Supplementary Questions from Hon. Judith Salvio Kapinga (23 total)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini napenda kuwashukuru kwa kuongeza rasilimali fedha katika miradi ya maendeleo ya Wizara. Nina swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha katika Bunge la Bajeti la 2019/2020 ilitoa maelekezo kwa Bodi ya Mikopo kuangalia uwezekano wa kufanyia kazi suala hili. Je, Wizara haioni umuhimu wa kufanyia kazi mapendekezo haya ya Wizara ya Fedha ili shughuli hii ya kuendeleza mitaji watu kama Wizara inavyosema iweze kufanyiwa kazi vizuri kwa kuitenganisha na Fungu 46? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ilikuwa ni mapendekezo na yalipendekezwa na Wizara ya Fedha na kwa vile yalikuwa ni mapendekezo ambayo yaliletwa kwenye Wizara yetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa mapendekezo hayo tutaendelea kuyafanyia kazi na pale muda muafaka utakapofika tutawasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Wilaya ya Mbinga ni mojawapo ya wilaya zinalima zao la kahawa kwa wingi lakini Vyama vya Ushirika vimekuwa vikichelewesha malipo na hivyo wakulima kushindwa kununua pembejeo za kuhudumia mazao yao kwa wakati.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika ili wananchi wa Wilaya ya Mbinga waweze kulipwa fedha kwa wakati na hivyo kuwawezesha kununua pembejeo za kuhudumia zao lao kahawa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kwasababu mfumo wa ulipaji siku zote umekuwa ni kwamba baada ya mnada fedha zinalipwa kwenye Chama Kikuu cha Ushirika, Chama Kikuu cha Ushirika kina hamishia fedha katika Chama cha Msingi. Kwa hiyo tumefanya kikao mwezi Aprili na Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya Wilaya ya Mbinga, utaratibu tunaoelekea sasa hivi kuutekeleza katika vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika ni kwamba mnada unapoisha mnunuzi anatakiwa alipe malipo ndani ya saa 48 na malipo yale yatakwenda moja kwa moja kwa mkulima hayatopitia kwenye ukiritimba wa kwenda kwenye chama kikuu chama kikuu kwenda kwenda kwenye chama cha msingi. Kwa hiyo nimuahidi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine tuna-perfect system ya kulipa baada yam nada malipo yaende moja kwa moja kwa mkulima badala ya kupitia kwenye vyama kwasababu huko kunaleta ukiritimba na kuchelewesha malipo.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba Sera yetu ya Sayansi na Teknolojia ni ya muda mrefu, ya miaka 25 nyuma, lakini vilevile kutokana na suala kwamba mapitio ya sera hii ili yaweze kuleta tija kwenye ubunifu yamekuwa yakichukua muda mrefu, tangu 2012, jambo linalosababisha programu za ubunifu chini ya COSTECH kutokutengewa fungu na kutegemea zaidi ufadhili na hivyo kukosesha vijana fursa nyingi zinazotokana na ubunifu: Je, Serikali haiwezi kutuambia ukomo wa muda wa mapitio haya ya sera ya kwamba yatakamilika lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu tumeambiwa maboresho yamekuwa yanafanyika toka 2012 lakini hadi leo hayajafanyiwa kazi. Tunaomba Wizara ituambie ukomo wa muda wa kufanyia maboresho ili programu za ubunifu ziweze kuwa na tija kwa vijana wa Tanzania. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Wizara imekuwa ikitenga fedha katika kila bajeti kwa lengo la kuhakikisha kwamba eneo hili la ubunifu linafanyiwa kazi sawa sawa. Nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara imetengeneza mwongozo wa mwaka 2018. Vilevile mwongozo huu tunaendelea kuuboresha mwaka huu, tena tunaendelea kuupitia upya ili kuweka mwongozo huu sawa sawa, nimtoe wasiwasi.
