Contributions by Hon. Kabula Enock Shitobela (6 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na amani tele hasa kwa kunipa kibali cha kuwa katika Bunge hili lako tukufu la Kumi na Mbili. (Makofi)
Napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi hasa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wote wa chama bila kusahau viongozi wangu wote wa chama wa UWT Mkoa na Taifa, bila kuwasahau wapiga kura wangu wote wakinamama wa mkoa wa Mwanza, ahsanteni sana kwa kuniamini nije kuwawakilisha katika Bunge hili tukufu la Kumi na Mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia napenda kuishukuru familia yangu kwa kuwa wamenipa faraja sana kipindi cha kutafuta kura na siku zote za maisha yangu na mpaka leo niko hapa ni kwa sababu ya faraja zao, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipo hapa kwa dhati kabisa kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, nimesoma hotuba hizi zote mbili ya mwaka 2015 na 2020.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite zaidi kwenye suala la afya. Katika ukurasa wa 32 miaka mitano iliyopita (Awamu ya Tano) ya Serikali hii imefanya mengi katika afya kama kujenga vituo vya afya na kutoa huduma ya afya kwa vituo 1887, zahanati 1198, vituo vya afya 487 na Hospitali za Wilaya 99 pamoja na Hospitali za Mkoa 10 na Hospitali za Rufaa Kanda tatu. Pia imeweza kupunguza vifo vya akinamama wajawazito, miaka mitano iliyopita ilikuwa kila mwaka wakinamama 11,000 wanafariki kwa mwaka mmoja. Lakini kutoka mwaka 2015 mpaka 2020 limeweza kupungua kabisa tatizo hilo na kurudi kuwa wanawake wajawazito wanaofariki dunia ni watu 3,000 tu kutoka kwenye 11,000. Kwa hiyo napenda kuipongeza sana Serikali na Wizara ya Afya kwa ujumla kwa kujitahidi kwa jitihada zao hizo nzuri ya kumuokoa mama mjamzito. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuiomba Serikali sasa iweke kipaumbele zaidi kumaliza kabisa tatizo hili kama ambavyo imeweza kupunguza tatizo kutoka wanawake 11,000 kwa mwaka kufikia wanawake 3,000 ninajua kwa jinsi spidi tuliyonayo Serikali hii ikisimamia vizuri na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dorothy Gwajima namuamini mama huyu ni shupavu, akisimama kama yeye pia ni mwanamke ambaye ameshaingia labor anaujua uchungu wa mama mjamzito jinsi gani anapata matatizo. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iliangalie kwa umakini kabisa jambo hili ili kumaliza kabisa vifo vya mwanamke na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niko mbele yako pia kuomba suala la pili katika hospitali zetu za wilaya za Mwanza Wilaya zote hasa Wilaya ya Ukerewe jiografia yake ya kufikika au ya kutoka kuja Mwanza kwenye Hospitali ya Rufaa ni ngumu. Mfano Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe hakuna chumba maalum au wodi maalum kwajili ya mtoto njiti. Sasa pale complication yoyote au mtoto akizaliwa kabla ya muda, kwa hiyo kumuokoa yule mtoto inakuwa taabu sana. Ombi langu kwa Serikali nilitaka niombe ikiwezekana kujengwe japo wodi ambayo ya kulingana na Wilaya ile kwa ajili ya kuokoa mtoto njiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema hata uhai pia. Napenda kumpongeza Rais wetu mpendwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazoendelea kuzifanya. Niende moja kwa moja kuchangia hoja hii ya Wizara ya Elimu. Tatizo la ajira katika nchi yetu limekuwa tatizo kubwa sana, kusababisha matatizo mengi kwenye familia hasa kwa kina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, wakinamama