzi Mkurugenzi wa TCRA alifanya mkutano akatuambia Tanzania kwa mara ya kwanza tunaenda kwenye majaribio ya 5G; mtandao ambao kama leo ulikuwa una-download movie yako ya 20GB kwa zaidi ya lisaa limoja unaenda kui- download kwa sekunde moja mambo ambayo sisi kama Taifa tulikuwa hatufikirii kama tutafika huko, lakini Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan anatuonesha mfano wa namna ambavyo tunapaswa kuongea lugha moja na ulimwengu wote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naongea haya Mheshimiwa Rais pia alijiuliza itawezekana vipi tukafikia malengo haya makubwa ya kimtandao kama Watanzania wengi kwa kiwango kikubwa hawana smartphone. Kodi ambayo imefutwa ya VAT labda kwa ambao hawafahamu ukileta simu hapa nchini kulikuwa kuna kodi tatu ambazo simu ilikuwa inatozwa; ya kwanza - custom processing fee; ya pili - railway development fee na ya tatu - VAT ambapo custom processing fee ilikuwa ni 0.6 percent, railway development fee ilikuwa ni 1.5 percent na VAT ilikuwa 18 percent. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani leo ukiingiza mzigo wako wa milioni 10 kodi ambayo ulikuwa unalipia ni asimilia 20.1, kodi ambayo imeondolewa ni asilimia 18 kwa hiyo, kodi ambayo imebaki kwenye simu ni asilimia 2.1 yaani labda niongee kwa lugha rahisi, ukiwa una mzigo wa milioni 10 kodi yako ilikuwa ni 2,010,000 yaani asilimia 20.1, lakini leo hii una mzigo wa milioni 10 kodi ambayo unachajiwa badala ya milioni 2,100,000 ni shilingi 210,000 ni zaidi ya asilimia 97 ya kodi katika hizi simu ambazo zinaingizwa yaani simu janja, vishikwambi na modem imeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema kufikia asilimia 80 ya watanzania wanaotumia mitandao ifikapo 2025 siyo ndoto ni suala ambalo linatekelezeka na litatekelezeka kabla ya 2025 na sisi kama vijana wa Taifa hili tunamshukuru Mheshimiwa Samia kwa sababu hapa ndipo ambapo tumejiajiri kwa kiasi kikubwa sana. Kwa kweli ndiyo maana naendelea kusema bajeti hii Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi kwelikweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunashukuru kwa haya yote tungependa tuishauri Serikali masuala machache ambayo inabidi ifanyie kazi; moja, tunaomba Serikali ifuatilie masuala ya fedha za mtandao za simu kwa watu ambao wanafariki, yaani Tigo Pesa, M-Pesa, Halotel Money, Zantel Pesa zote hizo naona kwamba utaratibu haujakaa vizuri na tunaona kwamba kuna fedha zinapotea za watu waliofariki kwenye mitandao ya simu ambazo haziwi claimed. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo sasa hivi tunatambua sheria inasema kwamba, ili uweze ku-claim fedha either katika mitandao ya simu au benki kuna utaratibu wa kufuata ule wa wasimamizi wa mirathi, lakini kwa dunia tunavyoenda sasa hivi tunaona huu utaratibu upo very complex kwa sababu ili uweze ku-claim hela za ndugu zako; kwanza huwezi kuambiwa salio mpaka uende na barua ya kuthibitishwa kama msimamizi wa mirathi na uende na viambatisho vingine ambavyo pamoja na hivyo. Lakini utaratibu huu wa kimahakama unachukua zaidi ya miezi mitatu au sita na sheria inasema kwenye mitandao ya simu line inafungwa baada ya miezi mitatu baada ya hapo hela inawekwa kwenye holding fee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi dunia inapoenda kwa nchi za wenzetu kama Uganda kuna mitandao ya simu ambayo mtu akienda next of kin wake yaani mnufaika wake pamoja na uthibitisho wa marehemu kwamba amefariki na cheti cha kufariki anapatiwa hizi fedha. Tunaomba kwenye suala hili utaratibu uimarishwe ili kuweza kuwalinda walaji, lakini vilevile kuhakikisha fedha hizi hazipotei na wanufaika wa makampuni ya simu hawanufaiki wao peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu pia hata line ikifungwa ndani ya miezi mitatu kuna fedha zinabaki kule, lakini hakuna utaratibu wa ku-claim fedha hizi kwa walaji ama kwa Serikali. Kwa hiyo, tunaomba suala hili fedha za watu wanaofariki kwa sababu siyo wote ambao wana-claim iangaliwe kwa namna moja ama nyingine ili hata Serikali iweze kuongeza fedha hapo ili makampuni ya simu wasinufaike wao peke yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Mheshimiwa Waziri alisema itakuja sheria ya Data Privacy and Protection Act, lakini tunaona suala hili ni la muhimu sana kuna fedha nyingi sana zinapotea hapa za waliofariki, tunaomba Serikali ifuatilie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa nishauri kuhusiana na charge za kwenye mitandao ya simu. Sasa hivi ukiwa unatoka kwenye simu unataka kuchukua hela benki yaani unatumia zile USSD code…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani naomba nimalizie kwa dakika moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano NMB *150*66# makampuni mengine yote ya simu una-dial nyota hiyo, yaani charge yako inaenda benki yaani uhitaji kuwa na salio ili uweze ku-access benki yako, lakini kwa Vodacom huwezi ku-access mpaka uweke salio la kawaida hata kama ukiwa na bundle hata kama ukiwa na bundle haikubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itusaidie Vodacom wabadilishe utaratibu huu ili sisi tuweze ku-access benki zetu na kama kuna ma-charge waende kwenye benki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa asilimia 100 bajeti hii na ninakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Sheria ndogo kwa jina lake zinaweza kudogoshwa, zinaweza zikachukuliwa kama kanuni na taratibu ambazo labda hazina umuhimu sana, lakini kiuhalisia sheria ndogo ndizo zinazoendesha maisha ya kila siku ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwa kuishukuru Serikali na mamlaka zilizokasimiwa kwa kutunga sheria ndogo. Kwa kweli kama wangekuwa wanatumia vibaya mamlaka hayo, pangekuwa pana mtifuano mtaani. Tunaamani na utulivu kwa sababu mamlaka zilizokasimiwa kutunga sheria ndogo zinatendea haki mamlaka hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo zimebeba mstakabali wa haki za watu, ndizo sheria ambazo zina-define haki na usawa wa watu katika jamii, ndizo sheria zinazoleta muongozo katika haki za msingi ikiwemo haki ya kupata kipato, haki ya kupata ujira, haki ya usalama na faraha na haki ya kushirikiana na watu wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, haki hizi hususan haki ya ajira na ya kupata kipato ambazo ni muhimu kwa maisha ya binadamu ya kila siku na ambazo ni haki za Kikatiba, ni za muhimu sana ziangaliwe pale ambapo sheria ndogo zinatungwa. Kwa sababu ndizo ambazo zinagusa uhalisia wa maisha ya watanzania ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo mchakato wake ni tofauti na sheria mama. Sheria ndogo zinapotungwa na mamlaka zilizokasimiwa mamlaka hayo na Bunge, zinaanza kutumika kabla hazijaletwa Bungeni kupitiwa na Bunge na ndiyo maana ni muhimu sana kwa mamlaka zilizokasimiwa madaraka hayo kuhakikisha sheria ndogo zinazotungwa zinalinda haki na ustawi wa Watanzania, lakini vilevile zinazingatia masharti ya maendeleo katika jamii zetu za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya changamoto ambazo zimesemwa na Kamati ni sheria ndogo kutokuzingatia masharti ya uhalisia katika jamii, yaani zinatungwa bila kuangalia uhalisia wa maisha ya Watanzania. Jambo hili limekuwa likileta changamoto za mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, na napenda nianze kwa kusema kuhusiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025. Dira ya Maendeleo ya Tanzania inasema tutajenga uchumi imara, anuai, himilivu na shindani ambao utazingatia mabadiliko ya masoko na teknolojia. Kwa hiyo, lazima sheria ndogo zinazotungwa ziende kwa mlengo huu ili kuhakikisha ya kwamba Taifa letu linapata maendeleo kwa kadri ya tulivyojiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa napenda nielezee masuala ya sheria ndogo yanavyoshika masuala ya teknolojia ambavyo siyo sahihi. Napenda nielezee kanuni elekezi za LATRA ambazo zimesababisha kampuni za teknolojia kama Bolt na Uber kusitisha huduma zake hapa nchini kwetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni elekezi za LATRA hazikuwa sahihi. Nasema hazikuwa sahihi kwa sababu zinaenda kinyume na Dira ya Maendeleo ya 2025, lakini pamoja na hilo, LATRA hawakuwa na mamlaka ya kutunga kanuni zile ambazo zinasababisha kampuni za ubunifu na teknolojia kusitisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA inahusiana na ku-regulate usafiri siyo masuala ya teknolojia. Bolt na Uber siyo kampuni ya usafirishaji, ni kampuni ya ubunifu na teknolojia. Kwa hiyo, LATRA hawakuwa na mamlaka ya kutunga kanuni ambazo zinaenda kufungia ubunifu wa teknolojia ya Uber na Bolt. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika nchi yetu yametapakaa. Kisera yako Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, lakini kiutendaji kwa kiasi kikubwa yako Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Sasa LATRA walipata wapi mamlaka ya kugusa masuala yanayoendana na teknolojia hali wakijua mamlaka yao ni kwenye masuala ya usafirishaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa napenda niishauri Serikali yangu, na ushauri huu niliutoa mwaka jana; masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yameparanganyika, ni wakati sasa tuwekee uratibu ili kuhakikisha wabunifu hawa hawawi frustrated.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni za Uber na Bolt kama zilivyo kampuni zingine za ubunifu, ni kampuni za hiyari kujiunga, mtu halazimishwi kujiunga, na kampuni hizi zinagusa maslahi ya pande mbili; zinagusa maslahi ya wananchi na zinagusa maslahi ya madereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA kwenye kanuni zao walisema wanafungia Uber na Bolt kwa sababu wana-charge madereva commission ya asilimia 20 mpaka 25. Wanataka Uber na Bolt wa-charge commission isiyozidi asilimia 15, sawa labda hoja ipo. Labda hoja ipo, lakini LATRA baada ya Uber na Bolt kusitisha huduma ndiyo wanasema tutakaa nao mezani. Jamani kila siku tunasema hapa, nyenzo namba moja ambayo inachagiza ajira duniani kote ni nyenzo zinazoendana na sayansi na teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka commitment ya ajira milioni 10. Ajira hii kwa urahisi itapatikana kwa nyenzo za sayansi na teknolojia, siyo popote pale. Sasa LATRA walitakiwa kukaa mezani na kujadili kabla ya kufunga na siyo wamefunga ndiyo wanasema watajadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii zaidi ya vijana 100,000 ambao walisema walikuwa wanawatetea wako mtaani. Ile asilimia 15 wanapata? Hawapati, wameanza upya kwa applications nyingine. Sasa tunaenda mbele, tunarudi nyuma? Wale waliokuwa wanawatetea hawafanyi biashara, wananchi ambao walikuwa wanapata ahueni na wenyewe mambo yao ni magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie, ile shilingi 30,000 ambayo labda mwananchi alikuwa analipa akitoka Mwenge kwenda Posta, alikuwa analipa kwa shilingi 10,000. LATRA unaumia nini mwananchi akilipa shilingi 10,000? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nia yetu, nia ya teknolojia ni kurahisisha maisha kwa wananchi. Mwananchi maisha yake yamerahisika sasa sisi tunaumia nini? Kama kulikuwa kuna jambo si wanakaa mezani tunalitatua? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uliangaliwa upande mmoja, upande wa wananchi ambao maslahi yao na haki zao ambao maisha yao yamerahisika hawakuangaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi napenda niishauri Serikali yangu wawashauri LATRA, kanuni hizi wazivute nyuma. Kwa kweli ni kanuni ambazo hazina maslahi kwa madereva wala kwa wananchi ambao walikuwa wananufaika kwa huduma ya Bolt na Uber. Lakini vilevile tuangalie na document zetu kama dira za maendeleo. Kwa sababu kama tukiwa tunatunga kanuni kama hizi kwakweli inakuwa hatuwatendei haki Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi Kampuni za Uber na Bolt hizi siyo teknolojia zao kwa hapa Tanzania, wananunua hakimiliki. Kwa hiyo, na wenyewe wanazilipia, walipaswa kusikilizwa kwenye commission wanayoipata asilimia ngapi ni faida yao wenyewe binafsi? Investment yao wanailipiaje? Lakini siyo kuwafungia tu, kwa sababu hizi siyo teknolojia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mfano wa nchi nyingine, kwa mfano ukilipa shilingi 70,000 kama nauli ya Bolt ama ya Uber kuna charge nyingine ambazo zinaenda kwa mwananchi ambazo zinakaribiana na nusu ya ile bei karibia shilingi 30,000. Lakini kwa wenzetu hizi Uber na Bolt zinaendeshwa na wale wamiliki wa gari wenyewe, yaani kama mimi nina IST yangu ndiyo najisajili naendesha mwenyewe. Kwa hiyo, ile faida ya moja kwa moja naipata mimi mwenyewe. Tofauti na sisi, watu wengi ambao wanaendesha Bolt siyo wamiliki, ni watu ambao wameenda kuomba ajira kwa wamiliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hapo ndiyo changamoto inapoanzia, kwa sababu ule ujira inabidi waugawanye ambao siyo tatizo la Uber. Kwa hiyo, kama mtu hanufaiki siyo tatizo la Uber, ni tatizo la mfumo wenyewe uliopo. Kwa hiyo, kanuni hizi zilitungwa kwa kuangalia juu juu siyo kwa kufanya utafiti wa kina na kuhakikisha kwamba tunalinda makundi yote. Wale vijana ambao wamejiajiri, lakini vilevile na wananchi ambao wanatumia huduma zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, LATRA ilibidi wajielekeze kwenye masuala ya muhimu kabisa na kanuni ambazo zinashika mustakabali wa Taifa, kwa mfano, suala la ving’amuzi kwenye mabasi. Ving’amuzi vilivyofungwa kwenye mabasi havidhibiti mwendo, vinatoa tuu alert kwamba speed imezidi, yaani baada ya pale dereva anakanyaga mwendo kama kawaida. Vinaishia kupigia abiria tu kelele gw’igw’igw’i kwenye mabasi, havidhibiti speed. Yaani siku hizi dereva speed inazidi 80 anakanyaga mwendo king’amuzi kinalia tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ving’amuzi vilivyofungwa kwenye mabasi havidhibiti mwendo. Labda tufikirie upya kanuni ambazo tumezitunga. Je, tuna ulazima wa kuweka ving’amuzi ambavyo vinadhibiti mwendo ambavyo mtu akizidi 80 gari yenyewe ina-stabilize palepale havizidi. Haya ndiyo masuala ya msingi kabisa ambayo mamlaka tulizozipa mamlaka zinapaswa kuyaangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi teknolojia zimekuwa, kwa hiyo lazima tuyaangalie masuala haya kwa umuhimu sana, lakini vilevile control systems zinafanya nini? Kwa sababu dereva anaongeza speed lakini no control systems. kwa hiyo, tuangalie ving’amuzi, lakini vilevile TBS hawakuthibitisha hivi ving’amuzi, walisema havina ubora lakini vimefungwa kwenye mabasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kweli mimi napenda kuhimiza mamlaka ambazo Bunge imezikasimu mamlaka ya kutunga kanuni kwa niaba yake lazima zitunge sheria ndogo kwa ufanisi mkubwa na kwa kuzingatia haki, usawa na maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla. Kwa kweli napenda kuishauri Serikali masuala haya, kanuni hizi elekezi za LATRA ziangaliwe kwa jicho la upekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Miradi inayohusisha fedha za umma ama fedha za Watanzania lazima itekelezwe kwa kuzingatia masuala yafuatayo; moja, lazima ichagize ufanisi; pili lazima iendane na thamani ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya mradi; tatu, lazima iwekewe ushindani; nne lazima ilete maendeleo ya kuiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya umma ni lazima zitekelezwe kwa uadilifu mithili ya matendo ya mke wa mfalme, isiwe hata ina thumni ya udanganyifu ama isiwe hata ina thumni ya ubadhirifu wa aina yoyote. Miradi inayoendeshwa kwa fedha za Watanzania ambazo ni fedha za umma lazima iendeshwe kwa uwazi, kwa sababu rushwa mwenzake ni siri. Miradi yoyote inayoendeshwa kwa usiri mkubwa bila sababu za msingi lazima ilete mianya ya rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima ifahamike, kwamba, wale waliopewa dhamana ya kusimamia miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha umma lazima wafahamu kuwa hawana hati miliki ya miradi hiyo. Zile fedha ni za Watanzania. na kwa sababu tumewaamini kwa majukumu hayo lazima watekeleze majukumu hayo kwa uadilifu mkubwa, kwa kuzingatia sheria na taratibu na wahakiishe fedha za umma zinatumika kwa maslahi ya Watanzania, lakini si kwa maslahi ya mtu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi hii inapambana na umasikini kwa kiasi kikubwa sana. Nchi hii mpaka leo tunapambana na kupeleka huduma za msingi kwenye jamii, tunapambana na huduma za afya, tunapambana na huduma za maji, tunapambana na huduma za umeme, barabara; ni kwa sababu wananchi hawajafikiwa. Nchi hii mpaka leo Watanzania asilimia 28 ni masikini wa kutupwa wa huduma za msingi.
