Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao (11 total)

MHE. ERIC J. SHIGONGO K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

(a) Je, ni lini Jimbo la Sengerema litapata Kivuko kipya angalau kimoja kati ya vivuko vitano ambavyo Serikali imepanga kujenga katika Ziwa Victoria kwa bajeti ya mwaka 2021-2022?

(b) Je, Serikali inafahamu adha ya usafiri wanayoipata wananchi wa Mji Mdogo wa Buyagu Wilayani Sengerema pamoja na wananchi wa Wilaya za Misungwi na Nyang’hwale kwa kukosa chombo madhubuti cha usafiri wa majini?
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamisi Mwagao, Mbunge wa Sengerema, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imepanga kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachohitajika katika eneo hilo. Mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na gharama za kivuko hicho kujulikana, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya katika Jimbo la Sengerema kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea changamoto ya adha ya usafiri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mbunge. Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2021/2022 itatumia wataalam kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la Buyagu Wilaya ya Sengerema na Nyang’wale Wilaya ya Misungwi. Upembuzi yakinifu huo utasaidia kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachofaa ili kiwekwe kwenye mpango wa utekelezaji katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, mpango wa kuzipandisha hadhi Sekondari za Ngweli, Ngoma A, Tamabu, Nyamatongo, Sima, Nyampande na Katunguru kuwa za Kidato cha Tano na Sita Wilayani Sengerema umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa spika, kabla ya shule kusajiliwa Kidato cha Tano na Sita inatakiwa kuwa na miundombinu ya msingi kwa ajili ya kupokea wanafunzi. Jukumu la ujenzi wa miundombinu hiyo si la Serikali kuu tu bali ni la halmashauri kupitia mapato yake ya ndani pamoja na wadau wa elimu na jamii nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya Sengerema na kuwasiliana na Ofisi ya Uthibiti Ubora kufanya tathmini katika Shule za Sekondari za Ngweli, Ngoma A, Tamabu, Nyamatongo, Sima, Nyampande na Katunguru ili kujiridhisha na hali ya miundombinu ya msingi kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga miundombinu katika baadhi ya shule zilizopendekezwa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha ili kuongeza fursa ya Elimu.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa banda la ukaguzi na kupokea samaki wabichi katika Kata ya Chifunfu utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa banda la kupokelea samaki Chifunfu uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ulianza mwezi Mei, 2021 chini ya Mkandarasi M/S Fast Construction Company Limited ya Mkoani Mwanza kwa thamani ya shilingi 124,592,064.00 ambapo hadi sasa ujenzi umefikia hatua ya kuezeka na Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi 95,768,193.00.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya ujenzi wa banda hilo ilipangwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita, hata hivyo Mkandarasi hakuweza kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba, hivyo Serikali imechukua hatua za kusitisha Mkataba wa Mkandarasi huyo na hatua zingine za kisheria zinaendelea dhidi yake.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawavuna tumbili katika Kisiwa cha Juma Wilayani Sengerema ambao wanakula mazao ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Jimbo la Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi ya kuyabaini na kuyadhibiti makundi (familia) ya tumbili yanayosumbua wananchi katika Kisiwa cha Juma, Wilayani Sengerema. Aidha, Serikali itaendelea kuhamisha makundi hayo na kuyapeleka katika hifadhi nyingine zenye mahitaji ya wanyamapori hao. Wizara itaendelea kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori waharibifu wakiwemo tumbili na nyani.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini miradi ya umwagiliaji katika Vijiji vya Nyamterela na Katunguru pamoja na Vijiji vya Kwinda na Isole itakamilika Wilayani Sengerema?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Katunguru yenye hekta 600 iliyopo kijiji cha Nyamterela Wilayani Sengerema.

