Supplementary Questions from Hon Norah Waziri Mzeru (12 total)
MHE. NORA W. MZERU: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kutokana na migogoro ya muda mrefu, baina ya wafugaji na wakulima nchini hususani Mkoa wangu wa Morogoro. Je, Serikali itawasaidiaje wafugaji maeneo ya malisho ili kuepusha migogoro na wakulima? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nora Waziri Mzeru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro, tunayo Ranch yetu ya Taifa ya Mkata. Tumekwisha kuanza utaratibu wa kuwagawia wafugaji wenyeji wa Mkoa wa Morogoro. Hadi sasa tumeshatoa vitalu saba, kwa ajili ya wafugaji katika eneo hili na utaratibu huu unaendelea. Pia, Wizara inayo mkakati wa maeneo yake ambayo tumekubaliana kwamba, yako chini ya kiwango cha matumizi ikiwemo baadhi ya Ranch LM News na Holding Grounds. Hizi zote tunazitazama na kuhakikisha kwamba tutazipima na kugawa vitalu baadhi kwa wafugaji walioko maeneo mbalimbali nchini. Ili kuweza kuwasaidia kuondokana na hamahama na kwenda kugombana na wafugaji na wakulima. Ahsante sana.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, je, kuna mpango gani wa kuwavutia wawekezaji katika sekta ya utalii Morogoro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Norah Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Norah kwa kuendelea kuimarisha utalii, lakini pia kuendelea kuhamasisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo maeneo yaliyohifadhiwa katika Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Spika, nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweza kuainisha maeneo mbalimbali kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya kuwekeza na shughuli hizi za uwekezaji zinahamasishwa katika maeneo mengine mengi ambayo utalii unafanyika. Hivyo, nimtoe wasiwasi katika hifadhi ya Udzungwa, Mikumi, pamoja na Nyerere, tumetenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji. Hivyo, tunaendelea kuwaalika wawekezaji wa ndani ya nchi na nje ya nchi waweze kufika katika maeneo hayo na kuwekeza kwa ajili ya kuongeza na kukuza utalii. Ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina swali langu la nyongeza, Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Watanzania wa hali ya chini wanapata elimu ya madhara ya kutumia nishati chafu ya kupikia na kuona umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya Wizara ya Nishati ya Mwaka huu wa Fedha, tulieleza moja ya kipaumbele kikubwa ni kuhakiksha kwamba nishati safi na salama ya kupikia inawafikia Watanzania walio wengi. Katika jitihada hizo, elimu kwa Watanzania kuhusu madhara ya nishati chafu ni jambo la muhimu. Itakumbukwa kwamba tarehe 01 Novemba mwaka uliopita Mheshimiwa Rais alizindua mjadala wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia na alitoa maelekezo mahusus ikiwemo ya mjadala ule kuendelea katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza, Serikali inaandaa dira ya kuelekea katika nishati safi ya kupikia, dira ambayo itajumuisha elimu kwa umma, elimu ambayo itawafikia Watanzania wote kila mahali walipo. Kwa hiyo, tutazindua dira hiyo mwezi Juni.
MHE. NORA W. MZERU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu mkubwa wa kutenga maeneo ambayo hayana migogoro na ardhi ili kuwaruhusu wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo hayo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka kujibu swali ambalo ameliuliza Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na masuala ya utengaji maeneo ya uwekezaji. Maelekezo ya Serikali katika mikoa yote na katika halmashauri zote ni kuhakikisha kwamba wanatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na maeneo yale lazima yatambuliwe ili yaweze kuwa tayari kwa ajili ya uwekezaji na kama kuna suala pengine la wananchi katika maeneo yale wanatakiwa waongee nao na waweze kuyamiliki kama ni halmashauri yenyewe au ni Serikali ya Kijiji ili muwekezaji anapopatikana kusiwe na mgogoro.