Mheshimiwa Spika, katika nchi hii Mtanzania wa kawaida pato lake la kila siku ni 2,798/= na si kila Mtanzania anaweza kupata kiasi hicho cha fedha. Nchi hii bado tunapambana na Watanzania. Sasa inasikitisha, inashangaza, inahuzunisha kuona baadhi ya watu wanaweza kupandisha mabega juu wakajivika viti vya ufalme na kutumia fedha za umma kwa udanganyifu, kwa kiburi kikubwa na kwa uthubutu uliopitiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Tanga ni mojawapo ya bandari zenye umuhimu mkubwa si tu kwa Taifa letu la Tanzania bali Afrika Mashariki. Bandari hii hivi karibuni imefanyiwa maboresho kwa kuongeza kina pamoja na ujenzi wa gati ili kuweza kuongeza ufanisi katika kuhudumia mizigo kutoka tani laki saba hadi tani milioni tatu. Zoezi hili lilifanyika kwa kuongeza kina cha maji mpaka kufikia mita 13, lakini vilevile pamoja na ujenzi wa gati.
Mheshimiwa Spika, wakati wa maboresho ya bandari hii kina cha maji kilichokuwa kinaongezwa ilikuwa ni katika eneo la kuingilia baharini ambapo zamani mizigo ilikuwa inaenda kuchukuliwa baharini kwa kadiri ya kilometa 1.7, kwa hiyo maboresho ilikuwa ili ule urefu upungue mpaka kufikia mita 200. Hili lilikuwa ni jambo jema na kwa dhamira njema kwa maslahi ya taifa letu, lakini katika mchakato huu tumepigwa.
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya CAG inasema, udanganyifu mkubwa umetokea katika zoezi hili la maboresho ya kuongeza na kufanya marekebisho katika Bandari hii ya Tanga. Tarehe 03 Agosti, 2019 Mamlaka ya Bandari Tanzania iliingia mkataba pamoja na mkandarasi mkuu kwa ajili ya kufanya maboresho katika Bandari ya Tanga. Mkandarasi huyu mkuu ni kampuni inaitwa kampuni ya CHEC.
Mheshimiwa Spika, wakati mkataba huu unaingia kazi iliyotakiwa ifanyike pale ilikuwa ni ya thamani ya bilioni 176.36 ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari iliiingia na Kampuni ya CHEC ambaye ndiye mkandarasi mkuu kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hii. Kampuni hii ilipewa kazi na Mamlaka ya Bandari kwa kazi kuu tatu; moja kuongeza kina cha lango na sehemu ya kugeuzia meli katika bandari ya Tanga; mbili kufanya tathmini ya athari ya kimazingira; tatu kununua vifaa kwa ajili ya shughuli za bandari.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu walioingia kati ya hawa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari pamoja na Kampuni ya CHEC ulikuwa ufanyike kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka tarehe 03 Agosti, 219 mpaka Agosti, 2020. Japo baadaye sasa kutokana na changamoto walizoelezea mkataba ulikuwa extended kwa mwaka mmoja kwa sababu haukuweza kumalizika mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, Mkataba ule ambao ni kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na mkandarasi mkuu, Kampuni ya CHEC, ulikuwa una mapungufu makubwa sana. Moja, Kampuni ya CHEC ambaye alikuwa ni mkandarasi mkuu kabla hajapewa mkataba na bandari alikuwa ameshaingia mkataba na mkandarasi ubia kwa ajili ya kumpa kazi ile ambayo alikuwa anaenda kufanya na usimamizi wa bandari. Yani kazi yake aliyokuwa anapewa alikuwa ameshaenda kumpa third part aifanye, na aliingia mkataba huo na kampuni ubia ya Kitanzania tarehe 01 Agosti, 2019 kabla hajapewa mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
Mheshimiwa Spika, baada ya siku mbili ndipo mkandarasi mkuu Kampuni ya CHEC akaenda kupewa kazi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. Katika mkataba aliousaini, Kifungu kidogo cha (4.4) kinasema, hairuhusiwi mkandarasi mkuu kwenda kugawa kazi ambazo amepewa kwenye mkataba, labda kama ni ulazima lazima atoe notice ya kabla ya siku 28 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, kama hiyo kazi ina umuhimu wa kwenda kuitoa. Cha kushangaza masharti hayo hayakufuatwa kwa sababu, mkandarasi mkuu tayari alikuwa ameshaingia mkataba na mkandarasi mbia wa kumpa kazi hata kabla hajasaini mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi mkandarasi mkuu, Kampuni ya CHEC baada ya kusaini mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, mkataba wa bilioni 176 akaenda kuigawa kazi ile kwa mkandarasi mbia kwa gharama za chini. Kazi aliyompa mkandarasi mbia ilikuwa ni ile kazi moja ya kuongeza kina na ujenzi wa gati, kazi ambayo ilikuwa inagharimu takribani asilimia 60 ya fedha yote bilioni 176, ile kazi ni ya bilioni 104 kwa ajili ya ile kazi ya kwanza ndiyo akampa mkandarasi mbia. Lakini badala ya kumpa kwa bilioni 104 aliyoichukua Serikalini akampa kwa bilioni 40. Kwa hiyo, mkandarasi mkuu hakufanya kazi, kazi akampa mkandarasi mbia kwa bilioni 40, bilioni 64 akaweka mfukoni.
Mheshimiwa Spika, wakati haya yanatokea Mamlaka ya Bandari ipo, Katibu Mkuu yupo, Naibu Katibu Mkuu yupo, Mkurugenzi wa Bandari yupo na Waziri yupo. Ubadhirifu kama huu unafanyika mbele ya macho yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo hili halikubaliki, bilioni 64 ingeweza kujenga madarasa 3,200, lakini kampuni, tena ya kigeni, bila ya woga wa aina yoyote, inaenda kinyume na masharti ya mkataba, anagawa kazi hata chini ya nusu ya bei ya fedha ya Watanzania aliyopewa. Zaidi ya nusu ya fedha, bilioni 64 kati ya bilioni 104 ya kazi moja tu anaweka mfukoni; inawezekana vipi? Kwenye nchi hii ya masikini asilimia 28 ya Watanzania inawezekana vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachonishangaza zaidi ni kwamba, Kamati hawakuliona? Mbona haipo kwenye ripoti yao? Imekuwaje? Hawakupata maelezo kutoka Serikalini? Wakati wanafanya majumuisho watuambie kwa nini hawakuliweka jambo kubwa kama hili linalogusa maslahi ya Watanzania na fedha za umma kwenye ripoti ya kamati? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haikubaliki.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilikuwa nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Kapinga; ukisoma Ripoti ya CAG na kile ambacho Kamati imeleta, hawaku-cover maeneo yote, it is hardly like 10 percent tu. Sasa labda kama Bunge na wewe Mheshimiwa Spika, nampa tu taarifa lakini, tuangalie uwezekano labda wa ku-extend muda ili kamati iweze kupata muda mwingi wa ku-cover ripoti nzima, lakini as it stands haija-cover maeneo yote.
SPIKA: Sasa hiyo ni taarifa kuhusu hoja gani? Au ni pendekezo? Mheshimiwa Judith endelea na mchango wako, nadhani yeye ametoa mapendekezo.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, hii imetoka kwenye Ripoti ya CAG kuhusiana na ukaguzi wa mashirika ya umma. Suala kama hili hata kama kamati ilikuwa ina muda mchache it can’t go under looked ni suala liko obvious na ubadhirifu wa wazi. Yaani hata ukipima yale masuala makuu yaliyoletwa na Kamati hili lilitakiwa liwepo ndani ya ripoti ya Kamati. Kwa hiyo, Kamati ya PAC itakapokuja kujumuisha watuambie ilikuwaje hapa hili halikuwekwa hata katika yale au wali- discuss nini? Serikali ilitoa majibu gani; ili tuweze kupata, kwa sababu huu ni wizi wa wazi kabisa; ni udanganyifu wa wazi kabisa, yaani hauna konakona. Kwa hiyo, kamati inavyokuja kufanya majumuisho watuambie.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba kupendekeza; kwa sababu fedha za umma ni fedha ambazo zinakusanywa kwa Watanzania kwa jasho, mpaka leo tunahangaika na mikopo ya watoto wetu vyuo vikuu, tunahangaika na vituo vya afya, tunahangaika na barabara, tunahangaika na TASAF, halafu anakuja mtu anachukua bilioni 64 kiurahisi namna hii. Imeshapita miaka miwili, vyombo vya ulinzi na usalama viko wapi? TAKUKURU iko wapi? Kuna mtu hapa hafanyi majukumu yake inavyotakiwa. Tunaomba maelezo ya kina (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashindwa hata kusema maazimio kwa sababu, sijui kamati wali-discuss ama hawaku-discuss ama ilikuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama kutakuwa kuna maelezo naomba tuazimie kwamba hatua za haraka zichukuliwe kwenye jambo hili na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya ulinzi na uaslama.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kengele ya pili ilishagonga, lakini nakuongeza dakika tatu umalizie hoja yako. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuhitimisha.
Mheshimiwa Spika, sisi kama taifa. Sisi kama Wabunge tuliopewa dhamana tuna haki ya kuwa vinara kwenye kulinda fedha za umma. Tuna haki ya kuwa vinara kwenye kulinda fedha za umma. Kama kuna watu waliambiwa walete taarifa, hawakuleta, wanapaswa kuwajibishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupelekana kwenye vyombo vya usalama ni end result. Tangu mchakato unaanza wahusika walikuwepo wapi? Sheria na taratibu zinaonesha, yaani kila siku tutakuwa tunashikana mashati mwishoni?
Mheshimiwa Spika, lazima kama Taifa tuhakikishe fedha za umma ambazo ni fedha za Watanzania zinatumika kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Aliyekuwa Rais wa South Afrika Hayati Nelson Mandela, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, aliwahi kusema na nitamnukuu: “From the poorest of countries to the richest of nations, education is the key to moving forward in any society”. Kwa lugha yetu ya Taifa anasema kuanzia kwenye nchi masikini kabisa hadi mataifa tajiri kabisa elimu ndiyo ufunguo pekee wa maendeleo katika jamii yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maneno haya kwa namna moja ama nyingine yalielezwa na Rais wetu mpendwa na anayewapenda Watanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Aprili, wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na alisema napenda nimnukuu: “Lazima kufanya tathmini ya elimu itakayomsaidia Mtanzania. Tuangalie mitaala yetu tuone mtaala utakaotupeleka mbele na kukuza Taifa letu”. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maneno haya ya Rais wetu mpendwa kwa namna moja ama nyingine yanatuonyesha umuhimu wa mfumo wa elimu katika kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa letu. Mfumo wa elimu kwa namna moja ama nyingine ndiyo unaoamua nguvu kazi ya taifa letu itasukuma vipi gurudumu la uchumi katika nchi yetu. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua ajira za wananchi wa Tanzania zitapatikana vipi na kwa kiasi gani. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua umaskini katika taifa letu utaondolewa ama utapungua kwa kiasi gani na kwa wakati gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu mengi yameongelewa kuhusiana na kubadilisha mfumo wa elimu lakini mimi napenda kujikita katika namna ya kulinda mfumo wa elimu. Hata kama tutafanya mabadiliko ya mfumo wa elimu tusipolinda mfumo wa elimu ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kueleza namna gani tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, hapa ningependa nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako; kwa kipindi hiki ambacho amekua Waziri tumeona mabadiliko yasiyo na tija na ya haraka katika mfumo wa elimu, kidogo yameweza kuwa contained. Huko nyuma mabadiliko katika mfumo wa elimu yalikuwa yanaweza yakafanyika abruptly, muda wowote na ku-disturb walaji ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana wa Taifa hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa kipindi hiki ambacho amekuwa Waziri, amejitahidi sana kuwalinda walaji ambao ni vijana wa Tanzania. Hongera sana mama yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda nijielekeze ni kwanini tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, kwa sababu mabadiliko yoyote katika Mfumo wa Elimu yanaweza kuathiri vijana wa Taifa hili kwa kiasi kikubwa sana. Tunashukuru Mungu leo tuna Mheshimiwa Prof. Ndalichako, kesho hatutakuwa naye. Kwa mantiki hiyo, inatupasa kulinda mfumo wa elimu kwa kuweka taratibu ambazo zitalinda misingi ya mfumo wa elimu. (Makofi)
Mhehimiwa Spika, hapa napenda kutoa mifano michache ili muweze kunielewa. Mwaka 1997 aliamka mtu akafuta UMITASHUMTA, lakini tunashukuru Serikali ilirudisha UMITASHUMTA mashuleni na sasa hivi inafanyika katika utaratibu mzuri tu. Hii ilikuwa hatari sana kwa sababu wote tunajua michezo namna ilivyo multibillion industry duniani.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa pili. Kuna kipindi pia kuna mtu aliamka akaamua akataka kuunganisha Chemistry na Physical; yaani kipindi kile somo hili lilitakiwa liitwe Physics with Chemistry. Tunashukuru mambo haya hayakuweza kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa tatu, mwaka 2014, Kidato cha Nne waliwekewa alama zao za ufaulu kwa kutumia wastani wa point ama kwa lugha nyingine GPA. Vijana waliomaliza 2014 na 2015 waliwekewa kwa mfumo huu na sababu zilizotolewa kipindi kile, ni ili tuwe na system inayofanana. Mwaka 2016 tukarudisha mfumo ambao tumeuzoea wa division. Kwa hiyo, tuna wanafunzi katika nchi hii ambao kuna kipindi waliwekewa marks zao kwa mfumo wa GPA, baadaye ikabadilishwa ikarudisha division. Nasema haya ili mnielewe ni kwa nini inatupasa kulinda mfumo wetu wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, Serikali iliwahi kugharamika kupeleka walimu nje waweze kujifunza programme za re-entry, kuwasaidia watoto wa kike wanaopata ujauzito waweze kuwa accommodated tena katika mfumo wa elimu. Zoezi hili lilikuwa frustrated kwa sababu lilikuwa halilindwi. Baadaye ikaonekana halina mantiki, likawekwa kwenye kapu, lakini tayari tuligharimika kuwasomesha walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, ilitokea programme ya voda fasta ya walimu kusomeshwa miezi mitatu. Walimu walisomeshwa na wakapelekwa kufundisha watoto wetu na kuambiwa kwamba wana-qualify. Miezi hii, mitatu! Naeleza haya ili kuonesha ni kwa nini tulinde mfumo wetu wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii mtoto wa miaka mitatu yuko boarding school. Mtoto wa miaka mitatu mama yake au baba yake amempeleka boarding school. Naeleza haya ili tuweze kuona hatari hizi na kuona umuhimu wa kulinda mfumo wetu wa elimu.
Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningependa sasa nilieleze hapa, leo hii kuna vijana katika nchi hii walisoma miaka mitatu chuo, walivyomaliza wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. Inawezekana sisi tukawa tumesahau, lakini wale vijana hawajasahau, wamelibeba hili kwenye mabega yao na kwa machozi zaidi ya miaka saba sasa wanatembea nalo bila kupata msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mnakumbuka, Chuo kilikuwa kinaitwa Chuo cha Kilimo Mbeya (Mbeya Polytechnic College) kati ya mwaka 2013 mpaka 2016. Chuo hiki kilipewa usajili na NACTE, vijana walisajiliwa na kudahiliwa na walisoma pale miaka mitatu. Baada ya kusoma miaka mitatu, vijana hawa wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. NACTE wakasema Chuo chenu kilikuwa hakilipi ada za usajili. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Jidith, muda hauko upande wako.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ambayo iko mezani na kwa kuanza ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba sekta hii ya Uwekezaji Viwanda na Bashara inaleta tija katika Taifa letu, lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo Wizara inafanya, lakini pia niwapongeze watendaji wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo inafanyika schini ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kipekee kwa sababu, wasilisho la Mheshimiwa Waziri limeonesha namna ambavyo Mheshimiwa Rais amefungua fursa za ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Waziri imetuambia kuanzia Julai, 2022 mpaka mwezi huu Machi, 2023 takribani ajira 81,8200 zimezalishwa katika sekta za miradi ya kimkakati na uwekezaji kwa kweli ni jambo ambalo linatia faraja sana kwa sababu wote tunafahamu changamoto ya ajira kwa vijana wetu. Kwa hiyo, kipekee sana nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tumeahidi ajira kwa vijana ifikapo 2025 inatekelezwa kwa kasi na kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kujikita kuchangia kuhusiana na programu za ubunifu ambazo Mheshimiwa Waziri ameziongea kwanza niipongeze Wizara kwa hatua ambazo inafanya katika kuhakikisha kuwa ajira kwa vijana zinapatikana na Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa namna ambavyo Wizara inawekeza katika programu za ubunifu za vijana ikiwemo kuatamia wabunifu vijana. Ameeleza hapa katika mwaka wa fedha uliopita waliwatmia vijana wabunifu 27 na kufikia Machi mwaka huu wamewatamia vijana watano.
Mheshimiwa Spika, ameeleza hapa, kwamba katika mwaka wa fedha uliopita waliatamia vijana wabunifu 27 na kufikia Machi mwaka huu wameatamia vijana watano. Niipongeze Wizara, lakini nimshauri Mheshimiwa Waziri, jitihada hizi hazijitoshelezi kulingana na maendeleo ya teknolojia ambayo tunayo, lakini vilevile kutokana na fursa ambazo vijana wanazihitaji programu hizi bado ni ndogo sana. Na sio kwamba, tunailaumu Wizara kwamba, haifanyi kwa kadiri ya ambavyo inatakiwa kufanya, mimi naamini Wizara hii ilitakiwa kufanya zaidi ya haya ambayo yanafanywa.
