Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Judith Salvio Kapinga (49 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini TANESCO watalipa fidia kwa wananchi wa Rorya waliopisha eneo la kupitisha umeme mkubwa toka mwaka 2011?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge ahsanteni sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele, naomba nitumie dakika moja kwa ajili ya shukrani. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya rehema na baraka. Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoiweka juu yangu na kuniteua niweze kumsaidia kama Naibu Waziri wa Nishati nikimsaidia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu. Napenda nimwahidi Mheshimiwa Rais imani hiyo aliyonijalia nitaitumikia kwa weledi na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, TANESCO tayari imekamilisha uthamini na uhakiki wa marudio ya mali zilizoathiriwa na mradi na kwa sasa ipo katika hatua za maandalizi ya malipo. Malipo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, tunawaomba wananchi wanaosubiri kulipwa fidia wawe na subira wakati maandalizi ya malipo yakiwa yanaendelea kufanyika.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke vitapewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme. Hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji sita vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kwisha tarehe 31 Desemba, 2023. Aidha, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimeshawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke bado linaendelea na nguzo tayari zimesimamishwa katika Kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme wa uhakika katika Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa muda mfupi wa kujenga kituo kidogo cha umeme (Switching Station) kwenye eneo la Nyamirangano lililopo kwenye Halmashauri ya Ushetu. Kupitia kituo hicho kidogo, TANESCO itaongeza njia nyingine za umeme kutokea kwenye kituo hicho kwenda Ushetu, Msalala na Kahama ambazo zitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme. Mradi huu unategemewa kukamilika 2024 na unagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.2, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imechukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni pamoja na kufunga transformer yenye ukubwa na uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Msamvu. Kazi hiyo ambayo inagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 inatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Novemba, 2023. Aidha, sambamba na hilo, TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya usambazaji wa umeme katika Manispaa ya Morogoro ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, lini Mkoa wa Rukwa utaunganishwa na Gridi ya Taifa ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Gridi ya Taifa, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovolt 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma kwa Mradi wa TAZA, umbali wa kilomita 620. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, Wakandarasi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wameshapatikana na Wakandarasi wa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme wapo katika hatua za majadiliano. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2025, ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme kwenye Kata za Kikeo, Kinda na MaskatI – Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mvomero ina jumla ya vijiji 129 ambapo kati ya hivyo, vijiji 92 tayari vimeshapatiwa umeme. Vijiji 37 vilivyosalia ambavyo baadhi vinapatikana katika Kata ya Kikeko, Kinda na Maskati vitapatiwa umeme na mkandarasi ambaye yupo maeneo ya mradi anaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu. Mkandarasi huyu anatarajia kukamilisha kazi ifikapo mwezi Juni, 2024, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, wakandarasi wangapi kutoka Mkoa wa Kagera wamepata kazi katika mnyororo wa ujenzi wa Bomba la Mafuta la Hoima – Tanga?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi Wakuu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga) wameendelea kushirikiana na Wakandarasi wadogo wajenzi pamoja na watoa huduma mbalimbali katika maeneo yote inayopitiwa na mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Kagera hadi sasa, jumla ya wakandarasi na watoa huduma 42 wamepatiwa kazi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ujenzi wa mradi huu, zikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za usafirishaji, ulinzi, usambazaji wa mafuta, huduma za umeme na hoteli, nashukuru.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inaielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati safi na vifaa sahihi vya kupikia. Kwa sasa Serikali inakamilisha kuandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimi 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2033. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka 2001, TPDC iliingia mkataba wa kuuziana gesi asilia iliyotengwa na Songas. Kiasi cha futi za ujazo bilioni 320 za gesi asilia iliyotengwa zilitengwa kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa miaka ishirini (20) kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2024. Mwaka 2004, TANESCO iliingia mkataba wa kuuziana umeme ambapo kwa sasa kiwango kinachozalishwa ni Megawatt 189.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa TPDC na TANESCO wameanza majadiliano na Songas kuhusu mikataba hiyo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa makubaliano ambayo yanazingatia maslahi ya pande zote mbili. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-

Je, ni tafiti ngapi za mafuta zimefanyika nchini na yapi matokeo ya tafiti hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, Kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni za Kimataifa za Nishati imeendelea na tafiti za mafuta na gesi nchini kwa maeneo ya baharini na nchi kavu ambapo hadi kufikia mwezi Januari, 2024, jumla ya tafiti 84 zimefanyika.