Mheshimiwa Spika, pia anataka kujua kwamba ni lini Serikali itakamilisha utungaji huu au mapitio haya ya sera? Ndani ya mwaka huu wa fedha tutalifanya hilo na kuhakikisha jambo hili linakaa sawa sawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na kuutangaza Mlima Kilimanjaro ningependa kufahamu, je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza vivutio vidogovidogo ambavyo vipo katika mikoa hasa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga, yenye vivutio vidogo vingi vya kihistoria vyenye kuvutia ili kupata watalii na kuongeza mapato ya ndani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na vivutio vidogovidogo ambavyo kwa nia moja au nyingine Serikali ilichelewa kuviibua, lakini Wizara ina mkakati wa kuhakikisha inaibua na kuvitangaza vivutio hivi katika kila mkoa, wilaya na kata.
Mheshimiwa Spika, vivutio vingi vidogovidogo havina GN, hivyo tumeendelea kuelimisha wananchi, kuelimisha Serikali za Vijiji, kata na halmashauri kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yanasimamiwa na halmashauri ama vijiji wayaibue na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itatoa wataalam wa kuweza kushauri na kutoa usaidizi wa kuhakikisha kwamba haya maeneo yanapata GN na kuyatangaza na wale watalii waweze kufika katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, moja, je, ni bunifu ngapi zimeweza kubiasharishwa kutokana na kupata support moja kwa moja na Serikali kupitia COSTECH?
Mheshimiwa Spika, lakini mbili, mwaka jana Serikali mlituahidi ikifika Disemba, 2021 tutaletewa Sera kuhusiana na sayansi, teknolojia na ubunifu. Sasa ningependa kupata commitment ya Serikali kwa sababu mwaka jana halikufanyika; sasa je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha katika mwaka huu Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu mpya inaletwa kwa sababu tuliyonayo ni ya mwaka 1996 na inahusisha sayansi na teknolojia peke yake, haina ubunifu na hivyo haiwezi kuwasaidia vijana katika kujipambanua katika masuala ya ajira ya sayansi, teknolojia na ubunifu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba sasa kujibu kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith Kapinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, amezuungumzia suala la bunifu ngapi; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa kati ya bunifu 200 zilizoibuliwa kwenye mashindano yetu ya MAKISATU, jumla ya bunifu 26 zinaendelea kuendelezwa na Serikali, ili kufikia dhamira ya kubiasharishwa ili kuleta tija katika jamii. Kwa hiyo, ni bunifu hizo 26. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili amezungumzia suala la sera, naomba tukiri kwamba kulikuwa na ucheleweshaji kidogo wa sera hii yam waka 1996, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hivi sasa Wizara yangu inaendelea na mapitio ya sera hii na ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023 tutaileta sera hiyo hapa Bungeni kwa ajili ya kupitishwa. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nina swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya ajira kwa vijana yanawekewa msingi na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya 2007. Serikali imekuwa katika mchakato wa kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana 2007 kuanzia mwaka 2016 mpaka 2018. Sasa swali ni: Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha Mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Vijana mwaka 2007 ambayo yameanza kutoka 2016 mpaka 2018 na mpaka leo hajahitimishwa ili mapitio haya yaweze kuratibu ajira kwa vijana na yaweze kuwa na tija zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kuhusiana na nil ini Serikali hasa itakamilisha mchakato huu wa sera. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa masuala ya vijana wakati wote, lakini tayari sisi kwa upande wa Serikali tumeshaenda kwenye hatua mbalimbali; imetoka kwenye hatua ya makundi na wadau mbalimbali kuweza kuwashirikisha ili waweze kutoa michango yao katika sera. Hivi karibuni nadhani kama haitachukua muda sana, ndani ya mwaka huu tutakuwa tumeenda kwenye hatua ya kutoa taarifa rasmi ya namna gani ambavyo tumeenda ukamilishaji wa sera hii ya vijana ya mwaka 2007. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naipongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye sekta ya maji na nina swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ambayo yanachagiza huduma za kijamii kufika viganjani mwa watumiaji. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuweka mpango kazi mahususi, yaani ikifika 2025 mita hizi janja ziweze kutumika na watu majumbani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwamba, tayari Wizara imeshakuwa na huo mpango na tayari umeshaanza kutekelezwa. Baadhi ya sisi hapa ndani pia tutakuwa mashahidi, hata mimi mwenyewe nyumbani kwangu natumia prepaid meter, kwa hiyo, sio kwamba, bado watu hawajaanza kutumia majumbani, tayari tumeanza, lakini kwa kuangalia kama modules za kufanya tu utafiti kuona kwamba, ufanisi wake umekaaje, lakini mpaka kufika hiyo 2025 anayoongelea Mheshimiwa Mbunge, nimtoe hofu jamii kubwa sana itakuwa tayari inatumia prepaid meters.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Watoto wa mitaani hususani watoto wa kiume wamekuwa wakipitia unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia hususan suala la kulawitiwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ikiwemo mabadiliko ya sheria ili kuweka sheria kali na za mfano kwa watu wanaotenda vitendo vya ulawiti kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na ukatili kwa watoto ambao wanalawitiwa. Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na maafisa wetu wa maendeleo na ustawi wa jamii, tunahakikisha kwamba, watuhumiwa wote ambao wanafanya vitendo vya ukatili kwa watoto wetu wanachukuliwa hatua kali pale inapostahiki. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsanta, nashukuru kwa majibu mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Kutokana na upungufu wa vifaa vya makuzi kwa watoto njiti kwenye hospitali zetu; njia kubwa inayotumika kulelea watoto ni kwa kukubambatiwa na mama zao yaani kangaroo style.
Je, Serikali haioni kuchelewesha marekebisho ya sheria kunaendelea kuhatarisha afya na uhai wa watoto hao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, watoto njiti wana haki ya kuishi na kulelewa katika mazingira mazuri kama watoto wengine.
Je, Serikali haina timeframe ya kufanyia marekebisho ili kuhakikisha kwamba uhai wa watoto hao unalindwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imekwishakuanza kuchukua hatua mbalimbali za kufanya maboresho katika sekta ya afya ikiwemo pamoja na ununuzi wa vifaa ambavyo vinawasaidia watoto hawa kuweza kukua.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, katika eneo hilo hilo, maboresho yamekuwa yanafanyika na Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ipo moja ya taasisi katika taasisi nyingi ambazo zinafanya na Serikali, Doris Mollel Foundation pamoja na Vodacom wamekuwa wakifanya kazi hii kwa kushirikiana na Serikali na maeneo mengi tumeona wamefanya kazi kubwa ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu haki ya watoto, tayari Serikali kwa kuona umuhimu wa watoto lakini pia generation tayari ilikwishatunga sheria ya mwaka 2009 sheria ya mtoto ambao inatoa haki, moja ya haki ya msingi ambayo iko kwenye Katiba, haki ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kufanya hivyo Serikali imeendelea kuboresha katika sekta ya afya na kuweza kuhakikisha kwamba katika mazingira haya hata mabadiliko ambayo yanatakiwa kufanyika kwa upande wa Serikali tunayachukua haraka sana na kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, niseme tu katika hatua ya awali, tulikwishakuwinda Dar es Salaam, na tukakutana na taasisi mbalimbali/Asasi za Kiraia ambazo zilikuwa na ajenda hii hii na nilikuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo ya kuweza kuona namna gani tunaweza tukachukua best practice katika nchi yetu kuweza kuona tunawasaidia mama hawa wanaojifungua watoto njiti na kupunguza vifo. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga siyo tu kwamba haina Daktari hata mmoja wa masuala ya viungo, lakini haina Daktari hata mmoja wa macho, meno na radiojia na anesthesia.
