Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Ummy Hamisi Nderiananga (22 total)

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kutoa maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamii iliyo kuwa inawaona watu wenye ulemavu hawawezi kufanya kazi ikiwemo ujasiriamali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha watu wenye ulemavu nao wajaikwamue kimaisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenda Zanzibar kwenda kuwaona watu wenye ulemavu jinsi wanavyojikita kuhusu suala la ujasiriamali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji. Amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana masuala yetu ya watu wenye ulemavu.

Niseme kwamba suala hili la watu kuwaona watu wenye ulemavu kama wanabaguliwa na hawawezi kufanya shughuli, nataka nimwambie tutaendelea kutoa elimu lakini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tutaendelea kuwasaka wale wote wanaowanyanyapaa na kuwatumikisha watu wenye ulemavu ili kuchukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tutaendelea kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu wao wenyewe waweze kujiamini na waone wana mchango katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari tuambatane naye baada ya kukamilika kwa bajeti hii na twende Zanzibar tukafanye kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia hapo Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kuonesha programu mbalimbali na nyingi ambazo Serikali inaendelea kuzifanya kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Sasa wanasema wakati mwingine kuona ni kuamini. Hebu anieleze sasa: Ni lini Serikali walau itaanzisha hata programu moja katika Jimbo langu ili vijana wangu nao waweze kuona haya mengi ambayo Serikali imeweza kuyazungumza? (Makofi)

Swali la pili; kwa kuwa vijana wanaopata umri wa miaka 18 kwenda juu wapo wengi; na mojawapo ya jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha kwamba vijana wanapata ajira: Je, ni kwa nini sasa Serikali isiwe na ule utaratibu kama iliyokuwa nao wa JKT wa crash programe ya miaka miwili au mitatu huko huko wanajifunza ukakamavu, kilimo, ufugaji wa samaki na mafunzo mbalimbali ili baada ya hapo Serikali iwape mitaji waweze kuendelea na maisha yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge Vedastus Mathayo Manyinyi kwa namna anavyojitolea katika kuhakikisha vijana katika Jimbo lake na nchi yetu wananufaika na progamu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kumhakikishia na kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kupitia bajeti ambayo mmetupitishia ambayo itaenda kutekelezwa kuanzia mwezi wa Saba mwaka huu tutapeleka programu ya greenhouse katika mikoa tisa iliyobakia ikiwemo Mkoa wa Mara na tutajenga greenhouse hizi katika kila Halmashauri. Kwa hiyo na Musoma Mjini ambapo anatoka kaka yangu Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi itapata greenhouse hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile programu hizo za uanagenzi tutafanya na vyuo mbalimbali vilivyopo Mkoa wa Mara ikiwemo Chuo kile cha Lake Victoria na vyuo vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu sana na wenzetu wa JKT. Utakumbuka pia katika wasilisho la bajeti la Wizara ambayo inahusika na masuala haya ya JKT, Waheshimiwa Wabunge tulipokea ushauri wenu kwa kuona namna ambavyo JKT inaweza ikatusaidia katika kuwajenga vijana na kuwaandaa kikamilifu ili waweze kujiajiri na kuajiriwa na hata kuajiri wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya maeneo yanayoweza kuongeza ajira kwa vijana ni eneo la kuongeza thamani kwenye bidhaa. Je, Serikali inamkakati gani wa kuja na programu zinazoweza kuwasaidia vikundi vya vijana vinavyopata mikopo ya halmashauri kuweza kuongeza thamani kwenye bidhaa ambazo inazalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ni kutokana na mabadiliko mbalimbali ikiwemo ya Sayansi na Teknolojia zipo ajira mbalimbali zinazoweza kuzalishwa kutokana na mabadiliko hayo. Je, Serikali inamkakati gani wa kufanya maboresho ya sera ya vijana ili vijana waweze kupata ajira kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea hususani katika Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwanza kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Judith Kapinga amekuwa akifanya kazi kubwa ya kutushauri Serikali katika eneo hili hongera sana Mheshimiwa Judith. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la kwanza anauliza kuhusu kuongeza thamani, Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tunaendelea kuhakikisha kwamba tunawaunganisha vijana na fursa hizi mbalimbali tunashirikiana na wenzetu wa SIDO na UNIDO tuna mfano hai wa vijana wetu wa Kampuni ya JATU wanafanya vizuri kuongeza thamani, mazao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna vijana wa Kiwanda cha Chaki kule Maswa, tuna vijana pia wa Kiwanda cha Mabegi Mwanza na vijana wengine na tunaendelea bado kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaongeza thamani vitu wanavyozalisha badala ya kuuza raw material na tutaendelea kuendelea kutilia mkazo katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anataka kufahamu ni lini tutaleta sera hii; tupo katika hatua nzuri na tayari kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeshakusanya maoni kwa wadau wote wanaohusika na masuala ya vijana na tumemaliza sasa tuna rasimu ya kwanza ambayo inafuata utaratibu wa kiserikali na baadaye tutaendelea kuwafahamisha kwamba tumefika hatua gani, lakini tunaweza kuahidi tu kwamba kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha tutakuwa tayari tuna sera ya vijana. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; hata hivyo, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ni mazuri na kwa kuwa wananchi wa Makambako eneo la kiutawala kama alivyojibu kwenye swali la msingi. Ni lini sasa Serikali pamoja na Tume hiyo Tukishiikiana mimi na Serikali tutakwenda kwenye Tume ili jambo hili liweze kutekelezwa haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Kesenyenda Sanga Mbunge wa Makambako kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majibu yangu niliyoyatoa katika swali la msingi, nimesema kwamba tunaendelea na maandalizi. Na niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sasa tuko katika maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura. Kwa hiyo kipindi kitakapofika Tume itatangaza na Mheshimiwa Deo ataweza kushirikiana na wananchi wenzake katika wilaya na mkoa ili kuleta mapendekezo ambayo wanaona yanafaa kwa ajili ya jambo hilo analoliomba, asante. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, asante sana Halmashauri ya Njombe DC ambayo ni Jimbo la Lupembe lina kata 12; na kata 4 kati ya hizo kata ya Ninga, Ikuna, Kichiwa,

Mtwango na Igongolo ziko halmashauri ya Makambako na Jimbo la Makambako na hii inaleta ugumu sana kwenye utawala wa shughuli za maendeleo.

Je, ni lini Serikali itarudisha kata hizi kwenye Halmashauri ya Njombe DC kwa ajili ya kiutawala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili pia linahusu wenzetu wa upande Ofisi ya Rais-TAMISEMI, na kwa kuwa suala la halmashauri linasimamiwa chini ya Sheria za Serikali ya Mtaa Sura ya 287 na 288 pamoja na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala wa mwaka 2014. Ninaomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge muendelee kufuata utaratibu wa vigezo na masharti ili kusudi kuweza kukamilisha jambo hilo; kwa kuanzia katika Serikali za vijiji kwenda kwenye DCC kwenda kwenye RCC halafu mkoa mama utatuletea sisi mapendekezo. Ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuwa na sisi Jimbo la Namtumbo lina ukubwa wa kilomita za mraba 20,375, na ukienda kwenye kata ya mwisho unatembea kilomita 254; na tumeshakaa vikao vya awali vya wilaya na mkoa ili kuweka mapendekezo ya kuomba jimbo letu ligawiwe.

