Contributions by Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza (32 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nipende kusema kwamba Serikali ya CCM inafanya vizuri kwenye eneo la elimu au Sekta ya Elimu kuna mafanikio makubwa sana tumeyapata kila mtu anayajua, lakini kwa vile kuna watu ambao wanajifanya hawayajui ni bora nirudie kidogo kwa ufupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kila Kata ina shule ya sekondari, nyingine mbili, nyingine tatu Kata moja. Kila Kijiji kina shule ya msingi, haya ni mafanikio makubwa; vyuo vya elimu ya juu mwaka 2005 kila mwaka tulidahili wanafunzi 36,000m leo tunadahili wanafunzi 150,000 vyuo vya elimu ya juum haya ni mafanikio makubwa. Leo tumesema elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi la kumi na mbilim haya ni mafanikio makubwa. Niipongeze Serikali, Wizara ya Elimu na CCM kwa ujumla, kazi nzuri, tumeweka misingi mizuri katika kuboresha elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kuna kazi ya kufanya, tuboreshe, tumeweka misingi mizuri sasa tuiboreshe. Shule binafsi zinafanya vizuri sana wamesema wenzangu jana hapa na mimi ni mmoja wa wamiliki wa shule binafsi, nitangaze maslahi, lakini shule binafsi zinafanya kazi nzuri sana. Niishauri Wizara isaidie shule hizi za binafsi, isizione kama zinafanya dhambi au kosa, zione kama ni mshirika katika kutoa elimu nzuri kusaidia kuelimisha Watanzania. Kwa hiyo, haya mambo ya ada elekezi wamesema Wabunge wengi, nisirudie, hayana maana, tuwaachie wenye shule wafanye shughuli zile, watoe elimu bora, ndio wanaoujua mzigo wanaobeba, mambo ya kupaka mabasi rangi ya njano tuachane nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake tusiwape masharti magumu na yakiwa magumu watashindwa, tutashindwa na mimi nikiwemo, tuwawezeshe ili tuweze kufanya kazi nzuri tuboreshe elimu. Kuhusu kodi wamesema Wabunge hapa kuna mzigo wa kodi haubebeki, watashindwa, tutashindwa kutoa elimu nzuri ambayo kwa kweli ndiyo msingi mzuri wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni kila kitu amesema Mbunge Mheshimiwa Mbatia, elimu ndio roho ya Taifa, ni kweli na mimi naungana naye elimu ndiyo roho ya Taifa, tushirikiane katika kuboresha elimu. Shule binafsi mwaka jana kidato cha nne katika wanafunzi 100 bora, wa kwanza wa pili mpaka wa 100, wanafunzi 97 wametoka shule binafsi. Serikali ni watoto watatu, hawa utawabeza kweli? Sasa hapa ni kuwapunguzia mzigo wa kodi na mzigo wa masharti, maana watashindwa na tutadidimiza elimu, tutadidimiza maendeleo ya Taifa hili. Nasema tuboreshe elimu, tupambane, tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Bukoba Vijijini tuna Sekondari kama nilivyosema za Kata, za wananchi na nyingine 31, lakini hatuna Sekondari ya juu, A Level, hata moja. Imeainishwa moja ya Mahoro Secondary School miaka mingi, lakini hakuna kilichofanyika. Niiombe Wizara, hii shule nayo iboreshwe ipate madarasa ya Form Five na Form Six ili hawa vijana kutoka shule 31 hizi waende kupata elimu pale, elimu ya A Level, tuzidi kupiga hatua twende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Nne ilikazania sana ujenzi wa maabara, jambo zuri sana. Tukajenga maabara kila shule ina majengo ya maabara, lakini hayajakamilika! Sasa naona mkazo umepungua pale, yale majengo mengine yamefika nusu, mengine kwenye linta pale, mengine yameezekwa, mengine hayajakamilika! Tusiyaache haya, yatabomoka, tumechanga pesa kwa tabu sana; kila mwananchi amechangia, hata mimi nimechangia hela nyingi sana kwenye majengo haya ya maabara, tusiyaache yakaporomoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itafute namna ya kusaidia kwa kusaidiana na wananchi hawa waliozijenga hizi maabara zikamilike, ziwe nyumba kamili, ziwekwe vifaa vya sayansi, zitumike kama ilivyokusudiwa; ndiyo maendeleo yenyewe ya elimu kila shule iwe na maabara iliyokamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuko kwenye kazi kubwa ya kuhakikisha kila shule inakuwa na madawati, shule za msingi na sekondari zina upungufu mkubwa sana wa madawati. Kazi inafanyika nishukuru, nimeona hapa katika taarifa Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itatoa mchango wa madawati 168,500 nawapongeza, lakini hayatoshi, waongeze kwa sababu, pale nasikia kuna shilingi bilioni sita kwenye Wizara hiyo ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kusaidia jamii. Hizo shilingi bilioni sita ziende kwenye madawati, ndiyo jamii yenyewe na Wizara nyingine zifanye ziige mfano wa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi nyingine ziige mfano huu, kama Bunge hili limetoa shilingi bilioni sita kwenye madawati na wengine waige mfano huo, ili baada ya muda mfupi madawati yatoshe, vijana hawa wasome katika mazingira mazuri, wasikae chini kwenye vumbi, wakae kwenye madawati ili waweze kusoma vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, kwangu mimi wana madai mengi sana, mafao yao hawalipwi. Mwalimu anahamishwa kituo anaambiwa nenda utalipwa baadaye! Anakaa miaka miwili au mitatu hajalipwa! Hili muliangalie wapate mafao yao. Mwalimu anapandishwa daraja haongezwi mshahara!
Mheshimiwa Naibu Spika, nina Mwalimu mmoja pale amekaa miaka 16 hajapanda daraja, tangu ameajiriwa hadi leo miaka 16, hajapanda daraja! Hajapewa warning kwamba, haendi kazini, anafanya kazi vizuri, miaka 16 hajapanda daraja! Mnamkatisha tamaa, hawezi kufundisha vizuri! Walimu waangaliwe, wapewe motisha inayotakiwa ili waweze kufanya kazi vizuri. Hawa ndiyo wanaotoa elimu, ndiyo wafundishaji, ndiyo wasimamiaji wa sekta nzima ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la juzi la wanafunzi wa Saint Joseph, wale karibu 500. Nasema hawa wasaidiwe wasifukuzwe, 55 ni wengi. Halafu wamekuwa admitted pale wamedahiliwa kwa vigezo vilivyokuwepo! TCU hata kama walikosea, lakini makosa yao siyo makubwa kiasi hicho. Kwa sababu, kama tunasema mtu ana D nne, wamesoma Certificate wakapanda Diploma, sasa wanafanya Degree; ndivyo hata CBE inavyofanya. CBE mtu anaingia ametoka Form Four ana D tatu, anasoma Certificate anamaliza, anaingia Diploma anamaliza, si anaingia Degree, kwa nini hawa watendewe tofauti? Wasaidiwe wapate msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbona tulichukua UPE miaka ya 70, walikuwa darasa la saba, wakapata mafunzo ya miezi mitatu wakawa Walimu wa UPE, mpaka leo ni Walimu wanafundisha shuleni. Baadaye tukachukua hawa vijana wa Form Six, wanaitwa Voda Faster sijui, wakapewa miezi mitatu kozi ya Ualimu, hadi leo ni Walimu wanafundisha! Sembuse hawa ambao wamefaulu vizuri D nne! Wameingia kwenye Certificate wamemaliza, wamesoma Dilpoma, leo wanasoma Degree mnawafukuza! Msiwafukuze, tumelipa hela nyingi Watanzania kwenye kodi zetu, wamesoma miaka mitatu, miaka minne na wengine miaka miwili. Wasaidiwe warudi chuoni wamalize ili wasaidie kupunguza pengo la upungufu wa Walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii uliyonipa ya kuweza kujumuisha hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waliochangia kwa kusema katika hoja hii ni Waheshimiwa Wabunge 22 na wale waliochangia kwa maandishi ni 14. Nitumie fursa hii kumshukuru sana Waziri, Mheshimiwa Angellah Kairuki na Waziri, Mheshimiwa George Simbachawene kwa maelezo yao ambayo wameyatoa hapa ambayo kwa kiasi kikubwa yamejibu hoja mbalimbali ambazo zimeboresha uelewa wa hoja ambazo ningezisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mwaka ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imepata wachangiaji 22 waliochangia kwa kuzungumza na 14 waliochangia kwa njia ya maandishi. Eneo la kwanza wamezungumzia Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) na wamegusia kero zinazowakabili walimu ambazo ni kama ifuatavyo:-
(i) Kutolipwa madai yao ya likizo;
(ii) Uhamisho;
(iii) Mishahara na kadhalika;
(iv) Walimu kunyimwa uhamisho;
(v) Mazingira magumu ya kazi;
(vi) Mrundikano wa wanafunzi darasani, ukosefu wa nyumba za kuishi na kadhalika.
(vii) Kushushwa vyeo kwa walimu na matamko ya watawala – Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya;
(viii) Bajeti ya Tume iongezwe ili iweze kujitanua katika wilaya nchi nzima;
(ix) Kasoro zilizobainika katika Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu zirekebishwe ili kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili walimu; na
(x) TAMISEMI ihakikishe inatenga fedha za kutosha katika bajeti ijayo ili kuondoa kero za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni la utawala bora na rushwa. Katika eneo hili wachangiaji wamebainisha mambo yafuatayo:-
(i) Wasimamizi wa Serikali hawafuati sheria, kanuni na taratibu za utawala;
(ii) Watendaji wasijielekeze katika kuwajibisha watumishi tu bali wawajengee uwezo na mazingira bora ya kazi kabla ya kuwawajibisha;
(iii) Vita ya rushwa asiachiwe Mheshimiwa Rais peke yake, viongozi wote na jamii nzima wahusike katika mapambano haya;
(iv) Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wazingatie dhana ya utawala bora pamoja na sheria zinazoongoza utendaji wao;
(v) Watendaji wa Serikali waheshimu dhana ya mgawanyo wa madaraka (separation of powers) kwa mihimili mitatu yaani Serikali, Mahakama na Bunge ili kuepusha mgongano wa kiutendaji;
(vi) Haki za binadamu zizingatiwe wakati wa kuwawajibisha watumishi wanaopatikana na makosa ya kiutumishi;
(vii) Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wapewe semina elekezi kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yao;
(viii) Watendaji wa Vijiji na Mitaa na Madiwani wapatiwe mafunzo ya kiutendaji na mishahara; na
(ix) Viongozi wawe makini kabla ya kutoa matamko na waache woga katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu, ni Halmashauri kutenga asilimia 10 ili kusaidia wanawake na vijana. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Halmashauri nyingi nchini zimeshindwa kutekeleza agizo hili la Serikali kwa kukosa uwezo wa kifedha;
(ii) Hatua ya Serikali kuondoa ukusanyaji wa kodi ya majengo (property tax) katika Halmashauri imeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa mapato ya Halmashauri;
(iii) Serikali haipeleki kikamilifu ruzuku katika Halmashauri; na
(iv) Serikali iangalie mpango wa kuelekeza shilingi milioni 50 za kila kijiji kusaidia vikundi vya vijana, akinamama na SACCOS. Katika eneo hili ni Halmashauri 13 tu ambazo zimepelekewa fedha katika kundi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni TASAF. TASAF Awamu ya III imejielekeza katika kunusuru kaya maskini. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Mpango huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa kusaidia kaya maskini kuweza kumudu mahitaji ya msingi kama vile chakula, elimu na afya;
(ii) Umepunguza utegemezi wa kaya maskini kwa Waheshimiwa Wabunge;
(iii) Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TASAF ishirikishe wananchi wanaonufaika; na
(iv) Wananchi waelimishwe kuhusiana na mpango wa TASAF wa kusaidia kaya maskini.
Hapa ni kweli kwamba Serikali haichangii mchango wake katika TASAF. Tunayo takwimu hapa, katika miaka mitano iliyopita Serikali imetoa mchango kidogo sana katika fungu hili. Mwaka 2012/2013 bajeti ya Serikali iliyopitishwa ilikuwa shilingi bilioni nne, kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni 2.5, kiasi kilichobaki ni shilingi bilioni 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliofuata kiasi kilichoidhinishwa ni shilingi bilioni 18.5, kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni tatu, kilichobaki ni shilingi bilioni 15.5. Mwaka uliofuata kiasi kilichoidhinishwa ni shilingi bilioni 14, kilichotolewa ni sifuri, kilichobaki ni shilingi bilioni 14. Mwaka uliofuata iliidhinishwa shilingi bilioni 14, ilitolewa shilingi milioni 600 ikabaki shilingi bilioni 13.4. Mwaka uliofuata (mwaka jana) iliidhinishwa shilingi bilioni 14, ilitolewa sifuri, ikabaki shilingi bilioni 14.
Kwa hiyo, katika miaka mitano hii Bunge liliidhinisha shilingi bilioni 64.5 na iliyotolewa ni shilingi bilioni 6.1, ikabaki shilingi bilioni 58.4. Kwa hiyo, kwa kweli Serikali haijatoa mchango wake mkubwa katika eneo la TASAF. Kamati inasisitiza kwamba Serikali iongeze mchango wake ili wananchi waweze kunufaika na mpango huu wa TASAF III.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ni utumishi wa umma. Katika eneo hili wachangiaji wamegusia mambo yafuatayo:-
(i) Hatua ya Serikali kusitisha ajira na upandishaji vyeo kwa watumishi imeathiri watumishi ambao wanakaribia kustaafu. Serikali iruhusu ajira kwani kuna wahitimu wengi ambao wako mitaani wakisubiri ajira za Serikali;
(ii) Watumishi wanaofanya kazi wapewe motisha;
(iii) Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri na Watendaji wengine ambao hawakuwa katika utumishi wa umma kabla ya uteuzi wao wapewe semina elekezi kuhusiana na namna ya kutekeleza majukumu yao; na
(iv) Maamuzi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya dhidi ya watumishi yanavunja moyo watumishi hao na kusababisha baadhi yao waone kwamba haina thamani kuwa mtumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la sita ni utoaji wa elimu ya msingi bila malipo. Katika eneo hili, wachangiaji wamepongeza hatua ya Serikali kwani imekuwa na mafanikio ambayo hata hivyo yana changamoto mbalimbali, nazo ni kama ifuatavyo:-
(i) Uhaba wa vyumba vya madarasa;
(ii) Uhaba wa nyumba za Walimu;
(iii) Matundu ya vyoo na kadhalika;
(iv) Uhaba wa Walimu;
(v) TAMISEMI inashindwa kugharamia uendeshaji wa shule za Serikali kutokana na kuwa na mambo mengi; na
(vi) Bado wazazi wanawajibika kuchangia mahitaji ya wanafunzi kwani Serikali ilichoondoa ni ada na michango ya uendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yalikuwa mambo ya jumla lakini Waheshimiwa Wabunge katika michango yao vilevile wamegusia mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara katika mchango wake amesema mambo kadhaa na akalaumu kwamba kuna viongozi ambao wanatoa matamshi ambayo yanakatisha tamaa, akamsema Rais kwamba ametoa matamshi ambayo sio mazuri. Mimi nasema hii siyo sahihi. Mheshimiwa Rais amejipambanua kwamba yeye hapendi rushwa, amesema wazi kwamba rushwa kwake ni mwiko. Hata ndani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndiyo chama chake, amesema uchaguzi mwaka huu atakayetoa rushwa hatateuliwa kugombea nafasi yoyote. Pia amefanya kazi kubwa sana ameanzisha Mahakama ya Mafisadi ambayo inapinga rushwa na mambo mengine ambayo tumeyaona. Amezungumzia mambo mengi lakini sitayasema yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kiteto amesema kwamba Mabaraza ya Madiwani, RCC na kadhalika visifanyike wakati wa vikao vya Bunge. Kamati inaunga mkono hoja hii nzuri kwani Waheshimiwa Wabunge wana mchango mkubwa kwenye Mabaraza ya Madiwani, vikao vya RCC na vikao vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Japhary Michael amezungumzia mambo mengi, mojawapo ni kuhusu elimu bure. Hakuna elimu bure, elimu inalipiwa na anayelipia ni Serikali na Serikali inalipia kutokana na kodi za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwalongo amesema kwamba Watendaji wa Vijiji, wa Mitaa na wengine waajiriwe wasikaimu muda mrefu. Kamati inaunga mkono, ni hoja nzuri, wakikaimu muda mrefu wanakuwa hawana maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia pia suala la kuwa na shule za awali katika shule za msingi na maeneo mengine na akasema kwamba ni vizuri shule za awali ziwe pale ambapo wanafunzi hao wapo kwa sababu ni wadogo kutembea umbali mrefu ni vigumu sana. Kamati inaunga mkono hoja hii ili kufanikisha ili azma ya kuwa na „K‟ tatu zile, Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Mtoto akianzia shule ya awali anapata msingi mzuri anapokwenda shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kupewa posho. Ni jambo jema, tunashauri Serikali ijitahidi kuongeza mapato ili iweze kuwalipa posho Wenyeviti wa Mitaa, Vitongoji na Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia TASAF II kwamba ni jambo zuri limewasaidia sana wananchi hasa kaya maskini. Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba katika miaka mitatu iliyopita TASAF III imetumia zaidi ya shilingi bilioni 400 na zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na mpango huu. Watu wengine wanatumia vizuri mpango huu na wanajinufaisha wanakuwa na miradi ya kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameshauri kwamba mpango huu uboreshwe ili fedha hizi zitumike vizuri zaidi. Kamati inaunga mkono hoja hii kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao wakipata hela hizi za TASAF wanalewea pombe na kuna wengine ambao sio watu maskini kama ilivyosemwa na wachangiaji wengi lakini wamo kwenye mpango huu. Kwa hiyo, Kamati inashauri kwamba ni vizuri mpango huu ukaboreshwa. Mpango mzuri zaidi ni kama alivyosema Mheshimiwa Rais kwamba hizi pesa badala ya kutolewa bure watu waajiriwe kwa kazi ndogondogo hizi za usafi kwenye mitaa, kuzibua mitaro, kupanda miti, kujenga madarasa, kujenga kliniki na kadhalika ili waendelee kupata pesa lakini vilevile tupate maendeleo kadha wa kadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab amezungumzia Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam. Amepongeza na kwa kweli Kamati inashukuru kwa mchango huo, mradi huu ni mzuri sana. Tangu uanze mwezi Mei, 2016, barabara ile ya Morogoro sasa haina msongamano wa magari, imekuwa ni barabara nzuri. Tunashauri kwamba mradi huu usimamiwe vizuri zaidi ili barabara nyingine Phase II, Phase III mpaka Phase VI zikamilike. Barabara ya Kilwa, Barabara ya Bagamoyo, Barabara ya Pugu na nyingine zijengwe kwa utaratibu huo wa mabasi yaendayo kasi ili Jiji la Dar es Salaam liondokane na kero za msongamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia pale kwenye mradi ambao umekamilika wa Kimara Ferry (Kivukoni), pale Ubungo interchange pajengwe flyover haraka sana basi linakaa pale dakika 10, 15 likisubiri kuruhusiwa kwenda. Sasa inakuwa tena siyo kasi ni kama mabasi mengine ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Richard Mbogo katika utawala bora amezungumzia kwamba baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wanatumia vibaya madaraka yao. Wanakamata watu hovyo, kuwaweka ndani hovyo, kuwapunguza madaraka na kadhalika. Kamati inaunga mkono hoja hii kwamba kwa kweli ni vizuri Serikali ikaangalia sheria inazingatiwa kwa sheria zipo. Kamati za nidhamu, za ajira zitumike na siyo mtu mmoja kutoa maamuzi ambayo wakati mwingine yanakinzana na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe amezungumzia mambo mengi lakini moja amesema kwamba hela ya TASAF hii inayotolewa kwa wananchi iwe accounted for. Kabla ya kupewa fedha nyingine aeleze ile ya kwanza ameitumiaje. Ni wazo zuri katika kuboresha utoaji wa fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tunza katika mchango wake wa maandishi amesema ni vizuri Serikali ikaangalia matumizi ya gesi na mafuta tuliyogundua. Watu wapate elimu kuhusu matumizi au fursa zilizopo katika utajiri huu. Inawezekana baadhi ya wananchi wakafikiri kwamba baada ya kugundua mafuta na gesi basi hakuna kufanya kazi, ni kula tu, hapana wafahamu kwamba kuna fursa na wazitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ruth Mollel amechangia akasema kwamba Bunge siyo huru na akatoa mfano kwamba hakuna Bunge live. Sisi tunasema hii siyo kweli, Bunge kutokuwa live haina uhusiano wowote na kutokuwa huru. Tuliamua wenyewe hapa ndani kwamba Bunge lisiwe live kwa sababu ambazo zilielezwa humu ndani pamoja na gharama, TBC ilishindwa kuendesha mradi huo wa Bunge kuwa live. Kwa hiyo, hii haina uhusiano na Bunge kutokuwa huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akatoa mfano mwingine kwamba Mahakama zimenyamaza kuhusu mikutano ya hadhara ya vyama. Mahakama haiwezi kutoa maamuzi bila mtu kwenda mahakamani. Ni lazima mtu afungue kesi na ndipo asikilizwe Mahakama itoe uamuzi. Kwa hiyo, Mahakama zipo huru mwenye malalamiko yoyote aende Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Omary Tebweta amezungumia mambo mengi lakini mojawapo ni kuhusu asilimia 10 kwenda kwa vijana na wanawake, asilimia 50 maendeleo na asilimia 40 kwenye Other Charges (Matumizi Mengineyo). Ameeleza vizuri na sisi tunakubaliana naye kwamba baadhi ya Halmashauri zinatumia mwanya huu kujipatia hela ya matumizi mengineyo. Inatenga fungu la asilimia 40 kwa Matumizi Mengineyo, inatenga labda shilingi bilioni mbili ikifahamu fika kwamba haiwezi kupata shilingi bilioni mbili kwa mapato mengine ya ndani lakini inapanga makusudi shilingi bilioni mbili ili hela yote iingie kwenye Matumizi Mengineyo. Tunashauri utaratibu huu udhibitiwe na asilimia 40 iwe ni kweli asilimia 40 ya yale mapato ambayo wamepata sio Mapato Mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza amezungumzia uchaguzi kutokuwa huru. Kamati haikubaliani naye. Uchaguzi ni huru na ni wa haki. Hata juzi kwenye kata zile zilizorudia uchaguzi CCM imeshinda kwa haki. Mtu yeyote ambaye haridhiki na matokeo Mahakama zipo, aende mahakamani alalamike, apeleke ushahidi ahukumiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niombe sasa Bunge lako Tukufu likubali Taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa na maoni na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii. Nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii, nianze kusema kwamba mmoja wa wasemaji pale wa UKAWA amesema kwamba taarifa yangu ya jana, mimi ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI ina tarehe zilizokosewa, imeandikwa Aprili, 2015, ni kweli imekosewa, lakini hili siyo kosa langu wala siyo la Kamati yangu, ni matatizo ya uchapaji tu ya Idara ya Takwimu Rasmi za Bunge, Hansard siyo kosa la Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna methali ya Kiingereza kwamba kama unaishi nyumba ya vioo usiwe wa kwanza kutupa mawe. Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Lucy Mollel ilisomwa jana baada ya mimi pale, tarehe 27 mwezi wa Nne, lakini imeandikwa tarehe 28 mwezi wa Nne; na yenyewe imekosewa sasa sijui alichokuwa anasema ni kitu gani. Bora angeangalia zote mbili kwanza akajiridhisha na hali ilivyo ni makosa si ya kwetu wala sio ya Lucy Mollel, ni ya Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kazi anazozifanya, kazi nzuri sana yenye tija, anatetea wanyonge, amesema sasa hivi hapa kutumbua majipu na mengine. Kubwa sana kupambana na ufisadi, aliahidi alipokuwa anagombea mwaka jana kwamba akiwa Rais ataanzisha Mahakama ya Mafisadi na juzi amesema kwamba mwezi wa Saba Mahakama hiyo inaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wanaohusika, Waziri wa Sheria na Mawaziri wengine, Mahakama hii ikianza ianze na fisadi namba moja anajulikana, fisadi namba moja nchi hii anajulikana. Aligombea urais kupitia chama fulani, alikuwa na ndege kadhaa za kukodi siku sitini na nne anakodi ndege kadhaa, hela aliipata wapi? Alikuwa na magari mengi, msururu, alikuwa na watu mia tano anahama nao kila Mkoa ili aonekane ana watu wengi, hiyo hela aliipata wapi, anawapa posho, anawapa nauli, malazi, hiyo hela aliipata wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ianze na huyo ajieleze kusudi kama sio fisadi mahakama itamsafisha. Hata hivyo, CHADEMA waliandika kwenye orodha yao ya list of Shame walimwandika kwamba ni fisadi namba moja, watafurahi sana nafikiri akishtakiwa yule. Ashtakiwe ili na wenyewe waridhike, wapate amani kwamba fisadi wao ameshtakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dkt. Magufuli alipokuwa kwenye kampeni Kagera mwaka jana aliahidi mambo kadhaa. Mojawapo ni meli pale ziwa Viktoria, bahati nzuri tumeona kazi zinafanyika, meli tumeiona kwenye vyombo vya habari inatengenezwa huko nchi za Ulaya. Tunaomba meli hiyo isimamiwe haraka, ikamilike na nyingine ya Lake Tanganyika, Lake Nyasa zije zituhudumie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bukoba leo mfuko wa cement shilingi elfu ishirini na moja, Dar es Salaam shilingi elfu kumi na tatu, tofauti hii ni sababu ya usafiri wa malori, gharama kubwa sana na inaharibu barabara. Tukipata meli tutapata nafuu kubwa, ni usafiri mzuri una nafuu hata ya gharama na ni salama zaidi, tupate meli hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia aliahidi kushughulikia suala la ushuru kwenye mazao ya kahawa, tulimwambia kuna kodi ishirini na sita na alivyokuwa hapa alirudia kwamba kodi hizi ataziondoa, Mawaziri wanaohusika naomba mshughulike na jambo hili, hu ushuru na kodi ziondolewe kwenye mazao, kahawa, korosho, pamba na kwingineko ili wakulima wapate jasho la matunda yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bukoba kahawa inapelekwa Uganda ambapo bei ipo juu, kwa nini Uganda bei iwe juu hapa iwe chini, ushuru upunguzwe, kodi zipunguzwe wananchi hawa wapate kuuza mazao yao hapa na tuweze kupata hela ya kigeni, tujenge barabara, tupate huduma ya maji, tujenge shule na hospitali badala ya kuwanufaisha wenzetu wale wa nchi jirani wa Uganda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mradi wa mabasi yaendayo kasi wa Dar es Salaam (DART). Nimesoma jana pale kwenye taarifa yangu lakini nisisitize, niishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya mradi umekamilika ule, barabara zimekamilika, vituo vimekamilika, miundombinu ipo sawasawa, mabasi yapo zaidi ya mia ngapi pale jangwani na vitu vingine. Sasa uanze bado vitu vidogo tu, gharama kubwa imetumika kwenye mradi ule, uanze tarehe 10 mwezi wa Mei, tuondokane na kero ya misongamano barabarani ambayo inaweka uchumi mbovu, watu wanachelewa kazini, wanachelewa hospitali na huduma nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu za NBS mwaka 2014 hasara ya foleni za Dar es Salaam wanasema ilisababisha hasara ya shilingi bilioni 411 kwa mwaka mmoja, foleni za Dar es Salaam. Ule mradi Awamu ya Kwanza Kimara mpaka feri na hii ya Morocco na Msimbazi imegharimu shilingi bilioni 622, ni chini ya hasara ya mwaka mmoja ya foleni za Dar es Salaam. Kwa hiyo, kwa kweli mradi huu uanze tuondokane na kero hii na hasara kubwa ambayo tunaipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tena kwamba niwapongeze wenzangu wa UKAWA, leo wameanza kuchangia baada ya mgomo waliokuwa nao, nawapongeza. Saa hizi asubuhi walianza kuchangia kwa kudai televisheni ya Taifa iwaonyeshe; nasema hakuna kwa sababu haiwezekani TV ije hapa kuonyesha miongozo, taarifa, fujo, matusi, haiwezekani. TBC hawana fedha wameshasema kwamba hela yao haitoshi hawawezi kuja hapa konyesha fujo na kelele. Tena wasije kabisa hata ile asubuhi ingefutwa, tufanya kazi humu ndani…
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti naendelea, nizungumzie vyuo vya VETA...
