Supplementary Questions from Hon. Janeth Elias Mahawanga (16 total)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa dawa katika zahanati zetu na vituo vya afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaruhusu maduka ya dawa ambayo yamesajiliwa kutoa huduma ya upatikanaji wa dawa ambazo wagonjwa wameandikiwa kupitia Bima ya Afya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kuanzisha upatikanaji wa Bima za Afya kwa wajasiriamali wadogo na wananchi wenye vipato duni kulipia Bima za Afya kwa awamu lakini vile vile kuendelea kupata matibabu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali ambalo ni muhimu sana hasa kwa mustakabali wa afya ya Watanzania. Swali la kwanza, Serikali ina mpango gani wa kuruhusu maduka yanayouza dawa kutumia bima. Mpango huo upo na una utaratibu wake ili kuweza kuruhusiwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, kimsingi mpango huo upo labda kama kuna eneo la kuboresha na kuongeza ufuatiliaji zaidi ili kuhakikisha kwamba yanafika sehemu nyingi. Hilo tutaenda kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusu wajasiriamali wadogo na kuhakikisha watu wanapata bima ya afya. Sisi tunachofikiri leo kwa sababu kwenye bajeti hii tunaenda kujadili Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, tuko tayari kupokea mawazo yenu na kupokea namna nyingi ambazo tunaweza tukaboresha hii huduma.
Hata hivyo, tunawashauri kwa sasa kuna hicho kitita ambacho kinatumika kwa wajasiriamali ambao hawajajisajili kwenye makundi maalum ambayo yanaangalia umri, ukubwa wa familia na kadhalika, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwahamasisha wajiunge kwa hilo, lakini wazo lake la kwamba tunafanyaje waweze kujiunga kidogo kidogo nalo hilo ni wazo tunalolichukua, wakati tunajadili huu muswada mpya wa sheria tuone tunalifanyaje na wakati hata mwingine kwenye simu na vitu vingine ili wazo lako ambalo ni zuri liweze kutekelezeka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa usalama ni jambo muhimu sana kwenye jamii yetu, je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia magofu ambayo yamejengwa na wananchi hususan maeneo ya pembezoni mwa miji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kutokana na changamoto ya kiusalama hasa maeneo ya pembezoni mwa miji je, Serikali imeandaa utaratibu gani au ina mpango gani wa kupeleka magari ya doria hasa nyakati za usiku kwenye maeneo ambayo hayana vituo vya polisi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza sasa maboma?
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inawapelekea wananchi huduma ya ulinzi na usalama karibu ya maeneo yao. Hiyo ni sehemu ya wajibu kabisa. Lakini na wananchi nao wanafika wakati wanakuwa wanao wajibu kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali kusaidia sasa kuona namna ambavyo nao wanajisaidia kujikaribishia hizo huduma kwa kushirikiana na Serikali. Kikubwa tu nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Tutajitahidi katika bajeti ijayo tutakapopanga mipango yetu basi tutajitahidi katika maeneo haya ya pembezoni hasa katika mkoa huu basi baadhi ya maeneo hayo tuyape kipaumbele ili tuone namna bora ambayo wananchi wanaweza wakafikishiwa hizo huduma kama ambavyo maeneo mengine yanafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini je, kutokana na changamoto hii Serikali sasa ina mpango gani katika kupeleka magari haya kwa ajili ya kufanya doria. Mpango upo, kama ambavyo tumefanya katika mikoa na wilaya na vituo vingine na maeneo mengine na hapa katika maeneo hayo ambayo Mheshimiwa ameyakusudia au ameyataja tunao mpango wa kupeleka magari hayo kufanya doria ili sasa wananchi na wao waweze kupata huduma hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho tumekifanya huko, tayari tuna mfumo au tuna utaratibu wa ulinzi shirikishi ambao askari polisi/Jeshi la Polisi wanashirikiana na raia/ jamii katika kuhakikisha kwamba maeneo ya wananchi yanapata huduma ya ulinzi kama maeneo mengine. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, atulie awe na Subira. Mambo mazuri yanakuja maana kazi inaendelea.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa ya kuuliza swali la nyongeza. Swali linasema: Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu mkakati wa muda mrefu wa kuendeleza vipaji vinavyopatikana kutokana na mashindano ya UMITASHUTA na UMISSETA?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janeth, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Janeth amependa kufahamu kauli ya Serikali kuhusu kuendeleza vipaji vya vijana wetu vinavyotokana na UMISSETA na UMITASHUMTA.