Mheshimiwa Spika, programu za ubunifu katika Taifa hili zinafanywa na kila Wizara, lakini hatuna uratibu ambao unaonesha ni programu ngapi zinafanya biashara na ambazo zimekuwa stahimilivu kwenye soko la biashara; na hii ndiyo Wizara ambayo ina jukumu la masuala yote ya kibiashara. Kwa hiyo mimi nilitegemea pamoja na kwamba Wizara inatuonesha program ambazo wao wanazifanya, walitakiwa kutuonesha uratibu wanaoufanya kwenye programu za ubunifu katika Wizara zote, na watuoneshe ni programu ngapi za vijana zinafanya biashara na zimechangia ajira kwa kiasi gani, ndiyo kazi ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapoendelea mbele, mimi nafahamu kwa mfano COSTECH ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu wameingia mkataba na CRDB hapa juzi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwenye programu za ubunifu. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pia inafanya programu hizo, Wizara ya Kilimo na Wizara nyingi sana, lakini Wizara hii itusaidie kufanya uratibu ili tuweze kujua programu gani za ubunifu zinastahimili kwenye soko la ajira na soko la kibiashara.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana kwa sababu, hapa tumesema ajira ambazo zinaratibiwa, ndizo hizi ambazo zimeripotiwa. Ajira hizi ambazo wanazalisha vija awenyewe ni muhimu sana kwa sababu tunakoelekea kila siku tunasema teknolojia ndiyo ambayo inaajiri vijana wengi zaidi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atusaidie ili tuhakikishe kwamba vijana hawa ambao wanaweka jitihada kubwa sana katika programu zao za ubunifu Serikali inawa-support na wanaratibiwe vizuri. Pale ambapo uratibu ukifanyika changamoto zikitokea ni rahisi sana kwa Wizara husika kuelekeza sekta inayohusika kuwasaidia vijana hawa ili wasiweze kudondoka katika soko la kibiashara.
Mheshimiwa Spika, naomba niongee kidogo pia kuhusiana na suala ambalo limezungumziwa hapa awali. Sisi kama Taifa wote tunafahamu, kwamba shughuli zote zinazohusisha utawala wa Taifa letu lazima ziongozwe na Katiba, Sheria, taratibu na kanuni ambazo tumejiwekea sisi wenyewe. Ibara ya 97 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalipa Bunge hili jukumu la kutunga sheria, lakini Katiba hiyohiyo inaipa Mahakama jukumu la kusimamia haki; na Kikatiba ndio taasisi ya mwisho ambayo inasimamia haki katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane; katika kutekeleza miongozo na shughuli ambazo zinaleta tija ya maendeleo katika Taifa letu ni busara na weledi mkubwa kwamba, taratibu na kanuni ambazo tumejiwekea sisi wenyewe na sheria ambazo Bunge hili limezitunga ni lazima zizingatiwe. Sheria yetu ya Ushindani inasema wazi kabisa; nasema hivi kwa sababu, tukicheza tusifuate wenyewe sheria ambazo tumejiwekea tutakuwa hatuendi katika mwenendo ambao ni sahihi; sheria ya ushindani inasema wazi kabisa kwamba kwenye makubaliano yoyote ambayo yanachagiza kuathiri soko ama yanachagiza kuathiri soko kwa maana ya ushindani, makubaliano yote ambayo yanajikita kwenye kuharibu ushindani ni makubaliano ambayo hayakubaliki kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sheria ambayo tulitunga sisi wenyewe ya ushindani, kifungu cha nane kifungu pia cha 5 kinatuambia wazi namna ya makubaliano ambayo yanakubalika katika soko letu la ushindani. Kifungu hicho kinasema kwamba makubaliano ambayo yanakubalika ni yale ambayo, moja, yanakuwa makubaliano ambayo hayazidi utawala wa soko kwa asilimia 35, lakini makubaliano haya ambayo sheria inatambua ni yale makubaliano ambayo yanalinda walaji dhidi ya soko la ushindani.
Mheshimiwa Spika, sasa hapa issue ni kufuata sheria na taratibu. Hakuna mwekezaji yeyote anayekatazwa kununua hisa za kampuni yoyote, issue kubwa ni kwamba taratibu ambazo tumejiwekea ni lazima zifuatwe.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu sababu ya sheria kuweka taratibu hizi, moja, ni lazima tudhibiti soko dhidi ya ushindani, lakini pili, lazima tuhakikishe walaji wanapata bidhaa kwenye soko, na tatu, bidhaa lazima ziwe stahimilivu kwenye soko. Sasa tusipohakikisha kwamba taratibu hizi zinafuatwa inakuwa ni jambo ambalo kwa kweli linaleta maswali mengi sana. Lakini mategemeo yetu yalikuwa ni kwamba, taasisi ambazo tumezikasimu madaraka haya ya kusimamia taratibu hizi zinafanya mambo hayo kwa weledi mkubwa sana, ili kuepuka hii tafaruku ambayo tunayo sasahivi.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme yafuatayo; wakati hii Kampuni ya Scancem inataka kununua hizi shares za AfriSam Mauritius ni jambo ambalo ni la heri, lakini mgogoro umeanzia kwenye kujiridhisha kama hawa wawili wakiwekwa kwa pamoja wanazidi utawala wa soko kwa asilimia 35. FCC wenyewe wamefanya tafiti na wana data za kuonesha kuwa hizi kampuni mbili zikiungana kwa pamoja zitasababisha utawala wa soko kwa zaidi ya asilimia 35.
Mheshimiwa Spika, na ningependa nitoe mfano; kigezo kikubwa ambacho Mahakama imetuongoza tukifuate ni kigezo cha utawala wa soko, kwamba ni nani anayeuza zaidi.
Ukiangalia takwimu za FCC ukiunganisha hizi kampuni mbili, Twiga Cement na Tanga Cement, kwa pamoja zitauza asilimia 52 katika soko. Lakini pia takwimu zinatuonesha, kwamba katika uuzaji, katika kanda tano kubwa, kanda nne zitatawaliwa na hizi kampuni mbili. Kwa mfano, Kaskazini watauza kwa asilimia 92, Kanda ya Ziwa asilimia 77, Pwani asilimia 60. Kanda ya Kati asilimia 49 ni Kanda ya Kusini tu pekee ambayo imeachwa kwa sababu, soko lake liko dominated na Dangote.
Mheshimiwa Spika, sasa kama sisi wenyewe, sheria tunazitunga wenyewe, takwimu tunafanya wenyewe na tunazo sisi wenyewe, ni kwa nini tunakwenda kinyume na taratibu ambazo sisi wenyewe tumejiwekea?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa hakuna mtu anayekatazwa kununua hisa, tunachoshauri, taratibu zifuatwe. Kama Scancem hisa zake zinaonekana zimezidi…
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kuna Taarifa kutoka kwa mtoa hoja.
TAARIFA
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nampongeza mchangiaji anavyochangia. Naomba tu kumpa taarifa kwenye eneo la kwamba, kanda nyingi zitakuwa zinahudumiwa na kampuni hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, uuzaji wa saruji kwenye nchi hii hauuzwi kikanda. Ukienda Kagera utakutana na Dangote, ukienda Tanga utakutana na Dangote, ukienda Mtwara utakutana na Dangote. Kwa hiyo, Tanzania nzima inauziwa saruji na kampuni zote 14. Kwa hiyo, hiyo hoja ya mwanzo ya analysis tutaijibu badaye, lakini nilitaka tu kumpa hiyo, soko la Tanzania halijagawanywa kikanda. Ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu Mheshimiwa Waziri hajanielewa. Hii sio ripoti yangu mimi, ni ripoti ya Tume ya Ushindani inayoeleza mauzo kwenye kila kanda; na ndiyo ripoti iliyotumika kuamua kama Scancem wanapewa hisa za Tanga Cement ama hapewi. Kwa hiyo, mimi nilichofanya hapa ni kudurufu kile ambacho FCC wenyewe wamesema. Na hii ripoti inaeleza tu kama hawa wawili watauzaje kwenye soko. Ndio kila kampuni inauza, lakini inategemea na percent ya kila kampuni kwenye kanda husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha, muda wangu umeisha. Tunachoshauri ni kwamba, taratibu zifuatwe, kama twiga anataka kununua wahakikishe manunuzi hayazidi ile threshold ambayo tumejiwekea, asilimia 35 mpaka 40 kwa vigezo maalum. Kwa sababu wao wenyewe, tunatambua, hata vigezo ambavyo amepewa na FCC vya kununua baadhi yake anavipinga. Sasa na sisi kama Watanzania lazima tuwe tuna maswali. Mama amefungua fursa, wawekezaji ni wengi, Serikali iweke mchakato vizuri, wawekezaji wengi wapo, mchakato uwe wa wazi, usilete maswali ili tuhakikishe kwamba, rasilimali za Watanzania zinalindwa na taratibu na sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe zinafuatwa, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya upendeleo. Awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na kwa dedication na dhamira ya dhati aliyonayo kwenye masuala mazima ya TEHAMA. Tumeona mipango yake mizuri kwenye masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa kweli nimpongeze Mheshimiwa Rais na nimwambie tu kwamba anawatendea haki Watanzania. Takwimu zinatuonesha kwamba ikifika mwaka 2065 katika nchi zote za Afrika, Nchi za Afrika Mashariki ndizo zitakazoongoza kwa idadi kubwa ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, takwimu zinatuambia katika nchi nne za Afrika Mashariki ikifika mwaka 2065 idadi kubwa ya watu watakuwa ni vijana yaani tutakuwa tuna the most youthful population Afrika nzima. Takwimu zinatuambia ikifika mwaka 2065 tutakuwa tumekwenda mara tatu ya idadi ya watu ambayo tunayo sasa hivi. Yaani kwa mfano Kenya watatoka milioni 56 watafika milioni 115, Uganda watatoka milioni 48 watakwenda milioni 141, Rwanda watatoka milioni 11 watakwenda milioni 25 na sisi Watanzania tutatoka milioni 60 mpaka milioni 186. Sasa takwimu hizo zinatuambia katika idadi hii ya watu asilimia 62 watakuwa ni vijana kuanzia miaka 18 mpaka miaka 35. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna nyingine takwimu zinatuambia hawa ndio watakuwa walipakodi wetu wakubwa. Idadi hii ya watu katika umri huu ndio ambao watakuwa tegemezi la Taifa letu kwa miaka kadhaa ijayo. Sasa nasema haya kwa sababu kwanza ningependa niwapongeze vijana wenzangu katika Taifa hili, pamoja na changamoto za ajira, vijana wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kujiajiri kwa shughuli ndogo ndogo. Kwa kweli niwapongeze sana, pamoja na changamoto mbalimbali za miundombinu, lakini vijana wa Taifa hili hawajaacha kupambana kwenye kujiajiri ili kusaidia shughuli za maendeleo ya Taifa lao. Niwatie shime vijana wenzangu na niwaambie waendelee katika kutafuta mbadala wa ajira bila kuchoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijana hawa wanajitahidi sana, ningependa nimwombe Mheshimiwa Waziri awafute jasho vijana. Awafute jasho vijana kwenye kuwasaidia kutengeneza faida kwenye shughuli za kimaendeleo wanazozifanya, kwa kuondoa vikwazo vidogo vidogo vya kibiashara ambavyo vinawarudisha nyuma. Wote tunafahamu katika vitu ambavyo vitasaidia kuondoa changamoto ya ajira katika Taifa hili ni teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna applications ndogo ndogo zinatumika ambavyo zimeajiri mamia ya vijana, wote tunaifahamu taxify pamoja na changamoto zake imewaondoa vijana mtaani imeajiri Malaki ya vijana, wanapata ajira ndogo ndogo. Kwa hiyo, tunafahamu kumbe application moja ikiajiri vijana karibu laki moja, tukiweka mazingira wenzeshi ina maana vijana wengi sana wataajirika kwenye hiyo, lakini sasa changamoto ni moja. Kama applications hizi zinaleta ajira tunajiuliza kwa nini vijana wengi sasa hawaleti ubunifu ili application hizi ziajiri wengine? Bunifu wanazo, tatizo ni uwezeshaji wa kimiundombinu, hawana fedha za kusimamisha biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mikopo tunayotoa leo tunataka vijana wetu waende wakajenge matofali, wakafanye ujenzi, wasage unga, haiwezekani ajira hizi haziwezi kuajiri vijana wengi kwa wakati mmoja. Kuna tatizo gani la hatimiliki za application za vijana kutumika kama dhamana ya mikopo yao? Kwa sababu ni vitu ambavyo ndio vinawaletea fedha. Duniani kote intellectual property inatumika kama dhamana kwenye mikopo, lakini hii mikopo yetu ya halmashauri nani ametuwekea uzio tusiwape vijana wabunifu mikopo ili iweze kuwasaidia? Kwa hiyo, nadhani tuanze kufikiria tofauti, sio lazima tu tufanye kazi hizi physical katika kuwapa vijana mikopo, tufikirie na hawa vijana ambao bunifu zao zitaajiri vijana wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka pia nishauri jambo moja, nimeliongea hapa Bungeni mara nyingi sana na nitaongea kwa masikitiko makubwa sana. Nilisema vijana wa Kitanzania wanapambana sana, lakini kuna mifumo ambayo ipo kwenye mikono ya Mheshimiwa Waziri, kanuni Mheshimiwa Waziri ndiye mwenye mamlaka nazo, suala la PayPal itatuingizia kodi, PayPal itaongeza fedha kwenye Serikali yetu, sasa kigugumizi kiko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilivyofuatilia kuhusu PayPal nikaambiwa kwamba, PayPal wenyewe wanasema hawana soko Tanzania. Jamani, Tanzania ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya watu Afrika Mashariki, soko lipo Tanzania, tatizo jirani yetu ni janjajanja sana, ndio maana anataka fedha zetu zipitie kwake. Sasa wataalam wetu wasipoenda hatua mbele zaidi kugundua vikwazo kama hivi vya majirani zetu ambao wanatufinya ili vijana wetu wasiweze kupata fursa kama hizi, inakuwa ni shida. Ndio maana leo hapa tunawalaani kwa kuingilia kwenye masuala yetu kama ya Loliondo.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri suala la PayPal, Tanzania is the biggest market, kwa hiyo, tusipoenda hatua mbele kujua kwamba, jirani yetu anatuwekea janjajanja ili fedha zetu tuzipitishe kwake, vijana wetu wataendelea kutaabika kwa kiasi kikubwa mno kwa sababu, kama kweli hamna biashara kwa nini wanaruhusu tuwalipe kupitia application yao? Kwa nini wao hawaruhusu sisi tusilipe kupitia application yao? Yaani tunalipa, lakini hatuwezi kulipwa, hatuwatendei haki vijana wa Kitanzania. Naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu, suala hili lina miaka 10 nyuma, hatuwezi kukaa hapa kila Bunge tukazungumza masuala ya PayPal. Mheshimiwa Spika alilitolea maelekezo mwaka jana, nilitegemea mpaka kufikia kipindi hiki tutakuwa tumepiga hatua kwenye masuala ya mustakabali wa vijana wa Taifa hili, wanaohangaika kutafuta ajira na kujiajiri. Hatuwezi kukubali wakwamishwe na vikwazo vidogo vidogo ambavyo vikitatuliwa vitaleta nafuu kwa wao pamoja na Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye suala la PayPal naomba alitafutie muarobaini kwa sababu, kama kuongea tumeshaongea sana. Labda sasa watuambie tufanye nini? Sisi kama vijana hatuwezi ku-match kwenda kwenye Makao Makuu ya PayPal kwa sababu, uwezo hatuna. Tunaamini Serikali yetu kama inataka kodi itatuwekea mazingira wezeshi ya kutusaidia ili tuweze kufanya biashara na tuweze kupata malipo ya kulipa kodi. Kama suala ni wao kuja kuweka physical presence in Tanzania wanaweza wakashirikiana na makampuni mengine kwa ajili ya kuwa wawakilishi wao hapa nchini kwetu Tanzania. Pia kama suala ni kodi, Serikali inaweza ikapata kodi kupitia mwakilishi ambaye ni kampuni. Kwa hiyo, kwa kweli kwenye suala la PayPal naomba Mheshimiwa Waziri alivalie njuga. Sisi tunalipa hatulipwi, hatuwezi kwenda kupitisha fedha kwa jirani. Naongea hili suala la PayPal l kwa uchungu kwa sababu tulishaliongea sana, Mheshimiwa Waziri naomba atusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye suala lingine la masuala ya ubunifu. Vijana wa Kitanzania hawajaanza kubuni magari leo, wameanza kubuni magari siku nyingi sana, lakini tujiulize kwa nini haviendelei? Hata hivyo, juzi alitokea mbunifu mmoja akabuni watu wote wakaenda kwake. Ni vizuri, lakini tumesahau vijana wa Taifa hili wameanza bunifu siku nyingi mno, lakini kuna vikwazo vya kibiashara na vikwazo vinaanzia TRA. Tunataka tu-recognize vitu tu ambavyo vinatoka nje ya nchi, yaani mpaka uthibitishwe kwamba, bidhaa yako uliyobuni inafaa kwa matumizi ya Watanzania, unasota ile mbaya. Sasa hawa vijana ambao wanabuni tunawarudisha hatua 10 nyuma, yaani mifumo nyetu yenyewe inatambua vitu vya wenzetu kuliko vitu vyetu sisi wenyewe. Naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri. Kama kweli tunataka mabadiliko kwenye masuala ya sayansi na teknolojia, lazima tuanze kwenye kubadili mifumo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimalize na jambo la mwisho kuhusiana na uwezeshwaji wa vijana. Wote tunafahamu maendeleo makubwa kwenye nchi mbalimbali yameletwa na viongozi ambao ni vijana, ikiwemo sisi hapa Tanzania; Uhuru wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliupambania akiwa na umri wa kijana. Kwa hiyo, nasema hivyo kwa maana moja, naunga mkono kwamba, yatupasa tuwe na vijana ambao wametayarishwa kwa ajili ya kushika nafasi za kimaamuzi, lakini haimaanishi vijana wa Taifa hili hawawezi kushika nyadhifa za uongozi katika Taifa hili, vijana wanaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa nishauri kwenye hili suala zima la nafasi za teuzi, pale ambapo wanashushwa nafasi. Huyu mtu kama alikuwepo Serikalini, ana nafasi yake ya mwisho, kuna nafasi ya mwisho ya juu kabisa kwenye rank husika. Kwa mfano, kama ulikuwa lawyer, nafasi ya mwisho kabisa pale juu kwenye lawyer basi arudishwe pale juu, lakini sio nafasi zote za teuzi ni kwa ajili ya watu ambao wako Serikalini peke yake, kuna watu wa sekta binafsi. Kwa hiyo, leo hii tukisema vijana wasipewe nafasi kisa tu hawakufanya kazi Serikalini, hatutendi haki na vilevile ikifika 2065 population kubwa ni vijana whether tunataka ama hatutaki, lazima tuwa-groom waweze kuja kuwa viongozi wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie vijana wanafaa kuwa viongozi wa Taifa hili, let’s groom them, tuwatayarishe kuja kushika nafasi za kimaamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote naomba kuanza kwa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya na uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye Wizara yetu kupitia sekta ndogo tunazozisimamia za umeme, mafuta na gesi.