Je, Serikali inatuahidi nini katika kupata watalaamu hawa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mbunge nampongeza sana jinsi ambavyo amekuwa na mchango mzuri sana hasa kwenye eneo la lishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuambie majibu ni yale yale kwamba kwenye ajira 32,000 pia tutachukua kwa kushirikiana na yeye lakini tutawauliza watalaam wa eneo husika kwa kuangalia load ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya mtengamao kwenye eneo alilolitaja ili tuweze kuamua mapema na kupeleka mahitaji Utumishi ili kuweza kupata hao watalaamu ambao Mheshimiwa anawataja.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vimekuwa vikiongezeka siku baada ya siku, na utaratibu wa kuendesha mashtaka ya kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto kulingana na Sheria ya Ushahidi (Evidence Act) inampa mtoto mzigo wa kuthibitisha kwamba amebakwa ama amelawitiwa.
Sasa Serikali haioni umuhimu wa kufanyia mapitio Sheria ya Ushahidi ili kuhakikisha mazingira ya kutoa ushahidi katika kesi za ubakaji za watoto pamoja na kesi za ulawiti kwa watoto zinawekewa mazingira zinazolinda haki za Watoto katika kesi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama alivyouliza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba matendo ya ulawiti kwa watoto na ubakaji yamekuwa yakikithiri, lakini halitokani na mapungufu kwenye sheria.
Moja, sheria kwenye makosa ya jinai, uthibitisho au threshold ya kiwango cha uthibitishaji wa makosa ya jinai ni beyond reasonable doubt yaani uthibitishe pasipo kuacha shaka yoyote na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuliona hili na akaunda Tume Maalum ya Haki Jinai ambayo jana ilifanya kazi hiyo, ikiwa mojawapo ni kuhakikisha kwanza vyombo vyetu ambavyo ni functionalize of the law ambapo ni Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Polisi ambao ndio wanawajibu kwanza wa kupokea ripoti ya uhalifu wa utendekaji wa kosa, lakini pili kufanya uchunguzi; na tatu kupeleka sasa kupitia Ofisi ya Solicitor General kupeleka mashtaka mahakamani; na nne kazi ya mahakama kwa maana ya dispensational of justice.
Sasa changamoto ya mambo haya na ukizungumzia na Sheria ya Ushahidi alivyoieleza Mheshimiwa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, sheria hii inaeleza kiwango cha uthibitishaji ni pasipokuacha shaka, kwa sababu ukiacha hivyo athari yake kuna watu wanaweza wakaumizwa kwa sababu ya kesi za kutengeneza. Ushahidi umeonekana unaharibika kwanza katika ngazi ya upelelezi, watoto wanafanyiwa matendo haya na wakati mwingine kunakuwa hakuna ushahidi kwa mfano ujazaji wa PF3, na kesi inavyoenda kule inakuwa imeharibika, lakini eneo lingine la uharibifu wa mashauri haya na kushindwa kuthibitisha ni pale ambapo waendesha mashtaka au wale wazazi kunapokuwa na dhamana, yule mtuhumiwa anatoka nje na anaharibu ushahidi. Wapo ambao ushahidi unaeleza wamekuwa waki bargain na wazazi na wanalipana huko na matokeo yake haendi mahakamani kwenda kutoa ushahidi na mahakamani huwezi ukashinda kesi bila kuwa na ushahidi.
Mheshimiwa mwenyekiti, pili; inatokea katika mazingira ambayo sheria zetu katika usimamizi wake ile enforcement katika dispensational of justice namna ya utoaji wa ushahidi kwa watoto wadogo, nimkumbushe tu Mheshimiwa Judith Kapinga kwamba Sheria ya Ushahidi inatoa usikilizaji wa mashauri haya in camera, kwamba hayasikilizwi kwenye public hearing kwa maana ya aibu na kutunza ile heshima ya mtoto. Kwa hiyo, wale wasaidizi wake wanaweza wakamsikiliza na bado Sheria hiyo ya Ushahidi inatoa haki pia ya kupima uwezo wa mtoto kama ana uwezo wa kutoa ushahidi mahakamani au mtu mwingine aweze kusimamia hilo.