Mheshimiwa Spika, sisi Wizara yetu kwanza tumshukuru tumshukuru Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, amehakikisha kwamba michezo hii imerudi na ametoa maelekezo kwa Serikali. Tunashirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Elimu, pamoja na Wizara yetu, kuhakikisha michezo hii inaendelea, kwa kuwa michezo hii ndiyo inatupatia vipaji vya vijana wetu wanaonzia huko chini kuingia timu za Taifa.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara yetu inaendelea ku-review kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya UMISSETA na UMITASHUMTA ili michezo hii iwe endelevu. Ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kufuatia majibu mazuri ya Serikali lakini bado changamoto inayoyakuta makundi haya ni pale unapokwenda kwenye taasisi za kifedha na kushindwa kufungua akaunti ya mtu mmoja. (Makofi)
Sasa ni lini Serikali itafanya makubaliano na mabenki ili makundi haya yaweze kunufaika na mikopo hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kufuatia hali ya watu wenye ulemavu na mazingira magumu ya biashara, je, Serikali haioni haja ya kuongezea muda marejesho makundi haya ikawa tofauti na makundi ya kinamama na vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janeth kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza naomba tulichukue kama ushauri na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji huo kwamba tutaona namna bora ya kuwasaidi watu wetu katika kuona utaratibu wa kupata mikopo kupitia taasisi hizo kama alivyoshauri.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, la kuhusiana na muda wa marejesho ni kweli tumekwishakuliona hilo Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba watu wenye ulemavu ni kweli kwamba wanachangamoto. Unaweza ukakuta mtu wa kawaida ni tofauti na mtu mwenye ulemavu kwa sababu kuna wakati anahitaji kuwa na msaidizi ambaye yeye amekopa sawa, kama ni milioni 10 na mtu ambaye ni mzima naye ana milioni 10 lakini akienda kununua bidhaa atajikuta anahitaji kwenda na mtu wa kumsaidia kuona hizo bidhaa au kumsaidia kwenye usafiri.
Mheshimiwa Spika, pili hata atakapopata hitaji la chakula atahitaji amnunulie tena chakula msaidizi wake, na tatu hata anapokuwa anafanya biashara yake kwenye yale mazingira kama ni ana ulemavu wa kutokuona, atalazimika awe na mtu pale. Kwa hiyo, gharama inakuwa kubwa tofauti na hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeliona hilo na tunaona sasa namna gani ambavyo tunaweza tukaona utaratibu wa kubadilisha kanuni ili kuweza kuwanufaisha zaidi watu wenye ulemavu kwa sababu kama unavyofahamu hujafa hujauumbika sisi wote ni watarajiwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, ahsante.