Je, Serikali wakati ukifika inaweza ikatuweka katika orodha ya kugawanywa jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba yapo majimbo ni makubwa na sisi tunafahamu. Hata hivyo, kama nilivyojibu katika swali la msingi lililoulizwa na Mheshimiwa Deo napenda nimhakikishie kwamba muda utakapofika na Tume itakapotangaza basi na yeye tutamweka kwenye orodha kwa kuzingatia vigezo na masharti, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tu. Lakini pia nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti, hakika uko vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo madogo ya utawala ni tofauti na maeneo makubwa ya utawala. Sasa je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maeneo madogo hayapewi rasilimali nyingi na watumishi wengi kuliko maeneo makubwa ya utawala? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; nini mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba maeneo yote makubwa ambayo yako sawa na Kilindi ambayo yanahitaji kugawanywa yanafanyiwa mkakati wa haraka ili yaweze kugawanywa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Omari Kigua kwa kazi nzuri anazofanya jimboni, lakini pia niendelee kumhakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunatambua uwepo wa maeneo haya makubwa na madogo ya kiutawala. Na kama nilivyojibu katika swali la msingi alilouliza, tutaendelea kufanya kazi kuona namna ambavyo tunaendelea kufikisha huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa ufafanuzi zaidi, vigezo tunavyovizingatia katika nchi za SADC ikiwemo na Tanzania tutaangalia pia ukubwa wa jimbo husika, mipaka ya kiutawala, hali ya kiuchumi na hali ya kijiografia pamoja na suala la idadi ya watu katika eneo husika, pamoja na uwezo pia wa Ukumbi wetu wa Bunge na idadi ya Wabunge wa Viti Maalum; yote hayo tutayaangalia katika mchakato huu alioulizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema pia maeneo makubwa; tunatambua na tunafahamu na nimelijibu swali hili hii ni mara ya pili ndani ya Bunge lako Tukufu. Maeneo haya ambayo ni makubwa tume kama ilivyopewa majukumu na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tutafanyia kazi maeneo hayo na tutaomba tuendelee kupata ushirikiano wa kutosha kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja na wadau wote wa masuala ya uchaguzi, ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Jimbo la Mbeya Mjini ni kubwa sana na lina kata zaidi ya 36 na wapigakura wengi; ni lini Serikali mtaamua kuligawa jimbo jilo ili liweze kumpa urahisi Mbunge husika waweze kugawa namna ya kulitumikia jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, nimesema Serikali tunatambua lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye ni Mheshimiwa Spika wetu, Mheshimiwa Dkt. Tulia, ameshawasilisha suala hili na lipo Mezani. Kwa hiyo, muda utakapofika Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatazama pia Jimbo la Mbeya Mjini, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jimbo la Kishapu lina jumla ya kata 29, lina square kilometers 48,000; lina vijiji 117. Eneo hili kiutawala ni kubwa sana; ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba jimbo hili linagawanywa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA
URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatambua uwepo wa maeneo makubwa, kama alivyosema huku Kishapu kata 26 na vijiji 117. Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao, muda utakapofika tutaangalia vigezo na masharti ili kuona kama jimbo hili linafaa kugawanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa niaba ya Serikali niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wote, kwenye eneo hili yapo majimbo mengi, kwa hiyo tutayafanyia kazi Waheshimiwa Wabunge. Karibu tuungane pamoja na wadau wengine wa Uchaguzi tutoe maoni na nina imani tutafanya vizuri tu, ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tabora Mjini lenye kata
29 na wakazi sasa katika sensa hii nadhani hawatapungua 500,000 kwenye jimbo moja, na tulishawasilisha maombi ya kuligawa jimbo hilo kwa muda mrefu: -

Lini Serikali itaweza kuligawa jimbo hilo ili liweze kuwa na majimbo angalau mawili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA
URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunatambua ukubwa pia wa Jimbo la Tabora Mjini. Lakini vilevile niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na Mheshimiwa Mwakasaka kwamba muda utakapofika, tume tayari tumeanza maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2025, tutashirikiana kwa ukaribu kuona namna ambavyo tunaweza tukagawa majimbo hayo kwa mujibu wa vigezo na masharti. Na niwaambie kwamba tutazingatia pia suala la idadi ya watu, hususan iliyotokana na Sensa yetu ya Watu na Makazi, itaendelea pia kutuongoza kwenye kipengele hicho namna ambavyo tunaweza kufanya, ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba fedha za wafanyakazi zinaweka uwekezaji ambao unaendelea, yaani unafanyika uwekezaji mfano kujenga majengo ambayo yanaongeza kipato kwenye Vyama vya Wafanyakazi. Ninatamani kufahamu.