Kwa hiyo, kwenye eneo la Sheria ya Ushahidi bado tutaweza kuona kama kuna mapendekezo ambayo anayaona, nishukuru tu kwamba ameweza kuliona tutayachukua na kuweza kushauriana na mamlaka kuweza kuona maeneo gani ambayo tunafikiri sheria ina mapungufu na kwa kufanya tu hilo hata Wizara ya Maendeleo ya Jamii tayari wamekwishakaa kikao na kuona kama tunaweza tukaondoa dhamana kwenye makosa ya aina hii, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa menyekiti, ahsante kwa swali lanyongeza. Barabara ya kutoka Mapera kuelekea Ilela iliyopo Mbinga Vijijini imeharibika sana na kukwamisha shughuli za maendeleo za wakazi wa Kata za Mapera, Kambarage pamoja na Mikaranga.
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura kwa ajili ya kurekebisha barabara hii ili wakazi wa maeneo haya shughuli zao za maendeleo ziweze kuendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, niagize tu TARURA mkoa wake waende waipitie hii barabra ya Mapera mpaka Ilela waangalie uharibifu ambao upo na watoe tathmini ili tutafute fedha iweze kurekebishwa, ahsante sana.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mapera kilichopo Mbinga Vijijini hakina vifaa tiba vya msingi ikiwemo ultrasound, x-ray na hamna generator hali inayozorotesha upasuaji hasa nyakati za usiku. Fedha ambazo Serikali imetenga, je, na Kituo cha Afya cha Mapera kimetengewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha afya cha Mapera kilichopo katika Halmashauri ya Mbinga ni moja ya vituo ambavyo vimeingia kwenye orodha ya kupelekewa vifaa tiba katika bajeti ya mwaka wa fedha huu 2022/2023, lakini pia tutaendelea kutenga katika bajeti ijayo ya 2023/2024, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini barabara ya kutoka Tanga, Mkumbi, Lugali inayoenda kuunganika na barabara ya Lutoho, Nyasa yenye takribani kilomita 18 itajengwa kwa kiwango cha lami, ikizingatia imekuwa na adha kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyoainisha ni kweli ipo na imeahidiwa na ipo hata kwenye ilani. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naishukuru Serikali kwa mujibu mazuri. Suala la ulinzi wa mlaji kwenye biashara za kimtandao hauwezi kusubiri Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kwa sababu tayari tumechelewa na hivyo madhara makubwa yanaonekana kwa walaji pamoja na wafanyabiashara.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utaratibu wa haraka labda kwa kuweka kanuni ili kuweza kumnufaisha mfanyabiashara huyu na mlaji katika mitandao hii ya kijamii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana kuhusu biashara na hasa biashara mtandaoni. Ni kweli tuna mkakati huo lakini hatuwezi kusubiri mkakati ili tuweze kutelekeza majukumu ya kumlinda mlaji kwa sababu biashara mtandaoni ziandelea. Ndiyo maana sasa tunafanya marekebisho ya Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo pia ina jukumu la kumlinda mlaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi tumeshachukua hatua zaidi, tumeanza kuhamasisha biashara mtandaoni na Waheshimiwa Wabunge watakumbuka mwaka 2021 wakati wa Maonesho ya Saba Saba tumefungua biashara mtandaoni kupitia Shirika letu la Posta; Posta hii ya commerce na mambo mengi yanafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hatuwezi kusubiri mkakati, kuna jitihada nyingi zinaendelea wakati pia na hili la mkakati linaendelea kufanyika ili kuhakikisha tuna uhakika wa kuwalinda walaji wanaotumia biashara mtandaoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Takwimu zinaonesha Watanzania takribani milioni kumi na tano, sawasawa na asilimia 34.2 ni maskini kabisa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa kadri ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais ili akina mama wajawazito waweze kupata huduma ya afya na kupunguza vifo vyao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jibu swali zuri la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, kama mnavyojua Wabunge, tayari kwenye Kamati ya Bunge ya huduma na Maendeleo ya Jamii tumewaelezea na tumewafafanulia hatua tulizozifikia kwenye suala zima la bima ya afya. Na nafikiri Bunge zima limeshaelekeza sisi Wabunge tuna uchaguzi. Kwa sababu ukiangalia mtu anaweza akasubiri akaacha kuweka luku kwenye nyumba yake umeme usiwepo na akasubiri kesho lakini akiugua haiwezi kusubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anaweza akaamka akiwa na afya yake kufuata maji mbali zaidi, lakini afya hawezi hata iliyopo ndani ya nyumba yake hawezi.
