Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kabula Enock Shitobela (14 total)

MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali langu la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na hali ya hewa au tabia nchi kwa mwaka huu Kenya haikuzalisha vizuri zao la parachichi, hivyo, wafanyabiashara wengi walikuja Tanzania kwa ajili ya kununua zao hili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha wakulima kuongeza kilimo hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima wa parachichi sio dhambi kumuuzia Mkenya kwa sababu ni export ambayo tunakwenda kuuza ingawa lengo letu ni kwenda kwenye final markets. Kwa hiyo, tunaendelea kuwahamasisha wauze.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili tunachukua hatua gani kuongeza uzalishaji? Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maagizo kwa Halmashauri zote ambazo mazao ya parachichi yanalimwa kutenga maeneo angalau ya ekari 10 kwa ajili ya kuzalisha miche na kuigawa kwa wakulima. Wizara ya Kilimo imeshaanza kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa, hii ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili ni kuwatambua wakulima na kuwa register ili mazao yao wanayozalisha yaweze ku-meet international standard na hii project tunafanya pamoja na wenzetu wa FAO ili ku-identify pest. Hatua ya tatu tunafungua masoko. Sasa hivi tunamalizia kufungua soko la South Africa lakini tumeanza negotiation na wenzetu wa China ili tuweze kufungua soko la China na ita-pull yenyewe uzalishaji na wakulima watakwenda sokoni wakiwa na soko la uhakika.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante ukizingatia sisi ndio mama zako au bibi zako lazima uturuhusu ahsante sana. Kutokana na shughuli za uchimbaji madini Mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, tatizo na ongezeko kubwa la kansa kwa Mkoa mzima wa Mwanza kumekuwa na tatizo kubwa la kansa na tunaamini kabisa hii zebaki ndio inayosababisha ongezeko hili la kansa. Je. Serikali ina mpango gani sasa wa kudhibiti kabisa uingiaji wa kemikali hizi, ili kunusuru wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Kabula kwa swali lake ambapo ameulizia kuhusiana na udhibiti.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, hatua ya kwanza tuliyochukua mahali ambako dhahabu inachenjuliwa, inaitwa mialo, mwanzo mialo ilikuwa holela, kila mahali mtu anajenga; sasa tumeamua kuidhibiti ile mialo yote iwekwe kwenye eneo maalum na jumla ya mialo 5,025 imesajiliwa kote nchini.

Mheshimiwa Spika, pili, Chama cha Wachimbaji Wadogo kinaitwa FEMATA pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali wanatengeneza umbrella moja ya namna ya kuagiza zebaki hapa nchini na Mkemia Mkuu wa Serikali ameshatoa hiyo go-ahead lakini changamoto tuliyonayo ni ndogo ndogo tu ya uratibu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya miezi hii miwili uagizaji wa zebaki tutakuwa tumeudhibiti na tutakuwa na source inayoeleka.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vya Mkoa wa Mwanza kama Nyanchenche -Segerema; Nyakafungwa - Buchosa; Gulumungu - Misungwi; Kawekamo, Mwambogwa, Kwimba na Ilemela?
NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo nimeeleza katika majibu ya muda uliopita na Mheshimiwa Naibu Waziri ulivyosema Mkoa wa Mwanza umebakiza vijiji 121; lakini yako maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge maeneo la Ilemela, Nyamagana, Nyamadoke, Nyamongolo pamoja na maeneo yote ya Rwanima tutawapekelea umeme mwezi disemba mwaka unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Mwanza tumepeleka wakandarasi wa aina mbili; wakandarasi wa peri-urbun wanaendelea na maeneo uliyotaja, lakini kuna maeneo ya vitongoji ambayo yana-cover Sengerema mpaka Buchosa ambao wakandarasi wameshafika site tayari. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara inayounganisha Hungumalwa - Ngudu Wilaya ya Magu, imekuwa ikiwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2005, 2010, 2015 mpaka 2020 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, sasa ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula, Mbunge wa Viti Maalum Mwanza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Hungumalwa kwenda Ngudu ipo kwenye mpango na ipo kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Serikali imeahidi kuifanya. Ahsante. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi napenda niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati miundombinu ya maji katika Jimbo la Kwimba, Misungwi, Ilemela, Sengerema na Nyamagana?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Serikali imeendelea kujitahidi na inaendelea kuwekeza kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga miundombinu mipya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Mathalani kwa eneo la Misungwi tumeshakwenda na Mheshimiwa Rais na tumekwishazindua mradi mkubwa wa zaidi ya Bilioni 12 katika kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wilaya ya Ilemela inajenga Kituo cha Polisi kwa nguvu za wananchi eneo la Nyamuhongolo. Aliyekuwa Waziri wa Mambo na Ndani Mheshimiwa Kange Lugola alitoa ahadi ya mifuko 100 ya cement. Je, ni lini Wizara ya Mambo ya Ndani itatimiza ahadi hiyo? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mwanza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Ilemela pamoja na halmashauri yao kwa kuanza ujenzi wa kituo cha Polisi eneo la Nyamuhongolo tunawaunga mkono. Tutafuatilia ikiwa kweli Waziri wetu alitoa ahadi hiyo kuona uwezekano wa kuitekeleza ili isionekane kwamba Serikali inadanganya raia wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa sana ya kuhamasisha wawekezaji kuja nchini. Mkoa wa Mwanza kuna eneo zuri sana na kubwa sana maeneo ya Nyamuhongoro lililopangwa kuwa industrial pack.

