Supplementary Questions from Hon Sagini Jumanne Abdallah (4 total)
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Jimbo la Butiama lina vitongoji 370, katika awamu zote mbili nilizopita za REA ni vitongoji 147 tu vilipata umeme sawa na asilimia 40. Sasa Naibu Waziri ananihakikishiaje kwamba pia kama njia ya kumwenzi baba wa Taifa, vitongoji 223 vilivyosalia vitapata umeme katika awamu ijayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; sera ya Wizara ni kwamba unapopita umeme taasisi za elimu au afya zilizoko katika maeneo hayo zinapaswa pia kuhakikisha kwamba zinafungiwa umeme, lakini ninazo taarifa katika Jimbo la Butiama zipo shule za sekondari, vituo vya afya na zahanati ambavyo havijapata umeme. Je, Waziri atanihakikishiaje kwamba vituo hivyo vinapata umeme, orodha ninayo ndefu lakini atuhakikishie kwamba TANESCO walioko kule wanaweza wakashusha umeme kabla ya utekelezaji ya awamu ijayo anayosema inayoanza mwezi Julai?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sagini, Mbunge wa Butiama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Butiama ni mojawapo ya Wilaya ambayo tayari zimepata umeme katika vijiji vyote vilivyoko na kweli kuna baadhi ya vitongoji ambavyo havijapata umeme. Upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ni zoezi endelevu na ni kwa awamu na tunapeleka umeme katika maeneo haya kupitia TANESCO kufanya kazi zao za kila siku lakini pia kupitia katika miradi tuliyokuwa nayo ambayo ilikuwepo densification I, densification IIA, IIB na sasa mwezi wa Saba tutaanza densification IIC ambapo kama tulivyosema tutapeleka vitongoji 648.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vitongoji vyote vilivyoko katika Wilaya ya Butiama, awamu kwa awamu vitapelekewa umeme na vyote vitapatiwa umeme vyote kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, nipende kusema kwamba ni kweli zipo baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikiachwa bila kupelekewa umeme, lakini wakati wa kuzindua mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, maelekezo ya Wizara ambayo yalitolewa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati, yalisema kwamba katika kupeleka umeme katika awamu hii ya tatu, kisiachwe kijiji au eneo lolote ambalo lina taasisi ya umma ambayo haitapelekewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu nirudie maelekezo yake kwamba wakandarasi wote wanaopeleka umeme katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili, wasiache kupeleka umeme katika taasisi zote za umma ambazo ziko katika maeneo yetu. Vile vile, uniruhusu nisisitize maelekezo mengine mawili ambayo Mheshimiwa Waziri aliyatoa, mojawapo ikiwa ni kwamba watakapokwenda Wakandarasi kupeleka umeme katika maeneo yetu, pamoja na watu wengine na taasisi nyingine watakazoenda, wahakikishe wanapiga hodi kwa Waheshimiwa Wabunge ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuwaonyesha maeneo ambayo yana changamoto zikiwa ni pamoja na hizo ambazo ni taasisi zetu za umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo la mwisho, alilolitoa ni kwamba ni lazima upelekaji wa umeme ukamilike ndani ya muda ambayo ni kufikia Disemba, 2022.
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu fasaha ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini kama alivyosema mradi huu wa Mugango, Kiabakari, Butiama ndio kwanza wanaanza utekelezaji. Lakini, kwa kuwa Mji wa Musoma una maji mengi kiasi Wizara imewahi kutamka kwamba, wingi wa maji mpaka mabomba yanapasuka na umbali kutoka Musoma mpaka baadhi ya hizi Kata anazozitaja ni mfupi. Kwa nini Serikali isiamue kutoa maji Musoma Mjini na kuyafikisha vijiji vya Kata za Bukabwa, Nyankanga na Bwiregi, ikiwemo Ryamisanga, Kamugendi, Kitasakwa na Masurura? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, ni lini Serikali itaanza kutumia Mto Mara kama chanzo cha maji na kuyapeleka kwenye vijiji vya Kata za Nyamimange, Buswahili na Sirorisimba? Vikiwemo Wegero, Paranga, Kongoto, Buswahili, Nyambiri, Rwasereta na Kitaramanka. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ameeleza Mji wa Musoma una maji mengi ni kweli na ni dhahiri wakati wote huduma ya usambazaji maji huwa ni rahisi, ila kupata chanzo cha maji ndio kazi. So, kwa sababu tayari maji Mji wa Musoma ni mengi, nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri tayari watendaji wetu wameweka katika mipango mikakati yao. Kadri tutakavyopata fedha, watahakikisha tunaendelea kutumia hiki chanzo tulichonacho, ili kunusuru yale mabomba yasiendelee kupasuka tutasogeza huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni matumizi ya Mto Mara. Naamini wakati wa usomaji wa bajeti hapa Mheshimiwa Waziri alijidadavua ya kutosha kwamba, maji yote ya mito mikuu huu ndio mpango wa kuona kwamba, Wizara inakwenda kuyatumia kwa vyanzo vya uhakika. Hivyo, Mto Mara pia, ni moja ya Mito ambayo kama Wizara, tunatarajia tuitumie kama chanzo cha uhakika. Hivyo, kulingana na namna tutukavyokuwa tunapata fedha, tutahakikisha mito na maziwa makuu yote tunakwenda kuyatumia kwa ufasaha. (Makofi)
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kuhusu maji Busega. Lakini tatizo la maji Busega linakaribia kufanana na tatizo la maji Butiama. Huu ni mwezi wa tano kwenye Kijiji cha Butiama cha Baba wa Taifa hawajapata maji na wataalam wanasema ni tatizo la mashine. Sasa Naibu Waziri atuambie lini wananchi wa Butiama wataweza kupata maji kutoka Ziwa Victoria? Na ambapo tayari kuna bomba lililochakaa lakini tatizo ni mtambo unashindwa kusukuma. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sagini, Mbunge wa Butiama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tunatambua eneo lile miradi ni mchakavu lakini tayari tumeshaelekeza wataalamu wetu kuweza kuipitia na ukarabati kufanyika, pamoja na mradi wa muda mrefu mradi wa Ziwa Victoria nao upo katika mipango mkakati ya Wizara.
MHE. JUMANNE A. SAGINI Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, kwa kweli yanaleta matumaini. Hofu yangu ni moja tu, kwamba hizi lugha za mchakato, mchakato wakati mwingine unaweza ikachukua muda mrefu. Wakati nachangia hotuba ya bajeti ya Wizara hii, waliniahidi kwamba mwaka wa fedha utakapoanza utaanza harakati za ujenzi. Lakini hadi leo wanazungumzia mchakato, sasa hebu atuhakikishie hii michakato ya ku- procure huyo consultant ili afanye review ya hizi design zitakamilika lini na ujenzi uweze kuanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini, Mbunge wa Butiama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika kama nilivyoeleza kwenye jawabu la msingi kwamba taratibu zote sasa zimekamilika; na upatikanaji huu wa fedha kama nilivyozungumza kwamba umeanza mwezi wa Septemba. Tunatarajia kama mambo yote yatakwenda vizuri mpaka kufika mwezi wa Februari shughuli za ujenzi katika eneo hili inawezekana zikawa zimeanza rasmi. Ahsante sana.