Mheshimiwa Spika, kupitia tafiti ambazo zimeshafanyika, tumeweza kugundua uwepo wa gesi asilia tu. Hata hivyo, TPDC inaendelea na utafutaji wa mafuta katika maeneo ambayo yana viashiria vya uwepo wa mafuta. Maeneo hayo yanajumuisha bonde la Eyasi Wembere, Ziwa Tanganyika na bonde la Kilosa-Kilombero, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka pipes za gesi Jijini Dar es Salaam kila nyumba ili wananchi wapikie nishati nafuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imeshasambaza miundombinu ya gesi asilia katika nyumba 880 katika Jiji la Dar es Salaam. Pia imejenga bomba la gesi (pipe) lenye urefu wa kilomita 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach kupitia barabara ya Bagamoyo na tayari viwanda viwili na hoteli sita zimeshaunganishwa na bomba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wananchi wengi Jijini Dar es Salaam wanatumia gesi asilia, TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya TAQA Dalbit inafanya utafiti za mahitaji ya gesi asilia kwa njia za kusambazia utakaokamilika Julai, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti huu utaonesha namna bora ya kufikisha mabomba kwenye maeneo yenye changamoto na utabainisha maeneo gani yanayoweza kupelekewa mabomba na maeneo gani hayawezi kupelekewa mabomba ambapo njia nyingine zitatumika kuhakikisha gesi inawafikia wananchi. Ahsante
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaajiri Madereva na Mafundi ambao wamekuwa vibarua wa muda mrefu TANESCO?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekuwa likiajiri watumishi wa kada mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya kiuendeshaji na uwezo wa kibajeti kwa mwaka husika. Katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka 2024/2025 pamoja na mambo mengine, shirika limetenga fedha kwa ajili ya nafasi 430 za ajira mpya kwa mchanganuo ufuatao:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wahandisi 67, fundi sanifu 135, fundi mchundo 205 na madereva 23. Aidha, ujazaji wa nafasi hizi utazingatia sheria na taratibu katika utumishi wa umma. Ahsante. (Makofi)
MH. ALLY J. MAKOA aliuliza:-

Je, lini umeme wa REA utapelekwa Mitaa ya Chemchem, Tampori, Kwamtwara, Guluma, Mongoroma, Chandimo, Chang’ombe na Tura?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imeendelea kutekeleza kazi ya kusambaza umeme katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mitaa ambayo ipo katika mamlaka za miji na miji midogo yenye hadhi sawa na vijiji. Kwa kuwa Jimbo la Kondoa Mjini lipo katika mamlaka ya mji, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, REA itapeleka umeme katika mitaa 15 ambayo imefikiwa na miundombinu ya msongo wa kati, ikiwemo Mitaa ya Chemchem, Tumbelo na Chang’ombe. Aidha Mitaa ya Tura na Tumbelo imepatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi Mbili (A). Serikali kupitia REA itaendelea kuratibu kazi ya kusambaza umeme katika vitongoji na mitaa ambayo haina umeme kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkuu Tabora – Mpanda utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, Katavi lengo likiwa ni kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 116. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Septemba, 2022 na umefikia 58%, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya upya tathimini ya maeneo kwenye Jimbo la Mbulu Mjini ambayo yalirukwa na Mradi wa REA I na II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu Mjini lina jumla ya vijiji 34, kati ya hivyo, vijiji 31 vimepatiwa umeme na vijiji vitatu vilivyosalia yaani Kwam, Aicho na Tsawa vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa II ambapo kazi imeshaanza na inatarajia kukamilika tarehe 30 Juni, 2024. Aidha, Jimbo la Mbulu Mjini lina mitaa 58 ambapo mitaa 46 imepatiwa umeme na mitaa 12 haina umeme. Kutokana na tathmini iliyofanywa na REA, mitaa 12 iliyosalia itapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa kupeleka umeme vitongojini ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA kwenye vijiji 20 vilivyobaki – Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mkalama lina vijiji 70 na vyote vimepatiwa umeme, vikiwemo vijiji 25 vilivyokuwa katika Mradi wa Kusambaza Umeme, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, uliotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Aidha, Jimbo hilo lina vitongoji 388 ambapo vitongoji 192 vimepatiwa umeme na vitongoji 196 bado havijapatiwa umeme. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia REA imetenga fedha za kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo ikiwemo Jimbo la Mkalama. Kwa sasa, REA inakamilisha taratibu za kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza mradi huu. Vitongoji vitakavyobakia vitapatiwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha zoezi la kupeleka umeme katika Shule zote na Taasisi za Dini katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma una vijiji 307 ambapo vijiji 257 vimepatiwa umeme na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 50 vilivyosalia inaendelea kupitia Mkandarasi aitwaye State Grid Electrical and Technical Works Limited anayetekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili. Wakati wa uunganishaji wa wateja katika miradi, wakala hutoa kipaumbele kwa taasisi za umma zikiwemo shule na taasisi za dini. Serikali kupitia Wakala, inaendelea kuratibu upatikanaji wa umeme katika taasisi za umma vijijini, hususan Shule na Taasisi za Dini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakuja na mkakati wa kutumia gesi asilia kuendesha magari nchini ili kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaanza programu mbalimbali za matumizi ya gesi iliyogandamizwa (CNG) kwenye magari. Mpaka sasa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kufungua vituo vitano na inatarajia kufungua vituo vingine vitatu ifikapo mwezi Desemba, 2024. Aidha, jumla ya vituo 16 (vituo mama viwili na vituo vidogo 14) vikijumuisha vituo vinavyohamishika vinatarajiwa kufunguliwa ifikapo mwezi Desemba, 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza upatikanaji wa gesi asilia, mwaka 2022 Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lilifunga seti tatu za compressor zilizoweza kuongeza pressure ya futi za ujazo milioni 20. Kwa sasa TPDC imeanza utaratibu wa kumpata mzabuni kwa ajili ya kufunga mitambo ya kuongeza mgandamizo wa gesi yenye futi za ujazo milioni 20 kwenye kitalu cha uzalishaji Songosongo. Kazi hiyo inatarajia kukamilika mwezi Machi, 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine ili kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia gesi asilia, Serikali inaendelea kutoa msamaha wa kodi kwenye mitungi ya kuhifadhi gesi iliyoshindiliwa kwenye magari na kupunguza ushuru wa magari yanayotumia gesi asilia. Tunaamini mikakati yote hii itachangia kuongeza idadi ya magari yanayotumia gesi nchini itakayopelekea kupunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi na mwisho kuokoa fedha za kigeni, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka transformer kwenye Vijiji vya Mpindo, Kata ya Bulyaga na Isumba, Kata ya Kinyara ili wananchi wanufaike na Mradi wa REA III Awamu ya II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unalenga kupeleka umeme katika vijiji 31 katika Jimbo la Rungwe. Hadi sasa, jumla ya vijiji 30 vimeunganishwa na umeme na kijiji kimoja kilichobaki ambacho kinaitwa Kyobo Juu kilichopo Kata ya Ikuti kazi inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Mpindo na Isumba vilivyopo Kata ya Bulyaga na Kinyara tayari vimeunganishiwa umeme na tayari transformer imefungwa tangu mwezi Mei, 2024. Kwa sasa kazi inayoendelea ni kuunganisha wateja wa awali katika vijiji hivyo ambapo jumla ya wateja 43 kati ya 44 tayari wameunganishiwa umeme, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza vituo vingi vya nishati ya gesi ya magari nchini baada ya Wananchi kuhamasika kutumia nishati hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa kuna vituo vitano vya CNG vinavyofanya kazi katika Mikoa ya Dar es Salaam (Ubungo Maziwa, TAZARA na Uwanja wa Ndege), Pwani (Mkuranga) na Mtwara (Dangote). Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia TPDC inajenga vituo viwili vya CNG katika maeneo ya Dar es Salaam (UDSM na Hospitali ya Taifa Muhimbili) na Pwani kituo kimoja (Kairuki Pharmaceuticals, Kibaha Zegereni).