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Vyuo vya VETA, naomba Wizara inayohusika...
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe na vyuo vya ufundi kila wilaya, ufundi ni kila kitu, maendeleo yote ni ufundi, nyumba nzuri kama hii ni ufundi ndiyo maendeleo, barabara ni ufundi, kuleta maji vijijini au mitaani ni ufundi, kujenga reli na barabara na madaraja ni ufundi, tuwe na vyuo vya ufundi kila mahali. Kagera hakuna chuo cha VETA mkoa mzima. Hii nitataka maelezo kwa mhusika atakapokuwa anatoa taarifa pale mwishoni, tupate maelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Halmashauri zetu kuna Halmashauri ambazo zina wizi wa kutisha, wanaiba pesa, wanahamisha matumizi, nimemwandikia CAG Halmashauri ya Bukoba kuna wizi nayo inataka maelezo, nimempa nakala Waziri, naomba waje wafanye ukaguzi maalum pale tubaini wezi ili washughulikiwe. Hili na lenyewe nitataka maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anajumuisha hoja yake,
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JASSON S. RWEIKIZA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuhitimisha hoja yangu niliyoitoa asubuhi.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja yangu ni Wabunge 18. Awali ya yote nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri; Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Mkuchika na Waheshimiwa Manaibu Waziri; Mheshimiwa Kandege, Mheshimiwa Waitara na Mheshimiwa Mwanjelwa kwa michango yao ambayo imesaidia kutoa baadhi ya majibu.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Wabunge kadhaa wamechangia sana kuhusu elimu. Kamati yangu inakubaliana na Wabunge hawa kwamba elimu kwa kweli kuna kazi za kufanya kubwa sana mbele yetu. Tunahitaji kuboresha Sekta ya Elimu na lazima Serikali iwe na mpango mkakati mzuri, mpango madhubuti wa kuboresha elimu. Walimu bado ni haba sana. Wanaostaafu nafasi zao hazijazwi, lakini wasomi wapo ambao wamesomea Ualimu na ingekuwa vizuri sana kuboresha sekta hii kwa kuajiri Walimu wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, huwezi kuwa na shule ina wanafunzi 600, una Walimu watatu. Kwa keli hutoi elimu, isipokuwa tu wanapita pale, wanahitimu, wanaondoka, lakini hawaelimiki. Vifaa, madawati, majengo, madarasa, vyoo; ni vizuri mkakati ukaboreshwa kusudi elimu iweze kuwa bora zaidi. Ndiyo maana hapa Mheshimiwa mmoja ametoa takwimu, amelinganisha shule binafsi na shule za Umma. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri Waitara akijibu, akasema kwamba shule binafsi zinakaririsha. Nitangaze maslahi kwamba mimi niko kwenye sekta hii ya shule binafsi.
Mheshimiwa Spika, kuna wakati ilikuwa ni fedheha kusoma shule binafsi huko nyuma miaka ya 1970, 1980; ilikuwa ni fedheha kwenda shule binafsi. Baadaye wazazi wakawa wanepeleka watoto wao Uganda, Kenya na nchi nyingine huko kupata elimu bora, lakini baadaye pia tena Watanzania wakajiongeza, wakajizatiti wakajenga shule humu ndani Tanzania nami ni mmojawapo. Sasa kwa kweli hawa wa binafsi wanazingatia sana ubora. Kwa hiyo, ndiyo tofauti iliyopo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ikiboresha hivi vitu; Walimu, vifaa, madawati, vyoo na vifaa vingine, elimu itakuwa bora. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli kwa kusema elimu ni bure. Baadaye shule hizi zitakufa zenyewe tu, zitaondoka zenyewe kwa sababu zina gharama kubwa kuziendesha na ndiyo maana tunasema kama mpango wa elimu bure utafanikiwa, shule za binafsi zitakufa zenyewe. Hakuna haja ya kuzipiga vita, tunafanya kazi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wamechangia kuhusu suala la Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kunyanyasa wananchi na kuwaweka ndani na mambo mengine. Nashukuru Serikali imechukua hatua, Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Jafo wamepambana sana na hawa watu, walikuwa wanakiuka sheria. Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli na Mheshimiwa Waziri Mkuu wamekemea sana tabia hii, lakini haijaisha, bado ipo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuna haja bado ya kuendelea kuwadhibiti Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waache kunyanyasa watu. Kazi yao siyo kunyanyasa watu, ni kuwatendea kazi, kuwasaidia kwenye harakati za kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Nkamia amezungumzia jambo la uchaguzi kwamba maendeleo hayaji kwa uchaguzi. Ni kweli jambo hili linazungumzika na linafikirisha. Sisi tumeingia humu tuna miaka mitatu, leo homa imeshaanza ya uchaguzi wa mwaka kesho. Watu Majimboni wanapita huko, wanajipitisha huko, wanasumbua; tunakaa humu nusu nusu, uko nusu; mguu mmoja ndani, mmoja nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tungekuwa na miaka saba, labda mtu angekuwa ametulia hapa mpaka 2022. Sasa kwa sababu tunaelekea mwakani kwenye uchaguzi, homa imeshaanza humu, presha inapanda, inashuka. Sasa inakuwa taabu sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kuna nchi nyingine nyingi Afrika humu, Rais anagombea vipindi vingi tu miaka mitano, mitano, hata mara 10 kama ana uwezo huo na anaendelea na wanafanya vizuri; nimeziorodhesha hapa nchi kama 22 au 21; Chad, Cameroon, Comoro, Congo, Djibout, Equatorial Guinea, Ethiopia, Gabon, Gambia, Liberia, Lesotho, Libya, Swaziland, Morocco, Mauritius, Sudan, Togo na Uganda hata Rwanda, nirudi nyuma tena sasa.
Mheshimiwa Spika, hawa hawana limit ya kugombea, hata kwa nafasi ya Rais, anagombea hata vipindi vitatu, vinne, vitano, kumi. Margaret Thatcher alikaa miaka 11, Waziri Mkuu wa Uingereza; Angela Markel ana miaka 16 na tusiseme kwamba sisi tumeendelea kuliko wao. Hata hao Waafrika, Ethiopia wanatuzidi maendeleo, Mauritius wanatuzidi maendeleo; Togo wako juu kuliko sisi, lakini wanagombea kwa muda mrefu na wanakaa. Wengine katika hawa wana vipindi vya miaka saba, saba kama Cameroon miaka saba, Gabon miaka saba na hakuna ukomo. Kwa hiyo, jambo hili ni la kuzingatia na inafaa kulijadili ili ikiwezekana Mheshimiwa Nkamia alete hoja yake hapa Bungeni tuijadili halafu tuone inakwenda vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wamechangia kuhusu TARURA. Kamati inasema kwamba TARURA ina kazi kubwa sana imeifanya. Tangu imeanzishwa muda mfupi uliopita, imesimamia kazi za barabara za vijijini na mijini. Barabara ndogo ndogo nyingi za Dar es Salaam ni za TARURA. Kwa hiyo, TARURA ina kazi kubwa sana lakini haina pesa. Kwa hiyo, tunasisitiza kwamba TARURA iongezewe fedha kutoka Mfuko wa Barabara (Road Fund) badala ya asilimia 30 iwe asilimia 50 ili barabara za TARURA ziweze kutengenezwa ziende vijijini kule kwenye mazao, zipeleke pembejeo mwaka mzima tuwe na huduma nzuri vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili la barabara za TARURA na TANROADS, barabara kuu zimekamilika bado kidogo tu; Katavi, Kigoma na sehemu nyingine. Kwa hiyo, ikienda asilimia 50 TANROADS itatosha kukarabati barabara ambazo zipo na kujenga zile mpya chache, lakini asilimia 50 iende TARURA ili nao waweze kupata uwezo wa kujenga barabara zao.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kuhusu TASAF. TASAF imefanya kazi nzuri sana ya kupigiwa mfano, lakini tunasisitiza kwamba Serikali itoe mchango wake kwenye TASAF, tusitegemee tu wafadhili pake yake. Serikali itoe mchango wake kusudi wale wa asilimia 30 ambao hawapati mchango wa TASAF wapate huduma hiyo na waweze kupata tija ya hela ya TASAF. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wamechangia kuhusu Sekta ya Afya. Naipongeza Serikali sana kwa kujenga hospitali 67 za Wilaya na Vituo vya Afya 650 kwa muda mfupi. Ni jambo kuba sana la kusifia, la kuishukuru Serikali. Kujenga hospitali moja inahitaji shilingi bilioni saba na nusu; fedha iliyotolea ambayo tunashukuru ni shilingi bilioni moja na nusu. Tunasisitiza kwamba hii iliyobaki shilingi bilioni sita itolewe kusudi hospitali hizi zijengwe ndani ya muda unaotakiwa na zikamilike kwa ukamilifu wake.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa lingine, wataalam watafutwe, waanze kuajiriwa na kuandaliwa. Kwa sababu mwezi wa Sita siyo mbali sana, Madaktari, Wauguzi, Manesi na wengine wawepo kwa sababu hospitali 67 ni nyingi sana Vituo vya Afya 350 ni vingi kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kuhusu maji vijijini na hali ya maji vijijini haijawa nzuri, bado ni mbaya. Tumesema sana humu Bungeni kwa miaka mingi kwamba tuunde Wakala wa Maji Vijijini. Tunashukuru kwamba juzi juzi hapa sheria imepitishwa hapa ya RUWASA kuunda Wakala wa Maji Vijijini.
Mheshimiwa Spika, Wakala huu tunataka uanze kazi mara moja, upewe fedha, uwezeshwe, kazi ianze. Kamati inaunga mkono kwamba ile shilingi 50 kwenye petrol na diesel ikatwe kusudi iende kwenye mfuko huu ambao unaanzishwa chini ya Wakala wa Maji kusudi huduma iweze kuwa nzuri kwa watu wa vijijini ambao wana shida kubwa sana ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho nimalizie kwa kusema kwamba, tumekuwa na dhana ya D by D (Devolution by Decentralization); kazi nyingi zinafanyika kwente Halmashauri kule, kwenye Madiwani, kwenye vijiji, kwenye vitongoji, na mitaa. Kumekuwepo na mwelekeo sasa hivi wa kuondoa huduma hizi huko kuzirudisha Makao Makuu ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, mambo ya maji, Hospitali za Mikoa zimesharudi Wizarani, kuna mambo ya ardhi yanarudishwa Wizarani. Sasa hii itakatisha tamaa, Halmashauri zitakosa kazi za kufanya; na iko kwenye Katiba kwamba Decentralization iendelee kuwepo ili wananchi waone kwamba wanamiliki miradi hii na wafanye kazi kwenye miradi hii kwa moyo na kwa kupenda.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa michango hii na mapendekezo haya ya Kamati yaweze kuazimiwa na Bunge hili ili Serikali iweze kuyatekeleza.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika bajeti ya Serikali, kama ilivyowasilishwa juzi hapa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Nipende kupongeza sana bajeti hii nzuri, ambayo Serikali imeiwasilisha hapa kwetu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa bajeti nzuri ya kwanza. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa bajeti nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya bajeti hii ni mazuri sana na hasa hasa ambaye imenigusa sana ni ile ya TARURA. Kuongeza fedha kwenye mamlaka hii au Wakala huu wa barabara vijijini, ili iweze kupata uwezo mkubwa wa kuboresha barabara za vijijini. Tunafahamu wote kwamba, vijijini ndio kuna uchumi, ndio kuna kilimo, kunapelekwa pembejeo, kuna huduma za afya kwenda kwenye zahanati na vituo vya afya, bila barabara huwezi kuzifikia huduma hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule kwa hiyo, kwa kuwa na fedha zaidi kwenye mfuko wa TARURA, ina maana huduma hizi zinakwenda kuboreshwa na kuonekana na kufikiwa na wananchi kirahisi zaidi. Lakini na mambo mengine mengi sio tu TARURA peke yake, ambayo bajeti imeyagusia na kuyazingatia. Nnaipongeza sana Serikali ya CCM kwa kuwa sikivu na kwa kuwa inaboresha maendeleo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo napenda nizungumzie suala la elimu kwa sababu, tunapoongelea bajeti hapa tunaongelea uchumi na huwezi kupanga uchumi kama huna elimu nzuri. Elimu ndio ufunguo wa maisha na ndio ufunguo. Sasa, kwa hiyo bila elimu nzuri huwezi kuwa na uchumi mzuri na elimu yetu bado ni ya mitihani. Mtoto akitaka asonge mbele ni lazima afanye mitihani, afaulu, aende hatua nyingine, hatua nyingine, mpaka vyuoni huko aweze kuhitimu, akifeli mitihani hawezi kwenda huko. Nchi nyingine hawatumii utaratibu huo, kama Ujerumani na nchi nyingine wana system tofauti ya vitendo sisi ni ya mitihani kwa hiyo, lazima mtoto afaulu mitihani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wiki iliyopita nilikwenda Jimboni, najitahidi mara kwa mara nakwenda jimboni, natembelea wapiga kura na safari hii nilitembelea shule. Na nawashauri Wabunge wenzangu mnapokwenda Majimboni, msisahau shule, mtembelee shule, shule za sekondari na za msingi. Kwa sababu, kama shule ina wanafunzi 500 ukaenda pale kusalimia wanafunzi 500, umesalimia jimbo zima karibu kwa sababu, ni kama watu 5,000. Kwa hiyo, nilifika pale nikaona shule zinavyoendelea, nikakuta shule zimefungwa kama ilivyo kawaida sasa hivi ni wakati wa likizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baadhi ya shule nilizozitembelea nikakuta vijana wa Form Four wamebaki. Shule za Kata wamebaki kwa mpango maalum wa kusoma ili waweze kufaulu mitihani. Nilitembelea shule ya Butura ni Sekondari, Shule ya Kaja Sekondari, Katoro Sekondari, Bujuko Sekondari na nyingine nyingi. Hizi zilikuwa na wanafunzi wapo wa Kidato cha Nne wanajisomea, kwa mpango wa kujaribu kufaulu mitihani ya Taifa ya mwezi wa kumi na moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na wanafunzi hawa wana shida nyingi sana. Mtoto anaweza akawa anaumwa hajahudhuria shule au amechelewa kwa sababu mbali mbali, hana uniform hajaenda shule, uwezo wa wazazi ni mdogo. Kwa hiyo, wanaamua kubaki ili waongeze muda wa kujisomea au walimu hawatoshi, kama tulivyosikia humu ndani kila siku walimu wa sayansi na wewe umesema kule kwako walimu wa sayansi ni pungufu. Kwa hiyo, walimu wanaamua kujitolea muda wa ziada, waweze kutoa elimu hii ambayo wanafunzi wameikosa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, ikatokea mtu mmoja Wizarani pale amezuia utaratibu huu. Kaandika waraka kwamba, shule zikifungwa zifungwe hakuna kubaki shule, nikashangaa sana! Hawa vijana wanaobaki shuleni, wanabaki ili wajiandae na mitihani na hawana uwezo wa kufaulu bila kubaki. Na sio kwamba, wana fedha nyingi wanabaki pale wanajitolea na wanakaa mabweni shule za kutwa zile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanaingia kwenye madarasa mle, hawana magodoro, wanaweka nyasi chini wanalala, ili wasome waweze kuongeza ufaulu. Walimu wanajitolea kufundisha bure bila malipo, wazazi wanachangia mihogo, ndizi, maharage, ili watoto wale usiku na mchana, wasome waendelee waweze kufaulu. Huyu mtu mmoja Kamishina wa Elimu amezuia utaratibu huo lengo lake silifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachelea kusema ana lengo la kuharibu elimu ya nchi hii na hivyo ana lengo la kuua uchumi wa nchi hii. Watoto wanajitolea, wazazi wanajitolea, walimu wanajitolea. Mtu mmoja anakaa pale Wizarani anaandika waraka anasema hii hairuhusiwi, Serikali, haichangii. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishina wa Elimu hachangii. Sasa inashangaza kweli kwa nini anazuia, inamuhusu nini yeye. Kuna mtu mmoja aliwahi kusema kwamba ukitaka kuua Taifa wala usipeleke sumu kwenye wananchi wale au kuharibu madaraja na barabara wewe ua elimu tu. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ua elimu na utakuwa umefanikiwa kuua Taifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rweikiza kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako.
T A A R I F A
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba, Wizara jukumu lake pia ni kuwalinda watoto. Kwa hiyo, Serikali haiwezi ikaruhusu mtu sehemu ambayo sio bweni tena amesema watoto wanaweka nyasi, wanalala mazingira yanakuwa ni hatarishi, miundombinu haiko salama kwenda pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpe taarifa tu kwamba, shule ambazo sisi tumezuia ni zile ambazo wanalazimisha wazazi kuchanga fedha. Kwa hiyo, suala la kwamba watu wanajitolea sio kweli, wanalazimisha na ni kinyume na maelekezo ya Serikali ya elimu bila malipo. Kwa hiyo, nilikuwa nataka tu nimpe taarifa hiyo, ili labda anapochangia aweze kutupatia maeneo mahususi ambayo anayalalamikia, ili Serikali iweze kufanyia kazi vizuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jasson Rweikiza, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza ulinde muda wangu. Lakini ninachosema ni kwamba, nchi hii inatumia utaratibu wa mitihani, mtu akifeli, amefeli, ameishia hapo ndio mwisho. Kwa hiyo, wazazi na watoto na walimu wanajitolea kusoma wala hakuna anayelazimisha michango. Niko kwenye sekta ya elimu yaani elimu ndio system yangu nafahamu utaratibu wa elimu. Sikutangaza maslahi kwa sababu haina masilahi yangu kifedha, lakini niko kwenye sekta ya elimu na ninaelewa vizuri ninachokisema. Serikali inaharibu elimu, Wizara ya Elimu inaharibu elimu kwa hiyo, taarifa hiyo siikubali, naikataa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nasema kwamba, kuna mtu aliwahi kusema, mtaalam wa elimu, mtaalam wa uchumi, mtaalam wa utawala kwamba, ukitaka kuua Taifa, ua elimu. Usihangaike na mambo mengine ua elimu. Huyu Kamishina wa Elimu amekusudia kuua elimu ya nchi hii, haiwezekani uzuie watu kusoma, watafauluje bila kusoma? Watashindwa mitihani, watapotea, wataishia darasa la saba, wataishia Form Four na ndio mwisho wao na watakuwa wanapata zero.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajitahidi watoto wasome, waende mbele, wafike vyuo vikuu na vyuo vingine, wapate stadi mbalimbali vyuo vya ufundi. Lakini hawawezi kufika huko bila kufaulu mitihani yao ya ngazi mbalimbali, ambayo lengo la kufanya hizo kambi na halikuanza leo, tangu enzi hizo. Yeye mwenyewe Waziri ni Profesa asingefikia U-Profesa kama asingefanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amesoma kwa bidii za wazazi, za walimu, za shule mbalimbali, za vyuo mbalimbali. Sasa kwa nini anazuia utaratibu huu ambao ni mzuri, nasema ni mzuri. Kule vijijini hawalipi fedha kwa sababu ya kulazimishwa, wanalipa fedha hizo ndogondogo mihogo hiyo, kwa sababu ya kupenda wenyewe na ndio walioomba. Ni Mbunge wa Jimbo nashiriki kwenye mikutano hiyo, watoto wanaomba, wazazi wanaomba. Wanazuiwa kufanya huu utaratibu ambao nafikiri ni kuua elimu. Kwa hiyo, tujitahidi na yeye akiwa ndio Waziri wa Elimu, azuie utaratibu huo wa kuua elimu asimamie, ili elimu iwe bora na tuweze kufanikiwa katika mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naomba kuishia hapo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi na mimi nichangie asubuhi ya leo. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge wenzangu wa CCM kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Katibu wao. Nawaahidi kwamba kazi naifanya vizuri kwa weledi na ustadi mkubwa, sitawaangusha!