Kwa hiyo ni uchaguzi wetu, tutakapoleta Mswada tuamue tunapata vyanzo gani ambavyo vitatusaidia kuweza kuweka kwenye mfuko wa afya; tupate bilioni 149.77 ambazo zitatusaidia na kuwasaidia wale Watanzania wasioweza kujilipia mfuko wa mima ili sasa tufikie hatua ya sisi kuanzisha bima ya afya kwa wote. Ahsante sana Wabunge. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna double standard baadhi ya makampuni yameondoa utaratibu wa kutumia salio la kawaida unapoingia kwenye menu za kibenki na makampuni mengine bado yanataka utumie salio la kawaida badala ya bando ulilonalo kwenye simu. Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha makampuni yote yanatoa huduma hii kwa usawa kwa kuondoa utaratibu wa kutumia salio la kawaida ili Watanzania wote waweze kunufaika na kurahisisha matumizi yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Pamoja na Serikali kusitisha gharama ya ongezeko la bando tokea Oktoba mwaka jana, kwa sasa hivi tatizo kubwa tulilokuwa nalo ni bando za kwenye simu zetu tunazoweka kuisha kwa kasi ya haraka sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha inaweka utaratibu maalum kwa ajili ya ku-regulate matumizi ya kasi za bando kwenye simu kama ilivyo limit kupanda gharama za matumizi ya bando kwenye simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la kibiashara ni kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi. Ni makubaliano kati ya mtoa huduma na benki na pale ambapo watoa huduma wanabadilisha wengine wanakuwa hawatozi ni masuala ya kiushindani ambapo sisi kama Serikali kazi yetu ni kuweka mazingira wezeshi ili ushindani uweze kutokea.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo unapotumia USSD, USSD maana yake si suala la kutuma meseji na kupokea, ni suala ambalo linakuwa linatoa options zingine ambazo mtumiaji anaweza kuona, na kuna hatua nyingi ambazo zinafanyika. Kwa hiyo, suala la kutumia bando ili uweze kukata huduma ya USSD inakuwa ni ngumu ni sawasawa na pale unapojiunga na bando halafu ukajaribu kupiga simu nje ya nchi. Hilo ni jambo haliwezekani, labda kama itawezekana tutakaa na watoa huduma ili tuangalie kama kuna uwezekano wa kuwepo na bando la USSD ili liweze kuhudumia huduma maalum.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili suala la kasi katika matumizi ya bando, kasi ni matumizi ya mtumiaji husika. Kama ana vitu vingi vya ku-download na kuna vitu vingi vya ku- upload matokeo yake ni kwamba kasi ya bando ambalo atakuwa amejiunga litaisha mapema. Kwa hiyo, naendelea kushauri kwamba watumiaji wa bando waweze kuangalia matumizi halisi katika simu zao na pale ambapo wanakuwa hawatumii basi waweze kuzima data ili data isiweze kuisha, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali iliahidi kwamba imetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambayo miundombinu yake imechakaa sana na ni hospitali ya siku nyingi. Je, ni lini ukarabati huo utaanza ili wananchi wa Wilaya ya Mbinga wapate huduma za afya bora na stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya Serikali ya 2023/2024 iliyopitishwa hapa Bungeni wiki iliyopita, Serikali imetenga Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali Kongwe ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mzauri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kuanza ukarabati wa majengo haya ila kwa kuwa yamekaa muda mrefu, nataka kufahamu kama mwaka huu wa fedha unaokuja fedha zimetengwa kwa ajili ya kumaliza ukarabati kwa ajili ya majengo yote yaliyobakia na ukarabati utategemea kumalizika kwa muda gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kwamba Serikali haioni umuhimu wa kujenga mradi kama ule wa Magomeni, Ukonga ili wananchi waweze kupata nyumba na majengo mengine waweze kukodiwa