wengi wanalea watoto kupitia biashara ndogo ndogo kama mama lishe na kutembeza hata vitu vidogo vidogo, kwa ajili ya kujipatia pesa kwa ajili ya kutunza watoto wao na vile vile kuwapeleka shule. Mama huyu wakati anampeleka mtoto shule anakuwa na imani kwamba, baada ya kuhitimu masomo mtoto yule ataweza kuwa mkombozi wake. Lakini, badala yake mtoto yule anapohitimu masomo anajikuta anaongeza mzigo tena kwa mama yule, anaanza tena kutembea kila siku na vyeti kwenda kutafuta kazi akitumia nauli ya mama yake, anaomba kila siku kwa mama nauli. Kwa hiyo, inazidi kumuongezea shida mama huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukizingatia mama huyu anakuwa amekopa mikopo kwenye SACCOS na sehemu mbalimbali kama VICOBA, ili aongezee ule mtaji wake na kuweza kupata school fees ya mtoto wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa naiomba Wizara ya Elimu ijaribu kuangalia mitaala yake lakini pia, iwajengee watoto confidence kuanzia utotoni kwamba, haendi kusoma kwa ajili ya kufanya kazi au kuajiriwa. Wawajenge kisaikolojia kwamba, anaenda shule kutoa ujinga au kuongeza elimu ya vitu mbalimbali. Lakini nia yake ni kupata biashara, akifanya biashara anauwezo wa kutengeneza maisha yake au kutengeneza faida kubwa kuliko hata huo mshahara ambao angeenda kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe sana Wizara ya Elimu ijaribu kuliangalia hilo, ili kuwajengea uwezo watoto wetu wa kujitegemea kuliko kutegemea ajira. Mfano, tukiangalia matajiri wengi duniani ni wale ambao hawakusoma sana je, tumejaribu kujiuliza ni kwa nini wale ambao hawakusoma sana wameweza kufanikiwa sana katika biashara au katika kujitegemea? Jibu ni kwamba, waliona hawana option nyingine hawakusoma hawana vyeti vizuri vya kuweza kuajiriwa katika nyadhifa nzuri. Kwa hiyo, ndio maana wakasimamia zile biashara zao au kazi yao, kama walikuwa wakilima walilima vizuri na kuhakikisha mazao yale yametoka kwa wingi na kuweza kuuza kupata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizidi kuiomba Wizara ya Elimu isimame vizuri kuangalia hiyo mitaala hata kama ni mtoto anakwenda kusoma kama anasomea kilimo, akitoka pale akaweze kulima na kuangalia ni nini kitakachoweza kumpatia manufaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio mchango wangu, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ya kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwa kunijaalia afya njema hata nimesimama katika Bunge hili na kuchangia hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Mapendekezo ya Mpango ni mazuri sana na yana faida kubwa kwa Watanzania wote. Nami nitajikita zaidi katika hoja ya kukuza na kuchangia uchumi wetu kupitia zao la parachichi. Nina- declare interest nami ni mdau katika biashara ya parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya parachichi ni kubwa sana na ni zao ambalo linaweza kutuletea kipato kikubwa hasa kutuletea pesa nyingi za kigeni kama tukilizingatia na kama Serikali hii itaweza kuliona ni zao bora kabisa la biashara kama mazao mengine kama korosho, pamba au kahawa. Zao hili likisimamiwa vizuri linaweza kutukuzia uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili limekuwa likilimwa na wakulima wadogo wadogo lakini kama likiwekewa mkakati, likatangazwa na wananchi wote wakahimizwa hasa wa Mikoa ya Njombe, Kilolo (Iringa) na Mbeya (Tukuyu) ambapo zao hili linapatikana kwa wingi na ni zao bora kabisa tutaweza kukuza uchumi wa Taifa. Zao