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie barabara yangu moja iliyoko Jimboni kwangu. Barabara hii inaanzia Kanazi kwenda hadi Katolo, hii barabara ni kubwa sana, ni barabara ya TANROAD, ni barabara ya TANROAD, kubwa, lakini ina hali mbaya sana! TANROAD ni kama vile wameitelekeza, hawaitengenezi mara kwa mara, hawaiweki lami hata kama si lami angalau wangekuwa wanaitunza inakuwa inapitika vizuri mwaka mzima! Mara nyingi inakuwa na mashimo makubwa sana na ni barabara ambayo inaunganisha wilaya tatu, Wilaya ya Bukoba yenyewe, Wilaya ya Misenyi na Wilaya ya Muleba sasa barabara kama hii ina umuhimu wa pekee, inahudumia Kata 19, watu karibu 300,000. Kata zenyewe ni Kata ya Kemondo, Kata ya Katerero, Kata ya Igwela…
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Kata ya Mikoni, kikomelo, Kishogo, Kashalu, Kibimbili, Kaibanja, Katolo, Kyamulaile, Mugajwale, Luhunga, Chaitoke, Izimbya, Kibilizi, Lukoma, Lubale na Butelankuzi, bila barabara hii hawa watu hawafiki Bukoba Mjini na wa mjini hawafiki kwenye Kata hizi, bila barabara hii. Sasa barabara hii ina umuhimu wa kipekee, kule tunalima mazao mengi sana, kahawa nyingi sana, ndizi nyingi sana, lakini ina hali mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana Mheshimiwa Savelina Mwijage aliongelea barabara hii ndiyo yenye daraja la Kalebe, daraja bovu kweli kweli ni hatari pale! Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri barabara hii ipewe fedha, kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Waziri haimo na ni barabara kama nilivyosema ya TANROAD.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna barabara nyingine ambayo inaanzia Mjini Bukoba kwenda Kabango Bay, kilometa 42 barabara ya mpaka, inakwenda Uganda, nimeisema mara nyingi hapa Bungeni, lakini kwenye kitabu hiki imepangiwa shilingi milioni 200, barabara ya mpaka, barabara ya usalama, barabara ya ulinzi, milioni 200 ni fedha kidogo sana! Tumeisema muda mrefu sana. Hata Mheshimiwa Shein alipokuwa Makamu wa Rais aliwahi kuisemea kwamba ijengwe kwa kiwango, miaka karibu 10 iliyopita hadi leo haijaguswa! Naomba na yenyewe ipewe fedha, itengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine kubwa, pale Halmashauri ya Bukoba Vijijini nilisema hapa Bungeni, wiki mbili zilizopita kulikuwa na ubadhirifu wa fedha za barabara. Fedha ya Road fund, fedha ya Mfuko wa Jimbo na fedha ya ombi maalum, fedha nyingi karibu bilioni moja. Nikapiga kelele kule kwenye Halmashauri, Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo ambaye sasa amehamishwa akaanzisha utaratibu wa kuwashughulikia hawa watu, akaunda Tume wakakamatwa, nashangaa mpaka leo hawajapelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliandika barua kwa CAG kwamba apeleke Tume ya Wakaguzi wakague fedha hii imeliwa namna gani, fedha nyingi namna hii. Cha kusikitisha, CAG amenijibu kwamba hana fedha ya kwenda kufanya kazi hii! Unamwambia fedha imeibiwa anasema sina fedha ya kwenda kukagua wizi, nasema inasikitisha sana! Anasema aliyeomba ndiye agharamie, sasa naangalia namna gani nitapata fedha ya kuwalipia watu wa CAG waende kule wakague wizi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbaya zaidi, nimesema jambo kubwa, kutokana na ubadhirifu huu watu wa Road Fund wamekataa kutoa fedha kwenye barabara za vijijini nyingine ambazo inabidi wazihudumie kwamba hadi fedha hii irudishwe ndiyo watoe fedha! Sasa anayeadhibiwa siyo aliyekula zile fedha, ni wananchi wa Bukoba Vijijini. Mkurugenzi amehamishwa, Engineer amehamishwa ingawa nasikia wamekamatwa na wenyewe sasa hivi, lakini anayeadhibiwa ambaye sasa hivi hana pa kupita, barabara zimekongoroka zote zimekuwa mashimo ni Wwnanchi ambao hawana hatia! Naomba sana jambo hili liangaliwe kwa kina kwa nini uwaadhibu wananchi ambao hawana hatia, uwaache wenye hatia hata leo hawajapelekwa Mahakamani, wanawaangalia tu, wako tu wanaangalia, hili kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini, nizungumzie SUMATRA, SUMATRA imeagiza kwamba mabasi ya shule yapakwe rangi ya njano, nitangaze maslahi mimi ni mliki wa shule na nina mabasi hayo mengi. Sasa wanaagiza kwamba yapigwe rangi ya njano, jambo hili ni la kuchekesha, ni kichekesho na si jipya waliwahi kusema huko nyuma tukamwambia Waziri aliyekuwepo, Mheshimiwa Nundu akazuia jambo hili, leo tena wamelirudisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi moja la Costa kulipaka rangi ya njano si chini ya milioni tatu, uchomelee chomelee kwanza kwenye kutu upige rangi ya njano, three milion shilings unazipata wapi, analipa mzazi? Unafanya shule ziwe na gharama kubwa bila sababu, haina faida yoyote kwa mzazi kwa shule wala kwa mwanafunzi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni uhuni wa hali ya juu sana, yamkini kuna mtu ana rangi zake kule, amenunua rangi nyingi Dubai au Japan anataka aziuze kwa nguvu. Jambo hili halikubaliki, lazima Mheshimiwa Waziri atoe maelezo kuhusu jambo hili kwa nini tunafanyiwa jambo ambalo ni la uovu kama hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na uwanja wa ndege wa Mkajunguti ambao uko Kagera, Wilaya ya Misenyi. Uwanja huu umezungumziwa siku nyingi sana. Michoro imefanyika, fidia imeandaliwa, lakini haikutolewa, uwanja huu ujengwe, kwenye bajeti hii haumo. Uwanja huu unaunganisha nchi tano, Uganda, Rwanda, Burundi, Tanzania na Congo, uko katikati, ni wa kimkakati kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ndege zikitoka Latin America zitatua pale zitaweka mafuta zitaenda Asia, zikitoka Afrika ya Kusini zitatua pale zitaenda Ulaya. Ni uwanja wa kimkakati kabisa, basi ujengwe! Fedha itengwe ipatikane kwenye bajeti na kazi iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo, nakushukuru sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika bajeti ya Wizara ya Elimu. Nimpongeze na kumshukuru Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda; Naibu Waziri, Mheshimiwa Omari Kipanga; Katibu Mkuu na Naibu wake na viongozi wote wa Wizara na watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri sana anayoifanya ya kuboresha elimu na hata sekta nyingine anazozisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pale Bukoba kwangu shule nyingi zimejengwa, madarasa mengi yamejengwa. Pale Mkoa wa Kagera leo tuna Chuo cha VETA, chuo kikubwa kizuri sana cha VETA kimejengwa, amekifungua mwaka jana yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais na hivi ninavyoongea tunajenga Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, branch ya Bukoba. Haya ni maendeleo makubwa ambayo kwa kweli nampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huku chini ngazi ya Wizara, Waziri na wasaidizi wake na watendaji wote, naomba tumsaidie Rais kwenye kazi hii, tumsaidie Rais kwa nguvu zote, kwa moyo wote, kwa bidii zote. Wamesema Wabunge hapa leo na siku zote wanasema, amesema msemaji wa mwisho hapa kwa mfano, uhaba wa Walimu ni tatizo kubwa sana kwenye shule zetu. Ni tatizo kubwa sana ambapo shule zimejengwa, madarasa yapo, lakini hakuna Mwalimu, sasa ni kama sifuri, kazi iliyofanyika ni zero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina shule pale Bukoba, Shule ya Msingi Musira ina wanafunzi kasoro kumi tu wafike elfu moja, ina Walimu saba. Nina Shule ya Msingi Nakigando ina wanafunzi 840, ina Walimu sita, upungufu wa Walimu kumi na tano. Matokeo yake hawa watoto wanakaa pale, wanashinda wanacheza, hawafundishwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina shule za sekondari, shule nzima haina Mwalimu wa hesabu, shule nzima haina Mwalimu wa kemia. Sasa haya ni matatizo makubwa ambayo nafikiri yako ndani ya uwezo wa Wizara kuyafanyia kazi na kuyatatua angalau kwa kiasi cha kutosha watoto wasome, wapate elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi zimezungumziwa na Wabunge wengi hapa, Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, Mheshimiwa Tunza, Mheshimiwa Minza amesema, Wizara iache kuziona shule binafsi kama washindani wao. Mheshimiwa Rais ana lengo la kuboresha elimu, elimu iwe na ustawi mzuri, ufanisi uonekane kwenye elimu na shule binafsi zinatoa mchango mkubwa kwenye eneo hili, kwenye kuboresha elimu. Sasa Wizara ya Elimu na Wizara nyingine kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinaiona hii sekta kama ni washindani wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko kwenye sekta ya shule binafsi, naendesha shule binafsi na ni Mwalimu pia, nilifundisha huko zamani, kwa hiyo, ninachokisema nakifahamu. Majuzi hapa, mwaka jana, Wizara ilifuta kupanga wanafunzi wa kwanza mpaka wa mwisho, wakafuta kupanga shule ya kwanza mpaka ya mwisho. Kuna Mheshimiwa Mbunge aliuliza swali hapa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akajibu vizuri sana, akajieleza vizuri sana watu wakapiga makofi, lakini ukweli uko pale pale, walifuta hiki kitu kwa sababu ya kuogopa shule binafsi, kwamba zinafaulisha zinawazidi, kwa hiyo, ili kuondoa hii noma ya kuwazidi basi angalau kufuta wote tuonekane tunalingana. Huo ndio ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawawezi kusoma bila usindani. Mtoto wa primary anasomaje? Hafahamu maana ya kusoma, lakini ile pride ya kujivunia kwamba, nimemzidi huyu, nimekuwa wa kwanza, nimekuwa wa kumi, nimewazidi thelathini, arobaini, inamwongezea motisha ya kusoma. Ukitoka mtihani amekuwa wa saba, amekuwa wa ishirini, amewazidi wenzake anaongeza motisha. Sasa wewe unafuta ranking? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni vita kati ya shule za Serikali na shule za binafsi, hii sio sawa. Kwa kweli, kufuta ranking wanaua elimu na ukiua elimu unaua nchi. Mheshimiwa Waziri, Profesa ataingia kwenye rekodi, kwenye historia kwamba, aliua elimu ya Tanzania kwa kufanya hiki kitendo cha kufuta ranking. Ushindani ndio kila kitu, hata kwenye maisha huku mtu anataka ajenge nyumba nzuri, avae vizuri kumzidi mwingine na shuleni hivyohivyo, mtoto akifaulu vizuri kumzidi mwenzake anajisikia anaongeza kasi anasoma kila siku anaongeza bidii na nchi inapata ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, kuonesha mapambano yaliyopo kati ya shule za Serikali na za binafsi. Mwaka jana matokeo ya darasa la saba, shule zaidi ya ishirini na kidogo hivi zilifutiwa matokeo kwamba, zimeiba mitihani, zikafutiwa matokeo, zikatangazwa, zikafutiwa vituo vya mitihani. Shule ya Serikali, Olympio, ilituhumiwa kwamba, imeiba mtihani, ikafutiwa matokeo. Haikutangazwa, haikufutiwa kituo, mpaka leo inaendelea na kituo chake. Sasa haya ni mambo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, za private zimetangazwa sana, zimeharibiwa sifa, zimeharibiwa jina, ya Serikali Olympio haikutangazwa, ikaonekana yenyewe haina matatizo, walirudia mtihani kama wengine wote walivyorudia, japo kimya kimya. Sasa haya mapambano ya namna hii kwa kweli, sio kujenga au kuboresha elimu bali ni kupambana na sekta ya binafsi ili kuiondolea uwezo wake na utendaji wake mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyaraka hizi ambazo amezisema Mheshimiwa Kikoyo, amezitaja kwa idadi, amefanya utafiti. Nafikiri baadhi ya nyaraka watoe, watu- consult au hawa wahusika na wadau wawashirikishe. Unaposema unafuta mabweni shule ya awali mpaka darasa la nne, hujawauliza wenye shule wanaoendesha, hujawauliza wazazi waliowapeleka kwa hiyari yao, unaboresha unaharibu au unabomoa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo Waziri anayemfutia mabweni ameomba kibali kwake kwamba, naenda kujenga shule ya bweni ya awali mpaka darasa la nne. Anampa kibali kwa maandishi, anacho, amekopa pesa benki amenunua vitanda, amejenga majengo, ameweka magodoro, kesho anamfutia kibali, anamfutia bweni, afanyaje? Alipe vipi hilo deni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia nyingi za kuzuia ushoga. Kama ni ushoga, hakuna anayeupenda katika nchi hii, nina hakika, ziko njia nyingine nzuri za kuzuia ushoga, sio kufuta mabweni. Weka kamera, weka masharti magumu, idadi ya wanafunzi, toa mafunzo, watu wajifunze namna ya kuendesha shughuli hii bila kufuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule pale Bukoba mwenye shule Kaizirege yeye ni bweni tupu. Ukisema hakuna bweni ina maana shule imefungwa, imekufa hiyo, unataka kuua hizi shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kodi 18, naona nimepigiwa kengele, sitazisoma zote ningezitaja hapa. Kodi ya mapato, VAT, kodi ya ardhi, majengo, leseni, WCF, vibali vya wafanyakazi wa nje, kodi ya zimamoto, usalama kazini OSHA, LATRA, kodi ya ukaguzi, mitihani ya Taifa ina kodi, ada ya mitihani ya mock ya Wilaya, ya kata, ya nini, kuna michango kibao. Matangazo kodi, hata ukiandika kwenye basi lako ukaandika jina la shule unalipia, basi lako mwenyewe uandike jina la shule unalipia TRA, yaani mambo ya ajabu sana. Kodi ya service levy, sheria inazuia service levy kwenye shule wenyewe wanatoza service levy, UMISETA, UMITASHUMTA, usipotoa unakipata chamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutafsiri mitihani na yenyewe inalipiwa, tunalipia siku hizi. Kutafsiri kutoka Kiswahili uende Kiingereza sharti ulipie shilingi 8,500 kila mtihani, kila mwanafunzi, yaani hii ni kuumiza wazazi na lengo ni kuua shule. Kwa hiyo, nafikiri ili kutafuta ufumbuzi wa mambo haya, nimesoma taarifa ya Kamati, sio iliyosomwa hapa, ile ni summary, ile taarifa kubwa nimeisoma; imependekeza tuunde chombo huru cha kusimamia elimu, chombo huru, tuondoe suala la ukewenza. Huwezi kuwa na wake wanne, halafu uchague mmoja ndiye awe msimamizi wa wenzake. Serikali ina shule na binafsi wana shule, halafu Serikali ndio isimamie shule zote hizi, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo ile TCU ya vyuo vikuu, Vyuo Vikuu vya Serikali kama Dar es Salaam, vya binafsi, viko chini ya TCU au TCIA ya ndege, ATCL za Serikali, Precision Air, ninii, ziko chini ya hiyo, basi na hii elimu iwe na chombo cha kusimamia shule zote Tanzania ili tuweze kuwa na ufanisi mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi kuchangia asubuhi hii. Mimi nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya, maana unapotaka mambo yapelekwe kwako au yasogezwe kwenye eneo lako vilevile lazima utambue kazi ambayo imefanyika. Kazi kubwa imefanyika na inaridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kusema hivyo sina maana kwamba tumemaliza, bado tuna kazi za kufanya na tunaendelea nao. Lakini nalinganisha na miaka nyuma ambapo umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara, kila mahali giza, sasa hivi hali hiyo haipo tumeweza kupambana nayo na tumekabiliana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mbalimbali inayoendelea, tunaona miradi mingi, tumepata gesi ya Mtwara, kutoka na gesi hiyo tumefungua miradi mikubwa ya kufua umeme pale Kinyerezi ambayo ikikamilika tutapiga hatua kubwa sana katika kuwa na umeme wa kutosha na mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna miradi mingine, kwa mfano ile njia kubwa ya umeme kutoka Iringa kwenda Shinyanga ambayo ikikamilika ni kama backbone, ina-cross kuanzia Iringa kwenda Shinyanga, itakuwa ni chanzo cha kupeleka umeme mikoa mengine ambayo imezungukwa mikoa hiyo, ambao ni umeme mkubwa KV 400. Hili ni jambo la kujisifia na kuishukuru Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niisemee REA. REA kazi yao vilevile ni nzuri sana, vijiji vingi nchi nzima vimepata umeme. Mimi najiuliza ingekuwa hakuna REA tungekuwa wapi? Kazi ya REA ni nzuri, nawashukuru na kuwapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema pamoja na kazi nzuri bado tuna kazi kubwa ya kufanya. Pale Kagera Mkoa mzima kuna tatizo la umeme kubwa sana. Hata leo ninavyoongea hivi sasa hivi hakuna umeme umezimika, jana hivyo hivyo, juzi hivyo hivyo, kila siku, mwaka mzima; wanazima umeme asubuhi unarudi jioni au haurudi kabisa, tatizo ni kwamba hatuko kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa Kagera unatokea Uganda, tunanunua Uganda hivi leo Uganda wanashida kubwa ya umeme, umeme ni pungufu. Kwa hiyo, wanakata umeme, Kagera tuko gizani muda mwingi sana. Kwa hiyo niombe Kagera iunganishwe kwenye Gridi ya Taifa. Nafahamu umesogea kama si Geita basi ni Chato wa Gridi umefika umeme. Kazi ifanyike kwa jitihada kubwa ufike mpaka Bukoba, mpaka Karagwe, mpaka Ngara kote tupate umeme wa Grid ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna mradi mwingine pale Rusumo wa umeme wa kuzalisha megawatts 80. Mradi huu umeanza kwa ushirikiano wa nchi tatu, Rwanda, Uganda na Tanzania, lakini kasi yake si kubwa hairidhishi. Kasi iongezwe kusudi mradi huu ukamilike tupate umeme huo. Umeme huo ukipatikana ni mwingi, megawatts 80 kwa Kagera tutapata megawatts 27 utatosha mahitaji yetu na utatusaidia kwa shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia miradi ya REA. Pale kwangu Bukoba Vijijini kwanza nishukuru vijiji vimepata umeme baadhi, lakini siyo vyote. Kuna vijiji vingi havijapata umeme, Kata nzima ya Kibirizi haina umeme. Kijiji cha Kibirizi chenyewe, Omubweya na Kamuli havina umeme. Kata nzima ya Rukoma haina umeme, Rukoma yenyewe, Nsheshe na kwingineko hakuna umeme. Kata ya Kikomelo umeme haujakanyaga. Niombe sana vijiji na kata hizi zipelekewe umeme na kwenye Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka jana kata hizi zimetajwa kwamba kutapelekwa umeme kwenye awamu hii ya mwaka 2015/2020. Niombe kazi ifanyike na umeme usogee Kata ya Kibirizi, Kata ya Lukoma na Kikomelo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata vile vijiji vingine ambavyo umefika, jambo ambalo nafikiri REA hawakulifanyia kazi vizuri, vijiji vya Bukoba ni vikubwa sana, vikubwa kweli kweli; unakuta kijiji kina kaya 400 wamepeleka umeme kaya 15, 20 au 10. Ni kweli kwenye kijiji umeme umefika lakini wananchi hawajapata umeme kama inavyostahili. Niombe sana kwamba jitihada ziendelee kwenye REA III, vijiji hivi viongezewe mgao au kazi isogee ndani zaidi kwenye vijiji ambako tayari wamefika lakini hawajafika maeneo mengi ya kutosha na vitongoji vingine ambavyo havijafikiwa nako vifikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kusema kwamba, umeme huo tunapoupeleka vijijini bado kuna mapungufu fulani fulani.Kwa mfano taasisi kama shule za sekondari au zahanati au sehemu kama hizo tunasema wananchi wajiwekee wenyewe ni kazi kubwa sana kufunga umeme kwenye sekondari uwake madarasani, maabara wafunge wiring mle ndani, nyumba za walimu, wananchi hawawezi, Serikali nayo iangalie uwezekano wa kufanya kazi hii yenyewe, iwe ni sehemu ya mradi, wasiishie tu kupeleka umeme kijijini labda kwenye center halafu wakaondoka.
Mheshimwia Mwenyekiti, taasisi kama shule REA yenyewe ifunge umeme mle ndani kwenye taasisi za Serikali; iwe shule, iwe zahanati kusudi matunda ya umeme yaonekane kwa wananchi walio wengi, taasisi zipate umeme, kama ni hospitali ziweze kuboresha huduma pale tuwe na beni za damu (blood bank) na huduma nyingine kutokana na kutokuwa na umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napenda kukupa hongera kwa kazi unayoifanya kwa ujasiri mkubwa na kukwambia kwamba endelea kuchapa kazi, wala usiwe na wasiwasi, tuko na wewe. Pambana na wote wanaovunja kanuni bila kurudi nyuma, usirudi nyuma, nasi haturudi nyuma, tuko na wewe bega kwa bega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wetu kwa kiasi kikubwa bado tunategemea kilimo kwa asilimia kubwa sana. Kilimo hiki bado ni duni sana, tunatumia jembe la mkono, mbegu hafifu, mbolea tabu, dawa tabu na kadhalika. Kwa hiyo, napenda kuona bajeti hii kama ingesisitiza kwenye kilimo kwa mtindo ambao nimewahi kuusema hapa siku za nyuma na bahati nzuri kwenye Ilani ya CCM mpango huo umeingizwa, kambi za kilimo za vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana wengi Dar es Salaam na miji mingine mingi tu wanakaa hawana kazi za kufanya, lakini tuna maeneo mengi sana nchi hii yana rutuba nyingi sana, yana maji ya kutosha na yanafaa kwa kilimo kizuri. Niliwahi kusema na leo naomba nirudie kwa umuhimu wake kwamba tuanzishe kambi za kilimo kwa vijana hawa ambao wanakaa bila kazi. Juzi Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli alisema kwamba wasiopenda kulima wapelekwe kwa nguvu, lakini mimi nasema wapelekwe kwenye hizo kambi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yenye maji, yenye rutuba yaainishwe, peleka vijana kama 500 kambi moja, wawe na msaada wa usimamizi. Bwana Shamba awepo, Daktari wa kuwatibu awepo wakiugua matumbo na malaria, wapewe mbolea, wapewe trekta kwa sababu kulima kwa jembe la mkono ni tatizo. Huwezi kutoka kwenye uchumi duni kwa jembe la mkono, wapeni matrekta ya mkopo moja au mawili. Wapewe power tillers tano au kumi, hazina gharama kubwa waanze kulima mahindi, maharage, karanga, alizeti na mazao mengine yenye thamani kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa jana nilikuwa hapa, nikaona watu wa Uganda, Kenya, wanakwenda kwa Waziri wa Kilimo aliyekuwepo wakati huo kutafuta mahindi kwa sababu kwao wana njaa lakini yakakosekana kwamba hatuna mahindi ya kutosha kupeleka nchi za nje. Tukiwa na mahindi, maharage, alizeti na kadhalika tutauza nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wakikaa kwenye kambi kwa mwaka mmoja, hata miezi tu, maharage ni siku 60, watavuna maharage mengi sana, watavuna mahindi mengi, tutapata chakula kingi nchini na tutauza nchi za nje lakini wasaidiwe, wasimamiwe, wafanye kazi, hapa kazi tu. Wafanye kazi vizuri, kwa ufasaha na kisasa kuliko kukaa wanazurura mitaani kule Dar es Salaam au humu barabarani Dodoma na sehemu nyingine bila kazi za kufanya. Kazi ni kilimo, wakivuna vizuri ni utajiri mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwaka mmoja watakuwa matajiri hawa. Zile kambi kama watajengewa nyumba za bati zile full suit baada ya miaka miwili watajenga nyumba nzuri za kudumu, watakuwa na fedha, utakuwa mji ule baada ya muda mfupi wa kufanya kilimo hiki kwa namna ambayo naipendekeza. Haya ndiyo mawazo yangu kuhusu kilimo. Maeneo ya namna hii yako mengi sana kote nilikopita, maeneo ya Morogoro kuna rutuba nyingi sana, kuna mito mingi sana, maji mengi, Kigoma rutuba nyingi sana, maji yapo, maeneo ya Ruvuma, Rukwa na maeneo mengine mengi ambayo kuna uwezekano huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo limesemwa na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kwamba Mkoa wa Kagera ni kati ya mikoa mitano maskini sana Tanzania. Ni kweli, Kagera ni mkoa maskini sana na sababu zinajulikana. Zao la biashara Kagera ni kahawa, kahawa hii ina kodi 26, kwa nini wananchi hawa wa Kagera wasiwe maskini? Hii kahawa ikiuzwa nje kwenye soko la dunia kila Sh. 100 mkulima anaambulia Sh. 20, ni wazi atakuwa maskini tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimelisema hili jambo, nilimwambia Mheshimiwa Rais kwenye kampeni, akaja akalisema hapa kwamba kodi hizi zitafutwa. Akasema Waziri wa Fedha, Waziri wa Biashara na Waziri wa Kilimo wafute kodi hizi haraka iwezekanavyo. Juzi nilirudia kuliuliza hapa kwenye swali, nikategemea kwamba kwenye bajeti hii kodi hizi zitaondoka, bado sijasikia zikiondoka lakini Waziri anatuambia Kagera ni maskini, sababu kubwa ndiyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hii haitoshi, kule Kagera barabarani kuna barriers za kutisha. Kila kilometa tano kizuizi barabarani, kama una ndizi toa Sh. 2,000, kama una nanasi toa Sh. 1,000, jamani, lazima wananchi hawa watakuwa maskini, lazima watakuwa maskini wa kutupwa. Hali ni ngumu sana, niombe sana jambo hili liangaliwe kwa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hii haitoshi, kule kuliingia ugonjwa wa mnyauko wa migomba, migomba yote imeungua na ugonjwa. Wananchi hawana chakula, hawana zao la biashara, kwa nini wasiwe maskini? Huu ugonjwa wa mnyauko si mkubwa, ulikuwepo Uganda wakauondoa kwa jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rahisi sana, sheria ndogo zinatungwa na zinasimamiwa. Sasa Kagera ugonjwa huu umekuwa kama vile UKIMWI, hauna dawa, lakini dawa yake ni ndogo mno, ni kuing‟oa migomba ile na wananchi wasimamiwe ugonjwa huo uondoke. Inatakiwa wananchi wapate msaada ugonjwa huu uondoke ili mkoa huu uondoke kwenye dimbwi la umasikini la mikoa mitano ya mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba miaka nyuma kidogo tumechangia sana kujenga maabara za sekondari. Tumejenga sekondari nyingi nchini chini ya mpango maalum, majengo mengi yamekamilika tukaanza kujenga maabara. Maabara hizi sasa zimeachwa, hazijengwi tena, nyingine ziko kwenye lenta pale, kwenye ring beam, nyingine ziko chini ya hapo, nyingine zimeezekwa lakini hazijakamilika. Ni jitihada nzuri iliyofanyika lakini zimeachwa tu hazina kazi, ujenzi haujakamilika na maabara hizi hazijaanza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe mpango ufanywe kwenye bajeti hii, maabara hizi zikamilike ili shule hizi zikamilike ziwe shule nzuri za sekondari, ziwe na vifaa vya maabara za kisayansi ili wanafunzi wasome masomo ya sayansi kwa vitendo. Zisiachwe zikaanza kuota ukungu, nyumba hazijakamilika na hazina vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Mimi ninachangia taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imezungukwa na mataifa kadha wa kadha tunayafahamu wote; Kenya, Burundi na mengine na tunafahamu kwamba pia baada ya Kenya pale mbele kidogo kuna Somalia, Sudan Kusini, kuna Sudan kuna nchi nyingine pale, Eritrea na nyingine ambazo zimekuwa na hali mbaya ya kiusalama. Pale Somalia tunafahamu kuna tatizo la Al-Shabaab kundi la magaidi ambao wanavuruga sana usalama wa nchi hiyo na siyo peke yake hata nchi jirani Kenya imekuwa inashambuliwa mara kwa mara na Al-Shabaab. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sisi Tanzania inaaminika mashambulizi yale ya mwaka jana au mwaka juzi pale Tanga na Mwanza walikuwa ni Al-Shabaab wamekuja ndiyo wakaua watu pale halafu wakaondoka, hatukujua imetokea nini baadaye kama walikamatwa au iliishia wapi. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali ya usalama siyo nzuri kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba tuko salama, ukanda huu tuko kwenye matatizo hayo ya ulinzi na usalama. Hao Al-Shabaab inasemekana wanafanya kazi pamoja na Boko Haram ambao wako Nigeria na kuna taarifa za uhakika kwamba Al-Shabaab na Boko Haram sasa hivi wanatafuta au wameshapata silaha za maangamizi, silaha za sumu (biological weapons) ambazo kwa kweli kama wakizitumia hizo ni hatari kubwa sana kwa yeyote ambaye zitamfikia. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mkataba wa Kimataifa wa Kupambana na Silaha za Maangamizi (Convention on Biological Weapons) na umekuwepo muda mrefu, umewekwa pale UN nafikiri mwaka 1972 kwa nchi kusaini na ku-ratify na kufikia mwaka jana mwishoni nchi nyingi zimeshasaini mkataba huo na zime-ratify, nafikiri kama taarifa zangu ziko sahihi nchi karibu 200 zimeusaini mkataba huo na zimeu-ratify na zinautekeleza. Tanzania bado hatujasaini mkataba huo wa Convention on Biological Weapons na Mwenyekiti amesema pale wakati akiwasilisha kwamba mikataba mingi haijawa ratified, haijawa signed, sababu hazijulikani. Huu wa Biological Weapons Convention kwa umuhimu wake kwa nchi hii ilibidi tuwe tumeusaini siku nyingi sana na tumeu-ratify na tunautekeleza ili tuweze kuwa wanachama katika hiyo convention tupate msaada unaotakiwa linapotokea tatizo au tishio la kutumiwa kwa silaha za maangamizi, silaha za sumu. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua Waziri atakapokuwa anatoa maelezo atuambie kwa nini hatujasaini mkataba huo na kuu-ratify, nini kimetuchelewesha tangu mwaka 1972 mpaka leo wenzetu wamesaini wengi tu nchi 200. Kwa nini, tumeshindwa kuusaini tunajiamini nini, tunasubiri tushambuliwe ndiyo tusaini mkataba huo au una matatizo gani, gharama labda kubwa sana au una masharti mbalimbali tujue nini kinazuia kuusaini mkataba huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa kwa mfano mkataba wa EPA juzi hapa, mwaka jana, hatukusaini kwa sababu kadha wa kadha za kibiashara, za kisiasa, huu wa kujikinga na silaha za maangamizi ni kitu gani kinatuzuia kusaini mkataba huu ili tujilinde zaidi na hali hiyo ambayo ni tishio kubwa sana kwetu. Tumeonja mashambulizi ya Al-Shabaab pale Tanga na Mwanza na siyo kwamba wameacha, tunasikia kila siku wanashambulia Kenya wako Somalia, kila mahali, Eritrea kule wanakwenda wanaua watu na maeneo mengine na mengine. Kwa hiyo napenda kujua sana hili jambo kwa nini hatukusaini na kama tunausaini hauna madhara tunausaini lini. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa dakika tano hizi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi kuja kuhitimisha hoja yangu. (Makofi)
Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa jinsi ambavyo wamepokea taarifa hiyo hususani waliochangia kwa kuunga mkono ambao ni Mheshimiwa Judith Kapinga, Mheshimiwa Priscus Tarimo, Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mheshimiwa Humphrey Polepole na Mheshimiwa Stella Manyanya ametoa taarifa ya kuunga mkono.