Mheshimiwa Spika, aidha, TPDC inaendelea na Ununuzi wa Vituo Vidogo vya kujaza CNG kwenye magari vinavyohamishika (Mobile CNG Filling Stations) ambavyo vitasimikwa katika maeneo ya Dar es Salaam vitatu; Morogoro kimoja na Dodoma viwili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta binafsi, Kampuni ya TAQA-Dalbit inaendelea na Ujenzi wa Kituo cha CNG katika Mkoa wa Dar es Salaam (barabara ya Sam Nujoma) eneo la Posta. Pia Kampuni ya Energo inaendelea na ujenzi wa kituo cha CNG eneo la Mikocheni – Dar es Salaam na Kampuni ya BQ inaendelea na ujenzi wa kituo cha CNG katika eneo la Goba – Dar es Salaam, ahsante.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza vituo vingi vya nishati ya gesi ya magari nchini baada ya Wananchi kuhamasika kutumia nishati hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa kuna vituo vitano vya CNG vinavyofanya kazi katika Mikoa ya Dar es Salaam (Ubungo Maziwa, TAZARA na Uwanja wa Ndege), Pwani (Mkuranga) na Mtwara (Dangote). Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia TPDC inajenga vituo viwili vya CNG katika maeneo ya Dar es Salaam (UDSM na Hospitali ya Taifa Muhimbili) na Pwani kituo kimoja (Kairuki Pharmaceuticals, Kibaha Zegereni).

Mheshimiwa Spika, aidha, TPDC inaendelea na Ununuzi wa Vituo Vidogo vya kujaza CNG kwenye magari vinavyohamishika (Mobile CNG Filling Stations) ambavyo vitasimikwa katika maeneo ya Dar es Salaam vitatu; Morogoro kimoja na Dodoma viwili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta binafsi, Kampuni ya TAQA-Dalbit inaendelea na Ujenzi wa Kituo cha CNG katika Mkoa wa Dar es Salaam (barabara ya Sam Nujoma) eneo la Posta. Pia Kampuni ya Energo inaendelea na ujenzi wa kituo cha CNG eneo la Mikocheni – Dar es Salaam na Kampuni ya BQ inaendelea na ujenzi wa kituo cha CNG katika eneo la Goba – Dar es Salaam, ahsante.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:-

Je, upi mkakati wa kuondoa kero ya kutokuwa na umeme wa uhakika na wa gharama kubwa kwenye Visiwa vya Ukara na Ilugwa – Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya kutokuwa na umeme wa uhakika na kupunguza gharama ya umeme katika Visiwa vya Ukara na Ilugwa, Serikali kupitia Mradi wa Gridi Imara unaotekelezwa na TANESCO imeanza kujenga njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 132 pamoja na kujenga kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye mashineumba mbili zenye uwezo wa MVA 120 katika eneo la Nansio Ukerewe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa kituo hicho, visiwa vya jirani kikiwemo Kisiwa cha Ukara vitaungwa na umeme wa Gridi ya Taifa. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutoa ruzuku kwa wazalishaji binafsi wa umeme wanaohudumia visiwa hivyo ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji. Kupitia ruzuku hiyo wazalishaji hao wataweza kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika visiwa hivyo na kuweza kupunguza bei ya kuuza umeme kwa wananchi wanaowahudumia, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, Serikali ina mipango gani wa kuharakisha Miradi ya LNG nchini ili kuchochea uchumi na kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Kampuni za Nishati za Kimataifa (International Energy Companies - IEC’s) kwa ajili ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG). Aidha, Serikali inaendelea na kazi za awali ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa msingi wa kimazingira na kijamii, uelimishaji kwa wananchi juu ya umuhimu na manufaa ya mradi kupitia uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani. Ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi 74 wa Kijiji cha Iseni, Kata ya Usagara, Misungwi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO imekamilisha zoezi la uthamini kwa ajili ya kutwaa eneo la Kituo cha kupoza umeme katika Kata ya Usagara ambapo wananchi 74 watalipwa jumla ya shilingi bilioni 1.2 kama fidia. Fidia hii inategemea kulipwa kuanzia Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025. Ahsante.