hili mpaka sasa limeajiri wanawake wengi sana katika viwanda vya ku- process wakati matunda haya yakipelekwa nje ya nchi. Wanawake wengi ndiyo wanatumika ku-process zao lile mpaka kusafirishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite kuzungumzia changamoto ya zao hili. Kama mimi nikiwa mdau nimeweza kuona changamoto mbalimbali hasa kwenye kusafirisha tunda hili. Matatizo yenyewe ni jinsi ya kusafirisha mazao haya kutoka Njombe kwenda nchi kama Europe kwa sababu zao hili linauzika zaidi Europe pia Middle East hapa Dubai na Arabuni yote kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa sasa ni usafiri hasa kwenye kontena aina ya CL. Kwa Tanzania katika bandari yetu ya Dar es Salaam hakuna kontena kama hizo, inabidi mfanyabiashara wa zao hili aweke booking Nairobi, kontena litoke Mombasa lije mpaka Njombe, likifika Njombe ndiyo upakie ule mzigo urudi tena Mombasa ndiyo uweze kuondoka. Sasa tatizo linakuja wapi? Pale inapotokea tatizo lolote au delay yoyote njiani na mkulima au mfanyabiashara anakuwa ameshachukua matunda yako pale kwenye park house, sasa inapochelewa labda siku moja au siku mbili yale matunda yakija kusafirishwa kufika sehemu husika tayari yanakuwa ni reject. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu iangalie jinsi gani itatusaidia au itawasaidia wakulima na wafanyabiashara wa zao hili kuhakikisha kuna zile kontena za CL au facility za usafiri madhubuti pale Dar es Salaam ili at least mkulima tunda linaposafirishwa kufika kule Ulaya liwe katika hadhi na ubora wa Kimataifa. Ombi langu sasa kwa Serikali ni kuangalia hivyo vitu muhimu hasa upande wa makontena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningeomba zao hili lihamasishwe sehemu mbalimbali, najua hata Bukoba au Ngara linakubali kabisa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika afya ya mama mjamzito na mtoto. Pamoja na jitihada za Serikali iliweza kupunguza vifo vya uzazi kwa kina mama kwa wastani kutoka 11,000 mwaka 2015 mpaka kufikia 2020 iliweza kupunguza wastani wa vifo 3000 kwa Taifa zima.
Mheshimiwa Spika, takwimu za Kanda ya Ziwa zinaonyesha kuwa mwaka 2019 wakinamama 448 walipoteza maisha; mwaka 2020 wakinamama 410 walipoteza maisha na mwaka 2021 wakinamama 374 walipoteza maisha pia. Ukiangalia takwimu hizi utaona vifo vinapungua lakini bado hali sio nzuri.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa zote za magonjwa sababishi ya vifo hivi ambayo ni kifafa cha mimba; kutoka damu nyingi kabla na baada ya kujifungua na uambukizi wa vimelea kwenye mfumo wa uzazi. Ushauri wangu mwingine ni kupeleka madaktari bingwa wa kinamama hasa katika hospitali za Wilaya na Mikoa kwani watabaini matatizo mapema na kuweza kuyapatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika, pia napenda kuchangia kuhusu ugonjwa wa saratani. Shirika ia Saratani Duniani (International Agency for Research on Cancer - IARC) takwimu zinaonesha kwa mwaka kuna visa vipya vya saratani 40,500 hapa Tanzania. Wagonjwa wengi wanatoka Kanda ya Ziwa na wanahudumiwa na Hospitali ya Rufaa Bugando. Wagonjwa wanaofika Bugando wanaongezeka kwa kasi sana kwa siku wanaohitaji huduma ya mionzi ni 180 lakini hospitali ya Bugando ina uwezo wa kutibu watu 80 tu kwa siku hali inayosababisha ucheleweshaji wa matibabu.