Je, Serikali ina mpango gani kuendeleza eneo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli lengo la Serikali sasa ni kuanzisha industrial pack nyingi katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo eneo hili la Mwanza. Katika Bajeti ya Mwaka huu tumeshaweka fedha kiasi kwa ajili ya kuanza kuweka maeneo haya ya industrial pack kwa ajili ya kuwezesha wenye viwanda kuwekeza katika maeneo ambayo yana miundombinu wezeshi ikiwemo majengo na barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunalichukua eneo hili pia la Mwanza ambalo ni muhimu sana kwa ajili ya kuwekeza viwanda nalo pia tutaliweka katika mipango ili kuhakikisha tunafikisha azma ya kujenga viwanda maeneo yote katika nchi yetu. Nakushukuru sana.
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, je, sasa Serikali imeshafanya utafiti kujua ni watumishi wangapi watawapeleka, na je, kwenye hizi ajira mpya watapeleka watumishi wangapi kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake specific kwa Mkoa wa Mwanza kwamba tutapeleka watumishi wangapi, labda tu nimwambie kwamba inajulikana kwamba kwenye level ya zahanati wanahitajika watumishi wangapi, kwenye level ya kituo cha afya inahitajika watumishi wa wangapi kwenye level ya hospitali ya wilaya wanahitajika watumishi wangapi mpaka tunapofika Taifa. Lakini kama kawaida kutokana na bajeti na uwezo wa Serikali imekuwa si rahisi kuhakikisha tunawapata wote kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali ilitangaza juzi ajira 32,000 nimuombe Mheshimiwa Mbunge ili nisije nikamwambia data ambazo si sahihi tuje tukae tuangalie specifically Mkoa wa Mwanza kwenye ajira hizi wanapata watumishi wangapi kwenye eneo hilo.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kuna uwepo wa teknolojia mbadala, je, Serikali Serikali itaanza lini kutoa elimu ya matumizi ya matumizi ya teknolojia mbadala?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba matumizi ya teknolojia mbadala yapo na yanafanyika kwa wachimbaji wa kati na wakubwa lakini wapo pia wachimbaji wadogo ambao wana uwezo wa kununua mahitaji hayo, wanaendelea nayo. Sasa, sisi kama Wizara tunaendelea kutoa elimu ya uchimbaji salama kwenye migodi ikiwemo matumizi ya teknolojia mbadala.
MHE. KABULA E. SHITOBELA; Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Serikali imeshaandaa mkakati maalum wa kukabiliana na changamoto ya viumbe vamizi. Je, ni lini mkakati huu utaanza kufanya kazi rasmi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shitobela kuwa mkakati huu umeshaanza kufanya kazi na umeshaanza kufanya kazi takribani karibu miaka miwili nyuma iliyopita. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta kama vile Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo lakini pia Wizara ya Mifugo na sisi Mazingira tumekuwa tukishirikiana kwa karibu sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunashirikiana kwa ajili ya kutoa elimu na takribani vikundi 40 tumeshavipa taaluma namna bora ya kutumia ziwa hili na kupunguza huu ueneaji wa haya magugu maji.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kutafuta fedha, lengo na madhumuni ikiwa ni kuhakikisha kwamba, tunapambana na hili jambo kwa sababu ni jambo ambalo Ziwa Victoria limeingiza nchi tatu au nchi nyingine.