Vilevile Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Usole yenye hekta 1,000 iliyopo katika kijiji cha Kishinda.
MHE. FURAHA N. MATONDO K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, mpango wa kutumia majengo ya Sekondari ya Sengerema kuwa Chuo cha Madini na Uvuvi umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari Sengerema ni miongoni mwa shule za Sekondari kongwe hapa nchini. Shule hii inachuka wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita kutoka nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapanga kuongeza nafasi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita, kutokana na wanafunzi wanao maliza kidato cha nne kuongezeka sana. Mpango wa kuifanya Shule ya Sekondari Sengerema kuwa Chuo cha Madini na Uvuvi hauwezekani kutokana na uhitaji wa shule hii kwani kubadili matumizi ya shule hii kutaongeza uhaba wa nafasi za wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais TAMISEMI haijashirikishwa kwa namna yoyote kuhusu kubadili matumizi ya shule ya Sekondari Sengerema. Hivyo, tunawaomba wenzetu wa Wizara ya Madini kuja mezani na kujadiliana juu ya jambo hili, hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa tuna uhitaji mkubwa wa shule za kidato cha tano na sita. Aidha tunaomba kuwashauri Wizara ya Madini kutafuta eneo na fedha kwa ajili ya kujenga chuo kitakachojihusisha na kada ya madini kuliko kubadili matumizi ya Sekondari hii.
MHE. TABASAM H. MWAGAO K.n.y. MHE. SHANIF M. JAMAL aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza Barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Mansoor Jamal, Mbunge wa Kwimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu yenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha lami kwa awamu; ambapo mkataba wa ujenzi wa kilomita tatu kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, mwaka huu wa 2024. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki, ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati viwanda vya kuchambua pamba vya Nyakarilo, Nyamirilo na Buyagu vilivyopo Sengerema?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu la Mheshimiwa Hamis Mwagao Tabasam, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, viwanda vya kuchambua pamba vilivyo na usajili wa Bodi ya Pamba hadi kufikia mwishoni mwa msimu 2022/2023 vilikuwa 92, na kati ya hivyo viwanda 57 vinamilikiwa na kampuni binafsi na 35 ni mali ya Vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha viwanda vyote vya kuchambua pamba vinafanya kazi. Serikali kupitia Bodi ya Pamba (TCB) mwaka 2020 ilifanya tathmini ambayo imewezesha baadhi ya viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika kupata mikopo kupitia Benki ya Kilimo iliyowezesha kukarabati viwanda vyao. Kupitia utaratibu huo, Serikali itahakikisha pia viwanda vya Nyakarilo, Nyamirilo na Buyagu vinakarabatiwa ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa sekta ya pamba. Nakushukuru.
MHE. TABASAM H. MWAGAO K.n.y. MHE. SHANIF M. JAMAL aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza mchakato wa kutangaza Barabara ya Mabuki – Jojiro hadi Ngudu ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Mansoor Jamal, Mbunge wa Kwimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mabuki – Jojiro – Ngudu yenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha lami kwa awamu; ambapo mkataba wa ujenzi wa kilomita tatu kuanzia eneo la Ngudu mjini kuelekea Jojiro umesainiwa tarehe 19 Januari, mwaka huu wa 2024. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa awamu kwa sehemu iliyobaki, ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, lini Serikali itafunga laini ya pili ya umeme kutoka Geita hadi Sengerema ili kutatua tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali Wilaya ya Sengerema ilikuwa ikipata umeme kutokea Mwanza Mjini kupitia njia ya umeme iliyokuwa inapita chini ya Ziwa Victoria. Aidha, wakati wa ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi, kwa bahati mbaya mkandarasi alikata submarine cable na tangu wakati huo Sengerema ikawa inapata umeme kutoka kituo kipya cha kupoza umeme cha Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANESCO imekubaliana na Mkandarasi kuweka sehemu ya kupitisha waya pembeni mwa Daraja la Kigongo – Busisi ambapo waya huo utapitishwa badala ya kupita kwenye maji. Aidha, kazi hiyo itafanyika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja na kuwezesha Wilaya ya Sengerema kuendelea kupata umeme kutokea Mwanza Mjini kama ilivyokuwa awali.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa kilometa 15 za barabara za Sengerema Mjini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano ya ujenzi wa barabara kilometa 15 katika Mji wa Sengerema kwa kiwango cha lami ambapo hadi kufikia sasa kilometa 1.69 zilizogharimu shilingi milioni 974 zimekwishakamilika. Barabara zilizokamilika ni Kabita – Sengerema Sekondari kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 0.97 na CCM - Bwawani na Pambalu yenye urefu wa kilometa 0.72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2024/2025 Serikali inajenga barabara ya Mapinda – Lubeho Hotel kilometa 0.57 na Mabimbi - Beipoa kilometa 0.43 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 570 ambapo mchakato wa ununuzi unaendelea. Aidha, Serikali inaendelea kufanya usanifu kwa barabara zilizosalia zenye urefu wa kilometa 12.31 kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi na pindi fedha inapopatikana ujenzi uanze mara moja.