MHE. JANET E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kufuatia changamoto ya Mkoa wa Dar es Salaam maeneo mengi kukosa vituo vidogo vya polisi hususan kata ya Makongo ambayo Serikali ilishaahidi kukamilisha ujenzi huo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janet kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa nyakati tofauti ilishasema iko tayari kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na Waheshimiwa Wabunge kukamilisha vituo vya polisi vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi. Sasa kupitia Bunge lako tukufu nimuombe Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, labda niseme IGP, kubaini vituo vyote vya Dar es Salaam ambavyo viko njiani havijakamilika kufanya tathmini ya kiwango cha ukamilifu unaohitajika ili viweze kutengewa fedha za kukamilisha vituo hivyo.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hamasa kubwa iliyofanywa na Serikali kuhusu matumizi ya teknolojia iliyosababisha wananchi wengi kutumia mtandao wa internet: Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwa na bundle maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo litakalowasaidia kutafuta masoko kwa njia ya mtandao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Ni lini sasa Serikali itahakikisha taasisi zote za elimu zinakuwa na huduma ya Wi- Fi itayaowasaidia walimu na wanafunzi kuongeza maarifa, na vilevile kutoa mchango wao katika ulimwengu wa elimu duniani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge alishaleta maombi yake kuhusu vikundi na vikoba kwa ajili ya kupata bundle maalum. Ni kweli kabisa kwamba, huwa tuna utaratibu kama maeneo ya vyuoni, na maeneo mbalimbali ambayo huwa yanapata special offer. Hilo tumeshalipokea na Serikali bado inalifanyia kazi, na pale ambapo tutakuwa tumekamilisha, basi tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha pili; ni wazi kabisa kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 61 (h), inayotutaka kuanzisha huduma ya mawasiliano ya internet ya kasi katika maeneo yote ya umma (Public Place) ikiwemo maeneo ya hospitali, taasisi za elimu na vituo vya usafiri hadi kufikia asilimia 40 mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaanza. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi, tumeshajenga vituo sita, na mwaka huu tayari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, tumejipanga kwa ajili ya kwenda kufikisha huduma ya internet ya Wi-Fi katika maeneo 20 na tutaendelea kufanya hivyo mpaka tutakapofikia katika lengo la Serikali ambalo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kufikia asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Vikundi vingi vya Majukwaa bado havina uelewa wa pamoja wa lengo mahsusi la uanzishaji wa majukwaa haya. Sasa nini kauli ya Serikali kuhusu hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni utaratibu upi unatumika kahakikisha waratibu wa majukwaa haya wanashuka kutoa elimu ya mwongozo wa uratibu wa majukwaa haya katika ngazi ya kata na mitaa?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunaendelea kutoa mafunzo kwa lengo la kukuza uelewa kwa majukwaa haya ya kuendeleza uchumi kwa ajili ya wanawake. Napenda kutoa rai kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, kuhakikisha kwamba wanatoa mafunzo kwa lengo la kuwaelewesha wananchi ni nini cha kufanya katika majukwaa haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wizara yangu inafuatilia na kufanya tathmini mbalimbali katika vikundi vyote vya majukwaa ya wanawake kiuchumi na kuhakikisha kwamba tunawatembelea kila baada ya robo ya mwaka wa fedha kuhakikisha vikundi vile vinafanya kazi vizuri na kuhakikisha wanafuata sera, sheria, kanuni na miongozo yote ambayo tumeipanga, ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza: Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo kutafuta masoko nje ya nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nini mkakati wa Serikali kuwaandaa wajasiriamali hawa wadogo kuwa wawekezaji ndani ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwatafutia masoko nje ya nchi, ndiyo maana utaona kuna majukwaa mbalimbali ya akina mama pamoja na makongamano yanayowakutanisha wafanyabiashara wanawake na wakati mwingine husafirishwa kwenda katika nchi mbalimbali kuhudhuria makongamano kama hayo kama njia ya kuwajengea uwezo na kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la kuwawezesha wawe wafanyabiashara wakubwa, nimesema katika jibu la msingi kwamba Serikali imetoa fursa mbalimbali za kuwakopesha wafanyabiashara wakiwemo akina mama ili waweze hatimaye kuimarisha mitaji yao kuikuza na hatimaye wawe wafanyabiashara wakubwa. Ni matarajio yetu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hususan hii Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itawezesha akina mama kuendelea kuongezeka katika idadi ya wafanyabiashara wakubwa katika nchi yetu, nakushukuru sana.