Mheshimiwa Spika, pili, napenda kumpongeza Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Mashaka Biteko, kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, tatu, napenda kukupongeza Mheshimiwa Spika, pamoja na Kamati kwa kazi nzuri ambazo mmefanya ya kuhakikisha kwamba mnatupa maelekezo na kutusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nne, napenda kumpongeza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuangazia masuala yanayofanywa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kwa pongezi, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuonesha uzalendo kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo napenda sasa nitolee ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumzia. Moja, kuhusiana na kampuni tanzu ya shirika letu la petroli, TPDC (TANOIL). Kampuni hii pamoja na historia ya huko nyuma, ilianza biashara mwaka 2021. Pamoja na majukumu ambayo wamepewa, kampuni ya TANOIL ilipewa jukumu la kununua mafuta lakini vile vile kuuza mafuta kwa wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wa rejareja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mafuta kwa Taifa letu ni uchumi. Kwa hiyo, kama Serikali isingewezekana kuwachia wafanyabiashara binafsi watawale soko kwa asilimia 100. Ninyi mnafahamu, Watanzania hawa ni watu masikini. Takribani Watanzania milioni 26 wanaishi chini wa mstari wa umasikini. Kwa hiyo, isingewezekana kwa Serikali makini kuachia soko la mafuta, soko ambalo linabeba uchumi wa Taifa hili liweze kutawaliwa na sekta binafsi peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo lazima kama Serikali tuhakikishe tuna sehemu kwenye soko la mafuta ili kulinda hali za Watanzania.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Simama kwa ajili ya taarifa. Mheshimiwa Mohamed?
TAARIFA
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa Mzungumzaji. Hatukuanziasha shirika hili kufanya wizi. Tumeanzisha shirika hili kuja kufanya biashara. Mpaka sasa hivi shirika hili lina hasara kubwa. Huyo anayezungumza atueleze, hii ripoti ya mkaguzi ni sawa ama si sawa? Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, siipokei na nadhani nikimaliza kuongea Waheshimiwa Wabunge watakuwa wamenielewa, kwa sababu ndiyo kwanza nipo kwenye introduction. Subiri kidogo Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu kama nilivyosema mafuta ni uchumi. Kwa kweli, adhma yetu kama Serikali ni kuhakikisha tuna sehemu kwenye soko la mafuta ili tuendelee kulinda hali za Watanzania. Ninyi mnafahamu, mwezi wa saba tulipata dhoruba ya kukosekana kwa mafuta katika Taifa letu. Wafanyabishara binafsi walikataa kuwauzia wafanyabiashara wa rejareja mafuta. Walileta mafuta kwa ajili ya kampuni zao. TANOIL ndiye aliyeagiza mafuta na kuweka mafuta kwa wafanyabiashara wa rejareja ambao wanawauzia mafuta watumiaji wa mafuta kwa asilimia 70. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, … (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mheshimiwa Judith Kapinga, kuna taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, Mheshimiwa Mtemvu.
TAARIFA
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, anavyoendelea kuzungumza anatuchanganya kidogo. Underpriced ambayo imefanywa na management ya TANOIL kwa shilingi 70, imesababisha economic wealth ya shilingi bilioni 53. Yaani wasingefanya kushusha hivyo, tungeweza kuokoa shilingi bilioni 53. Pia, kwa sababu unasema sababu ni market…
SPIKA: Mheshimiwa, taarifa ni moja.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, sababu ni moja hiyo hiyo, kwamba ni market penetration ndiyo maana wakawauzia wafanyabiashara wadogo. Ukweli ni kwamba, aliyeuziwa ni mmoja tu. Kituo cha mafuta kimoja tu. Hivyo ndivyo tulivyoambiwa na CAG. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, taarifa hii siipokei na kwenye ukweli lazima tutasema ukweli juu ya umuhimu wa TANOIL. Ninapoelekea mbele nitasema changamoto na hatua ambazo kama Serikali tumechukua. Pamoja na kazi ambayo TANOIL imefanya, zipo changamoto ambazo zimejitokoza. Wote tumeona, watumishi wasio waaminifu na wafanyabiashara wasio waminifu waliunda mtandao kwa ajili ya kuhujumu masuala yanayofanyika na TANOIL. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tunavyoongea, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutuongoza, alishaanza kuchukua hatua. Kwa upande wa watumishi, pamoja na watumishi wale kukaa kando, jana Mheshimiwa Waziri wa Nishati ameshapokea taarifa kutoka kwa TAKUKURU ya kwamba, wameshakamilisha uchunguzi na watumishi wale watapelekwa Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, sisi tumechukua taratibu za ndani.
MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu hawa ni watumishi, kwa taratibu na sheria ambazo tulizitunga sisi wenyewe, tumeshaanza utaratibu wa ndani ili kuhakikisha watumishi hao kwa kufata sheria, tunawaondoka kwenye utumishi. Wakiwa wanaenda Mahakamani, waende kushtakiwa wakiwa raia wa kawaida. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Condester Sichalwe.
TAARIFA
MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC. Taarifa tuliyowasilisha hapa, ni ambayo sisi Kamati tumejadili tukiwa na CAG mwenyewe na tukiwa tumewaita hao watu wa TANOIL. Anachotueleza Mheshimiwa Naibu Waziri, kinakinzana na kile ambacho kwenye majadiliano yetu tumejadiliana na CAG na tumewahoji wale watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tunataka kujua, tuitishe Hansard zije hapa kwa sababu Kamati yetu ni Oversight Committee. Tunazo taarifa ambazo tumewahoji wale watu mbele ya CAG, wakatujibu na hiki ambacho anatujibu kinakinzana. Tushike kipi? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, sipokei kwa sababu nimeongelea masuala kadhaa… (Kicheko)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hakuna taarifa juu ya taarifa. Mheshimiwa Judith Kapinga.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ameongezea masuala kadhaa, sasa sijajua mahsusi alikuwa anazungumzia eneo gani. Tumechukua hatua kama ambazo nimezisema lakini vile vile kuendelea mbele, suala hili lina sehemu mbili. Lina suala la watumishi na lina suala la wafanyabiashara. Wafanya biashara wale kwa mtandao wao, ndiyo ambao wamekubali kuchukua discount nje ya utaratibu. Vilevile, wamekuwa na madeni makubwa ambayo wamegoma kuyalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, kupitia Bunge lako Tukufu naomba niwataarifu…
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI:….kwamba kama ni mtumishi kama ni mfanya bishara anayehusika, wote hawako salama na tutachukua hatua kwa pande zote mbili. (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mwakasaka, nadhani ameshapewa taarifa tatu. Ameshapewa taarifa na Wabunge watatu tayari. Mseshimiwa Judith Kapinga.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, hatutaishia kwa watumishi kama nilivyosema. Mfanyabishara yeyote ambaye anafahamu amenufaika kwa discount ambaye anafahamu amechukua mafuta bila kulipa, tutachukua hatua. Kwa kumalizia, nafahamu baada ya leo hii simu zitakuwa nyingi. Message zitakuwa nyingi, vi-note vitakuwa vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie hatutaangalia. Msumeno ambao umewakata watumishi, ndiyo msumeo ambao utaenda kuwakata wafanya biashara bila kuangalia ni nani. Baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini. Kwa nini Mkoa wa Ruvuma unaongoza ni kwa sababu tuliwaambia Wanaruvuma nendeni mkalime muongeze chakula katika nchi hii na walitumia jembe la mkono na mbinu duni za kilimo na mpaka mwaka jana wakaongeza tani 50,628 za mahindi kwa ajili ya akiba ya chakula cha nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tuliwaambia Wanaruvuma nyie ni kati kati ya mikoa mnayozalisha mazao ya chakula kwa wingi katika nchi hii. Mwaka jana waliongeza ziada ya chakula tani 877,048 kwa kuwa mahitaji ya chakula ya kimkoa yalikuwa tani 469,172 na wao Wanaruvuma kwa mikono yao walizalisha tani 1,346,220.
Mheshimiwa Spika, leo hii baada ya kuwapetipeti sana wazalishe mazao ya chakula kwa ajili ya akiba ya nchi hii, tumewasahau. Tumesahau jasho walilolitoa kwa dhati ya mioyo yao kulima, tumesahau nguvu waliotumia kwa mikono yao kulima na leo hii wanalala na mahindi yao ndani, wanahangaika na mahindi yao ndani, wanalia na mahindi yao ndani. Kwa takribani miaka mitatu hakuna soko la mahindi Wilayani Mbinga na Mkoani Ruvuma kwa ujumla huku tukijua Mkoa wa Ruvuma ndiyo unaozalisha kwa kiasi kikubwa mahindi na chakula cha nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa uchungu sana kwa sababu wana Ruvuma wamekuwa disparate. Mwaka jana akatokea tajiri tapeli anayejulikana kwa jina la Njako akaenda pale Mbinga Kigonsera akachukua mahindi ya wakulima yenye thamani ya shilingi bilioni 5 na mpaka leo hii tunapozungumza tunaenda kwenye mzunguko mwingine wa kuuza mazao mpaka leo wakulima hawajapata fedha. Vilevile mpaka leo hawana soko ambalo wataenda kuuza mahindi yao.
Mheshimiwa Spika, wakati haya yote yanafanyika NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana walikuwepo na hawajawahi kununua hata debe moja la mahindi Wilayani Mbinga. NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana, wameweka vituo kwenye miji wamegeuka ma-God father, wanasubiri mkulima atembee kilomita 60, 100, 200 aende kuwapelekea gunia zake 10 za mahindi. Mkulima huyu ataweza vipi kwa sababu mpaka aende kilometa 100 gharama zote za uzalishaji zimeisha pale. NFRA watuambie kama wao wamegeuka ma-God father sisi tunataka usuluhisho wa masoko ya wakulima kwenye nchi hii ikiwemo Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wamelima kweli kweli mahindi mwaka huu, wananchi wa Mbinga wamelima mahindi kweli kweli, kuna kizungumkuti mwaka huu wanaenda kuuza wapi? Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri leo hapa nitamkamatia shilingi yake. Mwaka jana tumetapeliwa, fedha zetu hazijarudishwa mwaka huu bila kutuambia tunaenda wapi kuuza mahindi yetu tunakamata shilingi yake hapa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nakupa taarifa kabisa uje na majibu yanayoeleweka kwa wananchi wa Ruvuma na Mbinga kwamba mahindi yetu tunayapeleka wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais anazunguka nchi jirani kwenda kuongea na majirani zetu kuweza kujua mahindi yetu tunayauza wapi? Kinachotusikitisha wataalamu wetu wamekaa wanamshangaa Mheshimiwa Rais, yaani Mheshimiwa Rais kashatafuta masoko wanategemea mkulima atabeba gunia zake 10 aende akauze mahindi yake Malawi au Msumbiji, wataalamu wetu mnatuangusha. Haiwezekani mpaka tuje hapa tulalamike ndipo mtafute suluhu ya matatizo yetu, mlipaswa kuyaona mapema kabisa kwa sababu msimu wa mahindi sasa ndiyo umeanza. Sasa ndiyo tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie tunaenda kuuza wapi sisi mahindi yetu wananchi wa Ruvuma kwa sababu tumechoka na kutapeliwa na kwa muda mrefu sasa tunahangaika huku na huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasemaje kuhusiana suala la kilimo. Inasema: “Chama cha Mapinduzi kinatambua kwamba mageuzi ya kujenga uchumi wa viwanda ni lazima yaendane na mageuzi ya kuongeza tija kwenye kilimo”. Namkumbusha Mheshimiwa Waziri Ilani ya Chama chetu inasema nini kwenye masuala ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini naomba nimalizie kwa kumnukuu Mwalimu Nyerere alisema kama ifuatavyo: “Tarmac roads, too, are mostly found in towns and are of especial value to the motor-car owners. Yet if we have built those roads with loans, it is again the farmer who produces the goods which will pay for them”. Tutawalinda wakulima wa nchi hii Mheshimiwa Waziri tunaomba majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kuja na mkataba huu, kwa kuwa naamini kwamba mkataba huu una manufaa makubwa sana kwa nchi yetu ya Tanzania na nchi nyingine za Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba uanzishwaji wa maeneo huru ya biashara siyo jambo jipya duniani, ni jambo ambalo limeanza miaka mingi nyuma tangu miaka ya 1950; na mfano mzuri ni European Economic Community ambayo ilianza mwaka 1957 na baadaye kubadilishwa jina pale ambapo European Union iliundwa mwaka 1993. Kwa hiyo, inawezekana kwa sisi kama Bara la Afrika tumechelewa kutokana na changamoto mbalimbali na kuja na mkataba huu 2019 kwa sababu ni wazi kabisa sisi kama Afrika tumekuwa wahanga wa masuala ya ukoloni. Kwa hiyo, inawezekana tulichelewa kama Bara. hata hivyo, changamoto tulizonazo na ambazo tulikuwa nazo kama bara haziwezi kutunyima fursa ya sisi kama waafrika kuja na mbinu mbalimbali za kutuinua kiuchumi ikiwemo kuwa na soko huru la biashara kuelekea kutimiza malengo yetu ya ajenda 2063. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kwamba mojawapo ya hasara au changamoto ambazo tunaweza kuzipata kutokana na kuridhia mkataba huu ambao tumeelezwa na Serikali, moja ni kupungua kwa mapato ya kodi yanayotokana na ushuru wa forodha kwa bidhaa ambazo zitaondolewa kodi kwa takriban shilingi bilioni 41 ndani ya miaka 10, yaani wastani wa shilingi bilioni 4.1 kwa mwaka. Pia mojawapo ya changamoto nyingine ambazo tumeambiwa ni uwezekano wa kupoteza ajira kwa baadhi ya sekta hususan sekta za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachelea kusema kwamba changamoto hizi zinafikirisha ukilinganisha kwamba sisi kama Taifa bado tuna changamoto ya ajira, lakini niseme kwamba kuna baadhi ya masuala ambayo kama Taifa tukifanyia kazi, changamoto hizi ambazo tunaweza tukazipata kutokana na kuridhia mkataba huu, tunaweza tukazipunguza kwa kiasi kikubwa sana na njia mojawapo ni kuendelea kujenga uchumi shindani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi shindani una variables mbalimbali, lakini sisi kama taifa tukiendelea kujijenga tunaweza tukapunguza changamoto hizi kwa sababu tayari tuliishaanza. Mojawapo ya masuala ambayo tunaweza tukayajenga ili kuweza kuongeza uchumi shindani mojawapo ni kuendelea kuwa na miundombinu imara na wezeshi lakini vilevile kuendelea kuwa na taasisi imara, kuendelea kuwa na elimu ya juu inayotoa vijana ama watu ambao wanaweza kupambana kwenye soko la ajira la biashara, kuenzi mabadiliko ya teknolojia, kuenzi mabadiliko ya ubunifu na kuwa na masoko yenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini iwapo kama Taifa tutafanyia kazi masuala haya na kuwa na uchumi shindani, tunaweza tuka-penetrate kwenye masoko na vilevile athari ambazo tumeambiwa tunaweza tukawa nazo kama Taifa, tunaweza tukazipunguza ikiwemo suala la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia ripoti ya takwimu za biashara za benki yetu kuu kwenye kanda za kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine za jirani kwa mfano tukianzia biashara za bidhaa kati ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania tumekuwa tukifanya vizuri. Kwa mfano ukiangalia takwimu za miaka saba nyuma yaani kuanzia 2013 mpaka 2020 kwenye kuuza bidhaa tumekuwa tukifanya vizuri kwa sababu tumekuwa tukipanda, tulianza mwaka 2013 na US dola milioni 419, lakini mwaka jana 2020 tumeweza kupanda mpaka US dola milioni 812.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye kuuza bidhaa tumeweza ku- contained soko letu na kulinda soko letu kwa sababu tulianza na US dola milioni 394, lakini kwa mwaka jana tumeweza ku-contained na kushuka mpaka dola milioni 324. Kwa hiyo, inaonyesha kabisa sisi kama Watanzania tunafursa kwenye soko hili kwa sababu bidhaa zetu kwa uuzaji wa nje tumekuwa tukifanya vizuri sana na tumeweza kulinda soko letu la ndani kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye masuala ya ajira, ukweli ni kwamba ukipunguza kodi kwenye bidhaa unafanya makampuni yaweze kuzalisha zaidi, lakini generally hii ina-apply kote, ina-apply tu kwenye nchi ambazo gharama zao za maisha ni ndogo, ya kwamba kama gharama za maisha husika ni ndogo inamaana bidhaa zao zinaweza zika- penetrate kwenye masoko ya nchi nyingine kuliko nchi ambazo gharama za maisha ni kubwa mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukachukulia mfano, wamarekani wakati wamejiunga na mkataba wa North America na free trade area, wamarekani viwanda vyao vingi sana vilikosa ajira kwa sababu Mexico ilikuwa na gharama za chini ndogo kuliko Marekani, lakini sisi kama Tanzania cost of living inakuwa approximated kwa dola 0.32. ina maana tunafanya vizuri kuliko nchi nyingine za Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukauza zaidi ni kuimarisha tu baadhi ya masuala ya kiuchumi ili tuweze kushindana zaidi na kufanya vizuri katika soko. Na hapa sasa inabidi tufanyie masuala ambayo ni ya msingi sana ikiwemo kujiongeza kiji-digital, yaani huduma ambazo zinatolewa kiji-digital sasa tunafanya kazi kwa uharaka na ziweze kuwa reliable. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumzia suala la taasisi imara liweze kutuvusha lazima taasisi zetu ziweze kubadilika.