Kwa hiyo, sisi huku tukiyakata kwa wenzetu yanaendelea kumea, kwa hiyo na mwisho wa siku yanarudi tena kwetu, lakini hata hivyo tunaendelea kupambana changamoto hii, nakushukuru.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, je, ni lini ujenzi wa Barabara ya Hungumalwa – Kwimba kwenda Magu utaanza?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara aliyoitaja ya Hungumalwa – Ngudu – Bukwimba hadi Magu ni barabara ambayo kumekuwa na watu wengi ambao wameipigia kelele sana. Hata hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka wa fedha ambao bajeti tayari imeshapitishwa barabara hii imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sababu usanifu ulishakamilika tayari, ahsante.

MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkoa wa Mwanza una hospitali na vituo ambavyo bado havijapata huduma hii ya chumba cha mtoto njiti.

Je, Serikali lini itakamilisha kutuwekea vyumba maalum kwa mtoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anavyosema lakini kwenye hospitali ya Sekou-Toure ya Mkoa wa Mwanza ujenzi mkubwa sana unaendelea, suala ni kwenda kuamua na kuweka vifaa kwenye eneo hilo ili watoto waweze kupata huduma. Nafikiri anazungumzia Mkoa mzima kwa ujumla na hasa maeneo ya visiwani. Kwa mfano, Ukerewe ambako ni Visiwani sasa hospitali ya Wilaya ile inaenda kujengwa kwa level ya hospitali ya Mkoa ili mambo yote ya Rufaa ya Mkoa yaweze kutolewa huko huko Visiwani. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya ziara na kugundua matatizo mbalimbali kwenye maeneo na kuelekeza fedha kadri ya mahitaji ya maeneo husika. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kituo cha Polisi Kata ya Kiseke, Ilemela hakina nyumba ya askari na kusababisha kituo kufungwa saa 12.00 jioni. Je, Serikali itakamilisha lini nyumba hiyo ili kuepusha kituo kufungwa saa 12.00 jioni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo la Kiseke ni eneo ambalo lina shughuli nyingi za kiuchumi na kibiashara na msongamano mkubwa wa watu na matukio ya uhalifu yapo, na tunatambua kwa juhudi za Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum na Mbunge wa Jimbo la Ilemela wamekuwa mara kwa mara wakisumbua Wizarani ili waweze kujengewa nyumba hii.

Mheshimiwa Spika, kwa vile wameshaanza ujenzi niahidi tu kwamba kupitia Jeshi la Polisi chini ya Mfuko wa IGP wa Tuzo na Tozo, tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge ili kupata fedha za kukamilisha kituo hicho hasa baada ya kufanya tathmini ya kiwango cha fedha zinazohitajika. Nashukuru.
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkoa wa Mwanza una hospitali na vituo ambavyo bado havijapata huduma hii ya chumba cha mtoto njiti.

Je, Serikali lini itakamilisha kutuwekea vyumba maalum kwa mtoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anavyosema lakini kwenye hospitali ya Sekou-Toure ya Mkoa wa Mwanza ujenzi mkubwa sana unaendelea, suala ni kwenda kuamua na kuweka vifaa kwenye eneo hilo ili watoto waweze kupata huduma. Nafikiri anazungumzia Mkoa mzima kwa ujumla na hasa maeneo ya visiwani. Kwa mfano, Ukerewe ambako ni Visiwani sasa hospitali ya Wilaya ile inaenda kujengwa kwa level ya hospitali ya Mkoa ili mambo yote ya Rufaa ya Mkoa yaweze kutolewa huko huko Visiwani. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya ziara na kugundua matatizo mbalimbali kwenye maeneo na kuelekeza fedha kadri ya mahitaji ya maeneo husika. (Makofi)