Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Ummy Hamisi Nderiananga (12 total)

MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutoa mafunzo ya ujasiriliamali kwa Watu Wenye Ulemavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo : -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia bajeti ya kila mwaka wa fedha imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuwezesha mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu waliopo katika ngazi mbalimbali, zikiwemo halmashauri zote nchini. Tumekuwa tukifanya hivi ili kusudi watu wenye ulemavu wanaopewa fedha hizi waweze kuzifanyia kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imekuwa ikiendelea kushirikiana na wadau, na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu kwneye fani mbalimbali lengo la kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kuwaingizia kipato. Kwa mfano, katika mkoa wa Dar es Salaam pekee, kwa mwaka 2019/2020, zaidi ya wajasiriamali wenye ulemavu wapatao 160 walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na uanzishaji wa miradi endelevu. Mafunzo haya yalihusisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Benki Kuu ya Tanzania, mifuko yetu ya hifadhi ya jamii NSSF, Benki ya Exim, Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), na Vyama vya Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, uwezeshaji wa Watu Wenye Ulemavu katika mafunzo ya ujasiriamali umekuwa ukiendelea kufanyika kupitia vyama vyao wakati wa matukio mbalimbali kama maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu lakini vile vile tumekuwa tukiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo mbalimbali kwa mfano kule Mbeya – Kyela tunashirikiana na wenzetu wa trade craft exchange na mashirika mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wanapomaliza vyuo vikuu?

(b) Je, ni kwa nini vijana hao wasitumie vyeti vyao kama dhamana kupata mikopo ili wajishughulishe na shughuli mbalimbali za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, lenye sehemu
(a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wanapomaliza Vyuo Vikuu, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Fursa za Ajira ambao unatoa maelekezo kwa sekta zote za kiuchumi ya namna ya sekta hizo zinavyopaswa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili wawekeze na kuzalisha fursa za ajira za kutosha. Mikakati mingine ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha na kutekeleza programu ya mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu (internship program). Katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya wahitimu 5,975 wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika taasisi mbalimbali za Umma na binafsi ikiwa ni mkakati wa kuondoa kikwazo cha uzoefu kwa vijana wanapotafuta kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeanzisha na kutekeleza programu ya mafunzo ya ufundi na stadi katika fani mbalimbali kwa vijana wakiwemo wahitimu wa elimu ya juu ambapo katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya vijana 28,941 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kupitia mafunzo ya uanagenzi.

Mheshima Naibu Spika, vile vile Serikali imeanzisha na kutekeleza programu ya mafunzo na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio rasmi wa mafunzo kwa lengo la kuwawezesha vijana kuajiriwa na kujiajiri; na pia kujiendeleza kiujuzi katika taasisi mbalimbali za mafunzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeanzisha na kutekeleza Programu ya Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa vijana wakiwemo wahitimu wa elimu ya juu kupitia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali vile vile imeanzisha na kutekeleza programu ya vijana kufanya mafunzo katika nchi ambazo zimepiga hatua katika kilimo ambapo takribani vijana 136 wameweza kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa nchini Israeli. Pia, Serikali imeendelea na mkakati wa pamoja wa ajira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Utumishi na Wizara nyingine na hasa kupitia Miradi ya Maendeleo. Vilevile Serikali imeanza kufanya utafiti kuhusu Hali ya Rasilimali watu Nchini (Manpower Survey) na utafiti wa Hali ya Ajira Nchini (Labour Force Survey).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapokea ushauri Mheshimiwa Mbunge wa kutumia vyeti vya uhitimu mafunzo kama dhamana ya mikopo kwa vijana na kwenda kufanyia kazi. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha huduma ya utoaji mikopo kwa vijana kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. LATIFA K. JUAKALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahamasisha Vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira yatakayoleta tija kwa vijana na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali. Mikakati hiyo ni pamoja na ifuatayo:-

(i) Kutoa mikopo yenye riba nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana, ambapo hadi kufikia Oktoba, 2021 jumla ya vikundi vya vijana 957 vimewezeshwa kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 6.7 ambayo imechochea ufanyaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi;