Mheshimiwa Spika, kazi tunayoifanya kwenye Kamati ni kuhakikisha kwamba kazi mama ya Bunge ya kutunga sheria haiharibiwi na waliokasimiwa. Kazi ya kutunga sheria iwe ni sheria mama, sheria ndogo ni kazi ya Bunge, lakini Bunge kwa mamlaka yake chini ya Katiba inakasimu mamlaka hayo kwa mamlaka nyingine ziwe Halmashauri, ziwe Wizara na mamlaka nyingine kufanya kazi hiyo.
Kwa hiyo, Kamati hii kazi yake kubwa ni kama watchdog, ni kuangalia kwamba zile sheria ndogo ziko vizuri kwa niaba ya Bunge hili kwa sababu kama nilivyosema mwanzoni kwamba Bunge haliwezi kukwepa lawama iwapo sheria ndogo itakuwa inakinzana na sheria mama au Katiba au sheria nyingine au haitekelezeki, kwa hiyo hiyo ndiyo kazi kubwa ya Kamati.
Mheshimiwa Spika, ni kuweka ustawi wa wananchi ameongea Mheshimiwa Judith Kapinga hapa akasema kuna malipo ya fedha kwa njia ya mtandao ile PayPal na nchi inapoteza mapato. Hilo siyo jambo jema, ninaomba wahusika kama ni Wizara ya Fedha au wahusika wengine wanaohusika na jambo hilo walifanyie kazi ili kusudi nchi isipoteze mapato, ipate mapato ya kutosha na ustawi wa wananchi uweze kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, nimesema hapo awali nirudie kwa ajili ya msisitizo kwamba kuna baadhi ya mamlaka ambazo zimetoza kodi au tozo kwa jambo hilo mamlaka zaidi ya moja. Halmashauri ya Moshi inatoza kwenye kumbi za sinema na starehe kodi ambayo inatozwa pia na Bodi ya Filamu, kwa hiyo mwananchi anaumia analipa kodi mara mbili jambo ambalo siyo zuri, ndiyo kazi yetu kuangalia kwamba halitokei.
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Mamlaka mbalimbali, Wizara na wengine wanaitikia wito haraka na wanafanya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Wabunge wameunga mkono hoja, sina la kuongeza naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Bajeti hii ya Wizara ya Maji ambayo kwangu mimi ni moja ya Bajeti muhimu sana kwa nchi hii, ni muhimu sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji na wasaidizi wake wote katika Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Maji ni tatizo kubwa sana kwa nchi yetu. Maeneo mengi sana hayajapata maji safi na salama, hasa hasa majimbo ya vijijini. Ukiwauliza Waheshimiwa Wabunge wote hapa, wa vijijini, wote kilio ni maji. Kilio kikubwa sana ni kuhusu maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyoongea waliotangulia, inasikitisha sana kwamba bajeti ya mwaka huu tunayoijadili imepungua kutoka ile ya mwaka jana tunayomalizia. Kutoka bilioni 900 na pointi kwenda bilioni 600, hiki ni kitu cha kusikitisha na kwa kweli si jambo zuri. Serikali iangalie kwa makini hizi fedha zirudishwe katika bajeti ya maji angalau basi ifikie ile ile kama ya mwaka tunaoumalizia huu. Hata kama haikutoka yote lakini ifikie pale ikipatikana, itumike. Bajeti imepanda kutoka trilioni 29 hadi 32, kwa nini ya maji ipungue? Bajeti nzima ya Serikali ikipanda maana yake na za Wizara zote zinapanda, lakini ya maji imepungua, hili sio jambo jema hata kidogo ukizingatia kwamba uko tunakotoka vijijini hali ya maji ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulizungumza humu siku nyingi tu kuhusu Wakala wa Maji, tuwe na Mfuko wa Maji. Bahati nzuri ukaanzishwa lakini hauna pesa, kwa hiyo hauwezi kufanya kazi inayotakiwa au inayotegemewa kwa sababu hakuna pesa. Yale aliyoyasema Mheshimiwa Nagu kwamba tulisema itoke sh. 50 iende sh.100 na naiunga mkono. Tuongeze tozo katika mafuta ya diesel na petrol badala ya sh. 50 iwe sh. 100 ili angalau mfuko huu upate fedha ya kutosha kuhudumia maji vijijini. Hili ni jambo kubwa na litasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata habari kwamba jambo hili lilipofika kwa Waziri wa Fedha akasema kwamba si zuri maana tukiliruhusu litaleta inflation, si kweli! Hakuna inflation kwenye jambo hili. Leo unga umepanda mara nne kutoka bei ya mwaka jana je, ni kwa sababu ya petrol kupanda? Petrol haijapanda. Unga umepanda mara nne kutoka sh. 1,800 mpaka karibu sh. 2500. Kwa hiyo si sababu ya mafuta kupanda ndiyo maana unga umepanda, inflation iko pale pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukisema watu waendelee kunywa maji machafu vijijini maji ambayo sio safi na salama wataugua matumbo, typhoid, kuharisha na kadhalika utatumia shilingi ngapi kuwatibu hawa? Madawa, vifaa tiba, kulaza hospitalini, gharama yake ni kubwa kuliko hiyo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema kwamba itatokana na kupandisha bei ya mafuta kutoka sh. 50 kwenda sh. 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo si kweli kwamba kutakuwa na inflation isipokuwa kutokupandisha tozo hii ndiko kunasababisha inflation iwepo kwa sababu watu wanaugua sana. Zahanati na hospitali zinajaa wagonjwa, ambulance zinatumika sana kwa hiyo hali inakuwa ngumu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi ya maji kwa vijiji 10 kwenye kila Halmashauri, yote imekwama. Miradi hii si ya leo wala si ya jana, ina miaka minne, mitano, nane, imekwama. Pale kwangu kuna kijiji kimoja Ibwera kuna mabomba yaliletwa pale mengi sana, mabomba ya kutosha mradi mzima yako pale kando ya barabara yamekaa miaka minne hadi yamebadilika rangi kutoka nyeusi yamekuwa meupe na yametoboka. Sasa hasara kubwa sana kwa sababu ya kutokuwa na fedha za kumalizia mradi ule. Nashauri sana kwamba bajeti ya maji kwa kweli tuizingatie na tuongeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya Kibirizi kule kwangu imekwama, miradi ya Bituntu imekwama, Lubafu, Katoma yote imekwama; Miradi yote vijiji 10 haija-take off haijaweza kukamilika kwa sababu chanzo cha fedha kutoka Benki ya Dunia kimekoma. Lazima tusimamie Mfuko wa Maji upate fedha. Pamoja na kupandisha sh. 50 kwenda sh. 100 kwenye mafuta ya magari diesel na petrol mimi napendekeza yafuatayo yaongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni hilo, hiyo tozo mafuta toka sh. 50 kwenda sh. 100 iongezwe. Pia maji haya tunayokunywa mjini haya ya chupa, vijijini hamna maji ya chupa, yako mjini, watu wenye fedha wako mjini; wananunua maji nusu lita sh. 2000. Huku nako tuweke tozo angalau kwa lita sh. 50 kwenye maji ya chupa. Maji ya chupa yawe na tozo sh. 50 iende kwa Wakala wa Maji Vijijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bia; wanywaji wa bia wako mjini, nako kuwe na tozo kwa lita moja ya bia angalau sh. 50 iende Mfuko wa Maji Vijijini. Soda; wanywaji soda wako mijini, angalau kwa lita nzima ya soda sh. 20. Pendekezo langu, kiasi hicho kiende kwenye Mfuko wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipendekeze pia kwamba kwenye bill za maji, mijini kuna maji, miji yote ina maji ya bomba mazuri safi na salama. Kuna bill za maji za kila mwezi au za kila wakati angalau asilimia tano ya ile bill ikatwe iende katika Mfuko wa Maji Vijijini ili nao wapate maji. Wakazi wa mjini ni wa vijijini hawa, wanatoka vijijini wanakuja mjini, walipe angalau asilimia tano ya zile bill ziende kwenye Mfuko wa Maji Vijijini ili Wakala wa Maji Vijijini uwe na uwezo wa kuhudumia miradi ya maji vijijini. Vile vile wakala huu uimarishwe, watafutwe watu wenye uwezo, wajitegemee, watafute fedha ndani na nje ya nchi. Waombe kwa wafadhili, waseme tuna shida vijijini, watu wanaugua matumbo sababu ya maji machafu tutafute fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo REA, tujifunze REA, REA imefanikiwa baada ya miaka michache, sasa hivi imefanikiwa kwa asilimia 70% nchi nzima. Kwa hiyo wakala uimarishwe uweze kufanya kazi ya kusaidia kupata maji vijijini. Hata hivyo, Serikali na yenyewe kwa kweli kama nilivyosema mwanzoni, kupunguza bajeti ya kutoka milioni 900 kwenda 600 si sahihi. Fedha irudishwe, ibaki angalau 900 hiyo hiyo na itoke; kwa sababu ilikuwa milioni 900 lakini iliyotoka ni asilimia 19, ni kiasi kidogo sana itoke iende kwenye miradi ya maji ili wananchi wa vijijini wapate huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni muhimu sana, mimi ukiniuliza kati ya maji na umeme nitakwambia maji ni muhimu kuliko umeme. Umeme unaweza ukaona kwa kibatari lakini huwezi kuishi bila maji, kwa hiyo tuyape uzito unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa mradi wangu wa maji pale Bukoba Vijijini, mradi wa maji wa miaka mingi, miaka ya 60 na 70 mwanzoni, wa pale Maruku. Nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri, mradi huu ni mzuri, ulijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, ukafanya kazi nzuri sana, lakini miaka mingi imepita umechakaa. Mradi ule umechakaa yale mabomba tu, matanki yako vizuri na chanzo kiko vizuri. Kama tukipata milioni 300 ama 400 mradi ule unakarabatiwa unakuwa mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mradi huu ufufuliwe, upate fedha kidogo ili na wenyewe uweze kuhudumia Kata mbili, Maruku na Kanyangereko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ulinzi na Usalama, JKT na wasaidizi wake wote na Wakuu wa Majeshi kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri sana ya kuendelea kuiweka nchi yetu katika hali ya usalama na amani. Unaposikia amani inakuwepo si kazi rahisi, ni kazi ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye mchango wangu, na leo nitaongelea mikataba ya kimataifa; kwanza niweke vizuri Taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo imepotosha mambo mengi. Moja ya eneo ambalo imepotosha wanashauri kwamba jeshi litumike kufanya economic espionage; hii si kazi ya jeshi, economic espionage si kazi ya jeshi, tuwaachie wanaohusika na hiyo wafanye si wanajeshi. Lakini maeneo mengine ambako wamepotosha yako mengi, wanazungumzia kuhusu Al-Shabab na Boko Haram. Bahati mbaya hawajui hata historia ya Somalia wala ya Nigeria. Al-Shabaab ni kikundi cha kikabila kiko Somalia, ni watu wa kabila fulani huwa wanapingana na kabila lingine wamejiandaa na silaha zao ndiyo wanafanya mambo ya Al- Shabaab.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Boko Haram vilevile ina ukabila, ina element za ukabila kule Nigeria, lakini pia ni kutokana na matatizo ya kiuchumi, wanajiona kwamba wametengwa, wako marginalized ndiyo maana wameunda kikundi cha Boko Haram wanashambulia wananchi wengine wenzao wa Nigeria si mambo waliyoyasema wao ambao ni upotoshaji mtupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia suala la Malawi, kwamba Malawi imesema haitakubali usuluhishi, wameyapata wapi? Usuluhishi huu bado, unafanywa na Kamati Maalum inaongozwa na Mheshimiwa Joaquim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji na usuluhishi haujatolewa. Sasa kusema Malawi wamekataa wamekataa wapi na lini? Kwa hiyo, hili wao ndio wachonganishi, wanachonganisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya kuingia kwenye Kamati za Siasa za CCM, huu ni uchonganishi na upotoshaji. Tumewahi kuwa na Wakuu wa Mikoa ambao si wana-CCM, tuna mifano hai. Mkuu wa Mkoa wa Geita hakuwa mwana-CCM, alikuwa haingii kwenye Kamati ya Siasa. Tulikuwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma hakuwa mwana-CCM alikuwa haingii kwenye Kamati ya Siasa ya Mkoa, labda kama anaitwa kutoa taarifa maalum kwa sababu CCM ndicho Chama Tawala, kina majukumu ya kusimamia Ilani ya Uchaguzi. Hata wewe Waitara leo ukiwa Mkuu wa Wilaya ukaitwa kwenye Kamati ya Siasa utakwenda tu, huna ujanja kwa sababu CCM ndiyo inayoendesha Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaweke sawa haya ili kuondoa upotoshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la usalama na ulinzi. Nimesema namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweka nchi yetu katika hali ya usalama, lakini nishauri kidogo, usalama upo lakini lazima tuzidi kuuimarisha na kuulinda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasikia hivi karibuni kuna mashambulizi pale Mikoa ya Pwani, hasa Mkoa wa Pwani wenyewe, Rufiji, Kibiti watu wanauawa, jana au juzi kauawa Katibu wa CCM mmoja na wengine, lakini miaka miwili iliyopita tulisikia mauaji ya watu kule Tanga na mengine yalitokea pale Mwanza ya watu wengi na inaaminika kwamba haya mauaji yalifanywa na Al-Shabaab.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hii inayofanywa kule Pwani hatujui lakini inawezekana ikawa ni Al-Shabaab wanakuja wanaingia kwenye maeneo yetu, wanaleta madhara ambayo ni kuua watu. Sasa kuna taarifa kwamba Al-Shabaab wanaanza kufanya ushirikiano na Boko Haram, na kuna taarifa kwamba haya makundi mawili ya kigaidi wanajaribu kutafuta silaha za sumu (biological weapons), ambazo wazitumie kwenye mapambano yao na raia wasiokuwa na hatia huko Somalia, Nigeria na kwingineko. Tunasikia wanavyofanya Kenya wanaua watu huko shuleni, wanaua wanafunzi vyuo vikuu, wanafanya maangamizi sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama watapata silaha za sumu kama wanavyojitahidi kufanya, itakuwa ni hatari kubwa sana hata kwetu. Kama kweli waliingia wakafanya mauaji pale Tanga miaka miwili iliyopita, halafu wakiwa na silaha za sumu tutakuwa katika hali ngumu sana ya kiusalama. Tanzania na Somalia haziko mbali sana, kati yetu kuna Kenya tu kama kilometa 400 kutoka Somalia mpaka Tanga pale kwa kwenye Maji; kwa hiyo kuna haja ya kuimarisha ulinzi katika maeneo haya.
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru tena kwa fursa hii ya kuhitimisha taarifa yangu, lakini pia niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati yangu ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kazi kubwa sana walioifanya tulioifanya pamoja ambayo imetufikisha hatua hii ya sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kutoa shukrani kwa Wabunge wote waliochangia na waliosikiliza taarifa hii tangu asubuhi kwa umakini mkubwa. Wabunge waliochangia taarifa yangu wako jumla 19. Wa kuandika wako Mheshimiwa Susan Lyimo, Mheshimiwa Zaynabu Vullu, Mheshimiwa Ester Mahawe, Mheshimiwa Albert Obama, Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mheshimiwa Omary Mgumba, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Sebastian Kapufi, Mheshimiwa Ester Matiko, Mheshimiwa Angelina Malembeka, Mheshimiwa Rhoda Kunchela na Mheshimiwa Waitara Mwita na Wabunge saba wamechangia kwa kusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Mheshimiwa Naibu Waziri George Kakunda, Mheshimiwa Waziri Selemani Jafo na Mheshimiwa Waziri George Mkuchika kwa majibu waliyoyatoa wakijibu hoja za Wabunge ambao kwa kweli wamejibu kwa ufasaha na kwa ukamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee kwenye mambo kadhaa machache ambayo yametajwa katika michango ya Waheshimiwa Wabunge niliowataja, la kwanza ni MKURABITA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA ni mpango mzuri sana ambao unasaidia wananchi wanyonge kurasimisha biashara zao na mali zao, ardhi, lakini MKURABITA ina hela kidogo sana, ukiangalia kwenye bajeti inapata mgao kidogo sana. Kwa hiyo, kwa kweli nipende kusisitiza kwamba ni vizuri Serikali ikaangalia kuongeza bajeti kwenye MKURABITA kusudi kazi ya MKURABITA iweze kuonekana kwa manufaa yanayokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la pili, kwenye MKURABITA kusisitiza kwamba hati miliki za kimila zikubaliwe na mabenki. Kuna baadhi ya mabenki ambazo zinazikataa hati miliki hizi kwa sababu ile ardhi ambayo juu yake kuna hiyo hati miliki ya kimila haiuziki. Sasa niseme kwamba ni vizuri Serikali ingefanya utaratibu ili ardhi hiyo ikaweza kuuzika kama mkopaji ata-default, na ikiwa hivyo benki zitakubali kutoa mikopo kwa hati miliki hizi.Haki miliki hizi ziwe na manufaa kwa wananchi wanyonge waweze kukopa na kujiendeleza kiuchumi lakini pia kuondoa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni TASAF. TASAF nayo imefanya kazi nzuri sana kwa miaka iliyokuwepo; TASAF ya kwanza, TASAF ya pili, leo ya tatu. TASAF ya kwanza na ya pili zilijenga barabara nyingi, zilijenga madaraja kadhaa, zilijenga shule, madarasa na kadhalika. TASAF hii ya sasa inaweka mkazo kwenye kaya maskini sana, na kwa msaada wa TASAF kaya nyingi zimeweza kupata chakula kizuri, milo miwili kwa siku, milo mitatu kwa siku. Watoto wameweza kwenda kliniki na kwenda shule kwa ufasaha. Kwa hiyo, niiombe Serikali iongeze mchango wake kwenye TASAF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tulionao imetoa shilingi milioni 750 kati ya lengo la bilioni tatu; ni kidogo lakini si haba. Ni robo ya lengo la Serikali kutoa lakini si haba sana. Kwa hiyo, waongeze jitihada ya kutoa fedha kusudi na wale wafadhili waweze kuongeza fedha TASAF iweze kuendelea kutuneemesha Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limeongelewa na Wabunge wengi kwenye michango yao ni asilimia 10 kutoka Halmashauri kwenda kwenye wanawake na vijana. Jambo hili limekuwa gumu kwa sababu Halmashauri zinafanya kwa hiari, hazilazimiki kutoa asilimia 10, hakuna sheria inayowalazimisha kwamba watoe asilimia 10, tano kwa vijana na tano kwa wanawake. Tunasisitiza kwamba sheria ingetungwa ili Halmashauri hizi zilazimike kutoa michango hii kwenda kwa wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni TARURA. TARURA ni mamlaka au wakala changa sana ina miezi michache imeanzishwa lakini imefanya kazi nzuri sana. Kazi nzuri imeonekana, barabara nyingi za vijijini na mijini zimeanza kujengwa. Hata hivyo inapewa mgao kidogo sana kutoka Road Fund Board, asilimia 30. Kwa kweli hiki ni kiasi kidogo mno. Ina Halmashauri 185 barabara zote za Halmashauri za vijijini na za mijini. Kwa hiyo, ni kwakweli ni jambo jema kama walivyosema wabunge kiasi hiki kiongezwe ili kusudi TARURA iweze kufanya kazi ambayo inaonesha ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi hewa waliopunguzwa kutokana na vyeti hewa na vyeti Ifake wameathiri sana utendaji kazi Serikalini hasa kwenye afya na madereva. Kama walivyosema Wabunge madereva walikuwa na uzoefu mkubwa, lakini wana vyeti fake, basi nitoe wito kwamba wengine waajiriwe, waajiriwe wa kutosha kusudi upungufu huu uliojitokeza hata kwenye afya uweze kuondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya amesema Mheshimiwa Kahigi na Waheshimiwa wengine, kuna Wilaya hazina Hospitali za Wilaya. Halmashauri 64 hazina hospitali za wilaya. Hizi halmashauri 64 Mkoa wa Katavi wote hauna hospitali hata moja ya Wilaya. Mkoa wa Kagera wote, Kagera ina Wilaya nane hauna hata wilaya moja yenye hospitali ya Wilaya. Kwa kweli ni vizuri sana kama alivyosema Mheshimiwa Jafo tulimsikia, ametoa ahadi kwamba fedha zitatengwa na itajengwa Hospitali ya Wilaya kule Bukoba moja au mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya eimu imezungumziwa sana na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali, lakini mimi niongelee jambo moja kwenye sekta ya elimu. Ukosefu wa vyoo kwenye shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule nyingi hazina vyoo, hili ni jambo la fedheha kubwa sana. Jana liliongelewa jambo la taulo za wanafunzi wa kike, mimi nasema la vyoo ni kubwa zaidi, kwa sababu la linahusu wasichana na wavulana, wanakwenda wapi? Serikali iweke bidii na jitihada kubwa sana kujenga vyoo. Ni bora nyumba za walimu zikasubiri, shule mpya zisijengwe ili zilizopo zipate vyoo watoto wapate mahali pa kujisitiri, vijengwe vyoo vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nchi hii imeendelea na kupiga hatua. Barabara nyingi zimejengwa lami, tunajenga barabara za juu pale TAZARA na Ubungo, tunajenga reli ya umeme (standard gauge) lakini hatuna vyoo mashuleni, ni jambo la aibu, fedheha na adha kubwa kwa wanafunzi. Hili lingetiliwa mkazo kusudi liweze kutatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali ikitia nguvu akisema Rais kwamba liishe linaisha. Rais amesema madawati likaisha, tatizo la madawati limekwisha. Kwa hiyo, nafikiri hata Mawaziri wanaohusika na sekta hii ya elimu wakazanie suala la vyoo mashuleni na liondolewe matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji vijijini ni tatizo kubwa sana. Leo asubuhi nimesikia miongozo humu ndani kuhusu maji vijijini. Waheshimiwa Wabunge wamesimama wote wanalalamika kuhusu maji vijijini. Juzi alisema Naibu Waziri wa TAMISEMI kwamba kuna fedha shilingi bilioni 156 kwenye akaunti ya maji vijijini, lakini kitu kinachopungua ni wakala; wakala haujaanza kusudi huduma hii iweze kutolewa kwa vijiji. Nisisitize kwamba ni vizuri kama wakala huu angeanza mara moja kusudi ishughulikie adha ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa ufupi niombe tena Bunge lako Tukufu liazimie kama taarifa yetu ilivyosema na ninaomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi kuchangia asubuhi ya leo. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya jana ambayo imesheheni mambo makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Yeye mwenyewe Waziri Mkuu anafanya kazi nzuri ya kusimamia Serikali kuzunguka nchi nzima na kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri sana ya Serikali yake. Serikali inafanya kazi nzuri sana, kila mtu humu ni shahidi kazi inayofanyika kubwa sana. Kujenga reli ya kisasa ya kimataifa ya umeme, ndege zimenunuliwa zinakuja, barabara zinajengwa, madini hata kesho wanafungua ukuta mkubwa pale Mererani kuzuia wizi wa madini, sekta ya umeme, sekta mbalimbali zinashughulikiwa na zinapiga hatua kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi na nimesimama hapa kuchangia maeneo mawili, maji na kilimo. Katika maji vijijini kila Mbunge anaposimama hapa hasa Wabunge wa vijijini wanazungumzia maji vijijini, bado kuna tatizo kwenye maji vijijini. Niombe sana lile wazo tulilokwishalisema humu ndani, la kuanzisha Wakala wa Maji vijijini lianzishwe mara moja. Tuanzishe wakala wa maji vijijini. Maji vijijini bado ni changamoto kubwa, wananchi vijijini wana changamoto kubwa sana ya kupata maji salama na safi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kule kuna maeneo mengi ambayo ukiona maji wanayotumia wananchi utashangaa na kuogopa. Wanatembea kilometa tatu, kilomita nne kupata maji hayo, hayo maji yenyewe yanafanana na chai ya maziwa, ndio wanayotumia, ndio wanayokunywa, ndio wanayopikia. Sasa tukianzisha Wakala wa Maji tutapambana na hali hii tutaweza kupata maji mazuri kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliposimama juzi hapa kuzungumzia maji lilikuwa swali nikajibiwa kwamba tayari kuna pesa kwenye mfuko wa maji zaidi ya shilingi bilioni 160. Sasa kama kuna fedha lakini hazitumiki na yenyewe haina tija. Wakala aanze, hiyo fedha bilioni 160 ianze kutumika katika vijiji vyetu. Wakala aanze, atafute fedha, ajenge miradi ya maji vijiji. Kila Halmashauri ilikuwa na miradi 10 ya maji, mingi ya hii haijakamilika, asilimia kubwa haijakamilika hakuna fedha, Wakala wa Maji uanzishwe kusudi tupate ufumbuzi wa tatizo la maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa mfano kwamba REA imekuwa na mafanikio makubwa na REA ni Wakala wa Umeme Vijijini. Tuwe na Wakala wa Maji Vijijini tupate kufumbua tatizo la maji. Kule kwangu kwa mfano kata ya Ruhunga maeneo ya Rugaze kule Vijiji vya Rugaze, Kibirizi, Rubweya, Kyamolaile kuna sehemu nyingine nyingi, maji ni changamoto kubwa sana na ufumbuzi ni huo tu tupate Wakala wa Maji atafute fedha, kwenye bajeti kwenye vyanzo vingine, misaada na mikopo kutoka nje, kusudi tatizo la maji liweze kupata ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ninalotaka kuzungumzia ni kilimo, ukisoma Ilani ya CCM ya mwaka 2015, kuna makambi ya kilimo. Ukienda Dar es Salaam au miji mingine lakini Dar es Salaam hasa kuna vijana wengi sana maeneo ya mbalimbali Buguruni pale, Ubungo ukienda Mwenge, ukienda Tandale, Mbagala, Temeke, kila maeneo kuna vijana wengi sana ambao hawana kazi wanayofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wale wanauza pipi, wanauza kandambili, wanauza vitambaa vya mikononi na vijana wenye nguvu vijana wenye miaka 25, miaka 30, miaka 18 wanauza pipi, hawana kazi ya kufanya. Ukiwaambia waende kulima mashambani hawatakwenda kwa sababu jembe la mkono ni tatizo, wanaogopa jembe la mkono na wana haki ya kuliogopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema ndio maana ikaingia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi wa mwaka 2015 kwamba tuanzishe kambi za kilimo za vijana. Maeneo mengi Tanzania yana rutuba, maeneo mengi ya Morogoro kule Kilosa, Mvomero, ukienda Rukwa, ukienda Kigoma hata Dodoma hapa shida ni maji tu. Maeneo yana rutuba sana na maeneo makubwa ambayo hayajalimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema vijana wapelekwe kule ukisema kila kambi vijana 100, ukawapa trekta moja au mbili ya mkopo au power tiller kadhaa na msimamizi wa kuwasimamia bwana shamba ambaye amesomea hayo mambo ya kilimo kidogo, wakaanza kulima alizeti, wakaanza kulima maharage, mahindi, pamba na mazao mengine ya muda mfupi na ya muda mrefu, hawa vijana baada ya miezi sita watakuwa matajiri. Baada ya miezi sita kwa trekta moja au mbili nchi hii itakuwa na chakula kingi sana shida ya chakula itakwisha, Tanzania itakuwa tajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Bungeni humu miaka mitatu iliyopita nikaona Naibu Waziri mmoja anaenda kwa Waziri wa Kilimo wakati huo, anamwambia amepata maombi ya nchi nafikiri ilikuwa Ghana au Nigeria, wanaomba kununua chakula, akamjibu chakula hakipo kwa sababu kimeshauzwa Kenya, ile reserve ya chakula imekwisha. Sasa tungelima chakula kwa njia hii ya makambi ya vijana ambao ni wengi sana ardhi ipo tungepata mafanikio makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nchi ambazo hazilimi nchi za jangwa kama huku kaskazini au Uarabuni hawalimi wale lakini wanakula na wana fedha nyingi sana. Tulime kwa wingi sana kwa vijana hawa kwa kutumia trekta na power tiller na vifaa vingine, tupate mazao mengi sana, tupate ufumbuzi kwanza kwa ajira kwa vijana hawa na ufumbuzi wa kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusifanye makosa ambayo tuliyofanya huko nyuma miaka ya 1974 tulipoanzisha vijiji vya ujamaa tufanye kwa mpango mkakati mzuri. Moja, tunapoanzisha mkakati huu wa Makambi ya Kilimo kwenye Wizara husika kama ni ya Kilimo kama ni ya Masoko au kwingineko Serikalini, kuwe na vitengo maalum vya kutafuta masoko ya mazao haya nje. Huko Dafur Sudan huko, nchi za jangwani huko ambako hawalimi, nchi za Uarabuni huko, kuwe na mkakati maalum wa kutafuta masoko ya kuuza hayo mahindi, maharage, alizeti, korosho na mengine, kuwa aggressive kuuza mazao haya kwa bei nzuri na kwa wakati ili vijana hawa wapate fedha wanayohitaji ambayo wameifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo mwanzo, kilimo hiki kiratibiwe vizuri kuwe na Bwana shamba au Bibi shamba na researchers officers ambao watasaidia vijana hawa katika kulima kisasa, kutumia pembejeo, mbolea na madawa na kadhalika. Tusitegemee mvua, tusitegemee mvua, nchi hii maeneo mengi ina mvua mara mbili kwa mwaka. Hata pale ambako penye mvua moja kama Dodoma kuna mabwawa ambayo ukizuia ukapiga tuta pale mbele unazuia maji mengi sana huku nyuma, unamwagilia mwaka mzima au angalau miezi nane kwa mwaka wapate tija ya kilimo ambacho nakizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaondoa kilimo ambacho tumekizoea cha mkulima mmoja mmoja ambacho ni vigumu kumhudumia mkulima mmoja mmoja kumpelekea pembejeo, mbolea, madawa ni vigumu sana. Wakiwa kikundi cha 100 au 200 ni rahisi kuwahudumia na huduma ikawa nzuri ya kupeleka pembejeo na kuondoa mazao ukapeleka kwenye soko. Nchi zote duniani zilizoendelea Marekani, Ulaya wameendelea kwa kilimo. Tu-modernize kilimo chetu kwa vijana hawa wakapata ajira na nchi itapata neema kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda, uchumi wa viwanda, viwanda vingi vinategemea kilimo, kama mahindi, pamba na kahawa ambavyo baadaye unaweza kuvi-process. Kwa hiyo, baadhi ya viwanda tena vingi vitatumia mazao haya haya kuongezea uchumi wa viwanda katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii ya kuja kuhitimisha hoja yangu. Nianze kwa kuwashukuru Wabunge wote waliochangia na kuunga mkono na kwa kweli wamezungumza vizuri sana. Lakini nisisitize tu kwamba kwa kweli tukubali tusikubali, Rais, Dkt. Magufuli, ana utendaji uliotukuka, huo ndiyo ukweli, hiyo haina ubishi. Suala la siasa na mambo ya mlengo wa kushoto na kulia tusiyaweke hapa, mambo yanaonekana wazi kwamba utendaji wa Rais, Dkt. Magufuli, ni wa hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wamesema Wabunge wamechangia hapa, nami nilisema tunafahamu wote kabla ya Rais, Dkt. Magufuli, kuingia madarakani kulikuwa na kiwango cha rushwa kikubwa sana, ukuenda kwenye mahakama, ukienda zahanati uwe na hela ya kumpa nesi ili akupe huduma. Leo hiyo habari imekwisha, utendaji umekuwa mzuri sana.
