MHE. JUMANNE A. SAGINI Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itazipatia umeme kaya na vitongoji ambavyo havijapatiwa umeme Wilayani Butiama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini, Mbunge wa Butiama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika mitaa na vitongoji ambavyo havijapata umeme ikiwemo Wilaya ya Butiama. Serikali imeanza maandalizi ya kutekeleza mradi unaohusishwa ujenzi wa miundombinu ya umeme ya njia ya msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu wa kilometa 1,620, ufungwaji transforma 648 na kuunganisha wateja wa awali 48,600 katika vitongoji 648 nchini ikiwa ni pamoja na kaya na vitongoji vya Wilaya ya Butiama ambavyo havijapata umeme. Gharama ya mradi huuni shilingi bilioni 75. Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza julai, 2021 na kukamilika mwezi Desemba, 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huu kutatimiza azma ya Serikali ya kufikisha huduma ya umeme katika vitongoji vyote vya Wilaya ya Butiama.
MHE. JUMANNE A. SAGINI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Kata za Bwiregi, Nyamimange, Buswahili na Sirorisimba zinapata maji ya Ziwa Victoria kwa kuwa Mradi wa Maji wa Mgango – Kyabakari – Butiama hautazifikia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini, Mbunge wa Butiama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Kata za Bwiregi, Nyamimange, Buswahili na Sirorisimba zinapata huduma ya majisafi na salama, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 imekarabati miradi ya maji katika Vijiji vya Kamgendi, Masurura, Kongoto, Kitaramanka na Rwasereta.
Mheshimiwa Spika, kazi zilizofanyika ni ukarabati wa vituo 42 vya kuchotea maji, kukarabati bomba kuu na bomba la kusambaza maji kilometa 18.5. Ukarabati wa nyumba ya mitambo ya kusukuma maji, ununuzi na ufungaji wa pampu, ufungaji wa umeme wa TANESCO katika Kijiji cha Masurura. Ukarabati wa miradi hii umekamilika ambapo wananchi wapatao 12,220 wananufaika na huduma ya maji kuanzia mwezi Machi, 2021.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji katika Kata za Nyamimange, Buswahili, Bwiregi na Sirorisimba, Serikali imepanga kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji yenye lita za ujazo 150,000, 90,000. Ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 30, ulazaji wa bomba kuu na bomba la kusambaza maji jumla ya urefu wa kilometa 26. Ujenzi wa nyumba za mashine, ujenzi wa nyumba za jumuiya za watumia maji na ufungaji wa mfumo wa umeme.
Mheshimiwa Spika, miradi hii ikikamilika itanufaisha wakazi wapatao 7,024 wa kata hizo. Katika mpango wa muda mrefu, huduma ya maji itaboreshwa katika Kata ya Bwiregi, Nyamimange, Buswahili na Sirorisimba na maeneo mengine kupitia upanuzi wa mradi wa maji Mugango, Kabari na Butiama.
MHE. JUMANNE A. SAGINI aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Teknolojia na Kilimo, Butiama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini Mbunge wa Butiama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza mchakato wa kukijenga Chuo Kikuu cha Teknolojia ya Kilimo cha Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Butiama. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imetenga Dola za Kimarekani Millioni 44.5, sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 103 kupitia mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa ajili ya Elimu ya Juu uitwao Higher Education for Economic Transformation-HEET. Mradi wa HEET unatekelezwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na Benki ya Dunia kuanzia mwaka huu 2021 mwezi Septemba.
Mheshimiwa Spika, yapo baadhi ya maandalizi muhimu yaliyokamilika ambayo ni pamoja na: kupatikana kwa hati miliki ya eneo lenye ukubwa wa ekari 573.5; uandaaji wa mpango kabambe (master plan); tathmini ya athari ya mazingira (Environmental and Social Impact Assessment); na usanifu wa majengo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa taratibu zinazofuata ni kumtafuta mshauri mwelekezi, na atakapopatikana atafanya kazi ya mapitio ya michoro na kuandaa hadidu za rejea na makabrasha ya zabuni ili kutangaza na kumpata mkandarasi. Michakato hiyo itakapokamilika ujenzi huo utaanza rasmi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.