Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Janeth Elias Mahawanga (11 total)

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata Bima ya afya kupitia utaratibu wa vikundi ambao ulikuwa msaada mkubwa sana kwenye jamii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inatoa kitita mahususi cha mafao kwa makundi maalum ya wajasiriamali ambao wamejirasimisha shughuli zao kupitia mwamvuli wa jumuiya au vyama vyao vilivyorasimishwa.

Mheshimiwa Spika, makundi ya wajasirimali yanayonufaika na utaratibu wa bima ya afya ni pamoja na makundi ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika 225 vyenye idadi ya wanachama 6,196; vikundi 17 vya umoja wa wamachinga; wajasiriamali wadogo; wachimbaji wa madini; wavuvi; na mamalishe ambavyo vina idadi ya wanachama 2,315; na vikundi vya umoja wa madereva bodaboda, malori na daladala ambavyo vina idadi ya wanachama 303.

Mheshimiwa Spika, kwa makundi ya wananchi ambao ni wajasiriamali lakini hawamo katika mwamvuli wa jumuiya za wajasiriamali zilizorasimishwa, Mfuko umeanzisha vifurushi vya bima ya afya vya hiari ambavyo vinazingatia umri, ukubwa wa familia, aina ya huduma na gharama halisi za matibabu nchini ambapo hadi tarehe 31 Machi, 2021 wanachama 32,343 wameshajiunga na mpango huu.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa jamii na kwa kutambua matatizo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyaainisha, Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itawasilishwa Bungeni mwezi Juni, 2021.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya huduma ya kipolisi katika maeneo ya pembezoni mwa miji ikiwemo na mkoa wa Dar es Salaam?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine tena kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga Mbunge Wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatekeleza mpango wa Askari Polisi kata /shehia katika kata zote 3956 na shehia 335 za Tanzania, ambapo hadi kufikia mwezi Februari, 2021 jumla ya askari 3963 wameshapangwa kwenye kata/shehia zikiwemo kata zilizopo pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine kwa lengo la kutoa huduma za kipolisi pembezoni kuliko na idadi kubwa ya watu na huduma ya vituo vya polisi ipo mbali, lengo ni kushirikiana na wananchi katika ulinzi na kupunguza uhalifu katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa baadhi ya maeneo huduma za polisi ziko mbali, Jeshi la Polisi kupitia mpango wa askari kata limekuwa likishirikiana na walinzi wa jadi ikiwemo sungusungu ili kupambana na kutatua uhalifu huo. Nakushukuru.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawekeza katika Sekta ya Michezo hasa kwenye timu za wanawake ili kuibua vipaji kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elius Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Shilingi milioni 183.5 zimetengwa kama kianzio katika kutoa huduma kwa timu zetu za Taifa ikiwemo timu za wanawake na Shilingi bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Timu za Taifa za wanawake ambapo kupitia uwekezaji huu, timu hizi zimeendelea kufanya vizuri katika ukanda wa CECAFA na COSAFA na umewezesha timu ya Serengeti Girls kufuzu mashindano ya Kombe la Dunia nchini India. Ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuzungumza na taasisi za kifedha ili mikopo kwa watu wenye ulemavu itolewe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vikundi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mabenki zimekuwa zikitoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu. Aidha, wananchi wa kipato cha chini wakiwemo makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanashindwa kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi hizo kutokana na mikopo hiyo kuambatana na vigezo vinavyowekwa ikiwemo waombaji kuwa na dhamana au mali isiyohamishika kama viwanja, mashamba na nyumba.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikisimamia utoaji wa mikopo ya uwezeshaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mujibu wa kifungu 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2021. Sheria na Kanuni hizi zimeelekeza kuwa mikopo hii itatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia nne kwa wananwake; nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye walemavu kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, habari njema ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya marekebisho ya Kanuni mwaka 2021 ambayo yametoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu kuomba mkopo. Hivyo, niombe Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba tufikishe taarifa hii ya mabadiliko ya kanuni za mikopo hiyo ambayo imetoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye Ulemavu kuomba mkopo.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufunga mtandao wa Wi-Fi maeneo yote nchini kufuatia jamii kuhamasika na matumizi ya teknolojia?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kufunga mtandao wa Wi-Fi maeneo yote ya umma nchini kufuatia jamii kuhamasika na matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa utekelezaji wa kufunga mtandao wa Wi-Fi umefanyika katika vituo sita ambavyo vinatoa huduma ya internet ya wazi (Internet hotspot) katika maeneo mbalimbali. Maeneo hayo ni Stendi ya Nanenane, Dodoma; Buhongwa, Mwanza; Kiembesamaki, Unguja; Chuo Kikuu cha Dodoma, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu (CIVE) na Soko la Tabora, na Chuo cha Ustawi wa Jamii Lungemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji huo utaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutegemea upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, nini mpango wa kuhakikisha Majukwaa ya Kuwezesha Wanawake Kiuchumi yanaleta tija kwenye mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri?