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaunganisha Mkoa wa Kagera na Gridi ya Taifa ili kuondoa adha ya kukatika umeme mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya za Mkoa wa Kagera zilizounganishwa na Gridi ya Taifa ni Biharamulo na Ngara na katika Wilaya zilizobaki zinaendelea kupata umeme kutoka Nchi ya Uganda. Wilaya hizi zilizosalia zinategemewa kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa mara baada ya kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme ya Msongo wa Kilovolti 220 kutoka Benako hadi Kyaka ambapo Mtaalam Mshauri anaendelea na kazi ya kuandaa nyaraka kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi ambaye anatarajiwa kupatikana mwezi Desemba, 2024. Ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST K.n.y. MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, lini Mkoa wa Mtwara utaunganishwa umeme kwenye Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara utaunganishwa katika Gridi ya Taifa na kuufanya kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi. Mradi huu upo katika hatua za utekelezaji na unatarajiwa kukamilika katika Mwaka wa Fedha wa 2025/2026. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza changamoto ya umeme Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya umeme Wilayani Nkasi inatokana na Mkoa wa Rukwa, ikiwemo Wilaya ya Nkansi, kutokuwa kwenye Grid ya Taifa ambapo mara nyingi inapata umeme mdogo ukilinganisha na mahitaji. Ili kuondokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 wa Tanzania – Zambia Interconnector (TAZA) kutoka Iringa mpaka Rukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utaunganisha Mkoa wa Rukwa, ikiwemo Wilaya ya Nkansi, na Gridi ya Taifa na hivyo kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha kutoka kwenye Gridi. Aidha, kitajengwa kituo cha Kupoza Umeme cha Nkasi, ambacho kitasaidia kupoza umeme unaotoka Sumbawanga pamoja na kuweka feeder tatu za kulisha umeme Wilayani Nkasi. Feeder hizi zitasaidia ufuatiliaji hasa kunapokua na tatizo la umeme ukilinganisha na hali ilivyo sasa. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa nguzo za kilometa 2 katika Vijiji ambavyo REA III Mzunguko wa Pili unatekelezwa - Newala Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia REA, inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa R3R2 ambapo kwa upande wa Newala Vijijini inatekeleza katika vijiji 76 na imefanikiwa kuwasha umeme katika vijiji vyote 76 kwa umbali wa kilomita moja. Aidha, kwa nyongeza ya umbali wa kilometa mbili, REA kupitia mkandarasi aitwaye Central Electrical International Limited, anaendelea na kazi na amefanikiwa kufikisha umeme kwenye vijiji 32 kati ya vijiji 76. Vijiji vilivyosalia vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni, ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA K.n.y. MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO aliuliza:-

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu kutokuwepo uwiano katika bei ya kuunganisha umeme nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kutokuwepo kwa uwiano katika bei ya kuunganisha umeme nchini hasa katika maeneo ya mijini kunatokana na umbali alipo mteja kutoka sehemu unapochukuliwa umeme na aina ya njia ya umeme iliyoombwa na mteja (Single Phase/Three Phase), gharama hizi anazotozwa mteja ni zile zilizoidhinishwa na EWURA kupitia Tangazo la Serikali Na. 1020 la Mwaka 2020. Aidha, kwa upande wa vijijini, wateja wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya shillingi 27,000 tu, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -

Je, Serikali ina mipango gani wa kuharakisha Miradi ya LNG nchini ili kuchochea uchumi na kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Kampuni za Nishati za Kimataifa (International Energy Companies - IEC’s) kwa ajili ya Utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG). Aidha, Serikali inaendelea na kazi za awali ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti wa msingi wa kimazingira na kijamii, uelimishaji kwa wananchi juu ya umuhimu na manufaa ya mradi kupitia uhamasishaji wa matumizi ya gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:-