Mheshimiwa Spika, pia tunayo yale maeneo ya EPZ ambayo yapo yalikuwa yametengwa nayo yamewekwa kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo kwa maana ya Serikali tayari tunalitambua hilo katika kuepusha migogoro na wananchi. Na niombe Mbunge anione kama kuna eneo maalum ambalo pengine linahitaji maelezo ya ziada.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara ya Isimilo - Kilombero ili kuwasaidia wakulima kupitisha mazao yao kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii naamini inatengenezwa na inakarabatiwa, changamoto kubwa ambayo tunayo sasa hivi ni barabara nyingi katika kipindi hiki cha mvua kunatokea changamoto, pia nitoe tu maelekezo tena kwa Meneja wa Singida kuhakikisha kwamba anaisimamia hii barabara na inapitika muda wote wakati huu wa kilimo kwa wananchi, ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini Serikali itawekeza fedha kwenye kuutangaza Mlima Uluguru kama kivutio kizuri cha utalii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa maporomoko haya yanaleta mvutio mkubwa kwa utalii.
Je, ni lini Serikali ina mpango wa kuyatunza na kuhifandhi mazingira yaliyozunguka maporomoko hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutapita vizuri kwenye Jibu la msingi tulisema kwamba Serikali kupitia mfuko wa UVIKO tayari tulishawekeza pale takribani shilingi 214.3 ilikuwa lengo na madhumuni ni kujenga ile miundombinu ya barabara ya kilomita nane kutoka barabara kuu kuelekea kwenye kivutio hichi. Lakini kiubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti yetu ambayo tunategemea kusoma hivi karibuni tutahakikisha kwamba tutatenga fungu maalumu la kutengeneza miundombinu rafiki katika kituo ama katika kivutio hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili nimwambie tu kwamba ipo mikakati kabambe ambayo Serikali na Wizara tumeshaichukua kuhakikisha kwamba tunatunza mazingira katika eneo hili. Tumeshakaa sisi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini pia tumeshakaa na watu wa Halmashauri pamoja na TFS kuhakikisha kwamba, la kwanza tunakwenda kupanda miti ya kutosha, lakini tulishatoa maelekezo kwa kuwaambia wananchi waliozunguka maeneo yale kwamba wasifanye shughuli zozote za kibinadamu katika meneo yale, ikiwemo za ufugaji, kilimo na nyingine. Lengo na madhumuni ni ili tutunze kivutio, tuvute watalii lakini pia tuongeze pato, nakushukuru.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina swali moja la nyongeza.
Je, Serikali itawasaidiaje wamiliki wa nyumba za kulala wenye nia ya kubadilisha matumizi na kuzifanya hostel hasa katika suala la tozo za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mzeru kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la kubadilisha matumizi ya nyumba pamoja na ardhi yapo kwa mujibu wa sheria, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu hizo wamiliki wa nyumba pamoja na ardhi wanapaswa kuzifuata, lakini kwa vile wanafanya biashara ni lazima zile taratibu zingine za tozo pamoja na kodi ya Serikali ni lazima zilipwe. Kwa hiyo, ni muhimu kwa wale wamiliki wanapobadilisha matumizi kwenda kwenye mamlaka husika kutoa taarifa ya kubadilisha zile leseni zao za biashara ili waweze kupata tozo ambayo ni sahihi. Ninakushukuru.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii; je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati barabara ya kutoka Nanenane – Tungi kupita VETA kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tumekuwa na utaratibu wa kufanya matengenezo ya barabara zote kwa kiwango cha lami, kwa hiyo hata mwaka unaokuja wa fedha tumetenga kwa ajili ya kukarabati maeneo yote ambayo yameharibika ili kuhakikisha kwamba barabara inarudi kwenye ubora wake. Ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante ni upi sasa mkakati wa Serikali wa kujenga barabara zote za Morogoro ili ziweze kupitika msimu mzima?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE). Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba baabara zote za Mkoa wa Morogoro zinapitika ni pamoja na kuzijenga zile ambazo tumeziainisha kwa kiwango cha lami, lakini pia kuzitengea fedha barabara zote kwa ajili ya ukarabati na kuna barabara ambazo tayari zipo kwenye kutangazwa kwa ajili ya kuzijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha barabara zote zinapitika mwaka mzima, ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Serikali imejipangaje kuendeleza vipaji vya vijana hao? (Makofi)
Swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo mashuleni na kwenye vyuo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Norah kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mpango wa Serikali kuendeleza vipaji, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kwa kushirikiana na TFF tunaandaa mashindano mbalimbali ya vijana ili vipaji ambavyo vimeweza kupatikana viweze kukuzwa na kuendelezwa kupitia mashindano hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kuna ligi ya under 17, lengo ni kuonesha vipaji hivyo vinakuwa vipi, tuna UMISETA na UMITASHUMTA ambayo kesho Mheshimiwa Waziri Mkuu ataenda kufungua kule Tabora. Mashindano hayo yote yana lengo la kuhakikisha kwamba vipaji vinavyopatikana vinaweza kuendelezwa. Katika kituo cha TFF Tanga na Dar es salaam mafunzo ya kuendeleza vipaji hivyo yanaendelea na hata hivi sasa ninavyoongea wataalamu wapo wanatoa mafunzo hayo. Kwa hiyo, tunahakikisha vipaji hivyo vitaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, katika bajeti tuliyopitisha mwaka huu tarehe 23 Mei, tulisema Serikali ina mpango wa kujenga shule 56 ili kuzibadilisha kuwa shule za michezo. Shule hizo 56 ambazo zitakuwa ni shule mbili katika kila mkoa Tanzania Bara na Visiwani zitakuwa ni mahususi kwa kuchukua vipaji hivyo na kuviendeleza, lakini kuendeleza miundombinu ya michezo katika mashule hayo. (Makofi)
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri ya Serikali katika kuendelea kuajiri walimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira ya kazi na motisha kwa walimu, hususan wale wanaoishi na kufanya kazi vijijini? Hili ni muhimu, ili kuzuia walimu wengi wanaokimbilia mijini na kusababisha upungufu wa walimu vijijini. Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni hoja ya msingi na Serikali inatambua umuhimu wa motisha kwa walimu, hasa wale wanaofanya kazi vijijini, ili waweze kufanya kazi kwa hamasa. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali katika eneo hili kwanza ni kujenga nyumba za kuishi kwa walimu, ili kuboresha mazingira yao ya kazi wanapokuwa wanafanya kazi katika maeneo yao ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imekwishajenga nyumba 253 ambazo zinabeba familia mbili. Kwa hiyo, hii ni sehemu ya mkakati wa kuboresha mazingira ya walimu wanaofanya kazi vijijini.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, walimu wanalipwa malimbikizo yao na stahiki zao kwa wakati. Katika Mwaka 2022/2023 Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 22.73 za madeni ya walimu yasiyokuwa ya mishahara. Kwa hiyo, hii ndiyo mikakati ambayo Serikali inaendelea kufanya, ili kuhakikisha walimu wanaofanya kazi vijijini wanafanya kazi kwa hamasa.
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa moyo wake wa huruma kwa kufanya maamuzi magumu kwa kuwarejesha wasichana waliopata mimba na kukatiza masomo yao. Je, Serikali imetekeleza mikakati gani, ili kuhakikisha wahanga wa ubakaji wanapata sauti na mifumo ya Sheria na haki inaboreshwa, ili kuzuia wasichana wasikatishe masomo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Norah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali langu la msingi, zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuwalinda watoto wetu wa kike dhidi ya ubakaji na ukatili kwa ujumla. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi wawapo shuleni, ujenzi wa mabweni pamoja na hosteli, kuanzisha madawati ya ushauri nasaha kwenye maeneo yetu ya shule na mpaka vyuoni kwa ujumla. Aidha, Serikali imeendelea na utoaji wa elimu kwa jamii, hususan dhidi ya vitendo hivi vya ukatili kwa watoto.
Mheshimiwa Spika, vitendo vya ubakaji ni kosa la jinai na adhabu yake inatolewa chini ya Sheria ya Adhabu, Kifungu Na. 16 ya Sheria yetu ya Bunge. Sheria hiyo inatoa adhabu kali ikiwemo kifungo cha miaka 30 au zaidi ya hapo. Kwa hiyo, hii ni mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba, vitendo hivi vinakomeshwa kwenye jamii yetu. Nakushukuru sana.