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi yameleta tija kwenye asilimia 10 ya Halmashauri ya kuwezesha kuunda vikundi vya kiuchumi ambavyo hukutanisha wanawake katika ngazi zote za jamii ili kujadili fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi hususan biashara, kilimo, madini, ujenzi, uchukuzi, usindikaji wa maliasili na mazao ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika jamii, ahsante.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Vituo Maalum vya Masuala ya Uwekezaji na Masoko kwa Wanawake katika kila Kata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kwa ajili ya wazawa na wageni wakiwemo wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha majukwaa ya kiuchumi mahususi kwa ajili ya wanawake. Majukwa haya yanatoa fursa kwa ajili ya wanawake kuona fursa za uwekezaji na biashara na kuzitumia ikiwemo masoko ya bidhaa wanazozalisha. Aidha, Serikali imeendelea kutambua kundi la wanawake na kuwapa fursa ya kukopeshwa mikopo mbalimbali ikiwemo mikopo ya 10% kutoka kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuangalia fursa mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na pale itakapoonekana kuna haja ya kuanzisha vituo vya uwekezaji wa masoko mahususi kwa wanawake, basi kazi hiyo itafanyika katika ngazi ya kata, nashukuru.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la mimba za utotoni kwa watoto wa kike?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau, imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Ambapo Serikali inatarajia kuzindua Awamu ya Pili ya Mpango Kazi huo mwezi Machi, 2024; ambapo moja ya kipaumbele chake ni mikakati ya kudhibiti mimba za utotoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na afua zinazotekelezwa katika mpango huo Serikali itaendelea kutekeleza afua mambo yafuatayo: -

(i) Kufanya kazi kwa mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ambayo imeongeza adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mtoto/mwanafunzi shule/.

(ii) Kuendelea kutoa elimu ya stadi za maisha kwa watoto kupitia madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto na kutoa elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi au walezi na jamii kupitia kampeni katika vyombo vya habari na majukwaa ya madhehebu ya dini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imepanga kuzindua Kampeni ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni kwa ajili ya kuelimisha wazazi, walimu na watoto kuhusu athari za matumizi yasiyofaa ya mitandao ambayo pia yanachangia mimba za utotoni.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kuhamasisha watoto wadogo kukua katika misingi ya kutambua madhara ya ukatili wa kijinsia?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa mwongozo wa Taifa wa uundaji na uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto ya mwaka 2022, ambapo hadi Juni 2023, jumla ya Mabaraza ya Watoto 651 yameanzishwa kwenye ngazi za mitaa katika mikoa 12 ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, katika mabaraza haya, watoto wamejifunza mbinu na stadi za maisha zinazowapa ufahamu na viashiria vya ukatili. Aidha, katika Mabaraza ya Watoto wanajifunza kujieleza, kujiamini na kujisimamia katika masuala yanayowahusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewezesha uandaaji wa mwongozo wa Taifa wa dawati la ulinzi na usalama wa mtoto, ndani na nje ya shule wa mwaka 2022. Mwongozo huu unahimiza watoto wenyewe kushiriki katika ulinzi wao na kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili vinavyotokea shuleni, njiani na kuelekea nyumbani na vyumbani, ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha utekelezaji wa mpango wake wa kuanzisha vituo maalum vya masuala ya uwekezaji na masoko kwa wanawake kila kata?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha kanda maalum za kiuchumi katika mikoa mbalimbali nchini. Lengo kuu la kuanzisha maeneo haya ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuongeza thamani mazao mbalimbali yanayozalishwa nchini na kukuza mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani na pia kuzalisha bidhaa zinazoagizwa nje kwa soko la ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendeleza maeneo haya kuna sehemu zitatengwa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati (SME’s) wakiwemo wanawake na vijana ili waweze kuanzisha viwanda vya kuchakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ajili ya soko la ndani na nje. Aidha, maeneo haya yatatumika kama incubators kwa maana ya atamizi ili kukuza wajasiriamali wadogo. Nakushukuru.
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Daraja kuanzia Magomeni - Jangwani - Fire ili kuondoa adha wanayopata Wananchi wakati wa mvua?
WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANROADS imepanga kujenga daraja katika eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita 15. Ujenzi wa daraja hili utatumia fedha za mkopo nafuu wa Benki ya Dunia. Taratibu za manunuzi ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na unatarajiwa kuwa umesainiwa ndani ya mwezi Septemba, 2024, ahsante sana.