Je, lini changamoto za bei na mgao wa umeme Kata za Mawengi, Lubonde, Lugarawa, Lupanga, Mlangali, Madilu, Milo na Mawengi zitamalizika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mawengi, Lubonde, Lugarawa, Lupanga, Mlangali, Madilu, Milo na Mawengi Wilayani Ludewa zimekuwa zikipata umeme kutoka kwa wawekezaji binafsi (JUWUMA na MADOPE HCL). Hata hivyo, Serikali na wawekezaji hao wamefika makubaliano ya kisheria ili miundombinu ya usambazaji umeme katika kata hizo ikabidhiwe TANESCO ambapo kwa sasa wapo kwenye hatua ya uwekaji saini makubaliano hayo.

Mheshimiwa Spika, hatua hii, pamoja na hatua zote za makabidhiano zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2024. Baada ya hatua hii kukamilika, TANESCO watabadilisha mita za umeme ili ziendane na mifumo ya TANESCO ili kuanza kutumia umeme wa gridi. Aidha, kuhusu ujenzi wa line ya kuleta umeme kwa ajili ya kuziunganisha kata hizi na umeme wa gridi, mkandarasi aitwae Ok Electrical ameshafanya upimaji na usanifu wa kina na sasa yupo kwenye hatua ya kuagiza vifaa. Aidha, mkandarasi huyu ataanza kusimika nguzo za kujenga line ya umeme mwanzoni mwa mwezi wa Julai, 2024.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa Umeme wa REA katika Kata na Vijiji 23 vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mbulu Vijijini lina jumla vijiji 76 ambapo kati ya hivyo, vijiji 70 vimekwishapatiwa umeme kupitia miradi iliyotekelezwa na REA. Kazi ya ujenzi wa njia za kusambaza umeme katika vijiji sita vya Maheri, Gembakw, Endanyawish, Domanga, Umbul na Gidaludagau, vilivyosalia zinaendelea kwa sasa, ambapo mkandarasi anaendelea kuvuta waya na kuweka transfoma, ili aweze kuwasha umeme. Tunatarajia vijiji hivi kuwashwa umeme hivi karibuni. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, lini Mkataba kati ya Tanzania na Wawekezaji wa Gesi Asilia wenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 70 utaletwa Bungeni kwa ajili ya kuridhiwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Kampuni za Nishati za Kimataifa (International Energy Companies) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG). Kwa kuwa majadiliano bado yanaendelea, yakikamilika tutaendelea na hatua inayofuata. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu ili kupisha ujenzi wa Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Nanyumbu wananchi 689 wanapisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi. Taratibu za kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi zinaendelea ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.95 zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi hao. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hao ambapo fedha zitakapopatikana watalipwa stahiki zao kwa wakati, ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka umeme vitongoji visivyokuwa na umeme Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuunganisha vitongoji ambavyo havina umeme ambapo vitongoji 258 kati ya 515 vya Jimbo la Bukoba Vijijjini vimefikishiwa umeme. Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 27 ambavyo havina umeme katika Jimbo la Bukoba Vijijini inaendelea kupitia Miradi ya Ujazilizi 2B na mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji Awamu ya Pili A (HEP IIA). Serikali itaendelea kupeleka umeme katika vitongoji vya Jimbo la Bukoba Vijijini kupitia miradi inayotarajiwa kufanyika mbeleni, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Meatu inapata umeme kutokea Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli kilichopo Mkoani Shinyanga umbali wa kilomita 135. Kukatika kwa umeme Wilayani Meatu kunatokana na umbali mrefu wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kufungwa