Ni lini Serikali itakuja na sheria ambayo inampa haki mwanachama yule kuweza kupata gawio kwa fedha zinazopatikanika kwa uwekezaji huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Nataka kufahamu, kumekuwa na malalamiko mengi ya walimu kuhusiana na kulazimishwa kuingia kwenye vyama viwili viwili vya wafanyakazi: Ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba kujiunga na uanachama wa Vyama vya Wafanyakazi ni hiari ili kusikuwepo na huko kulazimishana kuingia kwenye vyama viwili viwili hususan kwa walimu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda nimjibu Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila na nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini kwenye eneo hili la uwekezaji nimefafanua vizuri na sheria ipo ambayo inaviruhusu vyama hivi vya wafanyakazi, pia zipo kanuni ambazo zinawaongoza katika vyama vya kwa misingi ya katiba walizojiwekea. Kwa hiyo, nichukue tu kama maoni katika eneo hili, nitaonana naye baada ya hapa ili tuweze kuzungumza zaidi kuona nini hasa alimaanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile amesema kwamba wanachama wanalazimishwa kujiunga. Niseme kwamba vyama hivi ni vya hiari, lakini Katiba zao ndiyo ambazo zinawabana kwamba pengine ujiunge au ukijiunga atanufaika na nini na kipi? Kwa hiyo, siyo kwamba ni lazima kwamba lazima sasa ujiunge kwenye chama hiki. Hapana, lakini pia nitakutana naye tufahamiane zaidi ili tuone namna ya kuliweka vizuri, ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri katika vyama hivi ulazima upo, maana mfanyakazi hasa mwalimu anapoingia tu kwenye ajira anakatwa pesa bila yeye kuwa na ridhaa yake: Je, kama unasema siyo lazima, unaweza ukatoa tamko leo ili mwalimu yeyote aingie chama chochote anachokitaka yeye? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya awali, nimesema zipo katiba ambazo zinavi-guide hivi vyama, kama pengine ni cha walimu au ni chama cha kada nyingine tofauti, wapo pale kwa mujibu wa katiba zao na makubaliano ambayo wanakubaliana wao kwa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu zipo baadhi ya changamoto pengine na migogoro katika vyama hivi. Serikali ya Awamu ya Sita chini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tutaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na vyama hivi kuboresha upungufu ambao upo au kusuluhisha migogoro ambayo inaendelea katika vyama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwatoe wasiwasi walimu, waendelee kukiamini Chama chao cha Walimu na sisi Serikali tuko pamoja nao. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa wafanyakazi ni mali ya Serikali na Serikali ina wajibu kwa wafanyakazi hawa.

Je, haioni sasa umefika wakati mfanyakazi halazimishwi kujiunga kwenye chama bila hiari yake? Nadhani ni muhimu sana kutoa tamko hili Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Sima. Kama ambavyo nimejibu, amesema wafanyakazi ni mali ya Serikali. Nami niseme, tunawapongeza sana wafanyakazi wa Tanzania kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii kuliletea maendeleo Taifa letu, lakini tutaendelea kufanya mashauriano na kutoa ushirikiano na vyama hivi vya wafanyakazi ili waendelee kuwa na imani na vyama vyao na kuendelea kuliletea maendeleo. Ni mafanikio makubwa yamepatikana kupitia vyama hivi vya wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaona hata Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amepandisha madaraja, ameongeza fedha, anaendelea kupigania maslahi ya wafanyakazi. Kwa hiyo, niwatoe shaka wafanyakazi, tuko pamoja na tutaendelea kuwaratibu vizuri kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ahsante. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kutokana na majibu aliyonipatia ni wastani wa wanawake 24 huwaguliwa kila baada ya Uchaguzi Mkuu. Kwa hiyo, naona kwamba ongezeko ni dogo wanawake 24 kila baada ya miaka mitano ni wachache sana kuwakulisha licha ya Serikali kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuongeza ushiriki wa wanawake. Swali langu ni mkakati gani mahususi unaopaswa kuwa revised ili kuongeza idadi ya wanawake kwenye siasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mkakati gani wa Serikali wa kubadilisha Political Parties Act ili kuweka kifungu kitakachovilazimisha vyama vya siasa kuwa na idadi maalumu ya wanawake watakaokuwa wagombea kwenye chaguzi mbalimbali kwenye hii nchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza nisema Serikali inatambua na kuthamini sana sana ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa na lakini na maeneo mengine. Niseme tu katika eneo hili mkakati uliopo ndani ya msajili wa vyama vya siasa ni kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wanawake kuendelea kujiamini na waweze kujiandaa kugombea nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, tutaleta Bungeni mabadiliko ya Sheria ya vyama vya siasa ili kuvitaka vyama sasa kuwa na Sera ambayo itaweka mwongozo mahususi wa kujumuisha wanawake kwenye kugombea nafasi mbalimbali. Kwa hiyo, niwaondoe shaka wanawake wenzangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajali anawathamini na tutaendelea kufanya vizuri kwenye eneo hili la kuhakikisha tunawajumuisha wanawake kwenye ngazi zote za maamuzi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Nina mambo mawili. La kwanza, naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu ya kujipanga kupambana na maafa ambayo kwa kweli sote kama Taifa tumeyaona. Tunawashukuru na tunawaomba waendelee kujipanga zaidi kwa sababu mambo haya ni ya kujirudia na hasa ukizingatia mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea na sote tunashuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwangu ni ushauri. Naomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sababu mambo ya majanga ni mambo ambayo yasiyotabirika, na yanahitaji mafunzo na uwezo kwenye taasisi zake zote, na kwa sababu ni kazi zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya Bara na Zanzibar, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, basi ione namna nzuri inavyoweza kuwasaidia wenzetu kwa upande wa pili ili nao waweze kujipanga vizuri kwa kuweza kukabiliana na maafa haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea pongezi za Mheshimiwa Zahor, nasi tunaendelea kumpongeza lakini pia tunampa pole kwa maafa yaliyotokea kule Jimboni kwake Mwera. Tunamhakikishia kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu tuko imara na tutaendelea kujipanga zaidi katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo la pili kuhusu ushauri, tumepokea ushauri wake. Kwa kuwa masuala haya pia yanaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza, nasi Ofisi ya Waziri Mkuu tuna vikao vyetu vya mashauriano tunapitia Ofisi ya Makamu wa Pili, tutaendelea kuboresha ushirikiano huo ili kuendelea kuwafikia wananchi katika maeneo yote katika nchi yetu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, naipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Pia naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa kujumuisha vijana wenye ulemavu katika programu mbalimbali. Vilevile, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, napenda kumuuliza swali dogo tu la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufuatilia na kuwaendeleza vijana hao ili lile lengo la Serikali liweze kutimia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea pongezi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mheshimiwa Mwantatu lakini na mimi nimpongeze sana Mheshimiwa Mwantatu kwa kazi nzuri anayofanya tangu nimemfahamu katika eneo letu hili la watu wenye ulemavu, anafanya kazi nzuri, lakini nimwambie kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia tunaendelea kuweka mikakati ya kuwafikia vijana hawa. Moja, Mheshimiwa Naibu Waziri anayehusika na eneo hili amekuwa akifanya programu za kuwatembelea na kuwaona vijana hawa na hata Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Profesa Ndalichako, anapita katika maeneo mbalimbali kuwatembelea kuona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia kitengo cha watu wenye ulemavu imeendelea kufanya programu za kuwapitia na kuendelea kuwahamasisha vijana hawa kwa kushirikiana na wenzetu upande wa TAMISEMI, Maafisa Maendeleo ya Jamii, kuona namna wanaendelea vizuri. Lakini mwisho tunafanya mapitia ya Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ili kuweka mikakati ambayo ni endelevu itakayowezesha kundi hili kuendelea kushiriki lakini niwape moyo na kuendelea kuwaambia wenzangu, watu wenye ulemavu hasa vijana, waendelee kuchangamkia fursa ambazo zinatolewa na Serikali na sisi tuko pamoja na wao. Ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, imekuwa takribani miezi kumi tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, atoe maelekezo ya kusitisha mikopo iliyokuwa inatolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kupisha utaratibu mpya ambao utakuwa na manufaa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni lini hasa Serikali itarejesha utaratibu huu, ili vijana waendelee kunufaika na mikopo hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Vijana, Mheshimiwa Ng’wasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kuwa lilifuata utaratbu na wenzetu wa TAMISEMI, wameendelea kulizungumzia, tuendelee kuwaachia wenzetu wa upande wa TAMISEMI watatupa taarifa rasmi ya wapi wamefikia na lini wataanza kutoa mikopo hiyo, lakini niwahakikishie kwamba, mikopo ile ipo, fedha ipo. Utaratibu utakapoanza makundi haya yajiandae kwa ajili ya kunufaika na programu hiyo.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi na naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jimbo la Nachingwea ni kubwa sana na lina kata ambazo zinapakana na Mkoa wa Morogoro lakini na Mkoa wa Ruvuma, Serikali pamoja na huo utaratibu haioni sasa ipo haja ya kugawanya maeneo ya kiutawala ili angalau kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Jimbo la Ndanda, limetawanyika pia kuelekea Mkoa wa Ruvuma, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Ndanda, ina sababishia wananchi watembee zaidi ya kilometa 80 kufuata huduma za Serikali. Je, Serikali haioni haja pia ya kugawa Jimbo hilo na kupatia halmashauri nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la kuongeza Maeneo ya Utawala nilikuwa namshauri Mheshimiwa Mbunge, aendelee kuwasiliana na wenzetu wa TAMISEMI, kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka, Wilaya sura ya 287 na kifungu cha 87(a)(1)(2) cha Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa, kama zilivyorekebishwa katika marekebisho ya Sheria mbalimbali ili waweze kufuata huo utaratibu wa kuanzia u-DC, DCC, RCC na baadaye kuja Taifa ili waweze kuona namna ya kuzingatiwa kipindi hiko ambacho TAMISEMI, watafanya jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili. Kuhusu Jimbo la Ndanda, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume imepewa mamlaka. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge, muda utakapofika Tume itakapotangaza basi na yeye afuatae utaratibu huo ambao utawekwa na Tume ili kusudi kuona jambo hilo utekelezaji wake, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwenye jibu la msingi, Waziri anasema Mbunge, aombe, mimi naamini kunakuwa kuna timu ya kufanya utafiti kutokana na vigezo. Hiyo habari ya Wabunge kuomba unakuta maeneo mengine yanagawanywa kisiasa, linaitwa Jimbo la Mjini, lina kata saba vijijini mwisho wa siku linaleta athari kwenye Mipango Miji ya maendeleo kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, ni vigezo gani vya msingi ambavyo mnavitumia ili kuhakikisha jimbo linagawanywa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nilipokuwa natoa maelezo yangu ya awali nilisema Mbunge aombe, maana yake ni baada ya Tume kuweka ule utaratibu sasa utafanya uweze kuomba, lakini vigezo naomba nivitaje kama ifuatavyo: -

(i) Ukubwa wa Jimbo husika, unaangaliwa;
(ii) Mipaka ya kiutawala;
(iii) Hali ya kiuchumi kama inaturuhusu;
(iv) Hali ya Kijiografia;
(v) Upatikanaji wa mawasiliano;
(vi) Jimbo lisiwe ndani ya Halmashauri au Wilaya mbili; na
(vii) Kata moja isiwe ndani ya Majimbo mawili.