watumishi ikiwemo watumishi wa Magereza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge yote kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo ya Ukonga kota ni majengo yale madogo na ya zamani na mpango wa Serikali kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi maeneo yote ambayo yalikuwa na majengo yale ya zamani yaboreshwe ama yabadilishwe na Ukonga ikiwa ni moja ya eneo ambalo mwezi huu wataalam wamekwenda ku–assess na kupata ukubwa wa eneo halisi ili paweze kubadilishwa na kujenga majengo makubwa ya ghorofa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mpango mzima ni kujenga majengo yanayokwenda juu badala ya kuejenga haya majengo madogo. Kwa hiyo, Ukonga kota ni sehemu mojawapo kama Temeke, Ilala kota, Kinondoni, Ghana Mwanza na hata Arusha. Kwa hiyo, maeneo yote haya tunafanya mabadiliko ya kujenga ghorofa kama ambavyo tumejenga Magomeni kota na tunavyoendelea Temeke, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, ila nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tayari Serikali ina kitengo maalum na tayari inafanya utambuzi na ukusanyaji wa kodi hizi: Je, tangu jitihada hizi zifanyike, mapato yanayotokana na biashara hizi yameongezeka kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Pamoja na mikakati mizuri ambayo Serikali inafanya, bado biashara nyingi za kimtandao hazijafanyiwa utambuzi na hazifanyiwi ukusanyaji ikiwemo biashara ya D & D; Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha mikakati hii ili biashara hizi ziweze kufanyiwa utambuzi wa ukusanyaji mapema ili kuongeza mapato? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza ni kiasi gani, naomba hili nijibu kwa njia ya maandishi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali imeendelea kulipa VAT na kwa taratibu zote na imechukua suala hilo na inaendelea kulifanyia kazi.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naishukuru Serikli kwa kuanza mchakato huu muhimu kwa nchi yetu, hata hivyo nina maswali mawili kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mchakato huu wa kusajili Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC)tumeambiwa uko kwenye mchakato kwa kipindi kirefu sana, takribani miaka thelathini sasa. Serikali sasa inatuambia mchakato utakamilika lini na mkataba kusainiwa ili shirika hili lianze kufanya kazi hapa nchini kwetu?
Swali la pili Serikali imejipanga vipi kulinda maslahi ya Watanzania katika mikataba itakayosainiwa ili kuhakikisha shirika hili la Kimataifa litakapoanzishwa ajira kwa Watanzania zitakuwepo kuliko kuajiri watu wa nje zaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze sana Red Cross Tanzania wamekuwa wakisimamia mchakato huu kwa muda mrefu sana kuweza kuhakikisha hata hatua hii inaweza kufikiwa na wamekuwa wakifanya kazi kubwa, kazi mbalimbali za Kitaifa, sherehe za Kimataifa, wakati wa maafa, pia wamekuwa wadau muhimu sana wa Serikali katika masuala ya maafa kwa hiyo ninawapongeza sana, pili ninawapongeza uongozi ambao umefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo ameeleza kuhusiana na kuchukua muda mrefu, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, tayari itifaki zote zimeshafanyika. Kwanza kuwasiliana na Shirikisho lenyewe; pili, kukutana na wadau na tatu, sasa iko kwenye hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje katika kukamilisha tu itifaki za Serikali na taratibu za ndani ili kuweza kufanikisha jambo hili. Ndiyo maana tukasema kama Serikali kwamba sasa limefikia mwisho. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa hatua za ufuatiliaji.
Mheshimiwa Spika, pili, swali lake la kuhusiana na masilahi, ni kweli kwamba mashirika haya kimataifa yamekuwa yakija kufanya kazi nchini lakini tunaangaliaje ajira za wazawa?
