Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdullah Ali Mwinyi (3 total)

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali imechukua hatua gani kutatua changamoto zinazoelezwa za ukiritimba zilizopelekea Kampuni ya Uber kusitisha huduma zake nchini Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa Mahonda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilianza kudhibiti huduma za taxi mtandao mwezi Mei, 2020 kwa kutumia Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Na. 3 ya mwaka 2019 pamoja na kanuni zake.

Mheshimiwa Spika, baada ya LATRA kuanza kudhibiti eneo hili kisheria, iliweka viwango vya tozo kwa huduma za taxi ili kupunguza migogoro kati ya madereva na wamiliki wa mifumo ya taxi ambao ni pamoja na Kampuni ya Uber. Kutokana na hatua ya LATRA kuweka tozo katika huduma za taxi mtandao, Kampuni ya Uber iliamua kusitisha kutoa baadhi ya huduma hapa nchini mwezi Aprili, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia LATRA inaendelea na mazungumzo na Kampuni ya Uber kwa lengo la kuhakikisha inarejesha huduma za taxi mtandao. Ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU K.n.y. MHE. ABDULLAH ALI MWINYI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa taarifa ya utekelezaji wa Blueprint for Regulatory Reforms za mwaka 2018 ili zijadiliwe?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Mahonda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianza rasmi utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (MKUMBI) ujulikanao kama blueprint hapo Julai Mosi, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba tarehe 24 Oktoba, 2022, Wizara iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa MKUMBI kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Katika taarifa hiyo ambayo inaonesha utekelezaji wa hadi kufikia Agosti, 2022 ilijadiliwa, ambapo Kamati ilitoa maelekezo mbalimbali ya kufanyiwa kazi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mpango huo, maelekezo hayo yanaendelea kuzingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI aliuliza:-

Je, nini maana ya non-aligned katika msimamo wa Tanzania Kimataifa wa kutofungamana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa Mahonda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, non-aligned ina maana ya kutofungamana ama kushikamana, kiitikadi na kimsimamo na nchi ama kundi la nchi zenye nguvu na ushawishi mkubwa duniani. Dhana hii ilikuja mara tu baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya dunia mwaka 1945, ambapo dunia ilishuhudia kuibuka kwa kambi mbili zilizokuwa zinahasimiana ambazo ni Marekani na washirika wake chini ya mwamvuli wa NATO na uliokuwa Umoja wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) na washirika wake chini ya mwamvuli wa Warsaw Pact.

Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, nchi ambazo ziliamini kutofungamana ama kuambatana na upande wowote zilianzisha Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement - NAM). Tanzania ilijiunga na umoja huu mwaka 1961 mara tu baada ya uhuru. Dhana ya kutofungamana na upande wowote ni miongoni mwa misingi ya sera yetu ya mambo ya nje.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama wa NAM kwa kutekeleza misingi ya kutofungamana na upande wowote katika maamuzi mbalimbali ambayo yanachukuliwa kwenye ajenda za kimataifa kwa kuzingatia uhuru na mipaka ya nchi (sovereignty and territorial integrity), kupinga matumizi ya nguvu za kijeshi, haki na usawa duniani na maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.