Mheshimiwa Spika, lakini lipo sharti lingine la Ofisi yako ya Bunge, kutuambia kama tunayo nafasi humu ndani yakuendelea ku-accommodate idadi kubwa zaidi ya Wabunge. Kwa hiyo, nimetaja kwa uchache naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, muda utakapofika Tume ikitangaza basi vigezo na masharti vitakavyowekwa vitatuongoza kuona kwamba Jimbo hili linafaa kugawa au halifai, ahsante. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini vile vile nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vyema zoezi hili la Serikali kuhamia Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kwamba taasisi 65 zimeshahamia hapa Dodoma, lakini mwisho kabisa wa taasisi zote kuhamia Dodoma ni lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Makao Makuu ya Nchi ambako viongozi wengi wa Serikali wanafanya kazi ni lazima kuwe na makazi yao rasmi. Je, ujenzi wa makazi rasmi ya viongozi wa Serikali utaanza lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, napokea pongezi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini mwisho wa taasisi za Serikali kuhamia Dodoma, kama nilivyojibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Kenneth Nollo kwamba tunaendelea na uchambuzi. Taarifa itakapokamilika, tutawaambia ni taasisi ngapi zimeshahamia na ngapi zimebaki. Tunatarajia mwaka 2025 taasisi zote ziwe zimeshahamia Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili, kwanza naendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri. Nimhakikishie kwamba Serikali ilianza ujenzi wa nyumba za viongozi kuanzia mwaka 2021/2022. Kupitia Wakala wa Majengo (TBA) tulijenga nyumba 20 na Septemba, 2023 nyumba 150 za watumishi zilizinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuko kwenye zoezi la kupanga eneo ambalo tumelitwaa kwa ajili ya kujenga nyumba za viongozi wa Serikali na watumishi. Sasa hivi tuko kwenye hatua ya kujipanga kwa kupitia hao wenzetu wa TBA watuainishie vizuri, na tutakuwa na ekari 4,654. Tumetwaa eneo kati ya Mji wa Serikali Mtumba na Ikulu hapo kwa ajili ya kujenga nyumba hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaendelea vizuri na uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba na kila jambo linaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwatoe mashaka na niwakaribishe sekta binafsi, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Serikali na natambua kwamba Kanuni za Maadili ya Uchaguzi huwa zinaandaliwa mwaka wa uchaguzi, lakini kwa kuzingatia unyeti na upekee wa makosa ya ukatili wa kijinsia katika uchaguzi yaliyoongezwa ningependa kujua, je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa kanuni hizi mapema zaidi ili wananchi wapate muda wa kutosha wa kuelimishwa kuhusu kanuni hizi na wale ambao watakuwa wanagombea wajue ni hatua gani za kuchukua pale ambapo wanapitia matukio ya ukatili wa kijinsia katika uchaguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Neema kwa namna ambavyo amelisema suala hili la ukatili wa kijinsia. Pia nimwambie kwamba ushauri wake tumeupokea, tutaendelea kuufanyia kazi. Pia niwatoe wasiwasi Watanzania kwamba tupo vizuri na tutaendelea kuhakikisha kwamba kanuni hizi zinafahamika kwa wananchi wote. Vile vile tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, Asasi za Kidini, vyombo vya habari na maeneo tofauti tofauti ili kuweza kutoa elimu.
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo hilo bado lipo na linajitokeza. Je, ni kwa kiasi gani watendaji wanaufahamu wa sera hii ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri umeisema?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, sasa Serikali haioni haja ya kutoa mwongozo tena mara nyingine kwa watendaji wanaohusika na masuala ya sherehe za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Keysha, kama nilivyojibu jibu la msingi tuna sera na sheria. Nitoe rai kwa wale wanaoandaa shughuli za Serikali na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Jenista, tumekuwa tukifanya jambo hili kwa pamoja. Maadhimisho mbalimbali ya sherehe tuna kitengo cha sherehe waendelee kuweka nafasi hizi za watu wenye Ualbino na watu wengine kwa sababu tunaweka masuala ya tenti kuweka vizuri ili waweze kukaa. Tuna mkakati gani? Tunaendelea kushirikiana na Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) pamoja na wadau wengine wanaofanya kazi kwenye eneo la watu wenye ulemavu kujengea elewa jamii ili kufahamu haki za watu wenye ulemavu na sera.

Mheshimiwa Spika, pia tuko kwenye marekebisho ya Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ambayo pia nayo inagusa kundi la watu wenye Ualbino. Kwa hiyo nimtoe mashaka Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya maarufu kama Keysha kwamba mambo yanaenda vizuri Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais, Daktari Samia tunaendelea kuwajali watu wenye ulemavu na watu wenye Ualbino. Ahsante. (Makofi)