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iharakishe uletaji wa mashine mpya za kisasa na kuongeza wataalamu ili kuboresha huduma hizi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na uhai na leo nipo katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa kwenye ushuru wa vitenge vinavyotoka nje ya nchi, ukilinganisha na nchi za jirani zinazotuzunguka. Hapo awali vitenge vilitozwa kodi ya 0.28 kwa yadi moja ambayo nadhani sijui ni mita moja, ambapo tulipata wateja wengi sana kutoka nchi mbalimbali za jirani kama vile Zambia, Comoro, Msumbiji, Kongo, Malawi na Zimbabwe, Kenya na Uganda, kwa sababu kodi hiyo ilikuwa ni Rafiki, ilikuwa inaweza kulipika na hata vile vitenge vikaweza kuuzwa kwa bei nafuu. Baada ya muda nchi yetu au Serikali iliongeza kodi kufikia 0.4 per yard ambapo sasa tulikosa tena wanunuzi kutoka nje tukawa na wanunuzi wa kutoka hapa hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia kuhusu uchumi, uchumi tunauchangia kwa namna nyingi ambapo huyu M-Comoro alipokuwa akija kuanzia anaposhuka Airport au Bandarini au stendi ya basi, anapochukua taxi, mnufaika pale ni dereva taxi au bodaboda au mwenye bajaji. Akifika hotelini atachukua hoteli atalala, lakini asubuhi akiamka anaweza kula kwa mama ntilie, mama ntilie naye akapata kipato chake. Vile vile anapokuja hapa, atahitaji mawasiliano atanunua labda ni vocha, atatumia. Kwa hiyo Kampuni zetu za simu zitapata mapato na vile vile Serikali itapata kodi pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wateja walivyokuwa wakija, hawanunui vitenge peke yake, bali wameweza kununua na bidhaa nyingine muhimu nyingi. Kwa hiyo ilikuwa ni faida kubwa kwa wao kuja hapa Tanzania. Sasa naona kodi mwaka jana ilipandishwa mpaka kufikia dola moja kwa yadi moja lakini katika bajeti hii nimeona wameshusha percent kufikia 0.5 kwa kitenge cha polyester na cotton wameweka ushuru kuanzia 0.6 hadi 0.8 ambayo kodi hii haitawezekana kabisa kulipika. Matokeo yake tutaongeza wafanyabiashara ambao watakuwa wanakwepa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wanunuzi watakwenda kununua nchi jirani, kwa sababu sasa hivi changamoto iliyopo, nchi hizi jirani zote zilizozitaja hapo awali, sasa hivi zinauza vitenge bei rahisi zaidi kuliko Tanzania kwa sababu ushuru wake ni reasonable. Kinachotokea sasa wafanyabiashara wanakwenda kununua nchi jirani vitenge, wanatafuta njia za panya, wanaingiza ili waweze kuuza bei nafuu, lakini vile vile kupata faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu inayoongozwa na Mama yetu mpendwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, najua mama yetu ni mwema na ni mwelewa aangalie katika hili suala zima la vitenge, kwa sababu vitenge hivi mvaaji wa mwisho ni mama, ni kitenge kama hiki nilichokivaa mimi leo na Waheshimiwa wengi walioko humu wamevaa vitenge hivi. Vile vile wauzaji wakubwa wa vitenge hivi ni akinamama, ndiyo wanaouza vitenge, kwa hiyo naomba waangalie kwa jicho lingine kwa kum-support mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie kwa kusema kwamba…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, taarifa.
T A A R I F A
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nilitaka nimpe taarifa mchangiajia anayeendelea kuchangia sasa kwamba kuhusiana na suala la kodi ya vitenge, imepanda kwa asilimia 100. Ilipokuwa asilimia 0.4 vitenge vilikuwa vinalipiwa kwa container la 40 feet shilingi milioni 128. Sasa hivi imepanda kwa asilimia 100 ina maana Watanzania wataenda kutoa container hilo la 40 feet kwa shilingi milioni 400 jambo ambalo biashara hii inakwenda kufa pale Kariakoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kabula.