Mheshimiwa Spika, huduma kwa wananchi, kwangu pale Bukoba Vijijini kuna mzee mmoja alikuwa ananisimulia alikwenda Ofisi ya DC, akapewa nafasi ya kumuona bila appointment, akasema huyu Mheshimiwa Dkt. Magufuli mtu wa ajabu sana, zamani usingeweza kwenda kwa DC bila appointment ukamuona, hili ni jambo ambalo utawala umekuwa mzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini wote tunaona huduma za maji zinaboreshwa, tumeanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) ambayo inafanya kazi vizuri, REA inazidi kushika kasi wote tunashuhudia. Alipoingia madarakani Rais, Dkt. Magufuli, alikuta vijiji kama 2,000 vyenye umeme, leo vijiji 7,000 vimepata umeme, jambo kubwa sana. Amesimamia ujenzi wa Stiegler’s Gorge licha ya kwamba nchi ni kubwa tajiri zinapinga sana jambo hili, amekuwa imara sana, hatetereki na tunajenga hili Bwawa la Stiegler’s Gorge na mambo mengine mengi ambayo anayafanya na Wabunge wamesema.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Salome Makamba amesema mambo kadhaa hapa na nimeshangaa. Anasema kukasimu hakuelewi, yeye ni mwanasheria wa viwango vya juu nashangaa anasema haelewi kukasimu. Leo Mheshimiwa Mbowe hayupo hapa amekasimu kwa Mheshimiwa Dkt. Sware, sasa ajabu iko wapi; Mheshimiwa Dkt. Sware amekaa pale, tunamuona Mheshimiwa Selasini hapa anakaimu nafasi ya Mheshimiwa Mbowe, jambo ambalo ni la kawaida. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, anasema haijaenda bajeti asilimia 50 kwenye mikoa na wilaya; leo ni Novemba, miezi minne tu ya bajeti ya mwaka wa fedha, tusubiri, na huduma zinafanyika kule vijijini tunaziona. Kwa hiyo, tuwe na subira, kazi zinakwenda na huduma zinazidi kusonga kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, leo tumesikia kwenye taarifa kwenye azimio humu, amejenga vituo vya afya 352 kwa mwaka mmoja; 352, katika historia ya nchi hii haijawahi kutokea, na amejenga kwa fedha ya chini sana ndogo. Kabla ya yeye Rais, Dkt. Magufuli, ilikuwa kituo kimoja cha afya shilingi bilioni 2.7, leo kituo hichohicho shilingi milioni 400, 500, ndiyo maana vimekuwa vingi kwa sababu ya usimamizi mzuri tunazidi kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli nahitimisha hoja yangu kwa kusema kwamba Rais, Dkt. Magufuli, anafanya kazi kwa utendaji uliotukuka na tuzidi kumuunga mkono. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. JASSON S. RWEIKIZA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi kuja kuhitimisha hoja yangu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Niwashukuru pia Wabunge wote waliochangia na kutoa mawazo mbalimbali kwenye hoja hii, ambayo yamekuwa ni ya msaada mkubwa lakini pia niwashukuru sana Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao wamejibu nyingi ya hoja hizo na kwahiyo kwenye majumuisho yangu sitagusia yale ambayo wameshajibu Mawaziri nitasema tu yale ambayo nataka kuweka msisitizo kidogo.
Mheshimiwa Lolesia Bukwimba alisisitiza sana kuhusu suala la TARURA. TARURA inapata pesa kidogo sana 30% ya hela ya road fund. Road Fund ina fedha za kutosha kujenga barabara za nchi hii lakini hela nyingi inaenda TANROADS, TANROADS barabara nyingi zimekwisha kamilika zimejengwa kwa lami madaraja yapo TARURA ina barabara nyingi sana za vijijini ambazo ni mpya ambazo zinapeleka pembejeo, zinatoa mazao mashambani huko.
Kwa hiyo kwa kweli nisisitize tu kwamba mchango wa Mheshimiwa Lolesia Bukwimba umekuwa ni wa msaada kuonesha umuhimu wa jinsi ambavyo tumekuwa tukisema mara nyingi kwamba TARURA iongezewe fedha kusudi iweze kumudu majukumu yake, inakwama kwasababu fedha zake ni ndogo sana, lakini pia ameongelea sekta ya afya ambayo Waheshimiwa Mawaziri wamejibu kwa kina na kwa ukamilifu. Kuhusu kuajiri watumishi na mambo mengine.
Mheshimiwa Pauline Gekul naye amezungumza suala la TARURA kupewa 50% amependekeza kwamba ipewe 50% maana yake na TANROADS ipewe 50% ya fedha za road fund hili ni jambo zuri, tunaliunga mkono sisi kama Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amesema pia Mheshimiwa Gekul mafunzo kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni jambo zuri sana, wamechaguliwa juzi hapa mwaka jana mwishoni, na kwa kweli hawana ujuzi ule unaotakiwa kumudu majukumu yao, ni vizuri waende kwenye mafunzo niseme tu kwamba mafunzo haya yako tayari, kile Chuo cha Hombolo kina kozi hizo za muda mfupi, za muda wa kati na muda mrefu. Halmashauri zijipange zipeleke hawa wenyeviti na viongozi wengine kwenye mafunzo hayo ili kuweza kupata mafunzo na kumudu shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia wazee iwekwe kwenye mpango wa 10% ni jambo zuri, ni wazo zuri kwa sababu wazee hao kwa kweli wengine hawana uwezo wa kujimudu maisha yao, ni vizuri wakapewa asilimia hizo angalau mbili kwenye hiyo 10 waweze kujisaidia katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama kamati tumekuwa wakali sana kwenye halmashauri hizi kwamba wahakikishe wanatenga asilimia 10 na kuzipeleka kwa wanawake na vijana na mwaka 2017 tuliwagomea hata bajeti zao, hatukupitisha bajeti zao kwamba yeyote ambaye hakutoa 10% asipewe fedha za bajeti, mwaka uliofuata wakawa wamefanya maboresho makubwa sana na fedha zikawa zimeongezeka. Kwa hiyo nazipongeza Halmashauri hizo ambazo zimeboresha matoleo hayo kwa walemavu, akinamama na vijana. Sasa pendekezo la Mheshimiwa Gekul ni zuri kwamba hata wazee wafikiriwe kuingizwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ruth Mollel ameongelea mambo kadhaa mambo mengi lakini mojawapo kubwa ni kwamba DART haijahama kutoka pale Jangwani kwenye mafuriko. Ni kweli na sisi tumeshatoa maagizo kwa DART kwamba wahame toka pale Jangwani waende sehemu ambayo ni ya juu haina mafuriko ya mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Godbless Lema ameongelea mambo mengi pia, moja amesema ushindi ni kwa mtutu badala ya kutumia kura, jambo hili siyo la kweli kwa sababu kama ni kweli hata yeye amegombea na ameshinda, ina maana ameshinda kwa mtutu pia, ameingia humu kwa mtutu ambayo siyo kweli hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Vedasto Ngombale amepongeza TASAF, ndugu Mussa Mbarouk amezungumzia mambo mengi amesema uchaguzi haukuwa huru na haki, siyo kweli CCM ilishinda kwa haki kwa kura nyingi, kwa sababu haki ni pamoja na kujitoa, waliojitoa walikuwa na haki ya kujitoa, walijitoa wenyewe CCM ikaendelea na uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jacqueline Msongozi amezungumza mambo kadhaa mengi, Mheshimiwa Mwanne Mchemba TARURA, MKURABITA, TAGLA na eGA, Mheshimiwa Joram Hongoli wote wamezungumzia mambo ya TARURA hii inaonesha kwamba TARURA kwa kweli inastahili kuongezewa fedha. Kwa hiyo ni msisitizo mzuri ambao na sisi Kamati tunasisitiza kwamba TARURA iongezewe mgao wa fedha za road fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuaajiri walimu Waheshimiwa Mawaziri wamejibu hiyo. Suala la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga kwamba uraia pacha uruhusiwe. Sisi tunaunga mkono kama kamati uraia pacha uruhusiwe kwa sababu hawa wanaokwenda kule nje kwanza hawajaasi uraia wa nchi hii, lakini hawajakimbia nchi pia wameenda kutafuta tu wanatafuta fedha wanarudi wapewe uraia pacha na waweze kuleta fedha Tanzania, tunaunga mkono, TARURA amezungumzia Wizara ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Lucy Mlowe uchaguzi mdogo amesema Wenyeviti hawakubaliki, uchaguzi haukuwa huru na haki, lakini hawakutuambia huo utafiti amefanya kwa njia gani, utafiti wake amefanyaje huo, hakutuambia ametumia mfumo gani wa utafiti, hakutuambia amehoji wananchi wangapi ambao wamesema hawawataki Wenyeviti hao. Kwa hiyo utafiti huo kwa kweli hauna mashiko.
Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia mambo mbalimbali ambayo kama nilivyosema mengi yamejibiwa na Waheshimiwa Mawaziri.
Nimalizie kwa kusema kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli amefanya mambo mengi sana mazuri, makubwa ya kujenga nchi hii kwa weledi na uadilifu mkubwa sana. Moja ambalo halijasemwa sana ni la kudhibiti ongezeko la maeneo ya utawala, huko nyuma ilikuwa ikikaribia uchaguzi au mdogo au uchaguzi wa mitaa, uchaguzi mkuu inatengwa kata, inatengwa wilaya yanatengwa majimbo, Mikoa, Wilaya sasa hivi hiyo imekoma kupunguza gharama za utawala na hizo fedha zinatumika kujenga hospitali, kujenga barabara, kujenga madarasa na kadhalika.
Kwa hiyo nahitimisha hoja yangu kwa kuwashukuru Wabunge wote waliochangia na nakushukuru mwenyekiti kwa nafasi hii ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja hii. Kwanza napenda kuwapongeza sana Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Manaibu wake Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Festo kwa kazi nzuri ambayo wamekwisha kuifanya hadi sasa ambayo inaonekana.
Mheshimiwa Spika, nipende pia kuipongeza Serikali ya CCM kwa kazi kubwa inayofanyika kwenye maeneo yetu. Kazi zinaonekana, shule zinaonekana hata kama zina matatizo madogo madogo, vituo vya afya kwa maana ya hospitali, zahanati, hospitali za wilaya na vituo vya afya, barabara zinatunzwa, zinarekebishwa, tunasonga mbele.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo niseme kwamba tunahitaji kuongeza jitihada na kuboresha miundombinu tuliyonayo. Sasa niongelee jimbo langu, pale kwenye jimbo langu, kuna Kata moja inaitwa Lukoma, haina shule ya sekondari kwa hiyo, wanafunzi kutoka pale Lukoma wanatembea kilomita 19 kwenda shule jirani kutafuta elimu. Nasema jirani kwa sababu ndiyo inayofuata lakini siyo jirani kilomita 19 kwenda tu, kurudi 19, jumla 38 kwa siku moja mtoto mdogo wa form one, wa form three au kidato chochote, anatembea kilomita 19 kwenda, hivyo hivyo kurudi, kwa hiyo kwa siku anatembea kilomita 38 karibu 40, ambayo ni adha kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba hii kata na yenyewe ipatiwe shule, shule tulishajenga tayari pale, tumefika katikati hapo kwenye ukuta, lakini hatuna uwezo wa kumalizia, wananchi wamechanga wameishiwa nguvu, tunaomba Serikali itoe msaada unaotakiwa pale iki shule hii ikamilike na hawa wananchi wapate shule ya kata, kama ilivyo sera ya CCM kila kata iwe na shule ya sekondari.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo zima la Bukoba Vijijini, hatuna shule ya A level, ya form five na form six, sasa hii nayo ingawa ngazi hii ni ya kitaifa, lakini ni vizuri tukawa na shule ya namna hiyo kusudi tuweze kupata huduma inayotokana na shule hiyo. Tuna shule za sekondari za form one hadi form four nyingi zaidi ya 30, lakini hatuna shule ngazi ya form five na form six. Kwa hiyo, wanafunzi wanapomaliza darasa la kumi na mbili hawawezi kusoma pale pale mpaka watafutiwe sehemu nyingine, nje ya mkoa au nje ya jimbo ambayo nayo inakuwa ni adha kubwa kwenda mbali.
Mheshimiwa Spika, nikiwa bado kwenye eneo la shule la elimu, tumejenga shule nyingi kwenye nchi hii, za kata za sekondari na zingine zilikuwepo, nyingi zimekuwa na matatizo kidogo kidogo ambayo yanasababisha huduma isiwe nzuri. Niongele sasa kwenye vyoo, shule nyingi hazina vyoo vizuri au havina vyoo kabisa, wanafunzi wanakwenda maporini hata Walimu na watumishi wengine wanakwenda kwenye maeneo ambayo siyo salama. Pale nina Shule moja inaitwa Kaishozi Sekondari, shule hii ni kubwa ni ya siku nyingi siyo ya kata, iko siku nyingi, lakini haina choo, choo kimeharibika siku nyingi na wanafunzi wanapata tabu sana inapofika kuwa na haja ya kwenda chooni.
Mheshimiwa Spika, nimalizie na suala la TARURA; Wabunge wengi wamezungumzia suala la TARURA, TARURA imekuwa ni mkombozi mkubwa wa barabara za vijijini na mijini zile ambazo siyo za TANROAD, lakini TARURA haina fedha kama walivyosema Wabunge wenzangu, ina fedha kidogo, nafikiri mpaka leo wanapewa asilimia 30 ya Road Fund (Mfuko wa Barabara), TANROADS wanapewa asilimia 70 na TARURA asilimia 30. Sasa fedha hizi ni ndogo sana, TARURA wana kilomita zaidi ya laki moja na kumi ambazo wanazihudumia ambazo kila mwaka zinaongezeka na ni barabara mpya, ndogondogo lakini za muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, hizi barabara ni muhimu kwa sababu ndizo zinawapeleka watu mbalimbali mashambani, zinapeleka pembejeo zinazoenda mashambani huko, zinawasaidia wanafunzi kwenda mashuleni, zinawasaidia wananchi kwenda katika vituo vya afya kupata huduma za afya, bila barabara inakuwa ngumu sana. Kwa hiyo, TARURA fedha hazitoshi.
Mheshimiwa Spika, hasahasa niongee Jimbo langu la Bukoba vijijini pale kama ilivyo majimbo mengine ya Kagera tuna mvua nyingi kwa hiyo ikija mvua moja au mbili barabara nyingi zinashindwa kupitika zinakuwa hazipitiki hazifai kabisa. Kwa hiyo, tunaomba kwamba tunapopangiwa hela ya TARURA iwe ndogo iliyopo tunatafuta namna ya kuiongeza hiyo ndogo iliyopo Kagera iangaliwe kwa jicho la pekee kwamba ipewe fedha za kutosha kusudi barabara ziweze kupanuliwa kutengenezwa na madaraja yaweze kufunguliwa nakupitika muda mwingi wa mwaka.
SPIKA: Ahsante sana!
MHE. JASSON S. RWEKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi kuchangia nami kwenye Wizara hii muhimu na awali ya yote nipende kumshukuru sana Waziri na kumpongeza kwa kazi nzuri na niishukuru Serikali ya CCM ambayo ni sikivu na imekuwa ikifanya kazi kubwa kuwapatia wananchi wake maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Bukoba linaathiriwa na mvua, tuna mvua nyingi sana miezi karibu kumi kwa mwaka. Kwa hiyo, barabara zinakuwa mbovu mara nyingi kutokana na mvua kuwa ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo niendeleze shukrani zangu kwamba Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa kwenye Jimbo langu. Hapa nina barabara kadhaa nitazitaja moja baada ya nyingine taratibu ambazo zinajengwa na zimejengwa huko nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapo mwanzoni barabara ya Kanyinya – Kanazi hadi Ketema ina lami. Niishukuru Serikali ya CCM kwa kazi hiyo kubwa. Barabara kuanzia Katoma – Gera kilometa 8 inajengwa lami na imekaribia kukamilika. Imejengwa, tumefuatilia tumepata lami. Sasa hivi ninavyozungumza pale Kyabalamba kati ya Kata ya Izimbya kulijifunga kutokana na mvua kubwa ambayo nimeisema. Mvua kubwa sana zikawa zimeziba ile njia, magari yakawa hayapiti. Wamejenga TANROADS, wamejenga caravat na barabara sasahivi inapitika, ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kuanzia pale mjini Bukoba kwenda Jimboni kwangu hadi mpaka na Uganda pale Kabango Bay, barabara ya Bugabo inavuka Kata za Nyakato, Bwendagabo, Kagya, Kishanje hadi Lubafu pale mpakani na Uganda inawekwa lami hivi ninavyozungumza. Ina kilometa 42 lakini kilometa 22 zimeshawekwa lami naishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza barabara moja pale Katokoro ilijifunga kutokana na mvua nyingi ambazo zimezisema. Ilijifunga ikawa haipitiki karibu mwaka mzima. Hapa ninapozungumza, juzi mwezi wa nne nimepata shilingi milioni 570 na hapo wapo kazini. Wakandarasi wanajenga njia hiyo ili ndani ya mwezi mmoja barabara hiyo iweze kupitika na kuwa inasaidia zile za jirani pale ambazo zinaizunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna barabara kubwa inaanzia Chetema inakwenda Kanazi, Ibwera, Katoro hadi Kyakambili, kilometa 60.2. Kama nilivyosema, iko kwenye Ilani na sasa hivi tuna shilingi bilioni moja ya kufanya upembuzi yanikifu. Kazi inaendelea na ninaomba barabara hii kasi isipotee, iendelee mpaka mwisho. Upembuzi yakinifu ukamilike na ujenzi uanze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ina kilometa 60.2 inahudumia kata 18 kati ya Jimbo zima ambalo lina kata 29. Kwa hiyo, asilimia 62 ya Jimbo linahudumiwa na barabara hii. Naomba kasi isirudi nyuma, tuendelee na barabara hii hii, ijengwe na ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Busimbe – Kyamnene – Maruku hadi Kanyangereko, nayo pia iko kwenye Ilani. Serikali imeiweka kwenye Ilani na ninaomba baadaye ujenzi na yenyewe uanze. Tuna barabara ambayo ilijifunga pia kutokana na mvua nyingi za Bukoba ambazo nimezisema, miezi kumi kwa mwaka. Pale sehemu za Kyaytoke ambayo inaenda eneo la Kibirizi. Ilijifunga ikawa haipitiki, leo imetengenzwa, daraja lipo, barabara inapitika vizuri na inakwenda vizuri.
Kwa hiyo, naomba shukrani hizi ziifikie CCM lakini kazi iendelee na tusirudi nyuma, tuongeze mkazo barabara hizi ziweze kupitika muda wote pamoja na mvua kuwa ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hotuba hii ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, lakini Mheshimiwa Spika nakubaliana na wewe kwamba NARCO imeshindwa moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeambiwa hapa na Mheshimiwa Mwijage kwamba Uganda maziwa peke yake yanachangia shilingi dola milioni mia moja, mapato ya mauzo ya maziwa nje ya nchi, sisi Tanzania maziwa kwanza hatuuzi, lakini Wanyama wote livestock nzima siyo maziwa item moja inazalisha mapato ya ndani asilimia kumi, siyo ile national product, gross GBP mapato ya ndani asilimia kumi peke yake, ng’ombe ambao ni maziwa ndani yake, nyama, ngozi, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku yaani kwa ujumla wote, livestock yote, asilimia kumi kwenye mapato ya ndani gross domestic product. Kwa hiyo kwa kweli hii ni kielelezo kwamba NARCO imeshindwa kabisa kazi, imekuwepo muda mrefu inafanya kazi ya kuendeleza mifugo ambayo haiiendelezi, nimesema, wabunge wamesema na wewe umesema ranch zote zimekuwa machaka, mapori imejaa miti hakuna Wanyama. Tunapoomba sisi kupewa hizo block tuanze kufuga hatupewi ili tuziendeleze ndiyo ile private sector kuingia kule kwenye ile sector wanabaki wana mapori ambayo hawayatumii.
Mheshimiwa Spika, hicho ni kielelezo kimoja cha kwamba wameshindwa, kingine kipo jimboni kwangu Bukoba nina kata mbili ambazo nashindwa kuelewa kwa nini NARCO inashindwa kuweka mipaka kati ya wananchi na hizo ranch au block hizo, wananchi wanapata shida kubwa sana. Kuna Kata ya Luhunga na Kata ya Kibirizi yaani watu wanaishi kwenye ranch humo, wanavurugana, juzi, juzi hapa katika Kata ya Luhunga NARCO ilitenga kipande hivi block hivi ikampa mtu mmoja, mfanyabiashara mmoja tena kiongozi mkubwa, akawaambia hiyo ni block yako, hiyo sehemu inawatu ndani yake, ina makazi ya watu, ina shule, ina makanisa, ina misikiti, ina maeneo wanaishi humo ndani, wakampa mtu aweke pale ng’ombe wake, akaweka ng’ombe wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi kwa hasira wakawaua hawa ng’ombe wote wale wakawaua zaidi ya mia, kwasababu wameingia kwenye makazi yao, wamekula mazao yao, mihogo, ndizi n.k. Sasa unashindwa kufahamu NARCO inafanya kazi gani inayofanya hii. Hii inaitwa ranch ya Mabale ipo pale karibu na Kata ya Luhunga vitongoji na vijiji vya Kayojwe, Tainoni, Kabanga, Milembe vipo mle ndani kwenye ranch, NARCO haiwezi kuweka mipaka ya wazi kwamba hili ni eneo la watu, hili ni eneo la mifugo hiyo ya ranch ambayo wameitenganisha. Hakuna mipaka inayoonekana wazi kwamba hapa ni watu hapa ni mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Kata ya Kibirizi mwaka jana Disemba, mwezi wa kumi na mbili akaenda Meneja wa ranch pale, ranch ya Kagoma akaweka mpaka mpya kwenye maeneo ya watu, akateka kaya 170 ndani ya ranch, akaingiza kwenye ranch, akaziingiza, ambazo zilikuwa nje ya ranch akaziingiza katika mpaka mpya kwa kufanya hivyo akawa amechukua maeneo ya wakazi 1,138 hawana pakukaa, wamekumbwa na ranch ambayo haikuwepo leo wanasemekana kwamba wapo ndani ya ranch.