NAIBU SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa kengele imeshangongwa.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa mfano taasisi za kiserikali kama AFTC lazima zitoke kwenye kufanya kazi kwa mazoea ya finically na ziende kwenye biashara za mitandao kwenda kulinda walaji kwenye mitandao. Sasa hivi ukiwauliza hawana hata mkakati wa kulinda walaji kwenye mtandao ambapo biashara kubwa imeamia huko. kwa hiyo, mimi sina shaka kama Taifa tutafanya vizuri tukiendelea kufanya kazi tu kwa ajili ya variable sisi ambazo tukazifanyisha ukiwa na uchumi shindani basi tunaweza tukafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku njema ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo, naomba kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaofanyika katika Sekta ya Nishati. Hii imejionesha kupitia miradi ya kielelezo na miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kupitia sekta zetu ndogo za mafuta, gesi pamoja na umeme.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ni kielelezo cha uchapakazi na uzalendo wa kweli. Tunaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu amwezeshe kutekeleza majukumu yake siku zote kwa heri na baraka tele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba kumshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kuendelea kutusimamia na kutuongoza vyema katika sekta yetu ya nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu mkubwa naomba kumshukuru sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wangu wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mshaka Biteko kwa kuendelea kutuongoza vyema. Amekuwa kiongozi mwema sana kwangu na watumishi wengine wote katika Wizara ya Nishati na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati. Amekuwa kiongozi anayetusimamia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yetu kwa azma na neema. Tunamwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumjalia aweze kutumikia majukumu yake kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukushukuru wewe, Naibu Spika pamoja na Katibu wa Bunge kwa kuendelea kutuongoza vizuri hapa Bungeni. Kipekee naomba niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili Tukufu kwa kuendelea kutuunga mkono. Tunathamini sana maoni yenu ambayo mnatupatia na ushirikiano mkubwa mnaotupatia katika kutekeleza majukumu yaliyo katika Wizara yetu ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nilishukuru Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ambao wao ndiyo walinipa dhamana ya Ubunge wa Vijana kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi. Baraza hili linaongozwa na kaka yangu Comrade Kawaida Mohammed Kawaida. Namshukuru sana yeye, Mwenyekiti wetu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Wajumbe wote wa Baraza kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Ubunge wa Vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvama. Ninapoelekea mwisho wa shukrani zangu, kwa kuwa mimi ni Diwani wa Halmashauri ya Mbinga Vijijini, naomba niwashukuru wananchi wa Wilaya ya Mbinga kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Naomba niwaahidi kwamba nitaendelea kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyomaliza shukurani zangu, naomba nimshukuru sana mume wangu na familia yangu kwa kuendelea kunivumilia na upendo mkubwa wanaonipatia. Nathamini sana, nami ninawapenda na kuwathamini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukurani hizo, naomba nijielekeze sasa kwenye kuchangia hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na nishati safi ya kupikia, nitasema kidogo kwa sababu Profesa ameeleza vizuri sana. Uhai na afya ya dunia yetu ya sasa ipo kwenye kutunza mazingiara yetu. Linapokuja suala la nishati safi ya kupikia, hii ndiyo nyenzo muhimu ya kutusaidia kutunza mazingira yetu kwa ajili ya afya na dunia ambayo tunaishi.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, ule Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambao tulikuwa tunaungoja, umeshapitishwa na Baraza la Mawaziri na upo tayari kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Nitakuwa mnyimi wa fadhila nisipomshukuru Mheshimiwa Rais ambaye ndiye amekuwa kinara wa nishati safi ya kupikia na ametusaidia sana kwa kuwa champion namba moja Tanzania, Afrika na ulimwenguni kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, azma yetu ni kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, lakini kubwa, pamoja na kuongeza kasi, tunataka tuwawezeshe wananchi waweze kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi ili tuweze kabisa kuondoa matumizi ya mkaa pamoja na kuni. Dhumuni la mkakati wetu ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati safi, salama, endelevu na yenye uhakika.
Mheshimiwa Spika, ninafahamu bado tuna hatua kubwa sana katika kuhakikisha tunaondoa kabisa matumizi ya mkaa, lakini ni suala ambalo hatuwezi sisi Serikali kulifanya peke yetu. Ndiyo maana tunaendelea kuomba Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kushirikiana katika kupiga vita matumizi ya mkaa na kuni ili kuhamasisha wananchi waendelee kwenda na matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ambavyo tumeanza kupitia mitungi ambayo tunaigawa.
Mheshimiwa Spika, mikakati ambayo tunayo inatekelezeka sana. Jambo ambalo linatutesa sisi ni mazoea tu ya mkaa kwa sababu wapo wengi ambao wana uwezo wa kutumia nishati ya gesi. Ni kwamba tu watu hawaamini kuwa wali nazi wa gesi pia ni mtamu au maharage ya kutumia pressure cooker ambayo inatumia umeme mdogo pia ni mtamu. Ni kuongeza tu mapishi. Kwa hiyo, tuendelee kushirikiana kwa pamoja kutoa elimu tuweze kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na gharama. Tayari tumeshaanza kufanyia kazi kupitia REA na wadau wetu wengine tunatoa ruzuku. Jambo kubwa lilikuwa ni kwenye kuanza matumizi ya gesi kwenye kupata jiko na vifaa, lakini kupitia REA tunatoa ruzuku ya mitungi na mpaka sasa hivi tumetoa mitungi 83,500 na tunao mkakati wa kutoa mitungi 450,000 ili kuweza kurahisisha matumizi ya awali ya gesi ili kuongeza kasi ya matumizi makubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, kwa kushirikiana na kampuni za gesi, tuna mpango wa kuongeza miundombinu ya kupokelea gesi pale bandarini kutoka tani 5,000 ambazo tunazo sasa hivi mpaka tani 45,000. Mikakati hiyo tunayo kwa sababu tunaamini tukifanya hivyo, basi tutakuwa tumepunguza bei. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na kuwa na mitungi ya kilo chache. Tayari kampuni zimeshaanza kufanyia kazi. Zipo kampuni ambazo zimeshaingiza sokoni mitungi ya kilo tatu. Tunaendelea kuzisihi kampuni nyingine waende na njia hiyo hiyo ili kuwarahisishia wananchi waweze kupata mitungi hii kwa gharama ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ameshafanya kikao na wadau wa LPG ili kuhakikisha tunakuwa na mawakala wengi zaidi hata kwenye maeneo ambayo yako mbali. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hoja zenu zote tumezichukua na majibu yake tunayo na tunazifanyia kazi kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye suala la CNG. Waheshimiwa Wabunge tumewasikia kuhusiana na umuhimu wa kuongeza vituo vya kujazia gesi, lakini vilevile vituo vya kubadilisha mifumo ya magari ili yaweze kutumia gesi. Waheshimiwa Wabunge, maoni yenu tumesikia na vilevile ni kweli kabisa kwenye Kituo cha Ubungo foleni ni kubwa, lakini mikakati ya muda mfupi tunayo.
Mheshimiwa Spika, kupitia TPDC tayari tumeanza ujenzi wa kituo mama pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile tuna ujenzi wa vituo vingine viwili ambavyo vinaendelea na ujenzi katika eneo la Kairuki pamoja na Muhimbili. Kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, tunaenda kufanya ujenzi wa vituo vingine 20. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, kwa kipindi cha muda huu mfupi tunayo mikakati ya kuhakikisha tunamaliza foleni na kurahisishia wananchi upatikanaji wa gesi kwenye magari yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la vitongoji, ili leo tuweze kufikia hapa kwenye kudai vitongoji ilikuwa ni lazima tuanzie sehemu na tuliweza kuanza kwenye kupeleka miundombinu vijijini. Kwa kuwa tayari tumeshafika huko, vitongoji vyote ambavyo vimebaki tutaenda kuvifikishia umeme.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunao mkakati wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000 na tunapeleka kwa awamu. Tutaanza na vile vya kila jimbo 3,060 ambapo tupo kwenye hatua za mwisho za manunuzi.
Mheshimiwa Spika, pia kwa mwaka huu wa fedha tunao mkakati wa kupeleka tena kwenye vitongoji 4,000. Kwa hiyo, mkakati wetu wa kupeleka kwenye vitongoji 20,000 ndiyo tunauanza Waheshimiwa Wabunge. Nawahakikishia kama ambavyo tunamaliza vijiji awamu kwa awamu, pia tutaenda kumaliza vitongoji.
Mheshimiwa Spika, ninapoenda kumalizia kuhusiana na wakandarasi ambao hawatekelezi majukumu yao vizuri. Waheshimiwa Wabunge tumewasikia na hususani mkandarasi wa Rukwa. Tuendelee kuwahimiza wakandarasi ambao tumewaamini katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi wafanye miradi hii kwa weledi mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tulishatoa maelekezo kwamba wakandarasi wote ambao hawafanyi kazi zao kwa weledi hatutaenda kuwapatia kazi chini ya taasisi ambazo zipo katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, kuhusiana na suala la huduma kwa wateja, kulikuwa na malalamiko kwamba simu hazipokelewi. Ni kweli, kipindi tuna mgao wa umeme tulikuwa tunapokea mpaka simu 40,000 kwa siku, lakini kutokana na kufanyia kazi changamoto hizi za umeme na umeme kupatikana, simu zimepungua kutoka kati ya 20,000 mpaka 17,000 kwa siku na uwezo wa kituo chetu ni simu kwa 87%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alitolea maelekezo ya namna ambavyo tutaweza kuwafikia wateja zaidi na tumefanyia kazi. Moja, tumerudisha huduma za simu kwenye kila mkoa. Kwa hiyo, kila mkoa wananchi wanaweza wakapiga simu kule. Pili, tumeboresha mawasiliano ya teknolojia kwa kuja na mbinu za kisasa. Tuna chatbot ambapo mtu kupitia WhatsApp anaweza akasema shida yake na akachati na akapata suluhisho la tatizo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, kuhusiana na toll-free, kwa kushirikiana na TCRA, tayari tumeshapata namba ambayo ni ya bure ambayo ni 180 na tupo kwenye mchakato wa mwisho wa kuhakikisha tunaanza kutumia namba ili wananchi waweze kupiga simu bure. Kwa hiyo, kwenye suala la huduma kwa wateja Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alilitolea maelekezo na vilevile tumelifanyia kazi kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, kipekee naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri wenu na michango yenu. Yawezekana tusiwe tunaweza kuyajibu yote kwa mmoja mmoja, lakini nataka niwahakikishie, michango yenu tunaithamini sana sana na yale ambayo yanatekelezeka tutahakikisha yanafanyiwa kazi kwa mustakabali wa Taifa letu na sekta yetu ya nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, awali ya yote ningependa niipongeze Kamati hii, ni mojawapo ya Kamati ambayo inafanya kazi kubwa sana kupitia sheria ndogo nyingi sana. (Makofi)
Kwa hiyo, kwa kweli nimpongeze Mwenyekiti na Kamati nzima kwa kazi kubwa sana ambayo wanaifanya. Inawezekana Kamati hii ikadogoshwa kwa maana inaitwa Sheria Ndogo, lakini niseme ni Kamati ambayo inagusa maisha ya Watanzania kwa kupitia Kanuni na miongozo mingi sana na kuirekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa kuleta mabadiliko ya Kanuni mbalimbali ambazo zinasaidia utekelezaji wa sheria mama, lakini pamoja na kuipongeza Serikali ningependa niishauri Serikali, zipo sheria mama nyingi ambazo Kanuni zake zimepitwa na wakati; zipo pia sheria mama nyingi ambazo zinahitaji kutungiwa Kanuni ili ziweze kuendana na nyakati ambazo tunazo sasa hivi. Ningependa nitoe mfano na vilevile niishauri Serikali kwamba kuna Kanuni ambazo ni za umuhimu sana ambazo, tungeshukuru kama zingeletwa kwenye Bunge kupitia Kamati mapema sana ili Watanzania waweze kuneemeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano wa kanuni hizo ni kanuni zinazohusiana na mifumo ya malipo ya fedha kwa njia za mtandao. Kanuni na sheria zinazohusiana na mifumo ya malipo kwa njia ya mtandao zinahitaji, kufanyiwa marekebisho ili yaweze kuendana na teknolojia ambayo tunayo sasa hivi. Mpaka leo ukiangalia sheria na kanuni zetu zinataka makampuni ya nje yanayofanya biashara na wafanyabiashara wanaouza huduma na bidhaa, hapa Tanzania kwenda nje ya nchi kuweza kufanya huduma za malipo ya fedha wakiwa na leseni ya hapa Tanzania (National Payment License). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni jema kwa sababu Serikali inalinda mapato, lakini lina changamoto kwa sababu badala ya kulinda mapato tunapoteza mapato. Ningependa niseme kwamba hapa nchini kwetu kuna njia kuu za malipo kwa wafanyabiashara, wanaofanya biashara kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi. Njia kuu ambayo imezoeleka ni watu wa nje ya nchi kufanya transfer benki kupitia visa au mastercard, lakini kwa dunia ambayo tunayo leo watu wangependa kufanya transactions hizi wakiwa wana simu zao kiganjani. Vilevile ili uweze kufanya njia hizi za malipo yaani kama wewe ni mfanyabiashara wa Tanzania uweze kulipwa na mtu wa nje, kama sio kwa transfer za benki inabidi ulipwe kupitia application mbalimbali za fedha ambazo zinakusaidia uweze kupata malipo ya moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa application hizi kwa hapa Tanzania wafanyabiashara wengi hawawezi kuzitumia kwa sababu ili application uweze kutumia makampuni yenye application hizo lazima ziwe zina leseni ambazo zimetolewa hapa Tanzania. Sasa jambo hili ni gumu kwa sababu makampuni haya ni giant companies, wana-own teknolojia kubwa sana, ni mabilionea hawawezi kuja ku-establish hapa makampuni yao kwa urahisi.
Kwa hiyo, sasa kinachotokea wafanyabiashara wengi waliokuwepo hapa wanapata ugumu wa kulipwa fedha, kwa hiyo, sisi tumegeuka wanunuzi. Kwa mfano, mojawapo ya application ni Pay Pal, mimi naweza kumlipa mtu wa nje, kama nauza bidhaa na huduma lakini mtu wa nje hawezi kunilipa mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilipenda niliongelee hili ili Serikali sasa iweze kuona umuhimu wa kutunga/kubadilisha kanuni ili wafanyabiashara wa hapa ndani waweze kunufaika kwa namna moja ama nyingine. Unaweza ukadhani kwamba kwa sababu kanuni haziruhusu ama sheria haziruhusu basi wafanyabiashara hawa hawafanyi hizi biashara, kwa mfano PayPal watu wana account za PayPal, lakini wamezifungulia Kenya. Wanafungua na account za fedha Kenya, kwa hiyo, wanafanya malipo kupitia Kenya, kwa hiyo, fedha zinakwenda Kenya. Kwa hiyo, sasa mwisho wa siku sisi tunapoteza mapato na fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, badala ya ku-demand leseni kwa makampuni haya labda ni njia sahihi kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha ama BOT, kuweka kitengo maalum cha ku-scrutinize njia hizi za mifumo ya malipo ya kimtandao na kuweza kuishauri Serikali; ni njia gani kama Taifa na wafanyabiashara wanaweza kuchukua ili waweze kufanya biashara na Serikali itanufaika kupitia fedha za kigeni na itanufaika kupitia kodi ya ongezeko la thamani pale ambapo mfanyabiashara atatoa fedha kwenye application yake kwenda kwenye account zetu za hapa Tanzania. Kwa hiyo, vijana wa Taifa hili wanafanya ubunifu mbalimbali sana na siku hizi huduma za kiteknolojia wapo vijana wanauza online. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali kama shida ni sheria nimeambiwa shida ni sheria na hizi license watuletee Kamati tuweze kufanya mabadiliko ili Watanzania vijana waweze kuuza biashara zao kwa urahisi. Leo unamuuzia mtu atoke huko nje alipo aende benki afanye transfer badala ya kulipa moja kwa moja kwenye simu yake. Kwa hiyo, hatuwezi kupigana na teknolojia, washauri wetu na wataalam kwenye Wizara watusaidie kuweza kuwaza mbele kuliko kusubiri teknolojia itufuate. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja ambayo iko Mezani.