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria hapa ya Mwaka 2005 inayoruhusu uratibu wa ajira za wageni. Imekuwa ni wakati wote, hata kwenye Sheria ya Usajili wa Makampuni Sura Na. 212 inaelekeza namna unaposajiliwa kama kampuni, taasisi au asasi za kiraia, sharti ni kwamba waajiriwe Watanzania. Inapotokea ameajiriwa mgeni ni pale tu ambapo aidha taaluma yake ni maalum sana, au ufahamu au knowledge aliyonayo ni adimu hapa nchini kwamba hatuwezi kumpata Mtanzania mwenye sifa hiyo. Kwa hiyo, nitoe agizo hapa kwa taasisi zote, mashirika ya Kimataifa pamoja na Makampuni ya kiuwekezaji ya nje yaendelee kuzingatia utekelezaji wa Sheria ya Mwaka 2005 ya Kuratibu Ajira za Wageni inayowataka waangalie matakwa ya ajira za Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pia usajili wa IFRC utakuwa chini ya msukumo wa Red Cross Tanzania. Tutawaomba Red Cross nao waendelee kutusaidia kupata taarifa na kuratibu ili ajira za Watanzania zisipotee, ahsante sana.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dunia ya sasa ipo katika mapinduzi ya nne ya viwanda kuelekea mapinduzi ya tano ya viwanda. Je, mitaala inayoboreshwa itaendana na kasi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; programu ya mageuzi ya kiuchumi ambayo imepelekea kuanzishwa kwa takribani programu 300 kwenye vyuo vikuu. Je, ni lini programu hizi zitahuishwa na kuanza kufundishwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya swali la msingi kwamba, sasa tuko katika hatua za mwisho za uboreshaji wa mitaala hii. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la kwanza anazungumza kuhusiana na suala la mitaala namna gani litaweza ku-cope na mapinduzi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala inayoboreshwa inalenga kumpatia mhitimu maarifa, study pamoja na ujuzi utakaomwezesha kukabiliana na mabadiliko ya kisayansi, teknolojia na kiuchumi kwa ujumla. Mitaala hii imesisitiza sana masomo ya TEHAMA pamoja na kompyuta ambayo, tutaanzia katika ngazi ya elimu ya msingi na kwenda katika ngazi zote. Lengo kuu la kufanya maboresho haya ni kujiandaa na mapinduzi haya ya nne pamoja na ya tano ya viwanda ambayo yanahusisha matumizi ya teknolojia pamoja na kompyuta kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaulizia kuhusiana na tunaanza lini? Mradi huu wa Higher Education for Economic Transformation ni mradi wa miaka mitano na utekelezaji wake ulianza tokea mwaka 2021/2022 na tunatarajia kukamilisha 2025/2026. Kwa hiyo, kazi hii imeshaanza, wataalam wetu wameshapata mafunzo kwa ajili ya uboreshaji wa mitaala pamoja na programu hizi. Kazi hii inaendelea na kwa vile ni kazi ya miaka mitano, tutakuwa tunaendelea kuifanya mpaka kipindi hicho chote kitakapokuwa kimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina utaratibu wa kuchapisha sheria na marekebisho yake kwa kuziunganisha pamoja kama ilivyo kwa law reports. Sasa tangu mwaka 2002 mchakato huo ulifanyika tena 2019.
Swali langu, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha utaratibu huu unafanyika mara kwa mara ili kuepusha matumizi ya sheria zilizopitwa na wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, sheria zinaporekebishwa huwekewa RE yaani Revised Edition. Mwaka 2019 siyo sheria zote ziliwekewa Revised Edition. Serikali ina mkakati gani wa kuwekea sheria zote Revised Edition ili kuweza kurahisisha matumizi kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ule mchakato swali lake la kwanza la nyongeza, nipende tu kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeendelea kujaribu kuziweka hizi sheria katika mfumo ambao ameusema, lakini sehemu kubwa sana ni mkwamo wa fedha kwa ajili ya process nzima ya kuzi-¬combine. Lakini haya marekebisho mengine ambayo ameyazungumza, tumechukua wazo lake na kimsingi tutaendelea kufanya michakato mbalimbali kwa ajili ya kuziunganisha. Ahsante.