Mheshimiwa Spika, uamuzi ambao ameuchukua mwenyewe hakushirikisha viongozi, hakuhusisha wananchi amekwenda kuweka mipaka mipya na akachukua maeneo ya wakazi ambayo yalikuwa tayari yana makazi ya watu. Sasa hiyo ni matatizo ambayo yanaonyesha kwamba NARCO kwa kweli kazi haiiwezi imekuwa ngumu kwao tuangalie njia nyingine ya kufanya NARCO waachie hii kazi kama inawashinda. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa, niko hapa Sanga.
SPIKA: Taarifa.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa pia mzungumzaji kwamba NARCO kwamba imeshindwa kuna mambo mawili ambayo pia yamejitokeza, kwenye hotuba ya Waziri ya mwaka 2016 na hata zilizofuata wanakiri wazi kwamba Serikali imeshindwa kuzalisha Mitamba kwa maana kwa mwaka 2015/2016 ilizalisha Mitamba 634, lakini Private Sector ilizalisha Mitamba 10,820 na kusambaza kwa wananchi kwa hiyo hicho ni kigezo mojawapo cha kwamba NARCO imeshindwa.
Mheshimiwa Spika, kitu kingine cha pili Ranch ya Ruvu ambayo inasimamiwa na NARCO kuna mradi wa 5.7 billion ambayo hadi sasa umekwama, lakini mashine zimenunuliwa zipo pale zinaoza kwenye makontena kwa hiyo ni kweli NARCO imeshindwa.
SPIKA: Nakuunga mkono katika taarifa hiyo, wakati Olelekaita anasema katika Wilaya ya Kiteto wana ng’ombe laki kadhaa, umesema laki ngapi, laki tano, NARCO nchi nzima ina ng’ombe haizidi 16,000 can you compare the two, ni wastage, yaani NARCO mmeshindwa endelea. (Makofi)
Mheshimiwa Rweikiza.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo naikubali na naiunga mkono ni taarifa nzuri.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kufahamu kwa nini Wizara inavumilia uozo huu wa NARCO kushindwa hasa kuchukua maeneo ya watu na kuwahamisha isivyo halali, watu wanauliwa, wanaua wanyama hawa, wanyama hawana hatia, hatia ni ya NARCO. Kwa nini Wizara inanyamaza na inafumbia macho jambo hili? Hatuwezi kuthamini wanyama kuliko watu, haiwezekani. Hili ni kosa kubwa linafanyika ni lazima litafutiwe ufumbuzi na tuweze kupata maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo navyozungumza hapa, hawa NARCO wako Karagwe katika Jimbo la Mheshimiwa Bashungwa wanapima kule, wanachukua maeneo ya watu wanawaingiza kwenye ranchi. Wako kwenye Kata inaitwa Lugela, wamechukua maeneo ya watu wameingiza kwenye ranchi, watu wako kule ndani, kuna shule na kadhalika. Sasa hawa watu wana nia gani? Wanaingiza watu kwenye ranchi maeneo ambayo hayakuwa ranchi hapo awali.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba miaka miwili iliyopita au mitatu Mheshimiwa Rais aliunda Tume au Kamati ya Mawaziri nane kwenda ku-monitor jambo hili nchi nzima. Wakazunguka maeneo ya ranchi na maeneo ya watu, wakaainisha kwamba watu wabaki huku na ranchi zibaki huku na nafikiri walitoa taarifa yao nzuri lakini NARCO au tuseme Wizara haitekelezi jambo hili ili shida hii iishe. Kwa hiyo, kwa kweli hili ni jambo kubwa linaathiri sana watu.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana kwenye kampeni pale kwangu ilikuwa patashika, wananchi wanasema hatukupi kura kwa sababu tunatishiwa na ranchi hizi, tutakupaje kura wewe na CCM kama hamuwezi kumaliza jambo hili? Kwa hiyo, jambo hili ni kubwa sana na ni la kisiasa, kisera, kiuchumi ni vizuri wananchi wakapata mipaka yao inayoeleweka. Kwa hiyo, niombe Wizara inapokuja kumalizia jambo hili itupe maelezo wanafikiria nini kulimaliza.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, wamesema Waheshimiwa Wabunge hapa ni la uvuvi, hata mimi linanihusu nina maeneo mengi ya uvuvi. Watu wanavua samaki wa ukubwa mbalimbali na wanatumia nyavu ambazo wanazinunua kihalali madukani. Nyavu zinalipiwa kodi na zinauzwa kihalalali, lakini wanakwenda kuchoma nyavu hizi kwenye mitumbwi kule ziwani, wanazikamata na kuzichoma moto. Samaki wanakamatwa, akina mama na wavuvi wengine wananyang’anywa, wamenunua kwa wavuvi ambao wamenunua nyavu zile kihalali.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini mnaruhusu nyavu hizi zitoke madukani au viwandani, watu wauziwe, halafu unasema hii sio halali. Mnakuwa wapi zinapotengenezwa, zinapoagizwa, zinapouzwa, usubiri mpaka zifike ziwani ndio uwazuie watu kutumia. Huu ni uonevu mkubwa ambao hauwezi kuvumiliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja lakini nataka majibu, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuja kuhitimisha hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata jumla ya wachangiaji 13 kwenye hoja yetu na niwashukuru sana wote waliochangia kwa umakini mkubwa na ufasaha mkubwa kiasi kwamba hoja imeeleweka vizuri kwa wote na imeonesha ufanisi mkubwa. Kipekee niwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri Mheshimiwa Damas Ndumbaro na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa majibu ya mwisho hapa ambayo yamezidi kuweka sawa sawa hoja nzima na kujibu zile hoja ambazo Wabunge wamezionesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapochambua sheria hizi ndogo tunachoweza kusema hapa ni kwamba tunaweka mazingira safi ya utawala bora, kama alivyosema mmoja ya wachangiaji Sheria Ndogo hizi zinawahusu sana wananchi wote siku kwa siku, ni sheria kama sheria nyingine zina nguvu sawa na sheria nyingine na niseme labda wakati mwingine kuzidi sheria nyingine, kwa sababu ziko huko chini kwenye grass root watu walipo na zinatumika kila siku iwe kwenye usafi wa mazingira kwenye kutunza miti na mazingira kwa ujumla uvuvi boda boda yaani ndiyo zinazohusika hasa katika maisha ya kila siku ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi zina nguvu sana kwa sababu zinatoa faini zinatoa vifungo kwenda jela kwa fidia ndogo unaweza kwenda jela, zinaweka mazuio na mipaka mbalimbali, zinahalalisha mambo mbalimbali na kuharamisha mambo mbalimbali kwa hiyo zina nguvu nyingi kama sheria nyengine za nchi, hakuna tofauti kwamba ile neno kwamba Sheria Ndogo basi ni Sheria Ndogo siyo ndogo ni sheria zenye nguvu kama sheria nyengine.
Kwa hiyo, zikitungwa hovyo hovyo zinaathiri sana maisha ya watu ya kila siku na tunayopitia kila siku hivyo inabidi zitungwe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba inatoa maelekezo mbalimabli na mamlaka mbalimbali sheria zitungwe vipi, kwa hiyo siyo sahihi kwa Sheria Ndogo kuja na mazingira ambayo yanakinzana na Katiba. Kwa mfano, amesema mchangiaji mmoja hapa Mheshimiwa mmoja amesema Katiba inatoa haki na wajibu wa kufanya kazi kwa mtu yoyote awe kampuni awe mtu binafsi, lakini wanasema kwamba ukitaka kufanya biashara ya samaki sharti uwe kampuni sasa hii inakiuka Katiba, siyo sahihi kuwepo na lazima ishughulikiwe na ifanyiwe masahihisho. Mfano mwingine anasema Mhifadhi wa Misitu anaweza kusitisha kibali cha kushughulika na mazao ya misitu na hana kikomo hana ukomo inaweza kuwa miaka 10 miaka 20 yaani daima dumu anakufutia tu kibali, sasa hii siyo sawa inakinzana na masharti ya Katiba na Sheria nyingine zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wameongea Wabunge wengi kuhusu Sheria ya Ombaomba katika Wilaya ya Chunya, wameeleza vizuri ni sheria ambayo kwa kweli ni ya kibaguzi, unambagua mtu kwa ulemavu siyo jambo zuri, unamwambia apelekwe Mkoa wa kwao akabidhiwe kwa RAS na RAS ampeleke kwa RAS wa kwao, sasa RAS huyu ampeleke wapi na kwao ni wapi ameuliza Mheshimiwa mmoja. Je, ina maana Chunya pale hakuna raia ambao ni ombaomba ambao wanafanya kazi za ombaomba pale pale, kwa hiyo Sheria hii ni ya kibaguzi na haifai kuendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Tanganyika wamesema lina kina kirefu zaidi ya mita 1,000 lakini samaki anaweza kuishi kwenye mita 150, unaporuhusu tu mita 20 ndiyo wavue hizi nyingine mita 130 avue nani? Samaki kama walivyosema hazina mipaka znaweza kwenda Congo zinawaza kwenda nchi nyingine jirani na watu wakafaidi kule na sisi tunajinyima uchumi ambao ni mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema Waheshimiwa Wabunge kwamba inasikitisha kwamba sheria hizi zinatumika huko kabla kuja Bungeni, kwa kweli hili ni jambo la msingi sana, bahati mbaya ni nyingi sana, ni nyingi kweli kwa maelfu kwa maelfu sasa ukisema zije kabla zitakuwa hazitumiki zitachukua muda mrefu sana kutumia kwa huko kwa wananchi, lakini kwa kweli ni jambo zuri la kufikirika ni la kufikirisha kwa sababu zikitungwa sheria mbovu anaelaumiwa ni Bunge nani anaelaumiwa, mtunga sheria ni mmoja ni Bunge wale wengine wote wamekasimiwa delegated awe Mkurugenzi awe ni shirika gani amekasimiwa na Bunge, Bunge ndiyo mwenye lawama kama sheria hiyo itaonekana kwamba ina kasoro au mapungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomruhusu mtu ambae ni interested part ana maslahi binafsi kwenye sheria fulani, halafu hashiriki humo tunafahamu kwa mfano katika Halmashauri Madiwani hawaruhusiwi kushiriki zabuni za ujenzi wa barabara mle za ndani kwa sababu wana maslahi binafsi, sasa unaporuhusu hawa wasimamizi wa mazingira washiriki kwenye ile kazi ya kusimamia mazingira ina maana umeruhusu conflict of interest mgongano wa maslahi, haiwezekani lazima sheria kama hiyo ifanyiwe kazi ya kurekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa hapa na tumeiona kwenye uchambuzi wetu, uvuvi katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika, mwenye chombo ana leseni mvuvi ana leseni, chombo chenyewe kina leseni na huyu mvuvi akihama kazi kwa mwenye chombo akaenda chombo kingine leseni ile inaisha nguvu haina kazi tena, akienda kwa chombo kingine alipie leseni nyingine na anaelipa ni mwenye chombo, sasa ni mateso ambayo tunawapa wenye vyombo na kuwaongezea gharama ambazo hazina maslahi wala hazina faida kwa nchi yetu, tunawatesa, tunawakosesha mapato tunawakosesha kazi na siyo jambo ambalo lina busara yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makosa ya uchapaji unapochapa sheria ovyo ovyo unainyima uhalali wa sheria, mkienda Mahakamani Wanasheria utaangushwa chini mara moja, kwa sababu watakwambia hii umeitungia chini ya sheria gani? uliyoweka umekosea! Kwa hiyo lazima uwe makini unapoandika sheria iwe ndogo iwe kubwa isikinzane na Sheria Mama au sheria nyingine kubwa au ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mheshimiwa mmoja hapa sheria Kubwa inaweza ikawa inasema faini ni Shilingi Laki Moja, Sheria Ndogo inasema faini Shilingi Laki Moja na Hamsini, hii ni kinyume kabisa na utaratibu wa utungaji wa sheria na haifai kuwepo, ni lazima hiyo ifutwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema na walivyosema Wabunge wengine sheria hizi zinahusu maisha ya wananchi wetu, wananchi wenzetu ya siku hadi siku, lengo lake ni kukuza utawala wa sheria, utulivu, amani na ustawi na maeneleo na si kinyume chake, siyo vinginevyo, amesema Mbunge mmoja kutoka Kilimanjaro pale nyumba ya mungu unasema samaki wasivuliwe chini ya nchi tatu, amesema kwa miaka 20 hao samaki hawajawahi kuwepo, sasa unashangaa unajiuliza hawa waliotunga sheria hii hawajui mambo haya walitunga kwa sababu gani? Unasema nchi tatu ndiyo kiwango cha chini lakini sasa hawajawahi kufika kwa miaka 20, kwa hiyo unakusudia nini unapotunga sheria ya namna hiyo na ili iwe nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, unazuia mtu kukata mti ambao aliupanda mwenyewe, sasa unashangaa kapanda mti mwenyewe ili aufaidi apate matunda yake unamzuia kuukata umekusudia nini? Kwa hiyo badala ya kusaidia watu kuwahimiza, hawatungi sheria ya kusema pandeni miti au boresha mazingira wanasema usikate mti ambao umepanda mwenyewe, kwa hiyo inazidi kuleta shida katika usimamizi wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yetu Kamati ya Sheria Ndogo kwamba sheria mbovu iwe Sheria Ndogo hasa hizi sheria ambazo sisi tunashughulika nazo zisiwe Sheria katika sheria za nchi hii zifutwe na zirekebishwe pale ambapo inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninalishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kuchangia na kwa Wabunge kuchangia kwa umakini mkubwa na kwa weledi mkubwa sana na kwa ufanisi wa hali ya juu sana, michango yao imekuwa ya manufaa makubwa na imesaidia kuweka jambo hili vizuri na hoja imezidi kueleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja yangu na nipende kusema kwamba nawashukuru sana Wabunge kwa michango mbalimbali mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata wachangiaji wa kuzungumza kumi na kwasababu siyo wengi naomba niwataje; Mheshimiwa Edwin Swalle, Mheshimiwa Simai Sadiki, Mheshimiwa Amour Mbarouk, Mheshimiwa Kunti Majala, Mheshimiwa Dkt. Leonard Chamuriho, Mheshimiwa Judith Kapinga, Mheshimiwa Francis Mtinga, Mheshimiwa Luhaga Mpina na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mheshimishimiwa Feleshi na Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru sana kwa michango yao mizuri waliyoitoa ambayo kwa kweli imekuwa kwanza wanaunga mkono hoja yetu, lakini wanaboresha pale ambapo panastahili na panawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kazi za kutunga sheria ni ya Bunge, sheria zote, sheria mama, sheria ndogo zote ni ya Bunge, lakini Bunge limekasimu kazi hii kwa mamlaka mbalimbali kwa sababu ni nyingi sana, inahusu sheria zenyewe, sheria ndogo, sheria kubwa zenyewe, sheria mama. Amesema Mheshimiwa Mpina zile zote zimo waraka, matangazo, amri, kanuni ile nyingine proclamation zimo kwenye sheria ndogo, zote zimo zinahusu humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Bunge haliwezi kutunga sheria zote hizi peke yake likamaliza, lazima likasimu kwenye mamlaka mbalimbali Halmashauri, Wizara mbalimbali, idara mbalimbali ili kazi hii iweze kutendeka vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lengo la sheria ndogo hizi zote nilizozitaja zikiwemo na waraka na nyingine hizo ni kusaidia kutekeleza sheria mama, kuzifafanua vizuri zaidi ili zieleweke vizuri, kurahisisha utekelezaji wa sheria mama, si kuzikwamisha au kuweka masharti ambayo yanaleta ukinzani kwenye sheria mama au yanakwamisha ufanisi na maslahi ya Watanzania na urahisi wa Maisha, ni kurahisisha sheria zenyewe ziweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawaomba watungaji wale wa sheria ndogo wawe makini, kule kwenye mamlaka kwenye halmashauri kwenye wizara kuna wanasheria kule wanaweza kufanya kazi hii kwa umakini na waondoe hizi kero ambazo tumezibainisha hapa na Wabunge wamechangia kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kama niliousema hapa sheria mama inasema kwenye kosa fulani adhabu ni shilingi isiyozidi shilingi 300,000 au kifungo kisichozidi miezi 15; sheria ndogo inakuja inasema kwenye kosa hilo hilo adhabu isiyopungua shilingi milioni tatu au kifungo kisichopungua miaka mitano. Sasa unashangaa hii sheria ndogo ya namna gani inakinzana na sheria mama na inaongeza adhabu kuliko ilivyosema sheria mama, hii siyo sawa sawa huu ni ukiukwaji ambao upo dhahiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Kamati inachofanya sisi tunachambua hizi na kubainisha mapungufu haya na makosa haya ambayo yamo na kuyarekebisha na kwamba tunawaambia wale warekebishe. Tatizo ni kwamba kama nilivyosema hapo mwanzoni tunawapelekea maelekezo hawaleti, ndiyo maana tumesema hapa angalau ikifika Novemba na Desemba tarehe 1 wawe wameleta. Sasa inavyoonesha kwamba itabidi tuanze kwenda kule kwenye hizo Wizara kuchunguza kwa nini hamjaleta, hili tuliwaelekeza hamjaleta mpaka leo watupe majibu; kama yanaridhisha kama hayaridhishi sisi tutawaambia maana yake inachafua taswira ya Bunge. Mwananchi akiumia kule analaumu Bunge halaumu ile mamlaka kule anasema Bunge hili namna gani imetunga sheria mbovu ambayo haitekelezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumemsikia Mheshimiwa Kapinga hapa anaongelea Bolt na Uber zimefunga kabisa biashara zao ambayo ilikuwa ni huduma nzuri, inagharama nafuu kwa mwananchi, unapiga simu dakika mbili umeshapata huduma, sasa hiyo imesimama; hii siyo kuboresha maslahi ya Watanzania au ufanisi wa maisha kuwa mazuri ni kukwamisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo hazina lengo hilo, wale wanaotunga hizo sheria wajitahidi kuzingatia sheria mama, kuwa na utu, kupenda maendeleo na si kukwamisha maendeleo. Wajitahidi kufanya hiyo kazi kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa maelekezo waliyoyatoa hapa kwanza wamekubali kwamba kuna dosari ndogo ndogo, nawashukuru sana kwa kazi waliyoisema kwamba wataenda kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme pia mwishoni kwa kumalizia kwamba dosari hizi si nyingi sana, zimepungua sana kadri tunavyokwenda mbele, mwanzoni zilikuwa nyingi sana sasa zimepungua na nitumie nafasi hii kuwapongeza wale ambao wanatunga sheria nzuri kwenye mamlaka mbalimbali huko kwenye halmashauri na sehemu nyingine wanajitahidi sana kufanyakazi nzuri ambayo ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi nami nichangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niseme kabisa kwamba, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imetuwekea misingi mizuri ya kupanua uchumi wetu na kuukuza kama nchi.
Mheshimiwa Naibu Sika, tunapozungumzia bajeti, tuko humu kwenye Bunge la Bajeti, tunazungumzia uchumi na uchumi imara ndiyo Taifa imara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuweka nguvu nyingi katika kukuza uchumi wetu. Nataka kuzungumzia suala la kilimo na majuzi hapa tumeona Mheshimiwa Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete kazi aliyoifanya ni kubwa sana ya kuboresha kilimo chetu. Nampongeza na kumshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka nizungumzie suala mahsusi kuhusu kilimo. Kilimo tunasema ndio uti wa mgongo na kwa kweli ndio ukweli wenyewe, bado uchumi wetu mkubwa unategemea kilimo. Tuna maeneo nchi hii ambayo ni mazuri yana rutuba sana, wote mnayafahamu maeneo mbalimbali ukienda Morogoro Mkoa mzima una rutuba kubwa sana, ukienda maeneo ya Kusini kule Tunduru, ukienda Katavi, ukienda Rukwa, ukienda Kigoma, maeneo mbalimbali yote Kahama, kule wapi, kuna rutuba nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nchi hii tumejaliwa tuna mito mingi. Licha ya mvua tuliyonayo ya kutosha kumwagilia mashamba yetu vilevile kama kuna shida ya mashaka ya mvua tuna mito kwa hiyo, tuna uwezo wa kulima kwa kutegemea umwagiliaji ambao sio wa gharama kubwa kwa sababu ya mito. Tuna mito kama Mto Mara, umeongelewa juzi hapa, tuna Mto Kagera, tuna Mto Pangani, tuna Mto Malagarasi, tuna Mto Ruvu, tuna Mto Ruvuma, kila mahali kuna mito mingi sana hiyo ni mikubwa. Iko mito midogo ambayo inaingia kwenye mito hiyo inapita maeneo ambayo nimeyataja yale ya ardhi ambayo ina rutuba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninapozungumzia kilimo leo nataka nizungumzie maeneo haya. Kabla sijaenda kwenye maeneo hayo niseme kwamba, tuna vijana wengi nchi hii ambao hawana kazi, lazima niseme wazi. Hawana ajira, hawana kazi wanayoifanya, hawana biashara wapo tu, wengi sana. Ukienda Dar-es-Salaam ndio kabisa, ukienda pale Mwenge, ukienda Manzese, Tandika, Buguruni, Miji yote ukienda Mwanza, ukienda Arusha, wako vijana wanauza pipi, wanauza vitambaa vya jasho, siku hizi charger ndio zimekuwa deal ya kuuza charger kama vile zina uadimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa vijana wana nguvu, miaka 25 miaka 20 hawana ajira, lakini mimi nasema tuna ardhi nzuri sana maeneo mengi ya nchi hii. Nchi hii ina hekta karibu Milioni Moja haijalimwa zaidi ya nusu haijaguswa, sasa nikasema vijana tulionao nguvu kazi hii kubwa ambayo haitumiki, siyo tu kwamba tunapata hasara kutokutumia vijana hawa, vilevile ni hatari kubwa ambayo tumeiangalia, tunakaanayo hatuitumii ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nipendekeze hapa jambo mahsusi. Nataka nipendekeze na Serikali naomba jambo hili ilichukue tuanze kilimo cha makambi. Peleka vijana kwa mfano 200 kwa mfano kwenye kambi moja, tafuta eneo pale na mchango wangu huu unahusu Wizara nyingi sio huyu wa kilimo peke yake, Wizara nyingi zaidi ya kumi, iundwe task force ya Wizara zaidi ya kumi jambo hili lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, peleka vijana kwa mfano 200 nimesema kwenye kambi moja, wape mkopo, Serikali itafute fedha iwape mikopo ili wanapokwenda pale vijana 200, maana yake ni mbugani, porini, hakuna nyumba, wajenge nyumba za full suit za kuanzia, juu bati chini bati. Wapate tractor, ukitumia jembe la mkono unajidanganya haina tija na ni mateso, wapate ma-tractor angalao mawili, power tiller angalao mbili, wapate mbolea, wapate mbegu, wapate pembejeo mbalimbali. Chakula cha kuanzia angalao miezi sita, wanunue chakula na mahitaji mengine waanze pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya hesabu hapa za kirejareja, ukipeleka vijana 200 kwenye kambi ukawapa eka 2,000, ukawapa Milioni 200 kama mkopo wakaanza kulima kwa tractor ndani ya muda mfupi utapata mazao mengi sana na pesa nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema nimefanya mahesabu ya kukadiria hao watakaoundwa, kama itakuwa imeundwa hiyo KAMATI itafanya hesabu za uhakika, lakini ukiwapa vijana eka 2,000 vijana 200 wakaanza kulima kwa utaratibu watakaokubaliana wa kambi, wakaanza na mazao ya muda, maharage, mahindi, alizeti, ufuta, mpunga na mazao mengine ndani ya miezi mitatu, miezi minne, wataweza kuvuna mazao mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, wakilima mahindi wakapata eka moja magunia 20 kwa kiwango cha chini, ndani ya miezi mitatu wamevuna mahindi ya kutosha kuuza kupata fedha ya kutosha. Ndani ya mwaka mmoja wakilima misimu miwili, misimu mitatu, kama wanamwagilia maji watalipa lile deni, wataanza kujiendeleza. Pale palipokuwa kambi ya muda ya mabati ya full suit watajenga nyumba za kudumu, watajenga shule, zahanati, wataweka mitaa na maendeleo mengine, tutaongeza ajira, vijana hawa ambao wako Mijini wanazurura tutakuwa tumewaondoa tumeleta maendeleo makubwa, tutauza chakula hiki nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutauza Uarabuni ambao hawalimi lakini wanakula vizuri. Tutauza Congo, tutauza hapa Kaskazini kote kuna shida ya kilimo tutapata fedha nyingi na vijana hawa tutakuwa tumewaondoa kwenye balaa ya kukosa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwangu Jimboni pale kuna vijana wanaendesha pikipiki bodaboda hizi wako nchi nzima. Kule vijijini unakuta kituo kidogo kina bodaboda 40, wanafanya kazi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, anakaa mpaka jioni hata abiria mmoja hampati anaondoka hana kipato. Wakiwa kwenye kambi ya kilimo hii baada ya mwaka mmoja wataweza kupata pesa hata kujilipa mshahara wa Shilingi Milioni Moja kwa mwezi, watajilipa watakuwa wamejiendeleza na watapata ufanisi mkubwa sana na nchi itapata chakula cha kutosha itaweza kuuza chakula hiki nje na kuboresha maisha ya Watanzania na kuboresha uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mchango wangu mimi ni huo kwamba, tufanye kilimo cha makambi ambacho kitaondoa baa la vijana kutokuwa na kazi, baa la kukosa chakula, amesema Mheshimiwa Mbunge hapa tunahangaika na mafuta, tukilima alizeti shida hii itakuwa imekwisha kwa wingi na tutapata mazao mengi sana. Nchi itaneemeka, hiyo mikopo italipwa na vijana itarudishwa Serikalini na tutakuwa tumepiga hatua ya maendeleo nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa fursa kuhitimisha hoja yangu, lakini pia nawashukuru sana waheshimiwa Wabunge kwa michango ambayo wametoa ambayo kusema kweli wameboresha hoja tumepata jumla ya wachangiaji 14; ambapo Wabunge ni tisa na Mawaziri watano ambao wameshehenesha na kuiboresha hoja yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo ni jicho la Bunge la kutazama jinsi gani ambavyo sheria ndogo zinatekelezwa, zinatungwa, zinakwenda na Sheria na Katiba na nchi yetu inafuata mfumo wa utawala bora. Sasa ili kuwe na utawala bora kuna mgawanyo wa majukumu kuna mihimili mitatu na Mhimili wa Bunge ndio wenye jukumu la kutunga sheria zote za nchi hii ziwe sheria mama, ziwe sheria ndogo na kadhalika, hiyo inaelezwa kwenye Ibara ya 64 ya Katiba yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa chini ya Ibara ya 97(5) Bunge linaweza kukasimu madaraka yake kwa vyombo mbalimbali, kwa mtu mmoja mmoja, kwa idara mbalimbali, kwa vyombo mbalimbali Serikalini ili kutunga sheria ndogo. Sasa kukasimu siyo kuachia, siyo kukabidhi, unabaki na madaraka yote, lakini unampa mtu mwingine afanye kwa niaba yako, akikosea au asipotekeleza unamrudi, unamwambia rudisha hapa unaendelea mwenyewe.