Mheshimiwa Spika, suala la elimu kwa nchi yoyote ama kwa jamii yoyote ndiyo mkombozi wa mtoto wa masikini yeyote katika taifa lolote. Elimu ndiyo imani ambayo mzazi anaweza kuiweka kwa mtoto wake, ndio urithi pekee ambao mzazi wa kimasikini wa Kitanzania anaweza kumpatia mtoto wake.
Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kuipongeza Serikali. Sasa hivi elimu msingi katika nchi yetu ni bure. Mtoto anaanza darasa la kwanza mpaka darasa la saba, anafuata form one mpaka form four, form five mpaka form six. Mazingira ni wezeshi kwa mtoto wa Kitanzania kuweza kupata elimu yake kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha sita. Kwa kweli napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa ambazo imefanya kwa ajili ya haya mazingira wezeshi.
Mheshimiwa Spika, elimu yetu ya Kitanzania mtoto yupo katika elimu kwa miaka takribani 16 hadi 17. Baada ya hapo mtoto huyu anategemewa kwenda elimu ya juu. Pale kwenye elimu ya juu kama atapata nafasi, au kama mkopo atapata ama asipopata, baada ya hapo anaenda mtaani. Tayari tuna-frustration kubwa ya changamoto ya ajira mtaani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba mtoto anakaa kwa takribani miaka 14 katika elimu, ile miaka mitatu ambayo inabidi amalizie, bado inakuwa kizungumkuti. Kwa hiyo tunakuwa tunavunja imani kwa watoto wetu kuweza kumalizia.
Mheshimiwa Spika, kwa Afrika Mashariki, ukitoa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo imejiunga sasa hivi, Tanzania ni mojawapo ya nchi ambayo ina-population kubwa ya watu. Ukilinganisha na nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, Tanzania iko hapo juu lakini kwa kipindi kirefu Tanzania siyo amabayo inaongoza kwa idadi ya wanafunzi ambao wanamaliza katika elimu ya juu. Inaongoza kwa idadi ya population lakini haiongozi kwa idadi ya wanafunzi ambao wanamaliza katika vyuo vikuu vyetu.
Mheshimiwa Spika, nchi zetu jirani kwa mfano, idadi ambazo zinamaliza ni laki moja mpaka laki na ishirini; nchi ambazo zina-population ndogo, lakini sisi idadi zetu ni sixty thousand, elfu hamsini, elfu arobaini na tano, hatuvuki hapo. Sababu ni nyingi lakini sababu mojawapo ni uwezeshaji wa wanafunzi kuweza kujiunga na elimu ya vyuo vikuu. Mikopo imekuwa changamoto kwa kipindi kirefu sana.
Mheshimiwa Spika, elimu ndiyo advantage ambayo tunaweza tukaitumia tukiwa tuna-population. Ukiwa na idadi kubwa ya watu walioelimika, ndipo hapo unaweza ku-explore opportunities nyingi kwa wananchi wa taifa lako. Sasa tukiwa tuna namna ambazo zinasababisha watoto kupata vizingiti vya kuendelea na elimu ya juu hapo kunakuwa kizungumkuti, na hapo ndipo ambapo tunajitahidi huku ngazi za chini tunakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao sasa wanakaa mtaani, wanakuwa frustrated, wanajiunga na wale ambao tayari wanachangamoto ya ajira, tunakuwa na taifa la vijana ambaao wako frustrated kwelikweli.
Mheshimiwa Spika, elimu kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki ya msingi kabisa. Kwa hiyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha fedha inapatikana kwa ajili ya wanafunzi kusoma, hususani masuala ya sayansi. Sayansi ndiyo ambayp inakomboa taifa lolote duniani kwa sasa masomo ya sayansi ndiyo msingi wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kwenye taifa lolote lile; na hapa ndipo ambapo vijana wengi wataweza kuajiriwa. Hatuwezi kutatua changamoto ya ajira taifa hili kwa kazi physical. Changamoto za ajira zinatatuliwa kwa uvumbuzi unaotokea kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia. Sasa tusipoweka mikopo watoto wakasoma kwenye masomo ya sayansi mpaka ngazi ya juu, sasa ubunifu tutatoa wapi?
Mheshimiwa Spika, ni lazima Serikali i-dedicate kwenye kuhakikisha fedha zinapatikana. Ukiangalia bajeti yetu ya Wizara ya Elimu 60% ni Bodi ya Mikopo. Hata hiyo Bodi ya Mikopo imewekwa kwenye list ya miradi ya maendeleo, lakini si mradi halisi wa maendeleo huu. Ilitakiwa iwe ina-vote yake tofauti, peke yake. Ndiyo maana ukiangalia Wizara ya Elimu unaona Bodi ya Mikopo inafedha kubwa lakini haina fedha kubwa. Imekaa kwenye bajeti ya Wizara, ilitakiwa iwe na vote peke yake. Ndiyo maana tukiona bajeti hapa tunaona bajeti ya Wizara ya Elimu ni Bodi ya Mikopo ina fedha kubwa lakini siyo fedha kubwa, ni 60% ya bajeti ya Wizara ya Elimu; lakini sio fedha kubwa. Tunashauri iwe na vote peke yake ili tuweze kui-monitor.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya ajira ni changamoto inayokumba nchi nyingi za Afrika na dunia kwa ujumla, tofauti pekee iliyopo kwa nchi ambazo tunakumbwa na changamoto ya ajira kwa vijana ni namna ama approaches tunazotumia kwenye kukabiliana na changamoto ya ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali kwa program mbalimbali zinazofanyika kwa vijana kwa ajili ya kutatua changamoto ya ajira ikiwemo program ya kukuza ujuzi kwa vijana ambayo mpaka sasa imewanufaisha vijana zaidi ya 5,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi ningependa nishauri masuala kadhaa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, program ya kukuza ujuzi ilitakiwa iongezwe na kuwa program ya kukuza ujuzi pamoja na mitaji. Nasema hivi kwa sababu ninaogopa kwamba tunapoelekea program hii ya ujuzi inaenda kuleta daraja lingine la wahitimu tofauti na wahitimu tulionao wa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, program hii kama nilivyosema imezalisha wahitimu zaidi ya elfu tano ambao hawana mitaji wapo mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti ya mhitimu wa program ya ujuzi na mhitimu wa Chuo Kikuu ni kwamba wa Chuo Kikuu anakuwa na ujuzi wa darasani huyu anakuwa na ujuzi wa stadi za kazi lakini wana-share kitu kimoja wote hawana ajira na hawana mitaji. Halmashauri zetu Tanzania nzima karibia 185 zinatoa takribani Shilingi Bilioni 28 kila mwaka kwa ajili ya mikopo ya vijana, program hii ya ujuzi imetengewa Bilioni Tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani haina tija program kutengewa Bilioni Tisa halafu iende kwenye mafunzo, mikutano, tathmini na masuala mengine ambayo hayaweki masuala ya mitaji kwa vijana halafu tumeweka Bilioni Moja ya mitaji kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, naona hapa hesabu hazijakaa sawa yaani Bilioni Tisa iishie kwenye mafunzo halafu Bilioni moja iende kwenye mitaji nadhani ilitakiwa iwe vice versa. Bilioni Moja ya mafunzo, Bilioni Tisa iwe ni mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ni muhimu lakini haiwezekani tukaweka Bilioni Tisa kwenye mafunzo halafu bilioni moja kwenye mitaji sisi kama vijana haturidhiki tuambiwe kwamba kuna vijana 5,000 wamepewa mafunzo na wako mtaani haiwezekani tunaomba Wizara itusaidie ili fedha hizi zinazotolewa ziweze kuwa na tija kwa vijana end result lazima iwe ajira ama mitaji kwa vijana lakini siyo kuongeza idadi ya wahitimu ambao wanaenda kukaa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatusaidia sana kuwekeza kwenye masuala ya ICT na kwa kweli nipongeze Serikali digital infrastructure imewekezwa kwa kiasi kikubwa, mfano ni National na Regional ICT broadband backbone ambayo imeweza kuwa connected kwenye three International undersea cables.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya uwekezaji kwenye ICT kwa maana ya kukuza matumizi ya teknolojia na tunategemea kwamba Wizara nyingine itaenda sambamba na utekelezaji wa mambo kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inayohusiana na masuala ya vijana ninadhani inabidi wawasaidie vijana kuwekeza katika program za ubunifu ili waweze kutumia hizi infrastructures ambazo zinatengenezwa na Serikali lakini leo hii startup programs tunawajima mikopo ya vijana. Sasa ninapenda niwaulize hivi tumeambiwa model ya kutoa mikopo ni ile tu ya kusaidia vijana ambao wanataka kufanya physical investment kama viwanda? tunapoelekea kweli tunahitaji kukumbushana kwamba sayansi na teknolojia ndiyo habari ya mjini? Kwa hiyo, Serikali inawekeza hii miundombinu ili tufanye nini sasa kama vijana hawawezi kupewa mikopo ili wawekeze kwenye startup programs?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini Serikali inaweka miundombinu ili vijana waweze kufanya program za ubunifu ambazo zitasaidia kutoa huduma lakini zitasaidia kuajiri wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, startup program ikiwa properly invested inaajiri zaidi ya vijana hata 100. Sasa kwanini hatuoni hili? Wataalam watusaidie! Haiwezekani tukawa tuna model moja ya kutoa mikopo ya vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wote ni sawa, wale wenye bunifu na ambao wanataka kufanya physical investments wote ni wa aina moja na wote ni vijana wa Tanzania. Wizara ipanue mawazo ku- accommodate vijana ambao they want kufanya startup programs.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunawaambia benki wawakopeshe, watawakopesha vipi kama sisi wenyewe tu tunashindwa kuwakopesha. Kwa hiyo tunaomba Serikali itusaidie vijana hawa wapo wengi mno, startup programs zipo tunahitaji uwekezaji hapa ili infrastructure zinapotengenezwa na Serikali ziweze kusaidia vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ndiyo tunaongoza East Africa kwa idadi kubwa ya watu (population), hapa tunavyoongea tupo kwenye kuweka sera kwa ajili ya uhamaji wa nguvukazi ndani ya East Africa. Tusipokuwa makini changamoto ya ajira itaendelea kukua hapa nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda nitoe mfano, startup program 24 katika Afrika Mashariki ziliomba capital ya pamoja na wakaweza kupatiwa zaidi ya USD Milioni Moja. Nataka niwaambie Tanzania startup program zilikuwa ngapi? Ilikuwa ni Moja, 17 Kenya, Sita Uganga. Sasa tunapoendelea huku kwenye masuala ya uhamaji wa nguvu kazi lazima tuhakikishe tunaweka mambo yetu vizuri ili tuweze ku-compete katika Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho kuhusiana na mikopo ya Halmashauri. Mikopo hii haina mjadala, inasaidia vijana wengi sana, lakini sasa hivi tumeenda kwenye aina ya kuweka mikopo kwa maana ya viwanda. Utaratibu uliokuwepo huko mwanzoni, ule muda wa vijana kuweza kufanya marejesho ya mikopo ilikuwa ni miezi mitatu, lakini ilikuwa ni kwa sababu tulikuwa tunatoa startup capitals za Milioni mbili mpaka Milioni tano, lakini model ya sasa hivi ni viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wakaanza kufanya marejesho ndani ya miezi mitatu kwa sababu wote tunafahamu mpaka uweze kupata vibali SIDO, uweze kupata vibali TBS sijui BRELA, ufungiwe umeme kule kwetu kijijini Mbinga ni zaidi ya miezi mitatu. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ipitie kanuni upya ili vijana hawa wanaopewa mikopo kwa maana ya kuanzisha viwanda, mikopo, majeresho yaweze kuongezeka muda, at least wapewe muda wa matazamio miezi Sita. Ndani ya miezi mitatu kwa kiwanda huwezi kufanya marejesho kuangalia na hali yetu ya Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho na hili suala sitaogopa kulirudia na naliongea mara nyingi sana. Wizara ya Vijana lazima msaidie Wizara nyingine iweze kuona mambo yenye tija kwa vijana, hususani pesa za kimtandao kwa malipo nje ya nchi. Nalirudia tena tunataka PayPal iweze kufanya kazi hapa Tanzania. Kama Wizara ya Fedha hawalioni, Waziri utusaidie kuwaonesha kwamba vijana wanaojiajiri hapa Tanzania wanahitaji kulipwa na wenyewe kupitia njia hizo, siyo tu sisi tulipe alafu tusilipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapoendelea kupambana na changamoto za ajira sisi kama vijana tunaumia roho kwamba sisi tunakuwa tu ni soko la watu wengine kuchukua bidhaa zetu lakini sisi hatuwezi kuuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara mtusaidie muwaambie Wizara nyingine kwamba vijana wa Kitanzania kwa sababu ninyi ndiyo mna uchungu na ajira za vijana, muwaambie Wizara nyingine haya masuala yanayohusiana na vijana ni lazima yachukuliwe kwa tahadhari kubwa sana na kwa u-serious mkubwa sana kwa sababu changamoto ya ajira ni kubwa sana nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunategemea katika Bunge hili la Bajeti suala la PayPal tunaomba litafutiwe ufumbuzi. Tumeshalizungumza hatuwezi kuzungumza kitu hapa zaidi ya miaka tisa hadi kumi na Serikali mpo. Tunaomba mtusaidie PayPal ifunguliwe, vijana wafanye malipo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule za vipaji maalumu ni shule ambazo ziliwekwa kwa ajili ya wanafunzi ambao wanafaulu kwa kiwango cha juu cha elimu. Lengo la kuweka shule hizi ni kuhakikisha wanafunzi ambao wapo katika shule hizi ambao tunasema wana akili yenye kiwango cha juu kidogo, wanafundishwa kwenye shule hizi ili kwa ajili ya kuimarisha ustawi wao. Lengo la shule hizi ni kuhakikisha tuna cream ya wanafunzi ambao wanaweza kuja kulisaidia Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sasa kwa trend ya shule za vipaji maalumu zilivyo nachelea kusema kwamba nina mashaka kama shule hizi bado zina- qualify kuwa shule za vipaji maalum kwa sababu hazizalishi matokeo. Shule za vipaji maalum zilipaswa kumsaidia mtoto na kumwendeleza kuanzia anavyoingia, anavyoendelea mpaka Vyuo Vikuu. Yaani tuwe tuna Database ya kumfuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtoto leo hii ana uwezo mkubwa kwenye kutatua mathematic concept au ana uwezo mkubwa kwenye fizikia ama biolojia ama kemia, alipaswa kusaidia ili zile akili alizonazo kwenye masomo hayo zizae maarifa na kisha baadaye zisaidie kwenye tafiti au bunifu ambazo zitasaidia Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyo kwa sasa hivi, wanafunzi hawa na akili zao nyingi kinachobakia ni kuwasifia kwamba wamepata A kwenye masomo. Yaani leo hii mwanafunzi mwenye akili tunamsifia amepata A, mwisho wa siku yupo mtaani anahangaika kutafuta ajira kama mwanafunzi mwingine aliyesoma kwenye shule za kawaida, wakati wanafunzi hawa walipaswa kusaidiwa kuwa lengo la kutatua changamoto za ajira katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu kama mtindo ndiyo huu, basi hizi shule za vipaji maalum hazina kazi yoyote. Kwa sababu mwisho wa siku mwanafunzi huyu hana tofauti na mwanafunzi aliyepo kwenye shule nyingine yoyote ya kawaida. Halafu bora wanafunzi wote kwenye shule hizi wangepata alama ya A; trend ya ufaulu kwenye shule za vipaji maalum imebadilika na ningependa nitoe mfano mchache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitasema shule nne. Mwaka 2018 Kilakala O’ Level kitaifa ilishika nafasi ya 76, A‘ Level ikashika nafasi ya 14. Msalato ilishika O’ Level nafasi ya 102, hii ni shule ya vipaji maalum A’ Level ikaja kushika nafasi ya 17. Tabora Girls O’ Level mwaka 2018 ilishika nafasi ya 90 Kitaifa A’ Level ndiyo ikajitahidi ikaja kuwa nafasi ya 11. Tabora Boys ilikuwa nafasi ya 67 A’ Level ikaja kuwa nafasi ya 15. Mwaka jana, 2021 Kilakala O’ Level Kitaifa ilishika nafasi ya 30 na A‘ Level ikashika nafasi ya 56. Ilboru O’ Level nafasi ya 23, A’level nafasi ya 18.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu hata trend yao ya ufaulu, wanafaulisha zaidi advance kuliko O’ Level kwa sababu gani? Kwa sababu wanashindwa ku- groom watoto kuanzia huku walikotokea. Kwa hiyo, ikifika advance wanaletewa watoto ambao walikuwa groomed na wengine. Hii siyo trend sawa kwa shule za vipaji maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wanaofundisha kwenye shule hizi ni wa kawaida sasa kama tulikuwa tunahitaji wanafunzi wenye vipaji maalumu wanafundishwa vipi na walimu wa kawaida ilipaswa tuwe tuna mpango wa kuhakikisha walimu wanaofundisha kwenye shule hizi ni walimu wa kipekee ili kuendena na akili ya mwanafunzi. Ndiyo maana shule hizi O’ Level hazi-perform kwa sababu wanafundishwa na walimu ambao wao wamewazidi akili, sasa watafaulu vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shule za vipaji maalum lazima ziwe redefined, la sivyo, kama Taifa tutasota sana.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe taarifa mchangiaji kwamba hata walimu wanaowafundisha hawa watoto hawawafundishi kwa namna ya kipekee kwa sababu wanaamini wale watoto wana uwezo wa kipekee. Kwa hiyo, wanawacha wajisomee badala ya kuwekeza kwao kuhakikisha wanafanya vizuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapinga, taarifa hiyo.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa lazima tujitafakari upya kuhakikisha kwamba wanafunzi wenye vipaji maalum wanawekewa mpango maalum ili wasaidie Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Watanzania wengi wenye akili nyingi wamechukuliwa na wenzetu na wengine hata wanafanya kazi google huko Marekani, wanasaidiwa, wameendelezwa lakini hata sisi hatuna database ya kufuatilia. Kwa hiyo, kama Taifa tujifunze kutumia watu wetu na tuwekeze kwenye bajeti ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya elimu ina changamoto. Bajeti ya sekta ya elimu imegawanywagawanywa, ipo kwenye Wizara tofauti. Sasa Wizara ya Elimu wana bajeti yake, lakini bajeti kubwa ya Sekta ya Elimu ipo TAMISEMI. Kwa hiyo, hata kwenye ufuatiliaji wake wa masuala ya msingi yenye kuendeleza watoto kama hao wenye vipaji maalum inakuwa ni changamoto. Kwa hiyo, tuangalie bajeti ya Sekta ya Elimu iwe centralized ili tuweze kujua tuna-prioritize vipi mambo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nizungumzie suala la pili kuhusiana na watoto ambao wapo kwenye shule za binafsi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu wazazi wao ama walezi wao hawawezi kuwalipia ada. Shule za Serikali ni za kila Mtanzania. Kila Mtanzania anapaswa kwenda kwenye shule ya Serikali bila kigezo ama bila kikwazo chochote kile. Nasi wenyewe tunasema kwamba kila mtoto wa kitanzania ana haki ya kupata elimu bila kikwazo cha namna yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanafunzi aliyekuwa kwenye shule binafsi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Kapinga kwa mchango mzuri. Ni kengele ya pili.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kadha wa kadha anazofanya kwa mustakabali wa Taifa letu. Napenda kumpongeza kwa jitihada za hivi karibuni za kuendelea kujali utumishi wa umma ambapo amegusa sekta zote ikiwemo sekta hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa maadhimisho ya sherehe za kitaifa za Mei Mosi, Mheshimiwa Rais alisema, mafanikio ya Taifa lolote hutokana na juhudi za wafanyakazi wake, yaani every nation owes its success to its labourers. Mheshimiwa Rais amedhihirisha maneno yake kwa matendo kwa kuwa mwaka jana alipunguza kodi ya mshahara kwa watumishi wa kima cha chini kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane na kama haitoshi mwaka huu amewaongeza mshahara wa asilimia 23.3 pamoja na kada zingine za mshahara. Mheshimiwa Rais kwa mtindo huu anaendelea kuupiga mwingi kweli kweli na kwa kweli Watanzania watarajie makubwa zaidi kutoka kwa Rais wetu anayewapenda sana.
Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu. Moyo wake wa dhati wa kuboresha sekta ya afya haujaanza leo. Tumeona jitihada zake nyingi za kuboresha sekta ya afya tangu alipoaminiwa kwa mara ya kwanza katika sekta hii. Mara zote amesimama kidete kupambania afya za Watanzania. Namuombea Mheshimiwa Waziri afya njema ili maono aliyonayo kwa sekta ya afya yatimie kwa mstakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, uviaji wa mimba ama utoaji wa mimba usio salama umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo vya kinamama wajawazito. Uviaji wa mimba ni utokaji wa mimba kabla ya wiki ya 28 ya ujauzito. Utokaji wa mimba unaweza kusababishwa na sababu ambazo sio za kukusudia ila kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu zinazotokana na mimba zisizotarajiwa na hivyo kupelekea wengi kutoa mimba kwa watu wasio na ujuzi wa kitabibu na katika maeneo yasiyo salama kabisa.
Mheshimiwa Spika, duniani kote, utoaji wa mimba upo kwa kiasi cha milioni 56 kila mwaka ambapo katika utoaji huo, takribani wanawake milioni 25 wanafanya utoaji wa mimba usio salama. Kila mwaka kati ya wanawake hao wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama asilimia 98 hutokea katika nchi zinazoendelea ambapo takribani milioni tatu ni watoto wa kike kati ya umri wa miaka 15 hadi 19 na takribani wanawake 47,000 wanafariki kila mwaka kutokana na utoaji huo wa mimba usio salama.
Mheshimiwa Spika, hapa kwetu Tanzania, takribani wanawake 405,000 wanatoa mimba kwa njia zisizo salama na asilimia 40 ya wanawake hupata madhara mbalimbali yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama. Asilimia 18 ya wanawake hawa wanatoa mimba kwa madaktari walio na ujuzi stahiki, asilimia 31 wanatolewa na wauguzi ambao hawana ujuzi stahiki na asilimia 51 wanatoa kwa njia za kienyeji ikiwemo kunywa dawa kiholela kwa kushauriwa na wafamasia au kwa njia nyingine ambazo sio za kitabibu.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa tatizo hili limepelekea matatizo mbalimbali ya uzazi kwa wanawake ikiwemo ugumba na matatizo mengine sugu ya uzazi ningependa kushauri, elimu zaidi inahitajika juu ya utoaji wa mimba usio salama. Pamoja na elimu, uboreshwaji wa vitendea kazi na dawa stahiki zinahitajika katika vituo vya afya ili kusaidia madhara yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama kwa sababu hatuwezi kusema tuache waathirike na matatizo hayo kisa tu ni jambo lisilo la kimaadili. Tuendelee kuwahimiza kuachana na utoaji mimba usio salama na uzazi salama lakini madhara yanapotokea tuwasaidie kwa kuweka dawa stahiki na vitendea kazi kwa sababu pamoja na yote wapo pia ambao wanapata matatizo ya kutoka kwa mimba bila kukusudi na wanahitaji kusafishwa ila sasa ili huduma zipatikane kwa urahisi ni vyema kuweka dawa na vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo naomba suala la Muswada wa Bima ya Afya kwa kadri Mheshimiwa Waziri alivyoeleza lifanyiwe kazi mapema ili Watanzania wengi wanufaike na huduma bora za afya.
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia na ninaomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na harakati anazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya mama Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa makubaliano zaidi ya 17 ambayo ameingia kwa maslahi ya Taifa letu. Mheshimiwa Rais anafahamu umuhimu wa sekta binafsi na ndiyo maana yeye mwenyewe amekuwa kipaumbele katika kuja na makubaliano haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, duniani kote, duniani kote na siyo maneno yangu ni maneno ya takwimu kwa sababu wanasema no research, no right to speak, siyo maneno yangu mimi. Duniani kote uwekezaji wa sekta binafsi ndiyo mhimili wa maendeleo ya Taifa lolote duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, takwimu za International Finance Corporation zinasema; kazi zote na ajira zote takribani 90% duniani kote zinachagizwa na zinaletwa na sekta binafsi. Shirika hili linasema 60% ya pato la Taifa kwa nchi zote duniani zinachagizwa na sekta binafsi. Benki ya Dunia inakadiria kwamba 90% ya kazi zote duniani katika mataifa yanayoendelea zinaletwa na sekta binafsi na sisi hata Watanzania hapa ni mashahidi kwa sababu kazi nyingi na ajira nyingi zipo kwenye sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile sekta binafsi ndiyo ambayo kwa takwimu inachagiza zaidi kwenye upatikanaji wa kodi na mapato kwa Serikali duniani kote na hayo siyo maneno yangu. Mataifa makubwa ama mashirika makubwa ya kitaifa ambayo tumeyakasimu madaraka kwa mfano Economic Cooperation and Development yamethibitisha, kwa mfano kodi ya makampuni ambayo hata sisi tunaitegemea kwa kiasi kikubwa kwenye kuendesha Serikali yetu duniani kote inaletwa zaidi na sekta binafsi. Kwa hiyo ni masuala ambayo kwa kweli yamejiweka wazi na yamejitanabaisha wazi kwenye umuhimu wa sekta binafsi na ndiyo maana makubaliano yoyote yanayoingiwa yanachagiza zaidi ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, asilimia 75 ya miundombinu yote duniani kwenye uwekezaji mkubwa wowote duniani unamilikiwa na sekta binafsi na ndiyo sekta ambayo imetusaidia kukidhi changamoto za miundombinu ambayo nchi yoyote duniani inayo kwa sababu sekta binafsi ndiyo ambayo inaweza kuwekeza zaidi kwenye teknolojia, ujasiriamali kwa sababu ndiyo ambayo inaweza kukidhi ushindani kuliko uwekezaji ambao unaweza kufanywa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo ushindani unaokua kwa kasi sana kutokana na maendeleo ya teknolojia huwezi kuacha kushirikisha sekta binafsi ili kukabiliana nao. Kila siku tunasimama hapa na tunasema jamani teknolojia haipigwi ngumi. Ukipiga ngumi teknolojia kwa zama hizi za sayansi na teknolojia umeenda na maji. Huwezi kuacha ku-involve sekta binafsi ili iwekeze kwenye teknolojia iweze kutusaidia sisi kusonga mbele kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote tunafahamu Tanzania ni nchi ya 141 kati ya nchi 177 kwenye uwekezaji wa biashara na mojawapo ya changamoto kubwa zinazotufanya tuwe nyuma ni changamoto za uendeshaji wa bandari kwa sababu ndiyo eneo ambalo lilipaswa kutuingizia mapato makubwa kama Taifa na ili tuweze kutoka kwenye 141 na tuende kwenye nafasi ambazo zinatufanya kama Taifa tuweze kushindana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kazi yetu kama Bunge ni kushauri na kwenye makubaliano haya kwa kweli tutasimama kidedea. Baada ya miaka 60 ya Uhuru hatuwezi kuendesha nchi yetu conventional, hilo ni jambo ambalo haliwezekani. Ni lazima tukubali Tanzania siyo kijiji. Ni lazima tukubali sisi tupo kwenye ushindani. Haiwezekani meli zichukue siku 4.5 mapaka tano kushushwa bandarini, wakati jirani yetu anatumia siku moja kushusha mzigo wake. Kwa akili ya kibiashara wafanyabiashara wote hawawezi kuja kwako kwa ajili ya biashara. Kwa hiyo, lazima tukubaliane wote tunasemaga hapa Serikali haiwezi kuwekeza yenyewe kwa sababu ya namna ambavyo Serikali zetu zinajiendesha, kwa hiyo ni lazima tu-involve sekta binafsi kwa sababu ndiyo sekta ambayo kwanza inafanya research kwa haraka sana na pia inaweza ku-adapt kwa sababu ya sera ya sekta binafsi inaweza ku-adapt mazingira kwa haraka sana, kwa hiyo hata teknolojia ina adapt kwa haraka mno. Kwa hiyo, ni lazima tu-involve sekta binafsi katika kuhakikisha maendeleo ya Taifa letu tunapiga hatua kwa kasi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, humu ndani hakuna Mbunge ambaye siyo Mtanzania, wote sisi ni Watanzania na hakuna Mbunge ambaye hana uzalendo kwa mama Tanzania, kila Mbunge humu ndani ana uzalendo wa hali ya juu sana kwa mama Tanzaniam kwa hiyo hakuna Mbunge ambaye anaweza kuidhinisha mkataba unaoenda kuuza rasilimali kubwa kama ya bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nielezee kuhusiana na mkataba; mkataba ule hakuna Mbunge humu ambaye ni mangungu wa Msovero hajui kusoma, wala hajui maslahi ambayo sisi kama Taifa tunaingia. Ule mkataba ni kwa sababu baadhi ya watu wanapenda kuwasomea wenzao baadhi tu ya vifungu labda nusu kingine hamalizii, lakini nitakupa mifano miwili tu ya umakini wa ule mkataba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huko nyuma tukienda kwenye ku-solve migogoro inayohusiana na mashirikiano kati ya sisi na makampuni ya kimataifa tulikuwa tunatumia sheria za wengine katika kutatua migogoro yetu sisi wenyewe, lakini mkataba huu umesema; migogoro yoyote itakayohusika na uendeshaji wa bandari kwenye mikataba ya HGA hata kama tutaenda kutumia usuluhishaji kwenye platform za kimataifa, tutatumia sheria zetu za Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sheria ya Uingereza ambayo inasemwa itatumika ni ile kwenye mkataba wa nchi kwa nchi kwa sababu sisi wote ni independent states, hatuwezi kutumia sheria ya Tanzania ama sheria ya Dubai kwa sababu lazima twende kwenye neutral point. Kwa hiyo, mikataba ya uendeshaji wa bandari itakuwa determined migogoro yake kwa kutumia sheria zetu za Tanzania hata kama tukienda ICSID ambako ndiyo migogoro mingi inaenda kutatuliwa hata kama tukikaa South Africa sheria ambayo itatumika kwanza ni Sheria ya Tanzania. Kwa hiyo, ni mkataba ambao unaangalia maslahi ya Watanzania kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwenye suala la ukomo; mkataba huu hauwezi kuweka ukomo kwa sababu tutakuwa hatujitendei haki kama Watanzania. Mkataba wa uendeshaji wa bandari ndiyo ambao utaweka ukomo, ukiweka miaka 15 ukomo ina maana mkataba huu miaka 15 ikiisha na mkataba huu utaisha. Sasa leo tuweke miaka 40 uendeshaji wa bandari tunaenda kuweka miaka 25, sasa inakuwaje tujifunge sisi wenyewe? Kwa hiyo, ndiyo maana nasema umakini umefanyika kwenye mkataba huu ili kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho Watanzania wana hofu kwa sababu uwekezaji huko nyuma kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wamewahi kutuingiza hasara Taifa letu. Kwa hiyo, sasa lazima vilevile tushauri na tutoe angalizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi Bunge ni tunaisimamia Serikali na kuishauri, hatuwezi kuhusika kwenye kutunga mkataba halafu baadaye pia tukaja kuusimamia huo mkataba husika, lakini tunataka tuwaambie watendaji ambao wamekasimiwa haya madaraka, huko nyuma kama Taifa tumeingia hasara sana, safari hii tutatoa macho kweli kweli, hatutakubali. Tutahakikisha mikataba yote inayopitiwa na inayopitishwa ina maslahi kwa mama Tanzania. (Makofi)
Kwa hiyo tutahakikisha tunatoa macho, tunasimamia na kama kuna mtendaji ambaye ataweka masuala yoyote ambayo yana maslahi binafsi au kwa kikundi cha watu kwa kweli tutahakikisha wanawajibishwa kulingana na sheria yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi nami nitumie nafasi hii kumpongeza Kaka yangu Mheshimiwa Waziri Nape kwa weledi mkubwa anaoufanya katika sekta ya habari. Kwa kweli uongozi wake wa kusaidia Vyombo vya Habari na sekta nzima ya habari tumeuona na mimi nimtie shime aendelee na mwendo huo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hoja mbili, kwanza ni kuhusiana na utaratibu wa kuambiwa tuombe loss reports pale ambapo unapoteza laini za simu. Kwa hapa tulipo kwa sasa hivi, mtu anavyosajili line ya simu anasajili kwa kitambulicho cha NIDA na anaweka finger prints kwa hiyo, utaratibu wa kuambiwa kutafuta loss reports wakati umepoteza laini ya simu naona ni utaratibu unaoleta urasimu ambao hauna maana yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani utaratibu huu labda walivyokuwa wanaweka waliwawekea watu wa Mjini, kwa sababu kwa huko Vijijini tunakotoka mtu tu afike kwenye Kituo cha Polisi kwenda kuomba loss report ameshatumia zaidi ya Shilingi 10,000 ama Shilingi 5,000 ama Shilingi 15,000 nauli. Anakwenda kutafuta loss report ya Shilingi 500 au siku hizi tunaambiwa kwamba unaweza kuomba kwenye simu, haya ni mambo ya watu wa Mjini Vijijini kule internet inasumbua. Mimi sina mashaka na Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Nape haya masuala madogo madogo, yanaleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi simu ndiyo maisha yetu, haiwezekani mtu akatafute loss report zaidi ya siku moja, siku mbili awe nje ya mtandao. Namuomba Mheshimiwa Waziri waweze kuangalia utaratibu huu uweze kuondoka, tayari tunatumia kitambulisho cha NIDA kwenye kusajili laini zetu. Kwa hiyo, tunaomba utaratibu wa kuambiwa tutafute loss report wakati tumepoteza laini ya simu uweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye suala langu la pili kuhusiana na ulinzi wa taarifa binafsi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 inasema: “kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake, unyumba wake, lakini pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia habari ya usiri na ulinzi wa taarifa binafsi za mtu. Kwa nyakati hizi ambazo tunazo, simu zetu zinabeba taarifa zetu nyeti na nzito, ambazo hata watu wetu wa karibu hawazifahamu. Simu zetu zinabeba siri zetu, zinabeba ulinzi wa fedha zetu na maisha yetu kwa ujumla ya kila siku, kwa hiyo, tusipokuwa na ulinzi wa taarifa zetu binafsi ni jambo ambalo kidogo linahatarisha. Naomba nieleze kwa lugha inayoeleweka, kwenye ukusanyaji wa taarifa kuna kitu kinaitwa data collection na kuna kitu kinaitwa data processing. Data collection ama ukusanyaji wa taarifa kwa mfano kampuni ya simu inavyosajili laini yangu inachukua jina langu, inachukua makazi yangu ninapokaa na umri wangu na taarifa za msingi siyo mbaya kwa sababu ni kwa ajili ya kutupatia huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa inapoanza kuchakata taarifa hapo ndiyo ugumu unapokuja. Kwa sababu, inachakata taarifa ina maana inazi-process halafu inawapa watumiaji wengine/makampuni mengine kwa kuyauza. Kwa mfano, unashangaa tu unatumiwa message za betting kwenye simu, ina maana wamechakata wamewapa wale makampuni ndiyo maana tunatumiwa taarifa. Namuomba Mheshimiwa Waziri, Sheria ile ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi lazima ije hapa Data Protection and Privacy ili tuweze kulinda taarifa za watu binafsi, lakini taarifa zetu zinazoenda pia nje ya nchi, kwa sababu taarifa zinatumika bila idhini yetu. Vilevile taarifa zinatumika kwa kuwanufaisha wengine bila sisi kutunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga…
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja namalizia. Kampuni za simu zinatupa terms of conditions wakati unasajili laini, zile terms of conditions zimeandikwa kwa lugha za kisheria na ngumu mno na tunaambiwa tutazikuta kwenye website. Kwa hiyo, tunaomba wakati tunasajili laini tupewe ule mkataba wa namna ya matumizi ili tuweze kuelewa kwamba tunaposajili laini tunajiingiza kwenye vitu gani ambavyo vya msingi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, awali ya yote ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Kwa kweli ni jambo lenye tija sana na kwa dhati ya moyo wangu naomba nimpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kubwa kati ya ubakaji na ulawiti kwa watu wazima na ubakaji na ulawiti kwa watoto, na tofauti ni kwamba mtu mzima ana haki ya kuipigania haki yake, anaweza kuipigania haki yake kwa sababu nguvu anazo, utashi anao na maarifa anayo. Sasa hii ni tofauti kwa mtoto mdogo kwa sababu mtoto hawezi kupigania haki yake, haki ya mtoto inapiganiwa kwa utashi wa mzazi wake ama mlezi wake, na hapa ndipo ambapo tatizo linakuja kwa sababu ili haki ya mtoto iweze kupiganiwa inategemea utayari wa mzazi wa kupigania haki hiyo. (Makofi)