(ii) Kutoa mikopo isiyo na riba kupitia asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ambapo hadi kufikia Juni, 2021 zaidi ya vikundi vya vijana 15,349 vimewezeshwa kupata mikopo yenye thamani ya Shillingi Bilioni 54.7;

(iii) Tumeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali, ambapo hadi sasa Halmashauri 111 zimetenga maeneo yenye ukubwa wa ekari 217,802 ambayo yamewanufaisha vijana 3,232; na

(iv) Tunaendelea kuendesha programu za mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo za ukuzaji ujuzi, Uanagenzi, Urasimishaji ujuzi pamoja na mafunzo ya kilimo cha kisasa. Kupitia mafunzo hayo, vijana 43,881 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi, Vijana 20,334 wamepata mafunzo ya kurasimisha ujuzi na Vijana 12,580 wamewezeshwa kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mikakati hii vijana wameweza kujipatia ajira pamoja na kujikita kwenye miradi ya uzalishaji mali ambayo imeendelea kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaangalia upya mipaka ya kiutawala katika Jimbo la Makambako?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kesenyenda Sanga Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo yenye dhamana ya kuchunguza mipaka na kuigawa nchi katika majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Katika maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume kwa kuzingatia matakwa ya Katiba itatangaza utaratibu na sifa za kugawa maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge anashauriwa kuwa pindi Tume itakapotoa tangazo la kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala, ashirikiane na Mamlaka za kiutawala katika Wilaya na Mkoa kuandaa na kuwasilisha mapendekezo kwa kuzingatia vigezo vitakavyokuwa vimewekwa na Tume. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, lini Serikali italigawa Jimbo la Kilindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Hivyo, kwa kuzingatia taratibu na vigezo, muda wa kugawa majimbo utakapofika tume itatoa tangazo rasmi kwa wadau wote wa uchaguzi juu ya kuanza kwa mchakato wa ugawaji wa majimbo ili wadau wawasilishe maoni na maombi yao na hivyo kushughulikiwa kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa Kikatiba, ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, ni faida gani ambayo Wafanyakazi wanapata kupitia uwekezaji wa fedha wanazokatwa na Vyama vya Wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ambayo wafanyakazi wanapata kupitia uwekezaji wa fedha wanazokatwa na Vyama vya Wafanyakazi ni pamoja na; Vyama vya Wafanyakazi kusuluhisha migogoro ya kikazi kwa niaba ya wanachama wake, kutoa huduma kwa wanachama kama vile ya utetezi katika Mahakama ya Kazi, na kutoa elimu kuhusu Sera na Sheria za kazi kwa ajili ya maslahi mapana ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama vya Wafanyakazi kupitia fedha wanazokusanya kutokana na ada za wanachama wao huzitumia kutekeleza majukumu ya vyama yaliyowekwa kikatiba na kisheria yanayotokana na uwepo wa vyama mahali pa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo baadhi ya Vyama vya Wafanyakazi ambavyo hutumia ada za uanachama kujenga majengo kwa ajili ya matumizi ya ofisi za vyama, kuwapangisha watu mbalimbali na kutoa huduma kwa wanachama wao. Fedha inayopatikana kutokana na uwekezaji hutumika kuongeza bajeti za Vyama vya Wafanyakazi ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na kisheria kikamilifu, ahsante.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza: -