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo nimeipokea kwa mikono miwili. Ni kweli kabisa. Labda niongeze tena kidogo kusema kwamba, pamoja na kwamba tunalinda viwanda vya ndani lakini viwanda vyetu vya ndani kwanza haviwezi kutosheleza soko lililopo. Soko ni kubwa sana na viwanda vya ndani bado havina hiyo capacity kubwa kiasi hicho, lakini pia kwenye ubora, tukubali tu kwamba bado ndiyo tunaanza, siyo vibaya, lakini ni vizuri tuwe na varieties, yaani tuwe na vitu vingi; vitenge vya aina tofauti. Atakayependa kununua cha Tanzania anunue, atakayependa kununua cha China anunue, atakayependa kununua cha Burundi anunue. Kwa hiyo, naona ni vyema tukaacha soko huria, kila mtu akaweza kuingiza na kuuza; na kila mtu awe na choice yake anayotaka kununua.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Ehe, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba sera ya nchi yetu ni kulinda viwanda vyetu vya ndani. Suala la kwamba vitenge vyetu labda havina ubora, aishauri Serikali kuboresha na suala la kwamba uzalishaji ni mdogo, aishauri Serikali namna ya kuongeza uzalishaji na siyo ku-entertain bidhaa kutoka nje. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa unapokea taarifa?
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana, siipokei kabisa kwa sababu hivi vitenge vya kutoka nje siyo kwamba vimezuia au vitamaliza hili soko la vitenge vinavyotengenezwa nchini. Bado nafasi ya kuuza vile vitenge ipo. Kila vitenge vina watu wake wanaoweza kununua. Siyo kwamba kile kitenge cha Tanzania; labda nitoe mfano mmoja. Mheshimiwa Msongozi anaweza akakinunua kwa sababu wanawake wa Kitanzania au wa Kiafrika kwanza wamejaaliwa, ni mashallah, wana miili mikubwa na maumbo makubwa, vitenge hivi ni vidogo, havitoshi. Hata kwa kufunga mama wa kisukuma aliyepanda kule kijijini, hakiwezi kumtosha, labda achukue vipande viwili. (Vicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa kitenge nimeshamaliza, meseji imeshafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu biashara ya mahoteli. Naomba ni-declare interest; nami ni mdau katika hoteli. Hali ya mahoteli nchini hasa Dar es Salaam na Arusha ni mbaya sana, lakini sijawahi kusikia Mbunge hata mmoja humu anaongelea. Nimekaa kimya, lakini leo nimeona ni vyema niongee kwa sababu hata mimi niko kwenye hiyo sekta. Kwa hiyo, ninaelewa hali halisi, wafanyabiashara wa mahoteli au mahotelia wanachokipitia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna biashara tena kwenye mahoteli hasa hoteli zilizopo Dar es Salaam na Arusha kama nilivyoongea awali, lakini sababu siyo Covid 19 kama watu wanavyotafsiri. Hili tatizo limekuwepo muda mrefu kabla ya Covid 19.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu Tukufu kurudisha tena biashara kwenye sekta binafsi hasa kwenye hoteli. Wajaribu kutuletea tena zile semina, wafanye kazi mbalimbali katika mahoteli yetu ili nasi tuweze kuchangia ushuru katika nchi yetu. Kwa mfano hoteli moja sitaitaja, walikuwa na wafanyakazi 80, lakini hivi ninavyoongea na wewe wana wafanyakazi 15; na waathirika wakubwa waliopunguzwa kwenye kazi hiyo ni wanawake, kwa sababu mahotelia wengi huwa ni wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali hii ijaribu kuangalia ni jinsi gani ita-rescue huu upande wa mahoteli. Kwa kweli hali ni ngumu sana na hatujui hatima yetu ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kutupa amani katika Taifa letu. Pili; napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza na kuiboresha sana Wizara ya Afya. Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya na Makamu wake, Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mollel na watu wote kwa kuongoza vizuri na kwa kuchapa kazi nzuri. Pia ningependa kuwapongeza sana wafanyakazi wote wa Wizara ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali, mwaka 2015 Serikali iliweza kupunguza wastani wa vifo kutoka akina mama 11,000; mpaka kufikia 2020 Serikali iliweza kupunguza vifo 3,000 kwa taifa zima. Nakiangalia takwimu ya Kanda ya Ziwa mwaka 2019 akina mama 448 walipoteza maisha kutokana na uzazi, na mwaka 2020 akina mama 410 walipoteza maisha pia. Mwaka 2021 vifo 374 pia kupoteza maisha mwaka huo, 2020/2021. Hali hii bado si nzuri japo namba zinaonesha kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa zote zinazotibu magonjwa haya yanayosababisha vifo hivi vya akina mama, kama vile magonjwa ya kifafa cha mimba, chinikizo la damu kutoka damu nyingi kabla na baada ya kujingua na uambukizo wa vimelea kwenye mfumo wa uzazi. Pili; kupeleka madaktari bingwa na waganga wa akina mama, hasa katika hospitali za wilaya na mikoa. Hii itasaidia sana kubaini matatizo mapema na kumaliza kabisa tatizo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mwanza Wilaya ya Buchosa Visiwani kuna tatizo kubwa hasa Visiwa vya Maisome, Migingo, Lubalagazi pamoja na Buzikimba. Visiwa hivi vinachangamoto kubwa ya boti maji au ambulance ya kwenye maji. Naiomba sana Serikali itupelekee kule ambulance kwasababu akina mama wengi wanafariki dunia kwa kukosa huduma za haraka.
Mheshimiwa Spika, pia katika Visiwa vya Ukerewe kuna upungufu wa asilimia 56 ya watumishi wa afya, Wilaya nzima ya Ukerewe pamoja na kuwa ni visiwani hakuna x-ray machine; iliyopo kwa sasa niyakizamani sana imekuwa na tatizo la kuharibika mara kwa mara na inapelekea usumbufu wa wagonjwa kutoka pale Ukerewe wapande boti mpaka Mwanza Mjini ndipo waende kutibiwa. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie sana hasa kwenye miundombinu migumu kama Ukerewe kwasababu hakuna usafiri mwingine zaidi ya kupanda meli au boti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba sana Wizara Ummy Mwalimu, namwamini kabisa, ni dada jemedari, hodari sana, ni jembe. Kwa hiyo naomba sana uangalie, hasa akina mama wenzangu kule Ukerewe na huku Bushosa Visiwani ambako kwakweli shida ni kubwa mno. Akina mama wanajifungulia njiani boti ikiharibika kidogo, mabapo inabidi wasubirie mpaka boti nyingine ifike ndiyo waweze kupata usafiri kuelekea Mwanza.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiangalia tena katika Wilaya ya Kwimba kijiji cha Nyambiti Kituo cha Afya cha Nyambiti hakina jengo la upasuaji. Wananchi wamenunua vifaa kwa kuchanga wao wenyewe. Sasa naiomba Serikali iharakishe kutusaidia kutuwekea japo hilo jengo kwasababu wananchi wameshatumia nguvu zao wenyewe kununua vifaa. Kwa hiyo, ninaomba sana, nakuomba sana ndugu yangu mtani wangu Ummy Mwalimu uwaangalie watani zako wa Kijiji cha Nyambiti na uwajengee hilo jengo ikiwezekana hata mwaka huu tutashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, sasa napenda kumwongelea mtoto njiti, ndani ya miezi minne watoto 1,000 huwa wanalazwa hospitalini kwa magonjwa ya aina mbalimbali, lakini asilimia 50 ya watoto hao huwa ni watoto njiti na asilimia 25 katika watoto hao kwenye 50 percent, asilimia 25 ya vifo hivi ni mtoto njiti kwa sababu hawana kinga mwilini. Ushauri wangu kwa Serikali wawekeze upatikanaji lishe inayotolewa kwa njia ya mpira, upatikanaji wa vifaa vya kutunza joto la mwili (incubator) hasa kwenye Vituo vya Afya vya Vijijini kwa sababu sehemu za wilaya nyingi hazina vyumba maalum kwa ajili mtoto njiti. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
MHE.KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)