vidhibiti umeme katika njia ya awali, kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkalama Mkoani Singida hadi Bukundi Wilayani Meatu na kuendelea na zoezi la kubadilisha nguzo zilizochakaa kwa kuweka nguzo za zege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme katika eneo la Imalilo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambapo itajengwa line ya umeme kutokea kwenye kituo hicho hadi Meatu. Jitihada hizi zimepunguza changamoto ya kukatika umeme kwa kiasi kikubwa sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini mradi wa umeme katika eneo la Kitume Kata ya Makurunge - Bagamoyo utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini yaani REA imeendelea kutekeleza miradi ya kupeleka umeme katika maeneo ya Bagamoyo ambapo katika Kata ya Makurunge eneo la Kitume, REA inatekeleza mradi uitwao Electrification of Small-Scale Mining, Industries and Agricultural Areas in Mainland Tanzania kupitia mkandarasi aitwae M/s Dieynem Company Limited.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ulioanza mwezi Machi 2023, umefikia asilimia 57 ambapo kwa sasa mkandarasi amekwisha simika nguzo kwa umbali wa kilometa 9. Mkandarasi anaendelea na kazi iliyobaki baada ya kusimama kutokana na maji ya mvua kujaa katika eneo kubwa ambalo mkandarasi anafanyia kazi. Mradi unategemea kukamilika mwishoni mwezi Desemba, 2024. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Biharamulo kwa kukamilisha sub-station ya Nyakanazi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Nyakanazi mwezi Desemba, 2023. Aidha, kukamilika kwa kituo hicho kumeenda sambamba na ufungaji wa circuit breakers kwenye laini ndefu iliyokuwa inapeleka umeme katika Wilaya za Bukombe, Mbogwe, Biharamulo na Chato hii imepelekea kutenganisha matumizi ya umeme kwenye wilaya hizo na kwa sasa kila wilaya inajitegemea hivyo kupunguza kukatika kwa umeme ndani ya Wilaya ya Biharamulo. TANESCO inaendelea na matengenezo ya kuimarisha miundombinu ya kusafirishia na kusambaza umeme wilayani humo ili kuwe na umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA K.n.y. MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme wa REA kwenye Vitongoji vya Jimbo la Lupembe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Lupembe lina vitongoji 227 ambapo vitongoji 118 vimekwishapatiwa umeme na vitongoji 109 bado havina umeme. Hata hivyo, vitongoji 19 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Ujazilizi IIB ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu. Vilevile vitongoji 15 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kila Jimbo, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi punde. Hivyo, vitasalia vitongoji 75 ambavyo vitapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa “Hamlet Electrification Project” ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Substation ya umeme katika eneo la Dumila – Kilosa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila yenye urefu wa kilometa 66 na ujenzi wa kituo cha kupoza Umeme katika eneo la Magole – Dumila kupitia mpango wa Gridi Imara awamu ya pili unaotarajia kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwaka 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizofanyika katika hatua za awali za mradi huu ni kufanya upembuzi yakinifu na taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu zinaendelea. Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha eneo la Dumila na maeneo jirani kuwa na umeme wa uhakika na gharama za mradi ni takribani dola za Marekani milioni 39, ahsante