Je, Wanawake wangapi wamekuwa Wabunge wa Majimbo na Madiwani katika chaguzi tatu mfululizo zilizopita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2020 zilifanyika chaguzi tatu katika ngazi ya Ubunge na Udiwani. Katika chaguzi hizo, jumla ya Wabunge Wanawake 73 walishinda chaguzi hizo na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Majimbo. Aidha, kwa upande wa Madiwani Jumla ya wanawake 654 waliweza kuchaguliwa na hivyo kuwa Madiwani katika Kata husika.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, zipi athari za mvua zilizonyesha Novemba, 2023 na Serikali imejipangaje kuzuia athari hizo kujirudia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohamed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba, 2023 hadi sasa, tumeshuhudia mvua kubwa ambazo zimenyesha katika maeneo mbalimbali nchini. Mvua hizo, zimeleta athari mbalimbali ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya milipuko kwa binadamu ikiwemo kipindupindu, matukio ya radi na matukio ya upepo mkali ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na athari hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na hali ikiwemo kuandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino kwa kipindi cha Septemba, 2023 mpaka Juni, 2024. Vilevile, kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa katika mikoa 18 nchini, kufuatilia mwenendo wa majanga, kutoa tahadhari kwa umma kupitia Kituo chetu cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia utekelezaji wa mikakati na mikataba ya Kikanda na Kimataifa, ikiwemo Mkakati wa Kimataifa wa Sendai wa Upunguzaji wa Athari za Maafa wa Mwaka 2015/2030; na Mkataba wa Makubaliano wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Oparesheni za Dharura cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, yapo madhara ambayo kwa msingi wake wa kuwa majanga ya asili pale yanapotekea hata athari zake hujirudia. Hivyo, Serikali imeendelea kujumuisha athari za majanga hayo katika mpango wa uzuiaji na urejeshaji wa hali pale inapobidi, ahsante.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza: -

Je, vijana wenye ulemavu wamenufaika vipi na mafunzo na mikopo inayotolewa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa mafunzo na mikopo kwa Vijana wenye Ulemavu inatekeleza mikakati na programu jumuishi mbalimbali inayolenga kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu, mafunzo na ujuzi kwa lengo la kuboresha hali zao za maisha na kukuza ushiriki wao katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi cha Mwaka 2022, kiasi cha mikopo ya shilingi bilioni 81.3 zilitolewa kwa watu 640,723 wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu. Mikopo hiyo imewezesha vijana wenye ulemavu kuanzisha au kuendeleza biashara zao na hivyo kupunguza utegemezi na kuwa na uwezo wa kuchangia kwa kiwango kikubwa katika mahitaji yao wenyewe na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, zaidi ya vijana wapatao 2000 wamenufaika na mafunzo yanayotolewa hapa nchini. Vijana hao wamepata mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali kupitia vyuo vya ufundi na marekebisho, vyuo vya VETA na kupitia programu ya ukuzaji ujuzi iliyopo nchini, ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO K.n.y. MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -

Je, lini Serikali italigawa Jimbo la Nachingwea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuchunguza na kugawa mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka kumi baada ya kupata kibali cha Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, katika maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza utaratibu na sifa za kugawa maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi. Hivyo, napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge, kuwa mara Tume itakapotangaza kugawa au kubadili majina ya Majimbo ya Uchaguzi, awasilishe ombi lake la kuligawa Jimbo la Nachingwea kwa kuzingatia utaratibu utakaotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Ahsante.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -

Je, lini zoezi la kuhamia Dodoma litakamilika na Taasisi ngapi zimeshahamia Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la kuhamisha Makao Makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma lilianza rasmi mnamo mwaka 2016. Hadi sasa jumla ya watumishi 25,039 kutoka Serikali Kuu, Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na taasisi 65 wameshahamia Dodoma na wanaendelea kutekeleza majukumu yao wakiwa Makao Makuu ya Nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatarajia kukamilisha mpango wake wa kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma kwa kuzingatia mpango kazi maalum na ujenzi wa awamu ya pili wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi utakaohitimishwa ifikapo mwaka 2025.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, lini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakuwa tayari baada ya makosa ya ukatili wa kijinsia kuongezwa kwenye Sheria za Uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 kinaeleza kuwa, Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya Siasa itaandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi. Aidha, kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 1.2 ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za mwaka 2020, Maadili ya Uchaguzi yatatumika katika Uchaguzi Mkuu na katika chaguzi ndogo. Kwa msingi huo, maadili mapya ya uchaguzi huandaliwa kila mwaka wa Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wakati ukifika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushauriana na vyama vyote vya siasa itaandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.