MHE JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini kanuni za MSA (Media Service Act) zitahuishwa na wadau kushirikishwa ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Mahawanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita tumepitisha marekebisho ya Media Service Act ambapo tunatarajia Mheshimiwa Rais akishasaini baada ya hapo Mheshimiwa Waziri atatangaza siku ya kuanza kutumika kwake, vilevile tutaanza mchakato wa kuhakikisha kwamba kanuni hizo ambazo zinaendana sambamba na mabadiliko hayo basi zitakuwa zimetungwa na zitapitia katika utaratibu uleule wa kuhakikisha kwamba tunahusisha wadau ili waweze kushiriki katika mchakato mzima na baada ya hapo kanuni zitakuwa tayari kwa ajili ya matumizi. Ahsante.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nini mkakati wa Serikali kushirikisha taasisi mbalimbali zinazojihusisha na elimu ya masuala ya afya ya uzazi. Je, Serikali haioni haja ya taasisi hii kupata vipindi kwenye mashule mbalimbali ili kutoa elimu kwa watoto wa kike?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile mimba za utotoni zinaenda sambamba na ndoa za utotoni. Nini sasa baada ya Serikali kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Lini Serikali italeta Muswada wa ndoa za utotoni?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau tunaimarisha mikakati ya uratibu za afua na kutoa huduma za afya shuleni kwa kushirikiana na majukwaa ya watoto walioko shuleni, vitabu vya watoto, madawati, ulinzi na usalama, mabaraza ya watoto, na kutumika katika elimu ya afya shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili. Wizara ya Maendeleo ya Jamii ikishirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni juu ya kujua umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike. Pia, mchakato huo ukimalizika Muswada huu utaletwa katika Bunge lako Tukufu na kujadiliwa na kupitishwa sheria ya kuthibiti ndoa za utotoni.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza. ukiacha mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo imefanikiwa kupata haya Mabaraza ya Watoto, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha mikoa 14 iliyobaki nayo inapata mabaraza haya? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; suala la vitendo vya ukatili kwa watoto limekuwa likiendelea siku hadi siku kwenye jamii yetu. Je, Serikali haioni haja sasa yakuja na sheria kali itakayo komesha vitendo hivi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuanzisha mabaraza haya katika shule zote za vijijini na mitaani nchi nzima. Serikali pia imeshasambaza Mwongozo wa Taifa wa uwaandaaji na uendeshaji wa Mabaraza ya Watoto katika halmashauri zote nchini, ambapo utawasaidia kuendesha mabaraza hayo kwa kushirikiana na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, Bunge lako Tukufu limeshapitisha sheria na adhabu kali za kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto. Niwaombe wananchi, waendelee kutoa ushirikiano kwa Maafisa Mahakama na kutoa ukweli pale wanapofika katika sheria. Niwasisitize kuwa, mahakama itaendelea kufanya kazi yake pale ukweli watakapoutoa katika sehemu za sheria, ahsante. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Nini kauli ya Serikali kuhusu usalama wa usafiri wa bodaboda kupakia abiria zaidi ya mmoja tena bila kuvaa helment?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatoa kauli wasafiri wote wa vyombo vya moto nchini, iwe bodaboda, iwe bajaji, na kadhalika, kuzingatia sheria pamoja na usalama kwa ajili yao wenyewe ikiwa ni sambamba na abiria wanaowabeba. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara hususan wale wanaokuwa na watoto wadogo kwa kuwatafutia maeneo ya muda wa kati wanasubiri kuwatengea maeneo husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini sasa kituo cha uwekezaji kitaona umuhimu wa kuwasaidia kutengeneza program ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo hususan wanufaika wa mikopo ya Serikali ili fedha zile ziweze kurudi kwa kuwekezwa sehemu sahihi na kuwaonesha fursa zinazowazunguka katika maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna changamoto kubwa ya maeneo ya ufanyaji biashara hasa kwa akinamama wajasiriamali wadogo na vijana ambao wanauza biashara ndogondogo na wengi wanatumia maeneo ya barabarani au kando ya barabara kuuza bidhaa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kutenga maeneo kwenye halmashauri na miji ambako tunahamasisha hawa akinamama na wengine ambao hawana maeneo maalum ili waweze kufanya biashara zao katika maeneo hayo ambayo ni salama na sahihi kulingana na ubora hasa kwenye vyakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo chetu cha uwekezaji kimekuwa kikitoa vivutio maalum kwa Watanzania na hasa kikilenga wajasiriamali au wafanyabiashara wanawake na vijana. Ndiyo maana kupitia program hii ya kuwezesha akinamama na vijana, Mheshimiwa Rais ameanza kuja na mpango maalum ambao kupitia mikopo hii ya 10% itakuwa ni sehemu ya kichocheo cha kuwasaidia akinamama hao ili wapate fursa za kuwekeza na kukua zaidi katika biashara zao. Nakushukuru.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kwa namna gani Serikali inaweza kusaidia uzalishaji wa chakula nchini badala ya kutegemea uagizaji? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema katika swali lililotangulia, Serikali tunaweka vivutio kwenye uzalishaji wa bidhaa hizo kwa wazalishaji wa ndani lengo likiwa ni kujitosheleza ndani ya nchi ili kuweza kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ambao kiuchumi una madhara tunapokuwa na uagizaji mwingi kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo tutakapokaa na Kamati yetu ya Bajeti tutaendelea kupitia item by item ili kuweza kuhakikisha kwamba tunakuwa na maeneo mengi ambayo uzalishaji wake unafanyika ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza maswali ya msingi, anaupiga mwingi kama ile timu ambayo hata ikifungwa haitumi wazee kufanya press. (Makofi)
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante! Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza nini mpango wa TBS kuhakikisha inawasaidia wajasiriamali wadogo kupata alama ya bidhaa zao, alama za ubora za bidhaa zao kwa gharama nafuu lakini pia kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, TBS ina mkakati gani kuhakikisha inafungua vituo vya kutoa huduma kwa wajasiriamali wadogo hususan kwenye maeneo ambayo hayawezi kufikika kwa urahisi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi ni dhamira ya Serikali ya TBS kuwaimarisha hawa wajasiriamali wadogo na ndiyo maana utaona tumeweza kuwafikia zaidi ya 14,354. Sasa kwa sababu kama ilivyoelezwa huenda kutokana na ukubwa wa eneo analotoka la Dar es Salaam wajasiriamali ni wengi tutaimarisha TBS kwa sababu makao makuu yake yapo Dar es Salaam kuwafikia kwenye ngazi za Wilaya ili wengi zaidi waweze kupata huduma kwa gharama nafuu, ninashukuru.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; ni lini SIDO itaanza kujiendesha kibiashara ili kukidhi mahitaji ya wajasiriamali wadogo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mpango wa Serikali katika kuboresha sera ya biashara na sera ya wajasiriamali wadogo ili ziendane na soko la ndani na mahitaji ya wajasiriamali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, lini SIDO itaanza kujiendesha kibiashara? Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imeainisha maeneo ya miradi ya kimkakati na tayari katika baadhi ya maeneo vibali kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo hayo kwa kupitia Msajili wa Hazina vimeshakwishaombwa. Pili, maandiko mbalimbali kwa ajili ya uanzishwaji wa miradi ikiwemo kongani za viwanda nayo pia ni moja ya mkakati ambao umepangwa kutekeleza azma hiyo.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusiana na sera; Serikali imeendelea kuboresha Sera ya Taifa ya Biashara na sasa tulipo tumekwishapeleka Sera hiyo katika Baraza la Mawaziri na Baraza limeridhia na sasa tupo katika hatua za mwisho kwa ajili ya uzinduzi wa sera hizo ili kuendana na mahitaji ya sasa katika ujasiriamali.