Kwa hiyo, mzazi anaweza akachagua mambo tofauti tofauti, kwanza anaweza akachagua aipiganie, lakini la pili anaweza akachugua asipiganie, la tatu akipewa mpunga anaweza akaamua akae kimya. Lakini kama yeye mwenyewe anahusika na matendo ya ukatili hataipigania haki hiyo kabisa. Sasa hapa lazima Wizara ikae na Wizara nyingine ambazo zinahusika ili kuweka mambo sawa. Na lazima wakubali kuweka uwekezaji kwa Maafisa Maendeleo wa Jamii. Nasema hivyo kwa sababu gani, Afisa Maendeleo ya Jamii ndiyo mtu kati ambaye anaweza kulinda haki ya mtoto na akamshurutisha mzazi atafute haki ya mtoto wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafahamu tutasema kwamba labda kuna tatizo la fedha na nini, lakini ulinzi wa haki ya mtoto unategemea hapa tutafanya uwekezaji wa aina gani. Lakini niende mbele zaidi kwenye kuishauri Wizara, sasa hivi hali ilivyo, namna ambavyo mashtaka yanaendeshwa ya masuala ya ubakaji na ulawiti kwa watoto yanaendeshwa sawasawa na mashtaka ya ubakaji na ulawiti kama ilivyo kwa watu wazima. Sasa hapa pia kuna tatizo lingine kwa sababu Mahakama inatuambia kwamba ushahidi mzuri unatoka kwa yule mtu ambaye amefanyiwa ukatili yeye mwenyewe na hapa tunamzungumzia mtoto mdogo yaani namna anavyotoa ushahidi wake lazima aseme alivyofanyiwa kile kitendo kwa maneno mahsusi yanavyotumika. Na akisema vile ambavyo sivyo ushahidi unapungua thamani yake. Sasa ukiangalia kwa mila zetu na desturi zetu za Kitanzania kwa maadili tuliyokuza nayo watoto wetu yale maneno kutamka ni ngumu sana. Kwa sababu mtoto lazima atamke zile nyenzo za kimwili zilizotumika kumfanyia uhalifu ambazo hata mimi mwenyewe binafsi siwezi kuzitamka. (Makofi)
Sasa nafahamu Mahakama inatumia utashi mara nyingine watoto wakishindwa kusema bado wanatumia utashi walionao kwa ajili ya ku-convict hawa watuhumiwa. Lakini lazima tuiweke kwenye sheria, lazima utaratibu wa kushughulikia matatizo ya ulawiti na ubakaji kwa watoto uwe tofauti kabisa na kifungu cha kushughulikia ubakaji na ulawiti kwa watu wazima kwa sababu watoto kama alivyo mtoto kama yeye mwenyewe hawezi kujipigania. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi namshauri Mheshimiwa Waziri akakae na Waziri wa Sheria na Katiba waone namna ya kutofautisha haya mambo. Namwambia yeye kwa sababu yeye ndiyo analinda ustawi wa watoto katika Taifa letu. Kwa hiyo bila kuweka mambo sawa hapa naona kidogo kutakuwa na mushkeli.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kushauri kuhusiana na ulinzi wa mtoto, hapa kwa muda mrefu tumeongelea kuhusiana na watoto kubeba mabegi mazito mgongoni na yalishatolewa maelekezo, lakini kinachosikitisha bado watoto wanabeba mizigo mikubwa sana wakienda shuleni na inahatarisha afya zao. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ndio anahusika na ustawi wa mtoto, yeye ndio anamlinda mtoto wa Kitanzania, naomba afanye jambo katika hili. Shule zetu zinaweza zikaweka utaratibu mzuri watoto wasibebeshwe mlima wa madaftari, ma-counter book na mlima wa vitabu migongoni mwao tunaharibu afya ya hawa watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala langu la mwisho ni kwenye ulinzi wa afya ya mwanamke. Afya bora ya mwanamke ni uwekezaji kwa Taifa letu kwa sababu mwanamke anatumika kama nyenzo ya maendeleo kwenye mambo mengi sana. Ninachosikitika suala la utoaji wa mimba holela mtaani limeachiwa kupita maelezo. Takwimu zinatuambia wanawake 400,000 kila mwaka wanatoa mimba mitaani na asilimia 70 wanatumia nyenzo ambazo sio za kiafya. Wanatumia nyenzo ambazo sio za madaktari wenye sifa, ni asilimia 30 tu wa mjini ambao watakwenda kwa madaktari wenye sifa. Sasa masuala ya utoaji huu wa mimba inawezekana tusiyaongee sana, lakini wanawake 400,000 kwa mwaka ni wanawake 1,100 kila siku wanatoa mimba kwa njia zisizo salama.
Mheshimiwa Spika, sasa tunaomba ulifanyie kazi hili suala, nafahamu kuna situation ambazo zinaruhusiwa mwanamke aweze kutoa mimba, lakini kuna mambo ambayo tunaweza tukayaboresha. Kuna mazingira magumu ambayo tunaweza tukaboresha ili masuala ya utoaji wa mimba huko mtaani, pasipo kutumia nyenzo sahihi yaweze kupungua na yaweze kuhalalishwa yakafanywa katika hospitali zetu. Kwa mfano, kwa sababu sasa hivi tunaambiwa takwimu karibu wanawake 1,000,000 kila mwaka wanapata mimba zisizotarajiwa, sasa tuone tunaboresha vipi ili wanawake wasikimbilie kule mtaani kwenye nyenzo ambazo sizo na waende wakafanye katika mahali ambapo panastahili kiafya katika suala hilo.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya chini ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo ameisoma hapa wiki iliyopita na pia nampongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, dada yangu Jenista Mhagama na kaka yangu Deo Ndejembi pamoja na Waheshimiwa Naibu Mawaziri, kaka yangu Patrobas Katambi na dada yangu Ummy Nderiananga.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naunga mkono hoja na kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa dhati ya mioyo yetu kwa ushauri, maono na mapendekezo mbalimbali ambayo wamechangia katika Sekta yetu ya Nishati na hususani katika Sekta Ndogo tunazozisimamia za Umeme, Mafuta pamoja na Gesi. Tumepata jumla ya wachangiaji 13 na yamkini naweza nisijibu hoja moja baada ya nyingine, lakini nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, kila hoja ambayo imezungumzwa hapa tumeipokea kwa uzito wa kipekee sana na zile ambazo zinaweza kutekelezeka, tunapenda kuwahakikishia kwamba, tutazitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na nishati safi ya kupikia. Waheshimiwa Wabunge wameeleza umuhimu wa kupunguza bei ya nishati safi ya kupikia, hususani gesi ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi waweze kutumia nishati hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha matumizi fanisi ya nishati safi ya kupikia na ili kuweza kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ni lazima nishati hii iwe na sifa kuu nne. Moja, ni lazima ipatikane kwa urahisi; Pili, ni lazima matumizi yake yaweze kuwa rahisi; Tatu ni lazima iwe na unafuu wa bei; na Nne, ni lazima iwe nishati salama ambayo inalinda usalama wa watumiaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha masuala yote haya na hususan suala la unafuu wa bei, Serikali ya Awamu ya Sita imeshaanza kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia. Mojawapo ya mikakati hiyo ni kupunguza gharama za awali ambazo zinahusiana na kuanza matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan vifaa pamoja na majiko ya gesi. Hii ni kwa sababu changamoto kubwa ilikuwa ni kwa wananchi kuanza kufanya matumizi kwa sababu gharama za awali huwa ni kubwa kwenye kupata vifaa pamoja na majiko. Jambo hili tayari tumeshaliwekea mikakati mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, tumeshaanza kutoa ruzuku ya mitungi ya gesi kwa ajili ya watumiaji mbalimbali wa Tanzania. Pili, kupitia miradi tunayoitekeleza na wabia wetu wa maendeleo hususan Umoja wa Ulaya pamoja na Wakala wetu wa Nishati Vijijini tayari tumeanza kuwawezesha mawakala wanaouza gesi mijini na vijijini kwa kuwapa ruzuku ili gesi inayoenda kwa mtumiaji wa mwisho iweze kuwa na gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi tunaoutekeleza na Umoja wa Ulaya, wananchi wataweza kupata unafuu kwa 45% mpaka 60%. Vilevile, kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini wananchi wataweza kupata unafuu kati ya 25% mpaka 30%. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwenye suala la kuanza matumizi ya nishati safi ya kupikia Serikali imejizatiti kupunguza gharama ili Watanzania wengi waanze matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunayo mikakati ikiwemo kuboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uzalishaji, upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati safi ya kupikia. Tunafanya hivi kwa sababu tukiboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu nishati safi ya kupikia itakuwa na bei rahisi kwa sababu tutakuwa tume-balance economic scale. Pamoja na mikakati hiyo kwa sasa hivi tunafanyia kazi kuhuisha na kuoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo wezeshi itakayofanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mikakati michache ambayo tunayo kuhakikisha kwa kadri ya maoni ya Mheshimiwa Rais ambaye ndio champion namba moja wa nishati safi ya kupikia, ikifikia 2033 Watanzania wengi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge agenda hii ya Mheshimiwa Rais ipo katika mikono salama sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili uweze kuzalisha tani moja ya mkaa unahitaji kuchoma magogo kati ya tani 10 mpaka 12. Ndio maana ni lazima tulinde mazingira yetu kwa wivu mkubwa sana na ndio maana ni lazima Waheshimiwa Wabunge na wananchi tuhamasishane kwenda kwenye nishati safi ya kupikia ili tuweze kutunza mazingira haya kwa manufaa yetu sisi na manufaa ya vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hoja hiyo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa kuhusiana na hoja ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo tumefanya kwa ufanisi mkubwa sana Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini na mpaka leo hii tumebakisha vijiji 468 tu kati ya vijiji 12,318, ndiyo hivyo tutahakikisha vitongoji vyote ambavyo ni 31,532 visivyo na umeme vitapata umeme ndugu zangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji hivi ni vingi, jumla ya vitongoji tulivyo navyo ni 64,359 na mpaka leo hii kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita tumeweza kupeleka umeme kwenye vitongoji 32,827. Kwa hiyo, utekelezaji wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaendelea. Niwahakikishie kama Mheshimiwa Rais anavyosema, maendeleo ni hatua tutaenda hatua kwa hatua kuhakikisha umeme kwenye vitongoji unapelekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Tarehe 13, Aprili, 2021 nilisimama hapa katika Bunge hili Tukufu kuishauri Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria hii ya Utakatishaji wa Fedha. Napenda niishukuru Serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko kwenye Sheria hii ya Utakatishaji Fedha. Pia kipekee nimshukuru Waziri wa Fedha pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta mabadiliko haya Bungeni. Kwa kweli ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria hii ya Utakatishaji wa Fedha ilikuwa inalalamikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu moja, kwamba ilikuwa ina mawanda mapana sana kiasi cha kwamba hata watu ambao walikuwa wanadhaniwa hawahusiki walikuwa wanajumuishwa kwenye makosa hayo ya utakatishaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa mapendekezo ya mabadiliko haya hususan kifungu cha 12 ambacho kinalenga kufanya kosa la utakatishaji fedha kujitegemea, tendo ambalo naamini litapunguza kiasi kikubwa kujumuisha makosa ambayo hayahusiki katika makosa ya utakatishaji fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi kwa Serikali, napenda niishauri Serikali yangu sikivu mambo matatu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mabadiliko haya yaliyopendekezwa na Serikali, makosa tangulizi ya utakatishaji fedha yalikuwa yametafsiriwa chini ya kifungu cha tatu kwa kujumuisha makosa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapendekezo haya, tafsiri ya makosa tangulizi imebadilishwa na kuwekewa mawanda mapana zaidi. Kulingana na mabadiliko haya, tafsiri hii imebadilishwa kwa kuelezwa kwamba, makosa tangulizi yanayoweza kupelekea utakatishaji wa fedha yatakuwa makosa makubwa ambayo yametafsiriwa katika Sheria ya Mazalia ya Uhalifu ama the Proceeds of Crimes Act. Sasa ukienda kwenye Sheria hii ya Mazalia ya Uhalifu ama Proceeds of Crimes Act, ina-define makosa haya tangulizi kama makosa ambayo adhabu yake ni kifo au kifungo kisichopungua miezi 12 (serious offences constitute a serious offence to which the punishment is either death or imprisonment for a period not less than 12 months). Hiyo ni sheria ya mazalia ya uhalifu revise edition 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa haya yanawekewa mawanda makubwa sana. Ukisema makosa yote ambayo punishment yake ni aidha ni kifo ama makosa ambayo adhabu yake siyo chini ya miezi 12, yanakuwa ni makosa mengi mno. Sasa ningependa kuishauri Serikali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mawanda haya yameongezwa kiasi cha kwamba hata kuna makosa ambayo hayatahusika yatakuwa humu, advantage tuliyonayo ni ulinzi wa kifungu cha 12. Hata hivyo, kwa sababu tuna historia ya kutumika vibaya kwa vifungu hivi vya uhujumu uchumi, napenda kuishauri Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi ili kuhakikisha vifungu kama hivi visijitokeze vikatumika vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano mbalimbali huko nyuma; na kifungu hicho kwangu mimi ni kifungu ambacho kipo very serious kwa sababu ukisoma makosa yote ambayo adhabu yake ni kifo au makosa yote ambayo adhabu yake ni kifungo ambacho siyo chini ya miaka 12, ni makosa mengi mno na ukizingatia kwamba nchi yetu ina sheria nyingi mno; kwa hiyo, ni muhimu Serikali kuendelea kuweka ulinzi wa mifumo ili kuhakikisha kifungu hiki hakitatumika vibaya. Sina mashaka kwamba kwa Serikali hii ya Mheshimiwa Rais ambayo inajali haki za Watanzania, mifumo itawekwa vizuri na vifungu kama hivi havitatumika vibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda niongelee, naungana na maoni ya Kamati kuhusiana na kuweka sera itakayohusu kudhibiti Ugaidi na Utakatishaji wa Fedha. Masuala yote yanayohusisha makosa ya kiuchumi ni masuala yanayohusisha haki za watu za kuhodhi mali, yanahusisha masuala ya watu ya kiuchumi. Wote tunafahamu hali ya mtu ya kiuchumi ndiyo uhai wake. Kwa hiyo, ni makosa ambayo kwa namna moja ama nyingine ni serious sana ndiyo maana ni muhimu sana kuja na sera hii ili kuhakikisha makosa yote ambayo yanakaa kwenye sheria yamewekewa misingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano mawanda ya sheria hii…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja namalizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mawanda ya sheria hii yamehusisha kwa kiasi kikubwa sana Sheria ya Ugaidi. Napenda niishauri Serikali, makosa ya ugaidi ni makosa makubwa sana; na kwa sababu tayari tuna Sheria ya Ugaidi, ingekuwa ni vyema makosa yote yanayohusisha ugaidi yawekwe kwenye Sheria ya Ugaidi na huku Money Laundering yabaki makosa ambayo yatahusisha utakatishaji wa fedha ili kuhakikisha kwamba haki za watu za kiuchumi zinalindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Kifungu cha 12 kime-introduce kifungu kipya cha Pili. Pale limeweka neno ambalo halijatafsiriwa kwenye sheria. Neno la “Underline Money Laundering Offence,” kama Serikali ilikuwa inamaanisha proceeds offence ingeweka hivyo badala ya kutumia neno ambalo halijawa defined kwenye sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. (Makofi)