Kwa hiyo, Bunge ndio linafanya kazi hiyo ya kuhakikisha kwamba sheria ndogo zlilizotungwa na mamlaka mbalimbali zinakwenda kulingana na Katiba, sheria mama na miongozo mingine ambayo tumejiwekea na ndio maana nasema Kamati hii ni jicho la Bunge la kutazama utungaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lina wajibu wa kuhakikisha kwamba hakuna sheria ndogo yoyote itakayotungwa ambayo ni kero kwa wananchi, na ikiwepo lazima Bunge liingilie na liseme.
Kwa hiyo, taarifa yetu inachosema ni kwamba kuna baadhi ya Wizara, Halmashauri na mamlaka nyingine ambazo zinatunga sheria mbovu au hazitungi sheria ambazo ni kero kwa wananchi, sasa tukinyamaza tutakuwa tunaachia wajibu wetu ambao tunatakiwa tuufanye, hatuwezi kunyamaza lazima tuseme na tusahihishe pale ambapo kuna matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziko nyingi Waheshimiwa wamesema Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda amesema hapa saa nane za usiku unaenda kumdai mtu ushuru nyumbani kwake kwa nini? Mheshimiwa Damas Ndumbaro, Waziri WA Katiba na Sheria amejibu, lakini nafikiri hakumwelewa Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kudai ushuru ni jambo la kawaida, ni jambo jema, lakini kwa nini umfuate saa nane za usiku? Mdai mchana, kama ni jambazi, ni gaidi huyo ameondoa haki yake ya kuwa na faragha, huyo mshughulikie kwa sheria zote zilizopo. Lakini huyu ni raia mwema, unamdai kodi, mdai kwa utaratibu ambao umewekwa na sheria usikiuke sheria mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko sheria nyingi ambazo ama hazitungwi vizuri au hazitungwi kabisa au hazisimamiwi, kuna mfano ambao kwenye taarifa haumo, siku hizi kwenye mitaa kwenye makazi ya watu unakuta kelele nyingi sana baa zinapiga miziki, spika kubwa hivi, anafungulia mpaka mwisho. Makanisa na misikiti yanapiga kelele kubwa sana kwenye mitaa ya watu, watu hawawezi kulala usiku wala kupumzika mchana NEMC ipo, BASATA ipo, Halmashauri zipo hazichukui hatua yoyote. Huu ni utekelezaji mbaya wa sheria ndogo na hatuwezi kunyamaza, lazima tuseme mtufuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Sylvia Sigula, Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka, Mheshimiwa Kasalali Mageni na wengine wamezungumzia pale mwishoni kwamba ni vizuri labda baadhi ya sheria hizi kabla ya kutumika, maana yake sheria ya sura ya kwanza inaruhusu sheria zitumike kabla ya kuja Bungeni, Halmashauri, za Wizara huko zitumike kabla ya kuja Bungeni angalau basi za Halmashauri zije kwanza Bungeni kabla ya kutumika kule kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hii iwe hoja ya Bunge na mimi naomba hii tuipitishe kama hoja ya Bunge, hoja ya Kamati kwamba sheria hizi ziletwe, zipitie kwanza kwenye Kamati yetu, zipitie Bungeni, halafu ndio zitumike kule kwenye kusimamia wananchi. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba hiyo iongezwe hii sura ya kwanza iletwe Bungeni ifanyiwe marekebisho kusudi sheria hizi zije kwanza Bungeni kabla ya kwenda kusimamia maslahi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuzungumza katika Wizara hii au sekta hii ya TAMISEMI. Awali ya yote, naomba nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara. Nimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Chalamila kwa kazi nzuri ya kusimamia maendeleo kwenye Mkoa wetu na wote wanaomsaidia.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie TARURA kwa kuanza. Kama walivyosema wenzangu hapa TARURA inafanya kazi nzuri, nzuri sana ya kupigiwa mfano chini ya Engineer Victor Seif, wanastahili kupongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa ujumla wake wanatakiwa waongezewe fedha. Kazi yao ni kubwa sana, barabara za udongo nchi nzima, fedha wanayopewa haitoshi. Nikisema hivyo nizungumzie kwenye Jimbo langu na Mkoa wangu wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, Kagera kuna mvua nyingi sana. Kama nilivyosema barabara za TARURA ni za udongo, ni changarawe, kifusi, kwa hiyo ikija mvua inakwangua zote. Wanatengeneza kwa kazi kubwa, wanafanya kazi nzuri lakini baada ya muda ikija mvua inakwangua. Kwa hiyo niombe wanapogawa mgao wa mikoa wajue kwamba Kagera kuna mvua nyingi sana. Tuna mvua miezi saba katika mwaka, mitano tu ndiyo ina ukame au minne. Kwa hiyo barabara zinaharibika sana, ziongezwe fedha katika Mfuko wa Barabara wa TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiwa TARURA bado kwenye Jimbo langu kuna maeneo mawili ambayo ni changamoto. Kivuko cha Chanyabasa na maeneo yanaitwa Kansinda hamna kivuko pale, ni mto mkubwa lakini hamna kivuko. Pale Chanyabasa jana Mheshimiwa Oliver alizungumzia kivuko hicho, ni mto mkubwa na wananchi wanavuka pale kwa tabu sana. Kivuko kipo cha miaka, tangu mwaka 1994, kimekuwa kibovu na kimezeeka sana. Wananchi wanavuka pale kwa tabu.
Mheshimiwa Spika, Kivuko hiki kinaunganisha Kata ya Kasharu, Kishogo, Lyamahoro, Nyakibimbiri, Ibwera, Kaibanja, Katoro, Kyamuraire na nyingine. Bila kivuko hiki hawawezi kwenda kwenye maeneo yao wala kuja kwenye maeneo mengine. Sasa ni ombi langu kwamba hapo pawekwe daraja badala ya kivuko. Pajengwe daraja la uhakika la kudumu ili kuondoa adha kwa wananchi hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia pale Kansinda ambako ni mto huo huo unakwenda hadi unaungana na Mto Kagera ni mto mkubwa na hakuna kivuko wala daraja. Wananchi wanavuka kwa mitumbwi ambao ni hatari sana kwa maisha yao. Naomba pale pajengewe daraja napo ili wananchi waweze kupata usalama wa maisha yao.
Mheshimiwa Spika, nikirudi Chanyabasa pale, leo ninavyozungumza ni mwezi wa nne hakuna kivuko. Vile vile wanavuka kwa mitumbwi ambayo inahatarisha usalama wa maisha yao. Kwa hiyo ni jambo jema sana kwamba pale tuwe na daraja ambalo litasaidia kuimarisha usafiri pale. Pale Kansinda ni njia mbadala ya kutokea Uganda. Ikitokea tatizo kwenye njia ya kuja Bukoba mjini pale ndiyo inachepuka inaenda Muleba hadi Dar es Salaam, ni njia pekee ya kupita pale. Kwa hiyo itumike pale kama nja mbadala au alternative route, likitokea tatizo la kuvuka pale.
Mheshimiwa Spika, nishukuru Serikali kwamba kwenye Sekta ya Elimu pale kwenye Jimbo langu nilikuwa na Kata moja ya Ukoma haikuwa na shule. Imejengwa shule ya sekondari nzuri chini ya mradi wa SEQUIP imekamilika kwa 95%. Bado majengo kama manne hayajakamilika. Niombe kwamba Wizara hii iangalie pale ikamilishe majengo hayo ili yatumike. Ni shule nzuri sana ikamilike ili iweze kukidhi malengo yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie vizuizi barabarani kwenye Jimbo langu (barrier). Kwenye jimbo langu kuna barrier nyingi sana, zinasumbua sana wananchi, ni kero kubwa sana na haziko pale tu kama mapambo, yanatoza kodi, ushuru na tozo. Sasa wananchi wanatozwa kodi nyingi sana, tozo nyingi sana. Mtu ana ndizi moja, ndizi mbili anatozwa kidogo, ana nanasi anatozwa, Mheshimiwa Waziri aangalie sana eneo hili kusudi wananchi wasipate kero hii ya usumbufu wa hizi barrier hivi vizuizi barabarani ambavyo havina tija.
Mheshimiwa Spika, niongelee eneo la shule binafsi ambazo hivi karibuni Serikali imetoa waraka wa kwanza, wa pili na watatu inafuta mabweni, inasema mabasi yaendeshwe na wanawake na mkondakta wawe wanawake. Haya ni matatizo makubwa. Nafahamu sababu ya kufanya hivyo, lakini hiyo siyo suluhisho. Mimi niko kwenye sekta ya shule binafsi lakini vile vile nina watu ambao nawawakilisha ambao wana shule binafsi. Sasa wangeshirikisha watu hawa wa shule binafsi kupata ufumbuzi, siyo kutoa tu nyaraka ambazo hazitekelezeki.
Mheshimiwa Spika, mwisho naona umewasha spika ya kunisimamisha, nimalizie kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara hii ya Maji, Wizara muhimu kwa mustakabali wa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, kwa kazi kubwa na nzuri sana anayoifanya ya kuboresha maisha ya Watanzania, mchapakazi, mpenda watu na kwa kweli tunajivunia kuwa nae. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji na wasaidizi wake kwa kazi nzuri, kwa wepesi wake na usikivu na kazi inasogea mbele. Kazi kubwa sana inafanywa na huduma za maji safi na salama na ya kutosha inasogezwa kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu miradi mingi ipo mikubwa na midogo na inakwenda vizuri. Mradi mmoja wapo kati ya miradi mikubwa ni ule wa Kemondo wa kata saba. Kata hizo Saba ni Kata ya Kemondo yenyewe, Kata za Katerero, Bujugo, Kanyangereko, Maruku na Kata mbili ziko kwa jirani yangu Mheshimiwa Charles Mwijage Mayondwe na Muhutwe. Mradi umesogea umefika asilimia 80 na zaidi ni kazi nzuri inasonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu umekuwa wa zamani una umri wa miaka minne, sasa hivi tuko awamu ya pili inatakiwa shilingi bilioni 4.8 ili awamu ya pili ikamilike. Kata kadhaa zipate maji na ninaomba hizi fedha zitolewe shilingi bilioni nne na milioni mia nane ili maji yasonge kwenye vijiji vya jirani pale ambavyo vinahusika na hiyo awamu ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa kuna vifaa vinatoka Dar es Salaam, vingine vinatoka Uturuki, pampu za maji, imekuwa ni hadithi ya muda mrefu tunaomba ziletwe ili kazi hiyo isonge mbele na kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vingine miradi ipo lakini Mradi wa Kata ya Karabagaine umekuwa ni kizungumkuti. Pale tumepeleka maji Vijiji vitatu vya Kizuru, Kitwe na Kawa. Serikali ya mama Samia imesogeza maji kwenye vijiji hivyo, na pale ni Bukoba Vijijini lakini ule mradi umekabidhiwa Mamlaka ya Mjini, BUWASA. Kwanza sielewi kwa nini hiki kinafanyika, wajenge RUWASA wakamilishe kazi halafu mradi ukabidhiwe watu wa mjini waendeshe. Watu wa mjini wana bei kubwa. Sasa hivi kuna tatizo la kuunganisha maji kwa wananchi, maji yameshafika vijijini lengo ni kuwatua wanawake ndoo kichwani, lakini wanawake hawawezi kumudu yale maji, wanakwenda na ndoo zao mbali huko walikozoea maji yale hawayafaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ni nini hawa BUWASA wanaweka gharama kubwa sana. Gharama yao ni kuanzia shilingi 200,000 hadi shilingi 1,300,000 ya kuunganisha maji kwenye nyumba ya mtu, 200,000 ndiyo gharama za chini wengine mpaka 1,300,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lengo la Serikali ya mama Samia ni kwamba watu wapate maji safi na salama na ya kutosha, lakini hawa BUWASA wanaweka gharama kubwa ambayo wananchi wa vijijini hawawezi kuimudu. Niombe hili Mheshimiwa Waziri uliangalie na uingilie kati. Kwa nini mradi uhamie mjini wakati ni wa vijijini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu mmoja ametumiwa bili ya kuunganisha maji kwenye nyumba yake, ngoja noisome, imeandikwa hivi, Ndugu Charles Tibenderwa gharama zako za kuunganishiwa maji ni shilingi 464,396.40 na Kumbukumbu Na. ya malipo ni 994440341104, tafadhali lipa mapema kufuatana na maelezo uliyopewa na mamlaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu bwana yuko mita 80 toka maji yalipofikia, anaambiwa gharama ni shilingi 464,000 na zaidi. Sasa kwa kweli hili ni tatizo kubwa, lazima wananchi wapate maji kama Serikali inavyokusudia. Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa sasa kusitokee watu ambao wanataka faida kubwa kuzuia mafanikio ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yanayotokea Karabagaine yametokea tena vijiji vingine kwa mfano Kijiji cha Burugo, Kata ya Nyakato, hivyohivyo. Hii iko vijijini mradi umekabidhiwa kwa watu wa mjini wa BUWASA, matokeo yake gharama inakuwa ni kubwa, hawawezi kuimudu, naomba hii iangaliwe upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama hizi za kuunganisha maji, kushimba mtaro na kulaza mabomba, kwa nini wananchi wasiruhusiwe kuchimba mitaro wenyewe? Mabomba yanajulikana yapo madukani, kwa nini BUWASA isisimamie kama inataka iendelee na huu mradi, isimamie tu uchimbaji wa mtaro wa kutosha, mabomba mazuri class c, bei iwe himilivu wananchi wapate maji kama walivyokusudiwa badala ya kupandisha bei wananchi wakashindwa kupata hayo maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine uko pale Kata ya Katoma, maji yamekamilika pale katika Kijiji cha Ilogero, Kijiji cha Kashenge na kwingineko. Lakini kuna vita ya chini kwa chini. Huu mradi umejengwa na RUWASA, umekamilika, kazi ni nzuri, maji yako ya kutosha mazuri kwa wananchi. Kuna vita vya ndani kwa ndani, wanataka wauhamishie BUWASA mjini. Mradi uko vijijini kwa nini wanapambana kuupeleka mjini, ili wapandishe bei wananchi washindwe kupata huduma hii ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimalizie kwa kuomba, kuna mradi mwingine wa Kata sita za Izimbya, Kaitoke, Mugajwale, Ruhunga, Katoro na Kaibanja. Mradi huu umesemwa siku nyingi sana, miaka mingi unasemwa, tunaambiwa hadithi ileile upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Usanifu huu hauishi? Miaka zaidi ya mitatu, minne, tunaambiwa usanifu wa kina na upembuzi yakinifu. Naomba upembuzi ukamilike, usanifu ukamilike mradi uanze.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kuna ziwa Ikimba, maji mengi ya kutosha lakini watu hawawezi kupata maji. Katikati ya hizi Kata sita kuna Ziwa Ikimba, kubwa la kutosha lakini maji hayawezi kuwafikia wananchi kwa sababu ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Tunaomba mradi huu ukamilike nao uanze kujengwa wananchi wapate huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mkutano wa Kumi na Moja pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Nane na Mkutano wa Tisa
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nihitimishe hoja yangu. Napenda kusema nawashukuru sana niseme nawashukuru sana Wabunge kwa kuchangia hoja yetu kwa kuiboresha. Tumepata wachangiaji kumi na moja na nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuongezea pale ambapo palistahili kuongezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Ndogo ni sheria muhimu sana. Ninaweza kusema ni muhimu kuliko hata sheria kubwa (sheria mama) kwa sababu kwanza zipo nyingi kuliko sheria mama. Unaweza kukuta sheria mama moja ina Sheria Ndogo kumi au ishirini chini yake. Pia Sheria Ndogo zinaathiri wananchi moja kwa moja ndio zinawagusa kwenye barrier, kwenye majumba yao, biashara zao, usafiri na siku hadi siku ndizo zinazowaathiri katika maisha yao. Kwa hiyo, sheria ndogo ni sheria muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza hapa na Wabunge wamechangia kwa urefu kabisa. Kuna upungufu mkubwa ambao tumeyabaini kwenye sheria hizi ndogo. Sasa nafikiri ni vizuri tukasisitiza kwamba wale ambao tumewakasimu mamlaka ya kutunga sheria ndogo, wizara, halmashauri na mashirika mbalimbali ya umma wawe makini zaidi katika kazi hii ambayo tumewakasimu. Bunge limewakasimu na tunategemea kazi yao itakuwa nzuri, isiwe ya hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasikiuke Katiba kwa kuwa ipo na wanaijua, kwenye mamlaka hizo kuna wanasheria, kuna wataalam, wanasiasa na wanajua madhara ambayo wakikiuka sheria mama au katiba basi wanakuwa wamesababisha madhara makubwa kwa wananchi. Kwa hiyo, waongeze umakini ili kuondoa adha hiyo ya kuathiri wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii tumeisema mara nyingi sana. Nimekaa Kamati hii mwaka wa tatu huu nikiwa Mwenyekiti na kila nikisimama hapa tunasema rekebisha hiki, rekebisha hiki. Wapo wanaorekebisha lakini wapo ambao hawarekebishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru ambao mmerekebisha wengi tu. Mwezi wa pili nilisimama hapa nikatoa Taarifa ya Kamati na moja ya mambo niliyoyasema ni makelele kwenye makazi ya wananchi. Baa zinapiga muziki mpaka asubuhi, kumbi za harusi na sherehe mbalimbali, makanisa na misikiti yanapiga kelele. Baada ya kutoka hapa BASATA na NEMC wakachukua hatua, leo shida hiyo imekwisha. Hawa nawapongeza sana kwa kazi nzuri walioifanya lakini wapo wengine ambao hawafanyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninamshukuru sana Waziri Mchengerwa wa TAMISEMI ameshawaambia watendaji kwenye Wizara yake waache kuchukulia yale mambo ya business as usual, bora liende, na mazoea. Wajirekebishe na waongeze umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji kati ya wale kumi na moja tuliowapata wapo ambao wamependekeza. Tatizo hili kubwa inawezekana kwa sababu sheria hizi zinatumika kwanza, kabla ya kuja Bungeni. Mheshimiwa Luhaga Mpina ni mojawapo Mheshimiwa Aida Khenani na wengine. Nafikiri ni hoja ya msingi kwa sababu hizi sheria zinatungwa kule kwenye mamlaka ndogondogo, zinatumika kabla ya kuja hapa kuchambuliwa na zinaadhiri wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni janga kubwa (disaster) mtu akionewa na sheria kwa sababu hana pa kwenda, ukimuendea aliyemuonea anakwambia mimi nina sheria bwana, utampeleka wapi? Anaonewa na sheria ambayo ipo imetugwa na ni sheria halali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaelekea kukubaliana na Mheshimiwa Mpina na Mheshimiwa Khenani kwamba ni vizuri sheria zije kwanza hapa Bungeni, zipitiwe kwanza kabla ya kutumika ili wananchi wasiathirike. Sheria zije kwanza Bungeni zichambuliwe kwenye Kamati, kamati iongezewe uwezo na muda ifanye kazi hii kwa umakini zaidi. Inawezekana sio ngumu kwa sababu, hii nchi sio mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii imekaa miaka 60 na kitu ikiwa huru na sheria nyingi zipo. Kwa hiyo, inayokuja ile mara nyingi ina-replace sheria mbalimbali au ina-amend. Kwa hiyo, ikiwa imekuja hapa ikachelewa kule hawatakosa sheria, hakutakuwa na vacuum. Sheria itakuwepo hadi hii tuipitie hapa ikamilike ndiyo iweze kutumika, isitumike kwanza hadi ipite hapa tumalize kuirekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika bajeti hii kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya na bajeti hii ni mfano mmoja wa muendelezo wa kazi zake za kuboresha maisha ya Watanzania. Nampongeza sana na kumshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Mwigulu na wenzake wote kwenye Wizara kwa kutuletea bajeti hii ambayo ni ya viwango. Mwaka jana kwenye bajeti kama hii, Bajeti Kuu ya Serikali nilipata fursa ya kuchangia na nikazungumzia jambo nililoliita makambi ya kilimo ya vijana. Nikasema kwamba ningetamani kabisa kama vijana wangewezeshwa waanze kilimo cha makambi, kilimo kikubwa, wapewe nyenzo, wapewe matrekta, wapewe power tiller, wapewe pembejeo kama mbolea na mbegu, madawa na nini. Makambi yajengwe kwa majengo ya muda halafu kilimo kiwe kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashukuru sana kwamba mpango huu umeanza Mheshimiwa Bashe nampongeza sana unaitwa BBT. Wameupa jina jingine BBT (Building a Better Tomorrow), napongeza sana kwa sababu mpango huu utaenda kuondoa shida ya ajira kwa vijana na kuongeza uchumi kwa sababu wanazalisha mazao mengi watauza ndani na nje ya nchi watapata pesa na kupata utajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hofu yangu ni moja kwamba mpango ulivyokwenda umekuwa mno wa kutumia fedha, kingereza wansema capital intensive. Hii sina hakika kama itatusaidia, bahati mbaya tuna watu wengi ambao ni wezi. Wanakaa wameangalia pesa ilipo wadokoe. Sasa ndiyo maana mimi nikapendekeza kwamba, tungefanya utaratibu ule wa labor intensive, vijana wanapelekwa makambini, wanajengewa makambi yale wanapewa hata chakula, mahindi, unga maharage ya kuanzia wanapewa usimamizi, matrekta yale wanazalisha. Pesa kidogo sana lakini zaidi vifaa vile pembejeo na vifaa vingine ili watu wasipate mwanya wa kuiba hizi fedha, kazi ifanyike na matunda yapatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mtindo uliopo vijana wanakaa kwenye vyuo pale kwangu Bukoba pale Maruku Chuo cha Kilimo, kuna vijana sijui wangapi wametoka sehemu mbalimbali za nchi. Semina ya miezi sijui mingapi, mimi naona ile haina tija. Tija ingekuwa ni kutafuta maeneo mazuri mashamba ambayo tunayo mengi nchi nzima imejaa maeneo yenye rutuba na mvua na mito ipo, kilimo hiki kikasonga mbele kwa sababu kwa kweli kikifanikiwa hiki tutapata tija kubwa sana. Kwa hiyo, tuwe macho sana na matumizi ya fedha kwenye mradi huu au mpango huu badala yake tutumie ile ambayo nilipendekeza, kwamba iwe ni kutumia vijana na nguvu zao na vifaa wapewe badala ya kuwapa fedha ambazo zitatuletea matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwe macho sana na matumizi ya fedha kwenye mradi huu au mpango huu, badala yake tutumie ile ambayo nilipendekeza kwamba, iwe ni kutumia vijana na nguvu zao na vifaa wapewe badala ya kuwapa fedha ambazo zitatuletea matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza, hata kwenye Wizara ya Elimu tumeletewa mpango mpya hapa ambao baadaye kidogo, wanasema mwakani ikiwezekana itaanza utaratibu wa masomo ya sekondari ambapo kutakuwa na njia mbili. Kwanza ni masomo ya kawaida, mwanafunzi atasoma mpaka Form Four, lakini upande mwingine akipenda mwanafunzi anasoma masomo ya amali; ufundi, kilimo, ufugaji, na masomo mbalimbali. Hii nayo ni njia mojawapo ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu ambao wanamaliza shule, japo itachukua muda mrefu. Kwa hiyo, ule mpango wa kwanza wa BBT ukiboreshwa utakuwa ndiyo njia ya kukomboa tatizo hili kubwa la kukosa ajira kwa vijana wetu na kuongeza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipendekeza hata Wizara ya Biashara na Viwanda iwe na idara maalum pale Wizarani ya kutafuta masoko kwa mazao ya vijana hawa. Nilisema mazao ya muda kwanza ndiyo waanzenayo. Wakilima mazao kama mahindi, maharage, mtama, alizeti, ambayo yanavunwa haraka sana; miezi mitatu, miezi minne, lakini kuwe na kitengo maalum kwenye Wizara ya Biashara ambacho kitashughulika na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya hawa vijana kwa mazao yao. Ziko nchi nyingi ambazo hawalimi kama kule Uarabuni, Afrika ya Kati hapa, Darfur, Sudani na wapi. Kwa hiyo, mazao haya kile kitengo kisaidie kutafuta masoko ya vina hawa na kuwapelekea mazao na kupata biashara nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye Jimbo langu pale Bukoba Vijijini. Nimesema mara kadhaa kuna maeneo ambayo bado yana tatizo la maji. Kwa hiyo, naomba kwenye bajeti hizi haya maeneo yaangaliwe kwa jicho la huruma. Yako maeneo mengi ambayo yana shida kubwa sana ya maji, maeneo kama Umbweya pale kwangu, Kagarama, Vijiji vya Rugaze, Amani, Nsheshe na maeneo mengine kama Kanyangeleko na wapi, maji hayajafika. Kwa hiyo, bajeti ziongezwe kusudi maeneo haya nayo wapate majisafi, salama na ya kutosha kusudi shida ya wananchi katika maeneo haya ipungue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Bukoba kumekuwa na tatizo la muda mrefu la umeme kuzimika mara kwa mara. Kwanza napongeza umeme unasonga kwenye vijiji na vitongoji, kila siku kuna hatua inapigwa, lakini pamoja na hatua hiyo, umeme huu hauaminiki, unazimika sana. Ukizimika, sasa tija yake haionekani, na vifaa vinaharibika; kama ni taa, zinaungua, kama una fridge au nini, vinaungua mara kwa mara na wananchi wanapata shida kubwa sana. Ni hasara kubwa. Kwa hiyo, kazi kubwa inatakiwa ifanyike pale, bajeti iongezwe, kutafutwe njia ya kuondoa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kazi inafanyika, lakini kasi iongezeke. Njia sahihi ni kuweka ile gridi badala ya kutumia umeme wa Uganda, tutumie umeme wa Tanzania. Gridi isogezwe ifike mpaka Kagera na Bukoba yote ipate umeme huu wa gridi kusudi tatizo hili la umeme kuzimikazimika liwe ni historia, liishe na wananchi wafaidi umeme huu na hili tatizo la vyombo vyao kuungua liishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na jambo moja la mwisho ambalo hivi karibuni Serikali imeruhusu tena mabasi ya abiria kusafiri usiku kucha. Mwaka 1987 nilikuwa nakaa Dodoma hapa nafanya kazi Wizara ya Serikali za Mitaa, lakini familia yangu ilikuwa inaishi Dar es Salaam. Kwa hiyo, nilikuwa nasafiri sana Dar es Salaam – Dodoma. Nilichokiona barabarani ni kitu kibaya sana. Usafiri wa usiku siyo mzuri. Hatujaweza kudhibiti madereva wetu kuwa na nidhamu ya kulala mchana wasafiri usiku. Mchana wanafanya kazi nyingine ya kubangaiza, usiku anaendesha gari. Ajali zilikuwa ni nyingi sana. Watu wanakufa, mabasi yanawachinja barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Malecela akiwa Waziri Mkuu, ndiye aliyefuta mabasi kusafiri usiku mwaka 1994. Sasa leo tumerudisha, sifahamu tumejiandaaje na jambo hili. Tutapata tatizo la kupata ajali nyingi sana barabarani usiku, watu watakufa sana. Tujiangalie kama hatujafikia uwezo wa kuyadhibiti magari haya, tusifanye hivyo. Tuendelee kusafiri mchana na tuache kusafiri usiku. Kama tunaweza, basi tuendeleenalo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri sana anayoifanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Anafanya kazi kubwa sana, wote tunaona miundombinu inavyojengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa natoka Dar es Salaam kwa njia ya barabara nikaona magari ya IT kutoka bandarini kwenda nchi jirani mengi sana msururu, foleni ya magari barabarani kuonyesha kwamba bandari imeboreshwa na magari mengi yanaingilia Dar es Salaam kwenda huko Malawi, Zambia, Rwanda na kwingineko. Hayo ni maendeleo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kuwa na mipango mizuri, sera, ilani na kadhalika ambapo yote kwa ujumla wake ni kuboresha maisha ya Watanzania, ipo vizuri na inajipanga vizuri. Naipongeza Wizara ya Ujenzi, Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri, Watendaji wote, TANROADS na taasisi nyingine ambao wako katika Wizara hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia mambo mawili ambayo yananihusu moja kwa moja. Kule Kagera miaka ya nyuma tulipima uwanja wa Kajunguti, home Kajunguti. Ulipimwa vizuri, vipimo vikaonekana kwamba uwanja unafaa pale, fidia kwa wananchi ikahesabiwa ikawa inatafutwa kwamba thamani ya uwanja ule ilikuwa ni nini? Ikabainishwa, ikajulikana, lakini baadaye haukujengwa ule uwanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule uwanja ni muhimu sana. Pale ulipopimwa kujengwa ni mahali sahihi kabisa. Leo tuna Jumuiya ya Afrika Mashariki, ina Kenya ndani yake, ina Uganda, Sudan ya Kusini, Rwanda, Burundi, Kongo DRC, na sisi wenyewe Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Kajunguti, home Kajunguti ni katikati ya nchi hizi saba. Kwa hiyo, uwanja huo ungejengwa pale ungekuwa ni kitovu kikibwa sana cha uchumi cha nchi hii. Kutoka pale kwenda Kampala kwa gari ni masaa mawili, kutoka pale kwenda Kigali, Rwanda kwa gari ni masaa mawili na nusu, kutoka pale kwenda Bunjumbura kwa gari ni masaa matatu, kutoka pale kuingia Uganda kwa gari ni nusu saa, kwenda Kenya kwa gari au kwa maji ni masaa mawili na nusu, na vilevile kwenda Sudan siyo mbali, Tanzania ndiyo sisi wenyewe tupo hapa. Kwa hiyo, ingekuwa ni kitovu cha uchumi na kuleta maendeleo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale yaliyozunguka pale yana mvua nyingi, yana rutuba. Mfano Masaka pale Uganda Kusini au Mbarara au Kisumu kule Kenya kwa wakulima wa maua na mboga mboga, tuna samaki pale Ziwa Victoria. Pale zingekuja ndege za mizigo, zingepeleka mizigo hii Ulaya, Marekani, na kadhalika na ndani ya muda mfupi maua au mboga mboga zikiwa fresh. Tungepata uchumi mkubwa sana kwa kuwa na uwanja ule. Kwa hiyo, napendekeza kwamba uwanja huu ujengwe na kazi iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili pale Jimbo la Bukoba Vijijini lina barabara moja kubwa muhimu, ni muhimu sana. Barabara inayoanzia Kietema kwenda Kanazi kutokea Igwela, Katoro hadi Kyaka kilomita 66. Barabara hii ni muhimu sana sana sana na nimeizungumzia sana barabara hii hapa Bungeni na nje ya Bunge. Humu ndani Bungeni peke yake leo ni mara ya tano naizungumzia barabara hii kwa njia ya mchango kwa njia ya maswali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wabunge wengine walioongea jana majibu ni tunajenga, tunajenga, tunafanya upembuzi yakinifu, tunajenga lakini barabara ile haijajengwa. Ile barabara ni muhimu kwa sababu inahudumia karibia jimbo zima, Wilaya nzima ya Bukoba Vijijini. Inahudumia kwenye Jimbo langu peke yake kata 20 kati ya Kata 29 ukiunganisha na Jimbo la Nkenge la Mheshimiwa Kyombo Kata tatu linahudumia jumla ya Kata 23 kupeleka mazao sokoni kule mjini, pembejeo kwenda kwa wananchi kule ndani ni barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wagonjwa, kule ndani kuna watu karibu 400,000 wanaohudumiwa na barabara hii. Ukiwa na watu 400,000 kwa siku moja wagonjwa hawapungui 1,000 ambao wanakwenda mjini kutibiwa wanatumia barabara hii. Sasa kila neema ina matatizo yake, kule kuna mvua nyingi sana. Mwezi uliopita, mwezi wa nne masika tulipata mvua siku tatu mfululizo bila kuacha, siku tatu usiku na mchana inanyesha. TANROADS wanajitahidi sana wanakarabati ile barabara mara kwa mara lakini wanakarabati leo kwa njia ya kifusi cha changalawe, kesho yake ni mashimo ni mahandaki haipitiki, kwa hiyo, haifai inatakiwa iwe kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanafia kule vijijini hakuna njia ya kupita kwenda hospitali, hakuna huduma. Uchumi unakwama, pembejeo haziwezi kwenda kule ndani, mbolea na mbegu na nini kwa ajili ya mazao ya kahawa na mazao mengine. Kwa hiyo, tunaomba barabara hii ijengwe. Na kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, CCM na Serikali yake imeweka kwenye Ilani ya Uchaguzi wa Mwaka huu 2020 - 2025. Hata iliyopita 2015 ilikuwemo kwenye Ilani lakini haikujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na siyo tu Ilani, nashukuru kwamba TANROADS wamefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na imekamilika lakini ujenzi haujaanza. Naomba ujenzi wa barabara hii uanze kwa sababu ni barabara muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina daraja kubwa sana pale katikati linaitwa Kalebe, daraja la Kalebe ni daraja kubwa sana, kubwa lakini la kizamani sana, limezeeka kweli kweli. Limejengwa miaka mingi na ndiyo njia pekee ya kutoka huko kwenye Kata 23 hizo kwenda Mjini Bukoba. Hakuna njia ya mchepuko, kama hiyo njia haipitiki au daraja halipitiki basi watu wanabaki huko ndani kama mtu anaumwa anafia huko hakuna njia mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lile daraja lilipojengwa lilikuwa na uwezo wa kubeba tani tano wakati huo likiwa jipya zima. Sasa limezeeka ninahakika limepungua uwezo lakini magari ya tani 15, malori ya kahawa, ya mbolea, watu wanakwenda kwenye harusi, kwenye sherehe mbalimbali, mabasi yanapita pale tani 10, tani 15, litauwa watu lile daraja, litaua. Miaka ya nyuma pale Dar es Salaam kulikuwa na daraja la chuma kutoka Banana kuja Kinyerezi tani saba ilikuwa mwisho.