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kupitia upya Mkataba wa REA ili kuifanya REA iwe na jukumu la kufikisha umeme kwenye vituo vya huduma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kupeleka umeme vijijini ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba, 2024 takribani 99% ya vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme. Katika utekelezaji wa miradi hiyo, vipaumbele hutolewa katika taasisi zinazotoa huduma kwa jamii zikiwemo shule, vituo vya afya, zahanati, pampu za maji na taasisi za dini ili kuboresha utolewaji wa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia mwezi Septemba, 2024 taasisi za kijamii zilizopatiwa umeme kupitia REA, taasisi za elimu ni 12,905, taasisi za afya ni 6,768, pampu za maji ni 5,872, nyumba za ibada ni 8,822 na maeneo ya biashara ni 29,294. Serikali itaendelea kuisimamia REA ili kuhakikisha inatoa kipaumbile kwenye upelekaji wa umeme kwenye taasisi za umma pale inapokuwa imekamilisha miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kakozi, Tunduma utaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa TAZA unaotekelezwa na TANESCO ipo katika hatua za awali za ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Nkangamo kilichopo takribani kilometa 28 kutoka Kijiji cha Kakozi. Ujenzi wa Kituo hiki unatarajia kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa mkataba kati ya TANESCO na mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari umeshasainiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa Kituo hicho kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi, ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia ya umeme ya msongo mkuu Tabora – Mpanda utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, Katavi lengo likiwa ni kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 116. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Septemba, 2022 na umefikia 58%, ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha Mradi wa Umeme Kakono – Misenyi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la tathmini ya fidia kwa wananchi wanaopisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa kilovoti 220 kutoka Kakono – Kyaka umekamilika na gharama za fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huu ni fedha za Kitanzania shillingi billioni 1.543. Malipo haya yanategemewa kuanza kulipwa hivi karibuni, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza mgao wa umeme unaokatika kila Jumanne na Alhamisi katika Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukatika kwa umeme katika Jimbo la Kilombero kulisababishwa na ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kidatu ambapo TANESCO ilikuwa na zoezi la kuhamisha nguzo za umeme zilizokuwa ndani ya barabara. Lengo lilikuwa kuruhusu ujenzi wa barabara kufanyika na zoezi hilo kwa sasa limekamilika. Aidha, kukamilika kwa Kituo cha Kupooza Umeme cha Ifakara kumepelekea kuimarika kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Jimbo la Kilombero, ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-

Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa ununuzi wa umeme kati ya TANESCO na SONGAS unafikia ukomo wake tarehe 31 Julai, 2024. Kwa sasa, Serikali imeunda Timu ya Wataalam (Government Negociation Team - GNT) iliyoanza majadiliano mwezi Aprili, 2023 na inatarajia kukamilisha majadiliano haya kabla ya mkataba kuisha. Serikali itahakikisha maslahi ya Taifa yanazingatiwa kabla ya makubaliano yatakayofuata. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Je, lini Serikali itarejesha gharama za kuunganishiwa umeme kuwa 177,000?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimwa Spika, kulingana na bei za umeme zilizopitishwa na EWURA, gharama za kuunganisha umeme wa njia moja katika maeneo ya vijijini ni shilingi 27,000 na mijini shilingi 320,960. Kwa kipindi cha nyuma, kwa miradi ya vijijini (REA) ilikuwa inatoza shilingi 27,000 na TANESCO shilingi 177,000.

Mheshimiwa Spika, kutokana na malalamiko ya wananchi ya utofauti wa bei kati ya REA na TANESCO ya kuunganisha umeme vijijini, Serikali iliamuru TANESCO kushusha bei ya kuunganisha umeme vijijini na kuwa 27,000 kama REA na tofauti ililipwa na Serikali kama ruzuku kwa TANESCO. Kwa hali hiyo, bei ya shilingi 177,000 iliyokuwa inatozwa na TANESCO vijijini, ilifutwa na kuwa 27,000 kwa vijijini kama ilivyo sasa, ahsante.