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Rweikiza kwa mchango mzuri; kengele ya pili.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja lakini naomba daraja hilo lijengwe. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie Wizara hii muhimu ya Nishati. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri January Makamba, Mheshimiwa Naibu Waziri Stephen Byabato na watumishi wote wa Wizara, viongozi na watumishi wa taasisi mbalimbali chini ya Wizara, REA na nyinginezo kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru pia kabla sijasahau, jambo la juzi la kutuletea wataalam hapa Bungeni wa TANESCO, REA na mashirika mengine lilikuwa ni jambo muhimu sana na zuri sana. Ahsanteni sana. Tumezungumza na wale watu, wametusaidia matatizo yetu kwenye majimbo na kasi imeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nizungumzie umeme na nizungumzie umeme Bukoba Vijijini. Kama walivyosema wenzangu umeme ni suala la maendeleo siyo suala la anasa, ni tija ya maendeleo, ni uchumi, umeme ni siasa kwa sisi ambao tuko kwenye siasa, unatusaidia mambo mengi yanakwenda, yanasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pale Bukoba nishukuru kwanza kwamba kasi ya maendeleo ya umeme ni kubwa ni nzuri lakini kuna tatizo kubwa sana. Bukoba na Kagera nzima kama walivyoongea wengine hapa wachache, umeme unazimika sana, ukiamka asubuhi ukakuta umeme unawaka, utakuwa na bahati kama utafika saa nne haujazimika. Saa sita utazimika tena, kwa siku unazimika mara nane, mara 10 au mara 20. Kwa hiyo, inakuwa ni matatizo makubwa na kama una kiwanda kidogo hutaona tija yoyote, itakuwa ni hasara kubwa kuwa na umeme kwenye kiwanda chako. Kama una taa zako zitaungua, kama ni fridge itaungua na vitu vingine vya umeme, unakuwa huna tija na umeme huo kwa sababu umeme unazimikazimika mara nyingi sana kwa kutwa moja usiku na mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu inafahamika, sababu ni kwamba umeme wa Bukoba unatoka Uganda tunaununua nchi jirani ya Uganda. Uganda wenyewe wana shida ya umeme, wana mgao. Kwa hiyo, wanapoleta umeme Bukoba ni umeme kidogo kuliko mahitaji yaliyopo na Kagera kwa ujumla. Kwa hiyo, wakipunguza kidogo, basi umeme unazimika kwenye maeneo yetu. Sasa mfumo, ile gridi ya Taifa imekaribia kufika kwenye maungio kule Bukoba, umeshaingia mkoani nafikiri uko sehemu za Muleba au nyuma kidogo pale. Naomba Wizara ifanye kazi kubwa ya kuongeza kasi kusudi mfumo huu, gridi ya Taifa iunganishwe na Mkoa wa Kagera tuondokane na umeme wa kutoka nchi jirani ambao hautoshi, matokeo yake ni kuzimika umeme mara kwa mara, hivyo, inakuwa shida kubwa sana kwa watumiaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nashukuru kwanza, kwamba kasi kama nilivyosema ya kufunga umeme kwenye vijiji mbalimbali ipo. Pale kwangu kuna vijiji vingi ambavyo havijapata umeme, Kijiji cha Buzi, Kijiji cha Buguluka, Kijiji cha Musira, Kijiji cha Butakya, Bituntu, Sheshe, Lukoma na vingine vingi, lakini kasi ipo, machimbo yamechimbwa na tunaanza kuwa na matumaini kwamba umeme utafungwa, nashukuru kwa hilo. Hata hivyo, tusifikiri kwamba kwa kufunga umeme kwenye vijiji hivi na vile ambavyo vimeshafungwa tayari, tumepiga hatua kubwa sana, bado kabisa, bado kabisa, vitongoji vingi vingi havina umeme, watu wengi sana hawana umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kijiji kizima nitakusomea mifano hapa michacho ya kata mbili. Kuna Kata moja inaitwa Kyamulaile. Kata ya Kyamulaile ina vijiji vinne, kijiji Omkihisi kina kaya 490 ni kaya 10 tu zenye umeme. Kijiji cha Kyamulaile yenyewe ina kaya 863, kaya zenye umeme ni 38. Nina Kijiji Mashule, kina kaya 1,085, kaya zenye umeme ni sifuri, hata moja yenye umeme hakuna, lakini kwenye mtandao wa TANESCO na REA wanahesabu na hiki kijiji kina umeme wamekimaliza. Kaya yenye umeme sifuri, walifunga umeme kwenye chanzo cha maji pale wakaondoka. Wananchi wote, kaya zote hazina umeme. Kata ya Nyakibimbili, Kijiji cha Bundasa kina kaya 610, kaya zenye umeme 19. Kijiji cha Bugengele, tuna kaya 368, kaya zenye umeme 28. Kijiji cha Kitaya kuna kaya 330, zenye umeme kaya 27.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inaonesha kazi ya kufunga umeme bado ni kubwa sana, tunahitaji msukumo mkubwa wa REA wa TANESCO kuongeza kasi. Tusifikiri kwamba kufunga vijiji vyote kama tunavyoambiwa Desemba walikuwa wanafunga vijiji vyote kazi imeisha, kazi bado ni mbichi kabisa, ni kubwa. Mbaya zaidi kule Bukoba wanapokwenda kufunga umeme kwenye kijiji kingine au kitongoji fulani wanapita juu ya nyumba za watu. Juu kuna waya za umeme, chini nyumba hazina umeme, sasa nafikiri kwamba ni rahisi ukishafika pale wateremshie watu umeme ambao wamepitiwa na zile waya ili nao wapate matunda ya kupitishiwa pale waya hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia unafyeka mazao yao, sisi kule mazao yetu ni kahawa na migomba, wanafyeka, yote wanatoa, mtu ana nusu heka, yote inafyekwa, lakini hapati umeme. Sasa unashangaa huyu mtu kwa nini wanamuadhibu na umeme hawampi. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ingekuwa bora sana hawa nao wafikishiwe huduma ya umeme kama ambavyo wanapelekewa wale wengine ambao wanapitishiwa pale juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na bajeti nzuri, lakini zaidi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuboresha uchumi wa nchi hii. Maana hapa tunachangia bajeti na hali ya uchumi wa Taifa na Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana katika muda mfupi kuboresha uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia hapa na tumeona wenyewe hata baada ya royal tour ameshafanya mambo mengi sana. Juzi akiwa Oman pale nikaona wanarusha documentary pale, filamu ya kuonesha mazingira ya Tanzania yalivyo ili kuvutia wawekezaji katika kilimo, katika viwanda na maeneo mengine. Yote haya ni mapambano anayofanya, anatupigania ili kuboresha uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda niongelee kuhusu Tanzania ilivyo katika nafasi nzuri ya kuwa kituo cha biashara. Nikisema Tanzania namaanisha Dar es Salaam. Dar es Salaam ni hub ya biashara ya nchi nyingi ambazo zinatuzunguka. Tuko katika nafasi ya kijiografia ya kuhudumia watu wengi sana. Sasa mpaka sasa hivi tunafanya kazi hiyo, lakini Dar es Salaam imekuwa kama kituo cha kupitishia bidhaa za watu kutoka nchi nyingine huko Uarabuni na Asia kuingia Dar es Salaam kwenye meli na kupita kwenda nchi hizo jirani. Sasa ninachotaka kusema ni kwamba, tuboreshe hii isiwe ni kituo cha kupitishia, tufanye zaidi Dar es Salaam iwe ni kituo cha biashara. Hii ya kuona makontena yanaingia Dar es Salaam yanabebwa na kwenda nchi nyingine, magari na mizigo mingine sawa ni nzuri kabisa, lakini tuongeze zaidi ya hapo, tuifanye kituo cha biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna nchi nyingi ambazo zinatuzunguka baada ya sisi wenyewe ambao ni wengi zaidi ya Milioni Sitini lakini tuna nchi kama Msumbiji tuna nchi kama Malawi, ambayo tena haina bandari, Zambia haina bandari, Zimbabwe haina bandari, Congo - DRC ingawa ina bandari kule Kinshasa lakini kutoka Lubumbashi kwenda Kinshasa ni kilomita 2,500, kutoka Lubumbashi kwenda Dar es Salaam ni kilomita 1,200, kwa hiyo lazima walubumbashi waje Dar es Salaam hawawezi kwenda kule Kinshasa na wa Kivu, Goma na wote wa Congo Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Rwanda kuna Burundi, Uganda tuna Sudani ya Kusini hata Kenya watakuja hapa tukifanya Dar es Salaam kiwe kituo cha biashara, tuna nchi kwenye bahari huku Seychelles, Madagasca, Comoro na nyingine. Hata Ethiopia siyo mbali, Central African Republic - Afrika ya Kati siyo mbali kutoka Dar es Salaam kwenda pale iwapo watajua kwamba Dar es Salaam ni kituo cha biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanatoka Congo wanatoka na nchi zote hizi nilizozitaja wanakwenda nchi za mbali huko Urabuni na Japan na wapi na Thailand kununua vitu, vitu hivyo viwe Dar es Salaam, ajue kwamba akija Dar es Salaam ataipata pale kama ni magari kama ni nguo, madawa, vipodozi, kama ni spare parts, ziwe Dar es Salaam. Dar es Salaam iwe kituo cha biashara tuongeze kwa maksudi uuzaji wa bidhaa, ujanja ni kuuza ukiuza zaidi unapata faida, ukiuza kidogo ndiyo nakisi (deficit), kwa hiyo tuongeze uuzaji wa bidhaa kwa ndugu zetu hawa majirani zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kazi ndogo sana, ni kubwa kwa maana kwamba inabidi tufanya maamuzi magumu inabidi kufuta kodi - VAT ili bei zipungue mtu asione umuhimu wa kwenda Dubai au Japan aone umuhimu wa kununua Dar es Salaam kitu kile kile. Kwa mfano gari mtumba ambalo angelinunua Japan anunue Dar es Salaam au nguo za Thailand anunue Dar es Salaam, tuondowe VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi kuna vifaa ambavyo kama mtu anapeleka nchi za nje anakwenda nacho akifika mpakani anakiacha pale inaitwa gadget ya customs kwamba ametoa nje kwa hiyo hakulipa VAT ni sahihi, tukisema tuwarudishie VAT zao hatuwarudishii, hata akienda hapo hatuwarudishii zile VAT inakuwa ni usumbufu mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dubai walifuta VAT miaka ya 90 na kitu mwanzoni ikawa kituo cha biashara sana, Afrika yote hii tukawa tunakwenda Dubai kufanya shopping kununua vitu kule, magari hayo vifaa mbalimbali stationary na vingine, mpaka siku moja nikakutana na mtu wa kutoka Spain ananunua tairi za Spain Dubai, kule kwao ni bei kubwa kuliko Dubai! Nikakuta kwamba siku moja nikawa nasoma maandishi pale Airport Dubai watu wanaotoa Dubai kwa siku moja mwaka 2001 walikuwa watu Laki Tano, wakati huo VISA ilikuwa Shilingi Dola 50 mara Laki Tano kwa siku moja walipata income ya VISA Dola Milioni 25 kwa siku moja VISA peke yake! Bado hajalipia hoteli anakolala, chakula anachokula, usafiri atakaopanda pale Mjini Dar es Salaam, VISA peke yake walikuwa wanapata Dola Milioni 25 kwa siku moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hii tukiifanya Dar es Salaam tukaongeza uuzaji wa bidhaa tutapata mapato makubwa, hata hayo ambayo tumefuta kwenye VAT itarudi kwa njia nyingine za kuuza bidhaa. Kwa hiyo, nafikiri tuifanye hii iwe ni mkakati maalum wa kuongeza uuzaji wa bidhaa pale Dar es Salaam tusibaki tu kupitisha mizigo ya watu kwenda nchi jirani, wapite ndiyo waje, meli zije na makontena na mizigo mingine lakini pia tuuze vya kwetu tuongeze ufanisi mkubwa kwenye kuuza.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kufuta ada ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, huu ni msaada mkubwa kwa Watanzania, wazazi imesaidia kuongeza urahisi katika kusomesha Watoto, ada imefutwa na ni jambo kubwa. Ninaamini kwamba Wasaidizi wake wanaotenda kazi hasa TAMISEMI wataacha kuzuia watoto kusoma. Maana yake unapozuia watoto kusoma na Rais anatoa kila njia kuongeza ufanisi kwenye kusoma inashangaza. Wanazuia kwamba watoto wasifanye tution wasibaki kwenye makambi kusoma, Rais anaongeza bidii watoto wasome lakini Watendaji wa Wizara hasa TAMISEMI wanazuia watoto kubaki shuleni kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanafunzi hajawahi kumwona Mwalimu wa Sayansi shuleni kwake, kwa hiyo shule zikifungwa, shule hii inaazima Mwalimu shule jirani aje pale afundishe masomo ya sayansi ambayo ameyakosa kule, sasa mnazuia kwamba wakifunga shule waondoke si sahihi! Mheshimiwa Rais anapambana elimu iboreshwe na ninyi mumsaidie. Mnasema tuition marufuku siyo sahihi. Kwanza Walimu kama nilivyosema hawapo, kuna vijana ambao wametoka Chuo Kikuu hawajapata ajira ya Serikali au ajira yeyote anafungua tuition center afundishe hesabu, afundishe masomo ambayo mwanafunzi kule ameyakosa shuleni apate naye kipato kidogo ajikimu, unazuia kwamba tuition siyo sahihi, siyo sawasawa hii ikome.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnazuia wanafunzi wasibaki mashuleni lakini mnaruhusu UMISETA wakae shuleni UMITASHUMTA ile ya Shule za Msingi wabaki shuleni wafanye michezo lakini kwenye kusoma wasibaki kwa nini kama siyo kuhujumu elimu? Hapo nafikiri tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada zake katika kuboresha elimu ya nchi hii na tukifanya hivyo sote tukamuunga mkono na juhudi alizonazo tutafanikiwa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja yangu, nakushukuru sana. pia, nami nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongoza nchi hii vizuri na kuhakikisha kwamba anailetea nchi hii maendeleo kwa kasi kubwa na tuna utulivu na amani ya kutosha kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru wachangiaji wote ambao wamechangia hoja yangu kwa umakini na ufasaha mkubwa, jumla tumepata wachangiaji 14 na wote wameunga mkono hoja, kufafanua na kuongeza nyama kwenye hoja yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu kwa maelezo aliyoyatoa, lakini siyo tu maelezo aliyoyatoa hapa bali hata mchango wake kwenye Kamati yetu. Kazi za Kamati zinakwenda vizuri kwa sababu ya msaada wake anaotupatia na uratibu mzuri sana. Vilevile, nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi hiyo, ofisi yake imekuwa msaada mkubwa kwenye Kamati yetu na watumishi chini yake wamekuwepo muda wote kwenye Kamati, tunakuwa nao kwenye uchambuzi kujadili mambo mbalimbali na wanatusaidia sana kwa utaalam na uzoefu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru na kuwapongeza Sekretarieti ya Kamati ambayo inafanya kazi masaa 24, Ofisi ya Katibu wa Bunge ambayo nayo inatusaidia kwenye uratibu wa shughuli za Kamati. Kipekee niwashukuru Wabunge wote ndani ya Bunge hili kwa kuunga mkono kazi za Kamati yetu, mmeona hapa michango iliyotoka Wabunge wote wanatuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo ni chombo cha Bunge hili. Ni chombo cha Bunge hili cha kutazama ubora wa sheria zinazotungwa na mamlaka nyingine na watu wengine huko tuliowakasimu kazi hiyo na kuchuja na kuona kama ziko bora na kukidhi viwango vya sheria zinazotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopata sheria hizi zinapowekwa mezani hapa, tunaanza kuchambua. Tunachambua na tunaona kama ziko sawa, baada ya hatua hiyo tunawaita wahusika, tunajadiliana nao, tunawasikiliza, tunawauliza maswali na wenyewe wanatuuliza maswali, tunakwenda pamoja na tunawashirikisha vizuri. Baada ya hatua hiyo tunachambua tena kwa niaba ya Bunge hili, lakini sisi ni Wabunge kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hii, tunakuwa na mawazo ya wapiga kura wetu na tunaangalia maslahi ya wapiga kura wetu. Kwa hiyo, tunafanya kazi hiyo kwa kuzingatia hasa maslahi makubwa ya wananchi tunaowawakilisha hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua hizo zote tunaleta taarifa yetu hapa Bungeni na Wabunge nao wanapata nafasi ya kujadili na kuchambua kwa umakini mkubwa kama walivyofanya leo, mmeona hapa na baada ya hatua hiyo Bunge linatoa maazimio ya kutekelezwa na wahusika wa kutunga zile Sheria Ndogo na wanapewa maelekezo hao waliotajwa hapo ambao ni watunga sheria hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kuondoa usumbufu kwa wananchi ili wananchi wapate sheria ambazo ni nzuri zinazotekelezeka vizuri, kusiwe na kero yoyote kwa wananchi au uonevu. Mmesikia michango ya Wabunge hapa, kuna baadhi ya sheria zina uonevu kama ile ya kupara samaki, unamtoza ushuru, kwa kweli ni uonevu kwa wananchi. Kwa hiyo, lengo letu sisi ni kuondoa kero hizo ili wananchi wasiwe na uonevu au usumbufu wa aina yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapochambua na kuangalia utekelezaji, tunazingatia kama Sheria zinakidhi misingi yote ya utungaji wa sheria, hazikinzani na Katiba ya Nchi, hazikinzani na Sheria Mama iliyotoa mamlaka ya kutunga sheria hiyo ndogo na hazikinzani na sheria nyingine yoyote, zinakuwa katika muktadha wote wa Sheria zote za Nchi. Hazikinzani na Sheria Na.1, Sura Na.1 (CAP.1) Sheria ya Tafsiri ya Sheria, kwa ujumla hazikinzani na maslahi ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sheria ni nyingi sana kama walivyosema wenzangu hapa Wajumbe wa Kamati, kazi ni kubwa lakini tunaifanya kwa umakini mkubwa na tunasonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jukumu hilo kwa kweli ni la Bunge, kama nilivyosema hii Kamati inafanya kazi hiyo kwa niaba ya Bunge na tunachambua kwa umakini mkubwa na tunasonga mbele. Sasa, Bunge lina wajibu wa kutunga sheria nzuri ambazo zinatekelezeka, zina uhalisia, majedwali yako vizuri na lazima liwe na wivu wa kazi yake. Sheria zikiwa nzuri sifa ni kwa wale waliotunga na Bunge pia, lakini zikiwa mbaya lawama ni kwa Bunge, wale wanasahaulika na lawama zinakuja kwa Wabunge kwamba, hili Bunge vipi linatunga sheria mbovu kama hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba wote waliopewa maelekezo mahsusi, kwa mfano tumesema hapa kuna baadhi wameambiwa hapa tarehe 27 mwezi huu Septemba saa 9.30 mchana walete kwa Katibu wa Bunge, kuitikia maelekezo ya Kamati na maelekezo ya Bunge. Wengine wamepewa maelekezo mahsusi tarehe 20 mwezi Desemba saa 9.30 mchana wawe wameleta majibu hayo kwa Katibu wa Bunge ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)